Mawimbi ya BBI yanavyoyumbisha kundi la Kieleweke

Na WANDERI KAMAU

HATUA ya Seneta Irungu Kang’ata wa Murang’a kumwandikia barua Rais Uhuru Kenyatta mapema wiki hii kwamba huenda wenyeji wa Mlima Kenya wakakosa kuunga mkono ripoti ya Jopokazi la Maridhiano (BBI), imeibua hali ya sintofahamu ya kisiasa katika kundi la ‘Kieleweke’.

Imeibuka kuwa baadhi ya wanasiasa katika kundi hilo sasa wanapanga kuhama na kujiunga na mirengo mingine ya siasa, baada ya kugundua kuwa idadi kubwa ya wenyeji hawaungi mkono ripoti hiyo.

Hilo linafuatia hatua ya Seneta Maalum Isaac Mwaura kutangaza kujiunga na kundi la ‘Tangatanga’ wiki iliyopita, ambapo alikaribishwa na viongozi wa mrengo huo, akiwemo Naibu Rais William Ruto.

Duru zimeliambia Jamvi la Siasa kuwa baadhi ya viongozi wanaopanga kuhama mrengo wa ‘Kieleweke’ ni wabunge Sabina Chege (Murang’a), Mary Wamaua (Maragua), Gathoni Wamucomba (Kiambu), Ngunjiri Wambugu (Nyeri Mjini) na wengine.Uamuzi wao umetajwa kuchangiwa na idadi kubwa ya wenyeji kuhisi kuwa huenda ripoti hiyo ikakosa kuwafaa kwa vyovyote vile, kutokana na kudorora kwa sekta muhimu kama vile kilimo.

“Wenyeji wengi wa Mlima Kenya wanahisi BBI ni njama ya kuwafaa viongozi wachache. Hivyo, idadi kubwa haitaki kusikia lolote kuihusu. Wanataka kujua ni mikakati ipi ambayo serikali imeweka ili kuimarisha masuala muhimu kama vile kilimo cha kahawa, majanichai, pareto kati ya mazao mengine. Ni kutokana na hilo ambapo niliamua kuhama ‘Kieleweke’,” akasema Bw Mwaura.

Baadhi ya viongozi waliozungumza na ukumbi huu walisema imekuwa vigumu kuipigia debe ripoti hiyo katika eneo hilo, kwani wenyeji pia wanahisi kusalitiwa na uongozi wa Rais Uhuru Kenyatta.

Baadhi yao pia wanaiona BBI kama mpango wa kumtengenezea njia kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga, njia ya kuwania urais mwaka wa 2022. “Imekuwa vigumu kuipigia debe BBI Mlima Kenya. Ndio uhalisia wa mambo, ila viongozi wengi katika ‘Kieleweke’ hawataki kusema hilo hadharani,” akasema mbunge Kimani Ichung’wa wa Kikuyu, ambaye ni miongoni mwa washirika wakuu wa karibu wa Dkt Ruto.

Wadadisi wa masuala ya siasa wanasema hatua ya Seneta Kang’ata inapaswa kumfungua macho Rais Kenyatta na washirika wake wanaoipigia debe ripoti hiyo kuwa huenda hali isiwe kama wengi wanavyofasiri.Kwa mujibu wa Prof Macharia Munene, ambaye ni mchanganuzi wa siasa na mhadhiri katika Chuo Kikuu cha USIU, Nairobi, huenda mwelekeo huo unaashiria kuna mengi yanayopaswa kufanywa kabla ya ripoti hiyo kuwasilishwa kwa wananchi.

“Huenda wakati umefika ambapo Rais Kenyatta na washirika wake wanafaa waende mashinani na kusikiliza hisia za wananchi kuhusu malalamishi yao. Pengine huenda hilo likampa taswira kamili kuhusu hali ya kisiasa ilivyo kuihusu ripoti hiyo,” akasema Prof Munene.

Baadhi ya viongozi ambao wamekuwa wakiendesha harakati za kuipigia debe ripoti hiyo ni Mbunge Maalum Maina Kamanda, Kiongozi wa Wengi Bungeni Amos Kimunya, magavana Francis Kimemia (Nyandarua), Anne Waiguru (Kirinyaga), Mutahi Kahiga (Nyeri), Ndiritu Muriithi (Laikipia), Kiraitu Murungi (Meru) kati ya wengine.

Viongozi hao wamekuwa wakishikilia kwamba kinyume na hisia za wanasiasa wa mrengo wa ‘Tangatanga’ ambao unamuunga mkono Dkt Ruto, ukanda huo ndio utakaofaidika zaidi ikiwa Wakenya wataipitisha ripoti hiyo.Hivyo, wanaeleza kuwa viongozi kama Dkt Kang’ata ni “wanasiasa wabinafsi ambao lengo lao ni kuipotosha nchi kuhusu hali ya kisiasa ilivyo katika ukanda huo.”

“Mimi hutangamana na wenyeji wa kaunti yangu kila siku kupitia shughuli mbalimbali. Ninawafahamu kwa undani kuliko viongozi kama maseneta, ambao huendesha shughuli zao nyingi jijini Nairobi. Kwa hivyo, Dkt Kang’ata na viongozi wengine wanapaswa kukoma kuipotosha nchi kuhusu uungwaji mkono wa BBI,” akasema Gavana Kiraitu Murungi wa Meru.

Kulingana na Bw Murungi, kuna uwezekano Dkt Kang’ata anatumiwa kimakusudi na ‘Tangatanga’ kuchora taswira na dhana ya uwongo kuhusu hali ilivyo katika eneo hilo na maeneo mengine nchini.Vilevile, alisema kuna uwezekano kiongozi huyo anapanga kuhamia ‘Tangatanga’ kwa maslahi yake binafsi ya kisiasa.

“Ikiwa kiongozi anapanga kuhama kutoka mrengo mmoja na kujiunga na mwingine, hapaswi kuzua mifarakano isiyofaa. Anapaswa kufanya maamuzi yake kwa njia ya amani. Huo ndio uungwana katika siasa kwani hakuna yeyote anayelazimishwa kufuata mrengo wowote ule,” akasema Bw Murungi.

Naye Bw Wycliffe Muga, ambaye ni mdadisi wa masuala ya siasa, anasema huu ni wakati wa wanasiasa kufanya maamuzi yatakayowafaa, hasa uchaguzi mkuu wa 2022 unapoendelea kukaribia.

“Yanayoendelea kwa sasa si nadra kwani hujitokeza kila uchaguzi mkuu unapokaribia. Wanasiasa lazima wahamie mirengo wanayohisi ina umaarufu miongoni mwa wafuasi wao,” akasema Bw Muga.

Mbunge Kanini Keega (Kieni) aliwataja wanasiasa wanaohama ‘Kieleweke’ kama “wasaliti” ambao kamwe hawawezi kuaminiwa kisiasa hata kidogo.Anasema kundi hilo bado liko imara, kwani linaendeleza ajenda za maendeleo za Rais Kenyatta.

Kieleweke sasa wataka Kiunjuri avuliwe uwaziri

Na NDUNGU GACHANE

VIONGOZI wa kundi la Kieleweke wamemtaka Waziri wa Kilimo Mwangi Kiunjuri ajiuzulu wadhifa wake kisha ajiunge na Tangatanga baada ya kuhudhuria mkutano wa mrengo huo wiki jana mjini Embu.

Mbunge wa Nyeri Mjini Ngunjiri Wambugu amesema Bw Kiunjuri ameonyesha kwamba hatilii maanani majukumu yake ya uwaziri na sasa macho yake yanalenga siasa za 2022.

Bw Kiunjuri na zaidi ya viongozi 50 walikutana katika hoteli moja mjini Embu wiki jana na kuapa kushinikiza kuboreshwa kwa sekta ya kilimo cha majani chai, kahawa, nyanya na viazi katika ukanda wa Mlima Kenya.

Aidha, Bw Wambugu alishangaa kwa nini waziri huyo alikuwa akijumuika na wabunge hao ilhali wizara yake ndiyo ina majukumu ya kuhakikisha kuna mageuzi makubwa kwenye sekta ya kilimo aliyorejelea.

“Wakati wa mkutano huo nilimwoma Kimani Ichungwa (Kikuyu) ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya bajeti bungeni, Moses Kuria (Gatundu Kusini), mwanachama wa kamati hiyo pamoja na Bw Kiunjiri ambaye anafaa kutatua masuala hayo kama waziri, akilalamikia kudorora kwa sekta zetu za kilimo badala ya kuyatatua,” akasema Bw Wambugu.

Mbunge huyo ambaye anaegemea mrengo wa Kieleweke katika mvutano ndani ya Jubilee, anataka waziri Kiunjuri aondoke afisini mara moja.

“Ameshindwa kutekeleza majukumu aliyopewa na sasa anafanya kampeni za afisi ya kisiasa anayolenga kuwania mwaka wa 2022,” akasema Bw Wambugu.

Mbunge huyo alishikilia kwamba ni waziri huyo anayefaa kulaumiwa kwa kukosa kuangazia maslahi ya wakulima kutoka ukanda wote wa Mlima Kenya.

Bw Wambugu amekuwa mstari wa mbele kutetea ushirikiano kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Kinara wa upinzani Raila Odinga.

Alidai kuwa viongozi wa Tangatanga wamekuwa wakijificha nyuma ya uungawaji mkono wa Naibu Rais William Ruto, ili kuwapumbaza wakazi wa Mlima Kenya.

“Nawaomba wakome kujificha nyuma ya uwaniaji wa Dkt Ruto 2022 kwa kutumia masaibu ya wakulima. Iwapo wanawajali basi hatungekuwa tukishuhudia malalamishi ya wakulima ikizingatiwa wanashikilia vyeo muhimu kwenye kamati za bunge na wizara,” akaongeza Bw Wambugu.

Kwa upande wake, mbunge wa Gatanga Nduati Ngugi alisema kwamba haikuwa vyema kwa Bw Kiunjuri kuhudhuria mkutano huo na kutoa wito kwa Rais Uhuru Kenyatta amfute kazi mara moja.

“Hatua lazima ichukuliwe dhidi ya Bw Kiunjuri kwa kuhudhuria mkutano ambao hauhusiani kivyovyote na utekelezaji wa sera za serikali. Rais Kenyatta ambaye ni kiongozi wa chama chetu pia amewaonya mawaziri wake mara kadhaa wakome kujihusisha na siasa,” akasema Bw Ngugi.

Aidha alisema mkutano huo wa Embu sasa umegawanya wakazi wa Mlima Kenya zaidi na akatoa wito kwa Naibu Rais awakomeshe viongozi wa Tangatanga ambao wamekuwa wakitoa matamshi makali dhidi ya mawaziri mbele yake.

“Chama chetu kinasimamia amani na umoja wa taifa hili na namrai Dkt Ruto awatulize wandani wake wenye tabia ya kupanda majukwaani na kuwatusi maafisa wa serikali ambao hawakubaliani nao kisiasa,” akaongeza Bw Ngugi.

Msajili akataa Tangatanga, Kieleweke

Na LEONARD ONYANGO

JUHUDI za baadhi ya wanasiasa kutaka kugeuza makundi ya ‘Kieleweke’ na ‘Tangatanga’ kuwa vyama vya kisiasa zimegonga mwamba, baada ya Msajili wa Vyama, Bi Ann Nderitu kuzuia majaribio hayo yaliyofanywa zaidi ya mara mbili.

Vilevile, Bi Nderitu alisema kuna kundi jingine lililotaka kusajili ‘Handshake’ kuwa chama cha kisiasa lakini pia jaribio hilo likatibuliwa.

Imebainika Afisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa imepokea maombi mara nne ya kutaka Tangatanga Movement kisajiliwe kuwa chama, na ombi la Kieleweke kutumwa kwa ofisi hiyo mara tatu.

Ombi la kwanza la kutaka Tangatanga Movement kusajiliwa kuwa chama liliwasilishwa mara tu baada ya makundi mawili; Tangatanga na Kieleweke kujitokeza katika chama cha Jubilee mwaka 2018, kulingana na Bi Nderitu.

Jaribio la mwisho lilikuwa wiki iliyopita ambapo makundi mawili yalimwandikia barua Bi Nderitu yakimtaka asajili Tangatanga Movement (TTM) na Mafisi Alliance Party (MAP) kuwa vyama vya kisiasa.

Lakini Bi Nderitu, alikataa kusajili Tangatanga na Mafisi akisema majina hayo yanakiuka Katiba na Sheria ya Vyama vya Kisiasa ya 2011.

“Majina Tangatanga, Mafisi yanakiuka maadili na yanakiuka Kifungu cha 91 cha Katiba. Tafadhali pendekeza majina mengine ili tuyachunguze,” Bi Nderitu akayaeleza makundi hayo.

Msajili wa vyama hivyo pia alitoa sababu sawa na hiyo alipokataa kusajili Kieleweke Movement kuwa chama.

Kundi la Tangatanga linaunga mkono Naibu wa Rais William Ruto huku Kieleweke likiunga mkono mwafaka (handisheki) wa kisiasa baina ya Rais Uhuru Kenyatta na kinara wa ODM Raila Odinga.

Hata hivyo haijulikani ikiwa makundi yaliyojaribu kusajili Tangatanga, Kieleweke au ‘Handshake’ yanafanya hivyo kwa niaba ya Dkt Ruto, Rais Kenyatta au Bw Odinga.

“Maombi ya kutaka kusajili vyama mara nyingi huwasilishwa na mawakili hivyo ni vigumu kujua mtu aliyewatuma,” akasema Bi Nderitu kwenye mahojiano na Taifa Leo.

Aibu

Kulingana na Sheria ya Vyama vya Kisiasa ya 2011, Msajili wa vyama anaweza kukataa kusajili chama ikiwa jina lake linaleta aibu au matusi, linafanana na vyama ambavyo tayari vimesajiliwa au nembo yake ni sawa na ya vyama vilivyopo.

“Ombi la hivi karibuni la kutaka Handshake Alliance kisajiliwe kuwa chama liliwasilishwa Jumatano, wiki hii, lakini nikakataa kukisajili. Makundi yaliyowasilisha maombi hayo hayakutimiza matakwa ya sheria,” akasema Bi Nderitu.

Kifungu cha 91 cha Katiba kinasema chama hakitasajiliwa ikiwa kimebuniwa kwa misingi ya dini, kabila, jinsia, vurugu au uchochezi.

“Chama cha kisiasa ni sharti kiwe na sura ya kitaifa, kionyeshe umoja wa nchi na kionyeshe maadili,” inasema Katiba.

Vyama vya kisiasa vilivyosajiliwa kuendesha shughuli za kisiasa nchini ni 68.

Vyama ambavyo vimetuma maombi lakini havijaidhinishwa kujihusisha na siasa ni 37, kulingana na Msajili wa Vyama vya Kisiasa.

Miongoni mwa vyama vinavyongojea kuidhinishwa ni Wema Wetu, Undugu Unity, Mwamba Wetu Social Party, Miradi People’s Socialist, Ajibika For Change Party, Haki na Utaifa Party kati ya vinginevyo.

Kieleweke wataka Ruto ajiuzulu

Na CHARLES WASONGA

WANASIASA wanaopinga azma ya Naibu Rais Dkt William Ruto kuwania urais mwaka 2022, Timu Kieleweke, wanataka ajiuzulu kwa ‘kuzua taharuki’ nchini kufuatia madai kwamba kuna njama ya kumwangamiza.

Wabunge 20 wa kundi la Kieleweke wamemtaka kujiuzulu kufuatia kukamatwa kwa Bw Dennis Itumbi kuhusiana na barua yenye madai ya njama ya kumwangamiza Ruto.

Wakiongea na wanahabari Alhamisi, wabunge hao pia wamemtaka Dkt Ruto kuandikisha taarifa kwa makao makuu ya Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) ili kuwezesha kukamilishwa haraka kwa tuhuma anazokabiliwa nazo Itumbi ambaye anarejelewa kama mwandani wake.

“Kando na kuandikisha taarifi kwa DCI, Dkt Ruto anafaa kuchunguzwa zaidi kwa sababu ni yeye aliyeibua madai hayo ambayo yamezua taharuki na uhasama wa kikabila miongoni mwa Wakenya,” akasema Mbunge wa Limuru Peter Mwathi ambaye alisoma taarifa hiyo kwa niaba ya wenzake.

Wabunge wameitaka Idara ya Mahakama kuhakikisha kuwa kesi ya Itumbi inakamilishwa haraka “ili Wakenya waweze kufahamu ukweli kamili kuhusu suala hilo”.

“Hilo ni suala lenye uzito wa kitaifa kwa sababu madai kama hayo yanaweza sio tu kulisambaratisha taifa kwa misingi ya kikabila bali kusababisha umwagikaji wa damu. Hii ndio maana tunaitaka mahakama kuhakikisha kuwa kesi inakamilishwa haraka na wahusika wote waadhibiwe kwa mujibu wa sheria,” ikasema taarifa hiyo.

Kieleweke wadai Ruto alimchokoza Rais ndipo akazomewa hadharani

Na NDUNGU GACHANE

WANACHAMA wa Jubilee wanaopinga kampeni za mapema za Naibu Rais William Ruto wamedai matamshi ya Rais Uhuru Kenyatta aliyotoa Jumapili yalisababishwa na jinsi naibu wake na wandani wake wamekuwa wakimkaidi kuhusu handisheki na kampeni za mapema.

Viongozi hao walio katika makundi ya Kieleweke na Team Embrace wanaotetea misimamo ya Rais, walidai kuwa hakuna uhusiano mwema kati ya viongozi hao wawili wakuu baada ya Ruto kumkaidi Rais Kenyatta kuhusu malengo ya amani na umoja wa taifa.

Mnamo Jumapili, Rais aliongea kwa ukali akisema hakuna chochote kitamzuia kutafuta umoja wa makabila yote nchini.

Matamshi hayo yalionekana kulenga wanaopinga muafaka wake na Kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga ambao huwa wanadai waziri huyo mkuu wa zamani ni tapeli aliye na nia ya kuvuruga Jubilee.

Viongozi wa Kieleweke wakiongozwa na mbunge wa Gatanga, Bw Nduati Ngugi, Kabando wa Kabando na wenzao wa Team Embrace wakiwemo Mbunge Mwakilishi wa Wanawake wa Murang’a, Bi Sabina Chege na Spika wa Bunge la Kaunti ya Nairobi Beatrice Elachi, walikashifu wenzao wa Tangatanga kwa kumkosea Rais heshima.

“Rais amewasilisha ujumbe kwa Dkt Ruto na wafuasi wake kwa hivyo wasisubiri ishara nyingine yoyote. Wakomeshe kampeni zao na kutangatanga nchini na badala yake wafanyie kazi wananchi kabla Rais aanze kufanya ziara Mlima Kenya ikiwa wanataka kuokoa nyadhifa zao,” akasema Bw Ngugi.

Idadi kubwa ya viongozi wa kikundi cha Tangatanga hutoka maeneo ya Mlima Kenya na hudai kwamba Rais ametelekeza eneo hilo kimaendeleo.

Kwa upande wake, Bw Kabando alimkashifu Dkt Ruto kwa kufanya kampeni za mapema na kuchochea wananchi eneo la kati kumchukia Bw Odinga ilhali Rais analenga kuacha nchi ikiwa na umoja wakati atakapoondoka mamlakani mwaka wa 2022.

“Unapinga handsheki, juhudi za upatanisho na vita dhidi ya ufisadi kisha bado unadai kuwa mwaminifu kwa mkubwa wako?” akashangaa.

Alikosoa pia ziara iliyofanywa na naibu rais hivi majuzi eneo la Mukurweini ambapo wakazi walifika kutoka Karatina wakiwa wamevaa fulana zenye maandishi ya ‘WSR 2022’ na ‘Hustler Nation’, akasema hatua hizo zinafanya kuwe na taharuki za kisiasa ilhali uchaguzi ungali mbali.

Lakini viongozi wanaomuunga mkono Dkt Ruto katika eneo la Mlima Kenya wakiongozwa na wabunge Kimani Ichungwa (Kikuyu) na Alice Wahome (Kandara) walilalamika kuhusu matamshi ya Rais wakisema ni dharau na kukosea heshima viongozi.

Wawili hao waliozungumza kwenye runinga tofauti walisema waliwachagua Rais Kenyatta na Dkt Ruto kwa pamoja na hivyo hawaoni tatizo kuandamana naye anapozuru maeneo tofauti ya nchi kufanya kazi.

“Haiwezekani kwamba wakati Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, Amani National Congress Musalia Mudavadi na Bw Odinga wanapozungumza kuhusu siasa hakuna tatizo ilhali Dkt Ruto anapozunguka nchini kuzindua miradi inakuwa ni siasa,” akasema Ichungwa.

Kwa upande wake, Bi Wahome alisema: “Kutuita wakora ni sawa na kutupiga rungu. Hafai kusema hatukumsaidia kupata kura za urais. Tumekuwa tukipitisha miswada yote ya serikali bungeni.”

JAMVI: Tangatanga na Kieleweke wazua uadui kati ya wazee na makanisa

Na WANDERI KAMAU

TOFAUTI za kisiasa kati ya mirengo ya ‘Tangatanga’ na ‘Kieleweke’ sasa zimewagawanya wazee na makanisa kuwili katika ukanda wa Mlima Kenya, hali inayozua hofu kuhusu mwelekeo wa kisiasa wa eneo hilo.

Migawanyiko hiyo imeenea kiasi kwamba, baadhi ya wanachama hao wametusiwa au hata kushambuliwa wanapozuru ngome za wapinzani wao.

Katika kisa cha Jumapili iliyopita, Mwakilishi wa Wanawake katika Kaunti ya Kiambu, Gathoni wa Muchomba, alizomewa katika kanisa moja katika Kaunti ya Murang’a, alipomkosoa mbunge wa Kandara, Alice Wahome kwa “kumtukana.”

Bi Wamuchomba ni wa kundi la ‘Kieleweke’ huku Bi Wahome akiwa wa kundi la ‘Tanga Tanga’ ambalo linamuunga mkono Naibu Rais William Ruto kuwania urais mnamo 2022.

Katika tukio jingine, zaidi ya wazee 2,000 walikutana katika uwanja wa Kabiru-ini katika Kaunti ya Nyeri Ijuma iliyopita, ambapo walipitisha kauli ya pamoja kutounga mkono azma ya Dkt Ruto, wakilalama kuwa “anazichukulia jamii za GEMA (Agikuyu, Aembu na Ameru) kwa urahisi.”

Mkutano huo, ambao ulipangwa kwa siri kubwa, unadaiwa kufadhiliwa na maafisa wakuu serikalini, ambao wanapinga azma ya Dkt Ruto kuwania urais.

Washiriki wake wakuu walikuwa wanachama wa Baraza la Wazee la Jamii ya Agikuyu (KCE) linaloongozwa na Bw Wachira Kiago.

“Wazee wamepitisha kwa pamoja lazima eneo hili litoe uamuzi huru kuhusu mwelekeo wake wa kisiasa bila kushurutishwa kwa namna yoyote ile,” akasema Bw Kiago.

Kando na kundi hilo, kumekuwa na makundi mengine ya wazee ambayo yamekuwa yakiwatembelea Dkt Ruto na kiongozi wa ODM, Raila Odinga, ambapo yote yamekuwa yakimwahidi kuwa jamii za GEMA zitawaunga mkono ikiwa watawania urais kwenye chaguzi hizo.

Wiki mbili zilizopita, kundi moja la wazee kutoka kaunti ya Nakuru lilimtembelea Bw Odinga katika makazi yake ya Oponda, Siaya, na kumwahidi uungwaji mkono wa eneo hilo. Wazee hao waliongozwa na aliyekuwa mbunge wa Molo, Bw Njenga Mungai.

Ni matukio ambayo wachanganuzi wa kisiasa wanaonya kuwa yanaendelea kufifisha umoja wa kisiasa na kuondoa uwezekano wa uwepo wa sauti moja kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022.

“Hali ya sasa ni ya kutia wasiwasi. Kwa mara ya kwanza, huenda eneo hili likashuhudia mgawanyiko mkubwa zaidi wa kisiasa, tangu mwanzo wa mfumo wa vyama vingi vya kisiasa mnamo 1992,” asema Prof Macharia Munene, ambaye ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha USIU, Nairobi.

Kulingana na mchanganuzi huyo, kugawanyika kwa wazee huenda kukahatarisha upatikanaji wa umoja wa kisiasa, hata ikiwa ukanda huo unatarajiwa kutoa mwelekeo wake rasmi wa kisiasa kwenye kongamamo la Limuru III, lililopangiwa kufanyika baadaye mwaka huu.

“Kwa mara ya kwanza, kuna hatari ya ukanda huo kutotii uamuzi ambao utatolewa katika kongamano la Limuru III. Ikumbukwe kuwa ingawa migawanyiko ya kisiasa huwa inashuhudiwa, ni nadra kwa wazee kugawanyika kama ilivyo sasa,” asema Prof Munene.

Makongamano hayo huwa muhimu katika kutoa mielekeo rasmi ya kisiasa ya ukanda huo, kila wakati unapojipata katika njiapanda ya kisiasa.

Kongamano la kwanza lilifayika mnamo 1963, wakati Mzee Jomo Kenyatta alitangaza kuvunjwa kwa nafasi ya makamu wa rais wa chama cha Kanu, na kubuni nafasi nane za uwakilishi katika mikoa yote minane.

Kongamano la pili lilifanyika mnamo 2012, wakati Rais Uhuru Kenyatta alitangaza kujiondoa katika Kanu na kubuni chama cha TNA, ambacho kiliibuka kama chama rasmi cha ukanda huo kwenyeu uchaguzi mkuu waa 2013.

Wachanganuzi wanasema kuwa katika nyakati zote mbili, ukanda huo ulitii maamuzi yaliyofikiwa kwani uliwaunga mkono kikamilifu Mzee Kenyatta na mwanawe, Rais Kenyatta.

“Hali ni tofauti sasa. Kuna uwezekano wa baadhi ya makundi ya wazee na makanisa kuzingatia maamuzi yao huru, kwa kisingizio cha kutojumuishwa, kutengwa ama kutofaidika kwa maamuzi yaliyofikiwa awali,” asema Prof Ngugi Njoroge, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.

Baada ya kuzomewa kwa Bi Wamuchomba, Kanisa la Kianglikana (ACK) katika Dayosisi ya Murang’a Kusini lilitangaza kuwapiga marufuku wanasiasa kuhutubu katika makanisa yake, hatua ambayo baadhi ya viongozi wameitaja kuegemea mrengo mmoja wa kisiasa.

“Uamuzi huo bila shaka unaonyesha mapendeleo ya kisiasa kwa mrengo wa Tanga Tanga. Mbona kanisa hilo limetoa agizo hilo tu baada ya kuzomewa kwa Bi Wamuchomba, ambaye ni wa mrengo wa ‘Kieleweke’? Hili ni dhihirisho wazi kuwa kanisa lenyewe linachangia katika migawanyiko ya kisiasa inayoendelea,” akasema mbunge mmoja wa kundi la ‘Kieleweke’ ambaye hakutaka kutajwa.

Lakini katika juhudi za kuzima migawanyiko hiyo, wachanganuzi wanasema kuwa ni lazima Rais Kenyatta avunje kimya chake, kwani kinachangia pakubwa.

“Kama kiongozi na msemaji wa kisiasa wa ukanda huo, Rais Kenyatta lazima ‘arudi nyumbani’ na kurejesha hali ya kawaida. La sivyo, kelele hizo zitazidi kuongezeka, hali inayohatarisha upatikanaji wa mwafaka maalum wa kisiasa,” asema Wycliffe Muga, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.

Jubilee imekufa, Kieleweke sasa wadai

Na NDUNGU GACHANE

KUNDI la wabunge wa chama cha Jubilee wanaopinga azma ya Naibu Rais William Ruto kuingia Ikulu mwaka wa 2022 sasa linadai kuwa chama hicho kimekufa licha ya wandani wa Dkt Ruto kushikilia kuwa kingali imara.

Wanachama wa kundi hilo maarufu kama Kieleweke wamemtaka Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga kubuni muungano mwingine kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao.

Mbunge Maalum Maina Kamanda, mwenzake wa Gatanga Nduati Ngugi na aliyekuwa Mbunge wa Mukurwe-ini Kabando wa Kabando wanasema kwamba sasa muungano kati ya mrengo wa Jubilee unaounga mkono Rais Kenyatta na ODM ndio utaleta mwamko mpya wa kisiasa nchini Kenya.

“Ili kuleta ufufuo mpya katika ulingo wa siasa, mbegu za mivutano ya kikabila zinapasa kuangamizwa ili kutoa nafasi ya kushamiri kwa mbegu ya uwiano wa kitaifa.

“Sharti tuhakikishe kuwa tunabuni uongozi utakaoshirikisha jamii zote nchini, wala si Wakikuyu na Wakalenjin pekee kwa hali hiyo inachangia kuongeza uhasama wa kikabila,” Bw Kamanda akaambia Taifa Jumapili.

Kwa upande wake Bw Kamanda alisema: “Jubilee imekufa. Ndoa yetu na Dkt William Ruto imekufa na wale wanaoitisha mkutano wa Kundi la Wabunge wa Jubilee wanafaa kusoma dalili za nyakati na kuendelea na shughuli zao nyingine badala ya kupoteza muda wao.”

Bw Ngugi alisema kwamba Rais Kenyatta na Bw Odinga wana ushawishi mkubwa wa kisiasa nchini na wataendeleza mpango wa kubuni muungano wa kisiasa kabla ya uchaguzi mkuu ujao.

“Kwa kuwa viongozi hawa wawili wanashabikiwa kwingi nchini, tumependekeza kuwa Jubilee na ODM ziungane na viongozi hao wawili wawanie uchaguzi mkuu kwa tiketi moja,” akaambia Taifa Jumapili.

JAMVI: ‘Kieleweke’ kutaka kutambuliwa Bungeni ni dalili ya Jubilee kufifia

Na CHARLES WASONGA

HATUA ya wabunge wanaopinga azma ya Naibu Rais William Ruto kuingia Ikulu mwaka wa 2022 kumwandikia Spika wa Bunge Justin Muturi wakitaka kundi lao almarufu “Kieleweke” litambuliwe bungeni imeibua hisia mseto katika ulingo wa siasa.

Wadadisi wa kisiasa wanafasiri hatua hiyo kuashiria uhalisia wa mpasuko ulioko ndani ya chama tawala cha Jubilee na kujitolea kwa mirengo ya Kieleweke na Tanga Tanga kuendelea kuendeleza tofauti zao kuelekea uchaguzi mkuu ujao.

Wabunge wa “Team Tanga Tanga” sasa wanamtaka Bw Muturi kukataa ombi hilo wakisema wabunge hao wanaongozwa na “nia mbaya ya kutumia bunge kama jukwaa la kuendelesha vita vyao dhidi ya Naibu Rais”.

“Tunamtaka Spika wetu kukataa ombi kama hilo. Hawa watu wamegundua kwamba wananchi hawataki propaganda ambao wao hueneza kila mara makanisani na kwenye hafla ya mazishi. Hii ndio maana sasa wanataka kutumia bunge kama jukwaa la kuendeleza porojo zao dhidi ya Naibu Rais. Tunamhimiza Spika kuwapuuzilia mbali,” akasema Mbunge wa Mathira Rigathi Gachagua ambaye ni mwanachana wa vuguvugu la Team Tanga Tanga.

Na kulingana na mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Martin Andati, ombi hilo la vuguvugu la Kieleweke kwa Bw Muturi ni ithibati tosha kuwa chama cha Jubilee kimesambaratisha kabisa kundi lake la wabunge.

“Hii ina maana kuwa licha ya ingawa Naibu Rais amekuwa akishikilia kuwa Jubilee bado iko pamoja, chama hiki kimesambaratika kuwili. Na ikiwa ni kweli wale wanaojiita Kieleweke wametuma ombi la kutaka watambuliwe bungeni, bado lile kundi la wabunge wa Jubilee (PG) haliko kabisa kwani sasa ni wazi kwamba hawako tayari kushiriki meza moja na wenzao ambao ni wandani wa Ruto,” anasema.

Wabunge wa mrengo wa Kieleweke wanataka waruhusiwe kuendesha shughuli zao bungeni kwa kutambuliwa kwa jina jipya la, “Wabunge Watetezi wa Umoja.” Kundi hilo linajumuisha wabunge wa chama tawala Jubilee na vyama vya upinzani kama vile, ODM, Wiper na ANC.

Chini ya uongozi wa Mbunge wa Nyeri Mjini Ngunjiri Wambugu na Mbunge Maalum Maina Kamanda, wabunge hao hawaelewani na kundi la “Team Tanga Tanga” ambalo limekuwa likimpigia debe Dkt Ruto na kumtaja kama mgombeaji urais anayefaa kuingia Ikulu baada ya Rais Uhuru Kenyatta kukamilisha muhula wake wa pili na wa mwisho mnamo 2022.

“Ni kweli tumemwandikia barua Spika Justin Muturi barua tukitaka kutambuliwa kama kundi rasmi la wabunge. Lengo letu ni kuendeleza ajenda ya rais ya kutumia bunge kama jukwaa la kuhimiza umoja na utangamano wa kitaifa,” Bw Wambugu akasema.

“Hatua hii ni kinyume na ile ambayo imechukuliwa na wenzetu ambao wameanza kampeni za urais mapema ilhali huu ni wakati wa kuhimiza umoja na kuendeleza ajenda nne kuu za maendeleo zilizotangazwa na serikali,” anaongeza

Wanachama wa vuguvugu la Kieleweke wamekuwa wakimshutumu Dkt Ruto na wandani wake katika Tanga Tanga wakidai wanahujumu vita dhidi ya ufisadi na muafaka wa maridhiano kati ya Rais Kenyatta na kiongozi wa ODM almaarufu Handisheki.

Isitoshe, wabunge hao wamemtaka Naibu Rais ajiuzulu kwa kuendelea kukaidi misimamo ya Rais Kenyatta.

“Unawezaje kudai kuwa wewe ni mdogo wa Rais ilhali unakwenda kinyume cha ushauri wake kwa kuanzisha kampeni za mapema ya kutaka kiti anachokalia sasa. Badala ya kuungana naye kuendelea ajenda za serikali kama vile vita dhidi ya ufisadi anadai vita hivyo vinalenga watu wake pekee,” anasema Bw Kamanda.

“Hii ndio maana sisi kama wabunge ambao tunapinga kampeni za mapema za urais, vita dhidi ya ufisadi na muafaka wa maridhiano ulioanzishwa na Rais pamoja na Bw Odinga, tunataka tutambuliwe bunge ili tuweze kuendeleza ajenda hiyo,” akaongeza.

Kulingana na Bw Kamanda, kundi la Kieleweke lina zaidi ya wabunge 70 kutoka vyama mbalimbali vya kisiasa. Hata hivyo, kando na Kamanda na Wambugu, wabunge wengine ambao huandamana na wao katika ibada za Jumapili na mikutano mingine ya kisiasa ni; Joshua Kutuny (Cherangany), Anthony Oluoch (Mathare), Paul Koinange (Githunguri, Jubilee), Robert Mbui (Kathiani, Wiper), Gathoni Wa Muchomba (Kiambu, Jubilee), Muturi Kigano (Kangema, Jubilee), Godffrey Osotsi (Mbunge Maalum, ANC).

Duru kutokana afisi ya Spika Muturi zilisema kuwa barua ya wabunge hao imepokewa na “itashughulikiwa kabla ya bunge kurejelea vikao vyake Jumanne”.

“Nadhani barua ya wabunge hao ni miongoni mwa barua nyingi ambazo afisi ya Spika itashughulikia kabla ya bunge kurejelea vikao vya Jumanne alasiri baada ya likizo fupi,” afisa mmoja, ambaye hakutaka kutajwa, aliambia ukumbi wa Jamvi.

Sheria za Bunge zinampa Spika wa Bunge kuidhinisha kuundwa kwa makundi mbalimbali ya wabunge baada ya kuridhinika na malengo yao. Kwa mfano, kando na makundi ya wabunge wanachama wa vyama mbalimbali vinavyowakilishwa bungeni, bunge la sasa la 12 lina makundi mengine.

Kundi la wabunge kutoka eneo la ukuzaji wa miwa kwa wingi linaloongozwa na Mbunge wa Muhoroni Onyango K’Oyoo, kundi la wabunge walemavu linaloongozwa na Seneta Maalum Isaac Mwaura, kundi la wabunge Waumini wa Kanisa Katoliki linaloongozwa na Mbunge wa Kiminini Chris Wamalwa, kati ya makundi mengine.

Makundi ya ‘Tangatanga’ na ‘Kieleweke’ yamchanganya Sonko

Na LEONARD ONYANGO

MGAWANYIKO ndani ya chama cha Jubilee umemwacha Gavana wa Nairobi Mike Sonko katika njiapanda kisiasa.

Gavana huyo ambaye ni mwandani wa Naibu Rais William Ruto, hata hivyo, anashikilia kuwa haungi mkono makundi yote mawili; ‘Kieleweke’ na ‘Tangatanga’, ambayo yamechipuka katika chama cha Jubilee.

Kundi la Tangatanga linaunga mkono Dkt Ruto kuwania urais katika kinyang’anyiro cha uchaguzi mkuu wa 2022 huku Kieleweke wakimpinga.

Wiki mbili zilizopita, Bw Sonko aliwashambulia hadharani aliyekuwa mwaniaji wa ugavana wa Nairobi Peter Kenneth na mbunge Maalumu Maina Kamanda huku akiwataja kuwa wafisadi mbele ya waumini wa kanisa la St Stephens ACK Nairobi.

Bw Kenneth na Bw Kamanda ni miongoni mwa wanasiasa wa kundi la Kieleweke linalopinga vikali Naibu wa Rais Dkt Ruto kuwania urais 2022.

Bw Kamanda ni miongoni mwa wanasiasa kutoka eneo la Kati waliopoteza kura za mchujo za Jubilee kabla ya uchaguzi wa Agosti 8, 2017 na wamekuwa wakishutumu Dkt Ruto kwa ‘kuwaangusha’.

Katika hotuba yake kanisani, Bw Sonko pia alishambulia kundi la Nairobi Regeneration, lililobuniwa na Rais Uhuru Kenyatta kusafisha na kupangilia upya jiji la Nairobi.

Gavana Sonko ni mwandani wa Naibu Rais William Ruto. Picha/ Maktaba

Bw Sonko alisitisha shughuli ya kubomoa vibanda na majumba yaliyojengwa katika hifadhi ya barabara au eneo la serikali hadi pale atakaposhauriana na rais.Sonko na Waziri wa Utalii Najib Balala ndio wenyeviti wa kamati ya Nairobi Regenaration.

Bw Sonko pia alikosoa Rais Kenyatta kwa kuwatoza wafanyakazi ada ya asilimia 1.5 ya mishahara kwa ajili ya Mpango wa Ujenzi wa Nyumba nafuu.

“Naunga mkono mradi wa ujenzi wa nyumba nafuu na miradi minne mikuu ya rais wetu mpendwa ambaye ni rafiki na ndugu yangu mkubwa. Mpango huo utawezesha Nairobi kupata nyumba 200,000 ndani ya kupindi cha miaka mitatu. Lakini napinga hatua ya Rais kutaka kuwatwika mzigo mkubwa wa kulipa ada wakazi wa Nairobi na Wakenya wote kwa ujumla,” akasema Bw Sonko.

Rais Kenyatta amekuwa akitetea ada hiyo akisema kuwa mpango huo utawezesha Wakenya wasioweza kumudu bei ya juu ya nyumba kujipatia makazi.Naibu wa Rais Dkt Ruto, hata hivyo, hajajitokeza wazi na kutangaza msimamo ikiwa anaunga mkono ada hiyo ya asilimia 1.5 au la.

Mapema 2018, Gavana Sonko alidai kuwa baadhi ya mabwanyenye kutoka eneo la Mlima Kenya walikuwa wakifanya vikao vya usiku kupanga njama ya kumzuia Dkt Ruto kuwa rais 2022.

Bw Sonko aliapa kukabiliana na yeyote ambaye angethubutu kumzuia Dkt Ruto kumrithi Rais Kenyatta.Ilikuwa baada ya matamshi hayo ambapo alijipata pabaya na Ikulu na kupunguziwa walinzi kutoka 26 hadi watano.

Bw Sonko aligura Nairobi na kwenda kusihi nyumbani kwake katika Kaunti ya Machakos akidai kuwa maisha yake yalikuwa hatarini.

Gavana Sonko pia amekuwa akishutumu baadhi ya watu katika afisi ya rais kwa kumlazimisha kuteua mtu fulani kuwa naibu wake.Bw Sonko amekuwa akihudumu bila kuwa na naibu gavana tangu kujiuzulu kwa Polycarp Igathe mwaka mmoja uliopita.

Mwaka wa ushirikiano kati ya Rais Kenyatta na kinara wa ODM Raila Odinga pia unaonekana kumkanganya zaidi Bw Sonko.Bw Sonko wiki mbili zilizopita aliambia Kamati ya Seneti kwamba amechelewa kuteua naibu wake kwa sababu alipokea ombi kutoka kwa chama cha ODM kikimtaka kuteua Bi Rahab Wangui.

Wadadisi wa masuala ya kisiasa wanasema kuwa Bw Sonko amekuwa akiungwa mkono na Dkt Ruto hata wakati wa kura za mchujo wa chama cha Jubilee.

“Viongozi wakuu serikalini waliunga mkono Bw Peter Kenneth, lakini Dkt Ruto alisimama na Bw Sonko. Hivyo ni rahisi kwa Sonko kuegemea Tanga Tanga kuliko Kieleweke,” anasema Bw George Mboya, mdadisi wa masuala ya kisiasa.

‘Kieleweke’ wadai Ruto anavuruga viongozi Mlima Kenya

Na NDUNGU GACHANE

VIONGOZI kadha wa Mlima Kenya wamemhusisha Naibu Rais, Dkt William Ruto na mgawanyiko unaokumba eneo hilo.

Wanadai mienendo yake ya kumkaidi Rais Uhuru Kenyatta, kuhusu kampeni za mapema ni chanzo cha mgawanyiko huo wa viongozi katika ngome ya Rais.

Wengi wao, wanahisi Dkt Ruto amekuwa akimkaidi Rais Kenyatta kwa ‘kufadhili’ viongozi wa Mlima Kenya ilhali wao ndio wanapasa kuwa katika mstari wa mbele kutekeleza ajenda za Rais.

Wakiongozwa na Mbunge Maalum, Bw Maina Kamanda, Mbunge Mwakilishi wa Kike kaunti ya Kiambu, Bi Gathoni wa Muchomba, na Mbunge wa Nyeri Mjini, Bw Ngunjiri Wambugu, viongozi hao walidai Dkt Ruto amesababisha mtafaruku katika eneo hilo ambalo limekuwa na umoja kisiasa kwa miaka mingi.

Kulingana na Bi Wamuchomba, shida zilianza wakati Rais alipoalika viongozi wote wa kisiasa walioshinda uchaguzini katika Ikulu ya Nairobi na ya Nyeri mnamo Septemba 30, 2018, akawaagiza wakomeshe kampeni za mapema zinazohusu uchaguzi wa urais wa 2022.

Alikuwa ameahidi wakati ukifika, atasimamia kampeni za urais kumpigia debe Dkt Ruto na kusisitiza wakati haujafika kuendeleza siasa nchini.

“Alifafanua maono yake ya nchi hii akatushauri tusiwe tukitangatanga maeneo tofauti ya nchi bali tukae katika maeneobunge yetu kufanyia kazi wapigakura. Lakini Dkt Ruto hakufuata agizo la mkubwa wake bali ‘alinunua’ viongozi kumpigia debe kwa urais na hatua hiyo ilitufanya tuzinduke kuipinga,”?akasema Bi Wamuchomba.

Alitaja matukio matatu ambayo yalionyesha Dkt Ruto hamtii Rais Kenyatta kama vile kuhusu utathmini wa utajiri wa watumishi wa umma, vita dhidi ya ufisadi ambapo alidai maafisa wanaoendesha juhudi hizo ni wakora, na kusitasita kwake kujisajili kwa Huduma Namba.

Alizidi kusema wakati wa kampeni, Rais hakuwahi kuzuru eneo la Rift Valley bila kuandamana na Dkt Ruto ilhali yeye amekuwa akienda katika ngome ya kisiasa ya Rais bila kushauriana naye.

Kwa upande wake, Bw Kamanda anaamini Dkt Ruto ndiye atapata hasara kubwa zaidi kwenye mgawanyiko aliosababisha kwani asipopata uungwaji mkono kikamilifu Mlima Kenya ifikapo 2022, itakuwa vigumu kwake kushinda urais.

“Ataona matokeo yake ifikapo Uchaguzi Mkuu mwaka wa 2022,” akasema Bw Kamanda.

Lakini kuna viongozi walio wandani wa Naibu Rais wanaohisi kwamba kimya cha Rais Kenyatta kuhusu mizozo ya kisiasa nchini ndio kimesababisha hali kuwa mbaya zaidi na wanataka kuwe na mkutano wa dharura wa wabunge ili kurekebisha hali.

Mbunge wa Kiharu, Bw Ndindi Nyoro alidai serikali inafadhili wapinzani wa Dkt Ruto kuendeleza kampeni dhidi yake, ingawa madai hayo hayangeweza kuthibitishwa.

“Huwa wanajigamba mbele zetu jinsi wanavyofadhiliwa kueneza chuki na kampeni dhidi ya Naibu Rais, lakini tunataka watangaze wanamuunga nani mkono kwa urais kwani sisi tayari tuna mgombeaji wetu,” akasema.

Mchanganuzi wa siasa katika Kaunti ya Murang’a, Bw George Nyoro pia alimlaumu Rais kwa misukosuko ya kisiasa Mlima Kenya na kusema Rais huonekana kana kwamba anachukia sana mrengo wa Tangatanga ilhali yuko kimya kuhusu Kieleweke ambayo pia inaendeleza siasa.

‘Tangatanga’ na ‘Kieleweke’ wakosa adabu kuraruana kanisani

Na CHARLES WASONGA

MGAWANYIKO ndani ya chama cha Jubilee uliendelea kushuhudiwa Jumapili pale kundi la wabunge wanaegemea mrengo wa Rais Uhuru Kenyatta (Kieleweke) na Naibu wake William Ruto (Tangatanga) walipofarakana katika kanisa moja katika eneobunge la Naivasha.

Hafla ya kutoa shukrani katika Kanisa la AIPCA mjini Naivasha iligeuka kuwa uwanja wa mirengo mahasimu ha  kunyoosheana kidole cha lawama na kurushiana cheche za maneno.

Vurugu zilianza baada ya kundi la ‘Kieleweke’ likiongozwa na Mbunge wa Nyeri Mjini Ngunjiri Wambugu, Joshua Kuttuny (Cherangany) na Gathoni Wa Muchomba (Mbunge Mwakilishi, Kiambu) na wengine walipowasili katika kanisa hilo bila kumfahamisha Mbunge wa eneo hilo Jane Kihara ambaye ni mwandani wa Dkt Ruto.

Isitoshe, wabunge hao walimshambulia Naibu Rais, na wabunge wanaomuunga mkono, hatua iliyomkera Bi Kihara ambaye alikuwepo kanisani humo.

Bw Wambugu ndiye alikuwa wa kwanza kumshutumu Naibu Rais kwa kumhujumu Rais Kenyatta badala ya kufanya kazi walivyowaahidi raia.

Alisema wanachama wa kundi lake wako nyuma ya Rais Kenyatta na kuwa hawatakaa kitako na kutizama huku Dkt Ruto akiendelea kuunga mkono wafisadi.

“Rais alituita sote baada ya uchaguzi na tukakubaliana kulenga maendeleo lakini miezi michache baadaye watu wengine wakaanza kuongea kuhusu uchaguzi wa 2022,” akasema.

Kauli yake iliungwa mkono na Bw Kuttuny aliyesema kuwa chama cha Jubilee kimegawanyika katika mirengo miwili, moja inaunga mkono vita dhidi ya ufisadi na nyingine inaunga mkono Dkt Ruto anayetetea washukiwa wa ufisadi.

Alishangaa ni kwa nini Naibu Rais anakula na kuwatetea magavana wa Samburu na Kiambua ambao wametuhumiwa kwa wizi wa pesa za umma.

“Tangu Rais Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga waliporidhiana kisiasa taifa hili limekuwa tulivu lakini watu wengine wanaounga mkono ufisadi hawaoni hii,” akasema.

Na Wa Muchomba aliwashambulia wabunge wanaomuunga mkono Ruto alisema haja yao ni kujitajirisha kwa kutumia pesa za umma zilizoibwa.

Alimsuta Ruto kwa kumhujumu Rais akiongeza kuwa wabunge kutoka eneo la Mlima Kenya hawatanyamaza ila watamkemea.

“Kuna Rais mmoja pekee nchini na hakuna aliyeruhusiwa kumdhalilisha kwa njia yoyote,” akasema.

Lakini alipoamka kuongea, Bi Kihara aliyeonekana mwenye hasira aliwasuta wenzake kwa kumkosea heshima Naibu Rais akisema kuwa hawajuti kumuunga mkono Dkt Ruto.

Aliwakashifu wabunge wa eneo la Mlima Kenya akiwataka kukoma kujaribu kugawanya Rift Valley akiongeza kuwa Dkt Ruto hajaanza kampeni kama wanavyodai.

“Wabunge kutoka Kati mwa Kenya wanafaa kusalia maeneo yao na wakome kuelekeza kuhusu yule tunapaswa kuuunga mkono kwani sisi sio washenzi,” Bi Kihara akasema kwa ghadhabu.

Wazee walaani ‘Tangatanga’ na ‘Kieleweke’

Na JOSEPH WANGUI

WAZEE wa jamii ya Agikuyu sasa wanataka makundi ya kisiasa ndani ya chama cha Jubilee yavunjwe huku wakikariri msimamo wao wa awali kwamba Naibu Rais William Ruto hatapata uungwaji mkono wa moja kwa moja kutoka jamii hiyo 2022.

Huku wakilaani kubuniwa kwa makundi ya ‘Tangatanga’ na ‘Kieleweke’, wanachama wa baraza la wazee wa jamii hiyo (KCE) waliwataka wanachama wa makundi hayo kusitisha shughuli zao na kampeni za urais na badala yake waelekeze juhudi zao kuimarisha hali ya kiuchumi ya wananchi.

Wakiwahutubia wanahabari Jumapili mjini Nyeri, wazee hao walisema hawataunga mrengo wowote, kati ya hiyo miwili, kwani kila mmoja unawagonganisha Wakenya.

“Hatujihusishi na mitazamo ya kisiasa na kundi linalojiita ‘Kieleweke’ au lile la ‘Tangatanga’. Tunaunga mkono Rais na Serikali yake. Kwa hakika wakati huu wote tumekuwa tukipinga shughuli za mirengo hii,” akasema naibu mwenyekiti wa KCE Peter Njogu Githinji akizungumza na wanahabari katika jumba la Umoja Chambers.

Baraza hilo pia liliunga mkono kauli ya awali ya naibu mwenyekiti wake David Muthoga kwamba ndoto ya urais ya Dkt Ruto haitaungwa mkono wa moja kwa moja kutoka kwa jamii ya Mlima Kenya mwaka 2022.

“KCE inawatambua Rais na naibu wake. Tunaunga mkono Kamati ya Maridhiano kama njia ya kuleta amani na uwiano nchini. KCE pia inaunga mkono Rais katika vita dhidi ya ufisadi. Tumeridhishwa na uongozi wa Bw Muthoga hapa Nyeri na Kenya kwa jumla,” akasema Bw Githinji.

Mwezi uliopita, Bw Muthoga alienda kinyume na ahadi ya Rais Kenyatta aliyotoa kabla ya 2013 na 2017 ya kuunga mkono azma ya Dkt Ruto kuingia Ikulu 2022 akisema si lazima kwa jamii hiyo kuheshimu ahadi hiyo. Alisema baraza hilo la wazee halikuwa na habari zozote kuhusu uwepo wa makubaliano kati ya wawili hao ambayo yalipaswa kuheshimiwa na jamii za Wakikuyu na Wakalenjin.

“Dkt Ruto anapaswa kuanza mazungumzo mapya na jamii yetu ikiwa anataka imuunge mkono 2022. Kwa sasa asitarajie uungwaji mkono wa moja kwa moja.”

2022: ‘Kieleweke’ wamrai Ruto amteue Muturi mgombea mwenza

NA DANIEL OGETTA

KUNDI la wabunge wa ‘Kieleweke’ kutoka Mlima Kenya sasa wanamtaka Naibu Rais, Dkt William Ruto kumteua Spika wa Bunge Justin muturi kama mwaniaji mwenza katika kinyang’anyiro cha urais hapo 2022.

Wakiongozwa na mbunge wa Mbeere Kaskazini Muriuki Njagagua, walisema watafurahia iwapo Naibu Rais atamteua Bw Muturi kama mwenza wake katika kinyang’anyiro hicho.

Wabunge hao wanasema kwamba Bw Muturi hajahusika kwa namna yoyote katika ufisadi wala unyakuzi wa mali ya umma na kwamba anayo tajriba katika kutumikia umma.

Hata hivyo, mnamo 1997, Bw Muturi alituhumiwa kula rushwa alipokuwa hakimu, lakini Tume ya Huduma ya Mahakama (JSC) ikafuta madai hayo.

Wabunge hawa walikuwa wakizungumza katika hafla ya kumpongeza mbunge wa Manyatta Bw John Muchiri. Bw Njagagua alisema kwamba Bw Muturi anamfaa Bw Ruto ambaye alihudhuria hafla hiyo, kama mwaniaji mwenza.

Bw Njagagua aliungwa mkono na Mbunge wa Kikuyu, Bw Kimani Ichungw’a aliyesema wakazi wa Embu wamekuwa wakiunga mkono serikali zilizopita hivyo basi hawafai kusahaulika katika uteuzi wa kujaza nafasi kubwa serikalini.

“Wakazi wa Embu walimuunga mkono Mzee Jomo Kenyatta, Daniel Moi na Mwai Kibaki na hata kuipigia serikali ya Jubilee kura. Hivyo basi kile ambacho wakazi hawa wa Embu wataamua ndicho kitafanyika,” alisema Ichungw’a.

Mbunge wa Tharaka Nithi, Bw Murugara Gitonga naye akasema atazungumza na Spika wa Seneti Bw Kithure Kindiki ambaye pia anamezea mate kuwa mgombea mwenza ili amruhusu Bw Muturi kuchukua nafasi hiyo.

Mbunge maalum Bi Cecile Mbarire naye alisema kwamba 2022 utakuwa wakati mwafaka wa wakazi wa Mlima Kenya kumshukuru Bw Ruto kwa kumuunga mkono rais Kenyatta. Akizungumzia pendekezo hilo, Naibu wa Rais alisema kwamba wakati ukiwadia, chama cha Jubilee ndiyo itaamua atakayenyakua wadhfa huo.

Akielezea kukubaliana na maoni ya wabunge hawa, Dkt Ruto alisema kwamba Bw Muturi ana ujuzi ufaao kwani alipokuwa kwenye upinzani, Bw Muturi alikuwa kiongozi katika chama. Dkt Ruto pia aliwarai wakazi wa Embu kuzidi kuunga mkono utendakazi wa serikali ya Jubilee kwa muda uliosalia.

Bw Muturi anyejulikana kwa jina la utani kama ‘JB’, alikuwa mbunge wa kwanza wa Siakago kuchaguliwa katika uchaguzi mdogo wa 1997 kwa tiketi ya KANU alipoaga Silas Ita.

Wabunge wengine waliohudhuria hafla hiyo ni Alice Wahome (Kandara), Geoffrey King’ang’i (Mbeere South), Erick Muchangi (Runyenjes), Gichohi Mwangi na Njeru Ndwiga (Seneta wa Embu).

OBARA: ‘Kieleweke’ wamenaswa na mtego wa ‘Tangatanga’

Na VALENTINE OBARA

VIONGOZI wa kisiasa wanaoegemea upande wa Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga, walikuwa kwa muda mrefu wakikashifu wale wanaoonekana kuendeleza kampeni za uchaguzi wa urais wa 2022 mapema.

Tangu Uchaguzi Mkuu wa 2017 ulipokamilika na kisha baadaye Rais na Bw Odinga wakaweka mwafaka wa maelewano almaarufu kama handsheki, wafuasi wao walitofautiana na kikundi kinachoegemea upande wa Naibu Rais William Ruto, kinachompigia debe kwa urais kumrithi Rais Kenyatta.

Lakini katika siku za hivi majuzi, mambo yamebadilika kwani viongozi hawa ambao wanafahamika kama ‘Team Kieleweke’ nao pia wanafuata tabia za wale wapinzani wao walio maarufu kama ‘Team Tangatanga’.

Kwa wiki kadhaa sasa, tumejionea wanasiasa wa Kieleweke wakihudhuria mikutano ya kuchangisha pesa makanisani na hata wakiandaa mikutano ya hadhara ya kisiasa.

Katika mikutano hii, wao hufanya yale yale ambayo awali walikuwa wakikashifu Tangatanga kuyahusu.

Kiongozi bora ni yule anayetenda yale anayoyasema kikamilifu, wala si anayetapatapa kwa kushikilia msimamo mmoja mchana kisha usiku yuko kwingine.

Wananchi waliokuwa wakidhani kuna viongozi wenye busara waliosimama wima kupinga siasa zinazoendelezwa makanisani na vile vile kampeni za mapema, sasa wamebaki midomo wazi kwani wale waliowadhania kuwa wangwana wamebadilika.

Hali hii ilifikia kiwango cha kuwa Sikukuu ya Leba Dei wiki iliyopita iligeuzwa kuwa ya kisiasa badala ya kusherehekea mchango wa wafanyakazi kwa uchumi wa kitaifa na kupigania masilahi yao. Zaidi ya hayo, wanasiasa wa Kieleweke walipanga kufanya mkutano wa hadhara Kakamega Jumamosi kwa madai ya kutaka kuhamasisha umma kuhusu msimamo wao wa vita dhidi ya ufisadi.

Yeyote yule anayefuatilia siasa za humu nchini kwa kina atakubaliana nami kwamba mkutano huo ulioahirishwa dakika za mwisho kama ungefanikiwa, ungekuwa tu wa kumshambulia Nibu Rais na wandani wake.

Kwa kweli, viongozi wa kundi la Kieleweke wameonyesha wazi kuwa wao ni bendera inayofuata upepo unaovumishwa na Tangatanga! B

ila shaka hii ni hali ambayo inawapa wale wa Tangatanga ari zaidi ya kuendeleza siasa zao zinazosababisha taharuki nchini kwani hakuna jinsi wataambiwa wakome, ilhali waliokuwa katika mstari wa mbele kuwakashifu nao wamejitosa ulingoni.

Tatizo linalotokea hapa ni kwamba majibizano yatazidi kutokota na kufanya iwe kama kwamba tumekaribia Uchaguzi Mkuu ilhali bado 2022 ni mbali mno.

Haya yote yatafanya wananchi wakose kuhudumiwa ipasavyo wakati huu ambapo wanakumbwa na changamoto tele za kimaisha hasa ongezeko la gharama ya bidhaa na huduma muhimu za matumizi ya kila siku.

Raia kwa sasa wanahitaji viongozi watendakazi, ambao watajiepusha na kampeni za mapema na kutekeleza wajibu waliochaguliwa kufanya.

Viongozi wanaounga mkono hatua za Rais Kenyatta na Bw Odinga za kuleta umoja na maendeleo kitaifa hawastahili kuonekana wakianguka kwenye mtego wa kampeni za 2022, na kutoa kisababu eti wanasiasa lazima wapige siasa.

‘Team Komboa Kenya’ yajitokeza kukabili ‘Tangatanga’ na ‘Kieleweke’

Na DERICK LUVEGA

SIKU moja baada ya mkutano wa kundi la ‘Kieleweke’kutibuka mjini Kakamega, vuguvugu jingine la kisiasa limejitokeza ili kuyakabili makundi ya ‘Kieleweke’ na ‘Tanga Tanga.’

Kundi hilo, linalojiita ‘Team Komboa Kenya’ linahusishwa na kiongozi wa Chama cha Amani (ANC) Musalia Mudavadi.

Duru zilisema kundi hilo lilibuniwa na washirika wa karibu wa Bw Mudavadi, baada ya mikutano kadhaa ya faragha.

Mbunge wa Sabatia, Alfred Agoi, ambaye ni mshirika wa karibu wa Bw Mudavadi, alithibitisha kubuniwa kwa kundi hilo.

Kwenye mahojiano na ‘Taifa Jumapili’, Bw Agoi alisema kiongozi huyo anafanya mikutano kadhaa jijini Nairobi, ili kuweka mikakati ya uzinduzi wa kundi hilo jijini Kakamega “hivi karibuni.”

Bw Agoi alisema makundi hayo mawili yalibuniwa kumuunga mkono au kumpinga Naibu Rais William Ruto, lakini kundi la ‘Team Komboa Kenya’ litapigania maslahi ya Wakenya.

Mkutano wa kundi la ‘Kieleweke’ ambalo linampinga Dkt Ruto, ulipangiwa kuandaliwa jana mjini Kakamega.

Chama cha Ford-Kenya tayari kimejitenga kuhusika kwa vyovyote katika maandalizi ya mkutano huo. Ilidaiwa kwamba kiongozi wake, Moses Wetang’ula ni miongoni mwa viongozi ambao wangehudhuria.

Duru zilieleza kuwa Bw Mudavadi alitarajiwa kuwa mwalikwa mkuu katika mkutano huo, ambapo angetoa mwelekeo rasmi wa kisiasa wa ukanda wa Magharibi.

Duru zilieleza kuwa, Bw Mudavadi alifutilia mbali mkutano huo dakika za mwisho mwisho, ili kumruhusu kila mmoja kuhudhuria, kwani wanasiasa wengi waliotarajiwa walikuwa mbali.

Na jana, waandani wa Bw Mudavadi walidai mkutano huo ulipangwa na Seneta Cleophas Malala wa Kakamega na mbunge maalum Godfrey Osotsi, wakilenga kuutumia kutafuta muafaka kati ya Otsosi na Mudavadi.

‘Kieleweke’ wamuumbua Ruto kuhusu ufisadi

Na CECIL ODONGO

MAOMBI yaliyoandaliwa na Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi (COTU), Jumapili yaligeuka kuwa jukwaa la wanasiasa wa kundi la Kieleweke kuwavamia wenzao wa Tangatanga ambao wanamvumisha Naibu Rais Willam Ruto.

Wabunge waliohutubu wakati wa maombi hayo yaliyoandaliwa kwenye Kanisa la ACK la St Stephen Cathderal, walimwomba Rais Uhuru Kenyatta kuzidisha vita dhidi ya ufisadi huku wakisifu hatua ya wiki jana ya Kanisa la Kianglikana kusitisha michango ya Harambee.

Mbunge Maalum Maina Kamanda alianzisha mjadala huo kwa kusema viongozi wafisadi nchini wanajulikana peupe na wakati umewadia kwa asasi za kisheria kuwajibika na kuwakamata wahusika.

“Nasifu hatua ya kiongozi wa ACK kukomesha Harambee kwa sababu wanasiasa wanaoleta mabilioni kanisani tunajua ni wafisadi wala hawajapata pesa hizo kwa njia ya ukweli. Hapa Kenya hata ukimuuliza mtoto mdogo kiongozi fisadi zaidi, atakuambia au akuandikie jina la kiongozi fulani pekee,” akasema Bw Kamanda.

Katibu wa COTU Francis Atwoli naye kwa mara nyingine alianika tofauti kati yake na Dkt Ruto, akidai hawezi kushinda kiti cha urais mwaka wa 2022 kwa sababu hawezi kupita mtihani wa maadili.

“Kama hamjatubu, kama hamjakomesha ubabe wenu kwa kutumia kifua, mwaniaji mnayeunga mkono kwa jina la William Ruto hatakuwa Rais mwaka 2022. Ningependa kushukuru serikali ya Rais Uhuru Kenyatta kwa kutoa ulinzi kwetu baada ya baadhi ya wanasiasa maarufu kupanga kuvuruga mkutano wa Lebadei kesho. Mimi nilianza kuhesabu pesa ya mshahara zamani, tafadhali usituambie wewe ni tajiri,” akasema Bw Atwoli.

“Ile serikali ya 2022, watakuwemo Kalonzo Musyoka, Gideon Moi, Musalia Mudavadi, Hassan Joho mimi sitakuwa kwenye serikali kwa sababu siwanii cheo cha kisiasa hata watu wa mkoa wa Kati watakuwa ndani,” akaongeza Atwoli kwenye matamashi makali dhidi ya Dkt Ruto.

Mbunge wa Igembe Kaskazini Maoka Maore pia aliwashutumu wanasiasa wanaotatiza Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI), Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) zinapotekeleza kazi zao.

Hata hivyo, hisia kali zilitanda kanisani humo, pale tofauti za wazi zilipodhihirika kati ya Gavana wa Nairobi Mike Sonko na Mabw Kamanda na Peter Kenneth kuhusu uongozi wa jiji. Bw Sonko aliyeonekana kuhamaki aliwahusisha wawili hao na baadhi ya sakata za ufisadi miaka ya nyuma na hata kuwaonya dhidi ya kumdharau na kukosoa serikali yake bila sababu.

Kinara wa Chama cha Wiper Kalonzo Musyoka akigusia visa dhidi ya ufisadi alisema uovu huo unaporomosha uchumi wa nchi.

Mbunge wa ‘Kieleweke’ anayetumia kila mbinu kuhakikisha Ruto hataingia Ikulu 2022

Na PETER MBURU

NDIYE alikuwa kiongozi wa kwanza kutoka eneo la Mlima Kenya na wa chama cha Jubilee kudai kuwa jamii ya eneo hilo haitamuunga mkono Naibu Rais William Ruto kugombea Urais mnamo 2022.

Hata kabla ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga kuzika tofauti zao kisiasa na kutuliza nchi wakati vurugu zilizidi mwaka jana, Ngunjiri Wambugu-mbunge wa Nyeri Mjini alikuwa ameanza vita na Dkt Ruto.

Akitoa matamshi hayo awali Januari 2018, miezi michache tu baada ya kuchaguliwa kwa mara ya kwanza kama mbunge, Bw Wambugu alisema Dkt Ruto hafai kuwa na uhakika sana kuwa Mlima Kenya utamuunga mkono.

Watu wengi, hata hivyo, walimpuuza kuwa aliyekuwa akitafuta umaarufu na hata viongozi wa eneo hilo wakajitokeza kwa haraka kutuliza hali, kwa kuhakikishia Naibu Rais kuwa kura za eneo hilo ni zake katika uchaguzi ujao.

Lakini Bw Wambugu, mwanaharakati, mwanafunzi wa siasa na mwandishi mpevu, hakuachia hapo kwani tangu wakati huo amekuwa akimshambulia Dkt Ruto kila wakati, kumkosoa kwa takriban kila jambo na hata akaanzisha vuguvugu liitwalo ‘Kitaeleweka’, ambalo sasa linavuma na kumkosesha Naibu Rais usingizi.

Huenda wengi walimpuuza alipoanza, lakini kadri jinsi muda umekuwa ukisonga, vuguvugu lake limekuwa likipata nguvu na uungwaji mkono, sasa likiwa na sehemu ya viongozi kutoka Mlima Kenya na Bonde la Ufa ambao wanaliunga mkono.

Kazi ya Kitaeleweka ni kutaja makosa ya Naibu Rais ama popote anapohusishwa na mambo ya kumchafulia jina, kisha kusema kuwa yataangaziwa mnamo 2022 kuwafanya Wakenya wasimchague.

Bw Wambugu na kundi lake wamekuwa wakimlaumu Dkt Ruto kuwa anaendesha kampeni za mapema kujitafutia umaarufu kabla ya 2022, hali wanayosema inalemaza juhudi za Rais Kenyatta kutekeleza ajenda zake kwa wananchi.

“Hatuna viongozi wawili katika Jubilee, tuna mmoja. William Ruto hana kazi yoyote yake isipokuwa zile anazopewa na Rais. Kwa hivyo, ukiniambia nimuunge mkono, unaniambia nimuunge mkono kufanya nini? Ikiwa namuunga mkono Rais, hiyo ni kumaanisha namuunga mkono naibu wake, lakini tu ikiwa anafanya kulingana na maagizo ya Rais,” mbunge huyo alisema majuzi.

Huu ndio umekuwa msimamo wake, kuwa Dkt Ruto anamkosea Rais heshima, kila wakati akiwa mstari wa mbele kumkosoa.

Ni kiongozi mwenye ujuzi wa kutumia mitandao ya kijamii kupitisha ujumbe, hali ambayo imemfanya kutumia akaunti zake za Facebook na Twitter kila wakati kuvumisha vuguvugu lake la Kitaeleweka.

Bw Wambugu huwa hachelei kumpiga Naibu Rais kisiasa kila fursa inapojitokeza.

“Wakati unavamia handisheki ukiwa wa kutoka Jubilee, mtu unayemvamia ni Uhuru Kenyatta kwani handisheki ilikuwa yake nusu, na ya Raila nusu,” akasema akirejelea Dkt Ruto.

Na kwa namna moja ama nyingine ujasiri wake na athari ambazo umesababisha Mlimani umemfanya kupata marafiki na maadui, hata Dkt Ruto akijipata kumjibu katika mikutano ya hadhara.

Kwa sasa, vuguvugu la Kitaeleweka limevutia viongozi mbalimbali, waliochaguliwa ama wa zamani, ambao wanatofautiana na Dkt Ruto, ndani na nje ya Mlima Kenya.

Wabunge kama Maina Kamanda (Maalum), Muturi Kigano (Kangema), Paul Koinange (Kiambaa) na aliyekuwa naibu mwenyekiti wa Jubilee David Murathe, pamoja na wengine tayari wameunga mkono vuguvugu hilo na kuanza kutoa wito kuwa eneo la Mlima Kenya halitampigia kura Dkt Ruto.

Hii ni licha ya viongozi wengine kutoka Bonde la Ufa ambao wanatofautiana na Naibu Rais kama mbunge wa Cherangany Joshua Kutuny, na viongozi wa chama cha KANU.

Wafuasi wa Dkt Ruto aidha sasa wanatumia kila mbinu kuvamia kundi hilo, ambalo nguvu zake zinapenyeza ndani ya Jubilee na kujiweka kama chaguo la viongozi wote wanaotofautiana na Dkt Ruto.

Mbunge huyo, ambaye alikuwa mwanachama wa ODM kati ya 2012 na 2017 amekuwa akilaumiwa na wafuasi wa Dkt Ruto kuwa anatumiwa na chama hicho kuvuruga Jubilee, lakini yeye anasisitiza kuwa anamtetea Rais Kenyatta.

Akianza hakuwa na upinzani mkubwa, wala uungwaji mkono wowote, lakini jinsi anavamiwa na kuungwa viongozi mashuhuri kwa sasa ni ishara tosha kuwa kile alichoanzisha kinawanyima wengi usingizi, na ishara kuhusu makabiliano yanayosubiriwa mbele.

Wabunge wa kike wa Jubilee wamtaka Rais kuitisha mkutano wa Kundi la Wabunge

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE wa kike wa chama cha Jubilee wamemtaka Rais Uhuru Kenyatta kuitisha mkutano wa Kundi la Wabunge (PG) kujadili migawanyiko ndani ya Jubilee.

Wabunge hao ni wawakilishi wa Wanawake wa kaunti kadha na wengine wa maeneobunge.

Rahab Mukami (Nyeri), Sabina Chege (Murang’a), Faith Gitau (Nyandarua), Joyce Korir (Bomet) na mbunge wa Maragua Mary Njoroge, walisema Jumanne wangetaka Rais Uhuru Kenyatta awaelezee katika mkutano huo ikiwa kuna mabadiliko katika mkataba kati yake na Naibu wake William Ruto.

Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Murang’a katika Bunge la Kitaifa Bi Sabina Chege. Picha/ Maktaba

Walielezea hofu kwamba ufa ndani ya Jubilee unaendelea kupanuka kila uchao wafuasi wa Dkt Ruto wakiendelea kushambuliana na wapinzani wao, wanaojiita Kieleweke.

“Chama cha Jubilee ni kinaunga na tunasimama nyuma ya Rais na naibu wake na tutaendelea kuwaunga mkono bila kuwaogopa wanaoututisha,” Bi Chege akasema mjini Nyeri wakati wa mkutano wa kundi la wanawake wa Kanisa la PCEA, Nyamakia kaunti ya Nyeri.

Lawama

Wakiongea katika mkutano wa kundi la wanawake la Nyamachaki PCEA Women Guild wabunge hao waliwalaumu wenzao Kieleweke kwa migawanyiko inayoshuhudiwa katika chama hicho.

“Ikiwa mgawanyiko katika Jubilee ni rasmi basi kiongozi wetu Rais Kenyatta anafaa kuwajulisha wanachama kupitia mkutano wa PG.

Bila kuwataja majina, wabunge hao walidai kuwa baadhi ya wenzao kutoka Mlima Kenya ndio wanachochea uhasama ndani ya Jubilee kwa kudai kuwa wandani wa Ruto wanamsaliti Rais Kenyatta.

“Tunataraji kwamba Rais ataongozwa na busara na kukoma kukoma kuwasikiliza wale ambao wanaongozwa na chuki,” akasema Bi Chege.

Bi Njoroge alisema eneo la Mlima Kenya lilimpia kuta Rais Kenyatta na Ruto kwa wingi akiongeza kuwa kiongozi wa taifa aliwapa wabunge ruhusa ya kufanyakazi kwa ukaribu na naibu rais.

“Sasa wanatuambia kwamba tukionekana na Naibu Rais hiyo inaonyesha kuwa tunampinga Rais. Nini kimebadilika. Rais anafaa kuitisha mkutano wa PG ili atoe tangazo rasmi kwamba kuna mgawanyiko,” akaeleza.

“Eneo la Mlima Kenya halitamsaliti Naibu Rais,” Bi Njoroge akaongeza.

Bi Korir na Bi Gitau walishikilia kuwa hawata hawatakoma kumuunga azma ya Dkt Ruto ya kuwania urais eti kwa sababu wamepokonywa walinzi.

Wabunge wadai muungano mpya wa kisiasa watokota 2022

STANLEY KIMUGE na WYCLIFF KIPSANG

BAADHI ya viongozi wa Jubilee wameelezea uwezekano wa muungano wa kisiasa kati ya kiongozi wa chama cha ODM, Raila Odinga na mwenyekiti wa Kanu, Gideon Moi kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Wabunge Maoka Maore (Igembe Kaskazini), Peter Mwathi (Limuru) na mbunge maaalum Maina Kamanda waliungana na wenzao wa Kanu William Kamket (Tiaty) na Gladwell Cheruiyot (Baringo) kwenye hafla ya kuchangisha fedha katika kanisa la AIC Churo Girls katika eneobunge la Tiaty mnamo wikendi.

Bw Kamanda alisema aliwahi kuhudumu kama mwenyekiti wa Kanu kwa muda mrefu katika tawi la Nairobi, hivyo hana tatizo kushirikiana na chama hicho.

“Nimesema muunge mkono Kanu, kwani kuna baadhi ya watu waliokuwa wakidai kuwa ndio wanalidhibiti eneo hili kisiasa. Nataka kuwaambia kuwa kesho watakuwa wenye wafuasi wachache na Kanu itakuwa na wengi,” akasema Bw Kamanda.

Mbunge huyo alidai eneo la Kati limebadilisha mwelekeo wake wa kisiasa, ambapo sasa linaunga mkono ajenda ya umoja wa nchi inayoendelezwa na Rais Uhuru Kenyatta, Raila Odinga, Seneta Gideon Moi, kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka, kiongozi wa Chama cha Amani (ANC) Musalia Mudavadi na kiongozi wa Ford-Kenya, Moses Wetang’ula.

“Ikiwa mtawaona baadhi ya wabunge kutoka Kati wakienda kinyume na msimamo huo, mfahamu kuwa wanajitafutia pesa. Wapiga kura wengi wanaunga mkono juhudi za Rais kuleta umoja nchini,” akasema Bw Kamanda katika matamshi yaliyoonekana kulilenga kundi la ‘Tanga Tanga’ ambalo linahusishwa na Naibu Rais William Ruto.

Bi Cheruiyot alisema kuwa, kama wanachama wa Kanu, hawana shida yoyote ikiwa Bw Odinga ama Seneta Moi atakuwa rais.

“Mrengo wetu unaunga mkono handisheki kikamilifu. Kuna baadhi yetu wanaomuunga mkono Odinga, huku wengine wakimuunga Gideon. Tutazungumza na kushauriana,” akasema Bi Cheruiyot.

Kwa upande wake, Bw Maore alisema kuwa wanashirikiana na wenzao katika Kanu kwa kuwa ni “marafiki wao wa zamani.”

“Kuna tofauti kubwa kati yetu tuliyo katika Team Kenya na wengine (Team Tanga Tanga). Sisi ni marafiki wa Kanu na tumekuja hapa kuwaambia kwamba ufisadi ndilo suala kuu linalomsumbua Rais Kenyatta kwa sasa,” akasema Bw Maore.

Seneta Moi alikuwa ametarajiwa kuhudhuria hafla hiyo lakini akatuma mchango wake kupitia Bw Kamket.

Bw Kamanda alisema kwamba Rais Kenyatta alimteua kama mbunge maalum baada ya kunyang’anywa ushindi wake na baadhi ya watu katika JP.

“Ninajua kuwa nilishinda uchaguzi huo lakini nikanyang’anywa na baadhi ya watu walio chamani. Hata hivyo, rais alinionea imani kwa kunirejesha tena Bungeni,” akasema.

Ijumaa iliyopita, baadhi ya viongozi, wakiongozwa na Seneta wa Nandi Samson Cherargei na mbunge wa Mumias Mashariki Benjamin Washiali walikitaka chama hicho kuwachukulia hatua viongozi wanaozua migawanyiko chamani.

Walisema kuwa lazima Bw Kamanda anyang’anywe wadhifa wake, kwani ni miongoni mwa watu wanaokigawanya chama.