Watumishi wa Kaunti kugoma ‘wasipothaminiwa’

Na COLLINS OMULO

WAFANYIKAZI zaidi ya 11,000 wa Kaunti ya Nairobi wametishia kugoma ikiwa Idara ya Huduma za Jiji (NMS) na viongozi wa serikali ya jiji hawatashughulikia malalamishi yao.

Wafanyikazi hao wanadai kuwa hawajapewa bima za kimatibabu, kucheleweshwa kwa mshahara na kutopandishwa vyeo.

Wanataka Mkurugenzi Mkuu wa NMS, Mohamed Badi na Naibu Gavana Ann Kananu waboreshe hali yao ya kikazi.

Wakiongozwa na katibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali ya Kaunti Tawi la Wafanyakazi wa Nairobi, Festus Ngari na Katibu wa Tawi la Jiji la Nairobi, Benson Olianga, wafanyikazi hao walisema wataanza rasmi mgomo Oktoba 13, 2021, ikiwa malalamishi yao hayatashughulikiwa.

“Ikiwa hatutaboreshewa hali ya kikazi, hatutafanya kazi. Wengi wetu tunaumia huku mshahara ukiwa ule ule,” akasema Bw Ngari.

Walisema tayari wamewasilisha malalamishi yao kwa wakuu wanaohusika.

“Hatujaona hatua yoyote iliyochukuliwa tangu tuwasilishe malalamishi yetu. Ikiwa hatutaongezewa mshahara, hatutafika kazini,” akasema Bw Ngari.

Kadhalika, alisema wafanyikazi wa kaunti hiyo hawajafurahia jinsi serikali ya kaunti imekuwa ikiwahudumia.

Kuhusiana na masuala ya kimatibabu, alisema baadhi ya wafanyikazi wamekuwa wakitumia pesa nyingi kupata matibabu kutokana na ukosefu wa bima.

Aliongeza kuwa hali hiyo inaenda kinyume na na Kifungu cha 34 (1) cha Sheria ya Ajira, 2007 na makubaliano ya pamoja kati ya wafanyikazi na serikali ya kaunti ya mwaka 2013.

Mgomo wa wahadhiri wasitishwa kupisha mashauriano ya mishahara

Na Francis Mureithi

MUUNGANO wa Wahadhiri wa Vyuo Vikuu nchini (UASU) jana ulisitisha kuwa mgomo uliotarajiwa kuanza leo huku pakiwapo hofu ungelemaza shughuli za mafunzo na masomo katika vyuo vikuu vyote 35 vya umma.

Kupitia taarifa, Katibu wa Kitaifa wa Uasu Dkt Constatine Wasonga alisema muungano huo ulifikia hatua hiyo ili kupisha mashauriano zaidi kati yake na wawakilishi wa serikali.

‘Kamati Kuu ya UASU imeamrisha kuwa muungano usitishe mgomo ili kuruhusu mazingumzo zaidi,’ akasema Dkt Wasonga.

Maafisa wakuu wa Uasu mnamo Jumapili jioni waliandaa mkutano na Katibu katika Wizara ya Elimu anayesimamia Elimu ya Juu na Utafiti, Simon Nabukwesi.Lengo la mkutano huo lilikuwa kutathmini hatua zilizochukuliwa na Wizara ya Leba kuanza utekelezaji wa mkataba wa nyongeza ya mshahara (CBA) ambao uliafikiwa hapo awali.

Kutotekelezwa kwa makubaliano hayo na usimamizi wa vyuo vikuu 35 ndiko kulikochochea Uasu kutoa notisi ya mgomo mnamo Agosti 23, ikidai wanachama wake wanaumia kimapato.

 

BENSON MATHEKA: Wakenya wamechoshwa na undumakuwili wa magavana

Na BENSON MATHEKA

HATUA ya magavana kukana makubaliano ambayo Wizara ya Afya iliafikiana na madaktari na maafisa wa kliniki ili wamalize mgomo wao, yadhihirisha kwamba wahudumu wa afya hawana mfumo thabiti wa kushughulikia matakwa yao.

Kulingana na magavana, Wizara ya Afya haikufaa kukubaliana na wahudumu hao warudi kazini bila kuhusisha serikali za kaunti. Kwa kile ambacho kinaonyesha ukosefu wa nia njema, magavana wanasema kwamba serikali za kaunti hazitaweza kutimiza yale ambayo wahudumu hao walikubaliana na wizara.

Inasikitisha kwamba badala ya kushukuru wizara kwa kusaidia kumaliza mgomo ambao umelemaza huduma katika hospitali za umma na kufanya wagonjwa kuteseka, magavana wanailaumu kwa kukubali kutimizia madaktari na maafisa wa kliniki matakwa yaliyowafanya kugoma.

Kauli ya magavana kwamba baadhi ya kaunti zilikuwa zimetimiza matakwa ya madaktari ilhali wanaendelea na mgomo, yaonyesha wakuu hao wa kaunti ndio chanzo cha migomo inayovuruga huduma za afya mara kwa mara nchini.

Badala ya kulaumu wizara kwa kukubali matakwa ya wahudumu hao, magavana wanafaa kufanya nayo mazungumzo kuelewa sababu za maafikiano hayo.

Pia kutafuta mbinu za kurekebisha makosa ambayo huenda yalitokea, badala ya kuyapuuza na kuwafuta kazi madaktari.Wizara iliamua kuketi chini na wahudumu hao wa afya ikifahamu kwamba huduma za afya zimegatuliwa.

Katiba inasema kwamba serikali ya kitaifa na za kaunti zinategemeana, kwa hivyo magavana hawafai kufanyia mzaha suala hili nzito linalohusu afya ya raia. Je, wizara inayofahamu kwamba huduma za afya zimegatuliwa inaweza kuzungumza na wahudumu bila ufahamu wa magavana? Ikiwa ilifanya hivyo, nia yake ilikuwa nini?

Je, magavana walizungumza na wizara kabla kutoa taarifa yao kuruka makubaliano ya kumaliza mgomo?Ikiwa mazungumzo yalifanyika, kwanini walitoa taarifa ya kulaumu wizara? Je, nini hatima ya madaktari waliokuwa wamegoma, baada ya magavana kukataa makubaliano ya kurudi kazini kati yao na wizara ya afya?

Ukweli ni kwamba hatua ya magavana inaweza kutumbukiza sekta ya afya katika mzozo mkubwa zaidi iwapo madaktari na maafisa wa kliniki wataendelea kugoma.Matokeo yatakuwa mabaya zaidi ikizingatiwa Wakenya wengi maskini hutegemea hospitali za umma kwa huduma za matibabu.

Labda wakati wa kurejesha huduma za afya kwa serikali ya kitaifa, kama wanavyopendekeza baadhi ya wataalamu, umewadia.Madhumuni ni kuepushia Wakenya mateso wanayopitia kila wakati wahudumu wa afya wanapogoma.

Ukweli ni kwamba sio madaktari wanaoumia huduma za afya zinapovurugika, ni Wakenya walalahoi.Magavana watafute mbinu za kurekebisha hali; si kuwafuta kazi wahudumu wa afya Wakenya wakiendelea kuteseka.

Kagwe anapotosha Wakenya – Madaktari

WANDERI KAMAU na WAIKWA MAINA

MADAKTARI na matabibu wameilaumu serikali ya kitaifa na zile za kaunti kwa kutumia mbinu chafu kwenye juhudi za kutafuta utatuzi kwa mgomo wao unaoendelea.

Hapo jana, viongozi wa vyama vya wahudumu hao walisema serikali imekuwa ikitumia vitisho na uongo, licha ya maafisa wa Wizara za Afya na ile ya Leba kususia vikao wanavyoandaa kujadili kuhusu malalamishi yao.

Katibu Mkuu wa Chama cha Wahudumu wa Kliniki (KUCO), Bw George Gibore na mwenzake wa Chama cha Madaktari na Wahudumu wa Meno (KMPDU), Dkt Chibanzi Mwachoda, walimlaumu Waziri wa Afya Mutahi Kagwe, kwa “kuwadanganya” Wakenya kwamba serikali imetoa vifaa vya kuwasaidia kujikinga kuambukizwa magojwa (PPEs).

“Bw Kagwe anawadanganya Wakenya kuwa Mamlaka ya Kusambaza Dawa (Kemsa) imetoa PPEs kwa hospitali za umma lakini huo ni uongo. Wakati vifaa kama hivyo vinapotolewa, kuna fomu maalum ambazo hujazwa ili kuonyesha ni vingapi vilivyotolewa, na muda ambao vitatumika. Hakuna hospitali yoyote ya umma inayoweza kuonyesha fomu hizo kama ushahidi wa kupokea PPEs kutoka kwa Kemsa,” akasema Bw Gibore.

Wawili hao walisema Bw Kagwe anatumia uwongo ili kuwapaka tope na kuonyesha kuwa wao ndio hawataki kushiriki kwenye mazungumzo ya kutafuta mwafaka.

“Ni vibaya kwa waziri kutumia uongo kwenye mzozo kama huu ambao unawaathiri Wakenya,” akasema Dkt Mwachoda.Mnamo Jumanne, mwenyekiti wa Baraza la Magavana (CoG), Bw Wycliffe Oparanya aliziandikia barua serikali za kaunti akiziagiza kuwafuta kazi wahudumu wote ambao wanashiriki mgomo na kuwaajiri wengine.

Hata hivyo, wahudumu walisema jana hawatababaishwa hata kidogo na vitisho hivyo, kwani hata wale wataajiriwa watakumbana na matatizo wanayolalamikia.

Wakati huo huo, Kamati ya Bunge Kuhusu Afya, jana ilimtaka Bw Kagwe kusuluhisha utata uliopo kuhusu mgomo huo kwa kutoa vifaa vya PPEs kutoka maghala ya Kemsa.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Bi Sabina Chege, aliwalaumu magavana kuwa kikwazo kwenye utatuzi wa mgomo huo wakati Wakenya wanahitaji huduma za afya kwa dharura.

Bi Chege aliwatetea madaktari na matatibu, akisema baadhi ya matakwa yao yangeweza kutimizwa wakati walipotoa makataa ya kuanza mgomo huo.

BENSON MATHEKA: Chanzo cha mgomo wa madaktari ni mapuuza

Na BENSON MATHEKA

Kwa miezi minane madaktari wanaogoma wamekuwa wakizungumza na serikali kuhusu maslahi yao hasa msimu huu wa janga la corona.

Ingawa maafisa wa serikali wamewalaumu kwa kususia kazi, ni muhimu Wakenya waelewe chanzo cha mzozo huo.

Madaktari walitoa ilani ya mgomo mazungumzo yalipokosa kuzaa matunda lakini wakaahirisha kwa siku 21 wabunge walipoashiria kuwapatanisha na serikali. Masaibu yao yaliwagusa baadhi ya wabunge waliowasikiliza hadi wakamwaga machozi.

Hata hivyo, kwa maafisa wa wizara ya afya na viongozi wanaopaswa kutatua mzozo huo, masaibu ambayo wahudumu hao wa afya wanapitia sio suala la kuwashtua.

Hii inadhihirishwa na kauli ya waziri wa afya Mutahi Kagwe kwamba wanaogoma wanafaa kufutwa kazi na wengine wapya kuajiriwa.Kwa waziri na viongozi wanaowakosoa kwa kuchukua hatua hiyo, suluhu ya mzozo huo ni kuwafuta kazi wahudumu hao kwa kukataa kufanya kazi.

Inasikitisha kwamba maafisa wa serikali hawashtushwi na vifo vya madaktari na wauguzi wanaoambukizwa corona wakiwa kazini kiasi cha kuwaambia sio wao wanaokufa peke yao.Inasikitisha kwamba serikali inashindwa kutatua mzozo huo ikijua kwamba ni Wakenya masikini watakaoumia kwa kukosa huduma za afya.

Badala ya kushughulikia malalamishi ya wahudumu wa afya, serikali ilianza zoezi la uhusiano mwema kwa kuwamiminia sifa katika kujitolea kwao kukabiliana na janga la corona kufanya watu kuamini ilikuwa inawajali.

Bw Kagwe alikuwa akikariri kwamba serikali imewapa wahudumu wa afya vifaa vya kujikinga dhidi ya corona, hadi ubora wa vifaa hivyo ulipotiliwa shaka walipoanza kuambukizwa virusi hivyo wakiwa kazini.

Mojawapo ya matakwa ya wahudumu hao ni kupatiwa vifaa bora za kujikinga na kusema kweli, wana haki ya kufanya hivyo.Kama wanavyosema viongozi wa vyama vya kutetea maslahi yao, kuhudumia wagonjwa bila vifaa bora vya kujikinga ni sawa na kujitia kitanzi.

Kwa maafisa wa serikali na viongozi wanaowakosoa, hili sio muhimu japo inahitaji nia njema tu na matumizi mazuri ya pesa kuwatimizia takwa hili.Tumeona serikali ikitoa pesa za kufadhili masuala na miradi mingine na kwa hivyo, ukosefu wa pesa haufai kuwa sababu ya kupuuza matakwa ya madaktari.

Pili, madaktari wanataka bima ya afya ili waweze kumudu gharama ya matibabu. Katika vikao vya kamati ya bunge kuhusu afya, ilibainika kuwa wizara ya afya ilirudisha pesa zilizotengewa mpango huo huku madaktari wakiendelea kuteseka.

Badala ya kuwakosoa na kutisha kuwafuta kazi, wizara inafaa kuwaomba msamaha kwa kukosa kutimiza takwa hili na kuwafanya wahangaike wakiugua.

Inasikitisha kuwa Bw Kagwe aliagiza serikali za kaunti kuwafuta kazi wahudumu wanaogoma ilhali anafahamu kwamba serikali hizo hazijapata pesa kutoka kwa serikali ya kitaifa kwa muda wa miezi mitatu sasa.

Hii inaonyesha kuwa serikali inakosa kutatua mzozo huo maksudi na kwa sababu inajua athari zake, inachotaka ni kuwatesa Wakenya wanaotegemea hospitali za umma kwa huduma za afya. Madaktari hawafai kulaumiwa kwa kugoma, ni serikali inayofaa kubeba lawama kwa kutojali maslahi ya raia wake.

Serikali yatisha kuwapiga kalamu madaktari wagonjwa wakizidi kuteseka

BENSON MATHEKA, DIANA MUTHEU, TITUS OMINDE na LEONARD ONYANGO

HUDUMA za matibabu ziliendelea kukwama katika hospitali za umma kote nchini jana, na kuacha wagonjwa wakizidi kutekesa, huku maafisa wa serikali na wahudumu wa afya wanaogoma wakilaumiana.

Maafisa wa Wizara ya Afya wanasisitiza kuwa madaktari hawafai kugoma, wakisema wametimiziwa matakwa yao. Kulingana na Waziri Mutahi Kagwe, madaktari wamelipwa mishahara yao na hawafai kuhadaa Wakenya.

Siku ya Jumatatu wakati wa mazishi ya Dkt Stephen Mogusu katika Kaunti ya Kisii, maafisa wa Chama cha Matabibu na Madaktari wa Meno (KMPDU) walisema baadhi ya madaktari hawajalipwa mishahara yao kwa miezi kadhaa.

Jana, hata hivyo, Bw Kagwe alisema ingawa mishahara ilicheleweshwa hakuna daktari anayedai malipo.

Waziri alisisitiza kuwa madaktari wanaogoma wanafaa kufutwa kazi, kauli ambayo magavana wanakubaliana nayo. “Hatuwezi kuacha wagonjwa wakiteseka,” akasema Bw Kagwe.

Miongoni mwa matakwa ya madaktari ni bima ya matibabu na maisha, vifaa vya kuwakinga dhidi ya maambukizi ya janga la Covid-19 wakiwa kazini na kupandishwa cheo.

Naibu Waziri wa Afya Dkt Mercy Mwangangi alisema matakwa saba kati ya tisa yametimizwa.“Kilichobaki na ambacho kinashughulikiwa ni marupurupu,” akaeleza.

Waziri Kagwe alifafanua kwamba kile madaktari wanataka ni kudumishwa kwa marupurupu ambayo walipewa wakati janga la Covid-19 lilipoanza.

Hata hivyo, wahudumu wa afya walilaumu serikali na magavana kwa kutojali maslahi yao. Jana, Gavana wa Kisumu Profesa Peter Nyong’o aliunga mkono kauli ya Waziri Kagwe kwamba madaktari waliolemaza huduma katika hospitali za umma watafutwa kazi.

Katika Kaunti ya Mombasa, wahudumu waliomlaumu Gavana Hassan Joho kwa kuwapuuza, huku wakisisitiza kuwa wataendelea na mgomo hadi watendewe haki.

Wakizungumza baada ya kuandamana hadi nje ya majengo ya ofisi za Bw Joho, wahudumu hao wa afya walimtaka gavana ashughulikie malalamishi yao haraka iwezekanavyo.

“Mara nyingi tumemuona gavana wetu akitilia maanani mambo ya siasa, lakini tunapokuwa na changamoto katika sekta ya afya huwa hajitokezi kwa mazungumzo,” alihoji Mwenyekiti wa Chama cha Wauguzi Nchini (KNUN), Bi Miriam Mbithe.

Kupitia kwa viongozi wao, wahudumu hao zaidi ya 850 walisema vitisho havitawazua kuendeleza mgomo wao kitaifa ulio katika wiki ya tatu.

“Hatuogopi kufutwa kazi. Zaidi, hatutaki kufanya kazi katika mazingira yanayohatarisha maisha yetu, na katika sekta inayopuuza malalamishi ya wafanyakazi wake,” akaeleza Katibu wa Chama cha Kutetea Haki za Matabibu (KUCO) Kaunti ya Mombasa, Bw Franklin Makanga.

Wahudumu wa afya 800 Uasin Gishu walilaumu serikali ya Gavana Jackson Mandago kwa kutowapandishwa vyeo kwa miaka zaidi ya kumi, licha yao kuhitimu.

Mwenyekiti wa KNUN tawi la Uasin Gishu, Bw Francis Chepkwony, alikanusha madai kwamba shughuli za kawaida za matibabu ziliendelea katika hospitali za kaunti hiyo

.“Wanaodanganya eti huduma za afya zinaendelea katika kaunti hii wanawakejeli wakazi maskini wanaotegemea vituo vya afya vya umma kwa matibabu,” akasema Bw Chepkwony.

Gavana Mandago ni mmoja wa magavana ambao wamewapuuza wafanyikazi wa afya kwa gharama ya shughuli ambazo haziongeza thamani kwa wakaazi wa kaunti hii,’ akaongeza.

Hofu ya maafa mgomo ukichacha

Na WAANDISHI WETU

MAAFA yanawakodolea macho wagonjwa nchini baada ya wahudumu wa afya wanaogoma kuacha hospitali na vituo vya afya vya umma vikiwa mahame.

Wagonjwa waliofika katika vituo hivyo kote nchini walisononeka kwa maumivu bila wa kuwahudumia huku walinzi wakiwaagiza kutafuta huduma katika hospitali za kibinafsi.

Madaktari walioanza mgomo jana, waliungana na wauguzi na matabibu kusema hakuna vitisho vinakavyowafanya kufuta mgomo huo kabla ya matakwa yao kutimizwa.

“Hakuna vitisho vitakavyofanya madaktari kurudi kazini. Maagizo ya mahakama hayatazuia madaktari kufariki au kuambukizwa maradhi,” alisema kaimu Katibu Mkuu wa chama cha Madaktari na wataalamu wa meno (KMPDU) Dkt Chibanzi Mwachonda alipozindua rasmi mgomo huo mjini Kisii.

Mnamo Jumamosi, waziri wa afya Mutahi Kagwe aliwalaumu wahudumu wa afya kwa kugoma licha ya mahakama kuharamisha mgomo wao na kuagiza serikali za kaunti kuwafuta kazi.

Dkt Mwachonda alitaja kauli hiyo kama vitisho na kuingiza siasa katika masuala ya afya.“Madaktari nchini Kenya hawawezi kusubiri, hawawezi kuendelea kuhudumu katika mazingira hatari,” alisema.

Katika hospitali ya rufaa ya Pwani, wagonjwa waliofika kutafuta huduma za dharura waliagizwa kwenda katika hospitali za kibinafsi, jambo ambalo ni mlima kwa Wakenya wengi wanaokabiliwa na hali ngumu ya maisha kutokana na athari za janga la corona.

Hali inatarajiwa kuwa mbaya zaidi huku maambukizi ya virusi vya corona yakiendelea kuongezeka nchini.Mkurugenzi wa huduma za uuguzi katika hospitali ya rufaa ya Pwani , Elizabeth Kivuva alidai wameajiri madaktari na wauguzi kwa kandarasi kusaidia kukabiliana na mzozo huo.

“Tunashughulikia wagonjwa wa corona pekee. Wengine wote wanahamishwa,” alisema.Katika kaunti ya Tana River, wagonjwa na akina mama wajawazito waliachwa katika wodi bila wahudumu wa kuwashughulikia.

Baadhi waliweka maisha yao hatarini kwa kutafuta huduma za wakunga wa kitamaduni kwa kukosa pesa za kwenda hospitali za kibinafsi.

“Nilikuja hapa na nikapata milango yote imefungwa, hakuna daktari au muuguzi hata mmoja,” alisema Mwanaharusi Jillo. Wagonjwa wa figo waliofika kusafishwa damu walisononeka wasijue pa kuelekea.

Katika kaunti ya Kilifi, hakuna hospitali ya umma iliyokuwa ikipokea wagonjwa. Baadhi ya walioonekana kupata nafuu waliruhusiwa kuondoka wodi hata kabla ya kupona.

Mwenyekiti wa tawi hilo la KMPDU, Dkt Sammy Kiptoo alisema kwamba, madaktari hawatarudi kazini matakwa yao yasipotimizwa.Huduma za afya katika kaunti ya Taita Taveta, pia zililemazwa huku maafisa wa chama hicho wakisema hawatarudi kazini.Hali ilikuwa sawa katika kaunti ya Lamu wagonjwa wakisononeka kwa kukosa huduma.

Wagonjwa wanaotafuta huduma za afya katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Uasin Gishu walitaabika wakitafuta matibabu bila wa kuwahudumia.

Mwanamke mwenye umri wa makamo ambaye alikuwa akitafuta huduma kujifungua mtoto alisema alielekezwa na walinzi kutafuta huduma kwingine.Doreen Rotich ambaye anatarajia mtoto wakati wowote aliomba magavana na serikali ya kitaifa kuingilia kati.

‘Nilikuja hapa mapema saa tatu asubuhi tangu wakati huo hakuna huduma ambazo nimepokea. Wafanyikazi wa pekee ambao tunakutana nao ni walinzi. Serikali zote za kitaifa na kaunti lazima zipate suluhisho la mgomo huu,”akasema Bi Rotich.

Mwenyekiti wa chama cha wauguzi kaunti ya Uasin Gishu, Francis Chekwony alisema hakuna huduma katika hospitali za kaunti.Hali ilikuwa sawa Elgeyo Marakwet ambapo zaidi ya wauguzi 600 na wahudumu wengine wa afya wamesusia kazi.

Katibu Mkuu wa tawi la kaunti hiyo la chama cha wauguzi, Benson Biwott alitaka viongozi wa kaunti hiyo kukoma kuwatishia wauguzi wanaogoma.

Ripoti za Ruth Mbula,Benson Matheka, Lucy Mkanyika, Maureen Ongalo, Kalume Kazungu, Stephen Oduor, Winnie Atieno, Titus Ominde

TAHARIRI: Mgomo wa maafisa wa afya utaleta maafa Krismasi

NA MHARIRI

IKIWA madaktari wataanza mgomo wao Jumatatu hii walivyotangaza, kuna hatari ya maafa makubwa kutokea Kenya wakati huu wa likizo ya Krismasi.

Hii ni kwa sababu sekta ya afya italemazwa kabisa kwa kuwa wahudumu wengine wa afya wanaendelea kugoma.

Madaktari wanagoma wiki mbili baada ya wauguzi na matibabu kugoma kumaanisha kuanzia leo hakutakuwa na huduma zozote katika hospitali za umma.

Kuna uwezekano hali hii huenda ikadumu kwa muda kufuatia kauli ya waziri wa afya Mutahi Kagwe kwamba wahudumu wote wa afya wanaogoma wanafaa kufutwa kazi na wengine kuajiriwa kuchukua nafasi zao.

Bila shaka, hii haitakuwa tiba kwa mzozo unaokumba sekta ya afya kwa sababu watakaoajiriwa, watajipata katika hali sawa na watangulizi wao na hali kujirudia.

Hii inavyofanyika, na ndivyo inavyotarajiwa, masikini wanaotegemea hospitali za umma kwa matibabu watakuwa katika hatari kubwa hasa wale wanaoambukizwa virusi vya corona.

Inasikitisha wanasiasa na maafisa wa serikali, baadhi yao madaktari waliohitimu, wanaweza kupuuza maslahi ya Wakenya wanaolipa ushuru wanaofurahia wanapoenda kutibiwa katika hospitali za kibinafsi ambao wengi hawawezi kumudu.

Inasikitisha badala ya kutoa mwelekeo unaoweza kupunguzia wagonjwa mateso, maafisa wa serikali wanatisha kuwafuta kazi. Kuna haja ya kutatua mzozo huu kwa njia ya mazungumzo na hii haiwezi kuafikiwa kupitia vitisho na misimamo mikali.

Maafisa wa serikali wanaelewa kwamba madaktari wameambukizwa corona na kufariki wakiwa kazini. Hawa ni wale ambao maafisa wa serikali walikuwa wakiwamiminia sifa na kuahidi kuwasaidia kukabiliana na virusi vya corona.

Je, ni nini kiligeuka ikafikia kutoka vitisho wahudumu wa afya wanapotaka wapatiwe vifaa bora vya kazi kuwakinga dhidi ya maambukizi wakiwa kazini?

Je, kuna njama ya kusababisha vifo vya halaiki kwa sababu ya Wakenya kukosa huduma za afya?

Serikali inataka Wakenya wangapi wakiwemo madaktari wafariki ili isikie kilio cha wahudumu wa afya? Kabla ya maswali haya kupata majibu huenda maafa makubwa yakatokea Kenya kwa sababu ya suala ambalo linahitaji nia njema kutatua.

 

Njoki Ndung’u alivyojitetea katika kesi ya kuongoza mgomo

Na RICHARD MUNGUTI

JAJI wa Mahakama ya Juu Njoki Ndung’u  amejitetea katika kesi anayoshtakiwa Mahakama Kuu ya kuchochea mgomo kufuatia agizo la kustaafishwa kwa majaji wawili na Tume ya kuajiri watumishi wa idara ya Mahakama (JSC) baada ya kuhitimu miaka 70 miaka mitano iliyopita.

Kufuatia uhaba huo ilimlazimu aliyekuwa Jaji Mkuu Dkt Willy Mutunga afanye kikao cha dharura cha JSC kilichohudhuriwa na Jaji Ndung’u na Jaji Jackon Ojwang kueleza malalamishi yao na uhaba wa majaji wa kufanyakazi mahakama hii ya upeo.

Jaji huyo alisema utata ulikumba idara ya mahakama baada ya kufahamika Jaji Mutunga alikuwa anatazamia kustaafu na aitha naibu wake Jaji Kalpana Rawal ama Jaji Philip Tunoi walioteuliwa chini ya katiba ya zamani wastaafu wakiwa miaka 74 angelichukua wadhifa wa CJ.

Katika kizaazaa hicho Jaji Ndung’u alisitisha hatua ya kumstaafisha Jaji Rawal na JSC.

Wakati huo Jaji Mutunga alimruhusu Jaji Rawal kuongoza kamati ya majaji wa Mahakama ya Juu waliokuwa wamenusa hali ya hatari kwa vile majaji watatu walikuwa wastaafu. Majaji hao ni Jaji Mutunga, Rawal na Tunoi.

“ Mahakama ya Juu ilikuwa isalie majaji wanne tu na hakungekuwa na kazi yoyote ambayo ingelifanyika,” alisema Jaji Ndung’u.

Ni katika hali hiyo yeye na Jaji Ojwang waliandikia JSC barua wakiishutumu kwa kutaka kumstaafisha Jaji Rawal ilhali miaka yake ya kustaafu ilikuwa 74 na wala sio 70.

Barua ya kumstaafisha ilikuwa imetiwa sahini na msajili wa idara ya mahakama Annah Amadi…

Jaji Mutunga na Jaji Smokin Wanjala walikuwa wanachama wa kamati ya JSC na waliitisha kikao cha dharura cha tume hiyo kikutane na Majaji Ndung’u na Ojwang wakabiliane nalo kwa vile suala la kustaafishwa kwa Jaji Rawal na Tunoi lilikuwa la dharura na la manufaa makubwa kwa umma.

“ Hakukuwa na majaji wa kutosha wa kusikiza kesi katika mahakama ya juu,” Jaji Ndung’u alimweleza Jaji Weldon Korir anayesikiza ya kushtakiwa kwa jaji huyo mbele ya JSC na wakili Apollo Mboya.

Baada ya kikao cha pamoja JSC na Majaji Ndung’u na Ojwang anayestaafu mwezi huu (Februari 2020) walishtakiwa na aliyekuwa afisa mkuu wa chama cha mawakili nchini LSK Apollo Mboya akiomba Rais Uhuru Kenyatta ateue jopo la kuwachunguza majaji hao wawili kwa lengo la kuwatimua kazini.

Jaji Ndung’u alisema kulikuwa na uhaba wa majaji katika mahakama hii ya upeo “hata ikambidi asiende likizo ya kujifungua.”

Jaji huyo alisema hali ya suinto fahamu ilikuwa nyingi hata inadaiwa wawili hao walimshawishi jaji mwingine ajiunge nao kususia kazi.

Kesi yao ilisikizwa na JSC na wakakemewa wote wawili (Njoki na Ojwang).

Njoki anaomba uamuzi huo wa JSC wa kumshutumu ufutiliwe mbali.

Lakini wawili hao walidumisha msimamo wao wa kupinga kustaafishwa kwa wenzao kwa mujibu wa barua waliyoandika na kumshutumu Jaji Mutunga.

“Barua ya arifa ya kustaafishwa kwa aliyekuwa naibu wa Jaji Mkuu (DCJ) Kalpana Rawal na Jaji Philip Tunoi waliokuwa wamehitimu miaka 70 ilizuia hali ya suinto fahamu katika Mahakama ya Upeo,” alisema Jaji Ndung’u.

Jaji huyo aliyetoa ushahidi mbele ya Jaji Weldon Korir alisema kutokana na uhaba wa majaji katika mahakama hiyo ya upeo , ilimbidi aiandikie barabara JSC kuhoji suala hilo.

“Miktano baina ya Majaji wa Mahakama ya Juu (CJ) Dkt Mutunga, Jaji Rawal, Jaji Tunoi, Jaji Mohammed Ibrahim , Jaji Ojwang, Jaji Smokin Wanjala na Jaji Ndung’u ilifanywa mara kwa mara kujadilia uhaba wa majaji na utenda kazi katika mahakama hii ya upezo,” Jaji Korir alifafamishwa.

Wakati wa mikutano hiyo suala nyeti lililozuka na kustaafishwa kwa Majaji Rawal na Tunoi.

Wawili hawa walikuwa wamepinga kustaafishwa wakisema “ waliteuliwa kwa mujibu wa katiba ya zamani iliyokuwa inasema majaji watastaafu wakihitimu umri wa miaka 74.”

Majaji Ndung’u , Ojwang walilalamikia kuhusu utenda kazi ikitiliwa maanani ni majaji aidha watano ama sita wanaoweza kuendeleza kesi.

Wakati wa mikutano iliyofanywa , yeye (Njoki) alinunukuu masuala yaliyojadiliwa na mara kwa mara ubishi ulizuka kuhusu uhalali wa masuala yaliyojadiliwa.

“Licha Jaji Mutunga kumtea Jaji Rawal aongoze vikao na kumwarifu baada kilichoafikianwa,” alisema Jaji Ndung’u.

Jaji Ndung’u alikuwa akitoa ushahidi katika waliyoshtakiwa na aliyekuwa afisa mkuu katika chama cha wanasheria nchini Apollo Mboya aliyewashtaki kwa JSC na kuiomba impendekezee Rais Uhuru Kenyatta ateue jopo la kuwachunguza Majaji Ndung’u na Ojwang kuchochea mgomo baridi katika mahakama ya juu.

Hatimaye Majaji Rawal na Tunoi waling’atuliwa baada ya Mahakama ya Juu ikiongozwa na Jaji Mutunga kuamua umri wa kustaafu kwa majaji wa Mahakama ni miaka 70 kwa mujibu wa Katiba iliyopitishwa 2010.

Awali majaji hawa wawili waliwasilisha kesi mahakama kuu kuamua umri wa kustaafu.

Kesi hiyo ilisikizwa na mahakama kuu , mahakama ya rufaa na Mahakama ya Juu ambayo ilifikia uamuzi umri wa kustaafu ni miaka 70 na wala sio 74.

“Ijapokuwa kesi hii ilikuwa inaendelea mbele ya mahakama kuu na rufaa majaji wa mahakama ya juu walikutana kujadilia suala hilo la kustaafishwa kwa majaji wawili chini ya uenyekiti wa Jaji Mutunga na Jaji Rawal mtawalia,” alisema Jaji Ndung’u

Kabla ya mahakama ya juu kuamua Jaji Tunoi ang’atuke kulitokea mlalamishi aliyedai jaji huyo aliyekuwa na tajriba ya juu alikuwa ameumishwa mlungula wa Sh200milioni na Gavana Evans Kidero awashawishi majaji wengine wa mahakama ya juu kutupilia mbali kesi aliyokuwa ameshtakiwa na aliyekuwa Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu.

Mwaka wa 2013 Bw Waititu alikuwa amewania Ugavana Nairobi na kunyoroshwa na Dkt Kidero.

Waititu alihama Nairobi wakati huo na kuwania Ubunge wa Kabete baada ya kuuawa kwa aliyekuwa Mbunge George Muchai 2015.

Kashfa hiyo ya Jaji Tunoi ya ulaji rushwa ilimtoa pumzi hata akaamua kustaafu kabla ya Jaji Mutunga , Jaji Smokin Wanjala na Jaji Mohamed Ibrahim,

Majaji Ndung’u na Ojwang walitofautiana na uamuzi wa Majaji Mutunga, Wanjala na Ibrahim.

Ni kufuatia mtafaruku huu Bw Mboya aliomba JSC impendekezee Rais Uhuru Kenyatta ateue jopo la kuwatimua kazini majaji hao wawili Ndung’u na Ojwang kwa kuchochea mgomo wa mahakama ya juu.

Badala ya kupendekeza wachunguzwe JSC iliwashutumu na ni uamuzi huu Jaji Ndung’u anaomba upigwe kalamu na Jaji Korir.

Kesi inaendelea Jumanne.

Mgomo sasa watatiza huduma nyingi kaunti

Na BONIFACE MWANIKI

HUDUMA za serikali zimekwama katika Kaunti ya Kitui kufuatia mgomo wa wafanyakazi katika idara tofauti za kaunti hiyo.

Wafanyakazi hao wanalalamikia kuchelewa kulipwa mishahara yao ya mwezi Julai.

Hii si mara ya kwanza kwa kaunti ya Kitui kukumbwa na masaibu ya aina hii, kwani mwezi uliopita wa Julai, wafanyakazi hao walikuwa kwenye mgomo kufuatia kuchelewa kwa mishahara yao.

Kufuatia kuchelewa kwa mishahara yao mwezi huu, wafanyakazi hao wamekuwa wakisusia kazi kuanzia mwanzoni mwa wiki hii, na mnamo Jumanne walisitisha kabisa huduma zao, huku wagonjwa waliolazwa katika hospitali za serikali wakiachwa hoi.

Shughuli za kawaida katika hospitali za Kitui zimesimama kabisa na Katibu Mkuu wa chama cha wafanyakazi katika kaunti ya Kitui, Bw Benjamin Munyalo, amewashauri wakazi waondoe wagonjwa wao kutoka hospitali za kaunti.

“Hakutakuwa na madaktari wa kuwahudumia hadi pale ambapo kaunti itawalipa wahudumu mishahara yao. Tunaomba kila aliye na mgonjwa wake amchukue na kutafuta tiba kwingine,” akasema Bw Munyalo.

Wafanyakazi kutoka idara tofauti za kaunti hiyo waliandamana hadi kwenye ofisi za Gavana Charity Ngilu wakitaka kujua uhakika wa mishahara yao ya Julai.

Baada ya kukosa nafasi ya kuzungumza na Bi Ngilu, wafanyakazi hao waliwataka wenzao wote kususia kazi na kuwasishi wauguzi waliobaki hospitalini kushughulikia huduma za dharura pia kuondoka.

“Hatuwezi kufanya kazi bila malipo kwani hata pia sisi tuna mahitaji yanayohitaji pesa. Ingekuwa heri serikali ya kitaifa ianze kushughulikia malipo ya wafanyikazi wa kaunti kwani magavana wamedhihirisha wazi kuwa hawawezi kulipa wafanyakazi wao kwa wakati unaofaa,” alisema Bw Munyalo.

Akizungumza kwa niama ya wafanyakazi wenzake, alisisitiza kuwa inampasa gavana Ngilu atafute mbinu mbadala za kuwalipa wafanyakazi wa Kitui kama vile kutumia ushuru unaokusanywa, jinsi inavyofanyika katika baadhi ya kaunti nchini.

“Tunaomba gavana wetu aige mfano wa kaunti ambazo zimewalipa wafanyakazi wao, badala ya kutumia kutoelewana baina ya bunge la kitaifa na lile la seneti kutugandamiza,” aliongeza katibu huyu mkuu.

Wagonjwa waumia

Nao wagonjwa katika hospitali tofauti katika kaunti hiyo, wameendelea kuumia kufuatia mgomo huo.

Shughuli za ukusanyaji ushuru katika maeneo tofauti haswa kwenye vituo vya mabasi pia zimesitishwa kutokana na mgomo huo wa wafanyakazi.

Bi Mary Ngava ambaye ni mmoja wa wagonjwa katika hospitali kuu ya kaunti hiyo mjini Kitui, alimsihi gavana wa kaunti hiyo kutafuta mwafaka baina yake na wafanyakazi, kwani wagonjwa wataendelea kuumia kwani wengi wao hawana fedha za kutafuta matibabu kwenye hospitali za kibinafsi.

“Wagonjwa wengi wanaotafuta matibabu katika hospitali za umma ni maskini, hivyo hawawezi kugharamia matibabu yao katika hospitali za kibinafsi; Iwapo huu mgomo hautasitishwa tutateseka sana,” alieleza.

Bw James Muturi ambaye mkewe pia amelazwa alieleza kuwa hana fedha za kumhamishia kwingine.

Serikali ilivyochezea wauguzi

Na BENSON MATHEKA

MGOMO wa wauguzi ulianza kufifia Alhamisi baada ya kuibuka kuwa walidanganywa kwenye mkataba wa pamoja waliotia sahihi na Serikali na Baraza la Magavana (CoG) mnamo 2017.

Hii ni baada ya Serikali kusema kuwa hata kaunti nne ambazo zimetekeleza mkataba huo zimefanya hivyo kinyume cha sheria, na hivyo zinapasa kusimamisha malipo hayo mara moja, na kurudisha fedha zote ambazo tayari zimewalipa wauguzi wao.

Matukio haya yanaonyesha kuwa Serikali na CoG walitumia hila na udanganyifu dhidi ya wauguzi.

Alhamisi, wauguzi katika kaunti za Bomet na Kakamega walirejea kazini baada ya serikali kusisitiza kwamba haina pesa za kuwalipa marupurupu waliyodai.

Cha kutamausha zaidi ni agizo la Mwelekezi wa Bajeti, Agnes Odhiambo ambaye amesema hatua ya kaunti nne kutekeleza mkataba wa 2017 ni kinyume cha sheria, kwa sababu marupurupu hayo hayakuidhinishwa na Tume ya Mishahara ya Watumishi wa Umma (SRC).

Hii inaonyesha kuwa Serikali ilifahamu kuwa mkataba huo ulikuwa feki kwa vile ilipoweka sahihi ilifaa kwanza kupata ushauri wa SRC.

Kwenye barua aliyoandikia kaunti za Migori, Machakos, Mombasa na Kwale, Bi Odhiambo anasema wauguzi hawafai kulipwa marupurupu ambayo hayajaidhinishwa na SRC.

“Ofisi yangu ina habari kwamba baadhi ya kaunti zinalipa wauguzi marupurupu kinyume cha yale yaliyoidhinishwa na SRC. Kulipa marupurupu bila idhini ya SRC ni kinyume cha sheria,” alionya Bi Odhiambo.

Mwenyekiti wa SRC, Lyn Mengich kwa upande wake anasema serikali za kaunti zinahitaji Sh3.5 bilioni kila mwaka kuwalipa wauguzi marupurupu wanayodai lakini pesa hizo hazipo.

Walipotangaza mgomo na kutaka CoG kusaidia kuhakikisha serikali za kaunti zimeheshimu mkataba huo, baraza hilo liliwakana wauguzi likisema wameajiriwa na kaunti husika na hivyo haliwezi kuingilia.

‘Hakuna pesa’

Rais Uhuru Kenyatta na mwenyekiti wa sasa wa COG Wycliffe Oparanya pia wanasisitiza kuwa serikali haina pesa za kulipa marupurupu hayo.

Hata hivyo Bw Panyako anapuuza kauli yao na ya Bi Odhiambo akisema hafai kuelekeza serikali za kaunti zinavyopaswa kuhudumu.

Ni chama chake pekee kinachorejelea mkataba wa 2017 ambao anasisitiza ni lazima utekelezwe kabla ya wauguzi kurejea kazini. Serikali na CoG hazionekani kuutambua.

“Kwa nini kila mtu anataka kuzungumzia mgomo wa wauguzi. Tulitia sahihi mkataba na serikali za kaunti na unafaa kutimizwa. Hatutaki kujua utatimizwa lini lakini ni lazima utimizwe. Tutapiganie haki za wauguzi wetu,” alisema.

Bw Panyako na maafisa wengine wa chama hicho, wameitwa kufika mbele ya mahakama kueleza kwa nini wasiadhibiwe kwa kukaidi agizo la kusitisha mgomo huo.

Wauguzi katika kaunti saba nao wajiunga na wenzao wanaogoma

Na WAANDISHI WETU

WAUGUZI katika kaunti zingine saba wamejiunga na mgomo wa kitaifa ambao umeingia wiki ya tatu sasa, huku kaunti kadha zikiamua kuajiri wauguzi kwa mkataba ili kukwepa migomo siku zijazo.

Wauguzi katika kaunti za Tana River, Narok, Nakuru, Siaya, Kakamega, Bomet na Busia walianza mgomo Jumatano baada ya makataa waliyotoa kwa serikali za kaunti zao kufikia kikomo.

Wenzao katika kaunti ya Uasin Gishu walitarajiwa kususia kazi kuanzia leo Jumanne.

Tayari wauguzi wa Pokot Magharibi, Kisumu, Kisii, Wajir, Taita Taveta, Trans-Nzoia, Homa Bay, Garissa, Samburu, na Marsabit wanaendelea na mgomo huo wa kitaifa ulioanza Jumatatu, Februari 04.

Wahudumu hao wa afya wameapa kutorudi kazini hadi matakwa yao yatimizwe, licha ya agizo la Rais Uhuru Kenyatta kuwaonya dhidi ya hatua hiyo.

Waziri mkuu wa zamani Raila Odinga akiwa mjini Busia Jumamosi pia aliwaomba wauguzi kurudi kazini kwa maslahi ya wagonjwa.

Wauguzi wanasisitiza Mkataba wa Malipo (CBA) baina yao na serikali kuu na za kaunti utekelezwe kikamilifu.

Mkataba huo uliotiwa saini Novemba 2017 na Muungano wa Kitaifa wa Wauguzi (KNUN) unahusu marupurupu ya kazi ya ziada na sare.

Marupurupu ya kazi yalifaa kuongezwa kutoka Sh 20,000 hadi Sh30,000 kila mwezi katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia 2017.

Nayo marupurupu ya sare yalistahili kuongezwa kutoka Sh10,000 hadi Sh30,000 kila mwaka.

Serikali ya Kaunti ya Murang’a jana ilitangaza kuajiri wauguzi 100 kwa mkataba kama njia ya kukwepa migomo siku zijazo.

Wauguzi hao waliajiriwa chini ya mpango wa Tiba Mashinani; mkataba wao utadumu kwa miaka mitano.

Akizungumza kwenye hafla ya kutiwa saini kwa mikataba hiyo katika uwanja wa Uhura, Gavana Mwangi Wa Iria alisema mtindo huo unanuia kukomesha tabia ya “muungano wa wauguzi kushika mateka taifa ili kudai nyongeza ya mshahara.”

“Katika kaunti hii wauguzi wataajiriwa kwa mkataba ili yeyote akiukiuka anafutwa kazi na nafasi yake kujazwa mara moja!” alieleza na kushukuru wauguzi katika kaunti yake kwa kukosa kujiunga na mgomo wao wa kitaifa.

Gavana Iria aliongeza kuwa watajadiliana na wauguzi wengine 100 ili kuwaajiri katika wiki mbili zijazo.

Kaunti ya Kisumu pia iliajiri wauguzi kadha kwa mkataba kazi wiki jana hususan kusaidia katika idara zilizoathiriwa zaidi na mgomo. Idara hizo katika Hospitali ya Kaunti ya Kisumu ni thieta, wadi ya akina mama kujifungua, kliniki ya watoto na utoaji chanjo.

Kufikia Jumanne, wauguzi 137 wanachama wa KNUN walikuwa wamerejea kazini huku 686 wakiwa bado katika mgomo.

Wauguzi wengine ambao wamerejea kazini ni wale wa Kaunti ya Kisii waliositisha mgomo wao Jumatatu jioni.

Baadhi ya waliorejea kazini awali ni wa Elgeyo Marakwet, Nyeri, Kirinyaga na Embu.

Katika hospitali ya akina mama kujifungua ya Pumwani, Nairobi, wauguzi wote wanachama wa KNUN walirudi kazini huku wale ambao ni wanachama wa Muungano wa Wafanyakazi wa Kaunti (CWU) bado wamesusia kazi.

TAARIFA za Stephen Oduor, Jadson Gichana, Gaitano Pessa, Ndungu Gachane na Francis Mureithi.

Imekusanywa na Carolyne Agosa

Mgomo wa walimu wazimwa

Na RICHARD MUNGUTI

MGOMO wa walimu uliotisha kusambaratisha ufunguzi wa shule zaidi ya 20,000 kote nchini ulifutiliwa mbali Jumatano na mahakama ya kuamua mizozo ya wafanyakazi na waajiri (ELRC).

Katika uamuzi wa kihistoria Jaji Byram Ongaya alisema haki za watoto ni jambo linalopasa kushughulikiwa na kila mmoja na kuamuru walimu walimu wafike shuleni asubuhi kuanza mughula wa kwanza 2019.

Agizo la mgomo ulioitishwa Desemba 2018 baada ya kukwama mashauri ya kuangazia masuala tata kuhusu kuhamishwa kwa walimu , kupandishwa vyeo, kujiendeleza kimasomo kwa walimu na kusambaratishwa shughuli za KNUT lilisitishwa.

Lakini Jaji Ongaya aliamuru kinara wa TSC Nancy Macharia na katibu mkuu wa KNUT Wilson Sossion wafike katika afisi ya Leba Alhamisi saa tatu kuendelea na mazugumzo ya kutatua mzozo kuhusu mishahara ya walimu na kuhakimishwa kwa walimu.

Mashauri ya kuboresha maslaha ya walimu yalikwama Oktoba 2018 wakati Bi Macharia alipoomba mashauri yahairishwe kuwezesha mitihani ya kitaifa kuendelea.

Jaji Byram Ongaya. Picha/ Richard Munguti

Jaji Ongaya alisema kutokana na mawasilisho ya mawakili wa Knut , Mabw Paul Muite, John Mbaluto na Hilary  Sigei, ni wazi TSC ndiyo imekwamisha mazugumzo na kupelekea KNUT kuitisha mgomo ambao ungeliathiri elimu ya wanafunzi 12,000,000 kote nchini.

Katika uamuzi ambao uliangazia pande zote Jaji Ongaya aliamuru TSC ifutilie mbali barua za kuwahamisha wanachama wa KNUT waliokuwa wamepelekwa nje ya maeneo wanayowakilisha.

Bw Mbaluto alisema kuwa matawi 10 ya KNUT yalikuwa yameathiriwa.

Jaji huyo alisema mawakili wa KNUT walisema walimu zaidi ya 40 kutoka kaunti ya Nairobi walikuwa wameathiriwa na agizo hilo la TSC.

Jaji Ongaya aliamuru tume ya kuajiri walimu (TSC) isikize  malalamishi ya walimu wakuu 3,094 waliohamishwa Desemba 14, 2018 kabla ya Feburuari 15 2019.

Jaji huyo alisema TSC imekuwa ikifanya mambo kiholela katika usimamizi na kuitaka ifuate muwafaka wa makubaliano kuhusu mishahara na maslahi ya walimu (CBA).

“ Hii mahakama imetilia maanani ushahidi na mawasilisho yote ya KNUT , TSC na Mwanasheria mkuu na kufikia uamuzi kuwa lazima haki za wanafunzi zitiliwe maanani,” alisema Jaji Ongaya.

Mahakama ilikiamuru KNUT isitekeleze vitisho vya kuwataka walimu wagome na “ kwamba wanafunzi wanataka kufika shuleni na kuwapata walimu wawapokee.”

Jaji alisema elimu ya watoto imepewa kipau mbele katika katiba na lazima kila anayejali maslaha ya watoto azingatie kwa ukamilifu haki hiyo.

Mahakama hiyo ya leba ilisema kwamba masuala ambayo walimu wanataka watimiziwe yanaweza kushughulikiwa kupitia majadiliano na ikaagiza pande zote kuendelea na juhudi za upatanishi zinazosimamiwa na kamati iliyoteuliwa na Wizara ya Leba.

Jaribio la walimu, kupitia wakili Paul Muite la kutaka shule kufunguliwa Januari 7, 2019 badala ya Alhamisi lilikataliwa mahakama iliposema ombi lake halikuwa mojawapo ya masuala makuu katika kesi.

Katibu mkuu wa KNUT Wilson Sossion wakati wa kesi. Picha/ Richard Munguti

Bw Muite aliwasilisha ombi baada ya Knut kuagizwa kufutilia mbali mgomo akisema chama kilihitaji muda wa kuwasiliana na wanachama kote nchini.

Hata hivyo, ilikuwa ni ushindi kwa walimu, mahakama ilipositisha uhamisho wa walimu zaidi ya 3094 na kuagiza TSC kuchunguza maombi ya wale waliokuwa tayari wamehamishwa. Mahakama iliagiza kesi hiyo kutajwa Januari 17 ili pande zote kueleza mahakama juhudi za upatanishi zitapokuwa zimefikia.

Mawakili wa TSC Mabw Calvin Ayuor na Timon Oyucho walipinga ombi hilo la kuahirishwa kwa tarehe ya kufunguliwa kutoka  Januari 3 hadi 7, 2019.

“Suala hili halikuwa katika masuala nyeti ambayo KNUT ilikuwa inalalamikia na hivyo shule zitafunguliwa jinsi ilivyokuwa imepangwa Januari 3, 2019,” Jaji Ongaya aliamuru.

Awali, walimu walikuwa wameomba mahakama kufutilia mbali agizo la kuharamisha mgomo ikidai TSC haikuwa na nia ya upatanishi baada ya kususia kikao cha Jumanne.

Mnamo Jumanne, Katibu Mkuu wa chama cha Walimu (Knut) Wilson Sossion alikuwa ameagiza walimu kutofika shuleni zikifunguliwa leo baada ya TSC kususia kikao cha upatanishi.

Alhamisi Bw Sossion alisema Knut itatii agizo la mahakama na akawaagiza walimu kufika kazini kuanza mughula kama ilivyokuwa imeratibiwa.

Knut iliitisha mgomo ikitaka TSC kubatilisha uamuzi wa kuhamisha walimu zaidi ya 3,094 kutoka kaunti wanazotoka na TSC ikaenda mahakamani na kupata agizo kuzuia walimu kugoma.

Lakini Bw Sossion aliagiza walimu kutofika shuleni TSC isipotimiza matakwa yao.

Alisema walimu wangefika mbele ya kamati ya upatanishi iliyoteuliwa na waziri wa Leba Ukur Yattani.

Hata hivyo, mnamo Jumatatu kikao hicho kilitibuka na Knut ikalaumu TSC kwa kutumia mahakama kuhangaisha walimu. Jana, mahakama iliamuru TSC kubatilisha uhamisho wa maafisa wa Knut kutoka matawi kumi waliyochaguliwa kuhudumu. Waziri wa Elimu, Amina Mohammed aliunga TSC na kusema kwamba shule zitafunguliwa leo.

“Tangazo lililotolewa Desemba mwaka jana linadumu. Shule zitafunguliwa kesho (leo) licha ya vitisho vyovyote (vya walimu kugoma) vilivyotolewa,” alisema Bi Mohammed akihutubia wanahabari katika Taasisi ya Ukuzaji wa Mitaala nchini (KICD).

Kutoka kulia: Wakili wa TSC Calvin Ayuor (aliyesimamaa) na mawakili wa KNUT Hilary Sigei , Paul Muite na John Mbaluto (kushoto) wakiwa kortini Jumatano. Picha/ Richard Munguti

Mnamo Desemba, Bi Mohammed alitangaza kuwa shule zitafunguliwa leo badala ya jana (Jumatano) ilivyotangazwa awali.

Awali, Bi Mohammed aliyeandamana na Katibu wa Elimu, Belio Kipsang alisema wizara iliunga msimamo wa TSC kwamba walimu wafike shuleni leo. Hata hivyo, muda mfupi baada ya tangazo lake, Jaji Byram Ongaya aliagiza walimu kusitisha mgomo wao na akaitaka TSC kutowahamisha walimu ambao ni maafisa wa Knut kutoka maeneo waliyochaguliwa.

Kuamuliwa kwa kesi hiyo kulikuwa afueni  kwa walimu kwa vile Jaji Ongaya aliamuru TSC ifuate muwafaka wa CBA uliotiwa saini 2017.

Arifa iliyotumiwa na TSC kuingilia utenda kazi wa walimu ya Mei 2018 ilisitishwa.

Kusitishwa kwa arifa hiyo kumelemaza nguvu za TSC iliyokuwa imejitwika kuchukua hatua bila ya kuishirikisha TSC.

Jaji huyo alisema TSC imekuwa ikihepa majukumu yake kwa kutohudhuria vikao vya masikizano.

Mahakama iliamuru TSC ikome kukwepa majukumu yake kwa vile KNUT imekuwa ikihudhuria vikao vyote katika sehemu ya Naivasha.

Mahakama ilifahamishwa kuwa tangu  Feburari 2018 TSC imekuwa ikiepuka majadiliano hayo yanayoshirikisha wizara ya leba.

2019: Mgomo kuanza Alhamisi huku Knut ikikaza kamba

Na CHARLES WASONGA

NI rasmi sasa kwamba shughuli za masomo katika shule zote za umma nchini zitatatizika kuanzia Alhamisi wiki hii shule zitakapofunguliwa kwa muhula wa kwanza mwaka huu.

Hii ni baada Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Nchini (Knut) Wilson Sossion kushikilia kuwa mgomo huo utaendelea ulivyopangwa baada mkutano wa kupatanisha chama hicho na Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) kufeli kughulikia malalamishi manne makuu ya walimu.

Kwenye barua kwa wenyeviti na waweka hazina wa matawi yote ya Knut nchini, Bw Sossion jana aliwataka viongozi hao kuhakikisha kuwa mgomo huo unaanza siku ya kwanza ya kufunguliwa kwa shule.

“Barua hii inalenga kujulisha kila mwanachama kwamba mgomo unaanza tarehe ya kwanza ya muhula wa kwanza. Walimu wote wasiripoti shuleni kwa muhula wa kwanza hadi mgomo utakapofutiliwa mbali rasmi na Katibu Mkuu kupitia uamuzi wa Baraza Kuu la Kitaifa (NEC) kwa mujibu wa Katiba yetu,” Bw Sossion akasema.

Akaongeza: “Tafadhali wafahamisheni walimu wote katika matawi yenu yote kuhusu mgomo huu kwa sababu ni wajibu wao kuungana kupigania masihali yao kama walimu wa taifa hili.”

Bw Sossion alitaja uhamisho wa walimu, kandarasi ya utendakazi, kupandishwa vyeo kwa walimu na mafunzo ya ziada ya walimu kama masuala makuu ambayo Knut inataka TSC ishughulikie kwa njia “itakayowaridhisha walimu” ndiposa walikubali kufutilia mbali mgomo.

Knut inaitaka TSC kufutilia mbali uhamisho wa zaidi ya walimu wakuu 3,000 iliutekeleza mwanzoni mwa mwezi jana pamoja na kuwapandisha vyeo walimu 30,000. Vile vile, walimu wanataka kusitishwa kwa sera ya utathmini wa utendakazi wa walimu ulioanza kutekelezwa mwaka jana na walimu wapewa nafasi ya kujiongeza kimasomo.

“Hatutarejea kazini hadi pale masuala haya yote yatakapotatuliwa. Tunawaomba walimu wote kushiriki mgomo huu wa kihistoria kama njia ya kutetea haki yetu,” akasisitiza Bw Sossion huku akishikilia kuwa mgomo huo ni halali kisheria na kikatiba.

Mnamo Jumamosi mkutano kati ya Knut na kamati ya upatanisho iliyobuniwa na Wizara ya Leba ilifeli kuzaa matunda.

Baada na mkutano huo ulioandaliwa katika makao makuu wa Knut, Nairobi, Bw Sossion alisema kuwa maelewano yalikosa kuafikiwa kwa sababu ya “ukosefu wa nia njema kutoka kwa TSC”.

“Kwa sababu TSC ilishikilia mpango wake wa awali wa kutekeleza uhamisho wa walimu, mwafaka hautapatikana,” akasema Bw Sossion ambaye pia ni Mbunge Maalum wa chama cha ODM.

Leo maafisa wa Wizara ya Leba, wakiongozwa na Waziri Ukur Yattani wanapangiwa kufanya mkutano mwingine na viongozi wa Knut katika jaribio la kuzuia mgomo huo ambao utawaathiri zaidi ya wanafunzi milioni nne. Hata hivyo, kufikia jana jioni kufanyika kwa mkutano huo hakukuwa kumethibitishwa.

Iwapo mgomo huo utafanyika, utawatatiza wazazi na wanafunzi ambao wamekuwa wakifanya maandalizi ya kuanza kwa muhula wa kwanza kuanzia Januari 3. Wanafunzi wa kidato cha kwanza wanaotarajiwa kuripoti shuleni kuanzia Januari 7 pia wataathirika.

Utata shuleni muhula ukianza

Na BENSON MATHEKA

SHULE zinatarajiwa kufunguliwa kuanzia Alhamisi wiki hii huku kukiwa na utata kuhusu masuala kadhaa ambayo huenda yakaathiri masomo.

Walimu wametishIa kugoma na kususia utekelezaji wa mtaala mpya wa elimu ambao serikali inasema ni lazima uanze kutumika mwaka huu. Walimu wanasema mtaala wa 2-6-6-3 unahitaji kupigwa msasa kwanza kabla ya kuanza kutekelezwa.

Masomo yanaweza kuathiriwa iwapo walimu watagoma serikali isipobatilisha uhamisho wa walimu, kuwapandisha vyeo na kukubali matakwa yao ya kuendelea kujiimarisha kikazi. Kwenye ilani kwa walimu jana, Katibu Mkuu wa Chama cha Kitaifa cha Walimu (KNUT) Bw Wilson Sossion alisema:

“Mnafahamishwa kwamba mgomo utaanza tarehe ya kufunguliwa kwa shule na hakuna mwalimu anayepaswa kuripoti kazini hadi mgomo utakapofutiliwa mbali na katibu mkuu kufuatia azimio na Baraza Kuu la chama.”

Kulingana na walimu, itakuwa vigumu kutekeleza mtaala huo kukiwa na mapengo yaliyotajwa na wataalamu walioutathmini. Waziri wa Elimu, Amina Mohammed, anasisitiza kuwa mtaala huo utaanzwa kutekelezwa kwa awamu shule zikifunguliwa Alhamisi ilivyokuwa imepanga serikali.

Bi Mohammed alikuwa ametilia shaka utekelezaji wa mtaala huo kuanzia mwaka ujao hadi utakapopigwa msasa kabla ya kubadilisha msimamo na kutangaza kwamba lazima utatekelezwa.

Kulingana na waziri, alishauriana na wadau katika sekta ya elimu yakiwemo mashirika ya kidini, Taasisi ya ukuzaji wa mitaala (KICD), Tume ya Walimu (TSC), Baraza la Kitaifa ya Mitihani (KNEC) na Wachapishaji wa vitabu nchini (KPA).

Hata hivyo, kulingana na Bw Sossion, walimu ambao wanapaswa kufanikisha utekelezaji wa mtaala huo hawakushauriwa. “Ni makosa kulazimisha mtaala huu wakati ambao tumefahamishwa udhaifu wake. Tunahitaji kuupiga msasa kwanza, pengine mwaka ujao, kabla ya kuanza kuutekekeza kitaifa,” alisema Bw Sossion.

Mnamo Oktoba, KICD ilitoa ripoti kuonyesha kuwa walimu hawajaandaliwa vyema kufanikisha mtaala huo.

Ripoti hiyo ilisema kwamba baadhi ya walimu hawana uwezo unaohitajika kufanikisha mtaala huo mpya na shule nyingi hazina vifaa vinavyohitajika kuutekeleza. Wazazi wengi wanasema siku tatu kabla ya shule kufunguliwa kwa muhula wa kwanza wa mwaka, hawajui vitabu ambavyo watanunua.

Aidha, wanalalamikia tarehe ya kufungua shule za msingi wakisema inakaribiana na ya kuripoti kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza ambayo ni wiki ijayo.

Kulingana na wazazi, muhula unaanza punde tu baada ya msimu wa sherehe ambapo kuna matatizo ya usafiri. Baadhi ya walimu wanasema hawakuweza kuwapa wazazi orodha ya vitabu vya kununua kufuatia utata uliogubika utekelezaji wa mtaala huo.

Akihojiwa na wanahabari mjini Mombasa Alhamisi wiki jana, Rais Uhuru Kenyatta alikiri kwamba serikali imekuwa ikikanganya Wakenya kuhusu utekelezaji wa mtaala huo na akaomba msamaha.

2018: Mgomo wa siku 76 ulisambaratisha masomo ya wanafunzi 600,000

Na WANDERI KAMAU

MWAKA huu utakuwa kama kumbukumbu kuu katika vyuo vikuu nchini, baada ya wahadhiri kushiriki katika mgomo uliodumu kwa siku 76.

Mgomo huo ulihusu utata wa kuongezwa mishahara kwa wahadhiri kwenye Mwafaka wa Malipo wa 2017-2021.

Muungano wa Wafanyakazi wa Vyuo Vikuu (UASU) uliamua kumaliza mgomo huo mnamo Machi 17 baada ya mazungumzo yaliyojiri kwa muda mrefu na Wizara ya Leba katika makao yake makuu. Mazungumzo hayo yaliongozwa na Bi Hellen Apiyo, aliyeteuliwa kuwa mpatanishi wa pande hizo mbili.

Wahadhiri walianza mgomo huo mnamo Desemba 2017 kwa kukataa Sh3.6 bilioni zilizotolewa na serikali kama sehemu ya Sh10 bilioni, walizotaka kuongeza mishahara yao. Wahadhiri walikuwa wakishinikiza nyongeza ya mishahara yao hadi asilimia 60. Hilo lilimaanisha kwamba mhadhiri angepata mshahara wa hadi Sh800,000 huku wa kiwango cha chini zaidi akipata Sh263,000.

Mgomo huo uliwaathiri zaidi ya wanafunzi 600,000 ambao wamo katika vyuo vikuu 31 vya umma.

Katibu Mkuu wa UASU Constantine Wasonga alisema kwamba walimaliza mgomo huo ili kutoa muda zaidi kwa mazungumzo.

Vile vile, waliamua hilo kwa kujali maslahi ya maelfu ya wanafunzi ambao walikuwa wakiendelea kuteseka kwa kutohudhuria masomo.

Licha ya kumaliza mgomo huo kighafla, iliibuka baadaye kwamba wahadhiri waliamua kurejea kazini baada ya serikali kutishia kuwafuta kazi.

Serikali pia iliamua kutekeleza nyongeza hiyo, ingawa kwa muda wa miaka minne, ambapo wahadhiri watatengewa jumla ya Sh38 bilioni.

Wahadhiri waliozungumza bila kutaka kutajwa walisema kwamba walishajiishwa kurejea kazini na wakuu wa vyuo kwa kutia saini barua maalum inayoonyesha kwamba hawatafanya hivyo bila kutoa masharti yoyote.

Wale waliokataa agizo hilo walitishiwa kufutwa kazi. Ripoti ziliibuka kwamba wahadhiri 35 katika Chuo Kikuu cha Nairobi ambao waliasi maagizo hayo walipewa likizo ya lazima, huku wengine zaidi ya 1,200 wakikosa kulipwa mishahara yao ya mwezi Machi.

Iliibuka pia kwamba vyuo vikuu viliwaagiza viongozi wa wanafunzi kuandaa vikao ili kuwashinikiza wahadhiri kurudi kazini. Baada ya shinikizo kuongezeka, vyuo vikuu vya umma kama Kenyatta, Moi, JKUAT kati ya vingine vililazimika kuwaagiza wahadhiri na wafanyakazi wa idara zingine kurejea kazini.

Licha ya kumaliza mgomo huo, sharti jingine kwa wahadhiri lilikuwa kuondoa kesi ambayo walikuwa wamewasilisha katika Mahakama Kuu kupinga utathmini wa mishahara na Tume ya Kutathmini Mishahara (SRC).

Tutasambaratisha masomo Januari ‘uhamisho kiholela’ usipokomeshwa, walimu waapa

Na WANDERI KAMAU

WALIMU wametangaza mgomo mkubwa wa kitaifa kuanzia Januari 2 2019, kwa kile wametaja kutozingatiwa kwa maslahi yao na Tume ya Kuwaajiri Walimu (TSC).

Katibu Mkuu wa Chama cha Kitaifa cha Walimu (KNUT) Wilson Sossion alisema juhudi zao kuirai tume hiyo kushughulikia matakwa hayo zimegonga mwamba, na hivyo kulazimika kuchukua hatua hiyo.

Miongoni mwa matakwa wanayotaka yashughulikiwe ni kuondolewa kwa haki ya walimu kupandishwa vyeo, walimu kutenganishwa na familia zao kupitia uhamishaji wa kiholela, kuwafanyia walimu tathmini ya utendakazi bila kushirikishwa na kuanzishwa kwa mfumo wa mafunzo ambapo walimu wanalazimika kuyagharamia kupitia mishahara yao.

Kwenye kikao na wanahabari jijini Nairobi jana, Bw Sossion alisema kwamba tume hiyo imekuwa ikipuuzilia mbali kila juhudi za kuishinikiza kutathmini upya mfumo wa kuwahamisha walimu.

Mnamo Jumanne, Afisa Mkuu Mtendaji wa TSC, Nancy Macharia, alitangaza kuhamishwa kwa walimu 3,094 wa shule za msingi na upili, jambo ambalo KNUT ilipinga vikali.

“Uhamisho huo haukupitishwa na kamati maalum inayopaswa kuidhinisha uhamisho wa mwalimu kutoka shule moja hadi nyingine. Ni kinaya kwamba walimu hao wamepewa maagizo tu, bila kufahamishwa lolote kuhusu hatua hizo,” akasema Bw Sossion.

Hata hivyo, TSC inashikilia kuwa uhamisho huo ulifanywa baada ya taratibu zote zinazohitajika, kabla ya kuidhinishwa na kamati maalum.

Tume pia iliwapa walimu hao hadi Desemba 28 wawe wamehamia katika shule mpya watakakoanza kuhudumu.

Bi Macharia aliwaagiza Wakurugenzi wa Elimu wa Kaunti (CDE) kuhakikisha kuwa agizo hilo limezingatiwa .

Lakini kulingana na Bw Sossion, ambaye alikuwa ameandamana na maafisa wakuu wapya wa chama hicho, walimu hawawezi kuendelea kuvumilia ukiukwaji wa haki zao hata baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuiagiza tume kutowahamisha tena.

“Inasikitisha kwamba TSC inaenda kinyume na agizo la rais kutowahamisha walimu kwani hilo linawafanya baadhi kutengana na familia zao,” akasema Bw Sossion.

Tayari, walimu wamepinga hatua ya seriiali kuwatoza asilimia 1.5 ya mishahara yao kama ada ya Mpango wa Kitaifa wa Ujenzi kuanzia Januari, wakitishia kuwa huenda wakajumuisha hilo miongoni mwa masuala watakayogomea.

Walimu wanautaja mpango huo ukiukaji wa haki zao, wakidai kwamba hawakushirikishwa katika uidhinishaji wake.

Hii ni licha ya Rais Kenyatta kusisitiza kwamba unawiana na utekelezaji wa Nguzo Nne Kuu za Maendeleo za serikali yake.

Mgomo huo huenda ukawaathiri wanafunzi wanaojiunga na Kidato cha Kwanza, ikizingatiwa kuwa wengi wao washapokea barua kutoka kwa shule za upili watakazojiunga nazo.

Wauguzi wafutilia mbali mgomo

Na BENSON AMADALA

WAUGUZI wamefutilia mbali mgomo wao uliokuwa umepangiwa kuanza usiku wa kuamkia Jumapili.

Notisi ya mgomo huo ulionuiwa kulalamikia kucheleweshwa kwa utekelezaji wa makubaliano ya pamoja ya malipo kati ya wauguzi na serikali sasa inasema mgomo huo utafanyika Februaru 4, 2019.

Chama cha Kitaifa cha Wauguzi (KNUN) kilisema hatua hii imechukuliwa ili kutoa muda zaidi kwa Tume ya Mishahara na Marupurupu (SRC) iagize serikali za kaunti kutekeleza marupurupu yaliyokuwa kwenye makubaliano ya pamoja.

Katibu Mkuu wa KNUN, Bw Seth Panyako, alisema wauguzi watasusia kazi Februari 4 mwaka ujao kama SRC itakosa kuarifu rasmi serikali za kaunti kulipa marupurupu mapya ya wauguzi na kutekeleza makubaliano yaliyowafanya kusitisha mgomo wa mwaka uliopita.

Uamuzi huu ulitangazwa baada ya mashauriano ya wanachama wa baraza kuu la kitaifa la chama hicho.

Akizungumza akiwa Kakamega, Bw Panyako alisema serikali nyingi za kaunti zimejumuisha marupurupu mapya ya wauguzi kwenye bajeti zao za 2018/2019 hivyo basi kuna matumaini kwamba wana nia ya kulipa.

“Tulichogundua ni kwamba SRC ndio kikwazo kwani haijaidhibisha serikali za kaunti kutoa malipo hayo kwa wauguzi. Kwa msingi huu, tunaagiza SRC iwasilishe taarifa mara moja kwa serikali za kaunti kuhusu utekelezaji wa marupurupu hayo ili kuzuia kutatizwa kwa shughuli za afya kwa umma,” akasema.

Katika awamu ya kwanza ya utekelezaji wa makubaliano ya pamoja, marupurupu ya wauguzi yaliongezwa kwa Sh3,000. Yanahitajika kupanda hadi Sh3,500 katika awamu ya pili na ya tatu ya utekelezaji wa maelewano hayo.

Naibu Katibu wa KNUN, Bw Maurice Opetu, alisema ikiwa SRC itakosa kuruhusu serikali za kaunti kutoa malipo hayo kabla Februari 4, 2019, wauguzi hawatakuwa na budi ila kugoma.

Tutagoma kuanzia Novemba 21 – Wauguzi

Na ALEX NJERU

KATIBU Mkuu wa Chama cha Wauguzi Kenya (KNUN), tawi la Kaunti ya Tharaka-Nithi, Bw Fabian Marigu amesisitiza kwamba mgomo wao wa kitaifa uliopangiwa kuanza Novemba 21 hautasitishwa isipokuwa kama serikali za kaunti zitatimiza makubaliano waliyoafikiania katika mkataba wa Novemba 2017.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Chogoria hapo jana, Bw Marigu alisema jitihada zake za kuzungumza na serikali ya Gavana Muthomi Njuki hazijazaa matuda yoyote na kwamba hawana budi kujiunga na wenzao katika mgomo huo.

“Isipokuwa serikali yetu ya kaunti itimize makubaliano ya mkataba wa Novemba 2017, wauguzi watagoma Novemba 21,” alisema Bw Marigu.

Aidha alisema ni jambo la kusikitisha kuona kwamba licha ya uvumilivu wa wauguzi na jitihada za chama hicho kuhakikisha kwamba makubaliano hayo yametekelezwa kwa utaratibu waliokubaliana, waajiri wao wamenyamaza tu.

Aliongeza kuwa ni hatari kubwa kusitisha huduma za afya wakati wa mvua ambapo magonjwa mengi yakiwemo yale ya kipindupindu utokea lakini hawana budi kwani ndio njia pekee ya kufungua masikio ya serikali.

Katika barua iliyotumwa kwa Afisa Mkuu Mtendaji Baraza la Magavana, Katibu wa Wizara ya Afya na Afisa Mkuu Mtendaji wa Tume ya Mishahara kutoka ofisi ya kitaifa ya chama cha wauguzi mnamo Novemba 7, waajiri wana siku 14 kutimiza makubaliano ya Novemba 2017.

Kwa mujibu wa mkataba huo, wauguzi walitakiwa kulipwa Sh15,000 kama posho ya sare na za hatari zinazohusiana na kazi yao kati ya Sh20,000 na Sh25,000, kulingana na kiwango cha kazi katika mwaka wa kwanza wa kifedha.

Kutiwa sahihi kwa makubaliano hayo kulisitisha mgomo uliokuwa umechukua mwezi mitano.

Madaktari bondeni waruhusiwa kujifua kimasomo, watisha kugoma

MAGDALENE WANJA NA RICHARD MAOSI

ZAIDI ya madaktari 30 kutoka kaunti tano za kusini mwa Bonde la Ufa wamepokea ruhusa ya kuendeleza masomo yao wakati wa likizo.

Hii ni baada yao kutishia kugoma huku wakiwa wamepatia serikali makataa ya siku 21 kuhusu ombi lao.Wanafamasia pamoja na madaktari wa meno kupitia chama chao cha KMPDU wakiungana na viongozi katika tume zao walithibitisha haya wakisema sio jambo la kufanyiwa mzaha.

Kwa mujibu wa katibu mkuu kutoka ukanda huu Dkt Davji Atella kaunti zote sita zilikuwa zimeshindwa kutekeleza  maagano yao na idara husika kupitia (CBA), hali iliyochochea madaktari kunyimwa fursa ya kujiendeleza kimasomo wakati wa likizo pamoja na kuongezewa cheo.

Dkt Atella alieleza kuwa kaunti tano tayari zemeafikiana kuwaruhusu madaktari kuendeleza taaluma zao pamoja na kuwapandisha cheo isipokua kaunti ya Laikipia ambayo bado haijatoa maoni yake kuhusu mpangilio huu.

“Iwapo Kaunti ya Laikipia haitatupatia majibu kwa muda wa siku 21 tutaitisha mgomo wa madaktari wanaofanya kazi katika eneo hilo hadi waafikiane na matakwa ya madaktari,’’ Dkt Atella alisema.

Hata hivyo taarifa kutoka kwenye idara ya mawasiliano katika kaunti ilieleza kwamba wamekuwa wakitumia takriban milioni 10 kila mwezi kuwagharamia madaktari wanaosoma wakati wa likizo.

Pia waliongezea kwamba kwamba madaktari 20 zaidi wameongezwa ili kujaza pengo la utendaji kazi huku wakisubiri wale walio katika likizo kurejea.

‘’Tumepokea maombi 18 kutoka kwa madaktari walio katika likizo wakiomba kuendelea kulipwa wakiwa likizoni lakini jambo hili limepuziliwa na serikali ya kaunti kutokana na uhaba wa fedha pamoja na uchache wa madaktari,’’ idara ya mawasiliano kaunti ya Laikipia ilieleza huku ikiaminika zaidi ya madaktari 12 tayari wameacha kutoa huduma kabisa wakisingizia kuendeleza masomo yao.

Dkt Atella aliongeza kwamba wataendelea kujadiliana na madaktari kutoka kaunti ya Laikipia hadi watakapofikia mwafaka. Iwapo hawatakubaliana basi madaktari wataanza mgomo rasmi.

Ni hospitali chache zilizowaruhusu madaktari kuendeleza masomo kama Nakuru (13), Kericho(9), Bomet (5) na Narok (3).

Dkt Atella alionya baadhi ya hospitali zinazopanga kuwaruhusu madaktari kupata likizo kwamba hawatalipwa.

“Ni jambo ambalo ni kinyume na sheria kwani bado tunahitaji madaktari wengi tuliowaelimisha bila kuwafuta kiholela,” aliongeza. Eneo la kusini mwa bonde hili la ufa kuna madaktari zaidi ya 600.

Serikali ndiyo chanzo cha migomo shuleni – KUPPET

Na Gaitano Pessa

KATIBU Mkuu wa Chama cha Walimu wa Vyuo Anuwai (KUPPET) ameilaumu serikali kwa kuwa kiini kikuu cha kuongezeka kwa mioto shuleni.

Bw Misori (pichani) alisema kwamba wimbi la uchomaji shule lililopo limechangiwa na hali sawa, ila serikali imeshindwa kuidhibiti.

Akizungumza Jumamosi mjini Busia kwenye mkutano wa kila mwaka wa chama, Bw Misori alisema kuwa sababu kuu za mioto hiyo ni matatizo ya masuala ya usimamizi ambayo serikali imeshindwa kuyatatua. Vile vile, alitaja hali mbaya ya miundomsingi kama kiini kingine kikuu.

“Hatuhitaji uchunguzi kufahamu kiini kikuu cha hali ya mioto na migomo shuleni. Serikali imechangia moja kwa moja, kwani mazingira ya masomo katika shule husika yako katika hali mbaya sana,” akasema.

Akaongeza: “Ni vipi utawaeleza wanafunzi kuendelea kukaa katika shule ya mabweni ambayo haina vyumba vya malazi, kumbi za maakuli na madarasa ya kutosha. Serikali inapaswa kuchukua lawama moja kwa moja.”

Katibu huyo alikuwa ameandamana na Mwakilishi wa Wanawaka katika kaunti hiyo, Catherine Wambilianga, msimamizi mkuu wa tawi hilo Mophat Okisai na maafisa kutoka kaunti jirani.

Bi Wambilianga, aliye pia ni Katibu wa Mipango katika chama alisema kuwa imefikia wakati ambapo lazima serikali imalize kimya chake kuhusu mioto hiyo.

“Tunakabiliwa na changamoto hizi kwa kuwa serikali imekataa kutoa Sh5 kwa shule, ili zitumiwe katika uimarishaji wa miundosmsingi husika. Hilo ndilo limezua hali ya kutotosheka miongoni mwa wanafunzi. Serikali inaonekana kusahau kwamba si walimu wanachangia wala kuwachochea wanafunzi,” akaongeza.

Aliapa kuhakikisha kwamba changamoto zote zinazowakabili walimu zimejadiliwa katika Bunge la Kitaifa.

#EndLecturersStrike: Kero mitandaoni wanachuo wakimsihi Uhuru asuluhishe mgomo

Na PETER MBURU

WANAFUNZI wa vyuo vikuu vya umma nchini wametumia mitandao ya kijamii kuonyesha ghadhabu zao, wakinuia kumfikishia Rais Uhuru Kenyatta ujumbe namna walivyoathirika kielimu na kumtaka asuluhishe mgomo huo.

Wanafunzi hao walifanya hamasisho la saa moja wikendi, kwa posti za Twitter wakiwajumuisha Rais, Waziri wa Elimu na mashirika ya habari kama mbinu ya kupasha taifa habari za adhari wanazopata kutokana na mgomo huo.

Hamasisho hilo lenye hashtegi #EndLecturersStrike na #OkoaUniversity  liliwataka wanafunzi kuchangia zaidi ya posti milioni moja zikieleza mahangaiko ya wanafunzi kufuatia mgomo huo.

Kila mwanafunzi alihitajika kutuma posti 20 na kuwahusisha Rais, Waziri wa Elimu Amina Mohamed na angalau mashirika makuu ya habari nchini.

Wakati wa zoezi hilo, maelfu ya wanafunzi walieleza namna wanavyoathirika, huku wakimtaka Rais mwenyewe kuingilia kati na kuwaokoa, wakisema masomo katika taasisi za juu za elimu yamedorora kwa viwango vikubwa.

Wanafunzi walisema waziwazi kuwa serikali ilikuwa ikijikokota sana kusuluhisha tatizo hilo sugu, wakitaka taifa kulitambua kama janga la kitaifa katika kampeni hiyo iliyodumu kati ya saa sita na saa saba mchana wa Jumapili.

“#okoaUniversity @UKenyatta mimi pamoja na wanafunzi wenzangu 600,000 tumechoka. Tunarudi darasani lini? Maliza mgomo wa wahadhiri #LecturersStrikeKE,” akaandika @connienyakio.

“#EndLecturersStrike wanasiasa ambao wana wao wanasomea vyuo kama Havard, Cambridge, Yale na Leeds hawatatishwa hata mgomo ukidumu miezi 20,” @IamNjokiKelvin.

“Tunamsihi Mheshimiwa Rais @UKenyatta na @AMB_A_Mohammed kumaliza mgomo wa wahadhiri. Wanafunzi wamechoshwa kabisa. Malizeni mgomo @KTNNews @citizentvkenya @RailaOdinga @WilliamsRuto @UASU_KE #EndLecturersStrike.”

Baadhi ya wanafunzi walieleza matatizo ya kifedha wanayopitia, haswa wanaoishi nje ya vyuo na ambao watalazimika kulipia kodi maradufu kutokana na muda uliopotea wakati wa mgomo.

“#EndLecturersStrike Kwa kawaida ninalipa Sh30,000 za makazi kwa kipingi cha mwaka wa masomo, sasa itanibidi kulipa Sh60,000 kwani mgomo umerefusha muda wa masomo, kwani nitalipa karo ama kodi.”

“@AMB_A_Mohammed tupeni ishara kuwa tutahudhuria madarasa. Mgomo wa wahadhiri sasa utajwe janga la kitaifa #okoauniversity.”

“#EndLecturersStrike @UKenyatta Ni wakati wako kuingilia kati sasa na kutoa suluhu ya kudumu kwa suala la mgomo wa wahadhiri. Kwa miaka mitatu iliyopita, wanafunzi wa vyuo vikuu hawajahudhuria masomo ifaavyo. Hii imewagharimu muda na pesa. @KTNNews @citizentvkenya.”

Wanafunzi hao walishikilia kuwa wataendelea na msukumo huo hadi Rais mwenyewe awape sikio na kushughulikia kilio chao.

 

Wahadhiri waapa kutumia njia zote kuendeleza mgomo wao

Na WANDERI KAMAU

WAHADHIRI wa vyuo vikuu vya umma Jumatano waliapa kutumia njia mbadala kuendeleza mgomo wao baada ya maandamano waliyopanga kufanya kusambaratishwa na polisi jijini Nairobi.

Wahadhiri hao walikuwa wakielekea katika makao makuu ya Wizara ya Elimu na Hazina ya Kitaifa jijini Nairobi, ila maandamano yao yakazimwa na polisi walipofika katika Jumba la Anniversary.

Aidha, walikuwa wamekusanyika katika Chuo Kikuu cha Nairobi, walikolalamikia kutojitolea kwa serikali katika kusuluhisha mgomo wao. Licha ya hayo, polisi waliingilia kati na kuwazuia, wakishikilia kwamba hawakuwa wamepokea notisi ya kuwakubalia kuandamana.

Polisi waliokuwa wamejihami vikali walidai kupokea “maagizo kutoka juu” walitishia kuwarushia vitoa machozi, iwapo hawangetii maagizo yao.

“Hatujapata kibali rasmi kuruhusu maandamano yoyote. Hivyo, lazima wanaondamana waondoke barabarani mara moja,” akasema Mkuu wa Polisi katika Kituo cha Central, Robinson Thuku, aliyeongoza kikosi hicho.

Ilibidi wahadhiri kurejea katika Chuo Kikuu cha Nairobi, ambako waliapa kutumia kila njia kuhakikisha kwamba hakuna shughuli zozote za masomo zinaendelea katika vyuo hivyo, hadi pale matakwa yao yao kushughulikiwa.

Wahadhiri hao wanashinikiza kutekelezwa kwa Mwafaka wa Malipo wa 2017-2021, ili kuongezwa mishahara na marupurupu wanayopata.

Kwenye hotuba zao, viongozi wa Chama cha Wahadhiri (UASU) na Wafanyakazi wa Vyuo Vikuu (KUSU) waliwalaumu Waziri wa Elimu Amina Mohamed na Katibu Japeh Ntiba kuwa kikwazo kikuu cha kupatikana kwa suluhisho kuu.

Mwenyekiti wa UASU Prof Muga K’Olale alisema kuwa wawili hao hawana ufahamu wa kindani kuhusu malalamishi halisi ya wahadhiri na wafanyakazi wengine, kwani wameluwa wakikubali kupotoshwa na Manaibu Chansela (VCs).

Prof K’Olale alisema kwamba juhudi za kuwafikia wawili hao zimegonga mwamba, hivyo wakibaki bila lingine ila kuendeleza mgomo huo.

“Nimekuwa katika harakati za kuwatetea wafanyakazi wa vyuo vikuu kwa muda mrefu, ila kinyume na migomo mingine, kikwzo kikuu kwa sasa ni waziri husika (Amina) kukubali kupotoshwa na wakuu wa vyuo kwamba hakuna ukweli wowote katika malalamishi yetu,” akasema.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa UASU Dkt Constantine Wasonga alisema kuwa wako tayari kumaliza mgomo huo, ikiwa serikali iko tayari kutoa mapendekezo yake kuhusiana na mkataba huo.

 

 

 

Mgomo huo ambao unaingia siku ya 49 leo umeathiri masomo katika vyuo vyote 31 vya umma nchini na wanafunzi zaidi ya 600,000.

 

Walimu wanaochochea wanafunzi kugoma waonywa

Na MUNEENI MUTHUSI

SUALA la baadhi ya walimu kuchochea migomo miongoni mwa wanafunzi shuleni liliangaziwa pakubwa hapo Jumatatu katika mchezo “Zahama” uliowasilishwa na shule ya upili wa wasichana ya Kichaka Simba kutoka kaunti ya Kwale.

Jumatatu ikiwa siku ya mwisho ya tamasha za michezo ya kuigiza kwa shule na vyuo ukumbini Lenana School, jijini Nairobi, mchezo huo uliibua uliibua hisia kali ukumbini.

Hayo yalikuwa wakati mchezo ulipofika hatua ya wanafunzi wa kidato cha tatu na cha nne walivyokula njama kuchukua mafuta ya petroli na kujaribu kuwachoma wenzao wa vidato vya kwanza na pili.

Ukumbi ulitulia tuli huku mioyo ya baadhi ya hadhira ikidunda dunda kana kwamba lilikuwa tukio la kweli lilivyokuwa likiendelea.

Wanafunzi hao walimwaga mafuta katika mabweni ya kidato cha kwanza na cha pili huku hadhira ikidundwa na roho, mmoja wa hao wanafunzi waasi alichukua kiberiti na kuwasha moto. Moto uliwaka kote mabwenini.

Lakini kwa bahati nzuri hayo mabweni hayakuwa na wanafunzi, kwani walikuwa wametahadharishwa na mmoja wa hao waasi (Karema) na kutorokea usalama kwengineko.

Swali ni, chuki hii dhidi ya wenzao waliitoa wapi? Walichochewa na mwalimu mwandamizi (Mwalimu Chocha) walipokataa kutekeleza njama yake ya kumkataa mwalimu mwenzake (mwalimu Tulivu).

Lakini ngoma ya kitamaduni kutoka St. Philips Mukomari ukanda wa Magharibi ilikuwepo kuziosha dukuduku zilizokuwa zimejijenga katika nyoyo za hadhira.

Katika densi hiyo kwa jina “Sonia” iliyopigwa kwa miondoko ya tamaduni ya Kiluhya, hatua kwa hatua ilionyesha kwa nini uwiano wa kifaifa ni muhimu kwa maisha yetu.

Wanafunzi walifanyikiwa kuonyesha hadhira kwamba baadhi ya matamshi ya chuki na kauli za kikabila zinazoendelezwa humu nchini, zinaweza kuwa na madhara makubwa, hata kwa wanaozitoa.

Vile vile shule ya upili ya wasichana ya Riara Springs, ambao ni wenyeji kutoka Jijini Nairobi walisisimua kupitia kwa mchezo wao “Scars of Yesterday”.

Mchezo huo ulitoa onyo dhidi ya tabia ya kutoyatambua na kujifunza kutokana na makosa ya siku za nyuma.

Mchezo huu hasa ulisisimua kwa vifaa ambavyo waigizaji hao walivitumia kuwasilisha ujumbe wao.

Baada ya kutamatika kwa mashindano hayo, sasa washindi kutoka kila kitengo watapata fursa ya kumtubuiza rais.

Wahadhiri: Tutagoma hadi tupewe haki yetu

Na CECIL ODONGO

VIONGOZI wa Miungano ya Vyama vya Wahadhiri na Wafanyakazi wa Vyuo Vikuu nchini Jumatatu walisisitiza kwamba mgomo wao bado unaendelea hadi pale serikali kuu itawatimizia mapendekezo kwenye makubaliano ya 2017-2022.

Katibu mkuu wa Muungano wa Wahadhiri (UASU) Constantine Wasonga (pichani kati), mwenzake wa Muungano wa Wafanyakazi wa Vyuo Vikuu (KUSU) Charles Mukhwana na Mwenyekiti wa UASU Muga K’olale wamesisitiza serikali haijajitolea kikamilifu kuhakikisha mgomo huo unasitishwa.

Wakizungumza na wanahabari wakiwa wameandamana na viongozi wengine, walisema kwamba suala la kusitisha ama kuendelea kwa mgomo huo linashughulikiwa na mahakama baada ya kuwasilisha rufaa kupinga uamuzi uliowataka kurejea kazini.

“Sisi hatutazungumzia suala tata linaloshughulikiwa mahakamani jinsi alivyoshauri jaji mkuu David Maraga wiki jana lakini kile tunapigania ni kujadiliwa na kutekelezwa kwa mwafaka wa 2017-2022”, akasema katibu wa UASU Constatine Wasonga.

Aidha, alitaka serikali kukoma kutoa vijisababu ambavyo havina mashiko na badala yake itafute njia za dharura kuhakikisha mgomo huo unaisha ili zaidi ya wanachuo 600,000 warejee darasani.

Hata hivyo, viongozi hao walionekana kulegeza msimamo kuhusu kutekelezwa kwa muafaka huo huku wakitoa pendekezo nafuu kwa serikali.

“Iwapo serikali inaona muafaka wetu ni mzigo mkubwa kwa uchumi basi tunawapendekezea watulipe awamu ya mwaka mmoja na malimbikizi ya marupurupu yetu kisha pesa zinazosalia wazitenge katika bajeti ya miaka inayofuatia hadi mwaka wa 2021,” akasema katibu wa KUSU Charles Mukwana.

Alidai kwamba serikali ina njama fiche ya kutaka kufanya mabadiliko katika vyuo vikuu nchini na kukishtumu Chuo kikuu cha Nairobi kwa kwenda mahakamani ili kushurutisha wafanyakazi na wahadhiri wake kurejea kazini.

“Chuo Kikuu cha Nairobi kinawalazimisha wanachama wetu kurudi kazini lakini tumekata rufaa kuhusu uamuzi uliotolewa na mahakama ya kuwataka wafanyakazi wa chuo hicho warejee kazini,” akasisitiza.

Viongozi hao walidai kwamba hazina kuu ya serikali imewatengea fedha ila serikali kuu ndiyo kikwazo kwa kutotoa idhini ya kutolewa kwa pesa hizo.
Pia, walikanusha habari kwamba walikutana na waziri wa Leba Ukur Yatani wiki jana kwa majadiliano kuhusu kusitishwa mgomo huo.

Viongozi hao walitarajiwa kukutana na Waziri wa Elimu Amina Mohamed jana na kisha kufika mbele ya kamati ya bunge kuhusu Elimu siku ya Alhamisi kujaribu kutafuta suluhu ya kumalizika kwa mgomo huo ambao umedumu kwa wiki sita hadi sasa na kulemeza shughuli za masomo kwenye vyuo 31 vya umma.

 

 

Walimu watisha kugoma wakiendelea kuhamishwa

Na BARACK ODUOR

WALIMU wametishia kugoma muhula ujao kama serikali haitabadilisha sera za kuhamisha walimu kutoka maeneo yao ya kijamii.

Katibu Mkuu wa Chama cha Kitaifa cha Walimu (Knut), Bw Wilson Sossion, alisema wanataka pia serikali ifutilie mbali mtindo wa kutathmini utendakazi wa walimu na badala yake walimu wawe wakipandishwa vyeo kwa msingi wa kisomo chao.

Akizungumza katika Shule ya Upili ya Homa Bay wakati wa mkutano wa mwaka wa Knut katika tawi hilo Jumapili, Bw Sossion alisema masuala hayo yanaathiri vibaya utendakazi wa walimu.

Akiandamana na Mbunge Mwakilishi wa Kaunti ya Homa Bay, Bi Gladys Wanga, aliipatia serikali siku 20 kuanzia leo kutimiza matakwa ya walimu.

“Hakuna shule itafunguliwa kwa muhula wa pili kama serikali haitatimiza mahitaji haya. Tutaitisha mgomo mkubwa humu nchini kuanzia siku ya kufungua shule,” akasema.

Kulingana naye, mgomo utaanzishwa na walimu ambao watapiga kambi katika afisi za Tume ya Kuajiri Walimu (TSC).

Bw Sossion alilalamika kuwa sera ya kuhamisha walimu kutoka maeneo yao ya kijamii itaathiri utendakazi wao kwani ndoa za wengi zitatatizwa.

“Hatua hii itavunja familia za walimu wengi wakihamishwa hadi maeneo yaliyo mbali na nyumbani kwao,” akasema.

Msimamo wake uliungwa mkono na Bi Wanga ambaye alisema hatua hiyo ya serikali itadhuru jamii za walimu husika.

Kulingana naye, walimu wanaofunza katika maeneo yao ya kijamii huwa wanategemewa kutoa aina zingine za usaidizi kwa jamii.

Alilaumu TSC kwa kupuuza wito wa kupandisha walimu vyeo wanapokamilisha elimu ya juu licha ya walimu kutumia rasilimali zao kuendeleza masomo.

“Inasikitisha kuwa walimu wengi walijitahidi kwa kutumia fedha kidogo kuendeleza elimu yao lakini TSC inasema itapuuzilia mbali vyeti vyao vya elimu kufanya uamuzi wa kuwapandisha vyeo,” akasema Bi Wanga.

Bw Sossion alisisitiza kuwa walimu walioendeleza masomo yao lazima wapandishwe vyeo.

Wahadhiri waagizwa kurejea kazini Jumatatu au wafutwe

Na OUMA WANZALA

WASIMAMIZI wa vyuo vikuu nchini wametishia kuwachukulia hatua kali wahadhiri ikiwa hawatarejea kazini kufikia Jumatatu Aprili 9.

Wakati wa mkutano na wanahabari jana katika Chuo Kikuu cha Kiufundi cha Nairobi (TUC), shirikisho la mabaraza ya vyuo vikuu (IPUCCF) liliwapa idhini wasimamizi wa vyuo vikuu kuwachukulia hatua wahadhiri watakaokosa kufika kazini Jumatatu.

“Hii ni kuwahimiza wasimamizi wa vyuo vikuu kuwachukulia hatua kali wahadhiri wa vyuo vyao ambao hawatafika kazini Jumatatu,” alisema mwenyekiti wa IPUCCF Profesa Paul Kanyari.

Aliwataka wahadhiri hao kutii agizo la Mahakama ya Leba na kurejea kazini na kuwaonya dhidi ya kuendelea kukaidi maagizo ya mahakama.
Kutokana na mgomo wa wahadhiri, vyama vingine vya wahudumu wa vyuo vikuu, KUSU na KUDHEIHA pia vimejiunga na mgomo huo.

Lakini wahadhiri wameapa kutorejea kazini ikiwa hawatatimizwa matakwa yao. Hii ni licha ya Mahakama ya Masuala ya Leba kuwataka kurejea kazini Jumatatu.

Kulingana na chama cha wahadhiri (UASU), tayari kimekata rufaa ya hukumu hiyo iliyotolewa Ijumaa.

Walisema mgomo utaendelea mpaka mahakama ya rufaa itoe uamuzi wake. Katibu Mkuu wa UASU Constantine Wasonga aliwataka wahadhiri kupuuza ilani zote zilizotolewa na wasimamizi wa vyuo vikuu.

Alisema mawasiliano yote yatatoka chamani humo mgomo unapoendelea na kuwataka kupuuza wasimamizi wa vyuo vikuu.

Ijumaa, Jaji wa Mahakama ya Masuala ya Leba Onesmus Makau alisema mgomo wa wahadhiri ulikuwa haramu na haukuwa umetambuliwa kisheria na kuwataka wahadhiri hao kurejea kazini. Jaji huyo alivitaka vyuo vikuu kuwasilisha mkataba wa makubaliano kati ya 2017 na 2021 kwa Waziri wa Leba katika muda wa siku 21.

Mahakama ya Rufaa inatarajiwa kutoa mwelekeo kuhusu hali hiyo Jumatatu. Mapema wiki hii, wahadhiri walifanya maandamano Nairobi na kuitaka serikali kuwasilisha ofa yake.

Migomo ya wahadhiri kuanzia mwaka jana imeathiri pakubwa mafunzo katika vyuo vikuu vya umma. “Vyuo vikuu vya umma havijaweza kupata nafuu kutokana na mgomo wa 2017 hali ambayo imeathiri masomo,” alisema Prof Kanyari.

Mgomo huo unaingia siku ya 40 Jumatatu.

Wafanyakazi wa Tuskys watisha kugoma

Na BERNARDINE MUTANU

Wafanyikazi wa Tuskys wanalenga kugoma katika muda wa wiki mbili zijazo kwa kulalamika kufanyiwa hila na mwajiri wao.

Walitoa notisi ya kwenda mgomo Jumanne kupitia kwa chama chao cha wafanyikazi. Wafanyikazi hao walilalamika kuhamishwa kwa wasimamizi wengi wa wafanyikazi wa maduka hayo na kukosa kwa mwajiri wao kuwatambua wasimamizi hao kama wawakilishi wao.

Miongoni mwa malalamishi yao ni kuhusiana na kukosa kwa kampuni hiyo kutii maagizo ya mahakama kuhusu huduma za kutoka nje na hatua za kinidhamu zilizochukuliwa dhidi ya wasimamizi wao.

Kulingana na katibu mkuu wa chama hicho Boniface Kavuvi, juhudi za kusuluhisha mzozo huo kwa njia ya mazungumzo zimegonga mwamba, hivyo, baada ya wiki mbili ikiwa malalamishi yao hayatakuwa yamesikilizwa na kusuluhishwa wataenda mgomo.