Kabras na KCB watinga fainali ya raga ya Kenya Cup baada ya kuzima Strathmore na Menengai

Na GEOFFREY ANENE

KABRAS Sugar imepiga Strathmore Leos 36-19 nayo KCB ikalima Menengai Oilers 35-17 katika mechi za nusu-fainali za Ligi Kuu ya raga ya wachezaji 15 kila upande maarufu Kenya Cup mnamo Agosti 28.

Wanasukari wa Kabras na wanabenki wa KCB sasa watapepetana Septemba 4 kuamua mshindi wa ligi hiyo ya klabu 11. Mabingwa wa mwaka 2016 Kabras walilemea wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Strathmore kupitia kwa miguso ya Derrick Ashiundu (mitatu) na Jone Kubu na Ntabeni Dukisa (mguso mmoja kila mmoja). Dukisa pia alichangia mikwaju mitatu na penalti mbili katika mchuano huo.

KCB ilipata alama kupitia kwa Jacob Ojee (miguso mitatu), Michael Wanjala (mguso mmoja), Darwin Mukidza (penalti mbili na mikwaju mitatu), na Shaaban Ahmed (mkwaju mmoja).

Kitakuwa kivumbi kati ya Kabras na mabingwa watetezi KCB. Kabras wamewahi kupiga KCB mara mbili pekee tangu waingie Kenya Cup kwa mara ya kwanza kabisa msimu 2014-2015.

Wanasukari wa Kabras, ambao wanatiwa makali na Dominique Habimana, walichapa KCB 19-3 msimu uliopita wa 2019-2020 na kuandikisha ushindi wa pili mfululizo waliponyuka vijana wa kocha Curtis Olago 30-23 zaidi ya wiki tatu zilizopita (Agosti 5). Kabla ya hapo, mabingwa mara saba KCB waligawa dozi kali kwa Kabras.

Takwimu za Kenya Cup za ana kwa ana za nusu-fainali 2021:

Kabras na Strathmore Leos

Kabras 33-19 Strathmore Leos

Strathmore Leos 9-35 Kabras

Kabras 54-7 Strathmore Leos

Strathmore 13-62 Kabras

Kabras 43-13 Strathmore Leos

Kabras 44-13 Strathmore Leos

KCB na Menengai Oilers

KCB 35-17 Menengai Oilers

Menengai Oilers 19-22 KCB

Menengai Oilers 13-43 KCB

KCB 43-13 Menengai Oilers

Menengai Oilers 20-29 KCB

KCB 27-3 Menengai Oilers

Shujaa yafunzwa umuhimu wa utimamu wa kiakili nao Lionesses wakianza mazoezi ya Olimpiki

Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya taifa ya raga ya wachezaji saba kila upande ya wanaume maarufu kama Shujaa, mnamo Alhamisi ilichukua mapumziko ya siku moja kupata mafunzo ya uhodari wa kiakili katika uchezaji mzuri.

Shujaa ya kocha Innocent “Namcos” Simiyu itakabana koo na Amerika, Afrika Kusini na Ireland katika mechi za Kundi C za Olimpiki 2020 zitakazofanyika jijini Tokyo, Japan mnamo Julai 23 hadi Agosti 8.

“Vipindi vilivyoendeshwa na daktari Kanyali Ilako, vilikuwa muhimu katika kuhakikisha wachezaji wanapata kuwa na mtazamo mzuri uwanjani, hata wakati kuna presha,” Simiyu alieleza Taifa Leo kutoka mjini Kurume ambako timu hiyo imepiga kambi kwa matayarisho ya mwisho.

Nahodha huyo wa zamani wa Shujaa aliongeza kuwa timu hiyo imejaa motisha.

“Tumefaulu katika kupata nafuu tena baada ya kusumbuliwa na usingizi kutokana na tofauti ya kimaeneo katika saa,” alisema.

Japan iko saa sita mbele ya Kenya. Mnamo Jumanne, Shujaa ilipigwa jeki baada ya nyota William Ambaka kufika kambini akitokea klabu yake mpya ya Narvskaya Zastava nchini Urusi. Hapo Jumatano, Shujaa pia ilikuwa na kipindi cha kukandwa.

Nayo, timu ya kina dada maarufu Lionesses ilikuwa na kipindi chake cha kwanza cha mazoezi ya uwanjani.

Wanaraga wa Kenya Lionesses wakifurahia kipindi chao cha kwanza cha mazoezi ya Olimpiki mjini Kurume, Japan mnamo Julai 15, 2021. Picha/ Hisani

Lionesses itamenyana na New Zealand, Urusi na Uingereza katika mechi za Olimpiki za Kundi A.

Ana matumaini tele kushiriki katika raga ya hadhi akifuata nyayo za Collins Injera

Na PATRICK KILAVUKA

MCHEZO wa raga hauhitaji tu usuli na nguvu bali unahitaji ujuzi na mazoezi si haba kuhimili makali yake.

Hii ni kauli ya mwanaraga Campbell Okello, 17, mwanafunzi wa Kidato cha Pili katika Shule ya Upili ya Sigome, Kaunti ya Siaya.

Alianza kuwa na hamu ya kuujua mchezo huu tangu akiwa katika Darasa la Sita katika Shule ya Msingi ya Buruburu 1, Kaunti ya Nairobi.

Alijenga imani mchezoni kutokana na vile alikuwa anaona ukichezwa hadi akanuia kuanza kutafuta mengi kuhusu kwenye mtandao wa youtube na kuhudhuria ukichezwa uwanjani.

Mchezaji wa hadhi ya kitaifa na kimataifa Collins Injera anampa kiu na hamasa ya kutia bidii mchezoni.

Anasema alipokuwa anamuona mchezaji huyo akichapa shughuli ugani, alikuwa anasisimuka kiasi cha kuweza kuongezea matumaini kuwa hai siku moja atashiriki katika ulingo wa fani hii mithili yake au kufuata nyayo zake unyounyo.

“Mimi hujifua zaidi ninapokuwa uwanjani kwani kupitia mazoezi makali, nimepata kushiriki katika mashindano ya shule za upili hadi kiwango cha kaunti kabla msambao wa ndwele ya corona,” anasema mchezaji huyo ambaye hucheza kama mwanaraga kiungo.

Isitoshe, alijiunga katika timu ya shule akiwa kidato cha kwanza, muhula wa tatu.

Mwanaraga Okello anasisitiza kwamba, pindi tu alipojiunga na shule ya upili, alijaribu kutathmini mchezo upi angejiunga kuucheza! Lakini dau lake halikuzama kwani, alimpata kocha Joel Ambani ambaye huinoa timu ya shule na akamshawishi kujiunga.

Mwanaraga Campbell Okello (kushoto) wa timu ya raga ya Umoja Innercore akiwa na mchezaji Andrew Njagi. Picha/ Patrick Kilavuka

Kwa vile alikuwa na ari tangu awali na mapenzi makubwa katika mchezo huu akiwa shule ya msingi, aliamua kulivalia njuga azimio lake na kujiunga na timu ya shule chini ya kocha huyo ambaye kwa sasa amemuamini nafasi katika kikosi cha kwanza na anafanya mambo kweli pasi na shauku.

Chini ya mkufunzi Ambani ambaye anamlea kipaji, anasema anaona atafikia upeo wa kuchezea timu za haiba nchini mfano KCB ambayo moyo wake unamdekadeka kuichezea kabla kuazimia kuyoyomea nchi za Afrika Kusini, Ufiji, Austraila au Unigereza ambako mchezo huu umekita mizizi.

Yeye hufanya mazoezi yake katika awamu tatu. Huanza saa 5.00 -5.30 am kwa kukimbia, 6.00 – 7.00 am mazoezi ya kupasha misuli na viungo na 8.00 – 9.00 am huchukua fursa ya kutizama mazoezi ya kujiweka mufti kwenye youtube na kuona jinsi anavyoweza kuyasawzisha kwenye yake mazoezi.

Kwingineko, huzoa maarifa ya kujinyanyua zaidi kutoka kwa kocha Ambani ambaye pia huchezea timu ya Rhino, Kaunti ya Kakamega.

Hata hivyo, kando na kupiga zoezi shuleni na kucheza, wakati wa likizo, hupata mwanya wa kuyaendeleza makali yake katika timu ya raga ya Umoja Innercore, mtaani Tena jijini Nairobi.

Yeye huhimizika sana kutia wengine motisha katika kukuza mchezo huu na anamnoa mchezaji Stower Otieno.

Anasema humtia mori ya kucheza kwa bidii ya mchwa kudhihirisha kwamba ana uwezo katika mchezo ili, azoe ujuzi, awe ari na kujiepusha na mawazo potovu kwamba, mchezo huu ni mgumu na hatari unapouchezea.

“Mimi humzindua kuzingatia mazoezi na kuendeleza kiu ya kuujua kwani unapopata majereha ni njia moja ya kujiimarisha na changamoto za mchezo,” asema mchezaji Okello.

Amewahi kufunga trai 30 na kwa kila mchezo, anasema yeye hujitahidi ukucha kwa jino kufunga zaidi ya trai moja.

Ana ndoto ya kukaa mkaao na wachezaji miamba kama mwanaraga Injera siku moja kupata mawili matatu ya kimaarifa.

Bonge la ushauri kwa wengineo wanaotaka kuvaa jezi ya raga ni kwamba, mchezo wa raga si mgumu mithili ya mwamba ila, ujuzi, ari na bidii ya mchwa mazoezi ndivyo vigezo muhimu vya kukuwezesha kufaulu!

Wanaraga wa Machine wazidia nguvu Egerton Wasps

Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya raga ya Chuo Kikuu cha Nairobi almaarufu Mean Machine imelipua Egerton Wasps ya Chuo Kikuu cha Egerton 37-0 jijini Nairobi mnamo Jumamosi na kuingia nusu-fainali ya kuwania tiketi ya kupandishwa daraja ya kushiriki Ligi Kuu.

Machine, ambayo ilitemwa kutoka Ligi Kuu (Kenya Cup) misimu kadhaa iliyopita, imetumia Chuo Kikuu cha Masinde Muliro (MMUST) onyo kali kwa kuzamisha Wasps kupitia miguso ya Grevis Onyino, Lawrence Ndung’u, Marvin Karungi na Bruce Odhiambo. Festus Shiasi alichangia penalti moja na mkwaju naye Trevor Asina alifunga penalti nne.

MMUST ilifuzu moja kwa moja kushiriki nusu-fainali ilipomaliza Ligi ya Daraja ya Pili katika nafasi ya pili katika msimu wa kawaida 2019-2020.

Itaaalika Machine mjini Kakamega kwa mechi ya nusu-fainali hapo Februari 13.

Mechi kati ya Machine na Wasps ilikuwa mechi ya kwanza ya raga kufanyika Kenya katika kipindi cha miezi 11 baada ya mkurupuko wa virusi vya corona kukatika shughuli ya msimu uliopita kwa ghafla Machi 2020. Machine ilifurahia uongozi wa alama 19-0 wakati wa mapumziko na haikuwapa Wasps nafasi ya kurudi kwenye mechi hiyo.

Matokeo hayo yanamaanisha kuwa Machine iko pazuri kurejea Kenya Cup muradi ifaulu kunyamazisha MMUST uwanjani mwao Kakamega.

Mshindi wa nusu-fainali hiyo atajikatia tiketi ya kujiunga na Kabras Sugar, KCB, Homeboyz, Impala Saracens, Mwamba, Menengai Oilers, Nakuru, Blak Blad, Kenya Harlequin na Nondescripts kwenye Ligi Kuu. Itakuwa mara ya kwanza kabisa MMUST kushiriki Kenya Cup ikikung’uta mabingwa wa mwaka 1977, 1989 na 1990 Machine.

Bingwa wa nusu-fainali nyingine kati ya Leos ya Chuo Kikuu cha Strathmore na Northern Suburbs pia ataingia Kenya Cup msimu ujao wa 2021. Leos ilishinda msimu wa kawaida wa ligi hiyo ya daraja ya pili kwa hivyo itakuwa mwenyeji wa Suburbs katika uwanja wake wa Madaraka.

KRU yasema vikosi viko tayari kwa Ligi Kuu ya Kenya Cup

Na CHRIS ADUNGO

SHIRIKISHO la Raga la Kenya (KRU) litaanza kutoa msaada wa fedha kwa vikosi vya Ligi Kuu ya Kenya wiki hii kwa nia ya kuwezesha wachezaji kufanyiwa vipimo vya corona kabla ya kipenga cha kuashiria mwanzo wa kampeni za msimu huu kupulizwa mwishoni mwa Februari.

Mwenyekiti wa KRU, Oduor Gangla, amesema fedha hizo zitalenga kuondolea washiriki wa Kenya Cup mzigo mkubwa baada ya hazina zao kuathiriwa na janga la corona ambalo limevuruga kalenda ya michezo mbalimbali duniani.

“Msaada huo wa kifedha utaanza kutolewa kwa vikosi wiki hii ili kufanikisha shughuli ya wanaraga wa Ligi Kuu kufanyiwa vipimo vya Covid-19,” akasema kinara huyo katika mahojiano yake na Taifa Leo.

Kivumbi cha Kenya Cup kimepangiwa kuanza Februari 27 baada ya kurejelewa kwa raga kuidhinishwa na Wizara ya Michezo.

Kuanza kwa ligi hiyo kutatanguliwa na mchujo wa kubaini vikosi vitakavyopanda ngazi kushiriki Ligi Kuu ya Kenya Cup kutoka klabu za daraja la chini (Championship).

Mean Machine ya Chuo Kikuu cha Nairobi itawaalika Wasps wa Chuo Kikuu cha Egerton wikendi hii ambapo mshindi atafuzu kuvaana na Chuo Kikuu cha Masinde Muliro kwenye nusu-fainali ya Februari 13.

USIU-A watakutana na Northern Suburbs na mshindi atajikatia tiketi ya kumenyana na Strathmore Leos kwenye nusu-fainali nyingine.

Washindi wa nusu-fainali hizo mbili watajaza nafasi za Western Bulls na Kisumu RFC walioshushwa ngazi kwenye Kenya Cup mwishoni mwa msimu wa 2019-20.

Mechi za ligi zitakuwa za mkondo mmoja pekee msimu huu na zitachezwa kwa kipindi cha wiki 11 ambapo vikosi vinne vya kwanza vitafuzu kwa nusu-fainali ambazo zimeratibiwa kupigwa Mei 22 kabla ya fainali kufuata wiki moja baadaye.

Katika siku ya kwanza ya kampeni za Kenya Cup msimu huu, Impala watavaana na Kenya Harlequins, Homeboyz wapepetana na Nondies nao Mwamba washuke ugani kukwaruzana na Blak Blad. Oilers watakuwa wenyeji wa Nakuru RFC.

Gangla amesema pia KRU itafichua kocha mpya atakayedhibiti mikoba ya timu ya taifa ya wanaraga chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20 wiki hii kabla ya kuanza shughuli ya kuteua kikosi kitakachowakilisha Kenya kwenye Raga ya Afrika kwa chipukizi almaarufu Barthes Cup.

Kenya ambayo imetiwa kwenye zizi moja na Zambia, Tunisia na Bukini, itakuwa mwenyeji wa kipute hicho 20 kuanzia Machi 25 hadi Aprili 4 jijini Nairobi.

Mshindi wa kivumbi hicho atafuzu kwa mapambano ya kuwania taji la dunia kwa chipukizi almaarufu Junior Rugby World Trophy kuanzia Septemba katika taifa litakalofichuliwa na Shirikisho la Raga la Dunia (WA) mwishoni mwa mwezi huu.

Chini ya mkufunzi Paul Odera, wanaraga chipukizi wa Kenya almaarufu Chipu, walitawazwa mabingwa wa kivumbi cha Barthes Cup mnamo 2019 baada ya kuwapokeza Namibia kichapo cha 21-18 kwenye fainali iliyoandaliwa jijini Nairobi.

Ushindi huo wa Chipu uliwakatia tiketi ya kunogesha Junior Rugby World Trophy nchini Brazil na wakaambulia nafasi ya tano mwishowe. Walipepeta wenyeji Brazil 26-24, wakapokezwa na Uruguay kichapo cha 63-11 na kucharazwa na 48-34 na Japan walioibuka kileleni mwa kundi.

Odera kwa sasa anadhibiti mikoba ya timu ya taifa ya wanaraga 15 kila upande, Kenya Simbas na nafasi aliyoicha kambini mwa Chipu inatazamiwa kutwaliwa na mkufunzi Paul Murunga.

Kati ya wachezaji waliopeperusha bendera ya Kenya kwenye kampeni za Barthes Cup miaka miwili iliyopita, ni wanaraga wanne pekee ambao wana uwezo wa kuwania nafasi ya kuwakilisha taifa kwa mara nyingine katika makala ya mwaka huu. Hao ni Mureithi Mwiti, Owain Ashley, Lorence Ishuga na George Kiriazi.

Ili kuweka hai matumaini ya kutwaa ubingwa wa Barthes Cup, KRU imethibitisha kuajiri wakufunzi wawili raia wa Afrika Kusini – Neil De Kock ambaye ni kocha wa zamani wa timu ya taifa ya Afrika Kusini almaarufu ‘Springbok’ na Ernst Joubert ambaye ni nahodha wa zamani wa kikosi cha Saracens ili kupiga jeki juhudi za atakayekuwa kocha mpya wa Chipu.

Homeboyz wakiri ni pigo kwao kupoteza wanaraga wanne

AYUMBA AYODI na GEOFFREY ANENE

Klabu ya raga ya Homeboyz huenda imetikiswa na kuondoka kwa wachezaji wanne na kukosa kurejea kwa kocha, lakini hawajakufa matumaini wanapojiandaa kwa msimu mpya.

‘Madeejay’ hao wamepoteza washambuliaji tegemeo Joshua Chisanga, Emmanuel Mavala na Philip Ikambili na mpigaji wa kiki Evin Asena, ambao wote wamejiunga na Kenya Harlequin.

Kuharibu mambo zaidi kocha wao kutoka Afrika Kusini Jason Hector hajarejea nchini tangu Kenya itangaze kufunga mipaka yake mwezi Machi 2020 kuzuia maambukizi ya virusi vya corona. Tetesi zinasema Hector amepata kazi nchini mwake.

Mwenyekiti wa Homeboyz Mike Rabar na kocha Simon Odongo wanaamini kuwa wachezaji waliobaki wana uwezo wa kujituma kiasi cha kuzua ushindani.

“Tuna kundi la wachezaji karibu 200 na nadhani pia hii ni fursa ya chipukizi kujionyesha,” alisema Rabar na kuongeza kuwa Homeboyz ilicheza mechi sita za mwisho za msimu 2019-2020 bila nyota hao ambao wamehamia Quins.

Homeboyz ilikamilisha msimu wa kawaida katika nafasi ya tatu kwa alama 66 kabla ya mkurupuko wa virusi vya corona kusababisha awamu ya muondoano kusimamishwa kwa ghafla. Mshindi hakupatikana msimu huo kwa sababu mechi za muondoano zilifutiliwa mbali.

Msimu mpya wa Ligi Kuu ya Kenya Cup unafaa kuanza Februari 27, lakini Rabar alitilia shaka tarehe hiyo akisema serikali bado haijaidhinisha mazoezi ya kugusana yaanze.

“Timu nyingi zinaendesha mazoezi ya wachezaji kufanya mazoezi kivyao ambayo yanajumuisha mazoezi ya viungo vya mwili na yale yanayofanywa kwenye chumba cha mazoezi,” alisema Rabar akidokeza kuwa bado wanahitaji huduma za Hector.

“Bila shaka, tumetikiswa hasa baada ya kupoteza wachezaji hao muhimu. Itaturudisha hatua kadhaa nyuma, lakini tutainuka tukiwa na nguvu zaidi,” alisema Odongo na kuongeza kuwa changamoto itakuwa jinsi wachezaji waliobaki wataongeza juhudi zao.

Odongo alisema kuwa mikakati iliyofanywa na Hector bado ina nguvu na itaendelea kutumika. “Tunafaa kuendelea na mahali tulipoacha msimu uliopita bila tatizo. Tutalenga kudhibiti chombo chetu jinsi ilivyokuwa msimu uliopita na kufika nusu-fainali.”

Homeboyz wamesajili mchezaji mmoja pekee ambaye ni Ochieng kutoka Nondescripts, lakini Odongo ametupia jicho kupandisha daraja wachezaji kutoka timu ya Homeboyz inayoshiriki kipute cha Eric Shirley Shield.

Chipukizi hao ni wachezaji wa timu ya taifa ya Under-20 Arnold Onyere na Ronald Ngaira na winga Pius Odera kutoka Shule ya Upili ya Upper Hill.

Odongo alikiri Homeboyz imekuwa ikipitia changamoto ya wachezaji kadhaa kukosekana kwa sababu si wachezaji wote wamerejelea mazoezi. “Wachezaji wengine waliamua kujiingiza katika shughuli nyingine wakati michezo ilipigwa marufuku. Huwezi kuwaita warejee bila mpango, hasa kwa sababu hakuna mwelekeo mzuri kuhusu masharti ya kudhibiti virusi vya corona,” alisema Odongo akiongeza kuwa fedha zitakiwa mzigo Mkubwa.

Shujaa waalikwa kucheza Uhispania na Ufaransa kabla ya msimu ujao wa Raga ya Dunia

Na CHRIS ADUNGO

TIMU ya taifa ya wanaraga saba kila upande almaarufu Shujaa, imepata mwaliko wa kucheza nchini Uhispania na Ufaransa mnamo Februari 2021, mwezi mmoja kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa kampeni za duru ya Raga ya Dunia.

Mwenyekiti wa Shirikisho la Raga la Kenya (KRU), Oduor Gangla amethibitisha kwamba wamepata mialiko hiyo kutoka Uhispania na Ufaransa na ameeleza matumaini kwamba vipute hivyo vitakuwa sehemu muhimu ya maandalizi ya Shujaa kwa muhula mpya.

“Mashindano ambayo tumealikwa kushiriki katika mataifa hayo yatapiga jeki maandalizi ya Shujaa kwa minajili ya Raga ya Dunia ya wachezaji saba kila upande na michezo ya Olimpiki ya Tokyo, Japan mnamo Julai 2021,” akasema Gangla.

Mbali na Kenya, vikosi vingine ambavyo vimealikwa kuchuana nchini Uhispania na Ufaransa ni New Zealand, Afrika Kusini, Australia, Fiji na Samoa.

Kwa mujibu wa Gangla, washindani wa Shujaa katika vipute vya Raga ya Dunia na Olimpiki wamekuwa wakiendelea na mazoezi pamoja na kushiriki mapambano mengine muhimu – jambo ambalo timu ya taifa inafaa pia kuanza kufanya.

“Hatuwezi kuendelea kukaa na kusubiri kwa sababu tuko nyuma ya ratiba. Washindani wetu wanafanya mazoezi na kushiriki mashindano mbalimbali katika mataifa yao,” akahoji Gangla.

Chini ya kocha mkuu, Innocent Simiyu, wanaraga wa Shujaa walifanyiwa vipimo vya corona wiki mbili zilizopita na wanatarajiwa sasa kuingia kambini kwa minajili ya kampeni za msimu ujao.

Kwa mujibu wa Gangla, kampeni za msimu mpya wa Ligi Kuu ya Kenya Cup zimeratibiwa kuanza rasmi mnamo Januari 16, hatua inayowapa vikosi muda wa kati ya wiki sita na nane kujiandaa.

Mnamo Novemba 12, 2020, KRU ilitaja kikosi cha wanaraga 29 ambao kwa sasa wataingia kambini kwa minajili ya kampeni za msimu ujao wa 2020-21 za kikosi cha Shujaa.

Mbali na ukaguzi wa kawaida utakaolenga kubaini hali zao za afya na uwezo wa miili kuhimili mazoezi makali, wanaraga wote hao walifanyiwa vipimo vya corona katika uwanja wa RFUEA, Nairobi kwa mujibu wa kanuni za mpya za serikali katika juhudi za kudhibiti msambao wa Covid-19.

Kati ya wanaraga ambao watategemewa na kocha Simiyu katika kampeni zijazo za Shujaa ni nahodha Andrew Amonde, kigogo Collins Injera anayeshikilia rekodi ya ufungaji wa idadi kubwa zaidi ya trai, Oscar Ouma, Willy Ambaka na Oscar Dennis.

Watano hao walikuwa sehemu ya kikosi cha SFX10 cha Afrika Kusini kilichonogesha kivumbi cha dunia cha wanaraga 10 kila upande cha IPL World 10’s nchini Bermuda majuzi.

Shirikisho la Raga Duniani (WR) tayari limefutilia mbali duru nne za kwanza za za Dubai, Cape Town, Sydney na Hamilton katika kampeni za Raga ya Dunia msimu ujao wa 2020-21.

Ina maana kwamba kipute cha Raga ya Dunia katika msimu wa 2020-21 kinaweza tu kung’oa nanga mnamo Machi 2021 kwa duru za Los Angeles (Amerika) na Vancouver (Canada).

Mbali na raga ya wachezaji saba kila kwa upande wa wanaume, Kenya itawakilishwa kwenye fani mbalimbali katika Olimpiki za Tokyo, Japan zikiwemo mbio za marathon, voliboli (wanawake), ndondi na taekwondo (wanawake na wanaume) na kupiga mbizi au uogeleaji (wanawake na wanaume).

“Nitategemea wanaraga waliopo kwa sasa katika orodha hii ya wachezaji wa Shujaa kabla ya kuwaweka kwenye mizani kwa mujibu wa viwango tunavyovihitaji. Tutaongeza orodha hiyo baadaye kwa kuleta wanaraga wapya kwa kuwa baadhi ya wachezaji tulionao kikosini wana mikataba inayoelekea kutamatika,” akasema Simiyu.

Simiyu, 37, aliteuliwa upya na Shirikisho la Raga la Kenya (KRU) mwanzoni mwa Septemba 2020 kunoa timu ya taifa baada ya Paul Feeney wa New Zealand kugura mwezi Juni.

KIKOSI CHA SHUJAA:

Andrew Amonde, Vincent Onyala, Jacob Ojee, Geoffrey Okwach, Johnstone Olindi, Levy Amunga (KCB); Collins Injera, Billy Odhiambo, Daniel Taabu, Tony Omondi, Mike Okello (Mwamba); Sammy Oliech, Alvin Marube (Impala); Willy Ambaka, Herman Humwa, Eden Agero (Harlequins), Oscar Ouma, Nelson Oyoo (Homeboyz); Jeffrey Oluoch, Bush Mwale, Alvin Otieno (Nakuru); Harold Anduvate, Derrick Keyoga, Mark Kwemoi (Oilers); Daniel Sikuta, Brian Tanga (Kabras); Oscar Dennis, Dennis Ombachi (Nondescripts); Archadius Khwesa (Blak Blad).

KRU kuandaa mchujo kwa ajili ya vikosi vya raga kupanda na kushuka ngazi katika ligi za chini

Na CHRIS ADUNGO

SHIRIKISHO la Raga la Kenya (KRU) limethibitisha kwamba kutaandaliwa mchujo wa ligi za madaraja ya chini ya Championship na Nationwide ili kuamua vikosi vitakavyopanda na kushuka ngazi kwa minajili ya msimu mpya wa 2020-21.

Boadi ya KRU pia imethibitisha kuwa hapatakuwepo mshindi wa Ligi Kuu ya Kenya Cup wala ligi zote nyinginezo za chini katika msimu wa 2019-20 uliotamatishwa ghafla kutokana na ugonjwa wa Covid-19.

Hali ya Kisumu RFC na Western Bulls, waliokuwa wameshushwa ngazi kwenye Kenya Cup; pamoja na Kisii RFC na Mombasa RFC waliokuwa wameteremshwa ngazi kwenye Championship itasalia vivyo hivyo kwa sababu kampeni zao zilikuwa zimetamatika kabla ya ujio wa corona.

“Kwa mujibu wa sheria za KRU, haitawezekana kwa mshindi wa ligi yoyote kupatikana bila ya mechi za mchujo kuandaliwa. Hivyo, matokeo yaliyokuwa yamesajiliwa hadi wakati wa kutamatishwa kwa kampeni za 2019-20 yatasalia jinsi yalivyo,” akasema Katibu wa KRU, Ian Mugambi.

“Hata hivyo, vikosi vilivyokuwa vimeteremshwa ngazi vitasalia kushuka daraja kwa kuwa mechi zao zilikuwa zimekamilika. Mchujo sasa utaandaliwa ili kuamua timu zitakazopanda na kushuka ngazi kwenye Championship na Nationwide,” akaongeza kinara huyo.

Kwa mujibu wa KRU, muhula wa uhamisho wa wanaraga kwa minajili ya msimu ujao utafunguliwa rasmi kuanzia Oktoba 7 hadi Novemba 30. Hata hivyo, ni wanaraga waliokuwa sehemu ya vikosi vyao katika kampeni za 2019-20 ndio wataruhusiwa kushiriki mchujo.

Vikosi vya raga ya Ligi Kuu ya Kenya Cup vimetaka waliokuwa washiriki wote wa kivumbi cha msimu uliofutiliwa mbali wa 2019-20 kusalia vivyo hivyo katika muhula ujao wa 2020-21.

“Tumependekeza kwamba vikosi vilivyonogesha kampeni za msimu jana visalie jinsi vilivyokuwa kwa minajili ya muhula mpya ujao,” akasema Xavier Makuba ambaye ni mwenyekiti wa vikosi vya Kenya Cup.

Hatua hiyo ni pigo kwa Mean Machine, Chuo Kikuu cha Masinde Muliro, Chuo Kikuu cha USIU, Northern Suburbs na Strathmore Leos ambao hadi kufutiliwa mbali kwa msimu huu, walikuwa wamefuzu kwa mchujo wa Championship wakilenga kujaza nafasi mbili katika Ligi ya Kuu ya Kenya Cup.

Kwa mujibu wa Makuba, vikosi vitakavyosalia kwenye Kenya Cup katika msimu mpya wa 2020-21 ni Kabras, Homeboyz, Impala Saracens, Mwamba, Menengai Oilers, Nakuru RFC, Nondies, Kenya Harlequins, Blak Blad na mabingwa wa 2018-19, KCB.

Japo Makuba amependekeza msimu mpya wa raga uanze Novemba, mkufunzi Mitch Ocholla wa Impala Saracens, ametaka msimu wa 2020-21 uanze Januari mwaka ujao.

“Zipo taratibu nyingine zinazohitaji kutimizwa ili Wizara ya Afya ikubalie michezo kurejelewa. Mojawapo ni kufanyia wanaraga, marefa na maafisa wote wa benchi za kiufundi wa kila klabu vipimo vya corona.”

“Hili ni zoezi ghali mno kutekeleza. Vyema tusubiri zaidi makali ya corona yapungue kabisa ndipo raga irejee kwa vishindo,” akasema Ocholla aliyewahi pia kunoa timu ya taifa ya Shujaa mnamo 2011-12.

Vikosi vya Kenya Cup vyafutilia mbali mpango wa kukamilisha msimu wa 2019-20

Na CHRIS ADUNGO

KLABU za raga ya humu nchini zimefutilia mbali mpango wa kukamilishwa kwa kampeni za msimu wa 2019-20 katika Ligi Kuu ya Kenya Cup na Ligi ya Daraja la Kwanza (Championship).

Awali, vikosi hivyo vilishikilia msimamo wa kurejelewa kwa mapambano yote yaliyositishwa kutokana na janga la corona kabla ya msimu mpya wa 2020-21 kung’oa nanga.

Mwenyekiti wa mashindano hayo, Xavier Makuba, sasa amesema klabu za Kenya Cup na Championship zimetupilia mbali mpango huo na zinasubiri utaratibu utakaotolewa na Wizara ya Michezo kabla ya kuanza kinyang’anyiro cha muhula ujao.

“Hatuna muda kabisa. Tumefika Septemba tayari. Taratibu zinatuhitaji kufanyia wachezaji, marefa na maafisa wote wa benchi za kiufundi wa klabu za Kenya Cup na Championship vipimo vya corona,” akatanguliza.

“Hilo ni jambo litakalowanyima wanaraga fursa ya kujifua kwa wiki kadhaa kabla ya msimu mpya kuanza. Imebidi tufutilie mbali mipango yote ya awali na kuelekeza macho kwa msimu mpya ambao tunatazamia kuanza Novemba,” akasema Makuba.

Ungamo la Makuba linamaanisha kwamba hapatakuwepo na mshindi wa Kenya Cup wala Championship katika msimu wa 2019-20. Aidha, hakuna kikosi kitakachopandishwa ngazi wala kuteremshwa daraja kutokana na matokeo ya 2019-20.

Mnamo Juni, Shirikisho la Raga la Kenya (KRU) lilifutilia mbali msimu mzima wa raga ya humu nchini katika hatua iliyoathiri vipute vyote vya Championship, ligi pana za kitaifa, ligi za madaraja ya chini, Enterprise Cup, Great Rift Valley Cup, Mwamba Cup na National Cirucit.

Hata hivyo, KRU ilipiga abautani mwezi mmoja baadaye na kuunda kamati ya watu sita waliopendekeza kurejelewa kwa kampeni za 2019-20 kabla ya muhula mpya kuanza.

Kamati hiyo ilijumuisha Hillary Itela (mkurugenzi wa ratiba za mechi katika KRU), Moses Ndale na Peris Mukoko (wanachama wa Bodi ya KRU), Makuba (KCB), Philip Jalango (Kabras Sugar) na George Mbaye (Mwamba RFC).

Kwa mujibu wa Oduor Gangla ambaye ni mwenyekiti wa KRU, shirikisho kwa sasa linatayarisha ripoti itakayowasilishwa kwa serikali ikitoa mwongozo kuhusu jinsi ya kurejelewa kwa raga ya humu nchini baada ya kutalii hali mbalimbali.

“KRU itafichua wiki ijayo ratiba ya kujifua kwa timu ya taifa ya raga ya wachezaji saba kila upande, Shujaa, kwa minajili ya Olimpiki zijazo jijini Tokyo, Japan na mechi za kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia mnamo 2022 jijini Cape Town, Afrika Kusini,” akasema Gangla.

Hadi kusitishwa kwa shughuli zote za michezo humu nchini mnamo Machi 2020, pambano la Enterprise Cup ambalo ndilo kongwe zaidi katika historia ya raga ya Kenya, lilikuwa limetinga hatua ya nusu-fainali.

Mabingwa watetezi Kabras Sugar walikuwa wavaane na Homeboyz huku wanabenki wa KCB wakimenyana na Impala Saracens.

Katika Kenya Cup, Homeboyz walitarajiwa kuchuana na Menengai Oilers ambapo mshindi angejikatia tiketi ya kukabiliana na mabingwa watetezi, KCB kwenye nusu-fainali ya Kenya Cup.

Kabras walitazamiwa kupimana ubabe na mshindi kati ya Impala na Mwamba RFC. Hadi kipute cha Kenya Cup kilipofutiliwa mbali, Kabras RFC walikuwa ikiselelea kileleni kwa alama 74, tatu zaidi mbele ya KCB.

Kwa upande wa KRU Championship, Strathmore Leos waliokuwa hawajapoteza mechi yoyote, walikuwa wakiongoza jedwali kwa alama 76, tisa zaidi kuliko Chuo Kikuu cha Masinde Muliro (MMUST) katika nafasi ya pili.

Leos walikuwa wakutane na mshindi kati ya Northern Suburbs na Chuo Kikuu cha USIU-A katika mojawapo ya nusu-fainali huku MMUST wakipimana ubabe na mshindi kati ya Mean Machine ya Chuo Kikuu cha Nairobi na Egerton Wasps.

Mikoba ya Shujaa yavutia makocha 11 wa kigeni na watatu wa humu nchini

Na CHRIS ADUNGO

JUMLA ya makocha 14 kutoka ughaibuni na humu nchini wamewasilisha maombi ya kupokezwa fursa ya kudhibiti mikoba ya timu ya taifa ya wanaraga saba kila upande, Shujaa.

Kati ya 14 hao, 11 ni raia wa kigeni hasa kutoka mataifa ya New Zealand, Australia, Afrika Kusini na Uingereza. Wote hao wanawania nafasi ya kurithi mikoba iliyoachwa na Paul Feeney – raia wa New Zealand aliyeagana rasmi na Shirikisho la Raga la Kenya (KRU) mnamo Mei 2020.

Japo mchakato wa kutafuta mrithi wa Feeney ulianzishwa na KRU mwezi Juni, shirikisho lilitangaza upya nafasi hiyo ya kazi mnamo Julai baada ya makocha watatu pekee wa humu nchini kuwasilisha maombi.

Lengo lilikuwa ni kutoa fursa kwa wakufunzi wa kigeni kutuma maombi yao ya kazi.

KRU inasaka kocha atakayetambisha wanaraga wa Shujaa kwenye Michezo ya Olimpiki itakayoandaliwa jijini Tokyo, Japan mwakani.

“Tunatafuta kocha kutoka nchi yoyote aliye na tajriba ya kudhibiti mikoba ya kikosi cha haiba kubwa kwa zaidi ya miaka mitatu. Awe amehitimu kiwango cha pili cha ukufunzi (Rugby Level 2 Certificate) katika kikosi cha wanaraga saba au 15 kwa mujibu wa viwango vya Raga ya Dunia,” ikasema taarifa ya KRU.

Thomas Odundo ambaye ni mkurugenzi wa raga wa KRU amethibitisha kwamba waliotuma maombi bado wanahojiwa na orodha fupi ya mwisho itafichuliwa wiki ijayo kabla ya kocha mpya kutambulishwa rasmi kwa kikosi na mashabiki kufikia mwisho wa wiki ya pili ya mwezi Agosti.

“Nia imekuwa kutoa fursa kwa kila mtu. Tunapania kupata kocha bora zaidi ambaye tajriba yake itafufua makali ya Shujaa, kurejesha uthabiti wa kikosi na kukifanya kiwe tishio kwa wapinzani wengine katika majukwaa ya  kimataifa kadri atakavyokuwa akikisuka kwa msimu ujao,” akasema Odundo kwa kusisitiza kwamba huenda wakalazimika kufutilia mbali kampeni za raga ya Ligi Kuu ya Kenya Cup msimu huu wa 2019-20 kwa sababu ya janga la corona.

Kenya imejivunia idadi kubwa ya wakufunzi wa raga katika kipindi cha miaka 10 iliyopita ambayo imeshuhudia mikoba ya Shujaa ikidhibitiwa na wakufunzi Mitch Ocholla, Mike Friday wa Amerika, Paul Treu wa Afrika Kusini, Felix Ochieng, Innocent Simiyu na Paul Murunga.

Kocha mpya wa Shujaa anatarajiwa kuanza kazi mnamo Oktoba 2020 kwa kibarua cha kuongoza Kenya kuwa mwenyeji wa kipute cha kimataifa cha Safari Sevens.

Feeney ambaye alikuwa kocha wa nne wa kigeni kuwahi kudhibiti mikoba ya Shujaa, alirejea kwao New Zealand baada ya kuongoza timu ya taifa kutia kibindoni ubingwa wa Raga ya Afrika jijini Johanesburg, Afrika Kusini. Ushindi huo uliwakatia Shujaa tiketi ya kufuzu kushiriki makala yajayo ya 32 ya Michezo ya Olimpiki.

Feeney aliyewahi kudhibiti mikoba ya timu ya taifa ya Fiji mnamo 2015, pia aliiongoza Kenya Morans kutinga fainali ya Tusker Safari Sevens mnamo 2019.

Chini yake, Shujaa walikamilisha kampeni za Raga ya Dunia muhula huu katika nafasi ya 12 katika orodha ya timu 17 baada ya msimu wote kufutiliwa mbali kwa sababu ya ugonjwa wa Covid-19 zikiwa zimesalia duru nne za London, Paris, Singapore na Hong Kong.

New Zealand walitawazwa mabingwa wa Raga ya Dunia msimu huu wa 2019-20 kwa pointi 115. Kenya ilijizolea jumla ya alama 35 ya kutinga robo-fainali za Main Cup mara mbili jijini Cape Town na Hamilton.

Shirikisho la Raga la Dunia (WR) limethibitisha pia kufutilia duru mbili za kwanza za Dubai na Cape Town katika Raga ya Dunia ya 7’s msimu ujao wa 2020-21.

AFUENI: Wachezaji wawili wa raga kusimama kizimbani tena

Na RICHARD MUNGUTI

WACHEZAJI wawili maarufu wa mchezo wa raga waliohukumiwa kifungo cha miaka 15 jela kwa kosa la ubakaji Jumanne walipata afueni Mahakama Kuu ilipofutilia mbali adhabu hiyo na kuamuru kesi ifanywe upya.

Jaji Grace Ngenye Macharia aliyesikiza rufaa ya Alex Olaba, 24 na Frank Wanyama, 23 aliamuru kesi hiyo isikizwe upya ndipo korti irekebishe kasoro zilizofanywa na upande wa mashtaka.

Sasa Olaba na Wanyana wataachiliwa kutoka gerezani walikokuwa wameanza kutumikia vifungo warudi nyumbani.

Ijapokuwa watafunguliwa mashtaka upya na kiongozi wa mashtaka Everlyne Onungo kuwaita mashahidi upya, wawili hao wataomba korti iwaachilie kwa dhamana wafanye kesi kutoka nje.

Wawili hao walikuwa wamekata rufaa kupinga hukumu dhidi yao wakidai hawakutendewa haki.

Walikuwa wameshtakiwa kumbaka mwanamke mnamo 2018 na walihukumiwa mnamo Agosti 16, 2019, na Bi Mutuku.

Hakimu huyo aliwapata na hatia ya kumbaka mwanamke huyo kwa zamu.

Akinukuu kifungu Nambari 10 ya Sheria za Ubakaji za mwaka wa 2006 hakimu alisema mmoja anayepatikana na hatia chini ya kifungu hiki cha sheria ataadhibiwa kwa kufungwa jela miaka 15.

Akipitisha adhabu, Bi Mutuku alisema ushahidi uliowasilishwa na kiongozi wa mashtaka Bi Onungo ni kwamba wawili hao walimbaka mwanamke huyo ambaye ni mwanamuziki katika makazi ya Seefar Apartments katika mtaa wa Nyayo Highrise.

Mawakili  waliowatetea wafungwa hao walimweleza Jaji Macharia sheria haikufuatwa ipasavyo wakati wa kusikizwa kwa kesi na pia wakati wa kupitisha hukumu.

“Baada ya kusikiza mawasilisho ya wafungwa hawa wawili, nakubaliana nao kwamba sheria haikufuatwa ipasavyo na kesi hii inastahili kusikizwa upya mbele ya hakimu mwingine, sio Bi Mutuku,” aliamuru Jaji Macharia.

Siku ya kusikizwa kwa kesi hiyo haijatengwa.

Rufaa hiyo ilisikizwa kwa njia ya mtandao wa Zoom.

Wakijitetea kabla ya kuhukumiwa washtakiwa walimweleza  hakimu kwamba wao na mlalamishi walikuwa wamelewa chakari na hakuna aliyekuwa anaweza kujidhibiti.

Walijitetea kwamba mlalamishi aliyekuwa na umri wa miaka 24 aliamua kulala katika makazi yao na baadaye akajaribu kudai apewe pesa ndipo awaondolee lawama na kufutilia mbali kesi hiyo ya ubakaji.

Wachezaji hao wa kimataifa wa Raga walikataa kutoa pesa.

Walikamatwa na kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Spring Valley.

Akitoa ushahidi kortini mlalamishi alisema yeye ni mwanamuziki na alishawishiwa na washtakiwa kuandamana nao hadi makazi yao.

Alidai wawili hao walimbaka kwa zamu.

Mawakili walieleza mahakama mmoja wachezaji hao alikuwa mwanafunzi katika chuo kikuu cha Strathmore na tayari alikuwa amepokea msaada wa masomo kujiunga na chuo kikuu cha Canada ilhali mwenzake alikuwa ametia sahihi kandarasi ya kuchezea klabu.

Wote wawili walikuwa wanachezea timu ya raga ya taifa ya Shujaa.

Olaba na Wanyama walianza kuchezea timu ya Raga ya Chuo Kikuu cha Strathmore maarufu kama Strathmore Leos kabla ya kujiunga na Kenya Harlequins.

Msiingize siasa katika timu zenu za taifa za raga, kocha Ben Ryan ashauri Kenya

Na GEOFFREY ANENE

WANARAGA wa Kenya walinufaika na mafunzo kutoka kwa kocha mtajika Benjamin Ryan kuhusu mbinu inazostahili kutumia kupata matokeo mazuri zikiwemo kutoingiza siasa kikosini, kuwa na maadili mema, kujiamini, kuwa na mtazamo bora na tabia inayokubalika na timu.

Kocha huyo Mwingereza, ambaye aliongoza timu ya wanaume ya Fiji kutwaa medali ya raga ya wachezaji saba kila upande kwenye Olimpiki 2016, alisema pia ni muhimu wachezaji wafanye wanachoweza kwa kuweka mipango kabambe, kujitolea pamoja na kudumisha uhusiano mwema na wachezaji wazoefu na makocha ili waweze kuendelea kupata matokeo mazuri.

“Umoja na uelewano kikosini ni vitu muhimu sana katika utafutaji wa matokeo mazuri katika viwango vya juu,” alisema mshindi huyo wa taji la Raga ya Dunia ya msimu 2014-2015 alilopata pia na Fiji.

Kama kocha, Ryan anasema, ana uhusiano mzuri na viongozi na anatumia mfumo rahisi kuhusu kinachostahili kufanywa. “Tunaweka viwango rahisi, kila mtu anafahamu kinachoendelea, hakuna siasa katika kundi letu la wachezaji ama benchi ya kiufundi,” anasema.

“Elewa wachezaji wako, fahamu kinachowachochea, kinachowapa motisha, punguza wasiwasi wao na mara kwa mara wapatie majibu wanapostahili kuimarika na kumbuka kuwapongeza wanapofanya vyema. Hakikisha unazungumza nao kila mara ili wajisikie salama,” Ryan alishauri katika warsha hiyo iliyofanyika Ijumaa usiku kupitia kwa mtandao.

Hofu ya Shujaa baada ya raga ya Afrika kufutiliwa mbali

Na CHRIS ADUNGO

KOCHA wa timu ya taifa ya wanaraga saba kila upande, Kevin Wambua, amesema kwamba kufutiliwa mbali kwa msimu wa Raga ya Afrika ni pigo kubwa kwa kikosi chake ambacho hutegemea mapambano ya humu barani kuwaweka wachezaji wake kwenye mizani.

Shujaa ambao ni mabingwa wa bara la Afrika, sasa hawatatetea ufalme wao waliojinyakulia jijini Johannesburg, Afrika Kusini mwaka 2019 baada ya fainali za mwaka 2020 kutupwa kutokana na janga la corona.

Wambua wanaraga wake sasa watakosa fursa ya kupimana ubabe na miamba wenzao kutoka humu barani.

“Ni fursa ambayo tutaikosa kwa sababu tumekuwa tukitumia mashindano hayo kuwapa wanaraga wetu chipukizi majukwaa ya kujipima uwezo katika ulingo wa kimataifa.”

Ingawa hivyo, Shujaa watapata fursa ya kunogesha duru nne za mwisho za Raga ya Dunia msimu huu jijini London na Paris mnamo Septemba kabla ya kutua Singapore na Hong Kong mnamo Oktoba, 2020.

Wambua amewataka wakufunzi wa klabu za raga za humu nchini kubuni mikakati kabambe itakayowapa wachezaji wao fursa maridhawa za kujifua vilivyo wakati huu wa ugonjwa wa Covid-19.

“Ipo haja kwa makocha wa klabu za Kenya Cup na Championship kufikiria uwezekano wa kubuni mbinu mpya za kuwashughulisha wachezaji kimazoezi ili wasiwe wamepoteza fomu wakati wa kurejelewa kwa mashindano. Hili litawaepushia pia wanaraga majeraha mabaya ya mara kwa mara ambayo huenda yakagharimu kabisa taaluma zao,” akasisitiza.

Chini ya kocha Felix Oloo, kikosi cha taifa cha wanaraga wa kike, Kenya Lionesses pia walikuwa wameratibiwa kuvaana na Colombia katika juhudi za kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia.

Wanaraga wa 7’s walikuwa wamepangwa kushiriki pia mchujo wa kufuzu kwa Raga ya Dunia nchini Afrika Kusini kabla ya kunogesha duru ya Langford Sevens nchini Canada.

Simbas kutumia kipute cha raga ya Afrika kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia

Na CHRIS ADUNGO

KIPUTE cha kuwania Raga ya Kombe la Afrika mnamo 2022 sasa kitatumiwa na Kenya Simbas kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia mnamo 2023 nchini Ufaransa.

Kivumbi cha Africa Cup hakijafanyika kwa kipindi cha misimu miwili iliyopita kutokana na uchechefu wa fedha na janga la corona mtawalia. Kampeni hizo zitarejelewa mwakani.

Mshindi wa Africa Cup atajikatia tiketi ya moja kwa moja ya kuingia fainali za Kombe la Dunia huku nambari mbili akilazimika kushiriki mchujo dhidi ya vikosi vingine vitatu kutoka mashirikisho tofauti.

Timu 12 tayari zimefuzu kwa fainali za 2023 nchini Ufaransa baada ya kukamata nafasi tatu za kwanza kwenye kampeni zao za Raga ya Dunia (RWC) katika msimu wa 2019. Hizi ni pamoja na Afrika, Uingereza, New Zealand, Wales, Japan, wenyeji Ufaransa, Australia, Ireland, Scotland, Italia, Argentina na Fiji.

Nafasi nane zilizosalia zitaamuliwa kupitia mchakato wa timu kushiriki mapambano ya mchujo katika kiwango cha kimaeneo. Shughuli hiyo itakamilika kwa mchujo wa mwisho utakaoshirikisha timu nne za mwisho mnamo Novemba 2022. Tarehe za kuandaliwa kwa mashindano ya msimu wa 2021 zitatolewa mapema wiki ijayo.

Kenya Simbas walikosa tiketi ya kunogesha fainali za Kombe la Dunia mnamo 2019 baada ya kuzidiwa maarifa na Canada kwenye mchujo wa mwisho uliotawaliwa na Ujerumani na Hong Kong nchini Ufaransa.

Chini ya kocha Paul Odera, Kenya Simbas watakuwa wakiwania fursa ya kushiriki fainali za Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza katika historia.

Mnamo 2018, Simbas waliambulia nafasi ya pili barani Afrika baada ya kuwapepeta Uganda, Tunisia na Zimbabwe kabla ya chombo chao kuzamishwa na Namibia jijini Windhoek.

Mnamo 2015, walikosa padogo kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia nchini Uingereza baada ya Zimbabwe kuwazaba 27-10.

Awali, Kenya ilikuwa imewapiga wenyeji Madagascar 34-0 na Namibia ambao hatimaye waliwakilisha bara la Afrika kwa 29-22 katika hatua ya makundi.

Odera amesema kutoandaliwa kwa Kombe la Afrika katika kipindi cha miaka miwili mfululizo ni pigo kubwa kwa maandalizi ya kikosi chake ambacho sasa hakitashiriki mapambano yoyote ya haiba kubwa mwaka huu.

“Yasikitisha kwamba tutakuwa na mwaka mmoja pekee wa kujiandaa kwa mechi za kufuzu kwa Kombe la Dunia. Ingawa jambo hili linatuweka katika hali ngumu, naamini ukubwa wa uwezo wa vijana wangu” akasema.

Mechi za Simbas katika Kombe la Afrika zilitarajiwa kuanza dhidi ya Morocco kisha Ivory Coast, Uganda na Zimbabwe.

Wanariadha waliosafiri India warudi humu nchini

NA DAVID MACHARIA

Wachezaji wa riadha wanne waliokuwa wamekwama India kwa sababu ya virusi vya corona wameeleza jinsi waliteseka huku wakilazimika kuishi kwa kula ugali na wali kila siku.

Wanne hao waliwasili humu nchini Ijumaa na wakawekwa kwenye karantini ya lazima kwenye kituo cha karantini cha serikali.

Wanariadha hao, Millicent Gathoni, Michael Kipyego, Isaac Kipkemoi na Benjamin Kipkasi watakaa kwenye karantini kwa siku 14 katika kituo cha karantini cha shule ya St George Nairobi.

“Nafurahi sana, kuwa nyumbani ni afadhali kuliko kuwa nchi ya kigeni mahali tulikuwa tumekwama. Tulikuwa na upweke,” alisema Gathoni huku akihojiwa kupitia simu na Taifa Leo.

Nauli ya kurudi humu nchini ililipwa na shirika la wanariadha.

Gathoni alielezea jinsi waliishi kwa ugali na wali huku kilo moja ya unga wa ugali ikiwagharimu Sh73.

“Tulikodisha nyumba na kujipikia kwa sababu hatungemudu kukaa hotelini,” alisema Gathoni. Gathoni, mkazi wa Nyahururu alifika India Februari ambapo alikuwa anatarajiwa kushiriki kwenye mbio nne.

Lakini kulipuka kwa ugonjwa wa corona kulipelekea kukatizwa kwa michezo na nchi kufungwa.

Pigo kwa Simbas msimu wa raga ukifutwa

Na CHRIS ADUNGO

KIPUTE cha raga cha Barthes Cup kilichokuwa kimeratibiwa upya kuandaliwa humu nchini mnamo Septemba 2020 sasa hakitafanyika.

Hii ni baada ya Shirikisho la Raga la Afrika kufutilia mbali kampeni zote za msimu huu kufuatia ushauri wa vinara wa mashirikisho wanachama waa Raga ya Afrika na maafisa wa afya kuhusu hali ya maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19 duniani.

Yalikuwa matumaini ya Shirikisho la Raga la Afrika kushuhudia mapambano mbalimbali yakirejelewa mwezi ujao lakini hilo halitawezekana kwa kuwa janga la corona bado halijadhibitiwa vilivyo.

Ina maana kwamba kampeni za kuwania ubingwa wa Africa Cup hazitafanyika kwa mwaka wa pili mfululizo. Mwaka jana, kivumbi hicho hakikuandaliwa kutokana na uchechefu wa fedha.

Aidha, mapambano ya raga ya wachezaji saba kila upande kwa wanaume na wanawake pamoja na Barthes Cup ambayo hushirikisha wanaraga chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20, hayatanogeshwa. Hata hivyo, nchi zilizokuwa zishiriki vipute hivyo zitakubaliwa kuvaana kirafiki iwapo hali itakuwa nafuu baadaye mwaka huu.

Kocha Paul Odera wa timu ya taifa ya wanaraga 15 kila upande almaarufu Simbas na kikosi cha U-20, amesema maamuzi hayo ni pigo kubwa kwa kikosi chake ambacho sasa hakitashiriki mapambano yoyote ya haiba kubwa mwaka huu. Isitoshe, matumaini yao ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za 2023 sasa yamedidimizwa zaidi.

“Yasikitisha kwamba tutakuwa na mwaka mmoja pekee wa kujiandaa kwa mechi za kufuzu kwa Kombe la Dunia. Hili ni jambo linalotuweka katika hali ngumu zaidi,” akasema.

Simbas kwa hivyo, watakosa fursa ya kuvaana na miamba wa raga ya Afrika, Namibia kwa mwaka wa pili mfululizo.

“Mataifa yote hayatalegeza masharti yaliyowawekea raia wao kwa wakati mmoja. Kuendelea na mapambano haya kutakwaza baadhi ya nchi zinazoshiriki. Aidha, gharama ya usafiri itakuwa ya juu na huenda baadhi ya timu zikalazimika kuwekwa karantini,” ikasema sehemu ya taarifa ya Shirikisho la Raga la Afrika.

Mechi za Simbas zilitarajiwa kuanza Juni 13 kwa pambano dhidi ya Morocco jijini Mombasa. Mchuano wa pili ungaliwashuhudia wakisafiri jijini Abidjan, Ivory Coast mnamo Juni 27. Waliratibiwa baadaye kuvaana na Uganda kwenye nusu-fainali za Victoria Cup mjini Kakamega mnamo Julai 11 kabla ya kuwaalika Zimbabwe mnamo Julai 18 mjini Nakuru.

Katika makala ya Raga ya Afrika mwaka jana, Simbas waliambulia nafasi ya pili nyuma ya Namibia barani kabla ya kupepetwa na Canada, Hong Kong na Ujerumani katika kundi la kufuzu kwa Kombe la Dunia.

Kenya ilitazamia kutumia mashindano ya Barthes Cup kufuzu kwa Raga ya Dunia kwa Chipukizi (JWRT) nchini Uhispania mnamo Disemba 2020 na kipute cha Africa Cup kujikatia tiketi ya fainali Kombe la Dunia nchini Ufaransa mnamo 2023.

Strathmore Leos kusajili wachezaji watano

Na CHRIS ADUNGO

VIONGOZI wa jedwali la Ligi ya Daraja la Kwanza la Raga ya Kenya (Championship), Strathmore Leos wamefichua azma ya kusajili wachezaji watano kadri wanavyopania kujisuka upya kwa minajili ya kampeni za msimu ujao.

Haya ni kwa mujibu wa kocha Louis Kisia ambaye amekariri kwamba tayari wametambua wanaraga hao wanaopania kujinasia huduma zao kutoka vikosi ambavyo ni wapinzani wao katika kivumbi cha Championship.

“Tunalenga kuimarisha zaidi idara yetu ya ushambuliaji ambayo imekuwa ikitukosesha usingizi kwa kipindi kirefu. Azma yetu ni kuwapiga jeki mafowadi waliopo ili kuweka hai matumaini ya kufuzu kwa Ligi Kuu ya Kenya na kutia fora katika kipute hicho,” akasema Kisia.

Hadi raga ya humu nchini iliposimamishwa mnamo Machi 2020 kutokana na janga la corona, Leos walikuwa wamejizolea jumla ya alama 76 kutokana na jumla ya 80 ambazo walikuwa na uwezo wa kutia kapuni.

“Nimeridhishwa na jinsi ambavyo tumecheza hadi kufikia sasa msimu huu. Kiu ya kusajili ushindi katika kila mechi na ari ya kutawala kila mchuano ni zao la msukumo wa kutaka kurejea katika Ligi Kuu baada ya kuteremshwa ngazi muhula jana,” akaongeza Kisia ambaye ni mwanaraga wa zamani wa Mwamba RFC.

Chini ya ukufunzi wake, Leos hawajazidiwa maarifa katika mchuano wowote kati ya 16 iliyopita.

Hadi kusitishwa kwa raga ya humu nchini, Leos walikuwa wameratibiwa kuchuana na mshindi kati ya Northern Suburbs na wasomi wa USIU-A kwenye nusu-fainali ya Championship.

Kwingineko, Mwamba RFC wamefichua kwamba Samurai Sportswear ndio watakaokuwa wadhamini wa jezi zao katika msimu huu wa 2020-21. Wanaraga wa Mwamba kwa sasa wataacha kuvalia jezi za BLK zilizotumiwa na kikosi hicho kwa minajili ya msimu wa 2019-20.

KRU yaunda kamati ya kuamua hatima ya msimu huu wa raga ya Kenya

Na CHRIS ADUNGO

SHIRIKISHO la Raga la Kenya (KRU) limeunda kamati ya watu sita ambao wametwikwa jukumu la kutathmini mapendekezo ya washikadau kisha kuamua hatima ya kampeni za raga ya humu nchini msimu huu wa 2019-20.

KRU itawakilishwa na mkurugenzi wa ratiba za mechi Hillary Itela kwa pamoja na wanachama wa bodi Moses Ndale na Peris Mukoko.

Xavier Makuba wa KCB ataungana na wenzake Philip Jalango wa Kabras Sugar na George Mbaye wa Mwamba RFC kuwakilisha vikosi vya Ligi Kuu ya Kenya Cup.

Kwa mujibu wa Oduor Gangla ambaye ni mwenyekiti wa KRU, kamati hiyo itatoa ripoti itakayotoa uamuzi wa ama kurejelewa kwa kampeni za muhula huu au kufutiliwa mbali ka msimu wote baada ya kutalii hali mbalimbali.

“Kamati iliyoundwa itakuwa na wajibu wa kushauriana na wadau kisha kutoa fomula itakayowezesha kurejelewa kwa mapambano mbalimbali au kufutiliwa mbali kwa msimu wote baada ya kutathmini masuala tofautitofauti,” akasema bila kufichua muda ambao ripoti ya kamati inastahili kutolewa.

Iwapo mechi za raga zitarejelewa baada ya serikali kuondoa marufuku ya sasa yanayoharamisha mikusanyiko ya umma, basi hilo huenda likafanyika Julai kwa kuwa wachezaji watahitaji angalau kipindi cha kati ya wiki 6-8 kujiandaa.

KRU ilibatilisha maamuzi yake ya kufutilia mbali msimu mzima wa 2019-20 baada ya presha kutoka kwa klabu za Kenya Cup zilizotishia kutafuta haki mahakamani kwa madai kwamba zilikuwa zimewekeza kiasi kikubwa cha fedha kwa minajili ya kampeni za muhula huu.

Kabras wanaselelea kileleni mwa jedwali la Kenya Cup kwa alama 74, tatu zaidi kuliko KCB ambao ni wa pili. Homeboyz walitarajiwa kuvaana na Menengai Oilers kwenye nusu-fainali ya mchujo wa Kenya Cup na mshindi kupepetana na KCB. Kabras watavaana na mshindi kati ya Impala Saracens na Mwamba.

Strathmore Leos wanaoongoza jedwali la KRU Championship kwa alama 76 wanapania kurejea katika Ligi Kuu ya Kenya Cup baada ya kuwa nje kwa miaka miwili. Wasomi wa Chuo Kikuu cha Masinde Muliro (MMUST) wanashikilia nafasi ya pili kwa alama 67.

Staa wa Shujaa Allan Makaka afariki

NA AYUMBA AYODI

MWANARAGA aliyekuwa na kasi ya kupindukia Allan Makaka wa timu za raga za taifa ya Shujaaa na Simba ameaga dunia.

Makaka ambaye alikuwa afisa wa mauzo katika kampuni ya Royal Media Services alipata ajali katika barabara kuu ya Mombasa, jijini Nairobi na ofisi za kampuni ya Airtel.

Royal Media Services ilisema kuwa alikuwa mfanyakazi kwa miaka 8 katika chapisho la habari hizo za kusikitisha Jumatano asubuhi kwenye tuvuti ya televisheni ya Citizen.

“Allan alijiunga nasi Februari 1, mwaka wa 2012 kama afisa wa mauzo na baadaye akawa meneja wa biashara katika stesheni ya Hot 96 nafasi aliyohudumu kwa kujitotela.

“Allan amekuwa chombo cha kuwafunza wengine wanaofanya kazi nzuri katika kazi zao. Amekuwa rafiki wa wengi kwenye kampuni.

“Tumekuwa tukishirikiana na familia yake kuomboleza  na tunaomba mtuunge mkono kwa maombi yenu katika wakati huu mgumu,’’ alisema mkurungezi wa RMS Rose Wajohi.

Mchezaji wa zamani wa Ulinzi stars anayehudumu kama kocha msaidizi wa KCB Dennis Mwanja, alimtaja Makaka kwa kumtaja kuwa mwenye nidhamu na maono.

“Tulisoma shule moja ya upili ya Musingu ambapo tulicheza raga pamoja. Nilihitimu mwaka wa 1999 naye Makaka alimaliza mwaka wa 2000 kabla ya kujiunga na Ulinzi,’’ alisema Mwanja, aliyecheza pamoja naye kwenye timu ya Kenya Sevens.

 

Tafsiri: Faustine Ngila

TANZIA: Nyota wa zamani wa timu ya taifa raga Allan Makaka afariki

Na GEOFFREY ANENE

KENYA imeamkia habari za kuhuzunisha Jumamosi baada ya kumpoteza nyota wake wa zamani wa timu ya taifa ya raga ya wachezaji saba kila upande Allan Makaka Shisiali katika ajali mbaya ya barabarani iliyotokea saa sita usiku.

Makaka, ambaye alipeperusha bendera ya Kenya katika Kombe la Dunia 2005 mjini Hong Kong na Jumuiya ya Madola 2006 mjini Melbourne nchini Australia, alikuwa katika gari ndogo alipogonga lori lililokuwa limesimama kwenye barabara ya Mombasa Road kutoka nyuma.

Mchezaji huyu wa zamani wa klabu za Ulinzi na Kenya Harlequin alizaliwa mnamo Juni 28 mwaka 1982.

Alisomea katika Shule ya Msingi ya Mumias Boys kabla ya kujiunga na Shule ya Upili ya Musingu katika Kaunti ya Kakamega na kisha kupata digrii katika Chuo Kikuu cha USIU katika eneobunge la Kasarani katika Kaunti ya Nairobi.

Wakati wa kifo chake, Makaka ambaye alichezea Kenya jumla ya mechi 57 na kuifungia miguso 28 kwenye Raga ya Dunia, alikuwa meneja katika Shirika la Habari la Royal Media Services.

Mwili wake umepelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Montenzuma kusubiri mazishi.

Mwanaraga wa zamani ateuliwa kocha wa Kenya Rugby League

Na CHRIS ADUNGO

MWANARAGA nguli Edward Rombo ameteuliwa kuwa kocha wa timu ya taifa ya Kenya Rugby League.

Rombo ataongoza programu ya timu ya taifa na kushirikiana na wakfu wa Giving Rugby Foundation kupiga jeki juhudi za benchi ya kiufundi na Shirikisho la Raga la Kenya katika makuzi ya vipaji miongoni mwa wanaraga wa humu nchini.

Nyota huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Kenya, anajivunia tajriba ya takriban miaka 30 ya uchezaji na ukufunzi katika Ligi na Shirikisho la Raga. Ndiye Mkenya wa kwanza kuwahi kusakatia kikosi cha Leeds Rugby, Dewsbury na Featherstone Rovers, Uingereza katika miaka ya 90.

Rombo ambaye ni fowadi, anajivunia misimu mingi ya kuridhisha katika Raga ya Shirikisho hasa ikizingatiwa kwamba aliwahi kuwaongoza Mean Machine kujizolea ubingwa wa Ligi Kuu ya Kenya Cup mnamo 1989 na 1990. Amewahi pia kuchezea klabu za Watembezi Pacesetters na Barclays RFC.

Rombo, anayemiliki kampuni ya masuala ya uanasheria ya Rombo and Co Advocates, amewahi pia kuwa kocha wa kikosi cha Mwamba RFC.

“Nikiwa mwasisi wa Rugby League nchini Kenya, itakuwa fahari yangu kuona mchezo huo ukikita mizizi na kuwa kivutio cha wanaraga wa haiba watakaojitolea kuunda kikosi thabiti kitakachovaana vilivyo na vigogo wengine duniani,” akasema Rombo.

Nyakwaka Adhere ambaye ni mwenyekiti wa Kenya Rugby League amesema kwamba shughuli za kuteua timu ya taifa na mazoezi ya wanaraga hao kwa sasa imeahirishwa kutokana na janga la corona.

Aliongeza kwamba pindi corona itakapodhibitiwa, maskauti wataanza kuteua wachezaji watakaounga timunya taifa kwa minajili ya mchuano utakaokutanisha Kenya na Afrika Kusini katika uwanja na tarehe itakayofichuliwa baadaye. Tofauti na Raga ya Shirikisho, Rugby League hutandazwa na jumla ya wachezaji 13.

Kipute hicho kiliasisiwa nchini Uingereza na pia kinasakatwa Australia na New Zealand.

Hapa Kenya, mechi za Rugby League huchezewa katika uwanja wa Railways Club, Nairobi.

COVID-19: Kombe la Enterprise kutupwa kando kupisha raga ya Kenya Cup

Na CHRIS ADUNGO

KIPUTE cha Enterprise Cup kitafutiliwa mbali katika kalenda ya raga ya humu nchini msimu huu ili kuwezesha vikosi kukamilisha kampeni za Ligi Kuu ya Kenya Cup.

Pendekezo hili la wasimamizi wa klabu mbalimbali linatarajiwa kuidhinishwa na Shirikisho la Raga la Kenya (KRU) ambao wamebatilisha maamuzi ya awali ya kufutilia mbali kabisa msimu huu mzima wa raga kutokana na janga la corona.

Hadi kusitishwa kwa shughuli zote za michezo humu nchini mnamo Machi 2020, kivumbi cha Enterprise Cup ambacho ndicho cha zamani zaidi katika historia ya raga ya Kenya, kilikuwa kimetinga hatua ya nusu-fainali.

Mabingwa watetezi Kabras RFC walikuwa wamepangwa kuvaana na Homeboyz huku wanabenki wa KCB wakiratibiwa kumenyana na Impala Saracens.

Kwa mujibu wa KRU, itakuwa busara kufutilia mbali kipute cha Enterprise Cup ili kupunguza mrundiko wa mechi katika kalenda ya msimu huu pindi michuano ya raga ya Kenya Cup itakaporejelewa baada ya corona kudhibitiwa vilivyo.

Kwa mujibu wa Xavier Makuba ambaye ni mwenyekiti wa kivumbi cha Kenya Cup, kinyang’anyiro hicho kimeratibiwa kurejelewa mnamo Julai 2020 na maamuzi hayo yamechochewa na ukubwa wa kiwango cha fedha zilizowekezwa kwa minajili ya mapambano hayo.

Kinyume na washikadau wengine, Makuba ametaka klabu husika kuwapa wanaraga wao muda wa hadi wiki tatu pekee za kujiandaa kwa mchujo wa Kenya Cup kisha fainali ya mashindano hayo.

“Sidhani tutahitaji wiki sita za kujiandaa kwa mechi zilizosalia msimu huu. Majuma matatu yanatosha wachezaji kupiga kambi na kujifua vilivyo kwa kibarua kilichopo mbele yao,” akatanguliza Makuba.

“Nina imani msimu huu wa Kenya Cup utakamilika kwa wakati ufaao na kupisha mapambano ya Raga ya Kitaifa ya Sevens Circuit. Iwapo mambo yawiana na mipangilio yetu na klabu zote zishirikiane nasi, basi sioni lolote litakalotuzuia kutamatisha rasmi kampeni za raga ya msimu huu kufikia katikati ya Julai,” akaongeza.

Mapendekezo hayo yamewasilishwa kwa kamati ya KRU inayosimamia ratiba za mechi za Kenya Cup chini ya uenyekiti wa Hillary Itela anayetazamiwa kutoa maamuzi yao mwishoni mwa wiki hii.

Homeboyz walitarajiwa kuchuana na Menengai Oilers ambapo mshindi angejikatia tiketi ya kukabiliana na mabingwa watetezi, KCB katika hatua ya nusu-fainali ya Kenya Cup. Kabras walitazamiwa kupimana ubabe na mshindi kati ya Impala na Mwamba RFC.

Hadi kufutiliwa mbali kwa Ligi Kuu ya Kenya Cup, Kabras ya kocha Henley Du Plessis ilikuwa ikiselelea kileleni kwa alama 74, tatu zaidi mbele ya KCB.

Janga la corona limeathiri pia kivumbi cha KRU Championship, ligi pana za kitaifa, ligi zote za madaraja ya chini, kipute cha Great Rift Valley Cup, Mwamba Cup na ligi ya kitaifa ya National Cirucit.

Kwa upande wa KRU Championship, Strathmore Leos waliokuwa hawajapoteza mechi yoyote, walikuwa wakiongoza jedwali kwa alama 76, tisa zaidi kuliko Chuo Kikuu cha Masinde Muliro (MMUST) katika nafasi ya pili.

Leos walikuwa wakutane na mshindi kati ya Northern Suburbs na Chuo Kikuu cha USIU-A katika mojawapo ya nusu-fainali huku MMUST wakipambana na mshindi kati ya Mean Machine ya Chuo Kikuu cha Nairobi na Egerton Wasps.

Simbas watoa mwongozo mpya wa kuboresha raga nchini Kenya

Na CHRIS ADUNGO

BENCHI ya kiufundi ya kikosi cha raga ya wachezaji 15 kila upande, Simbas, imebuni mwongozo mpya wa ukufunzi na usimamizi utakaosaidia pia klabu mbalimbali kujiimarisha na kuboresha maandalizi yao baada ya shughuli za michezo kurejelewa.

Michezo yote kwa sasa imesitishwa humu nchini na katika mataifa mengi duniani kote kutokana na mlipuko wa virusi vya corona.

Mwongozo huo unashughulikia masuala ya afya, jinsi ya kuimarisha mazoezi ya viungo vya mwili miongoni mwa wanaraga na namna ya kuboresha idara za ulinzi, kati na uvamizi za vikosi. Mwongozo huo unapania pia kuwapa maafisa wa mechi mbinu bora zaidi za kukumbatia kila wanaposimamia au kuendesha michuano mbalimbali.

Kocha Paul Odera amekiri kwamba analenga kuutumia mwongozo huo kwa kipindi chote kilichosalia katika mkataba wake na kikosi cha Simbas na kile cha wanaraga chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20, Chipu.

“Tutakuwa tukifanyia mwongozo huo mabadiliko ya mara kwa mara ili uwiane na mazingira na mahitaji yote ya raga ya humu nchini pamoja na viwango vya kimataifa,” akasema Odera.

Mwanaraga huyo wa zamani wa timu ya taifa ya wachezaji saba kila upande, Shujaa, amesema vikosi vya Kenya vinakosa mtindo ambao ni kitambulisho chao katika ulingo wa raga ikilinganishwa na Afrika Kusini, New Zealand, Uingereza, Australia na Ufaransa ambao ni miamba wa mchezo huo duniani.

“Mfumo na mtindo wetu wa kucheza unastahili kujumuisha upana wa utamaduni wetu bila ya yeyote kubaguliwa kwa misingi ya rangi, kabila au mahusiano ya kijamii. Uwezo wa wanaraga wetu kutumia uchache wa raslimali tulizonazo na kuchuma nafuu kutokana na vipaji vya mbio na ukubwa wa miili unastahili kuwa kitambulisho chetu,” akaongeza.

Simbas walikuwa wameanza kujifua mapema Machi 2020 kwa minajili ya kampeni mbalimbali za raga ya kimataifa kabla ya Serikali kusimamisha kwa muda michezo yote kutokana na janga la corona ambalo limetikisa ulimwengu mzima.

Chini ya Odera, kikosi cha Simbas kilikuwa kimepangiwa kuchuana na Morocco, Uganda na Zimbabwe katika kipute cha kuwania ufalme wa Raga ya Bara la Afrika mwishoni mwa Mei kabla ya kinyang’anyiro hicho kuahirishwa.

Simbas walikuwa pua na mdomo kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za Raga mnamo 2015 kabla ya kuzidiwa maarifa na Namibia.

Katika makala ya Raga ya Afrika mwaka jana, Simbas waliambulia nafasi ya pili nyuma ya Namibia barani kabla ya kupepetwa na Canada, Hong Kong na Ujerumani katika kundi la kufuzu kwa Kombe la Dunia.

Chipu nao walikuwa wakijifua kwa minajili ya kipute cha Barthes Cup kilichotarajiwa kuandaliwa jijini Nairobi mnamo kati ya Aprili 19-22. Odera aliwahi kukiri kwamba changamoto kubwa anayokabiliana nayo kambini mwa Chipu ni ugumu wa kuoanisha mitindo ya kucheza kwa wanaraga wake.

Hilo lilichochea Shirikisho la Raga la Kenya (KRU) kujinasia huduma za wakufunzi Hans Joubert na Neil De Kock kutoka Afrika Kusini mnamo Februari 2020. Wawili hao walikuwa washirikiane na Odera kuwanoa wanaraga wa Chipu kwa minajili ya kutetea ubingwa wa Barthes Cup mnamo Aprili 2020.

Kenya ilitazamia kutumia mashindano hayo kufuzu kwa Raga ya Dunia kwa Chipukizi (JWRT) nchini Uhispania mnamo 2020 na fainali za Kombe la Dunia nchini Ufaransa mnamo 2023.

Mikataba ya wanaraga nchini yafutwa

Na CHRIS ADUNGO

SHIRIKISHO la Raga la Kenya (KRU) limesimamisha kandarasi zote za wachezaji wa timu ya taifa ya wanaraga saba kila upande, Shujaa, kutokana na virusi vya homa ya corona.

Kwa kawaida, mikataba ya wanaraga wote ambao huvalia jezi za Shujaa hutamatika Julai ya kila mwaka baada ya kukamilika kwa duru zote za kampeni ya Raga ya Dunia. Mchuano ujao kwa Shujaa katika ulingo wa raga ya kimataifa umeratibiwa kufanyika Septemba 2020.

Ilivyo, huenda KRU ikaamua pia kupunguza mishahara ya wachezaji wa Shujaa ambao wamepangiwa kuanza upya mazoezi mnamo Julai. Haya ni kwa mujibu wa mwenyekiti wa KRU, Oduor Gangla ambaye amefichua mipango ya kubadilisha michakato mbalimbali kuhusu namna raga ya humu nchini inavyoendeshwa.

Kutokana na hatua hiyo ya KRU, Paul Feeney ambaye ni kocha mkuu wa Shujaa, amerejea nchini kwao New Zealand kwa likizo ya miezi minne bila malipo. Hii ni kutokana na hali ngumu ya kifedha ambayo imekuwa ikikabili Shirikisho la Raga la Kenya kwa miaka kadhaa iliyopita.

Kwa mujibu wa ratiba ya Shujaa, kikosi hicho kinatarajiwa kurejelea mazoezi ya wiki nane mnamo Julai kabla ya kuanza kunogesha duru nne zilizosalia katika kampeni za Raga ya Dunia msimu huu mnamo Septemba.

Baada ya kushiriki duru za Paris, Ufaransa na London, Uingereza mnamo Septemba, Shujaa wataelekea Hong Kong, China kisha Singapore nchini Malaysia.

“KRU lazima itafute mbinu za kufanikisha uendeshaji wa timu ya taifa na kubuni mikakati ya muda mfupi na ya kudumu kuhusu jinsi raga ya humu nchini itakavyostawishwa. Itatulazimu kufanya maamuzi magumu na mazito ili kukabiliana vilivyo na hali ya sasa ya corona,” akasema Gangla katika kauli iliyosisitizwa na Katibu Mkuu wa KRU, Ian Mugambi.

Bajeti ya kikosi cha Shujaa mwaka huu ilikadiriwa kufikia kati ya Sh60-70 milioni, fedha hizi zikijumuisha mishahara, marupurupu, ada za kambi za mazoezi, chakula na gharama nyinginezo.

Kuhusiana na utaratibu wa jinsi ujira wa wanaraga wa Shujaa hutolewa, nahodha Andrew Amonde, nyota Collins Injera, Oscar Ouma, Willy Ambaka na Billy Odhiambo ndio hupokezwa mishahara ya juu zaidi kutokana na urefu wa muda ambao wamehudumia timu ya taifa.

Kundi la pili la wanaraga ambao wamewajibikia Shujaa kwa kati ya miaka saba na nane ni lile linalowajumuishwa Dan Sikuta, Nelson Oyoo, Bush Mwale, Alvin ‘Buffa’ Otieno, Sammy Oliech na Jeff Oluoch ambaye ni nahodha msaidizi.

Kundi la tatu la wachezaji wanaopokea mishahara midogo ikilinganishwa na wenzao kwa sababu ya uchache wa miaka ambayo wamevalia jezi za Shujaa ni Johnstone Olindi, Vincent Onyala, Daniel Taabu, Herman Humwa, Geoffrey Okwach na wengineo.

Kufikia sasa, Shujaa wanashikilia nafasi ya 12 kwenye msimamo wa jedwali la Raga ya Dunia kwa alama 35 na wamefikia robo-fainali za Main Cup mara mbili msimu huu.

‘Shujaa na Lionesses pamoja na KRU hazitafaidika na hatua ya Rais Kenyatta kupunguza ushuru’

Na GEOFFREY ANENE

SHIRIKISHO la Raga Kenya (KRU) limesema limefurahishwa serikali kuondoa ushuru unaotozwa wananchi wanaokula mshahara wa Sh24,000 kurudi chini kwa asilimia 100 wakati huu mgumu wa virusi vya corona, japo hatua hiyo ‘haitasaidia wachezaji wa timu za taifa za raga za Kenya’.

Katika mahojiano na ‘Taifa Leo‘, Mwenyekiti wa KRU Oduor Gangla alisema, “Kwa kupunguzia watu ushuru, serikali imefanya kitu cha maana. Ni hatua nzuri ya kuondoa ushuru kwa watu wanaopata mshahara usiozidi Sh24, 000. Hata hivyo, wachezaji wetu wanapokea mshahara unaopita kiasi hicho. Kupunguza ushuru wa VAT (kutoka asilimia 16 hadi asilimia 14) kutasaidia katika bei ya bidhaa kushuka kwa hivyo tunasubiri kwa hamu kubwa kuona bei ya vitu tunatumia kila siku nyumbani ikishuka. Wafanyabiashara kupunguziwa asilimia tano ya ushuru ni kitulizo kikubwa. Inamaanisha kuwa kila mtu anaokoa fedha zaidi, ingawa haibadilishi gharama za KRU kivyovyote.”

Aidha, afisa huyo amekiri kuwa janga la virusi vya corona vimeweka KRU pabaya kwa sababu inaandamwa na majukumu mengi ikiwemo mishahara ya wachezaji wa timu za taifa, ingawa hakuna chochote kispoti watakuwa wakifanya mwezi Aprili, Mei, Juni, Julai na Agosti kwa sababu mashindano yote yamesimamishwa.

Suala la mishahara huwa nyeti, na si mara moja ama mbili, bali mara nyingi timu ya taifa ya raga ya wachezaji saba kila upande almaarufu Shujaa, imegoma baada ya mishahara kucheleweshwa ama kupunguzwa.

Alipoulizwa jinsi KRU inapanga kukabiliana na tatizo la kulipa mishahara ya wachezaji kandarasi zao zinavyosema, Gangla alisema, “Tunaishi katika wakati mgumu kwa sababu hakuna fedha mpya zinaingia katika akaunti ya KRU. Kila taasisi imelazimika kufanyia shughuli zake mabadiliko na KRU si tofauti. Matumaini yetu ni kuwa virusi hivi vitadhibitiwa ili maisha yarejelee hali ya kawaida. Tunazungumza na wadau wetu, lakini hali inasalia ya wasiwasi.”

Mwandishi huyu alipotaka kujua ikiwa KRU inawazia kukata mishahara ya wachezaji jinsi klabu nyingi barani Ulaya zimekuwa zikifanya, Gangla alisema, “Kila mtu anafahamu kinachoendelea duniani wakati huu. Kitu muhimu ni kufanya mambo kwa haki.”

Rais Uhuru Kenyatta alitangaza mabadiliko ya ushuru unaotozwa Wakenya na wakazi wa Kenya hapo Jumatano ili kuwapunguzia changamoto zilizoletwa na virusi vya corona, ambavyo vimeua zaidi ya watu 20,000 duniani na kuambukiza watu zaidi ya 400,000. Vimesimamisha shughuli nyingi ikiwemo michezo na masomo katika taasisi za elimu, miongoni mwa nyingine.

KRU yasimamisha msimu 2019-2020 kwa sababu ya COVID-19

Na GEOFFREY ANENE

SHIRIKISHO la Raga Kenya (KRU) limesimamisha mashindano yote ya msimu 2019-2020 ikiwemo Ligi Kuu baada ya Wizara ya Afya kuthibitisha Ijumaa kisa cha kwanza cha maakumbizi ya ugonjwa wa COVID-19 unaosababishwa na virusi vya corona.

“Kufuatia tangazo kuwa kuna mtu anaugua ugonjwa wa COVID-19 humu nchini na pia agizo la Wizara ya Afya kupiga marufuku mikusanyiko ya watu, KRU inatangaza kusitisha msimu wa 2019-2020.

Marufuku haya yataanza kutumikiwa katika mechi za Ligi Kuu, Ligi ya Daraja la Pili, Ligi ya Matawi na Eric Shirley Shield za wikendi hii,” shirikisho limesema na kuahidi kutoa mwelekeo zaidi baadaye.

Mechi za Ligi Kuu zilizokuwa zimeratibiwa kusakatwa Machi 14 ni kati ya Homeboyz na Menengai Oilers na ile inayokutanisha Impala Saracens na Stanbic Mwamba uwanjani Impala Club.

Mechi hizo ni za kuamua timu mbili zitakazomenyana na Kabras Sugar na mabingwa watetezi KCB katika nusu-fainali.

Shujaa yaridhika kuzoa alama tatu Los Angeles Sevens

Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya taifa ya raga ya wachezaji saba kila upande ya wanaume ya Kenya, Shujaa, iliambulia alama tatu katika duru ya tano ya Raga ya Dunia mjini Los Angeles, Marekani, mnamo Machi 1 usiku.

Vijana wa kocha Paul Feeney walizoa alama hizo baada ya kupoteza 29-24 dhidi ya Scotland katika mechi ya kutafuta nambari 13 na 14.

Walianza kampeni ya Los Angeles kwa kulemewa 31-5 na Afrika Kusini mnamo Februari 29 usiku katika mechi ya Kundi B ambayo William Ambaka alifunga mguso wa kufutia machozi.

Kenya kisha iliamka katika mchuano wa pili ilipokung’uta Ireland 29-12 kupitia miguso ya Vincent Onyala (mitatu), Oscar Dennis na Collins Injera kabla ya kuaibishwa 24-0 na Canada itakayoandaa duru ya sita hapo Machi 7-8.

Matokeo hayo yalisukuma Shujaa kuwania nafasi 9-16 ambapo ililimwa 28-19 na Samoa katika robo-fainali ya Challenge Trophy ikipata alama zake katika mchuano huo kupitia kwa miguso ya Onyala (miwili) na Samuel Oliech (mmoja). Daniel Taabu alipachika mikwaju ya miguso miwili.

Kichapo hicho kiliteremsha Shujaa katika mechi ya kuwania nusu-fainali ya kuorodheshwa kutoka nafasi ya 13 hadi 16. Ililipua Wales 29-5 na kujiondoa katika hatari ya kuvuta mkia tena baada ya kufanya hivyo katika duru ya nne mjini Sydney nchini Australia mapema Februari.

Vijana wa Feeney walizamisha Wales kupitia kwa miguso ya Ambaka, Oliech, Dennis, Oscar Ouma na Jeff Oluoch. Oliech na Taabu walifunga mkwaju mmoja kila mmoja katika mchuano huo.

Shujaa kisha iliingia mchuano wa kuamua nambari 13 na 14 dhidi ya Scotland ambapo ilipata miguso kutoka kwa Ambaka, Billy Odhiambo, Oliech na nahodha Andrew Amonde, lakini ikalemewa dakika ya mwisho. Oliech alifunga mikwaju miwili na mchuano huo.

Baada ya duru hiyo, Kenya imesalia katika nafasi ya 11 duniani kwa alama 29.

Mabingwa wa Cape Town na Hamilton New Zealand wanaongoza ligi hii ya mataifa 15 kwa alama 93, nne mbele ya washindi wa Dubai na Los Angeles Afrika Kusini nao washindi wa Sydney Sevens Fiji wanashikilia nafasi ya tatu kwa alama 72. Ufaransa (alama 67), Uingereza (64), Australia (62), Marekani (60), Argentina (53), Ireland (45) na Canada (40) zinafunga mduara wa 10-bora.

Scotaland ni ya 12 sako kwa bako kwa alama 29 na Kenya nayo Samoa ni ya 13 alama moja nyuma. Wales inakamata nafasi ya 15 ya kutemwa. Imezoa alama 11. Japan, ambayo ilialikwa kushiriki duru nne za kwanza, ina alama tisa nayo Korea ina alama moja baada ya kualikwa mjini Los Angeles na kuvuta mkia.

Kenya Shujaa yajikwaa 31-5 dhidi ya Afrika Kusini

Na GEOFFREY ANENE

KENYA Shujaa imeanza duru ya tano ya Raga ya Dunia kwa kujikwaa mjini Los Angeles baada ya kuaibishwa 31-5 na miamba Afrika Kusini nchini Marekani, Jumamosi.

Vijana wa kocha Paul Feeney walipata mguso wa kujituliza roho kutoka kwa William Ambaka kabla tu ya kipindi cha kwanza kutamatika baada ya Afrika Kusini kupachika miguso miwili kupitia kwa Angelo Davids na JC Pretorius.

Werner Kok, Muller du Plessis na Branco Du Preez waliongeza miguso ya Afrika Kusini katika kipindi cha pili. Selvyn Davids, Cecil Afrika na Du Preez pia walichangia mkwaju mmoja kila mmoja.

Shujaa itakabiliana Ireland katika mechi yake ijayo saa saba usiku Machi 1, 2020 na kumaliza mechi za Kundi B dhidi ya Canada (5.35 a.m.).

Ireland ilichabanga Canada 17-12 katika mechi ya kwanza ya kundi hili.

Kenya ilivuta mkia katika duru ya nne mjini Sydney nchini Australia na inalenga kuepuka aibu hiyo mjini Los Angeles katika ligi hii ya duru 10 na mataifa 15 ambayo timu ya mwisho hutemwa.