• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Vyama 38 vipya mbioni kusajiliwa kupigania mabilioni kutoka kwa Hazina ya Vyama vya Kisiasa

Vyama 38 vipya mbioni kusajiliwa kupigania mabilioni kutoka kwa Hazina ya Vyama vya Kisiasa

NA MOSES NYAMORI

ONGEZEKO la usajili wa vyama vipya vya kisiasa kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2027, limeonyesha jinsi mabilioni ya pesa zinazotolewa na serikali kufadhili vyama hivyo ulivyofanya uendeshaji wake kuwa kama biashara yenye faida kubwa.

Juhudi za kusajili vyama hivyo vipya pia zimeonyesha wasiwasi mkubwa unaohusishwa na shughuli za uteuzi katika vyama vikubwa vya kisiasa, ambapo wakati mwingine wawaniaji hudanganywa na hatimaye kunyimwa tiketi ya chama.
Hilo linajiri pia wakati ambapo Rais William Ruto anaendeleza juhudi za kuvunja vyama tanzu 13 katika mrengo wa Kenya Kwanza, ili kujiunga na chama chake tawala cha United Democratic Alliance (UDA).
Kulingana na stakabadhi zilizotolewa na Afisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa (ORPP), jumla ya vyama vipya 38 vimetuma maombi ya kusajiliwa.
Hili limetajwa kuchangiwa na ripoti kuhusu vile vyama vya kisiasa vimekuwa vikipokea mabilioni ya pesa kutoka kwa Hazina ya Vyama vya Kisiasa (PPF) kwa miaka 10 iliyopita.
Tayari, vyama vingine 23 vishapata vibali vya usajili wa muda. Vyama hivyo ni kando na vyama 90 vilivyosajiliwa nchini kwa sasa. Hilo linamaanisha kuwa kufikia 2027, huenda kukawa na jumla ya vyama 151 vya kisiasa nchini.
Vyama hivyo vipya 38, ambapo majina yao yameidhinishwa na Msajili wa Vyama vya Kisiasa, Bi Anne Nderitu, vinajumuisha Solidarity Africa Alliance (SAA), Independent Patriots for Change (IPC), Taifa Democratic Coalition (TDC), Kenya Ahadi Party (KAP), Centrists for Economic and Social Reforms Party (CESRP), Liberal Economic Affirmative Party (LEAP) na Inclusive Party (TIP TIP).
Vyama vingine ni National Harmony Party of Kenya (NHPK), Economic Liberation Alliance Party (ELAP), National Transformation Party (NTP), Ustawi Party of Kenya (UPK), Hope Party of Kenya (HPK), Justice Direction Party (JDP), Imarisha Uchumi Party (IUP) na Social Democratic Party of Kenya (SDP).
Stakabadhi hizo zimeonyesha jinsi vyama vinavyoongozwa na Rais Ruto, Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa Azimio la Umoja, Bw Raila Odinga, vimekuwa vikipata kiwango kikubwa cha fedha kutoka hazina hiyo kwa miaka kumi iliyopita.
Hata hivyo, mbunge wa zamani, Hassan Osman, ameenda mahakamani kumshinikiza Mkaguzi Mkuu wa Fedha za Serikali, Bi Nancy Gathungu, kutoa maelezo ya kina kuonyesha jinsi vyama vya kisiasa vimekuwa vikipokea fedha kutoka kwa hazina hiyo kwa muda wa miaka 10 iliyopita.
Uamuzi wa Bw Osman kwenda mahakamani unajiri baada ya Afisi ya Mkaguzi Mkuu wa Fedha za Serikali kukosa kutoa maelezo kuhusu jinsi vyama hivyo vimekuwa vikitumia fedha ambazo vimekuwa vikipokea kutoka kwa serikali.
Kwenye fedha zilizotolewa na hazina hiyo mwaka huu, chama cha UDA chake Rais Ruto kilipata Sh577 milioni huku kikifuatwa na ODM, chake Bw Odinga, kilichopata jumla ya Sh308 milioni. Vyama 48 vilipokea fedha kutoka kwa hazina hiyo.

  • Tags

You can share this post!

Jamii ya Wanandi yaitaka Uingereza kuilipa fidia ya Sh20...

Dalili Gachagua sasa anajipanga kulinda nafasi yake katika...

T L