Polisi kizimbani kwa kumumunya mamilioni ya NSSF

Na RICHARD MUNGUTI

MAAFISA wakuu wawili wa polisi akiwamo naibu wa afisa msimamizi wa Kituo cha Polisi cha Narok (OCS) walishtakiwa Jumatatu kwa kulaghai Hazina ya Malipo ya Uzeeni (NSSF) Sh3.4 milioni.

Bw Milton Odhiambo Barasa, aliye naibu wa OCS na James Thuo Njuguna, wa kitengo cha kupiga picha walishtakiwa mbele ya hakimu mkuu mahakama ya Milimani Nairobi Bi Martha Mutuku.

Walikanusha shtaka la kula njama za kumumunya hela za malipo ya uzeeni ya kikosi cha polisi Sh3,482,451 kwa kuidhinisha hati feki za Samuel Kiprotich Bett.

Washtakiwa hao walidaiwa walitekeleza uhalifu huo kati ya 2017 na 2018 katika makao makuu ya polisi jijini Nairobi.

Shtaka la pili lilisema hawakuchukua tahadhari iwapasavyo kuzuia kutoweka kwa pesa hizo..

Washtakiwa waliomba mahakama iwaachilie kwa dhamana wakifichua wamehudumia kikosi cha polisi kwa zaidi ya miaka 27 kila mmoja na “ wanaendelea kutekeleza majukumu yao.”

Mahakama ilifahamishwa washtakiwa walipigiwa simu kutoka stesheni wanakohudumu kufika katika makao makuu ya uchunguzi (DCI) kuhojiwa.

“Washtakiwa walizuiliwa tangu Ijumaa hadi leo walipofikishwa kortini,” hakimu alielezwa.

“Huduma za washtakiwa zingali zahitajiwa hasa wakati huu wa kupambana na ugonjwa wa Corona na visa vingine vya uhalifu,” Bi Mutuku alielezwa na wakili anayewatetea washtakiwa hao.

Hakimu aliwaamuru washtakiwa hao walipe kila mmoja dhamana ya Sh500,000 pesa tasilimu.

Pia aliwataka wafike kortini tena Julai 20, 2020 kutengewa siku ya kusikizwa kwa kesi inayowakabili.

Wizi wa Sh72m: Korti kufanya maamuzi

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA itaamua Jumanne ikiwa washukiwa sita wa wizi wa Sh72 milioni za benki ya Standard Chartered watazuiliwa kwa siku saba au la.

Jana, Hakimu Mkuu wa Milimani, Nairobi, Bi Matha Mutuku, aliagiza kuwa washukiwa hao wapelekwe katika Hospitali Kuu ya Kenyatta wapomwe na kujua kiwango cha majeraha waliyopataka.

Washukiwa hao ambao miongoni mwao ni maafisa watatu wa Polisi wa Utawala, walidai kuwa walipigwa na kuumizwa. Wengine sita, wakiwa wafanyikazi wa kampuni ya G4S mnamo Ijumaa iliamuliwa kuwa wazuiliwe kwa siku tano katika kituo cha polisi cha Langata.

Konstebo Chris Machogu, Koplo Duncan Kavesa Luvuga, Konstebo Boniface Mutua, Vincent Owuor, Alex Mutuku na Francis Muriuki waliposhtakiwa jana, Kiongozi wa mashtaka Anderson Gikunda aliomba wazuiliwe kwa siku saba.

“Washukiwa walitiwa nguvuni Ijumaa usiku na Jumamosi. Polisi wanahitaji siku saba kukamilisha uchunguzi,” alisema Bw Gikunda.

Alisema polisi wanahitaji muda kuchunguza simu za washukiwa hao kubaini watu waliowasiliana nao.

Alisema pia polisi watachunguza kamera za cctv kuwatambua washukiwa wengine wanaoendelea kusakwa.

Wakili Cliff Ombeta alipinga ombi washukiwa kuzuiliwa kwa siku saba akisema walipigwa na kuumizwa vibaya.

“Koplo Luvuga alipigwa na kuumizwa na polisi. Aliumizwa kichwani, mikono na miguu. Polisi walimfunga mshukiwa huyu mikono na miguu. Alifungwa kando ya chumba cha mbwa katika kituo cha polisi cha Muthaiga.Alizamishwa ndani ya maji akiendelea kuhojiwa,” Bw Ombeta alimweleza Bi Mutuku.

Aliongeza kusema Owuor alipigwa na kudungwa vidole na kuwekwa pili pili akilazimishwa kusema yeye ni afisa polisi.

“Mshukiwa huyu sio afisa wa polisi. Mkurugenzi wa uchunguzi wa jinai (DCI) alidai mshukiwa huyu ni afisa wa polisi,” akasema.

Aliomba korti iwaachilie washukiwa hao waende hospitali kwa vile polisi hawatawapeleka.

“Usikubali ombi la polisi la kuzuiliwa kwa washukiwa hawa kwa siku saba.Huenda hautakuwa na washukiwa kabla ya siku hizo kukamilika,” alisema Bw Ombeta.

Alisena washukiwa watafia mikononi mwa polisi kulingana na mateso wamepitia. Aliomba korti iwape dhamana washukiwa wajipeleke hospitali.

Aliomba korti itupilie mbali ombi la upande wa mashtaka akisema ” hawajawasilisha ushahidi wowote kuwezesha mahakama kuwazuilia washukiwa.”

Wakili huyo alisema polisi walienda katika makazi ya washukiwa na kusababisha uharibifu mkubwa wakisaka pesa hizo.

“Polisi walirarua viti kupasua dari, walipasua magodoro na hata pilo wakitafuta pesa hizo,” Ombeta.

Hata hivyo hakimu aliombwa awazuilie washukiwa hao kwa vile wengine sita waliamriwa wazuiliwe kwa siku saba.

Gavana ataka wabunge warejeshe mamilioni ya ziara ya Amerika

Na SIMON CIURI

GAVANA wa Machakos, Dkt Alfred Mutua anataka wabunge walazimishwe kurejesha mamilioni ya fedha za umma walizotumia katika ziara ya Amerika.

Dkt Mutua, aliyekuwa akizungumza katika jumba la kibiashara la Spur Mall, Ruiru, katika Kaunti ya Kiambu, alisema ziara hiyo haina manufaa kwa Wakenya, hivyo wabunge ni shati walazimishwe kurejesha fedha hizo.

“Idadi kubwa ya wabunge walioelekea nchini Amerika ni ithibati kwamba walikuwa wameenda likizo. Ziara hizo zisizokuwa na manufaa kwa walipa ushuru ndizo zimefanya gharama ya kuendesha mabunge ya kaunti kuwa juu,” akaongezea.

Gavana Mutua aliwataka viongozi kuzingatia agizo la serikali iliyopiga marufuku idadi kubwa ya watu kuhudhuria kongamano moja.

“Kuna sera ya serikali inayodhibiti idadi ya watu wanaofaa kuhudhuria kongamano moja. Inasikitisha kwamba serikali za kaunti tuliandikiwa barua tukitakiwa tusitume zaidi ya watu watatu katika kongamano ilhali bunge linatuma zaidi ya watu 60,” akasema kiongozi huyo wa chama cha Maendeleo Chap Chap.

Mbali na wabunge, wengine waliosafiri ni maseneta, madiwani na wafanyakazi wa bunge.

Inakadiriwa kuwa Wakenya walipoteza zaidi ya Sh100 milioni katika ziara hiyo.

Kiongozi wa ODM, Raila Odinga tayari ameshutumu ziara hiyo akisema kuwa ni uharibifu wa fedha za walipa ushuru.

Dkt Mutua, wakati huo huo, alitangaza kuwa atazindua kituo cha kutafiti maradhi ya kansa katika Kaunti ya Machakos.

“Tutatumia Sh100 milioni na baadaye tutaongezea Sh300 milioni kuhakikisha kuwa kituo hicho kitakuwa na vifaa vyote vinavyohitajika. Wakazi watapimwa kansa bila malipo,” akasema Gavana Mutua.

Ajisaliti kuweka benki mamilioni ya pesa za wizi kila siku

NA SAM KIPLAGAT

AFISA wa zamani wa Kaunti ya Nairobi aliyejisaliti kwa kuweka benki mamilioni ya pesa kila siku, ameagizwa na mahakama arejeshe mamilioni aliyoiba.

Jimmy Kiamba, ambaye alikuwa Afisa Mkuu wa Fedha katika kaunti hiyo, hakuweza kufafanulia mahakama jinsi alivyopata mamilioni aliyoweka kila siku, ikizingatiwa kuwa mshahara wake ulikuwa Sh85,000 kwa mwezi.

Jaji Hedwig Ong’udi vile vile alimwagiza Bw Kiamba alipe Sh35 milioni kwa serikali la sivyo nyumba yake ya kifahari katika mtaa wa Runda ichukuliwe.

“Naagiza serikali ilipwe Sh282,648,604 na mshtakiwa,” akaamuru Jaji Ong’udi.

Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC), ambayo iliwasilisha kesi hiyo, iligundua kwamba Bw Kiamba hakuweza kufafanua zilikotoka Sh317,648,604 pesa taslimu zilizowekwa kwenye akaunti yake nyakati tofauti na maafisa wa kaunti.

Afisa huy,o ambaye alihudumu chini ya aliyekuwa gavana Dkt Evans Kidero, awali alikuwa amewaeleza maafisa wa EACC kwamba alipata fedha hizo kutokana na mauzo ya ng’ombe, mawe ya ujenzi na ngano na biashara za uchukuzi.

Hata hivyo, Jaji Ong’udi alisema ilikuwa vigumu kujua kiasi cha fedha ambazo ziliwekezwa na afisa huyo kwenye biashara ya uchukuzi, ndiyo maana nyumba aliyonunua kwa Sh35 milioni iliwekwa chini ya mali ambayo maelezo ya jinsi ilivyopatikana yalikosa kuridhisha.

Mahakama ilielezwa kwamba EACC ilichunguza akaunti 11 za Bw Kiamba, ambazo zipo kwenye benki nane, na pia kuchunguza nakala ya jinsi alivyoweka na kutoa pesa. Ilipolinganishwa na mshahara wake, ndipo ikafikia uamuzi kwamba mali yake haikupatikana kwa njia halali.

Kati ya Januari na Novemba mwaka wa 2014, EACC ilipata kwamba Bw Kiamba alikuwa na Sh400 milioni kwenye benki, ilhali alikuwa akilipwa mshahara wa Sh85,000 kila mwezi akihudumu kwenye wadhifa wake.

Miaka michache baadaye, ilishangaza kwamba mshahara wake uliongezeka hadi Sh1.09 milioni kila mwezi na nyumba za kukodisha alizojenga mtaa wa Athi River pia zikimletea Sh2.7 milioni kwa mwezi.

Kati ya wafanyakazi wa kaunti ambao EACC ilipata na hatia ya kuwatumia kuweka pesa kwenye akaunti zake nyakati tofauti ni Joseph Njoroge (Sh66.8 milioni), Stephen Osiro (Sh4.1 milioni), Barnabas Ougo (Sh15.65 milioni), Ambrose Musau (Sh3.4 milioni) na Joseph Njoroge (Sh1.3 milioni).

Hata hivyo, korti ilieleza kushawishika na jinsi Bw Kiamba alivyopata mali yake nyingine kama nyumba maeneo ya Naivasha na Muthaiga.

Mtapokea mamilioni yenu Machi 2019, Harambee Stars yaambiwa

Na GEOFFREY ANENE

AHADI ya Harambee Stars kuzawadiwa na serikali Sh50 milioni ikifuzu kushiriki Kombe la Afrika mwaka 2019 ambayo ilitolewa na Naibu Rais William Ruto mwezi Oktoba 2018 itatimizwa Machi mwaka 2019.

Aidha, Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) liko na bajeti ya Sh200 milioni ya kushughulikia Harambee Stars kabla ya AFCON, wakati wa mashindano haya na pia kuizawadia kutegemea umbali itafika kwenye mashindano hayo ya mataifa 24.

Tangu Stars ichukue usukani wa Kundi F baada ya kukaba Ethiopia 0-0 mjini Awasa mnamo Oktoba 10, mashabiki wa Kenya wamekuwa wakitaka serikali iipe timu hiyo haki yake. Miito ya kutaka Stars ipokee zawadi hiyo iliongezeka pale ilipochapa Ethiopia 3-0 katika mechi ya marudiano jijini Nairobi mnamo Oktoba 14.

Wengi wa Wakenya waliamini Stars imeshafuzu kushiriki AFCON 2019 kwa sababu Sierra Leone ilikuwa imepigwa marufuku na Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) mnamo Oktoba 5.

Hata hivyo, CAF ilijikokota kutangaza hali ya kundi F hadi Novemba 30. Baada ya CAF kutoa hakikisho Kenya pamoja na nambari mbili kwenye kundi hilo, Ghana, zimefuzu, FKF sasa imesema itakuwa vigumu kugawana fedha hizo hadi wachezaji watakapokusanyika jijini Nairobi wakati wa kipindi cha mexhi za kimataifa mwezi Machi mwaka 2020.

Kulingana na Rais wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) Nick Mwendwa mikakati jinsi fedha hizo kutoka kwa Serikali zitagawanywa bado inafanywa.

“Wizara ya Michezo imekuwa ikisubiri thibitisho kwamba Kenya imefuzu ndiposa ishughulike zawadi hiyo ya Sh50 milioni kwa Stars. Naona ile ahadi ya Sh50 milioni kwa Stars itatimia mwezi Machi mwaka 2019 baada ya mechi ambayo tunapanga ya kutoa shukrani kwa mashabiki wetu jijini Nairobi. Mechi hii itakuwa baada ya ile mechi ya mwisho ya Harambee Stars ya kufuzu kushiriki AFCON dhidi ya Ghana. Kabla ya wakati huo, itakuwa vigumu kwa sababu wahusika wengi wakuu ambao ni wachezaji hawako nchini,” Mwendwa amesema jijini Nairobi.

Mechi ya kushukuru mashabiki inatarajiwa kusakatwa Jumanne ya kwanza baada ya Kenya kuvaana na Ghana ambayo ni Machi 26. Kenya itazuru Ghana mnamo Machi 22 kwa mechi ya mwisho ya kundi F ambayo itaamua mshindi wa kundi hili. Kenya na Ghana zinashikilia nafasi mbili za kwanza kwa alama saba na sita, mtawalia. Ethiopia ina alama moja baada ya ushindi wake wa bao 1-0 dhidi ya Sierra Leone hapo Septemba 9 kufutiliwa mbali.

Aidha, Mwendwa amesema FKF inashughulikia jinsi fedha FKF itagawana na Stars marupurupu. Amesema tayari kuna mpango jinsi benchi la kiufundi litapokea marupurupu. Kiasi cha bonasi kitategemea umbali Stars itafika.

“Kila hatua ambayo Stars itapiga katika AFCON, bonasi ya benchi la kiufundi itaongezeka kwa kiwango fulani ambacho tumeshakubaliana nalo. Tunataka pia mpango huo utumike pia kwa wachezaji,” amesema Mwendwa kabla ya kuongeza kwamba FKF pia itakuwa ikipokea kitu. “Tumekuwa tukiangalia jinsi mataifa mengine yanashughulikia suala hili la kugawana fedha na timu ya taifa.

Nchi kama Argentina kwa mafano, ina sheria ya asilimia 60-40. Asilimia 60 ya tuzo inaenda kwa timu nayo asilimia 40 inatumiwa na shirikisho kuendesha mipango yake. Sisi tunajadiliana kuhusu aslimia 70-30, ingawa kocha atakuwa na usemi jinsi tuzo ya wachezaji inavyogawanywa kwa sababu kuna wachezaji ambao wamesakata mechi zote za kufuzu, wengine moja ama mbili, wengine wamesakata mechi chache lakini mchango wao umekuwa mkubwa sana katika kampeni yetu ya kufika AFCON, na kadhalika.

Wakati wa Kombe la Afrika ya Kati na Mashariki (Cecafa) mwezi Desemba mwaka 2017, mpango uliokuwepo ni ule wa asilimia 80 ya tuzo kuendea timu na asilimia 20 kwa shirikisho.

Kenya, ambayo ilikuwa mwenyeji wa mashindano hayo ya Cecafa, iliibuka mshindi na kuzawadiwa Sh10 milioni. Kwa kufuzu kushiriki AFCON 2019, Kenya tayari imejihakikishia tuzo ya Sh48,751,625 kutoka kwa CAF ikiwa itavuta mkia katika mechi za makundi.

Wabunge na maseneta kumumunya Sh400 milioni michezoni Burundi

CHARLES WASONGA na PETER MBURU

HUKU nchi inapoendelea kuzongwa na changamoto za kifedha, wabunge na maseneta wamesafiri nchini Burundi kwa michezo baina ya mabunge ya mataifa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) kuanzia Jumamosi, ambapo watatumia takribani Sh400 milioni pesa za mlipa ushuru.

Timu ya Kenya inayojumuisha wabunge, maseneta na wafanyakazi wa bunge 390 imewasili jijini Bujumbura tayari kwa mashindano yatakayodumu siku kumi hadi Desemba 10.

Ijumaa, mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria alikejeli ziara hiyo ya viongozi ambayo itaacha taifa na gharama nyingine, licha ya kuwa haina faida ya moja kwa moja kwa uchumi wa taifa wala kuchangia kuinua viwango vya michezo nchini

Kwa lugha ya kejeli, Bw Kuria alirejelea kiwango kikubwa cha pesa kitakachotumika kwenye ziara hiyo na kushangaa manufaa yake.

“Kenya kweli ni taifa la michezo. Kuanzia wikendi hii kwa siku 10 zijazo, Kenya itatuma timu ndogo ya maseneta, wabunge na wafanyakazi wa bunge 390 kwa michezo ya mabunge chini Burundi. Sina shaka tutafanya vyema katika michezo hiyo haswa ule mchezo wa kuvuta kamba ambapo timu yetu ina washiriki wakubwa na wenye nguvu. Mje na mataji na mtumie vizuri Sh400milioni za kugharamia shughuli hizo vizuri. Uganda, Tanzania, Rwanda na Burundi sharti watutambue,” Bw Kuria akaandika kwenye akaunti yake ya Facebook jana.

Vilevile, alipozungumza na Taifa Leo, mbunge huyo alithibitisha madai yake kuwa ya kweli na kwamba, spika wa bunge Justin Muturi na wasimamizi wengine wa bunge wameidhinisha shughuli hiyo na gharama zote.

“Mimi nimepaza sauti na ambaye anaweza kudhani kuwa ni udaku wangu aulize spika wa bunge ama wasimamizi wengine wanaohusika na mambo hayo,” Bw Kuria akasema.

“Ni kweli kwamba wabunge wengi wamesafiri kwenda Burundi kwa michezo kati ya mabunge ya mataifa ya Afrika Mashariki, hali inayoomaanisha kuwa shughuli za mabunge yote mawili zitatatizika kuanzia Jumatatu. Hii ni kutokana na idadi ndogo ya waliosalia,” akathibitisha afisa mmoja wa bunge ambaye aliomba tulibane jina lake.

Bunge linatarajiwa kuahirisha vikao vyake Alhamisi Desemba 6, kwa likizo ndefu ya Chrismasi na Mwaka Mpya. Watarejea Februari 5 mwakani.

Sh400 milioni zinatarajiwa kugharamia nauli ya ndege, chakula, malazi, burudani na marupurupu ya wabunge hao pamoja na wahudumu wa bunge wanaoandamana nao.

Ziara ya Wabunge nchini Rwanda inajiri miezi miwili baada ya Spika Justin Muturi kufutilia mbali ombi la wabunge wanachama wa timu ya Voliboli la kutaka kusafiri hadi Tokyo, Japan kutizama mchuano wa Shirikisho la Voliboli Ulimwenguni (FIVB).

Bw Muturi alisema ziara hiyo haikuwa na maana kwa ustawi wa mchezo huo nchini. Ziara hiyo pia inajiri miezi mitano baada ya wabunge na maseneta 20 kwenda nchini Urusi kutazama michuano ya Kombe la Dunia kwa gharama ya Sh25 milioni, pesa za mlipa ushuru.

Lakini walisisitiza kuwa awalikwenda Urusi kujifunza jinsi Kenya inaweza kuandaa michuano ya hadhi na kiwango hicho.

Wananchi walikerwa na ziara ya wabunge hao baada Seneta Maalum Milicent Omanga na mwenzake James Orengo wakiwepa picha mitandaoni zikiwaonyesha wakijivinjari na mashabiki wa soka huko Urusi.

Waliporejea wabunge hao wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati Michezo Victor Munyaka waliandaa ripoti bandia iliyodondolewa kutoka tovuti mbalimbali za michezo.

Mabwanyenye Mlima Kenya wawanunulia polisi magari ya mamilioni

Na NICHOLAS KOMU

MABWANYENYE kutoka eneo la Mlima Kenya wakiongozwa na Mwenyekiti wa Benki ya Equity Peter Munga wamenunua magari 26 ya thamani ya Sh100 milioni yatakayotumiwa na maafisa wa utawala katika eneo hilo.

Matano kati ya magari hayo ya kifahari yaliyonunuliwa na Wakfu wa Mlima Kenya yalipokezwa Waziri wa Masuala ya Ndani, Dkt Fred Matiang’i Alhamisi mjini Nyeri.

Magari yaliyosalia yatawasilishwa kwa wizara hiyo baadaye. Bw Munga ambaye ndiye mwenyekiti wa Wakfu huo ndiye aliyewasilisha magari hayo kwa Waziri Matiang’i aliyeandamana na Waziri Msaidizi katika Wizara hiyo, Bw Patrick Ole Ntutu na Katibu wa Wizara Karanja Kibicho.

Shughuli hiyo iliendeshwa katika makazi rasmi ya Mshirikishi wa eneo la Kati. Magari hayo ni aina ya Toyota Land Cruiser TX na Mercedes Benz S350.

Bw Munga alisema hatua iliyochukuliwa na wakfu huo inalenga kurejeshwa sifa ya zamani ya utawala wa mkoa.

“Maafisa wa mkoa walikuwa watu wenye mamlaka makuu na ambao waliwakilisha Rais katika maeneo ya mashinani. Tunafaa kuwasaidia kwa kuwapa magari ya kuwawezesha kusafiri katika maeneo wanayosimamia kwa urahisi,” Bw Munga akasema.

Chini ya mpango huo, Washirikishi katika eneo zima la Mlima Kenya watapewa magari aina ya Mercedes Benz huku makamishna wa kaunti wakipewa magari aina ya Land Cruiser na Land Rover.

Magari hayo yataongezea yale ya serikali ambayo maafisa hao wamekuwa wakitumia.

Dkt Matiang’i alishabikia msaada huo huku akitoa wito kwa Wakenya wengine kuiga mfano huo kwa kuchangia katika uboreshaji wa utendakazi wa idara za serikali.

“Huu ni mfano mzuri na kielelezo cha uzalendo. Nyakati nyingi huwa tunalalamikia kutohusishwa kwa umma katika mipango ya serikali. Kila Mkenya ana uhuru wa kushiriki vitendo walivyofanya viongozi wa Wakfu huu,” akasema.

Maafisa 4 ndani miaka 3 kwa wizi na kutumia afisi kujinufaisha

Na RICHARD MUNGUTI

ALIYEKUWA Katibu wa Wizara ya Serikali za Wilaya, Sammy Kirui pamoja na maafisa wengine watatu wakuu wa baraza la jiji NCC Jumanne walisukumwa jela miaka mitatu na kupigwa faini ya Sh86 milioni.

Bw Kirui, aliyekuwa katibu mkuu wa NCC John Gakuo, katibu wa masuala ya sheria Mary Ng’ethe na mwanakamati wa kamati ya zabuni Alexander Musee wanajiunga na orodha ya waliokuwa maafisa wakuu wa serikali kusukumwa jela makatibu Sylvester Mwalikho na Rebecca Nabutola waliofungwa kwa ufisadi.

Wanne hao walipatikana na hatia ya kujihusisha na utowekaji wa Sh283milioni katika kashfa ya kununua ardhi ya kuwazika wafu katika eneo la Athi River kaunti ya Machakos miaka 10 iliyopita.

Mbali na kifungo hicho cha jela wanne waliofungwa walitozwa faini kati ya Sh1milioni hadi Sh52milioni.

Hakimu Douglas Ogoti aliyewapata na hatia Mabw Kirui, Bw Gakuo, Bi Mary Ng’ethe na mwanakamati Bw Alexander Museee alisema “upande wa mashtaka umethibitisha wanne hao walitumia vibaya mamlaka ya afisi zao na kupelekea Serikali kupoteza zaidi Sh283milioni.”

Bw Ogoti aliwatoza Mabw Kirui na Gakuo faini ya Sh1milioni kila mmoja pamoja na kifungo cha miaka mitatu.

Naye Bi Ng’ethe alitozwa faini ya Sh52milioni ilhali Bw Musee alitozwa faini ya Sh32milioni.

Akipitisha hukumu aliyosoma zaidi ya masaa mawili , Bw Ogoti alisema washtakiwa walikaidi mwongozo wa ununuzi wa mali ya umma na kuidhinisha ardhi hiyo inunuliwe katika eneo ambalo halikufaa kwa makaburi.

Ardhi hiyo ilinunuliwa kati ya Desemba 2008 na Aprili 2009.

“Mabw Kirui na Gakuo walikaidi ushauri wa wataalamu wa masuala ya ununuzi wa ardhi waliosema ardhi hiyo haikufaa kwa kuwazika wafu lakini wakaamuru ununuzi uendelee,” alisema Bw Ogoti.

Mahakama ilisema washtakiwa wanne hao walipuuza sheria na mwongozo uliowekwa na kuruhusu mamilioni ya pesa za umma zitumiwe kwa njia isiyofaa.

Bw Kirui alikuwa katibu mkuu wa Wizara ya Serikali za Wilaya ilhali Bw Gakuo alikuwa Katibu mkuu wa baraza la jiji la Nairobi wakati wizi huo ulitekelezwa.

“Maafisa hawa walikuwa na uwezo wa kuzuia pesa hizi kutotoweka lakini walitumia vibaya mamlaka yao,” alisema Bw Ogoti.

Mahakama ilisema kuwa mashahidi waliofika kortini walieleza jinsi walikuwa wanakopeshwa pesa hadi kiwango Sh18milioni na baadhi ya washtakiwa.

“Pesa hizi zilipopelekwa City Hall ziligawanwa na maafisa wakuu waliokaidi ushauri kuwa ardhi hiyo haikufaa kwa kuwazika wafu kwa vile ilikuwa na mawe mengi,” alisema Bw Ogoti.

Ardhi hiyo ilikuwa itumike na baraza la jiji la Nairobi kuwapeleka maiti kuwazika katika kaunti ya Machakos.

Wanne hawa walikuwa miongoni mwa washtakiwa 15 walioshtakiwa kwa kashfa hiyo ya makaburi.

Wengine waliofikishwa kortini ni pamoja na aliyekuwa Meya Geoffrey Majiwa (aliyeachiliwa kwa kukosekana ushahidi) , Mabw Maina Chege, Naen Rech Limited, Newton Osiemo, Wakili Alphonce Mutinda, Nelson Otido, Joseph Kojwando, Alexander Musee, Daniel Nguku, Herman Chavera, William Mayaka na mawakili Paul Chapia Onduso na Davies Odero.

 

Maafisa wengine wa serikali waliofungwa awali kwa ufisadi ni waliokuwa makatibu Sylvester Mwaliko miaka mitatu kwa kashfa ya Anglo-Leasing na Bi Rebecca Nabutola.

Wanachuo kizimbani kwa kuwapora wawekezaji wa Uchina mamilioni

Na RICHARD MUNGUTI

WANAFUNZI wawili wa chuo kikuu kimoja jijini walioshtakiwa Jumatatu walidaiwa ni wanachama wa genge la majambazi linaloongozwa na mwanamke Mkenya Levanda Akinyi Ogilo na wanawake wengine wawili raia wa Tanzania.

Kiongozi wa mashtaka Solomon Naulikha alimweleza hakimu mkuu Francis Andayi kwamba kesi tano walizoshtakiwa Tolbert Ouma Odhiambo na Don Odhiambo Ogutu (pichani) zitaunganoshwa na zile walizoshtakiwa Akinyi na wenzake.

Sasa kesi dhidi ya Odhiambo na  Ogutu zitaunganishwa na zile dhidi ya Akinyi alyeishtakiwa pamoja na raia watatu wa Tanzania Bi Teresa Richard , Bi Rose Richard, na Shimton Ambasa Khan.

Washtakiwa wanadaiwa waliwalenga wawekezaji kutoka Uchina pesa na mali ambayo thamani yake ni zaidi ya Sh8.4 milioni .

Bi Levanda Akinyi Ogilo alifikishwa kortini baada ya hakimu mkuu wa Nairobi Bw Andayi kuwaamuru polisi wamfungulie mashtaka baada ya kumzuia rumande kwa muda wa wiki moja.

Bi Akinyi alishtakiwa pamoja na raia watatu wa Tanzania Bi Teresa Richard , Bi Rose Richard, na Shimton Ambasa Khan.

Washtakiwa hao walikabiliwa na mashtaka zaidi ya kumi ya kuvunja nyumba na kuiba mali na pesa kutoka kwa Mabw Zhang Gong , Wan Baihui, Bi Zhia Qian, Moses Kironyo Pratt na  Mohamud Hussein Egeh.

Washtakiwa hao wanne walikana kuiba Vipakatalishi, Dola za Kimerekani, Euro na sarafu za Uchina zote zenywe thamani ya zaidi ya Sh8,463,000.

Wakili John Swaka anayewakilishtakiwa hao wote aliomba mahakama iwaachilie kwa dhamana akisema Akinyi ni mama aliyeacha watoto kwa nyumba.

Bw Swaka alisema washtakiwa hao walitiwa nguvuni Machi 30, 2018 na wamekuwa wakizuiliwa katika vituo mbali mbali vya polisi.

Hakimu Mkuu akisikiza kesi hiyo. Picha/ Richard Munguti

Jambo hilo lilimuudhi Bw Andayi ndipo akamwagiza kiongozi wa mashtaka Bw Solomon Naulikha apeleke uamuzi wa mahakama kuu katika kila kituo cha polisi jijini Nairobi unaosema hakuna mshukiwa wa wizi au kosa lingine lolote anayepasa kuzuiliwa kama hakuna shtaka la kushikilia.

“Lazima maafisa wote wa polisi wafahamishwe kwamba lazima wawasilishe kortini shtaka la kushikilia ndipo wakubaliwe kumweka rumande mshukiwa wakimhoji,” aliamuru hakimu.

Bw Andayi aligadhabishwa na tabia ya polisi ya kuwazuilia washtakiwa kwa siku nyingi kabla ya kuwashtaki.

Washtakiwa hao walikuwa wakizuiliwa katika kituo cha Kilimani kwa zaidi ya siku saba polisi wakiandikisha taarifa za mashahidi.

Akiomba washtakiwa hao wazuiliwe kuhojiwa na kuwasaidia polisi kutambua wanakoweka bidhaa walizoiba , hakimu alifahamishwa washtakiwa hawa hutorokea Tanzania.

“Punde tu washukiwa hawa wanapotekeleza uhalifu wanatorokea nchi jirani ya Tanzania,” alisema Konstebo James Wanjohi wa idara ya upelelezi.

 

CCTV

Hakimu alifahamishwa kwamba washukiwa hao wametambuliwa katika picha za CCTV ambapo wanaonekana wakiwa wamejihami na bastola.

“Punde tu wanapotekeleza uhalifu washukiwa hawa hutorokea nchi jirani ya Tanzania,” alisema Bw Wanjohi aliyeongeza , “ kwa muda wa miaka mitatu tumekuwa tukichunguza mienendo ya washukiwa hawa watano.

Mahakama ilifahamishwa washtakiwa walitekeleza wizi huo katika mtaa wa Kilimani Nairobi miezi ya Feburuari na Machi 2018.

Waliachiliwa kwa dhamana ya kati ya Sh300,000 hadi  Sh1milioni pesa tasilimu hadi. Akinyi atalipa zaidi ya Sh3milioni ikiwa atafaulu kulipa dhamana hiyo ndipo aachiliwe. Anakabiliwa na kesi tano tofauti.

Kesi zitasikizwa kati ya Mei 3 hadi 10 mwaka huu.

Mkenya na Watanzania wakana kuiba mamilioni

Levanda Akinyi almaarufu Ruth Wairimu (kushoto) akiwa kizimbani na raia wa Tanzania Teresa Richard, Rose Richard na Shimton Ambasa Aprili 11, 2018. Picha/ Richard Munguti

Na RICHARD MUNGUTI

MWANAMKE anayeshukiwa kushirikiana na majambazi kutoka nchini Tanzania alishtakiwa Jumatano kuwanyang’anya wawekezaji kutoka Uchina pesa na mali ambayo thamani yake ni zaidi ya Sh18.4 milioni mwezi Machi, uvunjaji wa nyumba na wizi wa mali na pesa zenye thamani ya Sh8 milioni.

Bi Levanda Akinyi Ogilo alifikishwa kortini baada ya hakimu mkuu wa Nairobi Bw Francis Andayi kuwaamuru polisi wamfungulie mashtaka baada ya kumzuia rumande kwa muda wa wiki moja.

Bi Akinyi alishtakiwa pamoja na raia watatu wa Tanzania Bi Teresa Richard , Bi Rose Richard, na Shimton Ambasa Khan.

Washtakiwa hao walikabiliwa na mashtaka zaidi ya kumi ya kuvunja nyumba na kuiba mali na pesa kutoka kwa Mabw Zhang Gong , Wan Baihui, Bi Zhia Qian, Moses Kironyo Pratt na  Mohamud Hussein Egeh.

Washtakiwa hao wanne walikana kuiba vipakatalishi, Dola za Kimarekani, Euro na sarafu za Uchina zote zenye thamani ya zaidi ya Sh18,463,000.

Wakili John Swaka anayewakilishtakiwa hao wote aliomba mahakama iwaachilie kwa dhamana akisema Akinyi ni mama aliyeacha watoto kwa nyumba.

Bw Swaka alisema washtakiwa hao walitiwa nguvuni Machi 30,2018 na wamekuwa wakizuiliwa katika vituo mbalimbali vya polisi.

Jambo hilo lilimuudhi Bw Andayi ndipo akamwagiza kiongozi wa mashtaka Bw Solomon Naulikha apeleke uamuzi wa mahakama kuu katika kila kituo cha polisi jijini Nairobi unaosema hakuna mshukiwa wa wizi au kosa lingine lolote anayepasa kuzuiliwa kama hakuna shtaka la kumshikilia.