Wamuua kaka yao wakipigania mahari ya dada

Na Titus Ominde

FURAHA ya kupokea pesa za mahari katika familia moja katika kijiji cha Cheplachabei, Kaunti Ndogo ya Soy iliyo Kaunti ya Uasin Gishu, iligeuka kuwa karaha baada ya ndugu wawili kumuua kaka yao wakizozania mahari ya dada yao.

Polisi walifanikiwa kukamata wawili hao na kuwazuilia katika kituo cha polisi cha Soy.

Wawili hao Jacob Kipkosgei, 27, na Daniel Kipchirchir, 44, wanadaiwa kumuua Darius Kiplimo. Inadaiwa mzozo uliibuka kuhusu jinsi wangegawana pesa ambazo kiasi chake hakijulikani ambazo baba yao alikuwa amepokea kama mahari kutoka kwa bintiye aliyeolewa hivi majuzi. Marehemu alivamiwa akakatwakatwa kwa panga na kisu.

Akithibitisha kisa hicho, kamanda wa polisi katika Kaunti ya Uasin Gishu, Bw Ayub Gitonga alisema polisi wanaendelea na uchunguzi kuhusiana na tukio hilo.

“Ni huzuni kwa mzee huyu kupoteza mtoto wake kutokana na mzozo wa mahari. Kwa sasa familia hii imepata pigo mara mbili ikiizangatiwa kuwa wawili hao wako katika na seli mwingine amefariki,” alisema Bw Gitonga.

 

Nilitoroka na mahari ya baba ili asioe mchumba wangu, kijana asimulia

Na STEPHEN ODUOR

MVULANA wa miaka 17 katika Kaunti ya Tana River, aliyetorosha mahari iliyokusudiwa kutumiwa na babake kuoa mke wa nne, amewaelezea wazee kwamba bi harusi mtarajiwa alikuwa mchumba wake, ndiposa akachukua hatua hiyo.

Mvulana huyo ambaye alirudi nyumbani Jumapili baada ya ushawishi kutoka kwa vijana waliotumwa kumtafuta kichakani alikotorosha ng’ombe waliokuwa watumiwe kulipia mahari, alisema alichukua hatua hiyo baada ya juhudi zake za kushawishi wazee kusimamisha babake asioe mchumba wake kugonga mwamba.

Kulingana na Mzee Hussein Barisa, ambaye aliongoza mchakato wa upatanishi, kijana huyo aliwaeleza kuwa bi harusi tayari ana mimba yake ya miezi mitatu.

“Msichana alikuwa aozwe kwa mzee huyo ili kuiepusha familia yake aibu baada ya wazazi kugundua alikuwa mjamzito nje ya ndoa na hakutaka kumtaja aliyehusika,” alisema Bw Barisa.

“Baada ya kijana kufichua kuhusu uhusiano wake na bi harusi, tulizungumza na babake na tukamwelezea kwamba kweli mwanamke huyo alikuwa na ujauzito wa mtoto wake na alishtuka sana,” alisema.

Kijana naye alisema waliamua kupata ujauzito na mchumbake kama njia ya kumshawishi babake akubali waoane, akidai babake alikuwa na tabia ya kukataa wachumba wake wote.

Sasa mzee huyo wa miaka 74 amekubali mapatano na mwanawe.

Katika mahojiano na Taifa Leo, mzee huyo alisema mtoto wake hakumuarifu kuhusu uhusiano wao na hata kuhusu ujauzito.

Alijitetea kuwa hamu yake ya kumuoa msichana huyo ilikuwa katika juhudi za kuondolea familia yake aibu, jambo alilosema linakubalika kitamaduni.

Baada ya kupatana, mzee huyo amemzawadia mwanawe mahari ya ng’ombe 17 aliotoroka nao awali, na ameahidi kumsaidia yeye na mchumba wake kuoana.

Wawili hao watashiriki katika sherehe ya uchumba kitamaduni mwezi ujao, sherehe itakayoongozwa na wazazi wa pande mbili, kabla ya harusi mwaka ujao.

Familia yateta chifu kuagiza warudishe mahari

Na MAUREEN ONGALA

FAMILIA katika kijiji cha Muhoni, eneobunge la Ganze imemkashifu chifu wa eneo hilo kwa kuwaagiza kurudisha mahari ya Sh34,000.Familia hiyo imedai chifu wa Ganze, Thaura Mweni alipanga njama na mume wa binti yao kuwahangaisha.

Mnamo Februari, Bi Sanita Kitsao ambaye ni mama wa watoto sita alirudi kwao akidai kupokea vitisho kutoka kwa mume wake.

Kulingana naye, mumewe alimlaumu kuwa mchawi na alipanga kumuua ndipo akaamua kurudi kwao na watoto wake wawili.

“Sitaki kurudi katika ndoa yangu kwa sababu mume wangu anadai nimeingizwa katika kikundi cha wachawi na baadhi ya jamaa zake kwa hivyo anataka kuniua. Pia sitarudisha mahari kwa sababu nimezaa watoto sita na mimi ndiye nimekuwa nikitafutia familia yangu riziki wakati huo wote,” akasema.

Kakake, Bw Lemmy Jefwa alisema chifu aliandaa mikutano mingi kujaribu kuwapatanisha lakini mwanamume akasisitiza arudishiwe pesa alizolipa kama mahari.

Mkutano wa mwisho ulifanywa Ijumaa iliyopita.Alisema waliripoti kuhusu vitisho vya maisha ya dadake kwa kituo cha polisi cha Ganze.

“Ni wazi kuwa chifu ana ubaguzi. Familia inachukulia suala hili kwa uzito. Hatutaki baadaye tuje kusikia dada yetu aliuliwa akimrudia mume wake,” akasema Bw Jefwa.

Hata hivyo, chifu alitetea msimamo wake na kusema ni utamaduni katika jamii za Mijikenda kwamba mahari inastahili kurudishwa wanandoa wakitengana.

Alisema uamuzi wake kuandaa vikao vingi kujaribu kupatanisha wanandoa hao ulikuwa kusudi ili mwanamke husika apate muda wa kuamua kama kweli anataka kuachana na mume wake au atamrudia.

“Mwanamke amekataa kurudi nyumbani kwake. Hatuwezi kuwalazimisha waishi pamoja na desturi ni kuwa anafaa kurudisha mahari ili mume wake aitumie kuoa mke mwingine akipenda, kwani bado angali ni kijana,” akasema Bw Mweni.

Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Kilifi, Bw James Mugera alisema polisi wanachunguza suala hilo.

Kulingana na Bi Jefwa, mumewe amekuwa akimpiga sana katika ndoa na wakati wote visa hivyo vilikuwa vikitatuliwa kwa mashauriano ya wazazi wake ambao walikuwa wakiwapatanisha.

MILA NA DESTURI: Utoaji mahari na ndoa katika jamii ya Wasomali

Na FARHIYA HUSSEIN

farhiyahusseiny@gmail.com

ILIKUWA fahari kubwa Taifa Leo kupata kupata fursa ya kujumuika na jamii ya Wasomali eneo la Kaskazini Mashariki, Kaunti ya Garissa kushuhudia jinsi harusi zao za kitamaduni zinavyofanywa.

Makaribisho ni mazuri katika uwanja mmojawapo. Shangwe na vigelegele vinahanikiza huku sauti nyororo za kina mama wakiimba nyimbo za kitamaduni zikizidi kunogesha uhondo.

Tunapatana na Bw Deqow Ali na mke wake Bi Barwaqa Adow ambaye anamtayarisha binti yao atakayefunga ndoa siku chache zijazo.

Binti yao karibu ataolewa katika harusi ya kitamaduni.

Bi Adow anasema harusi ni mojawapo ya tamaduni muhimu zaidi kwa jamii ya Wasomali.

“Harusi kwetu huashiria umoja pale nyoyo za wawili wapendanao zinakuja pamoja kutengeneza uhusiano baina ya familia hizo mbili,” anasema Bi Adow.

Bi Barwaqa Adow akitayarisha chakula nje ya nyumba yake ya kitamaduni. Picha/ Farhiya Hussein

Wasomali wanafahamika kwamba wao ni wa Kishiti (cushites) na wanapatikana zaidi Kaskazini Mashariki mwa Kenya.

Asili yao inaelezwa kwamba ni wa kutoka mkoa wa Ogaden, Kusini mwa Ethiopia.

Wasomali zaidi ya 500,000 wanaishi Kaskazini Mashariki, Kenya.

Familia nyingi za Kisomali zinazopatikana nchini Kenya ni zile za Ajuran na Ogaden na lugha yao ni ya Kisomali.

Ingawa hivyo, kunao wengine ambao pia wanazungumza lugha ya Kisomali na wanaitwa Garreh lakini si Wasomali kamili kwa sababu wamechanganya damu ya Borana.

Wasomali hujulikana kuwa ni wafugaji hasa wa ngamia, mbuzi, kondoo, na ng’ombe.

Wakigawanywa katika makundi tofauti ya kikoo – clans – wanapatikana Hawiye, Degoodiya, Ajuuraan, Isxaaq na Ogaadeen .

Wengi wao hupatikana sana jijini Nairobi, Mombasa na sehemu za Kaskazini Mashariki mwa Kenya.

Bw Ali anaelezea kuwa kuna methali katika lugha ya Kisomali inayosema “bahati ni wakati fursa inakutana na maandalizi” na ndivyo huwa wanaashiria wanaoelekea kufunga ndoa.

Bibi arusi kutoka jamii ya Wasomali akivishwa kitambaa na wanawake wa jamii kama njia ya kumpokeza baraka kwenye maisha yake ya ndoa. Picha/ Farhiya Hussein

Anafafanua kwamba katika jamii ya Wasomali, utoaji wa mahari – Meher – hufanyika siku chache kabla ya harusi na wakati mwingine hufanyika siku hiyo ya ndoa.

Ukweli ni kwamba ni jambo linalohitaji mtu kujikusuru na kujitolea kikamilifu. Si rahisi kwa upande wa bwana harusi kwani anapaswa kushughulikia familia ya bi harusi na na kuitunuka zawadi.

Bw Ali (babake biarusi) na ndugu zake walipokea kutoka kwa familia ya bwana harusi zawadi ikiwa ni pamoja na mtoto wa ngamia, hela zilizofunikwa kwa kitambaa ghali na ngamia 20 kama malipo ya mahari.

“Kuna zawadi nne kubwa ambazo bwana harusi anapaswa kutoa. Ya kwanza tunaita, Gabaati ambayo inahusisha nirigi – mtoto wa ngamia – na kawaida huletwa na bwana harusi na baba yake wanapokuja kuomba bi harusi. Ya pili ni Yarad ambayo ni zawadi inatolewa siku ya utoaji mahari ya kuthamini biarusi (Kawaida ni pamoja na pesa zilizofunikwa kwa kitambaa ghali). Tatu, Sooryo; pesa wanazopewa wanaume wa familia ya biarusi ama ndugu au binamu. Na mwishowe, bwana arusi huleta ngamia kama shukrani kwa kuruhusiwa kumuoa yule biarusi,” akaelezea Bw Ali.

Lakini alieleza kadri siku zinavyosonga utamaduni unapotea polepole.

Zama zile, biarusi angetolewa ngamia 100 kama mahari lakini sasa bwana harusi anaruhusiwa kulipa ngamia 10 kama mahari.

Wasomali wana historia pevu ya ufugaji wa ngamia. Picha/ Farhiya Hussein

“Bila malipo ya mahari hakuna arusi ambayo itafanyika na ina maana kwamba biarusi anapaswa kuwa wazi juu ya kile anataka na bila shaka bwana arusi atawajibika na kukitoa,” akasema Omar Abdullahi, mmoja wa wazee wa baraza katika kijiji hicho.

Harusi za Wasomali, nyingi hufanywa kabla ya jua kutua na hufanyika maeneo ambayo kila mtu ambaye huwa amealikwa kwa tarehe iliyowekwa anaweza kufika.

Taifa Leo ilipata fursa ya kushuhudia ndoa ya bintiye Bw Ali.

Wanawake walijitokeza wakiwa wamevalia mavazi yao ya rangi ijulikanayo kama baati. Ni kubwa, na hung’aa (glitters) na hutengenezwa kwa hariri. Nguo hizo ni kubwa kiasi kwamba wanawake hushikilia upande mmoja wakati wa kucheza na kuimba.

Wanawake basi wanamsindikiza biarusi kuelekea kwenye chumba ambacho kimejengwa maalum kwa wanandoa hao wapya huku wakipiga makofi na kucheza wakati wanapiga ngoma.

Bwana arusi anaonekana amesimama kwa umbali nje ya chumba hicho.

Kisha kundi la wanaume linakuja polepole huku wakiimba nyimbo za sifa na kucheza wakielekea kwenye hicho chumba, ambapo bibi arusi yuko.

Ndani ya kile chumba kumetandikwa shuka ndefu chini. Bi arusi amekalishwa katikati huku wanawake wakimzunguka na kuimba.

Wanawake wengine hukusanyika nje ya chumba, wakiacha nafasi ya kutosha kwa wanaume wanaokaribia.

Wanaume kisha hufika pale, wakiongozwa na wazee wa kijiji wanamzunguka bwana arusi kama kundi la nyuki.

Ndani ya chumba hicho, wanandoa hao wapya wanapitia mila kadhaa ikiwa ni pamoja na Todoba Bax, Xeedho, Shaash saar.

Kutumia kitambaa kipepesi wanawake huweka kitambaa juu ya kichwa cha biarusi ambacho huashiria baraka na kumtakia heri katika ndoa yake.

“Hii inategemea na ukoo na mbari ambapo bwana arusi na biarusi hutoka. Wengine huoana kutoka katika familia moja. Kulingana na ukoo, wale wanaofunga ndoa wanaweza kuhusishwa kupitia wazazi wao. Kwa mfano, mama ya bwana arusi na baba ya biarusi wanaweza kuwa wa kutoka kwa tumbo moja,” akabainisha Bw Ali.

Katika jamii zingine nchini, hii inaweza kuonekana kama mwiko yaani taboo.

Utamaduni wa Kisomali pia unaruhusu mwanamume kuoa hadi wake wanne; hasa chini ya sheria za Kiislamu.

Alazimika kutoa punda kama mahari

Na John Musyoki

SIAKAGO, Embu

JAMAA mmoja alilazimika kuwapa wakwe zake punda wawili ili kupunguza deni la kulipa mahari.

Inasemekana wazazi wa demu walikita kambi kwa polo wakidai walipwe mali iliyobakia.

Kulingana na mdokezi wetu, mwanamume huyo alikuwa akiahidi kulipa mahari lakini hakuwa akifanikiwa kupata pesa.

Majuzi, wazazi wa mkewe waliamua kwenda kupiga kambi kwake wakilalamika kwamba ameishi na binti yao kwa muda mrefu bila kuwapa chochote.

“Wewe, umepuuza kulipa mahari kwa muda mrefu. Umemtunga binti yangu mimba ya tatu na hujawahi kutulipa mahari licha ya ahadi nyingi.

“Hatuondoki hapa bila mahari na kama tutaondoka, hatutamuacha binti yetu,” mzee alimwambia jamaa kwa ukali.

Mjomba wa binti aliendelea kuwasha moto. “Msichana wetu alipotoka nyumbani hakuwa na mtoto. Sasa anajiandaa kupata wa tatu na haushughuliki kulipa mahari. Tutakuachia watoto wako uendelee kulea, sisi twende na binti yetu!” alifoka.

Jamaa alijaribu kuwaomba wakwe zake wampe muda zaidi ili atafute pesa, lakini walikataa katakata.

“Tupe chochote ulichonacho ama turudi na binti yetu,” baba ya demu alisisitiza.

Ilibidi kalameni awape wakwe punda wake wawili aliokuwa akiwategemea kubeba mizig nyumbani.

Inasemekana baada ya wageni hao kupewa punda walikubali shingo upande huku wakitisha kurejea tena kwa kalameni hivi karibuni, iwapo hataonyesha dalili za kumaliza kulipa mahari hiyo katika kipindi walichokubaliana.

Majirani walisema mwanamume huyo alikuwa akimpenda mkewe sana na vitisho vya wakwe havikumfurahisha kabisa, kwa sababu hakuwa na nia ya kutowalipa mahari.

 

Gavana ataka mahari sawa kwa mabinti waliosoma na wasiosoma

Na ALEX NJERU

GAVANA wa Tharaka-Nithi Muthomi Njuki amependekeza kwamba Baraza la Wazee wa Njuri Ncheke lipitishe uamuzi utakaofanya wasichana waliosoma na wasio na kisomo kulipiwa kiasi sawa cha mahari wanapoolewa.

Hii ni baada ya malalamishi kuzuka kwamba baadhi ya familia huomba kulipwa mahari ya juu, zikidai kwamba zilitumia fedha nyingi kuwaelimisha binti zao waliofuzu na shahada mbalimbali kutoka vyuo vikuu au vyuo anuwai.

Hali hii imechangia vijana wengi kushindwa kuoa na akasisitiza kuwa mila na tamaduni za jamii ya Ameru zinatoa mwongozo bora wa mahari ambayo familia ya mwanaume anayetaka kuoa inafaa kulipa.

“Bila kuzingatia kama wameelimika au la, mahari kwa wasichana wote inafaa kuwa sawa,” akasema Bw Njuki hapo jana mjini Chuka.

Kiongozi huyo alidai kwamba kulingana na desturi ya jamii ya Ameru, familia ya mwanaume huhitajika kulipa mahari kwa kutoa mifugo, pombe ya kitamaduni na asali kama njia ya shukrani kwa familia ya msichana badala ya maelfu ya fedha yanayoitishwa na wazazi wa kizazi cha sasa.

Alidai baadhi ya wazazi sasa wamegeuza ulipaji mahari kama kitega uchumi huku wakikosa kutilia manani iwapo mwanaume anayeoa mwanao amesoma au hakusoma.

“Kama wazazi tunafaa tukome kufanya biashara na wasichana wetu. Tunafaa kuwaombea na kuwabariki wanapoanzisha familia zao,” akaongeza mbunge huyo wa zamani wa Chuka Igambang’ombe.

Mnamo Oktoba mwaka huu, wazee wa Njuri Ncheke wakiongozwa na Katibu Mkuu wa baraza hilo, Bw Josphat Murangiri, walikutana na Gavana wa Meru, Bw Kiraitu Murungi kisha wakakubaliana kutunga sheria ambazo zitasawazisha mahari kwa wasichana wa kaunti za Tharaka-Nithi na Meru.

Wazee hao pia walitambua kwamba wazazi wamekuwa wakitaka mahari ya juu kabla ya mabinti zao kuolewa, hali ambayo imewazuia vijana wengi wa kiume kuingia kwenye asasi ya ndoa na kuanzisha familia zao.

Wakati wa mkutano huo, Bw Murungi aliwatahadharisha wazazi dhidi ya kuitisha mahari ya juu na kuvuruga maisha ya baadaye ya watoto wao wa kike.

Kamwe hatuwezi kutoza ushuru kwa mahari – KRA

Na MARY WANGARI

MAMKALA ya Kukusanya Ushuru (KRA)  imelazimika kukanusha madai kwamba ilikuwa na mipango ya kuanza kutoza ushuru kwa wanaopokea mahari.

Mamlaka hiyo iliandika katika mtandao wa Twitter ikijitetea dhidi ya madai hayo, ambayo tayari yalikuwa yamepingwa vikali na Wakenya.

“Hii stori hata sisi tumeisikia,” KRA ilichapisha katika ukurasa wake huku ikitaja ripoti hizo kama habari feki.

Awali, ripoti zilienezwa mitandaoni kuwa KRA ilikuwa imeafikia uamuzi wa kutoza ushuru wa mahari baada ya kushindwa kutimiza kiwango cha ushuru ilichohitajika kukusanya.

“Uzuri mumefafanua. Nilikuwa nishaanza kujipanga tulete mbuzi katika ofisi zenu,” aliandika Gakunga.

“Niliona habari hizi mapema asubuhi. Ahsante kwa kufafanua kuwa ni feki. Nilikuwa ninashangaa tu ikiwa ingetekelezwa basi kila bwana harusi moja kwa moja angekuwa ajenti wa kukusanya ushuru. Nikilipa mbuzi 10 naleta mmoja Times Tower,” Stano Mwasi akasema.

Baadhi ya Wakenya walifahamisha mamlaka hiyo kwamba vijana tayari wamelemewa na maisha, na hivyo hawakuhitaji mzigo mwingine wa ushuru.

“Msijaribu kutupima! Waambieni viongozi wenu kuwa Wakenya ni takriban milioni 47 na nyinyi hamfiki watu 1,000. Wasitubebe ujinga! Vijana wanashindwa kuoa kutokana na hali ngumu ya maisha halafu mnataka kuleta ushuru mwingine. Tunawaona!” akasema Maryam Omar.

Hata hivyo kuna wengine waliosisitiza kwamba KRA ilikuwa kweli imetoa tangazo hilo, lakini ikabadili nia haraka baada ya kuona hisia za Wakenya.

“Semeni tu mmeogopa. Mlijaribu kuweka miguu majini mkaona ni baridi sana,” alisema Omar Bamzer.

Kwa uhalisia, inaweza kuwa vigumu kwa KRA kutoza ushuru wa mahari, ikizingatiwa kuwa wanaooana hawana mitambo ya kielektroniki (ETR), ambayo hutumika kuweka ithibati ya malipo.

Warudi na mahari kwa kukosa ugali

Na TOBBIE WEKESA

KOYONZO, VIHIGA

KIOJA kilizuka kijijini hapa baada ya wazee kuamua kurudi nyumbani na mahari waliyokuwa wameleta, wakidai hawakupokelewa vizuri na wakwe zao.

Inasemekana wazee hao hawakufurahishwa na namna familia ya msichana iliandaa hafla hiyo maalum. Kulingana nao, hawakupewa mapokezi yaliyostahili ujumbe wao.

Duru zilizotufikia zinadai kuwa, wazee wa upande wa msichana hawakuwepo kuwapokea wazee wenzao walipowasili.

Wageni hao wakaamua kusubiri wakati mwafaka kulalamika. Baada ya muda mfupi, vyakula viliandaliwa kabla ya majadiliano na hapo ndipo kitumbua kiliingia mchanga.

Wazee walianza kunong’onezana kwa sauti ya chini. Vijana walioandamana nao pia walianza kuangaliana.“Mlo ni huu pekee ama kuna mwingine!” mzee mmoja akainuka.

Wenyeji walijaribu kubembeleza wageni waanze kula, lakini hakuna aliyesongeza karibu sahani yake. “Hawa vijana wametembea mwendo mrefu sana.

Wanataka kujua iwapo kuna ugali mwingine ama ni huu peke yake,” mzee huyo akasisitiza. Wenyeji walibaki vinywa wazi.

“Kidesturi, sisi hula ugali sampuli tatu katika hafla za kitamaduni kama hizi. Ugali wa mahindi, wa mhogo na wa wimbi. Nyama nayo lazima iwe kwa wingi,” mkongwe huyo aliendelea kunena huku vijana wakimpongeza.

Wenyeji walijitetea kuwa hawajui mila hiyo, na kwamba wageni wanafaa kula chochote walichoandaliwa.

“Hatuwezi kuwaletea ng’ombe na mbuzi hao wote halafu nyinyi mnatuandalia mlo ambao hatuwezi kushiba,” mzee mwingine akawafokea wakwe hao.

Wazee waliamka kwa pamoja na kuelekea walikokuwa mifugo wao. “Hii bado ni mali yetu na tunarudi nayo nyumbani. Tutakula huko!” wazee waliapa.

Walianza safari kurudi nyumbani. Familia ya msichana ilijaribu kuwashawishi waketi chini lakini wapi.

“Kuleni mlo wenu. Sisi si watoto wa kuletewa wali kwa supu. Mkiwa tayari kutupokea mtuarifu,” wazee walifoka huku wakienda zao.

Wazee sasa kuweka viwango vya mahari

Na CHARLES WANYORO

BARAZA la Wazee wa Jamii ya Ameru la Njuri Ncheke limetangaza mipango ya kusawazisha mahari yanayotolewa kwa familia za wanawake katika jamii yao ili kuhimiza vijana kuoa.

Katibu Mkuu wa baraza hilo, Bw Josephat Murangiri alisema wanandoa wengi hawafurahii ndoa zao kwa sababu ya mahitaji ya mahari.

Akizungumza katika makao makuu ya Kaunti ya Meru wakati wa kutia sahihi makubaliano ya pamoja kati ya kaunti na idara ya kitaifa ya kusimamia makavazi kuhusu ujenzi wa makavazi itakayogharimu Sh50 milioni, Bw Murungari alisema wazee watakutana hivi karibuni kujadili suala hilo.

Alisema wamegundua kwamba ugomvi wa kinyumbani husababishwa zaidi na jinsi wanandoa hawana furaha baada ya kushindwa kuoa wapenzi wao wa zamani kwa vile hawakuweza kuwalipia mahari.

“Ndoa si biashara kwamba aliye na uwezo wa kifedha ndiye anayemchukua binti, hata kama hawajapendana. Enzi za mababu zetu ambapo watu walifungishwa ndoa kisha wakapendana wakiwa wanaishi pamoja zimepitwa na wakati. Kuna haja ya kuweka mazingira ambapo mvulana na msichana wakipendana, watakuwa na uwezo wa kuoana,” akasema.

Bw Murangiri alisema baraza hilo linaunga mkono pendekezo la Gavana Kiraitu Murungi kusawazisha kiwango cha mahari kinachostahili kutolewa. Gavana huyo alikuwa ameeleza masikitiko yake kuhusu jinsi kuna watu wanaoitisha hata Sh1 milioni kutoka kwa vijana wanaotaka kuoa binti zao.

“Mababu wetu walikuwa na nia ya kuona kuwa kila mtu anaishi maisha ya furaha. Ugomvi mwingi wa kinyumbani hutokea kwa vile watu wengi wameoana ilhali si wapenzi. Tutakutana ili kuweka kiwango kimoja cha mahari lakini kama mtu atataka kulipa zaidi, basi yuko huru,” akasema Bw Murangiri.

Makavazi

Kikao hicho kilihudhuriwa pia na mkurugenzi wa idara ya kitaifa ya makavazi, Dkt Mzalendo Kibunjia.

Katika jamii nyingi za Kibantu, mahari kitamaduni huhusisha mbuzi, kondoo au kuku pamoja na pombe. Wazee hupokea kibuyu cha pombe na mama hupewa kikoi au nguo kuashiria nguo aliyotumia kubeba binti. Kisha watu hupika chakula na kula pamoja, ishara ya kuunganisha familia mbili.

Lakini kuingia kwa utamaduni wa Magharibi kumegeuza mambo, ambapo sasa mahari hutozwa kutegemea gharama ya wazazi kumlea binti, ikijumuisha hadi karo ya hadi Chuo Kikuu.

Demu pabaya kujilipia mahari

Na Leah Makena

MAGOGONI, THIKA

Kidosho wa hapa alikaripiwa na wazee kwa kuchukua mkopo kusaidia mumewe kulipa mahari.

Duru zasema kuwa kidosho na mpenzi wake walifika kwa wazee kuomba baraka zao ili waanze maisha kama mume na mke baada ya kuhitimu chuoni.

Kidosho alifanikiwa kupata ajira punde tu baada ya kukamilisha masomo, jambo lililomfanya babake kuwaita wazee wapinge pendekezo la binti kuolewa na jamaa ambaye hakuwa na kazi.

Mzee alisema alitaka kujengewa nyumba ya kifahari na binti yake.

Hata hivyo, hawakufanikiwa kushawishi bintiye kwani alikuwa ameamua kuolewa na jamaa huyo licha ya kuwa hakuwa amefanikiwa maishani.

Kama adhabu, wazee walimtoza jamaa maelfu ya pesa kama mahari licha ya kufahamu hakuwa amefanikiwa kupata ajira. Isitoshe, walimpa kipindi cha miezi michache kulipa mahari yote na kutishia kutwaa binti yao iwapo angeshindwa kutimiza matakwa yao.

Baada ya kuwaza na kuwazua, kidosho aliamua kuchukua loni ili asaidie jamaa kulipa mahari kwa hofu ya ndoa yao kusambaratika.

Siku ya sherehe, wapenzi walifanya ‘shopping’ na kisha wakawakabidhi wazee hela walizodai jambo lililowashtua na kutaka kujua iwapo jamaa alikuwa amefanikiwa kupata kazi.

Hawakuamini walipogundua mali yote waliyopata ilikuwa bidii ya binti yao. Hapo ndipo walipomuita kando na kumzomea kwa kudekeza jamaa.

“Unawezaje kukopa loni kulipa mahari kana kwamba umekuwa mume? Si ungemuacha apambane na hali yake? Utajengea wazazi wako nyumba ya kifahari au utaendelea kulea mume? Tahadhari kwani hili dume litageuka kupe likufyonze hadi kaburini”, wazee walionya.

Waliohudhuria kikao hicho wanasema kuwa kidosho alitia masikio nta na kuendelea na maisha yake.

Gharama ya juu ya mahari inavyozimia vijana ndoto ya ndoa

Na MWANGI MUIRURI

IKIWA kuna safu moja ya kimaisha ambayo inawalemea kuwapa imani na ndoa vijana wengi katika jamii, ni mahari.

Aliyekuwa mkuu wa kanisa katoliki katika Kaunti ya Nyeri, Askofu mstaafu Peter Kairo anasema kuwa “mahari imegeuzwa kuwa biashara ya kutajirisha wakwe kiasi kwamba vijana wengi hawana imani na ndoa.”

Anasema kuwa mahari iliwekwa katika tamaduni kama shukran kwa wazazi wa msichana anayepozwa, “lakini leo hii ni biashara ambayo hata inaweza ikasajiliwa katika soko la hisa.”

Anasema kuwa kunafaa kuwekwa mikakati ya kuwapa vijana hasa walio na pesa kidogo maishani kujiamini kwa kuwapa matumaini kuwa kesho yao wanaweza wakapata pesa za kulipa mahari.

“Lakini leo hii unapata kijana amesononeka kwa kuwa gharama za ndoa zimeenda juu lakini sio kwa kiwango kile cha kawaida bali ni kwa kusukumwa na wanaooza mabinti zao,” asema.

Mshirikishi wa Shirika la Wanawake waelimishaji Barani Afrika, Cecilia Wanjiku anasema kuwa katika jamii ya Agikuyu, vijana wengi hawaoi kwa kuwa gharama ya ndoa imetinga zaidi ya Sh moja Milioni.

“Ukienda kuomba harusi, utahesabiwa gharama nyingi na mashemeji hao watarajiwa. Ukishapita kigezo hicho, gharama za harusi ya hadhara zinakungoja, hali ambayo imewaelekeza hata wengi wa vijana kutekeleza ndoa zao kwa njia za kujificha,” asema.

Anasema kuwa ukifika ni wakati wa kuhesabiwa gharama za mahari, unapata kuwa kijana masikini amehesabiwa gharama ya msichana huyo kana kwamba ni dhahabu sokoni.

“Ndio sababu wengi wa vijana siku hizi wanatoroshana na wasichana na kuanza ndoa zao bila hata kuwafahamisha wazazi kwa kuhofia gharama,” ateta.

Anasema kuwa mahari ya Agikuyu kwa mfano huwa ni pamoja na pesa taslimu zisizopungua Sh100, 000 za kuwaandalia karamu marafiki wa kijiji cha msichana huyo, zawadi za Sh100, 000 kwa wakwe na pia pesazingine kiwango cha maelfu za kupishwa nyumbani kwa wakwe hao.

Hafla ya sherehe za ulipaji mahari katika kijiji hiki cha Kagwathi katika Kaunti ndogo ya Kigumo. Picha/ Mwangi Muiruri

“Shida kubwa sasa hutokea katika gharama ya msichana ambayo husemwa ni mbuzi 100 na ambao kulingana na hadhi ya familia, mbuzi mmoja huwekewa thamani ya kati ya Sh5, 000 na Sh15, 000. Hii ina maana kuwa bei ya msichana huyo ni kati ya Sh500, 0000 na Sh1.5 Milioni bila kujumlisha zile gharama za mwanzo,” asema Bi Wanjiku.

Anasema kuwa ndiyo sababu vijana wengi katika jamii wamezama katika ulevi kwa kuwa “ukioleka kwa ulevi, gharama ni chache na kuna kule kuzimia kwa mawazo na unajipa imani ghushi ya kimaisha.”

Na huku pombe haramu ikilaumiwa kwa kudhoofisha nguvu za kiume sasa Bi Wanjiku anasema kuwa Fawe imezindua harakati za kuwatuza wanaume ambao watakoma tembo, kuoa na kisha kupachika wake zao mimba.

Mashujaa hao watatunukiwa vifaa vya nyumba na pia kupimwa suti huku pia wakipewa kitita cha pesa cha kugharamia manguo ya mtoto atakayezaliwa.

Anasema kuwa Fawe inalenga kuwapa vijana motisha ya kuoa na ambapo itawapa uhamasisho kuhusu njia zingine nyingi za kuzindua familia zao bila kujipa stresi za kuhesabiwa gharama za juu.

“Kuna harusi za afisi za kisheria na pia kwa makamishna wa Kaunti. Kuna ndoa za kienyeji na pia kuna ndoa zile za kuishi pamoja bila kujificha mkingoja mkusanye mali ya kupeleka kwa wakwe….Sio lazima tufuate ule utaratibu wa kuhesabiwa gharama hata kabla ya kujaribu kama mnaweza mkawiana katika ndoa,” asema.

Bi Wanjiku anasema kuwa mpango huo utawalenga wanaume ambao wamefikisha umri wa miaka 30 na ambao hawajawahi kuoa na ni walevi.

“Hii ni kwa sababu mpango huu unaweza tumiwa vibaya na wanaume ambao tayari wameoa kwa kuwapachika mimba mabibi zao kiholela ili watuzwe,” akasema Bi Wanjiku.

Mpango huu umewadia wakati makasisi wengi makanisani wamekuwa wakilalamika kuwa wafuasi wao wamekoma kuleta watoto wapya duniani kinyume na sheria za Mungu kuwa tujaze ulimwengu.

Mwenyekiti wa Kanisa la Presybeterian la Mbogo-ini Bw Titus Njuguna aliteta katika ibada kuwa “Vijana kutooa na walio oa kukosa kuzaa kumezua wasiwasi mkubwa katika maeneo mengi ya Mkoa huu. Nataka kuwashukuru wale ambao wameshikilia hadhi ya eneo letu kwa kuendelea kujizatiti na kutomboa kutuzalia watoto wengine ingawa idadi yao ni chache sana.”

Hali hii inahusishwa na gharama za juu katika ndoa na ambazo huchochewa na mtazamo wa kibiashara katika kuwaoza mabinti katika  jamii.

Wakataa kutoa mahari hadi binti aolewe na kuzaa

SABATIA, VIHIGA

Kizaazaa kilizuka eneo hili baada ya mashemeji watarajiwa kuwatawanya wazee waliokuwa wakijadili harusi ya kijana wao kwa kudinda kutoa mahari hadi binti aolewe na kuzaa.

Inadaiwa kwamba makalameni waliamua kuwatawanya wazee hao wakiwalaumu kwa kutumia maneno yaliyowakosea heshima pamoja na dada yao kwa kudai lazima awathibitishie ana uwezo wa kuzaa.

Inasemekana bw harusi alikuwa ameitisha kikao na wazee wa familia nyumbani kwake ili kujadili mambo muhimu. Kikaoni, walikuwa mashemeji watarajiwa wa bi harusi ambao walikuwa wamealikwa.

Kulingana na mdokezi, wazee walipokuwa wakitoa hoja zao, mzee mmoja alisimama na kupinga kutolewa kwa mahari yote hadi mrembo atakapoolewa na hata kuwazalia watoto wawili.

“Hatuwezi kutoa mahari yote kwa sasa. Msichana lazima aolewe mwanzo na pia tuhakikishe kuwa ana uwezo wa kutupa wajukuu ndiposa tukamilishe mahari,” mzee mmoja alisema.

Duru zinasema makalameni waliinuka kwa pamoja na kumuonya mzee yule. “Una ushamba sana wewe. Hauwezi kusema hivyo tukiwa hapa. Tuheshimu pamoja na dada yetu,” kalameni mmoja aliteta.

Inadaiwa kwamba mzee mwingine alisimama na kumuunga mkono mzee mwenzake.

“Sisi wazee tunazungumza kwa busara. Kile ambacho kimesemwa hapa ni ukweli usiopingika kabisa,” alieleza.

Habari zilizotufikia zinasema makalameni walielekea walikokuwa wameketi wazee wale na kuwaamrisha waondoke mara moja.

“Kile mmesema hapa hakina busara wala mashiko yoyote. Vichwa vyenu vimejaa upepo. Ondokeni hapa,” makalameni waliwafokea wazee.

Duru zinasema wazee walisita kutii amri. “Hamkutuita hapa kuja kusikia haya. Leo mtatujua,” mapolo walionya.

Inadaiwa wazee walipoona mapolo wakichomoa viboko, wote walilazimika kukimbilia usalama wao.

Amuua baba yake kwa kumnyima kondoo wa kulipa mahari

 TITUS OMINDE na STEPHEN MUNYIRI

POLISI wa eneo la Eldoret Mashariki wamemkamata mwanaume mwenye umri wa miaka 28 ambaye anashukiwa kumuua babake alipokataa kumpa kondoo wa familia ili alipe mahari kukomboa mtoto wake wa kiume aliyepata nje ya ndoa.

Polisi walisema kuwa Andrew Kimutai alimvamia baba yake akiwa chumbani mwendo wa saa moja Jumapili usiku ambapo alimkata kichwa kwa kutumia shoka.

Marehemu Joseph Marindany alifariki kutokana na majeraha kichwani alipokuwa akikimbizwa hospitalini.

Kisa hicho kilitokea wakati Kimutai alipotaka babake amruhusu auze kondoo wa familia ili alipe mahari aweze kuruhusiwa kupewa mtoto wake aliyepata nje ya ndoa na mwanamke anayeishi mjini Nakuru.

Marehemu ambaye hakujua mwanawe ana mtoto nje ya ndoa, alikataa kumpa kondoo. Mshukiwa alikasirika kabla ya kumvamia kwa shoka chumbani usiku.

Akithibitisha kisa hicho, OCPD wa Eldoret Mashariki Bw Richard Omanga alisema mshukiwa amekamatwa.

“Marehemu alikataa kumpa mwanawe kondoo kwa sababu hakujua alikuwa amezaa mtoto nje ya ndoa kama alivyodai. Mshukiwa alikasirishwa na msimamo wa babake ndiposa akamkatakata kwa shoka,” alisema OCPD Omanga.

Mshukiwa kwa sasa anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Naiberi akisubiri kufunguliwa mashtaka baada ya uchunguzi kukamlika.

Katika mahakama ya Karatina, Kaunti ya Nyeri, mwanamume alieleza alivyopigwa na wanaume wawili kwa kukosa kulipa deni la Sh10. Bw Benson Kiprono Rotich, mfanyakazi wa shambani katika kijiji cha Itundu, Mathira Mashariki, alishangaza mahakama alipodai kwamba wanaume hao walimpiga kwa sababu hakuwa wa kabila lao.

Bw Rotich alimweleza Hakimu Elvis Michieka kuwa alienda katika hoteli mnamo Aprili 27 mwaka huu na kuagiza samosa mbili kwa bei ya Sh20 kila moja lakini baadaye aligundua hakuwa na pesa za kutosha na akamuomba mwenye hoteli amruhusu ampelekee siku iliyofuata.

Hata hivyo, alisema mwenye hoteli alikataa kumsikiliza na akamuita mfanyakazi wake na wote wawili wakaanza kumpiga kwa kipande cha mti kichwani kabla ya kuokolewa na wasamaria wema.? “Mheshimiwa, nimewafahamu vyema wawili hawa kwa muda kwa sababu ninafanya kazi karibu, mmoja alizoea kuniita mtu wa kabila tofauti lakini sikudhani ingekuwa mbaya hadi waliponishambulia.”

wakiniambia sitoki kabila lao kwa sababu ya Sh10,” alisema. Alikuwa akitoa ushahidi katika kesi ambayo Chem Kaburia na Peter Murimi wamekanusha kumpiga na kumjeruhi.

Polo atimuliwa na mahari yake ya kuku

Na LEAH MAKENA

Irunduni, Tharaka

POLO wa hapa nusura achapwe na mashemeji alipowapelekea kuku wawili kama mahari siku chache baada ya kuhepa na dada yao.

Yasemekana jamaa alikuwa akimchumbia mwanadada huyo kwa muda licha ya pingamizi kutoka kwa ndugu zake.

Kulingana na mdokezi, ndugu za mwanadada huyo walikuwa wameshindwa kumshawishi dada yao kumtema polo wakidai kwamba alikuwa mlala hoi.

“Mwanadada alitia masikio nta na kuhamia kwa polo licha ya kukatazwa na ndugu zake. Juhudi za kuwasiliana naye ziligonga mwamba alipozima simu,” alisema mdokezi.

Wiki moja baada ya kuona kuwa amefaulu kukaa na mrembo, ndipo polo alifika nyumbani na alipopata wazazi, akawa na muda wa kujitetea na kueleza sababu ya kuhepa na binti yao.

“Naomba mniwie radhi kwa sababu sikuwa na uwezo wa kuandaa karamu kubwa wala kufanya harusi. Ninaahidi kutia bidii angaa nipate cha kuwatunuku huku nikihakikisha kuwa binti yenu anakula na kuvaa vizuri,” polo alijitetea huku akiwataka wazazi kupokea kuku aliokuwa amebeba.

Duru zasema kuwa mashemeji walivutiwa waya na wakalazika kuacha vinywaji klabuni kwenda kumkabili polo.

Mkutano wa jamaa na wakwe ulikatizwa na mashemeji walipofika kwa fujo na kujaribu kumtia polo viganjani ila wakashindwa alitimua mbio na kutokomea.

“Unadhani unayedai kuwa mkeo ameokotwa ndipo ulete mahari ya kuku?Umetupa mbao kutonesha kidonda kwani tunakuhakikishia kuwa hutaishi naye kabisa,” ndugu wa mwanadada waliteta.

Habari zasema kuwa mashemeji walibeba kuku hao tayari kuwarudisha kwa polo huku wakiapa kumtwaa dada ili warudi naye nyumbani na kutishia kumkomesha iwapo angeendelea kuwa kero kwao.

…WAZO BONZO…

Wito kwa jamii ya Wakamba iitishe matangi ya maji kama mahari

Na PIUS MAUNDU

WAZIRI wa Maji katika Kaunti ya Makueni, Bw Robert Kisyula, ameomba jamii ya Wakamba itafakari upya utamaduni wake kuhusu mahari ili kukabiliana na uhaba wa maji unaokumba eneo hilo mara kwa mara.

Bw Kisyula alisema wazazi wanafaa wakome kuitisha mifugo kama mahari na badala yake wawe wakiitisha matangi ya maji ili kuhifadhi maji ya mvua.

“Wale wanaooza mabinti zao wanaafaa waitishe angalau matangi mawili ya lita 10,000 badala ya mbuzi na zawadi zingine,” akasema alipozindua mradi wa maji wa Masue.

Mradi huo wa Sh5.6 milioni, ambao utakuwa ukihifadhi maji ya mvua katika kijiji cha Masue, unatekelezwa kwa ushirikiano wa serikali ya kaunti na Shirika la Maendeleo la Anglikana tawi la Mashariki.

Eneo la Ukambani hutegemea uhifadhi wa maji ya mvua kwa sababu ya uhaba uliopo na kulingana na Bw Kisyula, kuitisha matangi kama mahari kutasaidia kuhakikisha familia nyingi zimehifadhi maji ya kutosha kutaimarishwa ikiwa wakazi wataukumbatia kibinafsi.

Ili kuimarisha uhifadhi wa maji zaidi, serikali ya kaunti hiyo huhitaji wanaojenga nyumba mjini waeleze kwanza jinsi wanavyopanga kuhifadhi maji ya mvua kabla waruhusiwe kujenga.

Pendekezo la Bw Kisyula limeibua mijadala hasa katika mitandao ya kijamii ambapo kuna wanaolisifu na kusema litasaidia kutatua changamoto ya uhaba wa maji Ukambani.

“Tayari tumekumbatia pendekezo la Bw Kisyula nyumbani kwangu. Hakuna vile nitakubali kuchukua mbuzi kama mahari ya binti yangu.

Anayetaka kumwoa lazima ajiandae kununua matangi makubwa ili kumwondolea mamake matatizo ya kusukuma maji kwa punda,” akasema Bw Benjamin Kitua, ambaye ni mfanyabiashara anayefanya kazi Nairobi.

Mbabazi akataa mahari kutoka kwa Ramaphosa

Kampala UGANDA

ALIYEKUWA waziri mkuu wa Uganda na mgombeaji wa urais Amama Mbabazi, amekataa mahari kutoka kwa familia ya Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa ambaye mwanawe anataka kumuoa binamu wa mke wake.

Bw Mbabazi aliwaambia jamaa wa Rais Ramaphosa, ambao walikuwa wameandamana na Andile Ramaphosa kumposa Bridget Birungi Rwakairu, kwamba mazoea ya wazazi kubadilisha mahari na binti zao yanadunisha wanawake.

Bw Mbabazi alisema mali ambayo wazazi hutumia kuwalea watoto wao ni ya thamani kuu kiasi kwamba haiwezi kufananishwa na wanyama (mahari).

“Hatugawi binti yetu. Angali wetu, kwa hivyo kile ambacho mnatupa leo, tutaipa familia hii changa (wanaooana) ili iweze kuisaidia katika kujenga familia yake,” Bw Mbabazi ambaye alimlea Bi Rwakairu aliwaambia jamaa wa Rais Ramaphosa.

Ilikuwa imeripotiwa kwamba Bw Ramaphosa alitarajiwa kulipa ng’ombe 100 na zawadi nyingine katika sherehe ya mahari ya mwanawe Andile.

Bw Mbabazi alisema akiwa mmoja wa waandalizi wa katiba, walihakikisha kwamba wamekabili changamoto za ukosefu wa usawa wa jinsia ikiwemo ulipaji wa mahari.

Alisema ulipaji wa mahari umemkosesha mwanamke utu na kusababisha misukosuko katika familia kwa kufanya wanawake kuonekana kama mali ya wanaume.

“Hii ni aina ya dhuluma iliyokuwapo kabla ya historia kuanza kuandikwa na tunafaa kuimaliza. Tunafaa kuwa tukijenga uhusiano kati ya familia zote mbili na kukuza mizizi ya familia. Hatupeani binti yetu kwa sababu yeye angali mmoja wetu,” alisema.

Alisema hayo baada ya Bw Charles Mbire, aliyekuwa msemaji wa ujumbe wa familia ya Ramaphosa kusema kwamba walikuwa tayari kulipa mahari ili wapewe Bi Rwakairu.

Kauli ya Bw Mbabazi pia iliungwa na waziri mkuu wa sasa

Dkt Ruhakana Rugunda ambaye alikuwa upande wa Bi Rwakatiru. “Hatutaki kusikia neno mahari katika mkutano huu kwa sababu hatumuuzi binti yetu. Mnaweza kutumia neno nyingine.

Pengine mseme zawadi ya kuwashukuru sisi wazazi kwa kumzaa na kumlea binti yetu,” alisema Dkt Rugunda.

Familia ya Bw Mbabazi na ujumbe wa watu 12 kutoka Afrika Kusini ulioongozwa na Bi Hope Ramaphosa, mama ya bw harusi walikubaliana ngombe watano na mbuzi watano.

Ngombe hao walikabidhiwa Andile Ramaphosa na bibi yake mtarajiwa. Mbuzi hao walipatiwa shangazi na wajomba wa Rwakairu kama shukrani kwa kumlea.

Hata hivyo, jamaa za Rwakairu walimtoza Andile faini ya mbuzi mmoja kwa kuzaa mtoto na binti yao nje ya ndoa.

Andile na Rwakairu walikutana China wakiwa masomoni na wanatarajiwa kuoana rasmi mwishoni mwa mwaka huu.

 

Gharama hii ya harusi na mahari inaogofya vijana kuasi ukapera – Duale

Na GALGALO BOCHA

KIONGOZI wa wengi bungeni Aden Duale amelalamikia gharama kubwa ya harusi na mahari za jamii ya waislamu kuwa chanzo cha maelfu ya vijana kushindwa kuasi ukapera.

Akizungumza wakati wa sherehe ya kitamaduni ya jamii ya Wasomali eneo la Eastleigh, Bw Duale amesema vijana wengi waliofika umri wa kuoa, wanashindwa kuposa kwa hofu ya kutozwa mamilioni kama ada ya mahari.

Mbunge huyo wa Garissa Mjini alitoa mfano wa jamii yake ya Kisomali aliyosema imefika kiwango cha kuitisha dola 10,000 kama mahari kabla ya ndoa kufungwa.

“Gharama ya ndoa za kiislamu lazima ishukishwe. Kutaka vijana kulipa dola 10,000 ili kuoa ni kosa. Kama waislamu tumekosea na lazima kufanya ndoa kuwa nyepesi na isiyokuwa na gharama ili vijana waachane na mambo mengine ya kando kando,”

Alisema atakutakana na viongozi wa kidini haswa mashekhe wa msikiti wa Jamia, Nairobi, kuanzisha mchakato wa kupunguza mahari na gharama za harusi.

Alisema tatizo hilo limepelekea idadi kubwa ya vijana wa Kiislamu kukosa matumaini ya kuoa na badala yake kujihusisha na hulka ya mapenzi kinyume na mafunzo ya dini.

“Jambo la kuitisha mahari ya dola elfu kumi kabla ya kufungisha binti yako nikaa, kama kwamba unanunua gorofa au gari lazima ikomeshwe. Nitakwenda msikiti wa Jamia siku ya Ijumaa na kuzungumza na mashekhe tutafute suluhisho,” akaeleza Bw Duale katika sherehe hiyo iliyofanyika Shule ya Upili ya Eastleigh.

Alisema jamii ya waislamu imekiuka utaratibu wa dini kuhusu jambo la ndoa.

Kiongozi huyo ya walio wengi bungeni, alisema harusi nyingi zinatekelezwa kinyume na mafundisho ya Mtume Muhammad.

“Wakati wa Mtume, unaulizwa kama una jamvi na kibanda cha kuanzia maisha kama wana ndoa kabla ya harusi kufanyika. Siku hizi unaulizwa uko na dola ngapi,” akalalama.

Bw Duale alisema chanzo cha jamii yake ya Kisomali kufanya ndoa kuwa na ghama ilitokana na watu wanaoishi mataifa ya ughaibuni ambao hulipa mari kwa dola za kimarekani.

Vile vile, mkoani Pwani vijana wengi wamekuwa wakilalamikia kiwango kikubwa cha mahari inayoitishwa na familia za wasichana.

Vijana wanaofanya kazi njee ya nchi haswa maeneo ya Mashariki ya Kati ndio wanaolaumiwa kufanya gharama ya ndoa kuwa juu.

Vijana hao wanalipwa mahari ya juu kutokana na thamani ya sarafu za mataifa za kiarabu, Uingereza na Marekani miongoni mwa zingine.

Aidha mbunge huyo wa Garissa Mjini amewahimiza wanawake wa kiislamu kuzingatia kwa dhati vazi la hijab ambalo alisema ndilo pambo rasmi la waislamu kote duniani.

Aliwahimiza waume pia kuhakikisha wamewajibika katika ndoa na vile vile mke zaidi ya mmoja

 

Mashemeji wamtaka alipe mahari kwa kurithi mke baada ya mume kuaga

Na TOBBIE WEKESA

AHERO, KISUMU

MAKALAMENI kutoka hapa waliwashangaza wakazi walipomdai polo mahari kwa kumrithi dada yao baada ya mumewe kufariki.

Inasemekana makalameni hao walimlazimisha polo kuwapa ng’ombe watatu ili kukamilisha deni alilokuwa ameacha marehemu mume wa dada yao.

Mume wa kipusa aliaga dunia miaka miwili iliyopita. Jamaa kutoka kwa familia ya marehemu alijitokeza na kumrithi mjane. Duru zinasema kabla ya marehemu kuaga dunia, alikuwa amepeleka ng’ombe wawili kama mahari na kuahidi kupeleka ng’ombe wengine wawili baada ya miaka miwili.

“Tunachojua marehemu shemeji yetu alikuwa amempa mama kitu kidogo na akaahidi kumalizia baadaye. Ni wewe utamalizia,” kalameni mmoja alimueleza polo.

Polo alijaribu kupinga madai ya makalameni lakini juhudi zake hazikufua dafu. “Unatuambia nini? Hata kuna fununu kwamba dada yetu ana mimba yako. Hatutoki hapa bila mahari,” makalameni waliapa.

Polo aliwaeleza makalameni kwamba alikuwa akimsaidia mjane ili asitaabike bali hakuwa amemrithi.

“Acha zako. Hadithi zote twazijua. Umemrithi tangu shemeji aage dunia. Kwa sasa tunachukulia kuwa umemuoa,” makalameni walimueleza polo.

Inadaiwa polo aliamua kuwaita wazee wa jamii ili kutatua mgogoro uliokuwa ukinukia.

Wazee walijaribu kutuliza joto lakini makalameni walisisitiza lazima polo atoe mahari.

“Kwanza huyu jamaa tumemsamehe sana. Angeanza kulipa mahari freshi. Kama hatatoa mahari anataka tumtambue kama nani? Hakuna vya bure. Lazima mahari atoe na ni leo,” makalameni walisisitiza.

Wazee walilazimika kuondoka na kumuacha polo ang’ang’ane na wageni wake.

…WAZO BONZO…
…WAZO BONZO…