Raila akanyagia ‘tosha’ ya urithi wa Joho

VALENTINE OBARA na ANTHONY KITIMO

KIONGOZI wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga, alijiepusha kumwidhinisha mwanasiasa yeyote anayepanga kuwania ugavana Mombasa kupitia chama hicho mwaka ujao alipozuru kaunti hiyo.

Wanasiasa wawili wanaotarajia kushindania tikiti ya chama hicho kuwania ugavana Mombasa mwaka 2022 walionekana kuzidisha juhudi za kutafuta ‘baraka’ za Bw Odinga.

Wawili hao ambao ni Mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir na mfanyabiashara Suleiman Shahbal, walionekana kung’ang’ania sikio la Bw Odinga alipozuru kaunti hiyo Alhamisi.

Bw Nassir na Bw Shahbal hawakukutana ana kwa ana hadharani katika hafla mbili ambazo Bw Odinga alihudhuria akiwa na Gavana wa Mombasa, Bw Hassan Joho.

Hafla ya kwanza ambayo Bw Odinga alihudhuria ilikuwa ni uzinduzi wa kituo cha mafuta cha Hass katika mtaa wa Nyali, ambapo Bw Shahbal alikuwepo.

Baada ya kuandamana kwa karibu katika uzinduzi huo, wawili hao walienda kufanya mkutano wa faragha nyumbani kwa Bw Shahbal katika mtaa huo.

Ingawa yale waliyozungumzia hayakuanikwa wazi, duru ziliambia Taifa Leo kwamba, Bw Odinga alimwahidi Bw Shahbal kutakuwa na kura ya mchujo kwa njia ya haki na uwazi kuamua watakaopewa tikiti ya chama kuwania viti vyote vya kisiasa.

Baadaye katika hafla ya kuzindua kitengo maalumu cha matibabu ya moyo katika Hospitali Kuu ya Rufaa ya Pwani, Bw Odinga alikumbwa na miito ya umati uliokuwa ukimtaja Bw Nassir kuwa ‘gavana mtarajiwa’.

Ijapokuwa Bw Joho ndiye alikuwa mwandalizi wa hafla, Bw Nassir ndiye alitembea na waziri huyo mkuu wa zamani sako kwa bako walipowasili katika hafla hiyo. Bw Joho alitembea nyuma yao.

Katika hotuba yake, Bw Odinga alimtambua tu Bw Nassir kama mbunge mahiri ambaye amechangia mengi hasa katika wadhifa wake wa uenyekiti katika kamati ya bunge ya kuchunguza matumizi ya fedha za umma.

“Nataka kutoa shukrani kwa mbunge wa hapa kwa kazi anayofanya kufichua ufisadi katika bunge. Tunataka wabunge wetu waendelee kufanya kazi yao,” akasema Bw Odinga, huku mbunge huyo akisimama kando yake.

Bw Nassir alisema mtu yeyote yuko huru kujiunga na ODM Mombasa lakini ana matumaini makubwa kwamba wapigakura watamchagua yeye kurithi kiti cha Bw Joho.

“Tumeona baadhi ya watu waliokuwa wakikashifu ODM katika uchaguzi uliopita wakirudi kutafuta kiti cha ugavana. Tunawakaribisha kuongezea nguvu chama chetu lakini tunataka wajue mimi ndiye nitakuwa gavana ajaye wa Mombasa. Wapigakura ni werevu, wanajua ni nani anataka kiti hiki kwa manufaa yake ya kibinafsi,” akasema Bw Nassir.

Bw Shahbal alitangaza rasmi kujiunga na ODM kutoka Jubilee wikendi iloyopita. Alikuwa amewania ugavana kupitia Wiper mwaka wa 2013 na Jubilee mwaka wa 2017, lakini Bw Joho akamshinda kwa kuwania kupitia kwa ODM.

Bw Joho alisema angali anatazamia kuwania urais 2022 atakapokamilisha kipindi chake cha pili cha ugavana ambacho ni cha mwisho kikatiba.

Jeshi la Ruto lapasuka ngome ya Raila

Na RUSHDIE OUDIA

MZOZO mkali umeibuka kati ya makundi yanayompigia debe Naibu Rais William Ruto katika ngome za kisiasa za Kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga.

Wafuasi wa Dkt Ruto na chama cha United Democratic Allince (UDA) katika Kaunti za Siaya na Kisumu, walijitokeza kulalamikia jinsi mipango ya kumvumisha kabla 2022 eneo hilo inavyosimamiwa.

Walimlaumu Bw Eliud Owalo, ambaye amejitokeza kuwa msemaji wa Dkt Ruto eneo la Nyanza kwa kujifanyia mambo bila kushauriana nao.

Kulingana na Mwenyekiti wa UDA katika Kaunti ya Kisumu, Bw Charles Ooko Okoth, ingekuwa vyema iwapo Dkt Ruto na wakuu wa UDA wangemwachia Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi mamlaka ya kusimamia eneo la Nyanza kwa ushirikiano nao, badala ya Bw Owalo.

“Kila mara tunapopanga shughuli zozote huwa tunashauriana naye, lakini anakataa mapendekezo yetu na kuyasitisha ilhali yeye huwa hayuko huku mashinani. Hali hii imekuwa pigo kwetu ilhali tulikuwa tumeanza kupiga hatua,” akasema Bw Okoth.

Kufikia sasa, chama hicho hakijafungua ofisi yoyote Kisumu.

Malalamishi sawa na hayo yalitolewa na mwenyekiti wa UDA kutoka Siaya, Bw Washington Alunga.

Hata hivyo, Bw Owalo aliwapuuzilia mbali akidai kile wanachotaka ni pesa ilhali yeye hana tabia ya kuombaomba kutoka kwa wanasiasa.

“Tangu mwanzo, niliwaambia hawa vijana kwamba mtu yeyote anayejiunga nasi kwa lengo la kuombaomba pesa, yuko huru kufanya hivyo bila kunihusisha. Sijawahi kufanya kitu kama hicho maishani mwangu na siko tayari kuanza sasa,” akasema.

Alijitetea kuwa uamuzi wake kujiunga na kikundi cha Dkt Ruto ni kwa vile anaamini mipango ya naibu rais kwa taifa hili na wala hakufanya hivyo ili kujinufaisha kifedha.

Wakati huo huo, maafisa wa UDA katika Kaunti ya Kisumu walisema wako tayari kuungana na wenzao wa ODM kuhamasisha kuwepo kwa muungano wa Dkt Ruto na Bw Odinga katika uchaguzi mkuu ujao.

Afisa wa UDA katika kaunti hiyo, Bw Oliver Ochieng, alisema ripoti zinazoenezwa kuhusu uwezekano wa wawili hao kuungana 2022 ni za kutia moyo kwani upinzani uliopo kati yao huzua uhasama wa kisiasa usiofaa.

JAMVI: ODM inacheza tu abrakadabra za danganyatoto, ukweli wajulikana

Na CHARLES WASONGA

SASA imedhihirika wazi kwamba kiongozi wa ODM Raila Odinga amejipata katika njiapanda kuhusu iwapo awanie urais 2022 au aunge mtu mwingine.

Hii ni kutokana na taarifa za kukanganya kutoka kwa chama hicho kuhusu suala zima la iwapo waziri huyu mkuu wa zamani ni miongoni mwa watakaoshindania tiketi ya ODM kuwania urais au la.

Wadadisi wanasema kuwa taarifa hizo kinzani kutoka kwa Bodi ya Kitaifa ya Uchaguzi (NEB) na afisi kuu ya chama hicho inaashiria kuwa Bw Odinga bado hajaamua iwapo atawania urais au aseme fulani “tosha”.

Siku moja baada ya mwenyekiti wa NEB Catherine Mumma kutoa taarifa iliyoorodhesha Bw Odinga miongoni mwa wale waliowasilisha maombi ya kutaka kuwania urais kwa tiketi ya ODM, Katibu Mkuu Edwin Sifuna alitoa taarifa kinzani.

Katika taarifa yake aliyoitoa Ijumaa na iliyoshangaza wengi, Bw Sifuna alifafanua kuwa kiongozi wa chama hicho hajawasilisha ombi la kutaka kugombea urais 2022.Bw Sifuna alisema kuwa taarifa ya awali iliyoeleza kuwa Bw Odinga aliwasilisha ombi lake kwa NEB ilikuwa ni mzaha wa Aprili 1.

Hii huwa ni siku ya wajinga ambapo watu hutoa taarifa za uwongo kisha kuweka ukweli baadaye. “Siasa ni suala la kuchukuliwa kwa uzito kila siku isipokuwa Aprili 1. Tuliamua kuadhimisha siku ya wajinga kupitia taarifa yetu jana (Aprili 1, tukifahamu fika kwamba wenzetu katika sekta ya habari watafahamu hilo lakini inaonekana kuwa walinoa,” akasema Bw Sifuna.

Alisema wale ambao wako kwenye kinyang’anyiro cha tiketi ya ODM ni Gavana Ali Hassan Joho (Mombasa) na mwenzake wa Kakamega Wycliffe Ambetsa Oparanya; akieleza kuwa Odinga atatoa msimamo wake baada ya kura ya maamuzi kuhusu Mswada wa BBI.

Bi Mumma alipoulizwa kuhusu madai ya Bw Sifuna kwamba Bw Odinga hakuwa ametuma maombi, alisema kuwa bodi yake ilichapisha majina ambayo ilipokea kutoka kwa sekritariati ya ODM.

“Sisi tulichapisha majina ambayo tulipokea kutoka wa sekritariati kuu ambako barua za maombi zilikuwa zikiwasilishwa. Ukitaka maelezo zaidi, tafadhali walisiliana na Katibu Mkuu au sekritariati,” Dkt Mumma akasema.Mchanganuzi wa masuala ya siasa Bw Mark Bichachi sasa anasema kuwa kuna uwezekano mkubwa kwamba taarifa ya Sifuna ilichochewa na mkutano kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Bw Odinga.

“Mabadiliko haya yamechangiwa na hatua ya Uhuru kumpigia simu Raila kabla ya kumtembelea nyumbani kwake Karen. Hatua hii ilionekana kama ya kutuliza kambi ya kiongozi huyo wa ODM ambayo imekuwa ikilalamikia kile inachodai ni hujuma kutoka kwa Afisi ya Rais,” asema Bw Bichachi.

Kwa mujibu wa mdadisi huyo, taarifa iliyotolewa na NEB na iliyoorodhesha Mbw Odinga, Joho na Oparanya kama watu waliokuwa wamewasilisha maombi yao na stakabadhi husika kufikia tarehe ya mwisho, Machi 31, 2021, ilikuwa sahihi.

“Taarifa ya NEB ilikuwa sahihi kwa sababu ilitolewa baada ya Raila kuongoza mkutano wa Kamati Simamizi ya Kitaifa (NMC) nyumbani kwake Jumatano. Hii ni baada ya madaktari kuthibitisha kwamba alikuwa amepona corona,” asema Bichachi.

“Lakini baada ya kupata hakikisho kutoka kwa Rais Kenyatta kwamba mchakato wa BBI ungalipo, Raila aliamuru kwamba jina lake liondolewe kutoka kwenye orodha hiyo, kama hatua ya kimkakati,” anasema.

Kauli ya Bw Bichachi inashabihiana na yake wakili James Mwamu ambaye anaongeza kuwa Bw Odinga alikuwa anaelekea kugura handisheki na BBI hadi pale Rais Kenyatta alipoingilia kati.

“Uliposikia watu kama Orengo, Sifuna na wabunge Junet Mohamed na Otiende Amollo wakimshambulia Kibicho kwa kile walichodai ni kuhujumu ndoto ya Raila kuingia Ikulu ilikuwa dalili tosha kwamba uhusiano kati ya Uhuru na Raila ulikuwa umeanza kudorora. Hii ndiyo maana ilimlazimu Rais Kenyatta kumfikia Raila kusudi atulize hali,” anasema Bw Mwamu ambaye pia ni wakili.

“Bw Sifuna asidanganye kwamba taarifa ya NEB ilitolewa kimzaha kuadhimisha Siku ya Wajinga, Aprili 1. Ukweli ni kwamba aliagizwa kutoa taarifa aliyoitoa Ijumaa baada ya mashauriano ya Jumatano kati ya Rais na Raila,” asema mwenyekiti huyo wa zamani wa Chama cha Wanasheria Afrika Mashariki (EALS).

Itakumbukwa kwamba mwezi jana Bw Orengo (James) ambaye ni Seneta wa Siaya, Amollo (Mbunge wa Rarieda) na Mohamed (Mbunge wa Suna Mashariki) walimwelekezea kidole cha lawama Dkt Kibicho wakidai anamhujumu Bw Odinga kwa lengo la kuzima ndoto yake ya kuingia Ikulu 2022.

Aidha, walidai kuwa Katibu huyo ameteka mchakato wa BBI, kwa lengo la kumweka kando Bw Odinga.Hapo ndipo kuliibuka madai ya uwezekano wa kiongozi huyo wa ODM kushirikiana na Naibu Rais Dkt William 2022 na hivyo kusababisha wasiwasi katika kambi ya Rais Kenyatta.

Ni wakati huo ambapo mwenyekiti wa ODM John Mbadi na Mbunge wa Ugunja Opiyo Wandayi walionya kwamba huenda handisheki ikasambaratika ikiwa Rais Kenyatta hataingilia kati na kurekebisha hali.Hata hivyo, walisema kuwa Bw Odinga yu mbioni kubuni muungano mwingine wa kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022.

Ilidaiwa kuwa washirika watarajiwa katika muungano huo ni; waziri wa zamani Mukhisa Kituyi, Gavana Kivutha Kibwana (Makueni) Charity Ngilu (Kitui) miongoni mwa wengine.

Hii ni baada ya fununu kutokea kwamba huenda Rais Kenyatta anaunga mkono muungano changa wa One Kenya Alliance unaoshirikisha waliokuwa vinara wenzake katika uliokuwa muungano wa upinzani (Nasa).

Wao ni Kalonzo Musyoka (Wiper), Musalia Mudavadi (ANC) na Moses Wetang’ula (Ford Kenya); na ambao wameshirikiana na mwenyekiti wa Kanu Gideon Moi.

Mbw Bichachi na Mwamu wanakubaliana kwamba, Bw Odinga atatoa mwelekeo kuhusu iwapo itawania urais au la kutegemea msimamo wa mwisho ambao Rais Kenyatta atatoa kuhusu suala hilo.

Dkt Ruto akiungana na Raila, kipi kitarajiwe Mlima Kenya 2022?

Na MWANGI MUIRURI

HABARI kuwa Naibu Rais Dkt William Ruto na kiongozi wa ODM Raila Odinga wanaweza wakaungana kusaka urais katika uchaguzi mkuu wa 2022 zimezua hisia mseto Mlima Kenya.

Hofu ni kuwa, ikiwa hilo litafanyika, eneo hilo ambalo limekuwa katika uongozi wa taifa hili katika serikali tatu tangu uhuru (Hayati Mzee Jomo Kenyatta 1963-1978, Mwai Kibaki 2002-2013 na Uhuru Kenyatta 2013 hadi sasa) litatengwa na lijipate katika upinzani.

Mchanganuzi wa kisiasa Bw Gasper Odhiambo anasema Dkt Ruto akiungana na Bw Odinga, basi itakuwa ni njia ya uhakika ya kuadhibu upande wa Rais Kenyatta iwapo kiongozi wa nchi atasaliti ahidi ya ‘Yangu Kumi na ya Ruto Kumi’.

“Ni hali inayoweza kuitupa jamii ya Rais katika pipa la giza kisiasa,” asema Bw Odhiambo.

Hata hivyo, anasema muungano wa Dkt Ruto na Bw Odinga unaweza ukasambaratishwa na Mlima Kenya nao wakiamua kujipanga upya na kusaka muungano wao kwa kuwa naye Bw Odinga anatengwa na Musalia Mudavadi wa ANC, Kalonzo Musyoka wa Wiper, Moses Wetang’ula wa Ford Kenya na Gideon Moi wa Kanu.

“Ukiangalia mpangilo huo, utapata kwamba Dkt Ruto na Bw Odinga wakiungana halafu Mlima Kenya ijitenge nao kabisa, basi huenda wasifaulu,” asema.

Anasema kuwa ule muungano hatari kwa Mlima Kenya ni ule ambao utawaleta pamoja Mudavadi, Kalonzo, Moi na Wetang’ula kisha Bw Odinga na Dkt Ruto waungane nao akisema kuwa hali kama hiyo itawaacha wapigakura wa Mlima Kenya wakiwa peke yao dhidi ya Wakenya wengine wote.

“Hao wote wakija pamoja dhidi ya Mlima Kenya na wapate mbinu ya kukubaliana kuhusu mwaniaji mmoja ambaye atakuwa ama Dkt Ruto au Bw Odinga na hawa wengine wote watii, basi hapo ndipo taharuki ya Gema kutengwa itaibuka, lakini sio katika hali nyingine yoyote ya miungano,” aeleza.

Hata hivyo, walio katika mrengo wa ‘Tangatanga’ ambao hufuata Dkt Ruto wamepuuzilia mbali muungano huo wakisema hata ukiibuka na utekelezwe, kile kitafanyika hakitaathiri uwezo wa Mlima Kenya kuwa ndani ya serikali.

“Habari hizo zilitokana na mahojiano ya Dkt Ruto na kituo cha Radio Citizen ambapo alikuwa muwazi kwamba ikiwa ataungana na Bw Odinga, itakuwa ni ODM ije ndani ya ‘Tangatanga’ wala sio sisi tuwaendee. Ina maana kuwa atakuja kwa masharti yetu,” akasema Mbunge wa Mathira Bw Rigathi Gachagua.

Bw Gachagua anasema kuwa msimamo wa ‘Tangatanga’ ni kuwa hata muungano wa kisiasa uwe wa nani kati ya mwingine nani au chama gani na kingine kipi, ni lazima iwe Dkt Ruto ndiye atakuwa mgombea wa urais.

Ikiwa Bw Odinga atajiunga na Dkt Ruto basi “aridhike na nafasi ya Waziri Mkuu na hilo itabidi kwanza BBI ipitishwe katika referenda na kisha awanie ubunge, ashinde ndipo ateuliwe kuwa Waziri Mkuu.”

Pendekezo la wadhifa wa Waziri Mkuu katika BBI ni kwamba atakayeteuliwa ni lazima awe mbunge.

Bw Gachagua alisema kuwa ikiwa Dkt Ruto ataingia kwa muungano wa kisiasa na Bw Odinga na akubali kutowania urais (Dkt Ruto) “basi sisi tutajitoa na tupange upya mikakati yetu ya kisiasa kwa kuwa Bw Odinga kamwe hawezi kuwa chaguo letu la kisiasa na hakuna vile tutamuunga mkono kama Mlima Kenya ndio awe rais.”

Seneta wa Murang’a Bw Irungu Kang’ata alisema huo muungano unaosemwa sio mbaya ila tu eneo la Mlima Kenya “limeamua kuwa mwaniaji wao wa urais ni Dkt Ruto wala sio mwingine yeyote na ikiwa hilo litasambaratika kupitia mikakati yoyote ile itaibuka katika miungano ya kisiasa, basi tuko tayari kuanza kujipanga upya.”

Aliyekuwa mbunge wa Gatanga Bw Peter Kenneth alisema kuwa uwezekano huo wa Dkt Ruto na Bw Odinga ni kiini cha kuwatuma wanasiasa wote wa Mlima Kenya kwanza waungane na wapange mikakati yao ya 2022 wakielewa kuwa “hata kina nani waungane Kenya hii, sisi tukiwa na umoja wetu wa kura na tukatae katakata kuzigawa katika debe, tutawatatiza pakubwa.”

Alisema kuwa hali ya siasa ni sawa na jinsi mto mkubwa hupewa maji na mito midogo katika safari ya kujaza bahari.

“Hii ina maana kuwa sisi kama walio na asilimia 35 ya kura zote hapa nchini, ikiwa tunatumbukiza katika kapu moja kisiasa, tunahitaji tu asilimia 16 ya nyongeza ya kura ili tuibuke na ushindi. Hakuna sheria imeundwa Kenya hii ya kutuzuilia kuwania urais na ikiwa mito midogo hupea maji mto mkubwa, hata wakiungana, kinga yetu ni umoja wetu,” akasema Bw Kenneth.

Bw Kenneth alisema kuna haja kubwa ya wanasiasa wa Mlima Kenya sasa kutupilia mbali tofauti zao na kwanza wavunje mirengo yao hasidi ya kisiasa na cha maana kama hali ya dharura, waungane na waanze kuongea kwa sauti moja ili uzito wao wa kura utambulike na uheshimiwe.

Alisema kuwa “tukiungana, liwe liwalo tutakuwa ndani ya serikali ya baada ya 2022 tukiwakilishwa na mtu wa eneo hili ama katika wadhifa wa rais, naibu wa rais au waziri mkuu.”

Kwa mujibu wa Seneta wa Nyeri Ephraim Maina, “nimekuwa nikionya kuwa tunapelekwa mbio isiyofaa na baadhi ya wanasiasa wetu ambao tangu 2013 wamekuwa wakituchuuza kwa mirengo fulani ya kisiasa bila kuzingatia athari za kutokuwa na subira darubini ya kisawasawa ipigwe kujua tunaelekezwa wapi na ni wapi kunatufaa zaidi.”

“Rais Kenyatta amekuwa akihofia hilo la kutengwa kufanyika na ndipo amekuwa akisisitiza umuhimu wa BBI ambayo inaunda serikali pana inayojumuisha maeneo hapa nchini kulingana na kura zao na kisha kugawa rasilimali kulingana na idadi ya watu,” akasema Bw Maina.

Bw Maina ameambia Taifa Leo “hii ndiyo hali ambayo Rais amekuwa akijaribu kuzima na ndiyo hali wale ambao wanatuchuuza kwa mrengo wa Dkt Ruto wamekuwa wakipinga bila kuzingatia kwamba kiongozi wa nchi huwa na ufahamu zaidi wa mitindo na njama za wanasiasa kupitia habari za ujasusi.”

Akasema: “Rais alijua haya yalikuwa na uwezekano wa kutokea na ndipo akazindua mpango wa kuhakikisha eneo la Mlima Kenya huwa linapangiwa njama za kulitenga kisiasa kutokana na wingi wa kura zao na mtindo wao wa kupendelea mwaniaji wao katika uchaguzi wa urais.”

Aliyekuwa mbunge wa Maragua Bw Elias Mbau naye akasema kuwa “sasa ni wazi kuwa busara ya Rais Kenyatta ya kuwataka watu wa Mlima Kenya waunge mkono mchakato wa BBI ilikuwa na kiini cha kumulika uwezekano wa kutengwa kwa Mlima Kenya.”

Hata hivyo, mchanganuzi wa kisiasa Prof Ngugi Njoroge anauliza: “Hili la kutiwa hofu kuwa huenda Mlima Kenya wakatengwa kisiasa na waingie upinzani lina mashiko kweli? Kuna ushahidi kuwa wapigakura wa eneo hilo wana tamaa ya kuwa ndani ya serikali?”

Anauliza pia: “Wakati wenyeji wa Mlima Kenya walianza kuonyesha nia ya kuunga mkono mwingine katika wadhifa wa urais 2022, ilikuwa ni ishara kuwa wamechoka kuhusishwa na serikali haswa baada ya kuibuka kuwa wadhifa huo huwa hauwasaidii sana kumaliza shida zao?”

Anasema kuwa hata miungano iundwe kwa msingi upi, Wakenya watafanya maamuzi yao “na sioni ule msukumo mkubwa wa jadi Mlima Kenya wa kupambana kufa kupona kuwa ndani ya serikali kama upo kwa sasa.”

“Wenyeji wamechoka kujumuishwa ndani ya ukabila wa kuwindia mtu binafsi ukubwa na hatimaye kuachwa kwa mataa kila mmoja wao akipambana na hali yake,” akasema.

Uhuru asukuma Ruto, Raila kona moja

WANDERI KAMAU na BENSON MATHEKA

HATUA ya Rais Uhuru Kenyatta kuonekana kupendelea muungano mpya wa ‘One Kenya Alliance’ imewasukuma naibu wake William Ruto na Kiongozi wa ODM Raila Odinga katika kona moja kisiasa.

Kwa kuhisi kusalitiwa na Rais, wawili hao wameanza kuelekeza makombora kwa muungano huo unaoshirikisha Musalia Mudavadi, Kalonzo Musyoka, Gideon Moi na Moses Wetangula, wakiutaja kama unaogawanya Wakenya kikabila badala ya kuwaunganisha kupitia vyama vyenye sura ya kitaifa.

Alhamisi, Dkt William Ruto alisema yuko tayari kufanya kazi na Bw Odinga, akieleza kuwa tofauti zao ni za kisiasa, lakini hilo halimaanishi hawawezi kushirikiana.

“Baadhi ya watu hudhani nina tatizo na Bw Odinga. Huo si ukweli. Tofauti hizo ni za kisiasa. Hata hivyo, kuna mambo ninayokubaliana naye, kama vile kubuniwa kwa vyama vya kisiasa vya kitaifa. Anakabiliwa na changamoto sawa ninazokumbwa nazo kutoka kwa viongozi wa kikabila. Tunaweza kushirikiana na kufanya kazi pamoja,” akasema Dkt Ruto.

Wawili hao wamekuwa maadui sugu kisiasa hasa kuhusu handisheki na BBI, lakini muungano wa ‘One Kenya Alliance’ umejitokeza kuwa kifaa kinachowaleta pamoja.

Matamshi ya Dkt Ruto jana yalitokea katika kipindi ambapo viongozi wanaoegemea mrengo wake chini ya chama cha United Democratic Alliance (UDA), wamekuwa wakijiegemeza upande wa wandani wa Bw Odinga bungeni.

Mnamo Ijumaa, maseneta wanaoegemea UDA waliunga mkono hatua ya ODM ya kumpokonya Seneta wa Kakamega, Cleophas Malala wa ANC wadhifa wa kiongozi wa wachache katika Seneti.

Maseneta wa ODM nao wamekubaliana na washirika wa naibu rais, kwamba bunge lifanyie mabadiliko mswada wa BBI hasa kipengele kuhusu maeneobunge mapya, jambo ambalo limepingwa na Jubilee.

Hivi majuzi, Seneta wa Siaya, Bw James Orengo aliongoza wandani wengine wa Bw Odinga kukashifu watumishi wa umma ambao wanadaiwa kula njama ya kuiba kura za urais 2022. Malalamishi kama haya yamekuwa yakitolewa kwa muda mrefu na Dkt Ruto.

Alhamisi, ODM ilidokeza uwezekano wa kuunda muungano wa kisiasa, ambao ilisema hautarajiwi na wengi.

“Rekodi yetu ya kuunda miungano, kujenga daraja na wanaochukuliwa kuwa maadui wetu na kuwakuza viongozi vijana wenye nguvu inajulikana. Kwa mara nyingine, tunapanga kufanya hivyo,” alisema Katibu Mkuu Edwin Sifuna.

Sawa na Dkt Ruto, Bw Sifuna alipuuzilia mbali “Kenya Moja Alliance” akiutaja kama muungano wa kikabila.

Wadadisi wa siasa wanasema si vigumu kwa Dkt Ruto na Bw Odinga kushirikiana tena kisiasa, kwani waliwahi kuwa pamoja katika ODM mnamo 2007, kupitia kundi la ‘Pentagon.’

“Hawa ni wanasiasa wenye uzoefu mkubwa. Wanafahamiana kwa undani kwani washawahi kuwa pamoja hapo awali. Huenda isiwe vigumu kwao kuungana tena,” akasema mchanganuzi wa siasa Javas Bigambo, kwenye mahojiano na Taifa Leo.

Lakini washirika wa ‘One Kenya Alliance’ wamejitetea wakisema wao ndio wa kuaminika kutatua changamoto zinazokumba nchi.

Katika kikao cha wanahabari jana, viongozi hao walidai ODM imethibitisha haiwezi kuaminika kwa kukiuka makubaliano ya awali katika muungano wa NASA ambapo vyama tanzu husisitiza kulikuwa na makubaliano Bw Odinga asiwanie urais tena 2022.

“Leo tunaanza safari tukiwa na lengo la kuunganisha nchi kupitia ajenda ya mabadiliko ambayo itabuni nafasi kwa Wakenya wote. Muungano huu ni pumzi safi kutoka kwa siasa za migawanyiko ambazo nchi imekuwa ikishuhudia,” akasema Bw Musyoka.

Muungano huo pia ulitangaza utaunga mkono wawaniaji wa ODM kwenye chaguzi ndogo dhidi ya wale wa ODM.

Matukio haya yanatarajiwa kutatiza juhudi za Rais Kenyatta kuleta pamoja vigogo wote wa kisiasa dhidi ya Dkt Ruto.

Uhuru ataweza Raila na Ruto?

Na BENSON MATHEKA

SIKU moja baada ya viongozi wa chama cha ODM kulalama kuwa kuna njama ya Rais Uhuru Kenyatta kumsaliti kiongozi wao Bw Raila Odinga, maswali yameibuka kuhusu iwapo Rais atafanikiwa kumlemea waziri huyo mkuu wa zamani pamoja na Naibu Rais William Ruto katika uchaguzi wa 2022.

Mnamo Jumamosi, Seneta wa Siaya, Bw James Orengo alidai kuwa baadhi ya maafisa wa serikali ambao hakuwataja majina wanapanga njama za kuhujumu ushirikiano kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga wakilenga kumzuia kushinda urais ilivyofanyika kwenye uchaguzi wa 2007, 2013 na 2017.

Bw Odinga na washirika wake wanaamini kwamba alishinda urais kwenye chaguzi hizo lakini akaibiwa kura, juhudi ambazo wanadai ziliongozwa na watu waliokuwa na ushawishi serikalini.

Pamezuka minong’ono kuwa iwapo Rais Uhuru atamkwepa Bw Raila katika uchaguzi mkuu ujao, pana uwezekano mkubwa wa ama kinara huyo wa chama cha Chungwa kuungana na Dkt Ruto au kila mmoja kati yao awanie kivyake kupingana na chaguo la Bw Uhuru.

Duru zinasema kwamba Rais Kenyatta huenda akaubariki muungano unaonukia kati ya kiongozi wa chama cha Amani National Congress (ANC), Bw Musalia Mudavadi, mwenyekiti wa chama cha Kanu, Bw Gideon Moi, Bw Kalonzo Musyoka wa Wiper na Moses Wetangula wa chama cha Ford Kenya.

Wanne hao waliungana katika kampeni za uchaguzi mdogo wa maeneobunge ya Matungu, Kaunti ya Kakamega ambao Peter Nabulindo wa ANC alimshinda David Were wa ODM na Kabuchai ambako Majimbo Kalasinga wa Ford Kenya alishinda.

Duru zinasema kwamba wandani wa Bw Odinga wanaamini kwamba watu wenye ushawishi serikalini walisaidia kuangushwa kwa mwaniaji wa chama cha ODM katika uchaguzi mdogo wa Matungu ili kumsawiri kiongozi wa chama chao kama aliyepungua umaarufu.

Mudavadi, Kalonzo na Wetangula ambao walikuwa washirika wa Bw Odinga kwenye muungano wa NASA katika uchaguzi mkuu wa 2017 wameashiria kuwa wataungana na Moi kwenye uchaguzi mkuu wa 2022 bila Raila. Mshirika mmoja wa Bw Odinga alisema kuna mipango ya Rais Kenyatta kumteua mwanasiasa kutoka Mlima Kenya kuungana na wanne hao huku yeye Rais akiwa mdhamini wao mkuu.

Ikiwa madai ya ODM ni ya kweli, huenda mabadiliko makubwa ya kisiasa yakashuhudiwa kabla au baada ya kura ya maamuzi. Wadadisi wanasema iwapo atamtema Bw Odinga, Rais Kenyatta atakuwa ameongeza mahasimu wake kisiasa ikizingatiwa kuwa uhusiano wake na Dkt Ruto umeingia doa.

“Siasa za usaliti, kutumiwa na kuzimwa si ngeni nchini Kenya na chanzo chake huwa si viongozi walio mamlakani bali huwa ni wanaofaidika na uongozi wao. Hapa ninazungumzia wanaolinda mamlaka na huwa wana nguvu sana,” asema mdadisi wa siasa Geoffrey Kamwanah.

Kumtema Raila na kumuunga yeyote katika muungano wa Mudavadi, Kalonzo, Moi na Wetangula, kunaweza kuunganisha Bw Odinga na Dkt Ruto tena licha ya wawili hao kushambuliana kuhusu handisheki na mchakato wa kubadilisha katiba.

Wadadisi wanasema kwamba wawili hao wanaweza kuungana kumkabili adui mmoja au kila mmoja agombee kivyake wakielekeza mishale yao kwa Rais Kenyatta.

“Dkt Ruto alimsaidia Uhuru kuingia mamlakani lakini akamtema, Raila alimsaidia kumtema Ruto na kuongoza kwa utulivu katika kipindi chake cha pili. Bila shaka Uhuru atakuwa na wakati mgumu kuuza chaguo lake kwa kuwa ataonekana msaliti,“ aeleza Bw Kamwanah.

Hisia za wandani wa Bw Odinga na Dkt Ruto ni kuwa Rais Kenyatta aliwatumia kutimiza maslahi yao ya kisiasa na kuwagonganisha wasishirikiane kisiasa ili chaguo lake lisiwe na upinzani mkubwa kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Handisheki ilivunja chama cha Jubilee ambacho ilitarajiwa Dkt Ruto angetumia kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu ujao na muungano wa Nasa ambao uliipa Jubilee ushindani mkali chini ya Bw Odinga.

Hata hivyo, Dkt Ruto amefaulu kujenga chama cha United Democratic Alliance (UDA) kupitia kampeni yake ya hasla na umaarufu wake umeongezeka nchini ikiwemo ngome ya Rais Kenyatta ya Mlima Kenya.

Wadadisi wanasema kuwa Bw Odinga ni mwanasiasa mzoefu anayeweza kusambaratisha mipango ya Rais Kenyatta ukiwemo mchakato wa kubadilisha katiba wa BBI akihisi kwamba anahujumiwa.

Bw Raila alitarajiwa kuzungumzia tetesi hizo za kusalitiwa katika uwanja wa Kamukunji, Kibera, Nairobi, Jumapili lakini baadaye ikasemekana kuwa Ikulu iliingilia kati na kumshauri kutohudhuria huku suluhu ikitafutwa.

Sihitaji BBI kuingia Ikulu, Raila asisitiza

WYCLIFFE NYABERI na VALENTINE OBARA

KIONGOZI wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga amejipiga kifua na kusema hahitaji msaada kupitia kwa Mpango wa Maridhiano (BBI) ili awe rais.

Akipuuzilia mbali wanasiasa wanaodai kuna njama ya viongozi wanaopigia debe marekebisho ya katiba kuitumia kama ngazi ya kuingia mamlakani kwa urahisi, Bw Odinga Ijumaa alisema akiwania urais wananchi watamchagua.

“Hii BBI sio eti ni Raila anatumia mlango wa nyuma kuingia Ikulu. Raila akitaka kuenda Ikulu wananchi watampeleka. BBI ni kitu ambacho kitadumu na kusaidia hadi vizazi vijavyo katika taifa letu,” akasema.

Alikuwa akihutubia waombolezaji waliohudhuria ibada ya mazishi ya aliyekuwa mbunge wa Bonchari, Oroo Oyioka.

Ibada hiyo ilifanyika katika Shule ya Upili ya Wavulana ya Itierio, Kaunti ya Kisii.

Kufikia sasa, Bw Odinga hajatangaza wazi ikiwa atawania urais mwaka wa 2022 ingawa hotuba zake za hivi karibuni zinaashiria ana mipango ya kuwania.

Gavana wa Mombasa Hassan Joho pekee ndiye amewasilisha ombi la kutaka kushiriki mchujo wa atakayepeperusha bendera ya ODM kwa urais mwaka 2022.

Chama hicho mnamo Alhamisi kiliongeza muda kwa wanaotaka kushiriki mchujo huo hadi Machi 31.

Bw Odinga akizungumza baadaye jana katika eneobunge la Ugunja, Kaunti ya Siaya, alisisitiza hatatangaza kama atawania urais hadi mpango wa kurekebisha katiba utakapokamilika.

Suala la kuwa marekebisho ya katiba ni njama ya kisiasa inayohusu urais 2022, limekuwa likivumishwa kwa muda mrefu na Naibu Rais William Ruto na wandani wake.

Mkutano ulioongozwa na Rais Uhuru Kenyatta katika Ikulu ya Nairobi mnamo Alhamisi ambao ulihudhuriwa na Bw Odinga, Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, mwenzake wa Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi na Seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula (Ford Kenya), uliibua upya mjadala kuhusu uwezekano wa wanaounga mkono BBI kuungana dhidi ya Dkt Ruto ifikapo 2022.

Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Seneta wa Baringo Gideon Moi anayeongoza Chama cha KANU, na Gavana wa Kitui Charity Ngilu aliye kiongozi wa Narc.

Katika taarifa iliyotolewa baada ya mkutano huo, walisema ulikuwa ni wa kujadili mipango ya kurekebisha katiba.

Ijumaa, Dkt Ruto alipokuwa katika Kaunti ya Nandi, alirejelea matukio hayo na kusisitiza hatababaishwa katika azimio lake la kumrithi Rais Kenyatta atakayestaafu urais mwaka 2022.

“Wanaume wamenipangia kule Nairobi lakini mimi niko na wananchi hapa chini. Wanatuambia watatupangia serikali kule Nairobi wakisema wale wadosi watatupangia. Mimi nawaambia serikali ya 2022 haiwezi kupangwa hivyo,” akasema.

Bw Odinga alisisitiza kuwa, mpango wake na Rais Kenyatta kuhusu BBI ni kuleta umoja wa nchi.

Alifichua kwamba Rais alikuwa amemdokezea mpango wa mabunge ya kaunti za Mlima Kenya kupitisha mswada wa urekebishaji katiba Jumanne iliyopita, na ikawa hivyo.

“Sisi tunasema Wakenya wataendelea mbele wakiwa na umoja. Gurudumu sasa limeenda kwa bunge (la kitaifa na seneti). Ikitoka kwa bunge itakuja mashinani kwa wananchi na tutakuja kuwaambia zaidi kuhusu ubora wa BBI,” akasema.

Kaunti za Nandi na Baringo pekee ndizo zimekataa kupitisha mswada huo kufikia sasa.

Raila amtetea Ruto

Na WAANDISHI WETU

KIONGOZI wa ODM, Bw Raila Odinga amewataka wabunge kutupilia mbali mswada unaolenga kuharamisha matumizi ya kaulimbiu ya ‘Hasla’ inayotumiwa na Naibu Rais William Ruto katika mikutano yake ya kampeni.

Bw Odinga alisema kuwa Naibu Rais pamoja na wandani wake hawafai kuzuiliwa kutumia kaulimbiu hiyo ambayo inahofiwa na baadhi ya viongozi kwamba huenda ikazua vita baina ya Wakenya maskini na mabwanyenye.

Katika juhudi za kuzima kampeni za Dkt Ruto zinazotoa taswira ya ulinganisho baina ya watu wa mapato ya chini na matajiri, kuna wabunge wanaopendekeza mswada unaopiga marufuku kauli hiyo katika mikutano ya kisiasa.

Wabunge wanapendekeza kiongozi anayepatikana na hatia ya kusababisha chuki za matabaka ya kiuchumi aondolewe ofisini.

Ikiwa mswada huo utapitishwa kuwa sheria, itakuwa pigo kwa kampeni ambazo Dkt Ruto amekuwa akitumia kupigia debe azma yake ya kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Dkt Ruto na wandani wake wamejipachika nembo ya mahasla wakidai kwamba matajiri wanataka kukwamilia mamlakani.

Amekuwa akiandaa mikutano kote nchini kuendeleza kampeni hiyo akitaja handisheki kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Bw Odinga kama muungano wa matajiri wanaotaka kubadilisha katiba kuwanyima watu wa mapato ya chini nafasi ya kuongoza.

Rais Kenyatta na Bw Odinga, wamekosoa kampeni hiyo wakisema inalenga kusababisha vita vya matabaka. Bw Odinga amekuwa akisisitiza kuwa familia yake na ya Rais Kenyatta zilitoka katika usuli wa kimaskini.

Mswada huo uliopendekezwa na Kamati ya Usalama ya Bunge chini ya uwenyekiti wa mbunge wa Kiambaa, Bw Paul Koinange, unapendekeza faini ya Sh5 milioni kwa wanaopatikana na hatia ya kugawanya Wakenya kwa misingi ya matabaka.

Kwenye mkutano na kamati ya usalama ya bunge mapema mwaka huu, Mwenyekiti wa NCIC, Bw Samuel Kobia alisema kampeni ya mahasla dhidi ya matajiri inaweza kutumbukiza nchi katika ghasia.

Alisema kampeni hiyo ni hatari nchi inapoelekea katika uchaguzi mkuu mwaka 2022.

Alipohutubia viongozi wa eneo la Mlima Kenya mwanzoni mwa mwezi huu, Rais Kenyatta pia alisema kampeni hizo zinawagawanya Wakenya kwa misingi ya matabaka.

Jumatano, waziri mkuu wa zamani, Bw Raila, alipomtetea Dkt Ruto kupitia mtandao wa kijamii, alisema hivi:

“Nimefahamishwa kwamba kuna mswada ambao unalenga kupiga marufuku kaulimbiu ya ‘mahasla’ yake Naibu wa Rais Ruto. Mswada huo unapendekeza adhabu kali kwa watakaopatikana wakitumia kauli hiyo.

“Hali sawa na hiyo ilitokea mnamo 1933 na 1945 nchini Ujerumani ambapo kiongozi wa nchi Adolf Hitler alichochea mauaji ya halaiki kwa misingi ya matabaka ya kiuchumi, rangi na kabila.” Kiongozi huyo wa ODM alisema kuwa japo anahofia kuwa matumizi ya kaulimbiu ya ‘mahasla’ huenda ikasababisha fujo nchini, Dkt Ruto pamoja na wandani wake hawafai kuzuiliwa kwani wana haki ya kujieleza.

“Badala yake, japo sisi tunaohofia kwamba huenda kauli hiyo ikazua machafuko nchini, tuna jukumu la kuelimisha Wakenya waiepuke ili wasijehadaiwa. Nina imani Wakenya watajua ukweli na kujitenga na udanganyifu huo,” akasema Bw Odinga.

Wandani wa Dkt Ruto wakiongozwa na Seneta wa Elgeyo Marakwet , Bw Kipchumba Murkomen, hata hivyo, jana walipuuzilia mbali madai kwamba wanagawanya Wakenya.

“Sisi hatujawahi kugonganisha maskini dhidi ya matajiri. Tumekuwa tukihimiza kwamba maskini (mahasla) wawezeshwe kujiinua kimapato,” akasema Seneta Murkomen.

Dkt Ruto amekuwa akijiita hasla huku akisema kuwa aliishi maisha ya umaskini ambapo aliuza kuku katika eneo la Turbo, Uasin Gishu kabla ya kuwa bwanyenye.

Wabunge wengine wanaoegemea upande wa Dkt Ruto walisema msimamo wao ni kutetea vijana ambao wengi wao huteseka kwa kukosa ajira.

Leonard Onyango, Benson Matheka na Onyango K’Onyango

ODM wahofia Jubilee inakoroga Raila

Na JUSTUS OCHIENG

CHAMA cha ODM kimeeleza hofu kwamba barua ambayo seneta wa Murang’a Irungu Kang’ata aliandikia Rais Uhuru Kenyatta kumweleza kuwa eneo la Mlima Kenya haliungi mkono BBI, ni njama ya kumsaliti kiongozi wake Raila Odinga katika handisheki yake na Rais Uhuru Kenyatta.

Baadhi ya maafisa wa chama hicho wanasema ingawa Bw Kang’ata alikiri kuandika barua hiyo, wanashuku alitumiwa kufanya hivyo kutoa ujumbe kwamba BBI haiungwi mkono na Wakenya hasa katika ngome ya Rais Kenyatta ya Mlima Kenya.

“Kusema kwamba Bw Kang’ata aliandika barua hiyo peke yake na kutumia mbinu alizotumia kupitisha ujumbe wake kwa umma ni kudaganya,” alisema mwekahazina wa kitaifa wa ODM Timothy Bosire.

Kulingana na Bw Bosire, barua hiyo inafanya Wakenya kuamini baadhi ya watu wamebadilisha nia kuhusu BBI.

Bw Kang’ata alikiri kwamba hakutoa barua hiyo kwa wanahabari na kulaumu viongozi wa chama cha Jubilee aliowatumia nakala kwa kufanya hivayo.

Alisema kuwa alituma nakala ya barua hiyo kwa Katibu Mkuu wa Jubilee Raphael Tuju, Kiongozi wa Wengi katika Seneti Samuel Poghisio, Mwenyekiti wa Jubilee Nelson Dzuya na wanachama wa kamati kuu ya chama hicho inayohusisha maafisa wote wa kitaifa.

Lakini Bw Bosire alitilia shaka nia ya barua hiyo akisema Bw Kang’ata ni mwanasheria anayefahamu utaratibu wa kuwasiliana na Rais.

“Bw Kang’ata ni mwanasheria anayefahamu athari za mawasiliano kama hayo na anaelewa itifaki zote na mbinu za kuwasiliana na Rais,” alisema.

Bw Tuju alikanusha kupokea barua hiyo na akamlaumu Bw Kang’ata kwa kumwandikia Rais moja kwa moja bila kushauriana na maafisa wa chama.

Msemaji wa Ikulu Kanze Dena alikataa kuthibitisha iwapo Rais Kenyatta alipokea barua hiyo.

Jumanne, kaka ya Bw Odinga, Dkt Oburu Oginga aliwalaumu washirika wa Naibu Rais William Ruto kuhusu madai ya Bw Kang’ata akisema wanafanya kila juhudi kuhujumu BBI na kuharibu uhusiano wa Bw Odinga na Rais Kenyatta.

“Hii sio mara ya kwanza wao kufanya hivyo. Wamewahi kufanya hivyo na wanafaa kufahamu kwamba ujanja wao hautafaulu,” Dkt Oburu aliongeza.

Kwenye barua yake, Bw Kang’ata alimweleza wazi Rais Kenyatta kwamba wakazi wa eneo la Mlima hawaungi BBI mkono.

“BBI si maarufu eneo la Mlima Kenya. Kwa kila watu kumi niliozungumza nao, sita wanaikataa, wawili wanaiunga na wawili hawajafanya uamuzi,” Seneta Kang’ata alimweleza Rais.

Alimuomba Rais Kenyatta kuchukua hatua ili kuepuka aibu ya kukataliwa kwa mchakato huo kwenye kura ya maamuzi.

Washirika wa Dkt Ruto walimuunga mkono Bw Kang’ata na kusema watapinga juhudi zozote za kumpokonya wadhifa wa Kiranja wa Wengi katika Seneti kuhusiana na kauli yake kuhusu BBI.

Seneta Kipchumba Murkomen wa Elgeyo Marakwet alisema ingawa Bw Kang’ata aliongoza juhudi za wandani wa Dkt Ruto kupokonywa nyadhifa katika Seneti mwaka jana, hawatalipiza kisasi dhidi yake mbali watamtetea.

“Iwapo uongozi wa Jubilee utaitisha mkutano wa kumwondoa Kang’ata, tutahudhuria na kupinga vikali kufurushwa kwake… Haijalishi alivyonitendea mimi na Susan Kihika,” akasema Bw Murkomen jana.

AFYA: Ruto amsuta Raila

Na CHARLES WASONGA

NAIBU Rais William Ruto amemshutumu aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga kwa kudunisha matakwa ya wahudumu wa afya walioko mstari wa mbele katika vita dhidi ya janga la Covid-19 nchini.

Akiongea katika Kaunti ya Kericho Dkt Ruto alisema Jumanne hatua ya Bw Odinga kuweka kando masuala yanayowaathiri wahudumu wa afya wakati huu wa janga lililoathiri uchumi na kusababisha vifo inaonyesha kuwa yeye (Odinga) ni kiongozi asiyewajibika.

“Haina maana mtu kusema masuala ya kisiasa kama vile marekebisho ya katiba kupitia mswada wa BBI yanapaswa kushughulikiwa kwanza kabla ya malalamishi yaliyoibuliwa na wahudumu wa afya ilhali wao ndio wanajeshi wetu katika vita dhidi ya janga la corona,” akasema Dkt Ruto.

Alikuwa akiongea katika Kericho Golf Club wakati wa ibada ya mazishi ya Kanali Jenerali (Mstaafu) John Koech aliyefariki majuzi.

Dkt Ruto aliwataka viongozi kulipa kipaumbele suala hili la janga la Covid-19 ambalo limevuruga uchumi badala ya masuala mengine kama vile mchakato wa kura ya maamuzi kupitia mswada wa BBI.

Mnamo Jumatatu Bw Odinga aliwataka wahudumu wa afya wanaogoma kuweka kandao matakwa yao wakati huu ambapo Kenya inakabiliwa na changamoto ya kiuchumi iliyosababishwa na janga la corona.

Akiongea mjini Kisumu, Bw Odinga aliwataka wahudumu hao kuendelea kushiriki mazungumzo na serikali kuu na zile za kaunti ili kupata muafaka kuhusu matakwa yao badala ya kugoma.

“Mgomo utasababisha hali ya sasa kuwa mbaya zaidi. Hii ni kwa sababu sio wahudumu wa afya pekee walioathirika na janga hili bali wananchi kwa ujumla,” akasema.

Lakini Jumanne Dkt Ruto akamjibu kwa kusema: “Tunafaa kulenga kuwapa wahudumu wa afya vifaa-kinga (PPE) na tuwalipe mishahara na marupurupu hitajika. Serikali za kaunti zinastahili kuyapa kipaumbele masuala yaliyoibuliwa na madaktari, wauguzi, maafisa wa kliniki na vitengo vingine vya wahudumu wa afya ambao wako katika mstari wa mbele katika vita dhidi ya janga la corona.”

Naibu Rais alisema serikali kuu imeagiza wizara ya afya kushirikiana na viongozi wa vyama vya kutetea masilahi ya wahudumu wa afya kusuluhisha masuala yaliyoibuliwa na wanachama wao.

“Ikiwa taasisi zetu za afya zilikuwa zikifanya kazi vizuri, kuna uwezekano mkubwa kwamba Jenerali Koech hangefariki. Kama viongozi twapaswa kuchukulia masuala ya afya kwa uzito,” Dkt Ruto akasema.

Viongozi wa kisiasa walioandamana na Naibu Rais pia walimshambulia Bw Odinga kwa kuendeleza kampeni za marekebisho ya Katiba wakati kama huu ambapo janga la Covid-19 ni kero kwa taifa.

Miongoni mwa wanasiasa hao walikuwa Gavana wa Kericho Paul Chepkwony, naibu wake, Susan Kikwai, maseneta; Kipchumba Murkomen (Elgeyo Marakwet ); Millicent Omanga (Seneta Maalum); Aaron Cheruiyot (Kericho ); Florence Bore (Mbunge Mwakilishi wa Wanawake Kericho ); Nelson Koech (Mbunge wa Belgut); Johana Ngeno (Mbunge wa Emurrua Dikirr), Silvanus Maritim (Mbunge wa Ainamoi) na Katibu Mkuu wa Kanu Nick Salat.

Msigome, Raila aambia wahudumu wa afya

Na CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa ODM Raila Odinga amewataka wahudumu wa afya kuwa na subira huku mazungumzo kuhusu matakwa yao yakiendelea.

Akiongea mjini Kisumu Jumatatu, Novemba 7, 2020, Bw Odinga alisema janga la corona limeleta changamoto kubwa zaidi kwa sekta zote za uchumi wa nchi hii.

“Kuenea kwa virusi vya corona nchini kwa miezi mingi kumevuruga sekta zote za uchumi. Kwa hivyo, wahudumu wa afya wanapaswa kuelewa kwamba Wakenya wote wameathirika na sio wao pekee ndio wanafariki bali wananchi pia wanafariki kutokana na Covid-19,” akasema.

Alisema huu sio wakati wa kuishika serikali mateka.

“Madaktari wenyewe walikula kiapo kulinda maisha. Sasa mbona mgome wakati watu wanafariki,?” akauliza Bw Odinga.

Wito wa kiongozi huyo wa ODM unajiri saa chache baada ya chama cha madaktari nchini (KMPDU) kutangaza kusimamishwa kwa mgomo kwa muda wa siku 14.

Kwenye taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari na kaimu Katibu Mkuu wa chama hicho Chibanzi Mwachonda, chama hicho kilichukua hatua hiyo ili kutoa nafasi kwa mazungumzo na wadau kuhusu matakwa yao.

Kulingana na Dkt Mwachonda, uamuzi huo ulifikiwa baada ya mkutano wa baraza la kitaifa la ushauri la KMPDU ambalo lilijadili ombi la bunge la kitaifa na seneti kwamba wasitishe mgomo kutoa nafasi kwa mashauriano.

KMPDU ilisema kuwa inapanga kukutana na Kamati ya Bunge kuhusu Afya na ile ya Seneti kuhusu Afya, mnamo Jumatano na Alhamisi wiki hii.

Chama hicho kilisema kuwa mgomo huo utaanza mnamo Desemba 21, 2020, ikiwa mazungumzo hayo hayatazaa matunda.

“Ikiwa malalamishi yetu hayatashughulikiwa baada ya wiki mbili ya mazungumzo, mgomo utaanza mnamo Desemba 21,” akaonya Dkt Mwachonda katika taarifa hiyo.

Raila, Mudavadi kujipima nguvu Matungu

VALENTINE OBARA na SHABAN MAKOKHA

KIONGOZI wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga, amepuuzilia mbali wito wa viongozi wa eneo la Magharibi kwamba chama hicho kisiwe na mgombea wakati uchaguzi mdogo utakapoitishwa eneobunge la Matungu, Kaunti ya Kakamega.

Kiti hicho cha ubunge kinatarajiwa kutangazwa wazi hivi karibuni, kufuatia kifo cha mbunge James Murunga ambaye alizikwa Jumamosi.

Katika mazishi hayo, viongozi wa Chama cha ANC walitoa wito pasiwepo na ushindani katika uchaguzi mdogo kwani Bw Murunga alikuwa mwanachama wao.

Seneta wa Kakamega, Bw Cleophas Malala, alimwomba Bw Odinga afuate nyayo za Chama cha Jubilee ambacho kiliamua kutoshindana na ODM katika chaguzi ndogo kadhaa zilizopita tangu 2018, ikiwemo katika eneobunge la Msambweni.

“Tunaomba kiti cha Matungu kiachiwe chama cha ANC,” akasema Bw Malala.

Seneta wa Bungoma, Bw Moses Wetang’ula aliye pia Kiongozi wa Ford Kenya, aliashiria kwamba chama chake hakitakuwa na mgombeaji katika uchaguzi mdogo wa eneo hilo.

Alisema wamefanikiwa kupata umoja na Kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi, kwa hivyo anatarajia kutokuwapo ushindani kati yao katika uwaniaji wa ubunge eneo hilo wala Kabuchai, ambako mbunge James Mukwe Lusweti aliaga dunia Ijumaa.

Hata hivyo, Bw Odinga aliposimama kuhutubu alikemea wazo la kutaka kiti hicho kiachiwe ANC huku akikashifu viongozi kwa kuzungumzia suala la urithi wa ubunge kabla Murunga kuzikwa.

“Katika mila yetu hufai kuanza kutamani bibi (wa marehemu) kabla marehemu hajazikwa. Majuzi tulikuwa na uchaguzi Kibra kukawa na wagombeaji wa vyama vingine, na sasa wanasema ODM isiweke mgombeaji hapa. Kwa nini? Sisi tunafuata demokrasia,” akasema.

Tangu Bw Odinga alipoweka mwafaka wa maelewano na Rais Kenyatta almaarufu handisheki, Chama cha Jubilee kimekuwa kikikosa kusimamisha wagombeaji katika chaguzi ndogo kwenye ngome za ODM.

Chama hicho cha Jubilee husema hatua hiyo inanuiwa kutimiza malengo ya handisheki kama vile kuepusha uhasama wa kisiasa.

Hata hivyo, hatua hizo huwa hazipokewi vyema na Naibu Rais William Ruto.

Katika uchaguzi mdogo wa Kibra, Dkt Ruto alimpigia kampeni McDonald Mariga licha ya kuwa viongozi wengine wa chama hicho walisaidia ODM kumpigia debe Bw Imran Okoth.

Katika uchaguzi mdogo wa Msambweni, Dkt Ruto alilalamika alipogundua chama kimeamua hakitakuwa na mgombeaji.

Raila aendesha BBI chini ya maji

Na JUSTUS OCHIENG

KIONGOZI wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga, anaendeleza kampeni za kura ya maamuzi kwa mbinu ya kipekee huku akijiandaa kwa shughuli ya kukusanya sahihi za wapigakura.

Bw Odinga jana Jumanne alikutana na viongozi wa mabunge ya kaunti, siku chache baada ya kukutana na magavana wa eneo la Magharibi.

Mikutano mingine aina hiyo imeratibiwa kufanyika katika siku zijazo kwa lengo la kukabiliana na wanaopinga Mpango wa Maridhiano (BBI) na kushawishi wapinzani kujiunga na upande wa ‘ndiyo’ katika kura ya maamuzi inayotarajiwa baadaye.

Mbinu hii ya kuandaa mikutano na viongozi watakaotarajiwa kupenyeza ujumbe wa BBI almaarufu ‘reggae’ hadi mashinani, inaaminika kusababishwa na janga la corona, ambapo mikutano ya hadhara imepigwa marufuku.

Wikendi, Bw Odinga alihudhuria mkutano nyumbani kwa Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi (COTU) Francis Atwoli eneo la Kajiado, uliohudhuriwa pia na Mwenyekiti wa Kanu Gideon Moi, Naibu Mwenyekiti wa Jubilee David Murathe, Kiranja wa Wengi katika Bunge la Taifa Emmanuel Wangwe, Kiongozi wa Wachache katika Seneti James Orengo na Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Taifa, Bw Junet Mohamed.

“Meli imeng’oa nanga. Wasimamizi wamechaguliwa na Junet alihudhuria mkutano wetu kutueleza hatua ambazo wamepiga kuhusu mipango waliyo nayo. Kuanzia sasa, jambo muhimu litakuwa kuanza kukusanya sahihi,” akasema Bw Murathe.

Jana, Bw Odinga alifichua kwamba shughuli ya ukusanyaji sahihi za wapigakura itazinduliwa rasmi Alhamisi katika kongamano ambalo Rais Uhuru Kenyatta pia anatarajiwa kuhudhuria.

Ijapokuwa kikatiba sahihi milioni moja ndizo zitakazohitajika, imefichuka kuwa kampeni inayoendelezwa ‘chini ya maji’ na Bw Odinga inalenga kukusanya hadi sahihi milioni nne.

Taifa Leo imebainisha kuwa, Bw Odinga na wapangaji wake wa mikakati tayari ambao wamegawa nchi kwa maeneo 14 yatakayojumuisha kati ya kaunti moja hadi nne ili kurahisisha uvumishaji wa ngoma ya BBI na kukusanya sahihi.

Maeneo hayo yatakuwa na waratibu ambao watakuwa chini ya kamati simamizi ya kitaifa itakayoongozwa na Bw Mohamed, na aliyekuwa Mbunge wa Dagoretti Kusini, Bw Dennis Waweru.

“Ifikapo Alhamisi tutazindua ukusanyaji wa sahihi na baadhi ya viongozi watatia sahihi zao siku hiyo hiyo. Baadaye, ripoti itapelekwa kwa kila kaunti, maeneobunge na wadi. Tunataka ukusanyaji sahihi ukamilike haraka iwezekanavyo ifikapo mwishoni mwa wiki ijayo,” akasema Bw Odinga.

Bw Mohamed alisema wana hakika kwamba mikakati yao itazaa matunda, licha ya pingamizi la marekebisho ya katiba kupitia BBI kutoka kwa makundi mbalimbali wakiwemo wanasiasa kama vile Naibu Rais William Ruto, baadhi ya viongozi wa kidini na mashirika ya kijamii.

“Ni kawaida katika shughuli yoyote aina hii kuwa na wapinzani ndiposa tuliwaambia tukutane uwanjani. Mtasema yenu nasi tutasema yetu. Tukutane huko,” Bw Odinga alisema, akipuuzilia mbali wanaotaka ripoti ya BBi ifanyiwe marekebisho kabla ya mchakato wa kuandaa kura ya maamuzi uanze.

Waasisi wa BBI wamegawanya nchi katika maeneo ya Pwani, Nairobi, Ukambani, Umaasaini, Nyanza, Magharibi, Gusii, Mlima Kenya Mashariki, Mlima Kenya Magharibi, Kaskazini mwa Rift Valley, Kusini mwa Rift Valley, Kaskazini Mashariki na nyanda za juu za Mashariki zinazojumuisha kaunti za Isiolo na Marsabit. Bw Odinga, Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, aliyekuwa Gavana wa Bomet Isaac Ruto anayeongoza Chama Cha Mashinani (CCM), Katibu Mkuu wa COTU Francis Atwoli na viongozi wengine wa vyama watashikilia usukani wa kuendesha BBI kitaifa.

Watahitajika kuzuru mashinani wakati wowote watakapohiotajika, kutafuta uungwaji mkono. Kikosi cha kiufundi kitasimamiwa na Mwakilishi Mwanamke wa Kisii Janet Ong’era na Bi Sarah Kilemi.

Eneo la Magharibi litasimamiwa na Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya, huku mwenzake wa Kisii James Ongwae akishikilia Gusii pamoja na Waziri wa Usalama, Dkt Fred Matiang’i.

Magavana wengine watakaoendesha gurudumu la BBI ni Anyang’ Nyong’o (Kisumu), Charity Ngilu (Ukambani), Lee Kinyanjui (Mlima Kenya Magharibi) na Alex Tolgos (Rift Valley Kaskazini).

Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru atasaidiana na Kiranja wa Wengi katika Seneti Irungu Kang’ata katika eneo la Kati huku Mbunge Maalumu Maina Kamanda akisimamia Nairobi. Gavana wa zamani, Ruto atasimamia Rift Valley Kusini.

Pwani, Gavana wa Mombasa Hassan Joho na wa Kilifi Amason Kingi wamepewa usukani, huku Joseph ole Lenku akisimamia kaunti za jamii ya Wamaasai.

Dkt Ruto amesisitiza kuwa mashauriano yanahitajika kabla ya kuitisha kura ya maamuzi ili kuzuia mgawanyiko.

, lakini Bw Odinga na wandani wake wanasema kulikuwa na muda wa kutosha kwa kila mtu kutoa maoni yake awali.

Uhuru, Raila wanusurika kufika mahakamani

Na RICHARD MUNGUTI

RAIS Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa ODM Raila Odinga, sasa hawatahitajika kutoa taarifa katika kesi inayokabili walinzi wawili wa hoteli ya New Stanley, Nairobi.

Wafanyakazi hao wawili wanakumbwa na mashtaka ya kusambaza mitandaoni kinyume cha sheria video ya Rais na Bw Odinga wakitembea katika barabara ya Kenyatta Avenue usiku kukagua mradi wa ujenzi wa barabara.

Hakimu Mwandamizi wa Mahakama ya Milimani, Bernard Ochoi, alisema Alhamisi ombi la washtakiwa Patrick Randing Ambogo na Janet Magoma kutaka taarifa hizo halina mashiko kisheria.

Walikuwa wamewasilisha ombi hilo kupitia kwa mawakili wao Danstan Omari na Apollo Mboya.

Randing na Janet wanakabiliwa na shtaka la kuchukua rekodi ya video za CCTV zilizoko katika hoteli ya New Stanley ya Rais Kenyatta na Bw Odinga wakitembea katika barabara ya Kenyatta usiku wa Juni 2, 2020.

Wawili hao walinaswa wakitembea kwenye kinjia kilichotengenezwa na Mamlaka ya Huduma za Nairobi (NMS).

Mawakili Omari na Mboya walikuwa wameeleza mahakama kuwa ushahidi wa walalamishi ambao ni Rais Kenyatta na Bw Odinga ni muhimu.

Walitaka pia viongozi hao wawili wahojiwe mahakamani.

Upande wa mashtaka ulisema kuwa hautazamii kuwaita Rais Kenyatta na Bw Odinga kuwa mashahidi katika kesi hiyo.

Katika uamuzi wake, Bw Ochoi alisema ni mkurugenzi wa mashtaka ya umma aliye na uhuru wa kuchagua mashahidi wataofika kortini.

Washtakiwa wako nje kwa dhamana ya Sh10,000 pesa tasilimu.

Raila kutua Kisii, Nyamira ‘kufuta nyayo za Ruto’

Na CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa ODM Raila Odinga anatarajiwa kuzuru kaunti za Kisii na Nyamira kuanzia Jumanne, Septemba 15, 2020, kuuza ajenda ya mpango wa maridhiano (BBI) na azma yake ya kuwania urais 2022.

Ziara ya Bw Odinga katika eneo la Gusii inajiri juma moja baada ya Naibu Rais William Ruto kuzuru Kaunti ya Kisii ambapo aliongoza shughuli za michango ya fedha kuyasaidia makundi ya vijana na akina mama katika maeneobunge ya Kitutu Chache Kusini na Mugirango Kusini.

Naibu Rais ameanzisha mkakati wa kuvamia maeneo ambayo yanasawiriwa kuwa ngome za Bw Odinga katika juhudi za kuimarisha azma yake ya kuingia Ikulu.

Bw Odinga amekuwa katika ziara ya kisiasa katika eneo la Pwani kwa siku tatu ambapo alihutubia mikutano ya hadhara katika kaunti za Taita Taveta, Kwale na Mombasa. Alifanya ziara hiyo siku chache baada ya Dkt Ruto kuzuru eneo hilo haswa kaunti za Taita Taveta na Mombasa

Duru za ODM ziliambia Taifa Leo kwamba Bw Odinga alipanga ziara ya haraka eneo la Kisii kutokana na umati mkubwa wa watu waliojitokeza kwenye mikutano ya Dkt Ruto eneo hilo na kauli za wandani wake walioitaja mikutano hiyo kama ishara ya kung’aa kwa nyota yake.

Naibu Gavana wa Kisii Joash Maangi, Mbunge wa Mugirango Kusini Sylvanus Osoro na mwenzake wa Mugirango Magharibi Vincent Kemosi walisema kujitokeza kwa watu wengi katika mikutano ya Dkt Ruto ni ishara ya kuimarika kwa ufuasi wake.

“Wapi wale wanaodai kuwa Kisii ni ngome ya ODM? Wako wapi? Leo tumethibitisha kuwa eneo hili linaunga mkono kiongozi ambaye amejitolea kuwafanyia kazi Wakenya sio yule ambaye hutoa ahadi tasa. Tutashirikiana na Naibu Rais hadi mwisho,” akasema Bw Maangi, kauli ambayo iliungwa mkono na wabunge Osoro na Kemosi.

Kwa upande wake, mwanasiasa na mfanyabiashara Don Bosco Gichana alisema kuwa Naibu Rais sasa amedhibiti eneo la Gusii kisiasa.

“Raila atakuwa na kibarua kikubwa kuwashawishi wakazi wa Kisii na Nyamira kumuunga mkono kwa sababu tayari wamefanya uamuzi wa kumfuata Dkt Ruto,” akasema.

Umati uliomlaki Dkt Ruto mjini Kisii ulimzuzua aliyekuwa Seneta wa Kakamega Boni Khalwale akasema kupitia Twitter: “Hii sio Eldoret. Hii ni Kisii na mambo bado. Dkt Ruto anawachangamsha wananchi kiasi kwamba Raila na Ogwae (Gavana wa Kisii) wameingiwa na wasiwasi. Mashinani DP anapendwa.”

Wandani wengine walioshabikia ziara hiyo ya Dkt Ruto Kisii ni aliyekuwa Seneta wa Machakos Johnson Muthama, Mbunge Mwakilishi wa Wanawake wa Nakuru Susan Kihika, Seneta Maalum Millicent Omanga, Seneta wa Meru Mithika Linturi na Mbunge wa Soy Caleb Kositany.

Raila awaweka wazee kando akijiandaa 2022

Na BENSON MATHEKA

KIONGOZI wa ODM, Bw Raila Odinga, amesajili washauri vijana katika juhudi za kutia nguvu azma yake ya kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Kinyume na awali alipotegemea wandani wakongwe kutoka ngome yake ya siasa ya Nyanza, sasa ametandaza nyavu zake na kuwasajili viongozi barobaro kutoka jamii na maeneo mengine nchini.

“Bw Odinga amekumbatia washauri vijana kufuta dhana kwamba aliotegemea kwa muda mrefu walikuwa wakimpotosha kwa kuwa na misimamo mikali. Walikuwa pia wepesi wa kutoa siri kwa vyombo vya habari. Hii ndiyo sababu aliwaacha nje wakati wa mazungumzo yake na Rais Kenyatta hadi wakaafikia handisheki,” asema mdadisi wa siasa, Bw Thomas Maosa, ambaye pia ni wakili wa Mahakama Kuu.

Anasema Bw Odinga anamwamini sana Mbunge wa Suna Mashariki, Bw Junet Mohammed na Gavana wa Mombasa, Bw Hassan Joho, kwa sababu ya uaminifu wao kwake.

“Wawili hao wako na nguvu, pesa na hawatoki katika jamii yake. Wanaweka siri ilivyoshuhudiwa wakati Junet alipoficha kuhusu mazungumzo yaliyozaa handisheki,” alisema Bw Maosa.

Wiki jana, wawili hao walienda hadi Dubai kwa ndege ya kukodisha kumuona Bw Odinga hospitalini, hatua ambayo wadadisi wanasema inadhihirisha imani yake kwao.

Hii ilikuwa siku mbili baada ya Bw Junet kukutana na Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Taifa, Bw Amos Kimunya, kutatua mzozo kuhusu uanachama wa kamati tatu muhimu za bunge.

Ripoti zilisema ni Bw Odinga aliyemtuma Bw Junet kutatua mzozo huo, baada ya kiongozi wa wachache , Bw John Mbadi kutofautiana na Bw Kimunya.

Bw Junet alikuwa mwanasiasa wa pekee aliyeandamana na Bw Odinga kutangaza muafaka wake na Rais Kenyatta. Waliokuwa wandani wake wa miaka mingi hawakuwa na habari kuhusu mazungumzo hayo.

Bw Joho amenukuliwa akisema kwamba Bw Odinga alikuwa amemdokezea mipango ya kuridhiana na Rais Kenyatta.

Wakati Gavana Anne Waiguru alipokuwa kwenye hatari ya kutimuliwa, Bw Junet ndiye aliyetangaza kuwa kama ODM walikuwa wameamua kumuokoa.

Kabla ya handisheki, Bw Odinga alikuwa akitegemea zaidi ushauri wa wandani wake wa kisiasa kutoka Nyanza hasa Seneta James Orengo wa Siaya na Gavana wa Kisumu, Prof Anyang’ Nyong’o.

“Sidhani amewatupa Orengo na Nyong’o. Anawahitaji sana kwa ushauri wao hasa kuhusu sera. Alichofanya ni kubadilisha mbinu. Raila anahitaji tajriba yao pana katika siasa, sheria na utawala,” akaeleza Bw Maosa.

“Baba hawezi kumtupa Orengo japo kuna nguvu mpya za kujiandaa kwa uchaguzi wa mwaka wa 2022,” alisema mbunge mmoja wa ODM ambaye aliomba tusitaje jina lake kwa sababu za kibinafsi.

Kwa sasa Bw Orengo ndiye kiongozi wa wachache katika Seneti.

Mdadisi wa siasa, Bw Joseph Mbindyo anasema kwamba Bw Odinga anaunda kundi la washauri waaminifu na wanaoelewa umuhimu wa handisheki.

“Anapanua kundi la washauri kwa vipimo vya uaminifu, eneo na ushawishi wao akilenga 2022,” asema Bw Mbindyo.

Anasema kwa kuwakumbatia Bw Joho na Bw Junet, Bw Odinga analenga pia kura za eneo la Kaskazini Mashariki, licha ya kuwa amechaguliwa Nyanza.

“Wawili hao wana mapato, ujasiri, ushawishi na uaminifu unaowafanya kutegemewa na Bw Odinga,” akasema Bw Mbindyo.

Ruto avamia ngome ya Raila

JUSTUS OCHIENG NA WANDERI KAMAU

KAMBI ya kisiasa ya Naibu Rais William Ruto imeanza kuvamia eneo la Nyanza kujaribu kushawishi wakazi hasa vijana kumuunga mkono.

Mnamo wikendi, washirika wawili wakuu wa Dkt Ruto, Ndindi Nyoro (Mbunge wa Kiharu) na Oscar Sudi (Mbunge wa Kapseret), walifanya ziara eneo la Bondo ambako ni nyumbani kwa Raila na Kisumu ambako walikutana na viongozi wa vijana.

Duru zilisema nia ya wawili hao ilikuwa ni kuwashawishi vijana kushiriki harakati za kumpigia debe Dkt Ruto mashinani katika eneo hilo ambako Bw Odinga anaungwa mkono kwa wingi.

Habari za kuaminika zilieleza kuwa pia kuna mpango wa kutuma ujumbe kutoka eneo la Luo Nyanza kwenda kumtembelea Naibu Rais nyumbani kwake Sugoi, Kaunti ya Uasin Gishu mara marufuku ya mikutano ya hadhara itakapoondolewa.

Tangu 2018 Dkt Ruto amekuwa akifanya juhudi za kujiimarisha katika maeneo yote ya nchi isipokuwa Luo Nyanza.

Taifa Leo imefahamu kuwa mpango wa kundi hilo unalenga kupenya eneo hilo kupitia makundi ya vijana, akina mama na makanisa.

HANDISHEKI

Pia wanaeneza ujumbe kuwa handisheki ilikusudiwa kutuliza nchi mbali sio kumpatia Bw Odinga urais hapo 2022.

“Kusudi la handisheki ni kumwezesha Rais Kenyatta kutawala kwa utulivu. Msitarajie atasema ‘Raila tosha’. Ahadi yake ilikuwa amalize miaka yake 10 ya utawala na kumpisha Ruto kuendelea,” akasema Bw Nyoro.

Mnamo Jumapili, Bw Sudi alikutana na kundi la vijana katika Ufuo wa Dunga wakiongozwa na Stephen Midenyo na aliyekuwa waziri wa biashara katika Kaunti ya Kisumu Richard Ogendo

Naye Bw George Ayugi alisema wako makini kumpigia debe Dkt Ruto eneo la Nyanza: “Hatuachi eneo lolote nje. Ingawa ODM ina ushawishi mkubwa Nyanza, mtaona mabadiliko. Hili ni eneo la ‘mahasla’ na tutawavuta wengi kwa Dkt Ruto.”

Waliokuwa maseneta, Johnston Muthama (Machakos) na Bony Khalwale nao waliambia Taifa Leo kuwa wanafanya kila juhudi kuhakikisha ushawishi wa Dkt Ruto umesambaa kila pembe ya nchi.

“Kuna kambi mbili za kisiasa nchini moja ikiongozwa na Uhuru, Raila na Gideon Moi na nyingine ni ya Ruto na Wakenya,” akasema Bw Muthama.

MATIBABU

Kwingineko, Bw Odinga alirejea nchini kimyakimya Jumapili usiku kutoka Dubai alikokuwa akipokea matibabu.

Kiongozi huyo aliondoka nchini siku chache kabla ya Juni 30, ambapo yeye na Rais Uhuru Kenyatta walitarajiwa kupokea rasmi ripoti ya jopo la BBI.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo mnamo Jumatatu, maafisa wakuu katika chama cha ODM walisema ingawa Bw Odinga anafahamu shauku walio nayo wafuasi wake kuhusu hali yake kiafya, atapumzika kwa siku kadhaa.

Jakom atapumzika kwanza ili kupata nafuu kiafya. Atatoa taarifa rasmi kwa Wakenya na wafuasi wake kuhusu masuala yote muhimu yanayoihusu nchi,” akasema Mkurugenzi wa Mawasiliano wa ODM, Philip Etale.

Ni kauli ambayo pia ilitolewa na msemaji wa Bw Odinga, Bw Dennis Onyango.

Ingawa wawili hao hawakueleza kwa kina masuala atakayogusia, Bw Odinga anarejea wakati ambapo kumekuwa na hali ya taharuki kati ya vyama vya ODM na Jubilee kuhusu ujumuishaji wa baadhi ya majina ya wabunge kwenye kamati muhimu za Bunge la Kitaifa.

ODM imekuwa ikilalamikia kujumuishwa kwa baadhi ya wabunge wa Jubilee kwenye kamati hizo, ikisema kuwa wengi wao wamekuwa wakipinga BBI.

Muungano wa Ruto na Raila ni ndoto – Kositany

Na ONYANGO K’ONYANGO

WANDANI wa Naibu wa Rais William Ruto, wamepuuzilia mbali uwezekano wa kufanya muungano wa kisiasa na kiongozi wa ODM Raila Odinga kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa 2022.

Naibu Katibu Mkuu wa Jubilee Caleb Kositany, alisema Bw Odinga ataharibu mipango yao ya 2022 iwapo ataungana na Naibu wa Rais.

Mbunge huyo wa Soy, alisema kuwa Naibu wa Rais ana ufuasi mkubwa katika eneo la Mlima Kenya na wakazi wa eneo hilo watamwacha endapo ataungana na Bw Odinga.

“Tukiungana na Bw Odinga tutapoteza uungwaji mkono katika eneo Mlima Kenya. Rais Uhuru Kenyatta anakumbana na upinzani mkubwa katika eneo la Mlima Kenya kwa sababu ya ushirikiano wake na Bw Odinga. Dkt Ruto hawezi kufanya makosa hayo, akasema Bw Kositany.

“Tuko tayari kuungana na mwanaisasa yeyote, wakiwemo Mudavadi na Wetang’ula, isipokuwa Raila,” akaeleza.

Mbunge wa Belgut Nelson Koech na mwenzake wa Keiyo Kusini Daniel Rono pia walipuuzilia mbali juhudi za mbunge wa Emurrua Dikir Johanna Ngeno kujaribu kuwaunganisha Bw Odinga na Dkt Ruto kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu ujao.

Wawili hao walisema kuwa Naibu wa Rais anaungwa mkono na idadi kubwa ya watu katika maeneo ya Magharibi na Mlima Kenya hivyo, Bw Odinga hatakuwa wa manufaa kwake endapo wataungana.

Bw Koech alisema kwamba Bw Odinga anaweza kusababisha wanasiasa wanaounga mkono Dkt Ruto kumtoroka.

Mbunge huyo anayehudumu kwa muhula wa kwanza, hata hivyo, alikiri kuwa Bw Odinga alihusika katika kumnoa kisiasa Dkt Ruto.

Naye Bw Rono, alisema Dkt Ruto yuko tayari kushindana na Bw Odinga katika kinyang’anyiro cha urais 2022.

“Suala la kuwapatanisha Naibu wa Rais na Raila ni sawa na ndoto ya mchana. Raila hawezi kumsaidia Dkt Ruto kushinda urais,” akasema Bw Rono.

“Sisi tutaungana na Bw Mudavadi na Wetang’ula; wao pia waungane na wasimamishe Raila na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka tukutane kwa debe 2022,” akasema.

Naibu wa Rais na Bw Odinga wamekuwa mahasimu wa kisiasa tangu Dkt Ruto alipogura chama cha ODM kabla ya uchaguzi wa 2013.

Tangu Rais Uhuru Kenyatta alipoungana na Bw Odinga miaka 2018, Dkt Ruto na kiongozi wa ODM wamekuwa wakirushiana cheche za maneno. Wadadisi wanasema kuwa uhasama wa kisiasa baina ya wawili hao unasababishwa na siasa za 2022.

Lakini kulingana na Bw Ngeno, baadhi ya wazee kutoka Bonde la Ufa wameelezea nia ya kutaka kuwapatanisha Dkt Ruto na Bw Odinga kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Mbunge huyo wa Kanu alisema inawezekana kwa Bw Odinga kufanya kazi pamoja na Dkt Ruto na kutikisa ulingo wa kisiasa kama ilivyokuwa 2007.

Nazo duru katika kambi ya Dkt Ruto zimedokezea Taifa Leo kwamba kumekuwa na shinikizo za kumtaka Naibu wa Rais kushirikiana kisiasa na Bw Odinga kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Raila ateka baraka za wazee Mlimani

Na WAIKWA MAINA

WAZEE wa jamii ya Wakikuyu wameapa kumtetea Kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga dhidi ya shutuma kutoka kwa baadhi ya wanachama wa Jubilee katika ngome hiyo ya kisiasa ya Rais Uhuru Kenyatta.

Baraza la Wazee wa Jamii ya Wakikuyu lilisema Jumapili kuwa, wanasiasa wa ‘Tangatanga’, hasa kutoka eneo la Mlima Kenya na Bonde la Ufa ambao wamekuwa wakimshambulia Bw Odinga kwa ushirikiano wake na Rais Kenyatta wanatatiza juhudi za serikali kufanikisha ajenda ya maendeleo.

Kwa muda mrefu, wanasiasa hao wanaomuunga mkono Naibu Rais William Ruto wamekuwa wakidai Bw Odinga alichangia kusambaratisha kwa chama chao.

Wengine hudai ushirikiano wake na Rais Kenyatta umefanya washukiwa wa ufisadi kupata mahali pa kujisitiri chini ya mwavuli wa Mpango wa Maridhiano (BBI).

Msemaji wa baraza hilo, Bw Peter Munga, alisema kelele za wanasiasa wa ‘Tangatanga’ hazifanikisha kampeni ya kupambana na ufisadi nchini.

Kulingana naye, badala ya kumshambulia Bw Odinga, viongozi hao wanafaa kupigania kuimarishwa kwa asasi tofauti za kuangamiza ufisadi nchini.

Alisema hayo baada ya Seneta wa Nakuru Susan Kihika na aliyekuwa Gavana wa Kiambu William Kabogo kudai kuwa Bw Odinga ameshindwa kukemea ufisadi tangu aanze kushirikiana na Rais Kenyatta.

Wawili hao waliokuwa wakizungumza katika kituo kimoja cha runinga cha lugha ya Kikuyu walisema kuwa, Bw Odinga ambaye alikuwa katika mstari wa mbele kufichua sakata za ufisadi amenyamaza tangu handisheki yake na Rais Kenyatta mnamo Machi 2018.

“Ili kushinda zimwi la ufisadi nchini, tunahitaji upinzani wenye nguvu. Bw Odinga alinyamaza baada ya kufanya handisheki na Rais Kenyatta. Kiongozi yeyote anayeshukiwa kuhusika na ufisadi, sasa anaenda katika afisi ya Bw Odinga katika jumba la Capitol Hill kutakaswa,” akadai Seneta Kihika.

Bw Munga alisema tatizo kubwa linalokumba Serikali ya Rais Kenyatta ni kutokana na jinsi Dkt Ruto na wandani wake wanavyofuata mkondo tofauti na ule wa Ikulu.

“Naibu wa Rais Ruto amechukua baadhi ya viongozi wa Jubilee na sasa anaendesha serikali mbadala. Zana za uongozi wa nchi hii zilikabidhiwa Rais Kenyatta na wala si kwa Ruto,” akasema Bw Munga.

Wakati huo huo, alimtaka Rais Kenyatta aendelee kuwatimua viongozi wanaomkaidi wakiwemo mawaziri na maafisa wengineo katika idara za serikali akisema wao ndio wamekuwa wakihujumu ajenda yake ya maendeleo.

Bw Munga ambaye huwa na ushawishi mkubwa katika siasa za Mlima Kenya alisema ni dhahiri kuwa Rais Kenyatta anataka kukumbukwa kwa kusaidia Kenya kustawi kimaendeleo hivyo hana budi kutimua yeyote anayemhujumu.

Yafichuka ODM ilipanga kuiba kura 2007

Na MWANDISHI WETU

SHIRIKA la kimataifa linalosifika kwa ufichuzi wa maovu ya kiuongozi, limetoa nakala ya siri ya Chama cha ODM inayoonyesha kilipanga kuiba kura katika Uchaguzi Mkuu wa 2007.

Kulingana na nakala hiyo iliyofichuliwa Jumapili na shirika la Wikileaks, imesemekana wizi wa kura ulikuwa miongoni mwa mikakati michafu ya kisiasa ambayo ODM iliweka katika juhudi za kujaribu kuhakikisha kiongozi wa chama Raila Odinga angeibuka mshindi.

Katika uchaguzi huo tatanishi, Rais Mstaafu Mwai Kibaki ndiye alitangazwa mshindi, hali iliyosababisha ghasia ambazo zilipelekea watu zaidi ya 1,000 kuuliwa na maelfu wengine kufurushwa makwao.

Wakenya sita, akiwemo Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto walifunguliwa mashtaka katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kwa kudaiwa kuhusika kupanga ghasia hizo.

“Tutahakikisha watu hawafuatilii mienendo yetu ili endapo tutapata mwanya, tutautumia kujiongezea kura katika ngome zetu,” inasema sehemu ya nakala hiyo.

Kando na wizi wa kura, nakala hiyo ya siri katika ODM imeonyesha kuwa chama hicho kilikusudia kuzua taharuki na ghasia endapo mipango yote ya kumfikisha Bw Odinga katika Ikulu haingezaa matunda.

Kwa mujibu wa nakala hiyo, mpango huu wa ghasia ungefanikishwa kwa kutumia maajenti wa ODM mashinani kuzua uhasama, kutoa misaada kwa makundi ya kivita Mlima Elgon na kusambaza karatasi zenye jumbe za chuki ya kikabila maeneo mbalimbali.

Jukumu hili lilitwikwa mmoja wa wanajeshi wastaafu wa daraja la juu aliyehudumu katika serikali ya mmojawapo wa rais wastaafu nchini.

Imesemekana siasa chafu za ODM hazikuishia hapo, kwani kulikuwa na mpango wa kusudi kufanya jamii mojawapo kubwa nchini ionekane kama ya waovu ili jamii nyingine zote kitaifa ziungane kumchagua Bw Odinga.

ODM pia imedaiwa ilipanga kuchochea wakazi wa maeneo wanaotamani utawala wa Majimbo dhidi ya serikali kuu kama vile Rift Valley, Magharibi na Pwani.

Ili kufanikisha hayo yote, ODM ilihitaji mabilioni ya pesa.

Imefichuka chama hicho hakikujali mahali pesa hizo zingetoka kwani orodha ya wafadhili wao inajumuisha mataifa maskini ya Afrika yanayotambulika kwa ukatili dhidi ya raia ambapo rasilimali huliwa na matajiri wachache wenye ushawishi mamlakani.

Wafadhili wengine walijumuisha mhubiri mashuhuri ambaye anakumbwa na mashtaka ya ulanguzi wa binadamu. Vile vile, kuna wahariri wa vyombo vya habari ambao imefichuka walitumikia chama hicho ili kuwezesha ajenda za ODM kujikita akilini mwa raia.

Siasa zateka misaada

Na BENSON MATHEKA

UHASAMA wa kisiasa kati ya Naibu Rais William Ruto na Kiongozi wa ODM Raila Odinga, ulichukua mkondo wa aibu jana wakati wafuasi wao walipogeuza uhisani wa wawili hao kwa jamii kuwa ushindani.

Tangu virusi vya corona vilipoibuka nchini, kumekuwepo wahisani wengi ambao hutoa misaada kwa jamii, na viongozi wa kisiasa hawajaachwa nyuma.

Wakati huo wote, kumekuwepo maswali kuhusu hatua ambazo Dkt Ruto amechukua kusaidia jamii kwani hajakuwa akionekana hadharani kama viongozi wengine wanaojitangaza wanapotoa misaada wakati huu wa janga la corona.

Ijumaa, ilifichuliwa kwenye mitandao ya kijamii kwamba Dkt Ruto amekuwa akigawa chakula na vifaa vya kujikinga kutokana na corona katika mitaa ya mabanda kupitia kwa viongozi wa kidini na wanasiasa wanaomuunga mkono, ila amekuwa akifanya hivyo kimyakimya.

Lakini kilichoibua aibu ni jinsi wafuasi wa Naibu Rais walivyogeuza suala hilo la uhisani kwa maskini katika jamii kuwa ushindani kati ya vigogo hao wawili wa kisiasa.

Walirushiana cheche za maneno, kila upande ukitaka kudhihirisha ukuu na uaminifu wa mikakati ya yule anayemfuata.

“Wengine walipokuwa wakiuliza alivyokuwa akifanya na pesa alizokuwa akipatia makanisa, alikuwa anazituma kwa makanisa, misikiti na washirika wake wa kisiasa kugawa chakula katika kaunti za Nairobi, Kajiado na Kiambu,” alisema aliyekuwa mkurugenzi wa mawasiliano ya kidijitali katika Ikulu Dennis Itumbi.

Bw Itumbi, ambaye ameibuka kuwa mtetezi mkubwa wa Naibu Rais alidai kuwa kufikia Jumapili, familia 40,122 zilikuwa zimenufaika misaada kutoka kwa Dkt Ruto.

Watetezi hao wa Dkt Ruto waliwaambia wafuasi wa Bw Odinga kwamba sio lazima fujo zizuke ndipo ijulikane Dkt Ruto anasaidia maskini kwa chakula

Walikuwa wakirejelea kisa cha mtaa wa Kibra ambapo ghasia zilizuka wakati maafisa wa serikali walipokuwa wakigawa msaada wa chakula uliotolewa na Bw Odinga.

Lakini wale waliomtetea Bw Odinga walisema ni kinaya wafuasi wa Dkt Ruto kusema hataki kujionyesha ilhali wanasambaza picha za misaada wanayodai alifadhili.

“Tinga (Bw Odinga) amekuwa akisaidia watu kila mara bila kuita wanahabari; hajawahi kufadhili hashtegi ili atambuliwe. Ruto amebanwa baada ya kunyamaza kwa muda mrefu. Hana uaminifu,” akasema mtumizi wa Twitter, Abuga Makori.

Mabishano hayo yalitiwa moto saa chache baada ya mfanyabiashara wa Mombasa Hussein Shahbal kutangaza kuwa Bw Odinga aliitikia wito wake na kumpa misaada ya chakula awasilishe kwa wakazi wa Mombasa.

Wakati alipowasilisha misaada hayo kwa Gavana wa Mombasa Hassan Joho jinsi inavyohitajika kikanuni, Bw Shahbal alitaka wanasiasa wakome kushindana katika mikakati ya vita dhidi ya coronavirus.

Mbunge wa kundi la ‘Tangatanga’ kutoka Mlima Kenya aliyeomba tusitaje jina lake, alithibitisha kwamba ni kweli kuna baadhi yao husambaza vyakula vilivyofadhiliwa na Naibu Rais.

Aprili 2020 Bw Odinga akionekana kumlenga Dkt Ruto, alikejeli wanasiasa ‘fulani’ kwa kunyamaza wakati Wakenya wakiteseka kwa janga la corona badala ya kuwasaidia ilhali walikuwa wakitoa mamilioni ya pesa kwenye michango makanisani kote nchini.

Wakenya wamkaanga Raila kwa kuwashauri wanawe mikono badala ya kuwapa msaada

Na GEOFFREY ANENE

KIONGOZI wa Chama cha ODM Raila Odinga amejipata pabaya baada ya kuandikia Wakenya barua akiwakumbusha kuepuka mikusanyiko, wajitenge, wanawe mikono, wakae nyumbani na wavalie barakoa, hata za kujishonea ili kupiga jeki vita dhidi ya ugonjwa wa Covid-19.

Licha ya ujumbe unaonekana kuwa wa busara kutoka kwa afisi ya Bw Odinga mnamo Aprili 3, watumiaji wengi wa mitandao ya kijamii wamemkaanga waziri huyo wa zamani mkuu wakitaka aonyeshe ukarimu wake kwa kuchangia kwa hali na mali katika kuzuia maambukizi ya virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa huo ambao umeua watu wanne nchini Kenya na karibu 16, 000 kote duniani.

Baada ya barua hiyo kuchapishwa kwenye mtandao wa Twitter, Chebet alimwambia Bw Odinga, “Wewe andika barua nyingi unavyotaka, lakini nakueleza kuwa Wakenya hawatakula barua. Wanahitaji chakula na hiyo ndio njia ya pekee itakayowafanya wasitoke nyumbani. Ambia watoto wako mambo hayo mengine unatuambia.”

Liverpool 001 anasema, “Sijawahi kuona Raila akitoa mchango wake kusaidia wanaohitaji msaada. Hutawahi kumuona akifanya kile (Gavana) Joho, (Naibu Rais) Ruto ama (Gavana) Sonko hufanya. Sijui huwa anafanyia nini fedha zake zote?”

Kevin Omenya hakuwa na maneno mengi kwa Bw Odinga. Alisema, “Sijawahi kukuona ukitoa mchango wako.”

Nick K Ruto alishukuru Bw Odinga kwa ujumbe wake akisema, “Asante kwa kukumbusha Wakenya kuwa tuko katika hali mbaya. Hata hivyo, Mungu atatulinda.”

Naye OnePeopleOneTribeOneKenya alisema hana imani na wanasiasa. “Imani yangu kwa wanasiasa wa Kenya iliisha. Sasa ni wakati wa kuomba Mungu jinsi maandiko ya Isaiah 26:20 yanasema, “Endeni nyumbani, watu wangu, na mfunge milango yenu! Jificheni kwa muda hadi hasira ya Mungu itakapoisha.”

E K Gitau alijibu Bw Odinga akisema, “Ni lini utatoa sehemu ya mabilioni hayo yako kwa kusaidia katika vita hivi? Ama fedha zako umetengea shughuli ya kura ya maamuzi ya mwezi Juni?”

Ochiro alitaka kujua kiasi cha fedha Bw Odinga anachangia katika vita hivi. “Wewe unachangia fedha kiasi gani kusaidia watu walio katika hatari ya kuambukizwa virusi hivi na ambao hawana uwezo wa kununua chakula?”

mwania Simon alisema hajaona Bw Odinga akitoa msaada wa chakula kwa mwananchi wa kawaida ambaye anategemea kufanya kibarua kila siku kujikimu.

Sylvia Wangeci alisema barua ya Bw Odinga imejaa maneno mazuri, lakini “tunahitaji chakula ili kutushawishi tukae nyumbani.”

Justus Sila alitaka Bw Odinga atumie urafiki wake ndani na nje ya Kenya kuomba rafiki zake kutoa misaada ya chakula “hasa kwa wakazi wa mtaa wa Kibra kwa sababu tunajua huwezi hata kuchangia hata pakiti moja unga kwa mtu aliye katika hatari ya kufa njaa.”

Hilda Nabiswa alitaka Bw Odinga aonyoshe anachosema kwa vitendo. “Hatuna tatizo na barua yako. Sasa, hebu tuma magunia ya chakula mtaani Kibera. Hebu kuwa mstari wa mbele kwa kuonyesha kwa vitendo.”

Simhitaji Uhuru kupenya Mlima Kenya, adai Raila

Na PETER MBURU

KIONGOZI wa chama cha ODM Raila Odinga amesema kuwa hahitaji kushikwa mkono na Rais Uhuru Kenyatta ili kupenya Mlima Kenya, akisema tayari ana uhusiano ulioanza zamani na eneo hilo na kuwa anakubalika kivyake.

Bw Odinga amejitaja kuwa shemeji na rafiki wa Mlima Kenya na kuwa wakazi wa eneo hilo wanampenda kutokana na uhusiano wake na viongozi wa mbeleni eneo hilo, na kuwa uhusiano wake na Mlimani ulianza enzi za babake Oginga Odinga.

Alipoulizwa ikiwa anaogopa kwenda eneo hilo ama anahitaji kwenda na Rais Kenyatta katika runinga ya Ktn News Jumatano, Bw Odinga alisema haogopi chochote.

“Mimi siogopi kwenda Mlima Kenya kwa kuwa fulani amesema (kitu), hayo yote ni maneno ya uzushi. Nakwenda kama rafiki ya Wakikuyu, naenda kama muthoniwa (shemeji), naenda kwa athoni (mashemeji),” Bw Odinga akasema.

Alieleza jinsi babake, Oginga alikataa wadhifa wa Waziri Mkuu ili Rais wa kwanza wa Kenya, Jomo Kenyatta aachiliwe; jinsi alifungwa pamoja na wanasiasa wa eneo hilo Kenneth Matiba na Charles Rubia miaka ya tisini; na alivyompigania Rais Mstaafu Mwai Kibaki hadi akashinda, akisema mifano hiyo yote ni msingi tosha wa kumpenyeza eneo hilo.

“Wakazi wa eneo hilo wananipenda. Hata Kibaki alipopata ajali wakati wa kampeni, nilitangaza kuwa japo nahodha (Kibaki) amejeruhiwa, sharti mchezo ungeendelea na nikasimamia kampeni. Tulipompeleka Kibaki Othaya, njiani nilikuwa nikiitwa Mutongoria Njamba (kiongozi shujaa) na Wakikuyu,” akasema.

Alitaja pingamizi za viongozi wafuasi wa Naibu Rais William Ruto eneo hilo dhidi yake (Raila) kuwa kelele za chura, na ambazo hazingemzuia kwenda Mlima Kenya.

“Waswahili husema migurumo za chura haizuii ng’ombe kunywa maji, yale unaskia ni ngurumo za chura, ngombe atakunywa maji,” akasema, akijirejelea kuwa ng’ombe na chura kuwa wafuasi wa Dkt Ruto Mlimani.

Kiongozi huyo Jumanne alikutana na viongozi wa eneo hilo, wakihusisha magavana Kiraitu Murungi (Meru), Anne Waiguru (Kirinyaga), Muthomi Njuki (Tharaka Nithi) na wabunge Kanini Kega (Kieni) na Maina Kamanda, kujadili kuhusu mkutano wa Mpango wa Maridhiano (BBI) uliopangwa kuandaliwa Meru kesho.

Bw Odinga alisema tayari viongozi wa eneo hilo wamemkaribisha, ishara kuwa eneo hilo halina ubaya naye.

“Tuliongea juu ya mambo ya maendeleo eneo hilo, kilimo, elimu, usalama na kadhalika na wakanikaribisha wenyewe kutembea huko,” akasema.

Matamshi yake yamekuja wakati kumekuwa na gumzo kuwa anajaribu kumtumia Rais Kenyatta na BBI ili akubalike Mlimani, na kuwa kuna pingamizi kali dhidi yake.

Lakini alishikilia kuwa maneno hayo si ya kweli, akisema yeye ni shemeji wa Mlimani, na “damu ni nzito kuliko maji.”

Raila anyakua kazi ya Ruto

Na VALENTINE OBARA

KIONGOZI wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga amezidi kuibua maswali kuhusu mamlaka aliyo nayo katika serikali inayoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta.

Jumapili alipoongoza mkutano wa hadhara kuhusu Mpango wa Maridhiano (BBI) katika Kaunti ya Garissa, Bw Odinga alijitwika majukumu ambayo kwa kawaida yanafaa yatekelezwe na viongozi wakuu serikalini, hasa Naibu Rais William Ruto.

Waziri huyo mkuu wa zamani alijitosa katika mdahalo unaohusu kuhamishwa kwa walimu wasio wenye asili ya maeneo ya Kaskazini Mashariki kufuatia mashambulio ya kigaidi yaliyokuwa yakiwalenga.

Katika hotuba yake, aliwaahidi wakazi wa Garissa kwamba serikali itatatua suala hilo na mabadiliko yataonekana hivi karibuni.

“Hakuna kitu kichungu zaidi kama watoto kwenda shuleni na kupata hakuna walimu. Hili ni jambo la kusikitisha na ni lazima tupate suluhu. Lazima tulete walimu hapa,” akasema.

Aliongeza kwamba alikuwa tayari amejadiliana na Rais Kenyatta, kwa hivyo, kuna uhakika serikali itachukua hatua.

Alisema inafaa vijana waliopata alama za C- na D+ katika Mtihani wa Kitaifa wa Shule za Upili (KCSE) kutoka kaunti zilizo Kaskazini Mashariki waruhusiwe kujiunga na taasisi za mafunzo ya walimu.

“Nimeongea na Rais Uhuru kabla nije hapa… na narudi kuongea naye tena. Wiki ijayo, mtaona matangazo kisha walimu wataletwa hapa,” akasema.

Mbali na hayo, Bw Odinga alitoa ahadi kuhusu masuala ya miundomsingi na usalama katika eneo hilo linalopakana na Somalia. Kulingana naye, mashambulio ya kigaidi yanayofanyika barabarani Kaskazini Mashariki, yanafaulu kwa sababu ya barabara mbovu ambazo zinatoa nafasi kwa magaidi kushambulia magari kila mara.

Alisema, alipokuwa waziri mkuu, alitoa mchango mkubwa katika mpango wa kujenga barabara inayotoka Garissa kupitia Wajir hadi Mandera, na akaongeza kuwa serikali itakamilisha mradi huo.

“Mimi ndiye niliyechora barabara za Garissa kupitia Wajir mpaka Mandera. Hiyo barabara itajengwa. Tunataka kuona eneo hili linafunguliwa. Tukifikisha lami kule Mandera, mambo haya ya ujambazi na ujangili yatakoma,” akasema.

Katika hotuba za awali, Dkt Ruto alisema jukumu la kutangaza au kuzindua miradi ya serikali ni lake kama naibu rais akisema kuwa huwa anapokea mshahara kufanya kazi hiyo.

Lakini wiki chache zilizopita, Rais Kenyatta alishangaza wengi alipokemea watu ambao hakuwataja, akisema wamemsaliti licha ya kuwa aliwaamini na kuwapa jukumu la kuendesha miradi mikuu ya serikali yake.

Tangu Bw Odinga alipokubali kushirikiana na Rais Kenyatta kupitia kwa handsheki mwaka wa 2018, hadhi yake imepanda sana serikalini.

Ahadi zake za Jumapili zimeongeza orodha ya matukio yanayomfanya kuonekana kama kiongozi mwenye mamlaka makubwa serikalini. Matukio mengine yanahusu ulinzi mkubwa anaopewa, ijapokuwa duru zingine hudai ulinzi huo unatokana na mamlaka yake kama Balozi wa Miundomsingi katika Muungano wa Afrika.

Vilevile, kumekuwa na wakati ambapo mawaziri serikalini walikuwa wakimtembelea afisini mwake kumwarifu kuhusu shughuli za serikali kuu.

Wandani wa Naibu Rais walio katika mrengo wa Tangatanga, humlaumu Bw Odinga wakidai alitumia handsheki kujiingiza serikalini kupitia mlango wa nyuma na kuvuruga Chama cha Jubilee.

Jumapili, Dkt Ruto na kikosi chake waliendelea kukemea mikutano ya BBI wakisema inatumiwa kugawanya nchi na kusababisha taharuki katika jamii.

Mbunge wa Gatundu Kusini, Bw Moses Kuria ambaye aliandamana na Naibu Rais kwa harambee ya Waislamu katika uwanja wa michezo wa Embu, alisema bunge litaanza kuchunguza ufadhili wa mikutano hiyo.

“Wanaita wengine wafisadi ilhali kile kinachofanyika katika mikutano ya BBI ndiyo ufisadi zaidi kwa kuwa bunge halijapitisha hata shilingi moja kufadhili mikutano hiyo. Wanaochukua pesa za umma, mtajikuta bungeni kujibu maswali,” akasema.

Rais Kenyatta amekuwa akitoa wito kwa viongozi wote kuunga mkono shughuli za BBI, akisema lengo ni kuleta umoja nchini. Wikendi ijayo, mkutano wa BBI unatarajiwa kufanyika katika Kaunti ya Meru ambapo waandalizi wanasema wamemualika pia Rais Kenyatta na Dkt Ruto.

Raila akemea ufisadi kanisani

CAROLINE WAFULA NA DICKENS WASONGA

KIONGOZI wa chama cha ODM, Bw Raila Odinga, Ijumaa alikemea vikali viongozi wanaotumia pesa wanazopata kupitia ufisadi kutoa michango makanisani. Bw Odinga alisema ufisadi umekolea Kenya hivi kwamba viongozi wanaopora pesa za umma wanapeleka kuzificha makanisani.

“Tunataka kukabiliana na ukosefu wa ajira, ukosefu wa usalama, ufisadi na maovu mengine. Tunataka kujenga Kenya ambapo ikiwa ninatoa pesa kanisani, tunajua ninatoa nini na inatoka wapi,” Bw Odinga alisema.

Alisema kanisa halifai kugeuzwa mahali pa kuficha mali iliyopatikana kupitia ufisadi.

“Tabia hii inaendeleza ufisadi. Hii ndiyo sababu tunataka kupigana na uovu huu katika nchi hii,” alisema.

Akizungumza katika hafla ya kuadhimisha miaka 100 tangu shule ya wavulana ya Maranda ilipoanzishwa akiandamana na Jaji Mkuu David Maraga, Bw Odinga alihimiza mahakama kusaidia katika vita dhidi ya ufisadi kwa kuhakikisha kuwa kesi za washukiwa zinasikilizwa na kuamuliwa haraka.

“Wanasema dhamana ni haki ya kikatiba lakini haifai kutumiwa vibaya na hata wakipewa haifai kuwa mwisho wa kesi,” alisema Bw Odinga. Waziri huyo mkuu wa zamani alisema kwamba mchakato wa maridhiano (BBI) alioanzisha na Rais Uhuru Kenyatta, utaleta mwamko mpya Kenya.

“Tulikubaliana na ndugu yangu Uhuru kwamba tunataka kuunda Kenya mpya iliyoungana ambapo ukabila si kisiki cha kupata kazi na maendeleo,” alisema.

Miongoni mwa masuala tisa waliyoazimia kushughulikia kupitia mchakato wa maridhiano ni kupigana na ufisadi nchini.

Naibu Rais William Ruto amekuwa akihudhuria harambee makanisani na hata akaapa kuendelea nazo huku viongozi wanaompiga vita wakimtaka aeleze anakotoa pesa hizo.

Bw Maraga alisikitika kuwa licha ya Wakenya wengi kuwa Wakristo na walioelimika, ufisadi bado unaendelea kukita mizizi katika jamii.

“Kenya inahitaji wanaume na wanawake wenye maadili mema. Hali ilivyo kwa sasa ni kwamba waliosoma vyema wanashikilia nafasi za uongozi lakini kutokana na hali kwamba hawawezi kufanya chochote, ni ishara kwamba tunahitaji mabadiliko kama jamii,” alisema.

Alisema viongozi wa sasa hawawezi kutegemewa kuwa mfano mwema wa kuigwa na vizazi vijavyo.

“Tuna uhaba mkubwa wa viongozi wa kuigwa. Tunaogopa kuuliza chanzo cha utajiri wa watu na badala yake tunawafuata tu na kuutamani,” alisema.

Bw Maraga alisema kwamba chanzo cha changamoto zinazokabili nchi hii ni ukosefu wa maadili.

“Changamoto nyingi zinazotukabili kama nchi zinatokana na ukosefu wa maadili, bila maadili mema elimu pekee haitoshi, tunahitaji zaidi ya elimu nzuri, tunahitaji kujitolea na nidhamu ya hali ya juu,” alisema. Vita dhidi ya ufisadi vilishika kasi baada ya handisheki kati ya Bw Odinga na Rais Kenyatta. Hata hivyo, viongozi hao wawili wamekuwa wakilaumu mahakama kwa kulemaza vita hivyo kwa kuwaachilia washukiwa.

Jana, Bw Odinga alisema vita hivyo haviwezi kufaulu bila mahakama kutekeleza kazi yake na kuwafunga jela wahusika.

Hata hivyo, Bw Maraga amekuwa akitetea mahakama akisema kesi huamuliwa kutegemea ushahidi unaowasilishwa kortini.

Hatimaye Raila atazama mwili wa Moi

Na CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa ODM Raila Odinga Jumatatu aliungana na Wakenya kutoa heshima zake za mwisho kwa Rais wa zamani marehemu Daniel Arap Moi katika majengo ya bunge, Nairobi.

Waziri huyo Mkuu wa zamani aliwasili katika majengo hayo mwendo wa saa nane na nusu alasiri akiwa ameandamana na mkewe Ida na mwanawe Raila Junior.

Bw Odinga alionekana kuinua mgwisho (fly-whisk) aliyopewa na Raila Junior mara tatu kabla ya kuinama kwa heshima na Mzee Moi aliyemtaja kama “mpiganiaji uhuru na kiongozi mcheshi aliyependa watu.”

Bw Odinga alifika katika majengo ya bunge saa chache baada ya kuwasili kutoka nchini Ethiopia ambako alihudhuria mkutano wa viongozi wa nchini wanachama wa Muungano wa Afrika (AU) jijini Addis Ababa.

Kwenye mkutano mfupi ya wanawe marehemu Moi, Raymond na Gideon, Bw Odinga alielezea namna ambayo mwendazake alishirikiana na babake Jaramogi Oginga Odinga kupigania uhuru wa Kenya.

“Mzee alikuwa mpiganiaji uhuru shupavu. Yeye pamoja na babangu walikuwa miongoni mwa Wakenya wa kwanza kuchaguliwa kama wajumbe katika Bunge la Kenya (Legco) mnamo 1957,” akasema.

Wengi walikuwa wametarajia kwamba Bw Odinga angefika kwenye majengo hayo na kumwomboleza Mzee Moi kulingana na tamaduni za jamii ya Waluo maarufu kama ‘Tero Buru’ lakini hilo halikufanyika.

Mnamo 2003, Bw Odinga alimwomboleza aliyekuwa Makamu wa Rais Kijana Wamalwa akiwa amevalia mavazi ya kitamaduni na kushika mkuki mkononi jinsi Waluo huomboleza watu mashuhuri walioaga dunia.

Baada ya kumaliza kuutazama mwili wa Mzee Moi, Waziri huyo Mkuu wa zamani alielekea kwenye chumba cha pembeni na kukutana na familia ya Mzee Moi wakiongozwa na seneta wa Baringo Gideon Moi na mbunge wa Rongai Raymond Moi.

Wawili hao walimwaarifu kuhusu mipango ya mazishi na kumwalika rasmi afike Nyayo leo na Kabarak kesho kwa mazishi.

“Tutakuwa na ibada Jumanne katika uwanja wa Nyayo na kesho Kabarak ambazo zitaanza saa tatu. Tunataka kumaliza mapema kisha tuwaruhusu watu warudi makwao kwa sababu wengi watafika na baadhi wanatoka maeneo ya mbali,” Gideon Moi akamweleza.

Bw Odinga naye alikubali wito wa kufika kwenye ibada hizo na akaeleza historia fupi kati ya familia ya babake marehemu Oginga Odinga na Mzee Moi kabla na baada ya uhuru.

“Kwa niaba ya familia ya marehemu Jaramogi Oginga Odinga na familia yangu tutafikisha rambirambi. Mzee alikuwa mpiganiaja na yeye na marehemu babangu walikuwa watu wa kwanza kuchaguliwa kwenye Bunge la Legco. Nimemjua tangu 1958. Leo ni siku ya kufikisha rambirambi zetu na nilipokea habari za kifo chake nikiwa na Rais Uhuru Kenyatta Marekani,” akasema.

“Nikiwa Addis Ababa niliwafahamisha Marais wa mataifa mbalimbali kuhusu tanzia hii na wameahidi kufika hapa kesho kwa mazishi. Mzee ameishi maisha kamilifu na Mungu ailaze roho yake mahala pema peponi,” akaongeza Bw Odinga.

Familia hiyo kisha ilimshukuru pamoja na Wakenya wengine kwa kuomboleza nao.

‘Tungependa kukushukuru kwa kufika na kukubali kuwa nasi kesho Nyayo na Kabarak. Tunakukaribisha na zaidi ya raia 200,000 ambao wamefika hapa kuona mwili wa Mzee Moi,” akasema Raymondi Moi.

Waziri huyo mkuu wa zamani aliwasili kutoka Addis Ababa Ethiopia Jumapili usiku ambako aliwakilisha Rais Kenyatta katika mkutano wa Muungano wa Afrika (AU) uliokamilika hapo jana.

Kando na Bw Odinga, maelfu ya Wakenya jana walifika majengo ya bunge kutazama mwili huo siku ya mwisho.

Mlolongo mrefu wa raia ulianza katika jumba la Kencom, ukapitia karibu na Mahakama ya Juu hadi majengo ya Bunge huku usalama ukiimarishwa na polisi na vijana wa NYS.

Baadhi ya raia waliokuwa kwenye foleni walilemewa na kuzirai kutokana na wakapewa huduma za kwanza na vijana wa NYS pamoja na wasamaria wema.

Wengi walivumilia miale mikali ya jua ili kuona mwili huo ambao umekuwa katika majengo ya bunge tangu siku ya Jumamosi.

Shughuli hizo zilikamilika saa 11 na mwili huo kurejeshwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Lee huku ibada ikitarajiwa kuandaliwa leo katika uwanja wa Nyayo na kuongozwa na madhehebu mbalimbali.

Rais Uhuru Kenyatta, Naibu wake William Ruto na Bw Odinga, viongozi mbalimbali na maafisa wa ngazi za juu wanatarajiwa kuhudhuria ibada ya leo na mazishi siku ya kesho.

Itakumbukwa kuwa Bw Odinga ni miongoni mwa wanasiasa na wanaharakati ambao walifungiwa katika vyumba vya mateso katika yaliyokuwepo katika jumba la Nyayo House, wakati wa utawala wa Moi. Alitupwa kizuizini kwa miaka minane kwa kuhusishwa na jaribio la mapinduzi ya serikali mnamo 1982.

Hata hivyo, katika risala zake za rambirambi wiki jana, Bw Odinga alisema kuwa amemsamehe Moi kwa mateso aliyopitia chini ya utawala wake.

Kabla ya kumpokeza Mwai Kibaki mnamo 2002, Mzee Moi aliomba msamaha hadharani kutoka kwa wale wote ambao huenda aliwakosea kwa njia moja ama nyingi wakati wa utawala wake wa miaka 24.

Miereka ya Uhuru na Ruto yamwinua Raila kisiasa

Na PETER NGARE

KIONGOZI wa ODM Raila Odinga amechukua fursa ya miereka baina ya Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto kujijenga kisiasa.

Huku Rais Kenyatta na Dkt Ruto wakipigana na kubomoa chama chao cha Jubilee, Bw Odinga amekuwa akijenga ODM na kutumia mchakato wa BBI kujiuza kwa Wakenya.

Malumbano baina ya wakuu hao wawili wa taifa yamewafanya kushindwa kuwa na msimamo mmoja kuhusu masuala ya nchi ikiwemo BBI na pia miradi ya maendeleo.

Rais na naibu wake pia wamefanikiwa kugawanya wafuasi wao katika mirengo ya ‘Kieleweke’ wake Rais Kenyatta na ‘Tangatanga’ wa Dkt Ruto.

Bw Odinga ametumia fursa hiyo kupenyeza Ikulu ambapo sasa anashirikiana na Rais Kenyatta katika masuala mbalimbali ya utawala wakati Dkt Ruto akitengwa.

Hatua hii inaweka ODM katika nafasi bora ya kujiimarisha kufikia uchaguzi mkuu wa 2022 huku Jubilee ikisambaratika kutokana na mizozo kati ya kinara na naibu wake.

Bw Odinga, ambaye aliacha siasa za upinzani mnamo 2018 na kujiunga na mrengo wa Rais Kenyatta katika Serikali Kuu, amefanikiwa kuonyesha kuwa ndiye mwenye usukani wa BBI, ambayo alianzisha pamoja na Rais Kenyatta baada ya handisheki mnamo 2018.

Lakini tangu ripoti ya BBI ilipozinduliwa Novemba mwaka jana, Rais Kenyatta na Dkt Ruto wametekwa na mivutano baina yao na kumwachia Bw Odinga usukani wa kusukuma mchakato huo.

Katika mikutano ya kupigia debe BBI iliyoanza mwezi uliopita, Bw Odinga amekuwa ndiye nyota, hatua ambayo imeinua hadhi yake kisiasa.

Kufikia sasa Bw Odinga ameongoza mikutano ya kupigia debe BBI katika ngome zake za Nyanza, Magharibi, Pwani na Ukambani.

Rais Kenyatta na Dkt Ruto hawakuhudhuria mikutano hiyo licha ya kusema kuwa wanaunga mkono BBI, jambo ambalo limempa Kiongozi wa ODM fursa ya kung’aa.

Juhudi za mrengo wa Dkt Ruto serikalini kuingia kwenye ‘basi’ la mchakato huo katika juhudi za kuzima nyota ya Bw Odinga zimegonga mwamba.

Washirika wake kama Moses Kuria (Mbunge wa Gatundu Kusini) na Seneta Kipchumba Murkomen wa Elgeyo Marakwet wamejipata matatani katika mikutano miwili waliyohudhuria Mombasa na Kitui.

Kwa upande mwingine, Rais Kenyatta na Dkt Ruto wangali wanavutana kuhusu BBI huku Naibu Rais akieleza kutoridhishwa na baadhi ya masuala yaliyo ndani ya ripoti hiyo.

Wanasiasa wa mrengo wa Rais Kenyatta ambao wamekuwa wakihudhuria mikutano ya BBI nao wameharibu mambo zaidi kwa kutumia fursa hiyo kumshambulia Dkt Ruto.

Hatua hiyo imeongeza uhasama kati ya Tangatanga na Kieleweke wakati ODM ikiendelea kujenga umoja wake.

Rais na naibu wake wamekuwa wakitumia kila fursa wanayopata kupimana nguvu huku siasa kati yao zikiingia hatua hatari kiasi cha wandani wao kudai kuwa kila mmoja anakula njama ya kumng’oa mwingine madarakani.

Rais Kenyatta amekuwa akimlaumu Dkt Ruto akidai anahujumu maendeleo kwa siasa za kila mara za 2022 na hivyo kutatiza utimizaji wa Ajenda Nne Kuu za Maendeleo.

Katika ngome zao za kisiasa hasa ya Rais Kenyatta katika eneo la Mlima Kenya, wakazi wamegawanyika kuhusu BBI huku walio upande wa Rais wakiunga mkono na wale wa mrengo wa Dkt Ruto wakiipinga.

Siwezi kufanya kazi na Ruto, asisitiza Raila

Na PETER MBURU

KIONGOZI wa ODM Raila Odinga amesisitiza kuwa hawezi kamwe kushirikiana na Naibu Rais William Ruto kisiasa kutokana na tofauti za kimaadili baina yao.

“Maadili yangu ni imara na wazi kabisa. Tunatofautiana naye kimaadili,” akasema Bw Odinga kwenye mahojiano na NTV mnamo Jumapili usiku.

Alieleza kuwa japo hana tatizo endapo Wakenya watamchagua Dkt Ruto kuongoza nchi, hawezi kufanya kazi naye. Hii ni licha ya kuwa wawili hao walikuwa upande mmoja wakati wa uchaguzi mkuu wa 2007.

Matamshi hayo ya Bw Odinga ni kinaya kwa msimamo ambao amekuwa akitangaza kuwa dhamira kuu ya handisheki pamoja na Mpango wa Maridhiano (BBI) ni kuwaunganisha Wakenya wote na kuwa wako tayari kushirikisha kila mtu katika juhudi hizo.

Bw Odinga pia alionekana kumlaumu Dkt Ruto kama kizingiti kikubwa zaidi katika mpango wa Jopo la Maridhiano (BBI) akimtaja kuwa kigeugeu.

“Ni mtu anayeangalia jinsi mpango huu utamuathiri yeye binafsi ama maslahi yake huko mbele. Mnamo 2010 tulipokuwa tukipigania katiba mpya tulifanyishwa kibarua kigumu sana kuifanya ipitishwe. Sasa unapata baadhi ya waliokuwa wakiipinga wakisema haina tatizo na kuwa lengo la BBI ni kuundia watu fulani kazi. Hiyo ni ishara ya unafiki tulio nao hapa nchini,” akaeleza.

Dkt Ruto ni mmoja wa waliopinga katiba ya 2010 na sasa amekuwa akipinga baadhi ya mapendekezo ya BBI akidai inalenga kuongeza nyadhifa kuu serikalini.

Bw Odinga pia alimtaja Dkt Ruto kama muongo na kukanusha madai ya Naibu Rais kuwa alimtafuta wafanye maafikiano kabla ya kupatana na Rais Kenyatta.

“Nilishtuka niliposikia Ruto akisema kuwa nilimtafuta kwa ajili ya handisheki. Sikuwahi kuzungumza naye kwani hakukuwa na sababu yoyote ya kumtafuta,” akasema Raila.

Kwenye mahojiano hayo Bw Odinga pia alisema yeye si ‘Rais wa wananchi’ kama ambavyo amekuwa akiitwa na wafuasi wake tangu alipokula kiapo mbadala Januari 30, 2018.

Bw Odinga alisema sasa anamtambua Rais Kenyatta kama Rais wa Jamhuri ya Kenya, na kuwa wanashirikiana kukuza na kuunganisha taifa tangu handisheki iliyofuata kiapo hicho.

“Nilikana kiapo pindi tuliposalimiana na Rais. Hiyo ilikuwa ishara ya mwanzo mpya,” akasema.

Bw Odinga pia alikanusha kuwa yeye ni sehemu ya serikali ya Rais Kenyatta akisisitiza kuwa angali kiongozi wa upinzani. Hii ni licha ya kuwa amekuwa akiunga mkono sera na maamuzi ya serikali kinyume na awali ambapo alikuwa akiikosoa kwa hatua ambazo zilinyanyasa wananchi.

Bw Odinga pia amekuwa akishauriana na Rais kuhusu masuala tofauti ya kitaifa, suala ambalo linakinzana na madai yake kuwa angali katika upinzani.

Katika Bunge, wajumbe wa chama chake cha ODM wamekuwa wakipiga kura kila mara pamoja na wenzao wa upande wa Serikali.

Baadhi ya masuala mengine ambayo kiongozi huyo alizungumzia ni kuhusu uchaguzi wa uongozi ndani ya ODM ambao alisema umeahirishwa kutokana na kampeni za BBI.

“Hatutaki kuchanganya uchaguzi na suala la BBI. Tutakuwa na mkutano wa NEC ambao utaamua na kutangaza tarehe mpya,” akasema.

Alikiri kuwa vita vya kisiasa ndani ya chama hicho na madai ya ufisadi wakati wa uchaguzi vilisababisha kipoteze viti kadhaa katika Uchaguzi Mkuu wa 2017.

“Kumekuwa na visa vichache vya ufisadi, haswa maeneo ambapo uchaguzi wa mchujo wa ODM huwa ndio kama unaamua atakayeshinda Uchaguzi Mkuu. Ni hali ambayo ilituumiza kwani tulipoteza viti kadha maeneo ya Nairobi, Kisii, Magharibi na mengine nchini,” akasema.

Kuhusu Idara ya Mahakama, Bw Odinga aliilaumu kuwa haijajitolea kukabiliana na ufisadi, haswa miongoni mwa maafisa wake, na kuwa inalemaza vita dhidi ya ufisadi kwa kuua kesi.

“Wanajitetea kuwa ni upungufu wa pesa unaosababisha kesi kuchukua muda mrefu kortini. Lakini pia kuna majaji wafisadi na ambao bado idara hiyo inaendelea kuwapa mamlaka. Nimekuwa nikitetea Idara ya Mahakama lakini pia nayo inahitaji mageuzi ili kusikiza kesi kwa haraka na kuwafunga wafisadi,” akasema.