Kilio serikali za kaunti zikikosa kulipa mishahara

Na WAANDISHI WETU

WAFANYAKAZI katika baadhi ya serikali za kaunti wanateseka baada ya kukosa mishahara kwa miezi kadhaa.

Wengi wamefurushwa katika nyumba za kukodisha na kuandamwa na mashirika ya kifedha kwa kukosa kulipa mikopo. Katika Kaunti ya Taita Taveta, wafanyakazi wapatao 3,000, wanakabiliwa na wakati mgumu baada ya mwajiri wao kutangaza kuwa mishahara yao itacheleweshwa kwa mara nyingine.

Hii ni kutokana na Wizara ya Fedha kuchelewesha pesa za serikali za kaunti. Wafanyakazi hao wamekaa bila kulipwa mishahara kwa miezi miwili tangu Februari.

“Fedha za mwisho zilizotolewa na Hazina ya Kitaifa zilikuwa za Januari huku serikali ya kaunti hiyo ikiwa imelipa mishahara hadi Februari 2021. Hata hivyo, tutalipa mishahara hiyo wakati fedha zitakapotolewa,” alisema katibu wa Kaunti, Liverson Mghendi, kupitia barua kwa wafanyakazi.

Baadhi yao walifichua kuwa wametakiwa na wamiliki wa nyumba wanazoishi kulipa kodi au wahame kwa sababu ya kukosa kulipa kodi mara kwa mara.

Katika Kaunti ya Migori, vilevile, wafanyakazi wanapitia hali ngumu huku benki zikikwamilia mishahara yao baada ya kaunti kuchelewa kulipa pesa inazowakata ili kulipa mikopo yao.

Taifa Leo imebaini kuwa walioathirika zaidi ni waajiriwa walio na akaunti katika benki za KCB na National Bank, ambazo zimezuilia mishahara yao tangu Machi baada ya idara ya Fedha kukosa kulipa mikopo.

“Tunakabiliwa na wakati mgumu kabisa, wafanyakazi wengi wanaoweka pesa KCB na National Bank hawajapokea mishahara yao kwa miezi miwili kwa sababu idara ya Fedha haijalipa mikopo. Serikali ya Kaunti hutoa tu mishahara kwa jumla ambayo imezuiliwa na benki hizo,” alisema afisa wa kaunti.

Wauguzi na maafisa wa kliniki walioshiriki migomo kati ya Januari na Machi nao bado hawajapokea malipo yao. Kwingineko katika Kaunti ya Murang’a, baadhi ya wafanyakazi wanaingia katika mwezi wa tano bila kulipwa mishahara. Hii ni baada ya benki kufutilia mbali muafaka wa malipo baina yazo na serikali ya kaunti hiyo baada ya miezi mitatu ya kukosa kulipa mikopo ya awali.

“Ni jambo la kuhuzunisha sana kwetu. Malipo ya mishahara yamekuwa na matatizo na wakati mwingine tumecheleweshewa hata kwa miezi minne. Hii ni sawa na mateso,” mfanyakazi mmoja wa kibarua alieleza Taifa Leo.

Ripoti za Lucy Mkanyika, Ian Byron na Mwangi Muiruri

LEONARD ONYANGO: BBI ikipita mshahara wa wabunge ukatwe

 

Na LEONARD ONYANGO

WATAALAMU wa masuala ya uchumi wanatabiri kuwa Wakenya watalazimika kutumia kati ya Sh60 milioni na Sh300 milioni zaidi kulipa mishahara na marupurupu ya wabunge na maseneta iwapo Mswada wa Mpango wa Maridhiano (BBI) utapitishwa na Wakenya katika kura ya maamuzi.

Kwa mujibu wa takwimu hizo zilizotolewa wiki iliyopita na Taasisi ya Masuala ya Kiuchumi (IEA), idadi ya wabunge katika Bunge la Kitaifa itaongezeka kutoka 349 wa sasa hadi 546 ambao wanapendekezwa na Mswada wa BBI.Iwapo Mswada wa BBI utapitishwa, idadi ya maseneta itaongezeka kutoka 67 hadi 94.

Kila seneta au mbunge hupokea jumla ya Sh1.3 milioni kila mwezi. Kiasi hicho kinajumuisha mshahara wa Sh710,000 na marupurupu ya aina mbalimbali kama vile Sh100,000 za kuketi kwenye vikao vya kamati, Sh150,000 maruprupu ya kuwajibika, Sh400,000 za usafiri na Sh15,000 za mawasiliano ya simu.

Kila mbunge au seneta hutengewa Sh10 milioni kwa ajili ya bima ya matibabu, mkopo wa Sh7 milioni za mkopo wa gari na Sh20 milioni za mkopo wa kununua nyumba.

Mikopo hii hulipwa katika muda wa miaka mitano.Fedha hizi za bwerere ndizo husukuma Wakenya, wakiwemo wasomi waliobobea katika nyanja mbalimbali, kujiuzulu na kujitosa kwenye siasa.

Ulafi wa kutaka mshahara huo mnono ndio husababisha wanasiasa kutumia hata mbinu chafu almuradi waingie Bungeni.Wabunge wa Kenya hulipwa mishahara minono kuliko baadhi ya marais wa nchi za Afrika.

Marais wa nchi kama vile Guinea, Cape Verde, Tunisia na Senegal hupokea mshahara wa chini ikilinganishwa na wabunge wa Kenya.

Waziri Mkuu

Mbali na kuongeza idadi ya wabunge na maseneta, Mswada wa BBI unapendekeza kuongezwa kwa afisi zilizopigwa marufuku na Katiba ya 2010, kama vile waziri mkuu, manaibu wa waziri mkuu na kiongozi rasmi wa upinzani.

Ni bayana kwamba Mswada wa BBI unalenga kuwatwika Wakenya mzigo mzito ambao tayari wanahangaika kutokana na uchumi mbovu ambao umesababisha ongezeko la ukosefu wa ajira, kuporomoka kwa viwanda kati ya changamoto nyinginezo.

Kwa mujibu wa Katiba, ulipofikia Mswada wa BBI haufai kufanyiwa mabadiliko Bungeni ili kupunguza idadi ya wabunge na maseneta.Hivyo basi kuna haja ya kupunguza mshahara na marupurupu ya wabunge na maafisa wengine wa serikali ili kuwaondolea Wakenya mzigo mzito wa kulipa ushuru endapo Mswada wa BBI utapitishwa.

Kwa mfano, hakuna haja ya kuwalipa wabunge marupurupu ya kuketi kwenye kamati ilhali hiyo ndiyo kazi waliyochaguliwa kufanya. Hakuna haja ya kulipa marupurupu ya usafiri ilhali wengi wa wabunge na maseneta hutumia fedha hizo katika kampeni zao za kibinafsi zisizo na manufaa kwa Wakenya.

Walimu sasa walia, wataka nyongeza mpya ya mshahara

Na ERIC MATARA

CHAMA cha walimU (Knut), kinataka Tume ya Huduma ya Walimu (TSC), kuharakisha mazungumzo kuhusu makubaliano ya pamoja (CBA), kuwawezesha walimu kuanza kupata mishahara mipya kuanzia Julai 1, 2021.

Katibu Mkuu wa chama hicho Wilson Sossion, aliyezungumza akiwa mjini Nakuru baada ya kukutana na walimu kutoka eneo la Rift Valley, alisema kwamba mkataba wa sasa utaisha Juni 30 na utekelezaji wa CBA mpya unafaa kuanza Julai 1 ilhali TSC haijakamilisha shughuli hiyo.

“Nilikutana na baraza la Knut la eneo la Rift Valley na tumejadili masuala kadhaa ikiwemo CBA inayokuja. Lililo wazi ni kuwa walimu wanafaa kuanza kupata mishahara mipya kuanzia Julai 1 kupitia mfumo ambao umejadiliwa vyema. Hili ndilo jukumu kuu la chama ,” alisema Bw Sossion baada ya mkutano uliofanyika katika hoteli ya Golden Palace Hotel.

Jumapili, Bw Sossion alikutana faraghani kwa takriban saa nne na wanachama wa tawi la Rift Valley la Knut ambapo walijadili masuala kadhaa ikiwa ni pamoja na CBA.Duru miongoni mwa waliohudhuria mkutano huo zilifichulia Taifa Leo kwamba mazungumzo hayo pia yalihusu uchaguzi ujao wa chama hicho.

Mwenyekiti wa tawi la Rift Valley la Knut, Bw Maurice Barchok pia alitaka TSC kuidhinisha CBA haraka.“Kwa niaba ya walimu ninaowakilisha, ninahimiza TSC kuharakisha utekelezaji wa CBA kuhakikisha walimu wanaanza kupokea mishahara mipya kuanzia Julai 1,” alisema Bw Barchok.

Knut imekataa pendekezo la nyongeza ya mishahara la kati ya asilimia 16-32 ambalo TSC iliwasilisha kwa Tume ya Mishahara (SRC), ikisema haikuhusishwa.

CHARLES WASONGA: Serikali ikome kuhujumu vyama vya kutetea wafanyakazi

Na CHARLES WASONGA

NI haki ya wafanyakazi kote ulimwenguni kujiunga na vyama vya kutetea masilahi yao kama vile nyongeza ya mishahara na marupurupu na kuboreshwa kwa mazingira yao ya kikazi.

Hii ndio maana kipengele cha 41 cha Katiba ya sasa kinalinda haki ya mwajiriwa kuunda au kujiunga na chama cha kutetea masilahi yake sawa na kushiriki majadiliano na waajiri wao kuhusiana na masuala hayo.

Sheria ya Leba ya 1997 pia inatambua wajibu wa vyama hivyo katika kujadiliana na waajiri kuhusiana na masuala ya ajira.

Kwa hivyo, juhudi zinazoendeshwa wakati huu na serikali kuu na zile za kaunti kuhujumu na kulemaza vyama vya kutetea masilahi ya wafanyakazi ni kinyume cha Katiba na sheria hii muhimu.

Baada ya kung’amua kuwa inafanikiwa kuua Chama cha kitaifa cha Walimu (Knut) kwa kutumia Tume ya Kuajiri Walimu (TSC), serikali kuu sasa inashirikiana na Baraza la Magavana Nchini (CoG) kuangamiza vyama vya kutetea masilahi ya wahudumu wa afya.

Waziri wa Afya Mutahi Kagwe na mwenzake wa Utumishi wa Umma Profesa Margaret Kobia, wamekubaliana na CoG kwamba kama waajiri wa wahudumu wa afya, hawatakuwa wakiwasilisha michango ya wafanyakazi hawa kwa vyama husika, kila mwezi, kama ilivyo ada.

Hii ina maana kuwa vyama kama vile, Chama cha kutetea masilahi ya madaktari (KMPDU), kile cha kutetea wauguzi (KNUN), kile cha matatibu (KUCO) miongoni mwa vingine vitalazimika kusubiri wanachama kuwasilisha michango yao baada ya kupokea mishahara.

Kuna uwezekano mkubwa kuwa wengi wa wanachama hawatawasilisha michango yao kivyao, hali ambayo itatumbukiza vyama hivyo katika lindi la changamoto za kifedha.

Hali hii bila shaka, itachangia vyama hivyo kukosa makali ya kutetea masilahi ya wahudumu wa afya ipasavyo na hatimaye kusambaratika. Knut inahujumiwa na TSC kwa namna hii kando na wanachama wake kunyimwa nyongeza ya mishahara na manufaa mengineyo.

Matokeo yake ni kwamba, Knut imepoteza uwezo wa kifedha wa kufadhili shughuli zake katika matawi kando na wanachama wake wengi kuhama na kujiunga na Chama cha Kutetea Masilahi ya Walimu wa Shule za Upili na Vyuo vya Kadri (KUPPET).

Naona hali kama hii ikikumba vyama vya kutetea masilahi ya wahudumu wa afya na kuvifanya kuwa butu kiasi cha kushindwa kutekeleza majukumu yao.

Matokeo yake ni kwamba huenda wahudumu wa afya wanaofanya kazi katika hospitali za umma watajiuzulu na kujiunga na zile za kibinafsi au kusaka ajira katika mataifa ya ng’ambo.

Atakayeumia ni mwananchi wa kawaida ambaye hutegemea huduma za afya zinatotolewa na hospitali za umma kwa kushindwa kumudu gharama ya juu ya huduma hizo katika hospitali za kibinafsi au zile za ughaibuni.

Serikali Kuu na CoG zimekome kuhujumu vyama vya kutetea masilahi ya wahudumu wa afya.

Polisi wengi wagura kazi, walia wanalipwa mshahara wa kitoto

Na Steve Njuguna

POLISI wengi wa akiba (NPRs) Kaunti ya Laikipia, wameacha kazi hiyo wakilalamika kwamba wanalipwa mshahara wa chini na kupokonywa silaha.

Polisi hao wamelaumu serikali kwa kuacha wakazi kwenye hatari ya kushambuliwa na majangili wanaotoka kaunti jirani.Mnamo 2019, serikali iliwapokonya silaha polisi wa akiba 3000 eneo la Kaskazini mwa Bonde la Ufa katika juhudi za kuangamiza ujangili.

Waliagizwa kurudisha silaha hizo katika vituo vya polisi ilipobainika baadhi yao walikuwa wakizitumia kwa vitendo vya uhalifu.Baadhi yao wanasema kwamba waliachwa bila uwezo wa kuwalinda wakazi wa maeneo yao baada ya kupokonywa silaha.

“Hatuwezi kusaidia maafisa wa polisi wahalifu wakivamia watu wetu kwa sababu hatuna silaha.

Hauwezi kwenda katika vita kupigana na adui aliye na bunduki ukiwa mikono mitupu kama baadhi ya wenzetu ambao wameuawa wakijaribu kusaidia maafisa wa polisi wakati wa mashambulizi,” alisema Bw Simon Ellman.

Alitaja kisa ambapo polisi wa akiba, Bw Simon Kipkemoi, aliuawa kwa kupigwa risasi na wezi wa mifugo. Bw Joel Kirui ambaye pia ni polisi wa akiba alisema tangu walipopokonywa silaha, wenzao 10 wameuawa.

Aibu kwa madiwani wa Nakuru kumeza mishahara ya bwerere kwa miezi sita

Na FRANCIS MUREITHI

MISWADA minne muhimu kutoka kwa madiwani wa wadi mbalimbali katika Kaunti ya Nakuru haijawahi kushughulikiwa na kamati mbalimbali za bunge la kaunti hiyo kwa zaidi ya miezi sita sasa.

Madiwani wa Bunge la Kaunti ya Nakuru wamelaumu uongozi mbaya katika bunge hilo kuwa kiini cha kutojadiliwa kwa baadhi ya miswada hiyo iliyowasilishwa kwa kamati husika kuanzia Machi 2020.

Mnamo Julai 16, Spika wa Bunge la Nakuru, Joel Maina Kairu alihimiza madiwani kujadili miswada yote iliyowasilishwa na kupisha upesi mchakato wa kuundwa kwa sheria mbalimbali.

Kwa mujibu wa kanuni 123 na 125 za Bunge la Kaunti, miswada yote inayowasilishwa kwa kamati husika bungeni inastahili kujadiliwa na madiwani chini ya kipindi cha siku 20.

Haya yanafanyika wakati ambapo baadhi ya wakazi wa kaunti wameanza kupoteza imani na Bunge la Kaunti ya Nakuru ambalo kwa mujibu wao, limeshindwa kabisa kushughulikia majukumu muhimu ya uundaji wa sheria.

Mswada kutoka kwa Diwani wa Gilgil, Jane Ngugi kuhusu jinsi shamba la eneo la Kembi Somali litakavyotumika haujajadiliwa kwa muda mrefu kwa sababu mwenyekiti wa kamati ya Ardhi, Ujenzi na Mipango ya Miji, Stephen Ngethe Chege wa Maai Mahiu, hajawahi kufika bungeni kwa muda ikiwemo Oktoba 30 iliyokuwa siku ya kujadiliwa kwa mswada wake.

Naibu mwenyekiti wa kamati hiyo, Gladys Nyambura Kairu, ambaye ni diwani mteule, alisema mustakabali wa mswada huo utajulikana baada ya wiki mbili zijazo.

Kwa upande wake, diwani wa Naivasha Mashariki, Stanley Karanja alisema sheria nyingi kuhusu jinsi masuala ya Kaunti ya Bunge la Nakuru yanavyoendeshwa zimekiukwa.

“Kukosekana kwa miswada ya kujadiliwa bungeni na ile iliyowasilishwa kutojadaliwa sasa ni jambo la kawaida katika Bunge la Kaunti ya Nakuru. Huu ni mtindo wa kutisha na ni ishara kwamba Kamati ya Masuala ya Bunge imetepetea,” akasema Karanja katika kauli iliyoungwa mkono na Kaimu Spika wa Bunge, Philip Wanjohi Nderitu (Lare) na Diwani wa Lanet/Umoja, Josphat Waweru Mwangi.

IMETAFSIRIWA NA: CHRIS ADUNGO

Gavana Roba na naibu wake watangaza kukatwa asilimia 30 ya mshahara

MANASE OTSIALO NA FAUSTINE NGILA

GAVANA wa Mandera Bw Ali Roba na naibu wake Bw Mohamed Arai wametangaza kuwa watakatwa mshahara kwa asilimia 30 kuanzia mwezi Aprili hadi Juni.

Bw Roba alisema kuwa pesa hizo zitatumika na maafisa wa kupambana na kuenea kwa virusi vya corona.

Kulingana na mkuu huyo wa kaunti, kupunguzwa kwa mishahara kama alivyofanya Rais Uhuru Kenyatta  hapo Jumatano kutasaidia Wakenya pakubwa katika nyakati hizi ngumu za kiuchumi.

“Kusisitiza agizo la rais na wito wa kujitolea kuchangia katika janga hili la corona, mimi na naibu wangu tumejitolea kukatwa asilimia 30 ya mshahara,” gavana huyo alisema mjini Mandera.

Aliongeza kuwa Kamati Simamizi ya Kaunti hiyo ilikutana na kupitisha uamuzi huo, ambapo pia wafanyakazi wa madaraja ya ajira ya T, S na R watakatwa mshahara.

Hofu ya walimu kuhusu mishahara yao na wanafunzi Covid-19 ikizidi kuhangaisha dunia

Na GEOFFREY ANENE

HUKU wazazi wakijipata wamegeuka kuwa walimu baada ya shule kufungwa kwa ghafla kutokana na janga la virusi vya corona kisa cha tatu kilipothibitishwanchini Kenya mnamo Machi 15, walimu wanaonekana kujawa na hofu masilahi yao yataathirika vibaya katika kipindi hiki kigumu.

Leo Alhamisi idadi jumla ya visa vya maambukizi imefikia wagonjwa 31 baada ya Waziri Msaidizi wa Afya Mercy Mwangangi kutangaza visa vitatu vipya vya wanawake wa umri wa kati ya miaka 30 na 61.

Katika mahojiano na walimu kadhaa, pia walikiri watalazimika kufanya kazi ya ziada hali ya kawaida itakaporejelewa ili kutimiza malengo waliyoweka kabla ya muhula wa kwanza kuanza.

Mwalimu Meshack Ambaisi wa shule ya msingi ya St Anne Junior School Lubao katika kaunti ya Kakamega anasema alikuwa amekamilisha masomo saba kati ya 11 aliyofaa kufundisha muhula huu. “Kifedha, kipindi hiki kimeathiri vibaya mapato yangu kwa sababu sitapata chochote mwezi huu. Hali itakuwa mbaya hata zaidi tusiporejea darasani hivi karibuni.”

Ambaisi, ambaye ni mwalimu wa hisabati na sayansi, anasema alishauri wanafunzi wake wafuata agizo la serikali la kukaa nyumbani wakati huu wasije wakaambuzikwa virusi hivyo, ambavyo vimetikisa dunia nzima.

Juddy kutoka shule ya msingi ya Smart Kids Angel Academy mtaani Kariobangi South jijini Nairobi ameambia ‘Taifa Leo’ kuwa hawakuwa wamemaliza robo ya masomo ya muhula huu.

“Muhula wa kwanza unajumuisha wiki 14. Tulikuwa katika wiki ya 11 kumaanisha kuwa hatukuwa tumekamilisha robo ya masomo ya muhula huu na pia kuyapitia tena.” “Bila shaka, kipindi ambacho hatujakuwa shuleni kitaathiri pakubwa malipo yetu,” anasema mwalimu huyo wa Kiingereza na Kiswahili.

Julius Otieno kutoka shule ya upili ya Buruburu Girls anasema, “Huwa tunasomesha masomo matatu kila muhula. Tulikuwa tumekamilisha masomo mawili. Ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona utakuwa na madhara makubwa katika kukamilisha silabasi. Itahitaji kazi ya ziada na pia ushirikiano kubwa ili kurejesha mfumo wa elimu unapofaa kuwa,” anasema.

Mwalimu huyo wa Kemia na Biolojia anasema alishauri wanafunzi wake kutumia mitandao kujinufaisha na masomo wakati huu ambapo shule zimefungwa. “Kuna mafunzo mengi kwenye mitandao ambayo itawasaidia. Mafunzo yanayotolewa na Tasisi ya Elimu nchini Kenya (KICD) kwenye redio pia itawasaidia pakubwa. Watumie muda wao vyema kwa sababu muda ni raslimali ambayo haiwezi kuongezwa,” anasema kabla ya kufichua kuwa wanafunzi wa shule hiyo walipewa kazi ya kufanyia nyumbani. “Tunawasiliana nao mara kwa mara kwa njia ya simu kujua wanavyoendea na masomo,” ameongeza.

Mwalimu wa shule za Nairobi Rabbani Group of Schools, Muchenya anasema walikuwa mbali sana katika kufikia malengo yao ya muhula wa kwanza.

“Tulifaa kukamilisha masomo manane, lakini kufikia wakati serikali ilitangaza kufunga shule, tulikuwa tumekamilisha angaa tatu hivi,” anasema Muchenya, ambaye aliongeza kuwa alishauri wanafunzi wake kutia bidii, hasa wanafunzi watakaofanya mtihani wa kitaifa baadaye mwaka 2020.

“Niliambia watahiniwa kuwa wazamie masomo yao wakisubiri mtihani wao wa mwisho.”

Kuhusu mshahara alisema: “Oooh! Mshahara wetu umeathirika na hali hii. Huenda tukapata nusu ya mshahara.”

Kevin Lugalia anayefundisha Kiingereza katika shule ya Upili ya St Anthony Kitale ni mmoja wa walimu wachache waliokuwa wamekamilisha sio tu masomo ya muhula, bali ya mwaka mzima.

“Mimi nafundisha Kiingereza katika kidato cha nne katika shule ya upili ya St Anthony Kitale. Sisi tulikuwa tumemaliza kufundisha masomo ya mwaka huu.”

Wafanyakazi wachafua jiji wakidai malipo ya miezi 3

SAMMY KIMATU na CECIL ODONGO

WAKAZI katika Kaunti ya Nairobi walipigwa na butwaa kufika katikati mwa jiji na kukuta jiji limegeuzwa kuwa jaa la taka Jumanne asubuhi.

Wengi wa waliokumbana na takataka hizo ni wale wanaorauka mapema asubuhi kwenda kununua bidhaa kutoka Soko la Gikomba, Muthurwa na pia soko la Wakulima linalofahamika na wengi kama Marikiti.

Waziri wa Mazingira wa Kaunti ya Nairobi, Bw Larry Wambua alikiri kwamba wazoaji taka hao hawajalipwa mishahara yao kwa miezi mitatu lakini hakufichua ni kiasi gani.

“Nafahamu kwamba mgomo huo umesababishwa na wafanyakazi kukosa kupokea mishahara kwa miezi mitatu. Hata hivyo, jukumu hilo ni la wizara ya fedha ambayo bado halina msimamizi,” akasema Bw Wambua.

Afisa Mkuu wa Mipango ya Kiuchumi wa Nairobi , Bw Washington Makodingo naye alilaumu idara ya mazingira, akisema haikuwasilisha orodha ya majina ya wanakandarasi wazoaji taka ili walipwe kwa wakati.

“Idara ya mazingira haifai kutulaumu kwa sababu wao ndio walikosa kutimiza wajibu wao,” akasema Bw Makodingo.

Asubuhi, wahudumu wa teksi na pia waendeshaji matatu walishuhudia kilichokuwa kikiendelea kati ya saa sita hadi za kumi asubuhi, ambapo taka hizo zilikuwa zikimwagwa.

Mfanyabiashara katika soko la Muthurwa ambaye hakutaka kutajwa jina, alisema malori ya kusafirisha taka yalitumika kueneza uchafu huo. Mama huyo anayeuza nyanya katika soko hilo, alisema kuwa malori hayo yalikuwa yakibeba takataka na kuzimwaga karibu na sehemu wanapouzia bidhaa zao.

“Kazi ya kuleta taka hapa ilikuwa ya malori yaliyopewa kandarasi na serikali ya Gavana Mike Sonko. Wanafanya hivyo kwa kukosa kulipwa kwa miezi mitatu,” mama huyo aliambia Taifa Leo.

Maeneo mengine ambapo pia taka zilimwagwa ni kituo cha mabasi cha Machakos, Soko la Retail, nje ya Soko la wakulima na mzunguko wa Haile selassie na barabara ya Landhies.

Kando na huko, sehemu nyingine za katikati mwa njiji pia zilikumbana na takataka hizo zilizotapakaa katika kituo cha mabas cha Bus Station, barabara ya Mfangano, Ronald Ngala, Kimathi Street, Uhuru Highway na Steji ya GPO.

Kilichowashangaza wengi asubuhi ni sababu ya takataka kusambazwa chini ya mapipa jijini, kabla ya kubaini mzozo unaoendelea.

“Watu hao hawakuwa wakiogopa kamera za CCTV zilizoko katikati mwa jiji wala kuogopa kukamatwa na polisi. Kuna wale tunajua ni wa Sonko wakichanganyikana mahasidi wake ili masaibu yake yaongezeke ndipo aonekane ni mbaya zaidi,” mlinzi katika jumba moja jijini aliambia Taifa Leo.

Wiki jana, Gavana Mike Sonko alitia saini mkataba na waziri wa Ugatuzi, Bw Eugene Wamalwa wa kupeana wizara nne kuu kutoka kwa kaunti na kuzikabidhi kwa serikali kuu. Mkataba huo ulifanyika katika Ikulu ya Nairobi na kushuhudiwa na Rais Uhuru Kenyatta.

Hatimaye vibarua Pumwani kulipwa mshahara wa miezi 4

Na Collins Omullo

NI afueni kwa vibarua wanaohudumu katika hospitali ya kujifungulia kinamama ya Pumwani, baada ya Kaunti ya Nairobi kusema kuwa mishahara yao ya miezi minne italipwa kufikia Alhamisi, wiki hii.

Akizungumza na waandishi wa habari, Washington Makodingo, Afisa Mkuu katika idara ya mipango ya kiuchumi alisema kuwa mnamo Jumatatu, kaunti hiyo ilitenga Sh8 milioni kutoka kwa mkaguzi wa bajeti, ambayo itatumika kulipa mishahara ya vibarua hao ambayo haijalipwa kuanzia Novemba, mwaka jana.

“Tulipata ombi la mishahara iliyochelewa kulipwa siku ya Ijumaa, wiki jana. Hata hivyo, tumetuma ombi kwa mkaguzi wa bajeti atoe angalau Sh8 milioni. Ombi letu likikubaliwa, tutalipa vibarua hao,” akasema Bw Makodingo.

Mnamo Jumatatu, vibarua na wauguzi wote walioathiriwa walikuwa na mgomo baridi huku wakiagiza serikali iwalipe mishahara yao iliyochelewa tangu Novemba, mwaka jana.

Katika barua moja iliyoandikwa Januari 31, 2020, Afisa Mkuu idara ya afya katika Kaunti, Mohamed Sahal aliomba msimamizi wa hospitali ya Pumwani kurefusha mkataba wa wafanyikazi 285 hadi Februari 31, 2020.

 

Vilio katika kaunti baada ya mishahara kucheleweshwa

Na WAANDISHI WETU

WAFANYAKAZI wa kaunti kadhaa wanateseka kwa kukosa mishahara tangu Desemba, huku wananchi wakikosa huduma muhimu kutokana na uhaba wa fedha.

Mwaka uliopita, Serikali Kuu ilisema haitatuma fedha kwa kaunti zinazodaiwa na wafanyabiashara hadi zimalize kulipa madeni.

Kaunti 28 ziliathirika na agizo hilo lililolenga kukomesha mtindo wa magavana wapya kukataa kulipia huduma zilizotolewa kwa kaunti zao wakati wa utawala uliotangulia.

Baadhi ya magavana wamekuwa wakijitetea kwamba hawaezi kulipia huduma au bidhaa ambazo zilitolewa kwa njia zilizokiuka sheria kwani watalaumiwa ikibainika kulikuwa na ufisadi.

Katika Kaunti ya Nandi, wafanyakazi wa bunge la kaunti hawajalipwa mishahara kwa miezi mitatu sasa. Spika wa bunge la kaunti hiyo, Bw Joshua Kiptoo alisema zaidi ya wafanyakazi 4,000 wanateseka kwani hawajalipwa tangu Novemba.

“Wengine wamefukuzwa katika nyumba walizokodisha na kuna baadhi ambao watoto wao wamefukuzwa shuleni kwani hawajalipiwa karo,” Katibu wa Chama cha Watumishi wa Umma, tawi la Nandi, Bw John Agaga akasema.

Katika Kaunti ya Kisii, zaidi ya wafanyakazi 6,000 waliambiwa mshahara wao wa Januari ungechelewa kwa kuwa Wizara ya Fedha ilichelewa kutuma pesa kwa kaunti hiyo.

Hali sawa na hii ilishuhudiwa katika Kaunti ya Trans Nzoia ambapo sasa wauguzi wametishia kususia kazi kwani hawajalipwa mishahara tangu Desemba.

Walisema suala la serikali kuu kuchelewesha pesa halifai kuwa sababu ya wao kutolipwa mishahara kwani wafanyakazi wa vyeo vya juu wanapokea malipo yao.

“Baadhi ya maafisa wakuu wanazidi kunenepa huku wanachama wangu wakikonda kwa ajili ya mahangaiko. Ni ukatili kwa maafisa hao kuendelea kushiba ilhali sisi tuna njaa,” akasema Katibu Mkuu wa Chama cha Kitaifa cha Wauguzi (KNUN), tawi la Trans Nzoia, Bw Willy Sifuna.

Wafanyakazi katika idara ya afya ya Meru pia walitishia kuanza mgomo wakisema serikali ya kaunti hiyo haijawasilisha ada mbalimbali zinazogharimu Sh38 milioni za Novemba na Desemba.

Ada hizo ni pamoja na mikopo ambayo wafanyakazi walichukua katika benki, hali inayotishia mali zao kupigwa mnada.

“Tetesi kwamba serikali ya kaunti itashauriana na mabenki kuhusu kuchelewa kulipa madeni halina msingi. Wanachama wetu wametuagiza tuitishe mgomo haraka iwezekanavyo,” akasema Mwenyekiti wa KNUN, tawi la Meru, Bw Bakari Munoru.

Wiki iliyopita, Waziri wa Fedha, Bw Ukur Yatani alisema kaunti ambazo zilikamilisha madeni yao niBaringo, Elegeyo Marakwet, Embu, Homabay, Kajiado, Kericho, Kilifi, Kitui, Kwale, Laikipia, Makueni and Nyamira, Nyandarua, Nyeri, Uasin Gishu na Lamu.

Kaunti nyingine tisa ambazo ni Nakuru, Taita Taveta, Tana River, Trans Nzoia, Machakos, Bungoma, Kakamega, Murang’a na Kisii zimepiga hatua vyema kulipa madeni.

Alisema Nandi, Marsabit, Kiambu, Meru, Kisumu, Tharaka-Nithi, Mombasa na Busia zimetoa mapendekezo kuhusu jinsi zitakamilisha madeni hayo kufikia Juni.

Kwa upande mwingine, kaunti za Turkana, Garissa, Wajir, Narok, Nairobi, West Pokot, Siaya, Kirinyaga, Bomet, Isiolo, Mandera, Samburu, Migori na Vihiga hazijapiga hatua.

Ripoti za Tom Matokeo, Sharon Achieng, Gerald Bwisa, David Muchui na Francis Mureithi

‘Asilimia kubwa ya mishahara ya wafanyakazi mijini huishia kwa mahitaji ya kimsingi’

Na MARY WANGARI

SERIKALI itahitajika kubuni sera mwafaka ili kuwezesha viwango vinavyofaa vya mishahara ya wafanyakazi wanaoishi mijini na katika sekta ya umma huku Kenya ikiorodheshwa miongoni mwa mataifa yenye viwango vya juu zaidi vya mishahara barani Afrika.

Kulingana na ripoti ya Benki ya Dunia, wafanyakazi nchini Kenya hulipwa mara mbili zaidi ya jumla ya uzalishaji (GDP) nchini, huku karibu asilimia 50 ikiishia katika kugharimia chakula, makao, na usafiri hasa kwa wanaoishi mijini.

Ripoti hiyo ambayo imejiri huku Wakenya wakisakamwa na ukosefu wa ajira na mishahara duni ilionyesha vilevile kwamba, katika kiwango chochote cha Jumla ya Uzalishaji Nchini (GDP), gharama ya mishahara ni ghali zaidi kwa viwanda vya uzalishaji barani Afrika.

Kutokana na hali hiyo, Kenya inakabiliwa na tishio la kukosa soko kimataifa katika sekta ya uzalishaji kutokana na viwango visivyofaa vya mishahara ya wafanyakazi nchini vinavyolemaza ushindani wa taifa hili katika soko la kimataifa.

Ripoti hiyo iliyozinduliwa kwa mara ya kwanza kuhusu Biashara kwa Maendeleo katika kizazi cha Misururu ya Thamani Ulimwenguni (GVC), ilitaja viwango vya juu kupindukia vya ubadilishanaji wa hela kama kiini mojawapo cha mishahara hiyo ghali.

Katika kukabiliana na tatizo hilo, Benki ya Dunia inapendekeza kurekebisha sera kali za kudhibiti leba pamoja na kuhakikisha ulinzi wa wafanyakazi.

“Ili kupata kiwango kinachofaa cha mishahara panahitajika sera zinazopita kiwango cha leba ili kuimarisha huduma za mijini na umma. Serikali pia ni sharti ziangazie vikwazo vingine vinavyolemaza mazingira ya uwekezaji kama vile miundomsingi duni na ujuzi, vinavyoongeza gharama ya mishahara kwa kulemaza ukuaji wa uzalishaji. Huku mataifa yakilenga kujiboresha katika GVC, vigezo vya sera vinavyopatiwa kipaumbele vinaegemea ubora badala ya wingi wa wafanyakazi. Uzalishaji bora unahitaji ujuzi wa hali ya juu na uzoefu,” alisema Rais wa Benki ya Dunia David R. Malpass, kupitia ripoti hiyo.

Utafiti huo uliohusisha kampuni 5,500 kutoka mataifa 29 ulidhihirisha kwamba katika viwango vyovyote vya GDP, gharama ya leba ni ghali zaidi kwa viwanda vya uzalishaji barani Afrika isipokuwa tu Uhabeshi iliyo na viwango vinavyofaa vya mishahara.

Aidha, ripoti hiyo ilisema kuwa, kutokana na gharama ya juu ya leba, mataifa barani Afrika huongeza bei ya rasilimali zake ili ziambatane na bei ya bidhaa zinazoagizwa kutoka nje.

Hatua hii huwa kikwazo kwa wawekezaji wa kimataifa wanaomiliki viwanda vinavyohitaji wafanyakazi wengi huku wawekezaji kutoka Kenya wakilazimika kuagizia bidhaa kutoka nje ili kufidia bei ghali ya mishahara katika mataifa yao.

Maadamu wawekezaji wa kimataifa hupendelea mataifa yenye usawa kati ya mishahara na kazi inayofanywa, Kenya huenda ikajipata mashakani katika kuvutia bidhaa kwenye soko la kimataifa endapo suala la viwango vya mishahara halitaangaziwa.

Kulingana na Benki ya Dunia, tatizo hili la viwango vya mishahara huathiri zaidi mataifa yanayoegemea rasilimali asilia na kugeuka tishio baada ya mataifa haya kuhamia katika misururu ya kimsingi ya thamani ya uzalishaji.

“Ni muhimu kuwa na usawazishaji. Tofauti hiyo haipo tu katika viwango vya mishahara bali pia malipo kuhusiana na GDP. Ni muhimu kuiga mataifa mengine katika viwango sawa vya maendeleo kama vile Uhabeshi na Bangladesh,” alisema Mtaalam Mkuu wa Masuala ya Kiuchumi katika Benki ya Dunia Pinelopi Goldberg.

Aibu ya mashirika kulipa walinzi Sh4,000

NA MARY WAMBUI

IMEBAINIKA kuwa mashirika mengi ya kiserikali huwalipa walinzi wa kibinafsi mshahara wa chini ya Sh27,000 ilhali kiwango kinachopendekezwa kisheria kinazidi kiasi hicho.

Kwa wastani, mashirika ya serikali ambayo yalitoa kandarasi kwa kampuni zinazotoa huduma za ulinzi, mara nyingi hulipa kila mlinzi kati ya Sh13,000 hadi Sh27,840 kwa mwezi.

Baada ya makato mengi kwenye pesa wanazolipwa, imebainika walinzi wengi huishia kutia mfukoni Sh4,000 pekee.

Hata hivyo, mashirika ya NCPB, KPLC, KR na KPLC ni kati ya yale yanayolipa vizuri, hii ikiwa ni Sh27,840, Sh26,100, Sh24,844 na Sh24,360 mtawalia.

Walinzi katika Shule ya Upili ya St Thomas Acquinas, Kitui, St Monica Girls Kitui, Shirika la Nyayo Tea Zone na Chuo Kikuu cha JKUAT ndio hulipwa vibaya kwa kuwa kila mwezi wao hupata Sh12,000, Sh13,000, Sh14,000 na Sh15,000 mtawalia.

Huku makataa ya kutekelezwa kikamilifu kwa sheria zinazoongoza sekta ya walinzi wa kibinafsi zilizopitishwa na bunge yakikaribia, mashirika haya ya serikali sasa huenda yakakumbatia Shirika la Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS) ambalo hutoa huduma kwa gharama ya chini mno.

Mkurugenzi wa NYS Matilda Sakwa alisema fedha ambazo hulipwa na mashirika ya serikali huelekezwa kwa shirika hilo, hii ikiwa na maana kwamba pesa anazolipwa kila mlinzi huwa haziongezeki.

Kaunti zajitahidi kulipa wafanyakazi mishahara

Na WAANDISHI WETU

SERIKALI za kaunti katika eneo la Kaskazini mwa Bonde la Ufa Jumanne zilizuia kufanyika kwa mgomo wa wafanyikazi kwa kuahidi kuwalipa wiki hii.

Ahadi hiyo ilifuatia majadiliano kati ya maafisa wa kaunti husika na wale wa muungano wa wafanyakazi.

Katibu wa muungano huo wa wafanyakazi Joseph Cheruiyot alifichua kuwa usimamizi wa kaunti umeanza shughuli ya kuwalipa wafanyakazi kufikia kesho.

Kwenye makubaliano hayo, kaunti zitalipa mishahara ya Julai katika muda wa siku mbili zijazo.

Kaunti hizo ni Uasin Gishu, Elgeyo Marakwet na Baringo.

Nazo zile za Nandi, Trans Nzoia na Turkana ziliwalipa wafanyakazi wao wiki iliyopita.

Mishahara hiyo imechelewa kutokana na mvutano kati ya Bunge la Kitaifa na Seneti kuhusu Mswada wa Ugavi wa Mapato 2019.

Gavana wa Kaunti ya Elgeyo Marakwet, Alex Tolgos alikutana na waakilishi wa muungano wa wafanyakazi na kufanya mkataba kuhusu malipo ya mishahara iliyocheleweshwa.

Aliahidi kufanya malipo hayo kabla ya mwisho wa wiki hii.

Katibu wa Tawi la Muungano wa Kitaifa wa Wauguzi, Patrick Biwott, aliwahimiza magavana kulipa mishahara ili kuwakinga wafanyakazi dhidi ya changamoto zaidi za kifedha.

Serikali ya Kaunti Baringo pia iliahidi kufanya malipo hayo wiki hii.

Uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo ulifichua kwamba shughuli zilikuwa zikiendelea vyema katika hospitali ya rufaa ya Kaunti ya Baringo na idara nyinginezo.

Katika eneo la Uasin Gishu, kaunti ilifanya mkataba na wafanyikazi ikiahidi kuwalipa.

Hofu mgomo wa watumishi wa kaunti ukinukia

DERICK LUVEGA na BENSON AMADALA

VIONGOZI wameeleza hofu yao kuhusu mgomo wa wafanyakazi wa kaunti ambao umepangiwa kuanza Jumanne.

Kiongozi wa chama cha ANC Musalia Mudavadi amewataka wabunge na maseneta kuandaa mazungumzo ili kusuluhisha utata kuhusu mswada wa ugavi wa mapato ili wafanyakazi wa kaunti walipwe mshahara wao wa mwezi Julai ndipo wafutilie mbali mgomo huo unaotarajiwa kukumba karibu kaunti zote 47.

“Naomba Bunge la Kitaifa na lile la Seneti kuandaa mazungumzo na kusuluhisha utata kuhusu mswada wa ugavi wa mapato. Jinsi tunavyoendelea na tofauti hizi ndivyo wafanyakazi wa kaunti wanavyoendelea kuumia,” akasema Bw Mudavadi.

Huku Bunge la Kitaifa likipigia upatu mswada unaopendekeza mgao wa Sh316 bilioni kwa kaunti, Bunge la Seneti limeshikilia kwamba kiasi hicho lazima kiwe Sh335 bilioni liwalo na liwe.

Ishara ya mgomo ilianza wiki jana baada ya Muungano wa Wafanyakazi wa Kaunti nchini kutangaza kuwa wanachama wao wataanza mgomo leo iwapo hawatakuwa wamelipwa mshahara wao wa Julai.

Mnamo Jumamosi, Mwenyekiti wa Baraza la Magavana Wycliffe Oparanya aliwakashifu wabunge kwa kuhujumu utendakazi wa kaunti baada ya kukataa kupitisha mswada wa bunge la seneti unaopendekeza nyongeza kwenye mgao wa fedha zilizotengewa serikali za ugatuzi mwaka huu.

Huku Seneti na Bunge la Kitaifa zikiendelea kushikilia misimamo yao mikali, sekta ya afya ndiyo itakayoathirika zaidi iwapo Muungano wa Kitaifa wa Wauguzi (KNUN) utawatangazia wanachama wao waanze mgomo.

Rais Uhuru Kenyatta naye mwezi uliopita alisema serikali haina pesa za kuongezea kaunti huku magavana nao wakielekea Mahakama ya Juu kupata suluhu kwa zogo la ugavi wa mapato kati ya seneti na bunge la kitaifa.

Akizungumza kwenye hafla tofauti, Gavana wa Vihiga Dkt Wilber Ottichilo alieleza hofu yake kwamba wauguzi katika kaunti hiyo wataandaa mgomo baada ya kukamilika kwa notisi waliyotoa kwa utawala wake.

Alidai kuwa hii inatokana na kucheleweshwa kwa mshahara wao wa mwezi jana.

“Wauguzi wametishia kuandaa mgomo kuanzia kesho iwapo hawatakuwa wamelipwa mshahara wao. Iwapo hili litatokea basi watu wetu watafariki. Nawaomba wabunge wakubaliane na kupitisha mswada wa ugavi wa mapato,” akasema Dkt Otichillo ambaye alifunguka na kusema kuwa hakuna hata mfanyakazi mmoja wa kaunti yake ambaye amepokea mshahara wa mwezi Julai.

Mbunge wa Nambale, Bw John Sakwa Bunyasi naye aliwasihi wabunge wenzake kumaliza utata kuhusu mgao wa fedha kwa kaunti 47.

“Hizi ni pesa za umma na si za magavana. Naomba tugawe fedha hizi kwa ajili ya miradi ya maendeleo,” akasema Bw Bunyasi alipohudhuria hafla ya umma mjini Vihiga.

Katibu wa KNUN tawi la Vihiga Caleb Maloba alisema wauguzi wamepoteza motisha ya kufanya kazi na wako tayari kuandaa mgomo kudai haki yao.

“Hatutaendelea na mazungumzo yoyote. Tumekuwa na subira ilhali wanachama wetu wanaumia. Iwapo hawatakuwa wamelipa, tutaanza mgomo wetu,” akasema Bw Maloba.

Gavana kikaangoni kutumia fedha zaidi kulipa mishahara

Na CHARLES WASONGA

SERIKALI ya kaunti ya Siaya inayoongozwa na Gavana Cornel Rasanga jana ilielekezewa lawama kwa kutumia pesa kuliko inavyohitajika kisheria, kugharimia ulipaji wa mishahara ya wafanyakazi huku miradi ya maendeleo ilitengewa mgao finyu.

Taarifa ya matumizi ya fedha ya kaunti hiyo katika mwaka wa kifedha wa 2017/2018 iliyowasilishwa mbele ya Kamati ya Seneti kuhusu Uhasibu wa Pesa za Umma (CPAIC) ilionyesha kuwa kaunti hiyo ilitumia asilimia 41 ya mapato yake kwa mishahara huku miradi ya maendeleo ikitengewa asilimia 17 pekee.

“Stakabadhi zilizoko mbele yetu zinaonyesha kuwa serikali ya Siaya ilitumia asilimia 41 ya mapato yake kulipia mishahara ya wafanyakazi, asilimia 12 ikatengewa Bunge la Kaunti na asilimia 30 ikatumika katika operesheni za kawaida. Hii ina maana kuwa ni asilimia 17 pekee zilitengewa miradi ya maendeleo badala ya asilimia 30 inavyohitajika kisheria,” akasema mwenyekiti wa kamati hiyo Moses Kajwang’.

Kulingana na sheria ya usimamizi wa fedha za umma (PFM Act) kaunti zinapasa kutumia asilimia 31 pekee ya mapato yao kugharimia mishahara ya wafanyakazi.

Gavana huyo alikabiliwa na wakati mgumu kutetea matumizi ya Sh351 milioni kulipia mishahara ya wafanyakazi katika mwaka huo wengi wao wakiwa nje ya orodha rasmi ya malipo ya wafanyakazi.

“Tunashuku kuwa huenda baadhi ya wafanyakazi hawa, haswa wale walioorodheshwa kama vibarua ni hewa kwa sababu wengi wana akaunti za benki nje ya kaunti ya Siaya. Orodha hii inaonyesha kuwa baadhi yao wamefungua akaunti katika matawi ya benki zilizoko katika miji ya Kisumu na Busia, ishara kwamba huenda ni wafanyakazi bandia,” akasema Seneta wa Kiambi Kimani Wa Matang’i.

Wanachama wa kamati ya CPAIC walilalamika kuwa licha ya kaunti ya Siaya kupokea Sh5.8 bilioni kama mgao kutoka hazina ya kitaifa na kukusanya Sh700 milioni kama ushuru na ada nyinginezo katika mwaka wa kifedha wa 2017/2018 haikutenga asilimia 30 ya fedha hizo kwa miradi ya maendeleo.

Seneta Fatuma Dullo (Isiolo) alihoji hatua ya serikali ya Gavana Rasanga kuajiri wafanyakazi wengi vibarua katika Idara za Mazingira na Usafi na ile ya Afya kuliko idara nyinginezo, akisema huenda hatua hiyo ilichukuliwa kimakusudi kutoa nafasi ya wizi wa fedha za umma.

Madiwani Kiambu wafuata ulafi wa wabunge

NA ERIC WAINAINA

MADIWANI katika Kaunti ya Kiambu wameshangaza Wakenya kwa kutenga zaidi ya Sh100 milioni kugharimia vikao vya umma kuhusu miradi mbalimbali kwenye bajeti iliyoidhinishwa na Gavana Ferdinand Waititu.

Kwenye bajeti hiyo, bunge la kaunti limetenga jumla ya Sh1.3 bilioni kwa matumizi ya jumla ya mwaka wa kifedha wa 2019/2020.

Kupitia afisi mpya iliyobuniwa ya Hazina ya Ushirikishaji wa Umma, kila diwani kati ya wawakilishi wadi 60 waliochaguliwa ametengewa Sh108,000 kila mwezi kufadhili mikutano ya umma katika afisi zao za wadi.

Hii ina maana kwamba kila diwani atapata Sh1.3 milioni kila mwaka kufadhili mikutano hiyo kulingana na bajeti hiyo.

Kisheria majukumu ya madiwani ni uwakilishi, kutunga sheria na kukosoa serikali ya kaunti inapohitajika kufanya hivyo.

Madiwani wateule, ambao idadi yao ni 32, nao hawataachwa mikono mitupu kwa kuwa watagawanya Sh14 milioni kutoka kwa Hazina ya Ushirikishaji wa umma kwa madiwani walioteuliwa.

Hii ina maana kuwa kila diwani aliyeteuliwa, ambao wengi wao ni wanawake waliopewa nyadhifa hizo ili kutimiza usawa wa kijinsia, atapokea Sh437,000 kwa mwaka.

Kwa kuwa hakuna sheria inayoruhusu matumizi hayo, maswali sasa yameibuka kuhusu uhalali wa hazina hiyo ikizingatiwa kwamba mikutano ya kushirikisha umma kuhusu maswala ya kaunti huwa haiandaliwi kila mwezi.

Hata hivyo, Kamati ya Bajeti la Bunge la Kaunti inayoongozwa na Diwani wa Kiu, Dan Ngugi na Naibu wake Nduta Muongi (mteule) walipendekeza sheria ibuniwe ya kuhalalisha matumizi hayo ili kuzima malalamishi yatakayoibuka.

Gharama ya matumizi ya kaunti pia inatarajiwa kuongezeka baada ya madiwani kujitengea Sh180 milioni kwa safari za ndani ya nchi huku Sh28.8 milioni zikitengewa kufadhili ziara zao nje ya nchi.

Dalili za matumizi haya ya kushangaza zilianza kuonekana mapema pale Karani wa bunge, Joseph Ndirangu alipofika mbele ya kamati ya kuandaa bajeti na kulalamika kwamba bunge hilo limekuwa likitengewa pesa kidogo kwenye bajeti, hali aliyodai inasababisha bunge hilo kutoweza kutekeleza majukumu yake kikamilifu.

Hatua ya madiwani wa Kiambu kijitengea kiasi kikubwa cha pesa kwenye matumizi yasiyo na umuhimu kwa wananchi, inafuata ile ya Bunge la Kitaifa ambapo wabunge wamependekeza kujiongezea mishahara kutoka Sh1.1 milioni kila mwezi hadi Sh2.9 milioni.

Magavana kuandamana kupinga wabunge kujiongezea hela

NA SHABAN MAKOKHA ALEX NJERU na CHARLES WASONGA

MAGAVANA na maseneta wametishia kuandamana katika Bunge la Kitaifa Jumatatu kulalamikia mvutano unaozingira kiasi cha fedha zinazopasa kutengewa serikali za kaunti.

Magavana hao walisema wataandamana katika majengo ya bunge, Nairobi kutaka wabunge waeleze sababu ya kupinga nyongeza ya fedha kwa serikali za kaunti.

“Tutaungana na maseneta katika maandamano hayo Jumatatu kuonyesha kuwa ugatuzi unauawa na Bunge la Kitaifa,” akasema Gavana wa Bungoma Wycliffe Wangamati.

Alikuwa miongoni mwa magavana saba waliokutana mjini Kakamega Ijumaa kuhudhuria sherehe ya uzinduzi wa mpango wa kuwapiga jeki kiuchumi vijana na wanawake katika kaunti hiyo.

Magavana hao walilalamikia mvutano kati ya maseneta na wabunge kuhusu suala hilo na ambao ulikwamisha kupitishwa kwa mswada huo kabla ya kusomwa kwa bajeti ya mwaka wa kifedha wa 2019/2020.

Wengine walioungana na Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya katika sherehe hiyo ni Paul Chepkwony (Kericho), Prof Anyang’ Nyong’o (Kisumu), Cornel Rasanga (Siaya), Ali Roba (Mandera) na Mwangi wa Iria (Murang’a).

Walidai Bunge la Kitaifa linatumiwa na Serikali Kuu kuhujumu utekelezaji wa ugatuzi.

“Kile tunachoshuhudia sasa ni sawa na kilichotendeka 1966 serikali kuu ilipoua utawala wa majimbo,” alisema Bw Wangamati ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Rasilmali katika Baraza la Magavana (CoG).

Bunge la Kitaifa na Hazina ya Kitaifa, zinapendekeza kuwa serikali za kaunti zigawiwe Sh310 bilioni katika mwaka huu wa kifedha huku Seneti na Tume ya Ugavi wa Mapato (CRA) zikipendekeza mgao wa Sh335 bilioni.

Bw Oparanya ambaye ni Mwenyekiti wa CoG alisema huenda shughuli katika kaunti zikakwama na hata zikakosa pesa za kuwalipa wafanyakazi ikiwa mvutano huo hautatatuliwa.

Wakati huo huo, Naibu Rais William Ruto amewashauri magavana kushiriki mazungumzo kutatua mvutano kuhusu Mswada wa Ugavi wa Mapato (DoRB) badala ya kwenda kortini huku magavana na maseneta wakipanga kufanya maandamano kesho kuhusu suala hilo.

Kuria akataa marupurupu, aamuru pesa hizo zipelekwe Hospitali ya Gatundu

Na CHARLES WASONGA

MBUNGE wa Gatundu Kusini Moses Kuria Jumanne aliagiza usimamizi wa bunge kuelekeza pesa ambazo angelipwa kama marupurupu ya malazi kwa Hospitali ya Wilaya ya Gatundu.

Kwenye barua aliyomwandikia Karani wa Bunge la Kitaifa Michael Sialai Jumanne Bw Kuria alisema kuwa hatapokea sehemu yoyote ya pesa hizo zinazopendekeza kulipwa wabunge.

“Marupurupu haya hayana maana yoyote. Naishi katika nyumba yangu Nairobi na siwezi kushawishi familia yangu kuhusu ni kwa nini walipa ushuru wanapaswa kunilipa ili niwe mbali nao,” sehemu ya barua yake iliyoonekana na Taifa Leo Dijitali ilisema.

Bw Kuria pia aliweka nakala ya barua hiyo katika ukurasa wake wa Facebook.

Akaendelea kusema: “Naamuru kuwa ikiwa sharti nilipwe marupurupu, bunge lielekeze pesa hizo kwa Hospitali ya Wilaya ya Gatundu katika muda wote unaosalia katika kipindi change cha kuhudumu katika bunge la 12.”

Ufichuzi kwamba kuna mipango ya wabunge kulipwa takriban Sh24,000 kila siku kama marupurupu ya malazi katika siku ambazo wao huhudhuria vikao vya bunge umeibua kero kubwa miongoni mwa Wakenya.

Lakini mnamo Jumapili, Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi alitetea marupurupu hayo akisema yataimarisha moyo wa utendakazi wa wabunge kuwa kuwatia shime kuhudhuria vikao vya bunge.

Mnamo Jumatano iliyopita, wabunge walipitisha Mswada wa Huduma za Bunge inayopendekeza walipwe marupurupu kadhaa, yakiwemo ya malazi wakiwa Nairobi kuhudhuria vikao vya bunge ya kati ya Sh18,000 hadi Sh24,000 kila wiki.

Mswada huo sasa unasubiri kuwatiwa saini Rais Uhuru Kenyatta na hivyo kutoa nafasi kwa wabunge kufurahia mafao mengine kando na marupurupu kadha.

Ubunge umenifanya nitafunwe na uchochole, alia Otiende Amollo

MARY WANGARI Na ANITA CHEPKOECH

MBUNGE wa Rarieda Otiende Amollo Jumanne ameibua ghadhabu mitandaoni baada ya kutangaza kwamba tangu achaguliwe mbunge amekuwa maskini hohehahe licha ya kupokea mshahara wa Sh621,000.

Bw Omollo alisema kwamba tangu alipochaguliwa hajawahi kununua chochote kutokana na uchochole.

Alikuwa akizungumza katika kipindi cha AM Live cha NTV mnamo Julai 9 wakati wa mjadala kuhusu hatua ya wabunge hivi majuzi ya kujiongezea mishahara iliyoibua hisia kali miongoni mwa Wakenya.

Nimekuwa mwenyekiti wa tume ya kupokea malalamishi na pia nimekuwa katika uanasheria usio wa kiserikali. Sijawahi kuwa fukara jinsi nilivyo kama mbunge,” alisema, akiongeza kwamba yeye hupata Sh500,000 licha ya kutokuwa na mkopo wa nyumba.

“Nilipochaguliwa, tayari nilikuwa na nyumba yangu jijini Nairobi, lakini tangu nilipotwaa mamlaka sijanunua nyumba, sijanunua chochote.”

Mwanasiasa huyo alidai kwamba wabunge hutumia mapato yao katika maeneo bunge yao.

Wabunge hupokea kiasi cha Sh250,000 kama marupurupu ya nyumba na wanataka waongezwe marupurupu ya “usiku” kwa jina “Fedha za Matumizi ya Kinyubani” ambapo watapata kati ya Sh18,200 na Sh24,000 kila siku.

Mbunge huyo aliyeonekana kukereka alisema hajawahi kushiriki kikao ambapo wabunge waliitisha nyongeza ya mishahara akisema ilikuwa kazi ya Tume ya Bunge (PSC) katika juhudi za kuwaokoa wanasiasa maskini.

Kulingana na mbunge huyi wa ODM, ripoti za vyombo vya habari za kila mara zilizowasawiri wabunge kama waroho zilisinya na hazikuwa za haki.

“Ukichukua mkopo wa nyumba kwa Sh20 milioni huwezi kuchukua mkop wa gari kwa sababu kiwango kinachokatwa mshahara ni cha juu kwa sababu ya muda mfupo wa kulipa. Nina hakika kuna baadhi ya wenzangu ambao wamechukua mkopo na wanapata sufuri mwisho wa mwezi,” alifafanua  Bw Amollo.

“Hii ndiyo mara ya mwisho nitakayozungumzia swala hili,” alisema.

Wanasiasa wengine wakiwemo Seneta wa Kiambu Kimani Wamatangi, Seneta wa Kericho Aaron Cheruiyot na aliyekuwa Mbunge wa Gem  Jakoyo Midiwo pia walitetea hatua ya kutaka nyongeza ya mshahara huku aliyekuwa Seneta wa Kakamega Boni Khalwale akipinga.

Seneta Wamatangi alifichua yeye hupokea Sh640 pekee baada ya mshahara wake kukatwa.

Mikopo wanayochukua wabunge hukatwa kwenye mishahara yao. Nakala yangu ya malipo sasa imeandikwa Sh640 baada ya kukatwa mishahara.

“Ikiwa sikuwa na biashara, watoto wangu wangeishi katika nyumba lakini hawangekula,” alisema.

Kwa upande wake Seneta Cheruiyot alishangaa wanachofaidika nacho wanahabari baada ya “kuwasawiri vibaya wabunge.”

“Suala tu lenye utata kwa sasa ni kuhusu marupurupu ya nyumba. Leo hii mfanyakazi wa serukali akienda Nakuru watalipwa marupurupu ya kuwastawisha, hakuna kitu ambacho tumewalipa wabunge ambacho hakijalipwa wafanyakazi wengine wa umma,” alisema Bw  Cheruiyot.

Bw Midiwo alisema: “Tatizo la gharama kubwa ya mishahara nchini halitasuluhisha kwa kuondoa mishahara ya watu, linaweza kutatuliwa kwa kukata nyama iliyooza.”

Serikali yatetea SRC dhidi ya vitisho vya wabunge

Na VALENTINE OBARA

SERIKALI Kuu imetetea Tume ya Mishahara na Marupurupu (SRC) dhidi ya wabunge wanaotaka kupunguzia tume hiyo fedha za kuendeleza shughuli zake mwaka huu.

Waziri wa Fedha, Bw Henry Rotich amesema SRC ina jukumu muhimu katika kusaidia serikali kupunguza gharama ya mishahara ya watumishi wa umma iliyopita Sh730 bilioni mwaka uliopita, ili fedha zitumiwe zaidi kwa miradi ya maendeleo na kuboresha utoaji huduma kwa wananchi.

Akizungumza Alhamisi wakati tume hiyo ilipozindua mwongozo wa utendakazi wake katika kipindi cha mwaka wa 2019 hadi 2024 jijini Nairobi, Bw Rotich alisema majukumu ya kikatiba ya SRC hayafai kutatizwa.

Majukumu hayo yanajumuisha kuhakikisha gharama ya mishahara ya watumishi wa umma si ya juu kupita kiasi, na watumishi wa umma wanalipwa mishahara inayolingana na kazi wanazofanya.

“Ninawahakikishia kwamba tutashauriana na bunge wakati wote ili mpate rasilimali zote mlizotengewa kufanya kazi yenu,” akasema Bw Rotich.

SRC inayosimamiwa na Bi Lyn Mengich ilipata pigo wiki iliyopita wakati Bunge la Taifa lilipoipunguzia bajeti yake kwa Sh95 milioni. Wakati huo, tume hiyo ilikuwa imetengewa Sh545.4 milioni kwenye bajeti na kabla ya hapo, ilikuwa imetengewa Sh645.4 milioni kabla wabunge kukata kiwango hicho kwa Sh125.6 milioni.

Hatua hizo zilionekana kama njia ya wabunge kulipiza kisasi kwa jinsi SRC ilivyopinga mahakamani uamuzi wao wa kujilipa marupurupu ya nyumba ya Sh250,000 kila mwezi.

Mojawapo na mikakati inayolengwa kutekelezwa na SRC kupunguzia Wakenya gharama ya kulipa mishahara ni kama vile kuajiri watumishi wa umma kwa kandarasi kabla kuamua iwapo wanastahili kupandishwa vyeo kwa kuzingatia utendakazi wao.

Bw Rotich alitaka tume hiyo ihakikishe mikakati yoyote itakayotumiwa kupunguza gharama ya mishahara ifanywe kwa njia ambayo haitaepusha wataalamu wenye ujuzi wa hali ya juu kutafuta kazi serikalini wakihofia hawatalipwa vyema.

“Mapendekezo yatahitaji kuhakikisha tunapopunguza gharama ya mishahara, bado serikali itaendelea kuvutia na kudumisha watumishi wa umma wenye utaalamu wa hali ya juu. Mataifa yaliyofanikiwa kutekeleza mfumo aina hii yalilazimika kuchukua hatua kali hasa katika kubadilisha muundo wa serikali na mashirika ya umma,” akasema.

Alitoa wito kwa wizara zote na mashirika ya umma kushirikiana na SRC ili kufanikisha malengo yake ndipo serikali ipate fedha za kutosha kutekeleza mipango ya maendeleo.

Walimu waunga mkono wabunge SRC ivunjwe

Na MWANDISHI WETU

CHAMA cha Kitaifa cha Walimu (KNUT) kinataka Tume ya Mishahara ya Watumishi wa Umma (SRC) ifutiliwe mbali.

Kulingana na Katibu Mkuu wa KNUT, Wilson Sossion, ambaye pia ni Mbunge Maalum, SRC inaleta utata na hali ya kutoelewana kwenye mashauriano kuhusu mishahara kati ya vyama vya wafanyikazi na waajiri.

“SRC inapasa kufutiliwa mbali ili kuokoa pesa za umma kwani kuwepo kwake kunaleta utata kati ya waajiri na wafanyikazi,” akasema Bw Sossion kwenye ujumbe wake kwa Kongamano la Kitaifa la Walimu Wakuu wa Sekondari (KESSHA) linaloanza Jumatatu jijini Mombasa.

SRC pia inakabiliwa na shinikizo kutoka kwa wabunge ambao wamekasirishwa na hatua yake kupinga malipo yao ya marupurupu ya nyumba ya Sh250,000 kila mwezi.Kulingana na Bw Sossion, Hazina Kuu ndiyo inayopaswa kuchukua jukumu la kusimamia masuala ya mishahara ya walimu, lakini mikataba ya malipo iendelee kuwa kati ya vyama vya walimu na Tume ya Kuwaajiri Walimu (TSC).

Bw Sossion pia amependekeza kuanzishwa kwa jopo kushughulikia masuala ya kinidhamu ya walimu pamoja na masuala mengine kama vile kusajili walimu, kuidhinisha vyuo vya mafunzo ya walimu, kusimamia udumishaji wa ubora wa masomo miongoni mwa mapendekezo mengine.

Naye Mwenyekiti wa KESSHA, Bw Indimuli Kahi anataka Serikali kuongeza mgao wa karo inayolipia wanafunzi katika shule za umma kwenye mpango wa Elimu Bila Malipo (FSE) akisema bei ya bidhaa imeongezeka kwa kiwango kikubwa.

“Mgao tunaopata uliwekwa 2014 lakini hautoshi kutokana na gharama ya juu ya maisha. Tunahimiza Serikali itathmini upya mgao huo ili kuhakikisha unatosheleza mahitaji,” akasema Bw Indimuli kwenye ujumbe wake kwa wanachama.

Mwenyekiti huyo alieleza kuwa shule nyingi zinakabiliwa na matatizo ya uhaba wa miundomsingi hasa madarasa na vyumba vya malazi, hali ambayo imesababisha misongamano mikubwa katika shule hizo.

Alieleza kuwa hali hii imetokana na kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi waliojiunga na Kidato cha Kwanza mwanzoni mwa mwaka huuu. Aliomba Serikali kuchukua hatua za haraka kusaidia ujenzi wa madarasa, vyumba vya malazi na mijengo mingine muhimu kwa mafunzo.

Kuhusu mfumo mpya wa elimu, Bw Indimuli alisema walimu wakuu wanataka Serikali ianze kuandaa shule za upili kwa ajili ya kutekeleza mtaala mpya wakati wanafunzi watakapokuwa wakiingia sekondari.

“Tunahimiza Wizara ya Elimu kuanza kuandaa shule za sekondari kwa ajili ya kutekeleza mtaala mpya kwa kuangazia vifaa na mafunzo ya walimu wanaohudumu kwa sasa na walio vyuoni,” akasema Bw Indimuli.

ULAFI: Wabunge watisha kuteka nchi wakipigania matumbo yao

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE na maseneta Alhamisi waliitaka Tume ya Kukadiria Mishahara na Marupurupu (SRC) ikubali waendelee kulipwa marupurupu ya nyumba ya Sh250,000 kila mwezi la sivyo wakatae kupitisha bajeti ya mwaka huu.

Waliamua kupambana mahakamani hadi amri iliyotolewa wiki jana ya kuzima malipo hayo itupiliwe mbali.

Walisema ni haki yao kisheria na kikatiba kulipwa pesa hizo sawa na maafisa wengine wakuu serikalini, wakiongeza kuwa SRC inafaa kuondoa kesi iliyowasilisha mahakamani kuzima malipo hayo.

Wabunge ambao tulizungumza nao baada ya mkutano wao wa faragha Alhamisi, walisema kuwa tayari fedha za kugharamia malipo ya marupurupu hayo zimetengwa kwenye bajeti ya Tume ya Huduma za Bunge (PSC) mwaka huu.

Mkutano huo, usio rasmi, uliongozwa na Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi na mwenzake wa Seneti Kenneth Lusaka.

“Marupurupu yetu ya nyumba tayari yamejumuishwa katika bajeti ya mwaka wa kifedha wa 2019/2020 ambao unaanza Julai 1, 2019. Kwa hivyo, malipo hayo hayataathiri mipango ya serikali kwa njia yoyote,” akasema mbunge mmoja ambaye aliomba tulibane jina lake kwa sababu walikubaliana katika “kamukunji” hiyo kutofahamisha wanahabari mambo waliyojadili.

Asasi ya bunge imetengewa Sh36.6 bilioni katika bajeti ijayo ambayo itasomwa na Waziri wa Fedha Henry Rotich kabla ya tarehe 20, mwezi huu.

“Ikiwa maafisa wa serikali kama vile mawaziri na makatibu wa wizara hupokea marupurupu ya nyumba, mbona sisi tunyimwe? Tumeamua kwa kauli moja kwamba PSC itaendelea kutulipa pesa hizo licha ya kesi inayoendelea mahakamani,” akasema.

Wiki jana, mahakama kuu iliiagiza tume ya PSC kutoendelea kuwalipa wabunge na maseneta 416 marupurupu hayo hadi kesi iliyowasilishwa na SRC itakaposikilizwa na kuamuliwa.

Vilevile, SRC chini ya mwenyekiti wake Bi Lyn Mengich inaitaka mahakama kuu kuamuru kwamba wabunge hao warejeshe fedha ambazo tayari wamelipwa kama marupurupu ya nyumba kwani hatua hiyo ni kinyume cha sheria.

Tume hiyo inashikilia kuwa ndiyo yenye mamlaka ya kukadiria na kuidhinisha mishahara na marupurupu yote ya maafisa wa serikali, wakiwemo wabunge.

Mwanaharakati Okiya Omtata Okoiti pia amewasilisha kesi mahakamani kupinga malipo hayo.

Katika kesi yake, Bw Omtata amewashtaki wabunge na maseneta wote 416 kama watu binafsi.

Katika mkutano wa jana, wabunge na maseneta walikubaliana kuwa kesi hizo mbili ziwekwe pamoja na iwe kesi moja ambapo mshtakiwa ni tume ya PSC wala sio wao kama watu binafsi.

“Vilevile, tumekubaliana kuwa PSC ndiyo iwe ikisimamia masuala yote ya mishahara na marupurupu yetu kwa sababu hii ni tume ya kikatiba ilivyo SRC,” akasema mbunge mmoja.

Baada ya mkutano huo, uliodumu kwa saa mbili kwenye ukumbi wa bunge, wabunge waliondoka wakiwa na furaha huku wakikataa kuongea na wanahabari waziwazi.

“Leo (jana) hatuongei na nyinyi. Haya ni masuala mazito yanayohusu sisi peke yetu,” akasema Kiongozi wa Wengi katika bunge la kitaifa Aden Duale, baada ya kikao hicho.

UROHO: Matumbo ya wabunge yasiyoshiba

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE na maseneta wanakutana Alhamisi kujadili mbinu za kuiadhibu Tume ya Kukadiria Mishahara na Marupurupu ya watumishi wa umma (SRC), kwa kupinga hatua yao kulipwa marupurupu ya nyumba ya Sh250,000 kila mwezi.

Kikao hicho kisicho rasmi, almaarufu, ‘Kamukunji’, kiliitishwa na Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi kufuatia ombi lililowasilishwa na Mbunge wa Homa Bay Mjini, Peter Kaluma.

Mnamo Ijumaa iliyopita, Mahakama Kuu iliamuru Tume ya Huduma za Bunge (PSC) isitishe kuwalipa wabunge marupurupu ya nyumba hadi kesi iliyowasilishwa na SRC kupinga malipo hayo itakaposikizwa na kuamuliwa.

SRC inayoongozwa na Bi Lyn Mengich inataka mahakama kuwaamuru wabunge warejeshe pesa ambazo tayari wamepokea kama marupurupu ya nyumba, ikisema PSC ililipa pesa hizo kinyume cha sheria.

Ikiwa tume itafaulu, wabunge na maseneta 416 watalazimika kurejesha Sh2.21 milioni ambazo kila mmoja wao alipokea mwishoni mwa Aprili ikiwa ni malimbikizi ya tangu mwezi Oktoba 2018.

Kuishtaki SRC

Duru ziliambia Taifa Leo kwamba wabunge na maseneta wananuia kutumia mkutano huo kupanga mikakati ya kuishtaki SRC kwa kutumia Sh99 milioni kununua magari ya kifahari bila idhini ya Bunge, kama njia ya kuiadhibu tume hiyo kwa kuzuia walipwe marupurupu.

Tayari Kamati ya Bunge kuhusu Fedha imekataa kuidhinisha matumizi ya fedha hizo kwa mujibu wa kipengee cha 223 kinachoziruhusu asasi za umma kutumia fedha katika shughuli za dharura hata kabla ya kupata idhini ya Bunge.

“Hawa watu wa SRC ni wanafiki. Mbona wanadai eti wabunge ni walafi ilhali wao wanatumia pesa za umma kujinunulia magari ya kifahari bila kufuata sheria?,” akauliza Mbunge wa Alego Usonga, Samuel Atandi.

Mnamo Jumanne, Spika Muturi alisema aliwaalika wabunge kwa mkutano huo ili kutoa nafasi kwao kufahamishwa kuhusu vuta nikuvute inayoendelea kati ya SRC na PSC.

“Bw Kaluma alikuwa ameibua mambo muhimu katika barua yake kwa Spika na kutupa fursa kujadili masuala hayo katika mkutano wa Alhamisi saa tano. Maseneta pia watahudhuria,” akasema Bw Muturi ambaye ndiye mwenyekiti wa PSC.

Swali kuu

Naye Bw Kaluma alisema wanapanga kuibua maswali kuhusu mishahara mikubwa ambayo makamishna wa SRC hupokea, marupurupu ya nyumba na yale ya vikao.

“Mbona wao wanapokea mishahara ya Sh1 milioni kila mwezi, marupurupu ya nyumba ya Sh320,000 na Sh50,000 za kila kikao ilhali hatawataki wabunge kupokea Sh250,000 za nyumba?” akauliza.

Hata hivyo, uchunguzi wetu ulibaini kuwa ni mwenyekiti wa SRC pekee ambaye hupokea mshahara wa Sh1,082, 528 huku makamishna wengine wakipata Sh717,568 kila mwezi.

Tayari Kamati ya Bunge kuhusu Bajeti imepunguza mgao wa fedha kwa SRC katika bajeti itakayosomwa mwezi huu kwa Sh104 milioni, hatua inayoonekana kama ya kuiadhibu tume hiyo.

Kando na hayo wabunge wamepinga ombi la SRC la kutaka itengewe Sh300 milioni za kujenga afisi mpya.

“Hakuna haja kwa SRC kuitisha pesa za kujenga afisi mpya ilhali kuna majengo mengi ya serikali ambayo wanaweza kutumia,” akasema Bw John Mbadi ambaye ni kiongozi wa wachache bungeni.

SRC yapinga kortini marupurupu ya wabunge

Na WALTER MENYA

HUENDA wabunge wakalazimika kurejesha mamilioni ya pesa ambazo walikuwa wamepokea kama marupurupu ya nyumba ikiwa Tume ya Kukadiria Mishahara (SRC) itashinda katika kesi ambayo imewasilisha kortini.

Ijumaa, tume hiyo kupitia wakili Peter Wanyama ilifika katika Mahakama Kuu kuwasilisha ombi ikitaka hatua ya kuwalipa marupurupu hayo ibatilishwe, na pesa ambazo tayari wamelipwa zirejeshwe.

SRC inataka korti kuwaamrisha makarani wa Bunge la Taifa na la Seneti “kurejesha pesa zote ambazo zimelipwa kama mishahara na marupurupu kwa wabunge na maseneta, kupitia uamuzi ambao inautaja kuwa kinyume cha katiba na maelekezo ya tume.”

Aidha, SRC inaitaka korti kuwafanya wanachama wa Tume ya Huduma za Bunge (PSC) kuwajibika binafsi, pamoja na katibu wa tume hiyo Jeremiah Nyegenye, kwa kulipa marupurupu hayo bila kufuata sheria.

Wanachama wote wa PSC wameorodheshwa kama washtakiwa katika kesi hiyo; wakiwa spika Justin Muturi, Dkt Naomi Shaban, Seneta Maalum Beth Mugo, Adan Keynan, Benson Momanyi, George Khaniri, Aisha Jumwa, Aaron Cheruiyot, Dkt Lorna Mumelo na Bw Nyegenye.

Katika kesi hiyo, SRC inawalaumu wabunge kwa kukiuka katiba ambayo inaipa tume hiyo pekee jukumu la kuamua mishahara na marupurupu watakayolipwa maafisa wote wa umma.

“Uamuzi wa PSC kutenga na kuwalipa wabunge na maseneta marupurupu ya nyumba ni kukiuka sheria, vilevile ni kukiuka katiba kuwa SRC ndiyo pekee inayofaa kuamua malipo kwa maafisa wote wa umma,” SRC inasema katika kesi hiyo.

“Maafisa ambao wamefadhiliwa kununua nyumba na serikali, hawafai kulipwa marupurupu ya nyumba,” SRC inasema.

Marupurupu

Wabunge na maseneta hivi majuzi walijiongezea Sh250,000 kila mmoja, kwa mwezi kama marupurupu ya nyumba na kupitisha kuwa pesa hizo zianze kulipwa kuanzia Oktoba 2018.

Lakini SRC inadai kuwa hatua hiyo itagharimu nchi Sh99.5 milioni kila mwezi na Sh1.194 bilioni kila mwaka.

“Uamuzi wa PSC unatoa mwongozo mbaya kuhusu jinsi pesa za umma zinavyofaa kusimamiwa,” tume hiyo inasema.

Aidha, SRC inasema kwa sasa wabunge wanalipwa vyema, mishahara ya kawaida na marupurupu mengine yakiunganishwa.

Kwa mfano, kila wiki wabunge hulipwa Sh109 kwa kila kilomita wanayosafiri kwenda maeneobunge yao, pamoja na marupurupu ya kila mwezi ya kutunza gari ya Sh356,525.

“Aidha, wanapata marupurupu mazuri ya afya yao wenyewe, wake wao ama waume wao na watoto hadi wanne wenye chini ya miaka 25. Vilevile wanapata marupurupu ya pesa za simu, bima za ajali na kuhudhuria vikao vya bunge na kamati za bunge.” Wanachama wa kawaida katika kamati hulipwa marupurupu ya Sh5,000 kwa kila kikao cha kamati ambacho wanahudhuria, na Sh8,000 kwa mwenyekiti wa kamati.

Aidha, wana bima ya matibabu ya Sh10 milioni ya kulazwa) na Sh300,000 (ya kutibiwa na kuruhusiwa kwenda nyumbani), mkopo wa Sh7 milioni kununua gari, wa hadi Sh20 milioni kununua nyumba, Sh15,000 za kutumia simu, pamoja na usalama.

Uhuru na Ruto waongezewa mshahara

Na BERNARDINE MUTANU

RAIS Uhuru Kenyatta na naibu wake Dkt William Ruto watapata nyongeza ya mshahara ya asilimia 3.9.

Nyongeza hiyo iliondolewa hapo 2017 wakati wa uchaguzi, pamoja na nyongeza ya viongozi wengine wakuu serikalini kukabiliana na ongezeko la mzigo wa mishahara nchini.

Kulingana na stakabadhi rasmi kutoka kwa Hazina Kuu, mshahara wao utaongezwa kutoka Sh36.6 milioni kwa mwaka hadi Sh38 milioni.

Baada ya kukatwa kwa nyongeza hiyo, mshahara wa rais ulipungua kutoka Sh1.65 milioni hadi Sh1.44 milioni na naibu wake kutoka Sh1.4 milioni hadi Sh1.23 milioni.

Nyongeza hiyo imepangiwa kutekelezwa wakati Hazina ya Fedha inalenga kuongeza kiwango cha fedha za maendeleo na huduma za kimsingi kama vile usalama, afya na elimu.

Lakini kumekuwa na changamoto ya uokotaji wa mapato, hali ambayo ililazimisha Hazina ya Fedha kutathmini bajeti yake.

Viongozi hao wawili pia watapata marupurupu ya Sh15.2 milioni kwa mwaka, mwaka wa kifedha unaoanzia Julai 2019.

Mshahara kwa wote wawili utakuwa ni Sh22.8 milioni kwa mwaka, hivyo kiwango cha jumla kitakuwa ni Sh38 milioni.

Hata hivyo, mshahara na marupurupu hayo, utakuwa wa chini ikilinganishwa na kabla ya Juni 2017, ambapo walikuwa wakipata kiwango cha jumla cha Sh51.2 milioni, kabla ya kiwango hicho kupunguzwa.

Mishahara ya viongozi hao wawili wakuu pamoja na maafisa wengine wa serikali ilikatwa kabla ya uchaguzi

Nyongeza kwa wakuu hao wa nchi inajiri wakati hazina kuu inaweka mikakati ya kupunguza pesa zinazoelekezwa katika miradi ya maendeleo hasa sekta muhimu kama Usalama, Afya na Elimu.

Serikali imekuwa ikipambana na uhaba mkubwa wa fedha kutokana na kutofikisha viwango vinavyolenga vya ushuru unaokusanywa, tatizo ambalo lililazimisha hazina kuu kuangalia bajeti yake upya mara kwa mara.

 

 

Wabunge waongezewe mishahara, Wakenya wamewageuza benki – Atwoli

Na CHARLES WASONGA

SIKU chache baada ya juhudi zake za kutaka serikali iwape wafanyakazi nyongeza ya mishahara ya asilimia 15 kugonga mwamba, Katibu Mkuu wa COTU Francis Atwoli sasa anaunga mkono nyongeza ya mishahara ya wabunge.

Akihutubia wanahabari Jumatatu jijini Nairobi, Bw Atwoli alisema mishahara ya wabunge inapasa kuongezwa ili kuwawezesha kutosheleza matakwa ya wananchi ambao huwaomba pesa kila mara.

“Huu mtindo wa wananchi kuwaomba wabunge pesa kila mara umepelekea baadhi ya viongozi hao kujihusisha katika ufisadi. Hii ndio maana ninaunga mkono, ninaonelelea kuwa wana kila haki ya kuongezewa mishahara,” Bw Atwoli akasema.

Kulingana na kinara huyo wa COTU, tabia ya Wakenya ya kuwaomba wabunge pesa kila mara ndiyo imechochea ufisadi nchini akisema; “hatuwezi kupambana na ufisadi wakati ambapo wale wanaoongozwa wanaendeleza tabia ya kuwaomba viongozi wao fedha kila mara,”

“Mkinichagua kisha mtarajie pesa kila mara kutoka kwangu, basi hiyo itamaanisha kuwa sharti nilipwe mshahara wa juu kama mbunge wenu,” akasema Bw Atwoli.

Akaongeza: “Ikiwa leo Mbunge anakuja katika eneobunge lako kuhudhuria mazishi na akatoa mchango wa Sh3,000 au Sh5,000 utawasikia watu wakilalamika kana kwamba ni lazima kwa mbunge huyo kutoa mchango mazishini. Watanung’unika kwa sababu wao hutarajia wabunge kutoa michango mikubwa; kuanzia Sh30,000 kwenda juu.”

Kianara huyo wa COTU alisema kuna baadhi ya wabunge ambao hutumia kati ya Sh300,000 na Sh600,000 kila wiki wanapotembelea maeneobunge yao; pesa ambazo wanatarajiwa kutoa kutoka kwa mishahara yao.

“Tumewageuza wabunge wetu kuwa mipango ya malipo ya uzeeni, tumewageuza mashirika ya akiba na mikopo (Sacco), tumewageuza wabunge wetu kuwa benki, tumewageuza wabunge wetu kuwa watu wa kutulipia karo na kila kitu…” Bw Atwoli akaongeza.

Kiongozi huyo wa Cotu alitoa wito kwa Wakenya kushiriki katika shughuli za kuwaletea mapato kama vile kilimo badala ya kutegemea viongozi wao kwa mahitaji yao ya kila siku.

“Hapa nchini, Mungu ametupa hali nzuri ya anga, tunaweza kufanya mambo mengi ya kutuletea mapato. Tunaweza kwenda shambani kuzalisha viazi kisha kuuza sokoni na kupata pesa kidogo… badala ya kugeuza wabunge wetu kuwa bima ya matibabu,” Bw Atwoli akasema.

Kauli ya Atwoli inajiri baada ya kutoa kwa habari kwamba wabunge na maseneta juzi walijitengea Sh936 milioni kama marupurupu ya nyumba iliyopendekezwa na Tume ya Huduma za Bunge (PSC) 2018.

Hii ina maana kuwa kando na mishahara yao, wabunge na maseneta (ambao idadi yao ni 416) watapokea Sh250,000 kwa mwezi kila mmoja kama marupurupu ya nyumba. Hii ni licha ya pingamizi iliyotolewa na Hazina ya Kitaifa na Tume ya Kukadiria Mishahara na Marupurupu ya Watumishi wa Umma (SRC).

Iliripotiwa kuwa kila mbunge na seneta alipokea Sh2.25 milioni mwishoni mwa Aprili kwa sababu marupurupu hayo ya nyumba yalianza kulipwa Agosti mwaka 2018 wakati ambapo PSC iliidhinisha bajeti yake.

TAHARIRI: Jambo lifanywe kuhusu mishahara

NA MHARIRI

JUMATANO hii ulimwengu unaposherehekea sikukuu ya Lebadei, Kenya kwa inahitaji kujali maslahi ya wafanyakazi wake hasa wakati huu wa gharama ya juu ya maisha pamoja na mfumko wa bei.

Mishahara na ujira wa Wakenya wengi hasa wenye malipo ya chini imekuwa ikidumaa huku mingine ikiongezeka kwa mwendo wa kobe ilhali maisha yanaruka kwa kasi ya swara.

Tusipokuwa waangalifu kama taifa na hasa viongozi wa serikali walio katika nafasi nzuri ya kuunda sera, tutagutuka kama watu wetu wameangamia.

Wazazi wengi kwa sasa hawajui watakakotoa karo ya shule wakati huu wa kufunguliwa kwa shule. Wengine wengi hawana kodi ya nyumba na hata bado wapo wale wasiokuwa na chakula.

Sharti mikakati mipya iwekwe ya kuwaauni Wakenya. Mojawapo wa mikakati faafu kwa wananchi hawa ni kuwapa nyongeza nzuri ya mishahara na kuhakikisha kila mwajiri ametekeleza amri ya kuongeza asilimia inayofaa.

Katibu wa chama cha wafanyakazi (COTU), Bw Francis Atwoli amependekeza asilimia 15 kama nyongeza ya mwaka huu.

Ametoa pendekezo hilo kama sharti la kuunga mkono Azimio la Makazi Nafuu la Rais Uhuru Kenyatta.

Azimio hilo linapangwa kutekelezwa kwa kuwakata wafanyakazi wote na waajiri wao asilimia moja na nusu ya mshahara wao.

Naam huenda asilimia hiyo ya COTU ni kubwa kwa serikali kumudu lakini ni aula nyongeza ya mwaka huu iwe ya maana wala lengo la nyongeza hiyo lisiwe tu ada ya makazi nafuu bali dhamira iwe kuboresha maisha ya Wakenya.

Mbali na mkakati wa kuongeza mishahara, itakuwa bora serikali ianze kutafuta njia za kuwapunguzia wananchi gharama ya maisha.

Kutokana na kupungua kwa thamani ya mishahara, hatua itakayowakinga Wakenya hasa wa tabaka la chini ni kuwapunguzia gharama ya maisha hususan bei za bidhaa muhimu za kimsingi kama vile unga na mafuta na hata ikiwezekana kuweka viwango vya nauli.

Jambo jingine linalowaumiza Wakenya zaidi ni mzigo wa karo ya shule. Japo serikali iliahidi kuhakikisha kuwa wanafunzi wa sekandari wanaosoma kwa kurejea nyumbani hawatozwi pesa zozote hakuna shule ambayo haiwatozi wanafunzi ada za masomo.

Wazazi wengi, kadhalika, wanatatizika na karo za juu za masomo ya vyuo vya kadri na vyuo vikuu. Sharti jambo lifanyike.