• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:33 AM
Wadukuzi wageuza Kenya mlo wao CA ikijitahidi kuziba mianya

Wadukuzi wageuza Kenya mlo wao CA ikijitahidi kuziba mianya

NA FARHIYA HUSSEIN

MAMLAKA ya Mawasiliano Nchini (CA) imesisitiza haja ya kuwawezesha na kuwapa ujuzi zaidi wataalam katika masuala ya mtandao, ikibainisha hitaji muhimu la kuwalinda watumiaji milioni 11 wa mitandao ya kijamii nchini dhidi ya mashambulio.

CA imeeleza kuwa idadi ya mashambulio ya mtandaoni imeongezeka hadi milioni 860 kutoka milioni 7.7 katika miaka mitano, na kuiweka Kenya pamoja na Afrika Kusini na Nigeria miongoni mwa mataifa matatu ya kwanza yanayolengwa zaidi barani Afrika.

Akizungumza mjini Mombasa, Naibu Mkurugenzi wa CA anayehusika na masuala ya Usalama wa Mtandao na Majukwaa ya Biashara Mtandaoni Dkt Vincent Ngundi, alisema kuwa mfumo wao wa kudhibiti uhalifu wa mtandaoni, unatoa wito kwa maajenti zaidi kushiriki, na kurahisisha kuwashtaki wahalifu wa mtandaoni.

“Lengo letu ni kuhakikisha Teknohama nchini inapiga hatua na tuweze kukabiliana na mashambulio mtandaoni yanayoongezeka kwa kasi, na yakiwa ya kisasa zaidi kumaanisha tunafaa kujiimarisha,” alisema Dkt Ngundi.

Mamlaka hiyo imeanzisha mradi wa Cybersecurity Bootcamp na Hackathon ili kuwahusisha vijana katika harakati na miradi ya kubadilisha taifa kidijitali.

Mashindano haya tayari yamefanyika katika kaunti za Nyeri, Kisumu, Eldoret, na Mombasa, ambapo vijana wenye uelewa wa masuala ya kiteknolojia kutoka taasisi mbalimbali za elimu ya juu wamepata mafunzo.

Ni sehemu ya mfululizo wa shughuli ambazo kilele chake kitakuwa Oktoba 2023 kuangazia Uelewa wa Usalama Mtandaoni yaani October Cyber Security Awareness Month (OCSAM).

“Mradi wa hackathon unalenga kujenga kizazi kipya cha wataalamu wa usalama mtandaoni, ambao watachukua jukumu muhimu katika kulinda mtandao wa nchi. Nikiri kwamba haikuwa rahisi hasa kwa wanafunzi wanaoshiriki zoezi hili, na kufika hapa kwao ni mafanikio yanayostahili kusherehekewa,” alisema Dkt Ngundi.

Kati ya 6,000, wanafunzi 566 kutoka Pwani walituma maombi kushiriki kwenye zoezi la Boot Camp na 332 kwenye hackathon. Kati ya hawa, 40 walishiriki katika zoezi la Boot Camp wiki hii huku 70 wakishiriki katika hackathon.

Boot Camp ni programu yenye ushindani wa hali ya juu ya kujifunza maswala mengi mtandaoni. Kwa kawaida Boot Camp hulenga kutoa ujuzi na maarifa ya kimsingi kuhusu usalama mtandaoni kwa wanafunzi wanaoendelea na elimu katika vyuo, vyuo vikuu na vyuo vya kiufundi.

Maeneo yanayoangaziwa yanatokana na mapengo yaliyotambuliwa na Mamlaka, kupitia KE-CIRT/CC ya Kitaifa kutokana na ripoti za vitisho vya mtandaoni vinavyoshuhudiwa mara kwa mara.

Hackathon imewaona wanafunzi wakishindana katika mfululizo wa changamoto za usalama mtandaoni zilizoratibiwa na kuchukua umbo la mchezo, kuruhusu wanafunzi kushiriki katika mitandao na kujifunza kutoka kwa kila mmoja, huku pia ikiwaangazia kwa ushauri na fursa za maendeleo ya kazi.

Dkt Ngundi alisema mafunzo hayo ni sehemu ya Kenya kuweka huduma zote za umma kwenye safu ya kidijitali, jambo ambalo huwaweka raia wake katika vitisho zaidi vya mashambulio mtandaoni na udukuzi.

“Kuna juhudi nyingi zinazoendelea na ni lazima ziendelee kuwekwa ili kuhakikisha huduma za umma mtandaoni zinabaki kuwa salama lakini pia idadi inayolingana ya watu na uwezo wa kuweza kulinda mali hizo za kidijitali katika huduma za umma inaafikiwa,” alisema Dkt Ngundi.

Mwanzilishi wa SwahiliPot Hub, Bw Mahmoud Noor alibainisha kuwa ilikuwa muhimu kuhusisha vijana.

“Inamaanisha kuwa vita dhidi ya mashambulio mtandaoni vitazaa matunda. Vijana ambao wamepitia mafunzo sasa watakuwa sehemu ya vita muhimu katika kukomesha mashambulio ya mtandaoni kote nchini,” alisema Bw Noor.

  • Tags

You can share this post!

Wakili azima ‘injili’ ya mambo matatu ya kufufua...

Joto la atakayevalia viatu vya Raila lashamiri

T L