Covid-19: Majaribio kufanikisha utoaji chanjo kwa watoto wa kuanzia umri wa miaka mitano

Na MARY WANGARI

WATOTO kuanzia umri wa miaka mitano huenda wakaanza kupatiwa chanjo dhidi ya Covid-19 iwapo matokeo ya utafiti uliofanywa na kampuni ya Pfizer yataidhinishwa.

Kampuni ya Pfizer vilevile inasubiri kwa hamu matokeo ya utafiti kuhusu chanjo hiyo uliofanyiwa watoto wachanga wenye umri wa hadi miezi sita, katika hatua ambayo huenda ikavutia hisia kali kutoka kwa jamii ya kimataifa.

Data kutoka kwa majaribio yaliyofanyiwa watoto wasiopungua 2,000 wenye umri kati ya miaka mitano na 11, iliashiria kinga imara ya mwili kutokana na kiwango cha chini cha chanjo hiyo bila athari zozote hasi, kulingana na utafiti huo uliochapishwa Jumatatu, Septemba 20.

Katika utafiti wake, Pfizer ilichunguza kiwango cha chembechembe za damu zinazopigana na ugonjwa huo ili kukadiria uwezo wake wa kutoa kinga ya mwili.

Utafiti huu ulitofautiana na ule wa awali ulioshirikisha watu wazima uliohusisha kulinganisha visa vya virusi vya corona miongoni mwa kundi moja na kundi la watu waliopokea chanjo hiyo.

Licha ya kuwepo kwa visa vya kutosha vya maambukizi miongoni mwa washiriki, Pfizer bado haijatangaza matokeo ya utafiti huo kuhusiana na ufaafu wa chanjo yake, kulingana na msemaji wa kampuni hiyo.

Iwapo itaidhinishwa na serikali ya Amerika ambayo kwa sasa inakagua chanjo hiyo, Pfizer itaweza kuanzisha mchakato wa kusambaza chanjo hiyo kwa watoto mwezi ujao Oktoba huku ikisubiri kibali kutoka kwa Uingereza na Uropa.

“Tuna furaha kujumuisha watoto katika ulinzi unaotolewa na chanjo punde tu tutakapopata kibali hasa tunapochunguza kusambaa kwa virusi aina ya Delta na tishio lake kwa watoto,”

“Visa vya Covid-19 miongoni mwa watoto Amerika vimeongezeka kwa karibu asilimia 240 tangu Julai na kuangazia haja ya utowaji chanjo,” alifafanua mkurugenzi wa Pfizer, Albert Bourla.

Haya yamejiri huku mjadala mkali ukitokota kuhusu kuwapa au kutowapa watoto chanjo ambapo Uingereza tayari imeanza mchakato wa kuwapa chanjo watoto wasio na virusi vya corona wenye umri wa kianzia miaka 12.

AFYA: Umuhimu wa mtu kula chakula kwa uwiano unaotakiwa

Na MARGARET MAINA

mwmaina@ke.nationmedia.com

ULAJI wa chakula unaofaa ni ule ambao mtu anahakikisha kwamba anakila chakula mchanganyiko, cha kutosha na chenye virutubisho vyote kwa uwiano unaotakiwa.

BNi muhimu mtu ale matunda angalau mara mbili kwa siku na ale mboga kwa wingi.

Ni muhimu kuhakikisha unatumia mafuta kwa kiasi kidogo. Mafuta ya nyama sio mazuri sana kwani yanahusishwa na magonjwa ya moyo. Badala yake inashauriwa mtu atumie zaidi mafuta yatokanayo na mimea.

Matumizi ya sukari na chumvi yawe ya kiasi. Pia kwa watu wanaokunywa pombe wasinywe kupita kiasi.

Kula chakula mchanganyiko

Chakula mchanganyiko hukuwezesha kupata virutubisho vyote vinavyohitajika mwilini. Kwa mfano vyakula vya wanga vinasaidia kuupa mwili nguvu na joto. Protini hutumika kujenga mwili navyo vitamini na madini hulinda mwili dhidi ya magonjwa. Kila siku jitahidi kula vyakula kutoka katika makundi yafuatatyo:

 • vyakula vya asili ya nafaka, ndizi za kupika na mizizi
 • vyakula vya jamii ya kunde, asili ya wanyama na mbegu za mafuta
 • mboga
 • matunda
 • sukari, asali na mafuta

Epuka mafuta mengi

Mafuta mengi mwilini hasa yale yenye asili ya wanyama yanaweza kusababisha ongezeko la magonjwa ya moyo na shinikizo kubwa la damu,. Hivyo inashauriwa kutumia zaidi mafuta yatokanayo na mimea.

Jinsi ya kupunguza mafuta

 • tumia mafuta kidogo wakati wa kupika
 • epuka kula vyakula vilivyokaangwa kwa mafuta na badala yake chemsha, oka au choma
 • punguza mafuta kwenye nyama iliyonona, na ikibidi ondoa ngozi ya kuku kabla ya kupika.
 • chagua nyama au samaki bila mafuta mengi.

Kula matunda na mbogamboga kwa wingi

Vyakula hivi huupatia mwili kinga dhidi ya magonjwa mbalimbali kama vile baadhi ya magonjwa ya moyo, saratani na kisukari.

Matunda ni chanzo cha virutubisho kama vile vitamini na madini ambayo hupatikana kwa wingi kwenye vyakula hivi kuliko kwenye vyakula vingine. Virutubisho hivi:

 • huifanya ngozi kung’aa na ionekane yenye afya pamoja na kusaidia vidonda kupona vizuri
 • huwezesha macho kuona vizuri
 • husaidia kuimarisha ufahamu
 • husaidia uyeyushaji wa vyakula tumboni na kufyonza madini ili yatumike mwilini
 • hutumika katika kutengeneza damu
 • husaidia katika uundaji wa chembe za uzazi

Virutubisho hivi havihifadhiki katika mwili wa binadamu hivyo ni vizuri matunda tofauti yajumlishwe kwenye mlo/milo ya siku.

Inashauriwa ifuatavyo kuhusu matunda na mbogamboga

 • pika mbogamboga kwa muda mfupi ili kupunguza upotevu wa vitamini na madini
 • tumia maji kidogo wakati wa kupika mbogamboga na hata maji yanayopikia mboga yaendelee kutumika sio kumwagwa

Vyakula vyenye nyuzinyuzi

Vyakula vyenye nyuzinyuzi (fibre) husaidia katika usagaji wa chakula tumboni na pia huweza kupunguza baadhi ya aina za saratani, magonjwa ya moyo na kisukari. Ili kuongeza nyuzinyuzi:

 • kula saladi na matunda mara kwa mara
 • kula tunda zima badala ya juisi
 • tumia unga usiokobolewa
 • kula vyakula vya jamii ya kunde mara kwa mara kwani vina nyuzinyuzi kwa wingi

Punguza chumvi

 • tumia chumvi kidogo wakati wa kupika
 • epuka vyakula vyenye chumvi nyingi
 • epuka uongezaji wa chumvi kwenye vyakula wakati kimeshawekwa kwenye sahani mezani

Punguza sukari

Sukari huongeza nishati mwilini, hivyo huchangia kuongezeka kwa uzito. Matumizi ya sukari huzalisha bakteria kinywani ambao husababisha meno kutoboka. Hivyo inashauriwa:

 • unywe vinywaji ambavyo havina sukari kama vile madafu na juisi za matunda badala ya soda zenye sukari
 • kama unatumia sukari, tumia kiasi kidogo
 • upunguze kula vitu vyenye sukari nyingi
 • na upunguza matumizi ya vyakula vilivyoongezwa sukari.

AFYA: Vidonda vya tumbo

Na MARGARET MAINA

mwmaina@ke.nationmedia.com

VIDONDA vya tumbo ni tatizo linalotokea baada ya kuta za tumbo au utumbo mdogo kuwa na vidonda.

Hali hii hutokea baada ya kuharibika kwa ukuta wenye ute unaozuia kemikali za kuyeyusha chakula.

Kemikali ambayo ni asidi inayozalishwa mwilini kiasili husaidia kuyeyusha chakula na kuua wadudu tumboni na kama ukuta wenye ute utaharibiwa na kushindwa kufanya kazi, basi hiyo kemikali (asidi) itaathiri tumbo au utumbo na kuruhusu bakteria kuendelea kusababisha vidonda vya tumbo.

Vidonda vya tumbo vinatibika kirahisi ila vikicheleweshwa bila kutibiwa huweza kusababisha tatizo kubwa.

Ni tatizo linalotesa sana na kuwanyima raha watu wengi. Pia husababisha magonjwa mengine kama kansa, amoeba (amiba), homa na kupungua uzani.

 • Vidonda vya tumbo kubwa (Gastric ulcers) – Hivi ni vidonda vya tumbo vinavyotokea ndani kwenye tumbo kubwa
 • Vidonda vya utumbo mdogo (Duodenal ulcers) – Hivi ni vidonda ambavyo hutokea kwenye utumbo mdogo (hasa juu)

Chanzo cha vidonda vya tumbo

Vidonda vya tumbo vina vyanzo tofauti ili vyote ni vile vinavyohusiana na mmeng’enyo. Vyanzo hivyo ni;

 • bakteria waitwao Helicobacter pylori (H. pylori)
 • matumizi ya dawa za kupunguza maumivu
 • kuwa na mawazo mengi
 • kula vyakula vinavyozalisha asidi kwa wingi
 • kunywa pombe na vinywaji vikali
 • uvutaji wa sigara
 • kukosa kula mlo kwa mpangilio

Dalili za vidonda vya tumbo

Dalili za vidonda vya tumbo hujitokeza baada ya kula au kabla ya kula, ila mara nyingi wengi huwa wanazipuuza na kuendelea kukuza tatizo. Vidonda vya tumbo vina dalili kama:

 • kupata maumivu ya tumbo yanayokuwa kama ya moto (kuunguza) baada na kabla ya kula
 • kusumbuliwa na kiungulia
 • tumbo kujaa gesi na kuvimbiwa
 • kichefuchefu na kutapika
 • kupoteza hamu ya kula na kupungua uzani
 • kushindwa kupumua vizuri

Cha kufanya ili kuepukana na vidonda vya tumbo

 • kunywa maji mengi
 • punguza mawazo, fanya mazoezi yatakuepushia mawazo
 • punguza kiwango cha halemu
 • usivute sigara
 • punguza au acha kunywa pombe
 • kula vizuri vyakula bora hasa asilia na sio vyakula vyenye kemikali
 • lala vizuri kwa muda mzuri, angalau saa 7 hadi 9

Maumivu yakizidi, pata ushauri wa daktari.

Gharama ya juu ya matibabu inavyobagua maskini

NA LEONARD ONYANGO

UGONJWA wa corona umejiongeza kwenye orodha ndefu ya maradhi hatari ambayo yamewalazimu Wakenya maskini kutumia mbinu mbadala kuokoa maisha yao baada ya kulemewa na gharama ya juu ya matibabu hospitalini.

Huku vyumba vya kulaza wagonjwa mahututi wa corona katika hospitali za umma vikiwa tayari vimejaa hadi pomoni kote nchini, ni pigo kwa maskini ambao hawamudu gharama ya juu ya matibabu katika hospitali za kibinafsi.

Hospitali za kibinafsi zinahitaji malipo ya awali ya hadi Sh600,000 kabla ya kukubali kulaza mgonjwa wa corona katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU).

Katika Hospitali ya Nairobi, kwa mfano, familia ya mgonjwa wa corona ni sharti ilipe Sh600,000 kwanza kabla ya jamaa yao kukubaliwa kulazwa katika kitanda cha ICU.Katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) familia ni sharti ilipe Sh200,000 kabla ya mgonjwa wa corona kuingizwa kwenye chumba cha ICU.

Familia nyingi zimekuwa zikizunguka kutoka hospitali moja hadi nyingine zikitafuta chumba cha kulaza jamaa wao wanaougua virusi vya corona.Japo vipimo vya corona vinafanywa bila malipo, haswa katika hospitali za kaunti, inagharimu hadi Sh20,000 katika baadhi ya hospitali za kibinafsi.

Katika Hospitali ya Nairobi West, kwa mfano, vipimo vya corona vinagharimu Sh6,000.Familia ya Julius Odhiambo, mnamo Machi, mwaka huu, ilisafirisha baba yao aliyekuwa na matatizo ya kupumua kutoka Kendu Bay, Kaunti ya Homa Bay, hadi jijini Nairobi ikiwa na matumaini kwamba ingepata matibabu ya haraka.

“Tulizunguka katika hospitali mbalimbali jijini Nairobi lakini tuliambiwa kulipa kati ya Sh200,000 na Sh400,000 kwanza kabla ya kulazwa. Sisi tulikuwa na Sh100,000 tu. Tulipiga simu kila mahali tukitafuta usaidizi.

“Hatimaye, nilipigia simu afisa mmoja wa wizara ya Afya, ambaye alitusaidia kupata kitanda katika Hospitali ya Mbagathi baada ya kuhangaika kwa siku tatu,” anasema Bw Odhiambo ambaye ni mwanahabari.

Hata hivyo, baba yake, Mzee James Odhiambo, aliaga dunia chini ya saa 24 baada ya kulazwa.Kwa kipindi cha mwezi mmoja sasa, wizara ya Afya imekuwa ikitangaza idadi ya juu ya vifo vilivyotokana na corona.

Kulingana na Mkurugenzi wa Matibabu nchini Dkt Patrick Amoth, idadi hiyo inajumuisha vifo vilivyotokea miezi ya nyuma lakini haikujumuishwa kwenye takwimu za wizara ya Afya.

“Kuna vifo vya waathiriwa wa corona vilivyotokea miezi iliyopita katika vituo vya afya au nyumbani ambavyo havikujumuishwa kwenye hesabu ya wizara ya Afya. Kwa sasa tunakagua rekodi za vituo vya afya na kutumia machifu kupata taarifa za vifo vya corona,” anasema Dkt Amoth.

Alhamisi iliyopita, kwa mfano, wizara ya Afya ilitangaza vifo 16 vya corona; idadi hiyo ilijumuisha kifo kimoja kilichotokea ndani ya saa 24, kimoja ndani ya mwezi mmoja na 14 vilivyotokea miezi mingi iliyopita.

Wataalamu wanasema kuwa takwimu hizo za wizara ya Afya ni ithibati kuwa idadi kubwa vya Wakenya wa mapato ya chini wamekuwa wakifariki kutokana na corona nyumbani kwa kushindwa kumudu gharama ya juu matibabu.

Wakili Donald Kipkorir hivi karibuni alielezea kuwa ametumia Sh4 milioni kupata huduma za matibabu alipoambukizwa na virusi vya corona.Wakili huyo aliezea namna alivyowekewa mitambo ya kumsaidia kupumua baada ya mapafu kulemewa.

Bw Emmanuel Atamba, wiki iliyopita, alitumia mtandao wa kijamii kuelezea jinsi mkewe alianza kujitibu kwa kutumia tembe za ‘azithromycin’ na kula matunda ya akila aina ‘kuimarisha’ kingamwili baada ya kupatikana na virusi vya corona.

Baada ya siku 10, dalili za ugonjwa wa corona zilitoweka lakini mkewe aliendelea kuwa dhaifu. Baada ya siku chache alikuwa na tatizo la kupumua.

“Mke wangu alipozidiwa nilimpeleka hospitalini na akalazwa ICU. Muuguzi alinieleza kuwa mke wangu alikuwa akisumbuliwa na tatizo la kumeza tembe za azithromycin,” akaelezea.

Tembe za azithromycin hutumika kutibu maradhi yanayosababishwa na bakteria kama vile nimonia.Kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO), tembe za kutibu maradhi yanayosababishwa na bakteria haziwezi kutibu magonjwa yanayosababishwa na virusi. Corona ni ugonjwa unaosababishwa na virusi.

Shirika la WHO linashauri kuwa dawa za bakteria (antibiotics) zinafaa kutumiwa tu baada ya kupewa ushauri na daktari.Idadi kubwa ya Wakenya maskini sasa wanatumia dawa za bakteria na matibabu ya kiasili kama vile kujifukiza, kunywa mchanganyiko wa ndimu, tangawizi na kitunguu saumu kati ya njia nyinginezo kujitibu virusi vya corona.

Ugonwja wa corona sasa umejiunga na maradhi mengine hatari kama vile, kansa, kisukari, moyo, shinikizo la damu, Hepatitis C, nakadhalika, ambayo ni ghali kutibu.

Kansa

Utafiti uliofanywa 2018 katika vituo mbalimbali vya kutibu kansa jijini Nairobi, ikiwemo Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH), Hospitali ya Nairobi na Hospitali ya Aga Khan, ulionyesha kuwa idadi kubwa ya Wakenya hawawezi kumudu matibabu ya saratani.Inagharimu kati ya Sh172,000 na Sh759,000 kutibu kansa ya mlango wa uzazi (cervical cancer), bila kufanyiwa upasuaji.

Inagharimu kati ya Sh672,000 na Sh1.25 milioni kwa mwathiriwa wa kansa ya mlango wa uzazi kufanyiwa upasuaji, kwa mujibu wa utafiti huo uliofanywa na Taasisi ya Kansa nchini (NCIK) na Idara ya Kudhibiti Kansa nchini (NCCPK).

Matibabu ya kawaida ya kansa ya matiti yanagharimu kati ya Sh175,200 na Sh1.98 milioni na gharama huongezeka hadi Sh2.48 milioni kufanyiwa upasuaji.

Kansa ya korodani (prostate) inagharimu kati ya Sh138,000 na Sh1.21 milioni huku kansa ya koo ikigharimu zaidi ya Sh1 milioni.Kupima kansa ya matiti ni inakagharimu Sh15,000, kwa mujibu wa wa ripoti hiyo.

Takwimu za WHO zinaonyesha kuwa Wakenya 47,000 hupatikana na kansa huku wengine 32,000 wakifariki kila mwaka.Inakadiriwa kuwa wanawake 5,900 hupatikana na kansa ya matiti kila mwaka. Asilimia 43 ya wanawake humu nchini wameshindwa kupata matibabu kutokana na gharama ya juu ya matibabu ya kansa.

Baadhi ya Wakenya wanaojimudu husafiri hadi katika mataifa ya kigeni kutafuta matibabu ya magonjwa sugu kama vile kansa.Kati ya Januari na 2019, wagonjwa 400 waliruhusiwa na wizara ya Afya na Baraza la Madaktari na Wataalamu wa Meno (KPDC) kwenda kutibiwa katika mataifa ya kigeni kama vile Afrika Kusini, Ujerumani, India na Uingereza, kulingana na mkurugenzi wa KPDC, Dkt Daniel Yumbya.

Kusafiri nje ya nchi huwa ghali kwani mgonjwa analazimika kulipia gharama ya matibabu, malazi hotelini au ndani ya hospitali, tiketi ya ndege na chakula.

Mara nyingi mgonjwa husafiri na mwangalizi ambaye anafanya gharama kwenda juu.Tafiti mbalimbali ambazo zimefanywa zimebaini kuwa inagharimu angalau Sh60,000 kutibu wagonjwa wa kisukari kwa mwaka. Wagonjwa wa kisukari huhitaji dawa ya kuteremsha kiwango cha sukari mwilini ambayo hutumia maisha yao yote.

Ni vigumu kwa watu wa mapato ya chini kupata kiasi hicho cha fedha kupata matibabu ya kisukari.Utafiti uliofanywa 2017 na wizara ya Afya kuhusu gharama ya maradhi ya kifua kikuu (TB) ulibaini asilimia 50 ya Wakenya hawapimwi au kutibiwa.

Kulingana na ripoti ya utafiti huo, familia zilizo na mgonjwa wa TB hutumia wastani wa Sh26,000 kutafuta matibabu kwa mwaka.Asilimia 27 ya waathiriwa wa TB hulazimika kuchukua mikopo au kuuza mali zao ili kutafuta matibabu.

pauline ongaji

Mwandishi wa NMG, Pauline Ongaji atuzwa

NA RICHARD MAOSI

MWANDISHI wa masuala ya afya na mazingira katika kampuni ya Nation Media Group (NMG) Bi Pauline Ongaji ametajwa kama mwanahabari bora zaidi katika uandishi wa makala ya kuzuia maradhi yasiyoambukizwa, katika tuzo za kwanza za Afrika Mashariki kwa Wanahabari wanaoripoti masuala hayo.

Akiwa na tajriba ya miaka kumi katika uanahabari, Bi Ongaji amejizolea umaarufu kote nchini kwa makala yake yenye mvuto wa kipekee yanayochapishwa na magazeti ya Taifa Leo, Daily Nation na Business Daily.

Akiashiria furaha yake baada ya kutuzwa katika hafla iliyoandaliwa jijini Kampala, Uganda hapo Ijumaa, Bi Ongaji alisema kuwa juhudi zake zimepata tuzo inayostahili baada ya miaka mingi ya kuandika makala yanayobadilisha jamii.

“Ninaona fahari kutambuliwa na shirika la hadhi kama hili. Furaha yangu inatokana na jinsi makala yangu yamesaidia mamilioni ya watu kwa lugha ya Kiingereza na Kiswahili hapa Afrika Mashariki,” aliambia Taifa Leo Dijitali.

Baadhi ya makala yaliyomshindia mwanahabari huyo tuzo hiyo ni ‘Kansa ya lango la uzazi bado changamoto mashambani’ iliyochapishwa na Taifa Leo, ‘When you get a donor but you can’t get treatment’ iliyochapishwa na Daily Nation na ‘Kidney patients grapple with transplant queues headache’ iliyotokea katika Business Daily.

“Nyakati zote mimi husafiri hadi mahali ambapo habari zinatendeka ili kupata hisia za waathiriwa. Lengo langu ni kuonyesha jinsi magonjwa haya yanaathiri jamii mbalimbali na suluhu zilizopo.”

Mamia ya wanahabari kutoka Kenya, Uganda, Tanzania, Zanzibar, Rwanda na Burundi walishiriki katika tuzo hizo ambazo ziliangazia makala yaliyofanyiwa utafiti wa kina na kuandikwa kwa lugha ya kipekee.

“Tulikuwa tunawazawidi wale ambao wameandika makala yaliyochanganuliwa vizuri. Pia tulitaka kuwatambua wanahabari wenye talanta ya kuandika habari kwa lugha rahisi, yenye mvuto mkuu na inayoeleweka na wasomaji wa jamii mbalimbali,” akasema Proscovia Nabatte, mratibu wa tuzo hizo.

MARY WANGARI: Elimu kuhusu afya ya uzazi itiliwe maanani hata zaidi

Na MARY WANGARI

MAJUZI, Waziri wa Elimu Profesa George Magoha aliamrisha wanafunzi wajawazito ambao hawajarejea shuleni kusakwa, akisisitiza kwamba ujauzito si ugonjwa.

Dkt Magoha alikuwa akizungumza katika Kaunti ya Bungoma alipoagiza machifu, maafisa wengine wa utawala na wadau kuhakikisha wasichana hao wanapata ushauri nasaha na kurejelea masomo yao.

Haya yanajiri wakati shule zimefunguliwa tena kote nchini baada ya likizo ya takriban miezi 10 tangu janga la Covid-19 kuzuka nchini.Kulingana na ripoti mpya iliyotolewa na Baraza la Kitaifa kuhusu Idadi ya Watu na Maendeleo (NCPD), wasichana 20,828 walio na umri wa kati ya miaka 10 na 14 tayari wamekuwa wazazi baada ya kujifungua.

Wengine 24,016 wenye umri wa kati ya miaka 15 na 19 ni wajawazito au tayari ni akina mama wachanga.Shinikizo kutoka kwa marika, matumizi ya intaneti yasiyodhibitiwa pamoja na malezi duni ni baadhi ya sababu kuu ambazo zimechangia idadi kubwa ya mimba za mapema miongoni mwa wanafunzi.

Serikali ya Rais Uhuru Kenyatta imejitahidi kuhakikisha kwamba hakuna mtoto atakayekatiza masomo kwa sababu zozote zile, ikiwemo uzazi.

Mnamo Julai, Rais aliagiza kuwa wasichana wote wajawazito wasajiliwe katika mpango wa afya ya uzazi ili kupata huduma mwafaka za uzazi.Hata hivyo, hatuwezi kupuuza uhalisia mchungu unaosubiri taifa baada ya shule kufunguliwa tena wiki jana. Idadi kubwa ya wanafunzi wa kike waliotungwa mimba wamelazimika kusalia nyumbani kutunza watoto wao wachanga.

Baadhi walikwisha ozwa na kuanza maisha ya ndoa huku wengine wakikosa hamu kabisa ya kurejea shuleni kwa kuhofia unyanyapaa na kudhalilishwa na wanafunzi wenzao.

Hatuwezi kusahau athari za kisaikolojia kwa wahasiriwa zinazoletwa na mimba za mapema, ndoa za mapema na kuwa mzazi umri mchanga; bila shaka zimeacha makovu yatakayodumu kwa muda mrefu.Ni dhahiri kwamba kama jamii tumewafeli mabinti zetu. Hata hivyo, halitakuwa jambo la busara kuendelea kuomboleza jinsi mambo yalivyokwenda mrama.

La muhimu kwa sasa ni kuchunguza tulipopotoka kama jamii kuhusu malezi ya watoto, na kujirekebisha ili kuhakikisha matineja wetu wanakomaa inavyofaa katika siku za usoni.Umuhimu wa kuwepo kwa elimu ya kina kuhusu afya ya uzazi hauwezi ukasisitizwa vya kutosha wakati huu ambapo shughuli za masomo zinarejelea.

Juhudi za serikali kuanzisha masomo mahususi kuhusu afya ya uzazi katika shule za msingi zimelemazwa kwa muda mrefu tangu 2013 kutokana na pingamizi kali za makundi ya kidini na wanaharakati wengineo.Kando na kuwaelimisha watoto kuhusu maambukizi na jinsi ya kujikinga dhidi ya HIV, wakati umewadia wa kutoa mafunzo ya kina kuhusu afya ya uzazi.

mwnyambura@ke.nationmedia.com

Dawa bandia za hamu ya mapenzi zinavyohatarisha maisha ya wanaume

NA PAULINE ONGAJI

 

WANAUME humu nchini wamekuwa wakihatarisha maisha yao kwa kutumia kiholela dawa za kuongeza hamu ya mapenzi au nguvu za kiume.

Uchunguzi uliofanywa na mamlaka ya kudhibiti ubora wa vyakula na dawa nchini Amerika (FDA) ulibaini kuwa nyingi ya dawa za kuongeza hamu ya mapenzi au nguvu za kiume ambazo zimekuwa zikiuzwa madukani na mitandaoni ni hatari kwa afya.

Mamlaka hiyo, wiki iliyopita, ilitoa orodha ya zaidi ya dawa 50 za kuongeza hamu ya mapenzi na kupunguza uzito zilizo na viungo fiche ambavyo vinaweza kuhatarisha maisha haswa miongoni mwa watu ambao wanatumia dawa za kisukari, presha, maradhi ya moyo, nakadhalika.

Baadhi ya dawa zilizo katika orodha hiyo zimekuwa zikiuzwa katika maduka na mitandao ya humu nchini hivyo kutia hatarini maisha ya maelfu ya wanaume ambao wamekuwa wakizitumia ili ‘kufurahisha’ wapenzi wao kitandani.

Mamlaka ya FDA ilinunua dawa hizo katika mitandao ya Amazon na eBay na baada ya kuzifanyia vipimo ilibaini kuwa zina viungo fiche ambavyo ni hatari kwa afya licha ya wauzaji wazo kudai kuwa ni salama.

Miongoni mwa tembe za kuongeza nguvu za kiume au hamu ya mapenzi zilizogunduliwa kuwa hatari kwa afya ni PremierZEN, U.S.A Viagra na Herb Viagra kati ya nyingine nyingi ambazo zimekuwa zikiuzwa madukani na mitandao ya humu nchini.

Kwa mfano, FDA ilibaini kuwa tembe zinazojulikana kama U.S.A Viagra zina kiungo kinachofahamika kama sildenafil ambacho hupatikana katika tembe ambazo hupewa wagonjwa walio na matatizo ya nguvu za kiume.

Tembe za Herb Viagra pia zilipatikana na kiungo hicho. Tembe za PremierZen zina viungo vya sildenafil na tadalafil ambazo hupatikana kwenye tembe za Viagra na Cialis ambazo zimeidhinishwa humu nchini kutumika kutibu wagonjwa walio na matatizo ya nguvu za kiume.

Japo tembe za Viagra na Cilialis zimeidhinishwa kutumika kutibu watu walio na matatizo ya nguvu za kiume, zimepigwa marufuku kuuzwa madukani – ni sharti zitumiwe chini ya usimamizi wa daktari aliyehitimu.

Tembe za PremierZen, kwa mfano, zinapatikana kwa urahisi mitandaoni na zinauzwa kwa kati ya Sh3,000 na Sh6,000 kulingana na idadi ya tembe.

Katika tovuti ya jiji.co.ke dawa ya Herb Viagra inauzwa kwa kati ya Sh2,000 na Sh4,000.Mafuta ya Beast yanayodai kumfanya mwanaume kuwa na nguvu za kiume kwa muda mrefu wakati wa kufanya mapenzi yanauzwa kwa Sh6,500 katika maduka mbalimbali nchini.

Mtandao wa G Spot Kenya, unauza mafuta ambayo unadai yanamwezesha mwanaume kuwa na nguvu za kiume kwa dakika 60. Mafuta hayo yanauzwa kwa Sh2,000.

Ripoti iliyotolewa na mtandao wa ePharmacy Kenya ilifichua kuwa tembe za kuongeza hamu ya mapenzi ni miongoni mwa dawa ambazo zinanunuliwa zaidi na Wakenya kupitia mitandaoni.

Wengi wanapendelea kununua dawa hizo kupitia mitandaoni ili kujificha.Watu wanaponunua dawa kupitia mitandaoni hupelekewa dawa hizo hadi nyumbani hivyo kuzitumia wanavyotaka bila kupata ushauri wa daktari.

Kulingana na Dkt Gitobu Mburugu, mtaalamu wa maradhi ya mfumo wa uzazi katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH), kuna aina tatu za dawa ambazo zimeidhinishwa kutumika kutibu wanaume walio na matatizo ya nguvu za kiume humu nchini.

Dawa hizo ni Viagra, Cialis na Vardenafil. Dawa hizo ni sharti zitolewe na daktari aliyehitimu na ni marufuku kuzinunua dukani.

Dawa ya Vardenafil inauzwa kwa kutumia majina ya Levitra, Vivanza na Staxyn.Dkt Mburugu anasema kuwa dawa feki zinazodai kuwa Viagra au Cialis zimejazana madukani ambazo huhatarisha maisha ya watumiaji wake.

Uchunguzi uliofanywa na kampuni ya Pfizer ambayo imetengeneza Viagra, ulionyesha kuwa asilimia 80 ya dawa zinazouzwa mitandaoni zikidai kuwa Viagra, ni feki.

Mnamo 2017, Bodi ya Dawa na Sumu nchini (PPB) ililalamikia kuhusu ongezeko la dawa ghushi zinazodai kuongeza hamu ya mapenzi au nguvu za kiume humu nchini.

Kulingana na mkurugenzi wa idara ya utekelezaji wa sheria kuhusu matumizi ya dawa wa PPB, Peter Mbwiiri Ikamati, tembe zinazodaiwa kuongeza hamu ya mapenzi ni miongoni mwa dawa zilizoghushiwa kwa wingi humu nchini.

Mnamo Agosti, mwaka huu, maafisa wa Idara ya Uchunguzi wa Uhalifu (DCI) walinasa mwanaume aliyepatikana akiuza tembe feki za Viagra katika mtaa wa Hurlingham, Nairobi.Kulingana na DCI, mshukiwa aliyetambuliwa kwa jina la Cummings Thatia alijitengenezea tembe zilizojulikana kama Viagra Pro na kisha kuuzia wateja wake.

Mamlaka ya Ushuru (KRA) mwaka jana iliharibu shehena ya tembe zilizodaiwa kuongeza hamu ya mapenzi zilizonaswa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Eldoret.

Kulingana na KRA shehena hiyo ilikuwa ikielekea mjini Nakuru lakini mwenyewe alikosa kujitokeza baada ya mzigo wake kunaswa.Soko la tembe za kuongeza hamu ya mapenzi linakua kwa kasi humu nchini.

“Wengi hawajui kuwa kununua tembe za Viagra dukani ni kinyume cha sheria na wanaweza kukamatwa. Tembe hizo zimeidhinishwa kwa ajili ya matibabu yanayotolewa na daktari na wala si kuzitumia kiholela katika starehe,” anasema Dkt Ikamati.

Dkt Ikamati anasema kuwa kutazama video za ngono ni miongoni mwa sababu zinazochochea watu, haswa vijana, kukimbilia tembe za kuongeza hamu ya mapenzi au nguvu za kiume.

Anasema kuwa wanaume wanaotazama video hizo chafu kwa muda mrefu hukosa nguvu za kiume au hudumu kwa muda mfupi wakati wa kufanya mapenzi.

Dkt Ikamati, hata hivyo, anasema kuwa tembe halali za Viagra zikitumiwa kwa kuzingatia maelekezo ya daktari zinaweza kusaidia watu walio na matatizo ya nguvu za kiume.

“Lakini tembe hizo zikitumiwa kiholela zinaweza kudhuru afya na hata kusababisha kifo. Ikiwa mwathiriwa anatumia aina fulani za dawa za presha, maradhi ya moyo au kisukari anaweza kufariki ghafla iwapo atameza Viagra. Hii ni kwa sababu dawa hizo huwa na ‘nitrate’ ambayo ikikutana na Viagra husababisha presha ya damu kushuka ghafla kuliko kawaida na kusababisha kifo,” anaelezea.

Mtu aliye na maradhi ya selimundu (sickle cell), vidonda vya tumbo, upungufu wa damu (anemia) matatizo ya ini, nakadhalika, hawafai kutumia Viagra.Matumizi ya Viagra kiholela kwa muda mrefu, Dkt Ikamati anaonya, yanamfanya mwanaume kuwa goigoi kitandani katika siku za usoni kwani tembe zitakosa uwezo wa kusisimua mwili.

Mnamo 2017, bodi ya PPB ilielezea wasiwasi wake kuhusu ongezeko la watu wanaotumia tembe za kuongeza hamu ya ngono katika maeneo ya Pwani.Bodi hiyo iliwataka wakazi wa Pwani kuripoti wauzaji wa tembe za kuongeza hamu ya mapenzi kwa watu wasiokuwa na barua ya daktari.

Anatumia mitandao ya kijamii kuhamasisha umma kuhusu Ukimwi

Na JOHN KIMWERE

NI mwalimu wa dini katika Kanisa la Bethlehem Judah Restoration, linalopatikana Bombolulu Kisimani steji, Mombasa, Florence Wairimu Irungu anayesema maisha yake yalichukua mkondo mwingine mwaka 2004 baada ya kugundua ameathirika na virusi vya ukimwi.

Dada huyu mwenye umri wa miaka 40 aliamua kupokea mafunzo ya kufunza dili mwaka 2016 alipoanza kukubali hali yake pia alipogundua imekuwa vigumu kupata bwana ambaye ameathirika kama yeye.

MSONGO WA MAWAZO

Pia anasema aliamua kumtumikia Mungu maana hawezi kufanya kazi ngumu kutokana na hali yake ya kiafya maana amewahi kuugua kifua kikuu mara mbili, Pneumonia, vidonda vya tumbo na msongo wa mawazo.

”Kusema ukweli nimepitia wakati mgumu ndani ya kipindi cha miaka 14 kabla ya kujikubali maana hata niliwahi wazia kujitoa uhai mara kumi,” mtumishi huyo alisema na kuongeza kuwa hali ya kuwa ameathirika imechangia zaidi ya wachumba 20 kuonyesha nia ya kuingia katika maisha yake kisha kusepa wakigunduaa hali yake.

Anasema alipojikubali ndio alianza kutumia kutumia mtandao wa kijamii wa Facebook kupitia ukurasa unaitwa ‘Encouragement Through life Experience’ kuzungumzia hali yake na kutia wengine moyo kujikubali.

Pia ameanzisha chaneli yake katika jukwaa la YouTube inaitwa ‘Florence Taylor Motivator’ ambapo hutupia video kuhusu jinsi waathiriwa wa Ukimwi wanavyoweza kuishi kwa amani.

Anasema alipitia wakati mgumu baada ya kujitenga na watu wengine akijiuliza watu wakifahamu hali yake watasema nini. ”Kiukweli nilihudhika sana wakati mmoja nilipoambia rafiki yangu nimeathirika lakini naye alianza kusambaza kwa watu wengine. Sikufurahi kabisa hali hiyo ilichangia hasira pia niliendelea kunyamaza na kuumia zaidi moyoni,” akasema.

MAKAO YA WATOTO YATIMA

Wairimu anashukuru askofu wake, Rahab Roberts na bwanake ambao waliweza kumkumbatia kama mtoto wao maana wameishi naye katika familia yao kwa kipindi cha miaka 13 sasa. ”Siwezi kuwatoa rangi kabisa maana kwa kipindi hicho hawajawahi kunionyesha madharau licha ya kuwa nimeathirika na ukimwi wala hawajawahi kuniuliza jinsi niliambukizwa,” akasema na kuongeza anawaombea Mungu awajalie maisha marefu.

Katika mpango mzima Wairimu amepania kuanzisha familia ya watoto yatima ambao wazazi wao walikufa kutokana na ugonjwa wa ukimwi. Kadhalika anashukuru familia yake wakiwamo wazazi, dada zake saba na ndugu zake wawili pia wanao ambao wamemuonyesha upendo tangia wafahamu hali yake.

Katika mpango mzima anashauri jamii ikome kuwatenga wale wameathirika na ukimwi maana huwa wanahitaji mapenzi zaidi kusudi kuhimili hali hiyo. Anasema upweke huchangia wengi kupoteza maisha yao baada ya kupoteza marafiki pia kuona hawana maana hapa duniani.

MAWAIDHA

”Ushauri wangu kwa wengine unaojikuta wameathirika nawaambia ni vizuri kujikubali na kuelewa Mungu ana sababu kwa hali hiyo pia sio mwisho wa maisha yao,” akasema na kuongeza kuwa wanastahili kuendelea kutumia dawa za kupunguza makali (ARVs), kula chakula vizuri pia kufanya mazoezi na bila shaka wataishi miaka mingi.

Aidha anasisitiza kuwa mtu anapogundua ameathirika kamwe hafai kunyamaza ila anastahili kufunguka ili kujiepusha na mahangaiko moyoni mwake. Pia anasema huwa jambo nzuri wakati mtu anapojikuta katika hali hiyo anatafuta hospitali nzuri hasa kuwa ikifuatilia hali yake ya kiafya.

”Pia ninashauri wale hupenda kuambukiza wengine kimakusudi kuwa huwa wanawakosea zaidi kwa kuwatumbukiza pabaya kimaisha. Imekuwa vigumu kwa waathiriwa wa ukimwi kupata wachumba wa kufunga ndoa nao pia kupata watoto maana baaadhi yao hushindwa kufunguka na kuishi kwa hasira,” alihoji.

Je, nini maana ya ugonjwa wa sciatica?

Na MARY WANGARI

Je, sciatica ni nini? Kwa mujibu wa Dkt Brian Rono, Mtaalam wa Viungo na Upasuaji, sciatica inayofahamika pia kama uchungu wa sehemu ya chini ya mgongo, ni hali inayotokea wakati kuna shinikizo kwenye neva za misuli.

“Uchungu wa sehemu ya chini ya mgongo unahusisha msisimuko wa misuli kwenye uti wa mgongo. Hali hiyo pia inahusu hisia ya kudungwadungwa kwenye makalio au uchungu mkali unachomokeza mgongoni.

“Hali hii hutokea wakati mizizi ya neva inaposhinikizwa hali inayosababisha umbo la mifuko ya neva kufura au kubadilika hivyo kusababisha uchungu mkali unaochomoza katika sehemu ya chini ya mgongo, wayo wa mguu, sehemu ya ndani au nje kwenye magoti,” anafafanua daktari huyo.

Mtaalam huyo wa afya jijini Nairobi, anaeleza kuwa maradhi hayo husababisha uchungu mkali mgongoni, kwenye miguu na hata huweza kusababisha kufa ganzi.

Takwimu zinaonyesha kuwa takriban asilimia 80 ya watu kote duniani wanaugua ugonjwa huo usiobagua jinsia wala umri huku ukiathiri wake kwa waume wenye umri wa miaka 20 na zaidi.

Ingawa ugonjwa wa sciaticva unafahamika vilevile kama uchungu wa sehemu ya chini ya mgongo, wataalam wanatahadharisha dhidi ya kukanganyikiwa kuhusu matatizo ya uchungu kwenye mgongo na hali hiyo.

Si maumivu yote ya mgongo ambayo ni sciatica kulingana na wataalam kutoka Kituo cha Kitaifa kuhusu Teknolojia ya Bayolojia ambacho ni tawi la Taasisi ya Afya America.

Tafiti zimeonyesha kuwa sciatica inaweza kupitishwa kijeni ambapo hurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine.

Masuala mengineyo yanayochangia ndwele hiyo ni pamoja na hali ya kikazi inayohusisha kusimama au kuketi katika hali fulani kwa muda mrefu kama vile madereva wa trela na wanaoendesha mashine.

Dkt Rono, anatahadharisha kuwa kuendelea kushinikizwa kwa mishipa ya neva kwa muda mrefu bila matibabu kunaweza kusababisha mgonjwa kupooza.

Isitoshe, dalili hizo zinaweza kuwa zikijirejelea hata baada ya mgonjwa kutibiwa na kuonekana kupona hali inayodhihirisha ni kwa nini ni muhimu kuzingatia mikakati ya kujikinga dhidi ya gonjwa hilo.

Kuna visababishi anuai vya sciatica jinsi vilivyoorodheshwa ifuatavyo:

Sciatica husababishwa na nini?

Misuli kukazwa kupita kiasi – Misuli ya sehemu ya chini ya mgongo ni nguzo inayowezesha utekelezaji wa shughuli za kila siku. Matatizo hayo hutokea wakati misuli inapofanyishwa kazi kupita kiasi au inapokuwa dhaifu.

Jeraha kwenye viungo – Kuna viungo maalum vinavyowezesha sehemu ya chini ya mgongo kuwa imara.

Sehemu hiyo inapojeruhiwa kutokana na kusongeshwa kwa nguvu au kushinikizwa kwa muda mrefu huweza kusababisha sciatica.

Mapozi duni ya kusimama au kuketi – Kwa mfano kujipinda unapoketi mbele ya televisheni ukitazama au kuketi ukiwa umepinda mgongo husababisha misuli kuchoka, pamoja na kushinikiza nyonga na viungo vinavyofunika mifupa ya uti wa mgongo.

Dhuluma – Dhuluma za muda mrefu kama vile kupigwa au mateso husababisha misuli kupoteza usawa kama vile kujikaza kunakofaa na kuidhoofisha hali ambayo inaweza kusababisha uchungu vilevile.

Umri – Kudhoofika kutokana na umri pamoja na masuala ya kurithishwa kiukoo yanaweza kusababisha mabadiliko ya kudhoofisah mifuko ya mifuka (inayofahamika pia kama maradhi ya kudhoofika kwa mifuko ya mifupa) na kudhoofika kwa nyonga za uti wa mgongo (kunakofahamika kama maradhi ya kudhoofika kwa nyonga)

Kulingana na wataalam wa afya, kuzeeka kwa kawaida husababisha kupungua kwa uzani wa mifupa, nguvu na mshikamano wa misuli na viungo athari zinazoweza kupunguzwa kupitia mazoezi ya viungo vya mwili mara kwa mara, mbinu inayofaa ya kuinua na kusogesha mizigo, lishe bora na uzani unaofaa mwilini na kuepuka uvutaji sigara.

Ugonjwa huo unapozorota zaidi kama vile mifuko ya neva inapoanza kufura, wataalam wanapendekeza vipindi vya mazoezi ya kimatibabu ili kuimarisha na kulainisha misuli pasipo kulazimika kufanyiwa upasuaji.

Saratani, maradhi ya figo, mfuko wa mkojo, mfuko wa uzazi na mayai ya kike ni miongoni mwa masuala mengineyo yanayosababisha sciatica.

Matibabu ya sciatica yanajumuisha:

Kupumzika kutokana na shughuli za kuchosha – Epuka kuketi, kuinama, kujipinda, kuendesha gari, mashine au mitambo au kuinua vitu vizito kwa muda mrefu.

Matibabu ya barafu – barafu inapogusishwa katika sehemu ya chini ya mgongo kwa dakika 15 kila baada ya saa 1-2 husaidia kupunguza uchungu na kuwashwa kwa misuli.

Wataalam pia wanatahadharisha dhidi ya kutumia joto kwa saa 48 baada ya kupata jeraha.

Matibabu ya kuzuia maumivu (NSAIDs): kama vile aspirin, advil, aleve, ibuprofen miongoni mwa dawa nyinginezo kuambatana na ushauri wa daktari.

Mazoezi ya viungo vya mwili – Epuka mtindo wa kukaa tu bila kufanya mazoezi, fanya mazoezi rahisi ya kusogesha viungo vya mwili na kuvilainisha (hasa misuli ya miguu na mgongo) ambayo inaweza kusaidia kupunguza kiwango na muda wa maumivu hayo pamoja na kujirejelea kwa maumivu ya sciatica.

Unapofanya mazoezi, hata hivyo, tahadhari usijihusishe na mazoezi ambayo badala yake yatakuzidishia maumivu.

Mtindo wa kulala – Badilisha mtindo wako wa kulala ili kupunguza shinikizo kwenye sehemu ya chini ya mgongo wako.

Hakikisha kitanda chako ni imara na kinachoweza kukustahimili vyema na pia lalisha kichwa chako kwenye mto.

Endapo unapendelea kulala chali, jaribu kulala ukiwa umeweka mto chini ya magoti yako.

Ikiwa unapenda kulala kwa ubavu, lala ukiwa umeweka mto katikati ya mapaja yako.

Iwapo unapenda kulala kwenye ubavu ukiwa umejipinda, kuweka taulo iliyokunjwa chini ya kiono chako kutakufaa mno.

Mbinu nyinginezo za kujikinga kutokana na sciatica ni pamoja na mazoezi ya kimatibabu ya kuimarisha mifupa ya sehemu ya tumbo, nyonga na mgongo ili kuzuia maradhi hayo kujirudia.

Umuhimu wa kutilia maanani mapozi ya mwili ama unapolala au kuketi hauwezi ukasisitizwa vya kutosha tunapozungumzia kuhusu kupunguza maumivu ya sehemu ya chini ya mgongo.

Hata hivyo, ni muhimu zaidi mgonjwa kumwona daktari anapoanza kuona dalili hizi:

Homa mwilini isiyoweza kufafanuliwa, maumivu makali yanayoendelea kwa zaidi ya wiki moja, uvimbe au kugeuka rangi kwenye mgongo au uti wa mgongo, hisia ya kudungwadungwa, uchungu au kufa gazi kunakosambaa kwenye miguu au magoti, miguu kuwa dhaifu, matatizo ya kwenda haja au kwenye kibofu, maumivu mgongoni kutokana na kugongwa, kuanguka pamoja na kupoteza uzani kwa njia isiyoweza kueleweka.

Mwnyambura@ke.nationmedia.com

SARATANI YA MATITI: ‘Nilidhani ni ugonjwa wa wanawake pekee…’

NA PAULINE ONGAJI

Alipogundua kwamba alikuwa anaugua kansa ya matiti mwaka jana, alishtuka sana kwani hakujua kwamba maradhi haya pia huwakumba wanaume.

Lakini ni uhalisia ambao Charles Maina, 60, mkazi wa eneo la Kieni, Kaunti ya Nyeri, alilazimika kukumbatia, suala ambalo limemwezesha kufuatilia matibabu vilivyo.

Masaibu ya Bw Maina yalianza Agosti 31, mwaka jana. “Nilianza kukumbwa na maumivu makali kwenye titi langu la kushoto. Mwanzoni nilidhani yalikuwa tu maumivu ya kawaida, lakini uchungu ulipozidi, nikaamua kwenda hospitalini,” aeleza.

Kulingana naye, madaktari walikabiliwa na changamoto ya kubaini nini hasa kilichokuwa kikimtatiza. “Si mara moja waliniambia kuwa huenda maumivu yanatokana na mafuta mwilini, hasa ikizingatiwa kwamba wakati huo nilikuwa mnene,” asema.

Anasema kwamba alipewa dawa ya kukabiliana na maumivu na kuruhusiwa kurudi nyumbani. Hata hivyo, kufikia Desemba mwaka jana, hali ikawa tete kwani ule uchungu ulikuja kwa mshindo, hivyo ikabidi arudi hospitalini kwa uchunguzi zaidi.

“Wakati huu madaktari walichukua muda wao kufanya chunguzi kadha wa kadha ila bado tatizo halikubainika mara moja. Uchunguzi huu uliendelea kwa muda huku madaktari wakitumia mbinu ya ultrasound-guided needle biopsy, na kufikia mwisho wa Februari mwaka huu, waliweza kutambua kwa kweli ilikuwa kansa ya matiti,” anasema.

Lakini kwa bahati mbaya maradhi haya yalikuwa tayari yameenea hadi kwenye mapafu na wakamshauri kuanzisha matibabu mara moja.

“Mwezi Machi mwaka huu, nilianza rasmi matibabu ya dawa hadi Juni. Nilikuwa nimeanza kupata nafuu angaa kulingana na uchunguzi uliofuatia lakini kufikia Septemba, kidonda kikachipuka kifuani. Nilipoenda hospitalini, nilianzishiwa matibabu ya tibaredio mara moja, ambapo nilikamilisha kikao cha mwisho wiki tatu zilizopita,” aeleza.

Kwa sasa amemaliza vikao kumi vya tibaredio na anajiandaa kuanza matibabu ya tibakemia.Japo Bw Maina ana matumaini kwamba yuko katika mkondo mwema kimatibabu kwani hali yake imekuwa ikiimarika, haijakuwa rahisi kwani mbali na mzigo wa kifedha unaotokana na gharama za matibabu, haikuwa rahisi kukubali kwa kweli alikuwa anaugua kansa ya matiti.

“Unapofichua habari kwamba unaugua kansa ya matiti; ugonjwa unaofahamika kuwakumba hasa wanawake, sio rahisi watu wakuelewe. Wengi waliotambua kuhusu hali yangu, mwanzoni hawakuamini,” aeleza.

Na ndiposa amejitokeza na kutangaza hali yake ili kuwapa wanaume wengine wanaogua maradhi haya nguvu ya kujitokeza waweze kupokea matibabu mapema.

“Hakuna nafasi ya aibu tena. Ukisikia kuna shughuli ya kupima watu, kama mwanamume jitokeze. Kuwa na mazoea ya kukagua sehemu hii hata kama waona sio jambo la kawaida,” aeleza.

Kulingana na Shirika la Afya Duniani- WHO, japo kansa ya matiti ni nadra mno miongoni mwa wanaume ikilinganishwa na wanawake, sio jambo la kupuuzwa.

Kwa makadirio ya WHO, takriban visa 2,620 vya kansa ya matiti kwa wanaume vilitarajiwa mwaka huu nchini Amerika, huku takriban vifo 520 vikitarajiwa kutokana na ugonjwa huu.

Hapa nchini hakuna takwimu kamili zinazoonyesha idadi ya wanaume wanaougua maradhi haya.Dkt Miriam Mutebi, daktari wa upasuaji wa kansa ya matiti katika hospitali ya Aga Khan, anasema kwamba sawa na wanawake, ishara za kansa ya matiti kwa wanaume ni pamoja na uvimbe usio na uchungu kwenye tishu ya matiti huku ngozi inayozingira titi lililoathirika ikibadilika rangi na kuwa nyekundu na kuonekana kana kwamba ina magamba.

“Pia, chuchu hubadilika na kuwa nyekundu na kuonekana kana kwamba ina magamba au kuanza kubadili na kuingia ndani ya ngozi,” aeleza.

Kulingana na WHO, ili kuongeza uwezekano wa mgonjwa kupona na hivyo kuzuia vifo, utambuzi wa mapema ni muhimu.Kuna mikakati miwili ya utambuzi wa kansa ya matiti.

Moja yazo ni utambuzi wa mapema na hivyo kuanzisha tiba haraka iwezekanavyo. Kisha kuna uchunguzi ili kutambua kansa kabla ya ishara kujitokeza (screening), ambapo ala za utaratibu huu zinahusisha mammography, kukaguliwa titi na mhudumu wa afya, na wewe mwenyewe kujikagua titi lako.

Lakini japo mbinu hizi zimesaidia wanawake wengi kutambua mapema maradhi haya na hivyo kuyadhibiti, huenda ukawa mlima mrefu kukwea kwa wanaume.

“Sio rahisi kwa wanaume kukubali au hata kufikiria kufanyiwa taratibu hizi, na hili ni tatizo katika vita dhidi ya maradhi haya miongoni mwa wanaume,” aeleza Catherine Wachira, Mwenyekiti wa shirika la Kenya Network of Cancer Organization.

Kulingana na Bi Wachira, changamoto kuu imekuwa kuwarai wanaume kufanyiwa uchunguzi wa matiti, ili kutambua maradhi haya mapema na kuanza matibabu kabla kuenea katika sehemu zingine mwilini.

“Tatizo ni kwamba wanaume wengi wanaogopa kujitokeza kwani wanachukulia kuwa ugonjwa wa wanawake,” aeleza Bi Wachira.Kulingana na Dkt Mutebi, kuna haja pia ya kuhamasisha wanaume kuhusu mambo yanayoongeza hatari ya kukumbwa na maradhi haya, na hivyo kuyaepuka baadaye.

Nini kinachoongeza hatari ya kukumbwa na saratani ya matiti kwa wanaume?

Dkt Mutebi kuna mambo kadha wa kadha ambayo huongeza hatari ya kukumbwa na maradhi haya miongoni mwa wanaume, ikiwa ni pamoja na umri, ambapo waathiriwa wa kansa ya matiti miongoni mwa wanaume huwa katika miaka ya sitini.

Pia anataja historia ya maradhi haya katika familia ambapo ikiwa una jamaa wa karibu ambaye amewahi ugua kansa ya matiti, basi kuna uwezekano mkubwa wa kuugua pia.

“Katika mataifa ya magharibi, imekadiriwa kwamba 10% ya wanaume wanaougua kansa ya matiti wana historia ya kifamilia ya kansa ya matiti au ya ovari. Pia, hali kama vile BRCA2 mutation and Klinefelter’s Syndrome (XXY) zinaongeza hatari, japo kinachochangia masuala haya ya kijenetiki barani Afrika, bado hakijatambulika,” anaeleza Dkt Mutebi.

Anasema kwamba kuna sababu zingine zinazosababisha mabadiliko ya matiti kwa wanaume kama vile ugonjwa wa gynaecomastia (ambapo matiti yanakuwa makubwa kutokana na sababu kadha wa kadha), kumaanisha kwamba ili kuwa kuwa salama, mabadiliko haya yanapaswa kukaguliwa na daktari.

Kulingana naye, kuna masuala yanayoweza kubadilishwa na kuna yale hayawezi kubadilishwa. “Kwa mfano haiwezekani kwa mtu kubadili historia ya familia yake, au aepuke uzee – baadhi ya masuala yanayochangia pakubwa hatari ya aina hii ya kansa. Lakini kuna mambo ambayo waweza badilisha kupunguza hatari hii. Mbinu mwafaka asema ni kubadili mtindo wa maisha kwa kula chakula chenye afya na kufanya mazoezi,” asema.

Kwa wanaume, aidha aongeza kuwa, kuna uwezekano wa kansa ya matiti kuenea kwa kasi katika sehemu zingine mwilini kwani tishu za matiti yao ni ndogo ikilinganishwa na wanawake, na ndiposa kansa ya matiti miongoni mwa wanaume huja kwa mshindo na ni rahisi kusambaa mapema.

“Tiba huhusisha upasuaji wa kuondoa tishu za titi lilioathirika, lakini pia kuna matibabu mengine kama vile tibakemia na tibaredio kuambatana na hali ya mwathiriwa. Sawa na aina nyingine za kansa, utambuzi wa mapema, ndio siri kuu ya kuimarisha uwezekano wa kupona baada ya kupokea matibabu,” asema Dkt Mutebi.

Mtaalamu huyu anasema kwamba waathiriwa wa kiume wa kansa ya matiti huenda wakahitajika kupokea matibabu yanayolengewa homoni za kike mwilini mwao, suala ambalo huwatia wengi aibu.

“Hii inamaanisha kwamba wanahitaji usaidizi hata zaidi katika safari hii ya matibabu,” aongeza.Kulingana na Bi Wachira, haya ni masuala ambayo wanaume wengi hawafahamu, kumaanisha kwamba hawana habari hata wanapokumbwa na hatari ya kiafya.

“Ndiposa shughuli za uhamasishaji miongoni mwa wanaume zinapaswa kushika kasi. Wanaume wanahitaji utambuzi wa mapema na kuhamasishwa kuhusu jinsi ya kukagua sehemu hii ya mwili, ili iwe kawaida kwao kufanya hivyo bila aibu,” asisitiza.

AFYA: Miaka 17 baadaye bado chozi linamtiririka…

NA PAULINE ONGAJI

Kwa miaka 17, maisha ya Risper Muhoma, 40, mkazi wa kitongoji duni cha Kibra, jijini Nairobi, yamekuwa magumu.

Katika muda huu wote, Bi Muhoma na mumewe, wamekumbwa na mzigo wa kumlea mtoto wao wa pili, Vincent Wanga, ambaye alizaliwa akiwa na utindio wa ubongo (Cerebral Palsy).

“Pindi baada ya kumzaa, tulitambua kwamba alikuwa na matatizo kwani hangeweza kunyonya vizuri. Baada ya kumpeleka hospitalini, madaktari waligundua kwamba alikuwa na utindio wa ubongo,” aeleza.

Tangu azaliwe, Vincent hajawahi kuzungumza, huku miguu na mikono yake ikiwa imelegea ambapo anategemea hasa kiti cha magurudumu kusonga. Aidha, mikono yake ni dhaifu kiasi kwamba hawezi jifanyia chochote.

“Tangu awe na miaka sita, amekuwa akipokea tiba ya maungo katika kituo cha Mary Rice Center, Kibra ambapo polepole alijifunza kujifanyia mambo madogo madogo kama vile kula, kuzungumza, kuvua na kuvaa nguo,” asema.

Lakini licha ya hayo, mazungumzo na uwezo wake wa kutembea na kutumia mikono yake kikamilifu bado ni dhaifu, kumaanisha kwamba lazima kuwe na mtu wa kumshughulikia kila wakati.

“Pia, lazima atumie kiti cha magurudumu ambacho kwa sasa hana, kwani alichokuwa nacho kiliungua nyumba yetu ilipoteketea miaka miwili iliyopita. Kwa hivyo ili kusonga kutoka sehemu moja hadi nyingine, inabidi atambae, kumaanisha kwamba bado anategemea usaidizi wangu pakubwa,” aeleza.

Huu ni mzigo mzito hasa kwa Bi Muhoma ambaye kama mama, yeye ndiye hukumbwa na jukumu kubwa la kumshughulikia mtoto huyu, vile vile wanawe wengine wanne, mumewe akiwa kazini.

Anasema kwamba mzigo wa kumlea mwanawe mlemavu umekuwa mzito kiasi cha kutostahimilika. “Nampenda sana lakini tangu mtoto huyu azaliwe, maisha yangu yamebadilika. Ilinilazimu kukatiza ndoto zangu ili nimshugulikie,” asikitika.

Pia, kama mlezi wake mkuu, kwa miaka hii yote amelazimika kustahimili unyanyapaa, kutengwa, kutukanwa na hata kulazwa hospitalini kutokana na msongo wa mawazo.

“Nimekumbana na watu ambao wamehusisha hali ya mwanangu na laana au uchawi. Hasa mwanzoni mambo yalikuwa magumu zaidi ambapo mara nyingi nilijipata nikilia. Kuna wakati nililazwa hospitalini kwa mwezi mmoja kutokana na msongo wa mawazo uliosababisha nishindwe kuzungumza,” aongeza.

Hali hii pia imekuwa na athari kubwa kwa maisha yao kifedha. “Kwa mfano, pindi alipozaliwa na kutambuliwa kuugua maradhi haya, mume wangu naye akaachishwa kazi kutokana na mazoea aliyokuwa nayo ya kuomba ruhusa kila wakati ili tumpeleke hospitalini. Tangu wakati huo, amekuwa akitegemea vibarua,” aeleza.

Maisha yamekuwa magumu hata zaidi wakati huu wa janga la Covid-19. “Kuna nyakati ambapo ningejikakamua na kufanya vibarua vya kufua nguo, lakini kwa sasa havipatikani. Aidha, mume wangu ambaye tegemeo lake limekuwa vibarua vya sulubu, hana riziki kwa sasa kwani kazi hizo hazipatikani.”

Katika haya yote, Bi Muhoma na mumewe, kama wazazi na walezi wa mtoto mwenye ulemavu wa kiakili wamekuwa, wakipambana bila ushauri nasaha au usaidizi mwingine wa kisaikolojia.

“Ni wakati mmoja tu ambapo nilipata mafunzo kupitia warsha moja niliyoalikwa, ambapo tulipewa mafunzo mbalimbali kuhusu jinsi ya kuwashughulikia watoto hawa na kuwakubali,” asema.

Bi Muhoma anawakilisha asilimia kubwa ya wazazi wanaowalea watoto wenye ulemavu wa kiakili hapa nchini, pasipo kupokea ushauri nasaha wa aina yoyote.

Kulingana na wataalamu wa kiafya, hii inahatarisha maisha sio tu ya mtoto mwenye ulemavu, bali pia hali ya kiakili ya mzazi.

Dkt Lincoln Kasakhala wa Idara ya tiba ya magonjwa ya akili katika Chuo Kikuu cha Nairobi, asema ushauri nasaha kwa mzazi anayemlea mtoto anayekumbwa na matatizo ya kiakili ni muhimu kwa sababu changamoto wanazokumbana nazo ni nyingi.

“Mara nyingi wazazi hawa huelekeza mawazo yao kwa mahitaji ya watoto hawa na vile vile majukumu mengine yanayowakabili na hao wenyewe kujisahau. Wengi wa wazazi hawa hawana muda wa kufanya mambo yao wenyewe kujifurahisha,” anasema

Dkt Kasakhala asema, hasa kwa watoto wanaougua utindio wa ubongo, changamoto kuu inayowakumba wazazi hawa ni jinsi ya kudhibiti tabia zao.

“Kuna wazazi wanaoona aibu kwa kutokuwa na uwezo wa kudhibiti tabia ya watoto wao katika maeneo ya umma na ili kuepuka hili, wanaonelea heri kujitenga,” anasema.

Ni suala linalowafanya wazazi hawa kutengwa na wenzao, familia na jamii kwa jumla, ambapo ni rahisi kwa mwanamume kutoroka na kumuacha mama akimlea mtoto kivyake.

Aidha, anasema wazazi hawa hukumbwa na matatizo ya kifedha kwani ni gharama kubwa kumlea mtoto anayekumbwa na ulemavu huu.

“Huduma kwa watoto wanaokumbwa na hali hii hazipatikani kwa urahisi hasa katika maeneo ya mashambani. Na hata mijini, huduma hizi zinapopatikana, wazazi wengi hawawezi kumudu. Aidha, jamii nyingi huwatenga wazazi wa aina hii, suala linalowafanya wengi wasijitokeze ili watoto wao wapate usaidizi,” aongeza.

Kwa wale wasioweza kumudu huduma hizi, mambo huwa mabaya kwani kuna hatari ya mzazi huyu kuhisi kana kwamba amefeli au ni makosa yake, suala linalowafanya kupoteza matumaini.

Mtaalamu huyu anasema kwamba hii ni hatari kwani kutokuwa na uwezo wa kufikia rasilmali za matibabu au ukosefu wa ufahamu huwasababishia wasiwasi, kupoteza matumaini na mawazo mengi, hali ambayo yaweza kuwaathiri kiakili kabisa.

“Wakati huu ni rahisi kwao kuanza kujilaumu na kukumbwa na hasira, ambapo kinachofuatia ni msongo wa akili. Mambo yakifikia hapa, sasa wataanza kuonyesha ishara kama vile kukosa usingizi, kukosa hamu ya kula, matatizo ya kumakinika na hivyo ugumu wa kufanya maamuzi, uchovu na maumivu ya mwili.

Dkt Kasakhala anasema kuna hatari ya mzazi huyu kukumbwa na hisia za kumuua mtoto huyu au yeye mwenyewe kujiua.

Lakini licha ya umuhimu wa matibabu haya miongoni mwa wazazi wa watoto hawa, asema kwamba hapa nchini bado ni changamoto.

“Ikiwa mtoto anaugua utindio wa ubongo, mzazi ana mahitaji tofauti ya ushauri nasaha. Katika kila awamu ya kukua, mtoto huyu atakuwa na mahitaji tofauti, kumaanisha kwamba lazima mzazi naye pia apokee ushauri tofauti wakati huu,” asema.

Kulingana naye, kuna hospitali za umma zinazotoa huduma hizi lakini bado kiwango cha mahitaji kiko juu. “Kwa upande mwingine, huduma hizi katika taasisi za kibinafsi zaweza kufikia Sh2, 000 kwa kila kipindi cha ushauri nasaha, kulingana na umri wa mtoto. Sio wazazi wengi wanaoweza kumudu gharama hii,” aongeza.

Japo kumekuwa na jitihada za kuhakikisha huduma za ushauri nasaha kwa wazazi hawa zinatolewa kwa viwango vya kaunti, mtaalamu huyu asema, kibarua kikubwa ni kuhakikisha kwamba wazazi hawa wanajitokeza na kupokea usaidizi.

Aidha anasema kwamba, pasipo usaidizi wa kijamii, kuna uwezekano mkubwa wa wazazi hawa kuathirika kiakili. “Kama jamii tunaweza ingilia kati. Kwa mfano, mbali na kuchangia kifedha kuhakikisha kwamba mzazi anaweza kumudu gharama ya kukidhi mahitaji ya mwanawe, unaweza jitolea muda wako na kumsaidia kumshughulikia mwanawe mara kwa mara, angalau naye apate fursa ya kwenda kazini au kupumzika,” asema.

Kwa upande mwingine anasisitiza umuhimu wa wazazi wahusika nao kutafuta usaidizi kupitia makundi tofauti ya kutoa usaidizi kwa watoto wanaougua maradhi ya aina hii. “Kwa mfano, kuna mashirika ambayo mbali na kusaidia wahusika kupokea tiba, mara nyingi huandaa warsha na vikao ambapo wanapata fursa ya kukutana na kuzungumzia changamoto zao na kusaidiana,” ahitimisha.

Jinsi ya kulinda afya ya meno ya mtoto

Lydia Njeri akiwa na mwanawe Ivan anayetabasamu. PICHA/ HISANI

NA WANGU KANURI

Ni jukumu la kila mzazi kuhakikisha kuwa mtoto wake mchanga anaota meno inavyofaa. Hali kadhalika, sio watoto wengi wadogo huota meno inavyofaa.

Meno ya watoto kubadili rangi yake halisi ambayo ni nyeupe na kuwa rangi ya hudhurungi, kijani kibichi, manjano na wakati mwingine nyeusi huchangiwa na mambo kadha wa kadha.

Kwanza ni kutompiga mswaki mwana wako vyema. Ukoga ama ukipenda uchafu wa meno hubadilisha rangi ya meno ya mtoto wako na kuwa katika rangi ya manjano.

Pili, kumpa mtoto wako mchanga peremende nyingi na vinywaji vilivyo na sukari nyingi kama juisi na soda. Licha ya kuwa vitu hivi hubadilisha rangi ya meno, vinaweza sababisha mashimo katika meno ya mtoto.

Ni vyema kwa wazazi kujua kuwa vitamini zingine zitakazomfaa mwana wako kama madini ya ayoni zinaweza kuyafanya meno ya mwana wako kuwa na madoadoa meusi. Hata hivyo, usisite kumpa mtoto wako vitamini hii kwa kuhofia kuyaharibu meno yake.

Kutumia dawa ya meno iliyo na floridi nyingi. Floridi hii huharibu enameli ya mtoto wako. Tano, mtoto aliyezaliwa na ugonjwa wa ngozi unaoifanya ngozi ya mtoto kuwa ya rangi ya manjano (jaundice) ajapoota meno, meno yake huwa na rangi ya kijani kibichi ama manjano.

Mtoto anaweza kuwa na meno yasiyo na rangi nyeupe kutokana na enameli isiyodhabiti kwa sababu ya chembechembe za DNA alizopata kupitia wazazi wake. Mwisho, mtoto aliyepata majeraha ya meno na mishipa ya damu yake ikavunjika na kutoka damu anaweza iathiri enameli yake.

Isitoshe, mtoto anaweza ota meno yaliyo na rangi ya kijani kibichi ama manjano kwa sababu ya kuwepo na bilirubini nyingi ndani ya damu yake.

Unaweza kuzuia meno ya mtoto wako mchanga kuwa ya rangi nyingine bali na rangi nyeupe kwa; kwanza kuyapiga mswaki meno ya mtoto huyo mara mbili kwa siku.

Pili, kuosha ufizi na meno yake ukitumia pamba hata ingawa meno hayajachipuka bado.  Kutompa mtoto wako peremende au vinywaji vilivyo na sukari nyingi.

Kumtembelea daktari baada ya miezi sita baada ya meno ya mtoto wako kuota.  Iwapo madini ya ayoni ndiyo sababu ya mtoto wako kuwa na meno yasiyo na rangi nyeupe, hakikisha umepangusa ama kupiga mswaki meno ya mtoto wako baada ya kumpa mtoto wako vitamini hiyo.

Usikubali mtoto wako alale akiwa na chupa chake cha maziwa mdomoni kwani maziwa na sukari hukuza bakteria katika meno ya mtoto wako. Mwisho, tumia dawa ya meno iliyo na upungufu wa floridi mpaka wakati ambapo mwana wako atajua kutema dawa ya meno baada ya kumpiga mswaki.

 

AFYA NA ULIMBWENDE: Ujauzito haumaanishi kupoteza mvuto

Na MARGARET MAINA

ZIPO njia mbalimbali za kukusaidia kufurahia urembo wako mwanamke hasa katika kipindi maalumu maishani mwako; ujauzito.

Kunywa maji

Kipindi cha ujauzito unahitajika kunywa maji mengi kwa siku. Yatakusaidia kusafisha na kutoa taka na sumu mwilini mwako. Maji ni muhimu zaidi kwa afya yako na mwana wako mtarajiwa. Kunywa angalau lita mbili za maji kwa siku.

Mlo sahihi

Unahitaji uangalizi na umakini wa ziada katika chakula unachokila wakati wa ujauzito ili kuilinda na kuimarisha afya yako. Unashauriwa kumhusisha daktari wako au mtaalamu wa lishe kukuandalia ratiba ya aina ya chakula unachotakiwa kula. Fuatilia ratiba hii kwa umakini, kula kwa afya; ikiwa pia ni muhimu kwa ajili ya mtoto wako.

Pata muda wa kulala

Hali ya uchovu ni dalili mojawapo anazopata mama mjamzito hasa katika kipindi cha mwanzo. Kupumzika vizuri ni muhimu kwa ajili ya mwili na akili yako mwenyewe. Hakikisha unapata muda mzuri na wa kutosha kupumzika kiasi kwamba mwili wako uwe unahisi uchovu kidogo. Jiweke huru wakati wa kulala. Hakikisha unapumzika pahala pazuri; unaweza kutaka kutumia mito au kitu kingine kama takia ili ujihisi mwepesi.

Uzani sahihi

Unahitajika kuangalia uzani wako kipindi cha ujauzito. Baadhi ya akina mama wanakula chochote na kila kitu pasipo kuhofia kuhusu uzani. Ikiwa ni kawaida kuongezeka uzani wakati wa ujauzito, si vema kiafya kupitiliza viwango. Uzani unaongezeka kwa kula vyakula ambavyo havina msaada mwilini. Mara kwa mara kula mlo sahihi. Unaweza kumhusisha daktari wako ili kupata chaguo bora.

Mazoezi

Mazoezi ni muhimu. Kuna mazoezi maalumu kwa ajili ya wajawazito. Hudhuria darasa la mazoezi ya yoga yaliyoandaliwa kwa ajili ya wajawazito, pata muda wa kukutana na wajawazito wengine na kujifunza na kupata uzoefu. Unaweza pia kumuomba ushauri daktari ni michezo gani unaweza kushiriki.

Epuka michirizi

Akina mama wengi wanalalamika kupata michirizi baada ya kujifungua. Kuwa mwangalifu ili kuepuka hali hii kuanzia kipindi cha ujauzito. Tumia krimu uliyoshauriwa au zinazouzwa kwa ajili ya kuondoa michirizi. Tumia kila siku kuukanda mwili wako. Aghalabu kwa muda mfupi jiepushe na kukimbia au kuruka kama njia ya kuepuka michirizi.

Itunze ngozi yako

Pamoja na yote wakati wa ujauzito, usisahau ngozi yako. Urembo katika kipindi cha ujauzito unahusisha mwonekano wa ngozi. Kutokana na mabadiliko ya homoni kunaweza kuwa na athari katika ngozi yako. Unaweza kutumia bidhaa za kutunza ngozi kwa kuzingatia aina ya ngozi yako, lakini hakikisha hutumii kemikali hatarishi.

Vipodozi

Kutokana na mabadiliko ya homoni, unaweza kupata madoa usoni. Vipodozi ndivyo mkombozi; tena angalia zile bidhaa ambazo hazitumii au hazitokani na kemikali kali.

Pumzika

Mwisho na muhimu zaidi ni; kukumbuka kupumzika. Lala chini kwa muda unapopata nafasi. Pumzisha mwili wako.

Mashirika kutoa mafunzo kuhusu hedhi kwa wavulana

Na DIANA MUTHEU

MASHIRIKA ya kibinafsi katika Kaunti za Mombasa na Kilifi yamependekeza watoto wa kiume wahusishwe katika mafunzo kuhusu hedhi ili kupunguza unyanyapaa katika jamii.

Akisema na Taifa Leo katika mkutano wa kuzungumzia jinsi mashirika hayo yataweza kuunda na kutekeleza sera za usimamizi wa maswala ya hedhi, meneja wa miradi na maswala ya uzazi katika shirika la Dream Achievers Youth Organisation, Bw Gaetano Muganda alisema kuwa swala la afya na hedhi ni la jamii nzima.

“Pakubwa, jamii inakosea kwa kudhania kuwa maswala kuhusu hedhi yanafaa kuelekezewa wanawake pekee. Ni vizuri kujumuisha wanaume na wavulana ili waweze kulielewa swala nzima na pia wawe miongoni mwa watu wanaoleta suluhu kwa changamoto zinazowakumba wasichana na wanawake wanaokosa vifaa muhimu vya kudumisha usafi wakati wa hedhi,” akasema Bw Muganda huku akiongeza kuwa mashirika zaidi ya 10 yaliokuwa katika mkutano huo yatafanya kazi kwa pamoja kuhakikisha kuwa wamefikia malengo yao.

Afisa huyo alitoa maoni kuwa wanaume wakihusihwa na pia kuhamasishwa kuhusu maswala ya hedhi, wataweza kuwa mstari wa mbele kuleta mabadiliko na hata kusaidia katika kupunguza mimba za mapema.

Baadhi ya sababu ambazo zimekuwa zikitajwa na mashirika mbalimbali kama chanzo cha mimba hizo ni ukosefu wa vifaa muhimu vya kutumiwa wakati wa hedhi, ambapo baadhi ya wasichana hujitosa katika ngono ili wapate fedha za kununua bidhaa hizo.

“Wasichana nao wataweza kujivunia swala la hedhi bila ya woga kuwa kutakuweko na aina yeyote ya unyanyapaa,” akasema.

Mshirikishi wa miradi katika shirika la Y-Act ambalo ni tawi katika Shirika la Amref, Bi Joyce Mbuthia alisema kuwa wanaume wengi ndio tegemeo katika familia zao, na hivyo wakihusishwa katika mazungumzo kuhusu hedhi, wataweza kuwasaidia watoto wao wa kike na wake zao pia.

“Nao wavulana shuleni hawatawacheka wasichana ambao huanza kupata hedhi bila kutarajia, bali wataelewa kuwa ni jambo la kawaida msichana au mwanamke kupata hedhi. Pia, watajua la kufanya iwapo dada zao watajikuta katika hali hio bila kutarajia,” akasema Bi Mbuthia.

TAFSIRI NA FAUSTINE NGILA

AFYA: Ngoja ngoja ya miezi tisa kaja na majonzi tele

NA PAULINE ONGAJI

Ni mwezi mmoja sasa tangu kumpoteza mwanawe na Fatuma Ibrahim, 27, bado anauguza jeraha lililotokana na upasuaji aliofanyiwa wakati huo.

Lakini licha ya kuwa kidonda kingali kibichi, hana budi kuendelea na shughuli yake ya kila siku ya uuzaji mboga ama ukipenda mama mboga.

Kwa Bi Ibrahim, Septemba 4, 2020 itasalia daima kwenye kumbukumbu zake.

Matumaini ya mkazi huyu wa eneo la Bura, Hola, Kaunti ya Tana River kwamba ngoja ngoja yake ya miezi tisa ya ujauzito ingemtunuku zawadi ya mtoto, yaligeuka kilio na majonzi tele moyoni.

“Nilianza kukumbwa na uchungu wa uzazi na nikaenda hospitalini. Niligundua kuna tatizo nilipoumwa kwa muda mrefu sana,” aeleza.

Alipofika hospitalini, kwa saa kadhaa madaktari walishindwa kumzalisha, suala ambalo hatimaye liliwalazimu kumrarua ukeni katika harakati za kumuondoa mtoto ambaye alikuwa amefika kwenye lango la uzazi tayari kutoka.

“Naam niliraruliwa ukeni na mtoto kuondolewa, lakini kwa bahati mbaya alifariki saa moja baadaye. Kulingana na madaktari, mtoto huyo alikuwa amekawia sana kwenye lango la uzazi, akakosa hewa na alikuwa amechoka pia,” aeleza.

Ni tukio lililomsababisha Bi Ibrahim kuvuja damu nyingi na hata kuzimia kwa saa kadhaa pindi baada ya kujifungua.

Haya sio masaibu ya kwanza ya aina hii kumkumba Bi Ibrahim. Mama huyu wa watoto watatu, amekuwa na shida ya kujifungua kila wakati.

Ni shida aliyokumbana nayo mwanzoni miaka 12 iliyopita akijifungua mtoto wake wa kwanza.

“Nakumbuka nilikumbwa na uchungu wa uzazi kwa siku saba ambapo hatimaye nilipojifungua, tayari mtoto alikuwa amechoka na alipozaliwa ikathibitishwa baadaye kwamba alikuwa na utindio wa ubongo (cerebral palsy),” aeleza.

Hii ndio hatima ya wanawake wengi katika jamii nyingi ambazo bado zinahimiza desturi ya ukeketaji katika Kaunti ya Tana River.

“Ukitembea katika kila boma kijijini humu, lazima ukumbane na hadithi ya kutisha kumhusu mwanamke aliyejifungua. Yaweza kuwa ni mama aliyefariki akijifungua, aliyempoteza mwanawe wakati wa kujifungua, au aliyepata nasuri ya uzazi kutokana na matatizo ya kujifungua,” aeleza.

Bi Ibrahim anatoka katika jamii ya Wardey ambayo bado inaendeleza utamaduni huu.

Ukeketaji

Jamii hutekeleza ukeketaji wa aina ya tatu yaani infibulation, ambapo sehemu zote zinazounda uke ikiwa ni pamoja na kinembe, mdomo wa uke na mrija wa mkojo (urethra), hukatwa na kuondolewa kabisa kabla ya sehemu iliyoachwa wazi kuzibwa na kuacha nafasi ndogo ya kupitisha mkojo na damu ya hedhi.

Ni shughuli inayosababisha uchungu usiomithilika sio tu wakati huo wa kukeketwa, bali pia baadaye wakati msichana anapoanza kushuhudia hedhi au wakati wa tendo la ndoa.

“Shimo linaloachwa huwa ndogo sana ambapo lazima lipanuliwe tena kwa kukatwa kwa wembe au kisu, ili mwanamume aweze kupenya wakati wa tendo la ndoa,” aeleza Nastehe Abubakar, mwanaharakati dhidi ya ukeketaji na mratibu wa chama cha Dayaa Women Group.

Hata hivyo ni madhara ya afya kwa mama na mtoto wakati wa kujifungua ndio yameonekana kuwa mabaya zaidi kutokana na ukeketaji.

Kulingana na Dkt Oscar Endekwa, Mkurugenzi wa masuala ya afya katika Kaunti ya Tana River, mambo huwa mabaya hata zaidi wakati wa kujifungua ambapo lazima uke ukatwe tena, suala ambalo laweza msababishia mama na mtoto matatizo ya kiafya wakati huu,” aeleza.

“Wakati wa uchungu wa uzazi, jukumu la daktari ni kumkagua mama na mtoto. Ukaguzi huu hufanyika hasa kupitia lango la uzazi, na ikiwa sehemu hii imezibwa kutokana na ukeketaji, basi inakuwa vigumu kufanya hivyo,” aeleza.

Pia, Dkt Endekwa asema kutokana na sababu kwamba lango la uzazi limezibwa, kuna uwezekano mkubwa wa sehemu hii kuraruka, na hivyo kusababisha maumivu makuu wakati wa kujifungua.

Kulingana na Bi Abubakar, ni sababu hii ambayo imefanya wanawake wengi katika eneo hili kuhofia kwenda hospitalini wanapotaka kujifungua. “Wengi wanahofia kwamba wakienda hospitalini, madaktari watalazimika kurarua uke kwa makasi, kumtoa mtoto kisha kushona tena. Hii husababisha maumivu ambayo hutisha hata zaidi wakati wa kujifungua mtoto mwingine, kwani jeraha hilo litakatwa tena,” aeleza.

“Wengi wanaonelea afadhali kwenda kwa mkunga wa kienyeji kukatwa sehemu hii kwa wembe na kuzibwa kwa njia za kiasili, ambapo wakati wa kujifungua kwa mara nyingine, hatalazimika kushonwa,” aongeza.

Ni dhana ambayo hata hivyo imekuwa na madhara mengi kwa akina mama wa sehemu hii, ambapo hofu hii yao mara nyingi imewasababisha kufika hospitalini wakiwa wamechelewa.

Kulingana na Dkt Endekwa, ni 50% pekee ya akina mama eneo hili wanaotumia huduma za mhudumu wa kiafya aliyehitimu wakati wa kujifungua, huku wengi wakiamua kujifungua mikononi mwa wakunga wa kienyeji.

Dkt Endekwa asema kwamba wengi wa akina mama huvumilia maumivu wakiwa nyumbani na wanapozidiwa na kuamua kwenda hospitalini, tayari afya ya mama na mtoto huwa hatarini.

“Kwa yule ambaye ashajifungua na kukatwa, kuna hatari ya maambukizi kwani vifaa vilivyotumika kufanya kazi hii sio vya kitaalamu na havijatibiwa. Aidha lazima majeraha hayo yashughulikiwe na kutibiwa kitaalamu, shughuli ambayo yaweza fanywa tu hospitalini” anasema.

Pia, Dkt Endekwa asema kwamba hatari kubwa hapa ni kwamba mama atavuja damu nyingi, kichocheo kikuu cha vifo vya akina mama wakati wa kujifungua,” aeleza.

Kulingana na Shirika la Afya Duniani, idadi ya wanawake wanaofariki kutokana na matatizo ya kujifungua, iko juu katika mataifa ambapo bado ukeketaji unaendelezwa.

Kwa mfano, kwa mujibu wa ripoti ya kiafya iliyochapishwa miaka miwili iliyopita, eneo la Mandera lilikuwa na idadi kubwa ya vifo vya akina mama kutokana na matatizo wakati wa kujifungua, kuliko sehemu yoyote nyingine ulimwenguni.

Vifo

Uchunguzi wa kiafya ya KDHS; KNBS and ICF Macro uliozinduliwa mwaka wa 2010 ulionyesha kwamba bado idadi ya wanawake wanaofariki wakati wa ujauzito na kujifungua kutokana na sababu ambazo zaweza zuiwa kama vile njia ya uzazi kuziba, tatizo ambalo hasa husababishwa na ukeketaji, ingali iko juu.

Lakini kando na matatizo wakati wa kujifungua, Dkt Endekwa asema kwamba, kuna matatizo mengine ya kiafya yanayotokana na utamaduni huu.

Vile vile asema matatizo mengine ya uzazi yanayotokana na ukeketaji yanayoshuhudiwa sana sehemu hii ni kama vile nasuri ya uzazi au mtoto kukumbwa na utindio wa ubongo.

“Wakati wa kujifungua, sharti kibofu kiondolewe mkojo ambapo ikiwa mwanamke amefanyiwa ukeketaji wa aina ya tatu, inakuwa vigumu kufikia mrija wa mkojo, ambapo mwanamke atakumbwa na uchungu wa uzazi akiwa na mkojo. Hali hii inaunda mazingira mwafaka kwa nasuri ya uzazi kutokea,” aeleza.

Wakati huo huo, Dkt Endekwa anasema kwamba suala la unyanyapaa katika eneo hili, limetatiza juhudi za kutambua na kudhibiti mapema nasuri ya uzazi na utindio wa ubongo.

“Pia, kuna wanawake kutoka vijiji vya mbali ambao hawawezi fika hospitalini mapema. Na kuna wahusika wanaojificha na kuficha watoto, na kutatiza juhudi za kakabiliana na tatizo hili,” asema.

Utatupwa ndani miezi 6 ukinaswa ukitema mate ovyo jijini Nairobi

COLLINS OMULO na JAMES MURIMI

MTU yeyote atakayepatikana akitema mate kwenye barabara ama kupenga kamasi bila kutumia kitambaa jijini Nairobi, atahukumiwa kifungo cha miezi sita gerezani au kutozwa faini ya Sh10,000.

Kwa mujibu wa mswada uliowasilishwa katika Bunge la Kaunti ya Nairobi, adhabu kama hiyo itapewa yeyote atakayebainika kushiriki ukahaba.

Mswada huo, ambao uko katika awamu ya kwanza, unalenga kuchukua mahali pa sheria za jiji la Nairobi, ambazo zilipitwa na wakati baada ya mfumo wa ugatuzi kuanza kutekelezwa.

Mswada huo umewasilishwa na diwani wa wadi ya Riruta, James Kiriba.

Wale ambao watapatikana wakiendesha magari au pikipiki kwenye vijia vilivyotengewa watumiaji miguu pia wataadhibiwa.

Kwenda haja kubwa ama ndogo kwenye barabara za jiji ama maeneo ya umma, kuwasha moto kwenye barabara za umma ama za jiji bila ruhusa ya Katibu wa Kaunti pia kutachukuliwa kuwa hatia.

Makosa mengine yaliyoorodheshwa na mswada huo ni kuacha mbwa ovyo kwenye barabara, kuosha ama kurekebisha gari kwenye barabara za jiji, kuvuta sigara kwenye maeneo ya umma na utingo kuwaita abiria kuabiri magari yao.

Kwa mujibu wa sheria hiyo, mtu ataruhusiwa kutengenezea gari lake barabarani tu ikiwa kuna hali ya dharura.

Kuchuuza, kuuza, kusambaza ama kutangaza maandishi yoyoye ama hafla katika barabara ya umma, kupiga kelele ama kutumia kengele, spika ama chombo chochote kile cha kupaaza sauti ama kuendesha gari ili kutangaza bidhaa bila kibali pia kumeorodheshwa kama kosa.

Hili pia litajumuisha kushiriki michezo kwa namna ambapo mtu anaweza kuharibu mali ama kusababisha majeraha.

Atakayefanya kosa lolote lililoorodheshwa hapo juu atakuwa kwenye hatari ya kuhukumiwa miezi sita gerezani, kupigwa faini ya Sh10,000 ama kupewa adhabu zote mbili.

Katika Kaunti ya Laikipia, yeyote atakayepatikana akienda haja ndogo, kutema mate ama kutupa taka katika maeneo ya umma atatozwa faini ya Sh5,000 ikiwa madiwani wataupitisha mswada huo.

Mswada unalenga kuhimiza umma kutilia maanani uhifadhi wa mazingira. Unaeleza kwamba yeyote anayepatikana akitupa vifaa vya ujenzi ovyo atatozwa faini ya Sh10,000.

“Atakayepatikana akitupa vifaa vya ujenzi kama mchanga, mawe ya kujengea ama kifaa kingine chochote cha ujenzi atapigwa faini ya Sh10,000,” unaeleza mswada ambao ushawasilishwa kwa Kamati ya Bunge kuhusu Fedha na Mipango.

Kwa mujibu wa kamati hiyo inayoongozwa na diwani Joseph Kiguru wa Wadi ya Igwamiti, mswada huo unalenga kuwaadhibu wale ambao hawatazingatia kanuni hizo.

“Mswada unalenga kuongeza mapato ya kaunti,” ikaeleza kamati.

Wale watakaopatikana wakipiga kelele ovyo kwa umma watatozwa faini ya Sh10,000.

“Hakuna yeyote atakayeruhusiwa kuwapigia wananchi kelele ovyo ikiwa hajapewa kibali maalum na idara husika kwenye kaunti,” unaeleza mswada.

“Yeyote atakayekiuka masharti hayo atatozwa faini ya Sh10,000,” unaeleza.

Mswada pia umeipa mamlaka Bodi ya Kukusanya Mapato ya Kaunti kuzikagua biashara zote kubaini ikiwa zimetimiza kanuni hizo.

Yeyote atakayeizuia kufanya ukaguzi kwenye biashara yake atatozwa faini ya Sh100,000.

Wakazi wa Marakwet waomboleza Padre Reinhard Bottner aliyewaletea ‘mwanga’ wa elimu, imani ya dini na huduma za afya

Na EVANS KIPKURA

PADRE raia wa Ujerumani, Reinhard Bottner alipotumwa Kenya kwa shughuli za kimisheni mnamo 1975, alijipata katika eneo la Embotut, Marakwet Mashariki.

Eneo hilo lilikuwa halipitiki kirahisi na visa vya upashaji tohara kwa wasichana vilikuwa vya kiwango cha juu.

Hizi ni miongoni mwa changamoto ambazo Bottner, 46, alilazimika kupitia katika kibarua chake cha kwanza cha kimataifa nje ya bara Ulaya.

Kwa kipindi cha miongo mitano, Bottner alikusanya rasilmali muhimu kutoka kwa viongozi na mashirika mbalimbali ya kidini ili kutoa majukwaa muhimu kwa masuala ya elimu, kilimo, ufugaji na ujenzi wa miundo-msingi muhimu.

Kasisi Bottner aliaga dunia katika Hospitali ya Mater Misercordiae, Nairobi mnamo Septemba 29, 2020 akiwa na umri wa miaka 86. Hadi kifo chake, alikuwa amelezwa katika hospitali hiyo kwa kipindi cha wiki mbili.

Kwa mujibu wa taarifa Kasisi Mkuu William Kipkemboi Kosgey wa Dayosisi ya Kanisa Katoliki la Eldoret, mipango ya mazishi ya Bottner inaendelea kwa sasa.

“Tunatoa rambirambi zetu na kuombea familia nzima ya wamisheni wa Benedictine. Tunaomba Mola aifariji familia ya Bottner katika kipindi hiki kigumu,” ikasema sehemu ya taarifa hiyo.

Licha ya kujihusisha na masuala mengi ya kimisheni, ambacho Kasisi Bottner anakumbukwa kwayo katika eneo la Marakwet Mashariki na Keiyo Kusini ni ukubwa wa mchango wake katika sekta mbalimbali za maendeleo.

Mengi ya makanisa ambayo yamejengwa na Kasisi Bottner katka maeneo hayo kwa sasa ni vivutio vya utalii huku Kanisa la St Kizito Wewo Embobut likisifiwa sana kwa upekee wa mtindo wa kisanaa uliotumiwa katika ujenzi wake. Kanisa hilo limejengwa kwa umbo la njiwa.

Bottner alitumia pia mtindo wa usanifu majengo uliotamalaki ujenzi wa makanisa nchini Ujerumani katika miaka ya 1970 kujenga makanisa Katoliki ya Lemeiywo, Korou, Kapchebau, St Michael na Kamwosor.

Mchango wa Bottner pia ulikuwa mkubwa katika ujenzi wa Hospitali ya St Michael na Shule ya Msingi na ya Upili ya St Michael Embobut.

Julius Belator, ambaye alikuwa msaidizi na mpishi wa Kasisi Bottner kwa kipindi cha miaka 40 alisema amepoteza mtu ambaye alikuwa sehemu ya maisha yake duniani.

IMETAFSIRIWA NA: CHRIS ADUNGO

Amina Abdalla: Tegemeo la watu wenye akili punguani Mombasa

Na DIANA MUTHEU

“KILA ‘mwendawazimu’ ana historia ndefu ya mambo yaliyopelekea hali yake,” anasema Bi Amina Abdalla, mwanamke ngangari kutoka kaunti ya Mombasa ambaye amejitolea kuwatunza na kuwajali wagonjwa wa akili, kupitia shirika lake la Women Empowerment Network.

Kwa miaka tisa sasa, Bi Amina amekuwa akizunguka katika mitaa tofauti katika kaunti hiyo, akiwakusanya wagonjwa hao na kuwapeleka katika kituo spesheli cha kuwahudumia cha Portreitz, Mombasa.

Pia, amekuwa akijitolea kugharamia matibabu yao, na baadhi yao wamepona na kurejeshwa makwao ambapo wengine walitokea sehemu kama vile Garissa, Somalia, Thika, Kwale, Kilifi, Machakos miongoni mwa sehemu zingine.

Anasema kuwa swala la kuwaona wagonjwa hao wakiishi bila hadhi yoyote mitaani, wakila vya pipani na kuogopwa na wanajamii, aliamua kuwa tegemeo lao.

“Nilianza programu hii mwaka wa 2011 kwa kuwa niliwaona watu hao wakiwa barabarani wakirandaranda ovyo bila chakula na maji. Baadhi ya wanawake walikuwa wanatembea uchi, jambo ambalo ni la kuabisha. Nilijiuliza ni mambo mangapi yanawakumba wagonjwa hao haswa wanawake hao na nikaamua kutafuta suluhu,” akasema Amina ambaye ni mkurugenzi katika shirika la Coast Development Authority.

Akisimulia safari yake katika programu hii kwa Taifa Leo Dijitali, Amina alisema kuwa mara ya kwanza kabisa kuianza programu ile, aliwakusanya wagonjwa wa akili saba na kuwapeleka katika kituo hicho cha Portreitz.

Zaidi, alinunua magodoro, vyakula na vitu vingine muhimu ambavyo wangehitaji pale, ndipo wagonjwa hao wakakubaliwa katika hospitali hiyo.

“Sikutaka wagonjwa hao waonekane kama mzigo kwa wahudumu katika hospitali hiyo, na nilichukua jukumu la kuhakikisha wanapata kila kitu walichohitaji,” akasema.

Bi Amina Abdalla akizungumza na waandishi wa habari katika Chuo Anwai cha Kenya, Mombasa. PICHA/ DIANA MUTHEU

Hata hivyo, anasema kuwa watu wengi hawakuwa na imani kuwa angeiweza kazi hiyo.

“Watu wengi waliniambia kuwa sitaiweza kazi hiyo lakini sikuwasikiliza kwani nilikuwa nimeandaa roho yangu kujitosa katika programu hiyo. Wengine walisema kuwa naendeleza siasa zangu kupitia programu hiyo lakini sikuwasikiliza kamwe,” akasema Amina.

Amina alisema kuwa baada ya miezi sita, miongoni mwa wagonjwa hao saba, wanne walipona na aliwarejesha makwao na kuwaanzishia biashara zao.

Hata hivyo, alisema kuwa alipata changamoto kwani baadhi ya wagonjwa waliopona na kurejeshwa nyumbani walirudi katika hali yao ya hapo awali, kwa sababu familia zao hazikufuata maagizo ya kuwapa lishe bora na dawa kwa wakati ufaao.

Lakini, hakufa moyo bali alijaribu tena na hadi wa leo wagonjwa 95 wameweza kufaidika kupitia shirika lake.

“Ili wagonjwa hawa wapone haraka, wanahitaji kuonyeshwa upendo, kutunzwa na pia wanaowahudumia wawe na subira,” akasema.

Kwa kawaida, gumzo mtaani ni kuwa wagonjwa wengi wa akili ni watu ambao walifanya jambo mbaya, ndipo wakaweza kufanyiwa uganga au ushirikina wa aina tofauti.

Kulingana na Bi Amina, hali hiyo ni ugonjwa kama vile magonjwa ya kawaida, na inaweza kutibiwa na mtu akarejea katika hali yake ya kawaida.

Alitaja baadhi ya sababu zinazopelekea mgonjwa kupata maradhi hayo kama kusongwa na mawazo na matumizi ya dawa za kulevya kupita kiasi.

“Mmoja wa wagonjwa ambaye nishawahi kumhudumia alikuwa ni daktari ambaye alisongwa na mawazo baada ya mipango yake ya kuendeleza masomo yake nchini Cairo iliambulia patupu na mwingine ni mzee aliyetengana na mkewe ambaye walikuwa katika ndoa kwa muda mrefu” akasema.

Mwaka huu mnamo Februari, Amina aliamua kutafuta makazi ambapo wagonjwa hao watashughulikiwa vilivyo kwa muda mrefu.

“Kuna wagonjwa tumekuwa tukiwahudumia kwa miaka miwili, na wanaendelea vizuri kiafya. Watu hawa wanahitaji matibabu, kuonyeshwa upendo, kupewa ushauri kwa muda mrefu, ili waweze kupona kikamilifu. Pia, wanahitaji kukubaliwa katika jamii,” akasema Bi Amina.

Janga la corona lilipoikumba nchi yetu, Bi Amina alijitahidi kuwasaidia wagonjwa 55 wa akili manake serikali ilikuwa imewatenga katika miradi yao ya kutoa vyakula vya msaada, barakoa n ahata vifaa vingine vya kudumiasha usafi kama vile sabuni na maji safi.

Bi Amina aliwatafutia wagonjwa hao maeneo salama katika Chuo Anwai cha Kenya, Mombasa, na hata kuiomba kaunti iwapime kuthibitisha iwapo walikuwa na corona.

Hii ni kwa sababu wengi wao walikuwa wamechukuliwa kutoka eneo la Old Town, ambapo marufuku ya kuingia na kutoka ilikuwa imetangazwa na Rais Uhuru Kenyatta kwa kuwa watu wengi pale walikuwa wameambukizwa virusi vya corona.

Watano kati ya wagonjwa hao walipatwa na maradhi ya Covid-19, ikiwemo mzee mmoja mwenye miaka 85.

Aliongeza kuwa wagonjwa wengi wa akili ambao amewahi kuwahudumia katika programu hiyo huwa kati ya miaka 29 na zaidi.

“Tulishirikiana na kaunti na nilipata madaktari, wauguzi na dawa. Wagonjwa hao walikuwa wanawekwa katika vyumba tofauti punde tu walipofika katika kituo hicho,hadi pale daktari alisema kuwa wako salama kujumuika na wenzao. Waliopatikana na virusi vya corona walitengwa hadi pale walipopona,” akasema Bi Amina.

Baada ya tangazo kutolewa kuwa shule zingefunguliwa, Bi Amina aliwahamisha wagonjwa wale hadi eneo la Shanzu ambapo wanatunzwa na wafanyikazi nane ambao wamejifunza kuishi nao kadri wanapoendelea kuwahudumia, pamoja na vijana wanne waliojitolea baada ya kupona maradhi ya akili.

“Vijana hao hutusaidia kuwalisha, kuwaogesha, kuwapa dawa na hata kucheza na wagonjwa,” akasema Bi Amina huku akieleza kuwa kuwatunza wagonjwa hawa nyumbani ndilo jambo muhimu zaidi.

“Wagonjwa wengi waliopona tuliwaregesha makwao, wengine sita watapata mafunzo ya kinyozi na kusafisha magari na watakapohitimu, tutawafungulia biashara hizo,” akasema.

Amina alisema kuwa anawategemea marafiki na wafadhili kuendeleza programu hiyo. Aliongeza kuwa kila mwezi anatumia Sh350,000 kugharamia kodi ya nyumba, chakula, dawa na mahitaji mengine ya wagonjwa hao.

“Familia yangu imekubali kuwa wagonjwa hawa wanatuhitaji. Mara ya kwanza nilipata changamoto kwa kuwa nilijishughulisha na wagonjwa mara kwa mara na wagonjwa hao, na kukaa na familia kwa muda mfupi tu. Kufikia leo, watoto wangu huja katika makazi ya wagonjwa wale, wakawalisha na kuwapa dawa,” akasema.

Bi Amina anasema kuwa angependa jamii iwache tabia ya kuwatenga wagonjwa hao na kufahamu kuwa maradhi ya akili yanaweza kutibiwa na mtu akapona.

“Pia, nawaomba wawe mstari wa mbele kuwakamata wagonjwa hawa na kuwapeleka hospitalini. Pia, ningeomba serikali itenge fedha kwa mashirika yanayowasaidia wagonjwa hao,” akasema Bi Amina.

Alisema kuwa tayari wametafuta ardhi eneo la Miritini ambapo watajenga makazi ya watu wenye maradhi ya akili ambapo wagonjwa 100 wanaweza kutunzwa.

“Tunaomba wasamaria wema wajitokeze na kusaidia programu yetu,” akasema huku akiongeza kuwa kuwasaidia wagonjwa wa akili kumemfundisha asiwe mwepesi wa kuhukumu, kila binadamu ana haki na pia imemfunza kuwa mvumilivu.

Aanzisha hazina ya kusaidia wanaougua kifafa

Na PAULINE ONGAJI

Baada ya kukumbwa na kifafa, ameamua kusaidia wengine wanaokumbwa na hali sawa na yake. Hii ni hadithi yake Bw Fredrick Kiserem, mwathriwa wa maradhi ya kifafa, na mwanzilishi wa Hazina ya Kiserem Epilepsy Foundation.

Hazina hii inayoendeshwa katika maeneo ya Mwihoko, Kaunti ya Kiambu, na Lwandeti, Kaunti ya Kakamega , imekuwa hifadhi kwa waathiriwa wa maradhi haya.

“Hasa mradi huu unanuia kuwapa waathiriwa wa maradhi haya, vile vile wengine wenye matatizo ya kiakili, uwezo wa kujitegemea hasa kiuchumi, ambapo tuna chuo cha mafunzo ya ujuzi kama vile ushonaji nguo na useremala, miongoni mwa nyingine,” asema.

Aidha, mradi huu umekuwa ukiangazia mahitaji ya waathiriwa wa kifafa ambapo linawapa sauti ya kuzungumzia wazi masaibu yao, na hivyo kuleta mabadiliko.

“Pia, tumekuwa tukijitahidi kuhamasisha jamii kuhusiana na hali hii hasa ikizingatiwa kwamba waathiriwa wengi hukumbwa na tatizo la kutengwa na unyanyapaa,” aeleeza Bw Kiserem.

Bw Kiserem hakuzaliwa akiwa na hali hii. Masaibu yake yalianza mwaka wa 2011 ambapo alianza kshuhudia mashambulio ya kifafa.

 “Wakati huo nilikuwa nafanya kazi nchini Iraq, na sikujua nini hasa kilichokuwa kikisababisha hali hii. Hata hivyo baada ya kuenda hospitalini, nilifanyiwa uchunguzi, na kutambuliwa kuugua kifafa ambapo  nilianza matibabu mara moja,” aeleza.

Dawa alizokuwa akitumia zilisaidia kudhibiti hali hii ambapo aliendelea kufanya kazi nchini humo kwa miaka miwili zaidi.

Hata hivyo, mwaka wa 2015 hali yake ilizidi kuwa mbaya na akalazimika kurejea nyumbani. “Mambo yaliendelea kuwa mabaya hata zaidi nikiwa nyumbani, ambapo mwaka wa 2016 shambulio la kifafa lilinisababishia majeraha mabaya kiasi cha kunifanya nilazwe hospitalini,” aeleza.

Akiwa hospitalini, gharama ya matibabu ilikuwa zaidi ya Sh 300,000, na anasema ni hapa ndipo alipopata maono ya kuangazia suala hili.

“Nilijiona kubahatika kuwa na pesa za kulipia matibabu hayo, ambapo nilijiuliza je hali ilikuwa vipi kwa wale wasio na uwezo huu? Na hapo nikajituma kuanza kuleta mabadiliko katika nyanja hii,” aeleza.

Japo kwa sasa hali yake imeimarika kabisa kutokana na dawa anazotumia, Bw Kiserem asema kwamba masaibu aliyopitia kutokana na maradhi haya yalikuwa mengi.

“Nakumbuka nikitemwa na mchumba wangu kutokana na hali yangu. Wajua kuna baadhi ya watu wanaohusisha hali hii na ushirikina ambapo kila siku wanawatenga waathiriwa wa maradhi haya.”

Kulingana na Bw Kiserem, umewadia wakati kwa jamii kutambua kwamba hali hii sio mwisho wa maisha. “Kwa kuhakikisha kwamba waathiriwa wanapokea matibabu vilivyo na wanapata usaidizi wa kimaisha, tunaweza ishi maisha ya kawaida,” aeleza.

Msanii atumia muziki kutuliza wagonjwa hospitalini

Na PAULINE ONGAJI

Anatumia muziki kuwatuliza wagonjwa waliolazwa hospitalini. Ni kazi ambayo Bw Willis Ochieng amekuwa akifanya kwa zaidi ya miaka mitatu sasa.

Kwa muda huu, Fololo, kama anavyojulikana kwenye ulingo wa muziki, amekuwa mmoja wa kikundi cha wanamuziki watano ambao wamekuwa wakitumbuiza wagonjwa katika hospitali ya Mater, jijini Nairobi, kila siku kati ya saa nne asubuhi na saa nane adhuhuri.

“Kwa kawaida shughuli hii huchukua kati ya saa tatu na nne kila siku, ambapo sisi huwatumbuiza wagonjwa katika vyumba tofauti vya wagonjwa, vile vile wafanyakazi wa hospitalini,” aongeza.

Tiba hii sio tu ya wagonjwa, bali pia kwa wafanyakazi na wateja ambao wameleta wagonjwa hospitalini. “Hii inasaidia kutuliza mazingira ya hospitalini, na hivyo kuwapa wahusika kumbukumbu nzuri,” asema.

Kwa kawaida wao hucheza mchanganyiko wa muziki wa injili, pop na rhumba miongoni mwa aina zingine za muziki.

Kulingana naye kwa kawaida wao huhudumia wagonjwa 50, huku wakati mwingine idadi hiyo ikiongezeka na kufikia 70 na kujumuisha pia wale ambao bado hawajalazwa.

Na anasema kwamba kuna mara nyingi ambapo huduma hii imesaidia wagonjwa kupata nafuu. “Kwa mfano, mwaka jana nakumbuka kulikuwa na mwanajeshi mmoja kutoka nchini Sierra Leone ambaye baada ya kumuimbia kwa siku kadhaa, alianza kuonyesha ishara ya kuimarika kiafya, na baadaye akapona,” asema.

Bwana huyu alitambulishwa katika shughuli hii ya tiba kutumia muziki mwaka wa 2017 kupitia rafiki yake. “Niliona kama mbinu mwafaka ya kutumia kipaji changu kusaidia watu walio na matatizo mbalimbali ya kiafya,” asema.

Mwaka mmoja baadaye alihitimu kama mhudumu wa kutumia tiba ya muziki na kupewa hati na kikundi cha madaktari kutoka nchini Amerika, waliokuwa wakifanya mradi sawa na huu nchini humo.

Mafunzo hayo ya wiki mbili yalihusisha ujuzi maalum uliohitajika kufanya kazi na wagonjwa tofauti, kama vile watoto walio na mahitaji maalum na watu waliolazwa katika vyumba vya wagonjwa mahututi.

Ni mradi ambao ni wa kujitolea kumaanisha kwamba hauna malipo, ila tu kwa marupurupu kidogo. Lakini licha ya haya, anasema kwamba inaridhisha kwamba anatumia kipaji chake kuwasaidia wagonjwa.

ONGAJI: Mashirika yameanika udhaifu wa sekta ya afya Afrika

Na PAULINE ONGAJI

Hivi majuzi kuliibuka mtafaruku baina ya mashirika mawili yasiyo ya kiserikali nchini, kuhusu udhibiti wa fedha zilizokuwa zimetolewa kwa minajili ya matibabu ya maradhi kadhaa nchini.

Uhasama huo ulikuwa kuhusu pesa za msaada zilizokuwa zimetolewa na shirika la Global Fund katika vita dhidi ya maradhi ya Ukimwi, malaria na kifua kikuu.

Ni suala lililosababisha shirika hilo kusitisha matumizi ya kitita hicho cha zaidi ya Sh12 bilioni, huku hazina hiyo ikilalamikia shughuli ya uteuzi wa shirika ambalo mwanzoni lilikuwa limepewa mamlaka ya udhibiti wa fedha hizo.

Tukio hili linaonyesha jinsi pesa za msaada hasa katika sekta ya afya sio tu nchini bali barani, zina thamani sana kiwango cha kusababisha uhasama mkali baina ya mashirika ambayo lengo lao kuu ni kushughulikia waathiriwa wa maradhi husika.

Kinachohuzunisha zaidi ni kwamba hili ni donda sugu katika sekta za matibabu katika mataifa mengi barani zinazoendeshwa na mashirika yasiyo ya kiserikali, tofauti na nchi zingine ambapo hili ni jukumu la serikali.

Kumbuka kwamba mashirika haya hasa hutegemea ufadhili na misaada kutoka ng’ambo, ambapo swali kuu ni je serikali kwa upande wake ina mfumo au uwezo wa kukagua matumizi ya fedha hizi?

Kunao wanaoohoji kwamba suluhisho ni kwa mataifa ya Afrika kuwekeza zaidi katika sekta za afya na matibabu, lakini hii itawezekanaje ikiwa mataifa ya Afrika hayako tayari kudhibiti sekta hii?

Kwa mfano, mwaka wa 2001, kupitia Azimio la Abuja (Abuja Declaration), nchi nyingi ziliahidi kutumia angaa asilimia 15 ya bajeti ya mwaka katika masuala ya kiafya, ilhali ni chache ambazo zilitimiza lengo hili.

Mwaka wa 2018, Andreas Seiter, kiongozi wa sekta ya kibinafsi katika masuala ya afya, lishe na idadi ya watu kwenye Benki ya Dunia alisema kwamba, kwa kawaida mataifa ya Afrika hayatengei sekta ya afya pesa za kutosha.

Aidha, kulingana na Seiter, hata ufadhili huu unapotolewa, mataifa mengi ya Afrika yamekuwa na tabia ya kuelekeza fedha zilizokuwa zimetengewa matumizi ya afya, katika sekta zingine.

Hii inamaanisha kwamba asilimia kubwa ya bajeti ya afya katika mataifa haya inaachiwa ufadhili wa kutoka nje. Ni suala linaloachia mashirika yasiyo ya kiserikali mwanya wa kudhibiti sekta hii, na hivyo kuhatarisha afya ya wagonjwa tukio la aina hii linapoibuka.

Mwanamume shupavu anayehamasisha umma kuhusu maswala ya hedhi

Na DIANA MUTHEU

KULINGANA na ripoti ya Benki ya Dunia ya mwaka wa 2018, wasichana 500 milioni ulimwenguni kote hawakuweza kupata vifaa vya kuwasaidia kuzingatia usafi wakati wa hedhi, na walilazimika kutumia matambara, majani, karatasi za chooni na hata blanketi.

Ripoti ya Wizara ya Afya nchini ya 2019 inasema kuwa swala la afya ya hedhi limebakia kuwa changamoto kwa wanawake na wasichana wa kipato cha chini.

“Ripoti za uchambuzi wa hali zinaonyesha kuwa wasichana wanakabiliwa na changamoto kila mwezi, na asilimia 58 ya wasichana vijijini na asilimia 53 ya wasichana katika maeneo ya mijini hawawezi kumudu usafi wakati wa hedhi,” ilisema sehemu ya ripoti hiyo.

Katika kaunti ya Mombasa, changamoto bado ni hizo hizo. Hata hivyo, mwanaume mmoja katika kaunti hiyo ameanza kampeni za kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa kuipa swala la afya ya hedhi kipaumbele, kinyume na hali ya kawaida ambapo wanawake ndio huwa mstari wa mbele kupigia debe swaa hilo manake linawahusu.

James Atito, 28, anayejitambulisha kama “The Period Man” alisema kuwa swala la hedhi ni la jamii nzima, na wanaume wanafaa kuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa wasichana na hata kina mama wanapata sodo za kutosha.

Hata amewahi kusafiriUbelgiji kuhutubia umati wa wanaume kuhusu maswala ya hedhi na wanachohitajika kufanya.

Bw Atito ni meneja wa maswala ya fedha katika shirika la kibinafsi la Stretchers Youth lakini pia ni mwanzilishi wa kampeni moja ya kuwahamasisha wanaume na jamii nzima kuhusu umuhimu wa kudumisha usafi wakati wa hedhi.

“Nilijitosa katika uwanja wa kuhamasisha jamii kuhusu kuwapa wasichana na kina mama visodo kwa kuwa kuna mashirika kadhaa yanayotoa msaada huo. Lakini tumeanza kuwanunulia sodo, karatasi za chooni na bidhaa zingine muhimu zinazohitajika, tukiwa katika mikutano na wasichana hao baada ya kugundua kuwa kuna wale ambao hawana uwezo wa kuzinunua,” akasema Bw Atito.

Akizungumza na Taifa Leo Dijitali, kijana huyo alisema kuwa alijikabidhi jina la utani la “The Period Man” baada ya kutembelea kaunti ya Turkana kuhamasisha wasichana na wanawake kuhusu matumizi ya sodo spesheli zenye umbo la vikombe vinavyotumika wakati wa hedhi (menstrual cup).

“Baada ya kuzungumza na kundi hilo, msichana mmoja alinifuata na kuniuliza kama huwa napata hedhi! Mwanzo, nilicheka, lakini wiki kadhaa baadaye, niliamua kujiita jina hilo kwa kuwa hiyo ndiyo ajenda kuu katika hamasa zangu. Ningependa wanaume wawe mstari wa mbele kuyazungumzia mambo haya na pia kutafuta suluhu za kudumu,” akasema Bw Atito.

‘The Period Man’ akiwapa wasichana visodo. PICHA/ DIANA MUTHEU

Kijana huyu anasema kuwa ilikuwa ni ndoto yake kusomea udaktari lakini kabla ya kujiunga na chuo cha kutoa mafunzo hayo, alifadhiliwa kufanya kozi ya uhandisi katika Chuo cha Ufundi cha Mombasa (TUM).

“Katika mwaka wangu wa tatu chuoni, mfadhili wangu alipata changamoto kunilipia karo. Nilijaribu kufanya kazi kama vile kuchoma kachiri na mihogo, lakini sikuweza kupata fedha za kutosha kukamilisha masomo yangu, na mwaka wa 2014, niliacha masomo hayo na kujihusisha kikamilifu na shughuli katika shirika la Stretchers Youth,” akasema.

Mnamo Januari 2 mwaka huu, Bw Atito alianza kampeni yenye mada “Menforperiods365” katika mtandao wake wa Facebook, akilenga kuelimisha jamii haswa wanaume kuhusu afya wakati wa hedhi.

Katika kampeni hiyo ameweza kupata wafuasi zaidi ya 9,000 katika mtandao huo. Kila siku huwa anaandika ujumbe kuhusu maswala ya hedhi, zikiambatana na picha au video na pia amekuwa akiwauliza wafuasi wake watoe maoni yao kuhusu mada husika.

“Kupata maarifa kuhusu mada hii, nilianza kusoma vitabu, nikazungumza na wataalamu, nikatafuta maarifa zaidi mtandaoni na ripoti za mashirika kama vile Amref, Shirika la Afya Duniani (WHO), Wizara ya Afya,” alisema huku akiongeza kuwa kuna wakati huwa anahisi uvivu kuweka jumbe hizo, lakini wanaomfuatilia humtia moyo aendelee zaidi.

Kufikia Septemba 8, amefikisha siku 251 akiweka jumbe hizo. Lengo lake ni kuhamasisha watu kwa siku 365. PICHA/ DIANA MUTHEU

Pia, ameweza kuwafikia zaidi ya wasichana 500 katika kaunti ya Mombasa na kutoa msaada wa sodo, karatasi za chooni, chupi na sabuni.

Zaidi, ameweza kuwaelekeza wanawake wanne waliokuwa na magonjwa yanayohusiana na uzazi kwa wataalamu kutoka mashirika tofauti.

“Ni huzuni kusikia kina dada zetu wakijihusisha na shughuli kama vile ukahaba ili kupata fedha za kununua sodo. Pia, katika kaunti nyingi, baadhi ya wasichana wamepata mimba za mapema wakiwa katika shughuli za kutafuta bidhaa hizo muhimu kwa maisha ya wanawake,” akasema Bw Atito.

Baadhi ya changamoto ambazo amezitaja ni swala la unyanyapaa unaozingira swala nzima la hedhi na pia mazungumzo kulihusu kuwa mwiko katika jamii.

“Pia, kupata fedha za kununua sodo ni changamoto, imenilazimu nitenge fedha kutoka kwa biashara yangu ya bodaboda. Zaidi, baadhi ya watu katika jamii wamekuwa wakinidhihaki kuwa natafuta sifa na huruma kutoka kwa umma,” akasema.

Mwandani wake, Bw Evans Ouma alisema kuwa wanaume wengi hutengwa katika maswala kuhusu hedhi.

Alisema wanaume wakihusishwa, wataweza kuwaelewa wanawake zaidi na hivyo kuchukua jukumu la kuwalinda.

“Tutajaribu kuwajumuisha wanaume wengi katika kampeni na mikutano yetu. Wanaume wanafaa kuwa mstari wa mbele kuzungumzia swala hili ili kina dada zetu, kina mama na hata shangazi zetu waweze kusaidika,” akasema Bw Ouma huku akiongeza kuwa swala la hedhi linahusu jamii nzima, na wanaume wanafaa kuhusishwa ili kuziba pengo la usawa lililo baina ya jinsia mbili.

Angela Cecilia, 13 alishukuru kupata msaada wa sodo kupitia kampeni hiyo. PICHA/ DIANA MUTHEU

 

“Mamangu alipoteza kazi wakati janga la corona lilipotukumba, na hivyo tulipata changamoto kupata fedha za kununua chakula na hata sodo,” akasema Cecilia.

Mwenzake Beatrice Adhiambo alisema ameweza kujieleza anapopata shida wakati wa hedhi baada ya kuhudhuria mikutano kadhaa iliyofanywa na Bw Atito.

“Hata kama ni mwanaume, ameweza kutueleza mengi kuhusu hedhi ambayo hatukuwa tunayajua,” akasema Adhiambo.

Bw Atito alisema kuwa ameweza kushirikiana na mashirika kama vile Stretchers Youth, Afripads na mashirika mengine ya kijamii kuhamasisha umma na kutoa misaada ya bidhaa muhimu zinazotumika wakati wa hedhi.

Alisema kuwa baada ya kukamilisha kampeni hiyo ya siku 365 atakuwa ameweka msingi thabiti wa kufanya hamasa zingine.

“Mazungumzo kuhusu hedhi yasiwe mwiko kwani ni swala muhimu sana katika maisha ya mwanadamu yeyote kwa kuwa dada zetu wanapata hedhi, pia mama zetu walikosa hedhi na badala yake wakapata mimba ndipo wakatuzaa,” akasisitiza huku akisema changamoto wanazopitia baadhi ya wasichana na kina mama zinampa motisha wa kuendelea na programu hiyo.

‘Wahudumu wa afya Mombasa hawana bima ya afya’

Na WINNIE ATIENO

WAHUDUMU wa afya katika Kaunti ya Mombasa wanafanya kazi bila bima ya afya wakiendelea kuhatarisha maisha yao wanapokabiliana na janga la corona.

Haya yalifichuka kwenye mahojiano kati ya kamati ya bunge la seneti kuhusu corona na vyama vya madaktari na wahudumu wa afya.

Madaktari walifichua namna mwenzao, Dkt Biabu Adam, alikuwa mgonjwa na kulazimika kugharimia matibabu alipolazwa hospitali moja ya mmiliki binafsi.

“Ugonjwa huo ulisababisha nijifungue kwa njia ya upasuaji ya dharura. Nilishangaa kwamba bima yangu ya afya ilikuwa haijalipwa ilhali sikuwa na uwezo wa kusimamia gharama hiyo kwa wakati huo, ” alisema Dkt Adam kwenye barua aliyomwandikia afisa wa afya Dkt Khadija Shikely mnamo Julai.

Baada ya upasuaji huo, daktari huyo ambaye anafanya kazi katika hospitali ya wilaya ya Tudor alipewa bili ya Sh190,000.

Mwezi mmoja baadaye anang’ang’ana kulipa pesa hizo huku wenzake wakiendelea na mchango.

“Alidhania bima yake ya afya itasimamia gharama hiyo lakini tukagundua kaunti ilisitisha malipo. Inasikitisha kuwa madaktari na wahudumu wengine wa afya wanakabiliana na janga hili na hawana bima ya afya,” alisema naibu katibu wa chama cha madaktari nchini tawi la Pwani Dkt Niko Gichana.

Hii ni taswira ambayo inawakumba zaidi ya madaktari 100 na wahudumu wa afya ambao wanalalamika kuwa hawana bima ya afya.

Hata hivyo, serikali ya Kaunti ya Mombasa ilijitetea huku ikiilaumu hazina ya bima ya afya chini NHIF kwa kukataa kuwapa wafanyakazi hao huduma hiyo.

Afisa wa afya ya umma Kaunti ya Mombasa Bi Pauline Oginga akihutubia wahudumu wa afya kwenye uzinduzi wa mafunzo ya namna ya kudhibiti maambukizi ya corona miongoni mwao. Picha/ Winnie Atieno

Walisema NHIF inawalazimu kulipa Sh142 milioni kabla wapewe bima hiyo.

Zaidi ya wahumudu wa afya 42 waliambukizwa virusi hivyo kaunti ya Mombasa.

Gavana Hassan Joho alisema serikali yake ilitafuta njia mbadala kwa kuwapa wafanyakazi hao matibabu ya bure katika hospitali kuu ya Pwani.

“Tumejaribu kukabiliana na swala hili lakini kuna changamoto,” Joho aliiambia kamati hiyo.

Kifafa hakijamzuia kutimiza ndoto yake

Na PAULINE ONGAJI

Licha ya changamoto anazokumbana nazo maishani kama mwathiriwa wa maradhi ya kifafa, kila siku anajizatiti kuishi maisha ya kawaida.

Huo ni uhalisi wa Bi Harriet Nyokabi, 25, mkazi wa mtaa wa Githurai 45, Kaunti ya Nairobi.

Bi Nyokabi ameishi na maradhi haya tokea utotoni, suala ambalo limeathiri maisha yake ya kaiwada.

Amekuwa akikabiliana na kifafa tangu awe na miaka minne baada ya kugongwa na gari. Ni tukio lililomlazimu kulazwa katika chumba cha watu mahututi kwa miezi sita, kabla ya kupona na kuruhusiwa kwenda nyumbani.

Lakini huo haukuwa mwisho wa masaibu yake kwani pindi baadaye, mashambulio ya kifafa yalianza.

“Ni suala lililoathiri pia masomo yangu ambapo nililazimika kuacha shule nikiwa katika darasa la nne kwani mashambulio hayo yalizidi,” aeleza.

Ni suala lililowakosesha amani sio tu wanafunzi, bali pia walimu wake huku jitihada za mamake kumtafutia shule zikigonga mwamba kila alipoeleza kuhusu hali yake.

Haya yote ni kando na matatizo ambayo amekuwa akikumbana nayo kama mwathiriwa wa maradhi ya kifafa ambapo analazimika kumeza tembe saba kila siku ili kjudhibiti hali hii.

Isitoshe, kila siku ni changamoto kwa mama huyu wa watoto wawili kwani anakumbwa na hatari ya kujeruhiwa kutokama na mashambulio ya kila mara, huku maisha yake yakiwa magumu hata zaidi hasa ikizingatiwa kwamba mkono wake wa kushoto umepooza kidogo.

Lakini licha ya hayo, badala ya kukaa kitako na kujionea huruma, Bi Nyokabi amejitahidi kimaisha. Kwa mfano, kwa sasa anamiliki duka la kushona nguo, kazi aliyoanzisha baada ya kupokea cherehani kutoka chuo cha mafunzo ya kiufundi ambapo alikuwa akijifunza.

“Mojawapo ya sababu zilizomfanya kujishindia mtambo huu ni bidii na ukamavu wake katika kipindi chote cha mafunzo kwani hakuwahi kosa chuoni licha ya changamoto za kiafya alizokumbana nazo,” asema Fred Kiserem, mwanzilishi wa chuo cha mafunzo ya kiufundi cha Kiserem Vocational Center.

Kumbuka alipokuwa akipokea mafunzo haya, pia alikuwa akifanya kazi ya kuchuuza matunda, ambapo alilazimika kutembea kwa kilomita kadhaa kila siku kufikishia wateja wake bidhaa hii.

Japo anakiri kwamba kwake, kila siku maisha ni kupambana, anatumai kwamba matatizo hayo hayatakuwa kizingiti katika harakati zake za kutimiza ndoto zake maishani. Ndoto yake ni kuimarisha biashara yake ya nguo na hata wakati mmoja kumiliki duka kubwa la biashara.

“Bila shaka kila siku ni changamoto, lakini watu wanapaswa kuelewa kwamba mimi binadamu kama wengine. Ningependa hadithi yangu iwe ushuhuda kwa kila mmoja anayekumbwa na hali kama yangu,” asema.

Wahudumu wa afya Mombasa watishia kugoma

Na WINNIE ATIENO

WAHUDUMU wa afya katika Kaunti ya Mombasa wametishia kuanza mgomo baridi kufuatia kucheleweshwa kwa mshahara wa Mei.

Madaktari na wauguzi walisema Ijumaa wamekuwa wakipitia hali ngumu kutokana na hali hiyo huku wakiendelea kutoa huduma za afya kwa wakazi wanapokabiliana na janga la corona.

Walimtaka Gavana Hassan Joho kutatua swala hilo mara moja la sivyo watagoma.

“Tunataka mishahara yetu ilipwe na marupurupu ya kupambana na Covid-19. Tumejitolea mhanga na hata kuhatarisha maisha yetu kuhudumia wakazi lakini tunatelekezwa na hatuthaminiwi na serikali hii. Tunahudumia Wakenya bila ya vifaa vya kujikinga na virusi vya corona,” alisema Dkt Niko Gichana mkuu wa chama cha madaktari tawi la Mombasa.

Akiongea na wanahabari nje ya hospitali kuu ya Pwani, Dkt Gichana alisema zaidi ya wahudumu wa afya 40 wamepata virusi vya corona wakiwa kazini.

“Tumechoka na unyanyasaji huu; familia zetu zinahangaika tukiendelea kuwa katika hatari ya maambukizi ya corona. Tunataka mazingira bora ya kufanya kazi,” alisisitiza.

Kwa upande wake, wa wauguzi, mwenyekiti wa chama chao cha kitaifa tawi la Bw Peter Maroko alisema wahudumu wa afya hawana hata nauli ya kwenda kazini.

“Hatuna nauli ya kwenda kazini, itabidi tusalie majumbani mwetu,” alisisitiza Bw Maroko.

COVID-19: Visa vipya ni 121

Na SAMMY WAWERU

KWA muda wa kipindi cha saa 24 zilizopita, Kenya imethibitisha visa vipya 121 vya Covid- 19, idadi jumla ya wagonjwa ikigonga 3,215

Alhamisi, kwenye taarifa Wizara ya Afya imesema visa hivyo vimethibitishwa kutoka kwa sampuli 3,291 zilizokusanywa, zikakaguliwa na kufanyiwa vipimo.

“Kufikia sasa, tumepima jumla ya sampuli 106,247,” wizara hiyo imeeleza.

Imetuma taarifa kwa vyombo vya habari ikiwa ni pamoja na kuchapisha kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii.

Imechukua hatua hiyo kufuatia makadirio ya bajeti mwaka wa Fedha 2020/2021 yaliyokamilika kusomwa hivi punde na Waziri wa Fedha Ukur Yatani, kuchukua muda unaotumika katika kikao na wanahabari.

Nairobi imesajili visa 49, Busia (37), Mombasa (20), Kajiado (5), Migori (4), Kiambu na Kilifi (mbili kila moja), huku Murang’a na Nyeri zikiwa na kisa kimoja kila kaunti.

Wizara ya Afya pia imedokeza kwamba katika muda wa kipindi cha saa 24 zilizopita, wagonjwa 44 wameruhusiwa kuondoka hospitalini baada ya kuthibitishwa kupona, idadi jumla ya waliopona ikifika 1,092

Idadi jumla ya walioangamia nchini kwa sababu ya Covid-19 ni 92 baada ya wagonjwa watatu kufariki kipindi hicho cha saa 24 hivyo kumaanisha ipo haja ya Wakenya kuendelea kufuata masharti na kanuni za wizara.

AFYA: Hatua za kumsaidia mjamzito kupunguza kichefuchefu

Na MARGARET MAINA

mwmaina@ke.nationmedia.com

MIEZI mitatu ya kwanza ya ujauzito, ni muda wa mabadiliko mbalimbali kimwili na kisaikolojia kutotokana na homoni za uzazi kuzalishwa kwa wingi zaidi.

Mabadiliko haya hutofautiana kutoka kwa mwanamke mmoja hadi mwingine, na pia kwa mwanamke mmoja kwa nyakati tofauti.

Kipindi hiki cha ujauzito, mwili wa mama unatengeneza homoni kwa wingi.

Ni vigumu sana kuzuia hii hali kwa mjamzito kwa sababu ni mabadiliko ya mwili ya kuuandaa kuweza kupokea kiumbe kijacho.

Ingawa hivyo, unaweza kupunguza kiasi tatizo na madhara yake.

Kula kidogo mara nyingi zaidi kwa siku

Ni vizuri kula kidogo kidogo mara nyingi kuliko kula chakula kingi kwa milo mitatu kwa siku. Kula mara nyingi husaidia kuongeza sukari mwilini sababu hali ya uchovu na ugonjwa huweza kusababishwa na kutokuwa na sukari ya kutosha kwenye damu. Sukari ndio chanzo cha nguvu mwilini. Chakula cha mara kwa mara humpa mama kiasi cha nguvu za kutosha kwake na kwa mtoto kwa muda wote.

Andaa chipsi za viazi

Chumvi iliyomo kwenye viazi husaidia kukausha mate ambayo huwafanya baadhi ya wajawazito kuhisi kutapika mara kwa mara. Pia, wanga katika viazi husaidia kurekebisha kiwango cha sukari kwenye damu.

Tumia limau au ndimu

Limau au ndimu vina uchachu ambao husaidia kukata hali ya kichefuchefu. Kata limau na unuse harufu ya tunda hili. Kufanya hivyo kutasaidia kupunguza hii hali ya kutapika. Pia unaweza ukakamulia limau kwenye chai au maji ukanywa. Unaweza pia kunusa maganda au majani ya limau maana husaidia pia kupunguza hali ya kichefuchefu.

Kula vyakula venye protini na vitamini B6

Vyakula venye protini kwa wingi na vile vyenye vitamini B6 humfanya mama apunguze hali ya kichefuchefu. Inashauriwa mjamzito aepuke kula vyakula venye viungo vingi, mafuta au vilivyokaangwa kwa muda mrefu sana. Vyakula hivi vinaweza kuzidisha hali ya kichefuchefu na mtu kuhisi kutapika.

Tangawizi

Tangawizi hupunguza hali ya kichefuchefu na hivyo unaweza kuitumia kwenye chai. Kuwa makini na hakikisha unatumia tangawizi kiasi na wala sio nyingi.

Kula kifungua kinywa kabla ya kutoka kitandani

Mjamzito anashauriwa apate kifungua kinywa akiwa bado kitandani. Hali ya kuamka na tumboni hakuna kitu huweza kuwa chanzo cha kuhisi kichefuchefu na kutapika.

Kunywa maji mengi

Kunywa maji mara kwa mara ili kuzuia mwili kuishiwa na maji (dehydradtion). Ni vizuri kunywa lita 2.5 kwa siku ikiwa pamoja na maji, chai au juisi za matunda zisizo na sukari ya kuongezewa au kemikali za viwandani.

Kunywa pregnancy multivitamin

Wakati mwingine ni vizuri kumwona daktari ili kupata maelekezo ya dawa ambazo ni salama kuzitumia kupunguza hali ya kutapika. Pia kama kuna uwezekano wa kupata dawa zinazoweza kurudisha virutubisho muhimu mwilini, ikiwa ni pamoja na folic acid na vitamini D, basi tumia. Tahadhari usitumie dawa bila ushauri wa daktari.

SIHA NA LISHE: Ulaji wa tende una manufaa kadhaa katika mwili wa binadamu

Na MARGARET MAINA

mwmaina@ke.nationmedia.com

TUNDA aina ya tende ni maarufu sana katika mataifa ya Arabuni kama vile Saudi Arabia na Oman.

Ni tunda la mtende ambalo likiwa limeiva huwa na kokwa ngumu yenye rangi baina ya zambarau na kahawia na nyama laini na tamu.

Kwa watu wenye matatizo ya tumbo, tende husaidia kurekebisha matatizo hayo na huleta afueni.

Tende husaidia kuuimarisha mapigo ya moyo

Ondoa mbegu katika tende kisha tumbukiza nyamanyama yenyewe katika maji kwa usiku mmoja na asubuhi kunywa maji hayo. Fanya hivyo mara mbili kwa wiki.

Utafiti umeonyesha kuwa tende husaidia kutanua misuli wakati mwanamke anapokaribia kujifungua, hii husaidia kumfanya mwanamke asipoteze damu nyingi wakati wa kujifungua.

Wataalamu wa vyakula, wanazichukulia tende kama chakula bora kwa wanawake na utafiti wao unaonyesha kwamba husaidia kuyapa maziwa virutubisho muhimu vinavyomfanya mtoto awe na afya njema.

Tende husaidia kupunguza kiwango cha kilevi (alcohol) kwenye damu. Maji ya kunywa ambayo tende imelowekwa ndani yake husaidia kuondoa haraka pombe mwilini.

Tende husaidia kuchelewesha dalili za uzee na pia husaidia kurekebisha ngozi na huondoa mabaka ya kuungua kutokana na athari za jua kali.

Madini ya chuma yanayopatikana katika tende yana umuhimu mkubwa kwa watu wenye upungufu wa damu. Ni ahueni kubwa kwao kula tende.

Vitamin B1 na B2 katika tende husaidia kuyapa nguvu maini.

Tende pia huleta ahueni kwa watu wenye kikohozi na mafua ya mara kwa mara.