• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 6:55 AM
Wavuvi 200 walifariki kabla ya kuonja fidia ya Lapsset – Ripoti

Wavuvi 200 walifariki kabla ya kuonja fidia ya Lapsset – Ripoti

NA KALUME KAZUNGU

ZAIDI ya wavuvi 200 wa Lamu waliokuwa miongoni mwa 4,734 waliofaa kulipwa fidia ya Sh1.76 bilioni kufuatia athari za ujenzi wa Bandari ya Lamu (LAPSSET) wamefariki katika kipindi cha miaka sita iliyopita.

Haya ni kulingana na ripoti kutoka kwa ofisi kuu ya Miungano ya Wavuvi (BMU) kaunti ya Lamu.

Katika mahojiano na Taifa Leo Alhamisi, Mwenyekiti wa miungano hiyo, Mohamed Somo anasema 200 hao waliaga dunia kati ya mwaka 2018 na 2023.

Lamu ina jumla ya BMU 37.

Kulingana na Bw Somo, baadhi ya waliofariki walikuwa tayari wametia sahihi za makubaliano ya kupokea fidia ilhali wengine wakiwa kwenye harakati za kumaliziwa utambulishi wao ili kuwa miongoni mwa waliostahili kufidiwa mgao wa Sh1.76 bilioni.

Mnamo 2018, Mahakama Kuu mjini Malindi ilipasisha jumla ya wavuvi hao 4,734 waliofaa kufidiwa na serikali kuu baada ya uchimbaji wa viegesho vitatu vya mizigo katika bandari ya Lamu kuharibu sehemu za asili za wavuvi hao kutekelezea shughuli zao.

Bw Somo alieleza kusikitishwa kwake na jinsi shughuli ya kuwafidia imekuwa ikitekelezwa kwa njia ya mwendo wa kobe ilhali wanaofaa kunufaika wakiendelea kuaga dunia kila kukicha bila kuonja fedha walizosubiri kwa muda mrefu.

Mnamo Aprili mwaka huu, shughuli iliyokuwa ikiendelezwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari nchini (KPA) ya kuwatambua wavuvi na kutwaa sahihi zao kwa minajili ya kulipwa fedha hizo ilisitishwa na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) kwa madai ya kuwepo kwa ufisadi uliozingira utayarishaji wa orodha ya majina ya waliofaa kulipwa.

Bw Somo anasema tangu kusimamishwa kwa zoezi hilo Aprili mwaka huu, wavuvi wameachwa gizani kwani hakuna lolote walilojulishwa kufikia sasa.

Aliiomba EACC kuharakisha uchunguzi wake na kutoa ripoti ili kupisha shughuli ya kuwafidia wavuvi kuendelezwa.

“Inasikitisha kuona wanachama na wavuvi wenzangu wakifariki kabla ya kulipwa fedha zao. Katika rekodi zetu, tuko na zaidi ya majina 200 ya wavuvi waliofariki na ambao walifaa kufidiwa na Lapsset. Walifariki kati ya 2018 na 2023. Tungeomba serikali, EACC, KPA na wengineo kutujali na kuharakisha uchunguzi na ukaguzi ili tulipwe. Si vyema kuachwa wengine wakifariki bila kupokea haki yao ya fidia ambayo tumesubiri kwa muda mrefu,” akasema Bw Somo.

Kwenye mfumo wa fidia hiyo ya Sh1.76 bilioni, wavuvi wa Lamu walipasishwa kulipwa pesa taslimu za asilimia 65 ilhali asilimia 35 iliyobakia ikipasishwa katika ununuzi wa vyombo vya kuvulia samaki na kuboresha miundomsingi mingine muhimu kwenye sekta ya uvuvi kote Lamu.

Abdallah Hassan, mvuvi wa kisiwa cha Lamu, alisema ipo haja ya asilimia 35 kupatiwa kipaumbele na kutolewa haraka wakati wavuvi wakisubiri fidia ya pesa taslimu ambayo ni asilimia 65.

“Matatizo yalikumba asilimia 65 ya fidia kwa wavuvi 4,734. Huku wakiendelea kuchunguza na kuibuka na orodha sahihi ya wavuvi watakaofidiwa, tunapendekeza ile asilimia 35 ya ununuzi wa vifaa na miundomsingi ya kuboresha uvuvi wetu Lamu itolewe mara moja ili tujiendeleze,” akasema Bw Hassan.

Mradi wa ujenzi wa viegesho vitatu vya Bandari ya Lamu ulitekelezwa eneo la Kililana, Lamu Magharibi na kugharimu serikali kuu kima cha Sh310 bilioni.

Viegesho hivyo vitatu vilikamilika na kufunguliwa rasmi Mei 20, 2021, siku iliyoshuhudia meli ya kwanza ya mizigo kwa jina MV CAP Carmel kutoka nchini Singapore ikitia nanga bandarini Lamu kuashiria mwanzo kamili wa shughuli za biashara na uchukuzi wa melini eneo hilo.

 

 

  • Tags

You can share this post!

Ndoa mashakani EACC ikitwaa pesa za mahari

Amerika yakataa nguo kutoka Kenya biashara ya mitumba nayo...

T L