PAUL THIONG’O: Amewahi kutuzwa zawadi maalum na Zinedine Zidane

Na ABDULRAHMAN SHERIFF

AMEKUWA nchini Italia kwa kipindi cha miaka 11 na hivi sasa ana hamu sana ya kuwa miongoni mwa wachezaji wanaowakilisha Kenya katika mashindano na michezo ya kimataifa.

Katika kipindi hicho, Paul Thiong’o amekuwa Italia akipata mafunzo hadi kucheza soka ya kulipwa na anaamini anaweza kuchezea timu ya taifa ya Harambee Stars ingawa huko aliko anachezea timu ya Supa Ligi ya Rocchese Football.

Thiong’o alianza kuwa katika chuo cha mafunzo ya soka cha klabu ya Empoli FC kabla ya kuzichezea klabu za Colligiana, Lanciotto, Montelupp, Angri na sasa Rocchese.

“Nina hamu kubwa ya kukipiga katika timu ya taifa langu Kenya – Harambee Stars – kwani naamini nikipewa nafasi nitafanya vizuri. Nawaomba wale wahusika na uteuzi pamoja na afisi ya Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) wanipe jaribio na ninaamini nitafuzu,” akasema kiungo huyo.

Ingawa mwanasoka huyu anachezea klabu ya Supa Ligi ya Italia, anaamini ana kiwango kikubwa cha kusakata soka na ana matumaini kama atafanyiwa majaribio ya kuichezea Stars, atawaridhisha wateuzi wa timu hiyo.

“Tuko Wakenya kadhaa tunaocheza klabu za madaraja ya chini lakini tuna viwango vikubwa vya kusakata kabumbu ya hali ya juu lakini tatizo kubwa ni kuwa wanaotambulika ni wale wanaocheza klabu zinazoshiriki katika Ligi Kuu pekee,” akasema.

Akiwa na umri wa miaka 24 sasa, Thiong’o amekuwa nchini Italia tangu alipokuwa kijana wa umri wa miaka 13, mwaka mmoja baada ya kuongoza kikosi cha timu ya Mombasa FC kilichoshiriki dimba la Danone Nations Cup mwaka 2007 mjini Lyon nchini Ufaransa.

Mwanasoka Paul Thiong’o (kulia) akiudhibiti mpira wakati akiwa na umri wa miaka ya utineja. Picha/ Hisani

Aliwavutia maskauti wa Empoli FC ya Italia iliyomfadhili kwa mafunzo ya soka pamoja na masomo.

Anasema anatamani Shirikisho la Soka Nchini Kenya (FKF) likishirikiana na serikali kuu pamoja na serikali za kaunti, kukusanhya na kuweka data za wachezaji wote Wakenya wanaosakata soka ng’ambo kwani kwa njia hiyo, wataweza kutambua wale wanaostahili kuchezea timu ya taifa.

“Sikuwa na bahati ya kiwango changu kutambulika nilipokuwa na umri wa miaka ambayo ningewakilisha taifa langu kwenye mashindano ya umri chini ya miaka 17, 20 na 23. Sasa nakumbusha kuwa tuko huku kwenye madaraja ya chini, FKF ifuatilie ijue hatua tunazopiga,” akasema.

Thiong’o ambaye ana hamu ya kupanda ngazi hadi kuchezea klabu ya Ligi Kuu ya Italia ya Serie A, amewahi kuibuka mchezaji bora katika mechi 11 kati ya mechi 18 timu yake imecheza.

Matukio hayo ya mchezaji bora yanaashiria kuwa ni mchezaji mwenye tajriba ya kusakata soka safi.

Mwanasoka Paul Thiong’o (kushoto). Picha/ Hisani

Wakati wa mashindano ya Danone Nations Cup, kiungo Thiong’o almaarufu ‘Zizzou’ aliibuka kuwa Mchezaji Bora na akatuzwa zawadi maalum na aliyekuwa mchezaji wa Ufaransa Zinedine Zidane ambaye kwa sasa ni kocha wa Real Madrid ya nchini Uhispania.

Anapoulizwa kuwa tangu aanze kukipiga huko Italia ni jambo gani alilotimiza maishani mwake na familia yake, Thiong’o anasema amemjengea nyumba mama yake mjini Kiambu.

“Nimeona umuhimu kwanza kumjengea nyumba mama yangu ndipo baadaye niangalie yale yangu ya binafsi,” akasema mwanasoka huyo.

Kwake, ametoa ombi kwa wachezaji wenzake Wakenya wanaocheza soka huko ng’ambo na hasa kwa timu za madaraja ya chini, wajitokeze kutambulika kwani huenda nao wakafuatiliwa maendeleo yao na kupata fursa ya kuchezea Harambee Stars.

KIPAJI: Mwalimu anayetumia talanta ya uimbaji kukuza wale chipukizi

Na SAMMY WAWERU

BI Annastacia Mitau ni mtunzi na mwimbaji wa nyimbo za Injili.

Mwanamuziki huyu kutoka kijiji cha Ngaa, Kaunti ya Kitui, anasema nyimbo zake ni ujio kupitia maandiko ya Biblia.

Ni kipaji alichotambua kujaaliwa akiwa katika shule ya msingi ambapo alitungia wanafunzi wenza nyimbo, na kuwapa waimbe na kutumbuiza, hasa katika gwaride na hafla zilizoandaliwa.

Katika shule ya upili, St Ursula Tungutu iliyoko Kitui, Annastacia anasema aliendelea kupalilia kipaji chake katika usanii wa uimbaji, akidokeza kuwa akiwa kidato cha tatu alichaguliwa kuwa kiongozi wa michezo ya kuigiza na muziki.

Anafichua kwamba aliimba nyimbo za Kiislamu; Taarabu na Kaswida pia Qaswida, ambapo alishiriki mashindano yake hadi katika daraja la kitaifa. “Hata ingawa sikuibuka kidedea, nilikabidhiwa vyeti kadhaa,” asema mwanadada huyu.

Alipohitimu elimu ya shule ya upili mwaka 2009 alijiunga na Chuo cha Ualimu cha Mosoriot, kilichoko Kaunti ya Nandi mwaka wa 2010 na aliendelea kubobea katika muziki.

“Uimbaji na utumbuizaji wowote chuoni nilikuwa katika mstari wa mbele,” anasema Annastacia.

Alikamilisha kusomea taaluma ya ualimu 2012.

Annastacia ambaye ni mama wa mtoto mmoja, ameimba nyimbo zake kwa lugha ya Swahili na Kikamba. Ana albamu moja yenye nyimbo sita; Mbiwie tei – ninakupenda Mungu, Neema, Niseng’ete – nimeshangaa, Lyikie vinya – jitie nguvu na Ninukilitye wasya – nimeinua sauti.

Kulingana na mwanamuziki huyu serikali ya kaunti ya Kitui kupitia wizara ya michezo, vijana na turathi ndiyo imemfadhili kurekodi zake.

Sauti (audio) alirekodi mwaka 2018 na video akiifanya mwaka huu, 2019, kupitia ufadhili wa serikali ya kaunti ya Kitui inayoongozwa na gavana Charity Ngilu.

Mbali na kuwa muimbaji, Annastacia ni mwalimu wa Somo la Hisabati na Kiingereza katika shule ya Msingi ya Kibinafsi na ya Bweni ya St Gabriel, Mwingi. Anasema amefanikiwa kubuni kilabu ya Muziki, Sanaa na Uigizaji shuleni humo.

“Niliteuliwa kiongozi wa kilabu hiyo. Kwa sasa ninajivunia mwanafunzi mmoja wa darasa la nne, ambaye amejaaliwa kipaji cha uimbaji. Anaendelea kutunga nyimbo na akitokota nitamsaidia kuingia studioni azirekodi,” asema, akiongeza kwamba ana orodha ya wanafunzi kadhaa ambao wakipaliliwa wataibuka kuwa wanamuziki wa kupigiwa upatu.

Anachozingatia kwenye mafunzo kupitia vipindi anavyoandaa ni utunzi wa nyimbo, sauti, namna ya kuimba, ujasiri kwa wanafunzi pamoja na vigezo muhimu katika ulingo mzima wa uanamuzi.

Nephat Mbau, ambaye ni produsa, anasema vipaji chipukizi wakipaliliwa wakiwa wangali wachanga wataibuka kuwa miongoni mwa wasanii bora nchini. “Cha muhimu zaidi ni upekee katika utunzi, sauti na ujasiri hususan wakiwa jukwaani. Msanii chipukizi akinolewa akiwa mdogo, ataishia kubobea siku za usoni na kuwa nguzo za wajao,” aeleza mweledi huyu.

Akipongeza hatua ya Annastacia, Bw Mbau anasema wasanii wengine wakiiga nyayo zake sekta ya uamuziki nchini itaimarika kwa kiasi kikubwa.

Changamoto

Changamoto kuu inayogubika wasanii chipukizi ni ukosefu wa hela kuingia studioni. Pia, kupata jukwaa kupromoti nyimbo haswa kwenye vyombo vya habari kama vile redio na runinga, ni pandashuka nyingo.

“Nyimbo za waimbaji chipukizi kuchezwa kwenye vyombo vya habari ndicho kizungumkuti kikuu. Lazima mmoja awe watangazaji anaofahamu na wenye moyo wa kusaidia,” asema Annastacia Mitau.

Isitoshe, kuna baadhi ya vyombo vya habari vinavyocheza nyimbo zao na kukosa kuwalipa, vingine vikizitumia kuimarisha biashara zao, matangazo.

Akizungumza katika mazishi ya mwanamuziki tajika wa benga John Mwangi Ng’ang’a maarufu kama John Demathew, Rais Uhuru Kenyatta aliahidi kuangazia masaibu yanayofika waimbaji nchini.

Kiongozi wa taifa pia aliagiza ofisi ya mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma, DPP Noordin Haji na mwenzake wa uhalifu na jinai, DCI George Kinoti kuchunguza muungano wa nyimbo nchini, MCSK kufuatia madai ya kunyanyasa wanamuziki.

KIPAJI: Aanzisha shule ya kutoa mafunzo ya usanii

Na MAGDALENE WANJA

KWA vijana wengi, kozi katika somo la kibiashara la uagizaji bidhaa na huduma – procurement – ni mojawapo ya njia za kuwa na uhakika wa kupata kazi nzuri, hasa nchini Kenya.

Hata hivyo, kwa Cane Mjomba ambaye ni DJ mjini Nakuru alifanya kozi hiyo ya kibiashara kuwafurahisha tu wazazi wake.

“Baada ya kujisajili kufanya kozi ya diploma katika somo la kibiashara katika Kenya Institute of Management (KIM), nilijua kuwa baada ya kufuzu nitapata kazi nzuri,” anasema Mjomba.

Akiwa chuoni, alianza kupata hamu ya ujuzi na kufanya kazi kama DJ, jambo lililomfanya kuanza mazoezi katika taaluma hiyo.

Alijifunza kwa kutumia vifaa alivyokodi kutoka kwa marafiki zake na wakati mwingine alitumia kompyuta yake kujifunza kwa kutumia programu ya VirtualDJ.

Cane Mjomba (kushoto) ni DJ mjini Nakuru. Hapa anamwelekeza mmoja wa wanafunzi wake. Picha/ Magdalene Wanja

“Nilikuwa na hamu sana ya kujifunza kwani nilianza kuazima vifaa hivyo kwa Sh400 kwa siku ili kujipa muda zaidi wa kujifunza,” akasema Mjomba wakati wa mahojiano.

Baada ya kukamilisha masomo yake mnamo mwaka 2015, alipata kazi katika idara ya Posta ambayo ilikuwa fahari kwake na kwa wazazi wake.

Kulingana na Mjomba, kazi hiyo ilimsaidia kuishi maisha mazuri ila haikumpa raha.

Alianza kuifanya kazi ya DJ mnamo wikendi. Ni kazi ambayo ilimpa hela zaidi.

“Nilifanya kazi katika Posta kwa muda wa miezi sita na baada ya hapo nikaiacha kwani nilitaka kuwa DJ,” akasema Mjomba.

Cane Mjomba ni DJ mjini Nakuru. Picha/ Magdalene Wanja

Alipata kazi katika maeneo ya burudani, sherehe kama vile harusi na mikutano ya aina mbalimbali.

Mnamo mwaka 2018, alianzisha shule ya kutoa mafunzo ya usanii ya kuwapa nafasi vijana kujifunza taaluma hiyo.

“Nilianzisha chuo cha mafunzo ili kuziba pengo kubwa lililokuwa kwani vijana wengi walisema kuwa hawakupata nafasi ya kujipatia ujuzi huo,” akasema Mjomba.

Chuo chatoa mafunzo

Chuo hicho hicho kinachojulikana kama Blueray DJ Academy kinatoa mafunzo kwa vijana na wazee wachache ambao wana hamu ya ujuzi huo.

Kozi nzima katika chuo hicho inachukua muda wa miezi miwili katika vitengo kama vile scratching, music blending, beat-matching na masomo ya darasani.

Karo ya kozi nzima ni Sh25,000 ila kuna baadhi ya wanafunzi ambao hulipia kozi zao kwa mpango wa malipo kila siku.

“Kuna kitengo cha watu ambao wana ujuzi ila wangetaka ujuzi zaidi, hao hulipa karo ya Sh15,000,” akasema Bw Mjomba.

Kila mwezi, Mjomba anaweza kupata faida ya kati ya Sh100,000 na Sh150,000 ambazo ni mara tatu ya mshahara aliopata katika kazi yake ya hapo awali.

Anasema kuwa japokuwa wazazi wake walipinga sana hatua yake ya kuacha kazi, baadaye walimuunga mkono baada yake kuwaelezea nia yake.

“Kwa muda wa miaka mitano ya usoni, nina ndoto ya kuanzisha shule za mafunzo ya usanii katika miji mingine nchini,” akasema Mjomba.

WATOTO: Mwanafunzi anayelenga kuwa msanii mtajika nchini

Na PATRICK KILAVUKA

PURITY Wangari, 10, ni mwanafunzi wa darasa la nne katika Shule ya Msingi ya ACK St Johns, Kangemi, Nairobi. Ni kitindamimba katika familia ya Bw John Mbugua na Bi Rosemary Wangui na  matamanio yake ni kuwa mwanamuziki mtajika siku za usoni.

Hata hivyo, anasema kulifikia lengo hilo, ameazamia kujijenga na kutengeneza barabara yake kwa kuwa kiongozi wa nyimbo na kufuatilia masuala ya muziki kwa makini shuleni na kanisani ambako anajiangaza na kuchochea kipawa chake.

Huongoza nyimbo katika ibada za watoto. Mwaka huu, nyota yake ya jaha iling’ara hadi akawashangaza wanafunzi wengine kwa weledi wake wa kuongoza nyimbo pale ambapo aliiwezesha shule yake kushiriki mashindano ya kitaifa katika kiwango cha 819 H na kutia fora kutokea mashinani hadi ya kitaifa.

Msanii chipukizi stadi Purity Wangari, 10, akionyesha tuzo aliyoshinda wakati wa mashindano ya Kanda ya Nairobi. Picha/ Patrick Kilavuka

Shule ilimaliza ya tano bora kitaifa japo huu ulikuwa mwaka wake wa kwanza kuongoza nyimbo shuleni. Mashindano ya Tamasha za Muziki ya Kitaifa yaliandaliwa Chuo Kikuu cha Dedan Kimathi, Kaunti ya Nyeri.

Alituzwa pia kombe la Kanda ya Nairobi katika mashindano hayo na kuiletea shule ya shime.

Wangari aliongoza kikosi cha wanadensi kuwasilisha wasilisho la Kimarakwet anwani ikiwa Chevukwet linalotumbuizwa na vijana wakati wa sherehe za harusi na kuibuka ya kwanza bora kaunti ya Westlands kabla kunogesha mashindano ya Kanda ya Nairobi na kuibuka washindi akiongoza kikundi chao. Hatimaye shule ikafuzu kitaifa.

Purity Wangari akiwa mwalimu wake Lencer Okoth. Picha/Patrick Kilavuka

Kulingana na mwalimu wake Lencer Okoth, Purity alionesha ukakamavu tokea mwanzo. Wakati alikuwa anataka kujua nani atayeongoza wimbo huo, alikuwa wa kwanza kujitokeza akiwa amejiamini na mwenye imani ya kuchukua jukumu hilo.

“Ujasiri wake ulinionyesha kwamba ataweza! Wimbo huu ulitaka kiongozi mkakamavu sana, mwepesi wa kuukariri na mchangamfu. Na kwa kweli pindi tulipoanza kufanya mazoezi ya wimbo, alikuwa mwepesi sana kuukariri jambo ambalo nilinipa moyo kwamba ataweza,” alieleza Okoth ambaye alimumiminia sifa kwa kukiongoza kikosi chake hadi fainali za kitaifa japo wimbo ulikuwa wa lugha tofuati na take ya mama lakini aliujua kwa muda mfupi sana.

Purity ashika taji katikati ya walimu wake. Picha/Patrick Kilavuka

Fauka ya hayo, alimtaja kama mwanafunzi ambaye ana upevu wa wastani kimasomo huku akijimarisha kila uchao katika masomo na kustawisha talanta yake.

Katika uamuzi wa wakaguzi wa nyimbo, walimsifu kwa kuwa kiongozi dhabiti, sauti mwororo na aliye na ari katika kuongoza wimbo kwa ueledi.

Purity akiongozi kikosi cha wasakataji densi kufanya mazoezi ya wasilisho la Kimarakwet Chevukwe ambalo liliibuka tano bora kitaifa. Picha/Patrick Kilavuka

Wangari aliamusha ari ya kipawa chake akiwa darasa la pili.Amekuwa mshiriki sugu wa ibada za watoto kanisa la ACK St Johns, Kangemi anakoongoza nyimbo pia na kiliwakilisha kanisa katika mashindano ya Dayosisi ya Mlima Kenya na yale vijana ambayo hufanyika kanisa la St James Cathedral, Kiambu.

Msanii huyu chipukizi anaonekana kufuata nyendo za ukoo katika kukiimarisha kipaji chake kwani, ndugu yake Naftali Mbugua aliye mwanamuziki alidokeza kwamba, mwanatalanta huyo hufuatilia nyayo zake unyounyo. Yeye hubaki nyuma baada ya ibada na kufanya mazoezi ya kuimba wakati yeye (Naftali) anafanyisha waimbaji wengine mazoezi kanisani.

Purity akiongoza wenzake. Picha/ Patrick Kilavuka

“Wakati tunafanya mazoezi kwa minajili ya kutumbuiza katika ibada au kwa maandalizi ya nyimbo za mashindano, amekuwa akisalia nyuma kufanya mazoezi nasi hali ambayo imemjenga katika tasnia hii,” anasema nduguye Mbugua ambaye pia mchezaji kinanda hodari kanisani na mwalimu wa nyimbo.

Wangari anasema kipaji chake kimenawiri kwa kumtumainia Maulana, nidhamu na kuyatilia maanani mawaidha na ushauri wa wazazi na walimu ambao wamekuwa wa msaada sana. Anajichochea katika kutunga mistari ya nyimbo japo anasema bado anaelekezwa na nduguye.

Purity apokea maagizo kutoka kwa mwalimu wake Lencer Okoth. Picha/Patrick Kilavuka

Anapenda sana somo la Dini na uraibu wake ni kuruka kamba na kucheza densi.

WATOTO: Subira yake katika uigizaji yamvutia heri KBC

Na PATRICK KILAVUKA

Ndoto yake ilikuwa siku moja awe mwigizaji kwenye vipindi vya runinga kwani alikuwa mraibu wa kutazama vipindi vya michezo ya kuigiza kama Machachari na kadhalika.

Ingawa hakujua ndoto yake itafika lini, aliamini na kushikilia msemo kwamba, hayawi hayawi huwa. Ushawishi wake ulitokea pale ambapo alienda majaribio ya kipindi cha Kenda Imani cha runinga KBC na kufua dafu kusajiliwa.

Nicole Wangui, 11, ywanafunzi wa darasa saba shule ya msingi ya Visa Oshwal, Westlands huigiza katika kipindi hicho kama ‘Bela’ binti wa tajiri ambaye maisha ya kifahari yalimuathiri kimaadili licha ya kwamba, alilelewa katika mazingira ya ukristo.

Kando na hayo, humkandamiza mjakazi. Hata hivyo, ana uwezo wa kuigiza uhusika wowote kulingana na jinsi kipindi kinavyoendelea.

Alijiunga na programu hiyo ambayo hupeperusha hewani Jumatano, saa moja usiku, baada ya mama yake Faith Mucheru, zamani mwigizaji wa kipindi cha Vioja Mahakamani kumkutanisha na produsa wa kipindi Jackie Njagi Lidubwii na kumfanyia majaribio kisha akaonesha ueledi wa kuigiza uhusika uliotajwa awali .

“Ni kipindi ambacho kinaangazia stori ya kuwa na matumaini katika changamoto za maisha. Pia, kinatia moyo wajakazi kuwa na imani mambo hubadilika licha ya hali kuwa ndivyo sivyo ,” anasema “Bela” ambaye hufanya igizo za kurekodi kipindi hicho siku ya Jumamosi au likizo.

Mwigizaji chipukizi Nicole Wangui,11, mwanafunzi wa darasa saba shule ya msingi ya Visa Oshwal, Westlands ambaye huigiza shuleni na katika kipindi Kenda Imani kwenye runinga ya KBC. Picha/Patrick Kilavuka

Tayari ameshiriki katika vipindi vitano. Wangui anasema kuigiza kwenye runinga si rahisi kwani kunahitaji kujitolea sana.

Isitoshe, unafaa ujue kwamba mambo ambayo unayaangazia yanakuwa na mashiko kwa jamii na watu huwa na mtazamo chanya kuyahusu kupitia uhusika wako hali ambayo huwapelekea wengine kukosa kuelewa kwamba, hilo ni igizo tu na halina ufafanisho na tabia yako kama mwigizaji japo unachora tu taswira ya kuelimisha au kuhamasisha jamii na umma.

“Kama msanii inakubidi kukubali mtazamo wa wasikilizaji wala watazamaji ndiposa uwe na mtagusano wa rahisi nao ili watambue juhudi zako za kukuza kipawa chako na kuwa kioo cha jamii.

Pamoja na hayo, kuikomboa kutokana na  kasumba za kijamii na mienendo mibovu ambayo inachipukia. Pia, wajue kwamba mwigizaji ni mjumbe tu,” adokeza Wangui ambaye uigizaji ni fani anaipendayo na hutumbuiza.

Fauka ya hayo, anasema ukitaka kushiriki katika kurekodi vipindi, unahitajika uwe mkakamavu wakati unaporekodi na ujaribu kuigiza pasipo kufikiria kwamba unatazamwa na hadhara na ulenga kamera kimasomaso.

Wangui anakiri kwamba  kuchoka wakati mnanasa vipindi mfululizo pamoja na kumakinika kutoka mwanzo hadi mwisho kuwa changamoto ambazo anazipitia.

Miongoni mwa waigizaji ambao anawapenda ni “Joy” wa kipindi cha Machachari na Ariana Grande wa kipindi cha Victories Sam and Cat,  kutokana na ujasiri wao wakati wanapoigiza.

Manufaa? Amepata fursa ya kujiwekea hazina ya kesho kutokana uigizaji wake na hata kukutana na waigizaji wa haiba na kujifunza mengi ya fani kutoka kwao.

Kando na kuigiza, angependa kusomea udaktari usoni na wakati wa kujisawazisha, yeye huogolea na kuimba.

Mwaka huu, ana matamanio ya kushiriki katika mashindano ya Muziki na Drama ya shule za msingi kuonesha uwezo wa kipawa chake katika fani ya uigizaji.

Ushauri? Anasema uigizaji kwenye runinga, huhitaji mwigizaji kuwa mjasiri na mkakamavu, mwenye nidhamu na kujiepusha na kiburi au ujuaji wa ukwasi.