‘Sherehe’ kwa walevi baa 1,800 zikitakiwa kuuza pombe yao yote leo

Na WAIKWA MAINA

WAMILIKI wa zaidi ya baa 1,800 katika Kaunti ya Nyandarua ambao leseni zao za kibiashara hazikuongezewa muda, wametakiwa kuuza pombe yao ya Sh100 milioni kufikia leo jioni kabla ya biashara zao kufungwa kesho Jumanne.

Baada ya ukaguzi, Kamati ya Kudhibiti Mauzo ya Vileo kwenye Kaunti ya Nyandarua ilitoa upya leseni kwa baa 600 pekee kati ya 900 ambayo wamiliki wao walituma maombi ili kuendelea kufanya biashara hiyo.

Kaunti hiyo ina baa 2,400 ila nyingi zimekuwa zikiendeleza biashara hiyo kiharamu bila kufuata sheria.

Wamiliki wa baa hizo pia walikataa kutuma maombi ya leseni mpya wakilalamikia masharti makali yaliyowekwa na kamati ya kaunti.

Mwenyekiti wa Muungano wa Wamiliki wa baa Kariu Ng’ang’a alikashifu kamati hiyo, akisema itakuwa vigumu kuuza pombe zote kufikia leo huku akiomba muda huo usongeshwe.
Buy bodybuilding anabolic steroid Masterone, buy steroids paris – HFPA clenbuterol for sale telecharger full bodybuilding program for men a – torrent.
“Itakuwa hasara kubwa na naomba kamati iwape wafanyabiashara hao muda zaidi wamalize kuuza pombe kwenye hazina yao na pia kutimiza masharti hayo mapya,” alisema.

Pombe haramu lita zaidi ya 300 yaharibiwa katika mitaa mitatu ya mabanda

Na SAMMY KIMATU

WASHUKIWA watatu walikamatwa huku lita zaidi ya 300 za pombe haramu zikiharibiwa katika mitaa mitatu ya mabanda, Kaunti ya Nairobi, Jumanne.

Aidha, msako huo ulifanyika katika mtaa wa mabanda wa Mukuru-Fuata Nyayo, Mariguini na Kisii kwenye maeneo ya South B, kaunti ndogo ya Starehe.

Msako huo uliongozwa na chifu wa eneo hilo, Bw Charles Mwatha, Naibuye Bw, Bw Paul Mulinge, maafisa wa polisi na viongozi wa Nyumba Kumi mtaani.

Chifu Mwatha aliambia Taifa Leo kwamba msako huo ulifanikiwa baada ya wakazi kushirikiana na kamati ya usalama mtaani.

“Msako wetu ulifaulu kwa sababu wananchi walishirikiana na kamati ya Nyumba Kumi mtaani kutupasha habari zozote zinazohusiana na usalama wa mitaa yetu,” Bw Mwatha akasema asema.

Wakati wa msako huo, pombe aina ya toivo, busaa na chang’aa zilinaswa na kuharibiwa huku milango ya nyumba ikibomolrewa na kubebwa.

Isitoshe, maafisa wa utawala waliharibu vifaa vilivyotumiwa kutengeneza pombe.

Fauka ya hayo, maafisa wa utawala walisema wauzaji wa pombe haramu walifanikiwa kutoroka baada ya kupashwa habari kuna msako.

Kufuatia mawasiliano kwa njia ya simu, polisi na machifu hawangeweza kupata stoo za pombe husika kwani pombe iliyonaswa ilikuwa ile iliyokuwa tayari kuuziwa wateja.

“Wauzaji wengi walifanikiwa kutoroka mtego wa machifu na polisi baada ya kupigiana simu. Hata hivyo, wajue chuma chao kimotoni kwani misako zaidi na itakayokuwa mikali imepangwa,’’ chifu Mwatha asema.

Wanawake watwaa majukumu ya kiume wazee wakilewa tu!

WANDERI KAMAU na STEVE NJUGUNA

ATHARI za matumizi ya mihadarati miongoni mwa vijana katika eneo la Mlima Kenya zimeanza kupita mipaka kiasi kwamba, wanawake sasa wamechukua majukumu yanayotekelezwa na wanaume.

Ingawa kuna majukumu yanayopaswa kutekelezwa na wanaume kulingana na mtindo wa kimaisha wa jamii za Kiafrika, hali imebadilika katika eneo hilo.

Wanawake wanasema “wamegeuka kuwa wanaume” kwani waume wao wamezamia kwenye ulevi na matumizi ya dawa za kulevya.

Ni hali ambayo imezua mdahalo na wasiwasi mkubwa, baada ya picha za wanawake wakichimba kaburi kusambaa katika mitandao ya kijamii.

Kisa hicho kilifanyika katika eneo la Wiyumiririe, Kaunti Ndogo ya Ngorika, Kaunti ya Nyandarua.

Kulingana na wenyeji, wanawake waliamua kuchukua jukumu hilo baada ya vijana waliotarajiwa kushiriki kwenye kazi hiyo kukataa kufika wakidai “kutukanwa na chifu wa eneo hilo.”

“Walikataa kushiriki wakisema chifu aliwakosea heshima kwa kuwaita wazembe na walevi kutokana na uraibu wao wa kuzamia kwa mihadarati,” akasema Bi Mary Wanjira ambaye ni mkazi, kwenye mahojiano na ‘Taifa Leo.’

Ingawa vijana walidai “kukosewa heshima”, kisa hicho kimeibua hofu kuhusu kukithiri kwa ulevi miongoni mwa wanaume katika ukanda huo.

Hilo pia linajiri baada ya mwanamume mmoja kufariki Jumapili mjini Nyahururu huku wengine tisa wakilazwa hospitalini baada ya kunywa pombe yenye sumu.

Eneo la Mlima Kenya linazishirikisha kaunti kumi, ambazo ni Nyeri, Nyandarua, Meru, Tharaka-Nithi, Embu, Laikipia, Murang’a, Kiambu, Kirinyaga na Nakuru.

Hata hivyo, athari za ulevi zimekuwa zikionekana sana kuathiri eneo la Kati.

Kulingana na aliyekuwa Mshirikishi Mkuu wa Mfumo wa Nyumba Kumi, Bw Joseph Kaguthi, inasikitisha kuwa vijana wengi wanaendelea kujiingiza kwenye ulevi licha ya juhudi ambazo zimekuwa zikiendeshwa na serikali kubuni ajira.

Anasema kwa muda mrefu, vijana wamekuwa wakitoa kisingizio cha ukosefu wa ajira na ugumu wa maisha kama sababu kuu ya kujiingiza kwenye uraibu huo.

“Serikali imejizatiti kuimarisha vita dhidi ya maovu hayo kupitia ujenzi wa vyuo vya kiufundi kuwawezesha vijana kujiendeleza kitaaluma. Kinyume na ilivyokuwa awali, hawahitajiki kulipa ada kubwa,” akasema.

Bw Kaguthi anawalaumu wazazi na walezi wa vijana, akisema hawatekelezi majukumu yao ya ulezi ifaavyo.

Anapendekeza wadau wote katika jamii kuungana ili kuhakikisha ushindi dhidi ya janga hilo.

Wakazi mbalimbali kutoka ukanda huo waliozungumza na ‘Taifa Leo’ waliwalaumu baadhi ya maafisa wa utawala, hasa machifu, kwa kuruhusu utengenezaji pombe kuendelea bila kukabiliwa hata kidogo.

Katika Kaunti ya Nyandarua, wenyeji walisema polisi huwa wanashirikiana na machifu kuchukua hongo kutoka kwa watengenezaji pombe hizo.

“Inasikitisha hata idadi ya watoto wanaoenda shuleni imepungua sana kwani vijana wengi wanachelewa kuoa kutokana na matumizi ya mihadarati. Idadi ndogo ya watoto katika shule zetu ni kama robo pekee ikilinganishwa na ilivyokuwa katika miaka ya awali,” asema Mzee Gitonga Mwangi, ambaye ni mwanachama wa Mfumo wa Nyumba Kumi katika eneo la Kinangop.

Mnamo 2015, Rais Uhuru Kenyatta alianza kampeni kali kukabili ulevi katika ukanda huo, akiutaja kuwa kizingiti cha maendeleo.

Walevi Gatundu waasi pombe kujishughulisha na kazi za manufaa

Na LAWRENCE ONGARO

WALEVI katika kaunti ndogo ya Gatundu wameasi unywaji wa pombe haramu na kujihusisha na kazi za ujenzi wa taifa.

Vijana wapatao 16 waliozamia ulevi kwa muda mrefu kutoka kijiji cha Wamuguthuko na kile cha Kinyango walisema kuwa wamesitisha ulevi na kutaka kujihusisha na kazi za kuwanufaisha maishani.

Meneja wa NACADA katika Kaunti ya Kiambu Amos Warui, alieleza kuridhika kwake na hatua iliyochukuliwa na vijana hao.

Alieleza kuwa afisi yake itafuatilia mienendo ya vijana hao ili wasije wakarejelea uraibu wa kunywa pombe kupindukia.

Wakazi wa eneo hilo walifurahia hatua hiyo wakiitaja kama mwamko mpya.

Naibu Kamishna wa Gatundu Kusini Bw Stanely Kamande na Askofu wa Kanisa la Pentekosti Bw John Gichuhi, walipongeza hatua hiyo na kuitaja kama ya kipekee itakayoleta mabadiliko kwa vijana wengi eneo hilo.

Naibu Kamishna aliwaamuru machifu wawe macho mashinani kuona ya kwamba vijana hawapotelei kwenye unywaji wa pombe.

“Wazazi wengi wamefurahia hatua hiyo na bila shaka vijana hao wataanza maisha mapya ya kuboresha hali zao,” alifafanua Bw Kamande.

Aliwataka machifu wawe macho kuona ya kwamba vijana hawarejelei unywaji wa pombe haramu ambayo imeathiri maisha ya wengi vijijini.

“Wazazi wanastahili pia kuwa mstari wa mbele kuona ya kwamba vijana wote wanajishughulisha na mambo yatakayowanufaishga kimaisha. Nina imani wakazi wa eneo hili watakuwa raia wema na watakuwa mfano kwa maeneo mengine,” akasema.

Vijana hao waliahidiwa kupewa fedha za mikopo kupitia hazina ya Uwezo Fund ili waweze kujiendeleza na kufanya kazi za kujitegemea kama vile uchomeleaji wa vyuma, ujenzi, upakaji wa rangi, na hata uoshaji wa magari.

Vijana hao wamekiri ya kwamba uraibu wa kunywa pombe ulikuwa umewateka nyara, lakini wakasema kwa sasa wako tayari kujirekebisha.

Waliotia ‘mchele’ kwa pombe ya mteja wakamatwa

Na GEORGE MUNENE

WANAWAKE wawili wanaodaiwa kumpumbaza mwanaume kisha kumwibia pesa baada ya kumtilia ‘mchele’ kwenye pombe yake, jana walikamatwa na polisi katika Kaunti ya Kirinyaga.

Wawili hao wanashukiwa kuwa kati ya genge la warembo ambao wamekuwa wakiwawekea dawa ya kuwapotezea fahamu kwenye kinywaji na kuwaibia. Walinaswa kutoka kwa maficho yao na wanaendelea kuzuiwa katika kituo cha polisi cha Wang’uru wanakohojiwa kuhusu tukio hilo.

Mkuu wa Polisi wa Mwea Mashariki Daniel Kitavi alieleza Taifa Leo kwamba, mwanaume aliyeibiwa bado hajapata fahamu na amelezwa katika hospitali ya misheni ya Mwea akiwa katika hali mahututi.

Kwa mujibu wa shahidi, mwanaume huyo aliingia kwenye baa moja maarufu mjini Ngurubani na akaagiza bia. Baada ya muda mchache wanawake hao wawili walifika kisha wakaomba wajumuike naye mezani.

Walipoendelea kunywa, mwanaume huyo alienda haja na hapo ndipo wanawake hao wakamtilia dawa katika kinywaji chake. Bila ufahamu wowote, alirejea kunywa kisha akapoteza fahamu na wanawake hao wakampora pesa, kadi yake ya ATM, kitambulisho na mali nyingine.

Mwanaume huyo aliokolewa na wasamaria wema ambao walimfikisha hospitalini baada ya kumpata hajijui hajitambui sakafuni.

“Hakuweza kuongea au kusimama. Nafikiri alikuwa amebururwa sakafuni baada ya kuibiwa,” akasema shahidi mwingine ambaye alikataa kufichua jina lake.

Polisi walipata vidokezo na kuvamia chumba moja ambako wanawake hao walikuwa wamejificha na kuwakamata na kupata baadhi ya dawa zinazodaiwa zilitumika.

Washukiwa wawili Thika wanaswa na lita 4,000 za pombe haramu

Na LAWRENCE ONGARO

WASHUKIWA wawili wamenaswa na maafisa wa upelezi wakitengeneza pombe katika jumba moja mjini Thika.

Hii ni baada ya wakazi wa kijiji cha Kisii mjini Thika kupiga ripoti kwa maafisa wa polisi ambao waliandamana na makachero ambao waliwatia nguvuni.

Wawili hao ilidaiwa wamepakana na shule moja ya msingi katika eneo hilo.

Maafisa hao waliovamia eneo hilo mnamo Jumatatu walinasa lita 4,000 za pombe ambayo ilikuwa imepakiwa kwa chupa na kuwekwa kwa katoni kadha.

Kamande wa polisi wa Thika Magharibi, Bi Beatrice Kiraguri, alisema washukiwa hao wamekuwa wakiendesha biashara hiyo kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa.

“Tumepata habari ya kwamba pombe hiyo hutengezwa usiku na kupakiwa kwa katoni ili isafirishwe hadi jijini Nairobi,” alisema Bi Kiraguri.

Naibu kamishna wa Thika Magharibi aliyeandamana na maafisa wakuu wa polisi, Bw Mbogo Mathioya, alisema ni hatia kubwa kwa mtu yeyote kuendesha biashara ya pombe karibu na eneo la shule.

“Wale ambao wanaendesha biashara hiyo wajue ya kwamba siku zao zimewadia,” alisema Bw Mathioya.

Alisema wawili hao watahojiwa zaidi kabla ya kufikishwa mahakamani kujibu mashtaka.

Hata hivyo washukiwa hao walijitetea vikali wakisema kuwa wao wanaendesha biashara halali na tayari wana leseni inayowaruhusu kuendesha biashara hiyo.

Lakini malalamishi yao yalikosa kutiliwa maanani na maafisa wa usalama.

Bw Mathioya alisema maafisa wa upelezi wataendelea na msako kuona ya kwamba watu hawaendeshi biashara haramu katika kaunti ndogo ya Thika.

Aliwapongeza wananchi kwa kuwa mstari wa mbele kuwatambua watu wanaotenda maovu miongoni mwao na baadaye kupiga ripoti kwa maafisa wa usalama.

Wakazi wafurahia corona kupunguza ulevi vijijini

NA KALUME KAZUNGU

WAKAZI wa mitaa ya Wiyoni na Mararani, kisiwani Lamu wamesifu kipindi cha janga la Covid-19 kwa kusaidia kupunguza fujo zilizokuwa zikishuhudiwa kutoka kwa walevi maeneo hayo.

Mara nyingi wakazi wa mitaa hiyo miwili walikuwa wakijitokeza kulalamikia makelele na fujo zilizokuwa zikichangiwa na kukithiri kwa mangwe kwenye mitaa yao, hali ambayo ilikuwa ikiwakosesha usingizi.

Wakazi waliambia Taifa Leo Jumatatu kwamba idadi ya walevi wanaozuru mangwe maeneo yao imepungua pakubwa ilhali baadhi ya mangwe zimefifia n ahata kufungwa.

Wakazi pia waliisifu serikali kupitia idara ya usalama kwa kuendeleza misako ya mara kwa mara ambayo imesaidia pakubwa kupunguza au kuzifunga mangwe kwenye mitaa mbalimbali ya Lamu.

Bi Halima Yusuf alisema siku za hivi karibuni wamekuwa wakilala bila kusumbuliwa na makelele au vita vya walevi kinyume na miaka iliyopita.

“Tunashukuru kwamba kipindi hiki cha Korona kimechangia baadhi ya mangwe kufungwa eneo hili. Kila mara tulikuwa tukiamsha au hata kukosa kulala kabisa kutokana na zahama za walevi ambao walikuwa wakiimba au kupigana,” akasema Bi Yusuf.

Karisa Charo ambaye ni mkazi wa Mararani alisema tangu Covid-19 ianze Machi mwaka jana, mtaa wao umegeuka kuwa mtulivu kwani walevi wengi hupendelea kunywa mchana pekee ilhali usiku wanakimbilia kwenye nyumba zao.

Aliiomba serikali kutoondoa kafyu, akisisitiza kuwa imegenyorosha tabia za wengi ambao usiku na mchana walikuwa wakibugia mtindi.

“Hapa Mararani ilikuwa ni kelele mchana kurwa na usiku kucha. Tunafurahia kafyu ya Covid-19. Imewatia woga walevi wengi. Wao hupendelea kunywa masaa machache na pia mchana pekee. Usiku mangwe zinafungwa mapema na watu kwenda kulala kinyume na awali ambapo makelele ya walevi yalikuwa yakiendelea usiku kucha hapa,” akasema Bw Charo.

Wakazi walisema sheria za Covid-19, ikiwemo kafyu pia imesaidia kuleta nidhamu miongoni mwa wanaume na vijana ambao hawakuwa wakiripoti nyumbani mapema.

“Mume wangu alikuwa akishinda na kukesha nje kula miraa na kunywa pombe. Nafurahi kwamba tangu Covid-19 kuanza, yeye amekuwa akifika nyumbani mapema n ahata kujukumikia masuala mengine ya kifamilia,” akasema Bi Sidi Kithi.

Walevi wakesha waumini wakilala

Na WAANDISHI WETU

WANANCHI wengi wanaopenda vileo walikiuka maagizo ya kukaa nyumbani usiku wa kuamkia jana Ijumaa, na badala yake wakaendelea kuburudika vilabuni hadi asubuhi kuukaribisha mwaka mpya.

Licha ya serikali kusisitiza kuwa sharti la kukaa nyumbani kuanzia saa nne usiku ili kuepusha maambukizi ya corona bado liko, uchunguzi wa Taifa Leo ulibainisha walevi wengi walipuuza hayo.

Kwa upande mwingine, makanisa yalitii agizo hilo na kufanya ibada zao za kuukaribisha mwaka mpya mapema kabla saa za kafyu na waumini wakarudi makwao.

Katika eneo la Nakuru Mashariki, Wateja katika kilabu cha Platinum 7D Lounge walikuwa miongoni mwa wanywaji pombe ambao waliendelea kuburudika hadi wakakaribisha mwaka mpya bila kujali kama wangekamatwa.

Kamanda wa polisi Ellena Kabukuru alisema maafisa wake walikamata magari matano na watu kadhaa waliokiuka kafyu mjini Nakuru mkesha wa mwaka mpya.

Katika Kaunti ya Murang’a, watu wengi walikuwa nje baada ya saa nne usiku licha ya polisi kushika doria.

“Leo naona kazi ni ngumu kiasi… Hata wenzetu wengine wamehepa kazi na wako kwa baa. Itabidi tufunge macho kiasi watu warukishe mwaka,” afisa mmoja aliambia Taifa Leo mjini Kiria-ini.

Hali ilikuwa sawa na hiyo katika miji ya Kangari, Thika, Kangema, Kenol, Sagana, Maragua, Kabati na Kamahuha ambapo watu walijifungia ndani ya baa kujificha, lakini wakapiga fujo za kukaribisha mwaka mpya ilipogonga saa sita usiku.

Mjini Elburgon, Kaunti ya Nakuru, Taifa Leo iligundua kwamba watu walikuwa wakitembea barabarani na wengine wakiwa ndani ya baa wakilewa.

Hali sawa na hii ilishuhudiwa katika Kaunti za Kwale na Taita Taveta ambako watu walikesha wakikwepa polisi kusherehekea mwaka mpya.

Baadhi ya wanaoishi karibu na mpaka walivuka hadi Tanzania kusherehekea hadi asubuhi.

Katika kaunti ya Kisumu, makanisa yaliandaa ibada kati ya saa kumi na saa mbili usiku ili kuruhusu waumini kufika nyumbani kabla ya saa za kafyu kuanza.

Kanisa katoliki mjini Kisumu liliagiza makanisa yake yote kumaliza ibada saa mbili usiku.

Mjini Eldoret Kaunti ya Uasin Gishu, waumini walianza kumiminika katika makanisa yao saa kumi na moja jioni kwa ibada ya kuvuka mwaka ili kuepuka kukamatwa kwa kukiuka maagizo ya kutotoka nje.

Mchungaji Job Simiyu wa Fountain of Wisdom Chapel Eldoret alitoa changamoto kwa Wakenya wote kusahau changamoto za 2020 na kukumbatia uaminifu ili kuruhusu uponyaji wa nchi yao.

Katika kaunti ya Mombasa Askofu Tom Arati wa Bible Way Ministries Bishop aliandaa ibada kupitia mtandao na kuwahimiza Wakenya wasiwe na woga mwaka huu.

Ripoti za Eric Matara, Mwangi Muiruri, John Njoroge, Rushdie Oudia, Titus Ominde, Anthony Kitimo Na Wachira Mwangi

Wamiliki wa baa wasema ‘wamesota’, hawana hela za kurejelea biashara

Na SAMMY WAWERU

Matamshi ya Rais Uhuru Kenyatta “sasa mnaweza kunywa pombe” yakiashiria kuruhusu ufunguzi wa mabaa, vilabu na maeneo ya burudani miezi sita baada ya kufungwa kama kati ya mikakati iliyotolewa kuzuia msambao wa Covid-19, yalikaribishwa na wengi hasa waraibu wa vileo.

Baada ya kiongozi wa nchi kutoa tangazo hilo mnamo Jumatatu, baadhi ya waraibu wa pombe walizua utani wakihoji, “Jumanne tutaamkia kuwa wageni wa mabaa”.

Huku kauli ya Rais Kenyatta ikiwa afueni kwa wamiliki wa mabaa na wapenzi wa pombe, baadhi yao wanasema hawana pesa kufufua biashara zao kutokana na athari za Homa ya virusi vya corona.

Margaret Wanjiku ni mmoja wa wafanyabiashara wa vileo Nairobi na ameiambia Taifa Leo kwamba baada ya amri ya mabaa, vileo na maeneo ya burudani kufungwa kutolewa, kipindi kilichofuata amekuwa akitumia fedha alizoweka kama akiba kukithi familia yake riziki.

Kulingana na Wanjiku, pia amekuwa akifanya vibarua vya hapa pale ili kukimu familia yake mahitaji muhimu ya kimsingi. “Ndio, tunafurahia tangazo la Rais mabaa yafunguliwe, ila kwa sasa hatuna pesa kuifufua,” akasema, akieleza kwamba chumba lilipokuwa baa lake alikuwa akikodi.

“Singeendelea kulipia kodi ilhali uuzaji wa pombe ulikuwa marufuku. Nililazimika kurejesha vifaa kwenye nyumba, nikisubiri uchumi ufunguliwe tena. Ukweli ni kwamba sina uwezo kufufua biashara yangu,” akasema mama huyo wa watoto wawili, akiomba serikali ipige jeki wafanyabiashara wa pombe.

Aidha, Rais Kenyatta amewataka wafanyabiashara wa vileo pindi watakapofungua mabaa na vilabu, watii sheria na mikakati iliyowekwa kuzuia kusambaa kwa corona.

“Kuanzisha biashara ya pombe iliyoafikia leseni na mahitaji yote si rahisi. Si ajabu mmiliki akitumia zaidi ya Sh500, 000 kuimarisha baa la kadri,” akadokeza mmiliki mwingine mtaa wa Githurai, ambaye alisema yuko katika harakati za kutafuta hela kurejea katika biashara ya pombe.

Kufuatia athari za corona kwa biashara na uchumi kuyumbishwa, kwenye uchunguzi wa Taifa Leo imedhihirika baadhi ya wamiliki wa mabaa na vilabu wamelazimika kukodi maeneo waliyotumia, kwa wenye uwezo kifedha kuwekeza katika biashara ya pombe.

Katika eneo la Mirema, mtaa wa Zimmerman, Nairobi, mmoja wa wamiliki wa vilabu ameweka notisi ya kukodisha kilabu chake na juhudi za kumfikia kwa njia ya simu kupitia nambari alizoweka hazikufua dafu, kwani ilikuwa imezimwa hadi wakati wa kuchapisha taarifa hii.

Kuna mabaa yaliyosalia kufungwa licha ya Rais kuyaruhusu kuhudumu. Aidha, mengine yamegeuzwa maduka ya bidhaa za kula.

Wenye maduka ya kuuza vileo vya kubebwa (take away), ndio wamekuwa wakihudumu chini ya kanuni walizowekewa na Wizara ya Afya.

Hofu pombe ikizidi kuua wakazi Kisii

Na Wycliffe Nyaberi

UTENGEZAJI pombe ya kienyeji umeongezeka katika maeneo kadhaa Kaunti ya Kisii, na kusababisha ongezeko la vifo na mauaji.

Walevi wengi wamegeukia maeneo yanayouza chang’aa baada ya serikali kufunga baa kote nchini katika juhudi za kuzuia msambao wa corona.

Ingawa serikali iliahidi kukabili pombe haramu, bado utengenezaji huo unazidi kukita mizizi na kuchangia vifo vya watu wanne katika maeneo ya kuuza chang’aa.

Mmoja kati ya wanne hao waliuawa ni afisa wa Nyumba Kumi aliyepigwa na bintiye mtengenezaji pombe baada ya mzee huyo kuandamana na chifu kwenye operesheni ya kuharibu pombe yao mwezi Juni mwaka huu katika kijiji cha Mashauri.

Mnamo Mei, mwalimu wa shule ya msingi aliuawa kufuatia sababu kama hizo katika kijiji cha Nyosia.

Mwalimu huyo alikwenda kujistarehesha kunakouzwa chang’aa lakini hakurejea.

Mauaji ya hivi punde yaliyowaghasi watu wengi yalitokea wiki moja tu iliyopita. Mwashi wa miaka 40 alichinjwa kijijini Kenyoro-Etangi, tarafa ya Kiogoro.

Ilisemekana mwashi huyo, Edward Omwamba aliuliwa na mmiliki mmoja mwenye kuuza chang’aa baada ya kuzozana kuhusu deni walilokuwa wakidaiana.

Siku chache tu kabla ya uhamisho wake kwenda Uasin- Gishu, aliyekuwa kamishina wa kaunti ya Kisii Stephen Kihara aliitaja tarafa ya Kiogoro kama mojawapo ya sehemu zenye ngome kuu za utengenezaji wa pombe haramu ambazo zafaa kuangaziwa.

Ni katika mazishi ya Edward Omwamba hiyo jana ambapo viongozi mbali mbali walichukua fursa ya kukemea watengenezaji wa pombe haramu na kumwomba kamishina mpywa Bw Abdirizak Jaldesa kulivalia njuga swala hilo.

Wakiwa na matumaini ya mwakilishi huyo mpya,waombolezaji mmoja baada ya mwingine, hasa kina mama walimwomba Bw Jaldesa kuwaokoa waume na watoto wao kutoka kwa minyororo ya chang’aa ili wawe na kizazi siku zijazo.

“Tafadhali sikieni kilio chetu na nyinyi serikali mkomeshe pombe haramu kwani wanetu wanapotea.Tusipoziba ufa tutakuja kujenga ukuta,” akasema Bi Jane Nyangenya, mmoja wa waliohutubu.

Mwenyekiti wa Nyumba Kumi Kisii Bw Stephen Onsare alidokeza kuwa iwapo pombe hiyo haitakomeshwa, basi jamii itajitokeza na kuwafurusha watengenezaji hao.

“Tumevumilia vya kutosha. Ni wakati sasa kuiga jinsi watu wengine wamefanya ili kukomesha jambo hili ambalo limekuwa sasa dondasugu. Tutahamasisha watu na kwa sauti moja, tutawafurusha wote wanaotengeneza na kuuza pombe haramu iwapo hawatatusikiza,” akasema mwenyekiti.

Zaidi, wenyeji waliomba haki itendeke kwa wote ambao wamepoteza maisha yao kwa kuuliwa kwenye maeneo ya pombe hiyo.

Ajitetea watoto wataumia asipouza pombe

Na Richard Munguti

Mama mwenye umri wa miaka 35 alilia kortini akisema shida za watoto wake kukosa chakula zilimsukuma akaidi agizo la Rais Uhuru Kenyatta walevi wasiuziwe pombe.

“Mimi sina mume. Kazi yangu ya kuuza pombe katika kilabu cha Black Oakwood ndiyo nategemea kupata pesa za kujikimu kimaisha na kuwalisha watoto wangu,” Esther alimweleza hakimu mkuu mahakama ya Kibera Abdulkadir Lorot akijitetea.

Esther alikiri shtaka la kupatikana akiuza pombe kinyume cha agizo la Rais Kenyatta kwamba vilabu visiuze pombe kabisa hadi ugonjwa wa Corona utokomee.

Aliomba msamaha akisema ni shida iliyomsukuma kuvunja sheria.

Alipatikana na polisi ametoa sanduku la pombe aina ya Pilsner akiwauzia wateja.

Hakimu alimtoza faini ya Sh20000 ama atumikie kifungo cha mwezi mmoja gerezani.

Akiondoka mbele ya hakimu Esther alilia huku akiuliza “kile watoto wake watakula.”

Katika mahakama hiyo hiyo Mary Njoki alitozwa faini ya Sh50000 ama atumikie kifungo cha miezi mitatu kwa kuuza pombe kinyume cha sheria na agizo la Rais Kenyatta kwamba vilabu visiuze pombe.

Mary Njoki alitupwa miezi mitatu jela kwa kuuza pombe kinyume cha sheria.. Picha/ Richard Munguti

Akijitetea alisema..”Mimi ni single mother na sina kazi ingine ni hii tu ya kilabu.”.

Akamweleza hakimu…”Watoto walinililia usiku kucha nikaamua kufungua baa niuze angalau ni pate chakula ya siku moja tu.lakini nikaangukia mikono ya sheria.Nisamehe..”

Hakimu alimweleza, “Hata mimi namwogopa Rais na kutii amri kwa hivyo utatumikia kifungo cha miezi mitatu ukikosa faini ya Sh50000.”

Bw Lorot aliamuru pombe aliyokutwa nayo ipelekwe Kemri kutengeneza sanitaiza.

Wazazi wanadhuru watoto kwa kunywa pombe nyumbani

Na LEONARD ONYANGO

loonyango@ke.nationmedia.com

KUFUNGWA kwa baa na maeneo ya burudani kumewaweka wazazi wanaopenda kubugia mvinyo kwenye kona mbaya.

Tofauti na hapo awali, ambapo siku za wikendi wazazi walikwepa watoto na kwenda kunywa pombe kwenye baa huku wakitazama mechi za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) iliyo na ushabiki mkubwa humu nchini, sasa hawana pa kujificha.

Wazazi hao sasa wamelazimika kutumia mbinu mbalimbali kuhakikisha kuwa wanaendelea kukata  kiu cha pombe.

Bw George Otieno ambaye ni mkazi wa mtaa wa Dandora jijini Nairobi anasema kuwa amelazimika kugeuza gari lake kuwa ‘baa’.

Anasema siku za wikendi ambazo haendi kazini, huwa ndani ya gari lake akinywa pombe.

“Sitaki watoto wangu wajue kwamba mimi hutumia mvinyo. Mimi hunywa pombe ya kadri tu na watoto wangu huwa hawana habari kwamba baba yao ni anatumia pombe, hawajawahi niona  nikinywa,” anasema Bw Otieno ambaye ni baba ya watoto watatu.

“Ukiwaeleza kwamba baba yao ni mlevi watakushangaa sana,” anaongezea.

Naye Eric Mbugua ambaye ni mkazi wa Kahawa West, Nairobi, anasema kuwa pombe anayonunua amehifadhi kwenye chumba chake cha kulala.

“Nina watoto wawili; mmoja ana umri wa miaka 10 na mwingine miaka 13. Watoto wangu hawana mazoea ya kuingia kwenye chumba cha kulala cha wazazi wao. Nimewafunza hivyo tangu walipokuwa  wachanga. Hivyo pombe yangu chumbani iko salama.

“Siku za wikendi, mimi hujifungia chumbani kwangu na kunywa pombe huku watoto wakijisomea au kutazama runinga sebuleni na mama yao ambaye hatumii mvinyo,” anasema.

Vileo vinavyotumiwa na watoto:

Pombe- asilimia 23

Miraa- asilimia 17

Tumbako- asilimia 15

Bangi- asilimia 8

Heroini- asilimia 1

Kokeni – asilimia 1

Katika eneo la Huruma jijini Nairobi, Willy Makokha anasema kuwa yeye na mkewe wamekuwa wakibugia pombe tu mbele ya watoto wao wawili.

“Tunaishi kwenye chumba kimoja. Chumba hicho ndicho sebule na sehemu ya kulala. Unajua nyumba hizi za mjini, haswa vitongoji duni, hazina maeneo ya kupumzika nje. Makarao (maafisa wa polisi) wakikupata unakunywa pombe nje wanakushika.

“Kuepuka balaaa ya kukamatwa, nanunua pombe yangu dukani na ninakunywa hapa chumbani kwangu,”anasema Bw Makokha anafanya kazi ya useremala mtaani Huruma.

Kulingana na Makokha, watoto hawawezi kuiga wazazi wao kunywa pombe.

“Mimi wazazi wangu hawakuwa wanakunywa pombe, lakini mimi ninakunywa. Hivyo watoto wangu watafanya uamuzi wao wenyewe wakiwa wakubwa. Kwa sasa nawahimiza kutia bidii katika masomo yao ili wajisaidie katika siku za usoni,” anasema.

Rais Uhuru Kenyatta mwezi uliopita alipiga marufuku kuuzwa kwa pombe katika baa, mikahawa na maeneo ya burudani. Rais Kenyatta pia alifunga baa kwa muda usiojulikana.

Rais Kenyatta alisema kuwa watu watumiaji wa pombe wanaweza kununua mvinyo madukani na kwenda kunywea nyumbani.

Wito huo wa Rais Kenyatta, unapingwa vikali na Mamlaka ya Kupambana na  Matumizi ya Dawa za Kulevya nchini (Nacada).

Watoto hutumia vileo wakati upi?

Likizo – asilimia 49

Njiani kutoka shuleni kwenda nyumbani – asilimia 36

Wikendi – asilimia 30

Ziara za wanafunzi = asilimia 27

 

Mamlaka ya Nacada linaonya kuwa hatua ya wazazi kunywea pombe nyumbani itasababisha watoto kujiingiza katika ulevi.

 Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa  Nacada Mabel Imbuga  pia anasema kuwa tangu kufungwa kwa baa pombe imekuwa ikiuzwa kupitia mitandaoni hivyo  watoto wa chini ya umri wa miaka 18 wanaweza kuipata bila kizuizi.

“Baadhi ya wanafunzi wanatumia mitandao kusoma hivyo wanaweza kutumia fursa hiyo kununua pombe bila wazazi wao kujua,”anasema.

“Kunywa pombe nyumbani kuna wanyima watoto mazingira bora na salama ya kusomea na kuishi wakati huu wa janga la virusi vya corona. Tunawashauri wazazi kutumia wakati huu kujiepusha na pombe na badala yake wajenge uhusiano wa karibu na watoto wao. Wazazi ndio wametwikwa jukumu la kuwalinda watoto wao hivyo ni sharti wawalinde dhidi ya mazingira yenye pombe,”anasema Prof Imbuga.

Wataalamu wa masuala ya kisaikolojia wanaonya  kuwa kunywa pombe nyumbani mbele ya watoto kuna madhara tele.

Bi Dorcas Okinyi ambaye ni mtaalamu wa masuala ya afya ya akili na mwasisi wa shirika la Healthy Minds Africa, anasema kuwa watoto huanza kutambua harufu ya pombe wakiwa na umri wa kati ya miaka mitatu na mitano.

“Watoto huanza maisha yao kwa kutangamana na watu katika familia zao. Watoto hujifunza na kuiga tabia fulani kwa kuangalia au kusoma watu wanaotangamana nao na  huchukulia wazazi wao kama kielelezo.

“Idadi kubwa ya watoto wanaoona wazazi wao wakinywa pombe wao pia huishia kuwa walevi baadaye na kupitisha tabia hiyo kwa kizazi kingine,” anasema.

Watoto hupata  wapi  vileo?

Marafiki – asilimia 32

Nyumbani- asilimia 29

Vibanda vilivyo karibu na shule – asilimia 25

Jamaa zao- asilimia 17

Wazazi – asilimia 8

 Bi Okinyi anasema kuwa hali huwa mbaya zaidi kwa watoto wazazi au walezi wao wanapolewa chakari na kuzua vurugu nyumbani.

“Wazazi wanapokunywa pombe na kuzua vurugu, watoto huathirika sana kiakili. Hiyo ndiyo maana watoto wa wazazi walevi huwa na matatizo ya kutangamana na wenzao shuleni au wanapocheza mitaani; wengi wao huepndelea kupigana.

“Mzazi anapolewa ndani ya nyumba na kuzua vurugu au kusumbua majirani, pia husababisha kuwa na tabia ya kuepuka wenzao kutokana na aibu. Hali hii humfanya mtoto kuwa na matatizo ya kiakili,” anasema.

Vilevile, Bi Okinyi anasema kuwa watoto wanaaishi kwa hofu iwapo mzazi au mlezi huwadhuru kwa kuwapiga baada ya kulewa.

“Watoto hujawa na hofu wanapokuwa nyumbani kwani hawajui watafanyiwa nini na mzazi au mlezi wao baada ya kulewa,” anasema.

“Hali hiyo huwafanya kuchukia mzazi au mlezi wao ambaye ni mlevi na hatimaye kukumbwa na msongo wa mawazo ambao unaweza kuwasukuma wao pia kujiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya,”anaongezea.

Je, nini hutokea ikiwa wazazi wanakunywa pombe  nyumbani kwa ustaarabu bila kuzua vurugu au kudhuru watoto wao?

Bi Okinyi anasema kuwa hata kunywa pombe kwa ustaarabu mbele ya watoto hakufai.

“Kuna baadhi ya wazazi ambao wanakunywa pombe kiungwana lakini wanaonya watoto wao wasithubutu kuweka mvinyo mdomoni.

“Hili husababisha watoto kuwa na shauku ya kutaka kuonja pombe ili washuhudie ‘utamu’ ambao wazazi wao hupata kwenye pombe. Kuonja huku husababisha watoto kuwa walevi chakari katika siku za usoni,” anasema Bi Okinyi.

“Wazazi hawafai kuwataka watoto wao kunywa maji na wao wanakunywa pombe. Wazazi wanafaa kuwa kielelezo bora kwa watoto wao,”anaongezea.

Watoto wanaotumia mihadarati wanaishi na nani?

Mama na baba- asilimia 70

Mama pekee – asilimia 17

Baba pekee – asilimia 3

Nyanya/babu- asilimia 2

 

Anasema kuwa watoto huiga zaidi mambo wanayoona kwa wazazi au walezi wao kuliko wanayosikia.

Bi Okinyi anashauri kuwa wazazi wanaokunywa pombe nyumbani wanafaa kuwaelimisha watoto wao kuhusu madhara ya kubugia mvinyo.

“Mzazi anaweza kumshauri mtoto kuhusu madhara ya kunywa pombe huku akitoa mfano wake kuhusu mambo yaliyomsukuma kufanya hivyo na changamoto anazopitia,” anasema.

“Mzazi anayetumia pombe anafaa kuzungumza na watoto kwa uwazi kuhusu madhara ya pombe badala ya kuwapa onyo kali na  kuwatishia kuwaadhibu iwapo watathubutu kunywa vileo. Watoto wanahitaji kuelezwa ni kwanini wanafaa kujiepusha na pombe  kabla ya kukamilisha masomo yao ya shule ya msingi na sekondari.”

Anawashauri wazazi walio na mazoea ya kulewa chakari mbele ya watoto kutafuta huduma za ushauri nasaha kutoka kwa wataalamu.

Prof Imbuga anasema kuwa wazazi walio na matatizo ya kulewa chakari wanaweza kuwasiliana na Nacada ili wapewe ushauri kuhusu namna ya kupata matibabu.

 Wataalamu wanaamini kuwa unywaji wa pombe nyumbani umechangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la visa vya dhuluma dhidi ya watoto wakati huu wa janga la virusi vya corona.

Adhabu ya kumweka mtoto kwenye mazingira yanayomweka kwenye hatari ya kutumia vileo

Miezi 12 gerezani

Faini ya Sh50,000

Rais  Uhuru Kenyatta mwezi  uliopita aliagiza kufanywa kwa uchunguzi ili kunasa watu anaohusika na dhuluma dhidi ya watoto na wanawake.

Agizo hilo lilifuatia baada ya  wizara ya masuala ya Jinsia kufichua kuwa visa vya ubakaji wa wanawake, unajisi wa wasichana na mizozo ya nyumbani imeongezeka mara 10 kati ya Aprili na Julai ikilinganishwa na Februari mwaka huu.

Ripoti zinaonyesha kuwa  visa vingi vya ubakaji na unajisi vinatekelezwa na jamaa za waathiriwa.

Utafiti uliofanywa na Nacada  miongoni mwa shule za msingi mnamo 2016, ulifichua kuwa wazazi wanachangia pakubwa katika kuwaingiza watoto wao katika utumiaji wa vileo.

Utafiti huo ulifichua kuwa pombe ndiyo hutumiwa kwa wingi miongoni mwa watoto walio chini ya umri wa miaka 17 ikilinganishwa na aina nyinginezo za vileo.

Kwa mujibu wa ripoti, pombe hutumiwa kwa asilimia 23, miraa (17), tumbako (15), bangi  (8), heroini (1), kokeni (1) kati ya aina nyinginezo za vileo..

Asilimia 48.5 ya watoto hutumia mihadarati wakati wa likizo na wengine asilimia 35.1 wanatumia njiani wanapotoka shuleni kuelekea nyumbani. Ripoti pia ilibaini kuwa asilimia 30 ya watoto hutumia vileo siku za wikendi, asilimia 27 hunywa pombe na vileo vingine wakati wa ziara za wanafunzi.

“Wanafunzi hao walipoulizwa mahali ambapo hutoa vileo hivyo, asilimia 32 walisema kuwa huwa wanapewa na rafiki zao. Jambo la kushangaza ni kwamba asilimia 29 walisema kuwa hutoa nyumbani,” ikasema ripoti hiyo.

Asilimia 25 walisema kuwa hununua vileo hivyo katika vibanda vilivyo karibu na shule, asilimia 17 walisema hupewa na jamaa zao na asilimia 8 walikiri kuwa walipata kutoka kwa wazazi wao.

Kutia msumari moto kwenye kidonda, asilimia tano ya wanafunzi waliohojiwa na Nacada walisema kuwa hupata mihadarati hiyo kutoka kwa walimu huku wengine asilimia nne wakisema hununua katika maduka yaliyo ndani ya shule.

Jambo la kushtua zaidi ni kwamba karibu asilimia 70 ya wanafunzi waliokiri kutumia mihadarati wanaishi na wazazi wao wote wawili. Asilimia 17 wanaishi na mama tu huku wengine  asilimia 3 wakiishi na baba pekee.

Katika mapendekezo yake, Nacada iliwataka wazazi kuepuka kunywa pombe mbele ya watoto wao.

“Wazazi pia wanafaa kusindikiza watoto wao hadi shuleni ili kuwazuia kushawishiwa na wenzao kutumia mihadarati wanapokuwa njiani kuelekea shuleni,” inapendekeza ripoti ya Nacada.

Ripoti pia inashauri wazazi kuwa na midahalo na watoto wao  kuhusu suala la mihadarati.

Sheria ya Watoto ya 2010 iliyofanyiwa marekebisho 2012, inasema kuwa kila mtoto ana haki ya kulindwa dhidi ya dawa za kulevya kama vile tumbaku, mihadarati, pombe. Sheria hiyo pia inapiga marufuku watoto kutumiwa kuzalisha au kusafirisha vileo.

Wazazi au mtu yeyote anayepatikana na hatia ya kuwaweka watoto katika mazingira ya vileo anakuwa katika hatari ya kufungwa kipindi kisichozidi miezi 12 gerezani au kutozwa faini isiyozidi Sh50,000.

Pigo kwa walevi sheria mpya ikipitishwa

Na VALENTINE OBARA

WALEVI na wafanyabiashara za vileo watapata pigo iwapo serikali itatekeleza pendekezo la kupiga marufuku unywaji wa pombe katika mikahawa.

Sheria mpya iliyopendekezwa na Wizara ya Afya, inataka mtu yeyote anayefanya biashara ya kuuza pombe, iwe ni katika mikahawa au madukani, ahakikishe wanunuzi hawanywi mahali hapo.

Ni sheria ambayo imelenga kupunguza ueneaji wa virusi vya corona, hasa baada ya kubainika kuwa kuna wafanyabiashara wa mikahawa ambao walitumia vibaya nafasi waliyopewa kuuza vyakula.

Kanuni zilizopo kwa sasa zinaruhusu watu kunywa pombe katika mikahawa wakati wanapokula, lakini imebainika hili lilitoa mwanya kwa watu kulewa bila kufuata masharti ya kujikinga kutokana na Covid-19.

Mkuu wa Afya ya Umma, Dkt Francis Kuria, alithibitisha wizara ilibuni pendekezo hilo jipya ambalo sasa linasubiri kuidhinishwa na Mwanasheria Mkuu.

‘Sheria hiyo inalenga kutatua changamoto zinazohusu unywaji wa pombe. Itakapopitishwa ndipo tutaweza kuijadili kwa mapana zaidi,’ akasema Dkt Kuria.

Katika mapendekezo hayo, mtu yeyote atakayekiuka sheria hizo atatozwa faini isiyozidi Sh20,000 au atumikie kifungo kwa miezi sita.

Alisema hayo katika kikao cha wanahabari kuhusu hali ya virusi vya corona nchini.Waziri Msaidizi wa Afya, Dkt Rashid Aman, alitangaza kuwa idadi ya maambukizi iliongezeka kwa 397 na kupelekea idadi jumla kuwa 14,168.

Wagonjwa 642 walipona, na hivyo kufikisha jumla ya waliopona hadi 6,258. Hata hivyo, wengine 12 walifariki na kufikisha idadi yao hadi 250.

Mikahawa sasa inauza pombe – Serikali

Na SAMMY WAWERU

Serikali Jumatatu imefichua kuwa wamiliki wa mikahawa sasa wamebadilisha biashara  na kuanza kuuza mvinyo bila leseni.

Waziri Msaidizi katika Wizara ya Afya Dkt Rashid Aman ametoa onyo kali kwa wanaoendesha biashara hiyo, akisema uchunguzi umeanzishwa na wahusika wataadhibiwa kisheria.

“Tumefikiwa na taarifa kuna mabaa yanayohudumu, isitoshe wakati wa utekelezaji saa za kafyu. Baadhi yao ni mikahawa inayotumia leseni ya mkahawa kuendesha biashara ya uuzaji wa pombe. Ifahamike wazi mabaa na vituo vya burudani yangali yamefungwa,” akasema.

“Inashangaza kuona maeneo ya kula yakigeuzwa kuwa mabaa. Uchunguzi unaendeshwa na wahusika watachukuliwa hatua kisheria,” alisema.

Kauli ya Dkt Aman imejiri siku moja baada ya seneta wa Nairobi Johnson Sakaja kukamatwa na maafisa wa polisi japo aliachiliwa, baada ya kupatikana akibugia pombe na watu kadhaa katika baa moja jijini Niarobi.

Kukamatwa kwa Sakaja kulifichuka kupitia video iliyosambaa mitandaoni, akionekana kufungiwa katika kituo cha polisi cha Kilimani, Nairobi baada ya kutiwa nguvuni.

Hata ingawa alikuwa amekanusha madai hayo, Jumatatu aliyakubali huku akiomba Wakenya msamaha kwa kukiuka sheria zilizowekwa kusaidia kudhibiti msambao wa Covid-19 kama kiongozi.

“Ni jambo la kusikitisha visa vinapozidi kuongezeka nayo mabaa yanaendelea kufunguliwa. Mengi ni mikahawa, na yatafungwa kwa kukiuka sheria,” akaonya Dkt Francis Kuria kutoka Wizara ya Afya na anayeshughulikia kufuata waliotangamana na waliothibitishwa kuambukizwa virusi vya corona.

Jumatatu, watu wanne walithibitishwa kufariki kutokana na Covid-19 katika kipindi cha saa 24 zilizopita.

Idadi hiyo imefikisha jumla ya watu 238 walioangamizwa na Covid-19 nchini, ugonjwa unaosababishwa na virusi vya corona.

Kati ya wanne hao, mwathiriwa wa umri mkubwa amekuwa na miaka 72 na ambaye Wizara ya Afya imesema aliugua maradhi ya Moyo, Kisukari na Figo. Wengine ni wenye umri wa miaka 51, 39 na 30.

Wizara ya Afya pia imethibitisha maambukizi mapya 418 kutoka kwa sampuli 2,474 zilizofanyiwa ukaguzi na vipimo katika kipindi cha saa 24 zilizopita.

Kufikia sasa, Kenya imefikisha jumla ya sampuli 246,361 zilizofanyiwa vipimo, na jumla ya visa 13,771 vya corona.

Kati ya maambukizi mapya ya Jumatatu, 408 ni Wakenya na 10 wakiwa raia wa kigeni, umri wa mgonjwa mdogo ukiwa mwaka mmoja na ule mkubwa miaka 86.

“Idadi ya wanaume imekuwa 263, na wanawake 155, mkondo wa wanaume kuwa waathiriwa wakuu unaendelea kushuhudiwa,” akasema Dkt  Aman.

Akipigia upatu jitihada za wahudumu wa afya, Dkt Aman alisema wagonjwa 494 wamethibitishwa kupona, 465 kati yao wakiwa wanaopokea matunzo na matibabu nyumbani huku 29 kutoka vituo mbalimbali vya afya.

Takwimu hiyo inafikisha jumla ya 5,616 waliothibitishwa kupona kabisa nchini virusi vya cona.

“Ninahimiza Wakenya kwa kuwa zuio la kusafiri liliondolewa pamoja na maeneo ya kuabudu kufunguliwa, wawajibike. Huu ndio wakati wa kulinda maisha ya ndugu na dada yako, linda maisha yangu nami nilinde yako,” Waziri Aman akasisitiza, wakati akitoa takwimu hizo katika makao makuu ya idara ya afya Nairobi.

Matatizo ya akili yazidi kutokana na sheria kali za coronavirus

Na WAANDISHI WETU

WATAALAMU wa afya ya akili wameitaka serikali kuweka mipango ya kupunguzia Wakenya msongo wa mawazo, inapopambana na virusi vya corona.

Hii ni kutokana na ongezeko la visa vya watu kujitoa uhai wakilalamikia hali ngumu ya maisha, kuongezeka kwa mizozo ya kinyumbani na wengi kulewa chakari nyumbani wakijaribu kujiondolea mawazo.

Mtaalamu wa saikolojia Prof Halimu Shauri, ameonya kwamba matukio aina hii yataendelea kushuhudiwa kama serikali haitajali kuhusu afya ya kiakili ya wananchi ikiwemo wanaowekwa karantini.

Alisema masharti makali kama yanayohitaji watu kutokongamana wala kukaribiana, kujifungua nyumbani, pamoja na hali ngumu za maisha ni sababu tosha za kufanya binadamu kutatizika kiakili, ingawa ni masharti muhimu kupambana na ueneaji wa virusi vya corona.

“Tumeathirika kihisia, kiuchumi na unapoambiwa ukae karantini, mara msikaribiane…unakosa ule usaidizi uliozoea kutoka kwa wengine. Hatuna marafiki wa kuzungumza nao tena,” akaeleza Prof Shauri.

Aliongeza kuwa watu wanapoachwa pweke huwa wanawaza sana kuhusu matatizo yanayowakumba kimaisha na kuchukua hatua zinazowadhuru.

Anusurika kifo

Mnamo Jumamosi mchana, mwanamume mwenye umri wa makamu alinusurika kifo katika Kaunti ya Nakuru baada ya kujirusha kutoka kwenye daraja la wapita njia katika barabara kuu ya Nakuru kuelekea Nairobi.

Marafiki wake walisema jamaa huyo alikuwa ni mhudumu wa hoteli mjini Nakuru na alishikwa na msongo wa mawazo aliposimamishwa kazi wakati biashara zilipoathirika na masharti ya kupambana na Covid-19.

Kisa hiki kilijiri siku chache baada ya kingine katika kijiji cha Wuoth Ogik, Kaunti ya Migori, ambapo mwanamke alimrusha mtoto wake mtoni kisha akajaribu kujitoa uhai.

Kulingana na walioshuhudia, mwanamke huyo alikuwa amelalamikia hali ngumu ya kiuchumi kutokana na janga la corona.

Katika Kaunti ya Nyandarua, mwanamume aliacha watu midomo wazi alipovaa gunia na kuandamana na binti yake mdogo hadi katika Hospitali ya JM Memorial akitaka mkewe atolewe hospitalini.

Alidai maadui wa kibiashara wa mkewe waliwadanganya polisi kuwa alisafiri Tanzania majuzi ndipo akawekwa karantini.

 

Ripoti za Samuel Baya, Waikwa Maina, Valentine Obara na Ian Byron

Watu 20 wafariki kwa kunywa pombe kuzuia kuambukizwa corona

Na MASHIRIKA

WATU 20 wamefariki nchini Iran baada ya kunywa pombe yenye sumu kwa imani kuwa inaweza kuzuia kuambukizwa virusi vya corona.

“Baadhi ya wajinga wanafikiri unywaji pombe unazuia kuambukizwa virusi vya corona. Kutokana na imani hiyo watu 331 walikunywa pombe yenye sumu na 20 miongoni mwao wakafariki,” akasema msemaji mkuu wa wizara ya afya nchini Iran.

Wataalamu wa afya walisema ni imani potovu kuwa pombe ina kinga dhidi ya virusi vya corona. Wanashauri kuwa inaweza kutumika kuua viini kwa kunawa nayo mikono ama kuosha sakafu.

Hayo yalitokea Rais Marcelo Rebelo de Sousa wa Ureno akifungiwa nyumbani kwake kwa siku 14 kwa hofu huenda ameambukizwa virusi vya corona.

Hii imetokea wakati watu zaidi ya 110,000 walithibitishwa kuugua homa hiyo kote duniani kufikia jana, huku 3,882 kati yao wakifariki.

Mataifa yaliyoathiriwa zaidi ni China, Korea Kusini, Italia, Iran, Ufaransa na Ujerumani.

Kulingana na ofisi ya rais nchini Ureno, mnamo Jumamosi Rais Sousa alitangamana na wanafunzi na hata kupigwa picha nao, na baadaye mmoja wao akagunduliwa anaugua homa iliyozuka China mwishoni mwa mwaka jana.

Kufikia Jumapili kulikuwa na visa 30 vya homa hiyo nchini Ureno.

Nchini Marekani, Seneta Ted Cruz wa Texas pia amejifungia nyumbani kwake baada ya kufahamu alitangamana na kusalimiana kwa mkono na mtu ambaye alithibitishwa kuugua homa hiyo baadaye.

“Kama tahadhari nimeamua kujitenga nyumbani kwangu,” alisema Seneta Cruz mnamo Jumapili.

Homa hiyo pia ilimlazimu Papa Francis wa Kanisa Katoliki kukosa kufanya mahubiri ya Jumapili hadharani na badala yake akayapeperusha kupitia intaneti.

Ofisi ya Papa Francis ilisema hatua hiyo ililenga kuzuia watu kukusanyika katika ukumbi wa St. Peter’s Square kwa ibada ya Jumapili kama ilivyo kawaida, katika tahadhari dhidi ya virusi vya corona.

Haya yamejiri Italia ikitangaza marufuku ya kutoka ama kuingia mikoa miwili yenye visa vingi vya virusi vya corona.

Marufuku hiyo imeathiri watu milioni 16 katika maeneo ya kaskazini mwa nchi hiyo.

Kufikia jana Italia ilikuwa imethibitisha visa zaidi ya 7,000 vya maambukizi na vifo zaidi ya 350.

Waziri Mkuu wa Italia Giuseppe Conte aliweka sahihi marufuku hiyo Jumapili ambayo yataathiri maeneo ya Lombardy na Veneto ambako miji ya Milan na Venice inapatikana mtawalia.

Yeyote atakayekiuka marufuku hiyo anaweza kufungwa gerezani kwa miezi mitatu.

Shughuli za kawaida ambazo zimepigwa marufuku ni harusi, mazishi, mikahawa na shughuli zingine zinazokutanisha halaiki ya watu.

Kulingana na marufuku hiyo, mabaa yataendelea na shughuli lakini watu watatakiwa kukaa umbali wa futi tatu kutoka kwa mtu mwingine.

Wafungwa katika magereza manne waligoma kulalamikia marufuku hiyo hasa kuhusu kutembelewa na jamaa.

zao.

Ligi Kuu ya soka nchini Italia (Serie A) pia imetatizika baada ya serikali kuagiza mechi kuchezwa bila mashabiki.

Mnamo Jumapili mechi kati ya miamba wa Italia, Juventus na Inter Milan pamoja na nyingine kati ya AC Milan na Genoa zilichezwa bila mashabiki.

Mechi ya Ligi ya UEFA kati ya PSG ya Ufaransa na Borussia Dortmund ya Ujerumani nayo itachezwa kesho usiku bila mashabiki.

Wakati huo huo, maafisa wa afya nchini Zanzibar wamepiga marufuku watalii kutoka Italia kuzuru kisiwa hicho.

Waziri wa Afya Hamad Rashid alisema hatua hiyo inalenga kuzuia virusi hivyo kuingia nchini humo.

Tunahangaishwa kwa kupiga vita pombe haramu – Nyumba Kumi

Na Phyllis Musasia

VIONGOZI wa Nyumba Kumi eneo la Kuresoi Kusini, wametishia kususia majukumu yao kwa madai ya kunyanyaswa na polisi.

Kupitia Michael Onyino wa Keringet mjini, walisema wamekuwa wakiteswa na hata kutishiwa maisha na polisi kila wanapotilia mkazo visa vya wakazi kujihusisha na biashara ya pombe haramu.

Wengi wao walidai kupigwa mbele ya washtakiwa na kutishiwa kukamatwa haswa wanapoonekana wakifuatilia na kusisitiza kuhusu baadhi ya kesi za jinai kwenye maeneo yao.

“Eneo hili limegeuka kuwa sehemu ambapo majangili wanaweza kutekeleza uhalifu wa aina yoyote ile na kisha waendelee kuishi maisha yao kama kawaida. Polisi wameonyesha kutoshughulika na yeyote hata unapowapa habari,” akasema Bw Onyino.

Aidha, baadhi ya wanafunzi wa shule za msingi wanatumika vibaya na majambazi kwa kununuliwa pombe na kisha kutumwa kuvunja nyumba za wakazi.

 

Kwenye kisa cha hivi maajuzi, Bw Onyino alidai kuwa kiongozi mmoja aliwakamata baadhi ya wanafunzi waliokuwa walevi na alipowapeleka katika kituo cha polisi cha Keringet, maafisa wa polisi waliokuwa kwenye zamu walimfukuza pamoja na wanafunzi hao na kudai kwamba kituo hicho hakina seli ya watoto.

“Alielezwa kuwa aondoke mara moja la sivyo akamatwe na kuwekwa ndani ya seli,” akaeleza Bw Onyino.

Kiongozi mwingine Bw Reuben Cheruiyot alisema mji wote wa Keringet uko gizani baada ya taa za usalama kuvunjwa na kuharibiwa na wezi usiku.

“Polisi wana habari hizi na hata machifu lakini muda umeyoyoma tangu kufanyika kwa kisa hiki bila yeyote kumatwa,” akasema.

Viongozi hao walisema wamedhalilishwa na kuonekana kama watu ambao hawafai kabisa katika jamii.

“Kazi yetu inatambulika na serikali lakini tunaifanya kama kazi ya kujitolea. Hakuna mshahara tunayopata lakini unapata kwamba tunadharauliwa kiasi cha haja,” akasema Bw Cheruiyot.

Walimkashifu naibu kamishna wa eneo hilo Patrick Mwangi kwa kukosa kuwahusisha katika mikutano ya maswala ya usalama.

Hata hivyo, Bw Mwangi alisema katika mahojiano kwamba hana habari kuwa viongozi wa Nyumba Kumi wanateswa na polisi. Aliwataka waandikishe malalamishi hayo katika ofisi yake.

Alisema anaheshimu viongozi wote wakubwa kwa wadogo kwa kazi wanayoifanya.

“Nimeandaa mkutano na machifu wa hapa utakaofanyika Jumanne wiki ijayo ili tujadiliane maswala haya. Kila kiongozi atahusishwa katika mipango wetu wa Keringet na hakuna atakayewachwa nje,” akasema.

Aliongeza kwamba yeye ni mgeni eneo hilo lakini ana matumaini kwamba malalamishi yote yatatatuliwa.

Aidha, kamanda wa polisi kaunti ya Nakuru Stephen Matu alisema hajapokea malalamishi hayo lakini yuko tayari kufuatilia na maafisa wa polisi wa eneo la Keringet ili kupata suluhu.

“Sina habari zozote kuhusu malalamishi haya lakini nitamtafuta naibu kamanda wa eneo bunge la Kuresoi Kusini kujua ni nini haswa kinachoendelea,” akasema Bw Matu.

Moi alichukia ulevi, asema mjukuu wake

Na FRANCIS MUREITHI

MJUKUU wa Rais mstaafu Daniel arap Moi, amefichua kuwa babu yake alichukia pombe na hakutaka walevi wajumuike naye kamwe.

“Babu yetu (Mzee Moi) hakufurahia kumwona yeyote akiwa mlevi. Hakuna mtu yeyote wa familia yetu angethubutu kuingia nyumbani kwake akiwa mlevi,” akasema mjukuu wake, Gerald, ambaye ni mwanawe marehemu Jonathan Moi.

Akiongea na Taifa Leo jana, Gerald alisema kwa sababu Mzee Moi alichukia pombe hakuna mtu wa familia hiyo alihudhuria hafla za kifamilia akiwa mlevi.

“Wale ambao hawakuwa waraibu wa pombe walipata misaada ya kifedha kutoka kwa babu yetu kila mara. Hii ndio sababu baadhi ya wanawe Mzee walikuwa karibu naye zaidi kwa sababu aliwapenda wasio waraibu wa pombe,” akaeleza Gerald.

Alifichua kuwa endapo Mzee Moi angegundua kuwa baadhi ya wanawe au wajukuwe walikuwa wakilewa alikuwa akiwakaripia papo hapo.

“Pindi babu angegundua kuwa mmoja wetu ni mlevi angemgombeza hapo hapo na kumwelezea kuhusu madhara ya pombe,” Gerald akaeleza.

Alimtaja babu yao kama mtu aliyekuwa mkarimu na mpole na aliyependa kuwasaidia watu bila ubaguzi.

“Mzee Moi alithamini elimu na wakati huu ninasomea kozi ya Uhandisi katika Chuo cha Mafunzo ya Kiufundi cha Rift Valley mjini Eldoret kwa sababu ya usadizi wa kifedha niliopata kutoka kwake,” akasema Gerald.

Alisema watamkosa Mzee Moi haswa wakati wa mkutano ya kifamilia kila Desemba ambapo wangempa zawadi.

“Baada ya kumpa zawadi hizo angetuhubiria na kunukuu vifungu vya Biblia. Neno la Mungu ndio zawadi kuu ambayo daima nitakumbuka kupewa na babu yangu. Vile vile, alitushauri kuwaheshimu wazee na wazazi,” akasema Gerald.

Alisema mkutano wa mwisho wa Mzee Moi pamoja na wajukuu ulifanyika Desemba 2018 na alikuwa akiwakumbuka wajukuu wake wote.

“Aliwatambua wajukuu wake wote kwa majina yao licha ya umri wake mkubwa,” akasema Gerald.

Polisi washirikianao na wauzaji pombe motoni

JUSTUS OCHIENG na VITALIS KIMUTAI

SERIKALI imelazimika kuchukua hatua ili kukomesha utengenezaji na uuzaji wa pombe haramu na dawa zingine za kulevya, ambayo inalaumiwa kuwa imewaharibu vijana wengi pamoja na kuvunja familia.

Kwa kupitia waziri wa usalama wa ndani Fred Matiang’i na katibu katika wizara hiyo Karanja Kibicho, serikali inapanga kutumia maafisa wa polisi wa kawaida, pamoja na wale wa utawala, kumaliza tatizo hili.

“Tunaanza juhudi za kukabiliana na uuzaji wa dawa za kulevya, najua itakuwa kazi ngumu, lakini tumejitayarisha kuanza hii safari,” Dkt Matiang’i akasema.

Waziri huyo alisema haya majuzi katika mkutano wa usalama, wakati maafisa wa polisi walioaminiwa kutekeleza mpango wenyewe wanaendelea kukinzana, na kushirikiana na wauzaji wa vileo hivyo haramu.

Katika Kaunti ya Homa Bay, baadhi ya maafisa wa polisi wanashirikiana na wafanyabiashara wa vileo hivyo kuendeleza biashara yenyewe, hali ambayo imelazimu wasimamizi wa serikali wa utawala kufanya misako bila kusaidiwa na polisi, wakihatarisha maisha yao.

“Tunapitia hatari sana kwani tunaweza kuvamiwa. Kwa sasa tunaenda peke yetu bila ulinzi wa polisi, kwani kila wakati tulipokuwa tukishirikiana nao hatukupata pombe haramu, kwa kuwa waliwafahamisha wafanyabiashara hao kuhusu msako hata kabla yetu kufika,” akasema mmoja wa maafisa ambao wamekuwa kipaumbele kukabiliana na pombe haramu kaunti hiyo.

Katika visa kadhaa, machifu na manaibu wao wamevamiwa wakati wanapofanya msako wa kutafuta pombe haramu, japo wizara ya usalama wa ndani inazidi kushikilia kuwa imejitolea kumaliza pombe hizo.

Polisi katika kituo cha kupiga doria cha Sindo, eneo la Suba wamelaumiwa vikali, kuwa walificha pombe haramu aina ya Chang’aa lita 140 ambayo ilikuwa imekamatwa na viongozi wa utawala eneo hilo, badala yake wakiweka maji.

Pombe hiyo ilikuwa sehemu ya lita 4,710 aina ya Kangara, ambayo ilipangiwa kuharibiwa wakati wa operesheni hiyo.

Operesheni hiyo iliongozwa na naibu kamishna wa kaunti eneo la wilaya ya kati, Abdullalahi Abdimalik pamoja na machifu, manaibu wao na wazee wa vijiji eneo hilo.

Inadaiwa polisi walificha pombe hiyo ili mshukiwa aliyekamatwa nayo, Vitalis Otieno, aachiliwe kwa ukosefu wa ushahidi.

Kamishna wa Kaunti ya Homa Bay David Kipkemei alisema malalamishi hayo yanachunguzwa na Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) kaunti hiyo.

“Ni kweli baadhi ya maafisa wa polisi walishirikiana na mshukiwa na kubadilisha lita 140 za Chang’aa na maji ili kukwepa korti lakini uchunguzi umeanzishwa na washukiwa watakamatwa,” Bw Kipkemei akasema.

AFYA: Yafahamu madhara ya unywaji pombe kupita kiasi

Na MARGARET MAINA

mwmaina@ke.nationmedia.com

WATU wengi wanapopumzika nyumbani au vilabuni, utawapata wakinywa pombe tofauti.

Lakini sio siri kuwa pombe husababisha matatizo makubwa ya kiafya, yakiwemo maradhi ya moyo, ini pamoja na majeraha yatokanayo na ajali zitokanazo na ulevi mathalani dereva kuendesha gari akiwa chakari.

Vinywaji vilivyotengenezwa kwa matunda bila kilevi ni bora zaidi kwa afya yako kuliko vile vyenye kilevi.

Matatizo ya moyo

Unywaji wa pombe kupindukia husababisha matatizo mbalimbali ya moyo. Mishipa ya moyo hudhoofika na kushindwa kusukuma damu. Hii inaweza kusababisha damu kuganda na kusababisha kiharusi.

Tatizo la ini

Unywaji wa pombe unaweza kusababisha maradhi ya ini. Uharibifu huu husababisha seli za ini kuwa makovu na kushindwa kufaya kazi vyema.

Shinikizo la damu

Unywaji wa pombe kupita kiasi kunaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa shinikizo la damu. Pombe inaweza kuathiri mfumo wa usukumaji wa damu mwilini; jambo ambalo husababisha shinikizo la damu na baadaye matatizo mengine kama kushindwa kwa figo, ini na kadhalika.

Ugonjwa wa anemia

Anemia ni ugonjwa unaotokana na kushindwa kwa seli nyekundu za damu kusafirisha oksijeni ya kutosha kwenda kwenye mwili. Hivyo, unywaji wa pombe hupunguza uwezo wa seli nyekundu za damu kusafirisha oksijeni ya kutosha hivyo kusababisha ugonjwa wa anemia.

Kusinyaa kwa ubongo

Mtu anapozeeka nao ubongo wake unazidi kusinyaa. Hivyo unywaji wa pombe huharakisha kusinyaa kwa ubongo. Hili husababisha matatizo yatokanayo na kusinyaa kwa ubongo kama vile kupoteza au kupungua kwa uwezo wa kumbukumbu.

Maumivu ya miguu (gout)

Gout ni ugonjwa wa miguu unaotokana na kukusanyika kwa asidi kwenye viungio vya mifupa. Mara nyingi ugonjwa huu hujitokeza sana majira ya baridi. Pombe imedhihirika kuchangia kwa kiasi kikubwa kutokea kwa ugonjwa huu.

Kusinyaa kwa uso na macho

Unywaji mkubwa wa pombe husababisha kusinyaa kwa uso na macho hasa kwa wale wanaokunywa usiku. Mara ngingi uwatazamapo wanywaji wakubwa wa pombe utaona hata sura zao zimebadilika na kuonekana zimezeeka au kuchoka kuliko awali.

Pombe, mitambo ya kamari na bangi yateketezwa Thika

Na LAWRENCE ONGARO

WALANGUZI wa dawa za kulevya, watengenezaji pombe haramu na wachezaji kamari wamepewa ilani wajiondoe kwa biashara hizo ama wakabiliwe vilivyo na Serikali.

Kamishna wa eneo lote la Kati Bw Wilfred Magwanga amesema Alhamisi kwamba huu mwaka mpya wa 2020 ni wa kuangamiza maovu hayo yote bila kusita.

“Leo nimekuja na kikosi chote cha wakuu wa serikali hapa, na lengo letu kuu ni kuona ya kwamba maovu yote yanayotendeka eneo la Kati yanaangamizwa mara moja,” amesema Bw Magwanga.

Katika mkutano huo mitambo ya kuchezea kamari zaidi ya 200 ilichomwa pamoja na pombe haramu na dawa za kulevya.

Amesema tayari wamegundua sehemu zote zinazoendesha biashara hizo haramu na kwa hivyo, vitengo vyote vya usalama katika eneo hilo vitafanya juhudi kuona ya kwamba wahusika wote wanaoendesha kazi hiyo chafu wanatiwa nguvuni mara moja.

“Tutaweka doria katika mipaka zetu zote na kuhakikisha maafisa wa usalama wanakagua wale wote wanaoshukiwa kuwa ni walanguzi ama wauzaji wa dawa za kulevya,” amesema Bw Magwanga.

Wakati wa hafla hiyo iliyoendeshwa mjini Thika katika uwanja wa Community, Starehe, kamishna huyo alikuwa ameandamana na wakuu wote wa usalama kutoka hilo.

Himizo

Kamishna wa Kaunti ya Kiambu Bw Wilson Wanyanga amewahimiza wazazi kuwapeleka watoto wao shuleni bila kuchelewa.

“Hakuna sababu ya kutoa vijisababu kuwa huna uwezo wa kumpeleka shuleni mtoto wako. Ni vyema uwasiliane na watu wanaohusika ili uweze kupata usaidizi,” amesema Bw Wanyanga.

Amesema serikali iko tayari kupambana na walanguzi wa dawa za kulevya na wale wanaopika pombe vijijini.

Mitambo ya kamari. Picha/ Lawrence Ongaro

Afisa huyo hata aliwapa wananchi matumaini kwa kuwapa nambari maalum ya kupiga ambayo ni 988, iwapo watashuku jambo baya likitendeka katika maeneo wanakoishi.

“Kuna haja kubwa ya kuchunga mwenzako na ukiona jambo baya ama kusikia mara moja piga simu,” amesema Bw Wanyanga.

Mwenyekiti wa Nyumba Kumi ambaye anahusika na hali ya usalama katika mji wa Thika, Bw Charles Owila, amewashauri wananchi popote pale walipo kushirikiana na kamati yake ili kuripoti mambo maovu yanayoshuhudiwa katika makazi yao.

“Wengi wenu mnaelewa mambo mengi yanayotendeka katika makazi yenu lakini ubaya ni kuogopa kutoa habari kwa kamati yetu,” amesema Bw Owila.

Afisa wa polisi na mwanafunzi washtakiwa kwa wizi wa pombe

Na LAWRENCE ONGARO

AFISA mmoja wa polisi na mwanafunzi wa chuo kikuu wamefikishwa mahakamani kwa wizi wa pombe kutoka katika kiwanda cha Thika.

Afisa huyo Bi Anastacia Muchungu na mwanafunzi huyo, Ben Kamau, walifikishwa mbele ya hakimu mkuu wa Thika Bw Oscar Wanyaga, wakituhumiwa kwamba walipatikana na katoni 11 za pombe aina ya whisky chapa ‘Furaha’ kutoka kiwanda cha African Spirits Limited mjini Thika.

Inadaiwa kuwa kiwanda hicho kilifungwa Januari 2019 baada ya kukosa kulipia ushuru ya mamilioni ya fedha.

Kulingana na maelezo yaliyokuwa katika faili ya washtakiwa ni kwamba mnamo Januari 4, 2020, wawili hao waliingia katika kiwanda hicho cha mvinyo na kuiba katoni 11 za whisky chapa ‘Furaha’ wakitumia gari aina ya Toyota Premio nambari KBP 770D.

Gari hilo lilinaswa katika kizuizi cha Polisi cha Makongeni mjini Thika likisafirisha pombe hiyo.

Miezi michache iliyopita inadaiwa afisa mwingine wa polisi alifariki katika kiwanda hicho akishika doria baada ya kudaiwa alianguka kutoka ghorofa ya juu.

Afisa anayechunguza kesi hiyo aliomba mahakama iruhusu ombi lake la kutaka washukiwa wasalie kizuizini kwa siku zingine saba huku akifanya uchunguzi zaidi.

Lakini hakimu huyo alikubali ombi la washukiwa na kuwaachilia kwa dhamana ya Sh100,000 na mdhamini wa kiwango sawa ama dhamana ya Sh50,000 pesa taslimu kila mmoja.

Kulingana na uamuzi wake hakimu huyo, hata ingawa afisa huyo wa kuendesha uchunguzi alikuwa na nia waendelee kuzuiliwa kwa muda huo, bado ni vyema kuzingatia haki zao za kimsingi ambazo ziko kwenye Katiba.

Kwa hivyo alitoa amri washtakiwa washtakiwe haraka iwezekanavyo ili wawe nje kwa dhamana wakingoja kuendelea kwa kesi hiyo.

Afisa anayeendesha uchunguzi huo Bw Pascal Omondi alisema bado kuna washukiwa wengine anaotarajia kufikisha mahakamani ili kujumuishwa na washukiwa hao wawili.

Alitaka apewe muda wa siku saba ili aweze kukamilisha uchunguzi wake na kuwafikisha mahakamani.

Hata hivyo, hakimu alipanga kesi hiyo kutajwa Januari 14, 2020, huku washukiwa wakiwakilishwa na wakili wao Bw Ishmael Nguring’a.

Washukiwa hao walifika mahakamani wakijifunika nyuso zao ili wasichukuliwe picha na waandishi wa habari.

Mahakama ilijaa pomoni huku watu waliofika huko wakitaka kujionea washukiwa hao ambao walikuwa chini ya ulinzi mkali.

Korti yamzuia DCI kufunga akaunti za kampuni ya pombe na mvinyo

Na RICHARD MUNGUTI

BIASHARA katika kiwanda cha kutengeneza pombe na mvinyo cha Africa Spirits na kampuni zingine nane zitaanza kutengeneza bidhaa baada ya Mahakama Kuu kuamuru akaunti zao zifunguliwe.

Na wakati huo huo, Jaji Luka Kimaru alimkosoea mkurugenzi wa uchunguzi wa jinai (DCI) kwa kujiingiza katika uchunguzi wa masuala ya ukwepaji ushuru.

Jaji Luka Kimaru aliyefutilia mbali agizo alilokuwa amepata la DCI kuchukunguza akaunti za kampuni tisa za bwanyenye Humphrey Kariuki, Jaji alisema mamlaka ya ushuru nchini (KRA) ina mamlaka na nguvu tosha za kuchunguza maswala ya ushuru bila kushirikisha polisi.

Jaji Kimaru aliiamuru KRA ichunguze masuala ya ushuru bila kumtegemea DCI jinsi sheria inavyoitaka.

Na wakati huo huo, Jaji Kimaru alifutilia mbali agizo la kufungwa kwa akaunti za kampuni tisa zikiwamo Africa Spirits Limited (ASL) na Wow Beverages Limited (WBL) zinazomilikiwa na Bw Kariuki.

Bw Kariuki na washukiwa wengine tisa wamekanusha mashtaka ya kukwepa kulipa ushuru wa Sh41 bilioni, kumiliki ethanol yenye thamani ya Sh7.9 milioni na kupatikana na risiti feki za ushuru.

Jaji Kimaru alikuwa ameombwa na mawakili Cecil Miller na Macmillan Ouma afutilie mbali agizo la mahakama ya Kiambu ya kufungwa kwa akaunti za makampuni tisa ya Bw Kariuki.

Akitoa uamuzi Jaji Kimaru alifutilia agizo la kufungwa kwa akaunti hizo akisema, “ Amri iliyotolewa na mahakama ya Kiambu ni kuchunguzwa kwa akaunti za kampuni tisa katika benki za Kenya Commercial (KCB) na National (NBK).”

Jaji huyo alisema kile polisi wameruhusiwa kufanya ni kuchunguza akaunti za mshukiwa na wala sio kuzifunga.

“Kwa mujibu wa sheria za KRA, maafisa wake wana uwezo na mamlaka ya kuchunguza akaunti na wala sio kuwaalika polisi kutenda yasiyowapasa,” alisema Jaji Kimaru.

Jaji aliamuru kesi iliyowasilishwa na DCI katika mahakama ya Kiambu iwasilishwe mbele yake kuisoma na kisha kutoa maagizo yanayofaa.

Kuhusu kusitisha kusikizwa kwa kesi alizoshtakiwa Bw Kariuki na wenzake, Jaji Kimaru alisema Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) na KRA wanaweza endelea nazo.

SENSA: Hofu ya wanasiasa Mlima Kenya

Na MWANGI MUIRURI

HAIJULIKANI hasa ni kwa msingi gani ambapo wanasiasa wengi wa Mlima Kenya hukesha wakilalamika kuwa “idadi zetu – jamii za Gema (ushirika wa Gikuyu, Embu na Ameru) – zinapungua kila uchao.”

Ingawa wanasiasa wengi katika eneo hilo huwa na kati ya watoto wawili na watatu katika ndoa zao au ulezi wao, bila kuzingatia wa nje ya ndoa, wao husukuma kampeni kali wakiwataka wenyeji wazaane.

Ni hali mbaya kiuchumi kuwataka raia wa kipato cha chini wazae kwa sababu tu za kisiasa bali sio kwa msingi wa uwezo wa malezi.

Siasa ni mchezo mchafu.

Hata somo la sayansi ya siasa lililemewa na kuipa maana dhana ya “siasa” na ikaafikiana kuwa “sisi wote ni wanasiasa katika hali zetu zote za kimaisha.”

Ni kauli anayopenda kutumia mhadhiri Gasper Odhiambo.

Ni katika hali hiyo ambapo Seneta wa Kiambu, Kimani wa Matangi alisema anaomba Mungu sensa ya mwaka 2019 isije ikathibitisha huenda “tumepitwa kwa idadi na jamii kama ya Akamba na Abaluhya.”

Analia kuwa katika eneo la Mlima Kenya, kumekuwa na maandamano tele ya wanawake wakiteta kuhusu kupotea kwa nguvu za kiume miongoni mwa wanaume wa eneo hilo hivyo basi kupunguza uwezo wa kuzaa.

Aidha, mbunge wa Gatundu Kusini, Moses Kuria anateta kuwa ulevi umekuwa tisho kuu kwa wenyeji.

“Hapa kwetu shule za msingi zinafungwa kwa kukosa watoto wa kusajiliwa kama wanafunzi,” akasema Kuria.

Anasema kuwa ulevi huo pamoja na utumizi wa dawa za kupanga uzazi miongoni mwa wanawake wa eneo hilo kumesababisha kukosa kuafikia malengo ya kuongezeka kwa takriban watu milioni moja kwa mwaka.

Gavana wa Nyandarua, Francis Kimemia anasema kuwa hesabu ya watu na nyumba iliyofanywa 2009  ilionyesha upungufu wa watu 1.8 Milioni kwa kuwa ilitarajiwa wafike  zaidi ya Millioni nane lakini wakawa 6.3 milioni.

“Tukaze tukiomba sensa hii ya sasa itupe matumaini ya kesho yetu katika siasa,” asema.

Ni hali ambayo imewaelekeza wengine wa wanasiasa wa eneo hilo kutangaza zawadi za pesa taslimu kwa walevi wote ambao watatema uraibu wao na watunge wanawake wao mimba, zawadi hiyo ikiwa kati ya Sh500 na Sh1,000!

Aidha, Bw Kimemia alidai kuwa pombe haramu zilielekezwa katika jamii hizo miaka ya 80 kwa misingi ya siasa ambapo nia ilikuwa kuwamaliza kizazi.

“Ni lazima watu wa jamii hizi wajiulize mbona ni kwao tu pombe hizi zilikubaliwa ziuzwe bila ya kuthibitiwa. Na tangu maeneo yenu yafanywe kuwa kiwanda na pia soko ya pombe hizi, hamuzai na serikali inaashiria kuunganisha baadhi ya mashule kwani mengi hayana idadi ya kuhudumiwa na walimu 10,” akasema.

Katika hali hiyo, wanawake wa eneo hilo wameshawishiwa walegeze kinga dhidi ya kupata uja uzito kupitia utumiaji dawa za kupanga uzazi na washirikiane na waume zao ili kupambana na upungufu wa watoto katika eneo hilo.

Mshirikishi wa kitaifa wa Shirika la Wanawake Waelimishaji (Fawe) Bi Cecilia Gitu anasema kuwa utumiaji wa dawa za kupanga uzazi bila ya kuwahusisha waume zao unasababisha upungufu wa watoto katika eneo hilo.

Alisema idadi ya watoto wanaozaliwa kila mwezi eneo hilo imepungua hadi wane kwa sasa ikilinganishwa na watoto saba waliokuwa wakizaliwa mwaka wa 1998.

Ripoti ya Shirika la Kenya Demographic Health Survey (KDHS) 2018 ilionyesha kuwa asilimia 67 ya wanawake wa Mlima Kenya hutumia dawa za kupanga uzazi na huwa hawaelezei waume zao kuhusu hali hiyo.

“Ukiambatanisha na idadi ya wazee wanaokunywa pombe kupindukia hivyo basi kulemewa na majukumu muhimu ya ndoa, utaona hali ya hatari kuhusu vizazi vijavyo kwani idadi yao itakuwa chache mno,” akasema.

Alilalamika kuwa kwa sasa hospitali nyingi hata hazipati waja wazito wa kuhudumia na shule nyingi za nasari imefungwa kwa kukosa watoto wa kusajili.

“Nyakati tulikuwa tunasikia shule moja ya msingi iko na watoto zaidi ya 2,000 zimeisha na sasa hata serikali inawaza kujumuisha shule kadhaa pamoja kwani hakuna idadi ya kufundishwa na walimu zaidi ya 10,” akateta.

Msako mkali wa pombe haramu wafanywa Githurai 

Na SAMMY WAWERU

MSAKO mkali dhidi ya pombe haramu katika mtaa wa Githurai 44, Kaunti ya Nairobi na Githurai 45 umeanzishwa.

Shughuli hii ilianza mnamo wikendi, watengenezaji wa chang’aa na baa na vilabu vinavyouza pombe ambayo haijatathminiwa na kupitishwa na shirika la ubora wa bidhaa nchini, Kebs, wakilengwa.

Jumatatu, maafisa kutoka kituo cha polisi cha Kimbo, Ruiru, walifanya operesheni katika mabaa kadhaa Githurai 44.

“Baadhi ya mabaa yenye leseni yanauza pombe haramu, ni hatia na hatutaruhusu hilo kufanyika,” mmoja wa maafisa walioshiriki msako huo na aliyeomba tusichapishe jina lake aliambia Taifa Leo.

Baa nyingi zimekiuka sheria maarufu kama za Mututho ambapo zinafunguliwa mchana.

Wakati akihudumu kama mwenyekiti wa shirika la kudhibiti utumizi wa dawa za kulevya na vileo, Nacada, aliyekuwa mbunge wa Naivasha John Mututho aliasisi sheria kukabiliana na pombe, mojawapo ikiwa baa zifunguliwe saa kumi na moja jioni.

“Baa eneo hili zinahudumu mchana peupe. Isitoshe, nyingi zinauza pombe haramu na hatari,” alilalamika mkazi.

Kukamata

Na kwenye operesheni ya Jumanne, baadhi ya wahudumu na waraibu wa vileo walikamatwa.

Kulingana na OCS wa Kimbo, Hassan Pole, katika mtaa wa Githurai 45 watengenezaji kadhaa wa chang’aa wametiwa nguvuni.

Progressive, Mumbi na Mwihoko, yametajwa kama maeneo yaliyoathirika pakubwa.

Baada ya kuchaguliwa, Gavana wa Kiambu 2017, afisi ya Ferdinand Waititu ilitwaa wajibu wa kutoa leseni za baa.

Bw Waititu alidai maafisa wa polisi katika kaunti hiyo wameshindwa kudhibiti uuzaji na unywaji wa pombe haramu.

Kiambu ni mojawapo ya kaunti zilizoathirika pakubwa na kero ya pombe haramu na hatari.

Afisa wa sensa anaswa kwa kuiba pombe ya watalii

Na WAANDISHI WETU

SHUGHULI ya kuhesabu watu iliendelea kukumbwa na visanga Jumatatu huku mmoja wa maafisa wa sensa akinaswa kwa kuwaibia watalii pombe hotelini.

Afisa huyo wa sensa aliyetambuliwa kama Antony Kantai, anadaiwa kuwaibia watalii pombe na bidhaa zingine za thamani ya Sh200,000 katika hoteli ya Angama Lodge iliyoko Mbuga ya Masai Mara, Kaunti ya Narok.

Kulingana na polisi, mshukiwa alienda kuhesabu wafanyakazi hotelini hapo kabla ya kuingia katika hema la watalii na kuiba fedha, darubini, tableti, chupa nne za pombe na shuka mbili.

Mshukiwa anazuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Lolgorian kusubiri kufikishwa mahakamani leo.

Katika Kaunti ya Nakuru, mwanamke alishtakiwa kwa kuchuuza pombe wakati wa sensa.

Katika Kisii na Nyamira, maafisa wa Sensa wameamua kuendesha shughuli ya kuhesabu watu mchana kutokana na hofu ya kukumabana na wachawi usiku.

Katika Kaunti ya Kisumu polisi wanazuilia watu wawili wanaoshukiwa kubaka afisa wa sensa katika eneo la Maseno.

Nao mume na mkewe walikamatwa kwa kuzuia maafisa wa sensa katika mtaa wa Nyalenda kufanya kazi yao.

Katika Homa Bay, afisa wa Sensa katika eneo la Gwassi alisimamishwa kazi baada ya kuacha kuhesabu watu na kwenda kufanya biashara ya boda boda.

Jijini Nairobi kulikuwa na kizaazaa katika mtaa wa mabanda wa Mukuru-Kaiyaba baada ya familia moja kukataa kuhesabiwa Jumapili jioni.

Nao wanawake zaidi ya 1,000 kutoka Tanzania walioolewa na Wakenya katika eneo la Taveta, Kaunti ya Taita Taveta wana matumaini ya kupata vitambulisho baada ya zoezi la sensa.

Katika Kaunti ya Nyandarua wakazi walilalamika kuwa wengi wao hawajahesabiwa licha ya shughuli hiyo kuanza siku tatu zilizopita.

Ripoti za George Sayagie, Lucy Mkanyika, Waikwa Maina, Joseph Openda, Dominic Magara, Sammy Kimatu, Rushdie Oudia, Benson Ayienda, Donnah Atola, Vitalis Kimutai, George Odiwuor Na Shaban Makokha

Saba wasakwa eneo la Makwa kwa kutajwa utengenezaji pombe haramu

Na LAWRENCE ONGARO

WATENGENEZAJI saba wa pombe haramu eneo la Makwa, Gatundu Kusini wanasakwa na polisi ili wafikishwe mahakamani na kufunguliwa mashtaka.

Kamishna wa Kaunti ya Kiambu, Bw Wilson Wayanga alitoa amri hiyo Jumanne akisema watengenezaji hao ni hatari kwa maisha ya binadamu.

Wakazi wa kijiji cha Makwa wanazidi kulalamika kuwa pombe haramu imerejea kwa kishindo huku vijana wengi wakiwa tayari wameathirika vibaya.

Bw Wanyanga alikuwa ameandamana na wakuu wa serikali na machifu wote wa eneo hilo.

“Watengenezaji pombe wameharibu kabisa maisha ya vijana katika eneo hili,” alisema Bw Wanyanga.

Alisema uchunguzi uliofanywa umedhibitisha kuwa maeneo yaliyoathirika kabisa na pombe haramu ni Mwea, Gatukuyu, Mang’u, na vitingoji vyake.

Kamishna wa Kaunti ya Kiambu Bw Wilson Wanyanga akagua vyombo vinavyotumika na watengenezaji wa pombe haramu katika kijiji cha Makwa, Gatundu Kaskazini. Picha/ Lawrence Ongaro

Wakazi hao waliohudhuria baraza lililoandaliwa na Kamishna huyo, walionekana kujawa na ghadhabu huku wakitaka hatua ya haraka ichukuliwe ili kudhibiti unywaji wa pombe haramu.

Mkazi mmoja wa eneo hilo, Bw Peter Chege, alipendekeza maafisa wa usalama ambao wametumikia serikali eneo hilo kwa muda mrefu wapewe uhamisho bila kuchelewa.

“Tunaelewa kuna maafisa wengi wa serikali ambao hushirikiana na watengenezaji pombe; jambo ambalo limeponza kabisa juhudi za serikali kukabiliana na pombe haramu,” alisema Bw Chege.

Kufika kujionea

Bw Wanyanga alisema watafanya juhudi kuzuru eneo hilo angalau mara moja kila wiki ili kujionea kazi ambayo inaendeshwa na maafisa wa serikali.

“Nitafika hapa kila wiki ili kujionea jinsi machifu na maafisa wa serikali wanavyopambana ili kuangamiza pombe haramu,” alisema afisa huyo.

Alisema kila naibu chifu na machifu wenyewe watalazimika kuzunguka vijijini ili kupambana na pombe haramu na dawa za kulevya.

“Kila mmoja atalazimika kuchunga eneo lake na kuwasilisha ripoti katika ofisi yangu kila wiki,” alisema Bw Wanyanga.

Mzee mmoja wa kijiji hicho Bw Michael Muchai alisema licha ya ukweli kwamba pombe hiyo ilikuwa imekabiliwa vilivyo, bado kuna watengenezaji wachache ambao “ni sugu.”

“Sisi tunaiomba serikali kufanya hima ili kuokoa vijana wetu ambao wametekwa nyara na pombe hiyo haramu. Tutahakikisha tunaungana kama wakazi ili kupambana nao,” alisema Muchai.

Naye mwanamke mmoja mkazi wa eneo hilo ambaye hakutaka jina lake lichapishwe, alisema vijana wao wengi wameathirika na wangetaka serikali kuingilia kati.

“Hatutakubali waje hapa kutuharibia vijana hapa Makwa. Sisi wakazi wa hapa tutaungana kuona ya kwamba pombe hiyo imeangamizwa kabisa,” alisema mama huyo.

Alionyesha mkono wake uliokatwa na mmoja wa wapikaji pombe haramu kwa sababu ya kile alikitaja ni “kukosoa mienendo yao.”

Demu aangua kilio alipokosa wa kumnunulia bia

Na JOHN MUSYOKI

EMBU MJINI

DEMU mmoja mjini hapa aliangua kilio wanaume walipokataa kumrushia mistari ya mapenzi na kumnunulia pombe.

Duru zinasema demu alifika kilabuni mwendo wa saa kumi na moja wanaume walipokuwa wakijaajaa kujiburudisha. Alisimama karibu na mlango kwa dakika kadhaa kisha akaingia ndani na alipoulizwa na wahudumu alichotaka kuuziwa hakusema chochote.

Kulingana na mdokezi, mwanadada huyo aliwakodolea macho wanaume waliokuwa wakiingia kilabuni na wengine wakiendelea kuteremsha dozi.

Mhudumu wa kilabu hicho alienda kumsalimia lakini demu akampuuza. “Nikusaidie vipi? Itisha unachotaka, hapa tunaruhusu wateja peke yake,” mhudumu huyo alisikika akimwambia demu. Inasemekana demu alikataa katakata kuondoka alikokuwa ameketi karibu na mlango.

“Sitaki kuongea na wewe. Mwanamke kama mimi utanisaidia na nini? Nashangaa sana. Kwani wanaume hawa wa huku kwenu ni wa aina gani, hata hawataki kunitongoza.

“Mimi ni mrembo lakini wanaume wa huku ni wachoyo sana,” demu alimwambia mhudumu huku akidondokwa na machozi.

“Sasa unalia kwa nini. Ni nani amekukosea hapa kilabuni? Kwenu ni wapi na unafanya kazi gani,” jamaa mmoja alimuuliza demu alipomuona akilia.

Hata hivyo baadhi ya wanaume walimkashifu mwanadada huyo. “Aondoke hapa kilabuni. Demu huyo hana nia nzuri na huenda ni tapeli.

“Mwambie wateja wa kilabu hiki ni wachoyo kwa machangudoa. Wanawake wa siku hizi wanapenda kuvuna wasikopanda,” jamaa mmoja alisikika akisema.

Inasemekana demu alianza kuzusha lakini akaondolewa juu juu na wahudumu wa kilabu hicho huku wakimfokea vikali. Ilibidi demu kuondoka huku akiangua kilio lakini hakuna mtu aliyemjali.