Agnes Odhiambo ateuliwa mkuu wa NTSA

Na CHARLES WASONGA

WIKI hii wabunge wanawake walilalama kwamba jinsia hiyo inadhulumiwa baada ya Seneta wa Nakuru Susan Kihika kupokonywa wadhifa wa kiranja wa wengi katika seneti na kupewa mwanaume, Irungu Kang’ata, lakini pia Rais Uhuru Kenyatta amewatuza wanawake wawili kwa vyeo serikalini.

Amemteua aliyekuwa Msimamizi wa Bajeti (CoB) Agnes Odhiambo kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kitaifa ya Usalama Barabarani (NTSA).

Vilevile, Rais Kenyatta amemteua aliyekuwa Naibu Chansela wa Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta (JKUAT) Profesa Mabel Imbuga kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Kudhibiti Matumizi ya Pombe na Mihadarati (Nacada).

Teuzi hizo ni miongoni mwa nyingine nyingi ambazo Rais Kenyatta alifanya katika mashirika ya serikali na kuchapishwa katika toleo la Ijumaa la Gazeti rasmi la Serikali.

Bi Odhiambo na Profesa Imbuga watashikilia nyadhifa hizo kwa miaka mitatu, kuanzia Mei 13, 2020.

Mnamo Alhamisi wabunge 12 wanawake wakiongozwa na Mbunge wa Kandara Alice Wahome, walisema sio haki kwa Rais Kenyatta kumpa mwanamume cheo cha Bi Kihika.

“Mbona wanawake wanadhulumiwa ndani ya Jubilee ilhali walikuwa mstari wa mbele kuifanyia kampeni kufa na kupona katika chaguzi mbili zilizopita? Hata kama hawakutaka Seneta Kihika aendelea kuhudumu kwa wadhifa wa kiranja wa seneti nafasi hiyo ingepewa mwanamke mwingine lakini sio mwanamume,” akasema Bi Wahome ambaye ni kiongozi wa vuguvugu la ‘Inua Mama Jenga Jamii’.

Maafisa wa NTSA wanaoshukiwa kuhusika kwa mauaji ya DusitD2 waachiliwa

Na RICHARD MUNGUTI

MAAFISA watano wa Mamlaka ya Kitaifa ya Usalama wa Uchukuzi (NTSA) waliotiwa nguvuni na kuzuiliwa kuhusishwa na shambulizi la hoteli ya DusitD2 ambapo watu 21 waliuawa waliachiliwa Ijumaa.

Hakimu mkazi Bi Muthoni Nzibe alifahamishwa na upande wa mashtaka kwamba hakuna ushahidi uliopatikana kuwahusisha moja kwa moja maafisa hao wa NTSA na shambulizi hilo lililotekelezwa na magaidi wa Al Shabaab mtaani Westlands, Nairobi.

Bi Nzibe alikuwa ameamuru watumishi hao sita wa wazuiliwe kwa muda wa siku 30 kuwasaidia polisi kukamilisha uchunguzi.

“Naomba hii mahakama iwaachilie washukiwa kwa vile hakuna ushahidi wa kuwahusisha na shambulizi hilo,” kiongozi wa mashtaka alimweleza Bi Nzibe Ijumaa alasiri.

Hakimu aliombwa awaachilie washukiwa hao watano kisha awaamuru wawe wakipiga ripoti kwa afisi ya kupambana na ugaidi ATPU kila Alhamisi hadi maagizo mengine yatolewe.

Hakimu alifahamishwa wafanyakazi hao wa NTSA walishukiwa waliwasaidia magaidi hao kwa kuandikisha magari mawili tofauti wakitumia nambari moja ya usajili – KCN 240E.

Gari hili muundo wa Toyota Ractis, ndilo lilitumiwa na magaidi hao kwenda DusitD2 mnamo Januari 15, 2019.

Watano kati ya maafisa hao sita wanadaiwa kuhusika kwenye kashfa ya kutengeneza nambari feki za usajili wa magari.

Bi Nzibe alielezwa na kiongozi wa mashtaka Bw Duncan Ondimu kuwa maafisa hao wa NTSA waliwasaidia magaidi hao kwa kuwapa nambari feki ya usajili.

“Naomba hii mahakama iwaruhusu polisi wawahoji washukiwa hawa kwa siku 30 ndipo ukweli ujulikane kuhusu kashfa ya utoaji nambari feki za usajili wa magari,” Bw Ondimu alimweleza hakimu washukiwa walipofikishwa mahakamani wiki iliyopita.

Wakili Dunstan Omari aliyewatetea maafisa hao wa NTS. Picha/ Richard Munguti

Lakini ombi hilo lilipingwa vikali na mawakili Dunstan Omari na Jotham Arwa waliosema muda unaoombwa na polisi ni mwingi na uchunguzi unaotakiwa kufanywa sio mwingi vile.

“Kuwapa polisi muda huo wa siku 30 ni ukandamizaji wa haki za washukiwa,” alisema Bw Omari.

Bw Arwa alimweleza hakimu kuwa mkurugenzi wa mashtaka ya umma anatakiwa kuwafikisha kortini washukiwa baada ya kukamilisha uchunguzi.

Bi Nzibe alikubalia ombi la DPP akisema polisi wanahitaji muda kukamilisha zoezi hilo.

Waliozuiliwa ni Bw Anthony Kadu, anayefanya kazi katika idara ya usajili. Kazi yake ni kuandikisha magari kwa wanunuzi wapya. Bi Jacqueline Githinji, mkurugenzi wa usajili na utoaji leseni, Bw Cosmas Ngeso, ambaye ni naibu wa Bi Githinji.

Wengine ni Bw Irving Irungu, Bw Stephen Kariuki, karani anayehusika na upeanaji wa nambari za usajili na Bw Charles Ndung’u anayefanya kazi katika idara ya utoaji wa hatimiliki za magari.

Wa mwisho ni Bw Augustine Mulwa Musembi aliyefikishwa kortini Jumatano. Polisi walikubaliwa kumzuilia Bw Musembi kwa muda wa mwezi mmoja.

Uchunguzi wa polisi ulibaini nambari ya usajili ya gari hilo -Toyota Ractis nambari ya usajili KCN 240E –  lililotumiwa na magaidi watano waliouawa limesajiliwa na gari lingine muundo tofauti lililopatikana Kitengela, Kaunti ya Kajiado.

Polisi wanasema usajili wa gari moja ni feki ama ulifanywa kwa njia ya udanganyifu.

Bw Musembi anahofiwa ndiye alisaidia katika usajili huo feki ilhali Bw Kadu anadaiwa ndiye alimwamuru Musembi kuandikisha tena nambari hiyo iliyotumiwa na magaidi hao.

Polisi waliomba muda kuwahoji maafisa hao wa NTSA na kuendeleza uchunguzi mwingine wa kina.

“Ni muhimu polisi kupewa muda kukamilisha uchunguzi na kubaini utengenezaji na utoaji wa nambari ya usajili inayopewa magari mawili tofauti,” korti iliombwa.

Hakimu aliamuru kesi hiyo itajwe Februari 28, 2019.

Vyama 7 vya matatu vyapigwa marufuku na NTSA

Na BERNARDINE MUTANU

Mamlaka ya Uchukuzi na Usalama (NTSA) imefutilia mbali usajili wa vyama saba vya magari ya uchukuzi wa umma.

Kulingana na taarifa iliyotolewa Jumanne, NTSA ilisema kuwa Sacco hizo zilisimamishwa Septemba 13, 2018, bila kuelezea sababu.

Lakini huenda ni kutokana na malalamishi ya uendeshaji mbaya wa magari au kusababisha ajali.

Sacco hizo ni Molo Shuttle ambayo hutumia barabara ya Nairobi, Nakuru, Olenguruone na Kisii, Nairobi Kiruline Sacco inayotumia barabara ya Nairobi, Murang’a, Othaya, Nyeri na Nyahururu, Gakanago Sacco ambayo hutumia barabara Nyeri, Gataragwa na Ngobit, New Lowland Sacco ambayo hutumia barabara ya Nakuru, Maraigat na Kabarnet, Hannover Commercial Enterprise inayotumia Kikuyu, Waiyaki Way, Westlands, Tom Mboya, Thika Road, Kasarani na Mwiki.

Sacco zingine zilizofutiliwa mbali ni Newlot Sacco ambayo hutumia barabara ya Nairobi, Machakos, Makueni, Kitui, Mutomo, Kibwezi, Ikutha, Voi na Mombasa.

Pia, magari yanayohudumu chini ya Peja Travellers katika mitaa ya Jericho, Maringo, Jogoo Road na Temple Road yalisimamishwa.

Kumekuwa na ongezeko la visa vya ajali nchini ambazo zimesababisha vifo vya mamia ya abiria na kujeruhi wengine.

NTSA kuwapa wenye magari vitabu vya kidijitali kuzima wizi

Na BERNARDINE MUTANU

Mamlaka ya Uchukuzi na Usalama Barabarani (NTSA) imetangaza mipango ya kuanzisha vitabu vya kielektroniki vya umiliki wa magari kwa lengo la kuzima wizi.

Mkurugenzi Mkuu wa NTSA Francis Meja alisema lengo kuu litakuwa ni kuimarisha utoaji wa habari kupitia sajili yake ya kimtandao (TIMS) katika tovuti ya mamlaka hiyo.

“Kwa sasa tunatathmini uwezekano wa kuanzisha vitabu vya kielektroniki vya kumiliki magari ambavyo vinaweza kuthibitishwa kwa njia rahisi katika mfumo wetu, na kuangalia jinsi mfumo huo unaweza kuunganishwa na kampuni za bima ili kujua mtoaji wa bima,” alisema Bw Meja katika taarifa.

Alisema mfumo huo unatoa nafasi kwa benki kukagua magari chini ya bima yake kielektroniki kwa lengo la kupunguza wizi.

Hii ni kutokana na kuwa mfumo huo unatoa nafasi ya benki kupekua habari kwa lengo la kuzuia wezi.

Hata hivyo hakueleza wakati kamili ambapo NTSA itazindua mpango huo. Septemba mwaka jana, wachunguzi walibaini kundi la wezi lililokuwa likitumia vitabu feki vya gari kwa lengo la kufidiwa.

NTSA yaanzisha vituo vya mapumziko kwa madereva

NA CECIL ODONGO

MAMLAKA ya Kitaifa ya usalama barabarani(NTSA) kwa ushirikiano na mashirika ya kibinafsi imeanzisha vituo 28 ambavyo vitakuwa vikitumika kama vituo vya mapumziko na matibabu  kwa madereva wa malori ya safari za masafa marefu.

Kupitia mpango ujulikanao kama  SWHAP (Swedish Workplace Hiv Aids Programme), NTSA inalenga  kupunguza idadi ya ajali zinazoshuhudiwa katika barabara kuu ya Mombasa-Nairobi-Malaba ambayo hutumiwa sana na madereva wa malori hayo.

Chini ya mpango wa uangalizi wa safari na mienendo wa madereva  maarufu kama CHECKMATE, zaidi ya madereva 1000 watahudumiwa  kila siku katika vituo ambavyo tayari vinafanya kazi  katika miji ya Maungu, Kericho, Garissa na Kisumu.

Akizungumza wakati wa kuzindua ushirikiano huo katika hoteli ya Panfric jijini Nairobi,  Mkurugenzi mkuu Francis Meja  alitaka mashirika nchini kuwasajili madereva wao chini ya mapango huo  ili kusaidia kuhakikisha usalama barabarani na kudhibiti mienendo ya madereva.

“Ninayaomba mashirika kuwasajili madereva wa masafa marefu katika mpango huu kwa kuwa tutafungua vituo 20 zaidi kando na hivi vinane ambavyo tunafurahia kusema  vimesaidia pakubwa kushusha idadi ya ajali kati ya Nairobi, Mombasa na mji wa mpakani wa malaba,” akasema Meja.

Aidha Bw Meja aliwaomba wadau katika sekta ya matatu i kukumbatia majadiliano kabla ya kushiriki mgomo unaotarajiwa wiki hii kufuatia ongezeko la bei ya mafuta huku wakitishia kuongeza nauli kwa wasafiri.

Mkurugenzi wa Shirika la kutoa ushauri kuhusu usalama barabarani(PRSC) Habel Okema, aliusifu mpango wa CHECKMATE na kusema imeweza kusiadia kutoa huduma za ukaguzi na ushikaji doria barabarani..

“Tunaamini kwamba mpango huu utaisaidia serikali kuhakikishia Wakenya usalama wao barabarani. Mashirika na kampuni ambazo zimetumia mpango huu zimepata ufanisi mkubwa na visa vichache vya utovu wa maadili miongoni mwa madereva wao,” akasema Bw Okema.

Mpango wa SWHAP hufadhiliwa na serikali ya Uswidi na umetumika katika  zaidi ya vituo 370 katika mataifa ya Botswana, DRC, Kenya, Mozambique, Namibia, Rwanda, Afrika Kusini, Tanzania, Uganda, Zambia na Zimbabwe.

Omtatah afika kortini kupinga sheria mpya kwa madereva

Na RICHARD MUNGUTI

MWANAHARAKATI Okiya Omtatah amewasilisha kesi mahakamani kupinga kuzinduliwa kwa maagizo mapya kuhusu madereva.

Bw Omtatah anaomba Mahakama Kuu ibatilishe sheria za mtaala mpya uliotangazwa na Mamlaka ya Kitaifa ya Uchukuzi na Usalama (NTSA).

Mtetezi huyo wa wanyonge anasema kuwa sheria mpya za utoaji mafunzo kwa madereva na kuwahoji madereva wa magari ya uchukuzi wa umma upya yanakinzana na haki zao.

Bw Omtatah anasema masharti kwamba kila shule inayotoa mafunzo kwa madereva iwe na uwanja wa ekari 1.7  haifai.

NTSA inazitaka shule zote za kutoa mafunzo kwa madereva ziwe na uwanja mkubwa ndipo kuwe na barabara za kuwafundisha makurutu.

Pia zinatakiwa kuwa na majengo mazuri ya kutoa mafunzo. Omtatah anasema umma hakushirikishwa na NTSA kabla ya kupitisha sheria hizi.

NTSA ilitoa maagizo haya baada ya ajali kuongezeka haswa mwishoni mwa mwaka 2017.

Pendekezo magari ya masafa marefu yawe na madereva wawili

Na BERNARDINE MUTANU

Pendekezo limetolewa ili magari ya umma yawe na madereva wawili ikiwa yanasafiri mwendo mrefu, zaidi ya kilomita 500.

Magari yanayoendeshwa kwa zaidi ya saa nane yanalengwa katika pendekezo hilo linalolenga kudhibiti idadi kubwa ya ajali za barabarani.

Ikiwa hakuna madereva wawili, dereva wa gari la masafa marefu anafaa kusimama kwa muda, baada ya kuwa barabarani kwa saa nyingi, kulingana na pendekezo hilo.

Pendekezo hilo lilitolewa na Shirika la Uchukuzi na Usalama barabarani (NTSA) katika notisi rasmi iliyochapishwa Januari 11.

Pendekezo hilo lilitolewa baada ya mamia ya Wakenya kuangamia katika ajali za barabarani hasa katika mwezi wa Desemba.

Ajali hizo zilisemekana kusababishwa na madereva wachovu na kuzembea kwa madereva. Kulingana na taratibu zilizopo, madereva wanafaa kuwa wawili usiku katika uchukuzi wa abiria kwa masafa marefu.

Kulingana na pendekezo jipya, madereva wanafaa kupumzika katika muda wa lisali moja baada ya kuendesha gari kwa saa nne.

Madereva wote kulipa Sh5,000 kupokea mafunzo mapya

Na BERNARDINE MUTANU

MADEREVA wote wa matatu, magari ya uchukuzi umma na malori ya kibiashara wanastahili kurejea darasani kwa mafunzo zaidi ya uendeshaji.

Mafunzo hayo yatakayotolewa katika taasisi tofauti za serikali yatawabidi madereva hao kulipa Sh5, 000.

Mafunzo hayo yatatolewa katika muda wa siku tano ambapo madereva 400,000 wanatarajiwa kushiriki.

Madereva hao watapewa mafunzo hayo kwa awamu katika muda wa siku hizo, na yataipa serikali Sh2 bilioni ikiwa wote watahudhuria.

Hatua hiyo ilitangazwa na serikali Januari katika hatua za kukabiliana na ongezeko la ajali za barabarani.

Kwa awamu ya kwanza, madereva 8,000 wa PSV za uchukuzi wa usiku wanatarajiwa kuhudhuria mafunzo hayo, alisema Francis Meja, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uchukuzi na Usalama nchini (NTSA).