Avokado husaidia hasa wanawake kuyeyusha mafuta tumboni – Utafiti

Na Leonard Onyango

KULA parachichi (avocado) kila siku kunaweza saidia wanawake kupunguza mafuta tumboni, kulingana na utafiti uliofanywa nchini Amerika.

Watafiti wa Chuo Kikuu cha Illinois Urbana-Champaign walisema mafuta ya avokado husaidia katika kuyeyusha mafuta tumboni.

“Utafiti wetu umebaini kuwa mafuta kutoka avokado husaidia sana katika kupunguza mafuta tumboni,” ikasema ripoti ya utafiti huo.

Kulingana na watafiti hao, kuna aina mbili za mafuta tumboni mwa binadamu; mafuta ambayo huwa chini ya ngozi (subcutaneous fat), na mafuta ambayo hujilimbikiza ndani ya tumbo, inayojulikana kama mafuta ya utumbo (visceral).

Mafuta ya utumbo huzunguka viungo vya ndani kwenye tumbo.Watu walio na idadi kubwa ya mafuta mazito ya utumbo huwa katika hatari kubwa ya kupata ugonjwa wa kisukari.“Ukikula avokado, kuna uwezekano wa mafuta ya utumbo kuyeyuka haraka,” wakasema watafiti hao.

Wanawake walioshiriki utafiti huo waligawanywa katika makundi mawili; kundi la kwanza walikula avakado kila siku na jingine walikula chakula bila tunda hilo.

Baada ya wiki 12 walipimwa na kubainika kwamba waliokula avokado kila siku walikuwa na kiwango cha chini cha mafuta ikilinganishwa na wenzao.

 

KILIMO: Wanachopaswa kuzingatia wakulima kupata soko la maparachichi ‘majuu’

Na SAMMY WAWERU

KWA mujibu wa takwimu za utafiti wa shirika la International Trade Centre (ITC) mwaka wa 2017, Kenya imeorodheshwa kuwa muuzaji mkuu wa maparachichi kutoka Barani Afrika.

Kulingana na ripoti hiyo ya ITC, Kenya huzalisha kadri ya tani 191,000 kila mwaka.

Aidha, huuza karibu tani 51,507 katika soko la kimataifa na kukadiriwa kuingiza mapato ya Sh8bilioni. Afrika Kusini inafuata kwa karibu, ambapo huuza tani 43,492 kwa mwaka.

Kuimarika kwa kilimo cha maparachichi almaarufu avocado nchini, mwaka uliopita kulitia wakulima wengi tabasamu baada ya kiongozi wa nchi Uhuru Kenyatta na Rais wa China Xi Jinping kutia saini mkataba wa makubaliano wa mazao ya Kenya kuuzwa nchini humo.

Hata hivyo, miezi tisa baadaye tabasamu hiyo haipo baada ya mamlaka ya Kilimo na Chakula Nchini, AFA, kusitisha kwa muda usiojulikana uuzaji wa maparachichi katika soko la nje.

Kulingana na AFA, baadhi ya kampuni na mashirika ya wauzaji mazao nje ya nchi na mawakala wanashinikiza wakulima kuvuna matunda ambayo hayajakomaa, suala ambalo linapaka tope sura ya Kenya katika soko la kimataifa.

Wataalamu wa kilimo wanahoji maparachichi yanapovunwa kabla kukomaa, kilele chake bila shaka kitakuwa kuharibika.

“Avocado ambazo hazijakomaa zikivunwa hazitaiva, zinaharibika,” anaonya Daniel Mwenda kutoka Mwenda D Agroforestry Solutions, shirika la kibinafsi linaloangazia masuala ya miti na matunda.

Kwa mujibu wa maelezo ya mdau huyo, kuna vigezo kadha wa kadha ambavyo vinapaswa kuongoza mkulima kujua iwapo maparachichi yamekomaa. Mosi, mengi hubadilisha rangi Mwenda akieleza kwamba kuna yanayogeuka kijani kuwa kijani kibichi (dark green). “Pia kuna aina ya maparachichi yanayogeuka kuwa meusi,” aongeza kueleza.

Mwenda pia anasema njia nyingine kutambua ikiwa matunda hayo yamehitimu kuvunwa, ni kwa kutikisa “ukiskia sauti ya mbegu inayocheza ndani ni ishara kuwa yamekomaa”.

Mtaalamu huyo hata hivyo anasema mkulima asipozingatia vigezo bora vya kilimo, matunda hayo huanza kuanguka kabla kukomaa. Anaiambia Akilimali kuwa kinachosababisha hilo ni mti wa parachichi kukosa madini faafu ambayo ni Boron na Nitrogen.

“Ni muhimu mkulima kabla kuingilia kilimo chochote kile akaguliwe udongo katika maabara ya shughuli hiyo kujua kiwango chake cha rutuba na asidi,” apendekeza, akiongeza kwamba shamba linalopaniwa kukuzwa avocado udongo utolewe hadi kimo cha futi tano na katika sehemu mbalimbali shambani.

Udongo

Anafafanua kuwa, miti ya maparachichi hupenyeza mizizi yake ardhini hivyo basi ni muhimu udongo kukaguliwa kwa kina. “Mimea kama nyanya udongo wake unaweza kutolewa hadi kimo cha futi mbili, mizizi yake si mirefu ikilinganishwa na ya avocado,” Mwenda asema.

Maparachichi yanastawi maeneo yanayopokea mvua ya kutosha, mtaalamu huyo akipendekeza wakulima kukumbatia mfumo wa kunyunyuzia mimea maji kwa mifereji, ndio Irrigation. Udongo tifutifu na usiotuamisha maji ndio bora.

Lucy Ndung’u ni mkulima wa maparachichi Kaunti ya Murang’a na anasema hukuza aina ya Hass ya kupandikiza. Yanathaminiwa kwa kiasi chake kikuu cha uzalishaji, miti inayodumu zaidi ya miaka 50 pamoja na kuwa na mafutahai. “Soko la Hass si kikwazo kamwe kwa mkulima,” Lucy anasema. Akitilia mkazo kauli hiyo, mtaalamu Mwenda anasema soko la aina ya Fuerte pia linaanza kunoga.

Mwenda anasema ikiwa kuna matunda rahisi mno kukuza yakupe mapato, “yaite maparachichi”. Shamba likiwa tayari, andaa mashimo yenye kina cha urefu wa futi mbili na upana wa futi mbili pia. “Kati ya mashimo na laini, isipungue nafasi ya mita tano,” mtaalamu huyo anashauri.

Udongo wa juu uchanganye na mbolea, kipimo cha asilimia 50 kwa 50. Mchanganyiko huo, urejeshe hadi kimo cha asilimia 90 ya shimo, panda mche kisha umwagilie maji. Asilimia 10 iliyosalia ni ya utunzaji, kwa njia ya mbolea, maji na kuweka nyasi za boji ili kuzuia uvukuzi.

Kulingana na Mwenda, muhimu zaidi katika kilimo cha avocado ni usafi; palizi kila makwekwe yanapomea.

“Mbali na maji na usafi wa hadhi ya juu shambani, pogoa matawi usalie na machache ili mazao yawe bora. Matawi mengi huleta ushindani mkali wa maji na mbolea. Mbolea tumia ile hai ya mifugo na fatalaiza kunawirisha mazao,” ashauri.

Magonjwa sugu katika kilimo cha maparachichi ni Damping-off na Bacterial wilt, wadudu wakiwa viwavi, mchwa na panzi.

Chini ya vigezo bora vya kilimo, mazao ya kwanza yanajiri miezi saba baada ya upanzi. Mwenda anasema kiwango cha mazao huongezeka mparachichi unapoendelea kukomaa, akidokeza kwamba mwaka wa pili na nne huzalisha wastani wa matunda 500, mwaka wa nane ukizalisha hata zaidi ya 1,000. Ekari moja inasitiri kati ya miti 80 – 100.

Maparachichi yanayouzwa nje ya nchi, moja hugharimu kati ya Sh15 – 22.

Mwangi Wa Iria aahidi kuachia Murang’a uchumi wa maparachichi wa hadi Sh32bn

Na MWANGI MUIRURI

GAVANA wa Murang’a, Mwangi wa Iria ameahidi kugeuza Kaunti hiyo kuwa ya uchumi wa maparachichi aina ya Hass ambapo analenga kuzidisha idadi ya miche ya zao hilo hadi 10 milioni akivuka mwaka wa 2023.

Ameambia Taifa Leo katika mahojiano kuwa kwa sasa idadi ya miche ya maparachichi eneo hilo imesimamia kwa 6 milioni na atakuwa akiwapa wakulima wake miche 1 milioni kila mwaka hadi mwaka 2022.

Alisema kuwa kwa sasa pato la ujumla kutokana na zao hilo ni Sh2.5 bilioni kwa mwaka, akiahidi kuwa pato hilo linafaa kupaa mwaka wa 2025 ambapo ile miche atakuwa amepeana hadi mwaka wa 2022 itakuwa imeungana pamoja kwa mavuno.

“Kwa kuwa miche ya Hass huchukua miaka mitatu ndipo ianze kuzaa mavuno ya uhakika.Ile tutakuwa tumepeana mwaka wa 2022 itakuwa imeanza kuvunwa mwaka wa 2025 na ndipo mavuno yote ya miche 10 milioni yatajumuishwa pamoja kama utajiri wa kaunti sokoni,” akasema Wa Iria.

Alisema kuwa mti mmoja wa Hass ukikomaa unaweza ukatoa maparachichi 1, 000 kumaanisha kuwa miche 10 milioni inaweza ikatoa maparachichi 1 bilioni.

“Sokoni, bei ya tunda moja la Hass kulingana na gredi huwa katika kiwango cha kati ya Sh8 na Sh32. Hii ina maana kuwa tunaweza tukaafikia pato la ujumla la kati ya Sh8 bilioni na Sh32 bilioni,” akasema.

Ushirika

Alisema kuwa kwa sasa ameunganisha wakulima 250, 000 katika vikundi vya uzalishaji Hass na ambapo wako katika makundi ndani ya wadi zao na hatimaye kuunda muungano mmoja wa ushirika wa Kaunti.

Alisema kuwa muungano huu umesaidia sana katika kuwafikia wakulima na vifaa muhimu na pia kusaka soko la uhakika na pia kupiga vita upenyo wa madalali katika sekta hii ya maparachichi.

Alisema kuwa kwa sasa bei imeimarika katika soko la Ulaya na pia la Bara Asia akiongeza kuwa kwa sasa serikali yake itaweka mikakati ya kuwasaidia wakulima hao kuafikia masharti ya soko la kimataifa.

Nyeri kupata kiwanda cha maparachichi

Na SAMMY WAWERU

GAVANA Mutahi Kahiga amesema serikali ya kaunti ya Nyeri inapania kuunda kiwanda cha maparachichi ili kupiga jeki ukuzaji wa zao hili.

Amesema hatua hii pia inalenga kufanya maparachichi kuwa miongoni mwa mazao yanayoingizia wakulima mapato.

Akizungumza Jumatatu akiwa Nyeri, Gavana Kahiga amesema mradi huu umepangiwa kugharimu kiasi cha Sh50 milioni.

“Wakulima eneo hili wamekuwa wakitegemea majanichai na kahawa, mazao ambayo hayajakuwa yakiwalipa vizuri. Tumeanza kuwekeza pakubwa katika kilimo cha maparachichi kwa sababu yana soko zuri ndani na nje ya nchi. Hayachukui nafasi kubwa ya shamba,” amesema Kahiga.

Kwa muda wa miaka miwili iliyopita, Serikali ya Kaunti ya Nyeri imeonekana kuwa katika mstari wa mbele kuhimiza wakulima humo kuvalia njuga ukuzaji wa matunda haya.

Aidha, imekuwa ikisambaza miche kwa wakulima bila malipo sawa na kaunti ya Murang’a.

“Kiwanda hicho kitakuwa cha kusindika; kuyasafisha, kuchagua na kuyapakia ili kuuzwa nje ya nchi,” amefafanua, akidokeza kwamba kitajengwa eneo la Kiawaiganjo.

Aprili 2019 Kenya ilitia saini mkataba wa kuuza maparachichi nchini China.

Rais Uhuru Kenyatta alisema mpango huo utasaidia kuinua kilimo cha avocado hapa nchini.

Ni hatua ambayo ilikabirishwa vyema na Wakenya, hasa wakulima.

Hata hivyo, kuna baadhi ya waliozua mjadala wakihoji mikakati maalum iwekwe ili kufanikisha mpango huo ili kuepuka kupunjwa na mawakala.

“Serikali inapaswa kuwa na miungano itakayoleta pamoja wakulima wa maparachichi ili wasipunjwe na mawakala. Itakuwa rahisi mazao yao kukusanywa na kuuzwa China,” anapendekeza Daniel Mwenda, mtaalamu wa masuala ya kilimo hasa matunda.

Mdau huyu pia anahimiza wakulima kujiunga na vyama vya ushirika (Sacco) ili kuwatafutia soko la mazao yao. Bw Mwenda anapongeza serikali ya kaunti ya Nyeri kwa mpango wa kubuni kiwanda cha maparachichi, akieleza kwamba hatua hiyo itawainua kimapato.

Bi Agnes Njambi, mkulima Nyeri ameambia Taifa Leo mikakati ya serikali ya kaunti hiyo italeta afueni kwa wakulima wa maparachichi.

Baadhi ya wakulima eneo hilo wamekuwa waking’oa mikahawa na majani chai ili kupanda maparachichi, hasa ya hass.

Hass ni maparachichi yaliyoimarishwa kwa njia ya kupandikiza na yenye mazao ya kuridhisha.

Mkondo huo umeonekana kuigwa na kaunti ya Kericho, Nandi na hata Uasin Gishu, kupitia shinikizo la viongozi. Avocado za kupandikiza huchukua muda wa kati ya miaka mitatu hadi minne ili kuanza kuzalisha matunda baada ya upanzi.

AKILIMALI: Mmoja wa walioitikia wito kukuza parachichi

Na CHRIS ADUNGO

INGAWA kilimo cha parachichi kinafanywa na wakulima wadogo wadogo wa hapa nchini, kuna pengo kubwa katika juhudi za kufanikisha soko la mazao haya kimataifa.

Katika viwanda, parachichi hutumiwa kutoa mafuta ya upishi na pia bidhaa nyingine za kutengenezea dawa za kila sampuli.

Katika kijiji cha Nyangati, eneo la Mwea katika Kaunti ya Kirinyaga, mkulima Judy Warware Kamanga anasema kwamba amekuwa akijishughulisha na kilimo cha parachichi na maembe kutoka mwaka wa 2002.

Kwa kawaida, mparachichi huchukua muda wa miaka mitatu kabla ya kukomaa na kuanza kutoa mazao.

Bi Warware alianza kwa kupanda mbegu katika kipande maalumu shambani mwake.

Baada ya miezi miwili, miche 12 ikawa imefaulu kuota na hapo akaihamisha na kuipanda katika sehemu nyinginezo za shamba lake kubwa.

Aliipanda miche hii katika mashimo aliyoyachimba hadi kufikia urefu wa futi moja na upana wa futi mbili.

Kisha katika siku za mwanzo mwanzo alihakikisha kuwa ananyunyizia mimea maji mara kwa mara.

Siku zilizofuata, Bi Warware alihakikisha kuwa amepalilia mimea yake ili kupunguza ushindani mkubwa wa kupata maji na madini muhimu kutokana na magugu.

Dawa

Kulingana naye, alihitajika pia kunyunyuzia dawa za kuzuia wadudu hatari.

Katika mwaka wa 2010 alipata mavuno kwa mara ya kwanza, ijapokuwa si kwa wingi.

Lakini miaka iliyofuata, mavuno yaliongezeka maradufu.

Kila mwaka, yeye huvuna parachichi kati ya Februari hadi Juni na kuwauzia wafanyabiashara wadogo wadogo au baadhi ya kampuni zinazouza parachichi au bidhaa kutokana na zao hili katika nchi za kigeni.

Miparachichi anayoipanda ni aina ya Kent na anapovuna, mparachichi mmoja huweza kumtolea zaidi ya maparachichi 1,000 katika msimu mzima wa mavuno.

Na kwa hivyo, katika msimu wa mavuno wa muda wa miezi minne hivi, ana uwezo wa kupata maparachichi zaidi ya 12,000.

Anapouza mazao yake, parachichi moja hunadiwa kwa kati ya shilingi tano hadi Sh10 kulingana na ukubwa wa tunda au hali ya soko ilivyo.

Anasema mparachichi mmoja una uwezo wa kutoa mazao mengi kadri mti unavyozidi kukomaa.

Kulingana na Bi Warware, kilimo cha parachchi kina faida na huwa kinamwezesha kupata riziki ya kila siku kwani shughuli za kilimo kwake ni sawa na ajira rasmi.

Zaidi, amewezeza pia kuwasomesha wanawe watatu kupitia kwa mapato yanayotokana na kilimo cha parachichi.

Anaeleza kuwa kilimo cha parachichi hakihitaji muda mwingi wa kuwa shambani kwani mmea unapokomaa, mkulima huhitajika tu kupalilia na kutilia dawa mimea yake ili kuitunza ipasavyo.

Baadhi ya changamoto anazokumbana nazo ni pamoja na bei ya chini ya parachichi anapowauzia wafanyabiashara wadogowadogo ambao hununua kwa bei ya chini ilhali wanapofikisha mazao haya sokoni, hupata faida kubwa kwa kuwauzia wateja kwa bei ghali zaidi.

Mbali na magonjwa ya kila sampuli hasa yanayotokana na kiangazi au baridi kali kupita kiasi, changamoto nyingine ni mvua ya mawe inayoharibu matunda au kuoza kwa maparachichi iwapo soko litakosekana baada ya zao kukomaa shambani.

Ushauri wake ni pawepo na mipango maalum kutoka kwa serikali ya Kaunti ya Kirinyaga, ya kutafuta masoko ya kigeni ili wakulima wa parachichi wafaidike zaidi.

“Wakulima wengi wa parachichi hawana ujuzi mwingi wa teknolojia ya kisasa inayohitajika kuboresha au kuongeza mazao yao. Hivyo basi, litakuwa jambo la busara kwa wakulima kuelimishwa na maafisa wa kilimo wa serikali,” Bi Warware anasema.

Mnamo 2012, aliboresha mradi wake akaanza kupandikiza (grafting) na hatimaye akazalisha aina ya avokado za kisasa ambazo ni chotara (Hass) kwa mtaji uliogharimu hadi Sh15,000.

Mavuno yake yanapokuwa tayari, huhifadhiwa vizuri katika eneo lenye joto kiasi na sehemu isiyokuwa na unyevu.

Kulingana na muda, mkulima atafahamu kuwa maparachichi yamekuwa mabivu na tayari kuliwa iwapo mazao yataanza kubadilisha rangi na unapotomasa tunda bivu au lililoiva, hubonyea.

Kinyume na maparachichi ya kawaida, mche mmoja uliopandikizwa unaweza kumpatia Bi Warware kati ya matunda 300-500 kwa msimu mmoja.

Uwezo wa kuzaliwa kwa matunda huongezeka kadri muda unavyokuwa.

Miche kukomaa

Miche inapotimu umri wa miaka mitano, huwa imekomaa na mkulima anaweza kupata hadi parachichi 1,500 kila mwaka.
Katika gunia moja lililoshonwa vizuri, Bi Warware hupakia kati ya avokado 400-600.

Bei ya maparachichi haya yaliyozaliwa kwa upandikizaji ya Hass ni Sh15 kwa kila tunda.

Inapomlazimu kusafirisha maparachichi yake hadi masoko ya mbali nje ya Kaunti ya Kirinyaga, tunda moja huuzwa kwa hadi Sh25 ili kufidia gharama kubwa ya usafirishaji.

Katika sehemu ya robo ekari ya shamba lake kwa sasa, amepanda mbegu 10,000 ambazo kabla ya kupandwa, alizitibu ili kuzuia magonjwa yanayotokana na mchanga.

Katika shughuli za upanzi, Bi Warware huwa anaajiri wafanyakazi ambao humsaidia kutia mbolea ya mbuzi katika mifuko ya vijikaratasi kisha kuweka mbegu.

Baada ya hapo, kazi huwa ni kunyunyizia maji kila siku na kwa kawaida, miparachichi hii huchukua mwezi mmoja ili kukua.

Kulingana naye, huwa anaanza kupandikiza miche hii baada ya miezi miwili kutoka siku ya upanzi.

Madhumuni ya upandikizi ni kupata aina bora ya maparachichi yatakayowavutia wateja.

Kwa kawaida, ana aina mbili za avokado ambazo ni ‘Hass’ na ‘Fuerte’. Anasema aina hizi mbili ndizo zinahitajika sokoni kwa wingi.

“Lengo hasa la kufanya upandikizi ni kuhakikisha kuwa aina sawa ya maparachichi imepatikana; na zaidi ni kupunguza muda wa parachichi kukua na kukomaa,” anasema.

Katika misimu ya mvua, huwa anauza miche mingi ya miparachichi ikilinganishwa na misimu mingine katika mwaka.

Anasema kwamba kila mwaka ana uwezo wa kuuza hadi miche 10,000 ambapo mche mmoja huuzwa kwa Sh150.

Ina maana kwamba kwa kipindi cha miezi 12, Bi Warware ana uwezo wa kujivunia zaidi ya Sh1.5 milioni.