• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 1:15 PM
Washukiwa saba wa wizi wa simu za rununu wanaswa Thika

Washukiwa saba wa wizi wa simu za rununu wanaswa Thika

Na LAWRENCE ONGARO

POLISI mjini Thika mnamo Ijumaa waliwanasa watu saba ambao inadaiwa wamekuwa wakiiba simu za wakazi.

Kamanda mkuu wa polisi katika Kaunti ya Kiambu Bw Ali Nuno, alieleza kuwa kwa muda wa miezi miwili mfululizo washukiwa hao wamewahangaisha wakazi wa Thika kwa kuwaibia simu zao.

Alisema washukiwa hao walifikishwa mahakamani lakini mmoja wao pekee ndiye aliachiliwa kwa dhamana ya laki mbili.

Akizungumza na wanahabari katika kitua cha polisi cha Thika, kamanda huyo wa polisi alisema wamiliki watatu wa simu hizo zilizoibwa walifika katika kituo cha polisi cha Thika na kutambua simu zao zilizoibwa hivi majuzi.

Aliwataja washukiwa hao kama hatari kwa usalama kwa sababu walikuwa wakitumia gari na pikipiki wanapotekeleza uhalifu huo.

Alisema uchunguzi wao unaonyesha wanatekeleza wizi huo asubuhi wananchi wakielekea kazini na jioni wanapotoka katika sehemu zao za kazi.

“Washukiwa hao baada ya kuiba simu wakiwa kwenye pikipiki, hurusha ndani ya gari simu hizo halafu linatoka kwa kasi huku nao wakilifuata kwa nyuma,” alifafanua kamanda huyo wa polisi.

Aliitaka mahakama kufanya juhudi kuona ya kwamba washukiwa hao wanapewa adhabu kali endapo watapatikana na hatia ili iwe funzo kwa wengine.

Alieleza kuwa maafisa wa kitengo maalum cha polisi wataendelea kushika doria kwa muda wa saa 24 ili kukabiliana na wahalifu.

Afisa huyo alisema changamoto kubwa wanazopitia kama walinda usalama ni kwamba hata wakipelekwa mahakamani, washukiwa wanaopatikana na makosa hupigwa faini nyepesi na baadaye wanarejelea wizi huo.

“Kwa hivyo tungetaka mahakama iwape adhabu kali ili wasije wakarejea katika tabia hiyo ya wizi,” alisema kamanda huyo wa polisi.

Bw Nuno alitoa wito kwa mtu yeyote aliyepoteza simu yake afike katika kituo cha polisi cha Thika ili aweze kukagua simu yake.

Aliwahimiza wananchi popote walipo washirikiane na maafisa wa usalama ili waweze kuwanasa wezi hao ambao wamekuwa kero kubwa kwa wakazi wa Thika.

Alieleza kuwa tayari wameweka mikakati ili kukabiliana na wezi hao ambao wameonyesha utovu wa nidhamu kwa wananchi.

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Wanasiasa waache kuhadaa kwa spoti

MUTUA: Serikali ya Ethiopia iko hatarini kupinduliwa

T L