• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 6:50 AM
Wanasiasa Kisii wanaopepeta moto wa fujo kuona cha mtema kuni  

Wanasiasa Kisii wanaopepeta moto wa fujo kuona cha mtema kuni  

NA WYCLIFFE NYABERI 

KAMISHINA wa Kisii Tom Anjere amewaonya viongozi wa eneo hilo dhidi ya kulifanyia mzaha suala la usalama wa wakazi.

Bw Anjere ameonyesha kusikitishwa kwake na baadhi ya wanasiasa aliodai hawashirikiani na walinda usalama kutokomeza visa vya uhalifu Kisii, lakini hawachelewi kuwakosoa polisi kwa kudai wanazembea kazini.

Akizungumza katika eneo la Mosocho wakati wa sherehe za Jamhuri Dei 2023 mnamo Desemba 12, kamishina huyo alilalamikia hatua ya wanasiasa kuwajia juu maafisa wa polisi na kamati za usalama kwenye majukwaa ya hafla za serikali.

“Hatuwezi kulaumiana kila mara kwenye majukwaa kama haya. Tumefanya mikutano mingi kuhusu usalama na wanasiasa ambao wanalaumu polisi kuhusu usalama hawaji kutoa taarifa hizo muhimu. Usalama si suala la kufanyia mzaha na wacha sekta hiyo iachiwe walinda usalama,” Bw Anjere alidokeza.

Katika sherehe hizo za Mosocho, Gavana Simba Arati na baadhi ya wawakilishi wa wadi (MCAs) walilalamikia utovu wa usalama ulikuwa umekithiri Kisii kutokana na mauaji ya kiholela.

Gavana alilalama kuwa baadhi ya wafuasi wake walikuwa wakiandamwa na kudhulumiwa kwa kumunga mkono.

Huku Rais William Ruto akitarajiwa kuzuru Kisii wikendi hii, mbunge huyo wa zamani wa Dagoretti Kaskazini alidokeza kwamba kuna baadhi ya watu waliokuwa wakipanga kuharibu mkutano huo kwa kuzua vurumai.

Dkt Ruto atazuru Kisii Jumamosi ijayo na gavana amezitaka asasi zote za usalama kuzima njama hiyo isiletee jamii aibu.

Rais anatarajiwa kuhudhuria hafla ya kanisa Katoliki eneo hilo hilo la Mosocho.

Bw Anjere alionyesha nia ya kuketi na viongozi wa Kisii waliochaguliwa pamoja na walinda usalama ili kujadili namna ya kuimarisha maendeleo ya gatuzi hilo.

 

  • Tags

You can share this post!

Wafanyabiashara wa ‘mahaba’ Kikopey walalamikia ukosefu...

Matamshi ya Gavana Kahiga kuhusu nguvu za umeme huenda...

T L