Mchakato kusaka Naibu Gavana wa Nairobi waanza

Na COLLINS OMULO

JUHUDI za kumtafuta yule atakayehudumu kama Naibu Gavana katika Kaunti ya Nairobi zinaendelea kushika kasi, huku Bi Ann Kananu akikaribia kuapishwa kama gavana wa tatu.

Chama cha Jubilee (JP) kimeandaa orodha ya watu wanane wanaotarajiwa kupewa nafasi hiyo.Mnamo Juni 24, Mahakama Kuu iliidhinisha mchakato wa uteuzi na upigaji msasa wa Bi Kananu kuwa halali, hali ambayo inatoa nafasi kwake kuapishwa rasmi kama gavana.

Uamuzi huo ambao uliotolewa na majaji watatu uliunga mkono kutolewa kwa Bw Mike Sonko kama gavana.

Mahakama pia ilifutilia mbali uwezekano wa kuandaliwa kwa uchaguzi mdogo kuwawezesha wenyeji kumchagua gavana mpya.

Muda wa siku kumi uliotolewa na mahakama kwa yeyote anayepinga uamuzi huo kuwasilisha rufaa unaisha Ijumaa hii.

Ingawa mawakili wa Bw Sonko walikuwa wameiomba mahakama kusimamisha utekelezaji wa uamuzi huo kwa siku 21 ili kuwasilisha rufaa, hawajaeleza chochote hadi sasa ikiwa watawasilisha rufaa hiyo.

Katibu Mkuu wa Jubilee, Bw Raphael Tuju, alisema kuwa chama hicho tayari kina orodha ya watu na kinangoja tu muda huo uishe.

“Orodha ya watu hao imekuwa tayari kwa muda mrefu. Tutakapomaliza taratibu za mahakama, tutafanya uamuzi,” akasema Bw Tuju.

Kulingana na Sheria ya Serikali za Kaunti ya 2017 iliyopitishwa na Bunge mwaka uliopita, magavana wanahitajika kuwateua manaibu wao katika muda wa siku 14.

Mwaka uliopita, watu tisa walijitokeza kuwania ugavana ijapokuwa uchaguzi mdogo haukufanyika kama ilivyotarajiwa.

Imeibuka miongoni mwao ni wale ambao huenda wakateuliwa kuhudumu katika nafasi hiyo.Wao ni mwanasiasa Peter Kenneth, Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna, mwenyekiti-mwenza wa Sekretariati kuhusu Mpango wa Maridhiano (BBI) Dennis Waweru, mfanyabiashara Agnes Kagure na aliyekuwa gavana wa Kiambu, William Kabogo.

Wengine ni Mkuu wa Kitengo cha Utekelezaji katika Ikulu (PDU) Nzioka Waita, Katibu wa Wizara ya Miundomsingi Charles Hinga, Katibu wa zamani katika Kaunti ya Nairobi Peter Kariuki na aliyekuwa Msajili katika Baraza la Jiji la Nairobi, Bw Philip Kisia.

Majina ya wakili Steve Ogolla na mfanyabiashara Fred Rabong’o pia yametajwa kuwa miongoni mwa watu hao.

Hata hivyo, Bw Tuju alikataa kutaja lolote kuhusu majina hayo. Badala yake, alisema orodha hiyo ni ndefu ambapo inawashirikisha watu kutoka vyama tofauti vya kisiasa.

Mnamo Januari, Mkurugenzi wa Chaguzi katika ODM, Bw Junet Mohamed, alisema huenda chama hicho kikajiondoa kwenye mkataba wake na Jubilee ikiwa hakitahakikishiwa kupata nafasi hiyo.

Wakazi wa Nairobi walia Krismasi imekuwa ‘kavu’

Na SAMMY WAWERU

Mabustani na majumba ya maduka ya jumla mbalimbali jijini Nairobi na viunga vyake siku ya Krismasi yalikuwa yenye pilkapilka za hapa na pale kufuatia wananchi waliomiminika kujivinjari na kupumzika na familia yao.

Idadi ya waliojitekeza hata hivyo ilikuwa ya chini ikilinganishwa na miaka ya awali, ambapo mabustani hushuhudia umati mkubwa wa watu wasiomudu kuenda mashambani kuungana na jamaa zao.

Licha ya idadi ndogo, wachuuzi wa mapochopo hasa yanayopendwa na watoto walijituma kuhudumia waliojitokeza. Katika majumba ya jumla ya Garden City Mall, Two Rivers Mall na Thika Road Mall familia nyingi zilijitokeza kuwapa raha watoto wao ila kiwango cha watu kilikuwa chini ikilinganishwa na mwaka uliopita.

Wakazi wengi waliofika eneo la Garden City walisalia kupiga picha na Mti wa Krismasi baada ya kukosa hela za mapochopocho ghali mle ndani. PICHA/ SAMMY WAWERU

Bei ya vyakula na vinywaji katika maeneo hayo matatu ilisalia juu, huku watoto wakilazimika kumeza mate tu kwani wazazi wao hawangemudu kuwanunulia.

“Iweje ninunue chakula cha Sh4,000 kwa watoto wangu wawili? Kisha niwapandishe teksi ya Sh2,000 hadi nyumbani. Maisha ni ghali mno na hela hakuna. Ni Krismasi kavu sana. Tutapanda matatu ya kawaida, nitawapikia chakula nyumbani,” akasema Judy Mwongeli aliyezuru enel la Garden City.

Taifa Leo Dijitali ilipozuru mabustani ya Uhuru Park, City Park na Uthiru Ijumaa, wafanyabishara walisema kuwa ingawa watu walijitokeza, hawakuwa na hela za kununua bidhaa za watoto na mapochopocha kwa wingi kama mwaka uliopita.

Katika bustani ya Uthiru, wazazi wengi waliwapeleka watoto kufurahia Krismasi ila walikosa hela za kuwalipa wanao huduma za michezo. PICHA/ SAMMY WAWERU

“Idadi ya watu mwaka huu kwenye mabustani ni ya chini mno. Isitoshe, watu wanalia kukosa pesa, biashara zimeathirika,” Ruth Wambui, mmoja wa wachuuzi wa peremende akasema.

Mkurupuko wa janga la Covid-19 nchini umeathiri sekta nyingi ikiwemo ya biashara, uchukuzi na utalii, hali iliyosabanisha wengi kusalia mijini kwa kukosa nauli ya kusafiri mashambani kuungana na familia zao.

Bustani ya TRM, iliyoko eneo la Roysambu, Thika Road, idadi ya watu ilikuwa ya chini. “Inaonekana wale ambao hawakusafiri wameamua kuadhimishia Krismasi kwenye nyumba. Awali, wakati wa shamrashamra za Sikukuu ya Krismasi huvuna pesa kupitia kazi ya kupiga picha,” akaeleza paparazzi mmoja.

Ni wakazi wachache tu waliojitokeza Bustani ya TRM, Roysambu kujivinjari na kupumzika Krismasi ya 2020. PICHA/ SAMMY WAWERU

Martha Thuo, mmoja wa waliofika katika bustani ya TRM alisema gharama ya juu ya usafiri ilimlazimisha kusalia Nairobi.

“Ninanotoka Nyeri nauli kipindi hiki imekuwa zaidi ya Sh800, safari ambayo hulipa kati ya Sh250 – 400 ada ya kawaida. Niliamua sitaungana na jamaa zangu mashambani kwa sababu ya pesa kuwa adimu, biashara zimeathirika. Januari karo inanisubiri,” akasema Martha ambaye ni mama wa watoto watatu.

Wahudumu wa matatu nao wameongeza nauli hadi zaidi ya maradufu, huku teksi za kidijitali kama Uber, Bolt na Little Ride nazo zikipandisha nauli mara tatu kwa kuwa ni msimu wa sherehe.

Badi aapa kuwakabili wanaotatiza kazi jijini

Na WANDERI KAMAU

MKURUGENZI Mkuu wa Idara ya Huduma za Jili la Nairobi (NMS), Meja Jenerali Mohamed Badi, amesema anafahamu mwenyewe jinsi atayakabili makundi ya watu wenye ushawishi ambayo yamekuwa yakiingilia utendakazi katika jili la Nairobi.

Jenerali Badi aliwataja watu hao kuwa “Wakenya wa kawaida”, akisema hawatamtatiza kwa vyovyote kutoa huduma muhimu kwa wakazi wa Nairobi.

Kwenye mahojiano na kituo kimoja cha televisheni Jumatano usiku, Jenerali Badi alitoa mfano wa jinsi makundi hayo yalijaribu kumzuia kutimiza malengo yake kwa kuchoma kituo cha kutengeneza lami lakini yakashindwa.

“Watu hao ni Wakenya wala si raia wa kigeni, hivyo tunafahamu jinsi ya kukabiliana nao. Walijaribu kunizuia kutimiza malengo yangu kwa kuchoma kiwanda cha kutengeneza lami, japo walinichelewesha kwa wiki tatu pekee. Niliepuka mtego wao,” akasema.

Kulingana naye, kuna makundi ya watu wenye nia ya kuendelea kufaidika kwa usimamizi mbaya wa jiji kuu.

Gavana Mike Sonko amekuwa akilalamikia “mwingilio” wa makundi hayo kwenye utendakazi wake, akiyataja “kuteka” karibu idara zote muhimu za serikali yake.

Mwaka uliopita, alimrai Rais Uhuru Kenyatta kumsaidia kuliendesha jiji, akisema makundi hayo yalikuwa yakitishia uongozi wa serikali yake.

“Nakuomba Rais utusaidie kuyakabili makundi hayo kwa kuchukua baadhi ya majukumu ya kaunti ili kuyazuia kutuingilia,” akasema Bw Sonko.

Jumatano, Jenerali Badi alirejelea mikakati ya halmashauri hiyo kulistawisha jiji, akisema lengo lake kuu ni kuendesha mikakati ya maendeleo kwa kumshirikisha kila mmoja.

Alisema miongoni mwa wale ambao amefanikiwa kushirikisha kwenye mikakati hiyo ni familia zinazoishi barabarani na mitaani, maarufu kama “chokoraa.”

“Cha kushangaza ni kuwa tumeshirikiana na baadhi ya familia hizo kuyasafisha baadhi ya maeneo jijini,” akaeleza.

Hata hivyo, alilalamikia hatua ya Bw Sonko kukataa kuidhinisha bajeti ya kaunti kama changamoto kuu inayomkabili katika kutimiza baadhi ya mipango ya halmashauri hiyo.

“Tuna mipango mingi tuliyo nayo lakini hatua ya Gavana Sonko kutoidhinisha bajeti imeathiri sana baadhi ya mipango yetu, ikiwemo kuwalipa madaktari mishahara,” akaeleza.

Wiki mbili zilizopita, Bw Sonko alikataa kuidhinisha Mswada wa Bajeti ya Kaunti 2020/2021, akisema bajeti hiyo “ilifanyiwa mageuzi” bila taratibu zifaazo kuzingatiwa. Kaunti ilikuwa imetengewa jumla ya Sh37.7 bilioni.

Bunge la Kaunti lilikuwa limepitisha bajeti ya Sh35.5 bilioni, huku NMS ikitengewa Sh27.1 bilioni nazo idara anazoshikilia Sonko zikitengewa Sh6.4 bilioni. Bunge lilitengewa Sh2 bilioni zilizobaki.

Bw Sonko alikataa kuidhinisha mswada huo akilalamikia “kubaguliwa” na Serikali ya Kitaifa.

Bw Sonko na Jenerali Badi wamekuwa wakitofautiana vikali, gavana akidai kuwa lengo kuu la mkurugenzi huyo ni “kutwaa” mamlaka yake.

Utatupwa ndani miezi 6 ukinaswa ukitema mate ovyo jijini Nairobi

COLLINS OMULO na JAMES MURIMI

MTU yeyote atakayepatikana akitema mate kwenye barabara ama kupenga kamasi bila kutumia kitambaa jijini Nairobi, atahukumiwa kifungo cha miezi sita gerezani au kutozwa faini ya Sh10,000.

Kwa mujibu wa mswada uliowasilishwa katika Bunge la Kaunti ya Nairobi, adhabu kama hiyo itapewa yeyote atakayebainika kushiriki ukahaba.

Mswada huo, ambao uko katika awamu ya kwanza, unalenga kuchukua mahali pa sheria za jiji la Nairobi, ambazo zilipitwa na wakati baada ya mfumo wa ugatuzi kuanza kutekelezwa.

Mswada huo umewasilishwa na diwani wa wadi ya Riruta, James Kiriba.

Wale ambao watapatikana wakiendesha magari au pikipiki kwenye vijia vilivyotengewa watumiaji miguu pia wataadhibiwa.

Kwenda haja kubwa ama ndogo kwenye barabara za jiji ama maeneo ya umma, kuwasha moto kwenye barabara za umma ama za jiji bila ruhusa ya Katibu wa Kaunti pia kutachukuliwa kuwa hatia.

Makosa mengine yaliyoorodheshwa na mswada huo ni kuacha mbwa ovyo kwenye barabara, kuosha ama kurekebisha gari kwenye barabara za jiji, kuvuta sigara kwenye maeneo ya umma na utingo kuwaita abiria kuabiri magari yao.

Kwa mujibu wa sheria hiyo, mtu ataruhusiwa kutengenezea gari lake barabarani tu ikiwa kuna hali ya dharura.

Kuchuuza, kuuza, kusambaza ama kutangaza maandishi yoyoye ama hafla katika barabara ya umma, kupiga kelele ama kutumia kengele, spika ama chombo chochote kile cha kupaaza sauti ama kuendesha gari ili kutangaza bidhaa bila kibali pia kumeorodheshwa kama kosa.

Hili pia litajumuisha kushiriki michezo kwa namna ambapo mtu anaweza kuharibu mali ama kusababisha majeraha.

Atakayefanya kosa lolote lililoorodheshwa hapo juu atakuwa kwenye hatari ya kuhukumiwa miezi sita gerezani, kupigwa faini ya Sh10,000 ama kupewa adhabu zote mbili.

Katika Kaunti ya Laikipia, yeyote atakayepatikana akienda haja ndogo, kutema mate ama kutupa taka katika maeneo ya umma atatozwa faini ya Sh5,000 ikiwa madiwani wataupitisha mswada huo.

Mswada unalenga kuhimiza umma kutilia maanani uhifadhi wa mazingira. Unaeleza kwamba yeyote anayepatikana akitupa vifaa vya ujenzi ovyo atatozwa faini ya Sh10,000.

“Atakayepatikana akitupa vifaa vya ujenzi kama mchanga, mawe ya kujengea ama kifaa kingine chochote cha ujenzi atapigwa faini ya Sh10,000,” unaeleza mswada ambao ushawasilishwa kwa Kamati ya Bunge kuhusu Fedha na Mipango.

Kwa mujibu wa kamati hiyo inayoongozwa na diwani Joseph Kiguru wa Wadi ya Igwamiti, mswada huo unalenga kuwaadhibu wale ambao hawatazingatia kanuni hizo.

“Mswada unalenga kuongeza mapato ya kaunti,” ikaeleza kamati.

Wale watakaopatikana wakipiga kelele ovyo kwa umma watatozwa faini ya Sh10,000.

“Hakuna yeyote atakayeruhusiwa kuwapigia wananchi kelele ovyo ikiwa hajapewa kibali maalum na idara husika kwenye kaunti,” unaeleza mswada.

“Yeyote atakayekiuka masharti hayo atatozwa faini ya Sh10,000,” unaeleza.

Mswada pia umeipa mamlaka Bodi ya Kukusanya Mapato ya Kaunti kuzikagua biashara zote kubaini ikiwa zimetimiza kanuni hizo.

Yeyote atakayeizuia kufanya ukaguzi kwenye biashara yake atatozwa faini ya Sh100,000.

JUBILEE: Tuju athibitisha kikao cha Rais Kenyatta na maseneta Ikuluni Jumatatu

Na CHARLES WASONGA

KATIBU Mkuu wa Jubilee Raphael Tuju amethibitisha kuwa maseneta wa chama hicho wamealikwa na Rais Uhuru Kenyatta kwa mkutano katika Ikulu ya Nairobi, Jumatatu, Mei 11, 2020.

Hatua hiyo inajiri baada ya wabunge na maseneta wanaoegemea mrengo wa Naibu Rais Dkt William Ruto kuwa katika malumbano ya mara kwa mara na wenzao wanaoegemea mrengo wa Rais Kenyatta.

Kimsingi, uhusiano wa Rais Kenyatta na Dkt Ruto haujakuwa mzuri na wa karibu katika siku za hivi karibuni kwani wawili hao hawajakuwa wakionekana pamoja kwa kipindi kirefu.

Wandani wa Dkt Ruto wamekuwa wakimshinikiza Rais Kenyatta aitishe mkutano wa Kundi la Wabunge (PG) wa Jubilee ili kujadili masuala ambayo yamekuwa yakileta mgawanyiko ndani ya chama hicho tawala.

Bw Tuju amenukuliwa akisema kuwa suala kuu ambalo litajadiliwa ni kuhamishwa kwa baadhi ya majukumu ya Kaunti ya Nairobi hadi Serikali Kuu, ambalo limezua utata.

“Hii ndiyo sababu Rais amewaalika maseneta pekee wala sio wajumbe wa Bunge la Kitaifa, kwani maseneta ndio hushughulikia masuala ya ugatuzi,” amesema Bw Tuju.

Hata hivyo, Katibu huyu Mkuu amefafanua kuwa mwaliko wa mkutano huo ulitoka moja kwa moja kwa Rais Kenyatta na “hivyo siwezi kuelezea mengi kuhusu ajenda yake.”

Mkutano huo unatarajiwa kuanza saa mbili na nusu asubuhi.

“Mnavyojua ni kwamba ni Rais mwenyewe aliyewaalika maseneta. Kwa hivyo, siwezi kutoa mwelekeo kuhusu masuala yatakayojadiliwa. Lakini kila ninachofahamu ni kwamba hali katika Kaunti ya Nairobi itajadiliwa kutokana na shida ambazo zimeizonga tangu kuhamishwa kwa baadhi ya majukumu kwa serikali kuu,” Tuju ameeleza.

Nairobi

Ingawa amehiari kuachilia majukumu manne makuu ya kaunti hiyo yaendeshwa na Serikali Kuu kwa kutia saini muafaka wa kufanikisha hilo Februari 2020 Gavana Mike Sonko alibadili msimamo juzi.

Anadai Serikali Kuu ilivuka mipaka na kutaka kusimamia hata yale majukumu ambayo yalifaa kusalia chini ya usimamizi wa serikali yake.

Kwa hivyo, ametisha kusambaratisha shughuli katika Kaunti hiyo kwa kujiondoa kutoka muafaka huo.

Hii ndiyo maana Aprili, Sonko alidinda kutia saini mswada ambao ulipendekeza Sh15 bilioni zitengewe mamlaka ya Nairobi Metropolitan Services (NMS) iliyobuniwa na Rais Kenyatta kuendesha majukumu hayo kwa niaba ya Serikali Kuu.

Hatua hiyo ilichangia mgongano kati yake na Ikulu na kuchangia kuondolewa kwa walinzi wake na baadhi ya madereva waliokuwa wakimhudumia.

Maseneta wakiongozwa na Kiongozi wa Wengi Kipchumba Murkomen pia wamepinga hatua ya Serikali Kuu kuwapeleka wanajeshi kusimamia NMS.

Afisi hiyo inaongozwa na Meja Jenerali Mstaafu Mohammed Badi kama Mkurugenzi Mkuu. Na majuzi Serikali Kuu iliwatuma maafisa wanne zaidi katika makao makuu ya kaunti ya Nairobi, City Hall.

Mkutano wa mwisho wa PG wa Jubilee ulifanyika mnamo 2017 baada ya Rais Kenyatta kushinda uchaguzi na kuanza kipindi chake cha pili na cha mwisho. Ni katika mkutano huo ambapo wenyeviti na manaibu wenyeviti wa kamati za bunge la kitaifa na seneti waliteuliwa.

Jiji la Nairobi lingali chafu chini ya usimamizi mpya

Na CHARLES WASONGA

ATHARI za hatua ya majuzi ya Gavana wa Kaunti ya Nairobi Mike Sonko kudinda kuidhinisha mgao wa Sh15 bilioni kwa Nairobi Metropolitan Services (NMS) zimeanza kuoneka kutokana na uchafu uliokithiri katikati mwa jiji.

Katika uchunguzi wetu katika barabara kadha za katikati mwa jijini la Nairobi jana, mandhari iliyotualika ni ya marundo ya taka katika barabara zenye shughuli haswa mitaa ya downtown town.

Na katika barabara mpya ya Luthuli ambayo ilipanuliwa na kuboreshwa mwaka jana kwa kima cha Sh236 milioni mapipa ya taka yalikuwa yamejaa pomoni. Takataka zilikuwa zimetapakaa kote katika barabara hiyo ya unaongana na River road (upande wa chini) na Tom Mboya Street (upande wa juu).

Hali hivyo hivyo katika barabara ya Kirinyaga Roas ambapo wafanyabiashara wengine wanalalamikia marundo ya takataka ambayo yametapakaa nje ya malango ya maduka yao.

Waziri wa Mazingira Larry Wambua hakujibu simu zetu wala ujumbe mfupi tulipotaka kufahamu ni kwa nini taka zimetapaka katikati mwa jiji haswa wakati huu wa janga la corona ambapo usafi ni muhimu.

Hata hivyo, afisa mmoja wa kaunti ambaye aliomba tusimtaje jina kwa sababu haruhusiwi kuongea na wanahabari alisema hali hiyo inachangiwa na sababu kwamba wengi wa wafanyakazi wa kampuni za kibinafsi ambazo huzoa taka hawajalipwa malimbikizi ya mishahara.

“Hali hii ni uchafu katika barabara za jiji zitaendelea hadi pale wazoaji taka walioanza kugoma mwezi jana watalipwa. Hata hivyo, nasikia kuwa wala ambao hufagia katika maeneo ya Moi Avenue kwenda juu wamelipwa sehemu ya pesa wanazodai,” akasema.

Mwanzoni mwa mwezi wa Machi wazoaji taka walifanya mgomo uliodumu kwa wiki tatu wakidai malipo ya mishahara yao ya kuanza Januari mwaka huu.

Wafanyakazi hao wa kampuni za kibinafis walifanya maandamano katikati mwa barabara za jijini wakirusha taka katika barabara kote. Bw Wambua aliondoa lawama kwa idara yake akielekeza kidole cha lawama kwa idara ya Fedha kufuatia sintoifahamu ilisababisha na mgogoro miongoni mwa maafisa husika.

Katika bajeti ya ziada iliyopitishwa na Kamati ya Bajeti ya Bunge la Kaunti ya Nairobi idara ya uzoaji taka, ambayo ni miongoni mwa majukumu ambayo ilihamishwa hadi NMS ilitengewa Sh400 milioni. NMS inaongozwa na Meja Jenarali Mstaafu Mohammed Badi ambaye aliteuliwa na Rais Uhuru Kenyatta kuwa kushikilia wadhifa wa Mkurugenzi Mkuu (DG)

Pesa hizo ambazo ni sehemu ya Sh15 bilioni ambazo zilipasa kuendea NMS ndizo zilitarajiwa kulipa mishahara ya wazoaji taka katikati mwa jiji.

Lakini Bw Sonko alikataa kuidhinisha bajeti hiyo akidai ilijumuisha majukumu mengine ambayo sehemu yake haikuhamisha hadi Serikali Kuu.

CORONA: Huenda serikali ikafunga jiji la Nairobi

Na JUMA NAMLOLA

SERIKALI Alhamisi ilitoa ishara kuwa huenda ikalazimika kufunga shughuli zote katika kaunti ya Nairobi, kama njia ya mwisho ya kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona.

Kwenye hotuba yake ya kila siku, Waziri wa Afya Bw Mutahi Kagwe, aliwataka waakazi wa Nairobi waanze kuzoea kutotoka nje, kwa kukaa kwenye makazi yao.

“Nataka nikariri kwamba tunaendelea kuonya watu wasiwe na vijisafari vya mara kwa mara, hasa kutoka Nairobi kwenye mashambani. Hatari ya jambo hili iko wazi. Ni rahisi sana kusambaza virusi vya corona kwa wanaoishi mashambani, hasa wakongwe, kama ilivyofanyika nchini Italia,” akasema Bw Kagwe.

Waziri alieleza kuwa hakuna haja kwa watu kuondoka Nairobi na kuwatembelea watu msimu wa Pasaka.

“Si lazima uende mashambani ndipo Pasaka yako ikamilike. Tunapendekeza kuwa kusiwe na misafara yoyote kutoka au kuingia Nairobi, isipokuwa magari ya kubeba vyakula pekee. Na nyinyi watu wa nje ya Nairobi, kama unaishi Nyeri, Kisumu au kaunti nyingine yoyote, kaa huko uliko. Si lazima uende Nairobi,” akasema.

Huenda hatua hiyo ya serikali inatokana na takwimu zinazoonyesha kuwa, idadi kubwa ya watu walioambukizwa virusi vya corona ni wa kaunti ya Nairobi. Kabla ya kuacha kueleza wagonjwa kutokana na wanakotoka, Nairobi ilikuwa ikiongoza kwa watu 37.

Kauli yake ilijiri huku akitangaza kuwa watu wawili waliokuwa katika hali mbaya jana walifariki kutokana na corona. Wawili hao walikuwa katika hospitali za miji ya Nairobi na Mombasa.

Vifo vya wawili hao sasa vinafikisha idadi ya waliouawa na corona nchini kuwa watatu, na walioambukizwa sasa ni 110.

“Katika saa 24 zilizopita, tulifanikiwa kuwapima watu 625 ambapo 29 wamegunduliwa kuwa wameambukizwa. Kati ya hawa, 28 ni Wakenya na mmoja ni raia wa Congo. Hii sasa inafanya idadi ya watu wote walioambukizwa hapa nchini kuwa watu 110,” akasema.

Wagonjwa hao ni wanaume 13 na wanawake 16 walio na umri wa kati ya miaka 15 na 64.

Waziri aliwataka Wakenya wasidanganywe na watu wachache wanaodhani kuwa corona ni maradhi ya kufikirika, na kuwataka wajilinde sasa kabla hawajachelewa.

“Wakenya wenzangu, sitaki kuwatisha lakini takwimu hizi zinaonyesha kuwa maradhi haya yanaendelea kuzagaa. Usitake kuuliza ni kwa nini hujaona mtu unayemjua akiwa ameuawa na maradhi haya. Wakati ukiona mtu huyo, utakuwa umechelewa sana,” akasema.

Virusi vya corona kinyume na maradhi mengine, havisambai vyenyewe.

Ili kusaidia katika juhudi za kupambana na maradhi hayo, waziri alisema serikali inapanga kuajiri wafanyikazi wa afya 5,000 kufikia Jumatano ijayo.

“Tumewaagiza Makamishna wa Kaunti na walimu wakuu wa shule za bweni kote nchini, waanze kutathmini uwezekano wa taasisi hizo kutumika kuwahifadhi wagonjwa,” akasema.

Ofisi ya ustawishaji jiji la Nairobi yabuniwa

Na SAMMY WAWERU

MAJUKUMU muhimu ya serikali ya Kaunti ya Nairobi yameelekezwa kwa ofisi mpya na maalum iliyobuniwa ili kustawisha jiji la Nairobi.

Ofisi hiyo, Nairobi Metropolitan Services (NMS) na itakayoongozwa na Meja Jenerali Mohammed Abdallah Badi, inatazamiwa kusimamia huduma za afya, uchukuzi, uimarishaji mji wa Nairobi ikiwa ni pamoja na huduma kwa umma.

Akizungumza Jumatano katika Ikulu jijini Nairobi, wakati wa utiaji saini mkataba wa kuhamisha majukumu hayo kutoka serikali ya kaunti hadi ile ya kitaifa, Rais Uhuru Keyatta ameeleza kusikitishwa kwake na hali ya jiji la Nairobi, “utupaji taka kiholela ukipaka tope sura ya nchi hii”.

Akielekeza NMS kuweka mikakati kabambe kwa muda wa siku 100 zijazo, itakavyoimarisha hali ya Nairobi, Kenyatta amesema upungufu wa maji ni suala ambalo ofisi hiyo inapaswa kuangazia ipasavyo.

Rais pia ametaja ufisadi kama donda ndugu lililoota na kukita mizizi pamoja na kutawala jumba la City Hall, ilipo ofisi ya Gavana wa Nairobi.

“Janga kuu linalogubika jiji la Nairobi hasa jumba la City Hall ni ufisadi. NMS ing’oe matapeli wote walioshika mateka jiji hili na kuzuia maendeleo na ukuaji wake,” ameagiza Rais Kenyatta.

Amesema utoaji wa leseni kwa wafanyabiashara na huduma mbalimbali pia umejawa na dosari, kufuatia ufisadi unaosakatwa.

Rais pia ameagiza ofisi hiyo kuhakikisha vipande vya ardhi na ploti zote za umma zilizonyakuliwa zimerejeshwa.

“NMS iwajibikie maendeleo ya jiji la Nairobi, tunataka huduma zifikie kile mkazi na raia,” akasema.

Gavana wa Nairobi Mike Sonko na Waziri wa Ugatuzi Eugene Wamalwa wametia sahihi uhamishaji wa huduma hizo.

Meja Jenerali Mohammed Abdallah Badi, atasaidiwa na naibu wake aliyeteuliwa, Enosh Onyango Momanyi.

Serikali kuu kusimamia Nairobi hadi 2022

Na JAMES KAHONGEH

MAELEWANO kati ya Gavana wa Nairobi Mike Sonko na Serikali Kuu kuhusu usimamizi wa kaunti hiyo yamepangiwa kuanza kutekelezwa Machi 15.

Makubaliano hayo yatadumu kwa miezi 24, kisha upande wowote husika, kati ya Serikali Kuu na ya kaunti utaamua ikiwa utaongezwa muda.

Kipindi hicho kinamaanisha kwamba, majukumu ya kusimamia afya, uchukuzi, ujenzi na mipango ya kaunti yatakuwa chini ya Serikali Kuu hadi Februari 25, 2022. Hii ni kumaanisha mkataba utakamilika miezi michache kabla Uchaguzi Mkuu kufanyika.

Kwa msingi huu, endapo Bw Sonko atang’olewa mamlakani, huenda atakayechukua nafasi yake asiwe na majukumu makubwa kwani idara hizo nne ni miongoni mwa kubwa zaidi za kaunti.

Kinachoshangaza ni kuwa, Serikali Kuu itachukua pia jukumu la kukusanya na kugawa mapato yote yanayopatikana katika idara hizo kupitia kwa Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru Kitaifa (KRA).

Kwa mujibu wa nakala iliyotiwa sahihi na Bw Sonko na Waziri wa Ugatuzi Eugene Wamalwa katika Ikulu ya Nairobi mnamo Jumanne, makubaliano hayo hayawezi kukatizwa na upande wowote kabla muda ulioekwa kukamilika isipokuwa kama pande zote mbili zitakubali kufanya hivyo.

Hata hivyo, imebainika makubaliano hayo yatahitaji kufanyiwa utathmini na bunge la kaunti kabla kutekelezwa, imefichuka.

Vilevile, wananchi watapewa muda kuwasilisha maoni yao kuhusu mpango huo wa kukabidhi utawala wa Rais Uhuru Kenyatta sehemu ya usimamizi wa jiji hilo kuu la Kenya.

Majukumu yaliyopeanwa kwa Serikali Kuu yatafadhiliwa na fedha kutoka kwa Hazina ya Mapato ya Kaunti au Hazina ya Jumla au zote mbili.

Hii ni kutokana na kuwa, Serikali ya Kaunti ya Nairobi itahitajika kufadhili idara hizo nne kikamilifu.

Maelewano mengine ni kwamba, Kaunti ya Nairobi itahitajika kupeana wafanyakazi kwa serikali kuu ili kufanikisha utekelezaji wa maelewano hayo.

Utwaaji wa serikali ya Nairobi huenda usilete nafuu

Na BENSON MATHEKA

HATUA ya serikali ya kitaifa ya kutwaa majukumu muhimu ya serikali ya kaunti ya Nairobi huenda isilete mabadiliko yoyote ikiwa yaliyoshuhudiwa miaka 37 chini ya utawala wa Kanu yatajirudia

Hatua hii imeibua kumbukumbu ya hali sawa mwaka wa 1983, wakati serikali ya Rais Daniel Moi kupitia aliyekuwa waziri wa serikali za wilaya Moses Mudavadi, ilipovunja baraza la jiji lililosimamiwa na aliyekuwa Meya Nathan Kahara.

Bw Mudavadi aliteua tume kusimamia jiji la Nairobi iliyojulikama kama Nairobi City Commission.

Ni chini ya tume hii ambapo unyakuzi wa ardhi ulichacha jijini hivi kwamba hata sehemu zilizotengewa vyoo vya umma zilitwaliwa na watu binafsi.

Tofauti na sasa ambapo Gavana Mike Sonko atabaki kuwa gavana, Bw Mudavadi aliwatimua Meya Kahara, Naibu wake Chadwick Adongo na madiwani wote pamoja na karani wa baraza la jiji George Wanjie. Wakuu wa idara tofauti pia hawakusazwa kwenye mabadiliko hayo.

Wadadisi wanasema bado ni mapema kusema kwamba hali sawa haitajirudia.

“Nafikiri mazingira sasa ni tofauti kwa sababu ya katiba ya serikali za kaunti. Hata hivyo kwa maoni yangu, madiwani wa kaunti ya Nairobi wanaelekea nyumbani kwa sababu sioni wakiwa na majukumu ya kutekeleza ikiwa watamtimua Gavana Sonko walivyopanga,” alisema mtaalamu wa masuala ya ugatuzi David Meto.

Wakati huo huo, serikali ilisema kwamba ilivunja baraza la jiji kwa sababu ya usimamizi mbaya uliosababisha ufisadi kukita mizizi. Huduma zilikuwa duni licha ya uchunguzi kubaini kwamba kulikuwa na zaidi ya wafanyakazi 17,000 baadhi hao wakiwa hewa.

Chini ya tume, matapeli waliteka shughuli za jiji na kukamua mapato yake huku huduma zikisambaratika zaidi jijini.

Sonko atimua kaimu katibu

Na COLLINS OMULO

GAVANA wa Nairobi anayekabiliwa na kesi kortini, Mike Sonko amemwachisha kazi Kaimu Katibu wa Kaunti, Bw Leboo Morintat.

Wawili hao walikuwa wandani kwa muda mrefu, hadi pale Bw Morintat alianza kuwasilisha stakabadhi za kaunti kwa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) na Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI), kila anapoagizwa na maafisa wa kuchunguza ufisadi kufanya hivyo.

Haijajulikana wazi kama Bw Morintat anachukuliwa kama shahidi au mshukiwa kuhusiana na kashfa zinazochunguzwa.

Nafasi ya Bw Morintat sasa itashikiliwa kwa muda na Afisa Mkuu wa Mipango wa Mji, Bw Justus Kathenge.

Bw Kathenge alirudi katika serikali ya kaunti mwezi uliopita kama afisa mkuu wa Upangaji wa Mji baada kusimamishwa na Gavana Sonko mnamo Agosti 2019.

Bw Morintat alikuwa akimtetea Bw Sonko, pamoja na kuongoza mikutano katika serikali ya kaunti tangu Gavana aagizwe kutoingia afisini mwake mwaka 2019.

Kuonyesha jinsi wawili hao walivyokuwa karibu, mnamo Septemba 2018 Bw Sonko alibuni nafasi ya naibu katibu wa kaunti – cheo ambacho hakitambuliwi kisheria – ikasimamiwa na Bw Morintat.

Lakini uhusiano kati yao umetatizwa na uchunguzi wa mara kwa mara katika Jiji la Nairobi na wapelelezi.

Wakati wa uchunguzi huo, Bw Morintat ameitwa katika mikutano kadhaa kuandikisha taarifa na kutoa hati kuhusu suala hilo.

Bw Sonko anakumbwa na masaibu tele ikiwemo kesi ya ufisadi iliyosababisha agizo la kumzuia asiingie afisini mwake katika makao makuu ya kaunti, na madiwani wameanzisha mchakato wa kutaka ang’olewe mamlakani.

Wiki iliyopita, ilani ya kuwasilisha hoja ya kumwondoa mamlakani ilipelekwa katika bunge la kaunti na kiongozi wa wachache Bw Peter Imwatok.

Hii si mara ya kwanza kwa Bw Sonko kutimua maafisa wa serikali yake ambao huonekana kwenda kinyume na matarajio yake.

Mwezi uliopita, alimsimamisha kazi Waziri wa Fedha katika kaunti, Bi Pauline Kahiga kuhusu ulipaji wa madeni yanayofika Sh1.4 bilioni ambayo kaunti inadaiwa.

Juhudi zake za awali kumtimua waziri huyo zilikuwa zimegonga mwamba. Alijaribu kujaza nafasi hiyo kwa kumteua Bw Allan Igambi, lakini serikali kuu ikakataa kuchapisha mabadiliko hayo kwenye gazeti rasmi la serikali.

Suala hilo sasa liko mbele ya Mwanasheria Mkuu, ijapokuwa dalili zaonyesha Bi Kahiga angali ana mamlaka katika Wizara ya Fedha ya kaunti.

Wiki iliyopita, Bi Kahiga aliidhinisha ulipaji wa Sh166.9 milioni kwa Mamlaka ya Usambazaji Dawa nchini (KEMSA).

Alisema Sh120 milioni zitatumiwa kugharamia madeni ambayo KEMSA inadai serikali ya kaunti, huku Sh46 milioni zikitumiwa kwa ununuzi wa dawa mpya zitakazosambazwa kwa hospitali za kaunti.

‘Wanafunzi Wuhan hawatasafirishwa kuja nchini’

Na DIANA MUTHEU

SERIKALI haijaweka mikakati yoyote kuwaondoa Wakenya kutoka China; taifa ambalo limeathirika pakubwa ma virusi vya Corona.

Msemaji wa serikali, Cyrus Oguna, akizungumza na wanahabari katika majengo ya GPO Posta, Nairobi alisema Alhamisi kuwa serikali imetuma Sh1.3 milioni zigawanywe miongoni mwa wanafunzi 91 na wanasarakasi tisa walio mjini Wuhan ambapo virusi hivi viliripotiwa kwa mara ya kwanza.

“Pia, tumetuma pesa zingine ambazo kupitia ubalozi wetu huko China wataweza kupata mahitaji ya kila siku,” alisema Bw Oguna.

Bw Oguna aliwaomba wazazi wa wanafunzi hao wasiwe na hofu kwani hakuna hata mmoja wao ameambukizwa homa hiyo ambayo wataalamu sasa wanaita Covid-19.

“Wako salama. Wanaishi katika vitongoji tofauti na tunahofia katika mchakato wa kuwakutanisha katika sehemu moja ili wasafirishwe kuja nchini, huenda wakaambukizwa. Ni heri watulie tukiendelea kuwapa msaada,” alisema.

Mkurugenzi wa Idara ya Afya katika Wizara ya Afya Dkt Patrick Amonth alisema wamejiandaa kupambana na virusi vya corona.

“Tuna vifaa 5,000 vya kuziba pua na mdomo, tumeongeza idadi ya wahudumu wa afya katika uwanja wa ndege, bandari na mipaka. Ni lazima kila mtu anayeingia nchini apimwe. Pia, ni vizuri wananchi wadumishe usafi na pia wapige ripoti kuhusu mtu yeyote wanayemshuku kuwa na dalili ya virusi hivi,” akasema Dkt Amoth.

Elachi aongoza sherehe ya kuapishwa kwa wanachama wapya wa bodi ya huduma za bunge la Nairobi

Na CHARLES WASONGA

SPIKA wa Bunge la Kaunti ya Nairobi Beatrice Elachi mnamo Jumatano aliongoza hafla fupi ya kuapishwa kwa wanachama wawili wapya wa Bodi ya Huduma za Bunge la Kaunti ya Nairobi (NCASB).

Wawili hao ni diwani wa Maringo Hamza Mark Ndung’u (Jubilee) na mwenzake wa wadi ya Nairobi West Maurice Gari (ODM).

Madiwani hao walichukua nafasi ya kiongozi wa wengi katika bunge hilo Abdi Guyo (Wadi ya Matopeni) na kiongozi wa wachache Elias Otieno (Kileleshwa).

Bodi hiyo pia inashirikisha mwananchi wa kawaida aliyetueliwa na bunge hilo la kaunti kutoka miongoni mwa watu wenye ufahamu na tajriba katika uendeshwaji wa masuala ya umma.

Bi Elachi ambaye ni mwenyekiti wa bodi hiyo alimteua Bw Ndung’u kuwa naibu mwenyekiti.

Bw Guyo ambaye amekuwa akipinga kurejea kwa Elachi, hali iliyosababisha fujo katika bunge hilo wiki moja iliyopita, hakuwepo katika sherehe hiyo ya kulishwa kiapo kwa Ndung’u na Gari.

Mabadiliko

Katibu Mkuu wa Jubilee Raphael Tuju ndiye alitangaza mabadiliko kuhusu uwakilishi wa Jubilee katika bodi hiyo (NCASB).

Alisema kuwa chama hicho bado kinajadiliana kuhusu mabadiliko mengine ambayo yanafaa kufanywa katika uongozi wa bunge hilo la Nairobi kufuatia mzozo uliotokea wiki jana.

Barua kuhusu mabadiliko hayo ilitumwa kwa Bi Elachi na kunakiliwa kwa Bw Guyo, Kiranja wa wengi Chege Mwaura na Ndung’u.

Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna kwa upande wake alimteua Gari ambaye atachukua mahala pa kiongozi wa wachache Bw Otieno.

Bw Gari ni mfuasi sugu wa Elachi.

Miongoni mwa wajibu wa Bodi hiyo ni kusimamia matumizi ya fedha katika Bunge la Kaunti ya Nairobi, kukadiria mishahara na mazingira ya kazi ya watumishi wa bunge hilo na masuala mengine yanayohusiana na masilahi ya wafanyakazi wa bunge hilo na madiwani wote.

Vuta n’kuvute yaendelea City Hall

Na CHARLES WASONGA

MZOZO katika bunge la kaunti ya Nairobi ulionekana kuendelea kutokota Alhamisi baada ya karani wa bunge hilo Jacob Ngwele kupewa likizo ya lazima ya siku 30.

Hatua hiyo ilichukuliwa na Bodi ya Huduma za Bunge hilo la Kaunti chini ya uenyekiti wa Spika Beatrice Elachi.

Akiwa likizoni, karani huyo atachunguzwa kuhusiana na madai kuwa alivuruga shughuli za bunge hilo la Kaunti ya Nairobi.

Duru zasema kuwa inadaiwa Bw Ngwele amekuwa akilemaza shughuli za bunge hilo kwa kuwachochea wafanyakazi wachelewe kuripoti kazini.

Vilevile, inasemekana kuwa karani huyo hajakuwa akihudhuria mikutano ya bodi hiyo.

“Tumekubaliana kama bodi kumtuma Karani wetu kwa likizo ya lazima ya siku 30 kuanzia Oktoba 24, 2019. Wakati wa kipindi hicho, ameagizwa asifike katika bunge la kaunti hadi uchunguzi kuhusu mienendo yake utakapokamilika,” akasema Elachi.

Apata agizo la mahakama

Hatua hii inajiri siku mbili baada ya Bw Ngwele kupata agizo la mahakama kuzuia bodi mpya iliyozinduliwa na Spika kuhudumu.

Pia agizo hilo lilisimamishwa kwa muda kuondolewa kwa kiongozi wa wengi Abdi Guyo na kiongozi wa wachache Elias Otieno kama wanachama wa bodi hiyo.

Wawili hao walipokonywa nafasi zao na vyama vyao.

Chama cha Jubilee kiliteua diwani wa wadi ya Maringo Hamza Mark Ndung’u mahala pa Guyo huku diwani wa Nairobi West Maurice Gari akipewa nafasi ya Bw Otieno ambaye ni diwani wa Kileleshwa.

Wengine walioondolewa kutoka bodi hiyo ni pamoja na Ada Onyango ambaye ni naibu karani wa bunge la Kaunti ya Nairobi, Philomena Nzuki ambaye ni Mhasibu Mkuu, Nancy Mutai ambaye ni afisa wa wafanyakazi na Garvin Castro ambaye ni msaidizi wa karani.

Agizo hilo lililotolewa na Jaji wa Mahakama ya Ajira na Masuala ya Leba Onesmus Makau linasitisha utekelezaji wa mabadiliko katika bodi kama ilivyochapishwa na Spika Elachi katika gazeti rasmi la serikali hadi kesi hiyo itakapoanza kusikizwa mnamo Novemba 11 na uamuzi kutolewa.

Licha ya kusimamishwa kwake, Bw Ngwele amesisitiza ataendelea kutekeleza majukumu yake kama karani, akisema hakuna mkutano wa bodi ulioitishwa kumsimamisha kazi kwa sababu shughuli zake zilizokuwa zimesimamishwa na agizo la mahakama.

“Kwa hivyo, uamuzi wa Spika hauna maana, na nitaukaidi. Vilevile, nitamshtaki kwa kudharau mahakama,” akasema Ngwele.

Karani huyo ambaye pia ndiye Katibu wa Bodi ya Huduma za Bunge la Kaunti ya Nairobi alisema bodi hiyo haiwezi kufanya mkutano bila Katiba na hivyo akataja uamuzi wa Spika Elachi kama batili.

MUTUA: Hadhi yetu isidhalilishwe kimataifa na wanaopora

Na DOUGLAS MUTUA

MOJAWAPO ya matusi maarufu zaidi dhidi ya raia wa kigeni nchini Rwanda humkanya mtu kutofanya mambo polepole kama Mtanzania.

Nalo tusi maarufu zaidi dhidi ya wageni nchini Tanzania ni kwamba, usiwe mwizi kama Mkenya.

Anayekutukana hakuchagulii tusi, hivyo kuyatilia maanani sana ni sawa na kumsaidia anayeyatema kuendeleza chuki na ubaguzi.

Bila shaka, matusi kama hayo si mzaha kwa maana hayatokani na mapenzi bali chuki ya jumla dhidi ya walengwa. Yanasikitisha.

Hata hivyo, ukizingatia kwamba kila jamii tangu hapo ikijituma kujilinda dhidi ya kukaliwa kimabavu na jamii au nchi nyingine yoyote, yanaeleweka.

Tatizo linaingia matusi yenyewe yanaporudiwa sana kiasi cha kumfanya mlengwa kuyaamini na kuanza kuenenda kama matusi yenyewe yanavyoashiria.

Kwa wakati huu, sitaki kujadili kasi au mwendo wa pole wa Mtanzania.

Hata hivyo, sitaisaza nchi yangu Kenya. Haidhuru kumjadili mbaya wako kwa madhumuni ya kumrekebisha. Kenya, taifa lenye nguvu zaidi kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki, limekuwa kivutio cha wengi kwa muda mrefu kutokana na maendeleo na ujasiriamali wetu.

Wakati mmoja, mwanzilishi wa taifa la Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kwa kuajabia maendeleo ya Kenya, aliwashauri Watanzania wakitaka kuzuru jiji la kisasa waje Nairobi, wasiende London.

Japo sisi wenyewe tumekuwa na matatizo yetu ya kisiasa na utovu wa usalama, tumepiga hatua kadhaa na kurejesha imani ya wengi kuhusu uthabiti wetu.

Ndiyo maana unawaona wakimbizi wakimiminika huku kila kunapotokea ghasia kokote Afrika Mashariki na Kati.

Kwa muda mrefu, Kenya imewahifadhi raia wa Uganda, Tanzania, Rwanda, Burundi, Sudan Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC); Ethiopia, Somalia na kadhalika.

Hata tusipokuwa na ujirani mwema, ni hulka ya binadamu kumtendea wema anayekumbwa na misukosuko ya kimaisha. Umoja wa Mataifa (U.N.) unaagiza hivyo.

Wasomi wa Kenya wametapakaa kila mahali Afrika na duniani ambako wanafanya kazi mbalimbali, kuu zaidi zikiwa kugawa maarifa kwa njia ya kudundisha.

Afrika, utawapata Rwanda, Burundi na Sudan wakifundisha Kiswahili, ukiteremka kidogo uwapate Botswana na Afrika Kusini wakifundisha vyuo vikuu.

Pia utawapata Watanzania, hasa kwenye shule binafsi, wakifundisha Kiingereza, Hisabati na masomo mengine mengi.

Ingawa Tanzania ingetaka kutusadikisha kwamba Kiswahili kinazungumzwa zaidi nchini humo, utaalamu wa kukifundisha ni milki ya Wakenya.

Idadi ya walimu wa Kiswahili kote duniani inaizidi sana ile ya Watanzania. Si siri. Bila shaka tumesaidiwa sana na uelewa wetu wa Kiingereza. Watanzania wanakijaribisha tu.

Hata hivyo, kuna tatizo kubwa. Maarifa yote tuliyonayo yanaweza kukosa tija yoyote ikiwa tusi la Watanzania kwamba sisi ni wezi litatokea kuwa kweli au liaminike kote barani.

Nchi ikipata aibu kiasi hiki inaelekea pabaya. Ikiwa huniamini, niambie kwa nini unaingia baridi unapojipata ukitekeleza muamala wa kifedha na raia wa Nigeria. Hao nao jina lao limeoza! Ni sharti tujirudi kabla ya dunia kutukataa.

 

mutua_muema@yahoo.com

United Bank for Africa yafanya usafi jijini Nairobi

Na GEOFFREY ANENE

HUKU jiji la Nairobi likikabiliwa na changamoto jinsi ya kukabiliana na utupaji wa taka, benki ya United Bank for Africa (UBA) iliamua kufanya usafi kwenye barabara ya Moi Avenue, Jumamosi.

Ikiongozwa na Afisa Mkuu Mtendaji wa Benki hiyo wa eneo la Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika, Emeke Iweriebor, wafanyakazi wa benki hiyo kutoka matawi yote nchini, wamesafisha eneo kati ya bustani ya Jeevanjee na jengo la Union Towers katikati mwa jiji.

Wafanyakazi wa United Bank for Africa (UBA) wafanya usafi jijini Nairobi, Jumamosi, Septemba 14, 2019. Picha/ Geoffrey Anene

“Hii ni sehemu ya mradi wetu wa kusafisha jiji. Tunashirikiana na serikali ya kaunti ya Nairobi kurembesha jiji na kuhamasisha wakazi kuhusu umuhimu wa usafi na njia salama za kulinda mazingira,” amesema Iweriebor.

Raia huyo wa Nigeria aliongeza kuwa benki hiyo itaendelea kusaidia miradi ambayo jamii imeweka ya kukabiliana na utupaji wa takataka.

Kuifanya shughuli kuwa mazoea

Ikiwa ni mara ya kwanza ya benki hiyo kujihusisha na usafishaji wa jiji, Iweriebor amehakikishia wakazi wa Nairobi kuwa wataendeleza shughuli hiyo mara kwa mara sio katkati mwa jiji tu, bali pia katika maeneo tofauti jijini.

“Mbali na lengo letu la kutoa huduma za benki, tunataka kujihusisha katika ufanisi wa jamii tunazojihudumia kwa njia tofauti ikiwa ni pamoja na kuchangia katika kuimarisha mazingira, michezo na kadhalika,” amesema afisa huyo baada ya kusafisha sehemu hiyo ya barabara hiyo yenye umbali wa kilomita moja.

Utupaji wa taka chini ya daraja Korogocho jijini Nairobi. Benki ya United Bank for Africa ilifanya usafi kwenye barabara ya Moi Avenue mnamo Septemba 14, 2019. Picha/ Geoffrey Anene

Nairobi yatajwa jiji bora la mikutano ya kibiashara Afrika

NA LEONARD ONYANGO

JIJI la Nairobi kwa mara nyingine limeibuka bora zaidi kwa safari za kibiashara barani Afrika katika Tuzo za Safari Duniani (WTA).

Katika makala hayo ya 26 ya tuzo za WTA yaliyofanyika Mauritius, Jumba la Kimataifa la Jomo Kenyatta (KICC) pia liliibuka bora kwa kuwa na kumbi murua za mikutano na makongamano barani Afrika.

“Tumefurahi sana kutuzwa kwa kuibuka bora Afrika. Tuzo hizo zimethibitisha kuwa kweli Nairobi na jumba la KICC ni bora zaidi barani,” akasema Mkurugenzi Mtendaji wa KICC Nana Gecaga aliyekuwa akizungumza alipopokezwa tuzo hizo.

“Tuzo hizo zitasaidia pakubwa katika kuinua sekta ya utalii humu nchini,” akaongezea.

Jumba la KICC lilibwaga majumba mengine barani Afrika kama vile ukumbi wa mikutano wa Cairo (Misri), Cape Town Convention Centre nchini Afrika Kusini, Durban Convention Centre (Afrika Kusini), Kigali Convention Centre (Rwanda), Palais Des Congress Marrakech (Morocco) na Sandton Convention Centre (Afrika Kusini).

Hii ni mara ya kwanza KICC kushiriki katika tuzo hizo na kulipiku jumba la Durban ambalo limeshinda tuzo kwa mara ya tisa.

Wakazi wa Nairobi walivyoteswa na Sonko 2018

Na RICHARD MUNGUTI

HUKU mwaka wa 2019 ukianza, wakazi wa jiji la Nairobi na wananchi kwa jumla hawatasahau siku walipozuiliwa kushushwa katikati ya jiji kama walivyozea.

Hii ilikuwa baada ya  Gavana Mike Sonko kuamuru magari ya uchukuzi wa abiria yasiingie kati kati mwa jiji kuwashusha na kuwachukua abiria.

Agizo hili liliwakera wengi kwa vile walemavu, kina mama wenye mimba, wakongwe, wagonjwa na wafanyakazi waliwajibika kutembea hadi makazini.

Mbali na kuwachosha wananchi wanaoingia kati kati mwa jiji kufanya na kununua bidhaa za biashara , uchumi uliathirika pakubwa.

Wachanganuzi wa masuala ya kibiashara walikadiria hasara iliyopatikana kufikia zaidi ya Sh3bilioni.

Mahoteli yalipata hasara , mabenki hayakuhudumu ipasavyo na wakazi wengi wa jijini na wale wanaopitia Nairobi wakielekea miji mingine waliteseka.

Lakini Mahakama kuu ilishughulikia kasoro hiyo katika utoaji maagizo na kufutilia mbali agizo hilo la Sonko.

Jaji Wilfrida Okwany alisema kuwa wakazi wa jijini hawakuulizwa maoni yao kabla ya Gavana Sonko kuamuru magari ya uchukuzi yasiingie kati kati mwa jiji.

Jaji Okwany aliratibisha kesi iliyowasilishwa na mfanya biashara na mwanasiasa wa Jubilee Paul Kobia akimshtaki Gavana na kuomba korti irudishe hali ilivyokuwa awali.

Jaji Okwany alisitisha kutekelezwa kwa arifa iliyochapishwa katika Gazeti rasmi yas Serikali mnamo Mei 12 2017 ikipinga kuingia kwa magari ya abiria jijini.

“Katiba inasema lazima maoni ya wananchi yasakwe kabla ya maongozi yanayomwathiri kuchukuliwa,” alisema Jaji Okwany na kuongeza ,” Sonkio hakusaka maoni ya wakazi wa jijini. Agizo hilo la kuzuia magari kuingia kati kati mwa jiji linakinzana na katiba.”

Jaji huyo aliamuru Bw Kobia amkabidhi Sonko nakala za kesi aliyomshtaki ndipo awasilishe majibu.

Akipokea ushahidi kutoka kwa Bw Kobia , Jaji Okwany alielezwa wiki iliyopita Bw Sonko aliamuru arifa ya magari ya matatu kutoingia kati kati mwa jiji la Nairobi kuwachukua abiria na kuwashusha ianze kutekelezwa.

“Mnamo 2011 , Bw Sonko alifaulu kusitisha kutekelezwa kwa arifa sawa na hii iliyochapishwa na lililokuwa baraza la jiji la Nairobi la kuzuia magari ya uchukuzi wa abiria kuingia jijini,” Jaji Okwany alifahamishwa.

Jaji huyo aliambiwa Mahakama kuu ilisitisha kutekelezwa kwa agizo hilo.

“Kabla ya kutekelezwa kwa agizo hilo , Bw Sonko , Serikali ya kaunti ya Nairobi na Polisi (NPS) hakukuwa na mipango kabambe jinsi abiria wakishushwa nje ya kati kati mwa jiji watakavyosafiri kuingia kati kati mwa jiji,” aliteta Bw Kobia.

Bw Kobia aliteta kuwa umma haukuulizwa maoni yake kabla ya kutelezwa kake.

Kabla ya Bw Kobia kumshtaki Sonko vyama 22 vya magari ya uchukuzi wa abiria yalimshtaki yakiomba agizo hilo lisitishwe. Lakini Jaji Pauline Nyamweya hakuisitisha kutekelezwa kwa agizo hilo magari ya matatu yasibebe abiria ama kuwashusha kati kati mwa jiji la alikataa kusitisha kutekelezwa kwa agizo kwamba magari yote ya Matatu yawashushe abirie nje ya eneo la kati kati mwa jiji (CBD) kupunguza msongamano.

Na si hii kesi tu wakili Boniface Nyamu aliwasilisha kesi ya kumtimua Sonko mamlakani kwa kukaidi katiba na sheria.

Bw Nyamu anadai Bw Sonko ameshindwa kumteua naibu wake na huenda kaunti hii ikatumbukia nyongo endapo kwa njia moja au nyingine akumbwe na matitizo.

Jaji Okwany aliratibisha kesi hii kuwa ya dharura.

 

Wakazi wa Nairobi kutozwa ushuru zaidi

Na BERNARDINE MUTANU

WAKAZI wa Kaunti ya Nairobi watalipa ushuru zaidi kutokana na kuanzishwa kwa aina mpya za madaraja ya ushuru na ushuru wa ziada katika baadhi ya sekta kupitia kwa mswada wa fedha ambao umependekezwa.

Hii ni kwa lengo la kujazilia pengo la bajeti ya 2018/2019.

Kutakuwa na ushuru mpya katika uokotaji wa takataka mitaani ambapo wanaoishi katika mitaa ya mabanda watalipa Sh100 kila mwezi.

Watu wanaoishi katika mitaa ya wastani watalipa Sh300 kwa mwezi ilhali wanaoishi katika mitaa ya kifaharu watalipa Sh500 kwa mwezi.

Shule pia zitalipa ada hiyo ambapo shule za kutwa, chekechea na zilizo na wanafunzi zaidi ya 850 zitatakiwa kulipa Sh30,000 kwa mwezi mmoja.

Shule za msingi za mabweni, sekondari, vyuo viku na taasisi za mafunzo ya juu zilizo na wanafunzi zaidi ya 2,000 zitalipa kufikia Sh65,000.

Kuegesha magari ya kibinafsi kutagharimu Sh400 kutoka Sh300 kwa siku.

Huenda mashine zote za ATM jijini zikatozwa ushuru, mabango ya matangazo yataongezewa ushuru pamoja na michezo ya kujipumbaza na bahati nasibu.

JAMVI: Mkono fiche wa mabilionea unaomtetemesha Sonko jijini

Na WYCLIFFE MUIA

KWA mara nyingine, Gavana wa Nairobi, Mike Sonko amemkabili vikali Katibu katika Wizara ya Usalama wa Ndani, Karanja Kibicho huku ikiaminika kuwa mabwenyenye kutoka Mlima Kenya ndio wanatashia kuangusha utawala wa Sonko jijini. 

Wadadisi wanasema wafanyabiashara wakuu jijini, hasa kutoka Mlima Kenya pamoja na wanasiasa kadhaa kutoka chama cha Jubilee wanahisi Bw Sonko anaendesha masuala ya kaunti bila kuwahusisha ilhali wamewekeza mabilioni ya pesa jijini humo.

“Bw Kibicho ni kipaza sauti tu cha watu wenye ushawishi kutoka Mlima Kenya ambao wanahisi kupuuzwa na uongozi wa Sonko. Uteuzi wa naibu gavana wa Nairobi ndio umesababisha kupanda kwa joto katika City Hall,” anasema Prof Herman Manyora, mhadhiri wa maswala ya kisiasa katika Chuo Kikuu cha Nairobi.

 

Madai ya Sonko ni kweli

Kwa mujibu wa Prof Manyora, kauli ya Sonko kuwa kuna baadhi ya viongozi wa Mlima Kenya wanaokutana usiku kupanga njama ya ‘kumruka’ Naibu Rais William Ruto ifikapo 2022, huenda ilikuwa ya kweli kutokana na hisia za kisiasa zinazotoka Mlima Kenya.

“Sonko ana habari zake za kijasusi ambazo amewekeza pesa nyingi. Haitakuwa ajabu watu anaowashutumu kwa kuvuruga utendakazi wake ndio wanaongoza mikutano hiyo,” anaongeza Prof Manyora.

Katika mahojiano na Kameme FM, Sonko alidai Bw Kibicho na maafisa wengine watatu wakuu serikalini wanaongoza kampeni za jamii ya Agikuyu kumtema Bw Ruto kuelekea 2022.

“Kwa sasa nitafichua watu wawili wanaolenga kumhujumu Ruto: Kibicho na Nancy Gitau. Kuna wengine ambao nitawataja baadaye,” Sonko aliambia gazeti moja.

Hata hivyo, Bw Kibicho alikanusha madai hayo akisema kama mkuu wa ujasusi nchini hana habari kuhusu mikutano hiyo ya usiku.

“Ambieni Sonko akome na akabiliane na watu anaotaka kukabiliana na wao kisiasa lakini si kupitia kwangu. Mimi si mwanasiasa na siwezi kuanza kupiga vita naibu rais,” alisema Bw Kibicho.

Kibicho anasema tofauti zake na Sonko zilianza baada ya kumwamrisha atoe bendera ya taifa katika gari lake.

“Ukianza kuzama, unatafuta vitu vya kujishikilia hata vile dhaifu…ambieni Sonko asafishe jiji na aachane na mimi,” alisema Bw Kibicho.

 

Igathe alitetea Jubilee

Masaibu ya Gavana Sonko yanasemekana kuchacha zaidi baada ya aliyekuwa naibu wake Polycarp Igathe kujiuzulu.  Bw Igathe alionekana kuwakilisha na kutetea maslahi ya mabwenyenye wa Mlima Kenya pamoja na wakuu wa chama cha Jubilee.

Ni wakati huo ambapo Sonko, kupitia mtandao wake wa Facebook alidokeza mpango wake wa kutaka kujiuzulu kutokana na ‘changamoto nyingi zinazomkumba.’

“Mjue hii kazi imekuwa ngumu na iko karibu kunishinda. Na sio mambo ya bendera. Hizo nimekubali kutoa kama nilivyoshauriwa na Bw Kibicho lakini nitawaambia hivi karibuni ni kwa nini nataka kung’atuka mnishauri,” taarifa iliyochapishwa katika Facebook yake ilinukuu.

Baadaye, Sonko alipuuzilia mbali taarifa hiyo akishutumu vyombo vya habari kwa kusambaza propaganda.

Miongoni mwa watu waliotajwa kwa kushawishi uteuzi wa Bw Igathe ni pamoja na mwenyekiti wa benki ya Equity Peter Munga, naibu mwenyekiti wa chama cha Jubilee David Murathe na mmoja wa mshauri wa Rais Uhuru Kenyatta kutoka Ikulu.

Mfanyabiashara Chris Kirubi ambaye alikataa nafasi ya kuwa mshauri wa Sonko vilevile alisemekana kuwa na ushawishi mkubwa katika uteuzi wa Bw Igathe.
Wafanyabiashara hao wanatoka Kaunti ya Murang’a.

 

Wawekezaji wa Murang’a

Mbunge wa Kiharu, Irungu Kang’ata anasema kuondoka kwa Igathe kulipangua mipango ya chama cha Jubilee jijini na sharti nafasi yake ichukuliwe na mtu kutoka eneo la Kati.

“Sisi watu wa Murang’a tumewekeza sana Nairobi na hata kuna mtaa unaofahamika kama ‘Murang’a ndogo’ jijini. Ni muhimu tupate mwakilishi katika usimamizi wa kaunti ya Nairobi,” alinukuliwa Bw Kang’ata.

Mchanganuzi wa kisiasa Martin Andati asema Mlima Kenya walimuunga mkono pakubwa Peter Kenneth katika ugavana wa Nairobi 2017 lakini umaarufu wa Sonko ulilazimu apewe tiketi ya Jubilee, hivyo bado hawana Imani na uongozi wake.

“Walikuwa wanataka mtu atakayechunga biashara zao lakini Sonko anaonekana kubomoa hata makundi haramu ya kibiashara jijini ili kuokoa mabilioni ya pesa zinazoishia kwa mikono ya watu wachache,” alisema Bw Andati.

Kulingana na Bw Andati, iwapo Gavana Sonko atawania tena ugavana, huenda hatatumia chama cha Jubilee.

Tayari Sonko, amefichua kwamba atachagua mwanamke mtaalamu kutoka jamii ya Wakikuyu kuchukua mahali pa Igathe.

 

Ushirikiano na Wakikuyu

“Ninajua nafasi ya naibu gavana inafaa iende kwa Mkikuyu kwa sababu wengi wao waliniunga mkono, lakini nataka niwe huru kumchagua Mkikuyu nimtakaye,” alisema Sonko.

“Nimeshirikiana vyema na Wakikuyu tangu 2010 ambapo walinipigia kura kwa wingi nikiwa Mbunge wa Makadara. Mnamo 2013, pia walinipigia kura kuwa seneta na baadaye nikawa gavana. Wao hawana ukabila na kama wangekuwa wakabila, singekuwa gavana,” akasema.

Miongoni mwa wanawake ambao wamekuwa wakisemekana kuwa kwenye orodha yake ni aliyekuwa Mbunge wa Starehe, Bi Margaret Wanjiru, gwiji wa kibiashara, Bi Agnes Kagure, na aliyekuwa Mwakilishi wa Kaunti ya Kiambu, Bi Ann Nyokabi.

Kutokana na matamshi yake, kuna uwezekano mkubwa kuwa atamchagua Bi Kagure (mzaliwa wa Nyeri) au Bi Nyokabi kwani wengine waliobaki hawajaafiki vigezo alivyoyataja.

Inadaiwa Ikulu pamoja na wafanyabiashara wakuu kutoka Murang’a wanashinikiza kuteuliwa kwa Bi Nyokabi ambaye ni binadmu wa Rais Kenyatta. Hata hivyo Sonko anapendelea Bi Kagure kwa kuwa hana ushawishi mkubwa wa kisiasa, hasa kutoka Mlima Kenya.

Tamasha zang’oa nanga kwa shairi la kusisimua

Na ANTHONY NJAGI

AWAMU ya 59 ya michezo ya kuigiza ya kitaifa baina ya shule na vyuo yalianza Jumanne katika shule ya wavulana ya Lenana, Kaunti ya Nairobi.

Shule ya Laiser Hill Academy ilikuwa ya kwanza jukwaani katika tamasha hizo ziliizofunguliwa rasmi na Kamishna wa eneo la Nairobi, Bw Kang’ethe Thuku.

Mwanafunzi Lennox Agwenge wa Laiser Hill Academy kutoka Rift Valley aliwasilisha shairi la kuigizwa lenye kichwa “The Hotbed” ambalo linatoa hadithi kuhusu shule katika kijiji maskini ambayo inashiriki mashindano hayo ya kuigiza kwa mara ya kwanza.

Wanafunzi hao wanaonekana kushtuliwa sana na jinsi shule nyingine zimewekeza katika mavazi na ala nyingine za kutumia jukwaani. Kutokana na hali hiyo, washiriki wanajawa na wasiwasi ikiwa wao kweli watafaulu ama kupitisha ujumbe wao.

Lakini mambo yanaenda kinyume na matarajio yao, baada ya kuhitimu kuendelea kwa kuwa ujumbe wao ulionekana kufaa.

Shairi hilo limeandikwa na Clifford Ouma al maarufu Nyakwar Dani, na linasheheni vichekesho tele.

Mwandishi huyo amewahi kushirikiana na Shule ya Sekondari ya Highway hata kwa shairi maarufu la Otonglo Time lililowasilishwa na Daniel Owira, mnamo 2010, na ambaye alidhaminiwa na Rais Uhuru Kenyatta kwa masomo yake, baada ya kushiriki tamasha hizo.

Shule ya Upili ya Kenya High ilikuwa na densi ya “Alando”. Densi hiyo inamzungumzia msichana kwa jina Alando ambaye anatelekezwa na wazazi wake ambao wamejali zaidi taaluma zao na kumwachia mjakazi “jakasi” jukumu la ulezi.

Jakasi ni mcha Mungu na mwenye kuamini sana maombi, na anaonekena akimuombea sana Alando. Lakini wazazi wanaishia kumshtumu kwa kujaribu kumbadilisha mtoto wao dini.

Jambo hilo, linamkasirisha Alando ambaye anaamua “kumwaga mtama” kuhusu wazazi wake ambao wamemsahau na anaelezea kuwa anayemlea ni Jakasi.

Densi hiyo inaongozwa na Janice Njuguna, Sumeiya Salim, Kellen Amimo, Brenda Ouma na ilitayarishwa na Henry Wanjala.

Shule ya Upili ya Menengai kutoka Rift Valley  ilikuwa na mchezo “Gorias Glory’’ ulioandikwa na Michael Kiguta. Mchezo huo unaelezea jinsi wavulana na wasichana wamewachwa kujitafutia maisha bila mwelekeo wowote.

“Kwa kipindi cha miaka mitano, tumekuwa kwa mashindano ya kitaifa na siri ni kushirikiana na wanafunzi kuanzia wakati wa kutayarisha hadithi hadi inapokamilika kutayarishwa,” alieleza Bw Kiguta.

Tamasha hizo pia zinashuhudia jinsi wazazi wanafaa kuzingatia talanta na sio masomo pekee.

 

Maji taka katikati ya jiji? Sonko amefeli, asema Atwoli

Bw Francis Atwoli katika mahojiano awali. Picha/ Maktaba

Na VALENTINE OBARA

KATIBU Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi (Cotu), Bw Francis Atwoli, amekashifu usimamizi wa Kaunti ya Nairobi kwa kile alichosema ni kutojali hali ya maisha ya wakazi.

Akizungumza Jumanne kwenye kikao cha wanahabari katika makao makuu ya Cotu jijini Nairobi, Bw Atwoli alisema inasikitisha jinsi kumekosekana mipangilio mwafaka jijini na matokeo yake ni jiji kuu linalofanana na mtaa mkubwa wa mabanda.

Kulingana naye, sura ya jiji imeharibiwa na ukosefu wa mpangilio bora wa uchukuzi wa umma, ujenzi wa vibanda kiholela na uchafu.

“Ningekuwa gavana leo hungeona matatu hata moja jijini. Nairobi ingekuwa jiji la kikweli, hata hivi vibanda hamngeviona. Kwa sasa hamna jiji bali ni mtaa wa mabanda na hakuna anayejali,” akasema.

Gavana wa Nairobi, Bw Mike Sonko, amekuwa akitangaza miradi mbalimbali ambayo inaendelezwa na utawala wake kuinua hadhi ya Nairobi kama jiji kuu linalotegemewa zaidi na mataifa ya ukanda wa Afrika Mashariki. Lakini hakuna mengi yametekelezwa.

Miongoni ambayo amekuwa akiahidi ni mpango wa kuzoa taka kwa mbinu za kisasa, ujenzi wa masoko ili kuhamisha wachuuzi wote kutoka katikati mwa jiji, na kushirikiana na serikali kuu ili kuwe na mabasi yatakayokuwa yakisafirisha abiria katikati mwa jiji badala ya kuruhusu matatu kuingia jijini.

Hata hivyo, wakosoaji wake wamekuwa wakilalamika jiji linazidi kuharibika chini ya uongozi wake.

 

Maji taka 

“Hapa nje kuna mfereji wa maji taka ambao umepasuka na hatujaona inspekta wa barabara, wa maji taka wala mtu yeyote kutoka Wizara ya Afya akikagua hatari iliyopo kwa afya ya wananchi,” akasema Bw Atwoli.

Alizungumza baada ya kukutana na Waziri wa Utumishi wa Umma, Prof Margaret Kobia ambapo alisema Cotu imejitolea kushirikiana na serikali ili kutimiza malengo ya nguzo nne kuu za maendeleo.

Bw Atwoli alisema ingawa wanajali zaidi nguzo kuhusu uimarishaji wa viwanda, nguzo zingine ikiwemo afya na ujenzi wa nyumba za bei nafuu kwa wananchi zitasaidia pakubwa kuboresha maisha ya wafanyakazi.

“Serikali inatambua kilichosababisha matatizo katika sekta ya viwanda nchini ndiposa inajitahidi kurekebisha na tunaiunga mkono. Tunaamini inaweza kufanikiwa kwa vile imeweka malengo yake chini ya nguzo nne pekee,” akasema.

Hatua hii itakuwa habari njema kwa serikali ya Jubilee kwani Rais Uhuru Kenyatta amekuwa akitoa wito wa ushirikiano kutoka kwa wadau wote ili kufanikisha maazimio yake kabla astaafu, na tayari alipata ushirikiano wa kiongozi wa upinzani, Bw Raila Odinga.

Bw Atwoli alisifu pia uamuzi wa serikali kutafuta madaktari zaidi kutoka nchi za kigeni kwani anaamini itasaidia kuboresha huduma za matibabu nchini.

Mabwanyenye wachache wanamiliki 80% ya utajiri Nairobi na Mombasa – Utafiti

Na BERNARDINE MUTANU

WAKAZI wachache wa Nairobi na Mombasa ndio matajiri zaidi nchini Kenya kulingana na utafiti wa hivi punde.

Utafiti huo, Kenya Integrated Household Budget Survey (KIHBS), ulipata kuwa asilimia 20 ya wakazi wa Nairobi na Mombasa wanamiliki asilimia 86.4 na 78.2 kwa mpangilio huo, ya utajiri wa maeneo hayo.

Hii ni kumaanisha zaidi ya asilimia 80 ya wananchi wanaoishi katika miji hiyo wana mapato ya chini zaidi.

Jijini Nairobi, asilimia 40 ya wakazi wa Nairobi ni maskini kupindukia kulingana na utafiti huo, na uwezo wao wa matumizi ya fedha ni asilimia 0.4 pekee.

Asilimia 60 ya wananchi wote nchini wana uwezo wa kutumia asilimia 2.7 ya mapato ya taifa, kumaanisha asilimia 40 ya wananchi wote wanatumia asilimia 97.3 ya rasilimali ya taifa.

Katika eneo la Mombasa, asilimia 60 ya wakazi wamedhibiti asilimia 4.7 ya rasilimali jijini humo.

Utafiti huo ulionyesha kuwa kuna tofauti kubwa zaidi ya kimapato kati ya wananchi huku wale tajiri zaidi wakipatikana katika maeneo ya miji ambako mapato hayalingani.

Huku wachache wakindeelea kwa utajiri, wengi zaidi wanazidi kuumizwa na umaskini.

Asilimia 60 ya rasilimali ya Kenya inamilikiwa na watu wachache zaidi (milioni 9) ilhali 36,296,000 wamesalia kuwa maskini kuambatana na makadirio ya idadi ya wananchi ya 2016.

Tofauti za kimapato zimejitokeza zaidi katika maeneo ya miji ikilinganishwa na maeneo ya mashambani.