Jagina wa soka raia wa Senegal, Papa Bouba Diop aaga dunia

Na MASHIRIKA

NYOTA wa zamani wa Fulham, Portsmouth na timu ya taifa ya Senegal, Papa Bouba Diop aliaga dunia mnamo Novemba 29, 2020 akiwa na umri wa miaka 42.

Diop aliyewahi kuchezea pia West Ham United na Birmingham City, aliwajibishwa mara 129 katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Alikuwa sehemu ya kikosi kilichotegemewa na Senegal katika fainali ya Kombe la Dunia mnamo 2002 na akafunga bao la pekee katika ushindi wa 1-0 uliosajiliwa na Senegal katika mchuano wa ufunguzi wa kivumbi hicho dhidi ya mabingwa watetezi Ufaransa.

“Diop alikuwa shujaa wa Kombe la Dunia. Hivyo ndivyo tunavyomjua,” ikasema sehemu ya taarifa iliyotolewa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) kwenye mtandao wao wa kijamii.

Kwa upande wao, Fulham walitumia mtandao wao wa Twitter kumwomboleza Diop. Usimamizi wa kikosi hicho ulisema: “Ni masikitiko makubwa kumpoteza Diop ambaye hapa kikosini tulimfahamu kama ‘Wardrobe’.

Ushawishi wa Diop uwanjani uliwasaidia Senegal kutinga hatua ya robo-fainali za Kombe la Dunia mnamo 2002 huku Diop akifunga mabao mawili zaidi katika sare ya 3-3 iliyosajiliwa na kikosi chake dhidi ya Uruguay kwenye hatua ya makundi.

Kabla ya kustaafu soka mnamo 2013, Diop alikuwa amenogesha fainali nne za Kombe la Afrika (AFCON) na alikuwa sehemu muhimu katika kikosi cha Senegal kilichoambulia nafasi ya pili kwenye kipute hicho mnamo 2002.

Diop alichochea pia Portsmouth kunyanyua ubingwa wa Kombe la FA mnamo 2008 chini ya mkufunzi Harry Redknapp.

“Kufa kwa Diop ni pigo kubwa kwa Senegal, makuzi na maendeleo ya soka ya taifa hilo,” akasema fowadi wa Liverpool Sadio Mane katika kauli iliyoshadidiwa na Rais wa Senegal, Macky Sall.

Huzuni watu 10 wakifa maji ziwani

Na DICKENS WASONGA

BIWI la simanzi lilitanda katika ufuo wa Ziwa Victoria, eneo la Bondo, Kaunti ya Siaya baada ya watu 10 kufa maji usiku wa kuamkia Jumatano.

Kufikia Jumatano, maafisa kutoka idara ya ulinzi wa pwani za Kenya walikuwa wanaendelea kutafuta miili ya waliozama.

Kamanda wa Polisi katika Kaunti ya Siaya, Bw Francis Kooli alithibitisha kisa hicho.

Bw Kooli alisema kwamba merikebu hiyo ilikuwa na abiria 20 wakati ilipozama saa tano usiku Jumanne.

Chombo hicho kiligongwa na mawimbi makali yaliyoandamana na dhoruba na kuzama karibu na eneo la Muda katika ufuo wa Honge, mjini Bondo.

Kisa hicho kiliripotiwa kwa polisi katika Ufuo wa Usenge na Bw Zachary Masinde ambaye ni mwenyekiti wa ufuo wa Honge.

“Kulingana na mwenyekiti huyo wa ufuo, merikebu ya Uganda ilikuwa inatoka kwenye ufuo unaofahamika kama Ufuo wa Nairobi katika taifa hilo jirani, ikiwa imebeba abiria 20,” alisema Bw Kooli.

Abiria hao walikuwa wafanyabiashara waliokuwa wamebeba ndizi na matunda wakielekea katika ufuo wa Usenge.

“Mawimbi makali yaligonga boti hiyo ilipokuwa ikikaribia ufuo wa Honge. Ilizama mara moja,” alisema.

Bw Masinde alieleza Taifa Leo kwamba watu 10 waliokolewa na wavuvi waliokuwa ziwani humo kwenye shughuli za uvuvi.

“Kwa bahati nzuri kulikuwa na wavuvi waliokuwa karibu na wakamudu kuwaokoa baadhi ya abiria,” alisema.

Polisi waliwatambulisha walionusurika mkasa huo kama Bw Sadam Idrissa, 44, Bw Mathius Stephen, 62, Bw Henry Shitindi, 33, Bw Kudamba Issa, 42, na Bw Wafula James 39.

Wengine ni pamoja na Bi Annette Kawara, 42, Bi Morine Amukula, 22, Bw Alex Opiyo, 36, Bw Kevin Kalai, 42, na Hailat Kauma, 30, wote ambao ni raia wa Uganda.

Waliozama walijumuisha nahodha wa merikebu hiyo.

Afa lojing’i akiwa na jamaa

Na MWANDISHI WETU

POLISI jijini Nairobi wanachunguza kisa ambapo mwanamke aliaga dunia baada ya kuugua akiwa katika lojing’i na shemejiye wa kiume.

Mwanamke huyo aliyekuwa na umri wa miaka 42, aliaga dunia punde alipofikishwa katika Hospitali Kuu ya Kenyatta kwa teksi, kutokana na kukohoa na kutapika.

Taarifa za polisi zinasema mama huyo ambaye huishi Mwiki, Kasarani, alifika jijini mwendo wa saa moja unusu usiku kukutana na kaka wa mumewe, aliyekuwa amesafiri kutoka Malindi.

“Walikodisha chumba cha malazi katika hoteli iliyoko barabara ya Dubois siku ya Alhamisi. Asubuhi mwendo wa saa kumi na mbili, mwanamke huyo alianza kukohoa na kutapika,” ikasema taarifa ya polisi.

Shemejiye alichukua teksi na kumkimbiza KNH ili atibiwe, lakini madaktari wakatangaza kuwa alikuwa tayari amekufa.

Polisi walisema wanangojea ripoti ya upasuaji wa maiti kujua kiini cha kifo cha mwanamke huyo.

Familia yataka ripoti ya daktari kuhusu mtoto wao aliyefariki

Na SAMMY KIMATU

skimatu@ke.nationmedia.com

MTOTO wa umri wa miaka tisa alifariki Jumatano katika kisa chenye utata katika mtaa mmoja wa mabanda kaunti ya Nairobi.

Kisa hicho kilitokea mwendo wa saa kumi na moja za jioni katika mtaa wa mabanda wa Mukuru-Kayaba ulioko wodi ya Landi Mawe katika kaunti ndogo ya Starehe.

Polisi walitambua mtoto huyo kwa jina David Nyabera, mwanafunzi wa darasa la tano katika Shule ya Msingi ya Mukuru.

Kwa mujibu wa mamake marehemu, Bi Rose Nyanjama, 32, mwanawe alikuwa ameenda kwa kakake mkubwa akiambatana na dadake kabla ya kifo chake kutokea.

“Alikuwa mchangamfu. Tulishiriki naye chakula cha mchana na kisha nikamtuma kununua kuni za kupika chipsi, ‘’ Bi Nyanjama, mchuuzi wa vyakula mtaani humo akasema.

Aliongeza kwamba mtoto wake hajawahi kuwa na historia ya ugonjwa wowote wala hakuwa na dadili ya maradhi kabla ya kufariki.

Babake marehemu, Bw Charles Nyabera, 58 aliiambia Taifa Leo kwamba marehemu aliambatana na dadake kwenda kwa kakao mkubwa kumtembelea takribani mita 200 kutoka kwao.

“Aliondoka hapa kwetu eneo la Budalangi-Cluster ‘A’ na wakiwa ndani ya nyumba kwa kaka yao, akaanguka na kuzirai papo hapo,” Bw Charles asema.

David Nyabera, aliyekuwa mwanafunzi wa darasa la tano katika Shule ya Msingi ya Mukuru. PICHA/ SAMMY KIMATU

Majirani pamoja na mamake walipoarifiwa kuhusu tukio hilo, walimpeleka mwanafunzi huyo katika kliniki moja mtaani.

“Alikuwa akitokwa na pofu iliyochanganyika na damu kutoka mapuani na mdomoni. Tulijaribu kumpea huduma ya kwanza lakini akakata roho,” muuguzi katika zahanati akaeleza.

Msemaji wa familia hiyo ambaye kadhalika ni mwenyekiti wa bodi ya Shule ya Msingi ya Mukuru, Bw Peter Okari alisema watasubiri ripoti ya daktari wa upasuaji ili wabaini kilichosababisha kifo cha mwanao.

‘’Kama familia, hatutaki habari sisizo sahihi kuenezwa mtaani hadi pale daktari atatoa ripoti yake baada ya upasuaji wa mwili wa marehemu kufanyika,” Bw Okari akanena.

Akizungumza katika boma ya marehemu, mwenyekiti wa usalama katika mtaa huo, Bw Jacob Ibrahim aliwaonya wenyeji kutosabaza habari za uwongo kuhusu tukio hilo.

Vilevile, aliwashauri wazazi kuhakikisha wamewacha wanao wakiwa kwenye ulinzi wa watu wazima wanapoelekea maeneo tofauti kufanya kazi zao za kila siku.

“Watoto wako katika likizo ndefu kufuatia janga la Corona. Ni muhimu wazazi kuhakikisha watoto wao wako salama nyumbani kabla ya kuelekea kazini,” Bw Jacob akanena.

Maafisa wa polisi kutoka kituo cha polisi cha Industrial Area walipeleka mwili wa marehemu katika chumba cha kuhifadhi maiti cha City.

Mwaka huu, watoto wanne kutoka mtaa wa Mukuru wamefariki wakiwa nyumbani tangu shule zilipofungwa baada ya janga la corona kutangazwa nchini.

Katika kisa cha kwanza, mvulana wa darasa la saba aligongwa na gari katika barabara ya Entreprise, Eneo la Viwandani.

Fauka ya hayo, msichana wa kidato cha pili katika Shule ya upili ya St Michael alifariki akiwa maeneo ya mashambani katika Kaunti ndogo ya Mbooni East.

Isitoshe, mwanafunzi wa mwaka wa pili katika Our Lady of Mercy Vocational Training Centre aliuawa na raia kwa kushukiwa kuwa mhalifu katika mtaa huo.

Ripoti ya visa vyote hivyo ilitolewa kutoka ofisi kuu ya Mukuru Promotion Centre (MPC).

MPC ni shirika la misingi ya dini linaloendeshwa na Watawa wa Mercy kutoka Ireland (Irish Sisters of Mercy).

Kadhalika, MPC ndilo mdhamini rasmi wa shule ya Msingi ya Mukuru na ya Upili ya St Michael na Chuo cha Mafunzo ya Ufundi cha Our Lady of Mercy.

Wakashifu tukio ambapo baba na wanawe wawili waliuawa kwa tuhuma za kujihusisha na al-Shabaab

Na MISHI GONGO

BAADHI ya viongozi wa dini ya Kiislamu Kusini mwa Pwani wamekashifu tukio la mauaji ya baba na wanawe wawili eneo la Diani wiki iliyopita kwa tuhuma walikuwa na mafungamano na kundi la al-Shabaab.

Viongozi hao kutoka baraza la maimamu na wahubiri nchini CIPK, KEMNAC, Supkem, na Shirika la vijana wa Kiislamu KMYA na muungano wa madrasa kanda ya Kusini mwa Pwani wameyataja mauaji hayo kuwa ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.

Mwenyekiti wa CIPK Kusini mwa Pwani, Sheikh Amir Zani ametaka kusimamishwa kazi kwa mkuu wa kituo cha polisi cha Diani pamoja na polisi waliohusika na mauwaji kushtakiwa.

“Serikali inapaswa kuwachukulia hatua maafisa waliotekeleza unyama huo ili kuwa funzo,” akasema.

Kwa upande wake mshirikishi wa vijana wa Supkem Kusini mwa Pwani Hamis Mwaguzo ametaja kuwa kinyume cha sheria kuwahusisha watoto na visa vya ugaidi, ikizingatiwa hawana ufahamu wowote kuhusu ugaidi.

“Watoto wasio na hatia wamepoteza maisha yao. Hawa watoto hawajui chochote kuhusu ugaidi,” akasema.

Ameitaka Mamlaka ya Kutathimini Utendakazi wa Polisi (Ipoa), kuchunguza mauaji hayo na kuwachukulia hatua maafisa waliotekeleza.

TANZIA: Mwanamuziki John Nzenze aliyevumisha ‘twisti’ afariki

Na DERICK LUVEGA

MWANAMUZIKI John Nzenze aliyeimba wimbo maarufu wa ‘Angelike’ amefariki hospitalini Mukumu alikokuwa amelazwa kwa kipindi cha mwezi mmoja.

Binamu yake Bw Sammy Ingati amethibitisha akisema amekuwa katika hospitali ya St Elizabeth Mukumu alikokuwa akipokea matibabu.

Nzenze aliyezaliwa mwaka wa 1940 Muthurwa, Nairobi amefariki akiwa na umri wa miaka 80.

“Nzenze ambaye aliimba nyimbo za kuelimisha jamii amefariki leo Jumamosi saa nane mchana,” amesema Bw Ingati akiitaka serikali kuifaa familia ya mwendazake wakati huu mgumu wa kumpoteza mpendwa.

Marehemu alikuwa maarufu sana hasa kutambulisha muziki wa mtindo wa ‘twisti’ miaka ya sitini (1960s).

Legnano na Atalanta zathibitisha kifo cha kiungo chipukizi Andrea Rinaldi

Na CHRIS ADUNGO

KIUNGO Andrea Rinaldi, ameaga dunia kutotakana na matatizo ya ubongo aliyoyapata wakati akishiriki mazoezi mepesi nyumbani kwake.

Matatizo hayo yalianza Ijumaa wiki jana.

Rinaldi aliwahi kuwa sehemu ya kikosi chipukizi cha Atalanta kwa kipindi kirefu na amewahi kuchezea kikosi cha Legnano katika soka ya daraja la chini nchini Italia. Baadhi ya vianzo kama shirika la Ansa vinasema amekuwa mali rasmi ya Legnano baada ya kununuliwa. Hata hivyo baadhi vimesema amekuwa huko kwa mkopo msimu huu.

“Ushawishi wake ulikuwa wa kuhisika uwanjani kila mara. Awe na mpira au la. Alifahamu jinsi ya kutangamana vyema na watu. Alipenda kila watu na akapendwa na kikosi kizima kwa kiwango sawa,” ikasema sehemu ya taarifa iliyotolewa na Atalanta.

Kwa upande wao, viongozi wa kikosi cha Legnano walisema, “Kifo cha Rinaldo kimetupiga pute johari adimu. Ametutoka ghafla na kutuachia pengo kubwa katika ulingo wa soka. Yasikitisha sana kifo chake kimekuwa cha kushangaza na kuondoka bila ya kuwaaga wenzake. Ni muhali sana kuamini au hata kufikiria kuwa hayuko nasi tena.”

Legnano ambao walithibitisha pia kiini cha kifo cha Rinaldi, walisema kwamba “sogora huyo aliwaarifu kwamba alikuwa hajihisi vizuri kwa kipindi cha siku tatu ila hapakuwa na lolote kubwa ambalo wangeweza kumfanyia.”

Vyombo vya habari nchini Italia viliripoti kwamba Rinaldo aliaga dunia akitibiwa katika hospitali ya Varese asubuhi ya Mei 11, 2020.

Rinaldi aliingia katika sajili rasmi ya Atalanta akiwa na umri wa miaka 13 pekee na akaichochea klabu hiyo ya Ligi Kuu ya Italia (Serie A) kunyanyua ubingwa wa Super Cup kwa chipukizi wasiozidi umri wa miaka 17 mnamo 2016.

Aliwahi pia kuwajibikia vikosi vya Imolese na Mezzolara kwa mkopo kabla ya kutua Legnano aliowachezea katika jumla ya mechi 23 na kuwafungia bao moja msimu huu.

COVID-19: Idadi ya Wakenya waliofariki ughaibuni yafika 20

Na CHARLES WASONGA

WIZARA ya Mashauri ya Kigeni imethibitisha kuwa jumla ya Wakenya 20 wamefariki kutokana na sababu zinazohusishwa na Covid-19.

Kwenye taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Jumapili, wizara hiyo ilisema kuwa Wakenya walipoteza maisha yao licha ya juhudi zilizochukuliwa kuwaokoa.

“Kati ya vifo hivyo 20, Wakenya 10 walifariki nchini Amerika, wanne wakafiriki nchini Uingereza, wawili nchini Italia huku Mkenya mmoja akifariki katika kila moja ya mataifa ya Uswisi, Saudi Arabia na Uswidi,” taarifa hiyo ikasema.

Wizara hiyo ilisema kuwa imekuwa ikiwasiliana na afisi za ubalozi wa Kenya katika mataifa ya kigeni kila mara tangu mlipuko wa ugonjwa huo ulipotokea.

Takwimu za wizara hiyo zinasema kuwa zaidi ya Wakenya milioni tatu wanaishi ughaibuni, wengi wao wakiwa Amerika Kaskazini (400,000), Mashariki ya Kati (150,000), Asia na Australia (30,000) huku wengine wakiwa Magharibi mwa Uropa na Kusini mwa Afrika.

Wizara hiyo iliongeza kuwa Wakenya wengi walioko mataifa ya kigeni wamekuwa wakijaribu kusaka usaidizi kutoka kwa serikali kuhusiana na haja ya kurejea nyumbani.

“Wizara imekuwa ikiwasaidia wale waliokwama ng’ambo kufuatia kusitishwa kwa safari za kigeni katika mataifa hayo. Wale ambao wanaweza kujilipia nauli zao wataendelea kusaidiwa kurejea nchini,” taarifa hiyo ikasema.

Mnamo Jumapili asubuhi ndege ya Kenya Airways iliyokuwa imewabeba Wakenya 165 ilitua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) kutoka Guangzhou, China.

“Wengi wa waliorejea kutoka China ni Wakenya walioathirika na mlipuko wa virusi vya corona na kupoteza ajira. Wengine ni wanafunzi waliokamilisha masomo na wafanyabiashara waliozuiliwa huko kwa sababu ya changamoto za usafiri wa ndege.

Walipowasili nchini Wakenya hao walipelekwa katika vituo vya karantini walivyovichagua japo watakuwa chini ya uangalizi wa madaktari kwa muda wa wiki mbili.

TANZIA: Dereva wa klabu ya Gor Mahia afariki

Na CECIL ODONGO

JUMUIYA ya klabu ya Gor Mahia imempoteza dereva wao wa muda wa miaka mingi Bw Patrick Osewe Agwambo aliyefariki Jumatano usiku.

Aliaga dunia njiani akisafirishwa kupokea matibabu zaidi katika eneo la Karachuonyo, Kaunti ya Homa Bay.

Alikuwa akiishi Kibra, Nairobi na amekuwa akikabiliwa na matatizo ya kiafya.

Ameugua kwa muda mrefu.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa benchi ya kiufundi wa Gor Jolawi Obondo, mwili wa marehemu upo kwenye mojawapo ya chumba cha kuhifadhia maiti eneo la Karachuonyo.

“Ni kwa masikitiko makuu tunatangaza kifo cha dereva wetu wa miaka mingi Patrick Osewe ‘Agwambo’. Aliaga dunia Jumatano baada ya kuugua kwa muda mrefu. Tafadhalini wekeni familia yake na jamaa kwa maombi. #Sirkal,” imesema taarifa ya klabu kwenye mitandao ya Facebook na Twitter.

Obondo alifichua kwamba alizungumza na marehemu Jumanne alipokuwa akiwalipa wachezaji na wanachama wa benchi ya kiufundi mishahara yao, na marehemu akamwambia hakuwa akijihisi vyema kiafya.

“Nilikuwa nimempokeza Samuel Onyango (mshambuliaji) fedha zake ili amfikishie kwa sababu wao ni marafiki wa karibu sana. Alikuwa mtu aliyependa kazi yake, mwenye utu na tutapeza sana huduma zake. Tunaomba Mwenyezi Mungu ailaze roho yake pahala pema penye wema,” akasema Obondo.

Nahodha wa Gor Kenneth Muguna aliwaongoza wachezaji wenzake kumwomboleza Osewe ambaye alipokezwa jina la msimbo ‘Agwambo’ kutokana na jinsi alivyoenzi siasa za Kinara wa ODM Raila Odinga ambaye pia ni mlezi wa klabu.

“Nimesikitika sana kusikia kifo cha Patrick Osewe dereva wa basi la timu yetu. Alikuwa mtu mpole, mkarimu, mwenye nidhamu na aliyekuwa na mlahaka mzuri na wachezaji. Tutampeza sana,” akasema Muguna.

Osewe aliajiriwa na Gor mnamo 2012 na amemwacha nyuma mjane pamoja na watoto wawili, mmoja wa kike na mwingine wa kiume.

Kifo cha Osewe kinajiri siku chache tu baada ya kile cha jagina wa K’Ogalo Martin Ouma ‘Ogwanjo’ Jumamosi iliyopita.

Ogwanjo ambaye alijizolea sifa kwa ustadi wake wa kuwapitisha wapinzani chenga za mauaji alizikwa mnamo Jumanne katika kijiji cha Hawinga, eneobunge la Alego Usonga, Kaunti ya Siaya.

 

Jagina wa Gor afariki, mazishi ni Jumanne

Na CECIL ODONGO

JAGINA wa Gor Mahia Martin Ouma ‘Ogwanjo’ ambaye aliaga dunia mnamo Jumamosi asubuhi akiwa na umri wa miaka 71, atazikwa mnamo Jumanne nyumbani kwake kijiji cha Hawinga, eneobunge la Alego Usonga, Kaunti ya Siaya.

Kulingana na mwanawe Tom Ouma, marehemu aliaga dunia baada ya kuugua kiharusi na mwili wake ukapelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Bama mjini Siaya.

“Babangu amekuwa akiugua kiharusi kwa muda wa miaka mitatu iliyopita. Alianguka na kuaga dunia akiwa nyumbani. Mipango ya mazishi inaendelea na atafukiwa mchangani mnamo Jumanne inshallah,” Tom akaeleza ‘Taifa Leo’.

Ouma atakumbukwa kwa kuongoza Gor Mahia kufika fainali ya Kombe la Klabu Bingwa Afrika (CAF winners cup) mnamo 1979 ambapo walipoteza 2-0 nyumbani na 4-0 ugenini.

Aliongoza Gor Mahia kushinda taji la Ligi Kuu (KPL) bila kushindwa mnamo 1976.

Pia alikuwa kati ya wachezaji walioshiriki Kombe la Taifa Bingwa Afrika na timu ya taifa Harambee Stars mnamo 1972.

Nahodha wa kikosi cha Gor Mahia kilichoshinda Kombe la Mandela Barani Afrika mnamo 1987, Austin Oduor ‘Makamu’ alisema Ouma ambaye walikuwa naye kwenye kikosi cha 1980, alikuwa mchezaji mahiri ambaye alijituma sana akiwa uwanjani kuhakikisha timu yake inapata ushindi.

“Alikuwa mchezaji aliyejaliwa talanta ya kuwachenga madifenda na kutoa pasi za uhakika. Wao ndio walivumisha Gor enzi hizo wakiwa na rafiki yangu Allan Thigo. Kando na kucheza naye kabla aondoke Gor mwisho wa msimu wa 1980, nilicheza dhidi yake akiwa K’Ogalo nami nikiwa Luo Stars 1978,” akasema Oduor.

Akaongeza: “Nilikutana naye mara ya mwisho mnamo 2017 uga wa Kasarani tulipoalikwa kama majagina kutazama debi ya Mashemeji.”

Kutokana na agizo la serikali inayopiga marufuku mikusanyiko ya watu katika maeneo ya umma kutokana na virusi vya corona, ni familia yake na jamaa wachache watakaohudhuria maziko yake.

Hospitali yajiondolea lawama kifo cha Walibora

Na CHARLES WASONGA

AFISA Mkuu Mtendaji wa Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) Dkt Evanson Kamuri amekana madai kuwa wahudumu wa hospitali hiyo walimtelekeza mwandishi mahiri Prof Ken Walibora alipofikishwa huko kwa matibabu Aprili 10.

Dkt Kamuri akihojiwa Jumatatu amewaelezea wanachama wa Kamati ya Seneti kuhusu Afya hatua kwa hatua jinsi Profesa Walibora alivyopoteza maisha yake katika hospitali hiyo huku madaktari wakijizatiti kadri wawezavyo kumnusuru.

“Madaktari wetu walijaribu kadri ya uwezo wao kuokoa maisha ya Profesa Walibora lakini kwa bahati mbaya alifariki,” Dkt Kamuri amewaambia wanachama wa kamati hiyo wakiongozwa na mwenyekiti wao Seneta wa Trans Nzoia Michael Mbito kwenye mkutano ulioendeshwa kwa njia ya video ya Zoom.

Kulingana na Dkt Kamuri, Walibora alifikishwa katika KNH na ambulensi ya Serikali ya Kaunti ya Nairobi saa tatu na dakika 53 asubuhi, Aprili 10, 2020, ambapo alitambuliwa kama Mwanamume Mwafrika asiyejulikana.

“Mgonjwa alikuwa akivuja damu na alikuwa na majeraha mabaya kichwani. Alihudumiwa katika kitengo cha wagonjwa waliojeruhiwa vibaya ambacho kina vifaa sawa na vilivyoko katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU),” ameeleza Dkt Kamuri.

Ameongeza kuwa Profesa Walibora alikaa katika eneo hilo hadi saa kumi za jioni, akihudumiwa, kisha akawekwa katika chumba chenye mitambo ya kumsaidia kupumua.

Dkt Kamuri amewaambia maseneta hao kwamba hali ya marehemu Profesa Walibora ilikuwa mbaya zaidi mwendo wa saa mbili za usiku kutokana na majeraha aliyopata kichwani; hali iliyomfanya kushindwa kupumua.

“Lakini kwa mara nyingine madaktari waliweza kumsaidia akapata uwezo wa kupumua,” ameongeza.

Lakini ilipotimu saa sita na dakika 10 za usiku, Dkt Kamuri amesema, hali ya Walibora ilidhoofika zaidi kutokana na hali kwamba damu iliingia ubongoni mwake.

“Na mwendo wa saa saba na dakika 10, muda wa saa moja baadaye ambapo tulimpoteza,” akasema.

Dkt Kamuri alisema madaktari waliomhudumia Profesa Walibora kwa muda huo wote walikuwa; Dkt Rono, Dkt Sigilai na Dkt Okutoyi.

“Dkt Okutoti ni mtaalamu katika utabibu wa majeraha mabaya, na alisaidiana na wauguzi pamoja na wahudumu wengine wa afya ambao walikuwepo katika Hospitali Kuu ya Kenyatta,” ameeleza alipokuwa akijibu maswali kutoka kwa maseneta; Fred Outa (Kisumu) na Beth Mugo (Seneta Maalum).

Dkt Kamuri amesema kuwa hospitali ya KNH huwa haibagui wagonjwa na kwamba ilimhudumia Walibora ipasavyo licha ya kwamba hakuwa ametambuliwa rasmi na hakuletwa huko na jamaa zake.

“Kwa hivyo, madai kwamba hospitali hii ilimtelekeza Profesa Walibora sio kweli hata kidogo,” akasisitiza.

“Katika KNH, mgonjwa anapoletwa, huwa hatujali kama una pesa au kadi ya NHIF au hadhi yako katika jamii. Kitu cha kwanza tunachofanya ni kutoa huduma za kwanza za kumtuliza mgonjwa kabla ya kuuliza malipo kwa sababu unaweza tu kulipwa ukiwa hai,” akaongeza.

COVID-19: Mkenya afariki nchini Saudi Arabia

Na CHARLES WASONGA

MKENYA amefariki kutokana na ugonjwa wa Covid-19 nchini Saudi Arabia, kulingana na balozi wa Kenya nchini humo Peter Ogego.

“Balozi Ogego ametuarifu kuwa tulimpoteza Mkenya mmoja aliyeambukizwa virusi vya corona. Hiki ni kisa cha kwanza kuhusu Wakenya nchini Saudi Arabia,” Mohamed Weliye, Mkenya ambaye ni mshauri katika Mamlaka ya Masuala ya Kifedha, Saudi Arabia, akasema kupitia Twitter.

Awali, iliripotiwa kuwa balozi Ogego alitoa taarifa akiwashauri Wakenya nchini humo kuzingatia kanuni zilizowekwa na serikali hiyo kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona.

Alisema ubalozi huo umesitisha shughuli zake za kawaida kwa muda usiojulikana. Wafanyakazi walihitajika kufanya kazi kupitia mtandao.

“Hii ni kulingana na juhudi za kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona na kupunguza hatari ya wahudumu na wateja kuambukizwa,” akasema.

Kifo cha Mkenya nchini Saudi Arabia kinafikisha 10, idadi ya Wakenya ambao wamefariki katika mataifa ya kigeni kutokana na Covid-19.

Sita wamefariki nchini Amerika huku wawili wakifariki nchini Uingereza.

Katibu katika Wizara ya Mashauri ya Kigeni Macharia Kamau wiki jana aliiambia Kamati ya Bunge kuhusu Ulinzi na Mahusiano ya Kigeni kwamba Wakenya watano waliofariki Amerika walikuwa na matatizo mengine ya kiafya ambayo yalichangia vifo vyao baada ya kuambukizwa virusi vya corona.

Hata hivyo, hamna Wakenya ambao wamefariki kutokana na Covid-19 nchini China ambako ndiko chimbuko la ugonjwa huo ambao tayari umewaua zaidi ya watu 200,000 kote duniani na 14 nchini Kenya.

Malaria kuua Wakenya elfu 44 juhudi zote zikielekezewa corona – WHO

Na PAULINE KAIRU

SHIRIKA la Afya Duniani (WHO), limeonya kuwa idadi ya vifo vinavyotokana na malaria huenda vikaongezeka maradufu Kenya na mataifa mengine ya Afrika kwani rasilimali nyingi zimeelekezwa kwa vita dhidi ya virusi vya corona.

Shirika la WHO linakadiria kuwa idadi ya vifo vinavyotokana na malaria itaongezeka hadi 769,000 barani Afrika mwaka 2020.

Jumla ya vifo 360,000 vya malaria viliripotiwa barani Afrika mnamo 2018, ambapo -Kenya ilipoteza watu 22,000 mwaka huo kutokana na malaria.

Kufikia sasa watu 14 wamekufa kutokana na Covid-19 nchini tangu mwezi Machi.

Mkurugenzi wa WHO barani Afrika Matshidiso Moeti, Jumamosi alihimiza mataifa ya Afrika kuendeleza juhudi za kukabiliana na malaria.

“Uchunguzi wa WHO umegundua kuwa ikiwa serikali za Afrika zitalegeza kamba katika vita dhidi ya malaria, vifo vinavyotokana na maradhi hayo vitaongezeka maradufu mwaka huu ikilinganishwa na 2018,” akasema afisa huyo.

Kiongozi wa kundi la waataalamu wa afya wanaoshughulikia malaria katika shirika la WHO, Dkt Akpaka Kalu, alisema kuwa dalili za ugonjwa wa corona na malaria zinafanana, hivyo huenda zikakanganya wahudumu wa afya.

Alitaka watu walio na dalili za virusi vya corona pia kupimwa malaria.

Alisema kuwa msimu huu wa mvua utasababisha ongezeko la visa vya malaria, na huenda waathiriwa wa ugonjwa huo unaoenezwa na mbu wakadhaniwa kuwa wagonjwa wa Covid-19.

“Tunahofia kuwa visa vya malaria vitaongezeka kwani mataifa mengi ya Afrika yanaingia kwenye msimu wa malaria. Visa vya malaria huwa vingi kati ya Julai na Septemba,”akasema.

“Ugonjwa wa malaria pia husababisha mwathiriwa kuwa na joto jingi sawa na virusi vya corona. Dalili nyingine za malaria ambazo hujitokeza kwa waathiriwa wa virusi vya corona ni uchovu, maumivu ya tumbo na kuhara. Hiyo ndiyo maana tunasema kuwa mtu akipatikana na joto jingi mwilini apimwe virusi vya corona na malaria,”akaongezea.

Shirika la WHO lilisema kuwa limepokea ripoti kuwa watu wanaoenda hospitalini wakiwa na malaria hawatibiwi na badala yake wanatumwa kupimwa virusi vya corona.

Idadi ya wastani

Mtu mmoja hufariki kutokana na maradhi ya malaria kila baada ya dakika mbili barani Afrika.

Wastani wa watu 200 milioni huugua malaria kila mwaka.

“Tumepokea ripoti kuhusu wahudumu wa afya wanaokimbia mgonjwa wa malaria anapofika hospitalini kutafuta matibabu ya malaria wakidhani ni corona,” akasema Dkt Kalu.

Kumekuwa pia na ripoti za wahudumu wa afya kuwapuuza watu wanaougua maradhi mengine wakisema wanashughulikia tu walio na corona.

Seneti kuchunguza kifo cha Walibora

Na CHARLES WASONGA

BUNGE la Seneti Jumatatu litaanzisha uchunguzi kuhusu kifo cha mwandishi hodari na mwanahabari marehemu Profesa Ken Walibora.

Kamati ya Seneti kuhusu Afya imemwagiza Afisa Mkuu Mtendaji wa Hospitali Kuu ya Kenyatta (KNH) Dkt Evans Kamuri kujibu maswali kuhusu madai kuwa Walibora alitelekezwa na wahudumu wa hospitali hiyo alipowahiwa huko baada ya kugongwa na matatu.

Kamati ya Seneti kuhusu Afya inayoongozwa na Seneta wa Trans Nzoia Michael Mbito inafuatilia ripoti kwamba marehemu Profesa Ken Walibora alifariki baada ya kutelekezwa katika kitengo cha kuwapokea majeruhi cha KNH.

“Kamati hiyo imemwagiza Afisa Mkuu Mtendaji wa hospitali hiyo kufika mbele yake Jumatatu, Aprili 27, 2020, ili aeleze kilichotokea katika kitengo cha majeruhi cha hospitali hiyo huku uchunguzi wa kifo hicho ukianza,” Seneti ikasema Ijumaa kupitia ukurasa wa akaunti ya Twitter.

Kando na Dkt Mbito, wanachama wengine wa kamati hiyo ni; Abdullahi Ibrahim (Wajir), Beth Mugo (Seneta Maalum), John Kinyua (Laikipia), Falhada Iman (Seneta Maaulum) Eric Mogeni (Nyamira), Petronilla Lokorio (Seneta Maaulum), Naomi Masitsa (Seneta Maaulum) na Fred Outa (Kisumu).

Profesa Walibora ambaye ni mwandishi wa riwaya maarufu ya ‘Siku Njema’ miongoni mwa kazi zingine za fasihi alifariki mnamo Ijumaa, Aprili 10, 2020, baada ya kugonjwa na matatu katika barabara ya Landhies, Nairobi.

Polisi wanachunguza chanzo cha kifo chake baada ya mpasuaji mkuu wa maiti aliye chini ya ajira ya serikali Johannsen Oduor kugundua kuwa kando na majeraha ya kugongwa na gari alidungwa na kifaa chenye makali kama ya kisu katika mkono wake wa kulia.

Baadhi ya watu waliokuwepo pahala pa mkasa waliwaambia wanahabari wa runinga kwamba marehemu alikuwa akikimbizwa na watu fulani na ndipo akagongwa na matatu akivuka barabara ya Landhies.

Walibora alizikwa Jumatano nyumbani kwao katika kijiji cha Huruma, Makutano, eneobunge la Cherangany, Kaunti ya Trans Nzoia.

TANZIA: Kenya yaripoti kifo cha kwanza cha mgonjwa wa Covid-19

Na MWANDISHI WETU

KIFO cha kwanza cha mgonjwa wa Covid-19 kimesharipotiwa nchini Kenya ambapo mhanga ni mzee aliyekuwa na umri wa miaka 66.

Akitoa tangazo na salamu za tanzia Waziri wa Afya Mutahi Kagwe kupitia taarifa kwa vyombo vya habari amesema mgonjwa huyo alikuwa na historia ya maradhi mengine.

“Mkenya aliyefariki leo Alhamisi alikuwa na umri wa miaka 66 na alikuwa amelazwa katika chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi wa karibu sana katika hospitali ya Aga Khan,” amesema waziri Kagwe.

Mwendazake alikuwa anaugua kisukari na alikuwa amewasili nchini Machi 13, 2020, akitoka Swaziland ambapo alikuwa amepitia Afrika Kusini katika safari yake ya kurejea.

Kenya kufikia sasa imetangaza visa jumla 31 vya maambukizi ya Covid-19.

NMG yamwomboleza mhariri wa The East African

Na AGGREY MUTAMBO

KAMPUNI ya Nation Media Group (NMG) kwa mara nyingine inaomboleza kifo cha mwanahabari katika kipindi kisichozidi mwezi mmoja.

Mhariri wa gazeti la The East African Bi Christine Omulando aliyekuwa na umri wa miaka 46, alifariki kufuatia ajali iliyotokea katika  mzunguko wa Khoja, jijini Nairobi hapo Machi 16.

Kulingana na ripoti ya polisi, mwanahabari huyo pamoja na wapita njia wengine waliligongwa na matatu iliyokosa udhibiti na kutoka barabarani kabla ya basi ndogo kumkanyaga.

“Bi Omulando alifariki papo hapo baada ya kugongwa na basi ndogo,” ilisema ripoti.

Mwili wake ulipelekwa kwenye nyumba ya kuhifadhia maiti jijini na wapita njia waliohusika wakakimbizwa katika hospitali kuu ya Kenyatta.

Mwanahabari huyo aliripotiwa kupotea Jumatano baada ya familia na marafiki kushindwa kumfikia kwa njia ya simu.

Asubuhi hiyo, alikuwa amefika kazini kisha baadaye akaondoka kwenda kula maankuli.

Hiki ni kisa cha pili, huku wanahabari wa NMG bado wakimwomboleza aliyekuwa mhariri wa video katika runinga ya NTV Raphael Nzioki.

Polisi walisema kuwa marehemu aligongwa kimaksudi na gari kwenye njia panda katika mtaa wa Kenyatta Avenue na Kimathi Street.

Madereva waliohusika katika visa vyote hivyo viwili tayari wamekamatwa.

Familia yalilia haki ya mtoto wao aliyegongwa na gari

Na SAMMY WAWERU

JUMAPILI Machi 8, 2020, mtoto Njeri alirauka alfajiri na mapema ili kujiandaa kuhudhuria ibada ya kanisa, misa ya watoto katika kanisa la PEFA Progressive eneobunge la Ruiru.

Asubuhi hiyo, mamake anasema alitangamana na watoto wenzake kwenye ploti na kama ilivyo kawaida wakacheza kabla kuelekea kanisani.

Walipoagana, mamake mtoto huyo wa darasa la pili, gredi ya pili chini ya mfumo wa kisasa wa elimu, uamilifu, ndio CBC, alikuwa katika harakati za kufua nguo.

Mwendo wa sita hivi za mchana, alipigiwa simu akiarifiwa kuwa mwanawe amehusika katika ajali na kwamba amepelekwa katika Hospitali ya St John iliyoko Githurai.

“Tulipofika pamoja na babake tulipata mwili ukiingizwa katika gari la polisi ili kupelekwa mochari,” mama huyo aliyezidiwa na huzuni akaambia Taifa Leo.

Alisema alifariki wakati akipelekwa hospitalini.

Inasemekana siku ya tukio, Njeri, 8, pamoja na watoto wenza walikuwa wakitoka kanisani.

“Walivuka barabara kwa kundi, na ndiye alikuwa wa nyuma, wakati gari lililoonekana kuendeshwa kasi lilipompiga dafrau,” akaeleza mmoja wa wakazi aliyeshuhudia.

Gari la kibinafsi lililosababisha maafa ya mtoto huyo lenye nambari ya usajili KCW 923X lilikuwa likiendeshwa na mama.

Inasemekana alikuwa akipeleka mwanawe hospitalini.

Kati ya eneo la ajali, kuna matuta mawili, pembezoni likiwa ni kanisa la PEFA na ambalo kila Jumapili hufurika washirika. Isitoshe, mita kama hamsini hivi kuelekea Githurai barabara hiyo imejipinda.

“Kandokando mwa barabara kuna ploti za kupangisha, magari hayaendeshwi kwa kasi na lazima dereva awe makini kwa kuwa ni eneo lenye idadi kubwa ya watu,” akasema mhudumu mmoja wa tuktuk.

Gari lililosababisha maafa ya mtoto Njeri lilipelekwa katika kituo cha polisi cha Kahawa Wendani, ambacho kina kitengo cha trafiki na kufikia sasa familia ya marehemu inalilia haki ikidai hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa.

Inasemekana mama aliyesababisha kifo cha mtoto wao aliachiliwa huru, ingawa gari limezuiliwa kituoni.

Afisa mmoja wa polisi na aliyeomba tusichapishe jina lake kwa sababu haruhusiwi kuzungumza na waandishi wa habari, alisema hatua ya kwanza ni gari kuzuiliwa kituoni ili kufanyiwa uchunguzi kubaini ikiwa inaruhusiwa kuwa barabarani.

“Uchunguzi umeanzishwa kujua iwapo imeafiki sheria za trafiki, ikiwamo kuwa na bima na ukaguzi wa kina (inspection),” akasema.

Pia alisema dereva atachunguzwa ikiwa amehitimu mafunzo ya udereva na kuwa na leseni ili kufunguliwa mashtaka.

Kwa nini mlinzi wa Ruto akafa?

Na BENSON MATHEKA

WAKENYA wameuliza maswali chungu nzima kuhusu kifo cha Sajini Kipyegon Kenei, aliyekuwa mmoja wa walinzi katika ofisi ya Naibu Rais William Ruto wakati washukiwa wa utapeli katika tenda feki ya silaha walipoitembelea.

Miongoni mwa maswali yasiyokuwa na majibu ni, kwa nini polisi walifikia uamuzi wa haraka kwamba afisa huyo alijiua bila kufanya uchunguzi na kwa nini wapelelezi hawakuandikisha taarifa kutoka kwa majirani wake katika mtaa wa Villa Franca, Nairobi?

Mwili wa Sajini Kenei ulipatikana kwenye nyumba yake Alhamisi alasiri ukiwa na jeraha la risasi. Kulingana na taarifa ya polisi, alijiua.

Hata hivyo, Wakenya hawakuridhirishwa na maelezo ya polisi hasa baada ya kubainika kuwa mlango wa nyumba ya afisa huyo ulikuwa wazi.

“Mtu anayepanga kujiua kwa kawaida huwa anajifungia ndani. Kwa kuwa mlango wa nyumba yake ulikuwa wazi, inazua maswali kuhusu kwa nini afisa huyo aliuawa,” alisema Mkenya mmoja kwenye Twitter.

Waliomfahamu afisa huyo walisema kwamba hakuwa mtu wa kufikiria kujiua.

“Nilifahamu kifo cha sajini Kenei kwa huzuni. Nilimfahamu kwa miaka mitano akiwa mlinzi wa Mheshimiwa Soita Shitanda na aliendelea kuwa rafiki baada ya kujiunga na walinzi wa Naibu Rais. Sifikirii alikuwa na akili za mhalifu,” alisema aliyekuwa seneta wa Kakamega Boni Khalwale.

Baadhi ya maswali ambayo Wakenya walitaka wapelelezi kuangazia katika uchunguzi wao ni kwa nini kifo chake kilitokea alipokuwa akitarajiwa kuandikisha taarifa kuhusu sakata hiyo katika ofisi ya Dkt Ruto huku wengine wakishuku huenda aliuawa mahali tofauti na mwili wake ukapelekwa kwake.

“Swali ni, kwa nini mlango wa nyumba yake ulikuwa wazi, nani aliuacha ukiwa wazi na ikiwa alijipiga risasi inavyodaiwa, mbona majirani hawakusikia mlio wa bastola?” aliuliza Mkenya mwingine.

Imeibuka kuwa polisi walifichua habari za kifo chake kabla ya kufahamisha familia yake inayoishi Nakuru.

Familia hiyo ilisema ilipata habari kupitia redio na ikapuuza madai kwamba alijiua.

Baba yake John Chesang alisema afisa huyo alitarajiwa kufanya harusi mwezi Agosti mwaka huu hivyo basi hakuamini macho yake aliposikia kuwa amejiua.

Kulingana na maelezo ya awali, Sajini Kenei alitakiwa kuandikisha taarifa kwa polisi kueleza jinsi aliyekuwa waziri wa michezo, Rashid Echesa na washukiwa wengine wanne walivyowaingiza raia wa kigeni katika ofisi ya Dkt Ruto, na hata kutia sahihi kandarasi feki ya kuuzia wizara ya ulinzi silaha.

Wakenya wanauliza ni habari gani alizokuwa nazo kuhusu sakata hiyo ambazo hakutaka zijulikane iwapo alijiua. Wengine wakawa wanajijazia kuwa kiwa alimalizwa, basi waliomuua hawakutaka zijulikane iwapo angeandikisha taarifa.

Habari za kifo chake zilijiri siku moja baada ya Dkt Ruto kumtaka Inspekta Jenerali wa polisi Hillary Mutyambai kuchunguza walinzi waliokuwa kazini wakati Echesa na washukiwa wenzake walipoingia katika jumba la Harambee Annexe.

Dkt Ruto alimwomboleza Sajini Kenei akimtaja kama afisa wa polisi aliyekuwa na nidhamu ya juu kazini.

“Kenei alikuwa afisa wa polisi mwenye umri mdogo na mwenye nidhamu. Ninaomba idara zinazohusika kuchunguza alivyokufa,” alisema Dkt Ruto.

Mbali na kutilia shaka maelezo ya polisi, Wakenya mtandaoni hawakuridhishwa na hatua ambazo ofisi ya Dkt Ruto ilichukua pale Sajini Kenei alipokosa kufika kazini Jumatano na kujiwasilisha kwa wapelelezi kuandikisha taarifa.

Wanasema ikizingatiwa kuwa kulikuwa na uchunguzi muhimu uliokuwa ukiendelea, hatua ya kwanza ingekuwa ni kufika kwake mapema kubaini hali yake.

Kabla ya mwili wa afisa huyo kupatikana Alhamisi alasiri, ofisi ya Ruto ilikuwa imetoa taarifa ikisema kwamba alikuwa ametoweka.

Mara yake ya mwisho kuonekana akiingia katika mtaa au nyumba yake ilikuwa lini? Kuna walinzi katika malango ya mtaa wa Villa Franca?

Je, walimuona mgeni yeyote baada yake kuingia au siku hiyo?

Je, mtu wa mwisho kuwasiliana na Kipyegon ni nani? Ni baadhi ya maswali ambayo Wakenya waliuliza kwenye mitandao ya kijamii.

Walitilia shaka taarifa ya polisi kwamba mwili wake uligunduliwa kufuatia harufu mbaya kutoka nyumba yake wakisema haiwezi kuaminika.

Wakazi wa Thika wazidi kuomboleza kifo cha Mundia

Na LAWRENCE  ONGARO

WAKAZI wa mji wa Thika wanaendelea kumuomboleza meya wa zamani wa Thika, Bw Douglas Kariuki Mundia.

Kulingana na maelezo ya familia yake, marehemu, alitoa wosia wake mapema kuwa iwapo atafariki azikwe mara moja bila maiti yake kuhifadhiwa mochari.

Wanahabari walipozuru boma lake katika mtaa wa Mundia Estate Thika leo Ijumaa, wamepokea habari ya kwamba alifariki Februari 13, 2020, na kuzikwa siku iliyofuatia Februari 14, 2020, katika kijiji cha Kang’oo, Gatundu Kaskazini.

Kulingana na mwanawe Bw Isaac Munene, baba yao Mundia aliwapa wosia wake  Julai 2016 ambapo alieleza matakwa yake kuwa kifo chake kikitokea, wamzike haraka iwezekanavyo bila kuchelewa.

“Sisi kama ‘familia nne’ tuko pamoja na hakuna mvutano wowote umekuwepo, na kwa hivyo tulimzika baba yetu kwa heshima alizohitaji,” amesema Bw Munene.

Amesema licha ya kuharakisha mazishi hayo wanapanga sherehe za kuonyesha heshima kwake pamoja na wakazi wa Thika mnamo Februari 28, 2020, katika uwanja wa michezo wa Thika Stadium.

“Tunajua kuna watu wengi walimuenzi na wangetaka kutoa heshima zao za mwisho kwa baba yetu. Sisi kama familia tumepanga kufanya misa kubwa ya kumuenzi marehemu katika uwanja huo huku tukialika marafiki wake wote,” amesema Bw Munene.

Amefafanua alikuwa anaugua kila mara kuanzia mwaka wa 2014 hadi kifo chake lakini alikuwa akifuatilia matibabu na ushauri kutoka kwa daktari.

Aliyekuwa meya wa Thika Bw David Njihia, amemsifu Bw Mundia akisema yeye ndiye baba ya mkuu wa mji wa Thika.

Marehemu Mundia amekuwa uongozini kama Meya kwa miaka 20 mfululizo ambapo ukuwaji wa mji wa  Thika umetokana na uwezo wake.

“Wakati alikuwa Meya alionyesha ujuzi wake wa kuwa kiongozi wa kutambulika baada ya kuweka miundomsingi inayoshuhudiwa kwa sasa. Alifanya kazi kwa uwajibikaji na uwazi bila mapendeleo,” amesema Bw Njihia ikiwa ni sehemu ya kutoa salamu za pole.

Amewataka viongozi wa sasa hasa madiwani – MCA waliochaguliwa kuiga mfano wake meya huyo  kwa kuwatumikia wananchi bila ubaguzi wowote.

Waandishi wa habari walipozuru  boma lake mjini Thika walipata  familia  nne za marehemu wakiwa  wamekusanyika wakitayarisha  jinsi misa ya wafu itakavyoendeshwa  katika uwanja wa Thika Stadium.

Walisema kinyume na jinsi watu walivyotarajia familia hiyo litaendelea kuwa kitu kimoja na hakuna mvutano wowote wa mali utashuhudiwa .

“Mzee wetu aliacha wosia  uliokuwa na hali ya umoja kwa kutusihi kuendelea kuishi kwa umoja amani na uelewano bila mvutano wowote,” alisema Bw Munene mmoja wa mwanaye marehemu.

Simanzi kuu kufuatia kifo cha aliyekuwa mwandishi wa ‘Taifa Leo’

Na Charles Wanyoro

SIMANZI imegubika jumuiya ya waandishi baada ya mmoja wao kutoka Meru, Bw Darlington Manyara, 29, kuaga dunia Jumanne.

Iliripotiwa kuwa Bw Manyara alifariki baada ya kuwa mgonjwa kwa kipindi kifupi. Alikuwa anapata matibabu katika hospitali ya Meru Level 5.

Bw Manyara aliwahi kufanya kazi katika kampuni ya kusambaza habari ya Nation Media kabla ya kuhamia Standard Media Group.

“Bw Manyara alikuwa mwandishi shupavu na ustadi wake ulionekana pale alipochambua siasa za Meru,” alisema Wainaina Ndung’u ambaye walifanya kazi pamoja.

Familia, jamaa, marafiki na waandishi wenzake walimtaja marehemu kama mwenye bidii na kupenda kutangamana na watu.

“Katika uandishi wake, aligusia siasa, uhalifu, korti na hata kilimo. Alijua kuunda uhusiano mzuri na wadokezi wake na hata marafiki,” akasema Bw Ndung’u.

Mwili wa marehemu ulipelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali ya Meru Level 5.

 

Mzee aenziwa kwa kuvumisha soka miaka ya 80

Na CECIL ODONGO

WANAMICHEZO wanaendelea kuomboleza kufuatia kifo cha Rais wa pili wa Kenya, Daniel Arap Moi aliyeaga dunia katika Nairobi Hospital.

Utawala wa Mzee Moi utakumbukwa kwa ujenzi wa uwanja wa Nyayo na ule wa Kimataifa wa MISC, Kasarani.

Uongozi wa klabu mbili kubwa nchini Gor Mahia na AFC Leopards, jana uliomboleza kifo cha Mzee Moi na kusema alichangia sana ufanisi ulioshuhudiwa miaka ya 80 na 90.

Mwenyekiti wa Gor Mahia Ambrose Rachier kwenye mahojiano na ‘Taifa Leo’, alisema Mzee Moi alipenda mchezo wa soka na alitoa msaada wa kifedha kwa klabu hiyo kila mara iliposhiriki mechi za Bara Ulaya na ligi ya nyumbani.

Rachier pia alithibitisha kwamba Mzee Moi aliipa klabu hiyo vipande viwili vya ardhi katika maeneo ya Embakasi na Kasarani.

Mapenzi yake kwa K’Ogalo yalishuhudia akifika uwanjani na kutazama ngarambe ya fainali ya Kombe la Mandela ambayo Gor ilipiga Esperance ya Tunisia na kutwaa ushindi.

“Mzee Moi alipenda michezo na alifika uwanjani Gor Mahia ilipokuwa ikishiriki mashindano mbalimbali. Ingawa alitupa vipande vya ardhi, inasikitisha kwamba hadi leo hatujapata hatimiliki japo tunaendeleza mchakato wa kuhakikisha tunazipata kutoka kwa serikali,” akasema Rachier.

Mwenyekiti wa AFC Leopards Dan Shikanda naye alisema walipewa ardhi na Mzee Moi na njia ya pekee ya kumuenzi kutokana na wema huo ni kuhakikisha wanapata hatimiliki ya ardhi hiyo iliyoko Kasarani.

“Natuma salamu za pole kwa familia ya Rais Mstaafu. Nilikuwa mchezaji alipotoa kipande hicho cha ardhi na najua mahali ipo. Kwa kuwa sasa mimi ni afisa wa klabu, nitajitahidi kuhakikisha tunapata hatimiliki ili kujenga pia uwanja wa mazoezi,” akasema Shikanda.

Aliyekuwa kocha wa Harambee Stars Jacob ‘Ghost’ Mulee pia alikumbuka jinsi aliwaalika Ikulu waliposhinda Kombe la Cecafa mnamo 2000.

“Mzee Moi alitukaribisha kwenye ikulu tuliposhinda taji la Cecafa Kagame na lilikuwa tukio la kupendeza mno. Kwa masikitiko hatukupewa fedha zozote lakini naamini maafisa walioandamana nasi walituchezea shere na kuchukua pesa zetu. Hakuna vile ungeenda Ikulu kisha ukose kupokezwa kitita enzi hizo,” akasema Mulee.

Nahodha wa zamani wa Harambee Stars Musa Otieno pia alituma salamu za pole kwa familia ya Mzee Moi na kusema alikuwa akihudhuria mechi za timu ya taifa.

Rais wa zamani wa Pakistan ahukumiwa kifo

Na AFP

ALIYEKUWA rais wa zamani Pakistan Pervez Musharraf Jumanne alihukumiwa kifo na mahakama maalum kwa kosa la uhaini uliokithiri.

Musharraf ndiye kiongozi wa kwanza wa kijeshi kuwahi kufanyiwa mashtaka na kuhukumiwa kwa kosa la uhaini.

Kesi hiyo, pamoja na rundo la kesi nyinginezo zinazomkabili, iliwasilishwa dhidi yake mnamo 2013, baada ya kurejea kwake nchini Pakistan kutoka ukimbizini alimokaa kwa miaka minne, akinuia kugombea ubunge ili ‘kuliokoa’ taifa hilo lililojihami kwa silaha za nuklia.

Katika kesi hiyo, alikabiliwa na mashtaka ya kulemaza, kusambaratisha na kupuuzilia mbali katiba, kushinikiza hali ya hatari nchini humo mnamo Novemba 2007 pamoja na kuwazuilia majaji wa mahakama kuu zaidi nchini Pakistan.

Musharraf, aliyeondoka Pakistan punde baada ya kujiuzulu kama rais mnamo 2008, aliondoka taifa hilo kwa mara ya pili mnamo Machi 2016 kwa lengo la kusaka matibabu nchini Dubai. Alitangazwa kama mtoro katika kesi hiyo.

Musharraf alishtakiwa rasmi mnamo Machi 31, 2014, ambapo upande wa mashtaka ulikuwa umewasilisha ushahidi wote mbele ya mahakama spesheli mnamo Septemba mwaka huo pia.

Lakini mchakato wa kusikizwa kwa kesi hiyo ukaendelea.Korti spesheli, iliyoongozwa na Jaji Mkuu wa Mahakama Kuu ya Peshawar Waqar Ahmad Seth, ilikuwa imetangaza kuwa ingetoa hukumu yake hapo.

Hata hivyo, upande wa mashtaka unaowakilisha serikali kupitia kwa Wakili Ali Zia Bajwa, ulisema ulikuwa umewasilisha kesi tatu.

Kesi moja inaitaka mahakama kuwafanya watu watatu wakiwemo – aliyekuwa waziri mkuu Shaukat Aziz, aliyekuwa Jaji Mkuu wa Mahakama ya Juu Zaidi Abdul Hameed Dogar pamoja na aliyekuwa Waziri wa Sheria Zahid Hamid – kuwa washukiwa katika kesi hiyo.

“Tunataka kuwafanya washiriki na wandani wa Musharraf kuwa washukiwa vilevile. Ni muhimu kwamba kesi ya washukiwa wote ifanyike katika wakati mmoja,” alisema Bajwa, kulingana na vyombo vya habari nchini humo.

Wakati wa kusikizwa kwa kesi hiyo, wakili wa Musharraf, Raza Bashir pia aliomba muda wa kati ya siku 15 hadi 20 ili mteja wake aandikishe taarifa. “Musharraf anastahili haki ya kufanyiwa mashtaka kwa njia ya haki,” alisema.

Inspekta apatikana amefariki katika baa eneo la Bombolulu

Na MOHAMED AHMED

AFISA mmoja wa polisi amepatikana amefariki Jumanne nje ya baa eneo la Bombolulu, Mombasa ambapo inadaiwa alikuwa anakunywa pombe.

Inspekta mkuu wa polisi William Chepkwony alipatikana amefariki akiwa amekaa nje ya baa hiyo iliyoko eneo la Sports.

Kulingana na maafisa wanaofanya kazi naye, Chepkwony alienda kwenye baa hiyo Jumatatu usiku na kuanza kunywa pombe.

Jumanne asubuhi alirudi tena na kuendelea kunywa pombe baada ya kupangia maafisa wenzake wadogo kazi ya siku.

“Alifikishwa kwenye baa hiyo na wenzake Jumatatu usiku. Amekuwa na shida nyingi za kikazi ambazo zilikuwa zinamsumbua,” amesema afisa mmoja ambaye haruhusiwi kuongea na wanahabari.

Kulingana na maafisa wengine wanaomtambua, afisa huyo alikuwa na shida ikiwemo kutopokea mshahara kama inavyotarajiwa.

Hali hiyo ilisababisha afisa huyo kulala katika kituo cha Dog Section ambapo hufanya kazi.

Maafisa wengine wamesema kuwa kwa muda mwingi Chepkwony amekuwa akikaa peke yake kwa sababu ya shida zilizokuwa zikimkumba.

Rekodi za polisi zimeonyesha kuwa afisa huyo pia alikuwa anakumbwa na kesi ya utovu wa nidhamu ya mwaka 2016 ambapo aliwahi kukamatwa kwa kosa la kuacha kazi bila ruhusa; jambo ambalo linakiuka sheria za polisi.

Jumanne, kamanda wa polisi eneobunge la Kisauni, Julius Kiragu amethibitisha kuwa afisa huyo amekuwa akihudumu katika kitengo cha mbwa.

“Huyu ni mmoja wetu na kwa wakati huu hatuwezi kubainisha sababu ya kifo chake. Mwili wake haujapatikana na majeraha yoyote hivyo basi tutasubiri matokeo ya upasuaji wa mwili kujua sababu ya kifo hicho,” amesema Bw Kiragu alipofika eneo hilo la tukio.

Mwili wa afisa huyo umepelekwa katika hospitali kuu ya ukanda wa Pwani ambapo inatarajiwa utafanyiwa upasuaji.

Mwanahabari apatikana amefariki chumbani mwa inspekta mwanamke

Na DICKENS WASONGA

MWANAHABARI Eric Oloo ambaye hufuatilia matukio Siaya akiwajibikia gazeti moja nchini amepatikana Alhamisi asubuhi akiwa amefariki katika nyumba ya inpekta mkuu wa polisi mwanamke Ugunja huku afisa huyo akiwa mafichoni.

Maiti ya mwanamume huyo aliyekuwa na umri wa miaka 40 ilikutwa kitandani kukiwa na damu kote.

Afisa huyo, imekuwa imefahamika kwamba alikuwa akiishi naye.

Maafisa wa polisi wamepeleka maiti katika mochwari ya Ambira, amethibitisha kamanda wa polisi wa kaunti ndogo ya Ugunja Bw Ibrahim Muchuma bila kutoa maelezo zaidi.

Mfanyakazi wa afisa huyo wa kike amerekodi taarifa kituo cha polisi cha Ugunja.

Afisa mmoja ambaye hafai kuzungumza na vyombo vya habari amesema wanaume wengine walikuwa katika chumba hicho ambapo imetokea farakano Jumatano usiku. Mmoja amekamatwa.

Kamanda wa polisi wa Siaya Bw Francis Kooli amesema mwanahabari alikuwa katika uhusiano wa kimapenzi na afisa.

“Hili ni suala zito hapa Siaya,” akasema.

Msomi mashuhuri Mkenya afariki

Na KITAVI MUTUA

ULIMWENGU Jumatatu uliomboleza kifo cha profesa wa masuala ya kidini, John Samuel Mbiti ambaye alikuwa maarufu kimataifa.

Prof Mbiti alifariki akiwa na umri wa miaka 88 mnamo Jumapili alipokuwa akitibiwa mjini Bergdorf, Uswizi ambako alikuwa akiishi kwa miongo mingi.

Alipata umaarufu kimataifa wakati alipoandika kitabu chake cha kwanza cha African Religions and Philosophy ambacho kilichapishwa mnamo 1969.

Katika kitabu hicho, alitilia shaka misimamo ya Kikristo kwamba dini na imani za Kiafrika ni za kishetani.

Prof Mbiti alikuwa kasisi wa Kanisa la Anglikana na alizaliwa katika eneo la Mulango, Kaunti ya Kitui.

Alikuwa mfasaha wa lugha ya Kigiriki ambayo ni mojawapo ya lugha za kwanza asili zilizotumiwa kuandika Biblia.

Marehemu alitumia miaka 12 ya uzeeni mwake kuanzia 2003 hadi 2015 kutafsiri Biblia asili ya Kigiriki kwa Kikamba ambapo alikosoa zaidi ya maneno 1,000 aliyosema yalitafsiriwa kimakosa katika Biblia.

TANZIA: Viongozi wamtumia Khalwale salamu za pole kwa kumpoteza mke

NA MARY WANGARI

WANASIASA mbalimbali wakiongozwa na Naibu Rais Dkt William Ruto, wameungana Jumamosi kumfariji aliyekuwa Seneta wa Kaunti ya Kakamega Dkt Boni Khalwale, kufuatia kifo cha mke wake wa kwanza Bi Adelaide Khalwale, aliyefariki kutokana na saratani.

Bi Khalwale alifariki Jumamosi asubuhi akiwa nyumbani kwake Malinya, eneobunge la Ikolomani, baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Mwili wake ulipelekwa katika mochari ya Hospitali ya St Elizabeth Mukumu.

Dkt Khalwale aliyezidiwa na majonzi, alijitosa katika ukurasa wa mojawapo ya akaunti zake za mitandao ya kijamii kutangaza kifo cha mkewe.

“Asubuhi yenye huzuni. Kifo kimenipokonya mke wangu wa kwanza,” aliandika Dkt Khalwale.

Viongozi wakiwemo Dkt Ruto na kiongozi wa ODM Raila Odinga, walituma salamu za pole wakimfariji.

“Salamu za pole ziendee familia na marafiki wa mheshimiwa Boni Khalwle kwa kumpoteza mkeo, Bi Adelaide. Mama Adelaide alikuwa nguzo maishani mwako, mkarimu na mwenye moyo safi. Tunajali na kuombea wapendwa wake. Lala salama,” alisema Naibu Rais.

Naye kiongozi wa ODM alikuwa na pole zake kwa Khalwale.

“Naomba upokee salamu zangu za pole; kwako na familia yako yote kufuatia kifo cha mkeo mpendwa Bi Adelaide. Mola na akupe nguvu kipindi hiki kigumu,” aliandika Raila.

Wanasiasa wengineo maarufu wakiwemo maseneta Moses Wetang’ula, Kipchumba Murkomen, Katibu Mkuu wa ODM, Edwin Sifuna pia hawakuachwa nyuma kumfariji Bw Khalwale.

Hadi kufikia kifo chake, Bi Khalwale alikuwa mfanyakazi wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Masinde Muliro (MMUST).

Polisi wachunguza kifo tata cha dadake mbunge wa Githunguri

DADAKE Mbunge wa Githunguri Gabriel Kago, Jane Murugi, alipatikana Ijumaa akiwa amefariki nyumbani kwake katika hali ya kutatanisha.

Maiti ya Bi Murugi, ambaye amekuwa ni muuguzi mkuu anayehudumu katika Kaunti ya Machakos, ilipatikana chooni nyumbani kwake katika mtaa wa Membley, Ruiru, Kaunti ya Kiambu, majira ya asubuhi.

Alifariki akiwa na umri wa miaka 41.

Taarifa za awali zimedokeza kuwa huenda mwendazake alijinyonga.

Hata hivyo, polisi wanashuku kuna njama ya kuficha ukweli kuhusu kifo cha Bi Murugi kwa sababu alipatikana amefariki akiwa ameketi kwenye bakuli la choo.

“Skafu iliyofungwa kwa tai ilipatikana ikining’inia kwenye dirisha la choo hicho,” Afisi Mkuu wa Polisi (OCPD) wa Ruiru Mutwiri Ringera alisema.

Mumewe, Dkt Stephen Ndoro, alisema aliamka saa kumi na moja alfajiri Ijumaa na hakumpata mkewe kitandani.

Ndoro, 38, ambaye ni daktari katika kaunti ya Makueni, alisema alienda chooni ndipo akampata mkewe amefariki.

Bi Murugi, ambaye alikuwa katika likizo ya uzazi, amemwacha mtoto mwenye umri wa miezi miwili.

Maiti yake ilipelekwa katika Hifadhi ya Maiti ya Chuo Kikuu cha Kenyatta ambako ilifanyiwa upasuaji jana jioni.

Afisa Mkuu wa Idara ya Upelelezi (DCI) Kaunti ya Kiambu Bw Ringera, Mheshimwa Kago na wabunge wengine walifika katika hifadhi hiyo saa saba kutizama maiti.

Polisi walisema watamdadisi mumewe Murugi katika uchunguzi wao kuhusu chanzo cha kifo chake.

DINI: Utakifanyaje kifo chako kuwa zawadi kwa wengi ili uombolezwe kwa heshima?

Na FAUSTIN KAMUGISHA

KIFO ni mtihani.

Kuna aliyesema dunia ni mahali pa hatari sana, hutoki ukiwa hai.

Hadithi inapokuwa nzuri kwenye gazeti hukatizwa na kuandikwa itaendelea toleo lijalo.

Mtu anapoaga dunia ni Mungu hukatiza hadithi ya maisha yake na kuandika kuwa itaendelea toleo lijalo.

Swali linabaki nani ataomboleza utakapoaga dunia?

Tunaalikwa kuwalilia walioaga dunia.

“Mwanangu, mlilie mtu aliyekufa;lia kwa uchungu, kuonesha huzuni yako. Uuzike mwili wake kwa heshima ipasavyo, wala usipuuze mazishi yake. Lia kwa uchungu na kwa moyo, hudhuria matanga kama anavyostahili marehemu, omboleza siku mbili tatu usije ukasemwa; kisha ufarijike kutokana na huzuni yako” (Yoshua Bin Sira 38:16-17).

Bila shaka marehemu anakuwa kwenye moyo wako, sababu alikugusa.

Kuna methali ya Ujerumani isemayo, hastahili kuishi anayeishi kwa ajili yake tu. Ukiwafia wengine, unakifanya kifo kiwe zawadi kwa wengine. Kwa namna hiyo utakapoaga dunia watu wengi wataomboleza. Kuomboleza kunahusishwa na kukuombea na kukupendekeza kwa Mungu.

“Ni baraka kufia jambo fulani, sababu unaweza kwa urahisi kufa bure,” alisema Andrew Young. Kuwafia wengine hakuhitaji kujipendelea. Mtu anayejipendelea hafikirii kama kuna wengine duniani anajiona kitinda mimba duniani.

Kuna hadithi juu ya mtu aliyekuwa kwenye kitanda cha mauti. Aliwaambia waliomzunguka: “Nilifia masomo ya kidato cha nne nikashinda mtihani. Nilifia masomo ya kidato cha sita, nikashinda mtihani. Nilifia masomo ya chuo kikuu, nikashinda. Nilipooa, niliifia familia. Baadaye niliwafia watoto, wapate maisha mazuri. Nilifia mambo mengi kama kusemwa vizuri, kuwapendeza watu lakini nilisahau kuishi.” Ndugu msomaji unafia nini? Usisahau kuishi.

Ukiacha umeandika wosia, kifo chako kinakuwa zawadi na si sababu ya malumbano. Ukiwaachia urithi wa elimu watoto wako kifo chako kinakuwa zawadi. Juu ya kufanya vifo vyetu viwe zawadi, Henri J.M.Nouwen mwandishi wa vitabu alikuwa na haya ya kusema, “Namna gani tunafanya vifo vyetu zawadi kwa wengine?

Mara nyingi maisha ya watu yanaharibiwa, yanadhuriwa au kuwa na majeraha maisha yao yote kwa vifo vya jamaa au marafiki zao. Lazima tufanye tuwezalo ili kukwepa hili.Tunapokuwa karibu kifariki, tunalowaambia wale ambao wako karibu nasi, iwe kwa kusema au kuandika ni muhimu. Tunapowashukuru, kuwaomba msamaha kwa makosa yetu na kuwasamehe na kuwaonesha nia ya kutaka waendelee na maisha yao bila kusutwa lakini wakikumbuka neema za maisha yetu, basi vifo vyetu vinakuwa zawadi kweli.”

Hasara kubwa si kifo bali kinachokufa ndani yetu. “Kifo si hasara kubwa sana katika maisha yetu. Hasara kubwa sana ni kile kinachokufa ndani yetu wakati tunaishi,” alisema Normani Cousins mtunga insha na mwariri wa Amerika (1912 – 1990). Wakati tunaishi kuna mambo ambayo yanaweza kufa kama shauku, moyo wa kutoa, moyo wa kujitolea, uchaji kwa Mungu, utii, usafi wa moyo. Vikifa ni hasara kubwa.

“Jambo baya sana maishani si kwamba tunakufa, bali kile kinachokufa ndani ya mtu wakati anaishi,” alisema Albert Schweitzer.

Jambo baya sana ni matumaini kufa wakati unaishi, utu kufa wakati unaishi, ukarimu kufa wakati unaishi, moyo wa kutendea wengine mema wakati unaishi, mtazamo chanya kufa wakati unaishi na moyo wa kazi kufa wakati unaishi. Huku ni kufa mara mbili kama mkaa. Mara ya kwanza ni tunu na fadhila moyoni mwako kufa. Na mara ya pili ni kuaga dunia. Hayo yakishasemwa kifo kinabaki kuwa mtihani. Takwimu kuhusu kifo ni za kutisha. Kati ya watu elfu moja, elfu moja wote wataaga dunia. Kifo ni mtihani. Mtoto anapozaliwa analia, watu wanafurahi. Mtu anapokufa watu wanalia.

“Kuaga kwangu dunia kutakuwaje? Sote tutaonja kuzama kwa jua! Je jambo hilo tunalitazamia kwa matumaini? Tunalitazamia na furaha ile ya kukaribishwa na Bwana?” alisema Papa Francis.

Kwake papa na ilivyo kwa waumini wa dini mbalimbali, kuna maisha baada ya maisha.