TAHARIRI: Siri 5 kali kwa serikali inayolenga kufaulu uongozini
SERIKALI inayojali raia wake ni ile inayotanguliza ustawi, mahitaji, na matarajio ya wananchi katika kufanya maamuzi, kuunda sera na utoaji wa huduma.
Serikali ya namna hii huangazia kuwezesha jamii, kukuza ushiriki, na kuhakikisha kwamba huduma za umma zinapatikana, ni zile zinazofaa na pia ni zile ambazo zinalenga kukabili changamoto za maisha halisi za watu.
Pili, serikali yoyote yenye uwajibikaji inafaa kuzingatia kanuni kama vile ushirikishaji wa umma na ujumuishaji. Serikali inahitaji kuwashirikisha wananchi kikamilifu katika kuunda sera kupitia mashauriano, mijadala ya umma na michakato mingine ya kidemokrasia kama ilivyoainishwa katika Katiba na sheria za nchi.

Kufanya hivi kuna tija na nafuu ya kuepushia serikali malalamishi ya umma ambayo yanaweza kuepukwa. Aidha, ni kupitia mbinu hii ndipo itakuwa dhahiri kwamba walio mamlakani wamejitolea kushughulikia maslahi ya wananchi wala si matakwa yao binafsi kama viongozi. Serikali huundwa ili kuwashughulikia raia wala si kwa maslahi ya kuwatumikia mabwana.
Uwazi
Tatu, namna nyingine ya serikali kudhihirisha kwamba imejitolea kutumikia umma ni kupitia kwa uwajibikaji wa dhati pamoja na kuwepo kwa uwazi. Shughuli zote za serikali hazifai kuwa na ufiche wowote. Uwazi utasaidia kukabili visa vya ufisadi, mapendeleo na ukabila ambavyo nidonda sugu hasa katika taifa la Kenya. Hatua zote za serikali zinafaa kuwa wazi kuchunguzwa na maafisa wote wawe radhi kuwajibishwa kuhusiana na maamuzi yao.
Nne, sifa nyingine ya serikali stahiki ambayo imejitolea kuwahudumia raia wake kwa dhati ni kuhakikisha kwamba kuna usawa na haki. Serikali inafaa kushughulikia ukosefu wa usawa na kuhakikisha kwamba hakuna anayeachwa nyuma, hasa makundi yaliyotengwa au yaliyo hatarini. Aghalabu serikali nyingi duniani zimekuwa na mazoea ya kusahau kushughulikia maslahi ya makundi yaliyotengwa kama vile wanawake, vijana, walemavu na hata makabila fulani.
Kujali hisia za raia
Tano, serikali pia inafaa kutambua hisia na hali mbalimbali za raia wake. Kwa kufanya hivi itaanzisha huduma na sera kulingana na uelewa wa maisha wa watu, kwa kuzingatia kuboresha ubora wa maisha yao. Kwa mfano, iwapo serikali itajiweka katika hali wanayopitia wazazi ambao watoto wao walitekwa nyara, basi visa vya utekaji nyara vitakomeshwa haraka upesi na suluhu mbadala kutafutwa ili kuwaepushia wazazi hawa machungu wanayopitia kutokana na kukosa kuwa na watoto wao.
Nchi zinazokumbatia mtindo huu mara nyingi huwekeza katika mabadiliko ya kidijitali, uvumbuzi wa sekta ya umma, na kutanua mifumo yake ili kuboresha ushirikishwaji na kufanya huduma za umma ziwafae wananchi.