Madiwani Kisumu walaumiwa kwa ziara ya Tanzania

Na RUSHDIE OUDIA

MADIWANI wa kaunti ya Kisumu wameshutumiwa vikali kwa kufanya ziara ya wiki moja ya mafunzo nchini Tanzania, ziara ambayo wakazi wanasema haina umuhimu wowote.

Madiwani hao walizuru taifa hilo jirani kujifunza kuhusu uchukuzi ziwani na jinsi wakazi wa Kisumu wanaweza kufaidi kutokana na rasilimali zilizoko Ziwa Victoria.

Wakazi walisema inasikitisha kuwa ziara hiyo ilijiri wakati kaunti ya Kisumu inaathirika na makali ya janga la corona na ukosefu wa fedha.

Japo idadi ya madiwani waliofanya ziara hiyo haijulikani, wakazi walielezea hasira zao kupitia mitandao ya kijamii wakiwasuta viongozi hao kwa kufuja pesa za umma.

Walisema ziara kama hiyo haisaidii kwa njia yoyote katika vita dhidi ya corona, wakisema ndio changamoto inapaswa kupewa kipaumbele.

Madiwani hao na baadhi ya wafanyakazi wa bunge la kaunti ya Kisumu inadaiwa kuwa wiki jana, Julai 26 walielekea Tanzania na kurejea jana baada ya kuzuru miji ya Arusha na Mwanza. Hivi majuzi, wafanyakazi wawili wa bunge hilo walifariki kutokana na ugonjwa wa Covid-19.

Bunge hilo la kaunti ya Kisumu linatarajiwa kujibu malalamishi ya wakazi kupitia taarifa ndefu na maelezo ya kina kuhusu ziara hiyo.

Hata hivyo, madiwani wawili walitetea ziara hiyo wakisema walijifunza mengi kutoka miji hiyo katika taifa jirani tofauti na madai kwamba ziara yao haikuwa na manufaa yoyote.

Diwani wa wadi ya Milimani Market Sethe Adui Kanga na mwenzake wa wadi ya Awasi Onjiko Maurice Ngeta na Stephe Owiti (wadi ya Kolwa Mashariki) walisifu ziara hiyo.

“Ziara hiyo ilikuwa yenye manufaa kwetu. Tunapanga kutekeleza yale ambayo tulijifunza,” akasema Bw Kanga.

Nyong’o aondoa hofu kuhusu corona inayoshuhudiwa India

Na KNA

GAVANA wa Kisumu Prof Anyang’ Nyong’o, amehimiza wakazi kuondoa hofu kuhusu kuzuka kwa aina ya virusi vya corona – vilivyoathiri watu wengi India – katika kaunti hiyo.

Akihutubia wanahabari Ijumaa, Gavana Nyong’o alisema kuwa Kaunti ya Kisumu haijarekodi kisa chochote kipya cha virusi hivyo tangu raia watano wa India walipopatikana na virusi vya corona mwezi mmoja uliopita.

“Tumeamua kuweka mambo wazi na kutangaza kwamba Kisumu haielekei mkondo wa India. Ni muhimu kuthibitisha kwamba aina ya Covid-19 kutoka India imedhibitiwa na kuangamizwa,” alifichua gavana huyo, ambaye vile vile ni mwenyekiti wa Kamati ya Baraza la Magavana kuhusu Afya.

Katika muda wa siku chache zilizopita, mji huo ulio karibu na Ziwa Victoria, umeripotiwa kuelekea katika hali hatari zaidi baada ya raia watano wa kigeni waliokuwa wakifanya kazi katika kiwanda kimoja kupatikana na aina ya virusi hivyo kutoka India.

Serikali ya Kaunti ilihusisha ufanisi wa kukomesha kusambaa kwa aina hiyo ya virusi kutoka nje ya nchi na juhudi za Idara yake ya Afya iliyochukua hatua haraka kuwaweka waathiriwa karantini iliyolindwa vikali.

Uhuru na Raila kusafiri kwa garimoshi hadi jijini Kisumu

Na RUSHDIE OUDIA

RAIS Uhuru Kenyatta na kiongozi wa chama cha ODM, Raila Odinga, wiki ijayo wanatarajiwa kufanya safari ya kwanza ya gari la moshi kutoka Naivasha hadi Kisumu kufungua reli ya zamani iliyokarabatiwa.

Kulingana na duru, baada ya kufika Kisumu, kiongozi wa nchi na Bw Odinga wanatarajiwa kufungua kituo kipya cha reli karibu na kiwanda cha nguo cha Kisumu Cotton Mills (Kicomi).

Huu ni mmoja wa miradi ambayo Rais Kenyatta atafungua katika ziara yake ya siku tano katika jiji la Kisumu.

Pia atafungua bandari ya Kisumu, uwanja wa michezo wa Jomo Kenyatta uliogharimu Sh350 milioni, jumba la kibiashara la Mamlaka ya Ustawi wa eneo la Ziwa, miongoni mwa miradi mingine.

Mnamo Mei 28, Rais Kenyatta atafungua rasmi Mbita Causeway.

Ataongoza sherehe za Madaraka Dei zitakazoandaliwa katika uwanja mpya wa michezo wa Jomo Kenyatta. Mnamo Jumatano, katibu wa usalama wa ndani Karanja Kibicho aliongoza kamati ya sherehe za kitaifa kuzuru uwanja huo kukagua hali yake. Kamati hiyo ilisema kwamba kazi husika itakamilika kwa wakati.

Akiongea na wanahabari baada ya ziara hiyo, Dkt Kibicho alieleza kwamba kwa sababu ya kanuni za kuzuia msambao wa corona, ni watu wachache watakaoruhusiwa ndani ya uwanja.

“Ni watu 3,000 pekee watakaoruhusiwa ndani ya uwanja wakati wa sherehe hizo huku wengine 20,000 wakifuatilia nje ya uwanja ambako kutawekwa runinga kubwa,” alisema.

Bw Kibicho alikuwa ameandamana na Gavana wa Kisumu Anyang’ Nyong’o na maafisa wengine wa serikali.

Kumekuwa na mabadiliko katika muundo wa uwanja huo ili uweze kusitiri watu wengi ikiwa ni pamoja na kupanuliwa kwa eneo la watu mashuhuri.

“Viwanja havijengwi ili kutumiwa kwa hafla kama hizi na kwa kawaida tungefanya upanuzi usio wa kudumu ili jukwaa la rais liweze kutoshea na kisha tulibomoe. Lakini kwa kuwa tuko na sehemu kubwa hapa tumeamua kujenga eneo la kudumu ambalo litasaidia kwa hafla nyingine siku zijazo,” alieleza Dkt Kibicho.

Kwa wiki kadhaa, jiji la Kisumu limekuwa na shughuli nyingi, huku barabara zinazoelekea katika uwanja huo zikikarabatiwa na kuwekwa alama.

Tayari, kazi ya ujenzi wa barabara ya kilomita 63 kutoka Mamboleo-Miwani-Chemelil itakayogharimu Sh4.9 bilioni imeanza.

Mwanakandarasi anayejenga barabara ya pande mbili ya Kisumu Boys-Mamboleo anajitahidi kumaliza kazi kwenye barabara hiyo ambayo itatumiwa na Rais na wageni wengine siku hiyo.

Barabara zinazoelekea uwanja huo tayari zimewekwa lami na taa za barabarani. Ikulu ndogo ya Kisumu pia inaendelea kufanyiwa mageuzi ikiwa ni pamoja na kuweka ua wa saruji.

Kuonekana kwa ndege za kijeshi katika anga ya kaunti hiyo zikifanya mazoezi ya sherehe hizo pia imefurahisha wakazi wengi.

Hata hivyo, haijabainika iwapo uwanja huo utatumiwa kwa mechi inayosubiriwa kwa hamu kati ya Gor Mahia na AFC Leopards alivyoahidi Rais Kenyatta kuashiria kufunguliwa rasmi.

Uhuru atoa amri miradi Kisumu ikamilike upesi

Na RUSHDIE OUDIA

RAIS Uhuru Kenyatta ametoa maagizo mapya ya kukamilishwa kwa miradi ya mabilioni ya pesa katika Kaunti ya Kisumu huku zabuni za ujenzi wa barabara muhimu zikitolewa upya kwa masharti makali.

Kutangazwa upya kwa zabuni hizo kunafuatia changamoto za kupata ardhi, kuhamishwa kwa makaburi na mabadiliko ya miundo yaliyofanya gharama kuongezeka.

Wakandarasi wameagizwa kuhakikisha kwamba miradi hiyo ya thamani ya Sh2.1 bilioni imekamilika kabla ya Novemba mwaka ujao wakati jiji la Kisumu linakapotarajiwa kuandaa kongamano la kimataifa la Afri-cities.

Kamishna wa kaunti hiyo Bi Josphine Ouko akifuata amri ya rais, aliagiza mkandarasi anayejenga daraja la Mamboleo kuhakikisha barabara zitakuwa tayari kufikia Aprili mwaka ujao wakati Rais Uhuru Kenyatta na aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga watakapotarajiwa kufungua uwanja wa kimataifa wa michezo wa Jomo Kenyatta unaojengwa kwa gharama ya Sh1.4 bilioni.

Kulingana na meneja wa eneo hilo wa shirika la barabara kuu nchini (KeNHA), Bw Cleophas Makau Mutua, kuna sababu nyingi na changamoto zinazoweza kucheleweshwa kukamilika kwa miradi hiyo.

“Mkandarasi alisimamisha kazi Juni 4, 2019 kwa kukosa kulipwa kazi aliyokuwa amefanya na baadaye akakatiza kandarasi akibakisha asilimia 50 kukamilisha mradi wenyewe,” alisema Mutua.

Hii imesababisha zabuni ya kukamilisha sehemu iliyobakia kutangazwa upya na kukabidhiwa kampuni ya Zhongmei Engineering Group Limited. Kampuni hiyo italipwa Sh809.9 milioni.

Ilitia saini kandarasi hiyo Septemba 18, 2020 na ikaanza kazi Novemba.Mkandarasi anayejenga barabara ya kilomita 4.5 kutoka shule ya wavulana ya Kisumu hadi Mamboleo ambaye gharama yake ni Sh2.8 bilioni ambayo ilikwama Juni 4, 2019 pia ameagizwa kuikamilisha.

Barabara hiyo ilianza kujengwa Julai 11, 2016.Ilitarajiwa kukamilika Januari 10, 2018, na licha ya muda kuongezwa hadi Disemba 21, 2019, ilikwama baada ya kampuni ya Israeli ya SBI, kusitisha kazi Juni 4, 2019 na baadaye kukatiza kandarasi Septemba 27, 2019 kwa kukosa kulipwa.

Bi Ouko alikuwa akizungumza baada ya kuongoza mkutano wa kamati ya utekelezaji miradi ya maendeleo katika Kaunti ya Kisumu.

Kaunti hiyo, ambayo ni mojawapo ya ngome kuu za kisiasa za kiongozi wa ODM Raila Odinga, imekuwa ikishuhudia mabadiliko makubwa kimaendeleo katika miaka ya hivi majuzi.

Miradi ya serikali kuu imeshika kasi tangu Rais Kenyatta alipoweka muafaka wa maelewano na Bw Odinga, almarufu handisheki, mnamo Machi 2018 baada ya uchaguzi mkuu wa 2017.

Haya yamefanya baadhi ya wadadisi wa kisiasa kutaja miradi hiyo kama ‘matunda ya handisheki’.Mradi mkuu ambao ni ukarabati wa bandari ya Kisumu haujazinduliwa rasmi hadi sasa, licha ya Rais na Bw Odinga kuuzuru mara kadhaa.

Uzinduzi uliotarajiwa uliahirishwa mara nyingi bila sababu mwafaka kutolewa na wahusika.

Uhuru azindua ujenzi wa uwanja mpya na wa kisasa mjini Kisumu

Na CHRIS ADUNGO

RAIS Uhuru Kenyatta amehakikishia vijana kwamba Serikali yake imejitolea kujenga viwanja vipya, kukarabati vile vilivyopo na kuimarisha miundo-msingi iliyopo ili kufanikisha ndoto zao katika fani mbalimbali za michezo.

Uhuru alisisitiza hayo mnamo Oktoba 22, 2020, katika mji wa Kisumu alikozindua mpango wa kujengwa kwa uwanja mpya wa kisasa na kuamuru ukarabati wa uga wa Moi mjini Kisumu kukamilishwa chini ya kipindi cha miezi sita ijayo.

Ujenzi na ukarabati huo umekadiriwa kugharimu Sh350 milioni.

Rais aliyewahutubia Wakenya katika uwanja wa Maonyesho ya Kilimo mjini Kisumu, alikuwa ameandamana na Kinara wa Chama cha ODM Raila Odinga, Waziri wa Michezo Amina Mohamed na Spika wa Seneti, Ken Lusaka.

“Niko hapa na ndugu yangu Raila (Odinga) kuweka msingi wa ujenzi wa uwanja mpya. Mkandarasi ametuhakikishia kwamba uga huu utakuwa tayari kufikia Aprili 2021. Kwa hivyo, tutarejea hapa kuufungua uwanja huo kwa mechi itakayowakutanisha Gor Mahia na AFC Leopards. Naomba Lusaka aanze mipango ya kuandaa kikosi chake (Leopards) kwa minajili ya gozi hilo,” akasema Uhuru huku akishangiliwa na wakazi wa jiji la Kisumu.

Uhuru alimtaka pia Waziri wa Usalama, Fred Matiang’i kuhakikisha kwamba barabara zote kuelekea katika uwanja huo zinakarabatiwa, kuwekwa lami na taa.

“Ni matarajio yetu makubwa kuona vijana wetu wakichezea vikosi vya haiba kubwa barani Ulaya kama vile Liverpool na Manchester. Tumepania kujenga viwanja hivi kwa ajili yenu. Ni wajibu wenu sasa kuazamia haja ya kutambua vipaji vyenu na kuvitumikisha ipasavyo,” akasema Uhuru.

“Tulikuwa na mpango wa kujenga uwanja mpya kwenye sehemu iliyoko uga wa Jomo Kenyatta kwa sasa. Lakini tulielezwa kwamba nafasi hiyo ni ndogo ndipo tukahamishia mradi huu hapa katika sehemu hii ya Mamboleo ambayo imekuwa ikitumiwa kwa maonyesho ya kilimo,” akaongeza kwa kusisitiza kwamba idhini hiyo ilitolewa na Gavana wa Kisumu Prof Anyang Nyong’o ambaye amejitolea mwenyewe kusimamia ujenzi huo uliozinduliwa na Rais.

Mbali na kutumiwa kwa maonyesho ya kilimo, uga wa Mamboleo umekuwa mwenyeji wa mechi mbalimbali za kikosi cha raga cha Kisumu RFC na mapambano ya kila mwaka ya Onge Ringo kwa wanaraga sita kila upande.

Kukamilika kwa uwanja huo mpya kutaufanya kuwa na uwezo wa kubeba zaidi ya mashabiki 30,000 walioketi kwa minajili ya mashindano mbalimbali ya Ligi Kuu ya Soka na michezo ya kila sampuli katika viwango vya kitaifa, kimaeneo na kimataifa.

Ua utakaozingira uwanja huo ambao utakuwa pia na uwezo wa kuandaa michezo ya hoki, voliboli, riadha, uogeleaji, mpira wa vikapu na netiboli; utakuwa wa kuta za saruji.

Utakuwa pia na mahali pa mashabiki, wachezaji wa akiba na maafisa wa benchi za kiufundi kukalia pamoja na vyumba vya wachezaji kubadilishia sare.

Vyumba vya mazoezi ya viungo, kumbi za burudani, sehemu za watoto kuchezea, vyoo vipya na maegesho ni kati ya maeneo yatakayokuwa na sura mpya katika uga huo utakaowekewa zulia jipya la kisasa.

Wauguzi wagoma kwa mara ya 4 mwaka huu Kisumu

ELIZABETH OJINA

Sekta ya afya kaunti ya Kisumu iko mashakani humu mgomo wa wauguzi na maafisa wa afya ukifikia wiki ya mbili.

Mwaka huu pekee maafisa hao wa afya wamefanya mgomo mara nne. Hospitali nyingi za umma zimebakia mahame huku watu wakilazimika kutafuta matibabu kwenye hospitali za kibinafsi.

Mafisa hao walisema hawatarudi kazini mpaka serikali ya kaunti izingatie maafikiano yao ya ajira ya 2017.

Katibu wa muungano wa wauguzi tawi la Kisumu Maurice Opetu alisema kwamba serikali ya kaunti inasema janga la corona ndio sababu ya kutowashughulikia..

Gavana Anyang Nyong’o alisema kwamba serikali ya kaunti si ya kulaumiwa kwa kuchelewa kwa mishahara.

Katika mawasialo na redio katika eneo hilo, gavana huyo alisema kwamba si Kisumu pekee imechelewesha mishaahara bali kaunti zingine zilikuwa zinapitia hayo pia.

Alisema kwamba si maafisa wa afya pekee walioathiriwa kwani wafanyakazi wengine wa kaunti walikuwa wameathirika..

Lakini mwenyekiti wa kamatii ya afya kaunti ya Kisumu Vincent Jagogo aliambia Taifa Leo kwamba kaunti hiyo ilikuwa na chaguo la kuweka mikakati na benki ya kulipa wafanyakzi.

Wauguzi Kisumu wasisitiza hawarudi kazini hadi walipwe mshahara wa Januari

Na BRENDA AWUOR

WAGONJWA katika hospitali zilizopo Kaunti ya Kisumu, watalazimika kupokea matibabu kutoka hospitali za wamiliki binafsi baada ya wauguzi kusisitiza hawarudi kazini hadi watakapopokea mshahara wao wa mwezi wa Januari.

Baada ya wafanyakazi wa Kaunti ya Kisumu kupokea ujumbe wa kupata msharaha wao kupitia hundi na kusubiri hadi Februari 10, walilazimika kutembelea ofisi ya gavana Prof Peter Anyang’ Nyong’o, huku wakimtaka mwenyewe kuwaeleza sababu ya wao kutolipwa jinsi walivyoagana.

Wafanyakazi hao waliowakilishwa na mwenyekiti wa wafanyikazi, Bw Edward Kojiema, Katibu wa idara ya wafanyakazi maabarani, Bw Hillary Awili na katibu wa wafanyakazi Bw Craus Okumu, wamesisitiza wataendelea kuandaa gwaride la kuitisha mshahara – salary parade – eneo la ofisi ya gavana na kutorudi kazini hadi watakapopokea mshahara wao wa Januari.

Msemaji wa gavana wa Kisumu, Bw Aloyce Ager, akiongea na wanahabari, amehimiza wafanyakazi hao warudi kazini kwa kuwa “kuanzia Jumatano wiki ijayo watapokea mshahara”.

Bw Ager ameeleza kuwa pesa tayari zipo kwenye benki na kufikia Jumatano hundi zote zitakuwa tayari kuchukuliwa na wafanyakazi.

Ameonya wafanyikazi dhidi ya kuandaa mgomo kila mara wanapokumbwa na tatizo lolote.

Kaunti ina wafanyakazi zaidi ya 4,000 na kila mmoja licha ya kutopokea mshahara wa Januari ni muhimu waendelee kufanya kazi huku wakiwa na imani ya kupokea mshahara wao wiki ijayo, amesema.

”Kila mfanyakazi wa kaunti, mimi mwenyewe nikiwemo, hatujapokea mshahara wa Januari ila tupo kazini na ndiposa nawasihi wauguzi warejee hospitalini wakiwa na matumaini ya kupokea mshahara wao Jumatano,” amesema Bw Ager.

Rais, Raila walihofia kuzomewa Kisumu

Na RUSHDIE OUDIA

Baadhi ya wakazi katika eneo la Kisumu walipanga kumwaibisha Rais Uhuru Kenyatta wakati wa kuzindua upya bandari jijini humo, hatua iliyopelekea shughuli hiyo kuahirishwa kwa mara nyingine, imefichuka.

Uzinduzi huo ulipangiwa kufanyika kesho lakini ukaaihirishwa kwa mara ya pili huku ripoti, mapema wiki jana, zikiarifu kwamba barua za mwaliko zilikuwa zimetumwa kwa wageni kutoka afisi kuu ya Halmashauri ya Bandari Kenya (KPA) jijini Mombasa.

Wageni hao baadaye waliarifiwa kuhusu kuahirishwa kwa hafla hiyo kupitia barua-pepe iliyotumwa kwa Afisa Mkuu wa Mauzo wa KPA Simon Meja.

“Kuhusiana na mwaliko wa kuhudhuria hafla ya uzinduzi wa Bandari ya Kisumu na miundomsingi mingine, ningependa kuwaarifu kuwa shughuli hiyo imeahirishwa hadi siku nyingine. Poleni kutokana na mabadiliko haya ya ratiba,” ikasema ujumbe huo.

Kuna ripoti ambazo hazijathibitishwa zilizosema kwamba hafla hiyo iliahirishwa kutokana na hofu ya kiusalama na kutokamilika kwa ujenzi wa baadhi ya sehemu za bandari.

Kwa mujibu wa ripoti fiche kutoka kwa kikosi cha utekelezaji wa maendeleo bandarini, hafla hiyo ilisukumwa mbele kutokana na habari za kijasusi kwamba makundi ya vijana yalikuwa yamepanga kuwaaibisha Rais Uhuru Kenyatta na kinara wa ODM Raila Odinga kwa kuwazoma.

“Wafanyabiashara hasa wa kitengo cha Jua-kali ambao walihamishwa eneo hilo kimabavu wana machungu na hadi leo wanaendelea kuhangaika,” ikaarifa ripoti hiyo.

Aidha, ripoti hiyo ilidai kuwa makundi hayo yalikuwa yakipanga kutumia utata unaozingira kurejea kwa mwanaharakati Miguna Miguna, kujaribu kuzua taharuki jijini Kisumu kabla ya kuwasili kwa Rais na Bw Odinga.

Mnamo Ijumaa wakati wa kikao cha kujadili mapendekezo ya ripoti ya Jopokazi la Maridhiano (BBI) mjini Kisii, Bw Odinga alisema kwamba serikali haiogopi Bw Miguna na anafaa aruhusiwe arejee nchini.

Kabla ya tangazo la kuahirishwa kwa uzinduzi huo, maandalizi yalikuwa yameshika kasi huku maswali yakiibuka kuhusu iwapo marais kutoka mataifa jirani wangefika na kuhudhuria hafla hiyo ya kipekee.

Ingawa siri kali ilidumishwa kuhusu majina ya watu mashuhuri ambao wangefika, kulikuwa na ripoti kwamba Rais wa Uganda Yoweri Museveni na mwenzake wa Tanzania John Pombe Magufuli wangehudhuria.

Mnamo Alhamisi, maafisa wa wizara za Uchukuzi na Miundomsingi wakiongozwa na Katibu katika wizara hiyo Esther Koimett waliandaa mkutano na kuzuru bandari ya Kisumu.

Kulikuwa na mikutano miwili kati ya saa mbili na saa nne asubuhi katika Taasisi ya Mafunzo ya Shirika la Reli ambayo mada yake ilikuwa kujadili namna ya kufanikisha uzinduzi huo.

Mikutano hiyo iliwajumuisha mameneja wa bandari hiyo na shirika la reli, maafisa wa usalama na wenzao kutoka kwa Mamlaka ya Ushuru(KRA).

Kwa mujibu wa afisa mmoja aliyehudhuria, ajenda kuu ilikuwa maandalizi ya mwisho kabla ya uzinduzi uliofaa kufanyika kesho.

Rais azuru Kisumu kwa mara ya saba

Na WAANDISHI WETU

RAIS Uhuru Kenyatta alizuru Bandari ya Kisumu kwa mara ya saba kukagua ujenzi wake unavyoendelea.

Rais alifanya ziara hiyo ya ghafla Jumanne na ambayo ilikuwa ya kufahamu hatua ambayo imepigwa kwenye ujenzi wa bandari ya kisasa inayojengwa kwa gharama ya Sh3 bilioni.

Duru ziliarifu Taifa Leo kwamba ziara hiyo ilichochewa na masuala ibuka kwenye ujenzi huo ambayo yalisababisha hafla ya kufunguliwa kwa mradi huo iliyofaa kuandaliwa Agosti 15 kuahirishwa.

Msemaji wa Ikulu, Bi Kanze Dena-Mararo hata hivyo alisema kwamba hakukuwa na habari zozote kuhusu ziara hiyo ya kushtukiza na hakutoa ufafanuzi zaidi.

Akiwa ameandamana na maafisa wachache, Rais Kenyatta alikaa kwenye bandari hiyo kwa saa mbili akikagua mambo kadhaa kisha akaondoka na kuandaa mkutano na wanaohusika na ujenzi huo katika Ikulu ya Kisumu.

Usalama ulikuwa umeimarishwa huku mamia ya wananchi waliogundua Rais alikuwa eneo hilo pamoja na wanahabari wakizuiwa kuingia kujionea kilichokuwa kikiendelea.

“Rais alisafiri kwa ndege moja kwa moja kutoka Suswa, Kaunti ya Narok alikokuwa akizindua awamu ya pili ya reli ya kisasa SGR hadi Kisumu,” akasema afisa ambaye hakutaka anukuliwe na vyombo vya habari.

Rais na walioandamana naye walitembelea sehemu kuu ya bandari na Taasisi ya Mafunzo ya Usafiri wa Majini.

Meli

Pia alikagua meli ya kale ya MV Uhuru, ambayo imekarabatiwa na hata imefanyiwa majaribio ziwani na kwa sasa imefika hadi nchi jirani ya Uganda.

Vifaa hitajika pia vilisafirishwa kutoka Mombasa, ishara tosha kwamba matayarisho yanaendelea kukamilika na kupisha ufunguzi wa bandari hiyo kwenye hafla ambayo itaongozwa na Rais Kenyatta, Kinara wa ODM Raila Odinga na marais kutoka mataifa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Taifa Leo imegundua kwamba tatizo kuu ambalo limechelewesha ukamilishaji wa mradi huo ni kero la gugumaji na shughuli ya kuchimba na kuondoa mchanga.

Ukarabati Bandari ya Kisumu waumiza wengi kibiashara

Na WAANDISHI WETU

MAELFU ya wafanyabiashara katika Kaunti ya Kisumu wanakadiria hasara kubwa baada ya majengo na vibanda vyao kubomolewa.

Ubomozi huo ulifanywa na serikali kuu katika juhudi za kukarabati Bandari ya Kisumu.

Ingawa mradi huo ni miongoni mwa ile inayochukuliwa kama minofu iliyotokana na handsheki ya Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa ODM Raila Odinga, wakazi wa eneo hilo lililo ngome ya Bw Odinga kisiasa sasa wameachwa mataani.

Mradi huo umesifiwa kwamba utageuza Kisumu kuwa kitovu cha kibiashara katika ukanda wa Afrika Mashariki kupitia kwa usafirishaji mizigo kwenye Ziwa Victoria.

Ripoti zinasema kuna wafanyabiashara wasiopungua 3,000 ambao wameathirika na bomoa bomoa ambayo inaendelea katika eneo hilo, wakiwemo wanasiasa.

Aliyekuwa Mbunge wa Gem, Bw Jakoyo Midiwo ambaye mkahawa wake ulibomolewa, jana alisema alipewa notisi ya siku 90 kuhama ambayo ilifaa kukamilika Oktoba 12 lakini akafurushwa siku 34 pekee baada ya kupokea notisi hiyo.

“Hii si haki. Nilikuwa nimeajiri watu zaidi ya 50 ambao maisha yao sasa yameathirika. Ombi langu kutaka Mkurugenzi Mkuu wa Kenya Railways, Bw Odinga na Gavana Anyang’ Ngong’o waingilie kati halikuzaa matunda,” akasema Bw Midiwo.

Naibu Gavana wa Kisumu, Bw Mathews Owili alidai serikali ya kaunti imeanza kuwapa watu walioathirika sehemu mpya za kufanyia biashara zao.

“Tunasikitishwa na hasara iliyotokea lakini haya mambo yanafanyika kwa kasi mno. Kuna hali ya dharura kwa hivyo pia sisi tunatafuta jinsi ya kuwapa wote walioathirika sehemu mpya za kufanyia biashara zao ili kupunguza athari zinazotokana na shughuli hii nzima,” akasema.

Hata hivyo, alisisitiza watu wote waliokuwa katika ardhi za Kenya Railways na Mamlaka ya Bandari Kenya (KPA) watahamishwa.

Kulingana naye, baadhi ya wafanyabiashara wadogo wameanza kujengewa vibanda karibu na uwanja wa Jomo Kenyatta na katika ufuo wa Dunga.

Mwenyekiti wa Shirikisho la Kitaifa la Biashara na Viwanda (KNCCI), Bw Israel Agina alisema ingawa ukarabati wa bandari ni muhimu, inapaswa wahusika waendeshe shughuli hiyo wakizingatia maisha ya binadamu.

“Tunafurahi na tumepokea maendeleo hayo kwa moyo mkunjufu lakini haistahili yalete masononeko kwa wakazi,” akasema Bw Agina.

Baadhi ya wafanyabiashara waliofurushwa wamesema sasa hawana budi ila kutafuta njia nyingine za kujikimu kimaisha, wakitumai watarudia hali yao ya awali angalau kabla watoto waanze kurudi shuleni mwezi ujao wakiwa na mahitaji chungu nzima.

Kuna wale ambao wateja sasa huwaita kuwahudumia nyumbani kama vile vinyozi na wasusi, huku wengine wakiamua kufanya biashara zao chini ya miti kama vile waliomiliki mikahawa midogo.

Bi Tabitha Ougo, ambaye ni mfanyabiashara aliyepoteza mkahawa, saluni na kinyozi katika eneo la Winmart ameamua kuendeleza huduma zake za uuzaji vyakula katika lango la Chuo Kikuu cha Maseno kilicho mjini.

Ripoti ya Justus Ochieng’, Victor Raballa, Rushdie Oudia na Lydia Ngugi

HANDISHEKI: Kisumu kupata taa za trafiki miaka 118 baadaye!

Na JUSTUS OCHIENG

KISUMU itapata taa za trafiki kwa mara ya kwanza kabisa, miaka 118 tangu jiji hilo la eneo la Nyanza kujengwa, ishara ya matunda ya handisheki kuzidi kuenea katika ngome za kiongozi wa chama cha ODM, Bw Raila Odinga.

Taa hizo zitatumika kudhibiti msongamano wa magari katika miungano ya barabara na vivuko vya wanaotembea kwa miguu.

Aidha, taa hizo za trafiki zitawekwa miaka 18 tangu rais mstaafu Daniel Arap Moi kutangaza rasmi Kisumu kuwa mji.

Mnamo 2001, Kisumu iliadhimisha miaka 100 tangu kuanzishwa kwake katika sherehe ya kufana iliyohudhuriwa na marais Daniel Moi, Yoweri Museveni wa Uganda na mstaafu Benjamin Mkapa wa Tanzania.

Ni katika maadhimisho hayo ambapo Moi alitangaza Kisumu kuwa mji.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Barabara Kuu (KeNHA) Bw Peter Mundinia, alisema jana kuwa taa hizo zitawekwa katika miungano mitatu mikuu kwenye barabara ya Kisumu-Kakamega.

Bw Mundinia alisema kando na kuimarisha miundomsingi na kujenga barabara hiyo kuu ili iwe ya pande mbili, kumekuwa na haja ya kuweka taa za trafiki ili kuleta usalama barabarani kwani hii itasaidia kupunguza ajali.

Alieleza: “Kuna vivuko vya wanaotembea kwa miguu na pia miungano ya magari kuvuka kutoka upande mmoja hadi mwingine, hivyo taa zitahakikisha miundomsingi hii inatumika vyema zaidi.”

Mkurugenzi huyo alisema kampuni ya NAS International ndiyo imegawiwa kandarasi ya kuweka taa hizo kutoka kwa kampuni ya SBI International Holdings ambayo ndiyo inajenga barabara ya pande mbili ya Kisumu-Nyang’ori.

Afisa Mkuu Mtendaji wa NAS Bw Nicholas Airo alisema taa hizo za trafiki zitawekwa katika mizunguko ya Kisumu Boys, Patels na Kondele.

“Tayari tumeanza kuweka taa Patels na tutaendelea katika miungano hiyo mingine,” Bw Airo aliambia Taifa Leo.

Aliongeza kuwa watafanya hamasisho kwa umma na shuleni kwa wanafunzi pamoja na kukutana na wadau wote wa uchukuzi ili kuwahamasisha kuhusu matumizi ya taa za trafiki.

Raila azomewa na wakazi wa Kisumu

RUSHDIE OUDIA Na PETER MBURU

WAKAZI wa Muhoroni katika Kaunti ya Kisumu, Jumatatu walimkemea kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga alipoenda kuzindua mradi wa viwanda eneo hilo.

Wakibeba mabango na kuandamana, wakazi hao walilalamika kuwa serikali inataka kutwaa ardhi yao kwa nguvu ili kujenga mradi huo, wakisisitiza kuwa hawaungi mkono mradi huo, wala hawakushauriwa kabla ya uamuzi huo kufikiwa.

Hatua hiyo ya mapokezi mabaya kwa Bw Odinga ilikuwa ya kushangaza katika ngome yake ya kisiasa, ambako amekuwa akiheshimika kwa miaka mingi na maamuzi yake kupokelewa bila maswali.

Vioja vilianza wakati Bw Odinga aliposema kuwa ujenzi wa mradi huo wa kiuchumi una umuhimu kuliko kuacha ardhi hiyo kuendelea kutumiwa kwa kilimo.

Mara baada ya kutamka hayo, wakazi walimkemea na kupiga makelele, wakisema wanataka kuachiwa ardhi yao badala ya ujenzi wa mradi huo.

“Kwa nini mnaniaibisha? Ninaleta maendeleo ilhali hamuoni miradi ambayo itawafaidi,” Bw Odinga akashangaa.

Vijana hao walichapwa na watu wanaounga mkono ujenzi wa mradi huo na mabango kuharibiwa, huku naye Bw Odinga akijaribu kutuliza hali na kuwarai wakazi kukubali mradi huo.

Alisema mradi huo utajengwa katika ardhi ya ekari 500 na ujenzi utaanza punde tu Sh500 milioni zikitolewa na serikali mwaka huu, huku Sh2.5 bilioni zikitarajiwa kutolewa na serikali mwaka ujao.

“Rais Uhuru Kenyatta, Rais wa Uganda Yoweri Museveni na wa DRC Felix Tshisekedi wanatarajiwa kuzindua rasmi ujenzi wa mradi huo hapo Agosti mwaka huu,” akasema Bw Odinga.

Alikuwa ameandamana na mawaziri Peter Munya wa Biashara na Viwanda, James Macharia wa Uchukuzi na John Munyes wa Madini.

Hata hivyo, ilikuja siku chache tu baada yake na Rais Kenyatta kurejea mikono mitupu kutoka China ambapo walikuwa wameenda kutafuta mkopo wa kuendeleza ujenzi wa Reli Ya Kisasa (SGR) hadi Kisumu, baada ykea kuahidi ujenzi huo.

“Reli mpya ya SGR itajengwa kutoka Naivasha, Narok, Bomet, Sondu hadi Kisumu,” Bw Odinga akaeleza wakazi wa Sondu kabla ya kuandamana na Rais Kenyatta nchini China kuomba mkopo.

Kisumu kuandaa Elgon Cup 2019, ni mara ya kwanza Kenya inaandaa kombe hili nje ya Nairobi

Na GEOFFREY ANENE

MJI wa Kisumu umeteuliwa kuandaa mechi ya nyumbani ya Kenya ya raga ya kimataifa ya wachezaji 15 kila upande ya Elgon Cup dhidi ya Uganda mwaka 2019.

Hii ni mara ya kwanza kabisa mkondo wa kombe hili unaenda nje ya Nairobi.

Taarifa kutoka Shirikisho la Raga la Kenya (KRU) inasema kwamba Kisumu ilituma ombi kuwa mwenyeji wa kombe hili mwaka 2018 na kukubaliwa na shirikisho hilo kama mpango wake wa kusambaza mechi za kimataifa. “Kuandaa mchuano huu mjini Kisumu ni mojawapo ya mpango wa KRU kusambaza mechi za kimataifa. Klabu zingine pia zinashawishiwa kuomba mashindano mengine ya kimataifa kwa sababu itachangia pakubwa katika kuimarisha vifaa vyao pamoja na kukuza mchezo wa raga. Tayari klabu zimeonyesha zina uwezo wa kuvutia umati wa mashabiki na tumeshuhudia hivyo mjini Kisumu wakati wa duru ya kitaifa ya raga ya wachezaji saba kila upande ya Dala Sevens,” alisema Naibu Mwenyekiti wa KRU, Thomas Opiyo.

Timu ya taifa ya raga ya wachezaji 15 kila upande ya Kenya almaarufu Simbas inatarajiwa kuanza matayarisho baada ya Ligi Kuu (Kenya Cup) kutamatika Mei 11.

Gavana afurahia

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mji wa Kisumu kuwa mwenyeji wa Elgon Cup mwaka 2019 hapo Machi 28, Gavana wa Kisumu, Profesa Anyang’ Nyong’o alisema, “Hii ni mara ya pili tunazindua shindano la raga katika kaunti ya Kisumu na tunatumai haitakuwa mara ya mwisho. Lengo letu ni kusaidia michezo kikamilifu katika kaunti hii ili Kenya iweze kupata sehemu ya kukuza wanariadha na wanaspoti wake kutoka kaunti hii. Ugatuzi unamaanisha kwamba kila mtu humu nchini ajihisi hajaachwa nje katika sehemu zote za maisha.”

“Nafurahia sana Elgon Cup kuja Kisumu mwezi Juni mwaka 2019. Tumekuwa tukilenga kukuza nafasi yetu mjini Kisumu kama mji wa mashindano makubwa na ninakaribisha timu ya Uganda pamoja na mashabiki wote kutoka eneo hili,” aliongeza Achie Alai, Waziri wa Utalii na Michezo wa kaunti ya Kisumu.

Kenya itakuwa ikitetea taji ililoshinda mwaka 2018 kwa kuchabanga Uganda 34-16 jijini Kampala mwezi Mei na kulemea majirani hao wake tena 38-22 Julai.

Kusafiri Kisumu kwa ndege sasa ni ghali kuliko Mombasa

 Na GERALD ANDAE

IDADI kubwa ya watu wanaotumia ndege kusafiri kuelekea Kisumu msimu huu wa krismasi kwa mara ya kwanza imesababisha nauli kupanda kiasi cha kuzidi ile ya kuelekea Mombasa kwa mara ya kwanza.

Watu wanaotumia ndege za Jambojet kuelekea Kisumu wakitoka Nairobi kuanzia jana walilipa Sh14,500, wakati safari za kuelekea Mombasa zitagharimu Sh11,500 msimu huu na kufikia Desemba 24 nauli hiyo itashuka hadi Sh4,500.

Ndege za Fly540 nazo jana kuelekea Kisumu zililipisha Sh11,270.

Wasafiri wa kuelekea Kisumu ka kawaida hulipa kati ya Sh4,500 na Sh6,500 lakini kutokana na kuongezeka kwa watu wanaotafuta huduma hizo sasa bei imepanda, ijapokuwa kwa kawaida nauli za kuelekea Mombasa kwa kawaida huwa juu ya zile za kuelekea huko.

Hata hivyo, nauli za kuelekea mjini Eldoret bado hazijapanda kwani si watu wengi wanatumia ndege kwa usafiri.

Kusafiri kutoka Eldoret hadi Nairobi kwa ndege za Jambojet kati ya Desemba 23 na 24 kutagharimu kati ya Sh9,500 na Sh8,500, kiwango cha juu, hata hivyo, ikilinganishwa na nyakati za kawaida ambapo huwa Sh4,500.

Nauli hizo zilikuwa kulingana na watu waliokuwa wamelipia usafiri kufikia jana, na zinatarajiwa kupanda kadri inavyokaribia krismasi.

Lakini siku ya krismasi yenyewe nauli zitashuka kwani ni watu wachache tu ambao watakuwa wakisafiri wakati huo.

Changamoto ambayo wahudumu wa ndege hizo wamekuwa wakikumbana nazo ni kama kuwafanya Wakenya kukubali kulipia ndege mapema ili kupata usafiri wa bei nafuu.

“Wakenya wanataka kulipia leo wakitaka kusafiri kesho, ama baada ya siku mbili,” akasema afisa wa Jambojet.

Aidha, idadi kubwa ya wasafiri imefanya treni ya SGR kulipiwa hadi Januari.

Nyanya, 76 afariki baada ya kukosa kumtumbuiza Rais Kisumu

Na JUSTUS OCHIENG

MWANAMKE aliyekosa nafasi ya kumtumbuiza Rais Uhuru Kenyatta kwenye ziara yake jijini Kisumu majuzi alizimia na kufariki Jumatatu.

Familia ya mwanamke huyo, aliyetambuliwa kama Wilfrida Abwajo mwenye umri wa miaka 76, ilisema alifariki kutokana na mshtuko aliopata baada ya kunyimwa nafasi hiyo.

Kulingana na Bi Pamela Ogal, ambaye ndiye mwenyekiti wa Kundi la Wanawake la Oruba, linalojumuisha Wachezaji Densi wa Kitamaduni wa Dodo, walikuwa wamealikwa na Waziri wa Utalii na Utamaduni wa Kaunti ya Kisumu Achie Alai.

Alisema kuwa waliteuliwa kuwa miongoni mwa watu ambao wangemtumbuiza Rais Kenyattta kwenye ziara hiyo, baada ya kushiriki katika hafla za sherehe ya Sikukuu ya Jamhuri mnamo Jumatano iliyopita.

“Tuliunganishwa na waziri huyo na aliyekuwa diwani wa Wadi ya Kolwa Mashariki Robert Otuge. Baadaye waziri huyo alituahidi kwamba angetuunganisha na Kikosi cha Kumtumbuiza Rais (PPMC) ili kupata nafasi ya kumtumbuiza pamoja na wageni wengine. Tulifanikiwa kufika alikokuwa Rais mwendo wa saa mbili asubuhi bila kuchelewa, ila hatukupata nafasi ya kumtumbuiza,” akasema Bi Ogal.

Hata hivyo, Bi Alai alijitetea vikali akisema kuwa kitengo cha Rais ndicho kinachopanga na kuamua wale ambao hutumbuiza katika hafla zake. “Hili ni jukumu la PPMC. Tulichagua makundi 30 ya muziki na kuyakabidhi kitengo hicho. Hata hivyo, ndicho chenye uamuzi wa mwisho kuhusu wale wanaopaswa kutumbuiza,” akasema Bi Alai.

Kwa upande wake, PPMC ilisema kuwa watumbuizaji wote ambao walimtumbuiza Rais siku hiyo walilipwa. Kwenye taarifa, mwakilishi wa kitengo hicho Donald Otoyo alisema kwamba watumbuizaji wote wanaoalikwa na serikali za kaunti huwa wanashughulikiwa na serikali husika ya ugatuzi wala si serikali kuu.

“Kulingana na taratibu zilizopo, watumbuizaji wote wanaoalikwa na serikali za kaunti wanapaswa kulipwa nayo kulingana na makubaliano kati yao. Hakikisho hili lilitolewa na afisi ya gavana na afisa wa utamaduni wa kaunti aliyekuwepo. Nitatoa maelezo zaidi,” akasema Dkt Otoyo, kwenye mazungumzo na ‘Taifa Leo.’

Marafiki wa marehemu walisema kuwa alijitolea kuwaongoza wanawake 15 wa kundi la Oruba kufanya mazoezi kwa matumaini kwamba wangepewa nafasi ya kutimiza ndoto yao ya kutumbuiza Rais. Vikundi mbalimbali vilimtumbuiza Rais wakati akizindua Majaribio ya Mpango wa Afya kwa Wote (UHC) uwanjani Mamboleo.

Uhuru na Raila washauriana kisiri usiku

Na WAANDISHI WETU

RAIS Uhuru Kenyatta alikutana kisiri na kiongozi wa ODM Raila Odinga mnamo Alhamisi usiku katika Ikulu ndogo ya Kisumu bila wandani wao.

Baada ya msururu wa mikutano ya hadhara Alhamisi, Rais Kenyatta kwanza alikutana na viongozi wa Luo Nyanza katika Ikulu ya Kisumu kabla baadaye kukutana na Bw Odinga wakiwa wawili.

Taifa Leo haikubaini ajenda ya mkutano kati ya Rais Kenyatta na viongozi wa Luo Nyanza ambao ulikuwa na usiri mkubwa kwani hata viongozi kutoka Kisii waliokuwepo waliagizwa kuondoka.

Gavana wa Kisii James Ongwae, na mwenzake wa Nyamira John Nyagarama pamoja na mbunge wa Kitutu Chache Kaskazini Jimmy Angwenyi waliombwa kuondoka katika mkutano huo uliohusisha magavana, wabunge na maseneta wa Luo Nyanza.

Hata hivyo, baadaye Rais Kenyatta vilevile alikutana na viongozi hao wa Kisii.

Seneta wa Siaya James Orengo na Kiongozi wa walio wachache Bungeni John Mbadi walisema Rais Kenyatta na Bw Odinga walitaka kukutana na viongozi wa Luo Nyanza pekee.

“Mnatakiwa muondoke kwa heshima kwani Rais angependa kukutana na viongozi wa Luo Nyanza, bila hata MCAs,” Bw Orengo alinukuliwa akisema.

Naye Mbadi akaongeza: “Ni ombi kwa heshima tu, Rais atakutana na kila mtu baadaye.” Naibu Rais William Ruto ambaye alikuwa ameandamana na Rais katika ziara hiyo ya siku mbili hakudhuria kikao hicho cha Ikulu ya Kisumu.

Gavana wa Migori Okoth Obado vilevile hakuhudhuria kikao hicho.

Baada ya mikutano na viongozi hao, Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki Oburu Odinga alifichua kuwa Rais Kenyatta baadaye alikutana na Bw Odinga faraghani kwa muda.

“Baadhi ya mambo ambayo walizungumzia ni mpango wa kuwafidia waathiriwa wa ghasia za baada ya uchaguzi wa 2017,” Bw Oburu aliambia kituo cha radio cha Ramogi katika mahojiano.

Jana asubuhi, Bw Odinga pamoja na mkewe Ida Odinga walimwandalia Rais Kenyatta kiamsha kinywa nyumbani kwao Bondo,

Baadaye, wawili hao walitunukiwa shahada za uzamifu (PHD) za heshima kutokana na hatua yao ya kukomesha uhasama wa kisiasa na kuamua kufanya kazi pamoja.

Walitunukiwa heshima hiyo na Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia ya Jaramogi Oginga Odinga (JOOUST) wakati wa sherehe ya mahafala mjini Bondo, Kaunti ya Siaya.

Wakihutubu baada ya kutunikiwa shahada hizo, viongozi hao waliapa kuhakikisha muafaka waliotia saini mnamo Machi 9 unazaa matunda ambayo yatawafaidi Wakenya wote.

“Nitajitolea kuendelea kufanya kazi na ndugu yangu Raila na Wakenya wote ili kujenga nchi yenye usalama, umoja na maafanikio kwa manufaa ya wote,” Rais akasema.

Bw Odinga alisema salamu yao nje ya Jumba la Harambee ilionyesha “kujitolea kwetu kama taifa kujifunza kutokana na makosa ya zamani ili kujiandaa kwa ufanisi.”

“Kama taifa, hatupaswi kukubali kugawanywa tena na siasa au chuki za kikabila,” kiongozi huyo wa chama cha ODM akasema.

Baadaye jana jioni, Rais Kenyatta alifufuliza hadi kaburi la babake Raila, hayati mzee Jaramogi Oginga Odinga ambapo aliweka shada la maua. Rais vilevile aliweka maua katika kaburi la Fidel Odinga, mwanawe, Raila.

“Tunataka kuishi vile Mzee Kenyatta na Mzee Jaramogi walikuwa wakiishi, kwa kuleta jamii zetu pamoja,”Rais Kenyatta aliambia jamaa za Bw Odinga.

Hoteli Kisumu zavuna matunda ya muafaka kwenye ziara ya Rais

Na ELIZABETH OJINA-250

MIKAHAWA ya kifahari jijini Kisumu imevuna pakubwa kutokana na ziara ya Rais Uhuru Kenyatta kuzindua mpango wa Afya kwa Wote hapo Alhamisi.

Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa Rais Kenyatta kuzuru kaunti hiyo baada ya kuingia kwa muafaka baina yake na kiongozi wa upinzani Bw Raila Odinga, ambao wamiliki wa hoteli walikiri umewaletea mapeni.

Kulingana na mwenyekiti wa Muungano wa Wamiliki wa Hoteli wa Magharibi mwa Kenya  Bw Robinson Anyal, hoteli kama Acacia, Imperial na Sovereign zilijaa wateja.

“Hoteli kuu tatu zimejaa. Acacia ina vitanda 91, Imperial 80 na Sovereign 40. Paliposalia na nafasi labda ni Grand Royal Swiss Hotel,” akaambia Taifa Leo.

Aliongeza, “Kando na malazi katika Hoteli ya Acacia, biashara ya vyakula imenoga. Tunatarajia mikahawa mingine hapa jijini kushuhudia kuongezeka kwa mapato.”

Alisema ziara ya Rais itafungua nafasi za biashara kwa mikahawa kama Kakwacha, Tilapia Resort na mikahawa mingine inayouza samaki eneo la ufuo wa Lwang’.

“Biashara ya teksi pia itaendelea kuvutia wateja katika siku mbili zijazo kufuatia ziara ya Rais,” akasema.

Alikariri kuwa ziara hiyo inapiga jeki biashara ya hoteli, huku nyingi zikitamatisha  biashara ya kukodisha maeneo ya hotuba.

“Ziara ya Rais ni hakikisho kuu kwamba jiji la Kisumu li salama. Biashara ya kumbi za hotuba inaendelea kutamatika. Hoteli nyingi zinategemea watalii wa humu nchini,” akasema.

Meneja wa Hoteli ya Acacia Duncan Mwangi alisema hoteli hiyo ilipata wateja wengi zaidi wiki hii kutokana na ziara hiyo.

“Ziara ya Rais imeleta imani kuu na kuyeyusha hisia na fikra potovu ambazo watu wamekuwa nazo kuhusu Kisumu. Tunatarajia kuwa itaimarisha utalii wetu. Kwa hakika, muafaka wa Bw Kenyatta na Bw Raila umezaa matunda,” akasema.

Referenda yaja, Uhuru adokezea Wakenya

Na VALENTINE OBARA

RAIS Uhuru Kenyatta Alhamisi alidokeza kuunga mkono marekebisho ya Katiba ili kuwe na nafasi zaidi za uongozi serikalini.

Pendekezo hilo limekuwa likipigiwa debe na Chama cha ODM kinachoongozwa na Bw Raila Odinga, huku likipingwa na wandani wa Naibu Rais William Ruto.

Akihutubu jana katika eneo la Ahero, na baadaye katika uwanja wa maonyesho ya kilimo wa Mamboleo, Kaunti ya Kisumu, Rais alisema kuwa walipoweka muafaka wa maelewano Machi 9 na Bw Odinga, walikubaliana kutafuta jinsi ya kuepusha umwagikaji damu nchini kila uchaguzi wa urais unapofanywa ambapo kila jamii hutaka mtu wao awe mamlakani huku jamii nyingine zikiachwa nje.

Kwa msingi huu, alisema wanatafuta suluhisho la kuepusha mshindi wa urais kutwikwa mamlaka yote ya uongozi.

“Hii siasa ya taifa letu la Kenya ambayo kila saa ni siasa ya mashindano, wengine wanaingia serikalini na wengine wanabaki nje, hatutaki mashindano aina hiyo. Tunataka mashindano ambayo yanatuwezesha kuhakikisha kila jamii, kila Mkenya ataona serikali ni yake. Hiyo ndiyo njia ya kuleta amani na maendeleo ya kudumu,” akasema.

Pendekezo la ODM ni kwamba, katiba irekebishwe ili kuwe na nafasi ya waziri mkuu na manaibu wake na rais awe akichaguliwa na Wabunge.

Wakati huo huo, Rais Kenyatta alisisimua wafuasi wa upinzani kwa kutangaza Bw Odinga yuko ndani ya serikali.

Tangu wawili hao walipoweka muafaka, baadhi ya viongozi wamekuwa wakitaka kujua kama Bw Odinga alipewa kiti serikalini ingawa yeye husisitiza angali katika upinzani.

“Jakom (Bw Odinga) sasa tunasema yuko ndani ya serikali. Huwa tunashauriana na tunaongea kuhusu mambo yanayohusu wananchi,” akasema alipohutubia wananchi waliomshangilia katika eneo la Ahero.

Bw Odinga aliambia wakazi kuwa walielewana na rais kurudisha umoja wa Kenya jinsi ilivyokuwa kabla taifa lilipopata uhuru wa kujitawala kutoka kwa wakoloni. Picha/ Ondari Ogega

Alikuwa Kisumu kuzindua mpango wa utoaji huduma bora za afya kwa wananchi kwa bei nafuu, ambayo ni mojawapo ya nguzo nne kuu za maendeleo anazolenga kutekeleza kabla akamilishe hatamu yake ya pili iliyo ya mwisho ya uongozi mnamo 2022.

Awamu ya kwanza ya mpango huo itatekelezwa Kisumu, Nyeri, Isiolo na Machakos kabla kusambazwa hadi kaunti zingine zote.

Bw Odinga aliambia wakazi kuwa walielewana na rais kurudisha umoja wa Kenya jinsi ilivyokuwa kabla taifa lilipopata uhuru wa kujitawala kutoka kwa wakoloni.

Kwa upande wake, Bw Ruto alisifu umoja ulioletwa na muafaka wa wawili hao na kusema viongozi wote wamekubali kuzika uhasama uliokuwepo awali.

“Mkiona Uhuru Kenyatta na muone Waziri Mkuu Raila na muone ‘hustler’ hapa katikati yao mjue mambo ni sawa. Sisi sote tumekubaliana tutatembea pamoja na kuunganisha Wakenya,” akasema.

Rais Kenyatta aliwasili kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Kisumu dakika chache baada ya saa tano asubuhi alipolakiwa rasmi na Bw Odinga pamoja na Bw Ruto, miongoni mwa viongozi wengine.

Ziara hiyo ilikuwa ya kwanza ya Rais Kenyatta Kisumu tangu muafaka huo maarufu na Bw Odinga.

Leo wawili hao wanatarajiwa katika Chuo Kikuu cha Jaramogi Oginga Odinga kilicho Bondo, Kaunti ya Siaya, ambako ni nyumbani kwa Bw Odinga.

MIMBA ZA MAPEMA: Chifu aliyejitolea kukuza maadili katika jamii

Na RUSHDIE OUDIA

HUKU taifa likiduwazwa na idadi kubwa ya wasichana wa shule za msingi na upili wanaogonga vichwa vya habari kwa kushika mimba za mapema, wakazi wa eneo la Nyawita, Maseno, Kaunti ya Kisumu, wanatamani enzi ambapo walikuwa na chifu mchapa kazi.

Mojawapo ya hatua ambazo zimechukuliwa na serikali kuu kutatua janga hilo la wasichana wadogo kupata uja uzito ni kutoa onyo kwa machifu ambao wamezembea kazini, kwani inaaminika baadhi yao hujihusisha katika maelewano kati ya familia za wasichana wanaonajisiwa ili wahusika wakwepe adhabu za kisheria.

Katika kata ndogo ya Nyawita, Chifu Mstaafu Harrison Okwema, amesalia kuwa maarufu na kipenzi cha wengi kwa misimamo mikali ya kunyorosha maadili katika jamii, aliyokuwa akichukua kabla kustaafu kwake miaka miwili iliyopita.

Bw Okwama, ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 64 anasifika sana kwa juhudi zake katika kukabiliana na ukahaba, utengenezaji pombe haramu hasa katika mtaa duni wa Obunga na kuwakabili wahalifu.

Juhudi zake zilirejesha hali ya nidhamu katika mtaa huo duni. Kutokana na kuwa jina lake na sura yake pekee zilitosha kuwatia wasiwasi waliotaka kuthubutu kupotoka kimaadili, alikuwa akiweka picha yake nje ya afisi alimohudumu, hali iliyoonekana kuwatia wasiwasi wahalifu.

Kwa sasa, umaarufu wake unalinganishwa na machifu wa awali kama Chifu Onunga wa Kisumu na Chifu Odera Akang’o, ambao walihudumu miaka mingi iliyopita. Machifu hao waliogopwa sana na wakazi kutokana na ukakamavu mkubwa wa kinidhamu katika utendakazi wao.

Bw Okwama amemwoa Bi Ludia Adoyo, na ni baba wa watoto watatu. Na licha ya ukakamavu wake kazini, mojawapo wa sifa zake kuu ni kuwa mcheshi.

Hata hivyo, hilo halikumfanya kushawishiwa na vitendo vya wahalifu. Alibaki mtetezi mkuu wa serikali ya kitaifa, hali iliyomfanya kujipatia umaarufu mkubwa unaomfuata hata baada ya kustaafu.

Wakati ‘Taifa Leo’ ilipomtembelea katika mtaa wa Migosi, alikuwa akiendelea na shughuli zake za kawaida.

Chifu huyo alizaliwa katika eneo la Kitutu Chache, Kaunti ya Kisii. Alisomea katika Shule ya Msingi ya Ong’icha ambapo baadaye alijiunga na Shule ya Upili ya Agoro Sare katika eneo la Oyugis, Kaunti ya Homa Bay. Alifanya Mtihani wa Baraza la Afrika Mashariki (EAEC) mnamo 1979.

Baadaye, alijunga na Kampuni ya Sukari ya Chemelil kutoka 1981 hadi 1988. Baada ya kuhudumu huko, alifanya kazi katika Wizara ya Kazi za Umma kama fundi wa mitambo kwa miaka sita.

Akiwa humo, serikali ilitangaza kazi katika za utawala wa mkoa, ambapo alituma maombi.

Aliitwa katika mahojiano na kupita. Aliajiriwa kama Naibu Chifu wa Kata Ndogo ya Nyawita alikohudumu hadi kustaafu kwake mnamo 2016. Baadhi ya maovu anayochukia hadi sasa ni ukahaba, wizi wa mabavu na ulevi.

“Nachukia sana pombe haramu, hasa zinazotengenezewa sehemu za Alego na Ugenga. Vile vile, nawachukia sana makahaba ambao huendesha shughuli zao hasa katika mtaa wa Kondele. Hao ndio wanawapotosha vijana wengi na kupoteza mwelekeo katika maisha yao. Hilo ndilo lilinifanya kuendeleza -misako mikali dhidi yao na kuwakamata,” akasema.

Katika kuukabili ukahaba, Bw Okwama alikuwa akiwakamata wasichana wadogo ambao walikuwa wakijihusisha katika vitendo hivyo na kuwapeleka katika vituo vya polisi vya Kondele na Obunga.

Hili lilimfanya kupendwa zaidi na wakazi, kwani suala la ukahaba miongoni mwa watoto limebaki kuwa tatizo sugu miongoni mwao.

Anaeleza kuwa alifanikiwa kupata habari kuhusu visa vilivyokuwa vikiendelea katika maeneo fiche kutokana na ushirikiano mwema na wakazi.

“Walikuwa wakinieleza kuhusu maovu yote yanayoendelea. Hilo liliifanya kuwa rahisi kuwakabili wahalifu wote waliohusika au kushiriki katika vitendo vyovyote vile,” anaeleza.

Kutokana na juhudi zake, baadhi ya mafanikio makuu aliyopata ni kupunguza kiwango cha ulevi katika eneo hilo. “Nilifanikiwa kupunguza ulevi katika kata ya Nyamita kwa zaidi ya asilimia 50,” asema.

Zaidi ya hayo, anajivunia kuwaondoa wahalifu katika kata hiyo, hali iliyowafanya kutorokea maeneo kama Riat na milima ya Nyahera.

“Wakati nilistaafu, nilizungumza na naibu chifu mpya, ambapo nilimwambia kuendeleza kazi yangu kwani ndipo ataweza kupata uungwaji mkono kutoka kwa wakazi,” akasema.

Baadhi ya mambo anayojivunia ni kutokamatwa au kushtakiwa kwa kujihusisha na kitendo chochote cha uhalifu katika muda wote aliohudumu kama naibu chifu.

Kwa sasa, Bw Okwama anajihusisha na kilimo katika kaunti za Kisii na Kisumu.

Na licha ya kustaafu kwake, anaamini kwamba bado ana uwezo wa kuwahudumia wananchi ikiwa anaweza kupewa nafasi ya msimamizi wa wadi ama kijiji chini ya mfumo mpya wa ugatuzi.

Asema kuwa anaweza kutumia mbinu zizo hizo katika utendakazi wake. “Ikiwa ninaweza kupewa jukumu hilo, nitatumia tajriba yangu kubwa kwa manufaa ya wananchi,” aliongeza.

Na kwa kuwa eneo hilo lina uongozi mpya, hakuwa na budi ila kuondoa picha yake iliyokuwepo afisini na kuipeleka nyumbani kwake Kisii.

Wakazi wanamsifia kwa kutekeleza yale yote aliyoyasema au kuahidi. “Ni mtu wa kipekee ambaye tungali tunatamani kuwa naye,” mkazi Collins Omondi, aliambia Taifa Leo.

Jaramogi ahusishwa na mzozo wa mpakani

TOM MATOKE na WYCLIFF KIPSANG

MZOZO wa mpaka kati ya Kaunti za Nandi na Kisumu ulichukua mwelekeo mpya Jumatatu baada ya jina la aliyekuwa makamu wa rais Jaramogi Oginga Odinga kutajwa.

Viongozi kutoka Kaunti ya Nandi walisema kaunti hizo mbili zilibuniwa Jaramogi alipokuwa makamu wa rais wa rais wa kwanza wa Kenya Mzee Jomo Kenyatta.

Viongozi hao wakiongozwa na aliyekuwa mwenyekiti wa lililokuwa baraza la mji wa Nandi Charles Tanui walidai kwamba Jaramogi alimuomba Mzee Kenyatta kuruhusu watu wa jamii ya Waluo waliokuwa wakiishi Kisumu kuhama na kuishi maeneo ya milimani ya Nandi msimu wa mvua kubwa ili wasisombwe na mafuriko.

Walisema Mzee Kenyatta alikubali ombi hilo na mamia ya watu kutoka Nyanza waliruhusiwa kuishi Nandi karibu na mpaka kwa muda hadi mvua ipungue.

“Wakati Jaramogi aliacha kazi ya makamu wa rais, wenzetu kutoka Kisumu waliendelea kuishi katika ardhi ndani ya Kaunti ya Nandi hadi Mzee Kenyatta alipokufa 1978,” alisema Bw Tanui.

Viongozi wa Kaunti ya Nandi wameunga mipango ya Gavana Stephen Sang mpaka huo uchunguzwe upya. Bw Sang na viongozi hao wanataka maeneobunge ya Muhoroni na Kisumu Mashariki wakisema yalitwaliwa wakati wa ujenzi wa reli.

Wanadai kwamba Waingereza waliwafukuza Wanandi kwa sababu ya kupinga ujenzi wa reli. Bw Sang aliongoza mkutano wa viongozi wa Nandi miezi mitatu iliyopita kabla ya Tume ya Ardhi kuzuru eneo hilo.

Mkutano huo ulipitisha azimio la kuhakikisha maeneo yanayozozaniwa yamerejeshwa Kaunti ya Nandi. Walitaja maeneo hayo kama miji ya Miwani, Kibos, Kibigori, Kopere, Chemelil, Fort Tenan na Muhoroni. Hatua hiyo ilizua taharuki kwenye mpaka wa kaunti hizo mbili na kuathiri uwekezaji katika kilimo.

Mwanamke ndani miaka 15 kwa kunajisi tineja

Na RUSHDIE OUDIA

KATIKA kisa kisicho cha kawaida, Mahakama ya Kisumu Jumatano ilimhukumu mwanamke wa miaka 24 kifungo kikali cha miaka 15 gerezani kwa kufanya mapenzi na mvulana tineja wa miaka 15.

Hukumu hiyo ilizua mjadala mkali miongoni mwa watumizi wa mitandao ya kijamii ya Twitter na Facebook kwani mara nyingi visa vingi kuhusu ubakaji na unajisi huhusisha wanaume kuwadhulumu wasichana na wanawake.

Bi Judith Wandera (pichani) alipatikana na hatia ya unajisi na kumfanyia mtoto kitendo kichafu kinyume na sheria mnamo Julai 5, 2017 katika Kaunti ya Kisumu.

Mashahidi saba walitoa ushahidi dhidi yake kwenye kesi hiyo huku Bi Wandera akijitetea kivyake.

Kwenye uamuzi wake, Hakimu Mkuu wa Kisumu, Bi Joan Wambilyanga alisema wawili hao walikamatwa Julai 17, mwaka mmoja baada ya kuanza uhusiano wa kimapenzi.

“Wote wawili walikiri kushiriki mapenzi, wakati mwingine walitumia kinga na wakati mwingine hawakutumia,” akasema Bi Wambilyanga alipokuwa akitoa hukumu.

Akijitetea, mshtakiwa alidai hangeweza kujua umri wa mvulana huyo walipokutana kwani alipomtazama hakuonekana kama mwenye umri wa chini ya miaka 18, na pia alikuwa ni mwendeshaji wa bodaboda.

Sheria inayohusu makosa ya vitendo vya ngono huruhusu mshtakiwa kujitetea kuwa hakufahamu umri wa mtu kutokana na maumbile, lakini mahakama ilipata kuwa Bi Wandera hakuweka juhudi zozote kubainisha umri wa tineja huyo.

Hakimu alipuuzilia mbali tetesi za mshtakiwa na kumwambia angethibitisha iwapo alichukua hatua yoyote kutambua umri wa mlalamishi.

“Hapakuwa na ushahidi wowote kuonyesha kuwa mlalamishi alidanganya kuhusu umri wake na utetezi wa mshtakiwa umetupwa nje kwa sababu alishindwa kuthibitisha hatua alizochukua kubainisha kama mvulana huyo alikuwa na umri wa chini ya miaka 18,” akasema Bi Wambilyanga.

Mshtakiwa aliambia korti kuwa tineja huyo alikuwa akitumia dawa za kulevya na alionekana tu mwenye umri mdogo alipokuja mahakamani kutoa ushahidi.

 

Aliacha masomo

Katika ushahidi wake, tineja huyo alieleza mahakama jinsi alivyoacha shule alipokuwa katika darasa la saba mwaka wa 2016 na akawa mhudumu wa bodaboda.

Hakimu alisema wawili hao walikamatwa mara mbili awali, mshtakiwa akaambiwa akomeshe uhusiano huo baada ya mama ya mvulana kulalamika kuhusu tofauti ya umri wao lakini mshtakiwa akapuuza hayo yote.

Bi Wandera aliomba asamehewe kwa sababu ana mtoto, kaka na mama ambao wanamtegemea kimaisha. “Mimi pekee ndiye ninategemewa. Tafadhali nisamehe sitarudia kosa hilo,” akaomba. Lakini ombi lake halikufua dafu.

Hukumu iliposomwa alijikuna kichwa huku macho yake yakionekana kana kwamba alitaka kulia, kisha akamtazama dadake aliyekuwa mahakamani.
Wakati wote kesi ilipokuwa ikisikilizwa, Bi Wandera alikuwa mtulivu lakini hukumu iliposomwa alibadilika kwani ni kama hakutarajia adhabu kali kiasi hicho.

Bila Miguna, hakuna amani, wakazi Kisumu waimba

RUSHDIE OUDIA na EDDY ODHIAMBO

WAKAZI wa Kisumu Jumatano waliandamana katika eneo la Kondele, kulalamikia kuendelea kuzuiliwa kwa wakili Miguna Miguna katika uwanja wa Kimataifa wa ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA) jijini Nairobi.

Familia ya Miguna inayoishi Ahero eneobunge la Nyando pia ililalamikia jinsi mwana wao anavyonyanyaswa na serikali na kumtaka Rais Uhuru Kenyatta kuingilia kati ili aachiliwe huru.

Waandamanaji walioanza kwa kusukuma mawe kufunga barabara inayounganisha miji ya Kisumu na Kakamega na kulazimisha wenye magari kutumia njia mbadala.

Waliimba “Bila Miguna, hakuna amani” na kubeba mabango wakitaka Miguna atendewe haki. Baadhi yao walichoma magurudumu ya magari na wengine kuvalia jezi zilizoandikwa kauli mbiu iliyobuniwa na wakili huyo ya “uasi.”

Familia ikiongozwa na kaka ya Miguna, Bw Ondiek Miguna, iliiomba serikali kumwachilia mwana wao kuingia nchini.

Dkt Miguna alifurushwa Kenya Februari lakini akarejea Jumatatu kufuatia agizo la korti la kumruhusu kuingia Kenya.

Hata hivyo, akiwa JKIA, alikataa kutoa paspoti yake ya Canada na kukataa kutia sahihi stakabadhi za kuomba uraia wa Kenya alizokabidhiwa na idara ya uhamiaji.

Ingawa idara hiyo inasema aliasi uraia wa Kenya miongo miwili iliyopita, Dkt Miguna anasema hakuwahi kuuasi na alizaliwa Kenya jambo linalompa haki ya kurudishiwa paspoti yake.

 

Huzuni

Bw Ondiek aliambia Taifa Leo kwamba familia inasononeshwa na jinsi Miguna anavyohangaishwa na polisi na serikali. Katika kijiji alichozaliwa cha Migina, wakazi walihuzunishwa na kuendelea kuzuiliwa kwake Nairobi.

“Hatujawahi kuwa na amani tangu Miguna alipokamatwa baada ya kumuapisha Raila Odinga hadi kisa cha hivi punde cha kuzuiliwa kwake. Baadhi yetu hatuli tukashiba tukisikiliza redio na kutazama runinga tukitarajia habari za kuachiliwa kwake,” alisema Bw Ondiek.

Wafuasi na familia ya Bw Miguna walisema wanahisi kusalitiwa na muungano wa NASA na mwafaka kati ya Rais na Bw Odinga.

“Tulifikiri mwafaka huo ungerahisisha mambo, ilhali wangali wanaendelea kuzuilia Miguna. Iwapo hawatamwachilia, tutakataa mwafaka huo na maridhiano,” alisema mwandamanaji mmoja.

Aliongeza: “Jaji Mkuu David Maraga anafaa kusimamisha shughuli zote za mahakama hadi maagizo ya korti yaheshimiwe”.

Ziara ya Rais Uhuru na Raila mjini Kisumu yaahirishwa

Na JUSTUS WANGA

MKUTANO wa pamoja kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa NASA Raila Odinga uliotaribiwa kufanyika wiki hii mjini Kisumu umeahirishwa kutoa nafasi kwa muda wa kushughulikia masuala ibuka yanayotisha kuathiri muafaka kati yao.

Wandani wa Bw Odinga wameanza kushuku kujitolea kwa Jubilee katika mchakato wa mazungumzo baada ya kiongozi wa wengine bunge Aden Duale kupinga kujumuishwa kwa suala ya mageuzi  katika mfumo wa uchaguzi ambalo ni mojawapo yale ambayo Rais na Odinga walikubali kujadili.

Akiongea katika runinga moja ya humu nchini Bw Duale ambaye ni Mbunge wa Garissa Mjini pia alipuuzilia mbali mageuzi katika mfumo wa uongozi nchini.

Wakati huo huo, mpango wa balozi Martin Kimani na Wakili Paul Mwangi kuwahutubia wanahabari Ijumaa ili kuelezea hatua iliyopigwa kuhusu suala hilo iliahirishwa dakika zake mwisho.

Mbw Kimani na Mwangi waliteuliwa na Rais Kenyatta pamoja na Bw Odinga kutayarisha mwongozo ambao utasaidia kufanikisha malengo ya mwafaka huo.
Duru zilisema kuwa “kuna masuala ambayo pande husika hawajakubaliana.” Walipofikiwa kwa njia ya siku wawili hao hawakutaja sababu ya kufutilia mbali kikao na wanahabari.

Taifa Jumapili pia imegundua kuwa Kamati hiyo itapanuliwa kwa kujumuisha angalau wanachama watano kutoka kila upande huku akianza kibarua rasmi.

Shauku ya kambi ya Bw Odinga inatokana na hali kwamba japo ameshawishi uongozi wa chama hicho kuunga mkono ushirikiano huo, kufikia sasa Rais Kenyatta hajaitisha mkutano wa kundi la wabunge wake (PG) au asasi yoyote ya chama hicho kuhimiza wafuasi wake kuunga mkono mwafaka huo. Vile vile, wanasema Rais Kenyatta hajaitisha kikao maalum cha baraza la mawaziri kuwajuza kuhusu yaliyomo ndani ya mkataba kati yake na Bw Odinga.

“Tunataka kuona taarifa kutoka afisi ya Rais ikielezea hatua ambazo zimewekwa kuafikia uwiano na masuala ambayo yalikubaliwa. Sawa na Odinga, tunaamini kwamba Rais ana nia njema. Tunataka kuona wakianza kazi,” mmoja wa wandani wa Bw Odinga alisema.

Chama cha ODM kinashikilia kuwa hatima ya mwafaka huo utategemea kama iwapo Rais alielekeza nchini kufunua ukurasa mpya huku masuala ya serikali yakiendeshwa kwa namna tofauti.

Hata hivyo, hakuna kiongozi kutoka kambi ya Kenyatta ambaye amepinga mwafaka huo isipokuwa Seneta wa Tharaka Nithi Profesa Kithure Kindiki ambaye ameonya Rais kutahadhari anapojadiliana na Bw Odinga kwa sababu, “ni mwanasiasa mjanja”.

Seneta wa Siaya James Orengo, ambaye ni mshirika wa karibu wa Bw Odinga aliwaonya Rais Kenyatta na kiongozi huo wa upinzani kuwaonya wafuasi wao dhidi ya kutoa matamshi ambayo yanaweza kusambaratisha mwafaka huo.

 

EABL yalenga kuunda lita milioni 100 za ‘Keg’ Kisumu

Na BERNARDINE MUTANU

Ufanisi wa kiwanda cha pombe Kisumu kilichozinduliwa na Kampuni ya EABL utategemea uzinduzi wa vilabu vya pombe takriban 4,000 eneo hilo.

Kiwanda hicho kitakachogharimu kampuni hiyo Sh15 bilioni kinatarajiwa kukamilika Julai mwaka 2019 na kinalenga kuwapa kazi wasambazaji.

Kampuni hiyo ilizindua kiwanda hicho kwa lengo la kutengeneza pombe aina ya KEG ambayo ni pombe ya bei ya chini.

Kiwanda hicho kitaajiri wafanyikazi 100 moja kwa moja huku idadi ya wakulima watakaokisambazia miwa wakiongezwa hadi 30,000.

Kiwanda hicho kinalenga kutengeneza lita milioni 100 za KEG kila mwaka.

Yabainika viwanja viwili vya ndege havina hati

Na LUCY KILALO

MAMLAKA ya Viwanja vya Ndege (KAA) imeagizwa kufafanua ni vipi haina hatimiliki za ardhi ya Kiwanja cha Ndege cha Manda, Kaunti ya Lamu na kile cha Kisumu.

“Itakuwaje ikiwa mtu atatokezea na kudai ardhi hii?” aliuliza mwenyekiti wa Kamati ya Bunge la Kitaifa ya Uwekezaji wa Umma, Abdulswamad Shariff Nassir.

Wasimamizi wa mamlaka hiyo ambao walikuwa wamefika mbele ya kamati hiyo kujibu maswali ya ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Matumizi ya Fedha za Umma, hawakuweza kufafanua kuhusu ziliko stakabadhi hiyo.

Bw Nassir alitaka pia kujua kwa nini baadhi ya hati miliki za ardhi ya viwanja vya Wilson, Eldoret ziko na mawakili, na ile ya Ukunda kuripotiwa na wasimamizi kuwa na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC).

“Tutajuwaje kuwa hati miliki hazijatumiwa kuchukulia mikopo?” aliuliza mwenyekiti.

“Ikiwa zilipotea, ziliwahi kuripotiwa kupotea? Hii ni kwa sababu tunaona mashirika ya serikali hata yakiweka matangazo magazetini ya vitabu vya risiti vilivyopotea,” alisema Bw Nassir.

 

Hofu

Mbunge wa Kiminini, Bw Chris Wamalwa, pia alielezea hofu yake kuwa isiwe kuwa ardhi hiyo imetumika kama rehani kuchukua mikopo mikubwa ambayo hatimaye, inafanya nchi zilizotoa mikopo kuichukua.

Afisa Mkuu mtendaji wa mamlaka hiyo, Jonny Andersen hata hivyo, alikana suala la wao kutumia ardhi hiyo kwa mikopo.

Hata hivyo, Bw Andersen aliahidi kuhakikisha kuwa wanawasilisha majibu yanayohitajika kuhusiana na hati miliki hizo.

Wakili wa kampuni, Bi Katherine Kisila, alikuwa na wakati mgumu kuelezea kuhusu hati miliki hizo, hata baada ya kuelezea kamati kuwa yeye ndiye anayestahili kuzihifadhi.

Kamati hiyo iliagiza mamlaka hiyo ihakikishe kuwa inawasiliana na Tume ya Kitaifa ya Ardhi, kubainisha ukweli kuhusu hati miliki hizo, pamoja na mawakili husika kuelezea sababu za kuwa wenye kuhifadhi hati miliki hizo.

 

Kandarasi za nyua

Mamlaka hiyo pia inakabiliwa na maswali mengine ya kuelezea sababu za kandarasi mbili ya kuweka ua katika mtaa wa Embakasi, na uwanja wa ndege ya

Ukunda za Sh24.5 milioni na Sh8.9 milioni zilifutiliwa mbali na kulazimu wakandarasi kulipwa kwa kukatiza mkataba.

Wanakamati hiyo walihofia kuwa miradi hiyo ilikuwa njama ya kufuja pesa za umma.

Mamlaka hiyo pia ilihitajika tena kuelezea vipi kampuni ya kibinafsi ya Transglobal iliongezewa muda wa kukodisha ardhi yake kutoka miaka 20 hadi 40 na ni vipi kampuni ilichukua mkopo wa zaidi ya Sh500 milioni.

Kamati hiyo ilielezea kuwa itamuita Waziri wa Fedha pamoja na Benki ya Standard Chartered kufafanua zaidi masuala hayo.

“Mkopo ulitolewa kwa madhumuni yapi, na ni nani aliyeidhinisha muda wa kukodi kutoka moaka 20 hadi 40?” aliuliza Bw Nassir.

Mkaguzi Mkuu Edward Ouko katika ripoti yake amekosoa masuala ya kifedha katika mamlaka hiyo ambayo huenda yakafanya mlipaji kodi kupoteza mabilioni ya pesa.

 

Filamu ya kimataifa ‘Black Panther’ yazinduliwa jijini Kisumu

Mwigizaji maarufu kutoka humu nchini Lupita Nyong’o (kushoto) akiigiza katika filamu mpya ya kimataifa ‘Black Panther’. Picha/ Hisani

NA CECIL ODONGO

FILAMU ya aina yake ya muigizaji maarufu nchini Lupita Nyong’o ‘Black Panther’ ilizinduliwa Jumanne rasmi kwa mara ya kwanza humu nchini na Afrika nzima kwenye hafla ya haiba kubwa iliyoandaliwa jijini Kisumu.

Lupita mwenye umri wa miaka 34, anatazamwa kama muigizaji bora kutoka bara la Afrika kwenye jukwaa la sinema za Hollywood.

Kuandaliwa kwa onyesho hilo hapa nchini ni njia moja ya kumpa heshima na kumtunuku kwa juhudi zake zilizomfikisha kwenye anga za juu za uigizaji.

Japo mshindi huyo wa tuzo za Oscar hakuhudhuria sherehe hiyo, viongozi wa kaunti ya Kisumu wakiongozwa na Naibu Gavana wa Kisumu Mathews Owili, waziri wa Michezo na Utamaduni kwenye kaunti Bi Achi Ojany Alai miongoni mwa wageni wengine mashuhuri kutoka ndani na nje ya nchi walikUwepo kushuhudia tukio hilo la kihistoria.

Ratiba ya Lupita iliwa na shughuli nyingi kwa hivyo hangeweza kupata muda wa kufika nchini.

 

Ujasusi

Kwenye sinema ‘Black Panther’ Lupita huigiza kama mhusika Nakia ambaye ni jasusi kwenye ufalme unaoitwa Wakanda. Yeye ni moja wa wa wenye usemi mkubwa kwenye familia ya Wakanda.

Ilikuwa ni fahari kubwa kwa mji wa Kisumu kuteuliwa kuandaa uzinduzi huo wa kwanza Afrika japo kuna miji kadhaa ya hadhi barani. Kaunti ya Kisumu ndiko anakotoka mwigizaji Lupita na babake Prof Peter Anyang’  Nyong’o ambaye ndiye gavana.

Hoteli nyingi za mji huo zilizaa wageni huku tiketi za ndege kuelekea mji huo kutoka kwingineko zikichukuliwa zote na wasafiri walioenda kushuhudia uzinduzi huo.

Vyombo vya habari vya kimataifa na vya ndani ya nchi pia havikusazwa kwa kuwa vyote vilikuwepo kunasa matukio yote.

Kutakuwa na utazamaji wa sinema hiyo Jumatano Siku ya Wapendanao kule Anga Sky Cinema, Nairobi na shoo ya kwanza kwa umma itafanyika Alhamisi Anga IMAX.

Uzinduzi huo aidha umetuliza joto la kisiasa katikakaunti hiyo anakotoka kinara wa NASA Raila Odinga aliyeapishwa kuwa ‘rais wa wananchi.’

Wakazi wa kaunti hiyo walionekana kufurahia kumuona mmoja wao akiigiza katika filamu ya Hollywood, hali iliyoondoa fikra za kisiasa katika Siku ya Valentino.