Leroy Sane aagana na Manchester City, ayoyomea Bayern Munich

Na CHRIS ADUNGO

KLABU ya Manchester City imekiri kwamba itamsajili kiungo na nahodha wa Aston Villa, Jack Grealish, kwa matarajio kwamba atakuwa kizibo kamili cha Leroy Sane ambaye ameagana nao rasmi.

Man-City wamefikia maamuzi ya kumuuza Sane ambaye kwa sasa atayoyomea Ujerumani kuvalia jezi za Bayern Munich kwa takriban Sh6.3 bilioni huku kiasi hicho cha fedha kikitarajiwa kuongezeka hadi Sh7.7 bilioni iwapo Bayern watatinga fainali ya kipute cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu huu.

Sane, 24, aliingia katika sajili rasmi ya Man-City mnamo 2016 baada ya kuagana na Schalke 04 ya Ujerumani kwa kima cha Sh5 bilioni.

Tangu wakati huo, Sane amewaongoza Man-City kutia kapuni mataji mawili ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Sane ambaye kwa sasa atalipwa mshahara wa Sh2.8 bilioni kwa mwaka kambini mwa Bayern, alikuwa sehemu muhimu ya kikosi cha Man-City kilichotia kapuni mataji matatu kwa mkupuo msimu uliopita.

Hata hivyo, amesalia mkekani kwa takriban msimu huu mzima wa 2019-20 kufuatia jeraha baya la goti alilolipata mwanzoni mwa muhula katika mechi ya Community Shield dhidi ya Liverpool.

Mnamo Juni 27, 2020, kocha Pep Guardiola alisema kwamba Sane ambaye mkataba wake na sasa na Man-City unatarajiwa kutamatika rasmi mwishoni mwa msimu ujao, alikuwa amekataa kurefusha muda wa kuhudumu kwake uwanjani Etihad na alikuwa amewasilisha ombi la kutaka kuachiliwa kujiunga na Bayern.

Sane anatazamiwa sasa kuyoyomea Ujerumani chini ya kipindi cha saa 24 zijazo ili kurasimisha uhamisho wake hadi Bayern waliotawazwa mabingwa wa soka ya Bundesliga msimu huu.

Ingawa hawezi kuchezea Bayern katika kipute cha UEFA msimu huu, Sane hatarejea tena kambini mwa Man-City na ina maana kwamba gozi dhidi ya Burnley mnamo Juni 22, 2020 ndio uliokuwa mchuano wake wa mwisho ndani ya jezi za Man-City. Sane aliwajibishwa kwa dakika 11 za mwisho wa kipindi cha pili katika mechi hiyo ya EPL.

Japo Guardiola amefichua haja ya kumsajili Grealish ambaye pia anawaniwa na Man-United, Man-City wameshikilia kwamba uwepo wa viungo Phil Foden, Riyad Mahrez, Bernardo Silva na Raheem Sterling bado utawasaza kuwa thabiti na imara zaidi.

Sane anaondoka ugani Etihad akijivunia kuchezea Man-City katika jumla ya mechi 192 na kufunga mabao 52.

Kubwa zaidi ambalo linamwaminisha Guardiola kwamba watajinasia maarifa ya Grealish ni hali tete ya sasa ya Villa kwenye kampeni za EPL huku wakikodolea jicho hatari ya kushushwa ngazi mwishoni mwa muhula huu.

City yasema heri Sane aozee benchi badala ya kuuzia Bayern kwa bei ya kutupa

Na CHRIS ADUNGO

MANCHESTER City wamesema itakuwa heri zaidi kwa kiungo Leroy Sane kuingia katika mwaka wa mwisho katika mkataba kati yake nao na awe huru kuondoka bila ada yoyote kuliko kuzinadi huduma zake hadi Bayern Munich kwa bei ya kutupa.

Bayern ambao ni miamba wa soka ya Ujerumani wamekuwa wakivizia huduma za Sane ambaye ni nyota wa zamani wa Schalke 04 nchini Ujerumani, kwa miezi 12 iliyopita.

Kubwa zaidi linachochochea hamasa yao ni ungamo la hivi karibuni la Sane ambaye amesisitiza kwamba hafurahii maisha yake uwanjani Etihad, Uingereza na atakuwa radhi kurejea Ujerumani kuvalia jezi za Bayern ambao kwa sasa wananolewa na kocha Flick Hansi.

Licha ya kutokuwa sehemu ya kikosi cha kwanza cha Man-City katika michuano muhimu, kocha Pep Guardiola amesisitiza kwamba Sane, 24, bado yupo katika mipango ya baadaye ya miamba hao wa soka ya Uingereza.

Ingawa amekiri kwamba Man-City watakuwa tayari kumtia Sane mnadani iwapo mnunuzi ‘mzuri zaidi’ atajitokeza, Guardiola ameshikilia kwamba Sh4.9 bilioni ambazo Bayern wametaka kuweka mezani kwa minajili ya kiungo huyo mvamizi ni “dharau” kubwa.

“Heri asalie nasi, mkataba wake utamatike na ateue pa kuelekea hata bila ya ada yoyote ya usajili. Itakuwa heri zaidi kushuhudia hilo kuliko kumpoteza Sane kwa fedha ambazo kimsingi, zinatosha kujinasia huduma za mwanasoka yeyote wa kawaida au hata wa kiwango cha chini zaidi. Mbona Bayern wanatudharau hivi?” akauliza Guardiola ambaye pia amewahi kudhibiti mikoba ya vikosi vya Barcelona (Uhispania) na Bayern.Kabla ya Sane kupata jeraha baya la goti ambalo limemweka nje kwa kipindi kirefu msimu huu, Man-City walikuwa radhi kumuuza kwa Sh14 bilioni huku Bayern wakijitokeza na Sh9 bilioni mwanzoni mwa muhula huu.

Kwa mujibu wa Guardiola, Sane alikuwa mhimili mkubwa katika mafanikio yao ya msimu wa 2017-18 katika EPL na bei yake kwa sasa, licha ya kusumbuliwa na jeraha, haistahili kushuka chini ya Sh10 bilioni.

Ilivyo, dalili zote zinaashiria kwamba Man-City hawapo tayari kumuuza Sane na watakuwa radhi kumdumisha ugani Etihad kwa msimu mwingine hata kama hatakuwa sehemu muhimu katika kampeni zao za muhula ujao wa 2020-21.

Hadi kusitishwa kwa shughuli zote za soka ya Uingereza kutokana na janga la corona mnamo Machi 2020, Sane hakuwa amewajibishwa katika mchuano wowote tangu apate jeraha katika gozi la Community Shield baina yao na Liverpool mnamo Agosti 2019.

Alirejelea mazoezi mepesi mwanzoni mwa Februari 2020 na mchuano wake wa kwanza ulitazamiwa kuwa dhidi ya Watford mnamo Mei 9 ugani Vicarage Road, Uingereza.

Manchester City juu ya EPL, Spurs na Blues wapaa

Na MASHIRIKA

MANCHESTER, Uingereza

WENYEJI Manchester City, Tottenham Hotspur na Chelsea walitumia ardhi yao vyema kutia kapuni alama tatu kwenye Ligi Kuu, Jumatano.

City ya kocha Pep Guardiola ililipua Cardiff 2-0 kupitia mabao ya wachezaji Kevin De Bruyne na Leroy Sane na kufungua mwanya wa alama moja juu ya jedwali dhidi ya wapinzani wao wa karibu Liverpool kwa kuzoa alama 80.

Guardiola ambaye timu yake itamenyana na Brighton katika nusu-fainali ya Kombe la FA hapo Jumamosi, alifanyia kikosi chake mabadiliko sita akipumzisha wachezaji muhimu akiwemo Sergio Aguero, ingawa alimtumia Gabriel Jesus.

Raia wa Brazil, Jesus alikosa nafasi kadha muhimu dhidi ya vijana wa Neil Warnock ambao wanakodolea macho kupoteza nafasi yao kwenye Ligi Kuu kwa sababu wako katika mduara hatari wa kutemwa.

De Bruyne alipachika bao lake la kwanza baada tu ya dakika tano akipokea pasi safi kutoka kwa Aymeric Laporte kabla ya Sane kuimarisha uongozi huo baada ya kumegewa krosi tamu na Riyad Mahrez zikisalia sekunde chache kipindi cha kwanza kitamatike.

Liverpool itakuwa uwanjani kuzichapa dhidi ya Southampton leo kwa hivyo uongozi wa ligi hii ya klabu 20 huenda ukabadilika vijana wa Jurgen Klopp wakishinda.

Spurs nambari tatu

Tottenham, ambayo Mkenya Victor Wanyama anachezea, ilimaliza ukame wa mechi tano bila ushindi kwa kupepeta Crystal Palace 2-0 kupitia mabao ya Son Heung-min na Christian Eriksen katika kipindi cha pili katika uwanja wao mpya wa Tottenham Hotspur.

Ushindi huu ulirejesha vijana wa Mauricio Pochettino katika nafasi ya tatu wakisukuma Arsenal nafasi moja chini hadi nambari nne.

Baada ya mechi, raia wa Argentina, Pochettino alidai kwamba klabu yake sasa ni “Washindi wa Kombe la Dunia” kwa sababu ya vifaa katika uwanja mpya na kutaka vijana wake waandikishe matokeo sawa na uwanja huo wa kisasa.

Naye Maurizio Sarri aliwasifu Callum Hudson-Odoi na Ruben Loftus-Cheek kama nyota wa siku zijazo wa Chelsea baada ya chipukizi hawa kuisaidia kulemea Brighton 3-0 uwanjani Stamford Bridge na kurukia nafasi ya tano iliyoshikiliwa na Manchester United.

Hudson-Odoi alimega pasi iliyofungwa na Olivier Giroud dakika ya 38 naye Loftus-Cheek akampa Eden Hazard pasi nzuri iliyozalisha bao la pili dakika ya 60. Loftus-Cheek alifungia Chelsea bao la tatu.