Wakazi wafurahia hatua ya Rais Kenyatta kupandisha hadhi kambi ya jeshi la wanamaji Manda

Na KALUME KAZUNGU

WAKAZI wa msitu wa Boni wamefurahishwa na hatua ya kupandishwa hadhi kwa kambi ya jeshi la wanamaji – nevi – ya Magogoni eneo la Manda, Kaunti ya Lamu.

Rais Uhuru Kenyatta Alhamisi aliongoza hafla ya kukabidhi bendera na rangi kwa kitengo hicho kwenye kambi hiyo ya Manda, ishara kwamba kambi hiyo sasa imetawazwa kuwa ya pili nchini baada ya ile ya Mtongwe iliyoko Kaunti ya Mombasa.

Katika hotuba yake wakati wa hafla hiyo, Rais Kenyatta aliitaja kambi ya nevi ya Manda kuwa muhimu kwani itasaidia kudhibiti usalama nchini na kuwezesha maendeleo kutekelezwa bila kutatizwa.

Aliwataka wakazi wa Lamu na viongozi kushirikiana kikamilifu na vitengo vya usalama katika kuhakikisha amani inadumishwa Lamu, Pwani na nchini kwa jumla.

“Najivunia leo hii kwamba ninakabidhi bendera na rangi rasmi kwa kambi ya nevi ya Manda. Kambi hii ni muhimu katika kukabiliana na ugaidi na kudhibiti usalama Kenya. Lamu ni eneo ambalo serikali inaendeleza miradi ya kitaifa na kimataifa kama vile ule wa bandari ya Lamu (Lapsset). Ninawahimiza wananchi na viongozi wa hapa kushirikiane ili kudhibiti usalama na kupisha ustawi wa kitaifa na maendeleo zaidi kutekelezwa katika eneo hili,” akasema Rais Kenyatta.

Wakizungumza na Taifa Leo Ijumaa, wakazi wa Lamu, hasa wale wa msitu wa Boni waliopakana na kambi hiyo ya nevi walisifu hatua ya Rais Kenyatta kuipandisha ngazi kambi hiyo ya jeshi.

Doza Diza ambaye ni mzee wa jamii ya Waboni eneo la Bar’goni alisema kupandishwa hadhi kwa kambi ya nevi ni kiashirio kuwa Lamu ni salama.

“Kambi ya nevi ya Manda imepandishwa hadhi na hii ina maana kuwa tumepokea ulinzi zaidi. Ninashukuru maafisa wa jeshi. Wamepigana vilivyo na al-Shabaab na kwa sasa tunafurahia amani na utulivu vijijini mwetu,” akasema Bw Diza.

Naye Bi Amina Abuli aliahidi ushirikiano wa dhati wa kijamii na walinda usalama ili kuona kwamba visa vya utovu wa usalama Lamu vinakomeshwa kabisa.

Alisema wamepokea mwito wa Rais wa ushirikiano wa jamii, viongozi na vitengo vya usalama kwa uzingativu mkuu.

“Hata kabla Rais Kenyatta aongee kuhusu ushirikiano wetu na maafisa wa usalama, sisi kama jamii tayari tumekuwa tukiendeleza ushirikiano huo. Umesaidia kuleta amani na utulivu na kuangamiza visa vya mashambulio ya al-Shabaab eneo hili. Tutaendeleza ushirikiano huo,” akasema Bi Abuli.

Abdulrahman Kedi, mkazi wa msitu wa Boni pia alisisitiza haja ya serikali kuhakikisha wamiliki wa ardhi zilizotwaliwa kufanikisha miradi ya serikali zinafidiwa kikamilifu.

“Tunashukuru kwamba Rais Kenyatta pia amegusia suala la matatizo ya kijamii kusuluhishwa kikamilifu ili kupisha miradi kuendelea. Nasihi serikali kufanya hivyo ili sisi kama wanajamii tusilalamike,” akasema Bw Kedi. 

Malalamiko tele chombo cha kukagua mizigo kikiharibika katika uwanja wa ndege wa Manda

Na KALUME KAZUNGU

WASAFIRI wa ndege wanaotumia uwanja wa ndege wa Manda, Kaunti ya Lamu wameisuta Mamlaka ya Usimamizi wa Viwanja vya Ndege nchini (KAA) kwa kuchelewa kurekebisha mashine ya kukagua mizigo na abiria kwenye uwanja huo.

Mashine hiyo ilileta hitilafu na kusita kufanya kazi karibu wiki mbili zilizopita, hali iliyolazimu maafisa wa usalama kufanya upekuzi kwa mikono.

Mashine iliyoharibika hupekua mizigo na abiria kupitia mfumo wa X-Ray, ambapo hakuna haja ya abiria au mizigo kushikwa na wahudumu wa viwanja vya ndege.

Wasafiri walisema mbali na kuhatarishwa kuambukizwa Covid-19, mfumo huo wa upekuzi wa moja kwa moja pia umekuwa ukiwapotezea muda mwingi kando na kuwa hauna hakikisho la kiusalama.

Bi Fatma Athman ambaye ni msafiri wa mara kwa mara kupitia uwanja wa ndege wa Manda alisema mara nyingi amelazimika kuunga foleni na mizigo yake akisubiri kukaguliwa, hali ambayo ni kinyume wakati mashine ya X-ray inapofnya kazi.

“Sipendelei hali ilivyo sasa. Warekebisha mashine yao ya kukagua abiria na mizigo,” akasema Bi Athman.

Msafiri mwingine, Bw Mohamed Omar, alilalamika kuwa mbinu ya kutumia mikono kwa upekuzi si salama kwani huenda ikatumiwa na wakora kuendeleza maovu yao.

“Mashine ya X-ray ndiyo mwafaka kwa shughuli hii ya upekuzi. Yanayofanyika yanahatarisha maisha yetu,” akasema Bw Omar.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa KAA Ukanda wa Pwani, Bw Peter Wafula alisema mashine ya X-Ray inayokagua mizigo pekee ndiyo ilileta hitilafu na tayari imerekebishwa.

“Tuligundua kuwa ukanda wake ulikuwa umeraruka. Tayari tumeushona na mashine inafanya kazi. Pia tumeagiza ukanda tofauti kutoka Malindi kufikishwa uwanja wa ndege wa Manda ili kurekebisha tatizo hilo kwa njia ya kudumu. Hakuna la kuhofia kwa sasa,” akasema Bw Wafula.

Upanuzi wa uwanja wa ndege wa Manda waanza

NA KALUME KAZUNGU

HALMASHAURI ya Usimamizi wa Viwanja vya Ndege nchini (KAA) limeanzisha ukarabati wa uwanja wa ndege wa Manda, Kaunti ya Lamu unaokadiriwa kugharimu serikali kima cha Sh 200 milioni.

Mradi huo ambao unahusisha ujenzi na upanuzi wa njia pamoja na mahali pa kupakisha ndege punde zinapotua umepangwa kuchukua muda wa miezi sita kukamilika.

Mkurugenzi wa KAA Ukanda wa Pwani, Peter Wafula, alisema shughuli ya ujenzi na upanuzi wa sehemu hizo za uwanja wa ndege wa Manda inaendelea baada ya kuanza rasmi mwezi Machi mwaka huu.

Bw Wafula alisema wanatarajia shughuli hiyo ya ujenzi kufikia kikomo ifikapo Agosti mwaka huu.

Afisa huyo alisema KAA iliafikia kupanua na kujenga sehemu husika ili kuwezesha ndege zaidi kutua na kupata nafasi ya kupaki kwenye uwanja huo kwa wakati mmoja.

Alisema sehemu zinazokarabatiwa kwa miaka kadhaa zimekuwa katika hali mbaya, hatua ambayo ilichangia baadhi ya kampuni za usafiri wa ndege nchini, ikiwemo Jambojet kukatiza safari zake kwenye eneo la Lamu.

Bw Wafula anasema anaamini kukamilika kwa ukarabati unaoendelea uwanjani humo kutasaidia kuvutia kampuni nyingi zaidi za ndege kuanzisha huduma zake za usafiri Lamu.

Ujenzi ukiendelea kwenye uwanja wa ndege wa Manda, Kaunti ya Lamu. Jumla ya Sh 200 milioni zimepangwa kutumika kwenye mradi huo. PICHA/ KALUME KAZUNGU

“Tumeanzisha ujenzi na upanuzi wa sehemu za kuegesha na kupaa kwa ndege uwanjani Manda, Kaunti ya Lamu. Sehemu zinazojengwa zilikuwa katika hali duni. Mradi umepangwa kutekelezwa kwa muda wa miezi sita. Shughuli zilianza Machi. Kufikia Agosti kila kitu kitakuwa tayari,” akasema Bw Wafula.

Hatua ya KAA ya kukarabati na kupanua kiwanja cha ndege cha Manda imepokelewa vyema na wadau wa utalii,wawekezaji na wasafiri eneo hilo.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wawekezaji katika sekta ya Utalii, Kaunti ya Lamu, Abdallah Fadhil alipongeza KAA kwa hatua hiyo, akiitaja kuwa yenye natija tele kwa sekta ya utalii Lamu.

“Nimefurahi kwamba KAA imeafikia kukarabati na kupanua kiwanja cha ndege cha Manda. Hii inamaanisha punde shughuli ikikamilika, kampuni nyingi zaidi za ndege zitaanzisha safari zake Lamu. Tutashuhudia watalii wakiingia hapa kwa wingi, hivyo kunogesha sekta hiyo muhimu,” akasema Bw Fadhil.

Mmoja wa wasafiri, Hussein Shukri pia alipongeza ukarabati na upanuzi unaoendelea wa kiwanja hicho cha ndege cha Manda, akisema hatua hiyo itaondoa woga miongoni mwa wasafiri kila wakati ndege zinapotua na kupaa kwenye uwanja huo ambao ulikuwa umesheheni miteremko na mabonde.

Naye Meneja wa Usimamizi na Maendeleo ya Bandari ya Lamu (Lasset), tawi la Lamu, Salim Bunu alisema ujenzi na upanuzi wa uwanja huo wa ndege wa Manda umejiri kwa wakati ufaao ambapo bandari ya Lamu iko kwenye harakati za kuzindua shughuli zake eneo hilo kufikia mwezi Juni mwaka huu.

“Lapsset itakapoanza kufanya kazi itaongeza idadi ya watu eneo hili ambao wengine watakuwa ni wafanyikazi. Wote hao watahitaji usafiri, iwe ni kwa ndege au gari,” akasema Bw Bunu.

Yaibuka uwanja wa ndege hutegemea vibuyu kuchota maji

Na KALUME KAZUNGU

WAFANYAKAZI katika uwanja wa ndege wa Manda, Kaunti ya Lamu hulazimika kuchota maji kwa vibuyu kutoka visimani kwa matumizi uwanjani humo unaokumbwa na uhaba mkubwa wa maji.

Uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo umebaini kuwa wafanyakazi kwenye uwanja huo wa ndege hutumia mitungi kusafirisha maji kwa mashua kutoka visima vya Shella hadi kwenye uwanja huo wa ndege wa Manda ambao ni umbali wa karibu kilomita 10.

Baadhi ya wafanyakazi waliozungumza na wanahabari na kudinda kutaja majina yao kwa kuhofia kufutwa kazi walisema tatizo hilo la maji lilianza karibu miezi miwili unusu iliyopita.

‘Mara nyingi tunalazimika kuamka alfajiri na kwenda kujaza maji kwa mitungi katika visima vya Shella. Baadaye tunaisafirisha kwa boti au mashua hadi kwenye uwanja wa ndege wa Manda,” akasema mmoja wa vibarua.

Vibarua kwenye uwanja wa ndege wa Manda wakisambaza maji vyooni na sehemu zingine. Uhaba wa maji unaendelea kukumba eneo hilo. PICHA/KALUME KAZUNGU

Wasafiri waliohojiwa pia walikiri kukumbwa na kipindi kigumu kila wanaposhuka uwanjani humo hasa tangu tatizo la maji lilipoanza kushuhudiwa.

Akijibu suala hilo, Mkurugenzi Mkuu wa Halmashauri ya Viwanja vya Ndege (KAA) Ukanda wa Pwani, Peter Wafula, alisema uhaba wa maji kwenye uwanja huo huenda umechangiwa na kupungua kwa kiwango cha maji kinachosambazwa kwenye kisiwa cha Manda na Bodi ya Kusambaza Maji ya Lamu (LAWASCO) hasa tangu msimu wa kiangazi ulipoanza eneo hilo.

Bw Wafula, aidha alisema uhaba huo wa maji haujaathiri pakubwa shughuli za kila siku katika uwanja huo wa ndege kwani wamekuwa wakitumia mbinu mbadala, ikiwemo kusafirisha maji kwa boti kutoka eneo la Shella hadi Manda kila mara.

Naye Meneja wa LAWASCO, Kimani Wainaina, alitaja kukauka kwa baadhi ya visima kwenye bwawa la Shella hasa tangu msimu wa kiangazi ulipoanza Lamu kuwa changizo kuu linalopelekea kiwango cha maji kinachosambazwa sehemu nyingi za Lamu, ikiwemo Uwanja wa Manda kupungua.

Mara nyingi wamekuwa wakiepuka kutumia vyoo kwani baadhi ni vichafu. PICHA/ KALUME KAZUNGU

Bw Wainaina pia alitaja hitilafu ya umeme ambayo imekuwa ikishuhudiwa mara kwa mara eneo la Lamu katika siku za hivi karibuni kuwa sababu mojawapo ya maji kukosa kusambazwa inavyostahili katika miji na vijiji vya Lamu.

‘Pia ningesihi KAA kukarabati mabomba yake ya maji kutoka Shella hadi uwanja wa ndege wa Manda kwani ni ya zamani na yanaathiri kiwango cha maji kinachosambazwa eneo hilo,” akasema Bw Wainaina.

Ali Zubeir alisema mara nyingi wamekuwa wakiepuka kutumia vyoo kwani baadhi ni vichafu. ‘Kuna vingine hata vimefungwa kutokana na ukosefu wa maji. Hiyo inamaanisha ukitaka kutumia choo lazima usubiri mwenzako,’ akasema Bw Zuberi.

Visiwa vya Mombasa na Manda huenda vikazama – Wanasayansi

Na WINNIE ATIENO

WANASAYANSI wameonya huenda visiwa vya Mombasa na Manda vikazama kufuatia mabadiliko ya tabianchi.

Kulingana na wanasayansi hao visiwa hivyo eneo la Pwani ya Kenya huenda vikazama kwa kipindi cha miaka 30 au 50 ijayo endapo juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuongezeka kwa kina cha maji baharini hazitazingatiwa.

Wanasayansi hao kutoka kwa Taasisi ya Utafiti wa Maswala ya Bahari na Samaki nchini Kenya yaani KMFRI wanaonya kuwa samaki katika bahari hiyo wako katika hatari ya kupotea huku mabaki ya plastiki yakisheheni Bahari Hindi.

Hii ni kwa sababu ya mienendo mibovu na mazoea ya baadhi ya Wakenya kutupa baharini bidhaa za plastiki ambazo zinaendelea kuchafua mazingira hayo.

Hata hivyo, wanasayansi hao wamebaini kuwa Wakenya wana fursa ya kubadilisha mkondo huo endapo watachukulia swala la uhifadhi wa mazingira kwa umakini na kulipa kipaumbele.

“Tunaweza kuokoa hali hii ili visiwa vyetu kuepuka majanga ya mabadiliko ya tabianchi. Sehemu hatari ni uwanja wa ndege pale Manda; sehemu inayotazamiwa kuzama kwenye Bahari Hindi mwaka 2030 au 2050 sababu iko mita moja kutoka kwa kingo za bahari. Kisiwa cha Mombasa pia kiko hatarini,” alisema Afisa Mkuu Mtendaji wa KMFRI Prof James Njiru.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo mnamo Jumatano, mwanasayansi huyo aliwahakikishia Wakenya kwamba kuna juhudi za serikali, wanaharakati na mashirika ya uhifadhi wa mazingira kuokoa visiwa hivyo maarufu katika utalii.

Afisa Mkuu Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Masuala ya Bahari na Samaki nchini Kenya (KMFRI) Prof James Njiru wakati wa mahojiano katika ofisi yake Mombasa Juni 8, 2020. Wataalamu wameonya wawekezaji dhidi ya kuendeleza ujenzi karibu sana na Bahari Hindi kwamba huenda wakapata hasara kwa sababu mabadiliko ya tabianchi yanasababisha kuongezeka kwa kina cha maji baharini. Picha/ Kevin Odit

“Bahari ni muhimu sana kwani tunapata manufaa mengi ikiwemo chakula (samaki), dawa, utalii, uchukuzi miongoni mwa mengine mengi. Lakini bahari zetu ziko katika hatari. Na tunapoadhimisha siku ya Bahari Ulimwengini hatuna budi kuwaelimishe Wakenya kuhusu hatari tunayokodolea macho ili tupate mshawasha wa kuhifadhi mazingira yetu,” alisema Prof Njiru wakati wa mahojiano.

Alisema kadri wakenya wanapotupa plastiki baharini nazo samaki zinasalia kuwa hatari ya kula uchafu huo.

“Mwaka 2050 plastiki zitakuwa nyingi kuliko samaki baharini. Tutakuwa na tani milioni 50 za plastiki kuliko samaki. Utakuwa unakula plastiki nyingi kuliko samaki. Lakini kama tutakoma kutupa plastiki basi tutaokoa samaki na mazingira baharini,” akasema Prof Njiru.

Katibu Mkuu katika Wizara ya Maswala ya Bahari na Samaki Prof Micheni Ntiba anawasihi Wakenya kupanda miti ili kuhifadhi mazingira.

Kwenye kikao na wanasayansi, Prof Ntiba alisema mvua inaponyesha na kusababisha maafa hususan katika sehemu za Pwani na Nyanza sababu kuu huwa ni athari hasi za uharibifu wa mazingira.

“Tukipanda miti kila mahali halafu mvua kubwa inyeshe, maji hayo yatamezwa ardhini badala ya kuteremka na kusababisha mafuriko baharini na sehemu za ziwa kama vile huko Nyanza kama inavyoendelea kushuhudiwa kwa sasa. Washikadau wote washirikiane na serikali kupanda miti ili kuepuka mmomonyoko wa ardhi,” Prof Ntiba akasisitiza.

Alisema Wakenya waliadhimisha siku ya Bahari Ulimwenguni wakati wa janga la corona ambalo limesababisha kusitishwa kwa kongamano muhimu wa Umoja wa Mataifa ambapo wenyeji washirika au wenza yalikuwa ni mataifa ya Kenya na Ureno.

Kongamano hilo la 2020 UN Ocean Conference lilikuwa lifanyike Juni 2 hadi 6 Kenya ikiwa mwenyeji wake.

Dkt James Kairo alisema mmomonyoko wa ardhi sehemu ya Pwani husababishwa kwa njia mbili.

“Ama kupitia wanadamu au ile njia ya kawaida (naturally mediated). Ile ya wanadamu hufanyika wakati miti ya bahari ambayo inazuia uchafuzi wa mazingira hayo na uharibifu huo hususan mikoko, nyasi za baharini (seagrasses) na miamba ya matumbawe yaani coral reefs huharibiwa. Inafaa tulinde mazingira yetu,” alisisitiza.

Shughuli za usafiri uwanja wa ndege wa Manda zarejelewa kama kawaida

Na KALUME KAZUNGU

SHUGHULI za usafiri katika uwanja wa ndege wa Manda, Kaunti ya Lamu zimerejelewa kama kawaida baada ya uwanja huo wa ndege kufungwa kwa muda Jumapili kufuatia shambulio la al-Shabaab lililolenga kambi ya wanajeshi wanamaji na ile ya wanajeshi wa Amerika iliyoko karibu na uwanja huo wa ndege.

Wapiganaji watano wa kundi hilo waliuawa huku wengine watano wakikamatwa wakiwa hai wakati wa shambulio hilo la majira ya saa kumi na moja na nusu alfajiri.

Halmashauri ya usimamizi wa viwanja vya ndege na usafiri nchini (KCAA) ilitangaza kurejelewa kwa shughuli za usafiri uwanjani hapo muda wa saa chache baada ya kufungwa kufuatia shambulio lililokuwa limetokea Jumapili asubuhi.

“Halmashauri ya KCAA ingependa kuwatangazia wadau wote wa usafiri wa ndege na umma kwamba baada ya uvamizi wa kigaidi asubuhi, kufungwa kwa muda kwa uwanja wa ndege wa Manda kulikokuwa kumetangazwa awali sasa kumeondolewa kupisha shughuli za kawaida kuendelea,” ikasema KCAA katika ujumbe wake.

Akizungumza Jumatatu na ‘Taifa Leo’, Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Bw Irungu Macharia amefafanua kwamba kufungwa kwa uwanja wa ndege wa Manda hakukutokana na kwamba uwanja huo ulikuwa umevamiwa bali ilikuwa tahadhari ya kiusalama.

Bw Macharia ameshikilia kuwa usalama umedhibitiwa vilivyo kwenye uwanja huo na kuwataka wafanyakazi na hata wasafiri wanaotumia uwanja huo kuondoa shaka.

“Shughuli zilisitishwa baada ya uvamizi wa kigaidi kutekelezwa kwenye kambi za wanamaji na ile ya Amerika eneo la Manda Bay na wala si ndani ya uwanja wa ndege wa Manda. Kwa sasa usalama umeimarishwa vilivyo na hakuna sababu ya watu kutishika,” akasema Bw Macharia.

Jeshi laua magaidi 4 waliovamia kambi yao

KALUME KAZUNGU na STEPHEN ODUOR

JESHI la Kenya (KDF) liliwaua washukiwa wanne wa al-Shabaab waliojaribu kuvamia kambi ya jeshi eneo la Manda, Kaunti ya Lamu Jumapili asubuhi.

Msemaji wa KDF, Kanali Paul Njuguna alisema kuwa wakati wa kutibuliwa kwa jaribio hilo la saa kumi na moja na nusu alfajiri, moto mkubwa ulizuka na kushika mapipa ya mafuta kwenye uwanja huo wa ndege, hivyo kusababisha moshi mkali.

Bw Njuguna alisema hakuna yeyote aliyejeruhiwa wala kuuawa kwa upande wa KDF waliokabiliana na kutibua uvamizi huo.

“Wanajeshi wetu walikabiliana nao na tayari miili minne ya magaidi imeonekana eneo hilo. Moto uliozuka ulikabiliwa na kuzimwa. Kwa sasa hali ni shwari na shughuli za kawaida zimerejelewa kwenye kiwanja hicho cha ndege,” akasema Bw Njuguna.

Hata hivyo, baadaye Halmashauri ya Kusimamia Safari za Ndege nchini (KCAA), ilitangaza kufungwa kwa uwanja huo.

Awali, duru za usalama zilisema kwamba magaidi wa Al-Shabaab walikuwa wamevamia kambi ya jeshi la Majini eneo la Manda-Magogoni na ile ya jeshi la Amerika, zote zikiwa kwenye kisiwa cha Manda-Bay, Kaunti ya Lamu.

Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Bw Irungu Macharia, alisema magaidi hao walivamia kambi hizo mbili majira ya saa kumi alfajiri na kufikia saa moja asubuhi, makabiliano bado yalikuwa yakiendelea.

Mwanamgambo wa kujitolea mhanga aliingia kambini na kujilipua na wengine wakajaribu kuingia kambini hapo kwa lazima. Wakazi wanaoishi karibu na kambi hizo pia walikiri kusikia milio ya risasi na milipuko ya mabomu kutoka eneo la kambi hizo.

“Tangu saa kumi na moja alfajiri, tumeamshwa na milio ya risasi na mabomu iliyotoka upande wa kambi ya jeshi. Pia tumekuwa tukiona wingu kubwa la moshi kutoka upande huo. Nashuku mambo si sawa eneo hilo. Huenda kuna uvamizi wa kigaidi. Tunawaombea wanajeshi wetu,” akasema Bw Paul Mwaniki.

Kutokana na tukio hilo, usalama uliimarishwa katika kaunti jirani ya Tana River na mpaka wa msitu wa Boni, baada ya wakazi wa Kilelengwani kuripoti kuwaona majeruhi wa al-Shabaab kijijini.

Kamanda wa polisi wa Tana River, Bw Fredrick Ochieng alisema ripoti ilipigwa katika kituo cha polisi cha Kilelengwani, ambapo mkazi mmoja alisema alikutana na washukiwa 11 akiwa anatafuta kuni msituni.

“Mkazi anasema jamaa hao walimkamata na kutisha kumuua iwapo atafichua habari kuhusu wao kuwepo kijijini,” akasema Bw Ochieng.