Tahariri

TAHARIRI: Maandamano yametosha, vijana wajipange kwa 2027

Na MHARIRI MKUU July 1st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

HATA wanapopambania mabadiliko ya uongozi nchini, vijana wanastahili sasa kuelekeza juhudi zao katika kujipanga kwa 2027.

Mwezi uliopita ulikuwa mgumu kwa nchi kutokana na maandamano ya kusaka haki kwa familia ya bloga na mwalimu Albert Ojwang’.

Yalifuatiwa maandamano ya kuadhimisha mwaka moja tangu tukio la vijana kuvamia bunge mnamo Juni 25, 2024.

Maadhimisho hayo yalikuwa ya kuwakumbusha watu 60 ambao waliuawa kwenye maandamano ya mwaka jana.

Inasikitisha kuwa maadhimisho hayo yalichangia mauaji ya watu 16 kwa mujibu wa mashirika ya kijamii japo serikali imeweka idadi hiyo kuwa watu 10.

Kwa sasa mauaji haya yametosha na mivutano haifai kuendelea ila mwelekeo uafikiwe jinsi ya kuendesha nchi hadi 2027.

Mjadala wa kuondoa serikali mamlakani kupitia maandamano ya kila mara ambayo tayari yameingiliwa na wanasiasa hayafai na yatachangia tu vifo zaidi na uharibifu wa mali.

Mwanzo, maandamano haya yameonyesha serikali kuwa raia hawako tayari kuvumilia maovu na uongozi mbaya, kwa hivyo walio mamlakani lazima wabadili mtazamo wao.

Kwa vijana, huu ni wakati wa kuanza kuweka mikakati ili 2027 iwe rahisi kuhakikisha Kenya inapata utawala bora.

Shirika la Takwimu (KNBS) linakadiria kuwa kufikia mnamo 2027, vijana watakaokuwa wamefikisha umri wa kupiga kura ambao ni miaka 18 watakuwa wameongezeka.

Takwimu hizo zinaonyesha kuwa zaidi ya vijana milioni 14 ambao hawakushiriki uchaguzi wa 2022 kwa sababu miaka yao ilikuwa chini, watakuwa na umri wa miaka 18 mnamo 2027.

Nayo sajili ya wapigakura iliyotumiwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka Nchini (IEBC) 2022  ilionyesha kuwa wapigakura milioni 8.8 walikuwa kati ya umri wa miaka 18-34.

Hi ilikuwa asilimia 40 ya kura zote na walikuwa na uwezo wa kuamua mustakabali wa nchi kupitia uongozi bora lakini wengi wao hawakupiga kura.

Kwa ujumla kufikia 2027, vijana wote (Gen Z wakijumuishwa) ambao watakuwa na umri kati ya miaka 18 na 34 watakuwa zaidi ya milioni 17.8

Mnamo 2027 iwapo vijana hawatapiga kura, bado haitakuwa rahisi kupata mabadiliko nchini na malalamishi yatakuwa yale yale.

Mchakato wa kubuniwa kwa IEBC ukikamilika tu, vijana wawe mstari wa mbele kujisajili kama wapigakura na pia wajizuie kurejea kwenye miegemeo ya kikabila siasa zikichacha kabla ya uchaguzi.

Pia iwapo vijana wanaona mchakato wa kisheria wa kumngóa rais ni mgumu, wasisahau  kumakinikia mabadiliko ya kisheria.