• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 3:03 PM
ZARAA: Afichua siri ya jinsi alivyofaulu katika kilimo cha magimbi ‘nduma’

ZARAA: Afichua siri ya jinsi alivyofaulu katika kilimo cha magimbi ‘nduma’

NA WYCLIFFE NYABERI

WAKAZI wengi katika kaunti ya Kisii, aghalabu hutenga sehemu ya chini ya mashamba yao iliyo karibu na mito au chemichemi za maji kwa upanzi wa miti aina ya Eucalyptus.

Baada ya kilimo cha majani chai kuonekana kudorora nchini, wakulima wengi Gusii walikimbilia upanzi wa miti hiyo lakini kwa James Nyagwoka,63, miti haikumpita akilini hata kidogo kama kimbilio ambalo lingemwokoa.

Badala yake, aliamua kujitosa katika ukulima wa nduma kijijini kwao Kegati, eneobunge la Nyaribari Chache.

Ni ukulima ambao ameufanya kwa zaidi ya miaka 20 baada ya kukosa kufaulu maishani alipokuwa akifanya vibarua.

Lakini sasa, mzee Nyagwoka ni mojawapo ya wakulima tajika wa nduma katika Kaunti ya Kisii iwapo si nchini.

Ukumbi wa Akilimali ulimtembelea mkulima huyo shambani kwake kueleza mengi kuhusu zaraa yake iliyomwezesha kusomesha watoto wake watano hadi vyuo vikuu, shule za sekondari na kujijengea nyumba ya kisasa anakoishi na mkewe.

“Nilianza ukulima wa nduma kama mchezo tu na miche 200. Miche hiyo ilikuwa imemea karibu na mto katika shamba hili nililoachiwa na baba yangu. Ni kutokana na miche hiyo 200 ambapo nimezalisha na kuendelea hadi kufikia sasa nina mimea ya nduma inayopita 100, 000,” Nyagwoka anafafanuaWakazi wengi hufikri nduma hupandwa tu kwa maeneo yaliyo na unyevunyevu lakini mkulima huyo anatuambiwa kuwa sivyo.

James Nyagwoka, akionyesha baadhi ya magimbi yaani nduma zilizovunwa shambani mwake katika kijiji cha Kegati, eneobunge la Nyaribari Chache, kaunti ya Kisii. PICHA | WYCLIFFE NYABERI

Japo nduma huhitaji kiasi cha haja cha maji, Nyagwoka anasema nduma zinaweza kupandwa katika mchango wowote mzuri bora uwe mzuri na rotuba nzuri na usiwe na mawe.

Anaeleza kuwa kabla mkulima yeyote aanze kilimo chochote, ni vyema kuwatembelea wakulima waliokubuhu kwa kilimo anachokitaka ili ajifunze mawili-matatu ya kutekeleza atakaporudi shambani kwake.

Hata hivyo, kilimo hiki hakijakosa changamoto baadhi ikiwa watu kumuibia nduma zake lakini anasema hilo halijamwathiri pakubwa kwani nduma zinazosalia zina uwezo wa kumletea faida.

Aina ya nduma alizozipanda Nyagwoka shambani kwake ni ile ya majani mabichi yaliyokolea kabisa. Kuna aina nyingine ya nduma zenye majani ya zambarau lakini mkulima huyo anadokeza zile za majani mabichi yaliyokolea zinampeleka vizuri.

Alitueleza kuwa laini moja ya mita 50 yenye nduma zilizokomaa humwekea kibindoni Sh 15, 000.

Kwa mwaka mmoja, Nyagwoka alisema hutengeneza zaidi ya Sh600, 000 kutokana na uuzaji wa nduma alizozipanda katika shamba lake la ekari sita.

Wateja wake wengi wapo katika mji wa Kisii. Wao hununua kutoka shambani mwake gunia dogo lililojaa nduma kwa Sh 3,000.

“Sasa nina wateja kutoka majiji ya Nairobi na Nakuru. Wao hununua hapa shambani na kujibebea wenyewe. Sigharamiki hata kidogo kuwasafirishia hadi barabarani,” anasema.

Ili kuhakikisha wateja wake hawakosi nduma kila mara, Nyagwoka ameligawanya shamba lake kusitiri mimea iliyoshindana wakati wa kupandwa.

Kuna mimea ya nduma iliyomaliza miezi miwili, mingine nne na kuendelea. Hili anasema linamsaidia pakubwa kuvuna kwa wakati tofauti ili wateja wake wasisumbuke.

Wakulima wengine kijijini kwao wameanza polepole kukuza nduma na mkulima huyo amejitolea kuwapa mafunzo ya bure ili nao wafaidi maishani.

Yeye pia huhudhuria maonyesho ya kilimo ili kujifunza mengi kuhusu kilimo.

“Laini nne za nduma zinaweza kunipa Sh60,000 kwa mwaka. Kati ya hizo pesa, ninaweza kutumia Sh40, 000 kununua mahindi nitakayoyala na familia yangu mwaka mzima. Kwa hivyo, kilimo hiki kina ukwasi,” anadokeza Nyagwoka.

Nduma zinaweza kutumiwa wakati wa kiamsha kinywa na zina kiwango kikubwa cha madini aina ya stachi.

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Kenya iige mfano wa Tanzania kuuza Kiswahili...

Shirika la Reli kuongeza safari za treni Kisumu

T L