AFYA: Umuhimu wa mtu kula chakula kwa uwiano unaotakiwa

Na MARGARET MAINA

mwmaina@ke.nationmedia.com

ULAJI wa chakula unaofaa ni ule ambao mtu anahakikisha kwamba anakila chakula mchanganyiko, cha kutosha na chenye virutubisho vyote kwa uwiano unaotakiwa.

BNi muhimu mtu ale matunda angalau mara mbili kwa siku na ale mboga kwa wingi.

Ni muhimu kuhakikisha unatumia mafuta kwa kiasi kidogo. Mafuta ya nyama sio mazuri sana kwani yanahusishwa na magonjwa ya moyo. Badala yake inashauriwa mtu atumie zaidi mafuta yatokanayo na mimea.

Matumizi ya sukari na chumvi yawe ya kiasi. Pia kwa watu wanaokunywa pombe wasinywe kupita kiasi.

Kula chakula mchanganyiko

Chakula mchanganyiko hukuwezesha kupata virutubisho vyote vinavyohitajika mwilini. Kwa mfano vyakula vya wanga vinasaidia kuupa mwili nguvu na joto. Protini hutumika kujenga mwili navyo vitamini na madini hulinda mwili dhidi ya magonjwa. Kila siku jitahidi kula vyakula kutoka katika makundi yafuatatyo:

 • vyakula vya asili ya nafaka, ndizi za kupika na mizizi
 • vyakula vya jamii ya kunde, asili ya wanyama na mbegu za mafuta
 • mboga
 • matunda
 • sukari, asali na mafuta

Epuka mafuta mengi

Mafuta mengi mwilini hasa yale yenye asili ya wanyama yanaweza kusababisha ongezeko la magonjwa ya moyo na shinikizo kubwa la damu,. Hivyo inashauriwa kutumia zaidi mafuta yatokanayo na mimea.

Jinsi ya kupunguza mafuta

 • tumia mafuta kidogo wakati wa kupika
 • epuka kula vyakula vilivyokaangwa kwa mafuta na badala yake chemsha, oka au choma
 • punguza mafuta kwenye nyama iliyonona, na ikibidi ondoa ngozi ya kuku kabla ya kupika.
 • chagua nyama au samaki bila mafuta mengi.

Kula matunda na mbogamboga kwa wingi

Vyakula hivi huupatia mwili kinga dhidi ya magonjwa mbalimbali kama vile baadhi ya magonjwa ya moyo, saratani na kisukari.

Matunda ni chanzo cha virutubisho kama vile vitamini na madini ambayo hupatikana kwa wingi kwenye vyakula hivi kuliko kwenye vyakula vingine. Virutubisho hivi:

 • huifanya ngozi kung’aa na ionekane yenye afya pamoja na kusaidia vidonda kupona vizuri
 • huwezesha macho kuona vizuri
 • husaidia kuimarisha ufahamu
 • husaidia uyeyushaji wa vyakula tumboni na kufyonza madini ili yatumike mwilini
 • hutumika katika kutengeneza damu
 • husaidia katika uundaji wa chembe za uzazi

Virutubisho hivi havihifadhiki katika mwili wa binadamu hivyo ni vizuri matunda tofauti yajumlishwe kwenye mlo/milo ya siku.

Inashauriwa ifuatavyo kuhusu matunda na mbogamboga

 • pika mbogamboga kwa muda mfupi ili kupunguza upotevu wa vitamini na madini
 • tumia maji kidogo wakati wa kupika mbogamboga na hata maji yanayopikia mboga yaendelee kutumika sio kumwagwa

Vyakula vyenye nyuzinyuzi

Vyakula vyenye nyuzinyuzi (fibre) husaidia katika usagaji wa chakula tumboni na pia huweza kupunguza baadhi ya aina za saratani, magonjwa ya moyo na kisukari. Ili kuongeza nyuzinyuzi:

 • kula saladi na matunda mara kwa mara
 • kula tunda zima badala ya juisi
 • tumia unga usiokobolewa
 • kula vyakula vya jamii ya kunde mara kwa mara kwani vina nyuzinyuzi kwa wingi

Punguza chumvi

 • tumia chumvi kidogo wakati wa kupika
 • epuka vyakula vyenye chumvi nyingi
 • epuka uongezaji wa chumvi kwenye vyakula wakati kimeshawekwa kwenye sahani mezani

Punguza sukari

Sukari huongeza nishati mwilini, hivyo huchangia kuongezeka kwa uzito. Matumizi ya sukari huzalisha bakteria kinywani ambao husababisha meno kutoboka. Hivyo inashauriwa:

 • unywe vinywaji ambavyo havina sukari kama vile madafu na juisi za matunda badala ya soda zenye sukari
 • kama unatumia sukari, tumia kiasi kidogo
 • upunguze kula vitu vyenye sukari nyingi
 • na upunguza matumizi ya vyakula vilivyoongezwa sukari.

Bawabu aliyeingia kwa nyumba aliyolinda kusaka chakula motoni

Na RICHARD MUNGUTI

BAWABU aliyeingia ndani ya nyumba aliyokuwa analinda kusaka chakula anasubiri uamuzi ikiwa atasukumwa gerezani au la.

Boniface Ngare alishtakiwa mbele ya hakimu mkazi Sharon Maroro alikiri aliingia ndani ya nyumba ya Bw Daniel Kamau kwa lengo la kuiba.

Mshtakiwa alikuwa ameajiriwa kulinda jumba la Bw Kamau katika mtaa wa Lang’ata.

Mnamo Julai 1, 2021 mshtakiwa alikutwa ndani ya nyumba na mjakazi akisaka chakula.

Mjakazi huyo alimwita Bw Kamau na kumweleza kulikuwa na mtu ndani ya nyumba ambaye nia yake ilikuwa haijulikani.

Mwajiri wa Bw Ngare alifahamishwa na alipokamatwa mlinzi huyo aliungama kwamba “ alikuwa anahisi njaa na ndipo aliamua kuingia mle chumbani mwa mlalamishi kusaka chakula.”

Mahakama ilielezwa mshtakiwa alikiri alikuwa anahisi njaa na ndipo akaamua kuingia mle ndani kutafuta chakula.

“Nilihisi njaa mithili ya kuangamia ndipo nikaamua na liwe liwalo nikaingia mle nyumbani nitafute chakula. Nilikutwa ndani ya chumba ambapo mlalamishi anahifadhi pombe kali,” hakimu alifahamishwa.

Mshtakiwa akijitetea alimweleza hakimu, “Mimi nilihisi njaa nusura nife ndipo nikaamua kuingia ndani ya nyumba kutafuta chakula.”

Mshtakiwa aliomba msamaha na kuomba korti “ipitishe hukumu afungwe nje aendelee kusaidia familia yake.”

Bi Maroro aliamuru idara ya urekebishaji tabia imhoji mshtakiwa pamoja na watu wa familia ndipo ukweli ukithiri.

Hakimu atatoa uamuzi mnamo Julai 14, 2021.

‘Nimeandaa mapishi 25 kutoka nchi mbalimbali Afrika na Ulayani’

Na MAGDALENE WANJA

Bi Ayumi Yamamoto alizaliwa na kulelewa katika mji wa Osaka nchini Japan ambapo alisoma na kuhitimu katika kozi ya Ukulima katika chuo kikuu.

Baadaye, alipata kazi ya kuwa mwalimu katika somo hilo hadimwaka 2011 alipoingia nchini Kenya.

Alisafiri hadi nchini Kenya kufanya kazi ya volunteer na shirika la Overseas Cooperative Volunteer ambalo ni shirika la serikali ya Japan.

Baada ya miaka miwili unusu,alianza biashara ya kuuza matunda yaliyokaushwa katika kampuni inayojulikana kama Kenya Fruits Solutions.

Alipokuwa akifanya kazi hizi, aligundua kwamba kulikuwana hitaji kubwa ya huduma za kuwapelekea wateja chakula(delivery) katika nyumba zao mjini Nairobi.

Aliwaza jinsi angeweza kuleta suluhisho katika sekta hii na akaamua kutengeneza mealkits.

“Baada ya kufanya kazi katika sekta mbalimbali za lishe, nilitamani sana kufanya biashara ya kuuza ama kuandaa chakula” alisema Yamamoto.

“Nilishangazwa piana insihitaji la chakula liliendelea kukua kila siku mjini Nairobina nikaiona kama nafasi nzuri ya biashara,” aliongeza Yamamoto.

Baadhi ya vyakula anavyoandaa Bi Ayumi Yamamoto. Picha- MAGDALENE WANJA

Baada ya kufanya matayarisho yote mnamo mwaka 2019, aliweza kuanzisha kampuni yake ambayo aliiita Love and Meals.

Wazo lake la kutengeneza Meal Kits pia lilichangiwa na ujuzi alioupata kutoka kwa watu aliotangamana naokutoka sehemu mbalimbali ulimwenguni.

Ndani ya meal kit, Bi Yamamoto humuandalia mteja wake vinavyohitajika kuandaa aina fulani ya chakula kisha anakuandalia maandishi ya muongozo wa jinsi ya kukitayarisha chakula hicho.

Kwa meal kit moja,kampuni yake hulipisha kuanzia Sh1,050 ambayo pia huhuandamana na iloe ya usafirishaji.

Huduma hii hupatikana mtandaoni ambapo mteja hujichagulia anachohitaji na kasha kupeana maagizo kupitia program hio ya simu.

“Lengo letu ni kuwafanya wateja wetu kuridhika na huduma zetu huku tukirahisisha kazi ya upishi haswa kwa watu ambao hawana muda wakutosha wa kujiandalia mlo wanaotaka kutokana na ukosefu wa muda au kutojua jinsi ya kuandaa,” aliongeza.

Kufikia sasa, Yamamoto ameweza kuandaa mapishi 25 kutoka nchi mbalimbali barani Afrika na Ulayani.

Ndoto yake ni yake ni kuendeleza huduma zake katika miji mingine mikuu nchini na mataifa mengine.

‘Mama ntilie’ mpishi kigogo wa kibandani

Na Ludovick Mbogholi

BI. Aisha Omar(40) anafanya kazi ya upishi katika eneo la Liwatoni, Ganjoni mkabala na eneo la viwanda na makampuni, na yeye ni mama anayetambuliwa sana kama ‘mama ntilie’. Mama huyu hajawahi kuingia darasani lakini kwa juhudi zake amepiga hatua kubwa kimaisha.

“Tangu nizaliwe sijaingia darasani kupata elimu na sijui masomo ni nini” apasha kwenye mahojiano yake na Akilimali.Bi. Aisha aliishi na wazazi huko Duga, Maforoni mkoani Tanga, Tanzania alikozaliwa.

“Kwa kuwa sina elimu, nilihisi afadhali nianze kujishughulisha na kazi ya upishi mitaani kwa kupika chapati, maharagwe, nyama, karanga, matumbo, githeri na muthokoi miongoni mwa vyakula vyengine” akariri Bi.

Aisha huku akidokeza kazi hiyo ndiyo iliyompatia jina la ‘mama ntilie’.Kazi ya upishi iliposhika kasi alitambuliwa zaidi na wateja huku umaarufu wake ukiwa kichocheo cha uamuzi wa kuhamisha shughuli zake katika eneo la Ganjoni huko Liwatoni kwenye watu wengi wanaofanya kazi viwandani na katika makampuni makubwa.

“Ilibidi nije hapa maana niliamini nitafanikiwa zaidi kimapato” akiri ‘mama ntilie’ huyu alipoendelea kuhojiwa na Akilimali kwenye eneo lake la kazi huku akisisitiza kusema kwa siku anatumia mifuko mitatu ya unga wa ngano kwa upishi wa chapati, na kila mfuko unampatia jumla ya chapati 28.

“Mfuko mmoja unanipatia chapati 28, na kila chapati nauza kwa Sh15” anadokezea Akilimali kwenye mahojiano huku ikiaminika anapata jumla ya chapati 84 kwa mifuko mitatu ya unga huo ambayo ni sawa na kilo 6 kwa jumla.Akilimali imebainisha kuwa kila siku Bi. Aisha huuza chapati 84 na kunufaika kwa Sh1,260.

Hata hivyo Bi. Aisha anasema anauza chapati hizo na maharagwe ambayo ndiyo mboga inayopendwa zaidi na wateja wake.

“Kila siku napika kilo mbili za maharagwe, na huwauzia wateja sahani moja kwa Sh30. Hii inamaanisha kuwa mteja akiagiza chapati mbili na maharagwe ananilipa Sh60” anaarifu zaidi kuhusu mapato anayojiingizia kwenye biashara yake hiyo.

Bi Aisha Omar hunufaika kwa pato la Sh2,760 kila siku kwani maharagwe pekee humwingizia takriban Sh1,500 kwa kilo mbili anazonunua kwa siku.Hata hivyo Akilimali imegundua kuwa ‘mama ntilie’ huyu hunufaika kwa takriban Sh82,800 kwa biashara ya chapati na maharagwe pekee kwa mwezi mbali na mauzo ya githeri, wali, muthokoi, ugali na chai miongoni mwa vyakula vingine anavyopikia wateja.Kwa jumla Bi.

Aisha Omar hujiingizia zaidi ya Sh100,000 kila mwezi, pato hilo huchangiwa na vyakula vingine vinavyomwingizia takriban Sh30,000 kila mwezi.“Hata hivyo nakumbana na changamoto nyingi zikiwemo kusumbuliwa na maafisa wa afya na wa kaunti” anapasha Akilimali huku akidai mafanikio hayo hayamtoshelezi maana kila siku anamlipa mfanyakazi wake Sh300 pesa taslimu.

Kwenye taarifa tofauti iliyogunduliwa na Akilimali, Bi. Aisha Omar amebahatika kufahamu zaidi ya lugha 20 za makabila tofauti yakiwemo ya Kimaasai, Kichagga, Kikuyu na Kisomali.

Mbunge ataka maafisa wasihujumu uchunguzi chakula kilichodhuru kadhaa Kikuyu

Na MWANGI MUIRURI

MBUNGE wa Kikuyu Kimani Ichung’wa ameteta kwamba kuna maafisa wakuu serikalini katika idara za kiusalama wanaohujumu uchunguzi kuhusu kisa ambacho wakazi wa eneobunge lake walipewa chakula chenye madhara kiafya.

Chakula hicho kilikuwa kimetolewa zaidi ya wiki mbili zilizopita kama cha msaada na ambapo kiliishia kuwaathiri wahanga kwa kuwatwika shida za kiafya na kuishia kulazwa hospitalini.

Bw Ichung’wa anadai maafisa hao ambao hakuwataja wanacheza siasa na kisa hicho ambacho hakikuwa na utu kamwe na kilichowaathiri watu 19.

“Chakula hicho kilipeanwa katika mtaa wa Gikambura na ambapo kilikuwa kimebandikwa majina ya mimi kama mbunge na pia lile la wakfu wa Dkt William Ruto akiwa ndiye naibu wa rais. Njama ilikuwa sisi wawili tuibuke kama waovu wa kudhuru watu wa Gikambura kwa chakula na hivyo basi tupoteze umaarufu wa kisiasa,” akasema.

Waliokisambaza chakula hicho alisema ni wa mrengo pinzani wa kisiasa na ambao nia yao kuu ni kumpotezea DP Ruto umaarufu katika eneo hilo la Gikambura na kitaifa.

Mbunge huyo aliteta kuwa hadi leo hii, hakuna lolote la kuwakamata waliohusika limetekelezwa na wachunguzi “licha ya kwamba tumetoa habari muhimu kuhusu kisa hicho kama nambari za usajili wa magari ambayo yalitumika pamoja na maelezo ya umbo na sura za waliosambaza chakula hicho”.

Chakula hicho kilisambazwa muda mfupi baada ya mbunge huyo na Dkt Ruto kutoa msaada wao wa chakula kupitia kwa wachungaji ambao walikongamana katika mji wa Kikuyu na kupewa misaada hiyo wawasilishe kwa waumini wao waliokuwa katika hali ya njaa kupitia mkurupuko wa maradhi ya Covid-19.

Alidai kuwa amepokezwa habari muhimu na baadhi ya maafisa wa polisi kwamba “kuna ilani zimetolewa tusithubutu kuwakamata waliohusika wala kuwaanika kwa umma kwa kuwa wako na ushawishi mkuu wa kisiasa na kiserikali”.

Ichung’wa alisema kuwa licha ya kuwa barabara ambazo zilitumika na wasafirishaji wa chakula hicho zimepambwa na kamera za siri za kiusalama na ambazo zilinakili mienendo ya wahaini hao, kuna maafisa ambao wamezitwaa picha hizo na kuzikatalia katika makao makuu ya polisi, Nairobi.

“Wametoa tu ilani kwa maafisa nyanjani wasahau kuwa kuna mikanda hiyo ya kamera na wakiulizwa waseme haikunakili lolote au chochote kama ushahidi wa kutatua kisa hicho,” akasema Bw Ichung’wa.

MAHANGAIKO: Baadhi ya wakazi wa Mayungu wategemea dampo kupata chakula

Na FARHIYA HUSSEIN

TUNAKARIBISHWA na taka zilizooza na kuozeana na kutapaka kila mahali huku zikitoa uvundo eneo la Mayungu, Malindi, Kaunti ya Kilifi.

Tunampata Bi Kadzo Kenga akichakura taka hizo.

Anasema anatafuta chakula. Eti haya ndiyo mazoea.

Kila siku hapa Mayungu, yeye hujiunga na wakazi wengine kutafuta chakula kutoka kwa mabaki yaliyoshushwa na lori la takataka.

Wengi hawawezi kuvumilia harufu hiyo kali wala kuishi sehemu kama hii, lakini kwao, hapa ni kama mgodi wa kujichumia riziki.

“Mume wangu mlemavu alichukuliwa na watu wa familia yao na wakaniacha hapa na watoto sita ambao ninawalea. Tumezoea maisha haya kwani hakuna kazi inayopatikana karibu na eneo hili,” anasema Bi Kenga ambaye ni mjamzito.

Taifa Leo imebaini kuwa mara tu lori linakaribia eneo hilo, nyuso za wakazi zinajawa na furaha.

Baadhi ya wakazi wa Mayungu, Malindi, Kaunti ya Kilifi wakichakura sehemu ya dampo kutafuta chakula. Wanasema ni maisha yao ya kawaida. Picha/ Farhiya Hussein

“Tunakula kila aina ya chakula kuanzia ngano, slesi za mkate na wali. Yaani kimsingi hakuna kilichooza kwetu. Ikiwa tutapata chakula hicho, tunayo bahati kwa sababu nyakati zingine tunalazimika kulala njaa,” anaeleza Bi Kenga.

Karibu na nyumba yake, kuna mwanamke mwingine anayeonekana akiwalisha wanawe.

“Hatuwezi kununua chakula kwa hivyo badala yake tunategemea lori linaloleta makombo kwenye dampo,” anasema mwanamke huyo anayejitambulisha kwamba anaitwa Bi Rehema Wanje.

Si wanawake tu. Nalo lipo kundi la wanaume wanaonekana wakichakura nao wapate cha kutia kinywani kiingie tumboni na kingine wapeleke nyumbani.

Baadhi ya wakazi wa Mayungu, Malindi, Kaunti ya Kilifi wakichakura sehemu ya dampo kutafuta chakula. Wanasema ni maisha yao ya kawaida. Picha/ Farhiya Hussein

Mwanamume kwa jina Bw Hamisi Changawa anasema amekosa njia nyinginezo halali za kujitafutia riziki.

“Tumelazimika kutafuta chakula hapa,” anasema.

Mkazi mwingine wa Mayungu, Bw Ngumbao Elvis anakubaliana na alichokisema Bw Changawa.

“Ndio; tunaugua kwa kula hivi vyakula, lakini ni kipi tunastahili kufanya? Tusibiri miujiza?”anauliza mkazi huyo.

Watoto nao pia hawajaachwa nyuma kwani nao wanahangaika papa hapa wakichukulia hali hii kuwa ya kawaida.

Mtoto mwenye umri wa miaka 12 anasema huamka asubuhi na mapema na hatua yake inayofuata ni kufika dampo kuona ikiwa lori la taka lilikuja na kuacha mabaki yoyote au la.

“Mimi ni mtoto wa pili katika familia ya watoto watano. Nimezaliwa na kukuzwa hapa. Hii imekuwa njia yetu ya kulelewa, kuamka na kwenda kutafuta chakula katika dampo,” kijana huyo alisema. Taifa Leo haiwezi kumtaja jina kwani yeye ni wa umri mdogo.

Kaunti yawapa chakula ombaomba kama njia ya kuwataka wasijazane mjini

Na WINNIE ATIENO

WAKATI huu wa janga la Covid-19 ni kipindi ambacho familia za kurandaranda na wale wa kuombaomba wanaendelea kumiminika Kaunti ya Mombasa kuomba chakula na pesa.

Hii ni kufuatia makali ya maisha yaliyoletwa na athari za virusi vya corona.

Kulingana na serikali zaidi ya watu laki 300,000 nchini wamepoteza ajira kufuatia athari za janga la corona huku biashara nyingi na hata hoteli zikifungwa.

Hata hivyo, serikali ya Kaunti ya Mombasa imeweka mikakati kuwaokoa wakazi hao kwa kuwapa vyakula ili warudi makwao.

“Tumebaini familia nyingi zinamiminika katikati mwa jiji la Mombasa kuomba vyakula na pesa kufuatia janga la corona ambalo limesababisha wengi kupoteza ajira,” alisema Bw Innocent Mugabe afisa wa kaunti anayesimamia lishe.

Kulingana na takwimu za kaunti, kuna takriban familia 1,809 za kurandaranda jiji hilo la kitalii.

Serikali ya kaunti hiyo ilishindwa kudhibiti na kukabiliana na idadi kubwa ya familia za kurandaranda na wale ombaomba hususan wakati huu wa janga la ugonjwa wa Covid-19.

Hata hivyo wadadisi wameonya kwamba wamo katika hatari ya maambukizi ya virusi vya corona wakisalia bila makao.

“Tunataka watu wa familia waache kujazana katikati mwa jiji kutokana kwa sababu wanajiweka katika hatari ya virusi vya corona. Tunawapa vyakula ili wasalie majumbani mwao ambako wako salama zaidi,” aliongeza Bw Mugabe.

Familia 200 za kurandaranda zinaendelea kunufaika na shughuli hiyo.

Ruto na Ichung’wa wakana kuwapa wakazi wa Kiambu chakula hatari

NA SIMON CIURI

Utata umeibuka kuhusu aliyetoa chakula cha msaada kilichopewa wakazi wa kaunti ya Kiambu Jumatatu ikidaiwa chakula hicho ni hatari kwa afya ya binadamu baada ya waliokipokea kulazimika kukirudisha.

Gavana wa Kiambu James Nyoro alisema kwamba watu 12 waliokula chakula hicho walikimbizwa katika hospitali za Tigoni, Kiambu na Thika baada ya kubebwa kutoka kwa nyumba zao kwa ambulansi.

Naibu Mshirikishi wa Kaunti ya Kiambu Wilson Wanyanga alisema kuwa chakula hicho kilipeanwa na mbunge wa Kikuyu Kimani Ichung’wa na kundi lililosemekana kuhusishwa na Naibu Rais William Ruto.

Lakini Dkt Ruto na Bw Ichung’wa walikana madai kwamba walihusika katika kupeanwa kwa chakula hicho kibaya huku ikiibuka kuwa kumekuwa na wahisani tofauti wa misaada ya chakula katika kaunti hiyo hivi karibuni.

Mkazi wa eneo la Gikambura David Githinji aliyepokea chakula hicho Jumapili alasiri aliambia Taifa Leo kuwa gari aina ya Land Cruiser ilifika mtaani humo na mtu aliyekuwa ndani yake akaita watu waje wapewe chakula na baadaye akaondoka.

“Ilikuwa ni mafuta ya kupikia, unga wa ugali na sukari. Tuligundua kwamba majani chai yalikuwa na rangi tofauti na ilikuwa chachu tulipoyatumia. Baadaye mmoja wa familia yangu akaanza kuwa na maumivu ya tumbo. Tumeandikisha taarifa hiyo kwenye kituo cha polisi,” Bw Githinji aliambia Taifa Leo.

Maafisa wa afya wa Kiambu walisema wamepeleka sampuli za chakula hicho kwa maabara kwa uchunguzi wa kisayansi kubaina iwapo kilikuwa na sumu.

Tafsiri: Faustine Ngila

‘Huenda uhaba wa chakula muhimu ukaanza kushuhudiwa’

Na SAMMY WAWERU

WIZARA ya Kilimo imeonya huenda upungufu wa chakula muhimu ukaanza kushuhudiwa hivi karibuni kufuatia mzozo wa maeneo ya mpakani baina ya Kenya na Tanzania.

Kulingana na wizara, bei za mahindi, mboga na matunda zinatarajiwa kupanda maradufu.

Onyo hilo limejiri licha ya Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta na mwenzake wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli kuahidi kutatua mzozo uliopo.

Rais Kenyatta mnamo Jumamosi alitangaza kufunga mipaka ya Kenya na Tanzania na vilevile Somalia, kutokana na ongezeko la visa vya Covid – 19 maeneo ya mipakani, ila malori ya mizigo pekee kuruhusiwa kuingia.

Amri hiyo aidha imezua tumbojoto kati ya mataifa haya mawili.

Akiahidi mzozano uliopo unaendelea kutatuliwa, Waziri wa Kilimo Peter Munya alisema Jumatano changamoto zinazidi kuibuka kuingiza chakula nchini.

“Shida iliyopo tunaendelea kuitatua. Hakika, kuna ugumu kuingiza chakula nchini,” waziri akasema.

Rais wa Tanzania Dkt Magufuli alinukuliwa Jumatano akisema Kenya na taifa lake ni ndugu, na mzozo uliojiri unasuluhishwa, akieleza kwamba athari za Covid-19 hazipaswi kusambaratisha usahibu wa mataifa haya mawili.

Sasa waziri Munya anahimiza wakulima wa Kenya kujibidiisha kuzalisha chakula.

“Hii ni fursa ya wakulima wetu kuweka bidii katika shughuli za kilimo,” waziri akasema.

Tanzania ni mzalishaji mkuu wa nafaka, mboga, nyanya, vitunguu, matunda, na mazao mengine, mengi yanayouzwa Nairobi na viunga vyake.

Uhaba wa chakula ni miongoni mwa athari zilizosababishwa na janga la Covid-19.

Usambazaji wa vyakula vya msaada kwa walio karantini waanza Wajir

Na FARHIYA HUSSEIN

KAUNTI ya Wajir imeanzisha shughuli ya ugavi wa vyakula kwa wakazi walioathirika na Ukimwi, walemavu na wale waliowekwa karantini kudhibiti Covid-19.

Akithibitisha, Gavana wa kaunti hiyo Bw Mohamed Abdi amesema lengo lao kuu ni kuhakikisha wale walio karantini wanapata vyakula vya kutosha.

“Tumenunua magunia 3,165 ya mahindi, vibuyu 1,819 vya mafuta ya kupikia na madebe 1,400 ya tende na vyote vitasambazwa kwa watu walio katika hali ngumu. Tunataka kuhakikisha katika msimu huu wa janga la korona na mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan watu wanapata msaada wa chakula,” gavana huyo akasema.

Shughuli hiyo ilianza Jumamosi na wale walio katika vituo vya karantini walipokea magunia 350 ya mahindi, vibuyu 90 vya mafuta ya kupikia na tende madebe 90.

Tangu kuzuka kwa ugonjwa wa Covid-19 nchini Kenya, Wajir ni miongoni mwa kaunti 23 kati ya 47 zilizoathiriwa na ugonjwa huo.

Kwa sasa kaunti hiyo imeripoti visa 15 huku watu 42 wakiwa katika vituo mbalimbali vya karantini.

“Hatuna vifo katika eneo letu na watu 15 walioambukizwa wako katika hali nzuri,” akasema Bw Abdi.

Makundi mengine ambayo yalilengwa katika msaada huo ni watu walio na Ukimwi, mayatima na watu walemavu.

“Tayari wale wanaoishi na ulemavu wamepokea magunia 100 ya mahindi, vibuyu 60 vya Mafuta ya kupikia na tende debe 80,” gavana huyo alisema.

Alizidi kusema kuwa tayari wametayarisha kikosi ambacho kitashughulika kuwakamata watu ambao wanapita kwenye mipaka ya kaunti hiyo na nchi ya Somalia.

“Katika maabara yetu hadi sasa sampuli 143 zimefanyiwa vipimo vya Covid-19 na wafanyakazi 31 wanaohudumu katika vituo mbalimbali vya karantini, na watu 27 walipimwa na wanasubiri matokeo ikiwemo wanne kutoka kambi ya wakimbizi ya Dadaab (Kaunti ya Garissa), na wawili kutoka Dobley nchini Somalia,” Bw Abdi alisema.

Kamishna wa Kaunti hiyo Jacob Narengo amewasihi wakazi waripoti wale wanaojaribu kuingia katika kaunti hiyo kupitia njia zisizokubalika.

“Mipaka yetu na nchi ya Somalia inaendelea kutuweka katika hatari ya maambukizi. Tunapaswa kuendelea kuwa macho kila wakati. Nawasihi muwe salama katika nyumba zenu,” Bw Narengo akasema.

Awamu ya kwanza ugavi wa chakula kwa familia za kipato cha chini Mombasa kukamilika kesho Jumanne

Na MISHI GONGO

AWAMU ya kwanza ya ugavi wa chakula kwa familia za kipato cha chini katika Kaunti ya Mombasa unatarajiwa kukamilika Jumanne.

Uzinduzi wa awamu hiyo ulifanyika wiki tatu zilizopita na tayari mpango huo umetekelezwa katika baadhi ya maeneo yakiwemo Jomvu na Nyali.

Hapo kesho ugavu utakuwa katika maeneo bunge ya Kisauni na Likoni ambayo ndiyo yatafanikisha awamu ya kwanza.

Kulingana na Mwenyekiti wa Shirika la Msalaba Mwekundu Bw Mahmoud Noor, awamu ya kwanza ya mradi huo ililenga familia 50,000 lakini kufikia sasa wamezifikia familia 35,000

“Tunalenga familia 237,000 katika Kaunti ya Mombasa. Ugavi wa chakula umegawanywa katika awamu mbili ambapo awamu ya kwanza inalenga familia 50,000 huku awamu ya pili ikikusudiwa itakamilisha mpango katika familia zilizosalia,” akasema Bw Noor.

Katika mradi huo familia zilizoandikishwa zinapokea maharagwe, mchele, mafuta ya kupikia, unga wa ugali na ule wa ngano pamoja na sodo kwa wanawake.

Mwenyekiti huyo alisema awamu ya pili itaanza baada ya wiki moja.

Alisema mpango huo unakumbwa na changamoto nyingi ambazo wanaendelea kuzitatua.

 

Mwenyekiti wa Shirika la Msalaba Mwekundu Mahmoud Noor (mwenye jaketi jekundu) pamoja na maafisa kadhaa wa Kaunti ya Mombasa wakikagua chakula cha msaada. Picha/ Hisani

Alisema kwamba baadhi ya watu waliotwikwa jukumu la kuzisajili familia hizo waliitekeleza shughuli hiyo kwa upendeleo hali ambayo imechangia kucheleweshwa kwa ugavi jinsi ilivyoratibiwa.

“Baadhi ya watu tuliowatwika jukumu la kugawa chakula, walifanya ubaguzi. Kuna wale waliosajili jamaa zao na wale walioandikisha watu wawili kutoka familia moja,” akasema Bw Noor.

Hata hivyo, alisema visa vya mapendeleo vilikuwa vichache, akisisitiza kuwa ni familia zisizojiweza tu ndizo zilizonufaika na mradi huo wa chakula.

Hata hivyo, Bw Noor alisema idadi ya familia walizozilenga inaweza ikaongezeka kufuatia Wakenya wengi kupoteza kazi ndani ya miezi mitatu iliyopita kutokana na kuingia kwa ugonjwa wa Covid-19.

“Kuna watu walikuwa wanajiweza, lakini kufuatia kampuni nyingi kupunguza wafanyakazi, wengi wameachwa bila ajira hivyo kuongeza idadi ya wasiojiweza,” akasema.

Alisema kuwa serikali haitaweza kusaidia kila mtu, hivyo aliwaomba wahisani kujitokeza kwa wingi.

“Watu wengi wanaumia kutokana na hali mbaya ya uchumi,” akasema.

Aidha alisema wamewapa wakazi wa Mji wa Kale kipaumbele katika ugavi wa chakula kufuatia serikali kuweka marufuko yanayowazuia wakazi kutoka au wengine kuingia eneo hilo kama njia ya kudhibiti virusi vya corona.

‘Chakula kinauzika sokoni kuliko bidhaa nyinginezo’

Na SAMMY WAWERU

BIASHARA ya chakula ndiyo inawaingizia wengi pesa kipindi hiki ambapo taifa linapambana kudhibiti maambukizi ya Covid-19.

Uchunguzi wa Taifa Leo katika masoko ya Jubilee na Migingo eneo la Githurai umebainisha kwamba wafanyabiashara wengi wameamua kuuza bidhaa za kula.

Hatua hiyo imetokana na biashara nyingi hasa zisizo za bidhaa za kula kudorora, athari zilizochangiwa na janga la corona ambalo limeathiri uchumi wa nchi na ulimwengu kwa jumla.

Baadhi ya wafanyabiashara Githurai tuliozungumza nao wamelazimika kufunga maduka, taswira inayoonyesha namna Wakenya wamepoteza nafasi za kazi katika kampuni, mashirika mbalimbali na hata kazi za wenyewe kujiajiri.

Waathirika wengi wamegeukia biashara ya bidhaa za kula kukidhi mahitaji ya kimsingi.

Eva Irungu alikuwa muuzaji wa nguo lakini sasa anasema ameamua kuuza ndizi.

“Kenya iliporipoti kuwa mwenyeji wa Covid-19, biashara ziliathirika pakubwa. Bidhaa za kula zinanunuliwa,” akaelezea Eva ambaye ni mama wa watoto wawili.

Anasema mumewe aliyefutwa kazi katika kampuni moja jijini Nairobi, sasa anauza vitunguu saumu katika soko la Marikiti.

Bw Samson Mukang’u aliyekuwa muuzaji wa viatu anasema alikuwa anapata hasara na hivyo ikamlazimu awazie biashara ya machungwa.

“Hata ingawa mapato si ya kuridhisha, yataniwezesha kukidhi mahitaji muhimu kwa familia yangu,” akasema.

Kiwango cha uchumi kimedorora kwa sababu ya athari za Covid-19, sekta ya juakali na inayochangia zaidi ya asilimia 75 ya nguvukazi nchini ikitajwa kuathirika kwa kiasi kikuu.

Wakenya wengi wanasema mapato wanayopokea kwa sasa ni ya kukimu riziki na mahitaji ya kimsingi.

“Biashara zinaanguka, mapato ninayopokea ni ya kula na kulipa kodi ya nyumba,” akasema Jack Muia, kinyozi eneo la Githurai.

Visa vya maambukizi ya virusi vya corona nchini vinaendelea kuongezeka, Wizara ya Afya ikihimiza umma kuzingatia taratibu na maagizo yaliyotolewa kudhibiti maambukizi.

Kanisa la PCEA lawapa chakula wahitaji wa msaada

Na LAWRENCE ONGARO

KANISA la PCEA Makongeni, Thika, linaendelea kuwasaidia watu wa kipato cha chini kwa kuwapa chakula ikiwa ni njia mojawapo ya kukabiliana na janga la corona.

Kulingana na mpangilio wanufaika wanapokea chakula hicho Jumatano, Alhamisi na Ijumaa.

Mchungaji Rev, Simon Githiora Njuguna, ambaye ndiye msimamizi wa shughuli hiyo alisema hata watu wa imani tofauti za kidini wananufaika na mpango huo lakini ni sharti wawe na barua maalum kutoka wasimamizi wao katika maswala ya kidini kuelezea kuwa wako katika hali ngumu.

“Tulianzisha mpango huo mwanzoni mwa Machi na tutazidi kuwafaa kwa kuwakabidhi chakula,” akasema Bw Njoroge.

Alisema hadi sasa familia zaidi ya 500 kutoka maeneo tofauti zimefaidika pakubwa ambapo mpango huo umekuwa wa kufana zaidi.

Kulingana na Bw Njuguna, watu hao wanapokea kila mmoja mafuta ya kupikia lita moja, unga wa ugali kilo nne, maharage kilo mbili, mchele kilo mbili, na sabuni ya kipande mti mmoja.

“Baada ya kuzunguka maeneo tofauti tuligundua ya kwamba watu wengi hawana uwezo wowote wa kujilisha na kwa hivyo tulilazimika kama washirika kuungana pamoja kwa lengo la kusaidia wasiojiweza,” alisema Bw Njuguna.

Alisema jumla ya makanisa sita kutoka kaunti za Kiambu na Murang’a yaliamua kutoa msaada huo.

Baadhi ya makanisa hayo ni lile la Makongeni PCEA , Delmonte, Amani, Nanga (Murang’a), Mwana Wikio (Murang’a) na Thika PCEA Makongeni.

Baadhi ya wanufaika wa msaada uliotolewa na kanisa la PCEA mjini Thika. PIcha/ Lawrence Ongaro

Alisema mpango huo umekuwa ukiendeshwa kwa uwazi ambapo kila mmoja hupata haki yake bila utata wowote.

“Wakati huo pia sisi huwa mstari wa mbele kuwahamasisha kuhusu umuhimu wa kuzingatia usafi jinsi serikali inavyoagiza,” alisema Bw Njuguna.

Alisema jambo muhimu wanaoshauriwa kufuata ni kunawa mikono kila mara, kuvalia barakoa, kuweka zingatio la umbali wa mita moja au zaidi baina ya mtu na mwingine.

CTWOO: Shirika lawafaa wengi kwa kusambaza chakula mitaa ya mabanda

Na SAMMY WAWERU

MOYO wa kutoa ulichangia pakubwa hatua ya Bi Dianah Kamande kuanzisha shirika moja lisilo la kiserikali (NGO) la kuwashughulikia wajane na mayatima la Come Together Widows and Orphans Organization (CTWOO).

CTWOO ni shirika linaloangazia na kusaidia vilevile waathiriwa wa dhuluma za kijinsia.

Janga la Covid-19 linaendelea kusambaratisha uchumi hapa nchini Kenya na ulimwengu kwa jumla, ambapo biashara nyingi zimeathirika kwa kiasi kikuu, idadi kubwa ya watu wakipoteza nafasi za kazi.

Waathiriwa wengi wanategemea vibarua vya kila siku na hali ya mkwamo wa baadhi ya shughuli hasa za juakali na biashara hizo imeathiri mapato na familia nyingi zinashinda na hata kulala njaa.

Kwa muda wa wiki moja iliyopita, CTWOO imejituma kutoa na kusambaza bidhaa za kula na mahitaji ya kimsingi katika mitaa ya mabanda.

Dianah ambaye pia ni mjane anasema linalenga kusaidia wajane, manusura wa vita vya kijinsia, mayatima, wagonjwa na wakongwe wasiojiweza kote nchini, wakati huu ambapo janga la corona linaendelea kuhangaisha na kutesa.

“Kwa sababu ya amri ya kuingia na kutotoka Nairobi, tuna timu ya wawakilishi wetu katika kila kaunti kusambaza misaada ya chakula na bidhaa za kimsingi,” Dianah anasema.

Kufikia sasa, CTWOO imeweza kufikia karibu familia 100 zinazoishi mitaa ya mabanda na Dianah anadokeza kwamba shirika hilo linalenga zaidi ya familia 500.

Dianah Kamande (kulia) akitangamana na wajane wenzake wakati wa kusambaza misaada ya chakula kufuatia athari za Covid–19. Picha/ Sammy Waweru

Aidha, linasambaza mchele, unga wa mahindi na wa ngano, majanichai, mafuta ya kupika, chumvi, bidhaa za kula zilizokaushwa na kuongezwa thamani ili kudumu muda mrefu, miongoni mwa bidhaa nyinginezo muhimu, pamoja na mahitaji ya kimsingi kama vile sodo.

Wakati wa mahojiano na Bi Dianah wakati akisambaza vyakula mitaa ya mabanda ya Babadogo na Chieko jijini Nairobi, aliambia Taifa Leo kwamba kufikia sasa CTWOO imetoa msaada wa bidhaa zenye thamani zaidi ya Sh100,000.

Mitaa mingine iliyofaidika kupitia ukarimu wa shirika hilo ni pamoja na Korogocho, Kiambiu na Ngomongo.

“Tunazingatia taratibu na maagizo ya Wizara ya Afya kuzuia maambukizi ya Covid-19. Aidha, tunashirikisha maafisa wa polisi katika shughuli hii nzima, na mitaa isiyoingilika kwa sababu ya utovu wa usalama tunatumia afisi za machifu na manaibu wao kutoa misaada. Huu ndio wakati ambao kama Wakenya wazalendo tunapaswa kujali wenzetu kwa kuwasaidia,” Dianah akasema.

Ili kufanikisha malengo ya CTWOO, Dianah alisema wanategemea mapato yao binafsi na ufadhili kupitia wasamaria wema.

“Katika kipindi hiki kigumu tumepata mfadhili wa hivi punde, Global Fund for Widows, shirika tunaloshirikiana kuhakikisha tunaafikia maazimio yetu, waathiriwa wapate chakula,” akaeleza, Millie Okombo mshirika akipongeza waliojitokeza kupiga jeki CTWOO.

Waliopokea misaada walikuwa na kila sababu ya kutabasamu, kufuatia ukarimu wa shirika hilo.

“Tunaombea CTWOO na waanzilishi wake heri njema, baraka na Mungu awajaalie mema. Kwa niaba ya wenzangu tunashukuru sana,” akasema mama mmoja mjane katika mtaa wa Chieko, Kasarani.

Licha ya jitihada za shirika hilo, halijakosa changamoto za hapa na pale.

“Katika visa kadhaa, wahudumu wetu wameporwa bidhaa na wahuni katika mitaa yenye utovu wa nidhamu na usalama, ndiposa tunashirikisha idara ya usalama kwa karibu,” Dianah anasema.

CTWOO ni shirika lililozinduliwa Septemba 2013.

“Wengi wanaopoteza wachumba, jamaa na marafiki huonekana wakati wa matanga na mazishi pekee, rambirambi zikiwa ‘salamu za pole, tutaonana hivi karibuni’, katu hakuna atakayeonekana tena. CTWOO ni kama boma linalopokea waathiriwa, pia mayatima na wahasiriwa wa dhuluma za kinyumbani ili kuwapa afueni maishani,” Dianah anafafanua.

Ni shirika linalotumika kama ukumbi na mtandao wa waathiriwa kujieleza, shabaha ikiwa kutetea haki zao na kuwahamasisha, ikiwa ni pamoja na kutoa mawaidha na wosia kuondoa jakamoyo.

Mbali na hayo, CTWOO pia huwasajili kupata kozi za mafunzo mbalimbali hasa za kiufundi, ili kuwaimarisha kibiashara na kimaisha.

Bi Millie Okombo (kulia), Mwenyekiti Tawi la Come Together Widows and Orphans Organization-Babadogo akiwa katika shughuli ya kusambaza misaada ya chakula kufuatia athari za Covid–19. Picha/ Sammy Waweru

Isitoshe, huwahimiza kubuni makundi ili kupata mikopo ya serikali, isiyotozwa riba.

“Makundi hayo huyaunganisha na maafisa wa Uwezo Fund, Women Enterprise Fund na Affirmative Action Fund (NGAAF), kupitia ushirikiano wetu, ambapo hupata mikopo isiyotozwa riba wawekeze katika biashara na kujiimarisha kimaendeleo,” Dianah anaelezea.

Aliasisi shirika hilo baada ya kushuhudia kisa cha mama mjane aliyechemsha mawe Mombasa, kwa sababu ya ukosefu wa chakula. CTWOO imeweza kuimarisha maisha ya zaidi ya familia 65, ambazo sasa zinaweza kujitegemea.

Ni kupitia jitihada zake, hata kabla kubuni CTWOO, mwaka 2012 Dianah alitambuliwa na Rais (mstaafu) Mwai Kibaki, ambapo alipokea tuzo ya kiongozi wa taifa, HSC, inayopokezwa walioafikia makuu katika jamii.

Mama huyo pia ametambuliwa katika ngazi ya kimataifa.

Huku akiendeleza juhudi za kutoa misaada wakati huu mgumu wa Covid-19, Dianah ana ujumbe kwa Wakenya;

“Kila mmoja awe ndugu mlinzi wa mwenzake. Wanaojiweza wajitokeze kusaidia wasiojiweza, kwa kuwa Mwenyezi Mungu ndiye hutujaalia na kutubariki kwa njia tofauti.”

Mkurugenzi wa Skyways, wazazi wawatunuka walimu chakula na bidhaa muhimu

Na MISHI GONGO

IMEKUWA furaha kwa walimu wa shule ya msingi ya mmiliki binafsi ya Skyways iliyoko VOK eneobunge la Nyali baada ya wazazi na mkurugenzi wa shule hiyo kuwatunukia walimu chakula na bidhaa nyingine muhimu.

Wamesema ufadhili huo ni wa kuwasaidia walimu na wafanyakazi katika shule hiyo wakati huu ambapo shughuli nyingi za kiuchumi zimesitishwa.

Mkurugenzi wa shule hiyo Bi Dorothy Oloo amesema waliamua kuchukua hatua hiyo ili kuwasaidia ‘mzigo wa maisha’ walimu wake.

Bi Oloo amesema mchango huo uliongozwa na wazazi kama shukurani kwa walimu hao.

“Wazo hili lilitoka kwa wazazi; tulifaulu kuchanga pesa kisha tukawanunulia vyakula kama unga wa ngano, unga wa sima, mafuta ya kupikia, mchele, sabuni, sodo na bidhaa nyinginezo,” amesema.

Bi Oloo aidha amewashauri wakuu katika kampuni mbalimbali nchini kuweka mikakati itakayowasaidia wafanyakazi wao wakati huu mgumu.

Amesema wafanyakazi wengi wamekuwa wakipitia hali ngumu ya maisha tangu kuingia kwa ugonjwa wa Covid-19 nchini.

Chakula na bidhaa nyinginezo muhimu. Picha/ Mishi Gongo

Mzazi mmoja, Bi Halima Fadhili, amesema wamefanya hivyo kama njia ya kutoa shukurani zao kwa walimu hao kwa kuwaangalilia watoto wao.

“Tumeamua kuwakumbuka walimu wetu katika hali hii ngumu, tunawashauri wazazi wengine kuiga na kuwatunuku walimu wao pia na wasiojiweza katika jamii,” amesema mzazi huyo.

Machi 15, 2020, serikali ilitangaza kufungwa kwa shule zote nchini ili kudhibiti virusi vya corona.

Hali hiyo imesababisha baadhi ya walimu katika shule za wamiliki binafsi kukatwa mishahara kama njia ya kuziwezesha shule hizo kuendelea kujimudu.

COVID-19: Walemavu Thika walalama chakula cha msaada hakiwafikii

Na LAWRENCE ONGARO

UGAWAJI wa chakula unastahili kuendeshwa kwa uwazi bila ubaguzi.

Walemavu na vipofu kutoka kijiji cha Kiandutu mjini Thika, wamelalamika kuwa wengi wao hawafikiwi na chakula hicho huku wakiachwa na njaa.

Wamezidi kulalamika kwamba watu wanaopewa majukumu ya kusambaza chakula hicho wana mapendeleo fulani huku wakiwajali jamaa zao na marafiki wao.

Bi Jecinta Syumbua ambaye ni mmoja wa wasiojiweza anasema wanapitia masaibu mengi ambapo wanaiomba afisi ya naibu kamishna Bw Douglas Mutai, kuingilia kati ili kuweka kamati inavyostahili kusambaza chakula hicho kwa uwazi.

Alisema hivi majuzi chakula kilipoletwa katika kijiji hicho walemavu wengi na vipofu waliachwa hoi huku watu waking’ang’ania chakula hicho.

Alisema jambo linalowakera zaidi ni kwamba wale wanaosambaza chakula hicho wamezoea kurusha hewani ili umati uweze kudaka lakini kitendo hicho hakiwafai waliolemaa kimaumbile.

Alisema kwa muda wa wiki mbili hivi wamelemewa na makali ya njaa, familia zao nyingi nazo zikikosa chakula.

Bw George Mwangu ambaye pia ni mkazi wa kijiji hicho anasema wameshindwa jinsi watakavyopata chakula kwa njia ya utaratibu kwa sababu wakati mwingi watu hung’ang’ania kwa fujo.

“Sisi kama wakazi wa hapa tunataka utaratibu mwafaka ufuatwe ili chakula kisambazwe kwa uwazi na uwajibikaji,” alisema Bw Mwangu.

Alipendekeza wanaosambaza chakula hicho washirikiane na machifu na wazee wa kijiji ili kuwe na mpangilio maalum baada ya kuandika majina ya kila mmoja anayestahili kupata chakula hicho.

Alisema iwapo mtindo huo utafuatwa kwa uwazi bila shaka kila mmoja atapata kitu cha kuweka tumboni.

“Kile kimeturegesha nyuma ni ubaguzi wa wazi kwani unaona wazi asiyestahili kupata ndiyo anapokea msaada huo wa chakula. Kwa hivyo serikali ije na mikakati kabambe itakayonufaisha wanaostahili.,” alisema Bw Mwangu.

Alisema cha muhimu pia ni kuona ya kwamba hali ya usalama inaimarishwa ili mambo iende shwari wakati wa kusambaza chakula hicho.

Wakazi hao pia walisema watu wengi katika kijiji hicho wanahitaji chakula ambapo idadi kamili inazidi watu 20,000.

Hata hivyo, wiki iliyopita Gavana wa Kiambu Dkt James Nyoro alisema amepata malalamiko mengi kutoka kwa wakazi kuwa chakula cha msaada hua hakiwafikii wakazi hao jinsi inavyostahili.

“Nitahakikisha majina yote ya wanaostastahili kupewa chakula orodha inapitishwa afisini mwangu ili yakaguliwe kwanza,” alinukuliwa akisema alipozuru kijiji hicho.

Alisema mpangilio maalum utafanywa ili angalau kila mmoja apate chakula kwa sababu “kuna chakula cha kutosha.”

Jamii ya Wamakonde yalalama imetengwa katika ugavi wa chakula

Na MISHI GONGO

JAMII ya Wamakonde wanaoishi eneo la Makongeni, Msambweni katika Kaunti ya Kwale, ina malalamiko kuhusu kutengwa katika ugavi wa chakula unaoendelea katika kaunti hiyo.

Wanasema japo Rais Uhuru Kenyatta aliitambua jamii hiyo kuwa kabila la 43 nchini, wameendelea kubaguliwa katika ugavi wa misaada ya chakula kinachoendelea kutolewa kuwasaidia wasiojiweza katika jamii kipindi hiki ambapo janga la corona limelemaza shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Baadhi ya wakazi hao wamelalamikia majina yao kutolewa katika orodha ya wanaofaa kusaidika na misaada ya chakula kutoka kwa serikali ya kaunti kwa kile wanachokitaja kuwa ni viongozi kudai kwamba jamii hio haitambuliwi

Maureen Thomas akisikitishwa na jinsi alivyokosa nafasi katika mradi wa kazi mtaani ulioanza siku tatu zilizopita ili kuwapiga jeki vijana wakati huu ambapo taifa linapigana na janga la corona.

Hata hivyo, mzungumzaji wa jamii hiyo aliwataka wakazi hao kuwa na subira shughuli hiyo itakapoendelea.

Awali Gavana wa Kaunti ya Kwale Salim Mvurya aliwahakikishia wakazi wa kaunti hiyo kuwa familia zote zisizojiweza zitanufaika na chakula hicho.

Wazee wamlaani gavana kuzuia mbunge kuwapa chakula

Na TITUS OMINDE

WAKONGWE wanaoishi katika mitaa ya mabanda katika Kaunti ya Uasin Gishu wamemshtumu Gavana Jackson Mandago kwa madai ya kumzuia mbunge wa Kesses, Bw Swarup Mishra kuwasambazia chakula cha msaada.

Chakula hicho kililenga kusambaziwa wazee wapatao 12,000 katika Kaunti-ndogo ya Kesses.

Wazee walengwa walidai kuwa hatua hiyo ilichochechewa kisiasa, licha ya Gavana Mandago kusisitiza kwamba hatua hiyo ililenga kuwalinda dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona.

Idadi kubwa ya wazee hao ambao wanaishi katika mtaa wa Sukunanga na Langas walisema ishara ya Dkt Mishra ilikuwa baraka iliyowasili kwa wakati muafaka. Walisema tangu kutangazwa kwa kafyu wameathiriwa vibaya na njaa.

“Dkt Mishra alikuwa malaika aliyetumwa na Mungu kutulisha na sasa amesimamishwa, serikali hii inataka tufe! Wametukataza kwenda mjini kuomba chakula na sasa wamemzuia Dk Mishra kutulisha,” alisema Bwana Steven Wanjio, mzee kutoka eneo la Sukunanga.

Kwa sasa wanataka serikali ya kaunti kushirikiana kwa haraka na Dkt Mishra na kuasambazia chakula hicho kwa kufuata hatua zote za kinga dhidi ya virusi.

Walitoa wito kwa Kamishna wa kaunti ya Uasin Gishu Abdirisack Jaldesa aingilie kati.

“Tunajua kamishna wetu si kiongozi wa kisiasa ana nia njema kwetu,tunatumai kwamba ataingilia kati na kuhakikisha tunapata chakula chetu kutoka kwa Dk Mishra,” alisema mmoja wa wazee hao.

Dkt Mishra amefichua kuwa eneo bunge lake limetenga shilingi 30 milioni kwa kununua na kusambazia wazee chakula cha msaada kwa wazee 12,000 katika wadi za Tarakwa, Kipchamo-Chereleret, Chuiyat / Tulwet na Racecourse kwa mwezi mmoja ujao.

Wakati huo huo baadhi ya wakaazi wa kaunti ndogo ya Kesses walikosoa njia ya usambazaji wa chakula hicho kutokana na hofu ya kuenea kwa Covid -19 katika mikutano iliyopangwa ili kugawa chakula hicho.

Jumapili, Kamishna wa kaunti ya Uasin Gishu alipiga marufuku usambazaji wa chakula katika eneo hilo baada ya kukutana na mbunge husika.

Kamshna huyo alisema akisema zoezi hilo linaweza kusababisha kuenea kwa virusi vya korona iwapo hatua za kiafya hazitachukuliwa.

 

Mashirika, viongozi waanza kutoa chakula cha msaada

Na WAANDISHI WETU

SERIKALI za Kaunti, viongozi wa makanisa na mashirika mbalimbali wameanza kutoa vyakula kwa familia zisizojiweza wakati nchi inaendelea kupambana na janga la virusi vya corona.

Serikali ya kaunti ya Mombasa imekusanya Sh13.5 milioni katika mradi utakaohakikisha zaidi ya familia 20,000 zimepata chakula cha msaada iwapo serikali itatangaza marufuku ya kutotoka nyumbani.

Mradi huu ulioanzishwa na Gavana wa Mombasa, Hassan Joho, unatarajia kukusanya zaidi ya Sh700 milioni ambazo zitasaidia kila familia kupata vyakula.

Akiongea Jumamosi wakati wa kuwashukuru wafadhili, wakiwemo wafanyibiashara katika kaunti hiyo, Bw Joho aliwarai watu wengi kujitokeza ili kusaidia, akisisitiza kuwa shughuli hiyo itafanywa kwa uwazi bila mapendeleo yoyote.

“Huu ni wakati wetu kutoa na kusaidiana. Iwapo hali hii itazidi, itabidi tulazimishe watu kukaa nyumbani. Hivyo basi lazima tutafute njia ya kuwasaidia,” Bw Joho alisema.

Kaunti hiyo pia ilisema itahitaji angalau Sh3,380 kulisha familia ya watu watano kila wiki.

Wakazi wanatarajia kupokea kilo 10 za mchele na unga wa ugali. Kilo saba za ndengu, mbili za sukari, lita tatu za mafuta ya kupika na pakiti mbili za sodo.

Visima 30 pia vinatarajiwa kuchimbwa kwa kila wadi ya kaunti hio.

Wakazi pia watapewa dawa za maumivu kwa kila familia baada ya mfanyibiashara mmoja kutoa dawa milioni moja almaarufu Paracetamol.

Kwingineko, katika barua iliyoandikwa Aprili 3 kwa makasisi wa dayosisi ya Mombasa, Askofu Martin Kivuva alisema tayari wameunda kamati ya kushugulikia dharura zinazoletwa na maradhi ya COVID-19, na itakusanya vyakula na fedha.

Pia, itapokea msaada kutoka kwa wasamaria wema, itasambaza bidhaa kwa watu wasiojiweza na kufanya kazi kwa ukaribu na mashirika mengine kuhakikisha wanahamasisha umma kuhusu virusi hivyo.

Katika kijiji cha Kiandutu mjini Thika mnamo Jumamosi, maskini na walemavu wapatao 200 walipokea msaada wa unga na mikate.

Spika wa bunge la kaunti ya Kiambu Bw Stephen Ndichu shughuli ya kusambaza msaada hiyo.

Aliyemwakilisha spika kwenye shughuli hiyo, Bw Francis Kilango, alisema walemavu wengi na maskini katika kijiji hicho wamepitia masaibu mengi huku wengi wao wakikosa chakula cha kila siku.

Alisema wengi wao hawana maji ya kunawa, sabuni, huku wakiwa katika hatari kubwa ya kupata maambukizi ya virusi.

Askofu Kilango alisema kijiji cha Kiandutu ambacho kina idadi ya wakazi zaidi ya 20,000 kinahitaji msaada wa dharura kwa kuwa bado wakazi hao hawazingatii hali ya usafi kutokana na hali ya maisha kuwa ngumu.

Naye mbunge wa Kimilili, Didimus Barasa alinunua magunia 200 ya mahindi yatakayogawanywa kwa familia maskini iwapo marufuku ya kutoka nje itawekwa.

Na katika eneo bunge la Kesses, kaunti ya Uasin Gishu, Mbunge wa sehemu hiyo Swarup Mishra (pichani) alinunua shehena kubwa ya chakula ambacho kitasambazwa kwa wazee katika kaunti hiyo.

Tayari Gavana wa sehemu hiyo Jackson Mandago amepiga marufuku wazee kuingia mijini.

Ripoti za DIANA MUTHEU, SIAGO CECE, LAWRENCE ONGARO na BRIAN OJAMAA

Hakuna chai wala chakula kwa maseneta kikaoni

NA DAVID MWERE

HUKU maseneta wote 67 wakikongamana Jumanne baada ya Seneti kusitisha vikao vyake hapo Machi 17 kutokana na janga la corona, watalazimika kuandaa kikao bila vitafunio walivyozoea wakati wanajadili masuala muhimu.

Hakutakuwa na vyakuala wala staftahi kama chai kwa viongozi hao. Hata hivyo, maji yatakuwa kwa wingi,

Kama sehemu ya mabadiliko yaliyowekwa huku watu wengi wakiendelea kuugua virusi vya corona nchini, itakuwa lazima kwa maseneta hao kunawa mikono kwanza kabla ya kuingia kwa eneo la mijadala, huku vioefu vikiwekwa kila mahali.

Shughuli ya kwanza itakuwa kusomwa kwa ujumbe kutoka kwa Bunge la Kitaifa kuhusu Mswada wa Ugavi wa Mapato 2020, kisha mswada huo kusomwa kwa mara ya kwanza katika kikao hicho.

 Mswada huo, ambao unatoa taarifa za ugavi wa mapato baina ya serikali kuu na zile za kaunti, ulipitishwa Machi 17 katika Bunge la Kitaifa kisha kupelekwa kwa Seneti ili kupelelezwa.

Mswada huo unatoa Sh2.7 trilioni za matumizi ya taifa huku Sh1.78 trilioni zikitengewa serikali ya kitaifa na Sh316 bilioni zikipewa serikali za kaunti kugawana.

IMETAFSIRIWA NA FAUSTINE NGILA

CORONA: Wakazi waonywa dhidi ya kula sahani moja

Na WAWERU WAIRIMU

SPIKA wa Bunge la Kaunti ya Isiolo Hussein Roba amewarai wakazi wakomeshe utamaduni wa kula kwenye sahani moja, wakati huu maambukizi ya virusi vya corona yanaendelea kutikisa nchi.

Wakazi wa jamii za kuhamahama na Waislamu huwa na tabia ya kula kutoka kwa sahani moja, itikadi ambayo inaweza kuwaweka kwenye hatari ya kuambukizwa virusi vya corona.

‘Ninawaomba wakazi hasa Waislamu kujizuia kula kwenye sahani moja hadi hivi virusi vituondokee,’ akasema Bw Roba.

Miongoni mwa jamii nyingi za Waislamu, kawaida chakula huwekwa kwenye sahani moja kubwa na kila mtu akamega kutoka upande wake.

Spika huyo pia aliamrisha kwamba sehemu ya Sh40 million ambazo zilipitishwa na bunge la kaunti ili zitumike kupigana na ueneaji wa corona, zitumike kuwafidia wafanyabiashara ambao wanaendelea kupata hasara kutokana na janga hilo.

Alisema serikali ya Gavana Mohammed Kuti inafaa kushirikiana na machifu na manaibu wao katika kutambua wafanyabiashara ambao wameathirika zaidi ili wapewe msaada wa kifedha.

‘Tutunzane na kujali maslahi ya majirani wetu. Tusihodhi vyakula ilhali wenzetu ambao mapato yao yameathirika wanalala njaa,’ akaongeza.

Pia aliwataka wazazi wawe waangalifu na kuwazuia watoto wao kurandaranda maeneo tofauti kama tahadhari ya kuwazuia wapate virusi vya corona.

Aliwahimiza wakazi kuheshimu na kuzingatia mikakati iliyotolewa na Wizara ya Afya kama vile kunawa mikono na kuzingatia kiwango vya juu vya usafi nyumbani na maeneo ya umma.

FAO yaonya uvamizi wa nzige unahatarisha upatikanaji wa chakula

Na MAGDALENE WANJA

SHIRIKA la Chakula na Kilimo (FAO) la Umoja wa Mataifa limetoa onyo likisema kwamba uvamizi wa nzige unaoshuhudiwa katika baadhi ya mataifa ya Afrika Mashariki ni tishio kubwa kwa upatikanaji wa chakula.

Kufikia sasa, mataifa yaliyoathirika zaidi ni pamoja na nchi za Ethiopia, Kenya, na Somalia na Uganda likiwa la hivi karibuni.

Katika taarifa iliyotolewa na shirika hilo, nzige wa jangwani ni tishio kubwa kwa upatikanaji wa chakula cha kutosha na kwa maisha ya watu katika eneo la Pembe ya Afrika.

“Mataifa ya Afrika Mashariki yamekekuwa yakikabiliana na nzige tangu mwaka wa 2020 kwa kile kinachotambuliwa kama uvamizi mbaya kuwahi kutokea katika eneo hilo,” ilisema taarifa hiyo.

Mtaalamu wa masuala ya mazingira na Afrika wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) Richard Munang aliyenukuliwa katika taarifa hiyo alisema kuwa mara nyingi, nzige wa jangwani huwa katika maeneo kame na jangwani.

Sehemu hizi ni pamoja na baadhi ya nchi barani Afrika, Maeneo ya Asia Mashariki na Kusini Mashariki mwa Asia.

“Haya ni maeneo ambayo hushuhudia kiwango cha mvua chini ya milimita 200 kila mwaka. Katika hali ya kawaida, idadi ya nzige hupungua kupitia kufa wenyewe au kwa kuhama,” alisema Bw Munang.

Kulingana na Bw Munang, hali ya hewa na tabianchi pia huvutia kuongezeka kwa nzige.

Kuongezeka kwa mvua kuliko kiwango cha kawaida kulishuhudiwa kwenye Pembe ya Afrika tangu Oktoba hadi Desemba mwaka wa 2019.

Alishauri kuwa wadudu hao wanaweza kudhibitiwa kwa kunyunyiziwa kemikali za oganofosfeti.

Nchini Kenya, zaidi ya kaunti 15 zimeathirika na nzige hao ambao wanazaana kwa kasi.

Nzige ni chakula kizuri, wataalamu washauri

Na WINNIE ATIENO

WATAALAMU wa hali ya hewa na tabianchi na wenzao wa lishe bora wamewasihi Wakenya wavune nzige waliovamia zaidi ya kaunti 10 nchini na kusababisha uharibifu mkubwa wa mimea.

Aidha wanasema nzige hao wanafaa kuvunwa, kukaushwa na baadaye kutumiwa kama lishe kwa binadamu, samaki na hata kuku huku wakisisitiza kuwa wadudu hao wanaweza kutumiwa kudhibiti baa la njaa.

“Kuna baadhi ya jamii ambazo hula nzige ama wakiwa wabichi au hata wakiwa wamechomwa na kupikwa. Kimsingi, nzige ni chakula duniani na kumekuwa na mjadala mkuu endapo wadudu wanaweza kuliwa kama chakula hasa wakati kuna baa la njaa ulimwenguni,” akasema Dkt Richard Muita.

Akiongea kwenye kongamano la kudadisi hali ya hewa na tabianchi barani Afrika, Dkt Muita alisema nzige hao wana protini zaidi kuliko hata nyama ya ng’ombe.

“Nzige wanalika na wana protini; nakumbuka ujana wangu nilikuwa nawala sana. Tusiangalie ubaya wa uvamizi wa nzige hawa nchini, badala yake tudadisi umuhimu wa wadudu hawa ambao wanaweza kutumika pia kama lishe kwa kuku na samaki,” alisema.

Dkt Muita ambaye anafanya kazi katika idara ya utabiri wa hali ya hewa nchini, alisema wadudu hao wanaweza kuvunwa, kukaushwa juani na baadaye kuliwa.

“Hapo tutakuwa tumeweza kudhibiti uvamizi huu, badala ya kunyunyizia dawa,” alisema.

Mtaalamu wa lishe bora, Bi Martina Adega alisema ulaji wa wadudu hao unaweza kupunguza maradhi ya moyo ikizingatiwa nzige wana protini.

Hata hivyo, changamoto kuu ambayo Kenya inakodolea macho ni ukosefu wa mashine za kutengeneza vyakula vya mifugo.

“Hata kama tunadhamiria kuvuna nzige hao, watakaushwa wapi? Je, tunamashini ya kuzisaga ili tutengeneza vyakula vya wanyama kama paka, mbwa, kuku, samaki?” aliuliza Bi Adega.

Alisema protini inayopatikana katika nzige ni ya ubora wa hali ya juu.

Naye mfanyakazi wa Wizara ya kilimo, Bw James Wanjohi, alisema wadudu hao walivamia Kenya Disemba 28, 2019, na kufikia sasa serikali imejizatiti kukabiliana na wadudu hao ili wasiendelee kuharibu mimea.

Bw Wanjohi alisema maafisa wengi wanafaa kupewa mafunzo ya kukabiliana na wadudu hao.

Kuku ndicho chakula maarufu nchini Kenya – Ripoti

Na MARY WANGARI

IDADI kubwa ya Wakenya hupendelea kuagiza mlo wa kuku na pizza ambavyo ni miongoni mwa vyakula vilivyojitwalia umaarufu mkubwa zaidi mtawalia nchini, ripoti mpya imesema.

Kulingana na ripoti ya Orodha ya Jumia kuhusu Vyakula 2019, iliyoangazia mikondo ya chakula katika kipindi cha miaka mitatau iliyopita, mlo wa kuku uliorodheshwa kama chakula maarufu zaidi kinachoagizwa miongoni mwa Wakenya.

Mlo wa Pizza ulichukua nafasi ya pili kwa umaarufu huku kaimati za nyama (burgers) zikiruka hadi nafasi ya tatu kutoka nafasi ya tano mnamo 2017, kulingana na ripoti hiyo.

Ripoti hiyo vilevile ilionyesha kuwa japo umaarufu wa chakula cha India umedorora, mlo huo ungali umeshikilia nafasi ya tano.

Aidha, ripoti hiyo ilionyesha kuwepo tofauti katika ladha baina ya miji mbalimbali Kenya. Huku wakazi wa Nakuru wakiibuka kupendelea chakula cha China, wenzao wa Nairobi hupendelea kuagizia mlo wa kuku, pizza na burgers nao wateja wa Mombasa wakiegemea zaidi vyakula vya kimataifa.

Mkurugenzi wa Jumia Food Kenya kuhusu Huduma zinazoagiziwa Afrika Mashariki, Shreenal Ruparelia, alisema takwimu za Jumia zilizokusanywa kwa kipindi cha miaka saba iliyopita, ziliashiria kuwa vichocheo vya ukuaji wa huduma za uagiziaji vyakula ni pamoja na kuwepo bei nafuu, uhamasishaji na uwezo wa kupatikana katika eneo fulani la kijiografia.

“Kiamsha kinywa na chamcha vinageuka kuwa maarufu zaidi huku umaarufu wa chamcha ukipanda hadi asilimia 4.6 mwaka huu ikilinganishwa na asilimia 3.8 mnamo 2017.

“Chamcha kiko katika asilimia 41.1 mwaka huu 2019 kutoka asilimia 36.2 mnamo 2017,” alisema Bi Ruparelia.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa ripoti hiyo Nairobi, Bi Ruparelia alisema mabadiliko hayo yalichangiwa na hali ya kuongezeka kwa vituo vya vyakula vinavyouza vyakula kwa bei ya chini hata kwa Sh300.

Kwa mujibu wa data iliyokusanywa, hata hivyo, mkurugenzi huyo alieleza kuwa maagizo ya chajio yalipungua hadi asilimia 54.2 mwaka 2019 kutoka asilimia 60 mnamo 2017.

Vyakula vinginevyo maarufu vilivyo na uwezo wa kukua zaidi ni pamoja na vyakula vya India, Uhabeshi, na Thai.

KILIMO NA BIASHARA MASHINANI: Kilimo cha mboga za aina tofauti kimesaidia aweze kulipia wanawe karo

Na CHARLES ONGADI

WAKULIMA wengi Kaunti ya Kisumu walikuwa na dhana kwamba kilimo cha mboga hakiwezi kushamiri kama ilivyo kwa kilimo cha miwa, pamba na mpunga.

Japo baadhi walilima mboga na matunda eneo hili lakini shingo upande, hawakuamini kwamba kiliweza kuwa kitega uchumi kwao.

Hata hivyo, Bi Mary Odenya kutoka kijiji cha Kamagaga, lokesheni ya Ombeyi kaunti ndogo ya Muhoroni, aliamua kuvalia njuga kilimo cha mboga aina mbali mbali .

“Wengi hapa waliamini kuwa kilimo cha mpunga na miwa pekee ndicho kinaweza kuwakwamua kiuchumi,” anasema Mary ambaye ni mjane.

Kulingana naye, maisha yalibadilika mumewe alipofariki 1991.

Aliwaza na kuwazua jinsi ambavyo angewalea wanawe ambao ndio walikuwa wako shule za chekechea na msingi.

“Nilianza maisha magumu kwa kuajiriwa kama mpishi katika mojawapo ya shule ya upili eneo hili kwa mshahara wa ksh 4,500 kwa mwezi,” anasema.

Hata hivyo, kadri miezi na miaka ilivyoyoyoma ndivyo maisha yalivyozidi kuwa magumu huku akikosa fedha za kuwalipia karo wanawe ambao walikuwa katika shule za upili.

Mnamo 2001, aliamua kujitosa kikamilifu katika kilimo cha mboga akianza na sukumawiki, lengo likiwa kujiinua kiuchumi.

Lakini mambo hayakumwendea vyema katika miaka ya mwanzo hadi pale alipoamua kusaka ushauri kutoka kwa wataalam wa kilimo eneo la Kisumu.

Anasema, mambo yalianza kumnyookea punde alipoanza kufuata kanuni za kilimo cha mboga hasa sukumawiki.

Kabla ya kupanda sukumawiki shambani, Mary huhakikisha ametengeza miche kwa kipindi cha siku 21.

Ni baada ya kumalizika kwa kipindi hicho ndipo anaipanda shambani huku akiwacha nafasi ya futi moja kutoka shimo moja hadi lingine na upana wa futi moja unusu. Kupata mboga za kuvutia na zinazonawiri, anatumia mbolea aina ya Sulphate na Urea.

Changamoto inayomkabili ni aina ya wadudu wanaotoboa matawi ya mboga hasa kipindi inapokaribia kukomaa.Anatumia dawa aina ya Halothin kuwakabili wadudu hao.

Shamba la sukumawiki la Bi Mary Odenya lililoko kijiji cha Ombeyi, Kaunti ya Kisumu. Picha/ Charles Ongadi

Ukosefu wa maji wakati wa kiangazi pia hutatiza kilimo chake na wakati mwingine hulazimika kukodisha mashine ya kuvuta maji kutoka mto ulio karibu na kunyunyizia shambani mwake.

Kulingana na Mary, mboga za sukumawiki huchukua siku 21 pekee kuanza kuvunwa na kipindi cha kati ya mwaka hadi miaka miwili ikiendelea kuvunwa.

Mara baada ya kuanza kupata faida katika kilimo cha sukumawiki, alijitosa katika kilimo cha mboga za kienyeji kama sagaa, mchicha na mnavu.

“Wengi wamebadilisha mtindo wao wa kula wakizingatia sana mboga za kienyeji jambo ambalo limenipatia faida na kuweza kubadilisha maisha yangu na familia yangu,” anaeleza.

Anavuna mara mbili kwa wiki ambapo anatia kibindoni kiasi cha Sh3,800 kwa sukumawiki, Sh2,500 kwa sagaa, Sh2,400 za mchicha na Sh 1600 kwa mboga za mnavu.

Wateja wake hufika asubuhi na mapema kila siku ya mavuno na kumrahishia mwendo wa kufika sokoni ama kuchuuza kwa wateja wake.

Kati ya mafanikio aliyoyapata hadi kufikia sasa katika kilimo cha mboga ni kwamba anawalipia karo wanawe wawili ambao ni watahiniwa wa Mtihani wa Kidato cha Nne mwaka huu na mmoja aliye katika chuo kikuu.

“Nawahimiza akina mama wenzangu hasa wajane eneo hili wasiketi wakisubiri kusubiri kuletewa kila kitu na warithi bali kujizatiti kwa kilimo ambacho ni uti wa mgongo maishani,” anasema.

Kwa sasa mama huyu ana mipango ya kukodisha shamba ekari moja zaidi ili kupanua kilimo chake.

WATU NA KAZI ZAO: Ukakamavu umemwezesha kujiimarisha licha ya changamoto

Na SAMMY WAWERU

BI Irene Maina amesomea upishi, na ni taaluma aliyoienzi tangu akiwa na umri mdogo.

Alifanikiwa kupata nafasi ya ajira Maralal, Kaunti ya Samburu.

Hata hivyo, baada ya kuifanya kwa miaka kadha aliipoteza mwaka 2012 na ni wakati anaosema aliihitaji kwa hali na mali.

“Nilikuwa nimejaaliwa mtoto akiwa na umri wa miaka miwili wakati huo,” anasema Irene.

Anasimulia kwamba hakuwa na budi ila kuungana na jamaa zake jijini Nairobi, ili kumsitiri pamoja na malaika wake.

Akufaaye kwa dhiki ndiye rafiki.

Irene anasema dada yake mzawa alimpokea, ingawa hakuhisi kutaka kuwa ‘mzigo’ kwake kwani pia alikuwa na familia yake. Isitoshe, chochote alichomiliki Maralal alikiacha kwa sababu ingekuwa ghali kusafirisha.

Aliyetarajia kufunga naye pingu za maisha, alisalia kimya wakati akipitia changamoto zote hizo. Hiyo ni licha ya kuwa nguzo yake kuu, hususan kumpiga jeki katika biashara.

“Hakuna jambo gumu maishani kama kujisimamia halafu unafilisika ghafla,” anasisitiza mama huyo wa mtoto mmoja.

Kwa kuwa alipokuwa kazini alikuwa mtu wa watu, na aliwatendea wema, dada yake hakuona ugumu wowote kumfaa.

Kulingana na Irene, alipata kazi ya uuzaji wa bima katika kampuni moja ya bima jijini Nairobi na ndipo alihamia eneo la Thika. Anasimulia kwamba dadake alimsaidia katika harakati hizo, na hata kugharamia kodi ya nyumba na mahitaji mengine.

Gange hiyo haikuwa rahisi kama alivyodhania, kwani ilikuwa na changamoto zake. Cha kusikitisha aliiraukia asubuhi na mapema, ikizingatiwa kwamba sharti angeandaa mwanawe na kumpeleka shuleni.

“Jioni mkondo ulikuwa ule ule wa marathon, kuendea mtoto shuleni, kumfulia sare na mavazi yake ya nyumbani na kumpikia. Keshoye pia nilitarajiwa ofisini. Ilikuwa kazi ya machovu,” anafafanua.

Mwanawe alikuwa angali mdogo, na wataalamu wa masuala ya watoto, wanasema mama ambaye ni mzazi wa karibu anapaswa kuwa sako kwa bako na mtoto kwa muda hadi atakapokomaa.

“Watoto pia hukumbwa na mawazo hasa wanapokosa uwepo wa mama. Lugha na malezi ya mama hayaambatani na ya yaya au mlezi tofauti. Kuna yale mapenzi ya mama kwa mtoto, yanayomfanya kukua kimawazo,” anaeleza Bi Karungari Mwangi, muuguzi mstaafu ambaye ni mtaalamu wa masuala ya watoto, wakiwamo ambao hawajafikisha umri wa kuzaliwa (pre-term babies) pamoja na masuala ya lishe.

Kwa mujibu wa maelezo ya mdau huyo, ni muhimu mama hata akiwa kazini kupata muda wa kutosha haswa jioni na likizo kutangamana na kucheza na mwanawe, akiwa angali mchanga.

“Muda anaotangamana naye ni muhimu katika malezi na ukuaji wa mtoto,” anahimiza.

Ni kufuatia ushauri unaowiana na huo Irene Maina alikata kauli kuacha kazi hiyo na kuwekeza katika biashara 2017.

“Biashara yenyewe ilinoga hadi mwanzoni mwa mwaka huu, 2019, nikaamua kuifunga kwa sababu nilianza kukadiria hasara,” anasema.

Mama huyu anasema pandashuka alizopitia awali zilimfanya kuwa mkakamavu, na kumtegemea Mungu kwa kila jambo. Licha ya kufunga biashara asijue atakachofanya kukimu mwanawe, Irene anasema alijaaliwa kupata kandarasi ya usafirishaji wa mawe ya ujenzi, gange anayoifanya kufikia sasa.

Hali kadhalika, amefufua taaluma yake ya upishi anayosema imenoga.

“Ninafanya mapishi ya nje (outside catering). Hasa tunapokaribisha msimu wa Krismasi, ninapata oda chungu nzima za kupika katika harusi,” aeleza.

Anaambia Taifa Leo kwamba anapania kufungua biashara yake ya chakula na mengineyo yanayohusu upishi, ambapo kwa sasa anashughulikia vifaa vya mapishi kama vile majiko, sufuria na vihifadhio vya chakula.

Mwanauchumi na mhasibu Charles Mwangi, anasema hilo ataliafikia upesi ikiwa amekuwa akiweka akiba.

“Ni muhimu unapofanya kazi ujifinze kufunga mshipi wa tumbo, ukilipwa mshahara wa Sh20, weka akiba ya Sh5. Haijalishi kidogo unachoweka kando, kitakufaa kuafikia malengo yako maishani,” anashauri Bw Mwangi.

ONYANGO: Rais alifaa kuwa mstari wa mbele Siku ya Chakula Duniani

Na LEONARD ONYANGO

ULIMWENGU, siku mbili zilizopita, uliadhimisha Siku ya Chakula Duniani japo maadhimisho hayo yalionekana ‘kama vile’ yalipuuzwa humu nchini.

Baadhi ya Wakenya walichangamkia maadhimisho hayo kupitia mitandao ya kijamii kama vile Twitter na Facebook lakini wengi walikuwa wakifuatilia kwa karibu shughuli ya uzinduzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kutoka Nairobi hadi eneo la Suswa (Kaunti ya Narok) iliyoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta.

Wizara ya Kilimo pia ilionekana kutotilia maanani maadhimisho hayo.

Maadhimisho ya kitaifa yaliongozwa na Katibu wa Wizara ya Kilimo Hamada Boga kwenye Taasisi ya Mafunzo ya Kilimo ya Kwa Kathoka, katika Kaunti ya Makueni.

Hafla hiyo ilitatizika baada ya kuvamiwa na wanaharakati wa vuguvugu la GreenPeace Africa waliobeba mabango ya kuitaka serikali kuelekeza nguvu zake katika suala la uzalishaji wa chakula badala ya kusema tu bila kutenda.

Waziri wa Kilimo Mwangi Kiunjuri bila shaka alihudhuria hafla ya uzinduzi wa reli ya SGR.

Uzalishaji wa chakula cha kutosha nchini ni miongoni mwa nguzo kuu za maendeleo ambayo Rais Kenyatta ameahidi kutekeleza ili kukumbukwa na Wakenya atakapostaafu 2022.

Hivyo, ilitarajiwa kwamba Rais Kenyatta au Waziri Kiunjuri angetumia siku ya Oktoba 16, kuwaelezea Wakenya hatua ambazo serikali imechukua kuboresha sekta ya kilimo kuwezesha Kenya kuwa na chakula cha kutosha kufikia 2022.

Ripoti kuhusu hali ya chakula duniani ya 2019 iliyoandaliwa na Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa (FAO) inaorodhesha Kenya miongoni mwa mataifa yanayohitaji chakula kwa dharura.

Kulingana na ripoti hiyo, Kenya inakumbwa na uhaba wa chakula sawa nchi kama vile Sudan, Yemen, Zimbabwe, Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) kati ya mataifa mengine ambayo yamekuwa yakikumbwa na machafuko ya mara kwa mara.

Ripoti ya FAO pia inaonyesha kuwa Kenya ni miongoni mwa nchi zaidi ya 30 za Afrika ambapo mamilioni ya watu wako katika hatari kubwa ya kukosa chakula.

Lishe bora

Kila Mkenya ana haki ya kupata lishe bora kwa mujibu wa Kifungu cha 43 cha Katiba. Kulingana na Katiba, kuwa kila Mkenya anafaa kulindwa dhidi ya makali ya njaa.

Mabadiliko ya tabianchi yamechangia katika kuzorota kwa uzalishaji wa chakula nchini kutokana na ukame au mafuriko yanayosababisha uharibifu wa mazao.

Inatabiriwa kuwa mavuno yataendelea kudorora kwa kiwango kikubwa kutokana na mabadiliko ya tabianchi.

Kando na changamoto hizo, ufisadi pia umekita mizizi katika sekta ya kilimo. Wakenya wangali hawajavuna matunda ya mradi wa unyunyiziaji maji wa Galana Kulalu licha ya walipa ushuru kutumia mabilioni.

Mabadiliko ya tabianchi, ufisadi na sera duni zimechangia katika uwepo wa njaa kila mwaka humu nchini.

Hivyo, tulitarajia serikali kutueleza hatua ambazo imechukua katika kuhakikisha kwamba Kenya inakuwa na chakula cha kutosha.

Siku ya Chakula Duniani: Kenya ingali inakabiliwa na ukosefu wa chakula cha kutosha

Na MAGDALENE WANJA na BARNABAS BII

HUKU ulimwengu ukiadhimisha Siku ya Chakula Duniani – World Food Day – leo Jumatano, Kenya ni mojawapo ya nchi ambazo zinaendelea kukabiliana na tatizo la njaa.

Kufikia Julai 2019, zaidi ya Wakenya 2 milioni walikuwa wanakabiliwa na ukosefu wa chakula.

Hii ni licha ya Kenya kutegemea ukulima kwa njia kubwa zaidi kujikimu kiuchumi.

Ukulima huchangia katika uchumi wa nchi kwa kiwango cha asilimia 24.

Kulingana na ripoti ya mwaka 2019 ya Taasisi ya Masomo ya Usalama – Institute for Security Studies – ili kufikia hatua ya kuwa na hakikisho la chakula cha kutosha kufikia mwaka 2030, iitahitajika kuongezea mapato na mavuno ya chakula kwa asilimia 75.

“Wakenya 3.4 milioni wameathirika na makali ya njaa kwa kiwango kikubwa ambapo 309,000 wamelazimika kuhama kutoka kwa makazi yao kutokana na njaa,” inasema sehemu ya ripoti hiyo.

Kaunti zilizoathirika zaidi ni zile za Marsabit na Turkana.

Mada kuu ya mwaka 2019 ni ‘Vitendo Vyetu Ndiyo Mustakabali Wetu: Lishe Bora kwa Dunia Isiyo na Njaa’ yaani kwa Kiingereza ‘Our Actions Are Our Future, Healthy Diets for A #ZeroHunger World’.

Bei ya mahindi

Haya yanajiri huku tayari bei ya unga wa mahindi ikitarajiwa kupanda tena baada ya wasagaji kumaliza magunia milioni 1.9 ya mahindi ambayo yalitolewa na serikali kwa bei nafuu Septemba 2019.

Hali imeharibiwa zaidi na kupungua kwa uagizaji mahindi kutoka Uganda na Tanzania.

“Uhaba wa mahindi nchini pamoja na upungufu wa uagizaji kutoka Uganda na Tanzania umefanya bei ya mahindi kupanda. Jinsi ilivyo kwa sasa, hatutakuwa na budi ila kupandisha bei ya unga,” akasema Bw David Kosgey, mmoja wa wasagaji mahindi mjini Eldoret.

Kiwango cha mahindi kinachoingizwa kutoka Uganda kimepungua katika muda wa miezi miwili iliyopita na kufanya gunia la kilo 90 kuuzwa kwa Sh3,200 kutoka Sh2,800.

Mahindi kutoka Tanzania yanauzwa kwa Sh3,400 kutoka Sh3,000 kwa kila gunia la kilo 90. Kulingana na Baraza la Nafaka Afrika Mashariki (EAGC), uhaba wa mvua unaweza kufanya mavuno ya mahindi kupungua Uganda, Tanzania na Kenya na hivyo basi kusababisha bei ya unga kupanda zaidi.