• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Voliboli: Kenya yafaa kujiandaa upya kabla ya African Games

Voliboli: Kenya yafaa kujiandaa upya kabla ya African Games

Na GEOFFREY ANENE

KENYA italazimika kujipanga tena kabla ya michezo ya African Games mwezi Agosti nchini Morocco, baada ya timu yake ya Malkia Strikers kuambulia nambari mbili kwenye Kombe la Voliboli ya Afrika ya Wanawake kwa mara ya pili mfululizo, Jumapili usiku.

Warembo wa kocha Shaileen Ramdoo walipoteza dhidi ya Cameroon kwa seti 3-2 (17-25, 27-25, 23-25, 25-23, 14-16) katika fainali kali jijini Cairo, Misri.

Jumatatu, Malkia Strikers walitarajiwa kuandaliwa dhifa ya chakula cha mchana na Balozi wa Kenya nchini Misri, Joff Otieno kabla ya kuabiri ndege ya kurejea Kenya saa nne kasorobo usiku. Walitarajiwa jijini Nairobi saa tisa na nusu leo asubuhi.

Mechi ya fainali kati ya Kenya na Cameroon ilikuwa marudiano ya mechi ya makundi pale Malkia Strikers ilipepeta Cameroon 3-2 na kuingia nusu-fainali.

Hata hivyo, Kenya ilionyesha ulegevu katika fainali ilipopiga mipira mibovu ilipopata nafasi ya kuanzisha ama kupokea visivyo na pia ulinzi wake ulikuwa ukivuja, hasa kuzuia makombora ya Cameroon.

Makosa haya yalishuhudiwa upande wa Kenya karibu katika mechi zote. Mabingwa wa Afrika mara tisa Kenya walianza mchuano huo vibaya walipolemewa kwa seti ya kwanza 25-17. Walipigana kufa-kupona na kusawazisha seti 1-1 waliposhinda seti ya pili 27-25. Hata hivyo, walijipata pabaya tena katika seti ya tatu 25-23.

Wakenya walisawazisha tena 2-2 baada ya kunyakua seti ya nne 25-23, lakini wakazidiwa maarifa katika seti ya mwisho ambayo mara mbili waliongoza 3-1 na 14-13 kabla ya kuachilia uongozi huo na kupoteza.

Ushindi katika kundi

Kabla ya kichapo hiki, Kenya ilikuwa imeshinda mechi zake zote za makundi dhidi ya Algeria 3-0, Botswana 3-0 na Cameroon 3-2 na kupepeta Senegal 3-0 katika nusu-fainali.

Nayo Cameroon ilikuwa imepoteza dhidi ya Kenya pekee na kulaza Botswana na Algeria 3-0 katika mechi za makundi na wenyeji Misri 3-0 katika nusu-fainali.

Ajabu ni kuwa licha ya makosa hayo, Kenya, ambayo inashikilia rekodi ya mataji mengi ya kombe hili baada ya kushinda kutoka mwaka 1991-1997, 2005-2006 na 2011-2015, ilipokea tuzo ya mwanzisha bora wa mipira Mercy Moim na mlinzi bora Agrippina Kundu.

Senegal iliridhika na nishani ya shaba baada ya kulemea mabingwa mara tatu Misri 3-1 (25-17, 25-17, 14-25, 28-26).

Nayo Algeria ilikamilisha kampeni yake katika nafasi ya tano baada ya kucharaza Morocco 3-0 (25-23, 25-14, 25-20) katika mechi ya kuamua nambari tano na sita. Botswana ilivuta mkia baada ya kulemewa na Morocco 3-2 (23-25, 25-23, 25-16, 24-26, 16-14).

Aidha, baada ya kuwasili kutoka Misri, Malkia Strikers inatarajiwa kupumzika siku chache kabla ya kurejelea mazoezi ya michezo ya African Games itakayoanza jijini Rabat nchini Morocco mnamo Agosti 19. Kenya ni mabingwa watetezi. Ilibwaga Cameroon 3-1 katika fainali ya makala yaliyopita jijini Brazzaville nchini Congo mwaka 2015.

You can share this post!

Ni mwenye nguvu nipishe The Eagles wakiwania 3-bora

Wanachama wa Urithi Housing Cooperative washauriwa wawe...

adminleo