LEONARD ONYANGO: Handisheki itakufa baada ya refarenda

Na LEONARD ONYANGO

MVUTANO uliopo baina ya chama cha ODM na baadhi ya maafisa serikalini kuhusu Mswada wa Mpango wa Maridhiano (BBI), ni ithibati kwamba mpango huo ulikuwa na njama fiche ambayo si kuunganisha Wakenya jinsi tumekuwa tukiambiwa.

Viongozi wa ODM, wakiongozwa na Seneta wa Siaya James Orengo na wabunge Otiende Amollo (Rarieda) na Junet Mohamed (Suna Mashariki), hivi karibuni walitishia kususia BBI.

Walidai kuwa Mswada huo ‘umenyakuliwa’ na baadhi ya watumishi serikalini na wanalenga kuutumia kutafuta mrithi wa Rais Uhuru Kenyatta baada ya 2022.Baadaye walitueleza kwamba Rais Kenyatta na kinara wa ODM, Raila Odinga, walifanikiwa kutatua utata uliokuwepo.Ni miaka mitatu sasa tangu kuanza kwa mchakato wa BBI.

Rais Kenyatta na Bw Odinga wamekuwa wakituambia kwamba malengo yao kuwa na mwafaka wa maridhiano, almaarufu handisheki, ni kuunganisha Wakenya na kumaliza vurugu ambazo zimekuwa zikishuhudiwa nchini kila baada ya uchaguzi.Lakini matukio ya hivi karibuni yameweka wazi kwamba mpango wa BBI unalenga siasa za urithi za 2022.

Jambo la wazi kabisa ambalo limejitokeza ni kwamba Rais Kenyatta na Bw Odinga wanalenga mambo tofauti, licha yao kuonekana kusukuma BBI kwa pamoja.Kuna uwezekano kwamba ukuruba baina ya Rais na kinara huyo wa ODM utaisha baada ya Wakenya kupitisha BBI.

Vile vile, kuna uwezekano kwamba baada ya kura ya maamuzi ya kurekebisha Katiba kukamilika, Rais Kenyatta ataweka wazi jina la mtu atakayemuunga mkono kumrithi katika Uchaguzi Mkuu 2022.

Seneta wa Baringo Gideon Moi, kiongozi wa chama cha Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi na kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka watakuwa kwenye kikosi hicho.Inaonekana mswada wa BBI umebuni nyadhifa za kuhakikisha kuwa kila mmoja wa vigogo hao katika orodha ya urithi, atajipatia kiti.

Kwa upande mwingine, kuna hatari ya Bw Odinga kuachwa mpweke. Inaonekana kinara huyo alitarajia kwamba Rais Kenyatta angemuidhinisha kuwa rais katika uchaguzi ujao, lakini mambo huenda yakamwendea upogo.

Hata hivyo, karata ya Rais yaweza kutibuka iwapo Bw Odinga ataamua kuungana na Naibu Rais William Ruto. Hapo basi mwaniaji atakayeungwa mkono na Rais Kenyatta atakuwa na kibarua kigumu kupambana na kikosi ngangari kitakachojumuisha Dkt Ruto na Bw Odinga.

ODM yadai viongozi 4 wamedandia handisheki kujifaidi

Na BENSON MATHEKA

CHAMA cha ODM kinalaumu viongozi wa vyama vinne vya kisiasa wanaounga mageuzi ya katiba kwa kudandia handisheki ya kiongozi wa chama chao Raila Odinga na Rais Uhuru Kenyatta kwa lengo la kujifaidi.

Katibu Mkuu wa chama hicho, Bw Edwin Sifuna, amesema kwamba baadhi ya viongozi wa vyama vya kisiasa wamekuwa wakitembelea Ikulu kujadili mswada wa marekebisho ya katiba wa BBI ambao ni matunda ya handisheki kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga.

Bila kutaja majina, Bw Sifuna alisema kuwa ni wanasiasa hao ambao wanapendelewa na baadhi ya maafisa wakuu serikalini ili kumrithi Rais Uhuru Kenyatta na kumzuia Bw Odinga kuingia ikulu.

Ingawa alisema viongozi hao walifanya vyema kuunga mkono BBI, alidai kwamba hawakuwa sehemu ya handisheki kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga.

“Ukweli wa mambo ni kuwa hawana lolote walilochangia katika matunda ya BBI. Hawana maoni yao. Sasa cha kushangaza ni kwamba wanataka kuonekana eti wao ndio wa kuendesha mpango huo wote, ndio unawakuta Ikulu wakinywa chai na mandazi pale wakiambia watu kwamba wao ndio wenye BBI. BBI gani? Wanajua nini kuhusu BBI?” alihoji Bw Sifuna.

Akizungumza katika redio Citizen Alhamisi asubuhi, Bw Sifuna alisema kwamba katika mswada huo, wanasiasa hao hawakuchangia lolote.

“Nini wanaweza kusema ni maoni yao ambayo walitoa? Tunawaambia watulie waache watu wenye maono. Waachie na kuheshimu wale waliowakaribisha kutembea nao katika safari hii,” Bw Sifuna alisema.

Baada ya mswada wa BBI kupitishwa na mabunge 43 ya kaunti, Rais Kenyatta alimwalika Bw Odinga na viongozi wa vyama sita vya kisiasa wanaounga mchakato huo katika Ikulu ya Nairobi kupanga mikakati ya kufanikisha kura ya maamuzi.

Waliohudhuria kikao hicho ni Bw Musalia Mudavadi wa Amani National Congress (ANC), Bw Kalonzo Musyoka wa Wiper, Bw Gideon Moi wa Kanu, Bi Charity Ngilu wa Narc na Bw Moses Wetangula wa Ford Kenya.

Katika taarifa iliyosomwa na Bw Moi, viongozi hao walipongeza mabunge ya kaunti kwa kupitisha mswada huo na kuahidi kukutana Machi 9 na viongozi wengine kupanga mikakati ya kufanikisha kura ya maamuzi.

Chama cha ODM hakikufurahishwa na hatua ya Rais Uhuru Kenyatta ya kuwaalika viongozi wa vyama hivyo kikidai baadhi yao wamekuwa wakimkosoa Bw Odinga.

Washirika wa Bw Odinga hawakufurahishwa na kuungana na ANC, Kanu, Wiper na Ford Kenya katika chaguzi ndogo za maeneobunge ya Matungu Kaunti ya Kakamega, Kabuchai kaunti ya Bungoma na useneta kaunti ya Machakos.

Mabw Mudavadi, Musyoka, Moi na Wetangula wameashiria kwamba wataungana kushindana na Bw Odinga na Naibu Rais William Ruto kwenye uchaguzi mkuu ujao.

ODM kinadai kwamba baadhi ya maafisa wakuu wa serikali wanawaunga wanne hao katika juhudi za kumzuia Bw Odinga kuingia ikulu baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.

Jana, Bw Sifuna alidai kwamba maafisa hao walimsaidia mgombeaji wa chama cha ANC, Bw Peter Nabulindo kumshinda Bw David Were wa ODM kwenye uchaguzi mkuu wa Matungu ili kumkweza Bw Mudavadi.

Ndoa ya BBI yaingia doa

Na WAANDISHI WETU

MVUTANO kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa ODM Raila Odinga ulizidi kuchacha Jumatatu, hali iliyolazimisha kuahirishwa kwa sherehe za leo Jumanne za kuadhimisha miaka mitatu ya handisheki.

Pia mkutano wa ushauriano uliopangwa kufanyika leo Jumanne wa viongozi wakuu wa BBI, magavana na wabunge uliahirishwa baada ya joto kati ya wahusika hao kupanda baada ya chama cha ODM kulalamika kuwa kinahujumiwa.

Hii imesababishwa na mvutano kati ya viongozi wakuu wanaounga mkono mchakato wa BBI kuhusu ni nani kati yao anayefaa kumrithi Rais Uhuru Kenyatta wakati atakapoenda nyumbani mwaka ujao.

Kundi hilo la wakuu wa BBI linaongozwa na Rais Kenyatta na linajumuisha Bw Odinga, Kalonzo Musyoka, Musalia Mudavadi, Moses Wetangula, Gideon Moi na Charity Ngilu.

Lakini sasa muungano huo unayumbayumba siku chache tu baada ya kubuniwa, hali inayotishia mchakato wa BBI, huku ODM kikidai hila ya maafisa wakuu serikalini kuhujumu Bw Odinga kwa ajili ya kumwangusha 2022.

Jumatatu, rafiki wa karibu wa Bw Odinga, Bw Junet Mohamed ambaye pia ni mwenyekiti-mwenza wa makao makuu ya BBI, alidai kuwa kuna njama kubwa zaidi ya kuvuruga ODM na kukiacha vigae ifikapo mwaka 2022.

Bw Mohamed alisema iwapo njama hiyo haitakomeshwa watachukua hatua kuhusu handisheki na BBI.

“Tunajua kuhusu mpango mkubwa wa kudunisha ODM mashinani kwa visingizio vya ushirikiano wa handisheki na BBI. Wabunge na magavana katika ngome zetu za Pwani, Magharibi na Nyanza wanahangaishwa na maafisa wakuu serikalini lakini hatutakubali haya,” akasema Bw Mohamed.

Kulingana na Bw Mohamed, lengo la kutikisa ODM ni kuhakikisha hakitakuwa na nguvu ifikapo uchaguzi wa 2022.

Mnamo Jumamosi, Seneta James Orengo wa Siaya alitisha kuwa ODM kitajiondoa kutoka handisheki na BBI iwapo baadhi ya maafisa wakuu serikali wataendelea kukihujumu.

Matamshi yake ambayo yalionekana kumlenga Katibu wa Wizara ya Usalama, Dkt Karanja Kibicho, yameibua cheche za majibizano ambayo sasa yanatishia kuporomosha maazimio ya Rais Kenyatta na Bw Odinga kuleta upatanisho wa viongozi wa kisiasa kupitia kwa BBI.

Katika hatua ambayo inaharibu zaidi muungano wa BBI na handisheki, chama cha ANC jana kilishambulia ODM kikisema malalamiko yake yamesababishwa na uchoyo wa viongozi wa chama hicho, ambao wanataka kusimamia raslimali zote za kuhamasisha umma kuhusu BBI.

Msemaji wa Bw Mudavadi, Kibisu Kabatesi alidai ODM kinataka kumiliki mpango mzima wa BBI bila kuhusisha vyama vingine vya kisiasa.

“Kile ambacho ANC kinaweza kufanya ni kuonya vyama vingine visilazimishwe katika uhusiano unaoendeshwa kwa msingi wa vitisho na siasa za kushikana mateka,” akasema Bw Kabatesi.

Kwa upande mwingine, viongozi wa Wiper walimwambia Bw Odinga avunje handisheki na Rais Kenyatta ikiwa haridhiki.

Viongozi hao walisema Bw Musyoka ana uwezo wa kuchukua nafasi ya Bw Odinga katika handisheki bila tatizo.

“Nikikualika nyumbani kwangu hufai kuja kuanza kuniagiza jinsi ninavyofaa kupika chakula changu. Hilo haliwezekani. Kama ODM haijaridhishwa, acha waondoke,” Seneta wa Kitui, Enock Wambua akasema.

Jumatatu, Bw Kabatesi alisema kulingana na ufahamu wao, mkutano uliopangwa kufanyika leo Jumanne kuhusu BBI ungalipo licha ya malalamishi yaliyotolewa na ODM kuhusu usimamizi wa BBI na urithi wa Rais Kenyatta.

Mnamo Jumapili, Bw Odinga alikosa kuhudhuria mkutano wa hadhara katika uwanja wa Kamukunji, eneobunge la Kibra, hatua ambayo wadadisi wa kisiasa walihusisha na uadui ambao umeibuka kuhusu usimamizi wa BBI.

Ripoti ya Charles Wasonga, Justus Ochieng na Valentine Obara

Raila asema Ruto aliarifiwa kuhusu handisheki na Rais

Na SAMMY WAWERU

Naibu wa Rais Bw William Ruto alifahamishwa kuhusu salamu za maridhiano (Handisheki) kati yangu na Rais Uhuru Kenyatta, amesisitiza kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Bw Odinga amesema baada ya mashauriano kati yake na Rais Kenyatta kuzika tofauti zao za kisiasa, kufuatia mgawanyiko ulioshuhudiwa katika uchaguzi mkuu wa 2013 na 2017, Rais alimuarifu naibu wake kuhusu mipango itakayojiri.

“Alipigia makamu wake simu nikiwa, akamwambia ‘ukiona mimi na Raila tunatoa taarifa usiwe na wasiwasi, nitakueleza mengi baadaye’…” akadokeza.

Kiongozi huyo wa upinzani pia amesema aliarifu mgombea mwenza, Bw Kalonzo Musyoka (Wiper) kuhusu matazamio ya salamu za maridhiano.

Rais Kenyatta na Bw Odinga walihutubia taifa mnamo Machi 9, 2018, wakiahidi kuzika tofauti zao za kisiasa ambapo pia walizindua Ripoti ya Mpango wa Maridhiano, BBI.

Akionekana kumsuta Naibu wa Rais William Ruto kufuatia madai yake kuwa hakuhusishwa katika hatua hiyo, Raila alisema Dkt Ruto pia alishirikishwa kuteua wanachama wa jopokazi la BBI lililobuniwa kukusanya maoni ya umma, katika mchakato mzima kuunganisha taifa.

Aidha, jopokazi hilo lina wanachama 14. “Kati ya wanachama hao, Rais aliwakilishwa na wataalamu saba, nami pia saba. Kati ya saba wa Rais, watatu walipendekezwa na Ruto,” Bw Odinga akafafanua.

Jopokazi hilo lilijukumika kukusanya maoni mseto ya Wakenya, kilele kikiwa mapendekezo ya Katiba kufanyiwa marekebisho kupitia BBI.

“Si haki kusema makamu wa rais alikuwa kwa giza, alikuwa ndani na hakushurutishwa na yeyote. Alielezwa atoe maoni yake kuhusu BBI ila hakutoa, watu wake ndio walitoa. Walikuwa wakimshauri na kumweleza yaliyojiri,” akaelezea.

Bw Odinga ametetea jopokazi la BBI, akihoji lilikuwa huru katika ukusanyaji wa maoni na uandaaji wa Ripoti ya Maridhiano.

Aidha, Dkt Ruto amenukuliwa hadharani akikosoa uhalisia wa BBI na Handisheki. Wandani wake wanadai salamu za maridhiano zililenga kuzima ndoto zake kuingia Ikulu 2022.

ODM wajuta kuingia katika handisheki bila utaratibu

LEONARD ONYANGO na VALENTINE OBARA

CHAMA cha ODM kimeonekana kujutia mkataba wa maelewano kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa chama hicho, Raila Odinga.Hii ni kufuatia mzozano wa kisheria ambao unatishia kunyima chama hicho nafasi ya unaibu gavana katika Kaunti ya Nairobi.

Baada ya madiwani wa ODM kuongoza wenzao katika kumng’oa mamlakani aliyekuwa gavana Mike Sonko, chama hicho kilitarajia kupewa nafasi ya naibu wa gavana.

Hata hivyo, wataalamu wa kisheria na duru katika Chama cha Jubilee wanasema huenda ODM isipate nafasi hiyo kwa vile hakuna mkataba rasmi wa ushirikiano kati ya vyama hivyo viwili.

Makubaliano ya handsheki yalihusu tu masuala ya kitaifa yanayofaa kurekebishwa, ilhali mikataba ya ushirikiano wa kisiasa huhitajika kuwasilishwa kwa afisi ya msajili wa vyama.Ijapokuwa Bw Odinga husisitiza kuwa ushirikiano wake na Rais hautatikisika, jana ishara zilionyesha hali si shwari.

Kamati Kuu ya kitaifa ya chama hicho ilikutana Nairobi na katika kikao cha wanahabari, Katibu Mkuu Edwin Sifuna akatangaza kuwa kuendelea mbele chama hicho kitajihadhari kuhusu makubaliano yake na vyama vingine.

‘Ili kulinda na kujenga maslahi ya chama kote nchini, kuanzia sasa kamati hii itasisitiza kuwe na makubaliano rasmi na vyama vingine kuhusu masuala ya aina yoyote,’ akasema Bw Sifuna.

Alisema ODM itasisitiza kuteua mwanachama awe naibu gavana, punde baada ya mahakama kuruhusu mchakato wa kumwapisha gavana mtarajiwa Anne Kananu kuendelea mbele.Katika siku za hivi majuzi, baadhi ya viongozi akiwemo Seneta wa Siaya James Orengo na Mbunge wa Makadara George Aladwa, wamekuwa wakieleza hofu kwamba huenda Jubilee ikamchezea shere Bw Odinga.

Wakati huo huo, chama hicho kimeanza mchakato wa kutafuta mwaniaji wa urais atakayepeperusha bendera ya chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa 2022.

Bodi ya Uchaguzi ya ODM (NEB) inatarajiwa kuchapisha tangazo magazetini wiki hii la kuwataka Wakenya wanaotaka kuwania urais kupitia chama hicho kutuma maombi.

Viongozi wa ODM ambao tayari wametangaza azma yao ya kutaka kuwania urais ni magavana Wycliffe Oparanya (Kakamega), Hassan Joho (Mombasa) na Amason Jeffah Kingi (Kilifi) pamoja na Bw Odinga ambaye aliwania urais kwenye chaguzi za 1997, 2017, 2013 na 2017.

Japo ameonyesha dalili kuwa huenda akawania urais 2022, Bw Odinga hajatangaza wazi kuwa atajitosa kwenye kinyang’anyiro. Tayari Bw Joho na Bw Kingi wametishia kuunda chama kipya kitakachotetea masilahi ya watu wa Pwani.Iwapo viongozi wawili hao wa Pwani watajiondoa, basi Bw Oparanya huenda akakabidhiwa tiketi ya ODM endapo Bw Odinga hatatuma maombi ya kutaka kuwania urais kwa mara ya tano.

Tangu chama cha ODM kubuniwa mara baada ya Wakenya kutupilia mbali kura ya maamuzi ya kutaka kubadilisha katiba mnamo 2005, hakuna mwanasiasa mwingine tofauti na Bw Odinga ambaye amewahi kuwania urais kupitia tiketi ya chama hicho.Bw Odinga alitumia tiketi ya ODM kuwania urais bila mafanikio katika uchaguzi wa 2007, 2013 na 2017.

Handisheki ilivyoimairsha ukuaji wa uchumi Nyanza

Na RUTH MBULA

ENEO la Nyanza limefaidika na miradi ya mabilioni ya fedha kutoka kwa serikali kuu ambayo imechochea uwezo wa kiuchumi eneo hilo baada ya miaka mingi ya kutengwa na serikali za awali.

Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i ambaye pia huendesha miradi ya serikali kuu, katika mahojiano na Taifa Leo alisema maeneo ya Waluo, Wakisii na Wakuria katika Kaunti ya Nyanza yamenufaika pakubwa sawa na maeneo mengine nchini.

Bw Matiang’i alisema utawala wa Rais Uhuru Kenyatta umemakinika kuhakikisha usawa nchini na azma hiyo imeangaziwa vyema katika utekelezaji wa mirdi ya maendeleo.

Waziri huyo alieleza kuwa ukuaji wa kiuchumi katika eneo hilo umechochewa na hatua ya viongozi kadhaa wakiongozwa na kiongozi wa chama cha Orange Democratic Movement Raila Odinga kuungana kisiasa.

Alisema miundomsingi ya barabara iliyoboreshwa katika maeneo ya mashinani, miundomsingi mipya ya vituo vya elimu na vilivyofanyiwa ukarabati, miradi ya kuimarisha kilimo na afya na miradi mikuu ni baadhi ya ukuaji kiuchumi uliofanikishwa na serikali kuu.

Wiki iliyopita katika mkutano ulioandaliwa katika hoteli ya Kisii State Lodge na uliohudhuriwa na Bw Odinga na mwenzake wa handisheki Rais Kenyatta, viongozi hao walikubaliana kuwa eneo la Nyanza litazungumza kwa sauti moja.

Viongozi hao waliafikiana kusonga kama kambi moja na kwamba hakutakuwepo tena migawanyiko baina ya Waluo, Wakisii na Wakuria katika Kaunti ya Nyanza.

Rais Kenyatta alipokuwa Nyanza wiki iliyopita alimwamrisha Waziri Matiang’i kuhakikisha kuanzishwa na kukamilishwa kwa miradi zaidi ikiwemo pia kukamilishwa kwa miradi iliyokwama.

Wakazi wamepongeza ukuaji kiuchumi wakisema hatimaye Nyanza inahisi uwepo wa serikali.

Katika eneo la Gusii, Kisii State Lodge, uwanja wa spoti uliofanyiwa ukarabati wa Gusii, kituo kipya cha fedha kilichofunguliwa majuzi mjini Kisii, barabara kuu yenye thamani ya Sh18 bilioni inayounganisha Ahero-Kisii-Isibania, Uwanja wa ndege wa Suneka, mradi wa maji wa Kegati na barabara yenye thamani ya Sh 3.5 bilioni inayounganisha Chebilat-Ikonge-Chabera-Kisumu, ni baadhi tu ya miradi kutoka kwa serikali kuu.

“Tuko na watu zaidi walioajiriwa katika sekta za kibinafsi na za umma,” alisema Waziri Matiang’i.

Rais alisema chini ya uongozi wa Matiang’i, taifa liko imara zaidi likiwa na visa vichache zaidi vya ukosefu wa usalama.

“Tangu nilipotoa Amri ya Rais Nambari 1 ya 2019, kazi nyingi imefanyika, mara 10 zaidi ya kile tulichokuwa tumefanya tangu nilipochaguliwa kama Rais mnamo 2013. Mbona nyinyi viongozi mruhusu watu kuja na kumtukana Bw Matiang’i?” alisema Kiongozi wa Taifa.

Handisheki yageuza ‘Baba’ bubu

NA WAANDISHI WETU

KIMYA kirefu cha Kiongozi wa ODM Raila Odinga kuhusiana na hatua za serikali zinazoenda kinyume na misimamo yake ya zamani, kimemsawiri kama kiongozi aliyebanwa kisiasa.

Kwa muda mrefu, Bw Odinga amejitokeza kama mtetezi wa demokrasia, mpiganiaji wa haki na usawa kimaendeleo na mtetezi wa haki za walalahoi.

Hata hivyo, kiongozi huyo wa upinzani amefyata ulimi tangu akumbatiane kisiasa na Rais Uhuru Kenyatta mnamo 2018 licha ya matukio yanayoendelea kukera wananchi kama vile ubomoaji wa nyumba na masoko kiholela, udhalimu wa polisi dhidi ya raia, na pendekezo jipya kuhusu ugavi wa fedha kwa kaunti.

Mfumo mpya wa ugavi wa fedha uliopendekezwa na Tume ya Ugavi wa Rasilimali (CRA) utahitaji fedha zigawanywe kwa msingi wa idadi ya watu katika kaunti badala ya ukubwa wa kaunti.

Umepingwa na viongozi, hasa wa Pwani na Kaskazini, ambao wanalalamika utachangia maeneo yao kuendelea kubaki nyuma kimaendeleo.

Ilibainika kuwa, Rais Uhuru Kenyatta anataka Seneti ipitishe hoja ya kuruhusu mfumo huo mpya haraka ili kuzuia mtafaruku wa kisheria.

Wadadisi wanasema Bw Odinga yumo kwenye njiapanda kwa kuwai, kwa upande mmoja, yeye ni mtetezi sugu wa haki kwa wananchi lakini kwa upande mwingine, hangependa kumuudhi Rais Kenyatta.

“Matumaini ya Bw Odinga kushinda urais 2022 iwapo ataamua kuwania yamo mikononi mwa Rais Kenyatta. Iwapo ataanza kukosoa serikali, kutakuwa na hatari ya wawili hao kutofautiana kabla ya 2022,” asema mchanganuzi wa siasa, Prof Medo Misama.

Seneta wa Kilifi, Bw Stewart Madzayo ambaye amekuwa katika mstari wa mbele kupinga mfumo huo kwa niaba ya viongozi wa Pwani, alisema amechukizwa na jinsi ODM inavyotaka kuchangia katika hatua ambayo itaumiza eneo lililo na wafuasi wake wengi.

“Tuna haki ya kujua ni nini kilitokea na ni lazima ukweli usemwe. Itakuaje Kilifi ipoteze Sh1.2 bilioni na maeneo mengine kama Mandera pia kupoteza hadi Sh2 bilioni ilhali ni maeneo yasiyo na hospitali, barabara wala shule za kitaifa?” akasema.

Aliyekuwa Mbunge wa Garsen, Bw Danson Mungatana aliomba maseneta kujitenga na uaminifu wao kwa vigogo wa kisiasa akiwemo Bw Raila watakapofanya uamuzi.

“Haya ndiyo mambo ambayo hufanya watu waanze kudhukia nchi zao na kuwazia kujitenga,” akasema.

Gavana wa Tana River, Bw Dhadho Godhana, alisihi maseneta wasipitishe hoja itakayoruhusu utekelezaji wa mfumo huo.

Alisema walioupendekeza hawakutilia maanani kwamba, wakati mfumo wa ugatuzi ulianzishwa, kuna kaunti zilikuwa zimenufaika sana kimaendeleo kuliko kaunti nyingine.

“Itatubidi tufutilie mbali mipango yote ya maendeleo kwa sababu fedha zitakazobaki zitakuwa ni za mishahara pekee,” akaeleza.

Mbunge wa Kacheliba, Kaunti ya Pokot Magharibi, Bw Mark Lomunokol, alisema kupitishwa kwa mfumo huo kutadhihirisha viongozi wanahadaa Wakenya wanaposema wanataka kuleta umoja na haki kitaifa.

Gavana wa Bungoma, Bw Wycliffe Wangamati ambaye ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha katika Baraza la Magavana alisema, kaunti yake ni mojawapo ya tano ambazo zina watu takriban milioni 1.8.

“Bungoma ni kaunti ya tano kwa wingi wa watu baada ya Nairobi, Kakamega, Nakuru na Kiambu. Naunga mkono mfumo huo mpya wa kugawa fedha lakini naomba kaunti zilizoachwa nyuma pia zitafutiwe jinsi zitalindwa,” akasema.

Bw Odinga, katika mahojiano na kituo kimoja cha redio miezi miwili iliyopita alisema hajazuia viongozi wa ODM kukosoa serikali ya Rais Kenyatta inapofanya mambo isivyostahili.

“Serikali ikienda kombo, wabunge ambao ni wawakilishi wa watu wako huru kuishutumu. Wakitaka kumfikia Rais Kenyatta wanaweza kupitia kwangu niwasaidie kumfikia,” alisema Bw Odinga.

Lakini baadhi ya wabunge kutoka Nyanza waliambia Taifa Leo imekuwa vigumu kwao kukosoa serikali hadharani kutokana na hofu ya kutengwa na kuhatarisha kushindwa katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Ripoti za Leonard Onyango, Brian Ojamaa, Charles Lwanga, Stephen Oduor, Oscar Kakai na Valentine Obara

Ubaguzi wa wazi?

DERICK LUVEGA na BENSON AMADALA

SERIKALI imekashifiwa kwa kuonekana kupendelea viongozi wa kisiasa wanaomuunga mkono Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM, Raila Odinga, katika utekelezaji wa kanuni za kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona.

Kwa upande mmoja, wanasiasa wanaounga mkono handisheki kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga waonekana kuruhusiwa kuandaa mikutano ya hadhara, huku wale wanaoegemea upande wa Naibu Rais, Dkt William Ruto wakitawanywa na polisi hata ndani ya maboma yao.

Serikali ilikuwa imepiga marufuku mikutano ya kisiasa kama njia mojawapo ya kuepusha mikusanyiko ya watu ambayo hutoa nafasi yao kuambukizana corona.

Jumamosi, hali hii ilishuhudiwa katika eneo la Magharibi mwa nchi ambapo wandani wa Dkt Ruto walifurushwa kikaoni kwa nguvu ilhali wale wa upande wa handisheki wakiendesha mikutano yao chini ya ulinzi wa polisi.

Katika Kaunti ya Vihiga, polisi Jumamosi walitumia vitoa machozi kuwatawanya wafuasi wa kikundi cha Tangatanga waliopanga kukutana nyumbani kwa Mbunge wa Hamisi, Charles Gimose, katika kijiji cha Simbi.

Polisi waliwalaumu wabunge hao kwa kukiuka kanuni za kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona.

Walipokuwa wakiwatawanya wabunge hao, Waziri wa Ugatuzi Eugene Wamalwa na Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya walikuwa wakiwahutubia viongozi waliokusanyika katika Chuo Kikuu cha Masinde Muliro na hawakuchukuliwa hatua.

Maafisa wa usalama walifika nyumbani kwa Bw Gimose saa moja asubuhi na kufunga njia zote za kuingia bomani humo.

Mbunge wa Mumias Mashariki, Bw Ben Washiali na aliyekuwa Seneta wa Kakamega, Dkt Boni Khalwale walifaulu kupenya hadi ndani ya makazi ya mbunge huyo.

Dkt Khalwale alianza kuwahutubia madiwani wachache waliokuwa wamefaulu kuingia lakini Mkuu wa polisi wa eneo la Hamisi, Bw Johana Chebii akaagiza warushiwe hewa ya kutoa machozi na wakalazimika kutimua mbio kwa usalama wao.

Bw Washiali aligubikwa na wingu la gesi hiyo huku Khalwale aliyekuwa amemmwagia maji mkuu wa polisi akafanikiwa kutoroka.

Alipotoka nje ya boma, Dkt Khalwale na madiwani kadhaa waliungana na wakazi kwenye barabara ya Gambogi-Jebrok na kuwarushia polisi mawe.

Dkt Khalwale aliyezungumza kwa niaba ya viongozi hao alilaumu serikali kwa kutumia nguvu kuzima mikutano ya wandani wa Dkt Ruto.

Alisema mnamo Ijumaa, Bw Oparanya aliruhusiwa kufanya mkutano mwingine pia katika Kaunti ya Vihiga. Bw Oparanya na kikundi chake wamekuwa wakifanya mikutano mingi eneo la Magharibi.

“Tulikuwa watu takriban 60 hapa na mkutano wetu umesimamishwa. Oparanya na wenzake kwa sasa wanakutana na watu karibu 2,000 Kakamega na wanalindwa na polisi,” akasema.

Katika mkutano wa Kakamega, Bw Wamalwa na Bw Oparanya walihimiza wakazi kuunga serikali na Mpango wa Maridhiano (BBI) wakiahidi miradi ya maendeleo eneo hilo.

“Kama jamii, tumeendelea kuwa katika baridi ya kisiasa kwa sababu tuko katika upinzani. Wakati huu hatutaki kurudia kosa hilo tena,” Bw Oparanya alisema.

“Ni lazima tuunge BBI mkono kwa sababu hii ndiyo njia itakayotuingiza serikalini. Tumechoka kupiga kelele katika upinzani,” aliongeza Bw Oparanya.

Wakati huo huo, viongozi wa Ford Kenya waliilaumu serikali kwa kuwahangaisha kila wanapotaka kukutana.

Katibu Mtendaji Chris Mandu Mandu alisema serikali inaonekana kuwa na nia ya kuwahangaisha wanachama, hasa wale wanaoegemea upande wa Seneta wa Bungoma, Bw Moses Wetang’ula.

Mnamo Ijumaa, viongozi wa chama hicho walikuwa wanajiandaa kukutana katika hoteli moja mjini Kakamega lakini polisi wakawasili ghafla na kuwaagiza waondoke.

“Tunahangaishwa na polisi kila tunapoandaa mikutano kujadili masuala ya chama. Polisi huvuruga mikutano yetu wakidai tunakiuka kanuni za Wizara ya Afya kuhusu Covid-19,” akasema Bw Mandu.

UhuRaila wakejeliwa kwa ‘kutakasa ufisadi’

NA MWANGI MUIRURI

USHIRIKA wa Rais Uhuru Kenyatta na Raila Odinga chini ya mwavuli wa handisheki umetajwa kama unaolemaza vita dhidi ya ufisadi, huku ukionyesha ubaguzi katika kuandama wezi wa rasilimali za kitaifa.

Katika siasa zinazoendelea katika ung’atuzi wa Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru, Rais na Bw Odinga wamekosolewa pakubwa kwa mapendeleo yao ya wazi ya kukinga baadhi ya washukiwa huku wakiwaandama wengine.

Hii ni baada ya bunge la Seneti kuonekana wazi kuwa lina mirengo miwili ya kisiasa ambayo inamenyana kumzamisha au kumnusuru Bi Waiguru, ule wa handisheki ukionekana wazi kuwa hauzingatii sana ushahidi wa bunge la Kaunti ya Kirinyaga bali unazingatia tu masilahi ya umoja wa Raila na Uhuru.

Tayari, mwandani wa Raila ambaye ni Seneta wa Siaya James Orengo ametangaza kuwa “kesi dhidi ya Waiguru haina msingi bali anawindwa kisiasa na mahasidi wa handisheki. Wanatafuta kichwa cha Waiguru!”

Naye kiranja wa wengi katika bunge hilo la Seneti Irungu Kang’ata ametangaza kuwa “mimi naunga mkono msimamo wa Rais wetu na kinara wetu wa chama cha Jubilee kuwa suala hili la Kirinyaga litatuliwe haraka ili kaunti hiyo itulie.”

Aliyekuwa Waziri wa masuala ya kikatiba na haki, Martha Karua amesema kuwa ushirika huo wa handisheki umepotoka kutoka nia njema ya kuleta amani na utengamano nchini na kugeuka kwanza kuwa mauti kwa demokrasia ya vyama vingi vya kisiasa na hatimaye kuondoa ule uwajibikaji wa upinzani kuwa nyapara wa utawala wa serikali.

Bi Karua aliye pia kinara wa chama cha Narc-Kenya aliambia Taifa Leo Dijitali kuwa kwa sasa hakuna uwezekano wa ushirika huo kuwafaa Wakenya na uchumi wao katika vita dhidi ya ufisadi na maovu mengine ya kiutawala.

Alisema kuwa “wawili hawa wamekuwa wakidai kuwa idara ya mahakama ndiyo imekuwa kizingiti kikuu katika vita dhidi ya ufisadi, lakini kwa sasa ni wazi kuwa hata katika fikira na utendakazi wa wawili hawa, hata wao ni visiki katika vita hivi.”

Mbunge wa Kikuyu Kimani Ichung’wa alisema kuwa kuna visa kadhaa ambapo akiwa mwenyekiti wa kamati ya bunge kuhusu bajeti alipata shinikizo za kutengea miradi ghusi pesa za kimaendeleo kutoka mrengo wa Handisheki.

“Kuna wizara za mawaziri wa handisheki ambazo zilikuwa zinasukuma pesa za kimagendo kutengewa miradi yao…Mimi nilikuwa nikikataa na mojawapo ya miradi hiyo ya ukora ni kuhusu utapeli wa shamba la Ruaraka ambapo Wizara ya Elimu ikiwa kwa wakati mmoja mikononi mwa Dkt Fred Matiang’i  ambapo hadi sasa hakuna taasisi inayofuatilia kesi hii kwa kuwa huyu Matiang’i ni wa Handisheki,” akasema.

Ni msimamo ambao ulitiliwa mkazo na Seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen aliyesema kuwa “vita dhidi ya ufisadi kwa sasa ni silaha ya kisiasa mikononi mwa baadhi ya mirengo ya kisiasa.”

Amesema kuwa wale ambao humuunga mkono naibu wa Rais Dkt William Ruto wakisingiziwa ufisadi huwa wanasukumwa mbio hadi nje ya nyadhifa huku wale wa handisheki wakiwa sasa na idhini rasmi ya kutapeli, kufuja, kuiba na kufisadi watakavyo kwa kuwa wako katika kambi ya wadosi.

Alisema kuwa Raila amekuwa akijipendekeza kama mpiganiaji wa haki za Wakenya na utawala bora lakini “amegeuka kuwa wa kutakasa wale ambao wamehusishwa na ufisadi bora tu watangaze kuwa wanamuunga mkono.”

Alisema kuwa Raila ameambukiza Uhuru msimamo huo dhidi ya ufisadi ambapo “ukionekana kuwa unaunga mkono muungano wa handisheki bila masharti, unatakaswa katika idara za kuchunguza ufisadi.”

Katika hali hiyo, Murkomen aliteta kuwa watu wa Kirinyaga sawia na wengine ambao wako katika mirengo tofauti ya kisiasa waelewe kuwa “vita dhidi ya ufisadi ni kwa wale ambao watakataa kujumuishwa katika mrengo mmoja wa kisiasa hapa nchini kwa lazima.”

Aliyeandaa mswada wa kumng’atua Bi Waiguru katika bunge la Kirinyaga, Kinyua wa Wangui alisema kuwa “mimi sitaki kuhusika kamwe na ukora na unafiki huu ambao umeonekana katika bunge la Seneti.”

Alisema kuwa “ni wazi kuwa kumeandaliwa njama ya kutupuuza kama bunge la Kaunti na Uhuru na Raila wanafaa waelewe kuwa hata wakimwokoa Waiguru katika Seneti, bado atakuja hapa Kirinyaga na tutawafunza adabu za kutuheshimu.”

Kiranja wa bunge hilo la Kirinyaga Pius Njogu alisema kuwa “huu ni utawala wa giza, ushirikiano wa hujuma na uliojaa unafiki wa kupambana na vita dhidi ya ufisadi,” huku aliyekuwa kiranja wa wengi, Kamau Murango akisema kuwa “Uhuru na Raila hawajaonyesha nia ya kuwa na uwazi dhidi ya kupambana na ufisadi.”

Handisheki bila matunda

Na WANDERI KAMAU

MUAFAKA wa maelewano kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM, Raila Odinga, maarufu kama handisheki haujazalisha matunda mengi mbali na kuleta hali ya utulivu wa kisiasa nchini unapoingia miaka miwili Jumatatu hii.

Ingawa lengo lao lilikuwa kuunganisha nchi na kuweka mandhari bora ya kukuza uchumi na kufanikisha utekelezaji wa Ajenda Nne za maendeleo, wadadisi wasema mipango mingi imekwama au kuvurugwa, huku ikisalia miaka miwili pekee kabla Uchaguzi Mkuu uandaliwe.

Wadadisi wanasema kwamba, handisheki imezua uhasama mkuu kinyume ya matarajio, hasa kwa kuonekana kumtenga kisiasa Naibu Rais William Ruto.

“Handisheki imeleta mgawanyiko wa kisiasa nchini. Rais Kenyatta na Bw Odinga wanaonekana kumtenga Dkt Ruto, ambapo hiyo ndiyo sababu kuu inamfanya aendelee kulalamika,” akasema Bw Andati  kwenye mahojiano na ‘Taifa Leo.’

Dkt Ruto amekuwa akidai kuwa, lengo kuu la Bw Odinga limekuwa kutumia handisheki na Mpango wa Maridhiano (BBI) kuendeleza azma yake ya kuwania urais mnamo 2022.

“Lengo la kwanza la handisheki lilikuwa zuri. Hata hivyo ujio wa Bw Odinga umeisambaratisha Jubilee. Ni kama sasa yuko serikalini, huku Dkt Ruto akibaki nje,” akasema Bw Andati.

Dalili za mgawanyiko Jubilee zilifika kileleni Jumamosi Dkt Ruto alipodai kuna watu serikalini wanafanya kila juhudi kumzima asiwe rais ifikapo 2022.

Wadadisi pia wanasema mpango huo umeondoa uwajibikaji serikalini, kwani hakuna kiongozi shupavu wa upinzani.

“Bw Odinga alikuwa kiongozi wa muungano wa NASA. Alikuwa akiikosoa serikali. Hakuna upinzani kwa sasa. Mashirika ya kijamii pia yamenyamazishwa,” akasema Bw Andati.

Mpango huo pia ulilaumiwa kuchangia mipango muhimu kama Ajenda Nne Kuu za Maendeleo kusambaratika.

Alipoanza muhula wake wa pili mnamo 2017, Rais Kenyatta aliorodhesha uzalishaji vyakula cha kutosha, ujenzi wa nyumba za bei nafuu, afya kwa wote na utengenezaji bidhaa kama masuala ambayo angeyapa kipaumbele katika serikali yake.

Lakini ikiwa imesalia chini ya miaka miwili ili kukamilisha muhula wake, miradi mingi chini ya mipango hiyo imekwama.

Mnamo Januari, Serikali ilipokea nyumba 228, ambazo ni sehemu ya nyumba 500,000 ambazo inalenga kukamilisha kujenga ifikiapo 2022.

Na licha ya taswishi ambazo zimekuwepo, Katibu katika Wizara ya Ujenzi Bw Charles Hinga anasisitiza kwamba serikali inajizatiti kufanikisha mpango huo.

Changamoto kama hii pia inaandama mpango wa uzalishaji chakula cha kutosha, hasa baada ya kubainika kuwa karibu Wakenya milioni kumi hawana chakula cha kutosha. Takwimu hizo zilitolewa na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Kenya (KARI).

Kuhusu mpango wa afya kwa wote uliozinduliwa mnamo 2018, wadadisi wameeleza wasiwasi ikiwa utafaulu.

Baadhi ya vikwazo vinavyoonekana kuukumba mpango huo ni mabadiliko yaliyotangazwa majuzi na Hazina ya Bima ya Kitaifa ya Hospitali (NHIF), kwamba kadi moja haiwezi kugharamia matibabu ya mtu aliye na zaidi ya mke mmoja.

Rais Kenyatta alilazimika kusimamisha mipango hiyo kwa muda baada ya malalamishi mengi kutoka kwa Wakenya.

Na kutokana na hayo, Prof Macharia Munene, ambaye ni mchanganuzi wa masuala ya kisiasa anasema kuwa, huu ni wakati muhimu kwa Rais Kenyatta kutathmini nafasi ya handisheni, ili kuhakikisha haizamishi malengo na ahadi alizotoa kwa Wakenya.

Handsheki: Wakazi wajuta kurushia Uhuru kiatu 2014

Na IAN BYRON

BAADHI ya wakazi katika Kaunti ya Migori wamejutia kisa ambapo Rais Uhuru Kenyatta alirushiwa kiatu jukwaani miaka sita iliyopita, wakishuku kisa hicho kimefanya wakose matunda ya handsheki.

Huku maeneo mengine ya Nyanza na ngome za kisiasa za Kiongozi wa ODM Raila Odinga kitaifa zikiendelea kupokea maendeleo tangu handsheki yake na Rais, wakazi hao wamesema miradi imekwama katika eneobunge la Suna Mashariki.

Kulingana nao, tukio hilo la aibu lililoshuhudiwa mnamo Septemba 8, 2014 huenda lilifanya wakaorodheshwa kama maadui wakubwa wa serikali ya Jubilee.

Kiatu kilirushwa jukwaani wakati Rais Kenyatta alipokuwa ameenda kuzindua ujenzi wa miradi mbalimbali ikiwemo Taasisi ya Mafunzo ya Kiufundi ya Kakrao na uwekaji lami barabara ya Migori kuelekea Muhuru.

Miaka sita baadaye, hata miradi hiyo iliyoenda kuzinduliwa haijaguswa.

Wakiongozwa na kiongozi wa vijana Migori, Bw Joseph Nyapete, wakazi hao walisema hawajaona dalili yoyote kwamba handsheki itawaokoa ili wafurahie maendeleo kutoka serikalini.

Taasisi ya Kakrao iliyonuiwa kuwa jengo la orofa tatu ilikwama wakati orofa ya chini ilikuwa inajengwa na sasa uwanja umejaa vichaka huku vifaa vya ujenzi vikiporwa.

“Mahali hapo panatisha. Ni aibu kwa handsheki kwani ni eneobunge la Bw Junet Mohamed ambaye yuko mstari wa mbele kutetea handsheki,” akasema Bw Nyapete.

Mzee Samuel Migore ambaye ni mkazi wa eneo hilo alisema ukarabati wa barabara ya Migori-Muhuru ilikwama katika eneo la Masara, kisha mradi ukaelekezwa mjini Kehancha ambako ni ngome ya Jubilee.

“Hakuna vile tunaweza kuzungumzia matunda ya handsheki wakati miradi hii imekwama,” akasema Bw Migore.

Ijapokuwa kisa hicho kilitokana na uhasama kati ya Gavana wa Migori Okoth Obado na baadhi ya wabunge katika kaunti hiyo, wakazi wanasema wananchi ndio wanaumia kutokana na athari zake.

Naibu Chansela wa Chuo Kikuu cha Rongo, Prof Gudu Samuel Gudu alitoa wito kwa Bw Junet na Gavana Obado kutoa ufadhili wa kukamilisha ujenzi wa taasisi ya Kakrao. Taasisi hiyo inastahili kusimamiwa na Chuo Kikuu cha Rongo.

Bw Charles Ochieng’ Ogejo, ambaye ni msaidizi wa kibinafsi wa Bw Junet alisema Hazina ya Ustawishaji Maeneobunge ya Suna Mashariki tayari ilitenga Sh10 milioni, lakini juhudi za afisi ya eneobunge zikavurugwa na serikali ya kaunti.

Ni njaa ilipeleka Raila kwa Uhuru, kitabu cha Mudavadi chafichua

JULIUS SIGEI Na BENSON MATHEKA

MATATIZO ya kifedha ni moja ya sababu kuu zilizomfanya Kiongozi wa ODM, Raila Odinga kukubali mwafaka wa maelewano kati yake na Rais Uhuru Kenyatta, maarufu kama handisheki 2018.

Kulingana na Kiongozi wa chama cha ANC, Musalia Mudavadi, ambaye wakati huo alikuwa mmoja wa vigogo wanne wa upinzani waliokuwa mrengo wa NASA, Bw Odinga pia alikuwa na presha kali kutoka mataifa ya kigeni yaliyomtaka kukomesha msimamo mkali kuhusu matokeo ya urais baada ya uchaguzi wa 2017.

Kwenye kitabu chake, “Soaring Above the Storms of Passion”, Bw Mudavadi anasema kulikuwa na kesi nyingi ambazo zilihitaji kiasi kikubwa cha pesa ambazo upinzani haukuwa nazo.

“Tuligundua hatukuwa na uwezo wa kifedha kukabili kesi zilizokuwepo. Ukweli ni kuwa hali ilikuwa mbaya,” asema Bw Mudavadi.

Pia anafichua jinsi Bw Odinga ‘alivyowaacha kwenye mataa’ yeye pamoja na Seneta Moses Wetangula wa Bungoma na Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka kuhusu kiapo alicholishwa na Miguna Miguna mnamo Januari 30, 2018 kuwa “rais wa wananchi”.

Kulingana na Bw Mudavadi, wote wanne walikuwa wamekubaliana kusitisha kiapo hicho kutokana na presha kali walizokuwa nazo kutoka pande tofauti.

Lakini walishtukia kupata habari kuwa Bw Odinga aliwapuuza na kwenda Uhuru Park alikoapishwa na Bw Miguna.

“Makubaliano yetu sote yalikuwa twende Uhuru Park siku hiyo na tuwaambie wafuasi wetu kuwa kiapo kimeahirishwa. Tulikubaliana tukutane asubuhi hiyo na kwenda Uhuru Park Pamoja,” adokeza.

Asubuhi hiyo, asema Bw Mudavadi, wote isipokuwa Bw Odinga walikutana nyumbani kwa Bw Wetang’ula: “Tulipopokea simu yake na alikuwa akizungumza kama mtu ambaye yumo kwenye hatari. Hatungeweza kuelewana. Muda mfupi baadaye tulipata habari alikuwa Uhuru Park akila kiapo.”

Anamtaja Bw Odinga kama mtu asiyeaminika na anayetaka watu wafuate anayotaka yeye, kiongozi ambaye kila mara yuko na mpango mbadala na anayeweza kubadilisha kauli wakati wowote.

Anasema wakati mmoja walipokuwa wakimshawishi kutokula kiapo, walifahamu kwamba Bw Odinga alikuwa nyumbani kwa Jimi Wanjigi akiwa na watu wa familia na wandani wake wakipanga kurekodi akila kiapo kisha itangazwe isambazwe katika vyombo vya habari.

Bw Mudavadi pia anasimulia kuwa Bw Odinga aliwaficha wakuu wenzake katika Nasa kuhusu handisheki.

“Nilikuwa nikielekea Mombasa nilipopokea simu kutoka kwa seneta wa Vihiga, George Khaniri kunifahamisha kuhusu handisheki nje ya Harambee House katika ofisi ya Rais.

“Baada ya hapo nilipokea simu nyingi. Kalonzo alinipigia akitaka kujua ikiwa nilikuwa na habari kuhusu kilichokuwa kikiendelea. Nilimweleza kwamba sikuwa na habari,” anasimulia Bw Mudavadi.

Anasema kuwa alipata presha kutoka kwa watu wa matabaka mbalimbali waliotaka kujua kilichokuwa kikiendelea ikizingatiwa kwamba alisimamia kampeni za urais za Bw Odinga.

“Walitaka kujua iwapo sasa tulikuwa katika serikali ya muungano na Jubilee,” anaeleza. Kiongozi huyo wa chama cha ANC.

Katika mkutano wa vinara wa Nasa uliofanyika Athi River baada ya handisheki, Bw Mudavadi anafichua kuwa joto lilipanda wakitaka Bw Odinga kueleza kwa nini mazungumzo yake na Rais Kenyatta yalikuwa ya siri.

“Kwenye mazungumzo hayo, iliibuka kuwa vikwazo kuhusu viza vilionekana kuwekewa watu wengine wengi,” anasimulia.

Anafichua kuwa katika mkutano mmoja kabla ya handisheki, Bw Odinga aliwaonyesha barua moja aliyoandikiwa na ubalozi wa nchi moja ya Ulaya kufuta viza yake.

Wakati mmoja, anaeleza, Odinga alikaidi ushauri wa aliyekuwa Rais wa Nigeria Olusegun Obasanjo.

JAMVI: BBI itakuwa msumari wa mwisho kwa jeneza la Jubilee

Na BENSON MATHEKA

Ripoti ya Jopokazi la Maridhiano, maarufu kama BBI, huenda ikawa msumari wa mwisho katika jeneza la chama cha Jubilee ambacho kimekumbwa na mgogoro wa ndani kwa ndani, wadadisi wameonya.

Wanasema kujitokeza hadharani kwa Naibu Rais William Ruto kupuuza jopokazi hilo lililoteuliwa na Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa upinzani Raila Odinga baada ya muafaka wao, ni ishara kwamba ripoti yake itazidisha mpasuko katika chama tawala.

Dkt Ruto na washirika wake katika kundi la Tanga Tanga wamekuwa wakikosoa muafaka huo na pendekezo la kura ya maamuzi tofauti na wale wa Kieleweke wanaompiga vita na ambao wameapa kuzima azima yake ya kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Wanachama wa Kieleweke wamekuwa wakipigia debe jopokazi hilo na kuunga kura ya maamuzi kubuni wadhifa wa waziri mkuu. Dkt Ruto na wandani wake wamekuwa wakipinga kura ya maamuzi inayolenga kubuni nyadhifa zaidi za uongozi.

Wiki jana, Dkt Ruto alipuuza kamati hiyo iliyokusanya maoni kutoka kwa umma kuhusu marekebisho wanayotaka yatekelezwe kuimarisha uwiano nchini akisema inapotezea wananchi wakati.

Kulingana na Dkt Ruto, BBI haikuwa na haja ya kuzunguka nchini kutafuta maoni ya wananchi, na badala yake ingepata tu maoni ya kiongozi wa ODM, Raila Odinga kuhusu namna ya kuzuia ghasia kila baada ya uchaguzi kwa kuwa yeye ndiye amekuwa akipinga matokeo ya kura.

Wadadisi wanasema kauli hiyo ya Dkt Ruto inaashiria kwamba atapinga vikali ripoti ya BBI inayotarajiwa wakati wowote na kuzidisha mgawanyiko katika chama tawala.

“Kwa kukosoa jopokazi ambalo Rais Kenyatta alihusika kuunda ni kuonyesha kuwa hayuko tayari kukubaliana na ripoti yake iwapo itatoa mapendekezo ya kubadilisha muundo wa serikali. Hii inaweza kuvunja Jubilee kabisa. Kumbuka chama hicho kimegawanyika huku Dkt Ruto na washirika wakilaumiana na wale wa Rais Kenyatta kuhusu kila kitu,” asema mdadisi wa siasa Geff Kamwanah.

Dkt Ruto na wandani wake wanahisi kwamba BBI inatumia rasilimali za serikali kutimiza malengo ya kuzima azima yake, kumaanisha kuwa hawatambui na hawatatambua mapendekezo yake.

“Kwa msingi huu pekee, kinachoweza kutarajiwa ni mvutano zaidi ndani ya chama cha Jubilee wandani wa Dkt Ruto wakikataa mapendekezo ya jopokazi hilo. Kwao, halikufaa kubuniwa na halina maana kwa sababu wanahisi linanuiwa kummaliza naibu rais kisiasa,” aeleza Bw Kamwanah.

Wadadisi wanasema uwezekano wa ripoti ya BBI kupendekeza kura ya maamuzi, ndio unaomkera Dkt Ruto ambaye amekuwa akidai pendekezo hilo linalenga kunufaisha watu au jamii chache.

“Kauli hii inalenga wanachama wa kundi la Kieleweke ambao wamekuwa wakiunga mkono maridhiano kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga na hii imekuwa ikimwasha Dkt Ruto na wandani wake. Wanahisi kwamba Bw Odinga amezua msukosuko katika chama cha Jubilee kwa lengo la kumwekea Ruto vikwazo, madai ambayo Rais Kenyatta mwenyewe amekanusha akisema muafaka wao haukuhusu uchaguzi wa 2022,” asema mdadisi wa siasa, Peter Wafula.

Anasema ishara kwamba ripoti ya kamati hiyo itazamisha chama cha Jubilee ni hatua ya wandani wa Dkt Ruto ya kuunga mswada wa kura ya maamuzi wa Punguza Mizigo ambao unapendekezwa na chama cha Third Way Alliance.

“Ikiwa kutakuwa na kura ya maamuzi kutokana na mapendekezo ya BBI, kutakuwa na kivumbi katika chama cha Jubilee, Dkt Ruto na washirika wake wakiyapinga. Sio kwa sababu mapendekezo hayo yatakuwa mabaya, yanaweza kuwa mazuri kwa nchi, lakini watayapinga kwa sababu Bw Odinga na Wanakieleweke watayaunga mkono,” asema Bw Wafula.

Anatoa mfano wa bunge la kaunti ya nyumbani ya Bw Odinga ya Siaya kukataa mswada wa Punguza Mizigo huku bunge la kaunti ya nyumbani ya Dkt Ruto ya Uasin Gishu ikipitisha mswada huo.

Kulingana na wandani wa Dkt Ruto, BBI inatumiwa kusambaratisha ndoto yake ya kushinda urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2022 na hawawezi kuunga mapendekezo.

Wadadisi wanasema Dkt Ruto anahisi kuwa hakushirikishwa kwenye BBI licha ya kuwa nguzo muhimu katika serikali ya Jubilee na siasa za humu nchini.

Wandani wake wamekosoa kamati hiyo wakidai kwamba inalenga kutimiza maslahi ya watu wachache wanaotaka kutenga jamii nyingine.

“Kwa chama ambacho kimekumbwa na migogoro ya ndani kwa ndani na madai ya usaliti kama Jubilee, ripoti ya BBI inaweza kukivunja kabisa ikizingatiwa tangu mwanzo, Dkt Ruto ambaye ni mshirika mkuu katika chama hicho hakuchangamkia muafaka uliozaa jopokazi hilo,” asema Bw Kamwanah.

Walivyozimwa kwa minofu

Na BENSON MATHEKA

WALIOKUWA viongozi wakuu wa upinzani kabla ya handisheki wametajwa kama wasaliti wa mwananchi wa kawaida.

Hii ni baada ya viongozi hao wakiongozwa na kinara wa ODM, Raila Odinga kumezwa na serikali ya Jubilee na hivyo sauti zao kuzimwa.

Wanasiasa hao na wakuu wa mashirika ya umma sasa wanakula ronjoronjo huku maisha ya Wanjiku yakiendelea kuwa magumu kutokana gharama ya juu ya bidhaa, ukosefu wa ajira kwa vijana, ushuru wa juu, ufisadi, madeni, maafisa wa serikali kupuuza sheria miongoni mwa matatizo mengine.

Hali ilibadilika tangu handisheki kwa kile Rais Uhuru Kenyatta na Bw Odinga walichotaja kuwa muafaka wa kuunganisha Wakenya.

KUKOSA SAUTI

Kulingana na wadadisi wa siasa, waliokuwa viongozi wa upinzani wakiongozwa na Bw Odinga wamekuwa wakitafuna minofu hivyo kukosa sauti ya kutetea Wanjiku.

“Hakuna mtu anayepiga kelele au kuzungumza akitafuna kwa sababu ni tabia mbaya kufanya hivyo,” asema mdadisi wa masuala ya kisiasa Martin Andati.

“Wamenufaika kwa kuacha kukosoa serikali. Kwa mfano, Bw Odinga ana wadhifa katika AU huku aliyekuwa mgombea mwenza wake Kalonzo Musyoka akiwa balozi wa amani Sudan Kusini. Nyadhifa hizi zina marupurupu,” aeleza mdadisi wa masuala ya kisiasa Tom Maosa.

“Kimya chao sio cha kushangaza. Hawakuwa katika upinzani kwa kupenda au kwa sababu ya imani na misimamo yao. Ni nafasi walikuwa wamekosa ya kufaidika kiuchumi,” asema Bw Maosa.

Anatoa mfano wa Gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho ambaye alikuwa mkosoaji mkuu wa serikali ya Jubilee kutoka Pwani, na majuzi ilifichuliwa kuwa anafaidika kibiashara kupitia kampuni zinazohusishwa na familia yake.

Kiongozi wa chama cha Ford Kenya Moses Wetangula pia amenyamaza.

Aliyekuwa seneta wa Machakos Johnstone Muthama, ambaye ni mwandani wa karibu wa Bw Musyoka pia ameacha kukosoa serikali na amekuwa akiwahimiza viongozi kumuunga mkono Rais Kenyatta.

Kimya cha upinzani kilipenya hadi bunge ambapo waliokuwa wakipaza sauti kukosoa serikali sasa ndio wapigaji debe wakuu wa Jubilee.

Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Taifa, John Mbadi amekuwa akisikika tu anapoimba wimbo wa kiongozi wa wengi Aden Duale, tofauti na awali ambapo alikuwa akimkosoa vikali.

Hali ni sawa katika Seneti ambapo James Orengo amekuwa mtetezi mkuu wa serikali ya Jubilee.

Bw Orengo alipata kiti cha Kiongozi wa Wachache katika Seneti baada ya handisheki kufuatia kubanduliwa kwa Bw Wetangula.

Wabunge wengine ambao wamezima sauti ni Millie Odhiambo (Mbita), Peter Kaluma (Homa Bay Mjini ), Otiende Amollo (Rarienda), Opiyo Wandayi (Ugunja), Gladys Wanga (Mwakilishi wa Wanawake Homa Bay) na T.J. Kajwang (Ruaraka).

Wadadisi wanasema japo wamekuwa wakidai kwamba waliamua kuunga mkono handisheki ili kutuliza joto la kisiasa, ukweli ni kuwa wanafaidika binafsi ndiposa wakanyamaza.

MANUFAA

Anasema walichofanya wanasiasa wa upinzani ni kujiunga na Bw Odinga ili wapate kunufaika hata kama hawakubaliani na maoni yake.

Sauti za viongozi wa mashirika ya kijamii ambao walikuwa wakikosoa serikali pia zilididimia baada ya muafaka.

Bw Andati anasema wanaharakati wengi walivutwa upande wa serikali na wachache waliobaki wakaingizwa baridi.

Kulingana na ripoti ya Uwazi Consortium iliyotolewa Mei mwaka huu, handisheki ndiyo iliyozima mashirika hayo.

Wanaharakati waliokuwa wakilaumu serikali kama vile Gladwel Otieno wa shirika la AfriCog, George Kegoro na Profesa Makau Mutua wa Kenya Human Rights Commission na Maina Kiai wa InformAction wamekuwa kimya.

Dkt Kennedy Orengo wa Uwazi Consortium alisema japo handisheki ilituliza joto la kisiasa, kwa upande mwingine imelemaza kustawi kwa demokrasia kwani ulimaliza upinzani.

Mtihani wa handisheki Jubilee ikiingia Kibra

Na CECIL ODONGO

USHIRIKIANO kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Kinara wa ODM Raila Odinga unatarajiwa kutiwa kwenye mizani baada ya chama cha Jubilee kutangaza kwamba kitakuwa mwaniaji kwenye uchaguzi mdogo wa Kibra hapo Novemba 7.

Katibu Mkuu wa Jubilee, Raphael Tuju alisema wanachama wa Jubilee ambao wangependa kurithi kiti hicho kilichokuwa kikishikiliwa na marehemu Ken Okoth, watume maombi kwa bodi ya uchaguzi ya chama hicho.

“Kufuatia mashauriano na uongozi wa Jubilee kuhusiana na uchaguzi mdogo wa eneobunge la Kibra Novemba 7, tungependa kuwaeleza wanachama wetu kwamba tutawasilisha mwaniaji wetu. Utathmini wetu umeonyesha kuwa chama kipo imara na kinaweza kutoa ushindani mkali kwa wawaniaji wengine,” ikasema taarifa ya Bw Tuju.

Bw Tuju alisema uamuzi huo umepigwa jeki na ushindi wa Nixon Korir katika eneobunge jirani la Langata kwenye uchaguzi wa 2017, kinyume na dhana kwamba eneo hilo lilikuwa ngome ya ODM.

Hata hivyo, taarifa hiyo haikubainisha masharti ambayo wenye azma ya kugombea kwa tiketi ya Jubilee wamewekewa kili kupewa tiket hiyo.

Huku hayo yakiendelea, chama cha ODM nacho kinatarajiwa kupokea vyeti vya wawaniaji leo kisha kuwaidhinisha watakaoshindana kwenye mchujo utakoafanyika Jumamosi hii.

Mwenyekiti wa Bodi ya Uchaguzi wa ODM, Judy Pareno., ambaye pia ni Seneta wa k,uteuliwa, anatarajiwa kuongoza maafisa wenzake kupokea vyeti hivyo, siku mbili tu baada ya Bw Odinga kuongoza hafla ya kuwatambulisha wawaniaji hao 24 kwa wananchi katika uwanja wa Kamkunji, Kibra.

Ripoti ya BBI kutayarishwa kuanzia leo, Haji atangaza

Na STEPHEN ODUOR

JOPOKAZI lililoundwa na Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa ODM Raila Odinga kuzunguka nchini likikusanya maoni ya wananchi kuhusu masuala ya uongozi, Building Bridges Initiative (BBI), limekamilisha ziara zake katika kaunti 47.

Akizungumza na wanahabari, mwenyekiti wa jopokazi hilo, Bw Yusuf Haji alisema wanakamati wamepanga kuanza kukutana faraghani Jumatatu ili kujumuisha maoni waliyopokea walipokutana na Wakenya mashinani.

Kulingana naye, kazi iliyobaki itakuwa ni kuchagua masuala yaliyotajwa sana na Wakenya kwa jumla ili kuchapisha ripoti mwafaka ya mapendekezo hayo.

Bw Haji alisema kuwa tayari walikuwa wamefanikiwa kupata maoni katika kaunti zote 47, yatakayozingatiwa kuamua kama kutahitajika kuwepo marekebisho ya katiba.

“Tumefanya lililopaswa na letu sasa ni kuchapisha nakala hiyo ya mapendekezo, ambayo itakuwa sauti ya Wakenya kwa jumla. Tutaiwasilisha kwa rais kabla wiki ya kwanza ya mwezi wa Septemba,” alieleza.

Timu hiyo inayojumuisha pia msomi wa masuala ya kisiasa, Adams Oloo, Seneta wa Busia Amos Wako, Said Mwaguni, Ole Ronkei na mhubiri Agnes Muthama , ilishiriki mjadala wa mwisho na wakazi wa Tana River, mjini Hola ambapo wakazi pamoja na viongozi walichangia maswala muhimu walioridhia yasajiliwe kama matakwa.

Mjadala huo ulishuhudia viongozi wa kaunti ya Tana River wakipendekeza mfumo wa uongozi utakaojumlisha viongozi kutoka kata zote za nchi katika ngazi za juu,wakiongozwa na rais atakayechaguliwa na wananchi.

Kamati ya BBI imepiga hatua hiyo kubwa wakati ambapo mapendekezo ya Chama cha Thirdway Alliance kinachoongozwa na Dkt Ekuru Aukot kurekebisha katiba, yanazidi kupata pingamizi.

Kufikia sasa, vyama vikubwa vya upinzani ikiwemo ODM kinachoongozwa na Raila Odinga, na Wiper kilicho chini ya Bw Kalonzo Musyoka vimesema havitaunga mkono mapendekezo ya Dkt Aukot katika mswada wa ‘Punguza Mizigo’.

Vilevile, kuna malalamishi yaliyowasilishwa mahakamani kuzuia mswada huo wa Punguza Mizigo kujadiliwa na madiwani, ambao wengi wao wametangaza wataupitisha.

Miongoni mwa sababu zinazotolewa na wapinzani wa Punguza Mizigo ni kwamba, mswada huo haujatoa nafasi ya kubadilisha mfumo wa uongozi kitaifa.

Manufaa ya Handisheki: Kisumu kupata miradi ya Sh50 bilioni

Na MWANGI MUIRURI

MRATIBU wa utekelezaji miradi ya serikali, Dkt Fred Matiang’i ametangaza kuwa Kaunti ya Kisumu itapokezwa na serikali kuu kitita cha Sh50 bilioni za miradi ya maendeleo katika mwaka 2019/20.

Eneo la Nyanza limekuwa likimulikwa kwa maendeleo mengi tangu kinara wa upinzani Raila Odinga asalimiane na Rais Uhuru Kenyatta na kuwa mmoja wa viungo thabiti kwa utawala wa Jubilee ambapo amezima kabisa harakati za kupinga serikali kwa lolote lile.

Akiongea Jumatano katika eneo la Migori, Dkt Matiang’i alisema miradi hiyo itakuwa njia moja ya kuharakisha maendeleo eneo hilo baada ya miaka ya kutelekezwa ambapo siasa za upinzani eneo hilo zilitajwa.

“Mradi wa kwanza utakuwa wa kujenga nyumba za makazi kwa walio katika pato la wastani na duni. Ujenzi huo ukishakamilika, nyumba zitauziwa wafanyakazi wa umma kwa bei rahisi ili kuwajenga katika maisha yao na hivyo basi kuwapa motisha ya kuendelea kuchapa kazi kwa roho safi wakiwa na uhakika wa kustaafu katika mazingira ya ustaarabu,” akasema Matiang’i.

Dkt Matiang’i alifafanua kuwa mradi huo unaoendeshwa kwa awamu kadha kote nchini unashirikishwa na mpango wa kisera wa Civil Servants Tenant Purchase Housing Scheme.

“Mradi wa Kisumu utatimizwa kwa kujengwa kwa nyumba 250 katika uwanja wa hekari 2.85 na ambao unakadiriwa kumalizika mwaka wa 2021,” akasema.

Alisema kuwa mradi huo utaimarisha sura ya eneo hilo kwa kuwa nyumba zote zitakuwa za ghorofa tano huku miundombinu katika mazingira yake ikiimarishwa.

“Tutaunda barabara, tuweke mitambo ya maji na kisha tuwatengenezee soko na eneo la burudani ndani ya mtaa huo mpya. Pia, nafasi ya kuegesha magari itakuwa pana na ya kuvutia,” akasema.

Yakikamilika, wafanyakazi wa umma watakaonufaika watazilipia kwa njia za mikopo ya polepole ambapo muda wa malipo umewekwa kuwa miaka 25.

Usalama

Waziri huyo anayewajibikia usalama wa ndani kwa sasa alisema kuwa kitita kingine ili kujumuisha Sh5 bilioni kitatumika katika ujenzi na ukarabati wa barabara za kaunti hiyo.

“Pia tutatumia pesa zingine katika uimarishaji wa utupaji majitaka, kuweka taa katika barabara za kaunti hiyo na pia kudhibiti maeneo hatari ya mafuriko,” akasema.

Mitaa ambayo itapewa kipaumbele ni Bandani, Manyatta Arabs, Nyalenda na Obunga ambapo ukarabati kuboresha mitaa ya mabanda utagharimu kitita cha Sh1.2 bilioni.

Alisema mradi huo wa uimarishaji mitaa duni utashirikishwa chini ya ufadhili wa pamoja wa serikali na Benki ya Dunia (WB).

Aidha, shirika la ujenzi wa nyumba la kiserikali (NHC) litazindua mradi wa kujenga 700 katika eneo Kanyakwar, zote kwa gharama ya Sh2.6 bilioni na pia mradi mwingine wa kutoa hatimiliki za mashamba uzinduliwe.

Ngome ya Rais Kiambu imechoshwa na handisheki – Kuria

Na PETER MBURU

MBUNGE wa Gatundu Kusini Moses Kuria sasa anadai kuwa wakazi wa Kaunti ya Kiambu ambako ni ngome ya Rais Uhuru Kenyatta hawataki lolote kuhusu ‘handisheki’ ya Rais na kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga

Mbunge huyo alisema kuwa wakazi hao wanaipinga vikali na kufanya yote wawezayo kuimaliza, maneno ya kushangaza ikizingatiwa kuwa ngome ya Rais ndiyo inatarajiwa kuwa ya kwanza kumuunga mkono.

Katika ujumbe kwenye akaunti yake ya Facebook Jumatatu, Bw Kuria alisema kuwa alizomewa na wakazi hao baada ya kuwasilisha mapendekezo yake kwa timu ya BBI ambayo imekuwa ikizunguka nchini kupokea maoni ya Wakenya.

Alisema japo amekuwa akiunga mkono handisheki, wakazi wa Kiambu na eneo lake, nyumbani kwa Rais hawaitaki.

“Ijumaa niliwasilisha maoni yangu kwa timu ya BBI Kiambu. Jumapili ilikuwa siku mbaya kwangu katika hafla uwanja wa Ruiru wakati watu wa eneo langu walinituma na ujumbe wazi. Hawataki lolote kuhusu handisheki,” akasema Bw Kuria.

Akijitetea kuwa yeye ni shabiki wa muafaka huo wa Rais na Bw Odinga, aliendelea kusema kuwa kwa wakazi wa Kiambu haijawafurahisha.

“Wanaipinga kabisa na wanaikashifu,” akasema, japo katika ujumbe wake akijaribu kuwarai wakazi kutokata tamaa mapema.

Hata hivyo, mbunge huyo alisema ni jukumu la viongozi kuwaeleza watu kuhusu maana halisi ya handisheki, jambo ambalo amekuwa akilalamika kutoka mbeleni kuwa hata viongozi hawaielewi.

“Tusikate tamaa wakati huu. Tufanye juhudi kuwaeleza kuwa handisheki ni kitu kitakachotufaa siku za usoni,” akasema.

Kuria ashangaa handisheki bado haimtoi kortini

RICHARD MUNGUTI na VALENTINE OBARA

MBUNGE wa Gatundu Kusini, Bw Moses Kuria ameshangaa kwamba kesi yake kuhusu uchochezi dhidi ya Kiongozi wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga ingali inaendelea licha ya kuwepo kwa handisheki.

Jana Bw Alexander Mathenge ambaye ni mtaalamu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano katika Mamlaka ya Mawasiliano Kenya (CA) alifika katika Mahakama ya Milimani, Nairobi kutoa ushahidi dhidi ya mbunge huyu katika kesi hiyo inayohusu uchochezi na uhasama wa kijamii.

“Nilitumiwa video kutoka kwa DCI nikaagizwa kuchunguza mienendo ya Kuria na matamshi yake ambayo yaliaminika kuchochea ghasia za kijamii na kumtusi Raila. Nilikagua video yote nikatambua kwamba, kwa maoni yangu, Bw Kuria alikiuka sheria aliposema watu waliompigia Raila kura 70,000 eneo la Kati wasakwe, na wakazi wa eneo la Kati wasikubali kutolewa nyama mdomoni,” akasema Bw Mathenge.

Matamshi hayo yalidaiwa kutolewa katika eneo la Wangige, Kiambu wakati Bw Kuria alipohutubia umma mnamo Septemba 19 baada ya kuharamishwa kwa ushindi wa Rais Kenyatta na Mahakama ya Juu.

Upande wa mashtaka umefunga kesi na Bw Kuria atajitetea Juni 27, ambapo anatarajiwa kuomba korti imwachilie huru. Alikuwa amekanusha madai hayo na yuko nje kwa dhamana.

Awali Jumatatu, Bw Kuria alielekea kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook kueleza hisia zake kuhusu masaibu hayo yanayomkumba licha ya kuwepo muafaka kati ya Bw Odinga na Rais Uhuru Kenyatta, almaarufu handsheki.

“Mwaka mmoja na robo baada ya handsheki, narejea katika Mahakama ya Milimani itakayosikiliza kesi ambapo nimeshtakiwa kwa kumwambia Raila Odinga “wembe ni ule ule” kabla ya marejeo ya uchaguzi wa urais Oktoba 26, 2017. Mungu nisaidie,” akasema, huku akijitaja kuwa ‘mfungwa wa mwisho wa kisiasa’.

Wakati Bw Odinga na Rais Kenyatta walipoweka muafaka wa maelewano mnamo Machi 9, 2018, taifa lilitazamia kusahau yaliyopita na hivyo basi huenda Bw Kuria naye alitarajia kesi hiyo ingeondolewa.

Kwenye ushahidi wake, Bw Mathenge alieleza mahakama jinsi Bw Kuria alivyotoa matamshi machafu tusiyoweza kuchapisha katika gazeti hili, dhidi ya Bw Odinga na mkewe Ida.

Video pia ilichezwa kortini upande wa mashtaka ukitaka kuthibitisha kuwa mbunge huyo alizua madai kwamba Bw Odinga alitoa watoto wake kafara na kamwe hawezi kuaminiwa na watoto wa Kenya akiwa rais.

Mapema Februari kesi hiyo iliposikilizwa, Inspekta Mkuu Kassim Baricha aliambia mahakama kwamba matamshi ya Bw Kuria yalikuwa na uwezo wa kusababisha taharuki nchini.

Bw Odinga alisusia uchaguzi wa marudio wa urais ambapo mgombea mwenza wake alikuwa ni Kiongozi wa Chama cha Wiper, Bw Kalonzo Musyoka chini ya Muungano wa NASA.

Uchaguzi huo wa marudio uliandaliwa baada ya Mahakama ya Juu ikiongozwa na Jaji Mkuu David Maraga, kufutilia mbali ushindi wa Rais Kenyatta katika uchaguzi uliofanywa Agosti 2017, kwa msingi kwamba Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ilikiuka sheria na hivyo kulazimu uchaguzi huo usiwe huru na wa haki.

Hatua ya Bw Odinga kususia uchaguzi ulimfanya Rais Kenyatta kuibuka mshindi tena, kwani hakuwa na upinzani mkali.

Barua kwa Wakenya: Amkeni mlete mageuzi

Na WANDERI KAMAU

MNAMO Desemba 1795, aliyekuwa mtawala wa Ufaransa mwenye uwezo mkubwa sana wa kijeshi, Napoleon Bonaparte, aliandika mojawapo ya barua maafuru sana za kimapenzi katika historia.

Alimwandikia Bi Josephine de Beauharnais, mwanamke ambaye aliibukia kumpenda sana, licha ya kumzidi umri kwa miaka sita.

Napoleon alionekana kutobabaishwa na tofauti hiyo, lakini alizidiwa na mapenzi aliyokuwa nayo kwake.

Akaandika: “Mpenzi wangu Josephine, unajua vile huwa unaifurahisha roho yangu? Huwa naanza kuhisi penzi lako kabla ya adhuhuri…natamani kukutana nawe. Hadi tutakapokutana tena, nakubusu mara elfu moja mpenzi wangu.”

Alimwandikia barua nyingi. Nyingi sana. Hatimaye alifanikiwa kuiteka roho yake na kumwoa, ingawa walitengana baadaye.

Vivyo hivyo, penzi hilo aliloonyesha Bonaparte kwa Josephine, ndilo nililo nalo kwa Wakenya wenzangu.

Maoni haya ni barua maalum kwao, kuwafahamisha kuwa Kenya imetekwa. Wao ni mahabusu wa kimfumo ambapo lazima wajikomboe.

Tu mahabusu wa ‘falme’ mbili kuu za kisiasa, ambazo lengo lake ni kuhakikisha zinaendeleza ukiritimba wao dhidi ya wananchi.

Lengo kuu la ‘abrakadabra’ za kisiasa zinazoendeshwa na familia za Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM, Raila Odinga ni kuendeleza udhibiti wao wa siasa za Kenya kupitia ushirikiano maalum uitwao “handisheki.”

Je, manufaa ya mwafaka huo yamekuwa yapi kwa mamilioni ya Wakenya? Katika eneo la Mlima Kenya, ambako ndiko ngome ya Rais Kenyatta, wakazi wanalia. Kilio chao kinafanana na kile cha Wayahudi walipolengwa na Adolf Hitler wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.

Kilimo, ambacho ndicho kitegauchumi kikuu cha wakazi, kimesambaratika. Ahadi zote walizopewa wakati wa kampeni zimegeuka hewa. Baadhi ya wakazi hata wamekaidi miiko na kung’oa mazao yao kama majanichai. Wakulima wa kahawa, miraa na pareto wametengwa. Kuna Kilio Kikuu Mlima Kenya.

Katika eneo la Nyanza, ambako ndiko ngome kuu ya Bw Odinga, hali ni kama iyo hiyo. Vilio vimegeuka chakula kwa maelfu ya wakazi waliojitoa mhanga ‘kumtetea’ Odinga kwa kila hali. Mamia walijeruhiwa, kuuawa na hata kufurushwa makwao. Amewasaliti kwa ‘kuungana’ na Rais Kenyatta, aliyechorwa kama ‘hasimu’ wa kisiasa wa Bw Odinga. Walisahau kuwa wao ni marafiki.

Wote waliwahadaa wafuasi wao.

Kilicho muhimu sasa kwa Wakenya ni kujikomboa. Amkeni! Amkeni kujitanzua kutokana na hadaa hii ya kisiasa. Amkeni kutetea mustakabali wa vizazi vyenu. Amkeni kuwachagua viongozi watakaojali maslahi yenu. Amkeni!

Nasema haya kwa mapenzi ya kweli; mapenzi aliyoonyesha Bonaparte kwa mpenziwe, Josephine au mapenzi aonyeshayo mama kwa mtoto wake.

Hata hivyo, taswira ya kisiasa inayoendelea kujengwa ielekeapo 2022 inaashiria wazi kuwa njama kuu iliyopo ni kwa familia hizo mbili kutumia ushawishi wake kuwafadhili viongozi watakaolinda maslahi yao. Hesabu ya Mkenya haipo!

Wakenya wenzangu, 2022 ni nafasi ya pekee ya kuzikaidi familia hizi mbili na kuanza mapambazuko mapya ya kisiasa. Amkeni!

akamau@ke.nationmedia.com

UCHAMBUZI: Handisheki yakanganya viongozi wa ODM

Na CHARLES WASONGA

MIKINZANO ya kimawazo inayodhihirika ndani ya ODM katika siku za hivi karibuni kuhusiana na baadhi ya sera za serikali imeonyesha kuwa siri za muafaka kati ya kiongozi wake Raila Odinga na Rais Uhuru Kenyatta zinakanganya viongozi wake.

Tangu Machi 9, 2018, wawili hao walipotia saini muafaka huo – maarufu kama handisheki – ambao ulileta utulivu katika ulingo wa siasa nchini, baadhi ya wabunge wa ODM wamekuwa wakionekana wakipinga baadhi ya maongozi ya serikali.

Miongoni mwao ni mwenyekiti John Mbadi na Seneta wa Siaya James Orengo, ambaye ni mwandani wa karibu wa Bw Odinga.

Kulingana na wadadisi, wabunge hao wameonekana kuchanganyikiwa kuhusu iwapo handisheki ilimaanisha kuwa wataunga mkono mipango, sera na maongozi yote ya serikali ndani na nje ya bunge.

Vilevile, huenda hawafahamu iwapo baada ya handisheki wanapaswa kuendelea kuvumisha azma ya Bw Odinga ya kuingia Ikulu au wanapaswa kusubiri hadi miezi kabla ya uchaguzi mkuu.

Na baadhi yao wamekanganyika kiasi kwamba hawafahamu kama kiongozi wao bado atawania urais mwaka 2022 au ataunga mkono mgombeaji mwingine kutoka ndani ya ODM, chama kingine au muungano wa kisiasa ambao huenda ukabuniwa.

Kutoa nafasi

Isitoshe, wabunge hao wanaonekana kutofahamu kama muafaka huo ulifaa kutoa nafasi kuandaliwe kura ya maamuzi ili kubadili mfumo wa uongozi kwa kubuniwa wadhifa wa Waziri Mkuu mwenye mamlaka.

Hali hii ya kukanyanganyikiwa kwa wabunge wa ODM na maafisa wake, ilidhihirika hivi majuzi pale Mbw Mbadi na Orengo walipinga uzinduzi wa noti mpya.

Walidai kuwa uwepo wa picha ya sanamu ya mwanzilishi wa taifa hili Mzee Jomo Kenyatta katika noti hizo mpya ni kinyume cha Katiba ambayo hairuhusu sarafu za Kenya kuwa na picha ya mtu yeyote.

Katibu Mkuu Edwin Sifuna pia alipinga noti hizo kwa misingi iyo hiyo.

Lakini msimamo huo ulipingwa vikali na wabunge wenzao Mbw Junet Mohammed (Suna Mashariki), T. J Kajwang’ (Ruaraka), Samuel Atandi (Alego Usonga) na Opiyo Wandayi (Ugunja).

Kiranja

Bw Mohammed ambaye pia ni kiranja wa wachache katika bunge la kitaifa alitaja suala hilo la uwepo wa picha ya Mzee Kenyatta kwenye noti kama “lisilo na maana”.

“Sisi tunaunga mkono noti mpya. Madai ya Mbadi na Orengo na wengineo kwamba noti hizo zinakiuka Katiba ni yao kama watu binafsi na sio ya chama chetu cha ODM. Kwa hivyo lalama zao hazina maana yoyote,” akasema.

Lakini siku mbili baadaye Bw Mbadi, ambaye ni kiongozi wa wachache katika bunge la kitaifa alibadili msimamo huo na kusema kuunga mkono noti.

Kati kile alichodai ni “msimamo halisi wa chama” Mbunge huyo wa Suba Kusini aliishauri serikali kuhakikisha kuwa noti zitakachapishwa siku zijazo haziwekwe picha za mtu yeyote. Naye Bw Orengo, ambaye pia ni kiongozi wa wachache katika Seneti aliamua kukimya.

Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Profesa Macharia Munene anasema hatua ya vigogo hao wa ODM kubadili msimamo kuhusu uhalali wa noti hizo mpya kulichangiwa na kiongozi wao Bw Odinga.

“Ni wazi kuwa “Baba” aliwaamuru wabunge hao kuunga mkono sarafu hizo mpya kwa ili kusionekane kwamba chama kinachukua msimamo kinzani na ule wa serikali ya Jubilee katika kipindi hiki cha handisheki,” anasema.

“Lakini ni muhimu kuzingatia kwamba taswira hii inachangiwa na hali kwamba wabunge hawa hawaelewi hasa siri fiche ndani ya handisheki. Hawajui kama bado wanafaa kuendelea kutekeleza wajibu wao wa kuhoji utendakazi wa serikali kama wabunge wa upinzani au wanafaa kuunga mkono sera na maongozi yote ya Jubilee.

“Ni wazi kuwa hawajapa ufafanuzi huu kutoka kwa Bw Odinga. Hii ndio maana hata majuzi walionekana kutoa matakaa ya Rais na kiongozi wao kuhusu kura ya maamuzi wakisema handisheki haitakuwa na maana yoyote ikiwa Katiba haitafanyiwa mabadiliko,” anasema Profesa Munene ambaye ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha USIU.

Na huku akionekana kulandana kifikra na Profesa Munene kuhusu suala hilo wakili James Mwamu anamshauri Bw Odinga kuandaa kikao na wabunge na viongozi wakuu wa ODM ili awape ufahamu kuhusu dhima kuu ya handisheki.

“Hii ni kwa sababu misimamo ya kinzani inayochukuliwa na wabunge wa ODM kuhusu sera za serikali ya Jubilee inaonyesha wazi kwamba kuna maafikiano fulani kati ya Bw Odinga na Rais Kenyatta ambayo hawajuzwa,” anasema.

Itakumbukwa kuwa wiki chache baada ya Machi 9 Bw Mbadi aliwasilisha hoja maalum katika bunge la kitaifa akisema ODM imekubaliana kwa kauli moja kuunga mkono ajenda za serikali ya Jubilee ndani na nje ya bunge.

Alitoa mfano, wa vita dhidi ya ufisadi ambayo ni mojawapo ya masuala tisa ambayo Rais Kenyatta na Odinga walikubaliana kuendeleza kupitia handisheki katika jitihada zao za kupalilia umoja na maridhiano ya kitaifa.

Hata hivyo, Bw Mbadi alifafanua kuwa wabunge wa chama hicho wataendelea kutekeleza majukumu yao kama wabunge wa upinzani kwa kuhoji maovu yanayoendelezwa na maafisa wa serikali.

Lakini wabunge wa vyama tanzu katika NASA kama vile Wiper, ANC na Ford Kenya walifasiri kauli hiyo ya Mbadi kumaanisha kuwa ODM kimehama upinzani na kujiunga na mrengo wa serikali bungeni.

Lakini licha ya Mbadi kudai kuwa “tutaunga serikali huku tukiendelea kuwa upinzani” Rais Kenyatta alipozuru Kisumu Desemba 2018 alitangaza kuwa Bw Odinga “yuko ndani ya serikali”.

Na akiongea katika mkutano wa kujadili maendeleo katika nyanja ya ujenzi wa miundombinu barani Afrika katika ukumbi wa Bomas, Nairobi, Rais Kenyatta alifichua kuwa yeye hushauriana na Bw Odinga kila mara kuhusiana na masuala ya kuendesha serikali.

Isitoshe, mawaziri wa serikali wamekuwa wakimtembelea Bw Odinga katika afisi zake zilizoko jumba la Capitol Hill, Nairobi kwa mashauriano kuhusu masuala mbalimbali ya serikali.

Hii, kulingana na Profesa Munene, imesababisha Bw Odinga kuonekana kuwa sehemu ya serikali wala sio kiongozi wa upinzani kama alivyotambuliwa kabla ya handisheki.

“Huenda siri ambayo akina Mbadi, Orengo, Sifuna na wengine hawajaelewa ni kwamba handisheki ilimweka kiongozi wao katika kitovu cha Serikali ya Jubilee kiasi kwamba hawezi kuipinga kwa njia yoyote,” anasema.

HANDISHEKI: Raila awaka

Na SAMWEL OWINO, PETER MBURU na VALENTINE OBARA

KIONGOZI wa chama cha ODM, Raila Odinga, amekasirishwa na jinsi wakuu wa chama hicho wameanza kuchukua misimamo inayokinzana na ya Serikali ya Jubilee.

Masuala ambayo yamemshikisha moto Bw Odinga ni hatua ya vigogo wa ODM kupinga uzinduzi wa noti mpya, pamoja na kusema kuwa handisheki haina maana iwapo referenda haitafanyika kufikia Machi 2020.

Duru za kuaminika ziliambia Taifa Leo kwamba Bw Odinga, ambaye alikuwa Uingereza aliwasiliana na baadhi ya viongozi wa chama hicho na kuwaamrisha waunge mkono uamuzi wa serikali kuzindua noti mpya.

Ni amri hiyo ambayo iliwafanya viongozi hao kuandaa kikao cha wanahabari jijini Nairobi jana na kubadilisha kauli yao kuhusu noti hizo.

Hapo wikendi, baadhi ya viongozi akiwemo Mwenyekiti John Mbadi, Katibu Mkuu Edwin Sifuna na Kiongozi wa Wachache katika Seneti James Orengo walipinga noti hizo kwa msingi kuwa Katiba hairuhusu sarafu za Kenya kuwa na sura ya mtu yeyote.

“Kiongozi wa chama anataka kuwe na msimamo mmoja chamani kuhusu noti mpya. Wanachama wetu wamekuwa wakitoa maoni yanayotofautiana kuhusu suala hilo,” mwanachama mwenye mamlaka makubwa katika chama hicho aliyeomba asitajwe jina aliambia Taifa Leo.

Abadili msimamo

Jumanne, Bw Mbadi aliye pia Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kitaifa alilazimika kubadili msimamo wake wa awali.

Kwenye kikao cha habari alichoitisha katika makao ya Bunge, Mbunge huyo wa Suba Kusini alithibitisha kuwa vigogo wa chama walishauriana ndipo akapewa jukumu la kutoa msimamo halisi wa chama kuhusu suala hilo.

Kulingana naye, uamuzi wa ODM kuchukua msimamo huo ulitokana na kuwa utasaidia kukabiliana na ufisadi kwa kuondoa pesa haramu mikononi mwa matapeli wanaopora pesa za umma na kuzificha manyumbani mwao.

Wanachama kadhaa pia wameanza kutilia shaka umuhimu wa handsheki hiyo kwani kulingana nao, Bw Odinga na Rais Kenyatta hawajaonyesha nia kikamilifu ya kuwezesha marekebisho ya Katiba kufanikishwa haraka iwezekanavyo.

Ushirikiano wa Bw Odinga na Rais umeonekana kufanya usemi wake ufifie kuhusu masuala mbalimbali.

Kwa mfano, wakati chama kilipokuwa kikiendeleza juhudi za kumwadhibu Mbunge wa Malindi, Bi Aisha Jumwa, ilifichuka Bw Odinga alijaribu kuingilia kati kumwokoa lakini hatua zake hazikufua dafu.

Vilevile, usemi wake ulitiliwa shaka zaidi kwenye uchaguzi mdogo wa Ugenya wakati Chris Karani wa ODM aliposhindwa na Bw David Ochieng wa MDG.

Handisheki haina maana bila mageuzi ya katiba – ODM

Na RUTH MBULA

VIONGOZI wa Chama cha ODM wamewapa Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wao Bw Raila Odinga makataa ya hadi Machi 2020 kuandaa kura ya maamuzi. Kulingana na viongozi hao waliojumuisha wakuu wa chama hicho, handisheki haitakuwa na maana yoyote ikiwa kura ya maamuzi haitafanywa kufikia wakati huo.

Walieleza wasiwasi wao kuwa kufikia sasa, Rais Kenyatta na Bw Odinga hawajaonyesha nia ya kuhimiza wabunge kujumuisha suala la kura ya maamuzi kwenye bajeti ya mwaka wa 2019/2020.

Vilevile, wametilia shaka hatua zinazopigwa na jopo maalumu lililoundwa na wawili hao kukusanya maoni ya wananchi kitaifa kuhusu marekebisho ya katiba.

Kwa kauli moja, Kiongozi wa Wachache katika Seneti James Orengo, Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kitaifa John Mbadi aliye pia Mwenyekiti wa ODM, na Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna walisema ni kura ya maamuzi pekee ambayo itadhihirisha kwamba handisheki ilikuwa ya kweli.

Viongozi hao walikuwa wakizungumza katika eneo la Rongo, Kaunti ya Migori walipokuwa wakiongoza mkutano wa kuchangisha fedha za kusaidia Kanisa Katoliki la St Martin De Pore.

“Ili kuonyesha kwamba handisheki kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga ilikuwa ya kweli, basi serikali haina budi kujumuisha kura ya maamuzi katika bajeti ya 2019/2020,” akasema Bw Orengo.

“Fedha za kuendesha kura ya maamuzi haziwezi kupatikana bila kuweka mipango kabambe. Ninachosema ni kwamba wabunge wanafaa kuongeza kura ya maamuzi katika bajeti ya mwaka wa fedha utakaoanza Julai mwaka huu,” akasema Bw Orengo.

Alisema Wakenya wanangojea kura ya maamuzi kwa hamu na ghamu na viongozi hawana budi kuwapa mwelekeo.

Bw Mbadi alimtaka Bw Odinga na Rais Kenyatta kuwahimiza wabunge kujumuisha kura ya maamuzi katika bajeti.

“Rais Kenyatta na Bw Odinga wanafaa kuwaagiza wabunge wao kuhakikisha kuwa fedha za kura ya maamuzi zinajumuishwa katika bajeti,” akasema.

Kwa upande wake, Bw Sifuna alisema: “Ninaomba kwa unyenyekevu mkubwa, Rais atende yale anayosema. Amekuwa akisema anataka kukomesha jinsi mshindi wa urais hunyakua mamlaka yote serikalini. Lazima tubadilishe mbinu zetu za kisiasa.”

Bw Odinga amekuwa akiwataka Wakenya kujiandaa kwa ajili ya mabadiliko ya katiba kupitia kura ya maamuzi.

Kwa upande mwingine, Rais Kenyatta hajatangaza wazi kuhusu kura ya maamuzi lakini matamshi yake katika hafla mbalimbali yanaashiria kwamba anaunga mkono mabadiliko.

Alipokuwa akihutubia Waislamu katika msikiti wa Jumia jijini Nairobi wiki jana, Rais Kenyatta alisema ni mabadiliko ya katiba pekee ambayo yatawezesha sherehe ya mwisho wa mfungo wa Ramadhan, Eid-Ul Fitr kuwa sikukuu ya kitaifa kila mwaka.

Raila apigia debe handisheki Uingereza

Na LEONARD ONYANGO

KIONGOZI wa ODM Raila Odinga ametumia ziara yake nchini Uingereza Jumatatu kupigia debe handisheki baina yake na Rais Uhuru Kenyatta.

Bw Odinga alisema kamati aliyobuni pamoja na Rais Kenyatta kukusanya maoni kutoka kwa wananchi kuhusu jinsi ya kumaliza uhasama wa kikabila nchini, maarufu BBI, itatoa mapendekezo yatakayosaidia kushughulikia dhuluma za kihistoria.

Alisema dhuluma za kihistoria zilizochochea vurugu za baada ya uchaguzi wa 2007, hazijapatiwa ufumbuzi kufikia sasa.

“Kofi Annan aliyetumwa kuja kunipatanisha na Rais Mwai Kibaki ili kumaliza vurugu alituhimiza kushughulikia dhuluma za kihistoria kama njia mojawapo ya kuepuka ghasia za uchaguzi katika siku za usoni.

‘Lakini kufikia sasa kuna mambo mengi ambayo hayajashughulikiwa na nina imani kamati ya BBI itatoa mapendekezo yatakayotusaidia kutafutia ufumbuzi dhuluma hizo,” akasema Bw Odinga aliyekuwa akihutubia wasomi katika taasisi ya Chatham House, Uingereza wakati wa kongamano la kukumbuka mafanikio ya mafanikio ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Kimataifa (UN) Kofi Anna.

Wakati wa hotuba yake Bw Odinga aliibua hisia kali kuhusu mauaji ya kinyama yaliyotokea baada ya uchaguzi wa 2007 ambapo zaidi ya watu 1,300 waliangamia na wengine maelfu kupoteza makao.

“Nilikuwa naongoza katika uchaguzi kwa zaidi ya kura milioni 2 lakini ilipofika jioni televisheni ziliagizwa kutopeperusha matokeo.chantha

“Muda mfupi baadaye, tuliambiwa kwamba mpinzani wangu ameibuka mshindi. Hapo ndipo Wakenya waligeukiana na kuanza kuuana. Kwa mfano, watu waliokuwa wamejisiti kanisani waliteketezwa kwa moto,” akasema.

Bw Odinga alielezea juhudi za Annan aliyeaga dunia mnamo, Agosti 2018, katika kumpatanisha na rais Kibaki ambaye sasa amestaafu.

“Vurugu zilipozuka nilipokea simu kutoka kwa Waziri Mkuu wa Uingereza Gordon Brown aliyeniuliza ikiwa nilikuwa tayari kupatanishwa,” akasimulia.

Waziri Mkuu wa zamani alisema kuwa Annan alikuwa amekataliwa na upande wa Bw Kibaki.

“Ilibidi waziri mkuu wa Uingereza Bw Brown kuingilia kati ndiposa upande wa Rais Kibaki ukamkubali,” akasema Bw Odinga.

Waziri Mkuu wa zamani alisema, Rais Kibaki alishinikizwa kukubali kuunda serikali ya mseto iliyomaliza mapigano ya kikabila.

“Watu tuliokuwa tumeteua kutuwakilisha katika meza ya mazungumzo walikosa kuafikiana. Hapo ndipo Annan alisisitiza kwamba alitaka kukutana na mimi pamoja na Rais Kibaki.

“Tulikutana katika afisi ya rais (Jumba la Harambee) na hapo ndipo Kibaki alilazimishwa kukubali mambo ambayo kikosi chake kilikuwa kimekataa kuhusiana na majukumu ya waziri kuu,” akasema.

MSAMAHA: Unafiki katika maombi

Na BENSON MATHEKA

VIONGOZI wanapokutana Alhamisi kwa maombi ya kitaifa ya mwaka huu katika hoteli ya Safari Park, Nairobi, unafiki wao unajitokeza kutokana na kukosa kutimiza msamaha waliotangaza hadharani kwenye sala za 2018.

Kwenye maombi ya mwaka uliopita, Rais Uhuru Kenyatta aliongoza naibu wake William Ruto, Kiongozi wa ODM Raila Odinga na Kalonzo Musyoka wa Wiper kukumbatiana na kutangaza kusameheana.

Hatua hiyo ilileta matumaini makubwa kuwa hatimaye wangeshirikiana kuleta umoja wa kitaifa, kukomesha siasa za chuki, kupigana na ufisadi na kujenga taifa lenye ustawi.

Wakisimama mbele ya wageni walioalikwa na kutazamwa moja kwa moja na Wakenya kwenye televisheni, viongozi hao waliahidi kutuliza joto la kisiasa hadi 2022, kuunganisha Wakenya, kuunga mkono vita dhidi ya ufisadi na kuhubiri umoja wa kitaifa.

Kilele cha maombi hayo kilikuwa ni vigogo hao kuombana msamaha hadharani na kukumbatiana kwa makosa waliyotendeana na kuwatendea Wakenya wakati wa chaguzi mbili za urais 2017 .

“Tulishiriki kampeni kali yenye ushindani, kuitana majina na kurushiana lawama za kila aina. Lakini hapa leo, mbele ya watu hawa na Wakenya kwa jumla, ninaomba msamaha bila masharti,” Rais Kenyatta alimwambia Bw Odinga

Naye Bw Odinga aliomba msamaha kwa niaba ya muungano wa NASA na tangu wakati huo wawili hao wanaonekana kudumisha ahadi yao.

“Kwa niaba yangu binafsi na chama chetu cha Jubilee, na kufuata nyayo za viongozi hawa wa kuigwa (Rais Kenyatta na Bw Odinga), ndugu yangu Stephen, ninakuomba msamaha,” Dkt Ruto naye alisema na kuwakumbatia Bw Musyoka na Bw Odinga.

Lakini mara baada ya kuteremka jukwaani, Dkt Ruto na Bw Odinga walisahau walikuwa wamesameheana na mara moja pamoja na wandani wao wakaendeleza malumbano ya kisiasa.

Tangu hapo wawili hao wamekuwa wakiongoza washirika wao kushambuliana vikali hasa kuhusu vita dhidi ya ufisadi na mageuzi ya kikatiba.

Tofauti zao zimezidi huku Dkt Ruto akimlaumu Bw Odinga kama tapeli wa kisiasa anayetaka kujiunga na serikali kupitia mlango wa nyuma na kuvuruga chama cha Jubilee.

“Hatutakubali propaganda katika serikali. Waliungana nasi kubadilisha nchi lakini nia yao ni kuvunja chama cha Jubilee na serikali. Tunawaambia kwamba tunawatazama,” Bw Ruto amekuwa akidai.

Uhusiano wa Rais Kenyatta na naibu wake pia umekuwa baridi tangu mwafaka wa handisheki mwaka jana.

Bw Odinga na washirika wake naye hajaachwa nyuma kumshambulia Dkt Ruto na wamekuwa wakieneza kampeni ya kutaka kumwonyesha Naibu Rais kama anayetatiza vita dhidi ya ufisadi.

Kwenye maombi ya kitaifa ya 2018, ambapo waliombana msamaha, Rais Kenyatta alisisitiza kuwa vita hivyo havilengi jamii moja, jambo ambalo Dkt Ruto na washirika wake wanasisitiza.

Uhasama wa kisiasa umezidi hivi kwamba wanasiasa wa upinzani wanaoshirikiana na Bw Ruto wamekuwa wakionywa na hata kutimuliwa katika vyama vyao.

Kulingana na Pasta Sam Mboto wa Great Mission Church, malumbano ya viongozi hawa yanaweza kuzua uhasama na chuki za kijamii nchini.

“Viongozi wanapaswa kuwa mfano mwema wa kuigwa na wanaoongoza. Wakitoa msamaha hewa, wafuasi wao watawaiga,” asema.

HANDISHEKI: Kisumu kupata taa za trafiki miaka 118 baadaye!

Na JUSTUS OCHIENG

KISUMU itapata taa za trafiki kwa mara ya kwanza kabisa, miaka 118 tangu jiji hilo la eneo la Nyanza kujengwa, ishara ya matunda ya handisheki kuzidi kuenea katika ngome za kiongozi wa chama cha ODM, Bw Raila Odinga.

Taa hizo zitatumika kudhibiti msongamano wa magari katika miungano ya barabara na vivuko vya wanaotembea kwa miguu.

Aidha, taa hizo za trafiki zitawekwa miaka 18 tangu rais mstaafu Daniel Arap Moi kutangaza rasmi Kisumu kuwa mji.

Mnamo 2001, Kisumu iliadhimisha miaka 100 tangu kuanzishwa kwake katika sherehe ya kufana iliyohudhuriwa na marais Daniel Moi, Yoweri Museveni wa Uganda na mstaafu Benjamin Mkapa wa Tanzania.

Ni katika maadhimisho hayo ambapo Moi alitangaza Kisumu kuwa mji.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Barabara Kuu (KeNHA) Bw Peter Mundinia, alisema jana kuwa taa hizo zitawekwa katika miungano mitatu mikuu kwenye barabara ya Kisumu-Kakamega.

Bw Mundinia alisema kando na kuimarisha miundomsingi na kujenga barabara hiyo kuu ili iwe ya pande mbili, kumekuwa na haja ya kuweka taa za trafiki ili kuleta usalama barabarani kwani hii itasaidia kupunguza ajali.

Alieleza: “Kuna vivuko vya wanaotembea kwa miguu na pia miungano ya magari kuvuka kutoka upande mmoja hadi mwingine, hivyo taa zitahakikisha miundomsingi hii inatumika vyema zaidi.”

Mkurugenzi huyo alisema kampuni ya NAS International ndiyo imegawiwa kandarasi ya kuweka taa hizo kutoka kwa kampuni ya SBI International Holdings ambayo ndiyo inajenga barabara ya pande mbili ya Kisumu-Nyang’ori.

Afisa Mkuu Mtendaji wa NAS Bw Nicholas Airo alisema taa hizo za trafiki zitawekwa katika mizunguko ya Kisumu Boys, Patels na Kondele.

“Tayari tumeanza kuweka taa Patels na tutaendelea katika miungano hiyo mingine,” Bw Airo aliambia Taifa Leo.

Aliongeza kuwa watafanya hamasisho kwa umma na shuleni kwa wanafunzi pamoja na kukutana na wadau wote wa uchukuzi ili kuwahamasisha kuhusu matumizi ya taa za trafiki.

Handisheki imewazima wanaharakati, walikuwa wakimtegemea Raila – Wasomi

Na PETER MBURU

WASOMI na viongozi wa nyanja zingine wamedai kuwa mashirika ya kutetea haki nchini yamekosa nguvu baada ya kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga kuanza kushirikiana na Rais Uhuru Kenyatta.

Wakizungumza mawazo yao katika kikao cha kujadili nafasi ya mashirika ya uanaharakati tangu muafaka wa Rais na Bw Odinga mnamo Machi 2018, viongozi na wasomi walisema kuwa mashirika yalikuwa yamezoea kubebwa na upinzani badala ya kujijenga yenyewe, na hivyo wakati upinzani uliamua kushirikiana na serikali yakabaki kama yatima.

Vilevile, wataalam hao walisema kuwa hali ya viongozi wa mashirika hayo kuwa na tamaa ya kupata pesa za ufadhili kutoka mashirika ya kimataifa badala ya kutetea wanyonge ilisababisha Wakenya kukosa imani nao, ndiposa kwa sasa hata yakiandaa maandamano hakuna anayejitokeza.

Kikao hicho cha muungano wa mashirika ya kijamii kwa jina ‘Uwazi Consortium’ kiliandaliwa Jumatatu, aliyekuwa naibu spika wa bunge Farah Maalim, Afisa Mkuu Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki Afrika Mashariki Joy Mdivo, Prof Macharia Munene wa chuo kikuu cha USIU na Dkt Duncan Ojwang wa Chuo Kikuu cha Africa Nazarene, wakiongoza mazungumzo.

“Mashirika ya kijamii yalikuwa yakibebwa na upinzani, ndiposa muafaka iliyamaliza kabisa. Yalidhani kuwa yana nguvu lakini sasa yamejua yalikuwa kama nyani anayebebwa na mamba kuvuka mto,” akasema Dkt Ojwang.

Bi Mdivo alisema hali ya mashirika hayo kukosa uhuru wa kujiamulia wanachotaka kwa sababu ya tamaa ya pesa za ufadhili imechangia pakubwa kwa hali yao kujimaliza.

“Hatukuwa na mashirika ya kijamii yenye msimamo ila yalikuwa tu ya kupaza sauti kuhusu mawazo ya watu fulani. Sharti yaanze kujijenga kutoka chini sasa na yalenge kuleta mabadiliko wala si kufurahisha mtu,” Prof Munene naye akasema.

Ukambani walia matunda ya handisheki hayajawafikia

Na PIUS MAUNDU

SIKU chache baada ya kiongozi wa ODM kuzindua miradi kadhaa katika ngome yake ya Nyanza kutokana na muafaka kati yake na Rais Uhuru Kenyatta, baadhi ya viongozi wa Ukambani sasa wanalalamika kuwa eneo hilo halijafaidi kutokana na maelewano hayo.

Hii ni licha ya kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka kutangaza kuwa anaunga mkono handisheki hiyo na kuahidi kufanya kazi kwa karibu na Rais Kenyatta.

Gavana wa Kitui Charity Ngilu na Seneta wa Makueni Mutula Kilonzo Junior wanasema kuwa Ukambani wamefaidi kwa kiwango kidogo zaidi kutokana muafaka huo ikilinganishwa na Nyanza.

“Mbali na watu wetu wachache kuteuliwa katika nyadhifa ndogo serikalini, eneo hilo halijavuna matunda yoyote kimaendeleo licha ya kushirikishwa katika handisheki,” Bi Ngilu akasema Jumamosi.

Aliunga mkono kauli ya Seneta Kilonzo Junior kwamba uteuzi wa baadhi ya wanasiasa kutoka Ukambani walioshindwa katika uchaguzi uliopita katika mashirika ya serikali una faida finyu zaidi kwa jamii ya eneo hilo.

Katika teuzi zilizofanywa na Rais Kenyatta, juzi wabunge kadhaa wa zamani kutoka eneo hilo walipewa nafasi katika mashirika ya serikali.

Baadhi yao ni; aliyekuwa mbunge wa Kibwezi Magharibi Kalembe Ndile, Kisoi Munyao (Mbooni), aliyewania kiti cha Mwingi Magharibi Mwende Mwinzi, aliyewania ugavana wa Machakos Wavinya Ndeti na aliyekuwa Gavana wa Kitui Julius Malombe.

“Hii handisheki ya kumwezesha mtu kupokea mshahara haina maana yoyote. Tunataka kusherehekea kuanzishwa kwa miradi kama Konza City na Bwawa la Thwake kwa sababu hiyo ni miradi ambayo italeta manufaa makubwa kwa jamii yetu,” akasema Bw Kilonzo Junior.

Walisema hayo katika Shule ya Msingi ya Yambae katika Kaunti ya Makueni wakati wa hafla ya mazishi ya aliyekuwa diwani wa Mbooni Joseph Musya na mwanawe, Steven Kyove.

Wawili hao walifariki katika ajali ya barabarani katika barabara ya Wote-Machakos majuma mawili yaliyopita. Shughuli hiyo pia ilihudhuriwa na Naibu Gavana wa Makueni Adelina Mwau na wabunge; Daniel Maanzo (Makueni), Patrick Makau (Mavoko) na Mbw Ndile na Kisoi.

Manung’uniko hayo kuhusu manufaa ya handisheki yanajiri wakati ambapo Bw MusyokA amekuwa akijitetea dhidi ya madai kuwa hakujali masilahi ya jamii yake alipotangaza kuwa atafanya kazi na Rais Kenyatta.

Gavana wa Makueni Prof Kivutha Kibwana ni miongoni mwa viongozi ambao wamemlaumu Bw Musyoka kwa kutopigania uanzishwaji wa miradi Ukambani wakati wa mazungumzo yake na Rais Kenyatta alivyofanya Bw Odinga.