Tahariri

TAHARIRI: Uhuni huu wa kisiasa haufai kuvumiliwa tena

Na MHARIRI MKUU January 27th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

MATUKIO ya hivi karibuni ya uhuni, uvamizi na vitisho vya kisiasa yanapaswa kulaaniwa vikali na Wakenya wote wanaoamini katika utawala wa sheria, heshima ya haki za binadamu na demokrasia ya kweli.

Tukio lililoshuhudiwa Jumapili katika kanisa la ACK Witima, eneobunge la Othaya, Kaunti ya Nyeri, si jambo la kawaida bali ni doa katika historia ya kisiasa na kiusalama ya taifa letu.

Hafla ya ibada iliyohudhuriwa na aliyekuwa Naibu wa Rais, ambaye kwa sasa ni kiongozi wa upinzani, Bw Rigathi Gachagua, ilivamiwa kwa vurugu na watu waliotajwa kuwa maafisa wa polisi.

Ingawa serikali kupitia idara zake za usalama imekanusha kuhusika, ikiahidi kuchunguza tukio hilo, madai ya Bw Gachagua kwamba waliohusika ni maafisa wa polisi yanaendana na ripoti za kuaminika za vyombo vya habari kuwa kikosi cha polisi kilipanga uvamizi huo jijini Nairobi.

Hali hii inazua maswali mazito kuhusu uwazi, uaminifu na matumizi ya vyombo vya dola.

Taswira iliyojitokeza kanisani humo ilikuwa ya kusikitisha na ya kuogofya. Vitoza machozi vilirushwa ndani ya kanisa, mahali patakatifu palipokusudiwa kuleta faraja na matumaini, na kusababisha watoto na wazee kuathirika vibaya.

Baadhi ya ripoti zisizothibitika hata zimeeleza kuwa mtoto mmoja alipoteza maisha.

Magari ya rubaa ya Bw Gachagua yalivunjwa vioo, risasi zikafyatuliwa, na hofu kubwa kuzuka miongoni mwa waumini.

Haya yote yalitokea mbele ya macho ya raia wasio na hatia.

Cha kusikitisha zaidi ni kwamba hili si tukio la kwanza. Ni karibu mara ya tano kwa hafla za kanisani za Bw Gachagua kushambuliwa, ikiwemo Mwiki na Kariobangi.

Mfululizo huu wa matukio haufai tena kutajwa kama bahati mbaya. Unazua taswira ya kampeni ya makusudi ya kuogofya, kunyamazisha na kudhalilisha upinzani kwa kutumia mbinu za kikatili.

Hatari ya mwenendo huu inaongezeka maradufu ikizingatiwa kuwa Uchaguzi Mkuu wa 2027 unakaribia.

Historia ya Kenya inaonyesha wazi kuwa kipindi cha uchaguzi aghalabu huandamana na joto la kisiasa, migawanyiko na wakati mwingine, fujo za kisiasa.

Endapo vitisho, uvamizi na matumizi mabaya ya vyombo vya usalama yatakosa kudhibitiwa, basi taifa linajiandaa kwa mazingira hatari zaidi kadri uchaguzi unavyokaribia.

Hili ni bomu linaloweza kulipuka wakati wowote iwapo halitazimwa mapema. Kenya haifai kuruhusu kurejea kwa siasa za vitisho, uhuni na matumizi mabaya ya vyombo vya dola.

Ni wakati mwafaka wa vyombo vya usalama kuacha kutumika kama zana za kisiasa na badala yake vitimize wajibu wake kwa weledi na haki.

Uchunguzi wa kweli, wa haraka na huru ufanywe, wahusika wote wachukuliwe hatua kali za kisheria, na ujumbe wazi utolewe kwamba Kenya ni taifa linaloheshimu demokrasia, utu na amani.