MAPISHI: Kuku kienyeji

Na MARGARET MAINA

mwmaina@ke.nationmedia

Muda wa kuandaa: Dakika 1

Muda wa mapishi: Saa 1

Walaji: 4

Vinavyohitajika

· kuku wa kienyeji 1

· vitunguu maji 3

· vitunguu saumu punje 2 zilizobondwa

· unga wa binzari

· pilipili manga

· mafuta ya kupikia

· giligilani

· tangawizi

· nyanya tatu

· juisi ya limau

Maelekezo

Katakata na uchemshe kuku wako pamoja na tangawizi, kitunguu saumu, unga wa binzari, pilipili manga, chumvi na ndimu ili kuweka ladha nzuri.

Acha vipande vya kuku viive.

Nyama ya kuku ikishaiva itoe katika supu na uiweke pembeni.

Katika sufuria tofauti, tia mafuta ya kupikia na yakishachemka, kaanga kuku wako hadi awe rangi ya kahawia. Kisha toa minofu ya kuku katika mafuta ili utumie mafuta hayo kwa kuweka vitunguu na ukaange kwa dakika tano.

Sasa weka unga wa binzari, unga wa giligilani, na mbegu za pilipili manga.

Changanya vizuri hadi upate mchanganyiko mzuri mkavu halafu miminia humo ile supu uliyoiacha hapo awali.

Weka pembeni ipoe kisha kaanga nyanya zako katika sufuria tofauti vile vile na upike hadi maji yaishe na ibakie kama mafuta yakielea kwa juu.

Mimina sosi yako katika kuku na punguza moto acha vichemke ili viungo vichanganyike na kuleta ladha nzuri. Utakapoona mchuzi umeisha, unaweza epua na kuweka pembeni.

Hapo nyama ya kuku itakuwa tayari kuliwa na chochote utakachopenda.

‘Nimeandaa mapishi 25 kutoka nchi mbalimbali Afrika na Ulayani’

Na MAGDALENE WANJA

Bi Ayumi Yamamoto alizaliwa na kulelewa katika mji wa Osaka nchini Japan ambapo alisoma na kuhitimu katika kozi ya Ukulima katika chuo kikuu.

Baadaye, alipata kazi ya kuwa mwalimu katika somo hilo hadimwaka 2011 alipoingia nchini Kenya.

Alisafiri hadi nchini Kenya kufanya kazi ya volunteer na shirika la Overseas Cooperative Volunteer ambalo ni shirika la serikali ya Japan.

Baada ya miaka miwili unusu,alianza biashara ya kuuza matunda yaliyokaushwa katika kampuni inayojulikana kama Kenya Fruits Solutions.

Alipokuwa akifanya kazi hizi, aligundua kwamba kulikuwana hitaji kubwa ya huduma za kuwapelekea wateja chakula(delivery) katika nyumba zao mjini Nairobi.

Aliwaza jinsi angeweza kuleta suluhisho katika sekta hii na akaamua kutengeneza mealkits.

“Baada ya kufanya kazi katika sekta mbalimbali za lishe, nilitamani sana kufanya biashara ya kuuza ama kuandaa chakula” alisema Yamamoto.

“Nilishangazwa piana insihitaji la chakula liliendelea kukua kila siku mjini Nairobina nikaiona kama nafasi nzuri ya biashara,” aliongeza Yamamoto.

Baadhi ya vyakula anavyoandaa Bi Ayumi Yamamoto. Picha- MAGDALENE WANJA

Baada ya kufanya matayarisho yote mnamo mwaka 2019, aliweza kuanzisha kampuni yake ambayo aliiita Love and Meals.

Wazo lake la kutengeneza Meal Kits pia lilichangiwa na ujuzi alioupata kutoka kwa watu aliotangamana naokutoka sehemu mbalimbali ulimwenguni.

Ndani ya meal kit, Bi Yamamoto humuandalia mteja wake vinavyohitajika kuandaa aina fulani ya chakula kisha anakuandalia maandishi ya muongozo wa jinsi ya kukitayarisha chakula hicho.

Kwa meal kit moja,kampuni yake hulipisha kuanzia Sh1,050 ambayo pia huhuandamana na iloe ya usafirishaji.

Huduma hii hupatikana mtandaoni ambapo mteja hujichagulia anachohitaji na kasha kupeana maagizo kupitia program hio ya simu.

“Lengo letu ni kuwafanya wateja wetu kuridhika na huduma zetu huku tukirahisisha kazi ya upishi haswa kwa watu ambao hawana muda wakutosha wa kujiandalia mlo wanaotaka kutokana na ukosefu wa muda au kutojua jinsi ya kuandaa,” aliongeza.

Kufikia sasa, Yamamoto ameweza kuandaa mapishi 25 kutoka nchi mbalimbali barani Afrika na Ulayani.

Ndoto yake ni yake ni kuendeleza huduma zake katika miji mingine mikuu nchini na mataifa mengine.

Vyakula hivi si vya kuliwa kila mara

Na MARGARET MAINA

mwmaina@ke.nationmedia.com

MWONEKANO wetu na afya ya mwili na akili unajengwa na chakula.

Madhara ya chakula tunachotumia vinazeesha ngozi kwa haraka na ni muhimu kuvijua na kuviepuka.

Ijapokua tunavipenda vyakula hivi, vina athari mbaya kwa miili yetu na muhimu kujifunza tabia ya kuviacha katika milo yetu. Kama si rahisi kuacha kabisa basi angalau kupunguza matumizi yake.

Nyama nyekundu

Mojawapo ya vyakula vinavyozeesha ngozi ni nyama hasa nyama nyekundu. Nyama nyekundu inayotokana na wanyama kama ng’ombe, mbuzi, kondoo na kadhalika, ni mbaya kwa afya njema ya binadamu na hivyo kwa ngozi pia.

Nyama nyekundu ina kemikali aina ya carnitine ambayo inafanya mishipa ya damu kukakamaa na kusababisha kuzeeka kwa ngozi.

Chumvi

Chumvi hasa yenye madini ya iodine ni mbaya sana kwa afya ya ngozi. Inasababisha chembechembe za nyama katika ngozi kuvimba.

Sukari

Sukari japo tunaipenda sana inaweza ikawa na madhara ya afya ya binadamu. Inadhoofisha mfumo wa kinga za mwili. Kiasi kingi cha sukari mwilini kinafanya ngozi kuwa kavu na kufanya mwili utengeneze makunyazi kwa sababu inaharibu kemikali ya collagen na elastin ambazo zinafanya kazi ya matengenezo ya ngozi kwa kuifanya isiharibike na kuwa chakavu.

Sukari nyingi inasababisha mwili kukosa nguvu ya kupambana na bakteria. Ongezeko la bakteria hufanya utengenezwaji wa kemikali mbaya ambazo husababisha uchakavu wa ngozi.

Watu wanashauriwa kutumia sukari asilia kama ya matunda na asali kuliko zile zinazopatikana katika vinywaji kama soda,biskuti au vitafunwa vingine vyenye sukari ya kuongeza.

Vyakula vya kukaangwa

Vyakula vya kukaangwa kama chips,nyama za kukaanga vinasababisha uingizaji wa mafuta mengi mwilini. Mafuta haya yana “Free Radicals” yanayosababisha uzibaji wa vijitundu katika ngozi. mafuta mengi mwilini yanasababisha madhara mengi mengine yakiwemo magonjwa ya moyo na kisukari.

Mkate mweupe, pasta na keki

Vyakula hivi vina kemikali ya glucemic kwa kiwango kikubwa ambayo inaleta madhara ya magonjwa ya ngozi

Pombe

Unywaji wa pombe unasababisha kupoteza maji mengi mwilini kwa njia ya mkojo na huleta madhara mabaya kwa ngozi kwa kuifanya iwe kavu.

Kahawa

Kemikali ya caffeine iliyomo kwenye kahawa na vinywaji vingine inasababisha ukosefu wa maji ya kutosha katika ngozi na kuifanya iwe kavu. Lakini pia caffeine inasababisha utengenezwaji wa kemikali ya cortisol ambayo inachangia uzeekaji wa ngozi.

Jinsi ya kuandaa mlo mtamu wa biriani ya nyama ya mbuzi

Na MARY WANGARI

WIKENDI ni wakati murwa sana wa kutangamana na kuwa na muda na familia na wapendwa.

Ni njia gani nyingine bora zaidi kama kufurahia wakati huo mkishiriki na kujiburudisha kwa mapochopocho ya chakula kitamu kilichoandaliwa kwa ustadi wa hali ya juu?

Hii leo tutajifahamisha jinsi ya kuandaa mlo mtamu wa biryani kwa nyama ya mbuzi.

Utahitaji viungo vifuatavyo

½ kilogramu ya mchele aina ya Basmati

¾ kilogramu ya nyama ya mbuzi

½ kilogramu mafuta ya kupikia

5 viazi mbatata vikubwa

1 karoti kubwa iliyoparwa

1 hoho iliyokatwa vipande vidogo vidogo

4 vitunguu maji vikubwa

4 nyanya kubwa

1 nyanya ya mkebe

I kijiko biryani masala

½ kijiko cha sukari

1kikombe cha mtindi au ukipenda maziwa yaliyogandishwa

½ kijiko cha chumvi unaweza ukongeza au kupunguza

1 ndimu moja kubwa au siki

1 kijiko cha iliki illiyotwangwa

1 kijiko cha tangawizi

1 kiijiko cha curry powder

Maji safi ya kupikia

Maandalizi

Safisha mchele na kisha uuroweke kwa maji robo saa.

Katakata nyama vipande vipande kisha uioshe na kuiweka katika karai safi.

Ongeza iliki, tangawizi, curry powder, chumvi na uchanganye viungo hivyo na nyama hadi vichanganyike vyema.

Menya vitunguum, vioshe, katakata vipande vyembamba vya mviringo na uviweke pembeni.

Menya viazi, vioshe na uviweke kando.

Saga nyama au uipare

Rosti la Biriani

Katika sufuria safi weka nyama na kuibandika kwenye moto wa wastan.

Iruhusu ikauke maji yake na kisha uongeze maji taratibu na usubiri itokote hadi kuwa laini.

Katika sufuria nyingine, mimina mafuta na kubandika kwenye moto kisha ongeza vitunguu na kuvikoroga koroga hadi vigeuke rangi kuwa ya dhahabu.

Toa vitunguu na kisha ukaange viazi mbatata kwa dakika chache, kisha kanga karoti, pilipili hoho na uongeze iliki.

Ongeza nyanya kwenye viazi na kuruhusu viive kwa dakika tatu.

Kisha mimina nyama na supu yake na kuacha mchanganyiko huo utokote kwa dakika kadhaa

Ongeza nyanya ya mkebe, siki na mtindi na kuviruhusu vitokote.

Ongeza viungo vilivyosalia kama vile pilau, biriani masala na sukari koroga na uace vichemke.

Ongeza vitunguu ulivyokaanga na kuweka kando hapo awali.

Ruhusu rosti lako litokote kwa dakika tano na kisha uepue.

Wali wa Biriani

Mimina maji kwenye sufuria safi na uongeze chumvi.

Yakishachemka, ongeza mchele na uache utokote kwenye moto wa wastan hadi uive.

Nyunyizia mafuta, funika na uruhusu ukauke maji.

Chukua rosti la biryani na weka kwenye wali wako kisha uchanganye vyema.

Biryani yako sasa ipo tayari kuliwa. Epua, pakua na ufurahie mlo wako.

Mapishi ya samaki aina ya salmon

Na MARGARET MAINA

mwmaina@ke.nationmedia.com

WAKATI mwingine mtu anakuwa amechoka na hangependa kupoteza muda jikoni.

Hivyo basi, kuandaa mlo wa haraka linakuwa ni wazo nzuri.

Mlo huu ni rahisi kuuandaa na hata haikuchukui zaidi ya dakika ishirini chakula kinakuwa tayari mezani.

Muda wa kuandaa: Dakika 15

Muda wa mapishi: Dakika 20

Walaji: 2

Vinavyohitajika

 • salmon fillet 2
 • viazi 2
 • mboga ya lettuce kiasi
 • nyanya 2
 • limau 1
 • saumu
 • chumvi
 • mafuta ya mizeituni

Maelekezo

Marinate samaki kwa kuhakikisha unaweka chumvi na kitunguu saumu kilichopondwa na nusu ya limau. Weke samaki pembeni.

Washa ovena kisha tia viazi ulivyovikatakata. Vikisha karibia kuiva, anza kupika samaki. Tia mafuta kidogo sana kama kijiko kimoja cha chai hivi katika kikaangio ambacho chakula hakishiki chini. Mafuta yakishachemka kiasi weka samaki wako (upande wenye ngozi chini kwanza).

Pika samaki mpaka uone rangi ya kahawia kwa chini kisha geuze upande wa pili.

Huku samaki wako akiwa anaendelea kuiva, tayarisha saladi yako kwa kusafisha mboga ya lettuce na nyanya kisha changanya pamoja. Kisha tengeneza salad dressing pembeni , kamua limau kisha tia mafuta ya mizeituni na chumvi kiasi.

Baada ya hapo samaki na viazi vitakuwa vimeiva. Andaa mlo wako na utakuwa tayari kuliwa.

Jinsi ya kujiandalia chipsi

Na DIANA MUTHEU

Muda: dakika 45

Walaji: watu 5

Chipsi ni miongoni mwa vyakula ambavyo vinapendwa na watu wengi haswa wanaoishi mjini, kutokana na wingi wa hoteli na hata vibanda vinavyouza chakula hicho. Kwa mtu yeyote ambaye anapenda chipsi, anaweza kujipikia mwenyewe nyumbani na akafurahia bila kulazimika kwenda hotelini kuinunua.

Vinavyohitajika

1.Viazi kilo 3

2.Mafuta ya kupika lita 1.5

3.Karai ya kukaangia viazi

4.Chumvi

5. Sosi ya nyanya (Tomato sauce)

Jinsi ya kuandaa

Vioshe viazi vyako ili uondoe matope yoyote kisha uvichambue ngozi na uviweke ndani ya maji safi kwa muda wa dakika 15.

Baada ya dakika 15, mwaga maji hayo kisha uvioshe viazi kwa maji mengine safi.

Kata viazi vyote katika umbo la mduara kwanza, kisha uvikate kate tena kwa vipande vilivyo na maumbo sawia na mstatili na uvitumbukize ndani ya maji safi kwa muda wa dakika 5.

Mwaga maji hayo, kisha utumie kichungi kikubwa kukausha maji kabisa katika viazi zako.

Injika karai yako ya kukaangia viazi juu ya moto, kisha uyamwage mafuta yako na uyawache yawe moto sana, kiwango cha kuchemka.

Chukua vipande vyako vya viazi na uvimwage taratibu ndani ya karai yenye mafuta moto, kisha uviwache viive vyenyewe kwa muda wa dakika 15, hadi vikauke vizuri.

Tumia kijiko chenye matundu kuepua viazi vyako ili kuhakikisha mafuta yanachungwa vizuri.

Katika mkebe au sahani unapoweka chipsi zako, tandika kitambaa au serviette ili visaidie kukausha mafuta zaidi katika chipsi hizo.

Waeza andaa pamoja na saladi na soseji.

 

 

LISHE: Meat pie yaweza ikaandaliwa kwa njia rahisi jinsi ilivyoelezwa hapa

Na MARGARET MAINA

mwmaina@ke.nationmedia.com

Muda wa kuandaa: Dakika 40

Muda wa mapishi: Dakika 50

Walaji: 5

Vinavyohitajika

• unga wa ngano kilo 1

• siagi kopo 1

• nyama ya kusaga kilo moja na nusu

• pilipili

• mayai 4

• chumvi kiasi

• sukari vijiko 3

• maziwa vikombe 3

• viazi 4

Meat pie. Picha/ Margaret Maina

Maelekezo

Weka unga wa ngano katika bakuli kubwa kisha chemsha siagi hadi iwe ya moto kabisa. Changanya mayai na siagi vizuri.

Weka chumvi na sukari katika bakuli ya unga changanya vizuri kisha mwagilia mchanganyiko wa siagi na mayai; endelea kuchanganya ili unga wote ukolee siagi na mayai.

Mimina hapo maziwa na uanze kukanda unga wako. Hakikisha unaukanda hadi uwe laini.

Chukua nyama ya kusaga – kima – ambayo umeikaanga kidogo kwa viungo, chumvi, pilipilipili, Royco na maji ya ndimu.

Chukua viazi ambavyo umechemsha na kuviponda; changanya pamoja kwenye nyama.

Kata sehemu kiasi ya unga kisha sukuma kama chapati.

Katikati tia mchanganyiko wako wa nyama na viazi kisha kunja kwa kukutanisha pembe ya mwanzo na mwisho. Chukua uma uutumie kubania.

Paka siaagi kwenye chombo cha kuokea na anza kupanga meat pie yako hapo.

Baada ya kupanga, paka kwenye kila meat pie kwa juu ukifuatia na siagi.

Halafu tia katika ovena uoke kwa dakika 40 kwa moto uliodhibitiwa kwa nyuzi 200

Epua na ikipoa furahia ama kwa chai, juisi au chochote ukipendacho.

Meat pie katika sahani. Picha/ Margaret Maina

MAPISHI: Bajia za manjano

Na DIANA MUTHEU

dmutheu@ke.ntionmedia.com

BAJIA ZA VIAZI (Manjano)

MUDA huu ambapo watu wametulia nyumbani kujikinga dhidi ya maambukizi ya maradhi ya Covid-19, ni vizuri kujitosa jikoni na kujifunza jinsi ya kupika vitafunio ambavyo havihitaji ujuzi mwingi.

Vinavyohitajika

 1. Unga wa bajia (gram flour)
 2. Viazi
 3. Mafuta ya kupika
 4. Maji
 5. Dania
 6. Sufuria nzito/ karai ya kupikia
 7. Chumvi

Maelekezo

Chonga viazi vyako kisha uvikate kwa vipande vyembamba vyenye umbo la duara kisha uviweke kwa sahani au bakuli safi.

Kata dania yako na uweke kwa sahani nyingine.

Katika bakuli nyingine safi, changanya unga wa bajia, chumvi ya kutosha na maji. Hakikisha kuwa mchanganyo huo unashikamana vizuri lakini usiwe mzito sana. Kisha ongeza dania yako na ukoroge vizuri.

Chukua viazi vyako kisha uvimwage ndani ya bakuli iliyo na mchanganyo wa unga, na uchanganye vizuri.

Choma viazi vyako katika mafuta moto.

Pakua na ufurahie.

Jinsi ya kupika spring rolls

Na MARGARET MAINA

mwmaina@ke.nationmedia.com

Muda wa matayarisho: Dakika 20

Muda wa mapishi: Dakika 30

Walaji: 5

Vinavyohitajika

 • kima nusu kilo
 • kabichi nusu kipande
 • kitunguu maji
 • pilipili mboga 1
 • kotmiri kifungu 1
 • chumvi kiasi
 • tangawizi 1
 • karoti 1
 • pilipili manga kijiko nusu
 • kitunguu saumu cha unga kiasi cha kijiko nusu
Spring rolls. Picha/ Margaret Maina

Maelekezo

Pika nyama na viungo; tangawizi, kitunguu maji, kitunguu saumu na pilipili manga hadi viwe na ukavu. Hakishisha maji yanakauka kabisa.

Chukua karoti na uikwangue.

Kata kabichi vipande vyembambavyembamba, kata pilipili mboga kwa vipande vidogovidogo. Unatakiwa uoshe vizuri kabla ya kukata.

Malizia kukata kotmiri kisha chukua sufuria bandika mekoni halafu tia mafuta kijiko kimoja cha kupikia. Mimina mbogamboga zako huku ukikoroga kisha weka kotmiri na uache kwa muda wa dakika moja.

Epua, changanya nyama na pilipili manga kisha acha ipoe kwanza wakati unakanda unga wa chapati za kufungia.

Jaza nyama sehemu ya mwanzo wa manda kwenye kona moja.

Fanya mkunjo wa roll, ukifika katikati fanya ni kama unaikunja pande mbili – kulia na kushoto – na endelea ku-roll kisha paka yai kwa kutumia brashi maalum inayotumika wakati wa mapishi. Vilevile paka upande wa sehemu ya umbo la pembe lililobaki na ukunje.

Tia mafuta ya kupikia katika kikaangio, yakipata moto, tia Spring rolls na ziikaange hadi zigeuke rangi na kuwa za kahawia.

Epua na zichuje mafuta tayari kuliwa.

MAPISHI NA UOKAJI: Jinsi ya kupika mkate tambarare uitwao naan

Na MARGARET MAINA

mwmaina@ke.nationmedia.com

Muda wa kuandaa: Saa moja

Muda wa mapishi: Dakika 30

Walaji: 5

Vinavyohitajika

• unga wa ngano gramu 500

• kijiko kidogo cha hamira

• maji fufutende kikombe 1

• kijiko 1 cha chai cha chumvi

• kijiko 1 cha sukari

• kijiko kikubwa cha siagi

Unga uliokandwa. Picha/ Margaret Maina

Maelekezo

Changanya katika bakuli hamira, maji fufutende na sukari kisha koroga mpaka hamira iyeyuke kabisa. Ukisha fanya hivyo, weka kando kwa muda wa dakika tano.

Weka unga wa ngano, chumvi na uchanganye vizuri.

Mwagia yale maji yenye mchanganyiko wa hamira na uanze kukanda vizuri unga wako. Hakikisha umeshikana na ni laini au mwororo.

Baada ya kukanda, funika bakuli lako kwa taulo ya jikoni kisha weka sehemu yenye joto la kutosha na acha unga uumuke kwa muda wa saa moja.

Sasa toa mchanganyiko wako wa unga na uanze kuukanda tena kwa dakika tano kabla ya kuanza kugawanisha katika maumbo madogo.

Mwagia unga kiasi juu ya meza kusaidia maumbo hayo yasishike – kukwama – na anza kusukuma kwa kutumia mpini.

Mkate wa naan ukiandaliwa katika kikaangio. Picha/ Margaret Maina

Kisha chukua mkate wako wa Naan, pika bila mafuta halafu paka siagi juu ya mkate wako. Unapoanza kubadilika rangi geuza na paka tena siagi upande wa pili.

Mkate wake huu wa naan ukiiva, epua na pakua na ule huku ukitumia rojo ya mchuzi au supu.

MAPISHI: Jinsi ya kupika matumbo ya mbuzi

Na MARGARET MAINA

mwmaina@ke.nationmedia.com

Muda wa kuandaa: Dakika 15

Muda wa kupika: Saa 1

Walaji :5

Vinavyohitajika

Matumbo kilo 1

Nyanya 2

Vitunguu maji 2

Dania

Kitunguu saumu

Mafuta ya kupikia

Pilipili mboga

Royco

Matumbo ya mbuzi. Picha/ Margaret Maina

Maelekezo

Yaoshe matumbo kisha uyachemshe kwa muda wa saa tatu kabla ya kuyakatakata kuwa vipande vidogovidogo.

Kaanga vitunguu vyote viwili ukitumia mafuta kiasi kwa muda wa dakika mbili hivi kisha uongeze viungo vingine uvipendavyo ili kuongeza ladha.

Ongeza matumbo yako yaliyokatwakatwa kisha mimina chumvi kiasi. Ongeza maji kiasi kisha upike kwa muda wa dakika tatu hivi.

Ongeza nyanya, dania na pilipili mboga. Koroga kisha ufunike kwa muda wa dakika tano.

Pakua kwa sima, wali au chochote ukipendacho na ufurahie.

MAPISHI: Mahamri

Na MARGARET MAINA

mwmaina@ke.nationmedia.com

Muda wa maandalizi: Dakika 20

Muda wa mapishi: Dakika 40

Walaji: 5

Vinavyohitajika

Unga wa ngano vikombe 4

Sukari ¼ kikombe

Tui la nazi kikombe 1½

Mafuta ya kupikia

Hamira kijiko 1

Iliki kijiko cha chai 1

Unga wa maziwa vijiko 2

Maelekezo

Weka unga wa ngano kwenye bakuli uchanganye na maziwa ya unga au maziwa ya poda yaani powder milk.

Kwenye mchanganyiko huo, weka sukari, hamira, iliki, mafuta na tui na ukoroge mpaka sukari iyeyuke.

Changanya pamoja na unga mpaka vyote vichanganyike vizuri. Hakikisha unga hauwi mgumu na hauwi laini sana kama wa chapati.

Tengeza madonge ya kiasi, uyachovye kwenye unga kisha uyapange kwenye sahani na uyafunike.

Hakikisha madonge hayo unayapanga mbali mbali ili uyapatie nafasi ya kuumuka.

Yaache madonge kwa muda wa saa nzima mpaka yafure vizuri.

Bandika sufuria au kikaangio chenye mafuta ya kupikia motoni ili yaendelee kushika moto.

Sukuma mahamri na uyakate kwa shepu au maumbo upendayo. Pia usisukume donge sana mpaka likawa lembamba kama chapati.

Mahamri kabla kutumbukizwa kwa mafuta yakiwa na maumbo ya pembetatu. Picha/ Margaret Maina

Mafuta yakishika moto vizuri, weka mahamri yako na uyapike mpaka yawe na rangi ya kupendeza – kahawia – pande zote mbili.

Epua; yakipoa pakua na ufurahie.

MAPISHI NA UOKAJI: Ivy Namulanda ni mpishi aliyetamani awe daktari wa maradhi ya ngozi

Na MAGDALENE WANJA

BI Ivy Namulanda alikuwa na ndoto ya kuwa daktari wa maradhi ya ngozi ili kuwasaidia watu wengi aliotangamana nao ambao walisumbuliwa na vipele, chunusi na matatizo mengineyo kama kuchubuka ngozi.

Hata hivyo, alipokamilisha elimu ya shule ya upili, ndoto yake ilionekana kuchukua mkondo tofauti.

Alitaka sana kuwa mpishi hodari ila ilimbidi – ilimlazimu – kujiunga na chuo kikuu ili asomee kozi ambayo ingewafurahisha wazazi wake.

Keki. Picha/ Magdalene Wanja

“Sikuwa na uhakika wa taaluma ambayo nilitaka kuisomea. Wakati mwingine, kuna baadhi ya watoto ambao huhitaji muda zaidi kuamua kile wanachokitaka maishani,” anasema Bi Namulanda.

Mwaka 2012 alijiunga na Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta (JKUAT) kufanya kozi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (IT) ambayo alifanya kwa muda wa miezi sita pekee lakini baadaye akagundua kuwa haikuwa ndoto yake kabisa.

Mnamo mwaka 2013, alijiunga na Chuo Kikuu cha Mount Kenya ambapo alifanya kozi ya Kuwahudumia Wateja – Hospitality Management – hasa katika maswala ya chakula na huduma za hoteli.

Keki. Picha/ Magdalene Wanja

“Ninapenda sana kupika na kugundua resipe mbalimbali. Nakumbuka hata nilipokuwa bado shuleni, ilinibidi kutumia njia za kale kama vile makaa ili kuoka mikate na keki,” anasema mpishi huyu.

Bi Namulanda sasa ana duka la kuoka mjini Nakuru ambapo anaandaa na kuuza aina mbalimbali za keki na mikate.

Duka lake kwa jina Pharaoh’s Cake House huwavutia wateja wa aina mbalimbali ama wa mitandaoni au wanunuzi wa wengine wanaofika hapo kufurahia aina mbalimbali za vyakula hivyo.

Keki. Picha/ Magdalene Wanja

MAPISHI: Jinsi ya kuandaa wali unaopendwa sana Afrika Magharibi

Na MARGARET MAINA

mwmaina@ke.nationmedia.com

Muda wa kuandaa: Dakika 10

Muda wa kupika: Saa moja

Walaji: 4

Vinavyohitajika

 • kuku vipande 8
 • kitungu 1 kilichokatwakatwa
 • nyanya 3
 • kitungu saumu kilichomenywa
 • gramu 400 za ‘tomato paste’
 • gramu 400 za mchele wa Basmati uliopikwa kiasi kuwa wali
 • pilipili mboga 1 lakini nyekundu 1 iliyokatwa
 • curry powder kijiko nusu
 • chumvi kijiko
 • mafuta ya kupikia
 • maji vikombe 3

Maelekezo ya wali

Zimenye nyanya, pilipili mboga na kitunguu saumu.

Bandika sufuria mekoni,weka mafuta ya kupika. Acha yapate moto vizuri kisha weka vitunguu. Koroga hadi vianze kubadilika rangi. Ongeza tomato paste kisha kaanga kwa dakika tatu.

Ongeza nyanya zilizomenywa na ukaange kwa dakika 10. Hakikisha unakoroga kuepuka kuungua.

Baada ya dakika 10 punguza moto na uongeze chumvi, curry powder na viungo vingine upendavyo. yaache yachemke kwa dakika 10.

Ongeza wali uliokuwa umechemshwa kiasi na ukoroge pamoja na nyanya. Ongeza maji kiasi na ufunike baada ya kupunguza moto ili chakula kiive polepole kwa dakika 10 au hadi yaishe maji. Chakula kiko tayari.

Maelekezo ya nyama

Andaa nyama kwa kuiosha na uweke pembeni ichuje maji. Nyunyizia chumvi kiasi.

Bandika sufuria mekoni, weka nyama na ufunike ukishaipunguza moto ili yaive polepole bila maji kwa dakika 10.

Bandika sufuria nyngine na uweke mafuta ya kupika vikombe vitatu na uache yawe moto kabisa.

Vitumbukize vipande vya kuku kwenye mafuta na pinduapindua kwa dakika 15 hadi vibadilike rangi.

Sasa chakula chako kiko tayari.

MAPISHI: Chipsi zilizochanganywa na nyama ya mbuzi

Na MARGARET MAINA

mwmaina@ke.nationmedia.com

Muda wa kuandaa: Dakika 20

Muda wa kupika: Dakika 40

Walaji: 4

Vinavyohitajika

 • kilo 1 ya nyama ya mbuzi
 • ½ limau
 • vijiko 1½ vya majani ya giligilani
 • vijiko 2 vya kitunguu saumu
 • vijiko 3 cha tangawizi ya unga
 • mafuta ya kupikia
 • chumvi
 • viazi ulaya 10
 • nyanya 2
 • kitunguu maji 1
 • vijiko 2 vya nyanya ya kopo
 • pilipili 1
 • ½ kikombe vitunguu vya majani
 • kipande cha mdalasini
 • kijiko 1 cha garam masala

Maelekezo

Anza kwa kuandaa viungo kwa kukatakata majani ya giligilani, kukamua limau na vilevile kutwangatwanga kitunguu saumu.

Changanya nyama na viungo vyote kwenye bakuli kubwa.

Funika bakuli; acha viungo vikolee kwa muda wa saa kama nane au vizuri zaidi usiku kucha.

Chonga na katakata viazi vipande vidogo vya chipsi.

Weka nyanya na kitunguu katika blenda ili kutengeneza rojo; weka pembeni.

Kwenye sufuria, katika moto wa wastani, mimina mafuta mengi na yanapoanza kuchemka, weka viazi vyako viive kisha epua.

Katika kikaangio kingine, mimina mafuta na utie vitunguu.

Ongeza nyama iliyokuwa marinated. Kaanga mpaka iwe ya kahawia.

Ongeza jani la bay, rojo ya nyanya pamoja na giligilani ya unga, tangawizi na garam masala. Ongeza chumvi kisha pika mpaka nyanya ziive.

Ongeza kikombe kimoja cha maji. Funika na acha nyama iive kwa moto wa chini kwa muda wa nusu saa.

Ongeza viazi kwenye nyama na sosi vichanganye kabla ya kuepua.

Kisha pakua na ufurahie.

MAPISHI: Jinsi ya kuandaa viazi vya kuponda, kuku na sosi

Na MARGARET MAINA

mwmaina@ke.nationmedia.com

Muda wa kuandaa: Dakika 10

Muda wa kupika: Dakika 20

Walaji: 3

Vinavyohitajika kwa viazi

 • kilo 1 ya viazi
 • lita 1 ya maji
 • maziwa ½ kikombe
 • vijiko 3 vya siagi
 • chumvi

Maelekezo

Menya, osha na kukatakata viazi vipande vikubwa vikubwa.

Weka viazi kwenye sufuria na ongeza maji ya kutosha.

Chemsha mpaka maji yachemke, kisha ongeza chumvi. Chemsha mpaka viazi viive vizuri.

Viazi vikishaiva vizuri, epua kisha chuja maji.

Anza kuponda viazi na uhakikishe hakuna mabonge mabonge.

Ongeza maziwa na siagi mpaka upate uzito na ladha utakayopenda.

Vinavyohitajika kwa kuku

 • kilo ½ minofu ya kuku
 • pilipili mboga 3 (nyekundu, kijani na njano)
 • kitunguu maji 1
 • mafuta ya kupikia
 • kijiko 1 cha chicken seasoning
 • kijiko 1 cha kitunguu saumu na tangawizi
 • chumvi na pilipili manga

Maelekezo

Andaa viungo kisha katakata kuku, kitunguu na pilipili mboga vipande virefu virefu.

Kwenye kikaangio katika moto wa wastani, chemsha mafuta, kisha ongeza nyama ya kuku, chicken seasoning, kitunguu saumu na tangawizi.

Kaanga mpaka nyama ikaribie kuiva, kisha ongeza kitunguu maji, pilipili hoho, chumvi na pilipili manga.

Endelea kukaanga kwa dakika chache, mpaka kuku iive vizuri.

Pakua na viazi vya kuponda,mboga na ufurahie.

MAPISHI: Jinsi ya kuandaa wali wa nazi na nyama ya kusaga

Na MARGARET MAINA

mwmaina@ke.nationmedia.com

Muda wa kuandaa: Dakika 10

Muda wa kupika: Dakika 30

Walaji: 4

Vinavyohitajika kwa wali

 • Mchele kilo ½
 • Tui la nazi kikombe 1
 • Maji lita
 • Chumvi kijiko ½

Maelekezo

Osha mchele.

Weka mchele kwenye sufuria na ongeza chumvi. Acha mchele hadi uanze kuchemka katika sufuria mekoni.

Ukishaanza kuchemka, ongeza tui la nazi. Usikoroge.

Acha mchanganyiko uive taratibu kwa dakika 10.

Punguza moto na uache mchele uive hadi maji yakauke.

Epua.

Vinavyohitajika kwa nyama ya kusaga

 • Nyama ya kusaga kilo 1
 • Vitunguu maji 2
 • Vitunguu saumu 2
 • Tangawizi 1
 • Nyanya 4
 • Mafuta ya kupikia
 • Chumvi kijiko 1
 • Karoti 2
 • Pilipili mboga 1
 • Juisi ya limau

Maelekezo

Menya vitunguu, karoti, pilipili mboga na ukate hadi kuwa vipande vyembamba sana.

Menya nyanya na tangawizi kisha ukate vipande vipande.

Twanga vitunguu saumu kisha bandika sufuria ya kupikia mekoni.

Weka nyama na anza kukoroga ili kuzuia isigandie kwenye sufuria na kuungua.

Weka kitunguu maji huku ukiendelea kukoroga kwa muda wa dakika 10. Ongeza kitunguu saumu na tangawiizi huku ukikoroga.

Weka au mimina mafuta ya kupikia kisha weka pilipili mboga, karoti na juisi ya limau. Ongeza chumvi kidogo. Endelea kukoroga.

Weka nyanya, koroga na funika sufuria uache kwa dakika 10.

Pakua na wali wa nazi na ufurahie.

WATU NA KAZI ZAO: Ukakamavu umemwezesha kujiimarisha licha ya changamoto

Na SAMMY WAWERU

BI Irene Maina amesomea upishi, na ni taaluma aliyoienzi tangu akiwa na umri mdogo.

Alifanikiwa kupata nafasi ya ajira Maralal, Kaunti ya Samburu.

Hata hivyo, baada ya kuifanya kwa miaka kadha aliipoteza mwaka 2012 na ni wakati anaosema aliihitaji kwa hali na mali.

“Nilikuwa nimejaaliwa mtoto akiwa na umri wa miaka miwili wakati huo,” anasema Irene.

Anasimulia kwamba hakuwa na budi ila kuungana na jamaa zake jijini Nairobi, ili kumsitiri pamoja na malaika wake.

Akufaaye kwa dhiki ndiye rafiki.

Irene anasema dada yake mzawa alimpokea, ingawa hakuhisi kutaka kuwa ‘mzigo’ kwake kwani pia alikuwa na familia yake. Isitoshe, chochote alichomiliki Maralal alikiacha kwa sababu ingekuwa ghali kusafirisha.

Aliyetarajia kufunga naye pingu za maisha, alisalia kimya wakati akipitia changamoto zote hizo. Hiyo ni licha ya kuwa nguzo yake kuu, hususan kumpiga jeki katika biashara.

“Hakuna jambo gumu maishani kama kujisimamia halafu unafilisika ghafla,” anasisitiza mama huyo wa mtoto mmoja.

Kwa kuwa alipokuwa kazini alikuwa mtu wa watu, na aliwatendea wema, dada yake hakuona ugumu wowote kumfaa.

Kulingana na Irene, alipata kazi ya uuzaji wa bima katika kampuni moja ya bima jijini Nairobi na ndipo alihamia eneo la Thika. Anasimulia kwamba dadake alimsaidia katika harakati hizo, na hata kugharamia kodi ya nyumba na mahitaji mengine.

Gange hiyo haikuwa rahisi kama alivyodhania, kwani ilikuwa na changamoto zake. Cha kusikitisha aliiraukia asubuhi na mapema, ikizingatiwa kwamba sharti angeandaa mwanawe na kumpeleka shuleni.

“Jioni mkondo ulikuwa ule ule wa marathon, kuendea mtoto shuleni, kumfulia sare na mavazi yake ya nyumbani na kumpikia. Keshoye pia nilitarajiwa ofisini. Ilikuwa kazi ya machovu,” anafafanua.

Mwanawe alikuwa angali mdogo, na wataalamu wa masuala ya watoto, wanasema mama ambaye ni mzazi wa karibu anapaswa kuwa sako kwa bako na mtoto kwa muda hadi atakapokomaa.

“Watoto pia hukumbwa na mawazo hasa wanapokosa uwepo wa mama. Lugha na malezi ya mama hayaambatani na ya yaya au mlezi tofauti. Kuna yale mapenzi ya mama kwa mtoto, yanayomfanya kukua kimawazo,” anaeleza Bi Karungari Mwangi, muuguzi mstaafu ambaye ni mtaalamu wa masuala ya watoto, wakiwamo ambao hawajafikisha umri wa kuzaliwa (pre-term babies) pamoja na masuala ya lishe.

Kwa mujibu wa maelezo ya mdau huyo, ni muhimu mama hata akiwa kazini kupata muda wa kutosha haswa jioni na likizo kutangamana na kucheza na mwanawe, akiwa angali mchanga.

“Muda anaotangamana naye ni muhimu katika malezi na ukuaji wa mtoto,” anahimiza.

Ni kufuatia ushauri unaowiana na huo Irene Maina alikata kauli kuacha kazi hiyo na kuwekeza katika biashara 2017.

“Biashara yenyewe ilinoga hadi mwanzoni mwa mwaka huu, 2019, nikaamua kuifunga kwa sababu nilianza kukadiria hasara,” anasema.

Mama huyu anasema pandashuka alizopitia awali zilimfanya kuwa mkakamavu, na kumtegemea Mungu kwa kila jambo. Licha ya kufunga biashara asijue atakachofanya kukimu mwanawe, Irene anasema alijaaliwa kupata kandarasi ya usafirishaji wa mawe ya ujenzi, gange anayoifanya kufikia sasa.

Hali kadhalika, amefufua taaluma yake ya upishi anayosema imenoga.

“Ninafanya mapishi ya nje (outside catering). Hasa tunapokaribisha msimu wa Krismasi, ninapata oda chungu nzima za kupika katika harusi,” aeleza.

Anaambia Taifa Leo kwamba anapania kufungua biashara yake ya chakula na mengineyo yanayohusu upishi, ambapo kwa sasa anashughulikia vifaa vya mapishi kama vile majiko, sufuria na vihifadhio vya chakula.

Mwanauchumi na mhasibu Charles Mwangi, anasema hilo ataliafikia upesi ikiwa amekuwa akiweka akiba.

“Ni muhimu unapofanya kazi ujifinze kufunga mshipi wa tumbo, ukilipwa mshahara wa Sh20, weka akiba ya Sh5. Haijalishi kidogo unachoweka kando, kitakufaa kuafikia malengo yako maishani,” anashauri Bw Mwangi.

MAPISHI: Jinsi ya kuandaa burger

Na MARGARET MAINA

mwmaina@ke.nationmedia.com

Muda wa kauandaa: Dakika 10

Muda wa mapishi: Dakika 10

Walaji: 5

Vipande vya nyama vya kutumika katika mapishi ya Burger. Picha/ Margaret Maina

Vinavyohitajika

 • mikate 5 ya burger
 • siagi ya kukaangia mikate
 • vitunguu maji 3
 • nyanya 2
 • majani ya salad
 • parachichi
 • sauce utakazopenda (tomato sauce, mayonnaise au BBQ sauce)
 • mafuta ya kupikia
 • kilo 1 ya nyama ya kusaga
 • chumvi na pilipili manga
 • vipande 5 vya jibini

Jibini huwa ni ule mgando utokanao na maziwa ya ng’ombe yaliyotolewa maji na kugandishwa.

Mapishi ya Burger huhitaji umakinifu . Picha/ Margaret Maina

Maelekezo

Katakata kitunguu na nyanya vipande vya mduara; katakata parachichi vipande virefu.

Osha, katakata na kukausha majani ya salad kwa kutumia kitambaa cha jikoni au karatasi shashi maalumu kwa matumizi ya jikoni.

Gawanya nyama kwenye madonge matano.

Finyafinya kutengeneza umbo mduara. Nyunyizia chumvi na pilipili manga juu.

Kwenye kikaangio kilicho kwenye meko yenye moto mkali kiasi, chemsha mafuta.

Weka nyama kwenye kikaangio, upande wenye chumvi na pilipili manga kwa chini halafu pia nyunyizia chumvi na pilipili manga kwa upande wa juu.

Acha nyama iive bila kugeuzwa kwa muda wa dakika nne. Geuza ili nayo iive upande mwingine hadi jinsi utakavyopenda.

Weka jibini juu sekunde kama 30 kabla ya kutoa nyama kwenye kikaangio au mpaka iyeyuke. Funika kwa sekunde utakazoweka jibini.

Kata mkate katikati kisha upake siagi juu kwenye upande wa ndani.

Kwenye kikaangio katika meko yenye moto wa wastani, weka mkate upande wenye siagi kwa chini. Kaanga mpaka uwe wa kahawia na ukauke kiasi; angalia usiungue.

Epua mkate, pangilia nyama na viungo vingine kwenye mkate kama utakavyopenda.

Pakua na ufurahie na kinywaji chochote ukipendacho.

MAPISHI: Biriani ya nyama ya mbuzi

Na MARGARET MAINA

mwmaina@ke.nationmedia.com

Muda wa kuandaa: Dakika 15

Muda wa mapishi: Dakika 40

Walaji: 5

Vinavyohitajika

 • Mchele wa Basmati kilo 1
 • Nyama ya mbuzi kilo 1
 • Tangawizi
 • Kitunguu saumu
 • Binzari
 • Pilipili manga
 • Vitunguu maji 6
 • Nyanya 4
 • Mafuta ya kupikia
 • Pilipili nyekundu kijiko 1
 • Giligilani vijiko 3
 • Chumvi
 • Hiliki

Maelekezo

Weka nyama iliyo kwenye sufuria hapo mekoni. Weka tangawizi, kitunguu saumu, binzari, pilipili manga na chumvi. Hakikisha nyama imeiva na haipotezi mchuzi. Epua.

Chukua vitunguu maji kisha vikate kwa umbo mviringo na nyanya zikate vipande vidogovidogo.

Bandika sufuria safi yenye mafuta mekoni kisha kaanga ile nyama mpaka iwe ya kahawia halafu iepue na uichuje mafuta. Weka pembeni.

Weka vitunguu – baadhi – kwenye yale mafuta na uvikaange kabla ya kutia binzari, unga wa pilipili nyekundu, giligilani, mbegu za hiliki na pilipili manga.

Changanya vizuri viungo upate mchanganyiko unaohitaji kisha mimina ule mchuzi wa nyama.

Weka nyanya kwenye ule mchanganyiko. Pika mpaka mchuzi wote ukauke.

Weka nyama halafu ongezea hapo chumvi kama unainyunyiza ikolee vizuri. Koroga vizuri na taratibu kwa muda wa dakika tano kisha epua.

Bandika sufuria nyingine; weka mafuta na vitunguu, weka majani ya giligilani, majani ya mint, funika kwa robo saa kisha weka wali wako.

Ongeza vikombe vitano vya maji na chumvi kisha funika chakula.

Punguza moto mpaka maji yakauke, halafu chukua ule mchanganyiko wenye nyama mwagia – nusu tu – juu ya wali kisha acha uive.

Baada ya dakika 10 funua chakula, geuza na upakue.

MAPISHI: Jinsi unavyoweza kuandaa ‘fluffy pancakes’

Na MARGARET MAINA

mwmaina@ke.nationmedia.com

Muda wa kuandaa: Dakika 10

Muda wa kupika: Dakika 15

Walaji: 5

Fluffy pancake. Picha/ Margaret Maina

Vinavyohitajika

 • unga wa ngano kilo ½
 • vijiko 3 vya sukari
 • kijiko ½ cha Baking Soda
 • kijiko ½ cha Baking Powder
 • kijiko ½ cha chumvi
 • mayai 2
 • kijiko 1 cha siagi
 • kijiko 1 cha vanilla
 • mafuta ya kupikia

Maelekezo

Chukua bakuli safi na kwalo – likiwa kavu – changanya unga wa ngano, sukari, chumvi, baking powder na baking soda.

Kisha chukua bakuli jingine safi na kavu kisha changanya pamoja mayai, vanilla essence, siagi na fresh cream. Kama huna, unaweza kutumia maziwa badala yake.

Mchanganyiko wa vinavyohitajika katika mapishi ya fluffy pancake. Picha/ Margaret Maina

Sasa chukua mchanganyiko wa mayai na maziwa umwagie kwenye mchanganyiko wa unga na halafu koroga polepole. Weka pembeni; acha kwa muda wa dakika tano. Si lazima lakini kama ukiweka kwa muda huo itulie, bila shaka pancake yako itatoka vizuri sana.

Chukua non stick pan, mimina mafuta kiasi na halafu hakikisha meko yako hayana moto mkali au moto mdogo.

Chukua kijiko kikubwa; chota mchanganyiko wako na mwagia katika kikaangio.

Pindua pancakes ikiwa rangi ya kahawia na uache iive upande mwingine.

Epua, pakua na ufurahie na chochote ukipendacho.

MAPISHI NA UOKAJI: Jinsi ya kuoka kuku kwenye ovena

Na MARGARET MAINA

mwmaina@ke.nationmedia.com

Muda wa kuandaa: Dakika 20

Muda wa mapishi: Saa 1

Walaji: 4

Vinavyohitajika

 • kuku 1 (usikate vipande)
 • siagi kikombe ½
 • chumvi
 • pilipili manga
 • thyme
 • majani ya rosemary
 • foil paper
 • curry powder
 • majani ya giligilani
 • juisi ya limau
Kuku safi kabla kuokwa. Picha/ Margaret Maina

Maelekezo

Washa ovena na acha ipate joto hadi nyuzi 325.

Weka kuku safi kwenye sinia ya kuokea au chombo chochote cha kutumika wakati wa kuoka na kinachoingia kwenye ovena.

Paka siagi juu ya kuku hadi ienee vizuri.

Paka curry powder kwa ndani ya kuku. Curry ni mchanganganyiko wa viungo vingi tofauti, hivyo ni mahsusi kuleta ladha tamu na harufu nzuri itakayofanya chakula kinukie vizuri.

Nyunyizia chumvi kisha sambaza kwa ndani na nje vizuri.

Paka pilipili manga ya kutosha juu ya kuku.

Nyunyizia juisi ya limaou ya kutosha, kisha weka majani yaliyosagwa ya thyme na rosemary.

Funga nyama ya kuku kwenye foil paper kisha weka kwenye ovena.

Oka kuku wako kwa muda wa saa moja. Huu ni muda mzuri kwa kuku kuiva vizuri nje na ndani.

Baada ya muda kuisha angalia kama nyama ya kuku imeiva vizuri.

Nyama hii ikiiva, itoe kwenye ovena. Weka pembeni ili ipoe kisha pakua, katakata na ufurahie.

MAPISHI: Namna ya kupika makaroni

Na MARGARET MAINA

mwmaina@ke.nationmeidia.com

Muda wa kuandaa: Dakika 5

Muda wa mapishi: Dakika 20

Walaji : 3

Vinavyohitajika

 • makaroni pakiti moja
 • chumvi
 • siagi
 • vitunguu saumu (utaviponda)
 • tangawizi (utaiponda)
 • pilipili
 • tui la nazi

Maelekezo

Tayarisha sufuria safi, weka maji ya kutosha. Ongeza chumvi kiasi na pilipili manga iliyosagwa.

Bandika mekoni na acha mpaka maji yachemke.

Weka makaroni kwenye maji yaliyochemka. Japokuwa maelekezo kwenye pakiti nyingi yanasema kuwa muda wa kupika ni dakika 10, hakikisha uivaji kwa kuyaonja. Baada ya kuiva, epua sufuria.

Tayarisha chujio na mimina makaroni ndani ya chujio ili kuchuja maji uliyochemshia makaroni.

Chukua maji yasiyo moto wala baridi miminia juu ya makaroni yakiwa bado ndani ya chujio.

Rejesha sufuria uliyochemshia makaroni mekoni huku ukiwa umepunguza sana moto.

Weka siagi ndani ya sufuria yako na iacha iyeyuke vyema. Rejesha makaroni ndani ya sufuria yenye siagi. Waweza ongeza pilipili manga iliyosagwa kama ukipenda.

Koroga vizuri kabisa kwa dakika mbili ili mchanganyiko wa makaroni, pilipili manga na siagi ukolee barabara.

Mackaroni yako yapo tayari kwa kuchanganywa na mboga.

Epua sufuria kisha pakua kwa kuku au chochote ukipendacho.

MAPISHI: Jinsi ya kupika nyama yenye viungo mbalimbali na mboga

Na MARGARET MAINA

mwmaina@ke.nationmedia.com

Muda wa kuandaa: Dakika 10

Muda wa mapishi: Dakika 40

Walaji: 2

Vinavyohitajika

 • Nyama nusu kilo
 • Tangawizi ya unga kijiko 1
 • Mafuta ya kupikia
 • Kitunguu maji 1,
 • Juisi ya Limau
 • Kitunguu saumu punje 5
 • Pilipili mboga 2 za rangi tofauti
 • Chumvi kijiko 1
 • Pilipili

Maelekezo

Andaa nyama kwa kuikata vipandevipande ili viive vizuri na kwa urahisi. Osha na kisha weka kando.

Paka chumvi katika pande zote za nyama. Nyunyizia limau, tangawizi, na kitunguu saumu kilichopondwa. Hakikisha umepaka vizuri katika pande zote na kuenea vizuri. Weka pilipili kisha acha nyama ikae pembeni iingie viungo kwa muda wa robo saa.

Bandika kikaangio mekoni na uache kipate moto kiasi. Weka nyama ila usiweke mafuta. Acha vipande vya nyama viive taratibu huku ukiwa unageuza hadi nyama iwe rangi ya kahawia pande zote.

Kama nyama haijaiva na inakauka, nyunyizia maji kiasi ili ipate kulainika vizuri na kuiva kabla ya kuila.

Osha kisha kata pilipili mboga, kitunguu saumu, kitunguu maji na pilipili za kawaida. Hifadhi kwenye chombo safi.

Nyama ikishaiva vizuri, weka mafuta ya kupikia kiasi cha vijiko viwili kisha acha yapate moto kabla ya kutumbukiza hapo kitunguu maji. Koroga.

Funika kiasi ili vitunguu viive na kuwa na rangi ya kahawia.

Weka mboga mboga huku ukikoroga kila wakati kisha funika.

Acha mboga iive kwa mvuke kwa dakika tano. Bandua mboga,

Pakua na chochote ukipendacho na ufurahie mlo wako.

MAPISHI: Jinsi ya kuoka biskuti iliyoongezwa chokoleti

Na MARGARET MAINA

mwmaina@ke.nationmedia.com

Muda wa kuandaa: Dakika 15

Muda wa kupika: Dakika 15

Walaji: 5

Vinavyohitajika

 • Vikombe 3 vya unga wa ngano
 • Kijiko 1 cha baking soda
 • Kijiko 1 cha chumvi
 • Kikombe ¾ ya siagi iliyoyeyuka
 • Kikombe ½ ya sukari nyeupe
 • Kikombe 1 cha sukari ya brown
 • Vijiko 2 vya vanilla extract
 • Mayai 2
 • Vikombe 2 vya chocolate chips

Maelekezo

Kwenye bakuli kubwa, changanya unga wa ngano, chumvi na baking soda.

Changanya unga wa ngano, chumvi na baking soda. Picha/ Margaret Maina

Kwenye bakuli jingine kubwa, changanya sukari nyeupe, siagi, mayai na vanilla mpaka mchanganyiko ulainike vizuri.

Changanya mchanganyiko wa unga na mchanganyiko wa sukari kisha ukande mpaka uchanganyike vizuri kabisa.

Changanya mchanganyiko wa unga na mchanganyiko wa sukari kisha ukande. Picha/ Margaret Maina

Ongeza chocolate chips. Changanya vizuri kisha funika bakuli. Acha unga ulale kwenye jokofu usiku kucha.

Gawanya mchanganyiko wa unga kwa kipimo cha vijiko vitatu vya chakula. Tengeneza mduara kama vijipira. Panga vizuri kwenye chombo cha kuokea ukitumia karatasi za kuokea.

Oka kwenye ovena iliyopata moto katika joto la nyuzi 175 sentigredi kwa robo saa au mpaka zianze kupata rangi ya kahawia.

Epua, acha zipoe kabla ya kuhamishia kwenye waya wa kupozea zipoe kabisa.

Pakua na ufurahie.

MAPISHI: Nyama iliyosagwa

Na MARY WANGARI

mwnyambura@ke.nationmedia.com

KATIKA jiko letu hii leo tutaandaa kitoweo cha nyama iliyosagwa au ukipenda kima.

Viungo:

 • 1 kilo nyama iliyosagwa
 • ¼ lita mafuta
 • 1 kijiko kidogo chumvi ya kuongeza ladha
 • 2 vitunguu maji kikubwa
 • 2 iliki
 • 1 Tangawizi
 • 4 nyanya kubwa
 • 1 pilipili mboga
 • 1 ndimu
 • 1 kijiko bizari
 • 1 kijiko cha karafuu iliyosagwa
 • 2 viazi vikubwa
 • 1 kikombe cha maharage ya kijani kibichi
 • 2 karoti kubwa
 • Mahindi yenye maziwa maziwa (ukipenda)

Utaratibu

Menya vitunguu na uvikate kate vipande vyembamba sana.

Chambua na uikwangue karoti iwe kama uji.

Katakata pilipili mboga katika vipande vyembamba.

Menya nyanya na uzikate katika vipande vya wastani.

Osha na uikwangue tangawizi.

Pondaponda na kutwanga vitunguu saumu.

Bandika sufuria ya kupikia jikoni.

Weka nyama na anza kukoroga ili kuzuia isigandie kwenye sufuria na kuungua.

Weka kitunguu maji huku ukiendelea kukoroga kwa muda wa dakika 10.

Weka kitunguu saumu na tangawizi. Endela kukoroga kwa muda wa dakika tano zaidi.

Weka mafuta kidogo sana ili kufanya viungo viize.

Weka pilipili mboga, karoti na kamulia ndimu. Ongeza chumvi kidogo. Endelea kukoroga.

Weka nyanya, koroga na funika sufuria na mfuniko kwa muda kama dakika 10.

Kisha ongeza viazi, maharage na mimina maji kiasi kwenye rojo. Makinika usiongeze maji kupita kiasi wala usipunguze mno na kuufanya mchuzi uwe mzito na kukauka.

Funika na uruhusu mchuzi wako kutokota hadi viazi vilainike.

Mimina tomato sauce na uchanganye vyema.

Sasa kitoweo chako kiko tayari, epua na ufurahie!

Unaweza kuambatisha na chapati, wali au hata kula kitoweo chako kavukavu kulingana na starehe yako.

MAPISHI: Jinsi ya kupika minofu ya kuku yenye siagi

Na MARGARET MAINA

mwmaina@ke.nationmedia.com

Muda wa kuandaa: Dakika 15

Muda wa mapishi: Nusu saa

Walaji: 4

Vinavyohitajika

 • minofu au vipande vya kuku kilo 1
 • juisi ya limau
 • chumvi kijiko 1
 • pilipili ya unga vijiko 3
 • tangawizi iliyosagwa kijiko 1
 • majani ya bay 3
 • mdalasini uliosagwa kijiko 1
 • siagi vijiko 3
 • vitunguu maji 2
 • vitunguu saumu vijiko 5
 • giligiliani vijiko 2
 • nyanya ya kopo vijiko 2
 • maziwa mala vijiko 2
 • mafuta ya kupikia
 • chumvi

Maelekezo

Andaa nyama ya kuku; isafishe vizuri.

Chukua pilipili manga, tangawizi, majani ya bay, mdalasini, maziwa mala, vitunguu maji, vitunguu saumu, giligilani, na nyanya ya kopo. Chukua blenda weka hivyo vitu vyote kisha saga, hakikisha vimelainika kabisa na viungo vimechanganyikana vizuri.

Chukua kuku; kata mapande makubwa.

Chukua bakuli kubwa, weka hayo mapande kisha changanya na juisi ya limau halafu nyunyizia chumvi kiasi.

Mwagia mafuta ya kupikia kwenye kuku, changanya vizuri mpaka uone mafuta yameenea vizuri.

Chukua ile rojo mwagia kwenye kuku kisha changanya. Ukimaliza, weka kwenye jokofu kwa muda wa saa moja. Yatoe mapande ya kuku na upake siagi halafu changanya kabla ya kurudisha tena kwenye jokofu.

Acha mapande hayo usiku kucha.

Toa kuku ukaange na viungo upendavyo. Unaweza kuoka au kuchoma. Uamuzi ni wako.

Angalia saa. Dakika 25 zikifika, chakula kitakuwa kimeiva.

Pakua na chochote ukipendacho na ufurahie mlo!

Minofu ya kuku yenye siagi. Picha/ Margaret Maina

MAPISHI: Meatballs

Na MARGARET MAINA

mwmaina@ke.nationmedia.com

Muda wa kuandaa: Dakika 15

Muda wa kupika: Dakika 20

Walaji: 4

Vinavyohitajika

Kwa ajili ya meatballs

· Vijiko 2 vya mafuta ya mizeituni

· Kitunguu maji 1 ambacho unafaa kukimenya na kisha kukikata vipande vidogovidogo

· Kitunguu saumu 1; menya na ponda

· Kilo 1 ya nyama iliyosagwa

· Kijiko 1 cha rosemary

· Yai 1

· Chumvi kijiko 1

· Pilipili manga ya unga kijiko 1

 

Kwa ajili ya sauce ‘sosi’

· Vijiko 3 vya mafuta ya mizeituni

· Kitunguu maji 1, kata vipande

· Kitunguu saumu punje 5, ponda

· Pilipili mboga 2, mie nimechanganya za rangi tofauti

· Chumvi kijiko 1

· Pilipili manga ya unga kijiko 1

· Pilipili 2

Maelekezo

Weka kikaango mekoni, acha kipate moto vizuri.

Weka vijiko viwili vya mafuta ya mizeituni kwenye moto wa wastani.

Mafuta yakipata moto, ongeza kitunguu maji na kitunguu saumu.

Funika na acha vichuje maji kwa dakika nne na viwe na rangi ya kahawia. Epua na acha vipoe.

Kwenye bakuli, changanya nyama iliyosagwa na vitunguu. Ongeza viungo vingine na mayai. Weka chumvi na pilipili kulingana na unavyopenda.

Gawa nyama mabonge 24, kulingana na ukubwa unaopenda.

Weka meatballs kwenye mfuko au chombo cha kuhifadhia kwenye jokofu.

Hifadhi kwenye jokofu ili zigande hadi pale unapohitaji kuzitumia.

Ukihitaji kupika, toa meatballs, bandika sufuria au kikaango jikoni kwenye moto mkali, weka mafuta ya kupikia, acha yapate moto vizuri kisha weka meatballs. Acha meatballs hadi ziive kisha toa na hifadhi pembeni. Hifadhi kwenye karatasi au tissue ili zichuje mafuta.

Kuandaa sauce

Sauce ya meatballs. Picha/ Margaret Maina

Osha kisha kata pilipili mboga, kitunguu saumu, kitunguu maji na pilipili za kawaida. Hifadhi kwenye chombo safi pembeni.

Bandika kikaango au sufuria mekoni. Kikipata moto weka mafuta ya kupikia vijiko viwili kisha acha yapate moto vizuri kabla ya kuweka kitunguu maji na kitunguu saumu.

Funika ili vilainike na kuchuja maji na kuwa rangi ya kahawia.

Weka pilipili mboga. Weka pia pilipili za kawaida na ukoroge zaidi.

Funika sufuria vizuri, acha vichemke pamoja kwa dakika tano.

Weka meatballs, koroga vizuri. Acha vichemka pamoja kwa dakika kama saba.

Epua na kisha pakua pamoja na wali, ugali au pasta.

Meatballs tayari kuliwa. Picha/ Margaret Maina