CHOCHEO: Zidisha mashamsham, sizubae!

Na BENSON MATHEKA

DELO alikuwa katika mkutano muhimu kazini mchumba wake Jane alipompigia simu.

Hakuweza kuijibu na akamtumia arafa kumweleza angempigia baada ya mkutano.

“Ok, switi, nakupenda sana,” Jane alijibu.

Baada ya mkutano, Delo alirudi katika ofisi yake na kumpigia Jane.

“Nilitaka kukuambia nakupenda sana mpenzi wangu,” Jane alimwambia.

Delo alihisi msisimko wa ajabu.

Akafurahi na kumjibu; “Switi, nakupenda zaidi.”

Uhusiano wa wawili hao umejengwa kwa kubadilishana jumbe na kutendeana mambo ya kudekezana jambo ambalo washauri wa masuala ya mapenzi wanasema ni muhimu sana kwa uhusiano wa kimapenzi.

“Shangaza mtu wako kwa mambo madogo. Usipofanya hivyo atakushangaa tu na kuchoka na uhusiano wenu. Mpigie simu na kwa sauti tamu ya upole umweleze unampenda na kumkosa. Kufanya hivi kunamchangamsha na kumfanya akuwaze kila wakati,” asema Titi Mueni, Mkurugenzi Mwandamizi wa kituo cha Big Hearts jijini Nairobi.

Titi asema makosa wanayofanya watu wengi ni kusahau wachumba wao wanapoondoka nyumbani kwenda kazini na kuwakumbuka wakiwaona jioni au wanapopata shida.

“Inashangaza watu hawakumbuki wachumba wao wakiachana asubuhi hadi wanapokutana jioni. Uhusiano wa aina hii ni sawa na ghorofa iliyojengwa kwenye changarawe. Inaweza kubomoka wakati wowote,” asema Titi.

Wataalamu wanasema kuwa hata kama mtu ana shughuli nyingi, anafaa kuwa akimshtua mchumba wake kwa ujumbe wa mapenzi mara kwa mara.

“Kukosa kumkumbuka mtu wako siku nzima kwa mwezi au mwaka kunaashiria hatari kubwa katika uhusiano wenu. Ikiwa haumkumbuki au kumuwaza asipokuwa karibu, kuna tatizo katika penzi lenu,” asema Francis Otiso mshauri wa wanandoa katika kituo cha Maisha Mema jijini Nairobi.

Kulingana na Otiso, hali hii inaashiria kuvunjika kwa mawasiliano jambo ambalo ni sumu kwa uhusiano wa mapenzi na ndoa.

“Uhusiano thabiti wa kimapenzi hujengwa kupitia mawasiliano bora. Yakikosa au kukatika huwa kuna hatari,” asema Otiso.

Vinette Wambui, mwanadada mwenye umri wa miaka 34, anasema kuwa aliokoa uhusiano wake wa kimapenzi kwa kuimarisha mawasiliano na mtu wake.

“Kuna demu aliyekuwa akimmezea mate mpenzi wangu. Nilipohisi hatari ya kupokonywa mpenzi wa roho yangu, nilijipanga, nikawa namtumia jumbe, maua, na kumpigia simu nikijua hana shughuli nyingi za kikazi. Hatimaye aliniposa tukafanya harusi,” asema Vinette.

Mwanadada huyu asema amedumisha mtindo huo hadi wakati huu, ikiwa ni mwaka wa sita katika ndoa.

Titi asema kuna watu wanaokosa kwa kusitisha waliyokuwa wakiwafanyia wapenzi wao kabla ya kuoana.

“Badala ya kusitisha uliyokuwa ukifanyia mtu wako kabla ya harusi, unafaa kuzidisha. Ikiwa anafanya kazi mbali na wewe, usilale bila kuwasiliana naye. Mrushie mabusu kwenye hewa na atalala akikuota ilivyokuwa alipokuwa akikurushia mistari,” asema Titi.

Mtaalamu huyu asema mawasiliano hayafai tu watu wakiwa mbali.

“Mtu wako akiwa nyumbani, usimpuuze uzame kwa mtandao. Mshirikishe kwa mambo anayopenda. Mpapase, mdekeze na umpikie mlo anaopenda. Ukifanya hivi utachota akili na roho yake na uhusiano wenu utakuwa imara,” aeleza Titi.

Kulingana na Otiso, mawasiliano ni moto unaoyeyusha matuta na matatizo yoyote yanayoweza kuibuka katika uhusiano wa kimapenzi.

“Tafiti kote ulimwenguni zimethibitisha kuwa mawasiliano yakisukwa vyema, ni tiba ya matatizo yanayovuruga mahusiano ya kimapenzi na kuvunja ndoa nyingi,” asema. Titi asema tatizo ni watu kuzoeana hasa baada ya kuoana.

“Shida ni kuwa watu wakiolewa au kuoa huwa wanahisi kuwa wamefika, wanamiliki wake na waume zao badala ya kupalilia uhusiano wao,” asema. “Kumiliki mtu wako ni kumuonyesha unamjali na hii ni kuimarisha mawasiliano,” aongeza.

CHOCHEO: Ukitunzwa, jitunze!

Na BENSON MATHEKA

VISA vya watu kumezea mate wachumba wa watu vimeongezeka na wakati mwingine kuzua maafa.

Pia imekuwa kama jambo la kawaida walio katika ndoa kuwa na mipango ya kando bila kujali athari zake.

Wanaume waliooa wamekuwa wakiweka vimada, wanawake nao wakiwa na masponsa.

Baadhi ya wanaohusika na michepuko hii wanadai hawaridhishwi na wenzao.

Wataalamu wa masuala ya mahusiano wanasema kwamba tabia hii inayotishia maisha ya ndoa inaweza kuepukwa.

“Tiba ya michepuko ni moja tu. Mume kuheshimu mkewe na mke kuheshimu mumewe. Mke kutunza mumewe na mumewe kutunza mkewe. Hakuna kitu hatari kwa ndoa kama kupuuza mtu wako kwa hali yoyote ile,” asema mtaalamu wa masuala ya mapenzi Samuel Femi.

“Ukitunza mkeo au mumeo apendeze, hautaona urembo wa mwingine. Ukitunza mumeo, hatavutiwa na mwanamke mwingine. Nawe ukitunzwa na mtu wako, elewa anafanya hivyo kwa sababu yake na sio ya watu wengine,” aeleza Femi.

Mtaalamu huyu anasema baadhi ya watu hukosea kwa kuanza michepuko wanapotunzwa na wachumba wao.

“Ni uchungu kuona mtu ambaye umejitolea kwa hali na mali kumtunza apendeze, awe mwanamume au mwanamke, akikusaliti na kuanza kuchangamkia wengine. Hili sio jambo geni, limekuwa likitendeka na linaendelea kutendeka lakini matokeo yake ni balaa na hasara,” aeleza Femi.

Kulingana na Bestella Auma, mwanasaikolojia wa shirika la Tella Counselling Services, hakuna shubiri kali kama mwanamke kugundua kwamba mwanamume aliyetumia muda na rasilmali kumtunza anamezea mate mwanamke mwingine.

“Mwanamke hawezi kuvumilia ushindani kutoka kwa mwanamke mwenzake. Huwa anahisi amedharauliwa, kudunishwa na kutumiwa vibaya,” asema.

Auma anasema uhusiano wa kimapenzi huwa unanawiri wachumba wakishirikiana kama kundi.

“Mume na mke wanaofanya maamuzi pamoja kwa lengo la kushinda huwa wanapata matokeo mazuri yanayojenga uhusiano wao. Katika hali hii, heshima ya dhati ndiyo nguzo,” aeleza.

Anashauri wanaume kubaini kuwa wanawake wa nje wanaowamezea mate, huvutia kwa sababu kuna mtu anayechangia wawe hivyo, au wamewekeza katika maslahi yao.

“Ukiona vimeelea, jua vimeundwa au mtu amejinyima kitu katika juhudi za kutaka avutie. Nyasi inayowekwa maji huwa ya kijani kibichi kila wakati. Vilevile, wekeza katika urembo wa mtu wako kila wakati. Kila mwanamume anaweza kutamani mwanamke mrembo, lakini inachukua mwanamume kamili kufanya mwanamke kuvutia na kuwa mrembo,” aeleza Auma.

Femi anasema wanawake walio katika ndoa wanaomezea mate wanaume wengine wanafaa kusaidia waume zao waweze kufanikiwa maishani.

“Kufaulu kwa ndoa hakuhitaji kuwa na nyumba kubwa ya kifahari au gari kubwa jinsi baadhi ya wanawake wanaochepuka wanavyodhani. Unaweza kupata hivi vyote uwe na raha na ukose furaha. Ukisimama na mtu wako na umsaidie kujikuza, uhakikishe yuko nadhifu, kuwe na uwazi na uaminifu kati yenu, basi mtakuwa sawa,” asema.

Auma ambaye pia ni mhubiri anashauri watu kuwaombea wachumba wao kila siku ili kushinda majaribu ya kushiriki michepuko.

“Ulimwengu umeharibika na majaribu ni mengi. Usisubiri jambo mbaya litendeke ndio uombee mtu wako. Usisubiri hadi mtu wako atumbukie kwenye majaribu. Mkinge kwa maombi,” aeleza.

Femi anakubali kuwa maombi, hasa wachumba wakishiriki sala pamoja, wanaweza kuepuka majaribu mengi ukiwemo mchepuko.

“Kinachofanya watu kuzama kwenye mipango ya kando ni ushawishi kutokana na hali na watu wanaojumuika nao. Chagua marafiki wako vyema. Mtu mmoja hawezi kujenga uhusiano mwenzake akiuharibu. Mapenzi hunawiri pale mume na mke wanashirikiana na sio kuchangamkia mipango ya kando iliyowavuta kando,” asema Femi.

CHOCHEO: Usiwe mwepesi wa kumeza chambo

Na BENSON MATHEKA

“NIMEANGUKIA, Mike ana kila kitu nilichotamani kwa mchumba wa maisha yangu,” Lena alikumbuka Brigitte akimwambia alipompata Mike.

Hii ilikuwa miaka minne iliyopita na juzi alijipata akimfariji rafiki yake ambaye amepitia maisha magumu katika ndoa yake na Mike.

“Nimejifunza kitu kimoja muhimu katika uhusiano wa Brigitte na Mike; usishawishike haraka na mistari ya mwanamume. Hiyo mistari mitamu na chambo anachokurushia haziakisi hali halisi ya tabia yake au maisha ya baadaye mtakayokuwa nayo,” asema Lena.

Mwanadada huyu anakumbuka kwamba Brigitte alikataa ushauri wake na hata wa wazazi wake waliomtaka achukue muda kufahamu tabia za Mike.

“Alikuwa amepagawishwa na mwanamume huyo. Alikataa ushauri wa marafiki, pasta na wazazi wake waliomtaka asimchangamkie Mike kabla ya kumfahamu vyema. Nafikiri ni magari na utanashati wa mwanamume huyo uliomuingiza boksi haraka. Pili, Mike alikuwa akimpeleka kujivinjari nje ya nchi jambo ambalo wachumba wetu hawakuweza kutufanyia. Brigitte alijiona amefaulu tofauti na sisi ambao wapenzi wetu hawakuweza kumudu maisha ya anasa,” asema Lena.

Kulingana na Seth Kamau, mtaalamu wa masuala ya mahusiano wa kituo cha Abundant Love Care jijini Nairobi, watu wanaoshawishika haraka na mistari ya mapenzi huwa katika hatari ya kutumbukia katika majuto baadaye.

“Nyuma ya hiyo mistari mitamu kunaweza kuwa uchungu usioweza kumezeka. Nyuma ya kinachokuvutia kwa mtu kunaweza kuwa na hatari kubwa. Hivyo basi, kabla ya kumeza chambo, kuwa makini kwa kuwa kinaweza kuwa na sumu,” asema Seth.

Anasema watu wengi huwa wanakosa au kupuuza ushauri kuhusu wachumba walio na mistari mitamu wakishawishika kuwa wamepata waliotamani.

“Kuna wanaoshawishika haraka, wanafunga ndoa wakifikiri watakuwa na maisha ya raha kisha wanajipata katika balaa. Wengi wanagundua kuwa waliodhani ni malaika ni sawa na ibilisi wanaowatesa. Ule utamu uliokuwa kwenye mistari unakosekana na kuwa kilio,” asema.

Kulingana na Pasta Patrick Kweyu wa kanisa la Souls Paradise, Nairobi ambaye amekuwa akishauri maharusi, mistari ya mapenzi huwa inanuiwa kuingiza mtu boksi pekee na wala haifai kuchukuliwa kama hali halisi ya maisha ya ndoa.

“Mtu akikuingiza boksi halafu atake kukuoa mara moja, usikubali. Chukua muda umfahamu vyema, hasa tabia zake. Usiamini chochote anachokuambia au usipagawishwe na anachokufanyia kabla ya kupata ukweli. Mazuri hayo yanaweza kuwa ya kuficha tabia zake mbovu. Chukua hatua wewe binafsi pasipo pupa umdadisi, tena kwa kina kabla ya kukata kauli kufunga naye pingu za maisha. Hii haraka ambayo watu huwa nayo kwa sababu ya utamu wa mistari ya mapenzi au zawadi za hapa na pale, haina baraka,” asema Kweyu.

Seth na Kweyu wanakubaliana kuwa misitari ya mapenzi hunuiwa kutimiza ajenda ya muda mfupi na haifai kuchukuliwa kama hali halisi ya maisha ya ndoa.

“Wanachokosa kufahamu watu wengi ni kuwa maneno matamu ambayo wapenzi hubadilishana huwa ya kutimiza malengo ya muda mfupi. Kwa mfano, mwanamume anaweza kutaka mrembo akatae wanaume wengine ampende yeye au nia iwe ni kuchovya asali tu. Mwanadada anaweza kumweleza mwanamume maneno ya kutoa nyoka pangoni lakini awe na lengo tofauti na uhusiano wa muda mrefu,” aeleza Seth.

Hata hivyo, wataalamu wanasema maneno matamu yanayoambatana na tabia nzuri, ukweli na vitendo, heshima na nidhamu yanaweza kuwa hakikisho ya maisha ya raha siku za baadaye.

“Hii ni pale tu watu wanapoendelea kubadilishana mistari hata baada ya kuwa kwenye uhusiano kwa muda na hata baada ya kuoana. Ikikatika baada ya kuingia boksi, elewa kwamba mambo sio mazuri, jiandae kwa balaa,” asema Kweyu.

CHOCHEO: Siri ya mapenzi yenye raha na yanayodumu

Na BENSON MATHEKA

“Unajua ni kwa nini ndoa zinavunjika?” Sam Femi, mwanasaokolojia wa shirika la Dreams and Counseling Services, alimuuliza Peter* kwenye kikao cha ushauri nasaha.

Peter alijibu kwa haraka: “Ni kwa sababu ya wahusika kutowajibika.”

Lakini hilo sio jibu ambalo Sam alitaka japo alilitarajia. “Ni kweli, lakini ninataka kukueleza sababu ya kuvunjika kwa ndoa nyingi na kwa kiwango fulani uhusiano wa kimapenzi. Ni kwa sababu mmoja wa wahusika haongezi thamani kwa mwenzake,” Sam akasema huku akimtazama Peter usoni.

Baada ya kusita kwa sekunde kadhaa, Peter alizusha pumzi. “Ni kweli, umesema kweli,” akasema akionekana kama mtu aliyefunguka macho.

Kulingana na Sam, wengi huvutiwa kimapenzi na lakini hawaongezi thamani katika maisha ya wenzao.

“Uhusiano wa mapenzi ni zaidi ya urembo na kulishana asali. Kila mtu anatarajia mpenzi wake kuongeza thamani katika maisha yake. Hii inamaanisha kuwa mtu anatarajia zaidi ya kupashwa joto. Anataka uchangie kuimarisha uhusiano wake, wenu na maisha yake pia,” asema Sam.

Kulingana na mwanasaikolojia huyo, kuishi au kupenda mtu asiyeongeza thamani katika maisha yako, iwe kimawazo au kwa mali, ni kujibebesha mzigo mkubwa moyoni na mabegani.

“Ni kujilazimisha na hali ikiwa hivi, heshima ukosekana. Heshima ikikosa katika uhusiano wa kimapenzi, hauna budi kusambaratika kwa majuto,” alisema.

Kulingana na Dkt Eva Kamau wa shirika la Big Hearts jijini Nairobi, uhusiano unapokosa thamani huwa ni wa kulazimisha.

“Ukijilazimisha kwa mtu, hatakuheshimu. Badala ya kufanya hivyo, tafuta jinsi unavyoweza kuongeza thamani katika maisha yake na uhusiano wenu utanawiri na atakuheshimu,” asema Eva.

Mtaalamu huyu asema kwamba baadhi ya watu huwa wanasahau umuhimu wa kuongeza thamani baada ya kuolewa au kuoana.

“Hata baada ya ndoa, unafaa kuzidisha thamani yako kwa mchumba wako. Wanaojua siri hii wana raha katika ndoa lakini wanaopuuza hujuta,” asema.

Eva anafichulia wanawake siri rahisi sana ya kuongeza thamani kwa waume zao. “Ukiwa mtu wa kuongeza thamani kwa ndoa, utamdhibiti mtu wako. Hivi ndivyo, Rachael alifanya na akawa anamtawala Yakub hata kimawazo inavyoelezwa katika Bibilia. Rachael alikuwa mchapa kazi na hata alikutana na Yakub kisimani akinywesha maji mifugo wa babake,” aeleza Eva.

Sam anakosoa watu wanaodhani kupata watoto na mtu kunatosha kuwa thamani ya uhusiano wao. “Kupata watoto ni kitu kizuri lakini fanya zaidi kuongeza thamani kwa mpenzi wako. Usifikiri utaweza mtu kwa sababu ya watoto. Kuna wanawake na wanaume wanaolea watoto wao peke yao. Unaweza kuzalia au kuzalisha mtu watoto lakini iwapo hauongezi thamani katika maisha yake, siku moja atakuacha tu,” aeleza Sam.

Kulingana na wataalamu, wazazi wanafaa kuwafunza watoto wao jinsi ya kuongeza thamani kwa wachumba wao kupitia hulka zao.

“Watu wanaweza kurithisha watoto wao hulka hii iwapo wanaitekeleza wenyewe na kuwaandaa vyema. Unaweza kuandaa watoto wako kwa kuwa msitari wa mbele kuongeza thamani kwa mchumba wako na pia kuhakikisha kuwa wanajitegemea maishani kama vile kuwapa elimu nzuri. Kwa mfano, ukitaka binti yako aheshimiwe na mume wake, mpe elimu bora awe na matumaini katika maisha yake ya baadaye,” aeleza.

Eva anasema kwamba wanawake ambao hawajafunzwa kuongeza thamani katika uhusiano huwa wanatendwa hata na wafanyakazi wao wa nyumbani wanaowapokonya waume zao.

“Sababu za baadhi ya wanawake kupokonywa waume wao na vijakazi wenye bidii wasio na urembo kama wao ni kwa kuwa hawatekelezi mambo muhimu ya kuongeza thamani katika ndoa zao. Utawezaje kuruhusu mjakazi kuzoeana na mumeo?” ahoji Eva.

CHOCHEO: Chunga ‘mboch’ asijepasha joto kitanda chako

 

Na BENSON MATHEKA

BAADA ya miaka sita ya ndoa, Eve aligundua kwamba mumewe alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na kijakazi wao.

Alikasirika sana lakini mumewe akamwambia kwamba anafaa kujilaumu mwenyewe. Alimwambia kwamba alimuachia kijakazi wao majukumu ya mke.

Baada ya kutafakari, Eve aligundua kwamba makosa yalikuwa yake. Alikubali kwamba alikuwa amempuuza mumewe huku akimwachia kijakazi wao kazi ya kumpikia na hata kumshughulikia kwa mahitaji yote ya nyumbani.

“Nilibaini kwamba nilikuwa nimefeli katika majukumu yangu kama mke naye akamtwaa aliyekuwa akimshughulikia. Nilijuta kwa kumwachia kijakazi kazi yangu kama mke. Niliamua kurekebisha hali hata baada ya kumfuta kazi mwanadada huyo na nikatia bidii katika kumshughulikia mume wangu,” Eve kafunguka.

Kulingana naye, ni makosa kwa wanawake kuwaamini wafanyakazi wao wa nyumbani hadi kiwango cha kuwaachia majukumu ya kuwatunza waume zao.

“Kufanya hivi ni kutelekeza mumeo na kujiweka katika hatari. Ni rahisi mwanamume kuingiwa na hisia za mapenzi kwa kijakazi anayemshughulikia kwa kila kitu nyumbani. Hii ndiyo inafanya wanawake wengi kupokonywa waume zao na wafanyakazi wa nyumbani,” asema Eve.

Majukumu

Kulingana na Sally Achieng, mshauri wa wanandoa wa shirika la Fountain of Love jijjni Nairobi, wanawake huwa wanasahau kwamba wao ndio wameolewa na sio wafanyakazi wao wa nyumbani.

“Daima kumbuka kuwa wewe ndo umeolewa. Wajibika kikamilifu ikiwa hautaki kupokonywa mumeo na huyo mwanadada unayemwachia jukumu la kwako. Kazi ya kuwa mke haiwakilishwi kamwe,” asema Achieng.

Mshauri huyu anasema wafanyakazi wa nyumbani wanafaa kumsaidia mke katika baadhi ya majukumu yasiyohusu waume zao moja kwa moja.

“Inashangaza baadhi ya wanawake hupatia vijakazi jukumu la kuamsha waume zao na kuwaandalia kiamsha kinywa na hata kuwachagulia suti za kuvaa. Kufanya hivi ni kukabidhi ‘mboch’ majukumu yako na kumpa nafasi ya kukupokonya mume au kuchepuka naye,” asema Achieng.

Ingawa wataalamu wanasema baadhi ya wanaume hutawaliwa na tamaa kiasi cha kufanya mapenzi na wafanyakazi wa nyumbani, wataalamu wanasema wanawake walioolewa wanafaa kutekeleza majukumu yao kikamilifu.

“Kamwe usimpatie au kumwachia mtu yeyote kazi inayoweza kumtia mumeo kwenye majaribu. Wacha watu wengine wafanye mambo mengine lakini zingatia kwamba unafaa kujukumika kwa mumeo peke yako,” asema Ashley Kombo wa shirika la Families For Tomorrow.

Kombo anasema mwanamume huwa anashawishika na kuchotwa akili na mwanamke yeyote anayewajibika kwake na masuala ya nyumbani.

“Kinga ndoa yako kwa kumtenga mjakazi na mumeo. Acha alee watoto chini ya uelekezi wako lakini usimpatie jukumu la kumkaribia mumeo. Kinga mkeo asitumbukie katika majaribu ya kumchangamkia house-boy kwa kumpa haki yake ya ndoa anapohitaji. Hakikisha humuachi kwa muda mrefu na yaya/kitwana nyumbani peke yao,” asema Kombo.

“Mke anayefahamu majukumu yake anajua kumkinga na kumshughulikia mumewe ili asitumbukie katika majaribu ya kuchangamkia wanawake wengine wakiwemo wafanyakazi wa nyumbani. Hii inawezekana kwa kumtengea yaya majukumu yake,” asema.

Achieng anasema kwamba baadhi ya wanawake huchangia uchepukaji kwa kutowekea wafanyakazi wa nyumbani mipaka ya majukumu.

Lakini kulingana na Simon Njagi wa kituo cha Liberty Center, hakuna sababu inayoweza kushawishi mwanamume kushiriki tendo la ndoa na mjakazi isipokuwa tamaa na kumkosea mkewe heshima.

“Huwezi kutakasa makosa ya kuzini na mjakazi kwa kudai mkeo alimwachia majukumu yake. Hauwezi kutakasa tamaa yako ya kulala na yaya kwa kudai mkeo alikutekeleza. Mtu anayemheshimu mkewe hawezi kumsaliti kwa vyovyote,” asema.

Hata hivyo anakiri kwamba wanawake wanafaa kuhakikisha kuna mipaka ya majukumu ya wafanyakazi wa nyumbani na majukumu yao kwa waume zao.

CHOCHEO: Usimkaribie tu, mguseguse…

Na BENSON MATHEKA

“SIO kwa ubaya lakini nimemchoka,” Carol aliambia wazazi wake walipomuuliza sababu ya kumwacha mumewe wa miaka mitatu. “Hanipi raha,” aliongeza na kuondoka kwenda kukutana na Dan, mpenzi wake mpya.

Kwake, Dan alikuwa akimfanyia anachohitaji kufurahia mapenzi. Alikuwa akimchangamkia na kumpapasa tofauti na mumewe ambaye alidai hakuwahi kumgusa isipokuwa wakati wa tendo la ndoa ambalo mwanadada huyo anasema hakulifurahia hata chembe.

Ikiwa Carol alichoshwa na mumewe baada ya miaka mitatu tu, sijui tusemeje kumhusu, Iba. Ni mwanamume mwenye umri wa miaka 35 aliyeteseka kwa miaka sita kabla ya kumtema mkewe. Iba anasema mkewe hakuwahi kumgusa hata siku moja.

“Hata tukiwa kitandani, tulikuwa sawa na milima miwili au pande mbili za sumaku zisokaribiana. Ile raha ambayo mwanamume hutarajia kupata kwa kuguswa na mpenzi wake haikuwepo. Nikijaribu kumgusa ilikuwa sawa na kushika mfu. Hakuhisi chochote na alikuwa na hasira mbaya,” asema.

Masaibu ya Carol na Iba ni sawa na yanayosababisha watu wengi kukosa raha ya ndoa. Wataalamu wa masuala ya mapenzi wanasema kuwa kugusa mpenzi wako kuna raha na faida ya kipekee inayokuza uhusiano. “Usipomgusa mpenzi wako na hasa yawe mazoea, utamkosesha raha na anaweza kukuacha. Hata kama hamtatengana, ataenda kutafuta raha kwingine,” asema Tito Umilyo, mwanasaikojia wa shirika la Ultimate Love jijjni Nairobi.

“Ikiwa hataki umguse au kukugusa, basi uhusiano wenu umo hatarini,” asema.

Kulingana na wataalamu, kukwepa mgusano ni mapuuza.

“Kupuuza mchumba ni moja ya sababu za kuvunjika kwa mahusiano. Kunachangiwa na mambo kadhaa ikiwemo ugomvi au kushindwa kutimiza mahitaji ya mwenzio kikamilifu. Pia, kunaweza kusababishwa na michepuko,” aeleza Tito.

Kukosa mgusano ni sawa na kukosa mapenzi kwa mwenzio, asema Frenz Kawira wa shirika la Love Care jijini Nairobi, mtu huwa anatoa ishara kwamba hana mapenzi kwake.

“Ninachojua kwa hakika ni kuwa mtu akikosa kumgusa mpenzi wake, huwa anajiweka katika hatari ya kuachwa. Kugusana kwa wachumba iwe ni kwa kutomasana, kupapasana, kudekezana na kupigana pambaja na mabusu, kunafanya uhusiano wao kuwa imara,” asema Kawira na kuongeza kuwa ni tendo linalohitaji ubunifu ili kuibua raha.

“Kitu kinachofifisha raha katika uhusiano ni mazoea. Kuwa mbunifu katika kila kitu unachofanya kujenga uhusiano wa kimapenzi na mtu wako hatakuchoka,” asema Kawira.

Tito anasema kugusa mchumba wako kunaonyesha kwamba unamthamini na kumtambua. “Ni kitendo kinachodhihirisha kuwa unamthamini mtu wako na pale mtu anapokataa kuguswa au kuchangamka mwenzake anapomgusa, huwa anaashiria kwamba hana hisia za mapenzi kwake,” aeleza.

Wataalamu wanasema kwamba mpenzi akikupuuza ukimgusa, huwa anaonyesha umuhimu wako kwake umeisha.

“Ni kitendo cha kuchochea mapenzi na kikikosekana au kisipokaribishwa, elewa mambo sio mazuri,” aeleza Tito.

Kawira asema kuwa kuna vitendo vya kugusana vinavyochangia kustawi kwa mahaba kwa wachumba.

“Kuna raha ya aina yake mwanadada kulala katika kifua cha mpenzi wake. Kuna raha mtu wako kukuvuta kifuani na kukumbatia na kuna raha ya kubebwa hadi kitandani,” asema Kawira.

Mshauri huyu asema kuwa wanaume hupenda kudekezwa, kupigwa mabusu na kukandwakandwa mwili. “Wanawake wanaotambua siri hii, hupagawisha watu wao, unaweza kuchota akili ya mwanamume kwa kumdekeza tu,”asema.

Aidha wataalamu wanakubaliana kuwa kugusana kunafaulu pale mawasiliano kati ya wachumba yako sawa.

“Mawasiliano yakiwa shwari, mili huwa inachangamkiana. Yakivurugika, ukimgusa mtu wako utakuwa ukijisumbua bure,” asema Tito.

CHOCHEO: Asali sio leseni ya ndoa

Na BENSON MATHEKA

UHUSIANO wa Maria na Mike ulikuwa mzuri kwa miaka minne.

Maria alikuwa amekata kauli kwamba kapata mpenzi wa maisha yake. Wote wawili walikuwa viongozi wa vijana kanisani na Maria alikuwa amemweleza Mike kwamba hangeonja asali hadi watakapooana.

Ingawa Mike alijaribu mara kadhaa kumshawishi mwanadada huyu kumfungulia mzinga, alikataa na kumweleza aharakishe wafunge pingu za maisha ili waweze kufurahia tendo la ndoa wakiwa mtu na mkewe.

Mike alikubaliana naye na Maria akawa anasubiri waanze mipango ya harusi hadi juzi aliposhtuka kugundua kuwa aliyedhani kuwa mpenzi wa maisha yake alikuwa ameoa mwanadada mwingine.

“Ulikataa kunifungulia mzinga kabla ya ndoa, nikamuoa aliyekubali kunionjesha kwanza. Wewe endelea kusubiri atakayekubali muoane ili aweze kujua utamu wa asali iliyo kwenye mzinga wako,” Mike alimweleza Maria alipomuuliza sababu ya kumvunja moyo licha ya kusubiri kwa miaka minne.

Maria alijituliza kwa kuamini kwamba Mike hakuwa akimpenda kwa dhati na alichotaka kwake ni kumtumia tu.

“Kama kumuonjesha asali mwanamume kabla ya ndoa ndiyo leseni ya kuolewa, wacha nibaki mseja,” aliapa Maria.

Mwanadada huyo ni mmoja miongoni mwa wengi wanaokataliwa na wanaume kwa kukaa ngumu na kukataa kushiriki uroda kabla ya ndoa.

“Kuna wanawake walio na msimamo kwamba kamwe hawataruhusu mwanamume kuwaonja kabla ya ndoa. Wanaume wanaweza kusema hawapo lakini wapo,” asema Annita Nameme, mshauri wa wanandoa katika kituo cha Endurance Life jijini Nairobi.

“Inapaswa kuwa hivyo na sio uhalifu jinsi baadhi ya watu wanavyotaka wengine kuamini. Mwanamume anayekupenda kwa dhati atasubiri muoane kabla ya kukuonja. Ukiona mwanamume anataka kukusukuma kitandani mnapoanza uhusiano wenu, nafasi ya kukuoa huwa ndogo sana,” asema Nameme.

Hii ndiyo stori ya Jessica, mwanadada mwenye umri wa miaka 26 anayesema kwamba aliachwa na mchumba wake siku aliyokubali kumuonjesha tunda.

“Inaniuma sana. Hebu fikiria mwanamume uliyeishi naye kwa miaka mitatu mkipanga maisha ya siku za baadaye akikuacha baada ya kumpakulia asali. Unajiuliza maswali mengi sana,” akasema Jessica.

Kulingana na Nameme, wanawake wanafaa kung’amua kwamba mwanamume anayesubiri waoane ndipo walishane uroda ana heshima.

“Wengi huwa wanataka burudani tu. Wakichovya asali wanatoweka. Mwanamume anayependa kidosho kwa dhati huwa anaheshimu maamuzi yake. Akiamua kwamba hatakufungulia mzinga hadi mtakapofunga ndoa, heshimu uamuzi wake,” asema.

Bosco Otunga, mshauri wa vijana katika kanisa la Life Celebration Center, Nairobi, anasema kwamba wasichana wengi wamevurugiwa maisha na wanaume wanaowashawishi wawaonjeshe asali kabla ya ndoa.

“Visa vya wanawake kujuta baada ya kuachwa na wanaume baada ya kumeza chambo na kuwapa mili yao vimejaa kote. Wengi wao huachwa baada ya kupachikwa mimba na kubebeshwa mzigo wa ulezi. Ni heri kukaa ngumu kuliko kulegeza msimamo kuridhisha uchu wa mwanamume ambaye atakufanya ujute,” asema Otunga.

Anakubaliana na Nameme kwamba uroda sio leseni ya ndoa.

“Kama ungekuwa leseni ya ndoa, hakungekuwa na vilio vya wanawake kuachwa na wanaume wanaowapakulia asali,” asema.

Wataalamu wa masuala ya mapenzi wanasema kwamba watu wanaoana kabla ya kulishana asali huwa na ndoa yenye furaha.

Kulingana na utafiti uliochapishwa kwenye jarida la Journal of Family Psychology mwaka jana, maisha ya wanaochangamkia uroda kabla ya ndoa huishia kwa majuto.

“Watu wanaokosa kushiriki tendo la ndoa hadi usiku wanaofunga harusi huwa na ndoa zenye furaha na thabiti kuliko wale wanaolishana asali kabla ya ndoa,” inasema sehemu ya utafiti huo.

Otunga anasema kila lililoandikwa katika maandiko matakatifu huwa na sababu zake na huwafaidi wanaozingatia na kutimiza.

“Imeandikwa kuwa tendo la ndoa ni kwa mtu na mkewe na sio mtu na mkewe watarajiwa,” asema.

CHOCHEO: Usimpe mpenzi wako sababu ya kukushuku

Na BENSON MATHEKA

JEPHINA alimtaliki mumewe Sammy kwa sababu ya kumchunga.

Kwa mwanadada huyu, hakuweza kuishi na mwanamume asiyeweza kumwamini.

“Alikuwa akifuatilia mienendo yangu hata kazini. Alinifanya nikose marafiki kwa kuwa alishuku kila mmoja; wanaume na hata wanawake. Alikuwa mzigo katika maisha yangu kwa miaka saba, mzigo ambao niliamua kuutua,” asema Jephina na kuongeza kuwa tangu apate talaka kutoka kwa Sammy, anajihisi huru.

“Nilikuwa ninapata kila kitu kwake isipokuwa imani. Alikuwa ameninunulia gari lakini kwa sasa ninapanda matatu kwenda na kutoka kazini nikifahamu hakuna mtu wa kunichunga kama mbuzi,” asema mwanadada huyu.

Masaibu sawa yalimfanya Maina, 32, kutengana na mkewe wa miaka mitano. Maina anasema kwamba mkewe alikuwa akimchunga hata zaidi ya mbuzi.

“Sikuwa na uhuru wa kuzungumza na wanawake. Ilikuwa kualika balaa kuwa na marafiki wanawake katika mitandao ya kijamii. Ilikuwa ngori hadi nikaamua kanuke,” asema Maina kwa sheng.

Wanasaikolojia wanasema kwamba kuchunga mchumba kiwango kwamba hawezi kuwa na uhuru wake kunamsababishia mfadhaiko.

“Kuna wengi wanaovumilia hali hii na ni makosa. Wanafaa kujitokeza na kutafuta ushauri nasaha. Hii ndiyo hatua ya kwanza. Suluhu ikikosa kupatikana hasa pale anayekuchunga anapoanza kukudhulumu kimwili kwa kukupiga, unaweza kuomba talaka au mtengane,” asema Brian Simiyu, mwansaikolojia wa kituo cha Maisha Mema jijini Nairobi.

Maisha ya mapenzi ya muda mrefu ikiwemo ndoa, yanafaa kuwa ya kuaminiana na sio kushukiana.

“Mtu anayechunga mchumba wake huwa na mapungufu mengi ikiwa ni pamoja na kukosa kumwamini mtu wake. Uhusiano wa aina hii hauwezi kudumu na ukidumu anayechungwa huwa mtumwa wa anayemchunga,” aeleza mwanasaikojia huyu. Hata hivyo, anasema mtu hafai kumpa mwenzake sababu za kumshuku na kumchunga.

“Baadhi ya watu huwafanya wachumba wao washuku tabia zao. Kwa mfano, ikiwa amekupata katika hali ya kutatanisha na mtu wa jinsia tofauti au mienendo ya watu unaotangamana nao katika shughuli za kijamii na kibiashara ni ya kutiliwa shaka basi utakuwa umempatia sababu za kukushuku na kukuchunga,” asema.

Tabia nyingine zinazofanya mtu kuanza kumchunga mpenzi wake ni kumpunguzia au kumnyima haki zake za ndoa. Kulingana na Zipporah Kinama, mshauri wa masuala ya mapenzi, mwanamume atashuku mke anayemkazia uroda na kumchunguza kubaini iwapo ana mipango ya kando..

“Vile vile, mke atashuku mume anayebadilisha tabia na kuanza kuchelewa kufika nyumbani au hata kulala nje,” asema. Zipporah asema sababu nyingine ya watu kuanza kushuku na kuwapiga darubini wachumba wao ni uraibu wa mitandao na matumizi ya simu.

“Simu zimezua balaa sana. Mtu anapigiwa simu na kuondoka aliko mchumba wake kwenda kuipokea. Katika kufuatilia kujua aliyepiga simu, balaa inazuka na uhusiano kuvurugika. Ni sawa na wanaozama katika mitandao na kukatiza mawasiliano na wachumba wao nyumbani,” asema Kinama.

Mtaalamu huyu ashauri watu kutowapa wachumba wao sababu za kuwachunga na wanaowachunga wapenzi wao bila sababu kukoma akisema kufanya hivyo kunaua imani katika uhusiano.

“Usimpe mtu wako sababu ya kukuchunga na vilevile usimchunge mtu wako bila sababu ya kufanya hivyo. Wacha kumpigia simu kumuuliza aliko kila dakika iwapo amekufahamisha kwamba atachelewa kazini au kwenye mkutano wa chama. Watu wanafaa kukomaa, kuheshimiana na kuaminiana. Kuchunga mchumba wako kunayumbisha uhusiano,” asema.

Hata hivyo, Simiyu asema hakuna makosa kuchunga mtu wako kuhakikisha usalama wake.

“Kuna watu wanaowajali zaidi wachumba wao kiasi kwamba wataenda kuwachukua wanapochelewa kazini au kuwapigia simu kila wakati kujua hali yao waliko. Baadhi ya wanaopigiwa simu huwa hawafurahii tabia ya wenzao wakishuku wanawachunga lakini wanafaa kuwashukuru,” asema Simiyu na kuongeza kuwa wanaokasirishwa na wachumba wanaowachunga kwa usalama wao wanawapa sababu za kuwashuku.

CHOCHEO: Kukataa mchezo wa huba ni kuhatarisha ndoa – Washauri

Na BENSON MATHEKA

CIDY anajuta kumkaushia mumewe Zack kwa uroda alipokataa kumnunulia zawadi siku yake ya kuzaliwa.

Zack alivumilia kwa miezi miwili akitumia kila mbinu kumshawishi Cidy lakini akakataa kumtimizia haki yake ya tendo la ndoa kisha akaamua kutafuta huduma kwingine na kumpata Rose ambaye baada ya kuchepuka naye mara tatu, alimweleza alikuwa na mimba yake.

“Uhusiano wangu na Zack umeingia doa na sasa anataka kumuoa Rose. Makosa yalikuwa yangu. Kama singemnyima haki yake ya tendo la ndoa singekuwa katika hali hii,” asema Cidy.

Ndoa yao ni ya kitamaduni na kisheria, Zack anaruhusiwa kuoa zaidi ya mke mmoja. Katika kisa sawa na cha Cidy, Kimani anasema kwamba mkewe alichepuka na mpenzi wake wa zamani baada ya kukosa kumchangamkia kitandani kwa miezi minne.

“Tulikosana nilipogundua kwamba alikuwa amechukua mkopo na kununua nyumba bila kunifahamisha. Japo sio vibaya kufanya hivyo, tuligombana na nikahama chumba cha kulala licha yake kutumia kila mbinu nirudi ikiwa ni pamoja na kuniomba msamaha na kunikabidhi stakabadhi zote za nyumba aliyonunua. Baadaye niligundua alikuwa akimchangamkia mpenzi wake wa zamani na nikajuta kwa tabia yangu,” asema Kimani.

Ingawa mkewe aliungama kwamba hakuwa amezini na jamaa huyo, Kimani alihisi kwamba tabia yake ilihatarisha ndoa yake na akatafuta ushauri nasaha kutoka kwa wataalamu ambao waliwapatanisha.

Kulingana na Dick Ipetu, mshauri mwandamizi katika shirika la Abundant Love jijini Nairobi, wachumba huwa wanaweka uhusiano wao kwenye hatari wanapokaushiana uroda baada ya kutofautiana na kugombana.

“Ni kweli ugomvi huwa unavuruga uhusiano kati ya wanandoa lakini wanaponyimana haki ya tendo huwa wanaangamiza ndoa yao. Ni kawaida ya tofauti kuzuka na kufanya mtu kukosa hisia za mapenzi kwa mwenzake lakini ili kuokoa ndoa, suluhu inafaa kupatikana haraka kabla ya jahazi kuzama,” aeleza Ipetu. Hivi ndivyo Cidy alikosa kufanya na ndoa yake sasa iko mashakani.

Wataalamu wa masuala ya ndoa wanasema kwamba haki ya tendo la ndoa ni gundi inayounganisha wachumba na mtu hafai kumnyima mwenzake kumwadhibu wanapotofautiana.

“Inasukuma mtu kuwa na mipango ya kando na huu ndio ukweli na ikifikia hapo huwa kuna uwezekano wa kuvunjika kwa ndoa na kusababisha majuto,” asema Ipetu.

Kulingana na Pasta Winnie Kibui wa shirika la First Love Restoration Center jijini Nairobi, kunyima mchumba wako haki ya tendo la ndoa bila sababu maalumu ni sawa na kujiondoa katika ndoa.

“Wakati ambao wanandoa hawafai kushiriki tendo la ndoa ni mmoja wao akiwa mgonjwa. Kuna wanandoa wanaoishi miji tofauti na kwa sababu wanajua siri hii wanasafiri muda mrefu kuhakikisha kuwa wanapeana haki yao ya ndoa. Ajabu ni kwamba unapata wanaoishi nyumba moja wananyimana kwa sababu ya mambo madogo wanayoweza kuepuka au kusuhuhisha,” asema Kibui.

Kulingana na wataalamu, wachumba wanaponyimana tendo la ndoa huwa wanatumbukiza wenzao kwa majaribu.

“Kwanza, unamtumbukiza mtu kwenye mateso ya kisaikolojia na kumweka katika majaribio. Akipata mtu wa kumchangamkia atapita naye na utakuwa umevuruga uhusiano wako,” asema.

Kulingana na Pasta Kibui, watu wakioana huwa ni kitu kimoja na kinachowaunganisha ni tendo la ndoa.

“Kama hakuna sababu ya kimazingira au maradhi, sioni sababu ya mtu kumnyima mpenzi wake haki ya ndoa. Ni sawa na kunyima mwili wako kwa kuwa mtu na mkewe ni kitu kimoja,” asema.

Hata hivyo, asema ili kufurahia tendo lazima kuwe na uhusiano mwema kati ya wachumba.

“Epukeni mizozo, eleweni kuwa ni kawaida kuwa na tofauti za kimaoni ambazo kamwe, narudia, kamwe, hazifai kufanya mtu amnyime mwenzake haki yake ya ndoa na ikizuka hali ambayo hamchangamkiani, tafuteni ushauri kutoka kwa wataalamu na viongozi wa kiroho,” asema.

Kulingana na sheria ya ndoa ya Kenya, moja ya sababu za kuvunjika kwa ndoa ni kunyimana haki ya ndoa.

CHOCHEO: Ukijua anachepuka, utafanyaje?

Na BENSON MATHEKA

HARRY alitarajia mkewe Cynthia amkasirikie na kununa alipogundua kwamba alikuwa amekula ufuska na kipusa mwingine.

Badala yake, Cynthia alimchangamkia zaidi kwa kumwandalia burudani murwa chumbani. Baada ya wiki moja alimwambia kwa upole na heshima.

“Darling, ukiona nimelegea kukupakulia asali, nieleze badala ya kutafuta mipango ya kando wanaoweza kuharibu uhusiano wetu. Nakupenda sana na nitafanya kila niwezalo kukupa raha na burudani uridhike”.

Harry alikiri kwamba tangu ale uroda nje ya ndoa, mkewe aliboresha shughuli chumbani japo alitarajia kwamba angemkasirikia alipogundua alikuwa amekula vya pembeni.

“Nilijipeleleza na kujuta kwa kumsaliti. Kama Cynthia hangekuwa mwanamke mwenye hekima, mchepuko ungevuruga ndoa yangu,” asema Harry.

Hali ilikuwa hivyo kwa Dave alipogundua mkewe alikuwa akichepuka na mfanyakazi mwenzake.

“Nilipomuuliza kwa nini anagawa asali, aliniambia kwamba ninafaa kujiuliza nilichokosa hadi akaamua kukitafuta kwa wanaume wengine. Niligundua kuwa sikuwa nikimpa muda wa kutosha na ikabidi nibadilishe tabia,” asema Dave.

Kulingana na ripoti ya shirika la Maisha Mema kuhusu kisa cha Dave, mkewe alifichua kwamba hakuwa akigawa asali japo alikuwa na uhusiano wa karibu na wafanyakazi wenzake wanaume.

“Lakini uhusiano huo ungemfanya ashawishike kuhanya kwa kuwa ilikuwa nadra kuketi na mumewe na kujadili masuala muhimu. Alihisi upweke hadi mumewe alipohisi kulikuwa na hatari ya kupokonywa mkewe na mafisi afisini mwao, akazidisha mapenzi ikiwa ni pamoja na nderemo chumbani na kumpeleka kujivinjari maeneo tofauti,” inasema ripoti iliyoandikwa na mshauri wa wanandoa Trizah Karimi.

Kulingana na mwansaikolojia huyu, kuna watu wanaowachangamkia wachumba wao zaidi wakigundua wanachepuka.

“Ni hatua inayohitaji ukomavu mkubwa ikizingatiwa kuwa kuchepuka ni kosa na usaliti wa hali ya juu ambao mtu anaweza kumfanyia mwenziwe,”asema Trizah na kuongeza kuwa kufanya hivi kunamzuia kuendelea na uhanyaji.

“Sio watu wengi wanaoweza kufanya hivyo lakini wanaozidisha upendo kwa wachumba wao wakigundua wanashiriki mipango ya kando, huwa wanaokoa uhusiano wao wa kimapenzi kuliko wale wanaonuna na kuzua ugomvi,” asema.

Hata hivyo, anasema hili linawezekana anayesalitiwa akigundua na kukubali mapungufu yake katika uhusiano.

“Sio lazima iwe ni kulegea chumbani. Inaweza kuwa lugha unayotumia au marafiki unaojumuika nao. Unaweza kuwa mpishi bora lakini uwe mtu wa kelele na ugomvi,” aeleza Trizah.

Gerald, mwanamume mwenye umri wa miaka 33 na Nekesa mwanadada mwenye umri wa miaka 27 wanasema kwamba waliamua kuhanya, wenzao walipopunguza makeke chumbani. Hata hivyo, Nekesa asema mumewe alipoingiwa na wivu na kuboresha tendo, aliacha tabia hiyo.

“Ilikuwa hatari sana,” asema na anashauri watu watafute mbinu mbadala za kunogesha mapenzi.

Mwansaikolojia Doreen Shigadi wa shirika la Big Hearts Nairobi, anasema kuwa sio watu wengi wanaochangamkia wachumba wahanyaji au wanaoshuku si waaminifu.

“Ni wachache sana hasa wanaume wanaoweza kuwasamehe wenzao wakigundua wanagawa asali nje ya ndoa. Tabia hii imevuruga ndoa na mahusiano ya mapenzi. Hauwezi kusaliti mtu wako na utarajie akuchangamkie roho safi,” asema.

Anashauri watu kuepuka tabia zinazoweza kutumbukiza wachumba wao kwenye majaribu ya ulaghai wa mapenzi.

“Adui mkubwa wa uhusiano wa mapenzi ni mchepuko. Unavunja uhusiano na hata msipotengana, penzi litakuwa limechuja.

Hata hivyo, kuna wanaotambua walichangia tabia ya michepuko na ndio sababu hurekebisha na kuwachangamkia wenzao,” asema Shigadi.

Lily Koech, mwanadada mwenye umri wa miaka 26 na Bonface Wambua mwenye umri wa miaka 35 wanasema hawawezi kuwakumbatia wachumba wao wakigundua wanachuuza asali.

“Siwezi kumkaribia. Hauwezi kunisaliti kwa sababu ya upungufu wangu kisha udai unanipenda,” asema Lily.

CHOCHEO: Kumchongoa sawa na kuchongea penzi lenu

Na BENSON MATHEKA

“MBONA huwezi kuwa kama mume wa Njoki ambaye hushinda na watoto wake na kumthamini mkewe?” Hii ilikuwa mara ya kumi Wangui kumlinganisha mumewe Teddy na waume wa wanawake wengine jambo lililomkwaza sana.

Ni sawa na anayopitia Lilian ambaye mumewe huwa anamlinganisha na wanawake wengine mtaani na anaowaona kazini au kukutana nao katika hafla mbalimbali.

“Ananichosha na akiendelea, nitamwambia aende akaishi nao au niondoke nimpatie nafasi ya kuchagua anayehisi anamfaa. Sitaendelea kuvumilia mchongoano wake kila siku,” asema Lilian.

Kwa Cindy, mumewe amekuwa akimtaka avalie kama wanawake wengine ilhali ni mitindo isiyomfurahisha.

“Patrick anataka niwe kama wanawake wengine. Kila wakati anasifu mitindo yao ya mavazi na nywele ambayo hainipendezi,” asema.

Cindy anashuku kuwa mumewe anachepuka na wanawake wengine anaoshinda akiwasifu.

Kulingana na wataalamu wa masuala ya mapenzi, ni makosa kumchongoa mchumba wako kwa vyovyote vile au kumlinganisha na mwanamume au mwanamke mwingine.

“Kufanya hivi kunamfanya ahisi kuwa haumpendi au mapenzi yako kwake yamepungua. Anaweza kutilia shaka uaminifu wako katika uhusiano wenu,” asema Stephen Karanja, mshauri mwandamizi katika shirika la Love Care jijini Nairobi.

Karanja anasema kwamba badala ya kumchongoa, au kumlinganisha mpenzi wako na mwanamume au mwanadada mwingine, unafaa kumsaidia na kumbadilisha awe utakavyo.

“Ikiwa ni mtindo wa nywele, hakikisha umemfadhili badala ya kumwambia fulani anapendeza. Ikiwa mtindo huo haumpendezi, usimlazimishe, kuna mingine inayoweza kumtoa vyema ikuvutie pia. Cha muhimu ni kuheshimu uamuzi wa mtu wako kwa sababu haukumpenda kwa kuwa alikuwa akifanana na unaomlinganisha nao,” asema Karanja.

Bezo na dharau

Wataalamu wanasema kuna wanaohisi wachumba wao wameanza michepuko wanapowalinganisha na wengine.

“Si lazima anayekulinganisha na mtu mwingine awe na mpango wa kando japo kuna uwezekano mkubwa wa kuchepuka akipata nafasi hiyo,” asema na kuongeza kuwa kuna wale ambao lengo lao huwa ni kuwahimiza wachumba wao kujiweka katika hali ya kuvutia.

Kulingana na Hellena Kwita wa shirika la Big Hearts jijini Nairobi, wachumba wanafaa kusaidiana kujiimarisha katika kila hali pasipo mchongoano, kubezana au dharau.

“Unapolinganisha mtu wako na mwingine kwa hali yoyote ile, unaonyesha unamdharau. Ni ishara ya mapungufu katika uhusiano wenu. Mnafaa kusaidiana na kujengana. Mapenzi ni kufanya mtu wako kuwa bora kila siku pasipo kuumizana moyo. Daima usimfananishe au kumlinganisha mtu wako na mwingine. Utabomoa penzi lenu na kuporomosha uhusiano wenu,” asema Kwita.

Cecilia Ambani, mwanadada mwenye umri wa miaka 32, asema alimbadilisha mumewe kuwa atakavyo bila kumlinganisha na mwanamume mwingine.

“ Nikiona mwanamume na suti nzuri, huwa nampeleka mume wangu dukani kujipima na ikimtoa vyema, namnunulia au namwambia anunue tukiwa na pesa. Simwambii niliona fulani akiwa ameivaa,” asema.

Wataalamu wanasema watu wengi wanavunja uhusiano wa mapenzi na hata ndoa zao kwa sababu ya tamaa. “Kuna wanaoongozwa na tamaa na hao ni rahisi kuchepuka au kuacha wapenzi wao baada ya kuwalinganisha na watu wengine hasa pale wanaowafananisha nao ni watu wenye mali, warembo au elimu au kazi nzuri,”asema Karanja.

Anasema watu wanafaa kubaini ukweli kuwa macho hayana pazia na sio kila wanachoona wanafaa kuiga.

“Hakuna wakati binadamu watatoshana au kufanana. Huu ndio urembo wa dunia. Yaani watu wa sura, umbo kimo, saizi na matabaka mbalimbali. Juhudi na bidii ni muhimu lakini wapenzi hasa walio katika ndoa hawafai kulinganisha watu wao na wengine isipokuwa pale ambapo waonekana bora kuliko hao wanaofananishwa nao. Na hata hivyo, hawafai kuwabeza au kudharau watu wengine kwa kuwa uwezo wa watu ni tofauti,” aeleza Karanja.

CHOCHEO: Utachombeza au kuyatema Valentino hii?

Na BENSON MATHEKA

KESHO ni siku ya wapendanao na Jenny anasema hatakuwa na raha kwa sababu mpenzi wake Ted hakumtimizia aliyotaka mwaka jana.

“Nilitarajia anipose lakini hakufanya hivyo. Nimevunjika moyo kwa sababu hata mwaka huu haonyeshi nia ya kunioa,” asema Jenny.

Mwanadada huyu asema Ted hampi sababu za kuchelewa kumuoa licha ya uhusiano wao kudumu kwa miaka mitao sasa.

“Marafiki zangu wamekuwa wakiolewa baada ya kuchumbiwa kwa muda wa chini ya miaka mitatu, nimevumilia vya kutosha na asiponipa mwelekeo kesho, nitamuacha,” asema Jenny.

Matarajio yake si tofauti na ya Scola, 27, ambaye amekuwa akisubiri mpenzi wake wa miaka sita amvishe pete ya posa bila mafanikio.

“Sitaki kuharibu muda zaidi. Ikiwa hatanipa mipango ya kunioa mwaka huu, nitabanduka,” asema.

Jenny na Scola hawako peke yao. Nic, mwanamume mwenye umri wa miaka 30 anasema mpenzi wake wa miaka minne, amekuwa akijivuta anapotaka waoane.

“Kila wakati nikimtaka tuanze mipango ya ndoa, huwa anasema tusubiri kwanza. Niko na kazi nzuri na ningetaka kutumia valentino mwaka huu kupata uamuzi wa mwisho kutoka kwake. Hii chelewa chelewa itavuruga mipango yangu ya maisha,” asema Nic.

Hawa ni baadhi ya watu ambao wanatarajia makubwa kutoka kwa wachumba wao siku ya wapendanao mwaka huu.

Kupima mapenzi

Wanasaikolojia wanasema kwamba watu huwa wanatumia siku hii kupima mapenzi ya wenzao kwao.

“Nazungumzia wale ambao wanaendelea kuchumbiana. Wengi wao, hasa vipusa, huitumia kupima kiwango cha mapenzi cha wenzi wao. Kuna wale wanaopima mapenzi kwa kutegemea zawadi wanazonunuliwa, wengine wanaamini wanapendwa kwa kupelekwa deti kali maeneo ya kifahari na wengine wanapima mapenzi ya wenzao wakiwavisha pete ya posa siku ya leo,” asema mwanasaikolojia Damaris Kawira wa shirika la Christ Apple jijini Nairobi.

Anasema wanaotarajia wachumba wao wawaeleze mipango ya kuoana siku ya valentine wanaweza kuvunjika moyo wakikosa kutimiziwa matarajio yao hasa ikiwa uhusiano wao umedumu kwa miaka mingi.

“Japo hii ni siku ya kusherehekea mapenzi, ushauri wangu ni kwamba usishinikize mtu akupe ahadi ya ndoa. Matarajio yanaweza kuwa mengi lakini katu usijaribu kumlazimisha akuvishe pete ya posa iwe siku ya valentino au siku nyingine ile,” asema.

Wanasaikolojia wanasema kuvunja uhusiano siku ya wapendanao kunaweza kuwa na athari zake kwa anayeachwa.

“Sio kwamba haiwezekani lakini sio vyema kukutana na mtu siku inayotazamiwa kuwa ya kusherehekea mapenzi na kisha umpe habari za kumtema. Heri ufanye hivyo kabla ya siku hiyo au ukose kukutana naye kabisa kisha baadaye umfahamishe sababu ya kuvunja deti,” asema Leticia Kananu, mshauri wa masuala ya mapenzi katika shirika la Maisha Mema jijini Nairobi.

Kulingana na Kananu kuacha mchumba siku ya wapendanao ni kumuachia donda la moyo. “Hii inafaa kuwa siku ya raha, ya kutathmini uhusiano wenu, kuufanya upya na kuutia nguvu,” asema.

Ingawa inafaa kuwa siku ya kusherehekea penzi la dhati, watu wengi wameibadilisha kuwa siku ya kulishana uroda na watu wanaowamezea mate.

“Ikiwa wewe ni mwanamke, usitumie siku hii kumlisha tunda mwanamume anayekumezea mate ukidhani atakupenda. Hayo ni matarajio hewa yanayofanya wengi kujuta,” asema.

Haya ndiyo makosa aliyofanya Dina Avendi, mwanadada mwenye umri wa miaka 26.

“Nilidhani kwa vile James alikuwa amenirushia chambo kwa siku nyingi baada ya kuachana na mpenzi wake wa awali, kumburudisha siku ya wapendanao kungemfanya awe wangu. Baada ya usiku huo hakunichangamkia tena na nikabaini alichotaka ni asali tu,” asema Avendi.

CHOCHEO: Ukikutana na EX itakuwaje?

Na BENSON MATHEKA

“NIMEFIKA mwisho. Nataka talaka. Siwezi kuvumilia maisha kama haya,” Liza alimweleza Peter.

Hii ilikuwa baada ya wawili hao kugombana vikali Peter akimlaumu kwa kutochangia katika bajeti ya nyumba licha ya kuwa na kazi na mshahara mkubwa.

Lakini pia alimsihi asimtaliki akisema kwamba kuvunja ndoa yao kungeathiri watoto wao wawili. Liza alimkumbusha kwamba ni yeye anayewashughulikia watoto hao na hangekubali awatumie kuendelea kumtesa. “Nimeamua na sibadilishi nia. Umenifanya mtumwa kwa miaka saba sasa,” akasema.

Siku iliyofuata, wakili wa Liza alimpelekea Peter stakabadhi za talaka na akazikubali. Ni miaka miwili sasa na Liza na Peter ni marafiki ingawa walitakiana. “Nafurahia uhuru wangu naye huniambia anafurahia maisha yake mapya. Anawatembelea watoto kwa kuwa ninaishi nao na huwa nawapeleka kwake pia na kumpatia uroda kwa kuwa nafurahia ustadi wake chumbani na siwezi kuchanganya wanaume sababu najua sio mhanyaji,” asema Liza.

Anasema uhusiano wao umeimarika baada ya kutalikiana. “Huwa anatimizia watoto mahitaji yote na siku yangu ya kuzaliwa alininunulia zawadi ambayo sijawahi kupata katika maisha yangu. Aliniambia alifanya hivyo kama rafiki. Mwaka jana alikuwa mgonjwa na nilimshughulikia hadi akapona,” asema Liza.

Wataalamu wa masuala ya mapenzi na ndoa wanasema kuwa watu wanaweza kuchangamkiana baada ya talaka kwa kuzingatia sababu zilizowafanya kuvunja ndoa.

“Inawezekana wanandoa waliotalikiana kuwa na uhusiano hata wa kimapenzi. Inategemea sababu ya kuvunja ndoa yao. Ikiwa hawakutalikiana kwa sababu ya dhuluma na uzinifu, ni rahisi wao kuchangamkiana na hata kulishana uroda,” asema Doreen Nameme wa shirika la Big Hearts jijini Nairobi.

Nameme anasema kuna watu wanaopapia kutaliki wachumba wao na baadaye wanagundua walikosea.

“Ndio sababu huwa nashauri watu kuchukua muda kutafakari kabla ya kuamua kutaliki wachumba wao. Kuna tofauti zinazoweza kutatuliwa kupitia mazungumzo badala ya talaka,” asema Nameme.

Kulingana na Pasta Lois Gichohi wa Kanisa la Glory Assembly jijini Nairobi, baadhi ya watu huwa wanataliki wachumba wao kwa kuiga wengine. “Kuna watu wanataliki wachumba wao kwa kuwa marafiki zao walifanya hivyo au walisikia walifanya hivyo. Baadaye wanagundua kwamba walikosea. Talaka inafaa kuwa kwa misingi ya kidini na kisheria ambayo imethibitishwa kikamilifu. Kwa maoni yangu, wanaotalikiana sio wanandoa tena na wakifanya mapenzi huwa wanatenda dhambi kwa kuwa sio mume na mke,” asema Gichohi.

Mshauri huyu anasema kukiwa na mawasiliano miongoni mwa wanaotalikiana, ni rahisi kwao kulishana uroda.

“Hii inawezekana ikiwa hawakuachana kwa sababu ya uzinifu au dhuluma,” asema.

Jessica Mwelu, mwanadada mwenye umri wa miaka 34 anasema hawezi kumfungulia mumewe wa zamani mzinga kwa sababu alikuwa akimpiga na kumtesa sana.

“Huwa sitaki kumuona kwa macho yangu. Niliyopitia katika mikono yake kwa miaka sita ni Mungu tu anajua,” asema.

Lakini David Okello anasema yeye na aliyekuwa mkewe huwa wanalishana tunda kila mwezi miaka mitatu baada ya kutalikiana rasmi.

“Alikuja kwangu baada ya mwezi mmoja na akaniambia hawezi kupatia mwanamume mwingine mwili wake nikiwa hai. Mimi sijawahi kuwa na mwanamke mwingine katika maisha yangu na ingawa alinitaliki kutokana na presha kutoka kwa wakwe, tungali tunaburudishana,” asema Okello.

Pasta Gichohi anasema kwamba watu waliowahi kulala kitanda kimoja sio rahisi kunyimana uroda licha ya kutengana. “Ndio sababu tunashauri watu kuvumiliana. Kuna presha nyingi zinazochangia talaka siku hizi ambazo zinaweza kuepukwa kupitia ushauri nasaha kutoka kwa wataalamu waliohitimu,” asema.

Nameme anasema kuna hatari ya watalaka kulishana uroda hasa ikiwa mmoja wa wahusika ameoa au kuolewa. “Itakuwa ni kuzini na pia inaweza kuvuruga maisha ambayo mtu alitamani baada ya kupata talaka. Lakini ikiwa hakuna aliyeoa au kuolewa na kwa hiari ya kila mmoja, wanaweza kulishana uroda katika mazingira salama,” asema.

CHOCHEO: Mume si suti, ni ujasiri!

NA BENSON MATHEKA

Faiza alishangaza marafiki wake kwa kumuacha Ali na kumchumbia Abdul ingawa mwanamume huyo alikuwa akimpenda na kumtunza vyema. Kwa mwanadada huyu, hakupata alichotafuta kwa mume katika Ali.

“Ni kweli ana pesa, ni jamala, nadhifu na ananipenda lakini ni mwoga. Siwezi kuishi na mume mwoga katika maisha yangu. Nani atanilinda nikiwa hatarini?” ahoji Faiza.

Mwanadada huyu anasema ingawa Abdul hana pesa kama Ali, ni jasiri. “Ninataka mume ambaye nitahisi kuwa salama sio mwoga atakayeniuliza atakachofanya kunitoa kwenye hatari,” asema.

Sally, mwanadada mwenye umri wa miaka 32 anasema aliolewa na Mwangi kwa sababu ya ujasiri wake. “Nilimuacha mwanamume aliyekuwa akinipatia chochote kwa sababu niligundua alikuwa mwoga.

Ingawa Mwangi ana pesa nyingi, ninajua kitu kimoja, kwamba hakuna anayeweza kunigusa kwa sababu ataona moto,” asema.Wataalamu wa masuala ya mapenzi wanasema kwamba hakuna mwanamke anayeweza kukubali mwanamume mwoga.

“Wanawake hupenda wanaume wanaoweza kuwahakikishia usalama wao, sio tu kwa kukidhi mahitaji yao, mbali pia kuwalinda dhidi ya hatari inayoweza kuwakabili. Unaweza kumpa mwanamke kila kitu anachohitaji lakini ikiwa hauwezi kumlinda akikumbwa na hatari, atakuacha,” asema Steven Omboki, mwanasaikolojia wa kituo cha Abundant Life mjini Athi River.

“Kigezo muhimu ambacho wanawake wanazingatia wanapotafuta mume ni ujasiri. Mtu jasiri anaweza kufanikiwa katika mambo mengi. Hata akishindwa anaweza kupigana hadi afaulu,” aeleza.Kulingana na Martha Kawira, mshauri mwandamizi wa shirika la Maisha Mema, wanawake wanaamini kwamba mwanamume mwoga hawezi kuwa mume bora.

“Kwa wanawake, mwanamume mwoga hafai kuwa mume wa mtu. Woga unafanya mwanamume kukosa mke kwa sababu wanawake wanapenda mtu atakayewahakikishia usalama wao na watoto wao,” asema Kawira.

Daisy Mukami, mwanadada mwenye umri wa miaka 32 na mama ya watoto wawili, asema alimuacha mumewe alipogundua alikuwa mwoga.

“Hakuweza kuua hata panya katika nyumba yetu. Hakuweza kukabili majirani wakituchokoza. Hakuweza kutetea mali yake ikitumiwa vibaya na watu wengine. Hivyo niliamua kumtema kwa sababu kuwa naye ni sawa na kuishi katika nyumba bila mlango,” asema Mukami. Kawira asema mume anafaa kuwa mlinzi wa mke, watoto na mali.

“Mume sio suti, mume ni zaidi ya kuwa na gari, sura nzuri na kumnunulia mkewe zawadi. Mume ni ngao ya mkewe na familia. Ukipungukiwa na ujasiri, unajiweka katika hatari ya kukosa mke,” asema Kawira.

Watalaamu wanasema wanawake wanaofahamu vigezo halisi vya mume bora huwa wanachunguza iwapo wanaowachumbia ni jasiri.

“Mwanamume jasiri huwa anajiamini na kwa kufanya hivyo, anaweza kufanikiwa. Mwanamume jasiri anaweza kuwa mfano mwema kwa wanawe,” aeleza Omboki.

Lakini Kawira anashauri wanawake kutofautisha aina za ujasiri akisema wanaweza kudhani mwanamume ni jasiri lakini awe katili.

“Hata unapotafuta mwanamume jasiri, chunga usiangukie katili atakayefanya maisha yako kuwa jehanamu. Wanawake wengi huwa wanakosea na hatimaye kujuta,” aeleza Kawira.Omboki anakubaliana na kauli hii akisema baadhi ya wanawake huwa wanajuta kwa kuolewa na wanaume katili wakidhani wamepata walio jasiri.

“Ni muhimu kufahamu chanzo cha ujasiri wa mtu. Kuna ujasiri unaotokana na elimu, mali, imani ya dini na kuna ujasiri wa kipumbavu pia wa kutumia kifua. Kuna watu jasiri lakini hawana hekima. Hao ni hatari,” aeleza.

Kulingana na wataalamu, mume anafaa kulinda mke lakini sio kuwa tishio kwake. Damaris* mwanadada mwenye umri wa miaka 28 anasema alidhani mumewe angekuwa ngao yake lakini akamkosesha amani kwa kumdhulumu kila wakati.

CHOCHEO: Kupata mchumba si muujiza, lazima utoke ukutane na watu

Na BENSON MATHEKA

NICK anakumbuka Januari 4 mwaka uliopita kama jana.

Ni tarehe ambayo pasta wa kanisa lake alimtabiria kuwa kabla ya mwaka kuisha, angepata muujiza kwa kujaliwa mke anayetamani.

“Aliniambia kwamba ningepata muujiza kwa kujaliwa mke ninayetamani. Nimekuwa nikisubiri muujiza huo na sijapata,” asema Nick akizama kwenye mawazo.

Mwaka umeisha na ni bayana kuwa barobaro huyu mwenye umri wa miaka 27 hatapata muujiza ambao amekuwa akisubiri. Faith Karimi, naye amekuwa akisubiri muujiza ajaliwe mume jamali, mwenye nidhamu na uwezo wa kifedha.

“Ninajua muujiza utatokea na nitajaliwa mume wa ndoto yangu,” asema mwanadada huyu mwenye umri wa miaka 30.

Wanasaikolojia wanasema kwamba japo ni vizuri mtu kuwa na imani kwa Mungu, kutafuta mume au mke hakuwezi kuwa muujiza.

“Ikiwa kuna mhuburi aliyekutabiria uketi kitako ukisubiri upate mume au mke kimiujiza, utasubiri milele. Hauwezi ukapata mchumba kwa kuketi tu. Ni lazima utoke, ukutane na watu, urushe na kurushiwa misitari, uchunguze tabia za watu nao wachunguze zako. Hakuna muujiza katika kutafuta mchumba wa maisha,” asema Daisy Simon wa shirika la Big Hearts jijini Nairobi. Mtaalamu huyu anasema baadhi ya wahubiri na hata waganga wamekuwa wakipotosha watu kwa kuwapa matumaini hewa ya kupata wachumba.

“Badala ya kuambia mtu asubiri muujiza wa kujaliwa mchumba, mshauri anavyoweza kupata mchumba mzuri. Mpe ushauri wa kiroho ajue jinsi ya kuchagua na kujua mtu anayeweza kuwa mume au mke mwema,” asema Daisy.

Kulingana na Steve Keli, mshauri wa wanandoa katika kituo cha Life Center, baadhi ya watu huwaelewa vibaya wahubiri wanapofunza kuhusu miujiza ya kupata wachumba.

“Huwa wanawapa matumaini wale ambao huenda wanakaribia kuvunjika moyo kwa kukosa wachumba lakini baadhi ya watu huchukulia ujumbe huo kuwa utabiri wa moja kwa moja kwamba Mungu atawateremshia wachumba kutoka mbinguni,” asema Keli.

Hata hivyo anakiri kwamba baadhi ya wahubiri huwa wanatoa mafunzo ya kupotosha kwa wanaosaka wachumba. Daisy anasema kanisa ni miongoni mwa maeneo salama ya watu kutafuta wachumba.

“Asilimia kubwa ya watu wanaooana hupatana kanisani au katika shughuli za kanisa. Wengine huwa wanapatana katika shughuli za kikazi au maeneo ya kazi. Kuna wanaokutana katika shughuli za kijamii na burudani. Bidii huwa inahitajika kwa kurusha misitari na kujukumika ili kuinasa roho ya mtu,” aeleza Daisy.

Wataalamu wanasema kuwa ni lazima mtu amshawishi mwingine kwamba atakuwa mke au mume mwema jambo ambalo haliwezi kutendeka kimiujiza. “Kuna kutoka na kukutana na mtu akuvutie, uanze kumvuta karibu nawe na hii inahitaji maombi, bidii, wakati na pesa. Inahitaji kujitoa mhanga sana. Kutafuta mke au mume hakuwezi kuwa muujiza baadhi ya watu wanavyodhani,” asema Keli.

Doreen Kuria, aliyefunga ndoa juzi anasema ilimchukua miaka mitatu kukubali kwamba alikuwa amepata mchumba aliyetamani.

“Mtu akikwambia utapata mchumba kimiujiza anakupotosha. Ni kazi inayohitaji bidii na kujitolea kwingi. Kwanza, ni kibarua kumfahamu vyema mchumba wako hadi uridhike ana sifa unazotaka. Wengine huwa wanajifanya,” asema.

Mwanadada huyu anawashauri watu kutokimbilia miujiza inayonadiwa na wahubiri au waganga wanapotafua wachumba.

“Watu wamepotoshwa na waganga eti watawafanyia vimbwanga wapate wachumba wenye sifa wanazotaka, wengine wamepotoshwa na mafunzo ya kidini hadi wakatulia kusubiri wachumba wawajie. Hizi ni porojo. Omba, amini, chukua hatua kwa hiyo imani. Jipambe na uwe tayari kwa gharama ya kutafuta mchumba kwa sababu ipo na anayekueleza vingine anakundanganya,” asema

CHOCHEO: Harusi inapoteleza…

Na BENSON MATHEKA

KWA miaka minne ambayo Aisha alikuwa mchumba wa Salim, alikuwa na furaha ambayo kila mtu hutamani katika uhusiano wa mapenzi.

Lakini walipotangaza harusi yao, mambo yalianza kubadilika. Sio kwa sababu ya Salim, bali changamoto walizopata hadi akadhani harusi yao haingefanyika.

“Tulikabiliwa na wakati mgumu wakati wa kuandaa harusi yetu. Baadhi ya changamoto zikitoka kwa jamaa zetu wa karibu na hata marafiki. Ilifikia hatua ambayo nilimwambia Salim tutoroke tukaishi mbali kama mume na mke bila nikaha rasmi,” asema Aisha. Hata hivyo, Salim alikataa, wakakabiliana na visiki vyote hadi wakafanya harusi ya kufana.

Kwa Pat, ni wakwe na mashemeji watarajiwa waliokuwa wakimwekea vizingiti alipotangaza nia ya kumuoa binti yao aliyekuwa amemchumbia kwa miaka sita. “Niliwekewa masharti makali ambayo Brenda hakufurahia. Niliambiwa mambo kumhusu yeye na familia yake ambayo kama singekuwa nampenda kwa dhati, ningebadilisha nia. Nilijikaza kama mwanamume na kumuoa kiosha roho wangu kwa harusi ya nguvu sana na sasa tunaishi kwa furaha,” asema Pat.

Baadhi ya vizingiti, huwekwa na viongozi wa kiroho jinsi alivyoshuhudia Myra alipoenda kumuomba pasta wa kanisa lake ushauri kuhusu ndoa. “Niliyoyasikia kutoka kwa pasta huyo sikuweza kuamini yalitoka kwa kinywa cha kiongozi wa kiroho. Siwezi kuyatamka. Yaliniuma sana na nilipokataa kutimiza aliyotaka, alikataa kuongoza harusi yangu,” asema Myra.

Washauri wa wanandoa wanasema kuwa vizingiti wanavyopata wachumba wanapopanga harusi huwa ni mtihani wa kupima upendo wao. “Japo baadhi ya vizingiti huwa vinasababishwa na watu wenye nia mbaya, huwa ni mtihani kwa wanaopanga ndoa. Kwa mfano, ikiwa vinawekwa na jamaa wa karibu, vinakufanya kuwaelewa vyema na kukuwezesha kupanga jinsi ya kuhusiana nao,” asema Steve Kiano wa kituo cha Liberty mjini Athi River.

Anasema kwamba baadhi ya watu huwa wanapata vikwazo kutoka kwa wazazi wao wakati wa kupanga harusi. Delphina Wangui mkazi wa mtaa wa Syokimau, Nairobi anasema alikuwa na wakati mgumu kuwashawishi wazazi wake kupokea mahari kutoka kwa mpenzi wake.

“Walikuwa wakimfahamu James kwa miaka mitatu. Lakini wakati tulipotangaza mipango ya kufanya harusi, walianza kisirani. Hawakuwa na sababu maalumu ya kukataa kutupatia baraka tufunge ndoa. Ilinibidi nitume wazee wa familia kumshawishi baba yangu na pia aliwatatiza sana. Alikubali kupokea mahari wazee walipotisha kumtenga,” alisema Wangui.

Viongozi wa kidini walaumiwa

Kiano analaumu viongozi wa kidini wanaowavunja moyo wachumba wanaotaka ushauri kuhusu ndoa.

“Wapo wanaofanya hivyo kwa sababu za kibinafsi, kuna wengine wanaofanya hivyo kwa sababu ya tamaa kama vile kuitisha pesa nyingi kufungisha harusi. Kuna wanaokataza waumini kusaidia vijana wa makanisa wanapopanga harusi na kuna wanaohisi kuwa watapoteza washirika wasichana wakiolewa. Haifai kuwa hivi. Jukumu la viongozi wa kidini ni kuwaelekeza wachumba kuoana katika ndoa takatifu na sio kuwawekea vikwazo,” asema.

Watalaamu wanasema vikwazo vingine vinavyotokea wakati watu wanapoanza kutayarisha harusi huwa vya kifedha.

“Unapata hali ambayo hukutarajia. Pesa zinakosa na kutishia mipango ya harusi dakika ya mwisho. Hali hii ikitokea, wachumba wanafaa kuketi na kurekebisha mipango yao kwa kupunguza bajeti yao,” asema Faith Kimondo wa shirika la Do It Right, jijini Nairobi.

Anashauri wanaopanga harusi kujiandaa kwa visirani, visiki na vibwanga vya kila aina. “Kufikia siku ya harusi, watu huwa wanakumbana na changamoto za kila aina. Muhimu ni kujipa moyo ili kupata mke na mume wa ndoto yako. Visiki hivi vinaweza kutoka popote na kwa yeyote wakati wowote wa kuandaa harusi,” asema Faith.

CHOCHEO: Krismasi bila sherehe, itakuwaje?

Na BENSON MATHEKA

KILA Desemba Shiru huwa anafurahia kukutana na jamaa zake ushago kwa sherehe za Krismasi kwa siku tatu kabla ya kurejea mjini kuungana na mpenzi wake Nderitu kuukaribisha mwaka mpya.

Lakini mwaka huu anahisi kuwa hataweza kusafiri mashambani Mathira, Kaunti ya Nyeri kwa sababu ya janga la corona.

“Tumekubaliana kama familia kwamba hatutakuwa na sherehe ya familia mwaka huu. Hatutaki kuhatarisha maisha yao msimu huu wa janga la corona hasa wale walio na umri mkubwa,” asema Shiru.

Hata kama hatua hii itampa fursa ya kuwa na mpenzi wake kwa muda mrefu wakati wa sherehe za Krismasi, itabidi wawe waangalifu sana. “Mimi na Nderitu tumeamua kutotembelea sehemu za burudani zilizo na watu wengi ili tuepuke kujiweka kwenye hatari ya kuambukizwa virusi hivi. Tungesafiri hadi Watamu lakini tumeamua kujivinjari Nairobi kwa usalama wa afya zetu,” asema.

Wataalamu wa afya na mahusiano wanasema kuwa sherehe za Krismasi mwaka huu zitakuwa tofauti kwa watu wanaoelewa hatari iliyomo. “Tunajua watu wamezoea kuthibitisha upendo kwa familia na mapenzi kwa wachumba wao wakati wa Krismasi. Familia huwa zinaandaa sherehe kubwa za kushukuru ambapo watu husafiri kutoka maeneo mbalimbali kuungana na jamaa zao. Tunashauri kwamba wafute sherehe na safari mwaka huu kuepusha hatari ya kusambaza virusi vya corona,” asema Meshack Omondi wa shirika la Love Care, Nairobi.

Meshack anasema kuwa tafiti zimeonyesha hata sherehe ndogo za kifamilia zinaweza kuchangia ongezeko la maambukizi ya corona jinsi ilivyofanyika Canada mwezi Oktoba familia zilipoandaa hafla za kutoa shukrani.

Kulingana na utafiti wa shirika la Ipsos Canada, nchi hiyo ilikuwa na watu 185,000 waliokuwa wameambukizwa corona kufikia Oktoba 12. Baada ya sherehe hizo, idadi hiyo iliongezeka maradufu. Hii ilitokana na watu kuandaa sherehe ndogo za kifamilia licha ya kuonywa kuziepuka. “Watu walionywa lakini familia chache zilipuuza na kukutana na wapendwa wao. Tunaona matokeo kutokana na maambukizi kuongezeka,” Ipsos ilisema kwenye ripoti yake.

Kulingana na Meshack, watu wanapaswa kuweka breki safari za mashambani na kuhudhuria burudani katika maeneo yaliyo na msongamano wa watu msimu huu wa sherehe. “Huu ndio wakati wa wapenzi kubuni mbinu mbadala za kudhihirisha mapenzi. Anayekupenda hatakushurutisha umpeleke katika kumbi za burudani au usafiri kwa matatu kwenda kumtembelea. Ikiwa anakulazimisha, basi hakupendi. Anayekupenda kwa dhati atakuambia kaa nyumbani kwa usalama wa afya yako,” asema Meshack.

Wataalamu wanasema hata hafla za chini ya watu kumi zimehusishwa na ongezeko la maambukizi katika nchi tofauti ulimwenguni. “Njia salama pekee ya watu kukutana msimu wa sherehe mwaka huu ni kupitia video mtandaoni. Mikutano hii ndiyo suluhu kwa wakati huu kote ulimwenguni,” Dkt Iahn Gonsenhauser, mkuu wa usalama wa wagonjwa katika Wexner Medical Center, chuo kikuu cha Ohio, Amerika aliambia jarida la Huffpost.

Anasema ili watu waweze kukinga wapendwa wao wasiambukizwe corona, wanafaa kuepuka kusafiri kukutana nao msimu wa sherehe mwaka huu. “Itabidi watu wavumilie mwaka huu ili kuweka jamii ikiwa salama. Kuna matumaini kwamba mambo yatakuwa sawa Desemba 2021 wakitii kanuni za kukabili janga hili na chanjo zikipatikana,” asema Dkt Iahn.

Hivi ndivyo anavyoamini Jerusha, mwanadada mwenye umri wa miaka 26 anayesema ingawa anampenda mchumba wake kwa dhati, hataweza kusafiri Afrika Kusini kuwa naye msimu huu. “Tulikubaliana kwamba kwa usalama wetu, tutawasiliana kwenye mtandao. Tungetaka kukumbatiana na kulishana mapenzi ‘mundu kumundu’ lakini afya yetu ni muhimu zaidi,” asema Jerusha.

Wataalamu wa afya wanasema ingawa maambukizi yamesambaa kote nchini, watu wanaweza kujikinga kwa kuepuka kusafiri msimu huu wa sherehe na kuepuka maeneo ya burudani yenye watu wengi.

CHOCHEO: Usiwe zuzu wa mapenzi

Na BENSON MATHEKA

“HUWEZI ukamfanya mtu mwingine kuwa bora usipojiboresha kwanza. Huwezi ukapata mpenzi unayemtamani usipotia bidii ya kufanya utamaniwe.” Huu ndio ushauri ambao Jimi huwa anakumbuka kila siku katika safari na maisha yake ya mapenzi.

Barobaro huyu anaamini kwamba japo hakuna mtu mkamilifu katika ulimwengu wa mapenzi, ili mtu apate mwanadada wa ndoto yake wa kuoa, ni sharti atie bidii kujiimarisha.

“Nilikuwa nimevunjika moyo kwa sababu ya kukosa mchumba hadi nilipokutana na wataalamu wa masuala ya mapenzi. Walinidadisi sana kuhusu aina ya mpenzi ninayesaka. Niliwaeleza natamani demu aliye na ajira, aliyejitunza, mcha Mungu na aliye na maono ya siku zijazo. Waliniambia kwamba mkunwa hujikuna na ninaweza kupata demu wa aina hiyo nikitimiza hayo kwanza,” asema Jimi.

Baada ya kupatiwa ushauri huu, aliutilia maanani na akajitahidi kwa kila hali. Alirudi chuo kikuu kuongeza masomo, akapata kazi katika benki, akanunua gari na akashikilia kwa dhati imani yake kwa Mungu hadi alipompata Irene, meneja wa shirika moja la kimataifa ambaye alikuwa na maono sawa na yake. Irene anasema alivutiwa na Jimi kwa sababu amejipanga katika maisha.

“Ni mcha Mungu kama mimi na anajua anachotaka maishani. Kama ni pesa niko na zakutosha. Jimi sio kama wanaume wanaotamani wanawake walio na pesa ilhali wao hawataki kuzitafuta. Nilipompata, maisha yetu yalikamilika na tunafurahia ndoa yetu,” asema.

Vigezo

Wataalamu wa masuala ya mapenzi wanasema njia ya pekee ya kupata mpenzi wa ndoto yako ni kuhakikisha unatimiza vigezo unavyotaka awe navyo. “Jitengeneze kwanza, jiandae kwanza. Jikarabati na ukarabati maisha yako. Ukitaka mpenzi aliye na gari, tia bidii ununue lako. Huwezi ukamtunza mtu ikiwa huwezi kujitunza binafsi,” asema Harry Okoth, mwanasaikolojia wa shirika la Life Beyond Today.

Kulingana na Harry, watu hujisononesha kwa kuwamezea mate watu ambao tayari wamefanikiwa ilhali wao hawataki kutia bidii kufanikiwa. “Siku hizi wanaume pia wanataka wanawake waliofanikiwa. Badala ya kuhangaika, tia bidii kujenga maisha yako na utawapata. Ukitaka mke au mume mcha Mungu, muogope Mola pia,” asema.

Cecilia Mathenge wa shirika la Center That Hold jijini Nairobi, anasema watu huwa wanakosea kwa kuamini kuwa wanaweza kubadilisha wenzao kuwa bora wakianza uhusiano wa kimapenzi. “Hauwezi ukabadilisha mtu asiyeweza kujibadilisha. Wale waliojaribu kufanya hivyo waliishia kujuta,” asema.

Eve Nekesa mkazi wa mtaa wa Umoja, Nairobi, anasema kwamba alijuta kufikiri kuwa angembadilisha mwanamume mlevi aliyevutiwa naye. “Haikuwezekana, nilijuta kwa kuchukua uamuzi huo. Jamaa hakuwa na maono na alidhani kila hatua niliyochukua kumfanya abadilike ilikuwa ya kumdhalilisha,” asema.

Mwanadada huyu asema baada ya kuachana na jamaa huyo alizingatia biashara yake na kushikilia imani yake katika Mungu hadi akampata Edu, mtaalamu wa masuala ya uwekezaji na sasa wanapanga harusi.

“Nilichojifunza ni kuwa mtu anafaa kujiimarisha kwanza kabla kusaka mpenzi wa kumfanya kuwa bora. Asiyeshughulika kujiboresha hawezi kumfanya mwingine kuwa bora,” asema.

Cecilia anasema ni makosa kuingia katika uhusiano wa mapenzi kwa kuhisi kuwa umechelewa. “Kuna watu waliofanikiwa maishani ambao hupoteza maono yao na kuanza uhusiano wa mapenzi na watu kwa kuhisi wamechelewa. Uamuzi kama huu ni hatari kwa kuwa unasambaratisha maono yako na kukufanya ujute baadaye. Utulivu, subira na umakini ni muhimu sana katika kupata mpenzi wa ndoto yako,” asema.

Hilda, mfanyakazi wa kampuni moja mjini Athi River, anakubaliana na kauli hii akisema alilazimika kumtema mwanamume aliyemrudisha nyuma kwa kukosa maono. “Nilikutana naye nikiwa na duka. Badala ya kunishika mkono alikuwa akichukua pesa za biashara kwenda kulewa. Sikumvumilia katu, nilimpiga teke haraka upesi,” asema.

CHOCHEO: Ufanyeje akipoteza figa?

Na BENSON MATHEKA

“PAT hanitaki siku hizi. Anasema mimi sio yule demu alioa miaka mitano iliyopita nilipokuwa na figa 8. Tatizo lake ni kuwa nimekuwa mnene baada ya kujifungua na sio kupenda kwangu,” Karimi mwanadada mwenye umri wa miaka 29, alalamika.

Mwanadada huyu anasema kwamba anahofia huenda mumewe akaanza kuhanya na vipusa wenye umbo analotamani. Cha kushangaza ni kuwa si Karimi peke anapitia hayo.

Mary, mwanadada mwenye umri wa miaka 33 anajichukia baada ya mumewe kulalamika kuwa sura na umbo lake zimebadilika tangu harusi yao miaka tisa iliyopita.

“Anasema ninafaa kudumisha sura na umbo langu, nibaki yule kidosho aliyefunga pingu za maisha naye ingawa sasa mimi ni mama wa watoto wawili,” asema Mary.

Kulingana na mwanadada huyu, hii imefanya uhusiano wake na mumewe kuingia doa.

Wataalamu wa masuala ya ndoa na lishe bora wanasema kwamba ingawa ni muhimu kudumisha umbo zuri, mtu hubadilika miaka inaposonga hasa wanawake wakiolewa na kujifungua.

“Wanaume wanafaa kuelewa kuwa sura na umbo la mwanamke hubadilika miaka inaposonga sanasana wanapojifungua. Kuna wale wanaorudia umbo lao la awali na kuna wale ambao hairudi hata wakijaribu lishe na mazoezi,” asema Rukia Hirsi, mtaalamu wa lishe na afya ya wanawake katika shirika la Mirage, jijini Nairobi.

“Kuna homoni za mwili wa mwanamke zinazosababisha mabadiliko umri unaposonga, anapopata watoto na hata anapokuwa kwenye ndoa isiyo na misukosuko. Kuridhika tu kunaweza kufanya mwanamke kuongeza uzani wa mwili na kupoteza umbo na sura aliyokuwa nayo kabla ya kuolewa,” asema Rukia.

Mtaalamu huyu anasema kuwa wanawake wanaweza kudumisha umbo lao kwa kuepuka vyakula vyenye mafuta na sukari nyingi na kufanya mazoezi.

“Usile kila kitu. Hakikisha unaepuka mapochopocho na upate chakula bora kisicho na mafuta mengi. Fanya mazoezi ambayo pia ni muhimu kwa afya yako,” asema.

Wataalamu wanasema badala ya kuwalaumu wake zao, wanaume wanafaa kuwasaidia kudumisha saizi ya mwili wanayopenda.

Lalama

“Kubadilika kwa umbo la mwili hakufai kuwa tisho kwa ndoa. Wanaume wanafaa kusaidia wachumba wao badala ya kuwalaumu na kutumia hicho kama kisingizio cha kuchepuka. Hata wanaume huwa wanajipata katika hali hii umri unaposonga, wakioa na wasipofanya mazoezi,” asema Godfrey Kyule, mshauri wa wanandoa wa shirika la Amani Purpose, mtaani Kitisuru, Nairobi.

Jairus Sumba, mwanamume mwenye umri wa miaka 31, alijipata katika hali hii miaka mitatu baada ya kuoa.

“Sijui nyama za mwili zilitoka wapi. Niliongeza uzani kutoka kilo 66 hadi 102 na mke wangu akaanza kulalamika kwamba nimekuwa mzembe chumbani. Tulijadili suala hilo na baada ya kupata ushauri kuhusu lishe na mazoezi, huwa ninachezea kilo 78 na 81,” asema Sumba.

Anasema kuwa mabadiliko katika mwili wake yalitokana na amani ambayo mkewe alimpatia baada ya harusi.

“Akili yangu ilitulia baada ya kuoa. Mke wangu hakunipa ‘stress’ hata kidogo,” asema.

Jayreen Chomba, mama ya watoto watatu anasema kwamba amedumisha umbo lake kwa kuzingatia lishe na mazoezi.

“Sijawahi kuwa na zaidi ya kilo 60 bila mimba. Hata baada ya kujifungua, huwa ninahakikisha ninapata lishe bora. Nashauri wanawake kutotafuna na kuchangamkia vyakula vya hotelini ikiwa wanataka kudumisha umbo bora,” asema.

Rukia anasisitiza kuwa wanaume hawafai kulaumu wake zao kwa mabadiliko ya umbo mbali wanafaa kuwasaidia.

“Mili ya wanawake ni tofauti na ya wanaume. Ikiwa unampenda mtu wako, elewa mabadiliko ya mwili wake na umsaidie badala ya kumlaumu,” asema.

“Sisemi wanawake wajiachilie lakini mara nyingi wanaume huwa wanachangia mabadiliko ya mili ya wake zao,” asema.

CHOCHEO: Uhusiano unaozaa ndoa bora huanza kwa urafiki

Na BENSON MATHEKA

DEBORAH anajuta kwa kukataa kuolewa na Sammy ambaye ni rafiki yake wa miaka mingi.

Mwanadada huyo anasema sio kwamba hakuwa akimpenda Sammy lakini alimkataa kwa sababu hakutimiza vigezo ambavyo alitaka kwa mume.

Alimchagua Deno kwa sababu alikuwa na mali na alipenda kusafiri kwenda kujivinjari katika maeneo ya burudani tofauti na Sammy ambaye hutumia muda mwingi akiwa kazini.

“Makosa niliyofanya ni kufikiri pesa za Deno na hulka yake vingenihakikishia furaha katika ndoa. Baada ya miaka minne, niligundua nilikosea nikaanza kujuta kwa kumkataa Sammy ambaye sasa ninaamini angekuwa mume mzuri hata kama hana mali nyingi,” asema Deborah, kauli ambayo Silvia Wariara, mwanasaikolojia katika kituo cha Maisha Mema, jijini Nairobi anakubaliana nayo.

“Ukitaka maisha mazuri ya ndoa, oa au olewa na rafiki yako wa dhati. Mtu akikosa kuwa na urafiki na mchumba wake, maisha ya ndoa huwa jinamizi,” asema Wariara.

Deborah anasema hakuweza kuelewana na Deno na walikuwa wakiishi ulimwengu tofauti ndani ya nyumba moja hadi akaamua yametosha na kuomba talaka.

“Ilikuwa jehanamu,” asema.

Wataalamu wa masuala ya ndoa wanasema kwamba kinachofanya ndoa iliyojikita katika misingi ya urafiki wa dhati kunawiri ni kwa sababu wachumba huwa wanaaminiana.

“Wanandoa wanafaa kuaminiana na hii inawezekana tu kwa marafiki. Uaminifu ukikosa, na hauwezi kununuliwa kwa mali, sura au umbo, ndoa inakuwa balaa,” asema Wariara.

Anasema kwamba umuhimu wa urafiki katika ndoa ni kuwa kila mchumba anamjali, kumwelewa na kumheshimu mwenzake.

“Mtu anapopata shida, huwa anampigia simu rafiki yake kwanza. Kwa marafiki, hakuna siri na hii ni moja ya vigezo muhimu vya ndoa yenye furaha. Kufichana mambo kumetambuliwa kama sumu katika ndoa. Rafiki wa dhati hatakuficha chochote,” asema Peter Simbi, mshauri wa wanandoa katika kanisa la Life Center, jijini Nairobi.

Simbi anasema kuwa raha ya marafiki wanaooana huchangiwa na wepesi wa mawasiliano kati yao.

“Ukosefu wa mawasiliano umetambuliwa kuwa sumu ya ndoa. Rafiki ni mtu unayefurahi kuwa karibu naye bila masharti. Mnayefaana wakati wa raha na wakati wa dhiki. Ukioa au kuolewa na mtu kama huyo na muendelee kupalilia urafiki wenu, utatoboa katika ndoa,” aeleza Simbi.

Uchu

Anasema inasononesha kuishi katika ndoa na mtu anayekuchangamkia wakati wa uroda pekee. “Ulaji uroda sio dhihirisho la urafiki. Kuna tofauti ya uchu na urafiki. Watu wengi huwa wanaolewa kwa sababu ya uchu, yaani tamaa ya kimwili na kisha kujipata wakiishi kwa dhiki,” asema.

Wariara anakubaliana na kauli hii akisema kinachofanya ndoa kati ya marafiki kushamiri ni kwa sababu huwa na tabia sawa na wanachangamkia vitu vinavyofanana.

“Marafiki huwa wanafunguliana roho, jambo ambalo ni muhimu sana katika ndoa. Kuwa na hulka zinazofanana kunarahisisha maamuzi ya mambo,” aeleza.

Wanasaikolojia wanasema kwamba kwa sababu ya kufahaminiana, kuaminiana na kuelewana, huwa ni vigumu kwa marafiki kukosana wakioana.

“Oa au olewa na rafiki yako. Ukishindwa kupalilia urafiki kati yako na mpenzi wako, usipige hatua ya kuoelewa. Utajipata katika balaa,” asema Isabel Kakui, mshauri wa shirika la Abudant Love Care, jijini Nairobi.

Anasema ni rahisi kubaini ikiwa mtu ni rafiki yako kwa kuwa marafiki huzungumza lugha moja.

“Ikiwa lugha ya mpenzi wako ina kuudhi, ni ya ukali na hakuelewi au analazimisha mambo kumfaa badala ya kuwafaa nyinyi wawili, basi epuka ndoa,” asema.

Kakui anasema rafiki hufanya mtu acheke na sio kulia, kuchangamka na sio kununa. “Hata kama watu wengine hawakuchamgamkii, ukiwa na rafiki mnaweza kucheka na kutaniana. Olewa na mtu kama huyo,” asema.

Wataalamu wanasema kwamba hata wakigombana, marafiki huwa wanazika tofauti zao, kutafuta suluhu na kusameheana.

“Kinachofanya ndoa kati ya marafiki kuwa ya kipekee ni kwa sababu wanasaidiana kwa hali na mali. Hii ndio hufanya ndoa kushamiri kwa kuwa wanaweza kupanga na kutekeleza mambo yao pamoja,” asema Wariara.

CHOCHEO: Kumbania unyumba ni kualika vidudumtu

Na BENSON MATHEKA

KWA miaka sita ambayo Eric amekuwa katika ndoa, hakuwa amemshuku mkewe Tabby.

Mwanadada huyo alikuwa akimheshimu na kukidhi mahitaji yake ya tendo la ndoa kikamilifu hata baada ya shughuli kuongezeka nyumbani alipojaliwa kifungua mimba.

Hata hivyo, matukio ya miezi minane iliyopita yamemfanya kuwa na wasiwasi. Anasema kwamba Tabby alibadilisha tabia, alianza kufika nyumbani akiwa amechelewa na kudai alikuwa na kazi nyingi ofisini madai ambayo Eric alishuku.

“Alianza kufika nyumbani baada ya saa moja jioni licha ya kuwa anafanya kazi katika ofisi ya serikali inayofungwa saa kumi na moja. Ofisi yao iko kilomita mbili kutoka nyumbani. Ameanza kunibania tendo la ndoa, mara anadai amechoka au anahisi usingizi na mazungumzo pia yamepungua. Ninashuku amepata kituliza roho huko nje,” asema Eric.

Kulingana na mwanamume huyo, mkewe ameacha kuwasiliana naye jinsi alivyokuwa akifanya na huwa anashinda akichati kwenye simu yake.

“Wakati mwingine huwa analala saa saba usiku akiwasiliana na watu ambao siwafahamu. Hilo, pamoja na kunibania tendo la ndoa, ni ishara kwamba anagawa tunda. Kwa nini aninyime haki yangu ya chumbani ikiwa hana mipango ya kando?” anahoji Eric.

Deborah Kanyi, ambaye amekuwa katika ndoa kwa miaka minne ana lawama sawa na Eric. Anasema mumewe Peter ameanza tabia ya kumbania uroda akidai amechoka. “Alikuwa akinipa burudani tosha lakini siku hizi amelegea. Pia anafika nyumbani usiku kabisa akidai huwa na shughuli nyingi na hataki nishike simu yake,” asema.

Kulingana na wanasaikolojia na washauri wa masuala ya ndoa, mtu akianza kumnyima mpenzi wake tendo la ndoa bila sababu maalumu, anaweza kuvuruga ndoa yake.

“Kubadilika ghafla na kuanza kumnyima mchumba wako tendo la ndoa kunaweza kufanya uhusiano wenu kuwa baridi. Vilevile, uhusiano ukiwa baridi unaweza kufanya mmoja wenu kutochangamkia tendo la ndoa. Hali kama hii inaweza kusuluhishwa kupitia mazungumzo ya wazi katika mazingira ya kuheshimiana,” asema Serah Karimi, mtaalamu wa wanandoa katika shirika la Forever Care, jijini Nairobi.

Ikiwa anayelaumiwa anakataa kufanikisha mawasiliano kama vile kutochukua simu au kukataa mazungumzo, huwa anampa mwenzake sababu za kuamini ana kimada anayemtuliza nje ya boma lake.

“Kuna tabia ambazo walio na mipango ya kando huwa nazo kama vile kutowachangamkia wachumba wao wakati wa tendo la ndoa. Hii huwa inasambaratisha uhusiano au kuufanya baridi kiasi cha kukosesha mtu raha,” asema.

Washauri wa ndoa wanasema kwamba wanandoa hawafai kubaniana tendo la ndoa ikiwa hali inaruhusu. “Jimwage mzima mzima kwa mtu wako. Mpe haki yake. Mke akitaka mpe, mume akitaka mpe, wakati wowote. Hii itaimarisha raha katika ndoa. Ukianza vijisababu, utakuwa unajipalilia makaa na kuchoma uhusiano wetu. Mchangamkie mtu wako bila mipaka,” asema Karimi.

David Kamau, mshauri wa wanandoa katika kanisa la Liberty Live Center, mjini Athi River, anasema kwamba mtu anapoanza kumbania au kumnyima mwenzake tendo la ndoa bila sababu maalumu, huwa anakiuka jukumu lake.

“Tendo la ndoa ni haki muhimu inayounganisha wanandoa. Hivyo basi, kumnyima mwenzako bila sababu maalumu, ni kuvunja ile nguzo ya ndoa,” anasema Kamau.

“Ushauri wangu ni kutoa mwili wako bila vikwazo kwa mwenzio,” asema.

Karimi anasema ingawa kuanza kuchelewa kufika nyumbani, kutochangamkia ngoma chumbani na kutotaka kuwasiliana na mchumba wako huwa ni ishara mtu ameanza michepuko, ni muhimu kuthibitisha kwanza kabla kukurupuka.

“Inaweza kuwa mtu wako anasema ukweli akikuambia amechelewa kazini au amechoka. Lakini hii haiwezi kuwa ni kila wakati au kwa siku fulani. Haiwezi kuwa ni kila Ijumaa au wikendi. Ikianza kuwa kawaida, basi una sababu ya kushuku lakini muhimu ni kuthibitisha kwanza,” asema.

Kulingana na Kamau, kumbania mchumba wako tendo la ndoa sio tu kukiuka sheria za ndoa mbali pia ni kumtia katika majaribu. “Mwandalie mtu wako burudani, mtimizie haki yake ya ndoa, mchangamshe ahisi raha naye hatakushuku,” asema.

CHOCHEO: Tendo la ndoa ni raha, si karaha

Na BENSON MATHEKA

“MTU wangu amezidi siku hizi. Silali. Sijui hanjamu zake zimetoka wapi na akiendelea hivi sitaweza kuvumilia,” Ciku* alimweleza rafiki yake wa karibu.

Alisema mumewe huwa anamhangaisha kila usiku akitaka haki ya ndoa.

“Hata mchana akiwa nyumbani, huwa anataka uroda. Kusema kweli he is just too much. I cannot cope,” akasema.

Lakini kwa rafiki yake Sue* mambo ni tofauti. Mumewe hashughuliki naye na amekuwa pia akifikiria kumuacha.

“Unalalamika wengine tukilia. Heri wako anakupepeta hadi unaogopa kupepetwa. Wangu ni baridi. Huchangamkia shughuli mara moja kwa wiki na kuniachia kiu. Nafikiria kuchepuka lakini naogopa hatari huko nje na naona heri nimuache rasmi nikatafute sogora wa ngoma kama huyo wako,” Sue alimwambia Ciku.

Ingawa marafiki hawa walikuwa na ujasiri wa kufunguliana roho zao, wataalamu wa masuala ya mapenzi wanasema ni miongoni mwa wengi wanaoteseka baada ya viwango vyao vya utekelezaji wa tendo la ndoa kutofautiana na vya wachumba wao. Wanasema kuwa baadhi ya wanawake hujipata hawamudu makombora ya wachumba wao nao wanaume wanapata hawawezi kutoshana na hanjamu za viosha roho wao.

“Hii huwa inatokea mara nyingi ambapo watu hupata hawakimu mahitaji ya tendo la ndoa la wachumba wao. Ni jambo la kawaida lakini linaloweza kuvunja uhusiano wa kimapenzi,” asema mwanasaikolojia Jimmy Gitau wa Shirika la Abundant Love, jijini Nairobi.

Anasema kuna wanawake walio na damu moto kuliko wachumba wao na wanataka ngoma kila siku iwe mchana au usiku na pia kuna wanaume ambao kwao burudani chumbani ni kama mlo.

“Tatizo kubwa ni kwamba hii inasababisha mateso ya kisaikolojia kwa aliye ni kiwango cha chini cha cha uroda na inaweza kumkosesha furaha. Hivyo basi, wachumba wakigundua uwezo wao wa kula uroda unatofautiana, wanafaa kutafuta mbinu za kusawazisha bila kuchepuka au kuachana,” asema Gitau.

Watalaamu wanapendekeza wachumba kujadili suala hili kwa uwazi bila hasira.

“Kuketi chini na kuzungumza kunaweza kusuluhisha tatizo hili kwa sababu linaweza kumpata kila mtu,” asema Gitau.

Kulingana na Mwanasaikolojia David Ouko wa shirika la Liberty Center, mtaani Athi River, kuna watu wanaoamini kuwa ujasiri wa kutekeleza tendo la ndoa ni kulishiriki kila siku.

“Kwao huwa wanataka kudhihirishia wachumba wao kwamba wanawapenda bila kubaini kwamba wanawatesa. Mazungumzo yanaweza kuwafanya waelewe kuwa wanaweza kudhihirisha mapenzi kwa njia mbadala,” asema.

Anasema kwamba watu wanaweza kuonyeshana upendo kwa kutendeana mema, kuandamana katika hafla za kijamii na kupakatana bila kushiriki tendo la ndoa.

“Kwa kufanya hivi, wachumba wanaweza kusawazisha viwango vyao vya ulaji uroda kwa sababu wanaelewana zaidi na kuaminiana. Ajabu ni kuwa wasiofanya hivi huwa wanashuku wenzao wana mipango ya kando wakisita kuwalisha uroda,” asema.

Wataalamu wanasema watu wanapojadili suala hili huwa wanakubaliana jinsi ya kukidhi hanjamu zao bila kutesana.

“Iwapo mmoja anataka kuchovya asali kila siku na mwingine mara tatu kwa mwezi, wakijadiliana wanaweza kukubaliana iwe mara mbili kwa wiki,” asema Ouko.

Mtaalamu huyu anasema uwezo wa kucheza ngoma chumbani hutegemea umri, afya na dhana ya mtu.

Nita Karimi, mtaalamu katika shirika la Sure and Refined Counseling Services, jijini Nairobi anasema njia bora ya kuweka viwango vyao utekelezaji wa tendo la ndoa katika kiwango sawa kwa wachumba ni kuwa na ratiba ya kulishana uroda.

“Wakati wachumba wanapoweka ratiba ya kulishana asali, taharuki huondoka katika akili zao wakijiandaa kwa siku ya ngoma,” asema.

Hata hivyo anasema watu hawafai kutumia ratiba ya kufanya mapenzi kuwaadhibu wachumba.

“Kila kitu kinafaa kuwa kwa kiasi na ustadi. Lisha mwenzako uroda kwa kumjali sio kumwadhibu ukijua kuna siku nyingine mliyopanga kupandishana mizuka,” asema.

Kulingana na Karimi watu wakiweka ratiba ya kulishana asali na kuidumisha, hawawezi kuchokana. Anasema hii huwa inasawazisha hanjamu zao na kuwaweka katika kiwango kimoja wanapomenyana chumbani.

CHOCHEO: Mfadhaiko wa corona wafanya miereka ya kitandani kupungua

Na BENSON MATHEKA

SIO siri kwamba janga la corona limeathiri pakubwa maisha ya mapenzi ya watu wengi. Marufuku ya kusafiri imenyima watu fursa ya kukutana na wapenzi wao.

Watu hawawezi kuzuru maeneo ya burudani kujivinjari na wachumba wao na hata kama maeneo hayo yangekuwa yamefunguliwa, mapato ya watu wengi yamepungua.

Wataalamu wa masuala ya mapenzi wanasema kwamba janga la corona limefanya watu wengi kukosa uwezo wa kutekeleza tendo la ndoa.

“Athari za janga la corona zimefanya watu wengi kukosa hamu ya kula uroda na hii inatishia ndoa nyingi kote ulimwenguni,” mwanasaikolojia Shannon Chavez, aliambia jarida la mtandaoni la Huffpost.

Mwanasaikolojia huyo anasema kwamba hali hii inachangiwa na shinikizo ambazo watu wanapitia kwa kupoteza kazi na mapato yao.

“Ni kawaida ya watu kukosa hamu ya kutekeleza tendo la ndoa wakiwa na mfadhaiko au wanapokabiliwa na masononeko au machungu maishani na athari za janga la corona zimewafanya wengi kukosa matumaini. Katika hali hii watu hukosa uwezo wa kutekeleza tendo la ndoa,” asema Chavez.

Wataalamu wanasema kwamba watu wengi wanafikiria jinsi ya kufufua uwezo wao wa kifedha.

“Janga la corona lilisukuma watu pabaya wakawa na mfadhaiko, wanakosa usingizi na hawana hamu ya kula uroda. Mtu akiwa na mfadhaiko uwezo wa kusakata ngoma chumbani huwa unapungua,” asema Daisy Kawira wa shirika la Maisha Mema jijini Nairobi.

Kulingana na Kawira, kukaa nyumbani kwa wanandoa kwa muda mrefu kunachangia kudorora kwa hamu ya kuburudishana chumbani.

“Wachumba wakikaa pamoja nyumbani, huwa wanaweza kukasirikiana, kuchokana na kukosa kuchangamkiana chumbani. Hali ikiwa hii, hamu ya tendo la ndoa hufifia,” asema Kawira.

Anakubaliana na Chavez kwamba corona imedidimiza hamu na uwezo wa tendo la ndoa wa wachumba wanaoishi pamoja.

Hata hivyo, mwanasaikolojia Christine Koli anasema kukaa nyumbani kunafaa kufanya wachumba kujipanga vyema.

“Muda mwingi wa kuwa pamoja wakati huu wa corona umefanya wanandoa kujipanga upya zaidi kuhusu tendo la ndoa. Wana muda wa kudekezana zaidi hata bila kujamiiana; jambo ambalo ni muhimu katika uhusiano wa kimapenzi,” asema Koli.

Wanasaikolojia wanasema kwamba baadhi ya watu wanakosa hamu na uwezo wa kula uroda kwa sababu ya kutazama picha na video za mapenzi mitandaoni.

“Katika uhusiano wa mapenzi, mchumba mmoja akizama katika ponografia uwezo wake wa tendo la ndoa hupungua na hali huwa mbaya,” aeleza Chavez.

Kulingana na Huffpost, idadi ya watu wanaotembelea mitandao ya ponografia iliongezeka wakati nchi nyingi zilipotangaza watu kukaa nyumbani kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona.

Tabia hii imefanya watu wengi kuanza kujichua, kitendo kinachofanya mtu kukosa hamu ya kushiriki tendo la ndoa na mke au mpenzi wake au hata kukosa uwezo wa kufanya mapenzi kabisa.

Koli anasema athari za corona zimesababishia watu matatizo ya kiakili na kuwafanya kutopatia tendo la ndoa kipaumbele katika maisha yao.

“Watu wamesongwa na mawazo. Hawajui kesho itakuwaje. Mawazo waliyo nayo ni jinsi wanaweza kujikwamua kutoka hali ya sasa. Kwao, shughuli za chumbani zinaweza kusubiri,” asema.

Kwa wachumba wanaokaa pamoja, aeleza, hii haifai kuponza uhusiano wao kuliko waliofungiwa maeneo tofauti. Hofu ya wanasaikolojia ni kwamba huenda wanaojichua wakawa watumwa wa tabia hii na kupoteza kabisa uwezo wa kuburudisha wachumba wao.

“Hii ni kwa wanaume na wanawake. Cha muhimu ni kuepuka kutazama ponografia inayovuta watu kuanza tabia hii,” asema Koli.

CHOCHEO: Siache corona kupangua harusi

Na BENSON MATHEKA

DERRICK na Eva walikuwa wamekamilisha mipango yote ya harusi yao kabla ya janga la corona kuvamia ghafla.

Walikuwa wamealika watu 500 wakiwa ni jamaa na marafiki wa mbali na karibu. Aidha walipanga kusafiri hadi Mauritius kwa fungate kabla ya kurejea nchini kuendelea na maisha ya ndoa.

Hata hivyo, mipango yote ilisambaratishwa na janga hili na wakalazimika kufunga harusi bila mbwembwe walizotarajia.

“Hatukuweza kuahirisha harusi kwa sababu tungepata hasara zaidi, sio ya kiasi cha pesa tulichotumia kuipanga bali hasara ya hisia zetu. Tulikuwa tumepanga kuanzisha familia na kuahirisha harusi ingekuwa sawa na kuahirisha hatua muhimu katika maisha yetu. Tuliamua kula kiapo mbele ya padre, wasimamizi na wazazi wetu pekee na tumesonga mbele na maisha huku tukijilinda na corona,” asema Eva.

Mwanadada huyu asema kwamba alikuwa amechumbiana na Derrick kwa miaka minne na hakuna chochote kingemzuia kuwa mke wake tarehe waliokuwa wamepanga.

“Corona haingebadilisha mipango yetu baada ya kujuana kwa miaka minne. Tumetimiza ndoto yetu kwa sababu ya upendo wetu na kwa kuuheshimu kwa dhati. Ndoa ni ya wawili na wengine ni mashabiki tu. Kukosa kwa wageni na mabusu hadharani hakufai kuwa kisiki katika ndoa wakati huu wa janga la corona,” asema Eva.

Kulingana na Derrick, ilibidi wafutilie mbali safari yao kwenda fungate baada ya safari za ndege kusitishwa na hata anakiri kuwa walitafuta ushauri wa wataalamu baada ya marufuku hiyo ya serikali.

“Kusema kweli, binafsi niliathirika sana serikali ilipofunga makanisa lakini mchumba wangu alinishawishi tumuone mshauri nasaha. Tuliamua kuwa harusi itaendelea kwa kuzingatia kanuni za serikali,” anasema Derrick.

Kulingana na wataalamu, mbwembwe zinazoshuhudiwa wakati wa harusi sio sehemu ya ndoa mbali ni nakshi kama mapambo mengine.

“Sio vibaya harusi kuwa na mbwembwe kwa kuhudhuriwa na walioalikwa na wasioalikwa. Hata hivyo, ndoa halisi ni maharusi kulishana viapo, kuwepo kwa mashahidi wanaotia sahihi cheti cha ndoa na harusi kufuata utaratibu wa kisheria kikamilifu,” asema mshauri wa ndoa Jeniffer Karimi wa kituo cha Maisha Mema, jijini Nairobi.

Karimi asema kanuni za kuzuia kusambaa kwa corona hazifai kuzuia watu kufunga harusi.

“Inachukua muda, nguvu na rasilmali kupanga harusi na janga la corona halikutarajiwa. Kwa hivyo, wachumba wanafaa kuzungumza na wakielewana, wafunge harusi yao kwa kuzingatia kanuni zilizowekwa. Ndoa ni ya wawili, wanaohudhuria hawaishiriki,” asema na kuongeza kuwa hali ya sasa imepunguza gharama ya harusi.

“Huwa nawaliwaza wanaosononeka baada ya mipango yao ya harusi kuvurugwa na corona kwa kuwaambia ni afueni kwao nyakati hizi ngumu kiuchumi. Huwa nawakumbusha kuwa watu waliokuwa wamealika wangewaachia hasara tu,” asema Karimi.

Kulingana na Daniel Kisesi, mshauri wa wanandoa katika shirika la Grace for life, mjini Machakos, uamuzi wa kuahirisha harusi unafaa kuwa wa wachumba wote wawili.

“Corona imevuruga ndoto za watu wengi waliotamani kuwa na harusi ya kufana na fungate ya kukumbuka. Kanuni za kuzuia janga hili ziliwaacha na chaguo mbili, kuahirisha harusi au kuzifanya faraghani. Uamuzi wa kuahirisha harusi unahitaji kuafikiwa na wachumba wote wawili,” asema Bw Kisesi.

Anasema kwamba watu wanafaa kubadilika jinsi nyakati zinavyobadilika.

“Kuna uwezekano kwamba hali iliyosababishwa na corona itaathiri mitindo ya maisha kwa muda mrefu ikiwa ni pamoja na sherehe za harusi na kwa hivyo ushauri wangu kwa watu ni kukumbatia mabadiliko hayo na kula yamini badala ya kuahirisha awamu hii muhimu katika maisha yao,” asema.

CHOCHEO: Mvuto wa dume la pembeni

Na BENSON MATHEKA

NI miaka mitano sasa tangu *Hellen afunge pingu za maisha na Daniel.

Kabla ya harusi na miaka minne ya ndoa yao, hakudhani kama kuna wanaume wengine duniani hadi mwaka 2019 alipokutana na Steve, mfanyakazi mwenzake aliyeteka moyo wake na kumpagawisha kabisa kimahaba.

“Siwezi kuficha, ninampenda Steve. Ninavyohisi kumhusu imenifanya kujitambua na kuchanganyikiwa,” asema Hellen. Hata hivyo, anasema ingawa huwa wanachat kwenye mitandao ya kijamii na kuzungumza wakiwa kazini, hajawahi kumweleza anavyohisi kumhusu.

“Nimeolewa lakini nimelemewa na hisia kwa jamaa huyu. Sijui nitafanyaje kwa sababu nimefungwa na viapo vya ndoa kwamba nitakuwa mwaminifu kwa mume wangu hadi kifo kitapotutenganisha,” asema mwanadada huyu.

Lakini kwa Glady’s* ndoa haikuwa kizingiti alipokutana na John, barobaro kutoka Nigeria aliyedunga mkuki wa mapenzi katika moyo wake.

“Tulifanya mipango kwa siri na baada ya muda nilimuacha mume wangu na kuondoka na barafu ya moyo wangu hadi Afrika Kusini kwa miaka sita kisha nikarejea nchini kuwasilisha kesi ya talaka,” asema.

Wataalamu wa masuala ya mapenzi wanasema kuwa ni kawaida ya akina dada walio katika ndoa au katika uhusiano wa mapenzi kujipata katika crush, wakizuzuliwa kimapenzi na wanaume wengine.

“Huwa inatendeka. Ni kawaida ya mtu kujipata amevutiwa na mwanamume mwingine kando na mumewe. Wakati mwingine hisia za mapenzi kwa mgeni huyo huwa na nguvu na kufanya mtu kuvunja ndoa akidhani amepata mwanamume bora kuliko mumewe,” aeleza mwanasaikolojia Lucy Karimi wa kituo cha Love Care jijini Nairobi.

Kulingana na Karimi, hii imefanya idadi ya wanawake walio na mipango ya kando kuongezeka.

“Kuna wanaoamua potelea mbali na kujitosa katika mapenzi nje ya ndoa na wanaume wanaowazuzua. Ninataka kusema ni kuwazuzua tu kwa sababu kwa kawaida huwa hakuna cha mno isipokuwa kujivinjari na kulishana uroda. Ni uhusiano ambao huwa hauna mipango ya maana isipokuwa kuchangamshana tu,” asema na kuongeza:

“Ole wao wanaovunja ndoa zao kwa sababu ya kupagawishwa na wapenzi wa kando.”

Anasema siku hizi, imekuwa rahisi kwa watu kuendeleza mipango ya kando kwa sababu ya mitandao ya kijamii lakini athari zake zimekuwa zikifanya wengi kujuta.

“Ni vizuri kujaribu kujiepusha nayo kwa sababu japo inaweza kuwa siri kwa muda, athari zake ni mbaya kwa wahusika wote,” aeleza.

Wataalamu wanasema makosa wanayofanya watu wengi ni kuchukulia hisia za mapenzi wanazopata kuhusu watu wengine kwa uzito.

“Watu wengi siku hizi hawaamini kuwa kuvutiwa kimapenzi na watu wengine nje ya ndoa ni kukosa heshima. Wanaamini kuwa hawafai kunyima moyo wao unachotaka. Wanasahau kwa kufanya hivyo, huwa wanatengeneza njia ya kuelekea masononeko,” asema Purity Kembi, mwanasaikolojia katika kituo cha Beyond Love jijini Nairobi.

“Fikiria mara mbili na zaidi, crush haiwi mapenzi ya dhati wanavyoamini watu wengi na hapa nazungumzia wanawake. Hatima yake huwa ni kuvunjwa moyo na hii inaweza kutokea baada ya mtu kumuacha mume wake wa ndoa. Usiache mbachao kwa msala upitao,” asema.

Karimi anasema wanawake wanaoamini kwamba wanafaa kujiachilia kwa crush wao huwa wanakata tiketi ya masononeko.

Mtaalamu huyu anakiri kwamba ujio wa mitandao ya kijamii iliyorahisisha mawasiliano umefanya watu wengi kuvuka mipaka ya ndoa na kuwa na mahusiano ya mapenzi isiyo na faida zaidi ya kuchangamkiana kwa ufuska.

“Enzi ambazo macho ya mtu yalikuwa yakimuona mume au mkewe pekee zinaonekana kutoweka. Enzi hizo, viwango vya talaka na dhuluma katika ndoa vilikuwa vya chini,” asema na kuongeza kuwa viwango vya maisha ya kijamii hubadilika katika kila kizazi.

Mtaalamu huyo anaonya watu dhidi ya kuacha wachumba wao wa dhati ili kuandama penzi la pembeni.

CHOCHEO: Ukarimu wake ni chambo tu!

Na BENSON MATHEKA

KWA kipindi cha miezi tisa, Betty alimchukulia Dan kuwa rafiki yake wa dhati.

Dan alimsaidia kwa mambo mengi kikazi na alimheshimu sana.

Dan alifahamu mumewe na marafiki zake wengi. Mwanadada huyu alihisi salama akiwa na Dan na hakufikiria kwamba mtu aliyemheshimu alikuwa na nia fiche katika moyo wake hadi majuzi.

“Nilishtuka aliponiambia kwamba ananipenda na kuomba nimlishe tunda,” afichua Betty.

Dan alimweleza kwamba alikuwa akimfanyia wema wote kwa sababu alikuwa akimpenda.

“Aliniambia alishindwa kuvumilia na akaamua kufungua moyo wake kwangu. Nilikataa kumeza chambo na tangu siku hiyo amenichukia na hanisalimii kamwe,” aeleza Betty.

Wataalamu wanasema kwamba kuna wanawake wengi wanaojipata katika hali aliyojipata mwanadada huyu.

“Wanaume wengi huwa ni fisi wanaovalia ngozi ya kondoo. Wanakuwa wakarimu kwa wanawake, wanawasaidia wakijifanya marafiki wa kawaida ilhali ndani wanasitiri hisia za mapenzi huku wakisubiri wakati wa kuwapasulia yaliyo katika mioyo yao,” aeleza Sammy Kariuki, mtaalamu katika shirika la Love Care, jijini Nairobi.

Anasema wanaume kama hao huwa wanawatendea mema wanawake wanaowalenga ili kuutumia kama chambo cha kuwanasa. “Wanajifanya marafiki wa kawaida na baada ya wanawake hao kuwaaamini, wanawafungulia mioyo yao. Kuna wanawake wanaoangukia mitego ya wanaume hawa na kuna wanaokataa kama Betty na kulinda heshima yao,” aeleza Kariuki.

Wataalamu wanasema wanaume kama hao hutumia muda kuelewa udhaifu wa wanawake hao ikiwa ni pamoja na matatizo wanayopitia katika ndoa zao au uhusiano wao wa kimapenzi. “Baadhi ya wanawake huwafungulia wanaume milango ya kutaka kushiriki ufuska nao kwa kuwasimulia matatizo wanayopitia katika ndoa zao au kujadili mahusiano yao. Kufanya hivi kunafanya mwanamume kama huyo kuwa na hisia za kutaka kujaza pengo lililopo katika maisha ya mapenzi ya mwanamke husika,” aeleza Jane Wausi wa shirika la Big Hearts, jijini Nairobi.

Anashauri wanawake kutochukulia wanaume wanaowatendea mema kama malaika. “Wema wowote, ukarimu wowote anaokuonyesha au kukutendea mwanamume asiye mumeo au mpenzi wako kwa muda mrefu, huwa sio wa kawaida. Huwa kuna njama fiche na usipokuwa mwangalifu ni rahisi kujipata ukishiriki ufuska,” aeleza Wausi.

Anasema pia kuna wanawake wanaotumia mbinu hii kuwanasa wanaume.

“Pia kuna wanawake wanaojifanya marafiki na wanaume wakiwa na nia ya kuwanasa kimapenzi. Wakikosa kufanikiwa, wanawachukia wanaume hao,” aeleza.

Kariuki anasema ni kawaida ya watu wanaohusiana kwa muda mrefu wakiwa marafiki kuanza kumezeana mate hasa ikiwa hakuna siri kati yao.

“Huwa inaanza watu wanaposimuliana wanayopitia katika maisha yao ya mapenzi. Kwa mfano mwanamke akimweleza rafiki yake mwanamume kuhusu mapungufu ya mumewe katika tendo la ndoa au mwanamume akimweleza mwanamke kuhusu tabia za mkewe,” asema.

Kulingana na Mhubiri Joseph Mugambi wa kanisa la Hope in Christ, jijini Nairobi, urafiki kati ya wanaume na wanawake walio katika ndoa unafaa kuwa na mipaka.

“Ni rahisi mtu kumtumbukiza rafiki katika majaribu akimsimulia kuhusu matatizo ya ndoa au mahusiano ya mapenzi. Hii ndiyo sababu unapata watu wakizini na wake au waume wa marafiki zao,” aeleza.

Anashauri watu kutafuta huduma za washauri waliohitimu wanapopata matatizo katika ndoa zao.

Wausi anakubaliana na Mhubiri Mugambi kuwa kuna haja ya watu kuweka mipaka wanapopiga gumzo na marafiki.

“Unafaa kupima kwa uangalifu kila tendo la wema unalofanyiwa na rafiki mwanamume au mwanamke ili asiwe analenga kukutumbukiza katika ufuska,” ashauri.

CHOCHEO: Usiende deti ukiwa mlevi, pombe ni adui wa penzi la dhati

Na BENSON MATHEKA

SALLY alipompigia simu James kuthibitisha deti yao ya kwanza, barobaro huyo hakuamini ilikuwa kweli.

Alikuwa amemrushia kipusa huyo mistari kwa miaka mingi lakini alichogundua siku hiyo ni kwamba hakuwa na ujasiri wa kumfungulia moyo wake kumweleza alivyompenda.

James alipitia katika baa iliyokuwa karibu na kubugia chupa kadhaa za bia ili kupata ujasiri wa kumwaga moyo wake kwa Sally.

“Ninajutia kitendo hicho. Japo Sally alivumilia kwa masaa manne akinisikiliza, ujumbe alionitumia baada ya deti yetu ulikuwa wa kutamausha. Alinikataa kwa sababu ya ulevi wangu ilhali ilikuwa mara yangu ya kwanza kunywa pombe na nilifanya hivyo kupata ujasiri wa kumuingiza boksi,” asema James.

Wataalamu wa masuala ya mapenzi wanasema ni makosa kwa mtu anayetafuta mpenzi wa kudumu kulewa wakati wa deti ya kwanza.

“Ikiwa unakutana na mtu unayetaka awe mchumba wako, basi epuka pombe siku ya kwanza. Kufika katika miadi ukiwa mlevi kunaonyesha kuwa haujiamini. Vipusa hutaka wanaume wanaojiamini na sio wanaotumia vileo kupata ujasiri wa kuwatongoza,” aeleza Bi Benta Asiyo, mwanasaikolojia katika kituo cha Afya Love jijini Nairobi.

Anasema wanawake waadilifu wanaotafuta mapenzi ya dhati huamini kuwa mtu akiwarushia chambo akiwa mlevi huwa anaficha tabia zake halisi.

“Kwa kawaida watu wanapolewa, huwa hawamaanishi wanachosema na hata kujielewa vizuri. Hivyo basi, mwanamke anayetafuta mpenzi wa dhati huchukulia maneno ya mwanamume mlevi kama mzaha tu,” aeleza Bi Asiyo.

Mtaalamu huyu anaongeza kuwa mtu anayekutana na mpenzi kwa mara ya kwanza akiwa mlevi anaweza kukosea heshima iwe kwa tabia au matamshi.

“Akina dada wengi huwa wanatafuta kitu spesheli kwa mtu kabla ya kukubali kuanza uhusiano wa kimapenzi. Tafiti zimeonyesha kuwa hakuna kitu spesheli kwa mtu mlevi kwa sababu tabia ya walevi wote ni sawa,” aeleza.

Kevin Nahai, mwanasaikolojia katika shirika Soul Mate anasema mtu akiwa mlevi hawezi kufanya maamuzi mema, hajitambui na hawezi hata kumfahamu vyema anayenuia kuwa mpenzi wake.

“Kukosa kulewa siku ya kwanza ya kujivinjari na mpenzi wako, kunakupatia fursa ya kumdadisi vyema na kuelewa tabia zake na kukuelewa pia,” aeleza Nahai.

Anasema kuepuka pombe katika mkutano wa kwanza na mtu unayemrushia chambo kunasaidia kung’amua iwapo uhusiano wako naye unaweza kunawiri.

“Mtu anapolewa akiwa na mtu anayemmezea mtu, anaweza kujidaganya kuna mapenzi kati yao hadi pale pombe inapomtoka anapogundua alijikosea mwenyewe,” aeleza.

Majuto

Kulingana na Bi Asiyo, watu wengi huwa wanajuta kwa maamuzi wanayofanya kwa sababu ya kulewa wanapokutana kujivinjari siku ya kwanza.

“Kuna wale wanaojipata wamelishana uroda na kujutia kitendo hicho hasa wote wakilewa. Mtu mlevi hawezi kufanya maamuzi ya busara. Usishawishiwe kulewa na mtu mnayekutana mara ya kwanza kwenye deti, utajuta,” asema.

Wataalamu wanashauri vipusa kuwaepuka wanaume wanaowaalika kujivinjari kwenye baa wakisema kuna hatari baada kulewa.

“Kuna maeneo mengi ya kuvutia mnayoweza kukutana kuzungumzia mambo yenu. Jiulize, kwa nini anataka tukutane eneo la burudani mara ya kwanza iwapo anataka kweli niwe mchumba wake wa dhati,” aeleza Nahai.

“Ukiona mwanamume anayekurushia mistari akikualika kilabuni kwa mkutano wenu wa kwanza, huyo hataki mpenzi wa dhati mbali ni kupitisha wakati tu. Mapenzi ya dhati hayapaliliwi katika ulevi,” asema.

Badala ya kubugia pombe kupata ujasiri wa kufungulia kipusa moyo wako, wataalamu wanashauri wanaume kujipeleleza kwanza.

“Uhusiano wa kwanza wa kimapenzi huwa unaanza na mtu binafsi. Tafuta njia za kujipenda kwanza na ulimwengu utakupenda na bila shaka sio kwa sababu ya ulevi. Ulevi unafanya mbegu za mapenzi kukosa kuota na zikiota hazinawiri na zikinawiri, hukauka kabla ya kukomaa,” asema Nahai.

CHOCHEO: Kukataliwa ni kawaida, jinyanyue na maisha yasonge

Na BENSON MATHEKA

DAVY, barobaro mwenye umri wa miaka 25 alipoanza kumrushia chambo Agie, 23, alikuwa na matumaini makubwa kuwa atakubali kuwa mpenzi wake.

Walikuwa wamejuana kwa miaka mingi, walikuwa wamefanya mengi pamoja na alikuwa ameridhika kuwa mwanadada huyo alikuwa mwenye nidhamu ya hali ya juu na mwaminifu.

Hata hivyo, jibu alilolipata kutoka wa Agie lilimvunja moyo akahisi kuwa hakufaa kuendelea kuishi ulimwenguni.

“Aliniambia hawezi kukubali kuwa mpenzi wangu. Kwamba alikuwa na mwanamume bora kuniliko. Kilichoniudhi ni jinsi alivyonijibu kwa dharau. Nilijiona kama mtu asiye na maana katika ulimwengu huu, asiyeweza kupendwa,” alisema Davy.

Kama haingekuwa rafiki yake aliyemshauri atafute ushauri nasaha, Davy angechukua hatua ambazo zingemfanya ajute.

“Kukataliwa na mchumba au mtu uliyeweka matumaini atakupenda sio rahisi, kuna uchungu na kunaweza kufanya mtu kujitumbukiza katika matatizo makuu,” asema mwanasaikolojia Beth Wandei wa shirika la Big Hearts jinini Nairobi.

Anasema watu wanafaa kufahamu kuwa kila mtu anaweza kukataliwa maishani hata na watu waliowekeza rasilmali, nguvu na wakati ili kuwasaidia wakidhani wanawapenda.

Wataalamu wanasema ni kawaida mtu kukasirika, kutamauka na kusononeka akikataliwa au kutemwa na mpenzi au mtu aliyekuwa akimezea mate.

“Ni tukio linaloweza kusababishia mtu matatizo ya kiafya kama kuumwa na kichwa, maumivu ya tumbo, mfadhaiko na shinikizo la damu na kumfanya apate matibabu,” asema Bi Wandei.

Hata hivyo, anasema ingawa ni kawaida mtu kujipata katika hali hii haifai kumlemaza kimaisha.

“Hakuna anayeweza kusema kuwa ana nguvu kiasi cha kutohisi athari za kukataliwa na mtu aliyewekea matumaini kuwa mchumba wake maishani. Unaweza kulia, kukasirika na hata kufadhaika ukajipata katika hospitali. Kilicho kibaya na hatari ni kuchukua sheria mikononi mwako kwa sababu unaweza kujuta zaidi,” aeleza.

Wataalamu wanasema hali inaweza kuwa mbaya kwa mtu anayekataliwa mara ya kwanza.

“Kwa watu kama hao ni kawaida kulia. Tunawashauri wakihisi kulia wasijizuie, wajifungie mahali salama walie ili wapunguze machungu moyoni,” aeleza.

Kulingana na Dkt Seth Aboo wa shirika la Light Care mjini Athi River, Machakos, baada ya mtu kupunguza hasira kwa kulia hafai kunyamaza.

“Zungumza na mtu unayemwamini umweleze kuhusu masaibu yako. Anaweza kuwa rafiki, kiongozi wa kidini au mtu aliyepitia hali sawa. Sikiliza wanayokueleza na unaweza kugundua kuwa wewe sio wa kwanza kukataliwa duniani. Watu wametendwa, wakazama, wakaibuka na kunawiri zaidi katika mapenzi,” aeleza Aboo.

Kufanya uchambuzi

Mtaalamu huyu ansema baada ya mtu kutulia anafaa kuchambua yaliyotendeka na manufaa yake kwa kukataliwa au kutemwa.

“Kukasirika kwa sababu umekataliwa ni sawa na kunywa sumu na kutarajia mtu mwingine afe. Unavyoendelea kusononeka, aliyekutema anaendelea na maisha yake kama kawaida,” asema Aboo.

Bi Wandei anasema watu wengi huwa wanakosea kwa kutaka kulipiza kisasi kwa kuzua ghasia.

“Mtu akikukataa, ana haki ya kufanya hivyo. Kamwe usiwahi kulipiza kisasi kwake na usipeleke hasira zako kwa watu wengine kwa kuwa mkali au kuzua vurugu. Ukifanya hivi, watu watakuepuka na ukataliwe zaidi,” asema.

Wataalamu wanashauri watu kuepuka hulka mbaya kama vile kulewa kupindukia, kuvuta sigara, kutumia dawa za kulevya au kujiingiza katika vitendo vya ufuska baada ya kukataliwa au kupigwa teke na wachumba wao.

“Hulka kama hizi ni hatari, zitakuongezea shida na kukuacha katika hali mbaya zaidi,” aeleza Aboo.

Kulingana na Davy, baada ya kupata ushauri nasaha, alisahau masuala ya mapenzi kwa muda, akajiunga na kilabu ya muziki kanisani kisha akajiunga na chuo kimoja jijini kwa masomo ya muda.

“Baada ya mwaka mmoja, hali yangu ilibadilika na kuwa bora zaidi. Niliwapata marafiki wapya na nikajifunza kuwa mwangalifu katika masuala ya mapenzi. Siko tayari kujipata katika hali aliyonisababishia Agie kwa kunikataa,” aeleza.