• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 6:27 PM
Wakongwe 200 wapokea matibabu na chakula eneo la Mavoloni

Wakongwe 200 wapokea matibabu na chakula eneo la Mavoloni

Na LAWRENCE ONGARO

WAGONJWA wakongwe wapatao 200 katika eneo la Mavoloni, Ndalani, kaunti ya Machakos mnamo Jumatatu walipokea matibabu ya bure kutoka kwa madaktari wa Thika Nursing Home.

Madaktari wawili waliongozwa na Dkt Vashti Shah kutoa matibabu ya bure, na kufanya juhudi kuona ya kwamba wakongwe hao wanapokea matibabu maalum baada ya kukosa huduma hiyo kwa muda mrefu.

Dkt Shah alisema wengi wa wakongwe hao pia walihitaji lishe bora ambapo walipokea unga, maharage na mafuta ya kupikia.

Alisema baada ya kuwapima, aligundua baadhi walipatikana na kisukari, shinikizo la damu, uchungu wa mifupa, matatizo ya macho, na matatizo ya moyo.

Alisema baada ya kutoa matibabu hayo, ataendelea kufuatilia magonjwa hayo.

“Wagonjwa hao wanastahili kufuatiliwa kila mara ili kukabiliana vilivyo na maradhi tofauti,” alifafanua Dkt Shah.

Alisema wakongwe wengi wanapitia changamoto tele kama kutembea kilomita kumi kutafuta matibabu.

“Sisi kama madaktari tunawahimiza wakongwe hao wazingatie kula chakula kilicho na afya,” alieleza Dkt Shah.

Bw Francis Kilango aliye mkazi wa kijiji hicho cha Mavoloni, alisema wakongwe wengi wanatembea mwendo mrefu ili kupata matibabu na hata wengine hawana pesa za matibabu.

“Hata wengi wao wakienda katika hospitali ya Machakos Level 5 huwa hawapati dawa na wanalazimika kurejea nyumbani bila dawa,” alifafanua Bw Kilango.

Alieleza pia kuwa hali ngumu ya maisha imesababisha hali yao ya kiafya kudhoofika.

Alisema kuwa wakongwe wengi wanaishi na upweke bila hata kupata chakula.

Naye mkazi mwingine wa kijiji hicho Bw Kennedy Muiruri aliye mhudumu wa bodaboda alisema wakongwe wengi hushindwa kusafiri mwendo mrefu kutokana na ukosefu wa pesa za usafiri.

“Hata wengi wao waliofikia umri wa miaka 70 hukosa kupokea fedha za wazee kutoka kwa serikali. Na hata wengi pia hawazuru hospitali kwa kukosa mtu wa kuwapeleka kupata matibabu. Wengine wanaishi peke yao katika boma zao,” alifafanua Bw Muiruri.

Alisema viongozi wengi wameshindwa kutekeleza wajibu wao wa kusaidia wananchi,” alieleza Muiruri.

  • Tags

You can share this post!

Nitaongoza Wakenya kupata uhuru wa kiuchumi – Raila

Anne Muratha apewa darasa baada ya kurushia watu keki

T L