• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 12:48 PM
Waruguru aponda wawaniaji UDA

Waruguru aponda wawaniaji UDA

Na JAMES MURIMI

MBUNGE Mwakilishi wa Kike wa Kaunti ya Laikipia Catherine Waruguru sasa anadai kuwa wanasiasa walioshinda mchujo wa UDA katika kaunti hiyo hawawezi kumvumisha Naibu Rais Dkt William Ruto ili azoe kura nyingi za eneo hilo.

Bi Waruguru amewataka wakazi wa kaunti hiyo wasiwachague wawaniaji wa UDA katika nyadhifa nyingine ila ile ya Urais ambayo Dkt Ruto atakuwa akiwania kupitia tikiti ya chama hicho.

Mwanasiasa huyo alishindwa katika uteuzi wa UDA kuwania kiti cha ubunge cha Laikipia Mashariki na ameibuka miongoni mwa wanasiasa wanaopinga raia kutakiwa kupiga kura kwa wawaniaji wa chama kimoja kwenye vyeo vyote sita vinavyowaniwa maarufu kama ‘suti’.

Mbunge huyo alidai kuwa wale ambao walishinda uteuzi wa UDA katika nyadhifa za Useneta, Ugavana, Mwakilishi wa Kike, Ubunge na Udiwani, hawajakuwa wakiendesha kampeni za kumvumisha Dkt Ruto wala hawajawahi kumwalika ili ashiriki kongamano la kiuchumi jinsi anavyofanya katika maeneo mengine.

“Namweleza waziwazi kiongozi wa chama changu kuwa wanasiasa walioshinda viti vya uteuzi hapa Laikipia hawamakinikii kampeni zake. Nawaomba raia wa Laikipia watathmini utendakazi wa kiongozi hapa chini kisha kura za Urais ndizo wampe Dkt Ruto,” akasema Bi Waruguru mjini Nanyuki Jumanne jioni.

Alisema kuwa kinyume na viongozi wa UDA, mrengo pinzani wa Azimio la Umoja nao umekuwa ukiendeleza kampeni zake katika kaunti hiyo kupitia Gavana Ndiritu Muriithi.

“Iwapo Ruto atakuwa akitegemea viongozi wa UDA hapa mashinani kumtafutia kura basi atalemewa na Azimio la Umoja hapa Laikipia. Wapinzani wetu wameungana ilhali walioshinda uteuzi wa UDA wamejawa na kiburi wakisema wanasubiri kuapishwa tu,” akaongeza.

“Ningependa kuwaeleza wenzangu chamani kuwa kutwaa tikiti ya UDA hakumaanishi kuwa umechaguliwa. Walitwaa tikiti na wakaanza kulaza damu lakini mara hii mambo yatakuwa tofauti,” akasema.

Kauli yake inakuja wakati ambapo kiongozi wa TSP Mwangi Kiunjuri alisema kuwa chama hicho kitaendesha kampeni za kuhakikisha kinashinda viti vingi Laikipia kuliko wenzao wa UDA.

Akizungumza baada ya kukutana na wawaniaji wa TSP, Bw Kiunjuri alisema kuwa vyama tanzu ndani ya Kenya Kwanza vinafaa kukubali kushindana kwa sababu hiyo ndio njia ya kukuza demokrasia na kuwapa wananchi nafasi ya kuchagua kiongozi wanayempenda.

  • Tags

You can share this post!

Bingwa Chebet abeba tuzo ya Mchezaji Bora

JKF yatenga Sh22.2 milioni kwa wanafunzi kutoka familia za...

T L