MAPOZI: Nadia

Na PAULINE ONGAJI

HAJADUMU katika fani ya muziki kwa muda mrefu lakini ushawishi wake unahisiwa katika kila pembe ya burudani nchini.

Jina lake ni Nadia Mukami Mwendo, mwimbaji, mwandishi wa nyimbo na mtumbuizaji ambaye sauti yake ya ninga; vilevile ustadi wake wa utunzi, vimemfanya kuorodheshwa miongoni mwa wasanii wanaovuma nchini Kenya kwa sasa.

Kwa vibao kama Yule Yule, African Lover, Lola na Si Rahisi  wimbo ambao umekuwa ukipokelewa vyema na mashabiki – wachache watapinga kwamba Nadia ameonyesha kila ishara za kuiteka fani hii.

Hasa kibao chake cha hivi punde Radio Love kimekuwa pambio kwa wengi huku kikizidi kutawala mawimbi ya stesheni za redio nchini, kwenye matatu na hata vilabuni.

Ni suala ambalo limempa umaarufu na hata fursa ya kutumbuiza pamoja na baadhi ya majina makuu katika ulingo wa muziki nchini.

Mzaliwa wa jiji la Nairobi, Nadia alisoma katika shule ya msingi ya Kari, kwenye barabara ya Nairobi-Mombasa, kabla ya kujiunga na shule ya upili ya Mount Laverna School, eneo la Kasarani, jijini Nairobi.

Katika shule ya upili, alifanya vyema kwenye mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne, na baadaye kujiunga na Chuo Kikuu cha Maseno ambapo alisomea masuala ya Fedha.

Safari yake kimuziki ilianza akiwa na umri wa miaka 17 pekee huku akichochewa na babake aliyekuwa shabiki sugu wa muziki wa taarab, vilevile mwanamuziki Ray C kutoka Tanzania.

Mara ya kwanza kwake kurekodi muziki ilikuwa baada ya mfanyakazi mwenzake alikokuwa ameajiriwa katika duka la jumla, kumhimiza kwenda studioni.

Ni ushauri ambao aliufuata na kurekodi kibao, Narudi, wimbo uliozungumzia mpenzi mpotevu.

Hata hivyo, safari yake ya uimbaji ilikatizwa kwa muda alipojiunga na Chuo Kikuu cha Maseno.

Hii haikumaanisha kwamba alikuwa ametupilia mbali ndoto yake ya kujihusisha na burudani, kwani alijiunga na idhaa ya redio ya chuo kikuu hicho kwa jina Equator FM, ambapo alikuwa na kipindi chake kwa jina Saturday Hip-hop Count kilichokuwa kikipeperushwa kila Jumamosi.

Baadaye mwaka huo alirejea katika muziki na mwaka wa 2015 alirekodi Barua Ya Siri, wimbo uliopokelewa vyema na mashabiki wake chuoni kutokana na mtiririko bomba wa mashairi.

Kibao hicho kilifuatiwa na Kesi, kilichorekodiwa na Cedo huku kikipeperushwa katika baadhi ya stesheni za televisheni na redio.

Aidha, kupitia wimbo huo aliweza kujihifadhia nafasi katika majukwaa mbalimbali ikiwa ni pamoja na Blaze By Safaricom (Kisumu), Tamasha za muziki za The Nile Festival na The Luo Festival, kando ya baadhi ya majina makuu katika fani ya muziki nchini.

Nyota yake iling’aa zaidi alipoanza kuhudhuria hafla ya Poetry After Lunch (PAL) inayoandaliwa kila Alhamisi katika ukumbi wa Kenya National Theatre.

Mwanamuziki Nadia. Picha/ Maktaba

Ni jukwaa hili lililomwezesha kupata mfichuo zaidi na hivyo kupata fursa ya kuonekana kwa mara ya kwanza kwenye shoo ya Kipawa Show ambapo alitoana kijasho na wanamuziki wengine na kuibuka mshindi.

Pia, alifika katika fainali za shindano la Jenga Talanta, suala lililozidi kumtambulisha na hata kumfanya kupokea mwaliko wa kutumbuiza kwenye Churchill Show, kando ya wasanii wa haiba ya juu kama vile Suzanne Owiyo.

Mwaka wa 2017 alikutana na David Guoro, ajenti wa kusaka vipaji jijini Nairobi, aliyefurahishwa na kipaji na bidii yake, na hivyo kumsajili kwenye lebo yake ya Hailemind Entertainment.

Licha ya kwamba bado hajakita mizizi ambapo machoni mwa wengi pengine bado limbukeni, ukweli ni kwamba Nadia yuko mbioni kuweka jina lake kwenye ramani ya muziki nchini.

MAPOZI: Bensoul

Na PAULINE ONGAJI

ALIKUWA mwanamuziki wa kwanza kusajiliwa na Sol Generation, lebo inayomilikiwa na bendi ya Sauti Sol.

Jina lake ni Benson Mutua al-maarufu Bensoul Muziki, mwanamuziki, mwandishi wa nyimbo, produsa na mcheza ala za muziki. Yeye ni mmoja kati ya wasanii sita walioshirikishwa kwenye kibao Extravaganza, chao Sauti Sol.

Lakini licha ya kwamba wimbo huo ulichangia pakubwa kumpa mfichuo na umaarufu, Bensoul anajivunia pia kazi zake kama mwanamuziki solo.

Anatambulikwa kwa nyimbo kama vile Lucy, Not Ready, Gloomy Morning, I Only Wanna Give It To You, Rastafari, Ningependa Nikuchukie na What We Lost miongoni mwa zingine.

Benson Mutua maarufu ‘Bensoul Muziki’ ni mwanamuziki wa kwanza kusajiliwa na Sol Generation, lebo inayomilikiwa na bendi ya Sauti Sol. Picha/ Maktaba

Kinachomtofautisha na wasanii wengine ni ustadi wake wa kucheza ala mbalimbali ikiwa ni pamoja na ngoma, fidla na gitaa.

Aidha, Bensoul anafahamika kwa ushupavu wake katika uandishi wa nyimbo. Anajivuinia kuandikia nyimbo baadhi ya majina makuu kama vile Sauti Sol, Kidum, AliKiba, Nyashinski, Benpol, H_Art the Band na Mercy Masika, miongoni mwa wengine.

Ni ustadi huu ambao umemfanya kutambuliwa na wasanii wengine wa haiba ya juu. Kwa mfano wakati mmoja, mmojawapo wa wanachama wa Sauti Sol – Bien-Aime, alimtaja kama mwandishi shupavu wa muziki.

Pia, mwaka 2018 aliungana jukwaani na mwanamuziki Chronixx kutoka Jamaica katika mojawapo ya shoo zake nchini, huku msanii huyu akimtambua kama mmojawapo wa wanamuziki shupavu wa kutazamiwa siku zijazo.

Ni suala hili ambalo limemfanya kuteuliwa katika tuzo mbalimbali. Mwaka wa 2017 aliteuliwa kama mwanamuziki bora wa mwaka wa mdundo wa soul katika tuzo za Café Ngoma Awards.

Aidha, mwaka jana, kibao Masheesha, alichoimba kwa ushirikiano na H_ART The Band kiliteuliwa katika kitengo cha kolabo bora ya mwaka kwenye tuzo za Pulse Music Video Awards (PMVA).

Huenda hii ndio mojawapo ya sababu ambazo zimemfanya kuwa kivutio hata miongoni mwa wanamuziki wenzake.

Bensoul alitambua kipaji chake akiwa angali mdogo, wakati huo akiishi mjini Embu pamoja na familia yake, huku akitumia jukwaa la kanisa kujikuza kimuziki.

Ajifunza kucheza ala

Akiwa pale alikuwa akichukua ala tofauti za muziki na kujifunza kuzicheza.

Baada ya kukamilisha masomo ya upili alihamia jijini Nairobi ambapo alikutana na wanachama wa bendi ya H_Art The Band na kuwa marafiki.

Alijiunga na chuo cha Sauti Academy na baadaye akasajiliwa na lebo ya Sol Generation kabla ya kuangusha kibao Lucy.

Baadaye alitunga vibao vingine ikiwa ni pamoja na Ntala Nawe, Not Ready, Don’t Question My Love na Ningependa Nikuchukie, wimbo uliopokelewa vyema hasa katika mtandao wa Soundcloud. Aliandika kibao hiki kuzungumzia jinsi mama yao alivyotaabika kumlea pamoja na nduguze bila usaidizi wowote hasa kutoka kwa baba mzazi.

“Nakumbuka kuna nyakati ambapo nyumba yetu ingefungwa kwa sababu ya kutolipa kodi. Wakati mmoja dada yangu alilazimika kuacha shule ili nipate fursa ya kuendelea na masomo. Kutokana na hayo, tulihangaika sana ambapo ujumbe huu ulinuia kumfikia babangu,” alisema wakati mmoja katika mahojiano.

Kwa sasa ingawa bado hajakita mizizi vilivyo katika fani ya muziki, ni dhahiri kwamba Bensoul anazidi kujiundia jina kama mojawapo ya majina yenye ushawishi katika fani hii. Lililosalia ni yeye kuhakikisha kwamba anatimiza utabiri wa wengi wanaotambua uwezo wake kimuziki.

MAPOZI: Nviiri

Na PAULINE ONGAJI

HUENDA baadhi wamemfahamu baada yake kushirikishwa kwenye kibao Extravaganza na Sauti Sol.

Ukweli ni kwamba Nviiri the Storyteller kama anavyofahamika miongoni mwa mashabiki wake, amekuwepo ulingoni kwa muda.

Ustadi wake unadhihirika kwani ni mmojawapo wa wanamuziki waliochaguliwa kupamba tamasha ya muziki ya Hype Festival 2019 jijini Nairobi na hivyo kuungana na majina makubwa kama vile mwanamuziki kutoka Nigeria, Maleek Berry.

Kwa wanaoshuku ushupavu wake kama mtunzi, ni muhimu kuwajulisha kwamba alishirikiana na Sauti Sol katika uandishi wa kibao Melanin, kilichowapa umaarufu nchini Kenya na mbali, huku kikiendelea kuvutia watazamaji zaidi ya milioni 15 kwenye mtandao wa YouTube.

Ni ustadi huu uliomfanya Nviiri ambaye pia ni mcheza gita na mhariri wa video, kuwa mmojawapo wa wasanii wachache ambao wamesajiliwa chini ya lebo ya Sol Generation Records, yao Sauti Sol.

Mbali kidogo na muunganisho wake na bendi hii, Nviiri pia amejiundia jina kupitia nyimbo zake ambapo anafahamika kwa vibao kadha; kimojawapo kikiwa ni wimbo Pombe Sigara ambao kinyume na kichwa chake, unazungumzia mapenzi kwa mabinti.

Aidha anafahamika kwa vibao vingine kama vile Penzi, suala ambalo linathibitisha mvuto wa ujumbe wa mahaba kwa kila kazi anazoshughulikia.

Kama mwandishi wa nyimbo, pia amepata fursa ya kushughulikia kazi za baadhi ya wanamuziki wa injili na nyimbo za kilimwengu.

Na ni uwezo huu wa kutobagua wasanii anaowafanyia kazi ambao umemtenga na wengine wanoshughulika katika fani ya uandishi wa nyimbo.

Siri yake ni gani?

Aidha, siri yake imekuwa kufanya kolabo na wasanii maarufu ili kufikia kiwango chao.

Pia, uwezo wa kuhaisha kazi zake, umemwezesha kupata shavu zaidi.

Hii haimaanishi kwamba hajakumbana na changamoto katika harakati hizi.

Kwa mfano. alipoanza kuandika nyimbo, haikuwa rahisi kwake kwani soko la muziki la hapa nyumbani lilimpa chenga kiasi.

Hata hivyo alipata ujasiri na nguvu kwa kushirikishwa katika uandishi wa kibao Melanin.

Ili kukabiliana na changamoto ya kunakiliwa kwa ngoma zake, amekuwa akisajili kila kazi anayoifanya.

Mbali na hayo, siri yake pia imekuwa kusikiza kazi za wanamuziki mbalimbali, vile vile kuwa na ufahamu wa mambo mengi yanayohusiana na burudani.

Fursa yake ya kuandikia kibao mojawapo ya bendi maarufu barani lilimjia baada ya kuwafanyia kazi kama produsa wa video. Ni hapa mkoko ulialika maua.

Licha ya kwamba hajakita mizizi katika tasnia ya muziki, umaarufu wake umekuwa ukiongezeka. Ni hali inayotarajiwa kuendelea hasa ikizingatiwa kwamba amebahatika kuwa mmoja wa wasanii wachache waliofichwa chini ya ubawa wa Sauti Sol, na ni bidii yake tu itaamua iwapo atadumu au kuchujuka.

MAPOZI: Crystal Asige

Na PAULINE ONGAJI

KUSHIRIKI kwake katika kibao Extravaganza cha bendi ya Sauti Sol kumemfichua katika ulingo wa burudani huku sauti yake yake ya ninga ikizidi kumzolea mashabiki sio haba.

Ushiriki huu ulimpa Crystal Asige fursa sio tu ya kuimba pamoja na mojawapo ya bendi kuu barani Afrika, bali pia kumkutanisha na wanamuziki wengine kama vile Bensoul, Nviiri na kikundi cha Kaskazini.

Ingawa hivyo, wasilolijua wengi ni kwamba Crystal si mgeni ulingoni.

Ni mwandishi wa nyimbo na ana vibao kadha pia. Baadhi ya nyimbo zake ni pamoja na Me and You, Karibia, Back to Me na Show Me More miongoni mwa zingine.

Hasa anafahamika kwa kibao chake Pulled Under, wimbo unaojumuisha albamu yake ya kwanza Karibia.

Wimbo huu ulipanda hadi nambari moja kwenye chati za burudani nchini Uingereza mwaka wa 2016.

Hii ilimletea sifa na mashabiki wengi waliomsifu kwa kuleta mdundo mpya kwenye fani hii.

Msanii Crystal Asige. Picha/ Maktaba

Aidha, kipaji chake cha uimbaji kimempa fursa ya kusafiri hapa nchini na ng’ambo na huenda hii ni mojawapo ya sababu zilizomfanya kuwa msanii wa kwanza na wa kike wa kipekee kusajiliwa chini ya lebo ya Sol Generation.

Crystal alilelewa mjini Mombasa ambapo alianza kuvutiwa na sanaa tokea utotoni huku ndoto yake ikiwa kuwa mwanamuziki au produsa wa filamu.

Akiwa katika shule ya upili aliendeleza ndoto hii huku akishiriki katika michezo ya thieta. Lakini matatizo yalibisha maishani mwake alipoanza kukumbwa na ugumu wa kusoma ubao na vitabu darasani kwa sababu ya kukosa kuona.

Ni suala lililomlazimu kupata matibabu lakini mambo yalizidi kuwa mabaya zaidi ambapo ili kuficha udhaifu wake, angejifanya kwamba anaweza kufanya mambo sawa na wanafunzi wenzake.

Mwaka wa 2007 alipokamilisha shule ya upili, alienda nchini Uingereza kusomea masuala ya filamu na thieta katika Chuo Kikuu cha West of England, Bristol.

Akiwa huku matatizo yake ya macho yalizidi na baada ya kufanyiwa uchunguzi zaidi wa kimatibabu, alipatikana anaugua maradhi ya glaucoma yanayojulikana kuangamiza retina, sehemu inayopokea nuru ndani ya jicho.

Na baada ya kufanyiwa upasuaji mara kadha, hatimaye alipoteza kabisa uwezo wake wa kuona.

Japo kupoteza uwezo wake wa kuona kulikuwa changamoto kuu kwake sio tu katika maisha yake ya kawaida bali pia kimuziki, alijikakamua na kuzidi kujiundia jina katika fani ya burudani.

Mwaka wa 2014 alizindua albamu yake ya kwanza Karibia, iliyomtambulisha na kumshindia mashabiki sio haba.

Kutalii hapa na pale

Kama mwanamuziki binafsi, vilevile mwanachama wa bendi ya ‘Chemi Chemi LIVE’, amepata fursa ya kusafiri hapa nchini na ng’ambo.

Aidha, mbali na kuwa mwanamuziki, yeye pia ni msemaji na mjumbe wa VIP (Visually Impaired Person), shirika linaloangazia masuala ya watu wanaokumbwa na ulemavu wa kuona, ambapo yeye huzungumzia changamoto hizi kupitia chaneli yake ya YouTube “Blind Girl Manenos”.

Mojawapo ya mambo yanayomng’arisha sio tu muziki, bali imani yake thabiti na ukakamavu ambao amezidi kuuonyesha licha ulemavu wake.

Crystal ni kigezo cha wengi kwamba inawezekana kukabiliana na changamoto zako maishani na kuibuka mshindi kwa kutimiza ndoto zako, na haina shaka kwamba hii inampa nguvu ya kuzidi kujiendeleza kimuziki na kujijengea himaya katika ukumbi huu ambao umemfumbia macho kwa muda mrefu.

MAPOZI: Cedo

Na PAULINE ONGAJI

JINA lake linapotajwa, basi huandamana na orodha ya baadhi ya majina makuu katika muziki nchini vilevile vibao maarufu.

Jina lake ni Cedric Kadenyi lakini miongoni mwa mashabiki anafahamika kama Cedo, mwelekezi na produsa wa muziki wa kampuni ya Pacho Group Limited, aliyeamua kuacha taaluma yake kama wakili na kujitosa katika burudani.

Anafahamika hasa kama produsa, mhandisi, mcheza piano na hata mwandishi wa nyimbo huku akisifika kwa kutoa huduma zake kwa baadhi ya wanamuziki wanaotambulika nchini na mbali.

Baadhi ya vigogo aliofanya kazi nao ni Sauti Sol, Nyota Ndogo, Hart the Band, Nyashinski, Dela, King Kaka, Kristoff, Everlast, Naiboi, Redsan, Amos and Josh, Frasha na Avril miongoni mwa wengine wengi.

Nje ya Kenya amefanya kazi na wasanii kama vile Chameleon kutoka Uganda, Vanessa Mdee na Rich Mavoko kutoka Tanzania miongoni mwa wengine.

Heshima na utambuzi wake unatokana na baadhi ya kazi maarufu ambazo amezishughulikia. Baadhi ya nyimbo ambazo amerekodi ni pamoja na Sura yako, Mungu Pekee, Masheesha, Adabu, Gudi Gudi, Problem na Badder than Most, miongoni mwa zingine.

Mbali na muziki, pia huduma zake amezipanua na kuhusisha kitambulisho cha baadhi ya mashirika na kampeni maarufu nchini kama vile SportPesa, Mkopa Solar, Mshwari, Kenya Charity Sweepstake, Tusker Jenga Game, Jubilee Insurance, Niko na Safaricom Live, Safaricom Kenya Live na zingine nyingi.

Aidha, alikuwa produsa kwenye msimu wa nne wa shindano la Coke Studio (Season 4).

Ni ustadi huu ambao umemfanya kutambuliwa sio tu humu nchini bali pia nje ya mipaka ya Kenya. Mwaka wa 2013 na 2014 alitambuliwa kama produsa bora wa mwaka kwenye tuzo za Groove Awards.

Mwaka wa 2015, alishinda tuzo ya produsa bora wa mwaka kwenye tuzo za AFRIMA.

Mojawapo ya mambo ambayo yanamtenganisha na maprodusa wengine nchini ni kwamba mbali na kurekodi muziki, yeye ni mcheza piano hodari, suala linalomwezesha kubuni midundo ya kipekee kila anapokaa chini kurekodi nyimbo.

Uwezo wake wa kufasiri mihemko ya mwandishi na kuwa kibao cha kuwasisimua wengi, aidha, umemfanya kujiundia jina, huku sifa yake ya kukumbatia ubunifu na kufanyia kazi aina tofauti za muziki ikimfanya kuwa kipenzi cha wengi.

Mbali na hayo, utaratibu na utafiti anaofanya kabla ya kurekodi nyimbo, umefanya kazi zake kuwa na kina, vilevile kipawa chake cha kuunda uhusiano wa kipekee na wasanii anaoshughulikia kazi zao, vikimfanya kuwa bingwa katika nyanja hii.

Alijitosa katika masuala ya kurekodi muziki kwa mara ya kwanza kati ya mwaka wa 2007 na 2008 huku hasa akishughulikia nyimbo za injili na hata kufanya kazi na baadhi ya majina makuu katika ulimwengu wa muziki wa injili nchini, ikiwa ni pamoja na Kevoh Yout, Mr. T, Maximum Melodies, Betty Bayo na marehemu Kaberere miongoni mwa wengine.

Mwanzo wa safari

Mwaka wa 2011 alikuwa akishughulikia hafla ya Niko na Safaricom Live, na ni wakati huu kazi yake ilivutia bendi ya Sauti Sol, na hivyo kuadhimisha mwanzo wa safari kama produsa wa mojawapo ya bendi maarufu barani.

Kumbuka kuwa wakati huo alikuwa pia akiwafanyia kazi baadhi ya wanamuziki maarufu ikiwa ni pamoja Size 8, Jimmy Gait, Jaguar, Camp Mulla na P-Unit.

Kama produsa wa bendi ya Sauti Sol, alisafiri nao kila mahali na kuhusika katika kila shughuli ya kurekodi muziki wao, suala lililompa mfichuo nchini na kimataifa.

Hata hivyo, baada ya kufanya kazi na bendi hii kwa muda, miaka miwili iliyopita aliamua kushika hamsini zake kujiundia jina kama produsa huru.

Lakini hilo kamwe halijazima azimio lake la kuzidi kung’aa kwani kuambatana na anavyozidisha kasi, bila shaka ni ishara tosha kwamba kamwe hana nia ya kurudi nyuma.

MAPOZI: Young Wallace

Na PAULINE ONGAJI

PINDI majina ya baadhi ya waelekezaji wa video matata nchini Kenya yanapotajwa, bila shaka lake huwepo.

Anafahamika miongoni mwa mashabiki kama Young Wallace, Afisa Mkuu Mtendaji wa Convex Media na mmojawapo ya waelekezaji maarufu wa video hapa nchini, huku baadhi ya kazi zake zikiendelea kung’aa karibu na mbali.

Baadhi ya video ambazo ameelekeza ni pamoja na Barua, Tam Tam, Dawa ya Moto, Take it Slow, Kingston Girl, No More, Kamua Leo, Story Yangu, Sijafika, Mpango Wa Kando, One Way, Mungu Yupo na Marungu miongoni mwa zingine.

Na katika harakati hizo ametangamana na baadhi ya vigogo katika ulimwengu wa muziki nchini ikiwa ni pamoja na Bahati, Willy Paul, Size 8, Sauti Sol, Wyre, Kidis, DNA, Wyre, Ameleena, Dennoh, Gloria Muliro, Kambua, Ringtone na Jimmy Gait kwa kutaja tu wachache.

Lakini Young Wallace hajang’aa katika uelekezaji wa video za muziki pekee kwani amepanua huduma zake na kujumuisha matangazo ya kibiashara, vipindi na hata filamu fupi.

Kinachomtenganisha na wenzake nchini ambao huenda vipaji vyao vinatokana na mafunzo pekee, ni ujuzi wake wa kipekee unaochochewa na kiu kiliomsukuma kujifunza kazi hii kupitia mtandao.

Vilevile, ustadi wake unatokana na wepesi wake kimawazo ambao umemwezesha kushughulikia nyimbo za midundo tofauti, vile vile nyimbo za kilimwengu na hata za injili.

Unyenyekevu

Aidha, unyenyekevu wake umekuwa siri ya ufanisi wake ambapo inasemekana kwamba wakati mmoja alimfanyia kazi mwelekezi mmoja nchini bila malipo, katika harakati za kupiga msasa ujuzi wake.

Penzi lake katika taaluma hii lilianza kutokana na kiu ya kusaka kipato.

Wazazi wake waliacha kazi na kuhamia katika maeneo ya mashambani, wakati huo akiwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia (JKUAT), ambapo pia alikuwa rapa chipukizi.

Lakini baada ya kuimba na kurekodi ngoma yake ya kwanza, hakuwa na senti za kumlipa mwelekezi wa video.

Baada ya jitihada zake za kutafuta pesa za shughuli hii kugonga mwamba, ilimbidi kutumia pesa alizokuwa amepewa na mamake kwa minajili ya kulipa karo kurekodi video, suala lililomlazimu kuacha chuo akiwa katika mwaka wake wa pili kutokana na ukosefu wa karo.

Hakuwa na pesa za kurekodi video yake, na hivyo alilazimika kufanya kazi katika ‘cyber café’ kwa miezi minne huku akijifunza kuhusu masuala ya kompyuta.

Young Wallace. Picha/ Maktaba

Aliamua kufanya utafiti mwenyewe mtandaoni, shughuli iliyomchukua wiki moja na baadaye aliweza kujihariria video hiyo katika studio moja eneo la River Road.

Cha kushangaza ni kwamba baada ya video hiyo kupeperushwa kwenye vituo vya televisheni, kazi yake ilipokelewa vyema na mashabiki.

Wasimamizi wa studio iliyohusika walifurahishwa sana na mapokezi haya hasa ikizingatiwa kwamba awali, kazi zao hazikuwa zimewahi kuchezwa hewani. Hii ilimpa heshima na kumfanya kupewa fursa ya kushughulikia video mle.

Ni hapa alimwendea mwelekezi J Blessing aliyekubali kumfanya msaidizi wake, baadaye akafanya kazi na kampuni ya LB Films kabla ya kuzindua kampuni yake ya Convex Media.

Lakini ufanisi huu haumaanishi kwamba ameweza kujificha kutokana na utata unaoandama wengi kwenye fani ya burudani. Wakati mmoja kuliibuka tetesi kwamba alikuwa ameshindwa kukamilisha kazi za baadhi ya wanamuziki hata baada ya kulipwa.

Lakini licha ya utata huo, amezidi kuwa thabiti katika harakazi zake za kujiundia jina katika fani hii na hivyo kustahili heshima kama mmoja wa waelekezaji video za muziki wanaoenziwa hapa Kenya.

MAPOZI: Mary Oyaya

Na PAULINE ONGAJI

WASHIKADAU na mashabiki wengi wa filamu nchini watadhani kwamba ni Mkenya mmoja tu; Lupita Nyong’o, ambaye amewahi kujiundia jina kule Hollywood, Amerika.

Ukweli ni kwamba kuna waigizaji kibao kutoka humu nchini ambao licha ya kutoangaziwa sana na vyombo vya habari, wamefaulu kufika kwenye upeo wa jukwaa hilo.

Mmoja wao ni Mary Oyaya, mwigizaji ambaye ameshiriki katika baadhi ya filamu za haiba ya juu ulimwenguni.

Umaarufu wake hasa ulitokana na filamu ya Star Wars: Episode II – Attack of the Clones ambapo aliigiza nafasi yake Luminara Unduli.

Huu ulikuwa mwaka wa 2002, nafasi iliyomweka kwenye orodha moja na waigizaji maarufu ambao wamewahi kupamba makala tofauti ya filamu hiyo.

Baadhi yao ni Barriss Offee, Samuel L. Jackson, Ewan McGregor, Natalie Portman na Ian McDiarmid miongoni mwa wengine.

Fursa ya kuigiza nafasi hii ilitolewa na ajenti wake ila ili kuifanikisha, ilimbidi kufanyiwa majaribio katika Fox Studios ambapo aliwapiku washindani wengine wengi.

Ni fursa iliyomwezesha kushiriki katika baadhi ya tamasha kuu za filamu katika mataifa mbalimbali Amerika na Ulaya. Miongoni mwazo Celebration; hafla kubwa zaidi ya filamu za Star Wars.

Aidha, ameshiriki katika nafasi ndogo katika sinema mbalimbali kama vile Lost Souls, Down and Under na Farscape.

Na katika harakati hizo anajivunia kuingia kwenye jukwaa moja na baadhi ya maprodusa na waigizaji maarufu, miongoni mwao George Lucas, Wynona Ryder na Barriss Offee.

Mzaliwa wa mji wa Mombasa, Pwani ya Kenya, Mary Oyaya aliishi katika mataifa kadha ikiwa ni pamoja na Canada, Sweden na Australia. Safari yake katika masuala ya burudani na hasa uigizaji ilianza tokea utotoni.

Lakini mbali na uigizaji, yeye pia ni mwanamitindo, shughuli iliyochangia pakubwa kujihusisha kwake katika masuala ya uigizaji.

Taaluma yake kama mwanamitindo ilianza mwaka wa 1996 baada ya kukamilisha kozi ya uigizaji. Kama mwanamitindo ameshirikishwa kwenye majarida tofauti ya kimataifa ikiwa ni pamoja na CAT and S.

Kampuni za haiba ya juu

Pia, anajivunia kufanyia matangazo wasanifu mavazi magwiji, vilevile kampuni za haiba ya juu za kimataifa ikiwa ni pamoja na Salvatore Ferragamo, Gucci, Chanel, Jan Logan, Sergio Rossi.

Kando na hayo, ameshiriki katika matangazo kibao ya kibiashara ikiwa ni pamoja na Telstra Communications na Hewlett Packard.

Lakini licha ya kujihusisha na masuala ya burudani, kimasomo pia amejipiga msasa kwani ana shahada mbili za uzamili; katika Masuala ya mahusiano ya kimataifa na katika Masuala ya ustawi wa kijamii wa kimataifa.

Aidha, sawa na wazazi wake ambao waliwahi kuhudumu kama wanadiplomasia kwa miaka mingi, amewahi kufanya kazi katika shirika la Umoja wa Mataifa na mashirika mengine yasiyo ya kiserikali, huku pia akiwahi kufanya kazi na wakimbizi nchini Australia.

Wahenga walisema kwamba mcheza kwao hutuzwa, lakini kwa Oyaya, utambuzi wake kimataifa umepiku umaarufu wake hapa nyumbani.

Ukweli ni kwamba sio wengi wanaomfahamu sana, suala linalohuzunisha hasa ikizingatiwa kwamba yeye ni mmojawapo wa vigezo vikuu vinavyopaswa kuigwa.

MAPOZI: Eric Musyoka

Na PAULINE ONGAJI

YEYE ni mmojawapo wa maprodusa wanaoheshimika nchini kutokana na kazi yake safi, huku akijivunia kufanyia kazi baadhi ya nyimbo maarufu nchini.

Jina lake ni Eric Musyoka, produsa wa nyimbo na mmiliki wa lebo ya Decimal Records, ambayo imekuwa kitambulisho cha baadhi ya nyimbo safi nchini na mbali.

Katika kipindi cha takriban miongo miwili, Musyoka kama anavyofahamika miongoni mwa mashabiki, anajivunia kufanyia kazi baadhi ya wasanii maarufu hapa Kenya na eneo la Afrika Mashariki.

Amerekodia albamu wasanii wa haiba ya juu kama vile Daddy Owen (Son of Man), Juliani (Mtaa Mentality), Monique (Color Black) miongoni mwa wengine.

Upande wa nyimbo, anajivunia kushughulikia kazi za baadhi ya wasanii maarufu miongoni mwao Prezzo, TID, SEMA, Mr Lenny, Bamzigi, Nameless, AY, Wyre, Peter Miles, Nikki na Nonini huku baadhi ya nyimbo zake maarufu zikiwa ni pamoja na Leta Wimbo, Nataka Kudunda, Watasema Sana, Make a Choice, Muwala, Nipe Nikupe, Hii Ngoma na Furahi Day miongoni mwa zingine.

Pia amehusika katika kuchanganya nyimbo za baadhi ya wasanii marufu kama vile Elani (KooKoo, Jana Usiku, Hapo Zamani), Sauti Sol (Sura Yako, Nerea), Octopizzo (Nani, Black Star, Salute Me), Nonini (LATT, Mbele) Nameless (African Beauty) kati ya wengine.

Aidha, ameshirikiana na baadhi ya majina makuu eneo la Afrika Mashariki ikiwa ni pamoja na Prof. Jay na Kleptomaniaks kurekodi kibao Njoo, wimbo ulipopata umaarufu sio tu hapa nchini Kenya bali pia Tanzania.

Mwaka wa 2010, alishirikiana na kikundi Just a Band, kwenye kibao Ha-He alichoandika na kurekodi. Wimbo huu uling’aa eneo la Afrika Mashariki na hata kutambuliwa na vyombo vya habari vya kimataifa na hivyo kuthibitisha uwepo wa bendi hii katika fani ya muziki.

Kama mtunzi wa nyimbo za filamu, kazi yake imesikika kwenye filamu Nairobi Half-Life na VeVe.

Pia ametunga muziki wa matangazo ya kibiashara, vilevile vitambulisho vya baadhi ya mashirika makubwa nchini.

Mwaka wa 2006 alitangazwa mshindi wa tuzo ya produsa bora wa mwaka kwenye tuzo za Kisima Awards.

Mojawapo ya sifa ambazo zimemtenganisha na wengine kwenye fani hii ni uwezo wake wa kukaa mbali na mwangaza mbaya wa vyombo vya habari, na badala yake kuacha kazi yake imwangazie.

Aidha, anafahamika kwa subira yake katika kazi anazofanya, suala linalomfanya kumakinika na kila mradi anaohusika nao.

Alijitosa katika shughuli za kurekodi muziki mwaka wa 1997 katika studio ya Sync Studio chini ya ukufunzi wa Muhammud Omar, Ambrose Mandugu na Ted Josiah.

Wakati huo alikuwa mmojawapo wa wanarepa kwenye kikundi cha Nannoma, kilichojumuisha marafiki zake kutoka shule ya upili.

Kikundi hiki kilitumbuiza pamoja hadi 2001, alipoamua kufuata ndoto yake ya kuwa produsa huku akifanya kazi na Ukoo Flani na Mau Mau.

Wasanii wa kwanza kuwarekodi walikuwa Juliani, Zakah na Kah. Wakati huo alirekodia kikundi Ukoo Flani na Mau Mau, vibao kama vile Dandora LOVE, DC na Sisi, Angalia Saa, Punchline Kibao na vingine vingi.

Baadaye aliajiriwa na lebo ya Homeboyz Entertainment kama produsa mkuu. Ili kujiimarisha kitaaluma, alienda ng’ambo kuzidisha masomo aliporejea alianzisha studio Decimal Media House.

Wakati huu alisajili kikundi cha P-Unit na kukirekodia ngoma kama vile Juu Tuu Sana, Kare, Hapa Kule, You Guy, Mobimba na Weka Weka kati ya vingine.

Yeye ni mfano wa kuigwa miongoni mwa maprodusa wengine nchini, sio tu kutokana na unyenyekevu wake bali pia umakini kila anaposhughulikia kazi zake.

Sasa kibarua kwake ni kuzidisha moto huu, vilevile kudumisha jina hili safi ambalo amejiundia kwa miaka.

MAPOZI: Philip Makanda

Na PAULINE ONGAJI

KILA unaposikia baadhi ya nyimbo maarufu humu nchini; hasa za kizazi cha sasa, basi kuna uwezekano kwamba huenda zimepitia mikononi mwake.

Kwa takriban miongo miwili, Philip Makanda au Philo kama anavyofahamika miongoni mwa mashabiki, amehusika pakubwa katika sekta ya burudani humu nchini, mwanzoni kama mwanamuziki, kisha kama produsa.

Yeye ni mwanzilishi na mmiliki wa studio ya Mainswitch, inayofahamika kwa kuturekodia baadhi ya kazi safi. Amerekodia baadhi ya wasanii mashuhuri nchini Kenya na mbali, huku kazi zake zikipata umaarufu.

Mojawapo ya masuala ambayo yamemweka kwenye kilele cha orodha ya maprodusa maarufu nchini, ni ubunifu wake.

Aidha, anasifika kwa uwezo wake wa kutobagua aina ya muziki au wasanii anaofanya kazi nao.

Ndiposa kazi yake inahusisha kufanya kazi na wasanii wa muziki wa injili na hata wa nyimbo za kilimwengu.

Baadhi ya nyimbo ambazo amezifanyia kazi ni pamoja na albamu nzima ya Utamu wa Maisha yake mwanamuziki Daddy Owen, inayojumuisha kibao cha kichwa hicho hicho, alichoimba kwa ushirikiano na Juliani, vilevile Kipepeo, Huu Mwaka na Kioo zake Jaguar.

Ustadi wake umedhihirika kupitia orodha ndefu ya wasanii wa haiba ya juu ambao amefanya nao kazi. Humu nchini amefanya kazi na wanamuziki kama vile Daddy Owen, Jaguar, Nameless, Redsan, Amani, Vivian, Janet Atieno, G-kon, Kidis, MOG, Papa Dennis na Big Pin.

Nje ya mipaka

Barani Afrika anajionea fahari kufanya kazi na wasanii kama vile Iyanya kutoka Nigeria na Mafikizolo wa Afrika Kusini.

Safari yake katika uwanja wa burudani ilianza miaka 17 iliyopita kama mwanamuziki, wakati huo akiwa mwanachama wa bendi ya muziki ya Boomba Clan.

Pamoja na wenzake kwenye kikundi hicho walifahamika hasa kwa vibao kama vile Chonga Viazi na African Timer.

Ni hapa ndipo kiu ya kutaka kujihusisha na muziki kiliiongezeka, nia ikiwa kuwa produsa.

Kwa hivyo fursa ilipojitokeza, pamoja na wenzake hawakusita kujaribu bahati yao katika fani ya kurekodi. Huku wenziwe wakifuata mkondo wa kurekodi video, aliamua kujitoma katika masuala ya sauti.

Msisimko huu ulimpeleka katika lebo ya Ogopa, kampuni aliyoifanyia kazi kwa muda mrefu na kumpa fursa ya kuhusika katika kurekodi baadhi ya nyimbo maarufu.

Hii ilikuwa hadi mwaka wa 2012 alipoamua kushika hamsini zake na kuzindua rasmi studio ya Mainswitch.

Huu ulikuwa mwanzo wa safari yake kama produsa binafsi na mumliki wa studio, na hivyo kufungua mfereji wa ufanisi ambao ulimkutanisha na baadhi ya wadau maarufu katika sekta ya burudani.

Weledi wake katika fani hii umehimiliwa na kisomo chake katika taaluma hii ambapo amesomea shahada ya digrii ya mifumo ya habari na teknolojia (Information Systems and Technology) kutoka chuo kikuu cha USIU.

Haina shaka kwamba Philo amejiundia jina kama mmoja wa maprodusa wanaojulikana nchini.

Lakini swali kuu ni iwapo atafanikiwa kuzidisha mng’ao huu na kuendelea kuvuma sio kutokana na kazi zake za zamani, bali zijazo, tofauti na baadhi ya maprodusa waliomtangulia ambao mwanzoni walibisha kwa kishindo, ila wakaja kufifia wasijulikane waliko kwa sasa.

MAPOZI: Nick Mutuma

Na PAULINE ONGAJI

ANATAMBULIKA sio tu kutokana na ustadi wake kama muigizaji, bali pia kama mwanamuziki, mwanamitindo, mtangazaji na produsa miongoni mwa kazi zingine.

Hasa Nicholas Munene Mutuma au ukipenda Nick Mutuma, anatambulika kutokana na uigizaji katika baadhi ya vipindi maarufu sio tu humu nchini, bali katika bara lote la Afrika.

Baadhi ya vipindi maarufu nchini Kenya na kwingineko barani Afrika ambavyo ameshiriki ni pamoja na Changes, Shuga, State House, Skinny Girl in Transit na This Is It kutoka Nigeria.

Aidha, ameshiriki kwenye filamu Disconnect iliyozinduliwa nchini kote Aprili 2018 na ambayo ilifanya vyema.

Mzawa wa eneo la Meru, nchini Kenya, Nick Mutuma alilelewa jijini Dar es Salaam, Tanzania, ambapo alisomea katika shule ya kimataifa ya The International School of Tanganyika.

Baadaye alijiunga na shule ya kimataifa ya Braeside School jijini Nairobi, ambapo alikamlisha masomo ya upili.

Mwaka wa 2005, alijiunga na chuo kikuu cha United States International University (Nairobi), hadi 2010 huku akihitimu shahada ya Usimamizi wa Kibiashara wa Kimataifa.

Ustadi ulianza kujitokeza akiwa angali mchanga alipogundua penzi lake kwa sanaa ambapo mara kwa mara angeshiriki katika michezo ya drama shuleni.

Alipata mfichuo wa kwanza kwenye televisheni ya Kenya mwaka wa 2008, alipopata nafasi ya kuigiza kama Luka, kijana mdogo wa chuo cha masomo ya juu anayeishi maisha ya umaskini, hali iliyomsukuma kujihusisha na shuga mami. Nafasi hii iliibua maoni mbalimbali.

Aidha, mwaka huo huo alishiriki kwenye kipindi Changes kilichokuwa kikipeperushwa na kituo cha MNET, ambapo aliigiza kama Richard, kijana anayegundua kwamba alitekwa nyara hospitalini baada ya kuzaliwa, nafasi aliyoihifadhi kwa misimu mitatu, na hivyo kudhihirisa ukomavu wake kama mwigizaji.

Hata hivyo nyota yake iling’aa aliposhiriki kwenye kipindi Shuga (2008)ambapo alivunja rekodi kwa kuwa muigizaji aliyehifadhi nafasi yake kwenye kipindi hicho kwa misimu yote mitano. Kipindi hicho kiliangazia maisha ya vijana jijini Nairobi na tabia ya kushiriki ngono kiholela.

Aidha, kipindi hiki kilizindua taaluma za uigizaji za baadhi ya majina makuu ulingoni, ikiwa ni pamoja na mshindi wa tuzo ya Oscars, Lupita Nyong’o.

Mwaka wa 2014, Mutuma alishiriki kwenye kipindi State House, ambapo aliigiza nafasi ya mwana mkorofi wa rais, anayenaswa na penzi la binti ya mmojawapo wa wafanyakazi.

Miaka miwili baadaye, alijihifadhia nafasi ya kuigiza kama Tomide kwenye kipindi This Is It cha Nigeria.

Kutokana na umaarufu wa kipindi hiki, mwaka 2018 kiliteuliwa kama kipindi bora kwenye tuzo za AMVCA.

Mwaka 2018 pia alishiriki kwenye filamu Disconnect iliyofanya vyema miongoni mwa mashabiki.

Baadaye alishiriki kwenye msimu wa tano wa kipindi Skinny Girl in Transit.

Utangazaji

Kama mtangazaji, Mutuma amekuwa mshiriki mkuu katika vipindi mbalimbali kwenye redio na televisheni.

Aliwahi kujumuishwa mara kadha miongoni mwa waigizaji wa kiume wanaovutia zaidi.

Mwaka wa 2013, alitangazwa kama mwigizaji mwenye kipato kikubwa.

Kimuziki, hajaachwa nyuma huku akifahamika kwa nyimbo kama vile 254 Anthem, kibao alichoimba kwa ushirikiano na Lyra Aoko.

Wimbo huu ulikuwa ukizungumzia mambo mazuri kuhusu Kenya.

Septemba 2014, alizindua kibao kingine kwa jina That Life kwa ushirikiano na Cool Kid Taffie.

Katika masuala ya mitindo amehusika katika utangazaji wa bidhaa mbalimbali ikiwa ni pamoja na Nivea Fresh Active.

Kwa kawaida huwa vigumu kwa wasanii kujihusisha katika tasnia mbalimbali na kung’aa, lakini kwa Nick Mutuma, mambo ni tofauti huku akidhihirishia wenzake kwamba kwa kweli inawezekana.

MAPOZI: Gerald Langiri

Na PAULINE ONGAJI

KENYA imetambulika katika ngazi za juu za uigizaji hasa kupitia mwigizaji Lupita Nyong’o aliyeiweka nchi hii kwenye ramani ya uigizaji alipojishindia tuzo ya Oscars.

Haiishii hapo tu kwani hapa nyumbani pia vipaji vya uigizaji ni vingi na Gerald Langiri, mwigizaji, produsa na mwelekezi wa filamu na vipindi ni mmoja wao.

Alitambulika kupitia kipindi cha ucheshi cha House of Lungula na hivyo kujiundia jina kama mmojawapo wa waigizaji wanaotambulika sana nchini.

Mbali na filamu hiyo ambapo aliigiza kama Harrison, pia alijiundia jina kupitia Fundimentals ambapo aliigiza kama Joseph.

Pia ameshiriki katika filamu zingine ikiwa ni pamoja na Inherited, Flowers and Bricks, Orphan, 24 hours to live, Accidental kidnapping, Gun theory miongoni mwa zingine.

Aidha, ameshiriki katika vipindi kama vile Santalal, Mali, Stay, Papa Shirandula, Pendo, Pray and Prey, In the forest na Shit Happens kati ya zingine.

Kama mwelekezi amechangia katika vipindi mbalimbali ikiwa ni pamoja na Selina, Veve, Going Bongo, The Unprotected bali na kuwa mwelekezi wa waigizaji wa kipekee kutoka Kenya katika msimu wa pili wa shindano la BET Top Actor Africa.

Ni ustadi huu ambao umemfanya kutambuliwa katika tuzo mbalimbali. Mwaka wa 2014 alituzwa kama muigizaji bora msaidizi katika vipindi katika tuzo za Kalasha Film and Television Awards kutokana na kushiriki kwake kama Nico kwenye kipindi Stay.

Mwaka wa 2015 aliteuliwa kama mwigizaji bora wa vichekesho katika tuzo za Africa Magic Viewers Choice Awards (AMVCA).

Aidha, aliteuliwa kama muigizaji bora wa mwaka katika tuzo za Nigerian Entertainment Awards (NEA) na kuwa muigizaji wa kipekee kutoka Afrika Mashariki kushirikishwa kwenye orodha hiyo.

Langiri hajang’aa tu kama muigizaji kwani pia ni mwandishi wa masuala ya filamu. Weledi wake ulidhihirika mwaka wa 2014 alipotuzwa kama mwanahabari/ bloga bora wa filamu katika tuzo za African Film Development Awards 2014.

Mjumbe

Mwaka 2018 aliteuliwa kama mjumbe wa kampuni ya mavazi ya Vazzi Clothing line na kuungana na watu wengine maarufu kama vile DJ UV, Camp Mulla, Huddah, DJ kayTrixx, DJ Crème, DJ Hypnotic na Shaffie Weru ambao wamewahi kushirikiana na kampuni hiyo.

Safari yake kama mwigizaji ilianza akiwa angali mdogo ambapo akiwa katika shule ya chekechea, tayari alikuwa ameanza kung’aa katika fani hii huku akishiriki katika michezo ya uigizaji katika mikutano ya wazazi.

Ni kipaji alichokiendeleza hata alipojiunga na shule ya msingi na ya upili, kabla ya kujitosa rasmi katika uigizaji mwaka wa 2011 huku ari yake ya uigizaji ikichochewa na miamba wa uigizaji nchini kama vile Lizz Njagah, Ken Ambani na Raymond Ofula. Hii ilikuwa baada ya kusomea shahada yake katika chuo kikuu na hata kuajiriwa.

Hata hivyo, ufanisi huu usikufanye udhani kwamba hajawahi kukumbana na changamoto.

Kama mwigizaji mwingine yeyote hasa humu nchini, mambo hayajakuwa rahisi huku akikabiliwa na uhaba wa nafasi za uigizaji.

Hata hivyo changamoto hizi hazijazima mwanga wake.

Ni ustadi ambao umemkutanisha na waigizaji wengi maarufu nchini na kimataifa ikiwa ni pamoja na Wakenya waliobobea katika fani hii kama vile Blessing Lungaho, Vera Atsango, Lydia Gitachu, Faith Munini na Innocent Njuguna miongoni mwa wengine, vile vile kigogo kutoka Nigeria, Desmond Elliot.

Bila shaka amejiundia jina kiasi cha kutambulika hata nchini Nigeria, taifa linalotawala fani ya filamu barani. Lakini linalosalia ni kuona iwapo utambuzi huu unatosha kumuinua na kumfikisha katika upeo wa Lupita kwa kuigiza kwenye jukwaa la Hollywood.

MAPOZI: Kendi

Na PAULINE ONGAJI

ALIJITOSA katika ulingo wa muziki akiwa na umri wa miaka 17 pekee na hata kusajiliwa na kampuni ya Calif Records, ambayo wakati huo ilikuwa mojawapo ya lebo kuu nchini.

Nyakati hizo Kendi aliachia vibao kadha vikiwa ni pamoja na Uko Fresh, wimbo uliovumisha jina lake na kumtambulisha kama mmojawapo wa wasanii wa kike walioheshimika nchini enzi hizo, suala lililomfanya kuwa kipenzi cha wengi.

Lakini hata kabla ya kudumu, muziki wake ulianza kudidimia, ishara iliyojitokeza kwenye wimbo wake Uko Fiti ambao haukufanya vyema na kadhalika hakuwahi kuutumbuiza jukwaani.

Haikuwa muda kabla ya msanii huyu kutoweka kutoka fani ya muziki kwa muda huku fununu zikienea kuhusu chanzo cha ukimya wake.

Wakati huu alipamba vichwa vya baadhi ya vyombo vya habari kutokana na uvumi uliohusisha maisha yake binafsi na kimuziki.

Kwa mfano kulizuka tetesi kuhusu ugomvi kati yake na lebo ya Grandpa Records huku akiamua kujitenga na lebo hiyo.

Kulingana naye, ugomvi huo ulitokana na video waliyorekodi lakini haikuzinduliwa, vile vile video nyingine ambayo alihisi kana kwamba haikusukumwa jinsi alivotarajia.

“Nyakati hizo ilikuwa vigumu sana kushirikiana na msanii wa lebo nyingine au kufanya kazi na kampuni nyingine ya kurekodi nyimbo. Wakati huo nilikuwa nataka kufanya kazi na lebo tofauti katika mradi fulani na uamuzi wangu ukafanya kidogo tukakosa kuelewana, tofauti kabisa na uvumi uliokuwa unaenea,” Kendi alisema katika mahojiano mwaka 2018.

Matatizo haya yalimuathiri nusura aachane na uimbaji isingalikuwa ni msukumo kutoka kwa wanamuziki wengine.

“Wasanii kama vile Avril, Atemi, Sanaipei Tande, Jua Cali, Jaguar na Bahati miongoni mwa wengine walijitokeza kunisaidia kuthibitisha kazi yangu. Isitoshe, Jaguar alinijia binafsi na kunipa moyo,” alisema.

Ni mawimbi yaliyomfanya kukaa mbali na mwangaza wa muziki kwa muda, hadi mwaka jana aliporejea katika fani ya muziki kwa kishindo na mwamko mpya, suala linalodhihirika katika kazi yake murwa.

Kwa mfano aliachia kibao Into You alichoimba kwa ushirikiano na Vinnie Banton.

Kampuni mpya

Vilevile alirudi huku akiwa ameshirikiana na kampuni mpya yenye makao yake nchini Uswidi.

Hapa Kenya kampuni hiyo ilinuiwa kushughulika na kuunda kitambulisho chake kabla ya kuanza kusajili wasanii wengine.

Aidha, tofauti na awali, lebo hii ilitarajiwa kuwa mwamko mpya kwa wasanii wa humu nchini ambapo wangehakikishiwa usalama wa kazi na mapato yao kama mbinu ya kuwapa jukwaa la kung’aa kimuziki.

Aliporejea aliwaahidi mashabiki kwamba tofauti na wasanii wengi nchini Kenya ambao wameshindwa kujinasua kutokana na akili finyu ya kumakinika na Genge, Kapuka na kadhalika, angewaiga wanamuzki kama vile bendi ya Sauti Sol, wanamuziki wa Nigeria na Tanzania ambao wameweza kupanua mawazo yao na kushirikisha mitindo mipya ili kupata mnato wa kimataifa.

Hata hivyo kibao Into You kilichofafanua ujio wake mpya hakikufanya vyema hasa kuambatana ‘views’ kwenye mtandao wa YouTube, suala ambalo hata hivyo alijitetea na kusema kwamba hategemei ‘views’ kubaini umaarufu wa kazi zake na kwamba mwendo wake kurejea katika ulingo wa muziki ni wa asteaste.

Sasa ni mwaka mmoja baada ya kurejea na iwapo kwa kweli ameweza kuafikia utabiri huu, mashabiki ndio wataamua.

MAPOZI: Ethan, Vince & Brandon

Na PAULINE ONGAJI

WANALETA msisimko mpya katika sekta ya RnB ambayo kidogo imesahaulika humu nchini Kenya huku utunzi wao ukihusisha muunganisho wa ladha mbalimbali za muziki tena kwa ustadi mkubwa.

Jukwaani wanafahamika kama Jadi, bendi iliyoundwa sio tu na waimbaji, bali pia watunzi, wacheza ala na hata washairi, suala ambalo limeongeza mvuto kwa kazi zao na kuzipa kina, na hivyo kuongeza hadhara.

Bendi hii ya wanachama watatu ambayo inajumuisha Edward’s Okoth Bryan al-maarufu Ethan, Vincent Mutuma al-maarufu Vince na Brandon Tumbo au kwa usahili Brandon, iko mbioni kuteka mioyo ya wapenzi wa muziki nchini.

Ethan ni mwimbaji, mwandishi wa nyimbo ambapo pia ana uwezo wa kutunga nyimbo za mitindo mbalimbali.

Yeye ndiye mwenye wajibu wa kuongeza lahani kwenye vibao vya kikundi hiki.

Msanii huyu alitambua kuwa angeimba akiwa na miaka sita pekee huku akipata chocheo kutoka kwa mamake ambaye alikuwa mwanachama wa kwaya ya kanisa.

Ili kuendeleza penzi lake la muziki aliamua kutumia kila fursa aliyopata ya uimbaji huku mara kwa mara akiwatumbuiza familia, jamaa na wageni nyumbani.

Ni kipaji kilichojitokeza hata zaidi aliposhiriki na hata kutwaa ushindi kwenye shindano la uimbaji wakati huo akiwa na miaka 12 pekee. Ushindi huu ulimpa ujasiri wa kufuata kwa uthabiti ndoto yake.

Kwa upande wake, Vince ambaye analeta mchango wa uimbaji, uandishi wa nyimbo na densi katika bendi hii, alianza kuimba akiwa angali mchanga, na hata kabla ya kujifunza kutembea alikuwa anaonyesha ishara ya kung’aa katika burudani.

Kama mtoto wa mhubiri, alikuwa na fursa nyingi za kutumbuiza tangu utotoni huku penzi lake katika densi likichochea uamuzi wake wa kujitosa katika muziki.

Vince aliingia katika ulimwengu wa burudani kupitia kikundi cha densi lakini akaamua kuondoka baada ya kutambua kwamba penzi lake katika uimbaji lilikuwa limepiku densi.

Na kwake Brandon ambaye ni muimbaji, mwandishi wa nyimbo, mcheza gitaa na mshairi, muziki umekolea kwenye mishipa ya damu hasa ikizingatiwa kwamba licha ya kuwa mwanafunzi wa ujarisiamali chuoni, bado anafuatilia ndoto yake ya kuwa mwanamuziki.

Bendi hii ilianzishwa Novemba 2018 na kampuni ya Kaka Empire huku muziki wao ukiunganisha mchanganyiko wa muziki wa RnB, Pop na Afro Soul katika kila kibao walichotunga.

Licha ya kwamba bado wabichi kimuziki, wanazidi kuteka wapenzi kwa sauti zao za kupendeza, vilevile vibao vyao vinavyotambulika kwa kunasa hisia za mashabiki.

Jibu

Wanasema kwamba wao ndio jibu kwa wapenzi wa aina zote za muziki nchini, huku wakitajwa kama nafuu ambayo sekta hii imekuwa ikisubiri.

Kinachowatenganisha na vikundi vingine vya kawaida nchini ni muunganisho thabiti kati yao, suala linalofanya iwe rahisi kwao kufanya kazi kwa pamoja.

Kwa sasa wanaendelea kupata umaarufu kupitia kibao chao Mimi na Wewe.

Ni sifa hizi zilizovutia jicho la Kaka Empire. Kulingana nao, kusajiliwa na kampuni hii kumewapa fursa ya kupanua hadhara yao na wanasisitiza kwamba hili litakuwa jukwaa la kuwaongezea umaarufu kimuziki.

Haina shaka kuwa kwa mashabiki wengi, Jadi wangali wachanga lakini kasi waliyojitosa nayo katika ulingo huu ni hakikisho la mwanzo wa ufanisi wao kimuziki.

Wajibu wao kwa sasa ni kudhihirisha iwapo wataendeleza msisimko huu na kudhihirishia ulimwengu kwamba mbio hizi sio mvuke tu!

MAPOZI: Azma Mponda

Na PAULINE ONGAJI

JINA lake sio geni katika ukumbi wa Hip Hop sio tu nchini Tanzania alikozaliwa, bali Afrika Mashariki kwa ujumla.

Alikuwa msanii wa kwanza wa mdundo huu Afrika Mashariki kutazamwa mara milioni moja kwenye mtandao wa YouTube.

Alipojitosa katika muziki kwa mara ya kwanza, Azma Mponda alijiundia jina kutokana na muziki wake uliojaa ujumbe mzito wa uhalisi wa maisha, mojawapo ya sababu zilizomtenganisha na wasanii wengine wa mdundo huo nchini mwao.

Kwa wasiomfahamu, Azma anafahamika kwa vibao kama vile Kidedea, Garagasha, Shubiliga alioimba kwa ushirikiano na Gilad, miongoni mwa vingine.

Kilichompa mvuto mwanzoni ulikuwa ujumbe mzito katika nyimbo zake, suala lililomfanya kudhaniwa kuwa na msimamo mkali.

Lakini licha ya kujivunia mashabiki kutokana na mdundo huu, ilimlazimu kulegeza kamba na kupunguza makali ya ujumbe wake kama mbinu ya kufikia soko jipya.

“Wajua awali nilikuwa naimba hip hop yenye ujumbe mzito, muziki ambao haukukubalika kabisa redioni na hivyo ilinibidi kupunguza makali kidogo na kutunga nyimbo ambazo zinahusisha mada za kufurahisha masikio kama vile mapenzi,” alisema kwenye mahojiano baada ya kurejea.

Kwa hivyo, mwaka wa 2016 alirejea baada ya kimya cha miaka mitatu huku akiwa na mkakati mpya wa kupunguza makali hayo, ambapo alianza kwa kuangusha kibao Astara Vaste alichoimba kwa ushirikiano na Belle.

Kama mbinu ya kuthibitisha uwepo wake katika jukwaa la muziki Afrika Mashariki, wakati huo alirejea akiwa na kikundi cha maprodusa na mapromota mbali na kuwa na usimamizi mzuri.

Hii kulingana naye ilikuwa mbinu ya kunasa mashabiki kutoka sehemu hizi zote hasa ikizingatiwa kwamba maprodusa hao walielewa muktadha wa nchi yao na hivyo wangemshauri kutunga nyimbo zinazofurahisha mashabiki katika nchi hizi tofauti.

Na haikuwa muda kabla ya mkakati huu kuanza kuzaa matunda kwani wakati huo alianzisha ziara mbalimbali hapa nchini, kwao Tanzania, na Uganda.

Pia, huo ulikuwa mwanzo wake wa kushirikiana na wanamuziki wa haiba ya juu kutoka humu nchini, Tanzania na Uganda.

Humu nchini, Azma ameshirikiana na wasanii kama vile Khaligraph Jones na Gilad. Nchini Tanzania ameshirikiana na wasanii kama vile Joseph Mbilinyi na Izzo Bizness miongoni mwa wengine, huku nchini Uganda akifanya kazi na mwanadada AVM kwenye kibao Whine Up.

Lakini haikuwa rahisi kwa Azma alipofanya uamuzi huu kwani alipowasili humu nchini ili kufanyia shughuli zake hapa, wengi walidhania kwamba kama wasanii wengine kutoka Tanzania waliofifia baada ya kuja Kenya, pia kwake hatima ingekuwa hiyo hiyo.

Lakini Azma ameenda kinyume na matarajio ya wakosoaji wake na kuzidi kung’aa huu ukiwa mwaka wake wa tatu tangu achukue uamuzi wake.

“Tatizo ni kuwa wasanii wanaokumbana na masaibu hayo wanapohamisha shughuli zao hapa Kenya huwa na tatizo la kusikiza ushauri. Wengi wao hawasikizi mapromota na maprodusa wao hivyo inakuwa vigumu kwao kunasa mashabiki kama inavyohitajika,” alisema katika mahojiano.

Pia, siri yake ya ufanisi ilikuwa mazoea yake ya kushiriki kwa kila kitu kinachofanywa kuhusiana na muziki wake, vile vile uhusiano wake mzuri na watu wote wanaohusika na muziki wake.

Huu ni mwaka wa tatu tangu Azma Mponda afanye uamuzi huu na huenda muda unavyozidi kusonga, atakuwa funzo kwa wenzake na kuwathibitishia kwamba inawezekana kuendesha shughuli katika mataifa yote ya Afrika Mashariki, na katika harakati hizo kunasa mashabiki.

MAPOZI: Kidum

Na PAULINE ONGAJI

NI mmojawapo wa wanamuziki wa kigeni wanaofanya vyema katika fani ya muziki nchini.

Kwa mashabiki zake anafahamika kama Kidum, lakini jina lake halisi ni Jean-Pierre Nimbona, msanii mzaliwa wa Burundi ambaye amejiundia jina sio tu kama mwanamuziki, bali pia utunzi na upigaji ngoma.

Mojawapo ya sababu ambazo zimemfanya kuendelea kung’aa kimuziki ni ushupavu wake katika utunzi ambapo anajumuisha wasanii wachache wanaotambulika kwa nyimbo zao zenye ujumbe na mdundo wa kuvutia huku mara nyingi nyimbo zake zikihusisha za kilimwengu na kiroho.

Baadhi ya nyimbo zake ni pamoja na ‘Nitafanya’, ‘Haturudi Nyuma’, ‘Mungu Anaweza’, ‘Kichuna’, ‘Pete’, ‘Mapenzi’, ‘Relax’, ‘Kimbia’ na ‘Mulika Mwizi’ miongoni mwa zingine.

Kazi hii nzuri imemfanya kutambuliwa katika baadhi ya tuzo za haiba ya juu sio tu Afrika Mashariki, bali barani kote huku akiwahi kupokea tuzo za Kora Awards.

Na katika harakati hizo amejiundia heshima kiasi cha wasanii wengi wanaofanya vyema katika eneo hili kutaka kushirikiana naye, na hata kutawazwa kama mjumbe wa amani kutokana na juhudi zake za kukuza matumaini na maridhiano eneo la Afrika Mashariki.

Albamu yake ya kwanza kwa jina Yaramenje aliyoizindua mwaka wa 2001 ndiyo iliyomthibitisha kama sauti ya amani katika eneo hili la Afrika.

Hii ilifuatiwa na albamu yake ya pili kwa jina Shamba, miaka miwili baadaye. Hakuonyesha ishara za kulegea kwani mwaka wa 2006 aliangusha albamu ya Ishano iliyojumuisha vibao vyake maarufu ikiwa ni pamoja na ‘Kichuna’.

Mwaka wa 2010 alizindua albamu yake Haturudi Nyuma iliyojumuisha vibao maarufu kama vile Mapenzi, Nitafanya na Haturudi Nyuma, na kwa mara ya kwanza kumshindia tuzo ya Kora Awards.
Mwaka wa 2012, alizindua albamu yake kwa jina Hali Na Mali iliyojumuisha vibao kama vile Mulika Mwizi, Kimbia, Enjoy na Hali Na Mali.

 

Msanii Jean-Pierre Nimbona ‘Kidum’ akitumbuiza katika mojawapo ya hafla awali. Picha/ Maktaba

Kidum alijihusisha na muziki kwa mara ya kwanza mwaka wa 1984 akiwa na miaka kumi pekee ambapo alianza kama mcheza ngoma.

Miaka miwili baadaye alijiunga na bendi ya Imvumero Band ambapo alifanya kazi hapo kwa miaka sita.

Baadaye alijiunga na bendi ya Imboneza Band, iliyokuwa inamilikiwa na chama tawala nchini Burundi UPRONA ambapo aliichezea kati ya mwaka wa 1992 na 1993.

Kujihusisha kwake na bendi hizi kulimpa mfichuo na tajriba katika muziki ambapo mwaka wa 1994 alizindua bendi yake kwa jina Electric Power.

Hata hivyo, kutokana na vita vya kikabila nchini humo, bendi hiyo ilidumu kwa mwaka mmoja pekee.

Ni matatizo hayo ya kisiasa yaliyomsababisha mwaka wa 1995 kutoroka kutoka nchini mwake na kuhamia hapa Kenya ambapo alitarajia kuendeleza kipaji chake cha uimbaji.

Na haikuwa muda kabla ya kuanza kuonyesha kipaji chake kwani pindi baadaye alijiunga na bendi ya Hot Rod Band ambapo aliimba hapo hadi mwaka wa 2003.

Hii ilikuwa hadi alipoanzisha bendi yake ya Boda Boda Band mwaka wa 2004, ambayo anaiendesha hadi sasa.

Bendi yake imefanya shoo katika sehemu mbali mbali ulimwenguni ikiwa ni pamoja Mashariki ya Kati, Ulaya, Amerika na Amerika Kusini.

Sifa kuu ambayo imezidi kumtenganisha na wasanii wengine wa kawaida ni vipaji vyake tofauti katika usanii kama muimbaji, mpiga ngoma na mtunzi, huku uwezo wake wa kupitisha ujumbe kwa lugha tofauti ikiwa ni pamoja na Kiswahili, Kiingereza na Kihispania pia ukipanua himaya yake ya mashabiki na hivyo kumtambulisha zaidi.

MAPOZI: Dr King’ori

Na PAULINE ONGAJI

IWAPO wewe ni mraibu wa vipindi vya televisheni, basi huenda u shabiki mkuu wa The Wicked Edition, kipindi kinachopeperushwa na kituo cha runinga cha NTV na ambacho mhusika mkuu ni Dr King’ori.

Kazi yake safi imemwezesha kushiriki katika baadhi ya vipindi maarufu vya ucheshi nchini ikiwa ni pamoja na Kenya Kona, Offside Show na hata Churchill Show, na katika harakati hizo kujiundia jina kama mmojawapo wa wacheshi wanaotambulika na kuheshimika nchini.

The Wicked Edition kinachotambulika kutokana na kuangazia masuala halisi kwa kutumia tashtiti kimelinganishwa na kile cha Daily Show, chake mcheshi Trevor Noah.

Lakini ni ucheshi wake ambao mara kwa mara unaakisi utafiti wa kina kuhusu masuala yanayokabili nchi uliomvumisha, kumjengea himaya ya mashabiki na kuweka jina lake kwenye ramani ya wacheshi wa kutajika.

Ufanisi wake umemfanya pia kutambulika na vigogo katika ulimwengu wa burudani na utangazaji nchini Kenya, kama vile mcheshi Kazungu Matano maarufu Captain Otoyo, na mtangazaji Larry Madowo.

Mzawa wa eneo la Blue Valley, Kaunti ya Embu, Dr King’ori alianza kuonyesha kipaji chake cha ucheshi akiwa angali mdogo ambapo akiwa katika darasa la tatu, tayari alikuwa ashabandikwa jina ‘Makokha’, lake mcheshi maarufu aliyetamba kupitia kipindi cha Vioja Mahakamani.

Wanafunzi wenzake kila mara wangemteua kila mnenaji au chale alipohitajika.

Cha kushangaza ni kwamba wakati huo hakuwa na ujasiri kuhusu uwezo wake ambapo kila alipovumbua kichekesho, angemweleza mwenzake ili akiwasilishe kwa wenzake darasani.

Kadhalika alikuwa akiwatangazia wenzake kuwa wakati mmoja atakuwa na shoo yake kwenye televisheni, ndoto ambayo wengi waliipuza.

Hata hivyo ujasiri na kujiamini kwake kulimwezesha kupiga msasa kipaji chake hasa kupitia uigizaji wake wa riwaya shuleni baada ya kukamilisha shule ya upili.

Baadaye alisafiri hadi jijini Nairobi na kutembelea jumba la Nation Centre kuwasilisha wazo la shoo yake.

Mwanzoni haikuwa rahisi kwani hata baada ya kupewa fursa ya kubuni jaribio la kipindi, alikumbana na changamoto ya pesa za kufadhili mradi huu.

Lakini hakufa moyo ambapo baadaye alibahatika rafiki yake alipompa ofa ya kuandika mswada wa ucheshi katika shindano la GBS.

Kazi yake safi ilimhifadhia mwaliko wa yeye pia kushiriki huku akiwa mmojawapo wa washindi.

Na ni hapa ndipo safari yake kama mcheshi wa kulipwa iling’oa nanga. Huo ulikuwa mwaka wa 2010, wakati ambao pia aligundua anaweza kujipatia kipato kwa kuchekesha watu.

Wakati huu alikuwa akitumbuiza hasa katika klabu, kabla ya kuanza kuchangia katika kipindi cha Kenya Kona ambapo alifanya kazi kwa mwaka mmoja.

Kazi yasifika

Akiwa hapa, kazi yake ilisifika sana hata miongoni mwa watu mashuhuri katika fani hii. Mmoja wao alikuwa mcheshi Kazungu Matano ambaye alifurahishwa na jinsi alivyokuwa akipanga ucheshi wake.

Mwaka wa 2013 alimuomba aandikie kipindi cha Offside Show katika kituo cha televisheni cha NTV ambapo pamoja waliunda vipindi 69 huku akiunda kitambulisho chake kama Kinyanjui.

Kinachomtenganisha na wacheshi wengine wa kawaida humu nchini ni uthabiti wake katika kutafiti na kuhusisha masuala muhimu katika ucheshi wake.

Anasema mambo bado na ndoto yake ni kuvunja kabisa mipaka ya ukabila nchini akitumia ucheshi na pia kuteka ulingo wa kimataifa karibuni.


MAPOZI: Produsa R Kay

Na PAULINE ONGAJI

KWA zaidi ya mwongo mmoja amejijengea himaya kubwa kama mmojawapo wa maprodusa mahiri sio tu humu nchini bali katika kanda ya Afrika Mashariki.

Miongoni mwa mashabiki anafahamika kama R Kay, lakini jina lake halisi ni Robert Kamanzi.

R Kay. Jina lake halisi ni Robert Kamanzi. Picha/ Hisani

Mojawapo ya sifa zinazomtambulisha ni jitihada zake katika harakati za kubadilisha muziki wa Afrika Mashariki kufikia viwango vya juu, suala ambalo limemfanya kuheshimika kiasi cha kuhusuka pakubwa katika kufanya kazi na wanamuziki wengi wanaotamba nchini na mbali.

Baadhi ya wanamuziki wa haiba ya juu kutoka Afrika Mashariki na mbali ambao amewafanyia kazi ni pamoja na Nameless, Ambassada, Jemimah Thiong’o, Esther Wahome, Bahati, Deux Vultures, Bobby Wine, Blue 3, Kidum, Lady Jay Dee, Ray C, Professor Jay, Massamba, Shanel, Jimmy Gait, marehemu Oliver Mtukudzi, Mercy Masika, Rufftone, Suzanna Owiyo, Prezzo na Sanna miongoni mwa wengine, huku mchango wake katika muziki ukidhihirika kupitia takriban albamu 100 ambazo amehusika katika kuzirekodi.

Mojawapo ya sifa ambazo zimezidi kumuundia jina ni msimamo wake mkali hasa inapowadia wakati wa kurekodi muziki, ambapo mara kwa mara amenukuliwa akisema kwamba hawezi kujihusisha na nyimbo ambazo kiwango cha ubora ni cha chini.

Ustadi wake umedhihirika pia kutokana na mchango wake ambao umefanya baadhi ya wanamuziki kutuzwa.

Kwa mfano, mwaka wa 2008 aliweka jina lake katika vitabu vya kumbukumbu kazi yake Sweet Love, wimbo ulioimbwa na Wahu, ulipopelekea mwanamuziki huyu kuwa Mkenya wa kwanza kutwaa tuzo ya MTV MAMA Awards, tuzo kuu barani Afrika.

Sio hayo tu, kibao Sunshine’, kilichoimbwa na Nameless kwa ushirikiano wa Habida, kilimfanya Nameless kutwaa tuzo ya Msanii Bora wa Mwaka wa kiume katika tuzo hizo hizo, mwaka mmoja baadaye.

Hajahusika tu katika kusaidia wengine kutambulika. Kama produsa, R Kay amepokea tuzo mbalimbali.

Ameshinda tuzo humu nchini, Afrika Mashariki na hata mbali ikiwa ni pamoja na Kisima Awards, CHAT Awards hapa Kenya, Channel O Awards (Afrika Kusini), Kilimanjaro Awards za Tanzania, PAM Awards za Uganda, na MTV MAMA Awards, zinazoandaliwa kuwatuza wasanii na washikadau wa burudani barani.

Na katika harakati hizo amezidi kujizolea heshima.

Mwaka wa 2015 alisemekana kupokea donge nono zaidi la kipato kutoka kwa chama cha ukusanyaji hakimiliki ya wanamuziki nchini -MCSK kwa upande wa majukwaa ya kieletroniki, huku pesa hizo zikitokana na mchango wake katika baadhi ya kazi za wanamuziki nchini ikiwa ni pamoja na Nameless, Esther Wahome, Mbuvi, Sarah Kiarie na Eunice Njeri miongoni mwa wengine.

Ushawishi wadhihirika

Ushawishi wake katika sekta hii ulidhihirika hata zaidi kati ya mwaka wa 2003 na 2004, Benki ya Dunia ilipomhusisha pakubwa katika utafiti kuhusu biashara ya muziki nchini.

Penzi lake kwa muziki lilianza akiwa mchanga huku akipata msukumo kutoka kwa babake ambaye alikuwa msanii.

Alihamia humu nchini mwaka wa 1998 kutoka Burundi.

Mwaka wa 1999 alipata ajira katika studio ya Nextlevel Productions ambapo alijifunza kazi yake.

Mwaka wa 2000, aliangusha albamu yake Solutions. Tokea hapo R Kay amefanya kazi na baadhi ya studio kuu humu nchini ikiwa ni pamoja na Homeboyz, Ketebul na Soundmind.

Mbali na kuwa produsa, yeye pia ni mtunzi wa nyimbo, muigizaji, muimbaji na mwelekezi, fani ambazo pia zimemwezesha kujitosa katika ujasiriamali katika masuala ya burudani.

MAPOZI: Eddie Butita

Na PAULINE ONGAJI

NI mmojawapo wa wachekeshaji wanaotamba nchini kwa sasa huku akijiundia jina kupitia kipindi cha Churchill Show na Churchill Raw.

Jina lake ni Edwin Butita, lakini jukwaani anafahamika kama Eddie Butita, mcheshi, mwigizaji, mwandishi wa miswada ya vipindi, mwelekezi wa thieta, produsa na mfawidhi, miongoni mwa mambo mengine mengi.

Lakini licha ya kujihusisha na mambo mengi, Butita hasa amenoa makali yake katika uvunjaji mbavu ambapo jitihada zake zimemfanya kuwa miongoni mwa wachekeshaji wanaothaminiwa sana katika kipindi cha Churchill Show.

Eddie Butita. Picha/ Maktaba

Mojawapo ya sifa zinazomtenganisha na wengine ni ustadi wake wa kutumia tashtiti hasa kuonyesha maisha ambayo wakazi wa vitongoji duni hukumbana nayo.

Ni suala ambalo kando na kuangazia uhalisia wa matatizo yanayowakumba wakazi wa maeneo haya, linawaacha mashabiki wakiangua vicheko.

Na ni uthabiti huu ambao umemuundia jina kiasi cha kumfanya kupata fursa za kutumbuiza katika shoo zingine zikiwemo Laugh Festival, Night of a Thousand Laughs, Kenya’s Biggest Laughs, The Hot Seat, Kenya Kona Comedy, The Trend, Crazy Monday Comedy Night, Nescafe Red Sensation Party, 3D Comedy na Kids Festival miongoni mwa zingine.

Lakini kando na masuala ya uchekeshaji, Eddie Butita amepanua himaya yake na kujiundia jina katika uandishi wa miswada na uelekezi wa vipindi, kiasi cha kuchangia katika baadhi ya vipindi vinavyotambulika kama vile Churchill Show, Churchill Raw na Eric Omondi Untamed miongoni mwa vingine.

Katika taaluma yake fupi kama chale, amechangia pakubwa katika kubuni mawazo na mikakati ambayo imeimarisha sekta ya burudani.

Ndiposa mwana burudani huyu ameenda hatua zaidi na kujihusisha katika ujasiriamali ambapo yeye ni mwanzilishi wa kampuni ya Stage Presence Media and Entertainment, inayohusika na maandalizi ya hafla na kusimamia vipaji.

Mzawa wa mtaa wa Kariobangi, jijini Nairobi, alianza kama mwanamuziki kabla ya kutambua kipaji chake cha ucheshi wakati huo akiwa katika shule ya upili, kipaji kilichochewa na wacheshi na waigizaji wa humu nchini na ng’ambo.

Baadhi ya watu waliompa msukumo wa kujitosa katika burudani ni pamoja na mchekeshaji Kevin Hart na mwigizaji Tyler Perry kutoka Amerika, vile vile mwana vichekesho Daniel ‘Churchill’ Ndambuki.

Ajitosa rasmi katika burudani

Mwaka wa 2010 baada ya kukamilisha elimu ya shule ya upili, aliamua kujitosa rasmi katika burudani baada ya kupata fursa ya kushiriki katika majaribio ya kipindi cha Churchill Live.

Ni hapa nyota yake iling’aa kwani katika shoo yake ya kwanza aliwashangaza wengi kwa kunasa macho ya mashabiki katika kipindi hicho licha ya kuwa limbukeni.

Na tangu wakati huo, ameendelea kusisimua mashabiki ambapo kwa sasa ni mmojawapo wa wachekeshaji wanaothaminiwa katika kipindi hicho, suala ambalo limempa fursa ya kushiriki katika vipindi vingine.

Huku akiongozwa na ndoto ya kuwa katika upeo wa ulimwengu wa burudani, swali ni ni iwapo ataepuka jinamizi ambalo limekuwa likiwaandama wengi katika fani hii; kung’aa kwa muda kisha kutoweka.

MAPOZI: Maqbul Mohammed

Na PAULINE ONGAJI

AMETUPAMBIA sebule zetu mara kadha kupitia vipindi vya televisheni ambavyo ni mmoja wa waigizaji.

Kwa wasiomfahamu, anaitwa Maqbul Mohammed, mmojawapo wa waigizaji shupavu nchini.

Hasa sura yake inatambulika kutokana na kushiriki kwake katika kipindi Auntie Boss kama Donovan, mchumbake Eve D’Souza.

Lakini pia mwigizaji huyu anafahamika kwa mchango wake katika vipindi kama vile Makutano Junction, kipindi kilichozinduliwa 2007 ambapo aliigiza kama Karis Mabuki; vingine ni Reflections na Lies that Bind, alipoigiza kama Justine Mareba.

Kando na vipindi, ameshiriki pia katika filamu ikiwa ni pamoja na Behind Closed Doors, Weakness, filamu iliyozinduliwa 2009 ambapo anaigiza kama Nicky na All Girls Together, sinema iliyozinduliwa 2008 na ambapo anaigiza kama Felix.

Ustadi huu umemwezesha kuigiza kando ya vigogo kama vile Eve D’ Souza, Ruth Maingi, Maureen Koech, Justine Mirichii na Florence Nduta, miongoni mwa wengine.

Safari yake katika uigizaji ilianza mwaka wa 1995 wakati huo akiwa shuleni ambapo mwalimu wake alimchagua kuigiza katika mchezo fulani kutokana na tabia yake ya kupiga kelele darasani.

Msanii Maqbul Mohammed. Picha/ Hisani

Hata hivyo, ilimbidi asubiri hadi baada ya kukamilisha shule ya upili ili kufufua kipaji chake.

Hii ilikuwa baada ya kutazama tangazo kwenye gazeti kuhusu mchezo fulani wa kuigiza katika Phoenix Theatre.

Aidha weledi huu umechangiwa na sababu kwamba kipaji hiki kimekolea katika familia yao, hasa ikizingatiwa kuwa dadake Shadya Delgush, pia ni mwigizaji.

Kabla ya kuingia kwenye ulingo wa televisheni, alikuwa ashajiundia kitambulisho kwenye thieta huku akiigiza katika michezo ya kuigiza kama vile Backlash, kazi yake Cajetan Boy, drama iliyoangazia unyanyapaa dhidi ya wanaougua Ukimwi.

Kadhalika alishiriki katika mchezo wa Enemy of the People, ulioundwa wakati ambapo nchi ilikuwa inakumbwa na matatizo ya kisiasa huku akitumbuiza mbele ya hadhira iliyojumuisha watu maarufu kama vile Gavana wa Kaunti ya Kisumu, Anyang’ Nyong’o.

Kuacha alama

Na tokea hapo Maqbul hajawahi kuangalia nyuma ambapo amekuwa akiendelea kukinoa kipaji chake huku akizidi kuacha alama thabiti katika safari yake.

Mara yake ya kwanza kujitosa kwenye televisheni ilikuwa mwaka wa 2003, wakati huo bado akiwa katika umri wa kubalehe, aliposhiriki katika kipindi Reflections kilichokuwa kikipeperushwa na kituo cha televisheni cha KBC.

Hata hivyo nyota yake iling’aa mwaka wa 2006 alipopata fursa ya kuigiza kama Karis katika Makutano Junction.

Ni mng’ao ulioendelea na mwaka wa 2011 alikuwa mmojawapo wa washiriki wakuu katika kipindi cha Lies that Bind. Kipindi hiki kilimwezesha kuteuliwa kama muigizaji bora msaidizi katika tuzo za Kalasha 2013.

Na haikushangaza alipopata fursa ya kuwa mhusika mkuu katika kipindi Auntie Boss.

Mbali na hayo yeye pia ni mtangazaji wa redio katika Capital FM.

Kwa sasa ndoto yake ni kung’aa katika jukwaa la kimataifa na hata kujumuika na Lupita Nyong’o kule Hollywood.

MAPOZI: Eve D’Souza

Na PAULINE ONGAJI

SURA yake sio geni katika uwanja wa burudani nchini ambapo ametupambia skrini zetu za televisheni kwa vipindi mbali mbali.

Anafahamika kama Eve D’Souza, mmojawapo wa waigizaji ambao wamejiundia umaarufu kupitia vipindi kwenye televisheni na hivyo kuorodheshwa miongoni mwa utumbuizaji wanaotambulika sana nchini Kenya.

Mchango wake katika ulingo wa burudani unadhihirika kupitia vipindi na filamu ambazo ameshiriki.

Hasa amefanikiwa kunasa macho ya wengi kupitia mchango wake kama mwigizaji mkuu katika kipindi Auntie Boss kinachopeperushwa kwenye kituo cha televisheni cha NTV ambapo anaigiza kama Varshita, kando yake Maqbul Mohammed.

Katika kipindi hiki Maqbul anajipata amekwama katika uhusiano mbaya na Varshita, fungamano linalozidi kukera kila kuchao.

Sio katika kipindi hicho tu anacholeta ladha ya ucheshi kwani pia katika kipindi Varshita kinachopeperushwa kupitia kituo cha Maisha Magic East, mkondo ni huo huo, suala ambalo linalodhihirisha ucheshi wake.

Lakini mbali na vipindi hivi viwili, ameshiriki katika Freelance, Big  Brother Africa 3, MCEE Africa, Vibe City, Travel Diaries ambapo aliigiza kama yeye mwenyewe na pia Mentality.

Na katika harakati hizo amepata fursa ya kufanya kazi na baadhi ya waigizaji wanaong’aa nchini ikiwa ni pamoja na Nyce Wanjeri, Grace Muna, Maqbul Mohammed, David Opondoe na Sandra Dacha miongoni mwa wengine.

Lakini hata anavyozidi kung’aa kama muigizaji, D’Souza hajatamba tu katika fani hiyo kwani pia amehusika katika nafasi mbali mbali kama vile produsa, msimamizi wa uundaji vipindi na mtangazaji wa redio.

Ustadi wake kama mtangazaji ulidhihirika alipojishinda tuzo ya mtangazaji bora wa kike kwenye tuzo za Chat Awards mfululizo katika mwaka wa 2003 na 2004.

Alizaliwa miaka 39 iliyopita katika Kaunti ya Mombasa kama mwanawe Andrew na Martina D’Souza ambapo alisoma katika shule za Loreto Convent na Aga Khan, Mombasa.

Baadaye alijunga na Chuo Kikuu cha Catholic University of Eastern Africa (Cuea) jijini Nairobi ambapo alisomea ualimu wa lugha ya Kingereza na fasihi ya Kiingereza.

Safari yake katika ulingo wa burudani iling’oa nanga mwaka wa 2001 alipojiunga na kituo cha redio cha 98.4 Capital FM, nafasi aliyohudumu hadi Novemba 2010 ambapo alikuwa mtangazaji mkuu wa vipindi Hits not Home work, The East African Chart na Capital in the Morning.

Lakini ufanisi huu haujamhepusha na majanga kwani wakati mmoja alifichua kwamba yeye ni mhanga wa ubakaji. Tukio hilo lililotokea mwaka wa 2005 baada ya kutekwa nyara, suala lilimuathiri kwa miaka.

Lakini licha ya hayo, hakuacha nyota yake ididimie kwani muigizaji huyu ameendelea kutumbuiza.

Kwa sasa kando na kuigiza katika vipindi mbali mbali, D’Souza anaendesha kampuni ya kuunda vipindi ya Moonbeam Productions kinachohusika katika kurekodi kipindi cha ucheshi cha Auntie Boss.Pia, yeye ni balozi wa kampuni ya mavazi ya Store 66, jijini Nairobi.

Japo hajapata tuzo yoyote kutokana na uigizaji licha ya kufumu katika fani hii kwa takriban miongo miwili, haina shaka kwamba amechangia pakubwa katika sekta ya kuzalisha vipindi nchini.

Sasa swali kuu ni iwapo atapanua himaya yake na kuongeza mawazo mengine kwenye kazi zake, kando na ucheshi tu!

MAPOZI: Lenana Kariba

Na PAULINE ONGAJI

KATIKA uwanja wa uigizaji, jina lake sio geni ikizingatiwa kwamba tayari ameshiriki katika baadhi ya vipindi na filamu maarufu nchini Kenya.

Licha ya ufanisi huu, kwa Lenana Kung’u Kariba au kwa usahili Lenana Kariba, kama waigizaji wengi nchini, hakijakuwa kibarua rahisi kujitambulisha miongoni mwa mashabiki.

Huku akiwa ameshiriki kwa vipindi na filamu kadha maarufu humu nchini, Lenana amethibitisha kipawa chake kama mmojawapo wa waigizaji wanaotamba sana nchini.

Baadhi ya vipindi na filamu ambavyo ameshiriki ni kama vile How to Find a Husband, Changing Times, Saints, Lies that Bind, House of Lungula na Live or Die miongoni mwa vingine na zingine.

Ni suala ambalo limemvunia sifa na utambulisho mkubwa huku kushiriki kwake katika baadhi ya vipindi maarufu nchini kukimpa nafasi ya kugusana mabega na baadhi ya majina makubwa katika ulingo wa uigizaji nchini ikiwa ni pamoja na Lizz Njagah, Ian Mbugua, na Gerald Langiri miongoni mwa wengine.

Lakini mbali na masuala ya uigizaji Lenana ni msomi kwani ana shahada ya Uanahabari na mauzo kutoka Chuo Kikuu cha Daystar.

Safari yake katika fani ya uigizaji ilianza akiwa bado katika shule ya upili, wakati huo kama mwanafunzi wa shule ya upili ya St. Christophers High School, Nairobi, ambapo alijiunga na chama cha drama.

Lakini cha kushangaza ni kuwa wakati huo uigizaji haukuwa penzi lake, na hivyo kujihusisha kwake na chama hiki kulitokana na sababu kwamba kama mwanafunzi mwingine yeyote, hakuwa na budi ila kujiunga na kikundi hiki.

Hata hivyo ni mtazamo ambao aliubadilisha mwisho wa mwaka wa 2009 baada ya kukamilisha shule ya upili, ambapo kwa usaidizi wa rafikiye alishiriki katika majaribio ya uigizaji katika Kenya National Theatre, na kwa bahati nzuri akapata nafasi hiyo.

Haikuwa muda kabla ya nyota ya muigizaji huyu kuanza kung’aa ambapo mwaka wa 2010 alibisha rasmi kwenye uga huu baada ya kupata nafasi katika kipindi cha Changing Times ambapo aliigiza kama Dr. Max. Kufikia hapa nyota yake ilikuwa inang’aa zaidi kwani mwaka wa mmoja baadaye alikuwa ashajivunia nafasi ingine, wakati huu ikiwa ya kushiriki kwenye kipindi cha Saints.

Kati ya mwaka 2012 na 2014, Lenana alishiriki kwenye kipindi Lies that Bind, huku akiigiza nafasi ya Joseph Juma. Katika kipindi hiki hiki alikuwa mojawapo ya washiriki wakuu kwenye kipindi House of Lungula ambapo aliigiza kama Alex Kijani.

Msururu wa fursa za uigizaji zilizomjia ulizidi kuwa mrefu kwani mwaka wa 2014 aliigiza nafasi ya Boi kwenye filamu Live or Die.

Mwaka mmoja baadaye alipata nafasi ya kuigiza kwenye kipindi cha How to Find a Husband.

Mwaka mmoja baadaye alishiriki katika kipindi News Just In ambapo aliigiza nafasi ya Simon Mambo huku mwaka jana akipata fursa ya kushiriki katika kipindi Selina, nafasi ambayo anaishikilia hadi sasa.

Sekta imenawiri?

Yeye ni mmojawapo wa waigizaji ambao japo bidii yao imedhihirika kupitia kazi zao za ubora wa hali ya juu, bado wanakumbwa na ugumu wa kupata mvuto miongoni mwa mashabiki wa vipindi na filamu nchini.

Huenda ni kutokana na sababu kwamba sekta hii haijanawiri  vilivyo nchini.

Licha ya hayo, Lenana hana budi kufurahia mambo ambayo ameafikia kama mwigizaji, na haitakuwa ajabu iwapo hivi karibuni tutaanza kumtazama katika filamu na vipindi vinavyonasa mvuto wa kimataifa.

Simanzi katika hafla ya waliokufa katika ajali ya ndege

Hafla ya mazishi ya watu wawili walioangamia katika ajali ya ndege Oktoba 21, 2017, yafanyika katika ufuo wa Ziwa Nakuru Februari 10, 2018. Picha/ Joseph Openda

Na PETER MBURU

Kwa muhtasari:

  • Mazishi hayakuwa na jeneza, bali maua na picha pekee
  • Sam G na Mapozi hawakuwahi kupatikana tangu ajali ya Nakuru itokee
  • Babake Mapozi naye alieleza huzuni yake, akisema mwanawe alikuwa amependekeza mahali alipotaka kujenga nyumba ya kifahari
Hafla ya mazishi ya watu wawili walioangamia katika ajali ya ndege Oktoba 21, 2017, yafanyika katika ufuo wa Ziwa Nakuru Februari 10, 2018. Picha/ Joseph Openda

MAJONZI yalitanda Jumamosi katika ufuo wa Ziwa Nakuru wakati wa sherehe ya mazishi ya ukumbusho wa pamoja kwa watu wawili kati ya watano walioangamia kwenye ajali ya ndege mwaka 2017.

Kinyume na mazishi ya kawaida ambapo kungekuwa na majeneza, ni picha zao nadhifu pamoja na maua vilivyowekwa mezani katika hema.

Wawili hao, Samuel Gitau (Sam G) na John Ndirangu Njuguna (Mapozi) waliangamia pamoja na wenzao watatu Anthony Kipyegon, rubani Apollo Malowa na mwanadada Veronica Muthoni.

Hafla ya mazishi ya watu wawili walioangamia katika ajali ya ndege Oktoba 21, 2017, yafanyika katika ufuo wa Ziwa Nakuru Februari 10, 2018. Picha/ Joseph Openda

Japo watatu hao walipatikana na maiti zao kuzikwa nyumbani mwao, Sam G na Mapozi hawakuwahi kupatikana, jambo lililosukumia viongozi, familia na marafiki kupendekeza sherehe ya aina hiyo, kama njia mojawapo ya kuliwaza familia zao.

Jumamosi wakati wa maombelezi hayo, viongozi wa tabaka mbalimbali waliungana na familia za wendazao katika ufuo huo tangu ajali hiyo mwezi Oktoba.

Picha za ‘Mapozi’ na ‘Sam G’ walioangamia katika ajali ya ndege Oktoba 21, 2017. Mazishi yao yalifanyika katika ufuo wa Ziwa Nakuru Februari 10, 2018. Picha/ Joseph Openda

“Tumepitia miezi mitatu na nusu ya kuchosha, kutamausha na kuvunja moyo tulipokuwa tukitafuta miili ya wapendwa wetu,” seneta wa Nakuru Susan Kihika, ambaye pia alikuwa mwajiri wao akasema.

Babake ‘Mapozi’ naye alieleza huzuni yake, akisema mwanawe alikuwa amependekeza mahali alipotaka kujenga nyumba ya kifahari, lakini akafa kabla ya kutimiza ndoto yake.