• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Vita baridi Mlimani kati ya Rigathi na Ndindi Nyoro

Vita baridi Mlimani kati ya Rigathi na Ndindi Nyoro

NA MWANGI MUIRURI

NAIBU Rais Rigathi Gachagua na mbunge wa Kiharu Bw Ndindi Nyoro wako katika mvutano fiche wa ubabe katika eneo la Mlima Kenya lakini wakijaribu juu chini kutorukiana moja kwa moja.

Hatua ya Bw Nyoro kuweka bango kubwa katika mji wa Kenol kumkaribisha Rais William Ruto alipofanya ziara ya siku tano mnamo Agosti 5, 2023 iliangazia mvutano huo.

Katika bango hilo, Bw Nyoro aliweka picha ya Rais Ruto pamoja na yake na kuweka maandishi “karibu shujaa”.

Siasa za mabango hapa nchini huwa muhimu sana kwa kuwa hudhihirisha uaminifu na ukuhani katika siasa.

“Hatua hiyo ya Bw Nyoro ya kuwa wa kipekee kumkaribisha Rais Ruto bango kama hilo ilikuwa na ujumbe fiche wa kisiasa. Walioona bango hilo ni lazima walimuona Bw Nyoro kama aliye na imani kuu kwa Rais Ruto kuwaliko wengine wote akiwemo Bw Gachagua,” asema Bw Charles Mwangi, mwanasiasa na mchanganuzi eneo la Murang’a.

Alisema kuwa bango hilo lilikuwa na ujumbe mkuu wa kisiasa ukiwemo uwezekano kwamba liliashiria hali huenda iwe namna gani mwaka 2027 Rais Ruto atakapokuwa akisaka awamu ya pili afisini.

“Hii ni siasa na huenda hata Bw Nyoro awe na maono ya kuwa Naibu Rais au hata Rais katika siku za usoni,” akasema.

Suala lingine ambalo limechipuka katika siasa za Bw Gachagua na Bw Nyoro eneo la Mlima Kenya ni kwamba ni vigumu uwapate wawili hao katika hafla moja isipokuwa wakati Rais Ruto amehudhuria.

Hata wakati ambapo Bw Gachagua ametembelea eneobunge la Bw Nyoro la Kiharu, mbunge huyo huwa hajitokezi.

Ajabu ni kwamba, wakati Bw Nyoro huwa hajitokezi katika hafla za Bw Gachagua katika eneobunge la Kiharu, mnamo Agosti 10, 2023, wakati mkewe Naibu Rais, Bi Dorcas Rigathi alikuwa ametembelea eneobunge hilo, mbunge huyo alijitokeza. Pasta Dorcus alikuwa ametembelea Shule ya Upili ya Kahuhia na ambapo Bw Nyoro alihudhuria.

Wakati Bw Gachagua alikuwa amehudhuria hafla ya serikali ya Kaunti ya Murang’a katika uwanja wa Ihura ulioko katikati mwa mji wa Murang’a na ulio katika eneobunge la Kiharu mnamo Januari 26, 2023, Bw Nyoro hakujitokeza katika hafla hiyo ya kuzindua mpango wa kaunti wa basari kwa wanafunzi.

Ni katika hafla hiyo ambapo Bw Gachagua alitangaza vita dhidi ya ulevi kiholela akisema “hawa wakinywa kiholela nani atatuchagua… nani atanichagua?”

Swali hilo huenda lilichukuliwa na wafuasi wa Bw Nyoro kuwa la kutangaza nia ya kuwania urais 2027 au 2032. Huenda walikerwa na hatua ya Bw Gachagua kuchagua eneobunge la Kiharu kufanya tangazo kama hilo huku Bw Nyoro akiwa hayuko.

Mnamo Februari 15, 2023, Bw Nyoro aliwaleta pamoja wanasiasa kadha katika hafla ya kuzindua ruzuku ya karo kwa wanafunzi wanyonge ambapo alipigiwa debe kama mfaafu zaidi kuchukua ufalme wa Mlima Kenya katika ulingo wa siasa siku za usoni.

Waliomsifu Bw Nyoro walimrejelea kuwa ni mwandani wa Rais Ruto, mwerevu na aliyekuwa na ‘nyota’ ya uongozi. Waliomtunuka sifa hizo ni mbunge wa Dagoretti Kusini Bw John Kiarie, Seneta wa Murang’a Bw Joe Nyutu, mwenzake wa Nandi Bw Samson Cherargei na Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Kaunti ya Nandi Bi Cynthia Muge.

Mbunge wa Kimilili Didmus Barasa na pia mbunge wa Mukurweini Bw John Kagucia walikuwepo.

Hafla hiyo ya Bw Nyoro ilipangwa kwa weledi mkuu ambapo hata ilipeperushwa moja kwa moja na kituo cha runinga cha Inooro.

Wakati habari hizo za wasifu wa Bw Nyoro zilichapishwa, Bw Gachagua katika hafla ya mazishi katika eneobunge la Gatanga mnamo Februari 23, 2023, alijitokeza kwa hasira akiwataja walioeneza habari hizo kama “walevi, wazushi na wafuasi wa siasa za upinzani”.

Baadhi ya wanasiasa hao waliripoti kuhangaishwa katika kuafikia marupurupu na mishahara ya wafanyakazi wao kutoka kwa afisi ya Naibu Rais.

Mnamo Machi 23, 2023, Bw Gachagua alikuwa katika eneobunge la Maragua ambapo alitembelea taasisi ya Kiufundi ya Maragua na pia Shule ya Msingi ya Thaara lakini Bw Nyoro hakujitokeza.

Wawili hawa, ambao pia humenyana kuhusu suala la Maumau hujitambulisha kama watoto sugu wa harakati hizo za kivita za kusaka uhuru wa Kenya. Hizi zote ni dalili kwamba wawili hawa wako katika vita baridi.

Katika mazishi hayo ya Gatanga, Bw Gachagua aliyeonekana mwenye hasira alisema kwamba “mimi sijali kile nitakuwa katika siasa za baadaye, kazi yangu kwa sasa ikiwa ni ile ya kufurahisha wakazi wa Mlima Kenya”.

Aliwataka “viongozi wenzangu kukoma siasa za uchaguzi mkuu na badala yake kwanza tuhudumie wananchi”.

Ni ushauri ulioonekana kumlenga Bw Nyoro na ‘makuhani’ wake wa kumpigia debe.

Mvutano huu unatazamiwa kuzidi makali na mawimbi na huenda uwe kimbunga kikuu jinsi uchaguzi mkuu wa 2027 unavyobisha.

  • Tags

You can share this post!

Kenya yaambulia patupu marathon ya wanawake jijini Budapest

Chirchir, Siror waagizwa kufika mbele ya Kamati ya Kawi...

T L