Fiji wahifadhi nishani ya dhahabu kwenye raga ya Olimpiki

Na MASHIRIKA

FIJI walipokeza New Zealand kichapo cha 27-12 na kutwaa dhahabu ya pili ya Olimpiki katika historia ya taifa hilo.

Fiji ilijishindia dhahabu ya kwanza kwenye Olimpiki miaka mitano iliyopita baada ya raga kujumuishwa kwenye michezo ya Olimpiki kwa mara ya kwanza. Fiji inajivunia idadi ya watu wasiozidi milioni moja pamoja huku ikikabiliwa pia na changamoto za uchache wa rasilimali.

Semi Radradra wa klabu ya Bristol ni miongoni mwa wanaraga wa Fiji wanaodumishwa kwa mshahara wa juu zaidi katika ulingo wa raga.

Chini ya kocha Gareth Baber ambaye ni raia wa Wales, Fiji watakosa makaribisho sawa na yale ambayo kikosi kilichozoa dhahabu ya Olimpiki miaka mitano iliyopita nchini Brazil kilipokezwa.

Kufikia Machi 2021, Fiji haikuwa imetikiswa hata kidogo na janga la corona huku vifo viwili pekee vikiripotiwa. Hata hivyo, idadi ya vifo iliongezeka na kufikia 200 tangu wakati huo huku kukiwa na hofu kwamba huenda sekta ya afya ikalemewa.

Uingereza waliokuwa wakipigiwa upatu wa kuzoa dhahabu waliambulia pakavu baada ya kupigwa 17-12 na Argentina katika mchuano wa kuwania nishani ya shaba.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

Corona hatari sana yaja hata kwa waliopata chanjo – WHO

Na MASHIRIKA

GENEVA, Uswisi

MKURUGENZI wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Tedros Adhanom Ghebreyesus, ameonya kwamba ulimwengu uko katika “kipindi hatari” cha janga la COVID-19.

Hii ni kutokana na virusi sugu aina ya Delta vinavyozidi kubadilika na kufanya mambo kuwa mabaya zaidi.

“Mataifa maskini yenye kiwango cha chini cha usambazaji wa chanjo, ambayo yanashuhudia matukio ya kushtusha ya hospitali kufurika wagonjwa, yamekuwa yakiendesha mambo kwa njia za kawaida.

Huku hali ikihatarishwa zaidi na aina ya virusi vinavyosambazwa upesi kama vile Delta ambavyo vinazidi kusambaa pakubwa katika mataifa mengi, tuko katika kipindi hatari cha janga hili.

“Bado hakuna taifa lililo salama. Virusi aina ya Delta ni hatari na vinaendelea kubadilika, jambo linalohitaji kutathmini na kubadilisha kwa makini mikakati ya afya ya umma,” alisema Ghebreyesus, kupitia taarifa Ijumaa.

Akifafanua kuwa virusi aina ya Delta vimegunduliwa katika mataifa 98 na kwamba vinasambaa kwa kasi katika nchi zenye kiwango cha chini na cha juu cha usambazaji chanjo, alisema kuna njia mbili muhimu kwa mataifa kuepuka mikurupuko mipya.

“Afya ya umma na mikakati ya kijamii kama vile mikakati thabiti ya kuchunguza, kupima na kugundua visa mapema, kutenga na kutoa huduma muhimu,” alisema.

Alifafanua kuwa kuvaa maski, kudumisha umbali wa kutangamana kijamii, kuepuka sehemu zenye misongamano ya watu na kuwa na sehemu za kuruhusu hewa ndio msingi wa hatua zote za kudhibiti gonjwa hilo.

Ghebreyesus alisisitiza kwamba ulimwengu ni sharti ugawane vifaa vya kujikinga, hewa ya oksijeni, vipimo, tiba na chanjo. Aliwahimiza viongozi kote duniani kushirikiana ili kuhakikisha kwamba kufikia wakati huu mwaka ujao, asilimia 70 ya watu katika kila nchi watakuwa wamepewa chanjo.

“Hii ndiyo njia bora zaidi ya kupunguza janga, kuokoa maisha, kuendesha mikakati ya kufufua uchumi kote duniani na wakati huohuo kuzuia kuzuka kwa aina nyingine hatari zaidi za virusi.

Kufikia mwisho wa Septemba hii, tunatoa wito kwa viongozi kutoa chanjo kwa asilimia 10 ya watu katika mataifa yote,” alisema.

Huku viwanda vipya vikiwemo vinavyounda chanjo za zmRNA, vikizidi kuanzishwa, bosi huyo wa WHO alisema mikakati hiyo inaweza ikaharakishwa kupitia usambazaji wazi wa teknolojia na maarifa baina ya kampuni.

“Ninahimiza hasa kampuni hizo – BioNTech, Pfizer na Moderna – kusambaza ujuzi wao ili tuharakishe uundaji wa chanjo mpya,” alisema.

Shujaa yalemewa na Fiji kwenye fainali

Na CHRIS ADUNGO

TIMU ya Kenya ya raga ya wachezaji saba kila upande, Shujaa, Jumapili ilipata kadi mbili za manjano katika kipindi cha kwanza na kuzima matumaini ya kutwaa ubingwa wa Hong Kong Sevens, baada ya fiji kuipiga 24-12 na kuetetea ubingwa wa kombe hilo.

Collins Injera na William Ambaka, ambao walikuwa mashujaa katika ushindi wa 21-12 dhidi ya New Zealand kwenye nusu fainali, walilishwa kadi ya manjano.

Fiji ilitumia wingi wao uwanjani kufunga trai mbili kupitia kwa Eroni Sau na Amenoni na kuongezea kwa trai ya ufunguzi ya Josua Vakurunabili.

Fiji iliongoza 17-0 katika kipindi cha mapumziko katikafainali hiyo iliyokuwa marudio ya fainali ya Canada Sevens ambapo Fiji pia ilishinda 29-7.

Kenya ilijaribu kuwafuata Fiji kupitia mchezo wa kuridhisha uliomwezesha Billy Odhiambo kufunga, lakini trai ya Valemo Ravouvou ilipoteea Kenya imani.

Nahodha Oscar Ouma alijaribu kuonyesha uwezo wa Kenya kwa trai yake kupitia penalti, lakini maji yalikuwa yashamwagika kwa Shujaa.

Shujaa kumenyana na Fiji na Ufaransa tena

Na GEOFFREY ANENE

MAKUNDI ya Raga za Dunia ya duru ya Vancouver Sevens yametangazwa, ambapo Kenya itafufua uhasama dhidi ya Fiji na Ufaransa tena.

Shujaa imetiwa katika Kundi C pamoja na Fiji na Ufaransa, ambazo ilikutana nazo katika duru iliyokamilika mjini Las Vegas nchini Marekani, Jumapili.

Ilishangaza Fiji 17-14 na kulimwa 19-14 na Ufaransa mjini Las Vegas. Mbali na Fiji na Ufaransa, Kenya pia itakabiliana na Uhispania katika mechi za makundi za duru hiyo ya sita.

Vijana wa kocha Innocent Simiyu, ambao walimaliza Las Vegas Sevens katika nafasi ya saba kwa alama 10, walimenyana na Uhispania mara ya mwisho msimu 2013-2014. Shujaa ilishinda Uhispania 12-7 katika nusu-fainali ya Ngao ya duru ya Hong Kong Sevens mnamo Machi 30, 2014.

Uhispania ilitemewa mwisho wa msimu huo baada ya kumaliza katika nafasi ya mwisho. Imerejea kwenye ligi hii ya mataifa 15 msimu huu wa 2017-2018. Mara ya mwisho Kenya ilikutana na Uhispania katika ziara ya Amerika Kaskazini ilikuwa Januari 25 ambapo Shujaa iliwika 24-0 katika robo-fainali ya Bakuli.

 

MAKUNDI

A – Marekani, Australia, Canada na Uruguay;

B – Argentina, Uingereza, Wales na Samoa;

C – Fiji, Kenya, Ufaransa na Uhispania;

D – Afrika Kusini, New Zealand, Scotland na Urusi.