Mjukuu wa Moi akubali watoto aliokana awali

Na JOSEPH OPENDA

MJUKUU wa aliyekuwa rais, Mzee Daniel Moi hatimaye amekubali kuwajibikia malezi ya watoto wawili anaoshutumiwa kuwatelekeza baada ya uchunguzi wa DNA kuthibitisha kwamba, ndiye baba mzazi.

Bw Collins Kibet Moi alieleza Mahakama ya Nakuru kwamba, yupo tayari kuchangia kwenye malezi ya watoto hao wawili aliowazaa na Bi Gladys Jeruto Tagi, kabla ya wao kutengana zaidi ya miaka minane iliyopita.

Alisema anadhamiria kuwasilisha mapendekezo rasmi mbele ya korti pamoja na Bi Tagi kuhusu jinsi atakavyowashughulikia watoto hao.

Bw Kibet, aliyekuwa amekanusha kuwazaa watoto hao, alilazimika kunyenyekea baada ya uchunguzi huo kufichua kuwa, ndiye baba mzazi wa watoto hao wenye umri wa miaka 11 na miaka tisa.

Kulingana na ripoti ya DNA, matokeo ya vipimo yaliyowasilishwa kortini mnamo Agosti 25, yalionyesha kuwa chembechembe za DNA za Bw Kibet zinafanana na za watoto hao wawili kwa asilimia 99.9, kumaanisha uwezekano wa kiwango cha juu zaidi kuwa ndiye baba mzazi wa watoto hao.

Akiwa mbele ya Hakimu Mkuu Benjamin Limo, Bw Kibet, kupitia wakili wake aliomba muda zaidi ili kuwasilisha mapendekezo yake kuhusu mchango wake katika malezi.

“Mshtakiwa amekubali kuwasaidia watoto lakini hana uwezo wa kulipa kiasi cha pesa kilichoitishwa na mlalamishi. Hivyo basi, anaomba idhini ya korti kuwasilisha mapendekezo rasmi kuhusu jinsi atakavyowasaidia watoto hao,” alisema wakili.

Bi Tagi aliyewasilisha kesi hiyo mnamo Machi alikuwa ameitisha Sh1 milioni kugharamia malezi ya watoto.Kupitia wakili wake David Mong’eri, mama huyo alidai pesa hizo ni za kugharamia mahitaji ya kibinafsi ya watoto hao.

Mjukuu wa Moi asusia DNA, hatarini kushtakiwa

Na JOSEPH OPENDA

MJUKUU wake Rais (mstaafu) Marehemu Daniel arap Moi, anayeandamwa na kesi ya malezi ya watoto kutoka kwa aliyekuwa mkewe, huenda akashtakiwa kwa kutoheshimu amri ya mahakama.

Hii ni baada ya kukosa kujiwasilisha kufanyiwa uchunguzi wa DNA ilivyoamrishwa na mahakama moja ya Nakuru.

Bi Glady’s Jeruto Tagi, ambaye amemshtaki Bw Collins Toroitich, (pichani) sasa ametishia kuwasilisha kesi kortini. Katika maagizo ya korti yaliyotolewa Juni 16 na Hakimu Mkuu Mkazi Benjamin Limo, Bw Moi alihitajika kujiwasilisha katika Maabara za Lancet mnamo Ijumaa, Juni 18.

Chembechembe zake zilipaswa kutolewa ili kubaini ikiwa yeye ndiye baba mzazi wa watoto wawili waliohusishwa kwenye kesi hiyo.

Chembechembe hizo zingelinganishwa na zile ambazo zingetolewa kwa watoto hao wawili ambao amekanusha kuwazaa.

“Wahusika wameamrishwa kujiwasilisha (wakiandamana na wawakilishi wao mawakili) katika maabara za Lancet, Nakuru Juni 18, ili chembechembe zao zitolewe kwa uchunguzi,” Bw Limo aliamrisha.

Hata hivyo, Bi Jeruto kupitia wakili wake David Mong’eri alieleza Taifa Leo kuwa, Bw Moi hakujitokeza katika hospitali hiyo na pia hakuwasiliana kuhusu alipokuwepo.

“Wateja wangu walijitokeza hospitalini humo Ijumaa asubuhi na kukaa hadi adhuhuri lakini Bw Moi hakuja. Simu yake binafsi wala ya mawakili wake haikuwa ikiingia,” alisema Bw Mongeri.

‘Kilio cha wanafunzi chuoni Moi kitafutiwe suluhu’

Na LYDIA OMAYA

MALALAMISHI ya njaa miongoni mwa wanafunzi katika vyuo vikuu humu nchini yamezidi hawa katika Chuo Kikuu cha Moi.

Wamekuwa wakidhihirisha hali yao mtandaoni kwa njia ya ‘memes’ ambayo wengi wanachukulia kuwa mzaha tu.

Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Vyuo (HELB) inalaumiwa pakubwa kusababisha hali hii chuoni Moi.

Wanafunzi wanadai kuwa fedha hizo zimecheleweshwa kwao tu kwani wanafunzi wengine wameshapokea mikopo.

Wana hofu kwamba hali hii huenda ikasababisha wengi kukosa mtihani wao kutokana na ukosefu wa karo. Tatizo la njaa tayari linashuhudiwa.

Wanafunzi wanaoathirika zaidi ni wale wanaoishi katika mabweni ya chuo.

Tangu kupika ipigwe marufuku chuoni Moi, wanafunzi wengi wamepata taabu kutafuta nyumba za kukodisha nje ya shule lakini sio wote wanaobahatika kutokana na ukosefu wa kodi maanake kupangisha ni bei ghali huenda wasiweze kulipa.

La pili ni kuwa nyumba ni chache na zile ambazo ziko mbali na shule ndizo za kodi nafuu ya kama Sh12,000 kwa muhula mmoja. Lakini itamlazimu kutumia nauli kila siku kuingia chuoni na baadaye kurejea chumbani.

Kutoruhusiwa kupika katika mabweni ya chuoni basi kunawalazimu kununua vyakula katika hoteli za shule na hata nje ya shule ambazo zinauza vyakula kwa bei wasioweza kumudu kwa muda mrefu.

“Tangu kupika shuleni kupigwe marufuku, wanafunzi wanaoishi mle wanateseka sana kwa kulazimika kutumia si chini ya Sh150 hotelini na mikahawani kila siku. Hapo awali hali ilikuwa afadhali kwa sababu wengi wangebeba vyakula kutoka nyumbani vya kupika kwa angalau muhula mmoja na hivyo basi pesa zingetumika kidogo,” alisema mwanafunzi wa mwaka wa nne Dan (sio jina lake halisi).

Mara kwa mara vyakula huisha kwa hizi hoteli na basi kulazimika kushinda njaa. Ni jambo la kushangaza kuwa wanafunzi wanazirai kutokana na njaa.

“Wanafunzi wengine wanazirai kwa kukaa siku nyingi bila chakula chochote. Mara mingi nyakati za usiku ambulensi inasikika ikichukua mwanafunzi ambaye ameathirika ili apelekwe hospitalini. Ni hali ya kuhuzunisha sana.” Cynthia Ainga ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa tatu anayeishi kwenye bweni anaeleza.

Mkuu wa Maslahi ya Wanafunzi – Dean – John Ayieko ametoa wito kwa wanafunzi wanaoathirika na njaa kujitokeza kupitia kwa vinara na viongozi wa wanafunzi ili kupata usaidizi.

Baadhi ya wanafunzi wanatoa ombi waruhusiwe kupika shuleni tena.

Ni muhimu HELB kutoa mikopo hiyo ya fedha baada ya wanafunzi hawa kuandamana mjini Eldoret, Jumanne. Huenda hali ikazidi kuwa mbaya ikiwa malalamishi haya hayatatiliwa maanani.

Lydia Omaya ni mtafiti

Wito serikali ibuni sera ya kuruhusu ndege kupaa na kutua uwanja wa Moi bila vikwazo

Na WINNIE ATIENO

WAWEKEZAJI katika sekta ya utalii wametoa wito kwa serikali ikubali sera inayoruhusu ndege kutua na kupaa katika uwanja wa ndege wa Moi moja kwa moja bila vikwazo.

Wawekezaji hao walisema sera hizo zitasaidia kufufua sekta ya utalii ambayo inaendelea kuzorota kufuatia janga la corona.

Hata hivyo walisisitiza kuwa ndege za moja kwa moja uwanja huo zitasaidia kukuza sekta nyingi ikiwemo ile ya utalii, biashara na uchukuzi hivyo basi kufungua ajira miongoni mwa wakenya.

“Watu wengi hupenda usafiri bila changamoto, serikali inafaa kukubali sera inayoruhusu ndege kutua na kupaa katika uwanja wa ndege wa Moi moja kwa moja bila vikwazo” alisema Bw Husnain Noorani kwenye mahojiano.

Akiongea kwa niaba ya wawekezaji wa sekta ya utalii na wamiliki wa hoteli za kifahari, Bw Noorani aliitaka serikali kuhakikisha bodi ya utalii nchini inafadhiliwa ili kuuza soko la Kenya kama kituo maalum cha utalii duniani.

Alisema endapo serikali itakubali sera hiyo, ndege nyingi zitapaa na kutua katika uwanja wa kimataifa wa ndege ya Moi na kuimarisha uchukuzi, utalii na biashara.

Uwanja huo ndio mkubwa zaidi sehemu ya Pwani.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa muungano wa wawekezaji wa utalii Bw Ishpal Oberoi, alisema biashara katika uwanja huo wa ndege unaweza kupigwa jeki endapo ndege zitakuwa zinapaa na kutua moja kwa moja.

“Kama tunataka kukuza eneo la Pwani kama soko la utalii, ni sharti tuweke mikakati kabambe ikiwemo kuhakikisha ndege zinatua na kupaa bila vikwazo. Ndege za kimataifa kutoka bara Uropa, Amerika na hata Asia zinaweza kuleta wageni,” alisema.

Bw Oberoi ambaye pia ni mkurugenzi wa kampuni maarufu ya kusafirisha watalii ya Kuldip, alisema sekta hiyo imeanza kuimarika hasa maeneo ya Diani, Kilifi, na Maasai Mara.

Hata hivyo alisema kuna matumaini ya utalii kuimarika kaunti ya Mombasa wakati wa likizo ya Agosti.

Lakini Waziri wa Utalii na Wanyama wa porini Bw Najib Balala alisema serikali itaweka mikakati kuhakikisha ndege za kimataifa zinatua uwanja huo.

“Ni dhahiri uchumi wa utalii umezorota duniani na kila mtu anaogopa. Kwa mfano barani Uropa, hakuna ndege ya inayokwenda Marekani sababu ya wasiwasi dhidi ya kuambukizwa virusi hivi. Tunaweka mipango ili uwanja huo upate ndege za kimataifa. Tuna Rwanda Air, Turkish Airways, Qatar Airways na Ethiopian Airways lakini tunataka ndege nyingine zisafirishe wageni Mombasa ili kukuza sekta hiyo,” alisema kwenye mahojiano wiki iliyopita.

Hata hivyo aliwataka wakenya kupiga jeki utalii wa humu nchini ili kufufua uchumi.

Gideon ahimizwa aanzishe ushirika na jamii ya Luhya

SHABAN MAKOKHA na CHARLES WASONGA

BAADHI ya wabunge kutoka jamii ya Abaluhya, sasa wanamtaka Seneta wa Baringo Gideon Moi kubuni muungano wa kisiasa na jamii hiyo kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022.

Wabunge wa chama cha ANC, Ayub Savula (Lugari) na Tindi Mwale (Butere), wamemtaka Seneta Moi ambaye alikabidhiwa uongozi wa kisiasa wa familia ya Rais wa zamani Daniel Moi aliyezikwa Jumatano, kushirikiana na mgombea urais kutoka jamii ya ‘Mulembe‘.

“Tunataka Gideon abuni muungano na mgombeaji urais ambaye sisi kama jamii ya Mulembe‘ tutamteua. Mzee Moi alipenda zaidi watu wetu na hakutubagua wakati wa utawala wake,” akasema Bw Savula akiongeza kuwa muungano kama huo utawezesha eneo la magharibi kupata angalau nyadhifa nane za uwaziri katika serikali ijayo.

Naye Bw Mwale akasema: “Tunatambua hadhi ambayo Gideon alipewa na familia yake. Kwa hivyo tunamuomba afanye kazi nasi alivyofanya marehemu babake. Tunataka kubuni muungano naye kuelekea uchaguzi mkuu ujao.”

Seneta Moi alipewa rungu ya usemi wa kisiasa na ndugu yake mkubwa Raymond Moi wakati wa mazishi ya baba yao kule Kabarak, Nakuru.

Hatua ya Gideon kupokezwa rungu imeibua maswali kuhusu endapo atachukua nafasi ya Mzee Moi ya kuwa kigogo wa kisiasa katika eneo zima la Rift Valley.

Marehemu alisalia kuwa kiongozi wa kisiasa wa eneo hilo hata baada ya kustaafu na kumpokeza Mwai Kibaki uongozi wa nchi mnamo mwaka wa 2002.

Hii ndiyo maana viongozi wengi wamekuwa wakizuru Kabarak kusaka ushauri wa kisiasa kutoka kwa Mzee Moi.

Bw Savula ambaye pia ni naibu kiongozi wa ANC alisema Seneta Moi anafaa kutambuliwa kama msemaji rasmi wa jamii ya Wakalenjin kwa “sababu ana uwezo wa kuongoza eneo zima la Rift Valley.”

Mbunge huyo wa Lugari alimwalika Seneta Moi kuzuru eneo la Magharibi ili kujitafutia uungwaji mkono kisiasa.

Bw Savula alisema hayo alipohudhuria mkutano wa wajumbe wa ANC mjini Butere kupanga mikakati ya kampeni za chama hicho kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022.

Bw Mwale alisema muungano kati ya mgombeaji urais kutoka jamii ya Abaluhya na Seneta Moi utaibuka na ushindi katika uchaguzi mkuu wa 2022.

“Tunamtaka Gideon kuongea na viongozi wakuu wa kisiasa kutoka jamii yetu kama vile Kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi, Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya na kiongozi wa Ford Kenya Moses Wetang’ula ili tubuni muungano wenye nguvu kuelekea 2022,” akasema Mwale.

Kauli za wabunge hao zinajiri siku chache baada ya Bw Mudavadi kuwapuuzilia mbali wanasiasa wa mrengo wa ‘Tangatanga’ ambao wamekuwa wakimshinikiza kubuni muungano na Naibu Rais William Ruto kueleleza uchaguzi mkuu ujao.

Kiongozi huyo wa ANC alisema kuwa chama chake kitafanya uamuzi kuhusu suala hilo wakati “unaofaa” lakini sio kutokana na shinikizo kutoka kwa wanasiasa.

Rungu la Moi sasa launganisha ‘vitoto vya kifalme’ nchini

Na BENSON MATHEKA

KUTEULIWA kwa Seneta wa Baringo, Gedion Moi kumrithi kisiasa baba yake Daniel Moi, na kauli ya ndugu yake Raymond kumtaka ashirikiane na Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga, kumefufua mjadala wa watatu hao waliozaliwa katika familia tajiri na zenye ushawishi kuendelea kuteka siasa za Kenya.

Wakati wa mazishi ya Mzee Moi eneo la Kabarak mnamo Jumatano, Bw Raymod Moi alitangaza kuwa familia ya baba yake, aliyekuwa rais wa pili wa Kenya, imemteua Gedion kuwa msemaji wake katika masuala ya kisiasa.

Alimtaka aimarishe chama cha Kanu na kukitumia kuunganisha Wakenya wote. “Sote tunaunga BBI nyuma ya Rais Kenyatta na Bw Odinga,” alisema mbunge huyo wa Rongai.

Gedion, kitinda mimba wa hayati Moi, alikubali wadhifa huo na atajiunga na Rais Uhuru ambaye ni msemaji wa familia ya Jomo Kenyatta aliyekuwa rais wa kwanza wa Kenya, na Raila mwana wa aliyekuwa makamu wa rais wa kwanza wa Kenya, Jaramogi Oginga Odinga.

Wadadisi wanasema hii inaashiria kujiri kwa muungano mkubwa wa kisiasa unaoshirikisha familia za Moi, Odinga na Kenyatta.

“Familia za Moi, Odinga na Kenyatta zina ushawishi mkubwa wa kisiasa nchini na chini ya BBI, zinaweza kuungana kuteka siasa za Kenya kwa miaka mingi,” asema wakili Thomas Maosa.

“Mbali na siasa, zina ushawishi wa kifedha na kimaeneo na wanasiasa wengine wenye majina makubwa walihusiana kwa njia moja na familia hizi,” aliongeza.

Bw Odinga ndiye kigogo wa kisiasa eneo la Nyanza, wadhifa aliorithi kutoka kwa baba yake, naye Uhuru ndiye msemaji wa eneo la Mlima Kenya ambalo baba yake alimiliki kwa miaka mingi hadi kifo chake. Kwa miaka mingi, Daniel Moi alikuwa kigogo wa siasa eneo la Rift Valley.

Naibu Rais William Ruto amekuwa akiwalaumu wakosoaji wake kwa kumpuuza kwa sababu hatoki familia zenye ushawishi. Akihutubia waombolezaji wakati wa mazishi ya Mzee Moi, Bw Odinga alipuulizia mbali madai kuwa familia za baba zao ni za kifalme akisema Moi, Odinga na Jomo Kenyatta walitoka familia maskini.

Wadadisi wanasema kwamba familia hizi zikiungana, itakuwa vigumu kubanduliwa uongozini.

“Vigogo wengine wa kisiasa nchini, akiwemo Bw Ruto walijengwa na familia hizi. Ruto alijengwa kisiasa na Moi lakini akakimbia mbio na kusahau Kenya ina wenyewe,” aeleza Bw Maosa.

Kulingana na wakili huyu, muungano wa familia hizi tatu unaweza kuzamisha azma za wanasiasa wengi, akiwemo Dkt Ruto. “Muungano wa familia hizi unaweza kuangamiza maisha ya kisiasa ya wasioelewa upepo wa siasa unavyovuma na wanaojiamini kama Dkt Ruto.”

Vigogo wa kisiasa kutoka maeneo mengine nchini kama vile Kalonzo Musyoka kiongozi wa chama cha Wiper, Musalia Mudavadi wa chama cha Amani National Congress, Moses Wetangula wa Ford Kenya na Ali Hassan Joho ambaye ni msemaji wa eneo la Pwani wameamua kuunga BBI.

“Kufaulu kwa viongozi hao kisiasa kulichangiwa na familia za Moi, Kenyatta na Odinga. Wanaelewa ni vigumu kuzipuuza na wanacheza kwa mbali kwa sasa,” anaeleza.

Mchanganuzi wa siasa, Bw Peter Gichara, anasema kuvunja ushawishi wa familia hizi ndio utakuwa mwisho wa ukoloni.

“Familia hizi hazina mapya kwa Wakenya kwa sababu zilifunzwa na wakoloni. Kuvunja ushawishi wao katika siasa za Kenya itakuwa ni kumaliza ukoloni kabisa. Kufanya hivi kutakuwa mwanzo wa kujenga demokrasia halisi,” aliongeza.

Rais Mstaafu Daniel Arap Moi azikwa nyumbani Kabarak

Na SAMMY WAWERU

MIAKA 42 iliyopita, taifa lilimpoteza Rais Mwanzilishi wa Jamhuri ya Kenya ndiye Mzee Jomo Kenyatta.

Rais huyo wa kwanza, aliaga dunia Agosti 22, 1978, akiwa madarakani na waliokuwa wamezaliwa wakati huo walishuhudia heshima alizopata Hayati Mzee Kenyatta akizikwa, katika hafla ya kitaifa na iliyoongozwa na kikosi cha kijeshi.

Rais aliye mamlakani ndiye Amiri Jeshi Mkuu, hivyo basi amri zote katika kikosi hicho ziko chini yake.

Kwa mujibu wa mila, itikadi na desturi za wanajeshi, mmoja wao anapofariki akiwa kazini, yaani kabla kustaafu, anazikwa katika hafla ya kipekee ambapo mizinga 21 hufyatuliwa hewani, kuonyesha heshima kwa mwendazake.

Rais akiwa ndiye Amiri Jeshi Mkuu, akifariki akiwa mamlakani anazikwa katika hafla ya kitaifa ambayo inaongozwa na wanajeshi wenye madaraka ya hadi ya juu katika kikosi cha KDF.

Wakati wa kuteremsha jeneza lake kaburini, mizinga 21 inafyatuliwa.

Kwa muda wa wiki moja iliyopita, kifo cha aliyekuwa Rais wa pili wa Kenya, Mzee Daniel Toroitich Arap Moi, kimefichua mengi kuhusu mila, itikadi na tamaduni za kikosi cha kijeshi. Pia, kimekumbusha walioshuhudia kifo cha Mzee Jomo Kenyatta, heshima alizopokezwa wakati akizikwa.

Mzee Moi alifariki mnamo Jumanne, Februari 4, 2020, Nairobi Hospital na Rais Uhuru Kenyatta ndiye alitangaza rasmi kifo cha Rais huyo mstaafu.

Kilichofuata, kikawa mwili wa mwendazake kusafirishwa na wanajeshi kutoka wadi ya kipekee aliyokuwa akihudumiwa ili kuhifadhiwa katika Hifadhi ya Maiti ya Lee jijini Nairobi.

Ulinzi uliimarishwa vikali katika hifadhi hiyo, wanajeshi waliovamilia sare rasmi, nyekundu, wakisimama kwenye lango usiku na mchana. Walioruhusiwa kuutazama mwili wa Mzee Moi ni watu wa familia, marafiki wa karibu na viongozi wakuu serikalini.

Wizara ya Usalama wa Ndani na Mikakati ya Serikali, chini ya Waziri Dkt Fred Matiang’i na Katibu wake Dkt Karanja Kibicho, ilichukua hatamu ya maandalizi ya mazishi, ikiwa ni pamoja na mikakati ya kumuomboleza Moi.

Baada ya kutangaza kifo cha Rais huyo Mstaafu, kiongozi wa taifa Uhuru Kenyatta, pia alisema Mzee Moi ataombolezwa hadi atakapozikwa, ikiwa ni Jumatano, Februari 12, 2020. Mzee Jomo Kenyatta, ambaye ni babake Rais Kenyatta, aliombolezwa kwa muda wa siku 30.

Wakenya walipata fursa ya kuutazama mwili wa Mzee Moi, katika majengo ya bunge jijini Nairobi, ambapo shughuli hiyo ilichukua siku tatu.

Kulingana na bunge ni kwamba zaidi ya watu 200,000 waliutazama mwili wa marehemu.

“Kufikia Jumatatu jioni, zaidi ya watu laki mbili walikuwa wameutazama mwili wa Rais Mstaafu Mzee Daniel Toroitich Arap Moi,” Spika wa bunge la kitaifa Justin Muturi alisema baada ya wabunge kushiriki kikao cha kutuma salamu zao za pole.

Majengo ya bunge na mazingira yake, usalama uliimarishwa, vikosi vya pamoja kutoka idara ya jeshi na polisi wakishika doria katika kila kona.

Mwili wa Mzee Moi ulikuwa ukisafirishwa kwa gari maalum la kijeshi, kutoka Hifadhi ya Lee Funeral hadi majengo ya bunge na pia kurejeshwa, chini ya ulinzi mkali.

Mapema Jumatano, mwili wa Mzee Moi ulisafirishwa kwa ndege ya kijeshi, seneta wa Baringo na ambaye pia ni mwanawe aliandamana nao hadi nyumbani Kabarak, Kaunti ya Nakuru kwa ibada ya mazishi.

Rais Kenyatta ameongoza Wakenya katika kumpungia mkono wa buriani.

Aidha, Mzee Moi amezikwa chini ya itakadi za kijeshi, na kwa kuwa aliwahi kuhudumu kama Amiri Jeshi Mkuu mizinga 19 imefyatuliwa. Ndege za kivita, pia zimepita angani, yote hayo yakiashiria heshima kwa Rais huyo Mstaafu.

Mzee Moi alitawala Kenya kati ya 1978 – 2002.

Viongozi mbalimbali wamemmiminia sifa kemkem, wakimtaja kama kiongozi mzalendo aliyependa nchi yake, amani na umoja na zaidi ya yote Mcha Mungu.

Buriani Mzee Daniel Toroitich Arap Moi.

Ndege iliyobeba mwili wa Rais Mstaafu Moi yawasili Kabarak

Na SAMMY WAWERU

MWILI wa Rais wa pili wa Jamhuri ya Kenya Daniel Toroitich Arap Moi umesafirishwa kwa ndege ya kijeshi kutoka Nairobi ukipelekwa nyumbani kwake Kabarak, Kaunti ya Nakuru, ambako anazikwa leo Jumatano.

Ndege hiyo imewasili uwanja mdogo wa Kabarak dakika chache kabla ya saa tatu za asubuhi.

Awali, ndege iliyobeba mwili wa Rais huyo mstaafu na aliyetawala Kenya kwa miaka 24 iliondoka katika uwanja wa ndege wa Wilson, Nairobi, mwendo wa saa moja na dakika arubaini na tano asubuhi.

Familia ya marehemu ikiongozwa na mwanawe Gedion Moi, imeshuhudia mwili wa marehemu ukiwekwa kwenye ndege ya kikosi cha wanajeshi wa nchi kavu, ndicho Kenya Army.

Kwa mujibu wa itikadi na desturi za hafla ya mazishi, familia na waombolozaji kwa jumla huvalia mavazi meusi, na kipande cha kitambaa hususan cheupe kwenye mfupo wa shati au blauzi. Kipande hicho pia hutundikwa begani.

Mwanawe marehemu, kitinda mimba na pia seneta wa Baringo Gedion Moi na familia yake, wote wamevalia mavazi meusi, kwa mujibu wa picha na video zilizonaswa uwanjani Wilson akishuhudia mwili wa Mzee Moi ukiwekwa kwenye ndege.

Ni taswira ambayo pia inaonekana kwa wengi wa waombolezaji ambao tayari wamefika nyumbani kwake (Mzee Moi) Kabarak. “Mavazi meusi ni ishara ya heshima kwa marehemu,” anasema Dennis Mugambi. Nyingi ya hafla za mazishi, waombolezaji huvalia mavazi meusi.

Mzee Moi aliaga dunia Februari 4, 2020, akiwa na anapewa mazishi ya hadhi ya heshima ya juu kitaifa na kama kiongozi aliyewahi kuwa Amiri Jeshi Mkuu, atasindikizwa na ufyatuaji wa mizinga 19.

Rais Uhuru Kenyatta ataongoza taifa katika kumpungia mkono wa buriani Mzee Moi, hafla ambayo itahudhuriwa na marais kadha wa kigeni pamoja na viongozi na wageni mashuri kutoka serikalini na nchi za kigeni.

Kwa mujibu wa waandalizi wa mazishi hayo, yanatarajiwa kuhudhuriwa na zaidi ya watu 30,000.

KINA CHA FIKIRA: Kiswahili kilipata utanuzi mkubwa mno katika enzi ya Moi, makiwa kwa wote

Na KEN WALIBORA

HUU si wakati mzuri wa kufa.

Hili halitokani na hatua alizopiga mwanadamu katika kuboresha miundumbinu na teknolojia kwa jumla. Rafiki yangu mmoja, na sasa simkumbuki nani, aliniambia mwaka 2019 kwamba huu si wakati mwafaka kufa kwa vile ukifa unapitwa na uhondo wa maendeleo ya mwanadamu katika uvumbuzi na ugunduzi wa mambo tumbi nzima.

Sikubaliani naye hata sasa na sikukubaliana naye alipoyatamka aliyoyatamka. Nakubaliana naye kuhusu suala la kwamba sasa si wakati mwafaka wa kufa, ila kwa sababu yake sikubaliani naye.

Leo nasema kwamba hakuna tija ya kufa sasa hasa kutokana na kizazi hiki cha watu makauleni wanaokusifu na kukukashifu kwa pumzi moja na kinywa kimoja.

Kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu wa kwanza mwanamke Margaret Thatcher 2013 ndicho kilichonizindua kwa tabia hii ya kukirihisha. Watu walijificha nyuma ya pazia la majina bandia ya majukwaa ya mtandaoni kukomoa na kuua maiti. Walisema walivyokuwa mwovu Bi Thatcher na kwamba dunia ilikuwa afadhali bila yeye. Nilimaka sana. Katika hukumu hakuna wakali kama watu wa kizazi kilichoko. Wanajua kuhukumu kuliko Mwenyeezi Mungu, yaani machoni pao. Hakimu wa haki kama wao hakuna. Wao ndio wajuao. Nani kama wao?

Nimeona tangu kifo cha Rais wa Pili wa Kenya, Mzee Daniel Toroitich arap Moi, mambo yamekuwa yale yale. Watu wanapozungumza hadharani kwenye runinga na mawanda rasmi, wanampalia sifa kiongozi huyo aliyetuacha mkono. Wakigeuka pahali ambapo si rasmi wanatema cheche za matusi na lawama. Wanatukana tu na kutusi kama cherehani. Na hakuna pahali ambapo hilo limebainika zaidi kama katika majukwaa yaitwayo ya kijamii mtandaoni kama Twitter, Facebook and kwengineko.

Wanasema mabaya mpaka yanakuchusha na kukuchosha. Mimi nishachoka.

Siwezi kufanya kazi ya Mwenyeezi Mungu ya kuhukumu watu. Wacha wafao wafe, na hukumu tumwachie mwenyewe Muumba. Niliwahi kuhudhuri mazishi ya Profesa mmoja maarufu sana. Yeye alikuwa miongoni mwa watu walionirai nipate kisomo cha tija.

Niliona vile waliopanda jukwaani walivyomsifu sana kwa umahiri wake wa kitaaluma na utu wake wema. Haya walikuwa wanayasema kwenye maikrofoni. Ila wakishuka toka jukwaaani wanasemezana wao wa wao kuhusu mapungukiwa au mapungufu ya marehemu. Mwone alivyokuwa hana mke, hana nyumba, kazikwa katika shamba la nduguye.

Hii ni nini hii? Wanamkosoa pakubwa mtu ambaye hayupo hapa kujitetea mwenyewe dhidi ya lawama zao.

Katika siku hii ya mazishi ya Mzee Daniel Toroitich arap Moi, sina nia ya kumsifu wala kumkashifu, kama nikikopa maneno ya Bruto katika tamthilia ya Shakespeare cha Juliasi Kaizari iliyotafsiriwa na Mwalimu Julius Nyerere.

Ninachotaka kusema ni kwamba ni katika enzi yake ambapo Kiswahili kilipata utanuzi mkubwa zaidi tangu kujipatia uhuru.

Ni Mzee Moi ndiye aliyekifanya Kiswahili somo la lazima katika mfumo wa elimu.

Nasema makiwa sana kwa wote wanaohusika na msiba wa kuondokewa na Baba Moi.

Moi alivyodumisha Uafrika

Na WANDERI KAMAU

KATIKA utawala wake, Rais Mstaafu Daniel Moi alithamini sana kauli zilizomjenga Mtu Mweusi na utamaduni wa Mwafrika.

Hivyo, alikabili vikali jambo lolote lililoonekana kukinzana na maadili ya Kiafrika, huku akitilia maanani masuala yaliyokuza tamaduni hizo.

Alifikia hayo kupitia nyimbo, vyombo vya habari, vipindi, mavazi, lugha, densi kati ya masuala mengine.

Vile vile, alitoa kauli mbalimbali kila wakati akihimiza umuhimu wa umoja miongoni mwa Wakenya.

Ni katika enzi ya utawala wake ambapo nyimbo kama ‘Fimbo ya Nyayo’, ‘Tawala Kenya Tawala’, ‘Tushangilie Kenya’, ‘Fuata Nyayo’, ‘Maziwa ya Nyayo’, ‘Enzi Zao’ kati ya zingine ambapo zilipata umaarufu mkubwa kwa kuhimiza uzalendo miongoni mwa Wakenya.

Mzee Moi angetumbuizwa na kwaya mbalimbali katika hafla muhimu kama sikukuu za kitaifa, ambapo baadaye angetumia nafasi hiyo kusisitiza jumbe zilizotolewa kwenye nyimbo hizo.

“Mimi mara kwa mara huwa nahimiza umuhimu wa umoja wa Waafrika. Na niliwaambia wananchi tusimame kwa kupendana, tusimame kwa kukaa na amani,” angesema Moi.

Mwalimu Thomas Wesonga, ambaye ameshiriki kwenye utunzi wa baadhi ya nyimbo alizopenda Mzee Moi, anasema kuwa kando na kumwongoa, nyimbo hizo zilikuwa nguzo kuu ya kuhimiza utamaduni wa Mkenya.

Mzee Moi pia hakusita kuwachukulia hatua wanamuziki ambao walitunga nyimbo zilizoukosoa utawala wake, kwani aliziona kama kikwazo cha kusambaratishwa mwito wa Uafrika.

Baadhi ya nyimbo zilizopigwa marufuku ni ‘Nchi ya Kitu Kidogo’ uliotungwa na mwanamuziki Eric Wainaina kwa kukashifu ufisadi katika serikali ya Mzee Moi.

Wimbo huo ulipigwa marufuku mnamo 1998, huku Bw Wainaina akitolewa jukwaani alipokuwa akiwatumbuiza wageni katika hafla moja.

Baada ya jaribio la mapinduzi ya 1982, serikali ya Mzee Moi ilipiga marufuku kwa muda muziki aina ya ‘Reggae’ kuchezwa vilabuni, kwa hofu kwamba “ulikuwa ukiwachochea wananchi.”

Baadhi ya wanamuziki waliokuwa wamebobea na kupata umaarufu nchini wakati huo ni Bob Marley kutoka Jamaica, Peter Tosh kati ya wengine.

Serikali ya Mzee Moi pia ilitumia vyombo vya habari kushinikiza umoja na thamani kuu ya Uafrika.

Ilifikia hilo kwa kutumia Shirika la Habari la Kenya (VOK) kupitia nyimbo na vipindi vilivyohimiza maadili hayo.

Baadhi ya nyimbo ambazo zilichezwa sana, hasa katika miaka ya themanini ni ‘Amka Kumekucha’ wa Maroon Comandos, ambao uliwahimiza Wakenya kuhusu umuhimu wa kutia bidii kazini ili kuijenga nchi.

Inaelezwa ni kutokana na hilo ambapo Moi aliwakabili vikali wale walioanzisha majarida yenye misimamo huru kama ‘Beyond’, ‘Weekly Review’ kati ya mengine ambayo yaliikosoa serikali yake.

Ingawa Kenya iliegemea mfumo wa chama kimoja katika enzi ya Mzee Moi, wanachama wa Kanu walikuwa na mavazi maalum.

Mavazi hayo yalikuwa yenye rangi nyekundu, kijani kibichi na nyeusi, ambazo ndizo rangi za bendera ya taifa.

Wale waliohudumu wanasema kuwa lengo kuu la mavazi hayo lilikuwa kuonyesha moyo wa uzalendo miongoni mwa Wakenya.

“Mzee Moi alipenda umoja miongoni mwa Wakenya. Aliamini umoja kama nguzo kuu ya Uafrika, ndipo akakita hilo kwenye falsafa ya Kanu,” asema Dkt Amukoa Anangwe, aliyehudumu kama waziri katika serikali ya Mzee Moi.

Wadadisi wanasema kuwa imani hiyo ndiyo ilimweka wasiwasi kukubali Kenya kuanza mfumo wa vyama vingi vya kisiasa.

Kwenye mojawapo ya hotuba yake, Moi alieleza kuwa mfumo huo ungesambaratisha umoja ambao alikuwa amejenga kupitia Falsafa ya Nyayo, iliyohimiza Amani, Upendo na Umoja.

Ni kutokana na wasiwasi huo ambapo kauli yake ya “Siasa mbaya, maisha mbaya” ilitoka.

Mzee Moi anadaiwa kuamini kwamba mfumo huo ulitokana Umagharibi, ambapo ungekuwa kikwazo kikubwa kuiunganisha nchi.

Kwenye hotuba zake nyingi, Mzee Moi alipendelea kutumia Kiswahili, wadadisi wakisema kuwa hilo liliwiana na lengo la kutilia maanani dhana ya uzalendo miongoni mwa Wakenya.

Mtindo huo ndio umeshinikiza baadhi ya wabunge katika Bunge la sasa kama Mohamed Ali (Nyali) kuwaomba wenzao kuanza kutumia Kiswahili kama lugha rasmi wanapowasilisha hoja zao bungeni.

“Ili kukuza uzalendo na Uafrika, lazima tuwaige viongozi kama Mzee Jomo Kenyatta na Mzee Moi, ambao walijivunia sana kutumia Kiswahili kila mara walipotoa hoja zao ama kuwahutubia Wakenya,” akasema mbunge huyo kwenye mojawapo ya michango yake.

Wakenya wamiminika uwanjani Nyayo kwa ibada maalumu kumuenzi Moi

Na PATRICK LANGAT

WAKENYA na waombolezaji wengine wamemiminika katika uwanja wa kitaifa wa Nyayo kwa ibada maalum kumuenzi Rais Mstaafu Daniel Toroitich Arap Moi aliyefariki Jumanne wiki jana na ambaye atazikwa kesho Jumatano.

Msafara uliobeba maiti ya Rais Mstaafu Daniel Moi umewawasili Ikulu ya Nairobi baada ya kutoka Lee Funeral saa mbili na dakika 27 asubuhi (8.27 a.m.).

Msafara huo ulikuwa chini ya ulinzi mkali wa wanajeshi.

Watu walianza kupanga laini mapema saa kumi na moja alfajiri ili waingie uwanjani Nyayo.

Mabasi ya shule mbalimbali kutoka maeneo mbalimbali nchini yamesafirisha waombolezaji waliolazimika kushuka na kuchukua barabara ya Access inayochipukia kutoka kwa barabara ya Bunyala kuingia uwanjani Nyayo.

Moi alikataa niwe Rais

MARY WANGARI na BENSON MATHEKA

NAIBU Rais, Dkt William Ruto, hatimaye amefichua kuwa uhusiano wake na aliyekuwa mlezi wake wa kisiasa, Daniel arap Moi, ulivurugika alipotangaza nia yake ya kugombea urais.

Dkt Ruto alisema kwamba tangu wakati huo, uhusiano wake na Mzee Moi ulianza kuwa baridi tofauti na kabla ya kutangaza azma yake.

“Tulikuwa na mkutano mjini Eldama Ravine ambapo nilitangaza azma yangu ya kuwania urais. Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa mafarakano yetu,” alieleza Bw Ruto.

Alisema kuanzia wakati huo Mzee Moi aliacha kumchangamkia kama awali na hata kumdhalilisha hadharani.

Kulingana na Naibu Rais, hakuchukulia tukio hilo kwa uzito hadi alipofungiwa nje ya lango la boma la Mzee Moi pamoja na wabunge wengine 15 walipoenda kumtembelea rais huyo mstaafu.

Dkt Ruto alisema walinzi waliwaarifu kwamba Mzee Moi hakutaka kukutana na mtu yeyote wakati huo.

Kabla ya tukio hilo, uhusiano wa Ruto na Moi ulikuwa mzuri. Alikuwa mmoja wa wanasiasa chipukizi kutoka jamii ya Wakalenjin ambao Mzee Moi alikuza.

“Kutoka Eldama Ravine nilifikiri ni kitu rahisi. Tulikuwa wabunge 15 na ilikuwa kawaida yetu kila mara tulipokuwa Nakuru, kumtembelea Mzee na kushiriki kikombe cha chai, kuzungumza kidogo kabla ya kurejea makwetu,” alisema akizungumza na runinga ya Citizen mnamo Alhamisi usiku.

“Safari hii tulipata lango likiwa limefungwa na tukaarifiwa kwamba Mzee hakutaka kukutana nasi,” alisimulia.

Aidha, Bw Ruto alieleza jinsi marehemu alivyotoa matamshi aliyohisi yalimdunisha alipopuuzilia mbali nia yake ya kugombea urais na zaidi uwezo wake wa kuongoza jamii.

Rais Moi, kulingana na Bw Ruto, alikuwa ameteua watu mbalimbali alioamini walikuwa na uzoefu wa siasa si tu katika jamii ya Bonde la Ufa bali pia katika ulingo wa siasa nchini.

Alisema hapo ndipo alipogundua kwamba mtu aliyemtazama kama kielelezo chake kisiasa alikuwa na mawazo tofauti na yake.

“Alitamka maneno ya kudhalilisha mno tangazo langu, akipuuza azma yangu na kusema nilikuwa ninapotosha jamii. Bw Moi alijitokeza na kusema Ruto hawezi kuwa kiongozi, mnapaswa kuchagua watu wenye ujuzi kama Bw Henry Kosgei na Bw Nicholas Biwott. Ninakumbuka wakati huo nikifafanua kwamba sikutaka kuwa kiongozi wa jamii bali niliazimia kuwa Rais,” alisema Dkt Ruto.

Matamshi ya Bw Ruto yamejiri huku Wakenya wakitazamiwa kutoa heshima za mwisho kwa Mzee Moi aliyefariki Jumanne, Februari 2, 2020, ambapo ripoti ziliibuka kwamba Naibu Rais alikuwa amezuiwa kuona mwili wa marehemu katika mochari ya Lee Funeral Home jijini Nairobi.

Mnamo Mei 2018 Dkt Ruto alimtembelea kiongozi huyo nyumbani kwake Kabarak lakini hakuweza kukutana naye huku ripoti zikiashiria kwamba Mzee Moi alikataa kukutana na Naibu Rais kutokana na chuki kati yao.

Hata hivyo, msemaji wa Bw Moi, Lee Njiru alieleza kwamba Rais huyo wa zamani alikuwa akifanyiwa uchunguzi na madaktari wake ndiposa mkutano huo haukufanyika.

Dkt Ruto na mwanawe Moi, Gideon ambaye ni Seneta wa Kaunti ya Baringo na mwenyekiti wa chama cha Kanu wamekuwa wakipigania ubabe wa kisiasa kila mmoja akitaka kuwa msemaji wa jamii ya Wakalenjin.

Wadadisi wanasema Gideon anapambana kudumisha jina la familia ya Moi katika ulingo wa kisiasa nchini.

Dkt Ruto ashauri maombolezo na mazishi ya Moi yasiingizwe siasa chafu

Na SAMMY WAWERU

NAIBU Rais Dkt William Ruto amesema safari ya kumpumzisha Rais Mstaafu Daniel Toroitich Arap Moi inafaa iwe tulivu na isihusishwe siasa chafu, “kwa kuwa ni baba yetu aliyetufanyia makuu”.

Dkt Ruto amesema wengi wa viongozi walio serikalini na pia wanasiasa walipitia mikononi mwa Mzee Moi, na kujumuisha siasa zisizo na mwelekeo katika harakati za kumpungia mkono wa buriani ni kumkosea heshima.

“Wengi wa viongozi tulioko serikalini na wanasiasa, karibu asilimia 60 tulipitia mikononi mwa Mzee Moi. Ametulea kisiasa. Moi alilea familia yake; wavulana na wasichana, pamoja na watoto wake kisiasa,” akasema Naibu wa Rais Alhamisi usiku kwenye mahojiano na kituo kimoja cha runinga.

Akionekana kushangazwa na tetesi kuwa hahusishwi katika maandalizi ya Rais huyo Mstaafu, Dkt Ruto alisema Mzee Moi ni kiongozi aliyefanyia Kenya mengi hususan maendeleo, akitaja sekta ya elimu kama aliyoipa kipau mbele katika utawala wake wa miaka 24.

“Anahitaji mapumziko ya hadhi, tuepuke siasa duni,” akasema.

Mzee Moi aliaga dunia mapema wiki hii, wakati akipokea matibabu katika Nairobi Hospital.

Saa chache baada ya kifo cha Rais huyo mstaafu kutangazwa, Dkt Ruto alihutubia taifa katika ofisi yake ya Harambee House Annex, jijini Nairobi, ambapo hakuwa ameandamana na afisa yeyote wa ngazi ya juu serikalini.

Baadaye, alifululiza hadi katika hifadhi ya maiti ya Lee Funeral, ambapo hakuna kiongozi aliyempokea.

Ni taswira ambayo Ruto amesalia kimya.

Waziri wa Usalama wa Ndani na Mikakati ya Serikali Dkt Fred Matiang’i, Mkuu wa Majeshi Samson Mwathethe na Inspekta Mkuu wa Polisi, IG, Hillary Mutyambai, waliandamana pamoja katika hifadhi ya Lee Funeral, na pia kuonekana kutoa mipangilio ya maombolezi ya Moi na mazishi yake, ambayo yatakuwa ya kitaifa.

Dkt Ruto na ambaye amewahi kuhudumu kwa karibu na Mzee Moi, alisema matamanio yake ni kuona marehemu amezikwa kwa njia ya heshima.

Alisema mara ya mwisho kuonana na Mzee Moi ilikuwa kati ya 2016 – 2017.

Rais Moi atazikwa Jumatano wiki ijayo, nyumbani kwake Kabarak, Kaunti ya Nakuru.

Rais Mstaafu Moi anazidi kukumbukwa kwa mengi aliyotenda

Na LAWRENCE ONGARO

RAIS mstaafu Daniel Arap Moi atakumbukwa kwa kuridhia hatua muhimu ya mchakato wa urejeshwaji wa mfumo wa vyama vingi kwa nchi ya Kenya.

Mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina, alituma salamu zake za pole alipozuru boma la Moi katika mtaa wa Kibera jijini Nairobi mnamo Jumatano.

Mbunge huyo alisema Moi anafaa kuheshimiwa sana kwa kuondoa kifungu cha 2A kilichoruhusu vyama vingi vya kisiasa kuingia nchini.

“Jambo hilo pekee ni muhimu kwa sababu atakumbukwa kwa miaka mingi kwa kuleta mabadiliko hayo licha ya wengi ‘kutabiri’ ya kwamba hilo halingetimia,” alisema Bw Wainaina.

Licha ya hayo alisema Bw Moi alifanya jambo la heshima na kung’atuka kutoka uongozini kwa heshima zake na kumkabidhi Bw Mwai Kibabi usukani mwaka wa 2002.

Aliongeza kuwa hata ingawa alisema kuwa atamkabidhi mwingine uongozi bado wengine walidai haingewezekana.

Jambo lingine la muhimu lililofanya akumbukwe na wengi ni kwamba shule za msingi zilipata fursa ya kunywa maziwa shuleni jambo lililosababisha watoto wengi kuhudhuria shule.

“Kutokana na mambo hayo matatu, Moi aliacha kielelezo ambacho kitakumbukwa na wengi katika kizazi kijacho,” alisema Bw Wainaina.

Bw James Karanja ambaye alikunywa maziwa ya ‘Nyayo’ anasema wanafunzi wengi walihudhuria shule bila kuchelewa kwa sababu ya kunywa maziwa shuleni.

“Mimi nakumbuka vyema ya kwamba wengi wetu tukiwa shule ya msingi hatukukosa kuhudhuria shule kwani tulijua ya kwamba tungekunywa maziwa shuleni. Hata familia maskini zilinufaika pakubwa na mradi huo wa kunywa maziwa shuleni,” alisema Bw Karanja.

Bw James Njuguna anakumbuka vyema wakimwimbia Moi njiani akielekea ziara za kukagua miradi ya maendeleo ambapo hakusahau kutoa fedha kidogo kwa wanafunzi wanywe soda.

“Nakumbuka vyema siku moja eneo la Nakuru tulimwimbia na baadaye akatoa pesa za soda kwa wanafunzi; jambo lililotufurahisha kabisa,” alisema Bw Njuguna.

Pia Moi alisifika kwa kufanya kazi kwa bidii bila kuchoka.

Imeelezwa alifanya mazoea kuingia Ikulu kabla ya saa moja za asubuhi na kuanza ziara zake za kukagua maendeleo mara moja.

Jambo lingine muhimu kwake ni kwamba alizuru karibu kila pembe ya nchi ya Kenya na kuelewa karibu kila kitu kilichotendeka nchini.

Wakuu wa mkoa hadi machifu walikuwa kiungo muhimu kwa utawala wa Moi ambapo waliweza kumjulisha karibu kila kitu kilichotendeka mashinani.

Serikali yatangaza Jumanne siku ya mapumziko Wakenya waomboleze Moi, mazishi kufanyika kesho yake

Na CHARLES WASONGA

SERIKALI imetangaza Jumanne, Februari 11, 2020, kuwa siku ya mapumziko kuwapa Wakenya nafasi kuomboleza Rais Mstaafu Daniel Arap Moi aliyefariki Jumanne Februari 4, 2020, katika Nairobi Hospital.

Tangazo hilo limetolewa Alhamisi na Mkuu wa Utumishi wa Umma Joseph Kinyua kwenye kikao na wanahabari nje ya jumba la Harambee.

Ibada ya wafu itafanyika siku hiyo Jumanne, Februari 11, 2020, katika uwanja wa michezo wa Nyayo.

Na mazishi yatafanyika Jumatano, Februari 12, 2020, nyumbani kwa marehemu, Kabarak, Kaunti ya Nakuru.

ONGARO: Yapo mengi atakayokumbukwa nayo Moi

Na LAWRENCE ONGARO

RAIS mstaafu Daniel Arap Moi aliyefariki Jumanne katika Nairobi Hospital ana historia ndefu ambapo atakumbukwa kwa kuiongoza Kenya, lakini pia kama mtu mnyenyekevu na mtulivu.

Alizaliwa mwaka wa Septemba 2, 1924, katika kijiji cha Kurieing’wo, Sacho, Wilaya ya Baringo kulingana na maelezo kwenye maandiko.

Akiwa na umri wa miaka minne pekee babake Kimoi arap Chebii alifariki.

Ingawa hivyo, mwaka wa kuzaliwa Moi unapingwa na watu wa karibu naye waliomjua vizuri.

Alibaki chini ya uangalizi wa nduguye mkubwa Bw William Tuitoek ambaye alimfaa pakubwa na kumwelekeza katika shughuli ya kulisha mifugo.

Baada ya kukamilisha masomo yake alijiunga na Chuo cha walimu cha Tambach Teachers’ Training College katika wilaya ya Keiyo kabla ya kuanza kazi ya ualimu.

Mara yake ya kwanza kujitosa katika ulingo wa siasa ilikuwa mwaka wa 1955 alipokuwa mwanachama mmojawapo wa LEGCO.

Mzee Moi alikuwa mmoja wa waanzilishi wa chama cha KADU kwa ushirikiano na Bw Ronald Ngala wa Pwani ambaye ndiye alikuwa kinara wa chama huku akiwa mwenyekiti wake.

Hata hivyo kwa upande wa siasa Moi alitajwa kama mkakamavu alipokuwa Makamu wa Rais huku akivumilia mawimbi makali yaliyomkabili kupitia wandani wa Rais wa kwanza wa Kenya Hayati Mzee Jomo Kenyatta.

Kila mara alipokosolewa na kupokea matusi kutoka kwa viongozi hao, Mzee Kenyatta alikuwa mstari wa mbele kumtetea na hiyo ilimfanya yeye kuhifadhi kiti hicho cha makamu wa rais kwa muda wa miaka 12.

Wakati mgumu zaidi aliopitia ni mwaka wa 1976 mjadala wa kubadilisha katiba ulipochacha huku wandani wa rais Kenyatta wakati huo wakitaka kumzuia asiwahi kuchukua nafasi ya urais iwapo nafasi hiyo ingebaki wazi.

Wale waliotaka mabadiliko hayo ni aliyekuwa Waziri wa Masuala ya Kigeni Dkt Njoroge Mungai,  aliyekuwa Waziri wa Fedha James Gichuru, aliyekuwa Waziri wa Ardhi Jackson Angaine, na aliyekuwa Waziri wa Ushirika na Maendeleo Paul Ngei.

Wakati huo pia kulikuwa na mrengo uliopinga kubadilishwa kwa Katiba nao ni wa aliyekuwa mbunge wa Mvita Shariff Nassir, na aliyekuwa mbunge wa Kajiado Kaskazini Stanley Oloi Tiptip pamoja na viongozi wengine 98.

Kulingana na mjadala wa kubadilisha Katiba, aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wakati huo Bw Charles Njonjo aliingilia kati na kuzima juhudi hizo wa viongozi hao walioshinikiza mpango huo.

Viongozi hao wote waliitwa na Rais Kenyatta mwaka wa 1976 kwa mkutano wa dharura katika Ikulu ya Nakuru, ambapo Rais aliwasuta na kuzima mjadala huo mbele ya Bw Njonjo ambaye aliidhinisha matamshi ya Kenyatta.

Kati ya mwaka wa 1977 na 78 mkuu wa polisi katika Bonde la Ufa Bw James Mungai alibuni kikosi maalum cha Ngoroko ambacho wakati fulani kiliweza pia kumhangaisha Rais Moi alipokuwa akielekea kwake Kabarak.

Hata hivyo kikosi hicho cha watu 250 kilivunjiliwa mbali mara tu Rais Moi alipochukua usukani huku afisa huyo wa polisi Bw Mungai akikimbilia ulaya nchini Uswisi akihofia kutiwa nguvuni.

Alilazimika kuchukua gari la serikali lililomfikisha Sudan, ambako aliabiri ndege na kutokomea Ulaya.

Baada ya kifo cha hayati Mzee Kenyatta mwaka wa Agosti 22, 1978, mwendo wa saa 9 za alfajiri mjini Mombasa, mkuu wa mkoa wa eneo hilo wakati huo Bw Eliud Mahihu, aliwasiliana na mzee Moi na kumwarifu ya kwamba ‘Taa ya Kenya imezimika’. Kwa hivyo alitakikana asafiri haraka Nairobi ili aapishwe kama rais wa pili.

Wandani wa mzee Kenyatta walishtushwa na habari hiyo huku rafikiye wa dhati Mbiyu Koinange,akipatwa na mshtuko mkubwa.

Baada ya kuapishwa kama rais alilazimika kukamilisha siku 90 kabla ya kushikilia usukani kamili.

Hata hivyo mapinduzi ya Agosti Mosi 1982, yalibadilisha mkondo wa uongozi wa Moi ambaye alikuwa mpole aligeuka kuwa mtu wa kipekee kwani hakumuamini yeyote yule na alikuwa na makachero kila sehemu hadi vijijini.

Mawaziri wengi walipata habari za kuteuluiwa nyadhifa zao kupitia taarifa ya habari ya KBC jambo lililofanya kila kiongozi kutekeleza wajibu wake kwa makini.

Ilipofika Machi 19, 2002, chama cha Kanu na NDP cha Raila Odinga viliungana na kufanya kazi pamoja.

Moi alichaguliwa kuwa Mwenyekiti, Raila Odinga akawa katibu mkuu naye Yusuf Haji alichaguliwa kama mwekahazina.

Wengine ni Uhuru Kenyatta, Musalia Mudavadi, Kalonzo Musyoka, na Katana Ngala ambao walikuwa manaibu wa mwenyekiti katika muungano huo.

Makamu wa Rais wakati huo marehemu Prof George Saitoti na Joseph Kamotho, wandani sugu wa Rais Moi walichujwa nje ya uchaguzi huo bila matarajio yao.

Siasa za kugeuza kipegee cha Katiba cha 2A ili kuwe na vyama vingi mwaka wa 1991 zilianza kugeuza siasa za nchi huku shinikizo zikitoka nchi za nje na mashirika za kutetea haki za wananchi zikija juu ili kuwe na mageuzi za uongozi.

Hata hivyo Mzee Moi alistaafu kwa heshima mwaka wa 2002 ambapo alimkabidhi mamlaka Bw Mwai Kibaki kama Rais wa tatu wa nchi ya Kenya naye akafululiza hadi kwake Kabarak ambako alikuwa akitembelewa na viongozi tofauti ili kupata ushauri kutoka kwake.

Baada ya kukabiliana na uzee na maradhi ya kimwili kwa miezi michache iliyopita aliaga dunia Februari 4, 2020, saa 5:20 alfajiri katika Nairobi Hospital.

Atwoli atoa salamu za pole kwa familia ya Moi, afananisha Nyayo na BBI

Na WANDERI KAMAU

KATIBU Mkuu wa Chama cha Kitaifa cha Wafanyakazi (Cotu-K) amesema kuwa Rais Mstaafu Daniel Toroitich Arap Moi alikuwa kiongozi wa kipekee aliyejali masilahi ya wafanyakazi.

Akiwahutubia wanahabari Jumatano katika makazi ya Mzee Moi katika Kabarnet Gardens, Nairobi, Atwoli amesema Mzee atakumbukwa kwa mchango wake katika sekta ya elimu.

Amesema falsafa ya Nyayo ambayo Mzee Moi alianzisha inafanana na Mpango wa Maridhiano (BBI) unaopigiwa debe na viongozi mbalimbali nchini kwa sasa.

“Furaha na fahari kuu ya Mzee Moi ilikuwa ni kuona umoja katika nchi. Mpango wa BBI ni mwendelezo wa ndoto hiyo,” amesema Bw Atwoli.

Mzee aenziwa kwa kuvumisha soka miaka ya 80

Na CECIL ODONGO

WANAMICHEZO wanaendelea kuomboleza kufuatia kifo cha Rais wa pili wa Kenya, Daniel Arap Moi aliyeaga dunia katika Nairobi Hospital.

Utawala wa Mzee Moi utakumbukwa kwa ujenzi wa uwanja wa Nyayo na ule wa Kimataifa wa MISC, Kasarani.

Uongozi wa klabu mbili kubwa nchini Gor Mahia na AFC Leopards, jana uliomboleza kifo cha Mzee Moi na kusema alichangia sana ufanisi ulioshuhudiwa miaka ya 80 na 90.

Mwenyekiti wa Gor Mahia Ambrose Rachier kwenye mahojiano na ‘Taifa Leo’, alisema Mzee Moi alipenda mchezo wa soka na alitoa msaada wa kifedha kwa klabu hiyo kila mara iliposhiriki mechi za Bara Ulaya na ligi ya nyumbani.

Rachier pia alithibitisha kwamba Mzee Moi aliipa klabu hiyo vipande viwili vya ardhi katika maeneo ya Embakasi na Kasarani.

Mapenzi yake kwa K’Ogalo yalishuhudia akifika uwanjani na kutazama ngarambe ya fainali ya Kombe la Mandela ambayo Gor ilipiga Esperance ya Tunisia na kutwaa ushindi.

“Mzee Moi alipenda michezo na alifika uwanjani Gor Mahia ilipokuwa ikishiriki mashindano mbalimbali. Ingawa alitupa vipande vya ardhi, inasikitisha kwamba hadi leo hatujapata hatimiliki japo tunaendeleza mchakato wa kuhakikisha tunazipata kutoka kwa serikali,” akasema Rachier.

Mwenyekiti wa AFC Leopards Dan Shikanda naye alisema walipewa ardhi na Mzee Moi na njia ya pekee ya kumuenzi kutokana na wema huo ni kuhakikisha wanapata hatimiliki ya ardhi hiyo iliyoko Kasarani.

“Natuma salamu za pole kwa familia ya Rais Mstaafu. Nilikuwa mchezaji alipotoa kipande hicho cha ardhi na najua mahali ipo. Kwa kuwa sasa mimi ni afisa wa klabu, nitajitahidi kuhakikisha tunapata hatimiliki ili kujenga pia uwanja wa mazoezi,” akasema Shikanda.

Aliyekuwa kocha wa Harambee Stars Jacob ‘Ghost’ Mulee pia alikumbuka jinsi aliwaalika Ikulu waliposhinda Kombe la Cecafa mnamo 2000.

“Mzee Moi alitukaribisha kwenye ikulu tuliposhinda taji la Cecafa Kagame na lilikuwa tukio la kupendeza mno. Kwa masikitiko hatukupewa fedha zozote lakini naamini maafisa walioandamana nasi walituchezea shere na kuchukua pesa zetu. Hakuna vile ungeenda Ikulu kisha ukose kupokezwa kitita enzi hizo,” akasema Mulee.

Nahodha wa zamani wa Harambee Stars Musa Otieno pia alituma salamu za pole kwa familia ya Mzee Moi na kusema alikuwa akihudhuria mechi za timu ya taifa.

Moi alihakikisha timu zimefadhiliwa vilivyo

AYUMBA AYODI na JOHN ASHIHUNDU

MWANARIADHA jagina Kipchoge Keino na Waziri wa Michezo Amina Mohamed waliongoza wapenzi wa michezo nchini kuomboleza kifo cha aliyekuwa Rais wa Kenya, Mzee Daniel Arap Moi aliyefariki Jumanne asubihi katika Nairobi Hospital.

Kadhalika, wakuu wa Kamati ya Kitaifa ya Olimpiki (Nock) na wale wa Chama cha Riadha Kenya (AK) walituma salamu zao za pole kufuatia kifo hicho.

Keino ambaye alikuwa kwenye timu ya taifa iliyovuma katika Michezo ya Olimpiki za 1968 na 1972, akiwakilisha taifa katika mbio za mita 1,500 na mita 3,000 alimtaja marehemu kama mtu aliyependa michezo.

Mwanariadha huyo mstaafu alisema Mzee Moi alihakikisha wanamichezo wanapata mazingara mazuri ya kuwafanya wafaulu.

“Kwa kuthibitisha madai yangu, Moi alijenga Nyayo Stadium mnamo 1983, akajenga MISC, Kasarani mnamo 1987. Alihakikisha viwanja vingine kama Ruring’u mjini Nyeri na Moi Stadium, Kisumu vinawekwa katika hali nzuri ya kuandaa michezo mbalimbali,” alisema Keino.

Kipchoge anaeleza kuwa kujengwa kwa viwanja hivi kuliiwezesha Kenya kupiga hatua kubwa michezoni, mbali na kupata fursa ya kuandaa mashindano mbalimbali ya kimataifa, pamoja na kuimarisha vipaji vya wanamichezo nchini ambao walivuma katika ngazi ya kimataifa.

Hata hivyo, mkongwe huyo alishutumu viongozi waliofuata kwa kuzembea katika jukumu hilo, huku akimsifu marehemi Moi kwa kuhakikisha vyuo vyote vikuu vya UoN na Kenyatta vimepata vifaa vya kisasa alipokuwa mamlakani.

“Moi alihakikisha timu zetu za kushiriki Michezo ya Olimpiki, Michezo ya Madola na mashindano mengine makubwa zimefadhiliwa ipasavyo na kufanya vyema.”

Kadhalika, Kipchoge anamkumbuka marehemu kwa kutambua wanamichezo walioletea taifa sifa za kimataifa.

“Wakati wake, hatukuwa na shida za ukosefu wa pesa za kugharamia timu ya taifa,” akasema.

Kwa upande wake, waziri Amina alimkumbuka marehemu Moi kama kiongozi aliyejali zaidi maisha ya akina mama na watoto. Moi alipenda kusaidia watoto wetu kupata elimu bora, kwa kuhakikisha kuna madarasa yanayofaa, mbali na maziwa kwa watoto wa shule.

‘Natoa salamu zangu za pole kwa Seneta Gideon Moi, familia nzima ya marehemu na Wakenya kwa jumla,” alisema Amina.

Taarifa ya Nock ilimwomboleza Moi kama shabiki mkubwa wa michezo wakati wote tangu Kenya ipate uhuru hata kabla ya kutwaa mamlaka mnamo 1978 kuongoza taifa hadi 2002.

Aliisaidia Kenya kupata tiketi ya kuandaa Michezo ya Bara Afrika kwa mara ya kwanza mnamo 1987 ambapo timu ya soka ilitinga fainali ya michuano hiyo kabla ya kushindwa 1-0 na Misri.

Moi anakumbukwa kwa kuwa katika kikosi cha Bunge FC cha miaka ya sitini ambacho pia kiliwajumuisha marehemu Tom Mboya, Bruce MacKenzie, Robert Ouma miongoni mwa wengine.

Nayo kamati ya AK ilipendekeza Serikali ihakikishe miradi yote aliyoanzisha Moi imekamilika kwa heshima yake.

Moi kupewa mazishi ya taadhima kuu

Na CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta ametangaza kipindi cha maombolezo ya kitaifa kufuatia kifo cha Rais wa zamani Daniel Arap Moi huku akiamuru bendera za kitaifa zipeperushwe nusu mlingoti kote nchini kuanzia leo Jumanne.

Kwenye taarifa rasmi kwa umma kuhusu kifo cha Rais huyo wa pili wa Kenya, Rais Kenyatta amesema kipindi hicho cha maombolezo kitadumu hadi siku ambapo Mzee Moi atazikwa.

Na Rais huyo mstaafu atapewa mazishi ya kitaifa yakiandamanishwa na heshima na taadhima zote za kijeshi, Rais Kenyatta akaongeza.

“Chini ya mamlaka niliyopewa kama Rais wa Jumhuri wa Kenya na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi yote nchini, naamuru kwamba kwa heshima ya kumbukumbu ya Marehemu Daniel Toroitich Arap Moi, natangaza kipindi cha maombolezo ya Kitaifa kuanzia leo (Jumanne) hadi wakati wa mazishi yake,” akasema kwenye taarifa hiyo iliyotumwa kwa vyumba vya habari.

Akaongeza: “Marehemu Daniel Toroitich Arap Moi atapewa Mazishi ya Kitaifa huku Heshima zote za Kiraia na Kijeshi zikitolewa.”

Awali, Rais Kenyatta alitangaza rasmi kifo cha Moi kilichotokea katika Nairobi Hospital ambako amekuwa akipokea matibabu kwa kipindi cha miezi minne.

“Ni kwa huzuni kuu, natangaza kifo cha Kiongozi Mkuu Afrika Mheshimiwa Daniel Toroitich Arap Moi, Rais wa Pili wa Jamhuri ya Kenya. Rais huyo wa zamani alifariki katika Nairobi Hospital asubuhi mnamo Februari 4, 2020, akiwa na familia yake,” Rais Kenyatta akasema kwenye taarifa.

“Sifa zake zinadumu nchini hadi siku ya leo (Jumanne), zikidhihirishwa ndani ya Filosofia ya Nyayo ya ‘Amani, Upendo na Umoja’ ambayo ilikuwa kaulimbiu yake alipihudumu kama Rais wetu.”

Katika hotuba fupi nje ya Nairobi Hospital Jumanne asubuhi mwanawe Seneta Gideon Moi alisema babake alifariki kwa utulivu.

Alisema familia inawashukuru kwa kumwombea Rais mstaafu alipokuwa amelazwa hospitalini humo akipokea matibabu.

“Nilikuwa kando yake, na kama familia tumekubali. Langu ni kutoa shukrani zangu kwa Wakenya wote kwa kuombea Mzee na familia yetu. Asanteni nyote,” amesema

Mwili wa Mzee Moi umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Lee, Nairobi.

Jinsi Moi alivyowakabili wapinzani na wakosoaji wake

Na WANDERI KAMAU

HAYATI Rais Mstaafu Daniel Moi atakumbukwa kwa kuwakabili vikali wale ambao walikosoa utawala wake.

Bw Moi hakujali ikiwa waliomkosoa walikuwa washirika wake wa karibu au la.

Miongoni mwa wale waliojikuta kwenye mkwaruzano wa kisiasa na Bw Moi ni Mwanasheria Mkuu wa zamani Charles Njonjo, mfanyabiashara Andrew Muthemba, wanachama wa kundi la Mwakenya, kiongozi wa ODM Raila Odinga, mwanasiasa Kenneth Matiba, Kasisi Timothy Njoya miongoni mwa wengine.

Masaibu ya Bw Njonjo yalianza kwenye mkutano mmoja wa Bw Moi Kaunti ya Kisii mnamo 1983.

Kwenye ziara katika eneo hilo, Bw Moi alisema kuwa baadhi ya nchi za Magharibi zilikuwa zikipanga kumsaidia mmoja wa “wasaliti wake” (Njonjo) kutwaa uongozi.

Kilichofuatia ni njama za kumhangaisha Bw Njonjo, wakati huo akihudumu kama Waziri wa Masuala ya Kikatiba.

Mahasimu wake wa kisiasa waliungana kumtaja kuwa “msaliti.”

Njonjo alijitosa siasani mnamo 1980 baada ya kustaafu kama Mwanasheria Mkuu.

Alitumia washirika aliobuni akiwa Mwanasheria Mkuu na ukaribu wake na Bw Moi kujijenga kama mojawapo ya wanasiasa wenye ushawishi mkubwa zaidi nchini.

Kwenye harakati hizo, alipata mahasimu wengi, kulingana na kitabu Moi: The Making of an African Statesman kilichoandikwa na Bw Andrew Morton.

Hatua ya Bw Njonjo kujitosa kwenye siasa pia ilizua uhasama kati yake na Rais Mstaafu Mwai Kibaki, aliyekuwa Makaku wa Rais.

Muda mfupi baada ya mkutano wa Kisii, mbunge wa Kericho ya Kati Francis Mutwol, alimtaja Njonjo kuwa “msaliti aliyepania kutwaa mamlaka kama rais, hata bila ya kuhudumu kama waziri.”

Kilichofuatia kilikuwa msururu matukio ya kumhangaisha Bw Njonjo, hali iliyomfanya kujiuzulu kama Waziri na Mbunge.

Bw Moi alibuni tume maalum ya kumchunguza mnamo Julai 1983, ambapo alipatikana na hatia.

Mnamo Juni 29, 1983, mbunge wa Butere Martin Shikuku aliwasilisha stakabadhi Bungeni akidai kwamba Bw Njonjo alimiliki biashara za siri nchini Afrika Kusini, na alikuwa ameingiza silaha hatari nchini kinyume cha sheria ili kuipindua serikali.

Licha ya kupinga madai hayo, Bw Njonjo aliondolewa serikalini na tume maalum iliyobuniwa ili kumchunguza.

Siku iliyofuata, aliondolewa kutoka chama cha Kanu, hali iliyomfanya kujiuzulu kama mbunge.

Mnamo Julai 1983 Bw Moi aliivunja Bunge mapema na kuandaa uchaguzi mnamo Septemba ili kuwaondoa wanasiasa walioonekana kumuunga mkono Bw Njonjo.

Licha ya kupatikana na hatia na tume hiyo mnamo 1984, Bw Moi alimsamehe Bw Njonjo. Hata hivyo, ushawishi wake siasani ulipungua kabisa.

Andrew Muthemba

Mnamo Machi 19, 1981, Wakenya waliamkia habari kwamba mfanyabiashara Andrew Muthemba kutoka Nairobi amekamatwa na kufunguliwa mashtaka kuhusu njama za kuipindua serikali.

Kulingana na mashtaka, Bw Muthemba alituhumiwa kwamba kati ya Desemba 15, 1980, na Februari 23, 1981, alikuwa “amedhamiria na kupanga njama za kumpindua Bw Moi kama Rais wa Kenya.”

Mashtaka dhidi ya Bw Muthemba yalijiri wakati Bw Moi alikuwa mwenye hofu kuhusu njama za kumwondoa mamlakani.

Mnamo Aprili 1980, alikuwa ameonya kwamba angewakamata wale waliokuwa wakipinga utawala wake na kuwaweka gerezani.

Kilichojulikana ni kuwa kati ya Desemba 15, 1980 na Februari 23, 1981, Bw Muthemba alikuwa amejaribu kupata usaidizi wa Koplo Joseph Njiru kuiba grunedi kumi na mabomu kadhaa.

Vilevile, alikuwa amejaribu kuomba msaada wa Kapteni Ricky Waithaka kuiba grunedi 100 kati ya silaha zingine za vita.

Katika kujitetea kwake, Bw Muthemba alimwambia Hakimu Fidahussein Abdullah kwamba “alikuwa akitekeleza majukumu yake kama kawaida.”

Polisi hawakuamini kauli yake.

Bw Muthemba alisema kwamba alikuwa akichunguza utoaji wa vibali vya kufanyia kazi kwa raia wa kigeni nchini kinyume cha sheria kwa ufahamu wa Bw Njonjo, aliyehudumu kama Waziri wa Masuala ya Kikatiba.

Serikali ya Moi ilianza kuwa yenye tashwishi kutokana na uhusiano wa karibu kati ya mfanyabiashara huyo na Bw Njonjo.

Kwa kumtaja Njonjo kwenye kesi yake, Muthemba alitumaini kwamba angemsaidia kujitoa kwa masaibu yaliyomkumba. Hata hivyo, hakufahamu kwamba Bw Njonjo pia alikuwa amelengwa na serikali ya Moi.

Ingawa kesi yake ilisikilizwa na kufutiliwa mbali baadaye, Bw Muthemba alisisitiza kuwa maafisa wote wakuu serikalini walifahamu kuhusu harakati zake za kutaka kuchunguza utoaji vibali vya kufanyia kazi nchini. Alidai kusalitiwa kwa kuwa jamaa wa Bw Njonjo.

Mwakenya

Baada ya kuifanya Kenya kuwa nchi ya chama cha Kanu pekee kufuatia jaribio la mapinduzi mnamo 1982, wanaharakati nchini walibuni kundi la Mwakenya (Muungano wa Wazalendo wa Kenya) ulioegemea mfumo wa utawala wa ujamaa.

Muungano huo uliwashirikisha wanahabari, wahadhiri, viongozi wa kidini na wanasiasa. Kundi hilo lilimlaumu Moi kwa maovu kama ufisadi, ukabila na ubadhirifu wa fedha za umma.

Wanaharakati hao pia walimtaka Bw Moi kurejesha mfumo wa vyama vingi nchini kwa kukifanyia mageuzi kipengele 2 (a) cha Katiba.

Msemaji wake mkuu alikuwa mwandishi maarufu wa vitabu Prof Ngugi wa Thiong’o.

Muda mfupi baada ya jaribio hilo, Shirika la Ujasusi (Special Branch) lilianza operesheni kali ya kuwakamata wale waliodaiwa kushiriki.

Waliokamatwa kwanza ni mhadhiri Maina wa Kinyatti, Prof Katama Mkangi, mwanasiasa Wanyiri Kihoro na Paddy Onyango.

Wengine waliokamatwa ni Kiongo Maina, Mwandawiro Mghanga, mwandishi Wahome Mutahi, Lumumba Odenda na Oduor Ong’wen.

Wengi wao walikamatwa na kufungwa gerezani bila kufunguliwa mashtaka. Wengine walidhulumiwa katika majumba ya dhuluma ya Nyayo na Nyati jijini Nairobi.

Bw Moi aliwaambia Wakenya kwamba wanachama wa muungano huo hawakuwa Wakenya, bali wasomi na wanaharakati ambao walikuwa wakiendeleza ajenda na maslahi ya nchi za kigeni.

Alisema kuwa wote walikuwa na paspoti ambapo wangetoroka nchini mara tu serikali ingeanza kuwakabili.

Mnamo 1992, mama za wanaharakati kutoka eneo la Kati ambao wanao walikuwa wamekamatwa kwa kujihusisha na kundi hilo walikusanyika katika Bustani ya Uhuru Park jijini Nairobi, wakimtaka Bw Moi kuwaachilia.

Miongoni mwa waliokuwepo ni Mshindi wa Tuzo la Nobel marehemu Wangari Mathai na Bi Monicah Wangu, mamake aliyekuwa mbunge wa Subukia Bw Koigi wa Wamwere.

Serikali ya Moi iliwatuma maafisa wa usalama kuwatawanya. Hata hivyo, walilipiza kisasi kwa kutoa nguo zao zote. Kufikia Julai 1993, wanaharakati wote walikuwa wameachiliwa.

Raila Odinga

Bw Odinga aliwekwa kizuizini nyumbani kwake baada ya ushahidi wa mwanzo kuonyesha kuwa alishirikiana na wale waliopanga jaribio la mapinduzi mnamo 1982 dhidi ya Bw Moi.

Baadaye, alifunguliwa mashtaka ya uhaini na kufungwa miaka sita gerezani bila kufunguliwa mashtaka.

Aliachiliwa mnamo Februari 1988 lakini akakamatwa tena mnamo Septemba mwaka uo huo.

Aliachiliwa mnamo Juni 1989 lakini akakamatwa tena mnamo Julai 1990 pamoja na mwanasiasa Kenneth Matiba na mwenzake Charles Rubia.

Matiba na Rubia

Chini ya maagizo ya Bw Moi, Bw Matiba alifungwa gerezani bila kufunguliwa mashtaka yoyote katika Gereza la Kamiti pamoja na Bw Rubia.

Wawili hao walishtakiwa kwa kushinikiza mageuzi ya Katiba ili kuruhusu uwepo wa vyama vingi ya kisiasa.

Akiwa gerezani, Bw Matiba alinyimwa nafasi ya kutibiwa, hali iliyomfanya kuugua kiharusi hadi kufariki kwake mnamo 2018.

Njoya na Muge

Serikali ya Bw Moi pia iliwakabili vikali viongozi wa kidini ambao walitumia nafasi na ushawishi wao kuikosoa.

Miongoni mwa wale ambao walijipata pabaya ni Kasisi Timothy Njoya wa Kanisa la PCEA, Askofu Alexander Kipsang Muge wa Kanisa la Anglikana (ACK) miongoni mwa wengine.

Njoya alikuwa mmoja wa viongozi wa maandamano ya Sabasaba mnamo Julai 7, 1990, yaliyoshinikiza kuanzishwa kwa mfumo wa vyam vingi nchini.

Hata hivyo, Njoya alikamatwa na kupigwa vibaya na polisi, kwa kushiriki kwenye maandamano hayo.

Naye Askofu Muge alifariki katika hali tatanishi mnamo Agosti 14, 1990, muda mfupi baada ya kuonywa na aliyekuwa Waziri wa Leba Peter Okodo dhidi ya kwenda Busia.

Hadi sasa, chanzo cha kifo chake hakijawahi kubainika.

Miradi ya Daniel Moi

Na CHARLES WASONGA

RAIS mstaafu Daniel Moi ambaye amefariki mapema Jumanne, wakati wa uhai wake alianzisha miradi mbalimbali ambayo inaakisi kumbukumbu ya utawala wake wa miaka 24.

Mojawapo ya miradi hiyo ni mfumo wa sasa wa elimu wa 8-4-4 ulioanishwa mnamo mwaka wa 1985 ambapo mwanafunzi anasoma kwa miaka minane katika shule ya msingi, miaka minne katika shule ya upili na miaka minne katika chuo kikuu au vyuo vya kadri.

Mfumo huu, ambao serikali inapanga kuufutilia mbali, ulichukua mahala pa mfumo wa zamani wa 7-4-2-3. Chini ya mfumo huu mwanafunzi alisoma kwa miaka saba katika shule ya msingi, kisha miaka nne katika kiwango cha chini ya shule ya upili (O-Level), kisha anajiunga na kidato cha tano na sita (maarufu kama A-Level) na miaka mitatu katika chuo kikuu.

Kimsingi, mfumo wa 8-4-4 ulianzisha masomo ya kiufundi kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne lengo likiwa ni kumpa mwanafunzi ujuzi ya kumwezesha kujitegemea maishani baada ya kufanya mtihani wa kitaifa wa darasa la nane (KCPE) na ule wa kidato cha nne (KCSE).

Watoto walifunzwa masomo kama vile; useremala, ushonaji nguo, uashi, muziki, sanaa ya uchoraji miongoni mwa masomo mengine ya kiufundi.

Lakini baada ya miaka kadhaa serikali ilianza kuonyesha dalili za kushindwa kufikia malengo asilia ya mfumo huu kwani ilishindwa kufadhili ujenzi wa karakana za kuendeshea masomo ya kiunfundi katika shule zote za umma.

Hatimaye katika miaka ya 1990s serikali iliifanyia mageuzi mfumo huo wa elimu kwa kuondoa masomo ya kiufundi kwenye orodha ya masomo ya lazima ya kutahiniwa katika mitihani ya KCPE na KCSE. Hata hivyo, masomo hayo yameendelea kufundishwa katika vyuo vikuu, vyuo vya kadri na vyuo anuwai.

Ni baada ya serikali ya sasa kung’amua kuwa mfumo wa 8-4-4 umekuwa ukizingatia zaidi uwezo wa mwanafunzi kupita mitihani ya kitaifa na kukosa umilisi wa masomo aliofundishwa ndipo ikaamua kuanzisha mfumo mpya wa elimu wa 2-6-3-3-3.

Chini ya mfumo huu mtoto atasoma kwa miaka miwili katika shule ya chekechea, miaka sita katika shule ya msingi, miaka mitatu katika daraja la chini la shule ya upili, miaka mitatu katika daraja la juu shule za upili na miaka mitatu katika vyuo vikuu.

Lakini akiongea katika shule ya upili ya Sunshine, Nairobi mnamo 2016 Mzee Moi alipinga kuondolewa kwa mfumo wa 8-4-4 akisema wale waliopitia mfumo huu wameng’aa kimasomo katika mataifa ya ng’ambo kama vile Amerika, Japan, na Uingereza.

“Isitoshe, kizazi cha sasa cha viongozi na wataalamu walipitia mfumo wa 8-4-4 na utendakazi wao umekuwa wa kupigiwa mfano,” akasema.

Mabasi ya Nyayo

Mabasi ya Uchukuzi ya Nyayo (NBS) yalianzishwa na Rais mstaafu Daniel Moi mnamo 1986 kwa lengo la kutoa huduma za uchukuzi jijini Nairobi. Mwanzoni, idadi ya mabasi yaliyozinduliwa ilikuwa 20.

Sababu ni kwamba serikali ilidai mabasi ya kampuni ya Kenya Bus Services (KBS) yalilemewa na ongezeko la idadi ya watu jijini nyakati hizo.

Lakini wakosaoji wa mpango huo walidai kuwa serikali alianzisha mabasi ya Nyayo kwa sababu ilitaka kudumaza kampuni ya KBS iliyoingia nchini mnamo 1934 ikiitwa Oversees Transport Company (OTC) baada ya kampuni hiyo ya Uingereza kukataa kuiuzia sehemu za hisa zake.

Mabasi hayo, ya rangi ya kijani kibichi yalikuwa yakitoza nauli nafuu kuliko mabasi ya KBS na wahudumu wake walitoka Shirika la Vijana kwa Huduma ya Taifa (NYS).

Kwa hivyo, mabasi hayo yalipendwa na wananchini kiasi kwamba miaka miwili baadaye, mnamo 1988, idadi ya mabasi hayo iliongezeka hadi 89. Iliingiza faida ya Sh9 milioni katika kipindi hicho cha miaka miwili kulingana na ripoti za vyombo vya habari zilizomnukuu mkurugenzi mkuu wa kampuni hiyo wakati huo Geoffrey Griffins.

Na katika miaka ya 1990s idadi ya mabasi ya NBS iliongezeka hadi zaidi ya 300 na huduma zake zikasambazwa kutoka Nairobi hadi maeneo mengine ya nchini.

Lakini kuanzia mwaka wa 1994, kutokana na usimamizi mbaya na ufisadi miongoni mwa wafanyakazi na wasimamizi wa mabasi hayo, kampuni hiyo ilianzia kufifia.

Mnamo Julai 1994 iliripotiwa kuwa kati ya mabasi 367 ambayo yalikuwa yakihudumu kote nchini ni mabasi 55 pekee ilikuwa imesalia barabarani huku mengine yakiwa yamekwama.

Hatimaye mnamo 1997 kampuni hiyo ilisitisha shughuli na mamia ya Wakenya kutoka NYS na vyuo vikuu wakaachwa bila ajira.

Siku hizi baadhi ya mabasi hayo, ambayo yamechakaa, yameagezwa katika karakana ya NYS eneo la Ruaraka. Mnamo 2004 serikali iliunza baada ya mabasi hayo, kuwa njia ya mnada.

Mwaka 2018 serikali ya Jubilee ilijaribu kuanzisha upya huduma za mabasi hayo jijini Nairobi lakini kwa kuzindua mabasi 27 lakini mpango huo umegonga mwamba.

Mabasi hayo yalikuwa yakihudumu katika ruti za mitaa ya Kibera, Githurai, Mwiki, Kariobangi, Mukuru Kwa Njenga, Dandora na Kawangware na katikati mwa jiji huku yakitoza nauli ya Sh20 pekee.

Hata hivyo mabasi hayo yamekuwa mara kwa mara yakisitisha huduma kutokana na kile kilichotajwa kama “kupanda kwa gharama ya utunzaji na huduma nyinginezo”.

Jinsi Moi alivyoenziwa kwa namna mbalimbali ikiwa ni pamoja na nyimbo

Na CHARLES WASONGA

NYIMBO nyingi zilitungwa kumsifu Hayati Rais (mstaafu) Daniel Moi na utawala wake uliodumu kwa kipindi cha miaka 24.

Wadadisi wanasema watunzi wa nyimbo hiyo walishawishiwa kuzitunga kama sehemu ya mpango mzima wa kukita falsafa ya Moi miongoni mwa Wakenya.

Hii ndio maana makundi ya kwaya, wanamuziki wa kibinafsi waling’ang’ania nafasi ya kumtumbuiza Moi wakati wa hafla za kitaifa na katika ziara zake kote nchini.

Nyimbo kama vile, “Tuashangilie Kenya” na “Tawala Kenya Tawala”, zilizotungwa msanii Thomas Wesonga ziliondokea kuwa maarufu zaidi wakati wa sherehe za kitaifa na hafla za chama tawala nyakati hizo-Kanu.

Ingawa ilidaiwa kuwa nyimbo kama hizo zilikuwa za kizalendo, ukweli ni kwamba zililenga kuvumisha na kuendeleza utawala wa Moi pamoja na chama cha KANU.

Njia nyingine ambayo Moi alitumia kukita utawala wake mawazoni mwa Wakenya ni kupitia vyombo vya habari.

Alihakikisha kuwa kila siku asilimia 80 ya taarifa za habari katika iliyokuwa Sauti ya Kenya (VOK), sasa Shirika la Habari Nchini (KBC) zilihusu shughuli alizoshiriki. Shughuli hizo ni kama vile michango ya harambee, ziara zake za ng’ambo, uzinduzi wa miradi ya serikali yake, ibada za Jumapili, miongoni mwa nyingine.

“Kwa njia hii Wakenya walielekezwa kuamini kuwa Moi ndiye alikuwa kiongozi pekee ambaye aliongoza katika kila kitu. Alichukulia kama mkulima nambari moja, mwalimu nambari moja na mwanasiasa nambari moja,” anasema mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Edward Kisiang’ani.

Kwa upande mwingine, taasisi za nyingi za umma zilipewa jina la Moi katika mpango huo huo wa kuendeleza falsafa ya uongozi wake. Shule za msingi na zile za upili, vyuo vya kiufundi, vyuo vikuu, hospitali za umma, viwanja vya michezo na asasi nyinginezo zilizoanzishwa wakati wa utawala wake, zilitajwa kwa jina lake.

Taasisi hizi zilipatikana katika tarafa, wilaya na mikoa mbalimbali nchini.

“Kwa namna hii, Mzee Moi alihakikisha kuwa amekolea katika fikra za Wakenya kila siku. Lengo hapa lilikuwa ni kuhakikisha Wakenya hawangewaza kuhusu kiongozi mwingine – hasa mwanasiasa – isipokuwa Moi,” anaeleza Profesa Kisiang’ani ambaye ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Kenyatta.

Hii ndio maana, anasema, ndio maana wanasiasa kama vile marehemu JJ Kamotho, Oloo Aringo, Wilson Letich miongoni mwa wengi walimuezi Moi kiasi cha kumuabudu.

Katika mkutano wa kisiasa eneo la Rift Valley mnamo 1999, marehemu Kamotho alipiga magoti mbele ya Moi jukwaa ili amnong’onezee jambo. Naye Bw Aringo alipenda kumsifu kama Mfalme wa Amani huku Leitich akitisha kukata kidole cha mtu yeyote ambaye angethubutu kumtusi Moi na chama cha Kanu.

Wanasiasa hawa walifanya haya yote kuonyesha uaminifu kwa Moi ili waendelea kudumu siasani.

Uhuru aiga Moi kuzima wakosoaji

Na MWANDISHI WETU

RAIS Uhuru Kenyatta ameiga mbinu za mlezi wake wa kisiasa, Rais Mstaafu Daniel Arap Moi kuwazima wanaokosoa utawala wake hasa wanasiasa.

Kati ya mbinu hizo ni kulemaza upinzani, kuwafuta kazi wanaoonekana kwenda kinyume na matakwa yake, kuvunjwa kwa mikutano ya kisiasa, kutumia polisi kuwanyanyasa na kuwatisha wakosoaji pamoja na kuanzisha uchunguzi wa madai ya uhalifu dhidi yao mara wanapoanza kukosoa utawala wake.

Rais Kenyatta sawa na Mzee Moi amefanikiwa kuhakikisha upinzani umekuwa dhaifu kwa kuwavuta wabunge wa upinzani upande wake alivyofanya Rais Kenyatta aliporidhiana na viongozi wa upinzani Raila Odinga na Kalonzo Musyoka.

Wakati wa utawala wake wa miaka 24, Mzee Moi alikuwa akiwafuta maafisa wa serikali kiholela kila alipohisi walikuwa wakikosoa utawala wake, sawa na alivyofanya Rais Kenyatta wiki iliyopita alipomfuta kazi aliyekuwa waziri wa kilimo, Mwangi Kiunjuri.

Ingawa awali alikuwa amemuonya Bw Kiunjuri kuhusu usimamizi wa sekta ya kilimo pamoja na sakata katika wizara, Rais hakumchukulia hatua hadi alipoanza kukosoa ripoti ya Jopokazi la Maridhiano (BBI) na kutangaza wazi anaegemea upande wa Naibu Rais William Ruto.

Mnamo Jumatatu wiki hii Bw Kiunjuri alihojiwa na maafisa wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) kuhusu baadhi ya sakata hizo ambazo zilisahaulika alipokuwa ndani ya serikali.

Chini ya utawala wa Mzee Moi, waliokosoa maamuzi yake walichukuliwa kuwa maadui wa serikali, walihangaishwa na maafisa wa polisi na hata kufunguliwa mashtaka na kutupwa jela ili kuwafunga midomo.

Kwa wale walioonyesha uaminifu kwake, Mzee Moi aliwatunuku vyeo na fursa zingine, lakini mara walipoanza kukosoa maamuzi ama sera zake waliona cha mtema kuni. Rais Kenyatta ameiga mbinu hii kwa wandani wake wanaomkosoa kama vile mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria.

Mbali na kukamatwa na kulala seli kwa siku mbili kwa madai ya kupiga mwanamke, Bw Kuria, ambaye amekuwa akikosoa sera za Rais Kenyatta, ameanza kuchunguzwa kwa madai ya kutoa zabuni za miradi ya hazina ya eneobunge lake (CDF) kwa watu wa familia yake katika kipindi chake cha kwanza akiwa mbunge.

Madai hayo hayakuibuka wakati ambao Bw Kuria alikuwa mtetezi mkuu wa utawala wa Jubilee.

Sawa na ilivyokuwa chini ya utawala wa Moi, utawala wa Rais Kenyatta umekuwa ukivunja mikutano ya kisiasa ya wanaopinga na kukosoa serikali kufuatia “amri kutoka juu”.

Katika kisa cha hivi punde, polisi walifuta mkutano mjini Mumias wa wabunge na wanasiasa wa eneo la Magharibi waliopinga mkutano wa BBI katika uwanja wa Bukhungu, Kaunti ya Kakamega.

Ingawa walikuwa wamewapa wabunge hao kibali cha kuandaa mkutano huo, duru zilisema baadaye waliamrishwa kuupiga marufuku na kuhakikisha haujafanyika.

Wanaharakati wanasema kutumia polisi kuvunja mikutano ya amani na kukandamiza uhuru wa kukutana, kujieleza na kushirikana ni ukiukaji wa Katiba.

Hali ilikuwa hivyo chini ya utawala wa Mzee Moi ambapo alikuwa akitumia maafisa wa usalama kutisha na kuwaandama waliomkosoa.

Mzee Moi pia alikuwa akiwapokonya walinzi maafisa wa serikali wakiwemo wabunge na mawaziri walitofautiana naye kama njia moja ya kuwatisha.

Wiki hii wabunge kadhaa akiwemo Bw Kuria na Kimani Ngunjiri (Bahati), ambao ni wakosoaji wakubwa wa Rais Kenyatta, walipokonywa walinzi na leseni zao za kumiliki silaha zikafutiliwa mbali.

Rais Kenyatta pia ameiga mlezi wake kisiasa katika vita dhidi ya ufisadi, ambapo anaapa kujitolea kukabili uovu huo na wakati huo huo utawala wake unachukua hatua za kulemaza Idara ya Mahakama, ambayo ina jukumu kubwa katika kupiga vita wizi wa mali ya umma.

Jubilee imelaumiwa kwa kulemaza vita dhidi ya ufisadi kwa kupunguzia mahakama pesa na kukosa kuidhinisha uteteuzi wa majaji licha ya kusisitiza kuwa serikali imejitolea kupambana na uovu huo.

Mbinu nyingine ni kutengwa kwa wakosoaji wa serikali kama ilivyofanyika wiki jana Mbunge wa Bahati David Gikaria na Seneta Susan Kihika wa Kaunti ya Nakuru walipozuiwa kuhudhuria mkutano wa Rais uliofanyika Nakuru.

Mwombeeni Mzee Moi, Gideon arai Wakenya wakumbuke babaye

Na FRANCIS MUREITHI

SENETA Gideon Moi wa Baringo amesema kuwa hali ya afya ya Rais Mstaafu Daniel Moi si nzuri, lakini anaendelea kupata nafuu.

Mzee Moi, 95, amelazwa katika Nairobi Hospital mara tatu mwaka huu. Taarifa kuhusu afya yake zimekuwa zikitolewa na msimamizi wake wa mawasiliano Bw Lee Njiru pekee.

Bw Moi alitoa kauli hiyo mnamo Ijumaa alipoongoza hafla ya kufuzu mahafali katika Chuo Kikuu cha Kabarak. Bw Moi aliwaomba Wakenya kuendelea kumwombea babake.

“Ningetaka kumshukuru kila mmoja wenu kwa niaba ya familia yangu kwa maombi yenu. Nawaomba kukubali shukrani zetu kwa kuendelea kumwombea Mzee Moi katika wakati huu ambapo hali yake ya afya si nzuri sana.

Kwa maombi, hali yake imekuwa ikiimarika kila siku,” akasema.

Kuhusu ufisadi, aliutaja kama “janga ambalo linaendelea kuwathiri vijana na ukuaji wa uchumi wa nchi.”

Aliwaomba mahafali 922 waliofuzu kwenye vitengo mbalimbali kuzingatia uwajibikaji na uzalendo na kujali maslahi ya wengine.

“Kutoka kwenu, tunatarajia kwamba mtakuwa na mienendo itakayomfaa kila mmoja katika jamii. Mnapaswa kuzingatia ukweli, hata wakati msimamo huo haumpendezi kila mtu,” akasema.

Spika wa Seneti Bw Keneth Lusaka, ambaye ndiye alikuwa mgeni mkuu mwalikwa, alisema kuwa suala kuu lililopo nchini kwa sasa ni jinsi ya kuhakikisha kuwa mfumo wa ugatuzi utamfaidi kila Mkenya.

‘Mzee Moi anaendelea vyema hospitalini’

Na ERIC MATARA

RAIS Mstaafu Daniel arap Moi anaendelea vyema na matibabu katika Hospitali ya Nairobi ambapo amelazwa.

Msemaji wake, Bw Lee Njiru Jumatano alisema Mzee Moi, 95, anatarajiwa kupata nafuu hivi karibuni ili aruhusiwe kurudi nyumbani.Alilazwa kwa mara nyingine Jumamosi, siku mbili tu baada ya kuruhusiwa kwenda nyumbani.

“Anaendelea vyema na anatarajiwa kukaa hospitalini hadi wakati madaktari wake wakiongozwa na Dkt David Silverstein watakapomruhusu kuondoka,” akasema Bw Njiru.

Ingawa hakutoa maelezo zaidi kuhusu ni lini Mzee Moi ataondoka hospitalini, alisema familia yake itatoa taarifa nyingine kesho kuhusu hali yake ya afya.

Kwa niaba ya familia ya Mzee Moi, msemaji huyo aliomba Wakenya na vyombo vya habari kujiepusha na uenezaji habari za kushtua kuhusu hali yake ya afya.

“Taarifa kuhusu afya yake zitatolewa kadri na jinsi inavyohitajika. Kwa sasa, Mzee Moi yuko thabiti na anaendelea kupokea matibabu kutoka kwa wataalamu wa kimatibabu wakiongozwa na daktari wake wa kibinafsi, Dkt David Silverstein,” akasema Bw Njiru.

Rais huyo wa zamani ambaye alilazwa hospitalini katika chumba cha watu mashuhuri alipelekwa huko mara ya kwanza Oktoba 12, ambapo familia yake ilisema alikuwa ameenda kwa ukaguzi wa kawaida wa kimatibabu.

Aliruhusiwa kuondoka hospitalini Alhamisi iliyopita baada ya kulazwa kwa wiki mbili, ikisemekana alikuwa akiugua maradhi ya kifua.

Mzee Moi alihitimisha umri wa miaka 95 mnamo Septemba 2, 2019.

Mwanafunzi mjanja wa Moi

Na BENSON MATHEKA

RAIS Uhuru Kenyatta amejitokeza kuwa kiongozi mjanja wa siasa sawa na alivyokuwa mlezi wake wa kisiasa, Rais mstaafu Daniel Moi hasa katika kumaliza nguvu taasisi kuu za kuendeleza demokrasia.

Ingawa anatawala katika mazingira tofauti na Mzee Moi aliyehudumu chini ya katiba iliyompa nguvu na mamlaka makuu, Rais Kenyatta amekuwa akitumia mbinu zinazofanana na alizotumia rais huyo wa pili wa Kenya kuzima upinzani na wanaokosoa serikali yake.

Wadadisi wanasema kwa sababu ya mipaka aliyowekewa na katiba ya sasa, Rais Kenyatta anatumia ujanja wa kisiasa kusukuma ajenda za serikali hata kama zinapingwa na Wakenya wengi, hatua ambayo imezorotesha demokrasia.

VYAMA VYA UPINZANI NA BUNGE

Hatua ya kwanza ya Rais Kenyatta katika kipindi chake cha pili cha utawala ilikuwa ni kumaliza upinzani dhidi ya serikali yake, sawa na alivyofanya Mzee Moi mnamo 1982 alipobadilisha katiba na kuweka kifungu cha 2A kufanya Kenya nchi ya chama kimoja.

Kutokana na vikwazo vya kikatiba, Rais Kenyatta alitumia mbinu iliyojaa ujanja. Kwanza aliunganisha vyama vya kisiasa kabla ya uchaguzi mkuu wa 2017 ili kuunda chama cha Jubilee Party.

Hatua hii ilikuwa sawa na ile Mzee Moi aliyotumia 1997 wakati alipomrai Raila Odinga kuunganisha chama chake cha National Development Party (NDP) na Kanu ili kubuni New Kanu.

Msumari wa mwisho uliolemaza upinzani ulikuwa ni handisheki na Bw Odinga, jambo ambalo lilizima sauti za wakosoaji ndani na nje ya bunge.

Hatua hii imempa Rais Kenyatta uhuru wa kupitisha kila anachotaka bungeni bila pingamizi zozote kwani waliokuwa wapinzani hasa katika ODM sasa wanacheza ngoma ya Jubilee.

VYOMBO VYA HABARI

Chini ya utawala wake, Mzee Moi hakuruhusu uhuru wa habari kunawiri inavyohitajika katika demokrasia.

Alihakikisha Wakenya walitegemea shirika la KBC pekee kupata habari, kuwanyima leseni watangazaji huru, kupiga marufuku majarida yaliyokosoa utawala wake pamoja na wanahabari kutishwa, kukamatwa na kutupwa kizuizini kwa madai ya uhaini.

Rais Kenyatta kwa upande wake amekuwa akilaumu vyombo vya habari kila vinapofichua kashfa ama kukosoa serikali yake, pamoja na kudhalilisha magazeti machoni pa umma hasa anaposema ni “ya kufunga nyama”.

Wanablogu wa serikali nao wamekuwa wakiwashambulia baadhi ya wanahabari ama mashirika ya habari yanayojaribu kukosoa utawala wa Jubilee.

Serikali pia imelemaza vyombo vya habari kifedha kwa kupunguza matangazo.

MASHIRIKA YA KIJAMII

Serikali imekuwa ikizima mashirika ya kijamii kupitia vitisho na kuyawekea vikwazo vya kisheria.

Baadhi ya wanaharakati wamekuwa wakikamatwa wakijaribu kuandamana kulalamikia au kupinga sera na maamuzi ya serikali licha ya kuwa maandamano ni haki ya kikatiba.

Vikwazo vya kisheria navyo vimehakikisha mashirika hayo hayawezi kupata misaada ya kifedha kutoka nje ya nchi ili yasiwe na nguvu za kukosoa serikali na bodi ya kuthibiti mashirika hayo imekuwa ikifunga yanayokosoa serikali ikidai yamekiuka sheria.

Hatua hizi ni sawa na mbinu za serikali ya Mzee Moi ambaye alitumia kila njia kuyanyamazisha. Katika miaka 24 ya utawala wake, mashirika yasiyo ya serikali hasa yaliyohudumu maeneo ya upinzani yalikuwa yakifungwa, wanaharakati kukamatwa na kutishwa hadharani.

KUZIMA VYAMA VYA WAFANYAKAZI

Moi hakutaka vyama vya wafanyakazi vilivyokuwa na nguvu au vilivyoweza kusababisha uasi dhidi ya serikali yake. Alipiga marufuku chama cha kutetea maslahi ya watumishi wa umma, muungano wa wenye matatu na kile cha wahadhiri wa vyuo vikuu na kuwakamata baadhi ya viongozi wake wakiwemo aliyekuwa Jaji Mkuu Willy Mutunga na Katama Mkangi.

Rais Kenyatta kwa upande wake anaonekana kutumia mbinu sawa na za mlezi wake kisiasa katika masaibu yanayoandama chama cha Knut, ambacho kimekuwa mwiba kwa serikali yako kinapotetea walimu.

Jubilee imetumia ujanja kuvuruga uongozi wa chama hicho. Baada ya kushindwa kuondoa Katibu Mkuu William Sossion kwa kupinga sera za elimu za serikali hasa mtaala mpya, Tume ya Uajiri wa Walimu (TSC) imemwondoa kwenye orodha ya walimu na sasa inataka kukivunjilia mbali Knut.

MAHAKAMA

Sio siri kwamba Rais Uhuru Kenyatta hafurahishwi na utendakazi wa mahakama ambayo chini ya katiba ya sasa imehakikishiwa uhuru wake.

Amefanya juhudi za wazi kupunguza uhuru huo kwa kukataa maazimio ya Tume ya Huduma ya Mahakama (JSC), kuinyima pesa, kutisha hadharani na kulaumu majaji kwa madai ya kutotekeleza majukumu yao.

Rais Kenyatta anajaribu kuiga Mzee Moi ambaye alitawala chini ya katiba iliyompa mamlaka ya kuteua majaji ambao angeweza kushawishi.

Wanaoishi karibu na Uhuru na Moi walia kukosa maji kwa miaka 10

RICHARD MAOSI NA KEVIN ROTICH

Eneo la Mangu linalopatikana katika kaunti ndogo ya Rongai, Nakuru linazungukwa na makazi ya rais wa zamani Mzee Daniel Moi na rais wa sasa Bw Uhuru Kenyatta.

Licha ya Mangu kuwa miongoni mwa maeneo ya kutajika, kutokana na uwepo wa viongozi hawa, maisha ni magumu. Tatizo la ukosefu wa maji limewalemaza kwa zaidi ya miaka 10.

Bi Hellen Njeri, mkazi wa Rongai, anasema maisha katika eneo la Rongai ni sawa na kuishi jehanamu kwani hali ya ukosefu wa maji imesababisha ukame.

“Kila mara tunalazimika kununua maji kutoka kwenye maboma ya watu wanaomiliki visima ingawa maji hayo yamekolea chumvi kupita kiasi,” Bi Njeri akasema.

Anasema lita 20 za maji huuzwa kwa Sh15, na bei yenyewe ni ghali kwa sababu wakazi wengi ni wa kipato cha chini kutokana na shughuli wanazotekeleza kujikimu.

“Ninalazimika kununua zaidi ya lita 100 ya maji kila siku, lakini kiwango hiki bado ni kidogo sana,” aliongezea.

Miaka 10 bila maji katika Soko la Menengai. Picha/ Richard Maosi

Anasema kuwa sio hakika kuwa wamiliki wa visima wataruhusu watu kuteka maji kutoka kwenye visima vyao, kwani baadhi yao huwanyima ruhusa ya kupata maji.

“Msimu wa kiangazi ndio matatizo huongezeka maradufu ndio maana wengi wetu hulazimika kusafiri masafa marefu kutafuta maji ambayo bei huwa juu,” aliongezea.

Lakini kufikia sasa msimu wa mvua umewapatia afueni wakazi wa Rongai angalau kupata maji ili kukidhi mahitaji yao ya kila siku.

“Isitoshe tumekuwa tukiwasilisha malalamishi yetu kupitia ofisi ya mbunge wetu lakini hajaanzisha miradi yoyote ya kutusaidia,” akasema.

Bi Alice Kuria, mchuuzi wa mboga na matunda katika soko la Rongai anasema ni muda mrefu tangu ashuhudie maji yakichiriza kutoka kwenye mfereji wake uliokauka kitambo.

Soko la Sobea: Wauzaji hawana maji ya kuosha matunda na mboga zao. Picha/ Richard Maosi

“Sina njia nyingine isipokuwa kununua maji kutoka kwa wachuuzi ingawa sio salama kwa matumizi ya binadamu,” Bi Kuria alisema.

Anasema anatumia hela nyingi kununua maji kila siku licha ya kuwa na miradi mingine ya kutekeleza kama kuwalipia watoto wake karo.

Hatua chache kutoka kwenye soko la Rongai Taifa Leo ilikutana na mzee Moses Njenga, mkulima anayekuza mahindi na kufuga ng’ombe.

Bw Njenga anasema amekuwa akipata matatizo ya kupata maji ya kuwanywesha mifugo wake.

“Mifugo kama ng’ombe wanahitaji maji mengi kila siku kinyume na binadamu ambao wanaweza kumaliza siku nzima bila kukata kiu,” alisema.

Alieleza kuwa kabla ya Rais mstaafu Daniel Moi kuondoka ofisini, wakazi walikuwa wakipata maji ya kutosha lakini mambo yalibadilika 2002.

Mifugo huteseka zaidi hasa msimu wa kiangazi wakati kuna uhaba wa maji. Picha/ Richard Maosi

“Tunasikia tu wakulima wa maua wamekuwa wakipewa kipaumbele, lakini pia sisi tunastahili kupewa nafasi sawa nao,” alisema.

Eliud Kimani, mwenyekiti wa miradi ya maji katika eneo la Mangu anasema tangu ahamie Rongai 1980, swala la ukosefu wa maji halikuwahi kushuhudiwa.

Anawalaumu matajiri wanaotumia hongo kubadilisha mikondo ya maji, hadi ielekee kwenye mashamba na maboma yao bila kujali maslahi ya maskini ambao ni wengi.

“Kabla ya 2002 tulikuwa tukipata maji siku saba kwa wiki lakini mambo yalibadilika pindi idadi ya watu ilipoanza kuongezeka,”Kimani alifichulia Taifa Leo.

Anasema kufikia sasa maeneo yanayopata maji yamegawika katika sehemu tatu ambazo ni Kayava,Sigei,na Sobea.

Eliud Kimani, msimamizi wa mradi wa maji katika eneo la Mangu, akionyesha baadhi ya matanki yanayotumika kuhifadhi maji. Picha/ Richard Maosi

“Tangu rais Moi astaafu siku za kuwapatia wakazi maji zilipunguzwa kutoka siku saba kwa wiki hadi siku tatu,”Kimani alisema.

Anasema kuwa majuzi wakati wa mazishi ya Kabage maji yalifunguliwa kwa siku nzima lakini ,pindi mazishi yalipokatika maji yalifungwa na wakazi kurejelea ugumu waliokuwa wamezoea.

Anaeleza kuwa kampuni ya maji NARUWASCO katika eneo la Rongai ilikuwa imefungwa, wala haikuwa katika nafasi ya kuwasaidia wakazi kutatua matatizo ya maji.

“Nimelazimika kupunguza idadi ya ng’ombe wangu kutoka 20 hadi 10 kwa sababu sikuwa na maji ya kutosha kuwahudumia,”akasema.

Alipozuru Nakuru Rural Water and Sanitation Limited NARUWASCO hakupata usaidizi kwani wasimamizi walimhepa.

“Kila mara ninapozuru ofisi za maji huwa ninaelezwa kuwa meneja yuko mkutanoni,jambo linalonifanya nisubiri hadi nianpochoka na baadae kuondoka,”akasema.

Hali ni mbaya zaidi katika kituo cha polisi cha Rongai ambapo hakuna mfereji wowote unaotiririka maji.

OCPD wa Rongai Richard Rotich anasema waliacha kutegemea maji ya NARUWASCO, na wao hulazimika kununua maji kutoka kwa wachuuzi na wakati mwingine kutegemea mvua.

Alieleza Taifa Leo kuwa kituo cha polisi cha Rongai kinabeba zaidi ya nyumba 69 ambazo ni makao ya GSU,polisi wa kawaida na wale wa trafiki.

“Nilipopata uhamisho hapa nilikuta polisi wakihangaika kutokana na tatizo la maji na ikabidi nibuni mbinu mbadala ya kuhakikisha kuwa wanapata maji,” Rotich alisema.

Bw Kimani akionyesha baadhi ya paipu za maji zilizokatwa tangu 2002 na wala NAWASCO hawajarejesha maji. Picha/ Richard Maosi

Mkurugenzi wa NARUWASCO Reuben Korir alisema watu wamekuwa wakipata mgao wa maji kila siku ya Jumanne,Alhamisi na Jumamosi kutegemea na eneo.

“Mikondo mingine hupata maji mara tatu kwa wiki ilhali mingine ikilazimika kupata mgao mara moja kwa wiki,”aliongezea.

Mnamo 2017 rais Uhuru aliamuru maji kutoka bwawa la Chemususu kutumika baada ya mradi huo kukamilika.

Pigo jingine kubwa lililopiga kaunti ya Nakuru ni pale mradi wa bwawa la Itare,lilipokwama kutokana na ufujaji wa Sh38 bilioni.

National Water Master Plan ya serikali ya Jubilee ndiyo iliasisi miradi hii ambayo bado haijaanza kuwafaidi wakazi wa Nakuru.

Bwawa lenyewe ambalo lina kina kirefu linatarajia kuwasaidia wakulima kunyunyizia mimea katika maeneo ya Mogotio,Rongai,Eldama Ravine na Emining.