Shule zakosa maji ya kupikia watoto

Na WAANDISHI WETU

WALIMU katika baadhi ya shule za Kaunti ya Tana River, wamelazimika kuwapa watoto chakula kibichi ili wakajipikie nyumbani kwa vile hakuna maji ya kupika.

Imebainika kuwa, watu zaidi ya 60,000 wako hatarini kuathirika na njaa katika maeneo tofauti ya kaunti hiyo.Mratibu wa Mamlaka ya Kitaifa ya Kudhibiti athari za Ukame, tawi la Tana River, Bw Abdi Musa, alisema Kaunti Ndogo za Bura, Tana Delta na Tana River ndizo zina mahitaji zaidi.

Katika maeneo ya Kone na Asa yaliyo Tana Delta, imeripotiwa zaidi ya familia 200 zilihama makwao ili kutafuta chakula na maji kwa kuwa mvua haijanyesha katika baadhi ya maeneo hayo tangu mwaka uliopita.

“Shuleni kuna chakula kilichohifadhiwa, lakini tatizo ni jinsi ya kupika chakula hicho. Hakuna maji. Masomo yanaathirika,” akasema.

Wanafunzi waliotegemea chakula cha shuleni sasa hupewa chakula kibichi ambacho watahitajika kupikiwa na wazazi wao, kisha wabebe wanapoenda shuleni ili wale wakati wa mchana.

Baadhi ya familia sasa hutegemea chakula hicho hicho ambacho watoto hupewa shuleni. Waziri wa Kilimo, Bw Peter Munya alisema baraza la mawaziri litakutana wiki ijayo kujadili baa la njaa linalokumba zaidi ya watu milioni katika takriban kaunti 12 nchini, ili kuamua njia mwafaka za kuepusha maafa.

Kati ya mikakati ambayo serikali inazingatia, ni kununua mifugo kutoka kwa wafugaji ili kuwaepushia hasara kwa sababu mifugo wameanza kufa katika baadhi ya maeneo.

Vile vile, serikali inatarajiwa kuamua jinsi ya kufikia idadi kubwa zaidi ya wananchi wenye mahitaji na kuwapa pesa za kununua chakula.

“Tumekuwa tukitathmini hali ilivyo. Tuna kamati katika la baraza la mawaziri ambayo inahusika na masuala ya ukame na baa la njaa. Kamati hiyo inaweka mikakati ya haraka ya kusaidia waathiriwa,” alisema Bw Munya.

Ijapokuwa Bw Munya alizidi kusema wizara yake imeanza kuandaa wakulima kwa msimu wa mvua, utabiri wa hali ya hewa uliotolewa mapema wiki hii, ulionyesha kuwa bado kutakuwa na uhaba wa mvua msimu huu.

Magavana wa kaunti za Kaskazini Mashariki, walimtaka Rais Uhuru Kenyatta, atangaze hali inayoshuhudiwa kuwa janga la kitaifa.

“Hali imeharibika zaidi kwa sababu ya uvamizi wa nzige ulioshuhudiwa awali ambapo mimea iliharibiwa. Sasa kuna ukame ambao tayari umeonyesha athari zake katika maeneo kama vile Kutolo na Mandera Magharibi, na vile vile sehemu za Kaunti ya Wajir,” akasema Gavana wa Mandera, Bw Ali Roba.

Kando na kuililia serikali kuu, walishauri kaunti zinazokumbwa na njaa kuhakikisha kuna bajeti ya kusaidia wananchi, kando na zile za kupambana na janga la corona.Katika Kaunti ya Lamu, Kamishna Irungu Macharia alisema takriban Sh100 milioni zinahitajika kwa dharura ili kusaidia waathiriwa wa njaa.

Mkurugenzi wa NDMA, Kaunti ya Lamu, Bw Mohamed Dahir, alisema wafugaji kutoka kaunti jirani za Tana River na Garissa, tayari wamefurika Lamu, na kusababisha hofu ya migogoro kuhusu sehemu za malisho.

Ripoti za Stephen Oduor, Winnie Atieno, Farhiya Hussein na Kalume Kazungu

Tumaini shirika la Ubelgiji likifadhili uchimbaji kisima eneobunge la Ganze

Na ALEX KALAMA

WAKAZI wa eneo la Kavunzoni, Kaunti ya Kilifi wana matumaini kwamba tatizo la uhaba wa maji ambalo limewakumba kwa miaka mingi litatatuliwa hivi karibuni.

Hii ni baada ya shirika la kutoka Ubelgiji kufadhili uchimbaji wa kisima katika eneo hilo lililo eneobunge la Ganze.

Wakiongozwa na Bw Robert Chengo, wakazi hao hata hivyo wameitaka serikali ya kaunti hiyo kuwasambazia wakazi maji wanaposubiri kisima hicho kukamilika.

“Hiki kisima kitasaidia wakazi wote wa Goshi na eneo la Mitangani. Huwa tunatoka hapa asubuhi saa moja tukifika mahali pa kuchota maji ni saa tano, kisha kurudi hapa ni saa nane au saa tisa ndipo tunashukisha maji,” akasema Bw Chengo.

Kulingana na mbunge wa eneo hilo Teddy Mwambire, serikali ya Kaunti ya Kilifi inafaa kushirikiana na mashirika mbali mbali ili kuhakikisha eneo hilo linapata maji.

“Hii sehemu ya Kavunzoni, Goshi kuenda mpaka karibu na Mnagoni imekuwa kame na maji unapata baada ya kutembea kilomita takribani 20. Mtungi mmoja ule wa lita 20 wanauziwa kwa Sh50. Ushirikiano utasaidia kuhakikisha kwamba hili eneo linapata maji kwa haraka,” alisema Bw Mwambire.

Wakazi wa eneo hilo waliupongeza ufadhili huo wakisema utawapunguzia changamoto ya kutembea mwendo mrefu kutafuta maji.

Boresha afya yako kwa kunywa maji fufutende

Na MARGARET MAINA

mwmaina@ke.nationmdia.com

MAJI ya kunywa ni sehenu muhimu katika kuboresha afya zetu kama binadamu, haswa katika kuimarisha miili dhidi ya magonjwa mengi.

Maji ya ufufutende, badala ya maji baridi kama ilivyozoeleka kwa watu wengi, yana faida tele kwa miili yetu.

Maji ya ufufutende yana manufaa zaidi mwilini kuliko maji baridi. Maji ya ufufutende husaidia katika uyeyushaji wa chakula, na pia huzilinda figo pamoja na viungo mbalimbali mwilini.

Jambo muhimu la kuzingatia ni kutambua kuwa maji ya ufufutende si yale ya moto, kwani yakiwa ya moto sana huwa na madhara kwa ngozi nyembamba ya ndani ya mdomo, ikiwemo ulimi.

Tufahamu kuwa maji baridi ya kunywa hugandisha mafuta yaliyopo ndani ya miili yetu, ikiwemo kuufanya mwili kutumia nguvu ya ziada kuyapasha joto maji hayo kabla ya kutumika mwilini.

Hali hiyo inapoendelea kwa muda mrefu, huweza kusababisha shinikizo la damu, kwani hukwamisha mzunguko mnyoofu wa damu mwilini; na hivyo kusababisha magonjwa mengine mengi kuibuka.

Pia ni vyema kutumia maji ya uvuguvugu yaliyotiwa limao au ndimu, ili kupunguza ‘radicals’ ndani ya mwili na pia kuleta ladha katika maji yenyewe.

Pia ni vyema kunywa maji hayo vuguvugu kabla ya kifungua kinywa, ili kurahisisha mfumo wa mwili kwa siku nzima.

Faida za kunywa maji ya ufufutende

  • Yanasaidia kupunguza uzito

Kama unasumbuliwa na uzito wa mwili wako na ungependa kuupunguza, unashauriwa kunywa maji ya ufufutende, kwani huweza kuongeza joto la mwili na kuupatia mwili uwezo wa kuchoma lehemu kwa siku nzima.

  • Yanaboresha mzunguko wa damu mwilini

Mwili unapokuwa na limbikizo kubwa la mafuta (ambayo pia husababishwa na unywaji wa maji baridi), kinachotokea ni madhara mbalimbali katika afya yako.

Lakini unapotumia maji ya ufufutende, yanaenda kuyeyusha na kuondoa mwilini hiyo migando ya mafuta.

Hatua hii pia husaidia kuondoa sumu yote ndani ya mwili, na kuufanya mzunguko wa damu kuwa mzuri, ikiwemo kuwezesha misuli kupumzika.

  • Yanasaidia kuondoa mikunjo mwilini

Hakuna mtu anayependa kuzeeka mapema kabla ya wakati wake, hali ambayo mara nyingi husababishwa na uwepo wa “sumu” mbalimbali katika miili yetu.

Hata hivyo, unapokunywa maji ya uvuguvugu, husaidia kuondoa sumu hizo na kuusafisha kabisa mwili wako kwa ndani.

Maji hii yatasaidia kurejesha seli za ngozi yako, ili iwe na muonekano wa kuvutia na kuwa nyororo.

  • Kuondoa sumu mwilini

Faida nyingine ya kunywa maji ya uvuguvugu ni kutoa sumu zilizopo kwenye mishipa yako ya fahamu, na pia kuisadia figo yako kufanya kazi yake kikamilifu.

Hii ni tofauti kabisa na maji ya baridi, ambayo yanagandisha na kuilazimisha figo kuyeyusha kwanza maji hayo na kisha kuyachuja kabla ya kuyapitisha kutumika mwilini.

  • Kupata choo kwa urahisi

Maji ya ufufutende ni mazuri hata kwa kupata choo, kwa vile yanarahisisha uyeyushaji na uchambuaji wa kile kinachotakiwa na kisichotakiwa kutumika ndani ya mwili.

Faida nyingine ya kutumia maji ya ufufutende ni pamoja na kusafisha haja ndogo, na pia kuchangamsha utendaji kazi wa ubongo wako.

Aidha, kama uwezo wa kiuchumi unaruhusu, waweza kuyaongezea maji hayo limau na/au asali, kwani vitu hivyo si tu huongeza ladha, bali pia vina faida nyingi kiafya.

Fanya hivyo kila unapoamka asubuhi, kabla ya kula kitu chochote.

Kunywa maji ya ufufutende glasi mbili kisha kaa kwa muda wa saa moja hivi bila kula kitu ili kutoa nafasi kwa maji hayo kutumika mwilini kama ilivyoada.

Baada ya hapo, endelea kutumia vyakula vingine kama kawaida bila kusahau kufanya mazoezi ya viungo ili kuzidi kuboresha afya yako.

Thiwasco yaweka mikakati ya uboreshaji wa huduma za maji safi

Na LAWRENCE ONGARO

KAMPUNI ya maji ya Thika, maarufu kama Thiwasco, imepanga mikakati ya miaka 20 ijayo kwa lengo la kutosheleza wateja wake kwa kuhakikisha wanapata maji safi.

Mkurugenzi wa kampuni hiyo Bw Moses Kinya, alieleza kuwa ifikapo mwaka wa 2040 kampuni hiyo itakuwa ikisambaza kiwango cha ujazo lita 63 milioni kwa siku ikilinganishwa na lita 17 milioni ya maji inayosambaza kwa sasa kila siku.

Alifafanua kuwa mradi wa maji wa Karimenu ulioko Gatundu Kaskazini, unaoendelea kwa sasa, ukikamilika, basi wakazi wa Thika na vitongoji vyake wapatao laki nne watanufaika pakubwa.

Alitaja maeneo ya Witeithie, Gatuanyaga, Munyu, Githima, na Kiganjo kama maeneo yanayostahili kupokea maji kwa wingi kutokana na idadi kubwa ya wakazi.

“Tunataka kuhakikisha ya kwamba baada ya miaka mitano ijayo hakuna mkazi yeyote wa Thika na vitongoji vyake atakuwa na shida ya kupata maji safi katika makazi yake,” alisema Bw Kinya.

Aliyasema hayo mjini Thika mnamo Jumatano wiki jana katika hafla iliyohudhuriwa na washika dau tofauti kwa lengo la kujadiliana kuhusu usambazaji wa maji safi mjini Thika.

Alisema pia wamebuni mikakati mipya ya teknolojia kutoa huduma zao kwa wateja wao wote ili kurahisisha kazi zao.

Tayari kampuni hiyo pia imechimba visima kadha katika maeneo tofauti kama Kilimambogo, Gatuanyaga na Matathia sehemu za Thika Mashariki.

Vile vile shirika moja la kimataifa la kutoka Denmark, DANIDA, litafadhili kampuni ya Thiwasco, kwa kitita cha Sh11 bilioni ili kuinua sekta hiyo ya maji mjini Thika na vitingoji vyake. Bw Kinya alisema wakati mradi huo utakamilika, utaweza kusambaza maji lita 36 milioni kwa siku.

“Miaka miwili ijayo shida ya maji kwa wakazi wa Thika itakuwa ndoto kwani kampuni ya Thiwasco itakuwa imesambaza maji sehemu nyingi,” alisema Bw Kinya.

Wapwani kukosa maji huku miradi ya Sh70b ikikwama

ANTHONY KITIMO, STANLEY NGOTHO na WACHIRA MWANGI

WAKAZI wa Mombasa, Kwale na Kilifi wataendelea kukabiliwa na uhaba wa maji baada ya miradi mitatu mikuu ya maji yenye thamani ya karibu Sh70 bilioni kukwama.

Licha ya kuwa na uungwaji mkono kutoka kwa Rais Uhuru Kenyatta, miradi hiyo ilikosa kuanza kwa wakati kwa kukosa ufadhili wa kutosha na mivutano kuhusu malipo ya fidia.

Mradi wa Mzima Spring II wenye thamani ya Sh35 bilioni, mradi wa Bwawa la Mwache wenye thamani ya Sh20 bilioni na kiwanda chenye thamani ya Sh16 bilioni, ilitarajiwa kusuluhisha matatizo ya maji yanayokabili kaunti hizo tatu.

Bwawa la Mwache lililopangiwa kuanza kujengwa mapema mwaka huu, limekumbwa na mizozo huku familia 2,452, taasisi nane za kijamii na umma zinazotazamiwa kufidiwa zikipanga kushtaki Tume ya Ardhi Nchini (NLC) kwa kutathmini mali yao isivyofaa na kuwalipa fidia duni.

Wakazi hao walishutumu NLC kwa kuwashawishi kukubali fidia ya Sh120,000 kwa kila ekari badala ya Sh350,000 jinsi ilivyoafikiwa hapo mbeleni.

“Hakuna maafikiano kati ya muuzaji na mnunuzi wa kujitakia kwa hiari na tunashinikizwa kufanya wanavyotaka, jambo ambalo ni la kusikitisha mno,” alisema mkazi kwa jina Uchi Mwero.

Gavana Salim Mvurya alisema wamekubaliana kuwasilisha kesi dhidi ya NLC kupitia njia mbalimbali wanazoweza ili kuhakikisha raia wanapata wanachostahili.

Alisema kuwa takriban wakazi 609 walioathiriwa miongoni mwa 624 katika eneo la ujenzi wa miradi hiyo linalozozaniwa la Fulugani, walishinikizwa kutia saini kiwango hicho duni cha fidia pasipo hiari yao.

Aidha, alieleza kwamba kundi lingine la wahasiriwa 736 katika eneo hilo walilazimishwa vilevile kutia saini malipo hayo duni.Kwingineko, wakazi katika vijiji kadhaa katika Kaunti Ndogo ya Kajiado ya Kati, wameachwa bila la kufanya baada ya maeneo hayo kukumbwa na mafuriko.

Mafuriko hayo yaliyotokea Jumamosi yalisomba daraja kadhaa na kuharibu barabara kiasi cha kutopitika.

Kutokana na mafuriko hayo, wakazi wa vijiji vya Torosei na Olongosua hawawezi kufika katika mji wa Illbisil kukunua vyakula na bidhaa nyingine muhimu kutokana na kiwango kikubwa cha maji kilicho kati ya maeneo hayo mawili.

Wanahofia huenda hali ikadorora zaidi, hasa baada ya barabara na daraja kuharibiwa.Wale waliokuwa mjini humo walilazimika kulala huko, huku watu waliokuwa wameenda katika soko la Torosei wakishindwa kurejea majumbani mwao.Wengine walikesha usiku kucha katika magari yao baada ya madaraja kusombwa.

Wanawake ndio walioathiriwa zaidi, hasa walio na watoto wachanga.“Tulilala kwenye magari chini ya baridi kubwa. Hatungeweza kurejea Torosei kutokana na hali mbaya ya barabara. Hatukula chalula chochote,” akasema Bi Jane Kores.

Wafanyabiashara Muthurwa waitaka NMS iwape maji safi

Na SAMMY KIMATU

WACHUUZI katika soko la Muthurwa, Kaunti ya Nairobi wameliomba Shirika la Huduma katika jiji la Nairobi (NMS) kuzindua mradi wa maji ambao ulikamilika mwaka 2020 kwa sababu wao hutaabika kwa kukosa maji.

Akiongea na Taifa Leo jana Jumapili, mwenyekiti wa soko hilo, Bw Nelson Githaiga alisema wafanyabiashara hulazimika kununua maji ya kutumia sokoni kutoka kwa wachuuzi wa maji.

Hata hivyo, aliongeza kuwa wanahofia mkurupuko wa magonjwa ya kuambukizana kwani hawajui maji hayo huchotwa wapi.

Vilevile, alisisitiza kuna umuhimu wa maji masafi kuwa sokoni hasa wakati huu wizara ya afya imetoa kanuni za kufuata ili kuzuia msambao wa korona.

“Mradi wa maji ya Muthurwa utakuwa wa msaada mkubwa kwa wateja na wafanyabiashara hasa wakati huu tunapowauliza watu wote kudumisha kanuni za wizara ya afya ili kupunguza msambao wa Korona,” Bw Githaiga akaambia Taifa Leo.

Bw Githaiga aliongeza kwamba hali si hali sokoni kufuatia msongamano wa magari yanayoingia na kutoka katika kituo cha matatu cha Muthurwa.

Katika eneo la wachuuzi wa nyaya na viazi vitamu, malori, matatu na mikokoteni huwatatiza wanaokuwa sokoni pamoja na wananchi watembeao kwa miguu wakielekea kazini.

“Tunaomba wahusika kupanga mikakati ya kuleta utaratibu mwafaka ili kila kitu kiende shwari bila kumkwaza yeyote,’’ Bw Githaiga alisema.

Aliongeza kwamba wafanyabiashara wanaouza nyanya na viazi vitamu hutatizika kutokana na matope yaliyojaa kwenye sehemu waliyotengewa na serikali ya kaunti ya Nairobi.

Kadhalika, alisema kuwa ni wakati wa mvua au wakati kuna Jua Kali ni lazima wachuuzi na wateja wao wavalie buti za kujikinga na matope.

“Matope yamekithiri kwenye sehemu tuliyotengewa kuuza nyanya na viazi vitamu. Huwezi kuingia katika soko hili bila kuvalia buti. Twaomba serikali kupitia NMS kukarabati soko letu kwa kuweka simiti na kutujengea vibanda vya kujikinga mvua na jua,’’ Bw Githaiga akasema.

Wakazi wa mitaa ya mabanda Nairobi wahangaika kupata maji

Na SAMMY KIMATU

WAKAZI katika mitaa mitatu ya mabanda katika Kaunti ya Nairobi wameomba serikali kuwachukulia hatua kali maafisa katika idara ya maji ambao hushirikiana na wachuuzi wa maji kuwahangaisha.

Kwa wiki ya pili mfululizo, wakazi hao kutoka mtaa wa mabanda wa Maasai, Kayaba na Hazina kwenye kaunti ndogo ya Starehe wamekosa maji safi ya kutumia nyumbani.

Aidha, kufuatia ukosefu huo, wanalazimika kuchota maji ya visima yaliyo na chumvi baada ya Idara ya Huduma za Jiji la Nairobi (NMS) kuchimba visima vitatu.

Njia nyingine badala ni kulazimika kununua maji yanayochuuzwa mitaani na wenye mikokoteni japo wanahofia mkurupuko wa magonjwa ya kuambukizana kwani hawajui maji hayo yanakotoka.

“Baada ya kukosa maji yanayosambazwa na kampuni ya maji mitaani, hatuna budi ila kuchota hayo ya kutoka visimani licha ya maji hayo kuwa na chumvi,’’ Bw Stephen Ndichu akaambia Taifa Leo.

Ofisa mmoja wa NWC alisema uhaba wa maji umetokana na ujenzi wa barabara mpya inayounganisha Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa JKIA na Westlands mkabala wa barabara Kuu ya Mombasa.

Wakazi walidai kuna njama ya maafisa wa maji kushirikiana na wachuuzi ili wakifunga maji, wachuuzi wapate fursa ya kuuza maji kwa bei ya juu.

“Kuna mifereji ambayo imefungwa hadi barabara mpya itakapomalizika hivyo tunawauliza walioathirika watuvumilie kwa muda,” afisa huyo ambaye hatuwezi kutaja jina lake kwa sababu za itifaki akasema.

Wakazi wa mitaa hiyo wakati huu hutegemea maji ya kisima katika Shule ya Msingi ya Mukuru katika mtaa wa mabanda wa Mukuru na yale ya kisima cha Goal Kenya kilichoko mtaani wa mabanda wa Hazina.

Chifu wa eneo la Mukuru-Nyayo, Bw Charles Mwatha alisema maji hayo hufunguliwa kuanzia saa kumi na mbili asubuhi na kufungwa saa kumi na mbili za jioni.

‘’Maji haya hufunguliwa kila siku kuanzia saa kumi na mbili za asubuhi hadi saa kumi na mbili za jioni na hayalipwi bali wakazi huchota bila kulipishwa pesa kwa sababu ni ya serikali,’’ Bw Mwatha akasema.

Jana, katika mtaa wa Hazina, kulikuwa na milolongo mirefu ya mitungi kufuatia ukosefu wa maji miferejini. Akinamama waling’ang’ania nafasi huku purukushani ilkishuhudiwa na kulazimu maji hayo kufungwa.

‘’Wanawake walizozana na kupigania maji jambo lililopelekea maji hayo kufungwa hadi hali itulie,’’ Bw James Mulandi akasema.

Ilimlazimu mwenyekiti wa kisima hicho aliye kadhalika mwanachama wa kamati ya Nyumba Kumi, Bw Hussein Mohammed kuwahutubia waliokuwa wakichota maji na kuwauliza wawe na utaratibu wanapochota maji na baadaye hali ikatulia.

Katika kisima cha Kaiyaba, mama mmoja alifurushwa na mitungi yake alipokabiliana na watoto wakitofautiana ni nani atakayechota maji kwanza kuliko mwingine.

Wakazi waikejeli serikali kusitisha usambazaji wa maji

NA KALUME KAZUNGU

WAKAZI wa vijiji vya Witu na viungani mwake wameikejeli serikali ya Kaunti ya Lamu kwa kusitisha ghafla huduma ya usambazaji maji kupitia lori vijijini mwao.

Wakazi hao, wengi wao wakiwa ni kutoka vijiji vya Dide Waride na Bulto walitisha kushiriki maandamano kupinga hatua hiyo ya kaunti kuondoa gari la kusambaza maji eneo hilo bila ya kuwashauri.

Zaidi ya familia 400 kwa sasa zimekuwa zikihangaika kutokana na ukosefu wa maji tangu lori hilo lilipositisha huduma zake karibu miezi miwili iliyopita.

Lori hilo lilikuwa likisambaza maji kwa wananchi kila wiki ili kusaidia kukabiliana na ukame ambao umechangia kushuhudiwa kwa uhaba mkubwa wa maji kwenye vijiji mbalimbali vya Lamu.

Wananchi na mifugo wanalazimika kutembea kwa miguu hadi mjini Witu, ambako ni karibu kilomita 16 ili kununua maji ya matumizi ya nyumbani ambayo huuzwa kwa bei ghali.

Wakazi sasa wanawashurutisha maafisa wa serikali ya kaunti ya Lamu kurejesha huduma ya kusambaza maji kupitia lori mara moja la sivyo washiriki maandamano barabarani ili kilio chao kisikike nchini.

Hassan Ali alisema wamechoka kukaa bila maji, hivyo akaisisitizia kaunti na wahisani kuwaonea imani na kuwapumzisha mahangaiko wanayopitia kila kukicha wakitafuta maji.

Mifugo kwenye kijiji cha Dide Waride na viungani mwake pia wameripotiwa kufariki kutokana na kiangazi na ukosefu wa maji.

“Ni mwezi karibu wa pili huu tangu lori la kusambaza maji lilipoondolewa eneo hili. Hatukuarifiwa kwa nini gari hilo lilikomeshwa kusambaza maji kijijini kwetu. Tunalazimika kutumia pikipiki kubeba maji kutoka Witu hadi Dide Waride, ambapo huwa tunalipa kati ya Sh 200 na Sh 400 ili kufikishiwa maji hapa. Kaunti itusaidie kutatua shida hii,” akasema Bw Ali.

Bi Fatma Said alisema mara nyingi wamelazimika kulala bila kula kutokana na uhaba wa maji unaoendelea kukumba eneo lao.

Bi Said alieleza kusikitishwa kwake na hatua ya kaunti ya kusitisha huduma ya kusambaza maji vijijini mwao.

“Tunalala kwa njaa kwa kukosa maji. Dide Waride ni mojawapo ya maeneo ambayo yanashuhudia ukame mkali kila mwaka. Ninashangaa kwa nini kaunti ikaamua kusitisha huduma hiyo ya kutusambazia maji kupitia lori hapa. Warekebishe hali hii. Tunaumia.” akasema Bi Said.

Kwa upande wake aidha, Waziri wa Masuala ya Huduma za Umma na Majanga ya Dharura wa Kaunti ya Lamu, Abdu Godana alipinga madai kuwa kaunti ilikuwa imesitisha huduma za kusambazia maji wakazi wa Dide Waride kupitia lori.

Badala yake, Bw Godana alisema mikakati inaendelea katika ofisi yake na kwamba kabla ya mwisho wa juma hili tatizo la maji kijijini Dide Waride litakuwa limeshughulikiwa.

Bw Godana alisema huduma za lori hilo la kubeba maji zilisitishwa kwa muda kijijini humo ili kupisha nafasi kwa wakazi wa kijiji cha Bar’goni, ambacho pia kinakabiliwa na uhaba wa maji wapate huduma hiyo.

Alisema idara yake ina mpango wa kuongeza malori yatakayokuwa yakisambazia wananchi maji vijijini hivi karibuni.

“Hatujaacha kusambazia wananchi maji. Gari ni moja na linasambaza maji vijijini kwa zamu. Juma lililopita na hata sasa lori limekuwa likisambaza maji Bar’goni, Basuba, Kiangwe na Kiunga. Tutarejelea usambazaji wa maji Dide Waride,Wit una viungani mwake kufikia kesho. Pia tuna mpango wa kuongeza malori hivi karibuni ili maji yasambazwe kila mahali bila kukoma,” akasema Bw Godana.

Juma lililopita, wakazi zaidi ya 3000 wa vijiji vya Siyu, Shanga-Rubu, Shanga-Ishakani na Pate, kaunti ndogo ya Lamu Mashariki walijitokeza kulalamikia uhaba wa maji ambao unakumba eneo hilo tangu msimu wa kiangazi ulipoanza Lamu na nchini kwa jumla.

Zaidi ya watu 3000 wakumbwa na uhaba wa maji Lamu Mashariki

Na KALUME KAZUNGU

ZAIDI ya wakazi 3000 wa vijiji vya Siyu, Shanga-Ishakani na Shanga-Rubu kwenye kisiwa cha Pate, Kaunti ya Lamu wanakumbwa na uhaba wa maji.

Wakazi wa vijiji hivyo tangu jadi wamekuwa wakitegemea maji ya mvua yanayohifadhiwa kwenye matangi maalum yanayotambulika na wenyeji kama jabia.

Wakazi pia hutegemea maji kutoka kwa visima.

Aidha tangu kiangazi kilipoanza kushuhudiwa kwenye maeneo mbalimbali ya Lamu, idadi kubwa ya majabia na visima vimekauka, hivyo kuwaacha wakazi bila maji.

Ni visima vichache ambavyo kwa sasa vimesalia kutoa maji ilhali vingine maji yake yakibadilika kuwa ya chumvi.

Katika mahojiano na wanahabari kwenye vijiji husika, wakazi walisema mara nyingi wamelazimika kuamka alfajiri kuelekea kisimani ili kuchota maji na kuepuka milolongo mirefu.

Wengine wamekuwa wakitembelea visima usiku wa manane ilmradi wachote maji bila kero la milolongo mirefu.

Kwenye kijiji cha Siyu ambacho kina karibu watu 2000, ni kisima kimoja pekee kinachotoa maji safi.

Bi Aisha Kassim aliiomba serikali ya kaunti na wahisani kuwasambazia maji kupitia malori ili wapumzike mahangaiko wanayopitia wakitafuta rasilimali hiyo.

“Wengi wetu hatulali usiku hapa. Tunakesha kisimani kusubiria maji. Kisima ni kimoja tu kinachotoa maji safi hapa Siyu. Visima vigine vimekauka ilhali baadhi vikitoa maji ya chumvi. Serikali ituonee imani,” akasema Bi Kassim.

Abdalla Yusuf alisema mara kwa mara wamekuwa wakilazimika kukodisha pikipiki ili kwenda kuchota maji eneo la Faza ambalo liko zaidi ya kilomita 30 kutoka Siyu.

Bw Yusuf anasema mtungi wa lita 20 wa maji huuzwa kwa hadi Sh50, bei ambayo wengi hawawezi kuimudu.

“Ukikosa nafasi ya kuchota maji kisimani basi hutakuwa na budi ila kuagiza maji kutoka Faza. Unakodisha pikipiki. Isitoshe, maji yenyewe unayanunua kwa bei ghali ya hadi Sh 50 kwa kila mtungu wa lita 20. Tunateseka,” akasema Bw Yusuf.

Katika vijiji vya Shanga-Rubu na Shanga-Ishakani, wakazi wamelazimika kutumia maji ya chumvi kutoka visimani.

Bi Mwanaisha Bamkuu alieleza hofu kwamba huenda wakaugua maradhi ya tumbo kutokana na matumizi ya maji chafu.

“Ukiangalia watoto na watu wazima hapa meno yao yameharibiwa na haya maji ya chumvi. Meno yako na rangi ambayo haiondoki. Watoto wetu pia wako na maradhi ya ngozi kutokana na matumizi ya haya maji chafu,” akasema Bi Bamkuu.

Vijiji vingine ambavyo uhaba wa maji unaendelea kusheheni ni vile vya msitu wa Boni, ikiwemo Milimani, Mangai, Mararani, Basuba, Bodhai na Kiangwe.

Kwa upande wake, Meneja wa Bodi ya Kusambaza Maji, Kaunti ya Lamu (LAWASCO), Kimani Wanaina alisema uhaba wa maji unaokumba baadhi ya vijiji vya eneo hilo umesababishwa na kiangazi kinachoendelea.

“Kiangazi kimepelekea baadhi ya mabwawa yetu kukauka, hivyo kupunguza kiwango cha maji kinachosambazwa Lamu kila siku. Natumai hali itarejea kuwa ya kawaida punde kiangazi kitakapofikia kikomo,” akasema Bw Wainaina.

Tisho la baa la njaa kutokana na ukosefu wa maji Lamu

NA KALUME KAZUNGU

UHABA wa maji unaokumba vijiji vingi vya kaunti ya Lamu umewasukuma wakazi wengi kulala njaa katika wiki za hivi majuzi.

Wakazi wa vijiji vya Bar’goni, Kwasasi, Ingini, Kiangwe, Mokowe na maeneo mengine ya Lamu wamekuwa wakipitia kipindi kigumu cha kukosa maji na chakula, hasa baada ya visima walivyotegemea kupata maji kukauka kutokana na ukame unaoendelea eneo hilo.

Taifa Leo ilibaini kuwa wakazi wa vijiji kama vile Bar’goni,Ingini na Kwasasi kila siku hulazimika kutembea mwendo wa zaidi ya kilomita 20 kutafuta maji.

Mtungi mmoja wa lita 20 wa maji huuzwa kwa kati ya Sh 50 na Sh100. Akizungumza na wanahabari Jumapili, Mzee wa Nyumba Kumi kwenye Kijiji cha Bar’goni, Diza Doza, alisema wanalazimika kuishi bila chakula kutokana na ukosefu wa maji ya kupikia chakula hicho.

Bw Doza aliiomba serikali ya kaunti na ile ya kitaifa kufikiria kuwasambazia maji kwa kutumia malori kwani wanaumia.

“Kila siku tunaamka na kulala bila kuogakwani maji ni tatizo hapa. Isitoshe, baadhi ya familia hapa hulala kwa njaa kwa kukosa maji ya kutayarishia mlo. Kusafiri kutoka hapa Bar’goni hadi mjini Hindi ambako maji huuzwa ni karibu kilomita 21. Maji yenyewe yanauzwa kwa bei ghali. Serikali iangazie hali hii na kuitatua,” akasema Bw Doza.

Bi Amina Abuli akieleza mahangaiko wanayopitia kwa kukosa maji maeneo yao. PICHA/KALUME KAZUNGU

Bi Amina Abuli alisema wanawake na wanafunzi wa shule ndio huumia zaidi kwani hulazimika kuamka mapema na kutembea masafa marefu kwa miguu ili kutafuta maji.

Kulingana na Bi Abuli, idadi kubwa ya wanafunzi kijijini Bar’goni wamekuwa wakikwepa madarasa ili kuandamana na wazazi wao kutafuta maji kwenye maeneo ya mbali.

“Hapa Bar’goni visima vyote tulivyotegemea vilikauka kutokana na kiangazi. Kilichobakia ni uwe na uwezo wa kukodisha pikipiki kwa pesa nyingi ili ukanunuliwe maji Hindi. Ikiwa hilo huwezi kulimudu, basi unalazimika kutembea guu mosi guu pili hadi Hindi kununua maji. Wanafunzi hapa wamekuwa wakikosekana madarasani wakisaidia wazazi kutafuta maji,” akasema Bi Abuli.

Katikka mji wa Mokowe, wakazi wanalazimika kutumia maji ya chumvi kutoka kwa visima vilivyoko mkabala na ufuo wa Bahari Hindi eneo hilo.

Wakazi waliambia Taifa Leo kuwa huenda maji hayo yakawaathiri kiafya kwani mbali na kwamba ni ya chumvi, pia ni chafu.

Waliiomba serikali ya kaunti kupitia bodi ya kusambaza maji (LAWASCO) kuwaunganishia mifereji ya maji safi kwenye vijiji vyao ili wapumzike mahangaiko.

Kwa upande wake aidha, Afisa Mkurugenzi wa LAWASCO, Kimani Wainaina aliwashauri wakazi kujiandaa kushuhudia uhaba zaidi wa maji kote Lamu hasa msimu huu ambapo kiangazi kinaendelea kuathiri maeneo mengi nchini.

Bw Wainaina alisema karibu visima vitatu kwenye vyanzo vikuu vya maji ya Lamu eneo la Shella tayari vimekauka kufuatia ukame.

“Watu watarajie kushuhudia uhaba zaidi wa maji kwani kiangazi kinachoshuhudiwa kimechangia baadhi ya visima vya Shella kukauka. Hali ikiendelea hivi inamaanisha visima zaidi vitakauka, hivyo kuzidi kupunguza kiwango cha maji yanayosambazwa majumbani eneo hili,” akasema Bw Wainaina.

Yaibuka uwanja wa ndege hutegemea vibuyu kuchota maji

Na KALUME KAZUNGU

WAFANYAKAZI katika uwanja wa ndege wa Manda, Kaunti ya Lamu hulazimika kuchota maji kwa vibuyu kutoka visimani kwa matumizi uwanjani humo unaokumbwa na uhaba mkubwa wa maji.

Uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo umebaini kuwa wafanyakazi kwenye uwanja huo wa ndege hutumia mitungi kusafirisha maji kwa mashua kutoka visima vya Shella hadi kwenye uwanja huo wa ndege wa Manda ambao ni umbali wa karibu kilomita 10.

Baadhi ya wafanyakazi waliozungumza na wanahabari na kudinda kutaja majina yao kwa kuhofia kufutwa kazi walisema tatizo hilo la maji lilianza karibu miezi miwili unusu iliyopita.

‘Mara nyingi tunalazimika kuamka alfajiri na kwenda kujaza maji kwa mitungi katika visima vya Shella. Baadaye tunaisafirisha kwa boti au mashua hadi kwenye uwanja wa ndege wa Manda,” akasema mmoja wa vibarua.

Vibarua kwenye uwanja wa ndege wa Manda wakisambaza maji vyooni na sehemu zingine. Uhaba wa maji unaendelea kukumba eneo hilo. PICHA/KALUME KAZUNGU

Wasafiri waliohojiwa pia walikiri kukumbwa na kipindi kigumu kila wanaposhuka uwanjani humo hasa tangu tatizo la maji lilipoanza kushuhudiwa.

Akijibu suala hilo, Mkurugenzi Mkuu wa Halmashauri ya Viwanja vya Ndege (KAA) Ukanda wa Pwani, Peter Wafula, alisema uhaba wa maji kwenye uwanja huo huenda umechangiwa na kupungua kwa kiwango cha maji kinachosambazwa kwenye kisiwa cha Manda na Bodi ya Kusambaza Maji ya Lamu (LAWASCO) hasa tangu msimu wa kiangazi ulipoanza eneo hilo.

Bw Wafula, aidha alisema uhaba huo wa maji haujaathiri pakubwa shughuli za kila siku katika uwanja huo wa ndege kwani wamekuwa wakitumia mbinu mbadala, ikiwemo kusafirisha maji kwa boti kutoka eneo la Shella hadi Manda kila mara.

Naye Meneja wa LAWASCO, Kimani Wainaina, alitaja kukauka kwa baadhi ya visima kwenye bwawa la Shella hasa tangu msimu wa kiangazi ulipoanza Lamu kuwa changizo kuu linalopelekea kiwango cha maji kinachosambazwa sehemu nyingi za Lamu, ikiwemo Uwanja wa Manda kupungua.

Mara nyingi wamekuwa wakiepuka kutumia vyoo kwani baadhi ni vichafu. PICHA/ KALUME KAZUNGU

Bw Wainaina pia alitaja hitilafu ya umeme ambayo imekuwa ikishuhudiwa mara kwa mara eneo la Lamu katika siku za hivi karibuni kuwa sababu mojawapo ya maji kukosa kusambazwa inavyostahili katika miji na vijiji vya Lamu.

‘Pia ningesihi KAA kukarabati mabomba yake ya maji kutoka Shella hadi uwanja wa ndege wa Manda kwani ni ya zamani na yanaathiri kiwango cha maji kinachosambazwa eneo hilo,” akasema Bw Wainaina.

Ali Zubeir alisema mara nyingi wamekuwa wakiepuka kutumia vyoo kwani baadhi ni vichafu. ‘Kuna vingine hata vimefungwa kutokana na ukosefu wa maji. Hiyo inamaanisha ukitaka kutumia choo lazima usubiri mwenzako,’ akasema Bw Zuberi.

Bomba lililochakaa lasababisha uhaba wa maji Pwani

Na WINNIE ATIENO

TATIZO la uhaba wa maji unaokumba maelfu ya wakazi wa Pwani kila mara, husababishwa na kutegemea bomba lililojengwa mnamo 1953.

Shirika la Maji la Pwani (CWWDA), lilisema bomba hilo la urefu wa kilomita 220 kutoka chemchemi ya Mzima, Kaunti ya Taita Taveta halina uwezo wa kusambazia maji wakazi wote wa Pwani kwa mpigo, na hupasuka mara kwa mara kutokana na kuchakaa kwake.

Bomba hilo husambaza asilimia 75 ya maji safi kwa wakazi wa Kilifi, Kwale na Mombasa.

“Tunataka kufahamisha umma kwamba bomba la maji la urefu wa kilomita 220 kutoka Mzima lililojengwa 1953 limezeeka na kuharibika, kupasuka kila wakati na kumwaga maji. Bomba hilo haliwezi kusafirisha maji ya kutosha kusambaziwa wakazi ambao idadi yao inazidi kuongezeka,” alisema Afisa Mkuu Mtendaji wa CWWDA, Jacob Torutt.

Shirika hili husambaza maji kutoka chemchemi ya Mzima kwa vipimo katika mpango uliokubaliwa na wasimamizi wa maji wa kaunti za Mombasa na Kilifi.

“Mpango wa kusambaza maji kwa vipimo katika laini ya Mazeras–Rabai unatekelezwa na kituo cha CWWDA huko Mazeras. CWWDA husambaza lita 6 milioni za maji kila siku kwa kampuni ya maji ya Kilifi–Mariakani na lita 10 milioni kwa siku kwa kampuni ya maji ya Mombasa,” alieleza Bw Torutt.

CWWDA imeweka mpango wa kusambaza maji unaoshirikisha kampuni tano za maji ambazo ni Mombasa, Kilifi-Mariakani, Malindi, Kwale na Taita-Voi.

Bw Torutt alisema jukumu la kampuni hizo ni kuhakikisha usawa katika usambazaji wa maji katika maeneo yao baada ya CWWDA kuzisambazia bidhaa hiyo.

Alisema shirika hilo huwa linafahamisha kampuni hizo kukiwa na hitilafu katika usambazaji wa maji.

“Kampuni hizo nazo zinafaa kufahamisha wateja wa maeneo yanayoathiriwa,” alisema na kuongeza kuwa CWWDA haipendelei kampuni yoyote.

Bw Torutt alishtumu kuharibiwa kwa mabomba ya maji na waandamanaji mnamo Januari 27 eneo la Mazeras, ambako kulisababisha hasara kubwa.

“CWWDA haina malalamishi yoyote kutoka kwa waandamanaji. Hata hivyo ilidaiwa kwamba walilenga CWWDA kwa kukataa kusambaza maji eneo la Rabai. Tunaomba wananchi wakome kuharibu mabomba ya maji,” akasema afisa huyo.

Wakazi wa Kilifi walalamika kutembea kilomita 10 kutafuta maji

MAUREEN ONGALA na ANTHONY KITIMO

WAKAZI wa Kaunti ya Kilifi wanalalamika kwamba wanaendelea kutozwa pesa na Kampuni ya Maji ya Mariakani (KIMAWASCO) ilhali wamekuwa wakitembea kwa zaidi ya kilomita 10 kutafuta bidhaa hiyo muhimu.

Hii ni licha ya kwamba, kampuni hiyo iliwasambazia maji kwenye maboma yao ambayo sasa hayana hata tone moja. Wakazi hao wa vijiji vya Kaptukuz, Ganze, Kaloleni na Magarini sasa wanahofia kuambukizwa magonjwa yanayotokana na uchafu kwa kuwa wanalazimika kuteka maji kwenye visima vya wazi ambavyo pia hutumika kuwanyeshwa mifugo.

Wakazi hao wanataka Kimawasco ikome kuwatoza Sh411 kwa mwezi kwa kuwa hawajapata maji kwa zaidi ya miezi minne.

“Tunalipia maji ilhali mifereji yetu ni mikavu kwa zaidi ya miezi minne. Kila mwezi wanatutumia bili ya Sh410 jambo ambalo halikubaliki kamwe. Kwa nini wanakusanya ada za kila mwezi ilhali maji hatuna?” akasema mkazi wa Kaptukus, Khadija Kadzo.

Wakazi hao walisema wanashuku kampuni chache zinazopatikana katika kaunti hiyo zimeelekeza maji kwao na kusababisha ukosefu huo.

“Tunatumia bomba moja pamoja na kampuni zinazopatikana hapa. Tumejaribu kurai wasimamizi wa kampuni hizi kutuachia maji hata kwa siku nne pekee kwa wiki lakini hawajali kwa sababu bomba hilo liko kwenye eneo kunakopatikana kampuni zao na hatuwezi kuwadhibiti,” akasema Mkurugenzi wa Kimawasco Hezekiah Mwaura.

“Madai kwamba baadhi ya kampuni zimeelekeza maji upande wao si ya kweli ila nitachunguza na usimamizi wetu upande wa Mariakani kubaini msingi wa madai hayo,” akaongeza.

Katika kijiji cha Bomani, Kaunti ndogo ya Magarini, wanawake hulazimika kupiga foleni ndefu na kukesha usiku wakiteka maji kutoka kwa visima vilivyochimbwa na wenyeji.

Ukosefu wa maji Eastleigh wapandisha bei hadi Sh50 kwa mtungi

Na PETER CHANGTOEK

UKOSEFU wa katika mitaa mingi jijini Nairobi, umekuwa ukiwatatiza mno wakazi wa mitaa husika. Watu wengi wamekuwa wakitatizika sana katika mitaa kama vile Eastleigh, Pangani, Ngara, South B, South C na Nairobi West.

Wengi hulazimika kuyanunua maji kutoka kwa wauzaji wanaobeba kwa mikokoteni, licha ya kuwa baadhi ya wauzaji hao huwa hawazingatii usafi unaofaa.

Hata hivyo, wengi wa wauzaji wa maji hayo huvuna pakubwa kutokana na changamoto hiyo ya ukosefu wa bidhaa hiyo, ambayo ni muhimu kwa uhai wa wanadamu.

Kwa mujibu wa baadhi ya wauzaji wa maji wanaoitumia mikokoteni kuyasambaza maji kwa wakazi wa mitaa kadha wa kadha jijini Nairobi, bei ya maji huwa juu katika mitaa mingineyo, kama vile Eastleigh.

“Sisi huuza kwa bei ya Sh50 kwa mtungi mmoja wa lita ishirini,” akadokeza mwuzaji mmoja, ambaye huyauza maji katika mtaa wa Eastleigh, kwa kuutumia mkokoteni.

Wengi wao huyanunua maji kutoka mtaani Majengo, Pumwani, kwa jumla ya Sh40-Sh70 kwa mkokoteni mmoja ulio na mitungi 30 hadi 70. Hii yamaanisha kuwa wao huuziwa maji mtungi mmoja wa lita 20 kwa Sh1, na wao hupata faida ya Sh49, kwa mtungi mmoja, wauzapo kwa Sh50, na endapo watayauza kwa Sh40, hupata faida ya Sh39 kwa mtungi mmoja.

Kwa jumla, wauzaji hao wa maji hupata faida ya Sh1,950-Sh2,450 kwa mkokoteni mmoja wenye maji mitungi ishirini.

Wakazi wengi waliozungumza na Taifa Leo Dijitali, waliomba serikali kusaidia kulitatua tatizo la maji ambalo limekuwa likiwakumba kwa muda mrefu sana.

Afueni kwa wakulima wa Laikipia mradi wa uchimbaji wa mabwawa ukianza

Na SAMMY WAWERU

Zaidi ya wakulima 500 Laikipia wanatarajia kunufaika kufuatia mradi wa uchimbaji wa mabwawa ya kuvuna maji kupitia ufadhili wa serikali ya kaunti hiyo.

Kwenye mahojiano ya kipekee na Taifa Leo, Waziri wa Maji, Mazingira na Raslimalihai, Laikipia, Bw Njenga Kahiro amesema shughuli za uchimbaji wa mabwawa hayo zinatarajiwa kuanza kabla ya mwezi Februari 2021.

Amesema mradi huo wa kufanikisha uvunaji maji unalenga kupiga jeki wakulima Laikipia na kuimarisha sekta ya kilimo.

“Tunataka kuinua wakulima ili waendelee kubuni nafasi za ajira,” Bw Kahiro akasema.

Alidokeza kwamba bwawa moja linatarajiwa kugharimu kima cha Sh300, 000.

“Mradi huu utaendeshwa katika wadi mbalimbali Laikipia, na kwa sasa tumelenga wakulima 500. Tunapania kuchimbia kila mmoja bwawa linalositiri lita milioni 2 za maji,” Waziri huyo akaelezea, akisema hatua hiyo itasaidia kuangazia uhaba na ukosefu wa maji Laikipia.

Kaunti ya Laikipia ni kati ya kaunti kame nchini. Serikali ya kaunti hiyo imekuwa ikifanya ziara kwa wakulima wanaofanya kilimo cha kipekee.

Baadhi ya wakulima wamekumbatia mfumo wa kuvuna maji kwa mabawa na pia kwa kutumia matenki, huku wakitumia mifereji kunyunyizia mashamba na mimea maji.

Licha ya mahangaiko ya maji, Kaunti ya Laikipia ni miongoni mwa wazalishaji wa mimea inayochukua muda mfupi kama vile nyanya, vitunguu, viazi, kati ya mingineyo.

Afisa wa serikali apondwa kutangatanga akijipigia debe kwa miradi ya maji

 

NA MWANGI MUIRURI

KATIBU katika Wizara ya Maji Joseph Wairagu ameteswa na wanasiasa katika Kaunti ya Murang’a kwa madai ya kutumia miradi ya serikali kujipigia debe akilenga kutwaa ugavana wa kaunti hiyo 2022.

Analaumiwa kuweka mabango ya kuelezea miradi ya maji ambayo serikali inazindua katika kaunti hiyo yakiwa na maandishi bunifu ya kumpa umaarufu miongoni mwa wapiga kura wa Murang’a.

Katika kibango kimoja kilicho katika eneo la Nginda katika Kaunti Ndogo ya Maragua na ambacho kimezua malalamishi tele, Bw Wairagu amejiweka kama mwajiri wa mradi huo wa maji ya Maragua na ambao ulizinduliwa miezi mapema mwaka huu na Waziri wa Usalama wa ndani, Dkt Fred Matiang’i.

Wanaongoza kampeni zake katika eneo hilo wamezindua hatrakati za kusajili vibarua katika mradi huo wakliwaambia Bw Waioragu ndiye mwaajiri wao ilihali mwanakandarasi Sinohydro kutoka Uchina ndiye mwenye hela za kulipa.

“Mimi ninashindwa ni nini kinamsumbua huyu mfanyakazi wa serikali. Anarandaranda hapa Murang’a akiweka mabango yaliyo na jumbe za kupotosha akilenga kujipa umaariufu wa bwerere badala ya azingatie kazi aliyopewa na Rais Uhuru Kenyatta,” akateta gavana Mwangi wa Iria.

Alimkumbusha Bw Wairagu kuwa ni hatia katika sheria za uchaguzi kujipigia debe kisiasa ukitumia rasilimali za serikali.

Hata hivyo, Bw Wairagu amejipa uungwaji mkono wa Seneta wa Murang’a, Irungu Kang’ata ambaye aliambia Taifa Leo kuwa “sioni shida kubwa kwa Wairagu kujiangazia kama mwenye miradi hiyo.”

Alisema kuwa kwa sasa Wairagu akiwa ndiye Katibu maalum wa maji anafaa kupewa fursa ya kusambaza miradi Murang’a bila kukwamizwa na masuala ya tetesi kuhusu mabango.

“Mimi sijaona shida kubwa katika hali hii…tuzingatie kupata maji wala sio maandishi katika mabango,” akasema.

Bw Kang’ata ambaye pia analenga kuwania ugavana wa Murang’a 2022 hushirikiana na Wairagu katika ziara za Kaunti kukagua miradi na husemwa kuwa huenda wakawania pamoja, mmoja akiwa Naibu gavana.

Wengine ambao wamejikusanya pamoja kuwania ugavana wa Kaunti hiyo ambapo Wa Iria atastaafu 2022 baada ya kuhudumu kwa miaka 10 ni aliyekuwa mbunge wa Kigumo, Jamleck Kamau.

Kamau aliwania ugavana 2017 lakini akashindwa na Wa Iria katika mchujo wa Jubilee.

Katika mrengo wa Kamau kuna Mkurugenzi wa Shirika la Ahadi Kenya, Stanley Kamau, aliyekuwa Seneta wa Murang’a Kembi Gitura na aliyekuwa Naibu Gavana Gakure Monyo.

Wote wamesema kuwa wangetaka kampeni za wadhifa huo zizingatie sheria na kusiwe na wengine ambao watakiuka masharti ya uchaguzi ili kujipa guu mbele.

“Sisi tungependa sana serikali ya Rais Uhuru Kenyatta iafikie malengo yake ya kimaendeleo hasa katika safu ya usambazaji maji mashinani. Lakini hatutaki kuwe na mmoja wetu ambaye atapinda au avunje sheria ili ajipe umaarufu wa miradi ya rais,” wakasema katika taarifa ya pamoja Wikendi iliyopita wakiwa katika hospitali ya Kiria-ini walipopeleka misaada ya chakula na mavazi spesheli ya madaktari katika mapambano na janga la Covid-19.

Sato Tap, ubunifu wa kisasa wa kunawa mikono

NA MWANDISHI WETU

Sato, biashara ya kijamii ya Kikundi cha LIXIL kutoka Japan ambayo inakusudia kutatua shida za maji, usafi wa mazingira humu nchini kwa kutoa mifumo ya bei rahisi kwa jamii kote ulimwenguni, imeanzisha mpango wa kunawa mkono kwa jina ‘Sato Tap’.

Kulingana na Hazina ya Watoto ya Umoja wa Mataifa (UNICEF), asilimia 40 ya watu ulimwenguni hawana vifaa vya kunawia mikono nyumbani.

Nchini Kenya, asilimia 29 pekee ndio wenye uwezo wa kuishi kwenye mazingira safi, wakati asilimia 41 ya watu hawana maji.

Ili kusuluhisha changamoto hii, LIXIL imetenga Sh100 milioni kusaidia mashirika wa maendeleo ambayo yanaweza kuwasaidia watu milioni 5 kuboresha kunawa mikono.

“Hali ya Covid-19 imezua uhaba mkubwa wa maji, usafi wa mazingira, na usafi kwa jamii barani Afrika na kimataifa. Tunajua kwamba kunawa mikono kwa sabuni ni mojawapo ya hatua madhubuti dhidi ya maambukizi ya magonjwa,” alisema Erin McCusker, Mkuu wa Sato.

“Kwa kuleta muundo na utaalam wa uhandisi wa Sato, pamoja na msaada wa LIXIL, tunakusudia kuharakisha uvumbuzi huu mpya wa mikono kwa soko, na kuifanya iwepo kwa jamii kwa kuimarisha mabadiliko ya usafi.”

Sato ilifanya kazi na washirika wakati wa mchakato wa kubuni, kupokea pembejeo muhimu za kiufundi na kusaidia kuhalalisha ufanisi wa muundo wa Sato Tap unaotumia chupa za plastiki zinazopatikana kwa urahisi.

Sato Tap inaweza kutumika ndani ya nyumba na kama kituo cha kuosha mikono katika maeneo ya umma. Ina ubunifu wa kipekee ambao unapunguza kukaribiana kati ya mtumiaji na bomba, na hivyo kupunguza kuenea kwa magonjwa, wakati inapunguza matumizi ya maji.

Mbali na Sato Tap,ushirikiano uliopo wa LIXIL na UNICEF utapanua shughuli ya kuhakikisha kwamba jamii ina uwezo wa kuwa na mazingira safi.

“Tunajua kuwa njia bora zaidi ya kupunguza kuenea kwa magonjwa ni kunawa mikono. Lakini kwa watoto na familia walio katika mazingira magumu zaidi na hatarishi, hatari ya  Covid-19 inaongezewa na ukosefu wa vifaa vya kunawia mikono, “alisema Kelly Ann Naylor, Mkurugenzi wa UNICEF.

Akihutubu kuhusu umuhimu wa suluhisho la ubunifu wa usafi, Daigo Ishiyama, Afisa Mkuu wa Teknolojia na Masoko katika Sato, alisema Sato Tap itasaidia kuibua mienendo itakayobadilisha maisha.

“Itaimarisha usafi na kuimarisha mabadiliko ya tabia ya kunawa mikono ili kupunguza hatari ya maradhi na kuhifadhi maji. Maoni yetu yanaambatana na Serikali na maoni ya vipaumbele vya Serikali ya Kenya kwa watu wake katika kuimarisha afya, ” alisema.

 

Kaunti kusambazia wakazi wa vitongojini maji

Na WINNIE ATIENO

SERIKALI ya Kaunti ya Mombasa imeanza kuweka mikakati kusambaza maji vitongojini ili kuimarisha afya za wakazi wa maeneo hayo.

Wakazi wa vitongoji duni wamekuwa wakikabiliana na hali ngumu ya maisha hasa ukosefu wa maji safi ya kunywa na hata kupikia.

Hali hii huwasababishia kuwa katika hatari ya maambukizi ya magonjwa hatari kama kipindupindu, kuendesha na hata kuumwa na tumbo.

Waziri wa kaunti anayesimamia maji na usafi Bw Tawfiq Balala amesema ufukara unachangia pakubwa hali hiyo.

“Ndiyo maana tumeanza kuweka mikakati kuimarisha maisha ya wasiojiweza katika vitongoji duni waweze kupata maji safi ili kuepuka magonjwa,” alisema Bw Balala.

Ametaja mitaa ya Muroto iliyoko Tudor kisiwani Mombasa kuwa mojawapo ya sehemu zinazolengwa sababu wakazi hawana maji safi.

Amesema wakazi hao wakipata maji safi wataepuka maradhi ambayo mara nyingi watoto ndio huwa hatarini zaidi.

“Wakazi wakipata maji, wanaweza kujiendeleza kifamilia na kibiashara na hata kupata mapato bora kuimarisha maisha yao lakini swala muhimu zaidi ni wakazi wapate maji safi, ” amesema Bw Balala.

Naibu Gavana wa Mombasa Dkt William Kingi amesema serikali ya kaunti inaendelea kuhakikisha wakazi wanapata maji wakati huu ambapo ulimwengu unakabiliana na janga la corona.

Shule za msingi Thika zapata matangi ya maji

Na LAWRENCE ONGARO

SHULE za msingi mjini Thika zimenufaika kwa kupata matangi ya maji ili kukabiliana na janga la Covid-19.

Mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina alisema wakati huu taifa linapopambana na homa ya corona ni vyema shule zote za msingi na hata za upili ziwe na maji ya kutosha.

“Kabla ya shule kurejelea shughuli zake ni vyema mikakati iwekwe ili kukabiliana na Covid-19,” alisema Bw Wainaina.

Alisema kati ya shule za msingi 32 mjini Thika, tayari 15 zimefanyiwa ukarabati kupitia fedha za hazina ya maendeleo za NG-CDF.

Alisema amefanya juhudi kuona ya kwamba baadhi ya shule hizo zimepokea matangi ya maji ya lita 10,000 kwa kila moja.

Alipendekeza serikali itathmini kwa makini hali ya mambo kabla ya kuruhusu wanafunzi kote nchini kurejea shuleni.

“Si neno hata shule zikifunguliwa Januari 2021. Aidha si vyema kujipata pabaya ghafla,” alifafanua Bw Wainaina.

Mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina akitandaza sakafu ya darasa mojawapo katika Shule ya Msingi ya Kamenu mjini Thika alipozuru kujionea jinsi inavyofanyiwa ukarabati. Picha/ Lawrence Ongaro

Ameitaka serikali kufanya juhudi kuona ya kwamba walimu wanapokea kiinua mgongo ili kuwapa motisha ya kuchapa kazi kwa bidii.

Baadhi ya shule ambazo tayari zimefanyiwa ukarabati wa kisasa ni Makongeni, Kimuchu, Kiganjo, Kilimambogo, Mbagathi, na Komo.

Mwalimu mkuu wa shule ya msingi ya Mbagathi Bw Muchemi Maguru, alipongeza juhudi za mbunge huyo kwa kujitolea na kuona ya kwamba shule karibu zote za msingi zinafanyiwa ukarabati.

“Wakati shule zitafunguliwa wanafunzi watafurahia mazingira mapya na tutaweza kuwahamasisha ili wawe na ufahamu zaidi kuhusu umuhimu wa kuzingatia usafi kujizuia kuambukizwa homa ya corona,” alisema Bw Maguru.

Alisema kwa muda mrefu shule nyingi za msingi hasa zile za Thika Mashariki zimepata shida ya maji.

“Hapo awali tulitafuta maji hadi mwendo wa kilomita tatu katika Mto Athi. Lakini kwa sasa shida hiyo itakwisha baada ya kupokea matangi ya maji,” alisema mwalimu huyo mkuu.

Alisema kutokana na janga la corona walimu watakuwa na kazi ya ziada kuwahamasisha wanafunzi kila mara kufuata maagizo ya Wizara ya Afya.

Watalazimika kuzingatia kunawa mikono kila mara, kuvalia barakoa, na kuweka nafasi ya umbali wa mita moja hivi kutoka mmoja hadi kwa mwingine.

Hata hivyo, changamoto kubwa ni wanafunzi kuwa wengi katika madarasa na wanapojumuika pamoja wakiwa michezoni na kwingineko.

“Wakati huu ushirikiano unahitajika baina ya walimu na wazazi pamoja na wanafunzi ili kukabiliana na janga hili la Covid-19. Kuna changamoto kubwa bado inayotusubiri,” alisema Bw Maguru.

Naye mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi ya Kilimambogo Bi Philis Kavura Ngige alisema walikuwa wakichota maji kutoka chuo cha walimu cha St Johns Kilimambogo, lakini sasa watajitegemea wenyewe.

Maji ya Bahari Hindi yafurika na kuenea katika makazi Lamu

Na KALUME KAZUNGU

NYUMBA nyingi zilizojengwa karibu na ufuo wa Bahari Hindi katika mji wa kale wa Lamu hazikaliki baada ya maji ya bahari kufurika na kuenea katika makazi.

Mafuriko hayo yanayosababishwa na kufura kwa maji ya Bahari Hindi hushuhudiwa mara moja kila mwaka hasa kila wakati kipindi cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kinapowadia.

Shughuli za usafiri na biashara zimekuwa zikitatizika juma hili kwani sehemu nyingi zinazotumiwa hasa na waendeshaji pikipiki, punda na mikokoteni katika eneo la Huduma Centre, Ofisi ya Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Kituo cha Matibabu ya Punda, eneo la Bunge la Kaunti ya Lamu na pia sehemu yote iliyoko mkabala na ufuo wa Bahari mjini humo yote yakijaa maji.

Baadhi ya wakazi wamelazimika kuhama nyumba zao kwa muda baada ya makazi yao kusombwa na maji hayo.

Katika mahojiano na Taifa Leo mjini Lamu, mmoja wa viongozi wa kidini, Ustadh Ahmed Alwy, ameeleza kuwa kutapakaa kwa maji hayo ni jambo la kawaida ambalo wamekuwa wakishuhudia tangu zama za mababu zao.

Kulingana na Bw Alwy, kutapakaa kwa maji ya Bahari Hindi hadi kwenye makazi ya binadamu ni kiashirio kwamba Bahari imefura kutokana na wingi wa maji yanayosababishwa na dhoruba na upepo, hasa ule wa kusi.

Kiongozi wa kidini, Ustadh Ahmed Alwy, aeleza kuhusu hali ambapo maji ya Bahari Hindi yamekuwa yakifurika na kuenea hadi katika makazi kisiwani Lamu Mei 12, 2020. Picha/ Kalume Kazungu

Kiongozi huyo wa dini amesema wakazi wa Lamu, hasa Waislamu wamekuwa wakitumia hali hiyo ya kutapakaa kwa maji ya Bahari Hindi kila mwaka kutambua nyakati na majira fulani ya Mwaka wa Kiislamu.

“Mafuriko haya ya maji ya Bahari Hindi si jambo la kustaajabisha kwetu sisi wakazi wa Lamu. Mara nyingi hali hii hushuhudiwa hasa katika kipindi cha mwisho cha mwezi wa Shaaban katika kalenda ya Kiislamu, ambapo huo ndio mwezi unaokaribisha Ramadhani. Licha ya maji kutapakaa hadi kwenye nyumba zetu, sisi hatuna cha kuhofia kwani baada ya muda maji hayo hupungua yenyewe,” akasema Bw Alwy.

Naye Bw Mohamed Abdulkadir amewasisitizia Waislamu na wakazi wote wa Lamu waombe kila mara msimu huo wa kushuhudiwa kwa maji ya mafuriko kutoka baharini hapo kisiwani Lamu.

Kulingana na Bw Abdulkadir, maji hayo mara nyingi huashiria neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

“Sisi wakazi wa Lamu huichukulia hali hii kuwa ni baraka kutoka kwa Mungu. Hii ndiyo sababu kila mara mafuriko hayo yanaposhuhudiwa, sisi viongozi wa kidini huwahimiza sana waumini kumuwelekea Mwenyezi Mungu na kuomba ili heri na neema zisipotee kwetu,” akasema Bw Abdulkadir.

UHABA: Foleni ndefu wachukuzi wenye mikokoteni wakitafuta maji mtaani Kariobangi South Civil Servants

Na GEOFFREY ANENE

SI kawaida kuona mamia ya mahamali kufika mtaani Kariobangi South Civil Servants kwa siku moja.

Hata hivyo, mambo yalikuwa tofauti Mei 10 pale wafanyabiashara hao wa kuchota maji na kuyauza walipomiminika katika kisima kimoja mtaani hapa kutokana na uhaba wa maji unaotatiza jiji la Nairobi.

Wengi waliofika hapa walitoka mtaa huu pamoja na mitaa jirani ya Mutarakwa, Kariobangi South, Dayspring, Doctor Mwenje, Gaza na Baraka na pia sehemu kadhaa za Umoja III.

Mitungi ya maji inaoshwa sokoni kabla ya kuuziwa wateja wakiwemo wachukuzi wenye mikokoteni. Picha/ Geoffrey Anene

Kutoka saa mbili asubuhi Jumapili hadi saa kumi na mbili na nusu jioni, shughuli ya kuhudumia wenye mikokoteni ilikuwa ni kibarua cha ziada kwa Bwana Ndegwa, ambaye ni mmiliki wa kisima hicho alichochimba Mei 2015.

Wateja hao walifika hapa na mitungi ya lita 20.

Wao huuziwa mtungi mmoja katika kisima hiki kwa Sh5.

Mmoja baada ya mwingine, waliwasili hapa, kila mmoja na mkokoteni uliojaa kati ya mitungi 20 na 30, ambayo wanauzia wateja kwa kati ya Sh30 na 40 kila mtungi.

Mkokotaji wa mkokoteni asafirisha mitungi ya maji ya lita 20 kuoshwa kabla ya kutumiwa na wachukuzi kuchota na kuuzia wateja katika mitaa ya Nairobi. Picha/ Geoffrey Anene

Mhudumu mmoja wa kisima hicho alieleza Taifa Leo kuwa kwa siku ya kawaida wao huuza kati ya lita 70,000 na 90,000 za maji kila siku.

“Leo ilikuwa siku tofauti kabisa kwa sababu tuliuza zaidi ya mara tatu ya lita tunazouza kila siku. Kuna visima kadhaa mbali na hiki hapa ambavyo wenyewe hawakufungua biashara. Pia, kuna uhaba wa maji jijini Nairobi. Kutoka Alhamisi, wakazi wamekuwa wakitatizika masuala ya maji, ingawa umati huu nimeushuhudia tu leo. Kutoka asubuhi sijapumzika kwa sababu ya foleni hii ndefu unaona hapa,” alisema mhudumu huyo, ambaye alifichua kuwa aliraushwa saa kumi na mbili asubuhi na mteja wa kwanza kabla ya foleni ya wenye mikokoteni kuanza kushuhudiwa dakika chache tu baada ya saa mbili asubuhi.

Watu wanne wasombwa na maji eneo la Ngoliba

Na LAWRENCE ONGARO

BAADA ya wakazi wanne kusombwa na maji katika mto Athi, eneo la Ngoliba Thika Mashabiki, wakazi wanaiomba Kaunti ya Kiambu usaidizi.

Mnamo Jumatano wakazi wanne wa kijiji cha Ngoliba walisombwa na maji walipokuwa wakivuka Mto Athi wakiwa kwenye boti.

Wakazi wa eneo hilo walisema ya kwamba walikuwa watu sita katika mashua hiyo lakini wawili miongoni mwao walijinusuru na wakaogelea hadi upande wa pili.

Mnamo Jumatano naibu gavana wa Kiambu Bi Joyce Ngugi alizuru kijiji hicho ambapo aliwahakikishia wakazi kuwa kaunti hiyo itajenga daraja la kuvukia upande wa pili.

Chakula kwa wakazi

Alisema serikali ya kaunti inapanga kusambaza chakula kwa wakazi wa eneo hilo.

Bi Ngugi aliwashauri viongozi waache kuingiza siasa katika shughuli hiyo ya kusambaza chakula.

“Sisi kama viongozi tunastahili kuugana na kusaidia wananchi bila kuegemea upande wowote,” alisema Bi Ngugi.

Alisema kaunti ya Kiambu itafanya juhudi kuona ya kwamba kila mwanachi anapata chakula bila kubaguliwa.

Aliwashauri madiwani, machifu na wazee wa vijiji kuketi pamoja na kupanga vizuri jinsi wananchi wanavyostahili kupewa chakula.

Bi Judy Nyaguthii Wang’ombe, alisema mwanaye wa kiume alisombwa na maji alipoungana wa wenzake watano kwenda kuvua samaki.

Hata hivyo, alisema ilidaiwa mawimbi mazito ndiyo yalisababisha sita hao kusombwa na maji.

Licha ya kikosi cha uokozi kufika eneo hilo kwa juhudi za kuokoa watu hao bado walishindwa kuwapata.

Lakini watu wawili pekee ndio walifanikiwa kujinusuru kutoka kwa mto huo ambao unavuma kwa kasi kubwa.

Alisema kwa muda wa siku tatu mfululizo mvua kubwa imenyesha katika eneo hilo.

Bi Wang’ombe alitoa mwito kwa serikali kuwatafutia ajira vijana wengi ambao hawana kazi ya kufanya.

“Kijana yangu alikuwa ana ujuzi wa kurekebisha umeme, lakini hajafanikiwa kupata kazi,” alisema Bi Wang’ ombe.

Wakazi wa kijiji hicho wanaiomba serikali iingilie kati mara moja kuona ya kwamba daraja la kisasa linajengwa ili watu waweze kuvuka kwa urahisi hadi upande wa pili.

Mvua kubwa yasababisha hasara Ruiru

Na LAWRENCE ONGARO

FAMILIA zaidi ya 200 katika vijiji vya Kimbo na Juja wameachwa na mahangaiko baada ya mvua kubwa kusababisha maji ya mafuriko kuingia katika nyumba zao.

Wakazi hao walisema usiku wa kuamkia Jumamosi walipata maji mengi ndani ya nyumba zao.

Kwa wakati huu wamebaki bila makazi maalum huku wakiomba serikali kuingilia kati ili kuwajali.

Mkazi wa Kimbo katika mji wa Ruiru, Kaunti ya Kiambu, Bi Jane Njeri alisema walirauka kuchota maji yaliyofurika katika nyumba zao.

“Nilirauka mwendo wa saa tisa za alfajiri na nikapata maji kwenye nyumba yangu. Sasa mali yangu yote imeloa maji huku nikishindwa jambo la kufanya,” alisema Bi Njeri.

Wakazi hao wanalaumu barabara kuu ya Thika Superhighway kwa sababu ndiyo inayosomba maji yote ya mvua hadi katika makazi yao.

“Wakati huu ndiyo viongozi wanastahili kujitokeza ili kusaidia wananchi walioathirika. Sasa tumeshindwa hata kuendesha biashara zetu. Tunaomba usaidizi wa dharura,” alisema.

Kwa muda wa wiki moja iliyopita mvua kubwa imenyesha kote nchini na kusababisha maafa mengi katika maeneo mengi.

Wakazi hao pia wanadai wezi wanaendelea kutekeleza wizi hata wakati huu mvua inaponyesha.

Mkazi wa Juja Bw James Mwangi alisema ilipofika usiku wa manane, kuamkia Jumamosi, alilazimika kukesha hadi asubuhi baada ya maji kufurika katika nyumba yake.

“Sisi wakazi wa hapa Juja tumepata hasara kubwa kabisa kwa sababu biashara nyingi zimekwama. Sasa tunaomba serikali kuingilia kati ili kutusaidia,” alisema Bw Mwangi.

Naye mkazi wa kijiji cha Kimbo, Ruiru Bi Jane Wangari alisema biashara nyingi zimekwama baada ya mafuriko hayo kushuhudiwa.

“Wakazi wa kijiji chetu wameathirika kabisa ambapo serikali inastahili kutusaidia ili tuendelee na shughuli zetu,” alisema Bi Wangari.

Alisema hata mifugo yao imeathirika ambapo wanakosa malisho maalum kufuatia mvua hiyo.

Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa imesema mnamo wikendi kwamba mvua nyingi inayoshuhudiwa kote nchini itaanza kupungua Mei 1, 2020.

Lamu yaanza kufufua visima vya kale

NA KALUME KAZUNGU

SERIKALI ya Kaunti ya Lamu imeanzisha mpango wa kufufua visima vya kale, ikiwemo vile vya miaka 100 na zaidi ili kuongeza kiwango cha usambazaji maji eneo hilo katika harakati za kukabiliana na janga la Covid-19.

Afisa Mkuu wa Idara ya Masuala ya Huduma za Jamii, ambaye pia anasimamia Idara ya Biashara, Utalii, Uwekezaji na Utamaduni eneo hilo, Atwa Salim, alisema kufikia sasa tayari wametambua visima vipatavyo 15 kwenye maeneo ya Kibaki Grounds, Jua Kali, Kinooni, Kanu, Manda-Okoe, Langoni, Gadeni, Kashmir na sehemu zingine ambapo tayari shughuli ya kuvifufua visima hivyo inaendelea.

Aliwataka wananchi kote Lamu kutoa ripoti kwa idara yake endapo wako na ufahamu wa visima zaidi vinavyohitaji kufufuliwa ili kuongeza usambazaji maji eneo hilo.

“Kutokana na kupanda kwa uhitaji wa maji ambayo msimu huu wa Corona yanatumika kwa wingi ili kudumisha usafi wa miili na mazingira yetu, serikali ya kaunti imeafikia kufufua visima vyote vya kale vilivyosahaulika.

“Tuko na visima vingi eneo hili ambavyo vimedumu kwa zaidi ya karne moja lakini bado viko na maji safi. Tumeamua kuvisafisha ili kutoa maji kwa mitaa inayokabiliwa na changamoto za rasilimali hiyo. Wakazi, ikiwemo maskini watakuwa wakipata maji ya bure kutoka kwa visima hivyo. Tayari tumeanza kushughulikia visima vipatavyo 15 eneo hili,” akasema Bw Salim.

Baadhi ya visima vya kale ambavyo serikali ya kaunti inafufua ili kupata maji ya kukabiliana na Covid-19 kaunti ya Lamu. Picha/ Kalume Kazungu

Meneja wa Bodi ya Kusambaza Maji, Kaunti ya Lamu (LAWASCO), Bw Paul Wainaina, alisema ofisi yake inashirikiana kwa karibu na serikali ya kaunti katika mpango huo wa kufufua visima vya zamani.

Alisema juma hili ofisi yake itatoa dawa za kutibu visima vyote vitakavyofufuliwa ili kutoa maji ya kusaidia kukabiliana na Coronavirus.

“Tunashirikiana kufanikisha mpango huo wa kufufua visima vya kale kote Lamu. Juma hili LAWASCO itatoa dawa aina ya chlorine ili kunyunyiza visima vyote vitakavyofufuliwa ili maji yawe salama kwa matumizi ya binadamu,” akasema Bw Wainaina.

Kwa upande wake, Afisa msimamizi wa mradi huo wa ufufuzi wa visima vya kale, Abdulaziz Sadique, aliusifu mpoango huo wa kaunti, akisema utasaidia pakubwa watu wa tabaka la chini kupata maji kwa urahisi.

Miongoni mwa wanaolengwa kunufaika na mradi huo ni wahudumu zaidi ya 200 wa soko la manispaa ya Lamu ambao hivi majuzi walihamishwa kutoka eneo la Mkunguni hadi Kibaki Grounds katika harakati za kutafuta nafasi mwafaka ya wanabiashara kudhibiti umbali wa mita moja ili kuepuka maambukizi ya Covid-19.

“Mahali kama vile Kibaki Grounds kumekuwa na changamoto ya maji. Eneo lile hata hivyo limezingirwa na visima vingi vya kale. Ninaamini vikifufuliwa wahudumu 200 walioko sehemu ile watanufaika pakubwa,” akasema Bw Sadique.

 

Thiwasco yashirikiana na kaunti kuweka vituo vya usafi Thika

Na LAWRENCE ONGARO

WANANCHI mjini Thika wameanza kuzingatia hali ya usafi kwa kunawa mikono kila mara baada ya vituo vitano vya kunawa mikono kuwekwa.

Kampuni ya Thiwasco Water Company Ltd imezindua mikakati ya kuwawekea watumiaji vituo vitano vya kunawa mikono kwa juhudi za kukabiliana na COVID-19.

Mkurugenzi wa kampuni hiyo Bw Moses Kinya amesema hiyo ni njia mojawapo ya kuwapa wananchi matumaini ya kukabiliana na COVID-19.

“Kampuni yetu imechukua hatua hiyo kwa ushirikiano na Kaunti ya Kiambu, ili tuweze kupambana na COVID-19,” amesema Bw Kinya.

Amesema maafisa wake wameweka vituo hivyo katika maeneo tofauti mjini Thika ambako watu wengi hujumuika.

Eneo la kwanza ni katika hospitali kuu ya Thika Level Five ambapo kuna mifereji miwili ya maji safi ya kutumika wakati mtu ananawa na kusafisha mikono.

Kituo cha pili ni katika kituo cha Polisi cha Thika.

Halafu Soko kuu la Jamhuri kuna mifereji na pia katika lango kuu la kuingia kampuni ya Thiwasco Water Company Ltd.

Janga la COVID-19 limegeuza mawazo, tabia na mienendo ya wananchi kuhusu usafi huku kila mahali pa biashara watu wakiwekewa jeli spesheli ya kunawa mikono ambayo inaua viini.

Maeneo yanayozingatia usafi kamili ni mikahawa na kweye maduka.

Wakazi wengi waliohojiwa wamepongeza juhudi za kampuni ya Thiwasco Water Company Ltd kwa kuletea watu maji kwa wingi katika kila kona.

“Tumefurahia hatua hiyo kwani kila mmoja atajichunga mwenyewe kwa kunawa bila kulazimishwa. Hiyo ni njia moja ya kuzingatia usafi,” amesema Bw Peter Macharia ambaye ni mkazi wa Thika.

Kutokana na janga hilo la COVID-19 kila mwananchi yuko chonjo ambapo hakuna yeyote angetaka kuchezea afya yake.

Hata ingawa sio matatu nyingi zinazingatia kunawisha wasafiri lakini wengi wa wasafiri wanaonekana kufungua madirisha wakiingia katika matatu.

“Mimi ninapoingia ndani ya matatu ninahakikisha kuwa ninafungua dirisha ili hewa safi iingie. Sasa hakuna kuleta mchezo kwa sababu jambo hili ni hatari,” amesema John Kimani ambaye alikuwa kwenye matatu moja ya kutoka Thika kuelekea Ruiru.

Uchunguzi uliofanywa umebainisha ya kwamba jeli ya kunawa – Sanitiser – imepungua sana katika supamaketi baada ya wateja wengi kununua kwa fujo.

Imebainika kuwa hakuna mwananchi yeyote anayechukua jambo hilo kwa mzaha kwa sababu kila mara mtu anatamani kunawa mikono.

Lawama kwa Lapsset uhaba wa maji safi na salama Lamu

Na KALUME KAZUNGU

BODI ya Kusambaza Maji, Kaunti ya Lamu (Lawasco) imenyooshea kidole cha lawama ujenzi unaoendelea wa mradi wa Bandari ya Lamu (Lapsset) kwa kusababisha uhaba mkubwa wa maji ambao umekuwa ukishuhudiwa kwenye baadhi ya miji eneo hilo siku za hivi karibuni.

Wiki iliyopita, mamia ya wakazi wa mji wa Mokowe na viungani mwake waliandamana barabarani na kufululiza hadi ofisi za Lawasco na pia makao makuu ya Kaunti ya Lamu mjini Mokowe kushinikiza serikali ya kaunti kutatua tatizo la maji walilodai limedumu eneo hilo kwa zaidi ya muda wa miezi mitano.

Katika mahojiano na ‘Taifa Leo’ ofisini mwake, Meneja wa Lawasco, Bw Paul Wainaina amesema Jumatano tangu mradi wa ujenzi wa Lapsset kuanzishwa eneo hilo, visima vingi vimeishia kukauka ilhali vingine maji yake yamegeuka kuwa ya chumvi kutokana na kutumiwa sana kwenye ujenzi huo unaojumuisha viegesho vitatu vya kwanza vya Lapsset.

Bw Kimani amesema tangu jadi, miji mingi ya Lamu, ikiwemo Mokowe, Hindi na viunga vyake, imekuwa ikitegemea maji ya visima ambavyo vilichimbwa tangu miaka ya 1990.

Alisema ujio wa Lapsset umesababisha maji mengi kupita kiasi kutumiwa kutoka kwa visima hivyo ili kutekelezea ujenzi wa mradi huo, hatua ambayo sasa imechangia kukauka kwa visima hivyo ilhali vingine vikitoa maji ya chumvi ambayo hayawezi kutumiwa na binadamu.

“Ninakubali malalamishi ya wakazi kwamba miji yao haina maji, lakini Lawasco inajitahidi kufikisha maji majumbani,” akasema Bw Wainaina.

Akaongeza: “Isitoshe, miji kama vile Mokowe tangu jadi imekuwa ikitumia maji ya visima. Tangu ujenzi wa viegesho vitatu vya Lapsset kuanza, visima hivyo pia vimekuwa vikitegemewa kusambaza maji ya kutekelezea ujenzi huo. Hii ndiyo sababu visima vingi vimekauka ilhali vingine vikitoa maji ya chumvi kutokana na kutumiwa sana kupita kiasi.”

Afisa huyo aidha amesema serikali ya Kaunti ya Lamu iko mbioni kuchimba visima vipya kwenye maeneo mbalimbali ya Lamu, ikiwemo Belebele na Hongwe ili kusaidia kukabiliana na uhaba huo wa maji unaokumba wakazi.

Amesema kaunti kwa ushirikiano na wafadhili mbalimbali na serikali kuu pia wako mbioni kujenga mitambo ya kusafisha maji ya chumvi na kuyagauza kuwa safi kwa matumizi ya binadamu katika harakati zake za kukabiliana na uhaba wa maji Lamu.

Bw Wainaina aidha ameisihi serikali kuu kutoa fedha za kusaidia katika usawa na maendeleo ya maeneobunge (Equalisation Funds) ili kusaidia kutekeleza miradi hiyo ya maji eneo la Lamu.

“Mbali na kuchimba visima, kaunti ikishirikiana na wafadhili mbalimbali pamoja na serikali kuu pia wako na mpango wa kuanzisha mitambo ya kusafisha maji ya chumvi kutoka Bahari Hindi ili yawe safi kwa matumizi ya binadamu. Ombi langu kwa serikali kuu ni kwamba waharakishe utoaji wa fedha za usawa na maendeleo ya maeneo bunge ili kusaidia kufaulisha miradi yetu ya maji hapa Lamu,” amesema Bw Wainaina.

Wakazi wa Thika wapata maji kwa wingi

Na LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa Landless, Thika na maeneo ya karibu wamepata afueni baada ya kuletewa maji kwa wingi katika makazi yao.

Kikosi cha jeshi cha 12th Engineering Batalion, kwa mapatano na mbunge wa Thika Bw Patrick Wainaina kilifanikisha juhudi hiyo ya kupata maji.

Maji hayo yalichimbwa na kikosi hicho kwa siku mbili pekee kabla ya maji hayo kuonekana.

Bw Wainaina alisema alilazimika kuzungumza na kikosi cha jeshi kwa sababu wao wana uwezo wa kuchimba maji katika maeneo tofauti nchini.

“Ninapongeza juhudi za wanajeshi hao ambao walionyesha ujasiri wao kwa kufanya kazi hiyo mara moja bila kusita. Nimeridhika kwa sababu wakazi wa Thika sasa watanufaika na maji safi,” alisema Wainaina.

Alisema baadhi ya mitaa itakayonufaika pakubwa na maji hayo ni Landless, Gatundu, Muguga, na Ngoliba.

Alisema baada ya wakazi hao kupitia shida hiyo ya maji sasa atafanya juhudi kuona ya kwamba barabara za kisasa zinakarabatiwa ili waweze kuendesha biashara zao bila matata.

Afisa mkuu wa jeshi kikosi cha 12th Batalion Brigadier Geoffrey Radina, alisema maji hayo yatazidi kunywewa kwa muda mrefu na wakazi wa Thika.

“Sisi tayari tumefanya kazi yetu na sasa kilichobaki ni wananchi walinde mali yao ili wahalifu wasije wakaiba vifaa vilivyo hapo,” alisema Bw Radina.

Alisema kikosi chao cha Engineering Batalion kinafanya kazi kila sehemu nchini na kwa hivyo wameridhika na kazi hiyo waliyofanya.

Alieleza ya kwamba mradi huo umegharimu takribani Sh720 milioni, huku ukiwa ni wa kima cha urefu wa mita 130 ambapo ni fiti 400.

Mkurugenzi wa kampuni ya maji ya Thiwasco Water Company Ltd Bw Moses Kinya alisema kampuni hiyo itafanya juhudi kuona ya kwamba maji hayo yamefanyiwa ukaguzi maalum katika maabara ili kuhakikisha ni safi kwa binadamu.

Mbunge wa Thika Bw Patrick Wainaina ahutubu. Picha/ Lawrence Ongaro

Alisema watalazimika kuona ya kwamba wanaweka mabomba za kisasa za kusambaza maji katika mitaa tofauti.

“Tayari Benki ya Dunia imewasilisha Sh764 milioni kwa kampuni ya Thiwasco Water Company Ltd ili kujenga kituo cha kusambaza maji katika eneo la Mary Hill Mang’u,” alisema Bw Kinya.

Alisema kuongezeka kwa wakazi wa Thika kumewapatia changamoto kubwa na hivyo kutakikana kutafuta mbinu ya kuongeza maji kwa wingi.

Bi Stella Njeri ambaye ni mkazi wa mtaa wa Landless amefurahia kupata maji katika nyumba yake akisema shida ya zaidi ya miaka sita imekwisha.

“Kwa muda mrefu sasa sisi kama wakazi wa eneo hili tumepata shida kubwa ya maji lakini kwa huruma wa mbunge wetu sasa tuna maji,” alisema Bi Njeri na kuongeza “tutahakikisha tunalinda eneo hili lisije likavamiwa na wezi wa vifaa vya maji”.

Ukosefu wa maji washuhudiwa Thika

Na LAWRENCE ONGARO

MAENEO mengi mjini Thika yanaendelea kukosa maji safi ya kunywa huku wakazi wakitaka kampuni ya Thiwasco Water Company Ltd kuingilia kati kutoa suluhisho.

Wakazi wengi wamekuwa wakilalamika kuwa mitaa wanakoishi zinakosa maji huku wakilazimika kutafuta maeneo mengine ama kununua kwa wachuuzi.

Mitaa iliyoathirika kutokana na ukosefu huo ni Landless, Muguga na Kisii mjini Thika.

Bw Joseph Kimani wa mtaa wa Landless, Thika, anasema watu wachache wamechimba maji ya visima lakini anadai maji hayo sio safi ya kunywa kwa sababu yanaonja chumvi.

“Wakazi wengi wa hapa wamekuwa na matatizo ya maji kwa muda mrefu na kwa hivyo tunaiomba kampuni ya Thiwasco Water Company Ltd waingilie kati kuona ya kwamba wanasambaza maji hadi maeneo haya,” alisema mkazi huyo.

Hata hivyo katika mkutano wa kila mwaka ulofanyika mjini Thika mnamo Ijumaa, mkurugenzi wa kampuni hiyo ya Thiwasco, Bw Moses Kinya, alisema tayari wanafanya mikakati kuona ya kwamba wananunua mabomba ya kisasa ya kusambaza maji.

“Kumekuwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa maji katika mitaa kadhaa Thika na kwa hivyo kampuni ya Thiwasco inafanya juhudi kuona ya kwamba wakazi wa mitaa hiyo wanapata maji baada ya wiki chache zijazo,” alisema Bw Kinya.

Alisema mabomba ya maji yaliyokuwepo hapo awali ni madogo kwa upana na kwa hivyo hayatoshelezi mahitaji ya wateja wao.

Alisema pia kwa wakati huu kampuni hiyo inahudumia wakazi wa Thika na vitongoji vyake; watu wapatao 300,000 baada ya wao kuongezeka.

Alisema kulngana na changamoto hiyo ni sharti watafute njia mwafaka kuona ya kwamba wanatosheleza mahitaji ya wateja wao kwa njia ifaayo.

Alizidi kueleza ya kwamba watazidi kutumia teknolojia ya kisasa kwa usambazaji wa maji hayo ili kutosheleza mahitaji ya wakazi hao.

Mnamo Jumamosi mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina alisema shida ya maji imekuwa changamoto katika maeneo mengi Thika na vitongoji vyake.

“Tayari nimefanya mipango ya kuona ya kwamba siku chache zijazo mtambo wa kuchimba maji unaanza mradi huo katika maeneo yaliyoathirika kwa kukosa maji. Tunalenga maeneo ya Landless, Kilimambogo, na Ngoliba ambapo kazi itaanza mara moja,” alisema Bw Wainaina.

Alisema mabomba ya kusambaza maji katika kituo cha Ngoliba yalipelekwa huko miezi mitatu iliyopita ambapo kile kilichobaki ni kuyaunganisha baada ya uchimbaji wa maji ili bidhaa hiyo iwafikie wananchi.