Wakereketwa wa BBI waomba kukubaliwa kucheza reggae

Na JUMA NAMLOLA

KIONGOZI wa ODM Raila Odinga anataka Mahakama ya Rufaa iruhusu kufanyika kwa kura ya maamuzi kuhusu BBI, wakati kesi ya kupinga mchakato huo inapoendelea kusikizwa.

Kwenye ilani ambayo Bw Odinga ameandaa kwa ajili ya kuwasilishwa katika Mahakama ya Rufaa kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu uliozima mchakato wa BBI, anasema shughuli hiyo isipoendelea itatumbukiza Kenya kwenye mgogoro wa kikatiba.

Kulingana na nakala zilizoandaliwa na wakili Paul Mwangi kwa niaba ya Bw Odinga na sekretariati ya BBI, shughuli hiyo ina umuhimu mkubwa wa kikatiba na hivyo inabidi iendelee kama ilivyopangwa.

“Shughuli ya kubadilisha Katiba ina kazi nyingi kwani ina muda mahsusi unaofaa kuzingatiwa. Hivyo ni muhimu kuhakikisha kuwa nia ya walioanzisha mchakato huu inaheshimiwa,” anasema Bw Odinga kwenye ombi lake.

Anasema Wakenya watapata hasara kubwa iwapo Mahakama ya Rufaa haitabatilisha uamuzi wa majaji watano wa Mahakama Kuu, uliosimamisha marekebisho hayo ya Katiba kupitia BBI.

Pia anasisitiza kuwa mchakato huo haukuanzishwa na Rais Uhuru Kenyatta kama walivyoamua majaji wa Mahakama Kuu, mbali na Mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohamed na aliyekuwa mbunge wa Dagoretti Dennis Waweru.

Bw Odinga anasema Mahakama Kuu ilijitwika mamlaka ya Wakenya milioni tatu waliotia saini kuidhinisha mchakato huo, jambo analoamini ni ukiukaji wa Katiba.

“Mahakama kimakusudi, ilipuuza ushahidi uliowasilishwa kuonyesha watu milioni tatu waliidhinisha marekebisho ya Katiba baada ya kuusoma na kuuelewa mswada wa BBI 2020,” inasema ilani hiyo ya rufaa.

Ilani hiyo ya rufaa yenye kurasa 438, inatoa sababu kadhaa zinazowakosoa majaji waliotoa hukumu ya kuzima rege ya BBI.Inasema walitoa uamuzi wao wakati ambapo tayari Wakenya milioni tatu, Mabunge ya kaunti zaidi ya 40 na Bunge la Taifa na Seneti yalikuwa yameshapitisha mswada huo.

Mnamo Mei 13, majaji Joel Ngugi, George Odunga, Jairus Ngaah, Chacha Mwita na Teresia Matheka walitupilia mbali mswada wa marekebisho ya Katiba kupitia BBI. wakisema unakiuka Katiba.

BBI: Majaji watano walivyozima midundo ya Reggae

Na SAMMY WAWERU

MAHAKAMA Kuu  Alhamisi jioni ilizima mchakato wa Ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI) ikiutaja kuwa haramu, batili na tupu hatua ambayo imetafsiriwa kuwa pigo kubwa kwa jitihada za Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM, Raila Odinga kufanyia Katiba marekebisho.

Korti kupitia uamuzi wake, ilihoji Rais Kenyatta alitumia vibaya mamlaka yake na kuenda kinyume cha sheria kukarabati Katiba.

Jopo la majaji watano wa mahakama kuu pia lilisema Rais alienda kinyume na kipengele cha sita cha Katiba, kinachoeleza kuhusu uongozi na uadilifu (wa Rais), kwa kujaribu kubadilisha Katiba kupitia mswada haramu wa BBI.

Uamuzi huo uliotolewa saa tatu na nusu usiku, uliorodhesha makosa kadhaa aliyotekeleza Rais Kenyatta katika jitihada zake kufanyia Katiba marekebisho. Aidha, mahakama kuu ilisema mengine yalifanywa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Korti ilitoa amri ya kudumu kwa IEBC kutoandaa zoezi la kura ya maoni, hadi pale itakapotayarisha rejista halali ya wapiga kura na hamasisho kuhusu haja ya Katiba kurekebishwa kufanywa.

BBI iliasisiwa na Rais Kenyatta na Bw Odinga, baada ya kutangaza kuzika tofauti zao za kisiasa mnamo Machi 2018, kupitia salamu za maridhiano maarufu kama Handisheki.

Masuala yaliyoibuliwa kupitia ripoti ya uamuzi wa Alhamisi wa korti, ulitolewa kiasi kuwa hakutakuwa na ukataji rufaa wowote.

Baadhi ya wanaharakati na mashirika yalielekea mahakamani kupinga uhalisia wa BBI. Viongozi kadha wa upinzani nchini walikuwa wanaunga mkono BBI.

Handisheki kati ya Rais Kenyatta na Odinga, ilichangia mrengo tawala wa Jubilee kugawanyika, vuguvugu moja, Kieleweke, likiegemea upande wa Rais na lingine, Tangatanga upande wa Naibu wa Rais, Dkt William Ruto.

“Kuna Mungu aliye juu mbinguni anayependa Kenya bila kipimo. Jina la Mungu liinuliwe,” Dkt Ruto na ambaye amekuwa mkosoaji wa BBI akachapisha katika ukurasa wake wa Twitter, baada ya uamuzi kuharamisha BBI kutolewa.

Azma ya Rais Kenyatta kubadilisha Katiba kupitia BBI, ilichangia baadhi ya viongozi na wanasiasa Jubilee kufurushwa kutoka nyadhifa zao bungeni na pia katika kamati mbalimbali, kama vile mbunge wa Garissa Mjini, Bw Aden Duale na Seneta wa Elgeyo Marakwet, Bw Kipchumba Murkomen kutokana na msimamo wao mkali, kukosoa mswada huo.

Mahakama kuu kwenye uamuzi wake uliosomwa kwa muda wa saa tano na nusu mfululizo, ilisema kamati ya kiufundi ya wanachama 14 walioteuliwa kukusanya maoni ya Wakenya na kuandaa BBI, ilikuwa haramu na ambayo haikutambulika kisheria.

Kamati hiyo iliongozwa na aliyekuwa seneta wa Garissa, Bw Yusuf Hajii.

Uamuzi huo wa aya 743, ulikuwa mrefu kiasi kuwa majaji waliusoma kila mmoja kwa awamu yake.

Jopo la majaji hao watano, na lililoongozwa na Prof Joel Ngugi, lilisema Rais Kenyatta alifanya kosa kubwa kwa kujaribu kurekebisha Katiba kupitia mswada maarufu, na ambao haukufuata sheria.

Ilieleza, badala yake Rais angetumia bunge la kitaifa kupitia Mwanasheria Mkuu, kukarabati Katiba.

Aidha, korti ilisema marekebisho ya Katiba hayana shotikati ila kutumia asasi ya bunge na mswada maarufu uliofuata sheria.

Mahakama kuu ilisema BBI ilikuwa “mpango” wa Rais, uliochukuliwa kama njia halali kubadilisha Katiba, na kuruhusu sheria kubadilishwa kupitia mkondo huo ingeonekana kama kumpa Rais mwanya wa urefarii kuafikia mipango yake.

“Haiwezi ikawa Rais ndiye mwasisi au mwanzilishi wa Katiba kufanyiwa marekebisho,” mahakama hiyo ikasema, ikiongeza kuwa BBI iliongozwa na tamaa za ubinafsi.

Majaji walisema Rais alivuka mipaka ya mamlaka yake, kupendekeza Katiba ikarabatiwe, ilhali sheria imeweka wazi majukumu yake kama kiongozi wa nchi.

Kwa waliodhania Rais Kenyatta alilenga kuleta umoja wa taifa kupitia pointi tisa zilizoorodheshwa katika mswada huo, korti ilisema dai hilo limesalitiwa na ukweli kuwa jopokazi la BBI liliundwa na Rais mwenyewe na lilikuwa likiripoti kwake.

“Ukweli ni kwamba BBI ilikuwa mpango wa Rais na uliokiuka kipengele cha 257 cha Katiba. Jopokazi lililoundwa lilikuwa haramu tangia mwanzo,” majaji wakasema.

Jopo la majaji hao lilizima tetesi za waliolinganisha BBI na jitihada za Rais (Mstaafu) Mwai Kibaki kubadilisha Katiba 2005 na 2010, chini ya utawala wake.

Majaji walisema Bw Kibaki alifanya mabadiliko kwa kufuatia sheria za Katiba ya awali, iliyoasisiwa wakati wa utawala wa Mbeberu. Katiba ya sasa, ilizinduliwa 2010 na kuanza kutumika 2013.

Chini ya Katiba ya sasa, majaji hao walisema imeweka wazi kuhusu marekebisho, ila kupitia mswada maarufu na Rais aliye madarakani, afisi ya Rais au asasi ya serikali, hazijaorodheshwa.

Walisema kisheria mapendekezo ya marekebisho ya Katiba yanapaswa kuanzishwa na raia binafsi au kundi la raia binafsi, lakini si asasi ya serikali.

Wanaounga mkono BBI waliambia mahakama kuwa Rais alitumia haki yake Kikatiba, kufanya ukarabati. Majaji hata hivyo walisema Rais alishindwa kulinda Katiba, na kukiuka kifungu kinachoeleza kuhusu uongozi wake na uadilifu.

“Huku jitihada zake kuunganisha taifa na kuleta umoja zikipigiwa upatu, hawezi akaanzisha mpango kurekebisha Katiba. Hatua hiyo haipo chini ya majukumu yake kama kiongozi wa nchi,” korti ikasisitiza.

Majaji walisema kwa sababu mpango huo ulikuwa haramu tangia awali, yote yaliyolengwa kuafikiwa hayataleta mtafaruku wowote kisheria, baada ya kuuharamisha.

Mahakama kuu pia ilisema Rais Uhuru Kenyatta (kama rais aliye madarakani) anaweza kushtakiwa binafsi kufuatia matendo yake au kukiuka Katiba.

Katiba inasema mashtaka ambayo hawezi kufunguliwa ni ya uhalifu, wakati akiwa mamlakani.

BBI: Reggae yazimwa kwa mara ya tatu

NA BENSON MATHEKA

Kwa mara ya tatu juhudi za kubadilisha Katiba ya Kenya ya 2010 zimegongwa mwamba Mahakama Kuu ilipozima mchakato wa BBI ulioanzishwa na Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga.

Hii ilikuwa mara ya pili kwa juhudi anazoshiriki Bw Odinga kubadilisha katiba aliyopigania kukosa kufua dafu. Mnamo 2015 akishirikiana na vinara wenzake katika uliokuwa muungano wa Cord, walianzisha mchakato wa Okoa Kenya kwa lengo la kubadilisha Katiba.

Walikusanya saini kutoka kwa wafuasi wao walizowasilisha kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC). Hata hivyo, tume ilizima mchakato huo ikisema haukuungwa mkono na wapigakura 1 milioni inavyohitajika kikatiba.

Mnamo 2019, chama cha Third Way Alliance kikiongozwa na wakili Ekuro Aukot, kiliwasilisha mswada wa kubadilisha katiba wa Punguza Mzigo uliolenga kupunguza idadi ya wabunge miongoni mwa mapendekezo mengine ya kupunguza gharama ya kuendesha serikali na kukabili ufisadi ili kutenga pesa zaidi za maendeleo.

Mswada huo ulipata umaarufu na kupiga hatua baada ya IEBC kuamua uliungwa na zaidi ya wapigakura 1 milioni. Hata hivyo, vigogo wa kisiasa nchini akiwemo Bw Odinga waliupinga na kushawishi madiwani katika kaunti zilizo ngome zao kuukataa.

Lengo la Bw Odinga na wenzake kukataa mswada huo ni kuwa ulipunguza nyadhifa serikalini ambazo wanasiasa hutumia kujinufaisha.

Mswada wa Punguza Mzigo, ulishika kasi wakati kamati ya BBI iliyoundwa na Rais Kenyatta na Bw Odinga ilikuwa ikiendelea kukusanya maoni kutoka kwa umma.

Bw Odinga aliwataka wanasiasa wa chama chake kuunga BBI badala ya Punguza Mzigo kwa kuwa ilibuni nyadhifa zaidi za uongozi yakiwemo maeneobunge zaidi.

Hata hivyo, licha ya mswada wa BBI kupiga hatua hadi ukafika bungeni, juhudi za kubadilisha katiba ya 2010 zilitibuka kwa mara ya tatu. Kulingana na wataalamu wa katiba, kutibuka kwa juhudi kubadilisha katiba mara tatu kunaonyesha kwamba walioandika katiba ya 2010 walihakikisha haingevurugwa kwa urahisi na viongozi ili kutimiza maslahi yao ya kibinafsi dhidi ya raia wa kawaida.

“ Msingi uliowekwa katika katiba ya 2010 unaikinga ili isibadilishwe kiholela kutimiza maslahi ya wachache walio mamlakani. Hii ilijitokeza wazi katika uamuzi wa majaji watano Alhamisi,” asema wakili na mwanaharakati Waikwa Wanyoike.

Wakili Ahmednassir Abdullahi alisema kwamba uamuzi ni onyo kwa Rais Kenyatta kwamba Wakenya sio watumwa wake. “ Kwa muhtsari uamuzi wa majaji watano unamaanisha: “Bw Rais, wewe sio Mfalme na Wakenya sio watumwa wako. Mamlaka Makuu ni ya Wanjiku,” alisema Bw Ahmednassir kupitia Twitter

Kiunjuri abadilisha wimbo, sasa asakata Reggae ya BBI

Na JAMES MURIMI

ALIYEKUWA waziri wa Kilimo Mwangi Kiunjuri, amebadili msimamo wake kuhusu Mpango wa Maridhiano (BBI) na kuwataka Wakenya kupitisha mswada huo kupitia kura ya maamuzi.

Kiongozi huyo wa chama cha Service Party (TSP) na mwandani wa Naibu wa Rais William Ruto, amekuwa akipinga vikali mswada wa BBI unaoungwa mkono na Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga.

“Nimechunguza mswada wa BBI na nimebaini kuwa asilimia 80 ya mambo yaliyomo kwenye mswada huo ni sawa kabisa. Mimi na Naibu wa Rais tumeamua kutopinga BBI.

“Mtu yeyote anayejaribu kutusukuma tupinge BBI atapata aibu. Hatutapinga ng’o,” akasema Bw Kiunjuri katika mahojiano na runinga moja ya humu nchini.

Msimamo wa Bw Kiunjuri uliambatana pia na kauli ya Naibu Rais William Ruto, ambaye alisema kuwa hatajiingiza kwenye mtego ambapo atachukua hatua itakayoleta mgawanyiko nchini. Dkt Ruto alisema hayo jana akiwa katika Kaunti ya Narok.

Bw Kiunjuri anaamini atakayemrithi Rais Kenyatta mwaka ujao, atatekeleza mabadiliko yaliyomo kwenye mswada wa BBI.

“Mabadiliko yaliyomo kwenye mswada huo yatafaidi Wakenya wote na wala si viongozi wachache. Kiongozi wa nchi atakayechukua hatamu za uongozi baada ya Rais Kenyatta kustaafu, atatekeleza mapendekezo yaliyomo katika Mswada wa BBI,” akasema.

“Hakuna serikali mbili. Rais Kenyatta ametekeleza majukumu yake vyema. Tunahimiza mrithi wake kuhakikisha kuwa asilimia 35 ya mapato ya nchi inapelekwa katika kaunti kama ilivyopendekezwa katika Mswada wa BBI,” akaongezea.

Kabla ya kuvuliwa wadhifa wa uwaziri, Bw Kiunjuri mnamo Oktoba 2019, alikutana na kundi la wabunge 42 kutoka eneo la Mlima Kenya katika majengo ya Bunge ambapo waliafikiana kuwa wangepinga ripoti ya BBI.

Baada ya kikao, viongozi hao waliapa kupinga pendekezo la kutaka rais au waziri mkuu kuchaguliwa na wabunge.

Waziri huyo wa zamani alidokeza mwaka jana kuwa atakuwa mwaniaji mwenza wa Dkt Ruto katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Jana, alisema kuwa atashukuru Mungu iwapo atateuliwa na Dkt Ruto kuwa mwaniaji mwenza wake.

Mbunge huyo wa zamani wa Laikipia Mashariki, alishikilia kuwa eneo la Mlima Kenya ni sharti litoe mwaniaji mwenza ambaye atapigania masilahi yao katika serikali ijayo.

“Nimekuwa nikisikia uvumi kwamba ninalenga kuwa mwaniaji mwenza wa Dkt Ruto, lakini mimi sijawahi kutamka hilo. Lakini ikiwa hivyo, basi yatakuwa mapenzi ya Mungu ambayo hayawezi kuzuilika,” akasema Bw Kiunjuri.

Aliongeza, “Siasa za 2022 zimeshika kasi lakini sisi watu wa jamii ya Wakikuyu tumenyamaza tu. Tunafaa kuanza mikakati ya kutafuta mtu atakayetuwakilisha serikalini.”

Raila atua Pwani kufunza wakazi kusakata Reggae

KIONGOZI wa Chama cha ODM, Raila Odinga leo amepangiwa kuanza rasmi ziara yake eneo la Pwani kupigia debe mswada wa marekebisho ya katiba kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI).

Bw Odinga jana alitua katika Kaunti ya Taita Taveta lakini hakufanya mkutano wowote wa hadhara ilivyotarajiwa na wengi.Amepangiwa kuzuru kaunti za Mombasa, Kwale, Kilifi, Lamu na Tana River ili kuendeleza kampeni za BBI katika ukanda huo.

Bw Odinga leo amepangiwa kukagua soko la kisasa la Mwatate, mradi wa ujenzi wa hospitali ya ugonjwa wa corona mjini humo kisha kuhutubia wenyeji wa mji huo kabla ya kufungua shule ya Mwakinyungu katika eneo la Rong’e.

Baadaye atahutubia wenyeji wa Voi kabla ya kuendeleza safari yake Kaunti ya Mombasa.’Safari yake inalenga kuzindua kampeni za BBI katika eneo la Pwani,’ alisema mwenyekiti wa ODM katika Kaunti ya Taita Taveta, Richard Tairo.

Kiongozi huyo pia atakutana na viongozi wa kaunti hiyo ili kujadili mikakati ya kuendeleza kampeni za BBI katika eneo hilo.Baadhi ya viongozi wanaotarajiwa kuhudhuria mkutano huo ni gavana Granton Samboja, seneta wa kaunti hiyo Jones Mwaruma, wabunge Jones Mlolwa (Voi), Andrew Mwadime (Mwatate), aliyekuwa mbunge wa Wundanyi Thomas Mwadeghu na madiwani.

Vilevile ziara ya kiongozi huyo inapania kufufua umaarufu wake unaotishiwa kudidimia viongozi wengi wakipigania chama huru cha Wapwani.

Chama cha ODM, ambacho kimekuwa kikipata uungwaji mkono mkubwa katika eneo hilo, kilipata pigo baada ya baadhi ya wanasiasa kuhamia mrengo wa Tangatanga unaounga mkono azma ya Naibu Rais William Ruto.

Viongozi hao vilevile wamekuwa mstari wa mbele kupinga BBI na hivyo kuzua tumbojoto ikiwa mswada huo utapenya ifikapo kura ya maoni mnamo Juni.

Ziara ya kiongozi huyo inajiri baada ya Dkt Ruto kuzuru eneo hilo wiki chache zilizopita. Bw Raila ananuia kupoza ziara ya Bw Ruto ambaye anaaminika kuwa anaendelea kupata umaarufu katika eneo hilo.

Corona yasimamisha ‘Reggae’ Pwani

Na MOHAMED AHMED

KIVUMBI cha kisiasa kilichoanza kushika kasi katika kampeni za uchaguzi mdogo wa Msambweni kimeanza kufifia kufuatia agizo la serikali kusitisha mikutano ya kisiasa.

Rais Uhuru Kenyatta alitoa agizo hilo wiki jana na kuelekeza wanasiasa nchini kusitisha mikutano ya hadhara kwa siku 60 ili kupunguza maambukizi ya virusi vya corona.

Tayari, mgombeaji wa kiti cha ODM, Omar Boga ametangaza kuwa ameambukizwa corona na yuko karantini.Rais Kenyatta alisema kuwa, wanasiasa wataruhusiwa kufanya mikutano katika kumbi ambazo zitaruhusu watu wachache pekee.

Agizo hilo, hivyo basi limefifisha ubabe wa kisiasa uliokuwa unatazamiwa kujitokeza kati ya Naibu Rais William Ruto na mpinzani wake kinara wa ODM Raila Odinga.

Wawili hao walitarajiwa kuongoza kampeni katika eneo bunge hilo ili kuwapigia debe wawaniaji wanaowaunga mkono kwenye uchaguzi huo ambao utafanyika mnamo Disemba 15.

Bw Odinga anampigia debe Omar Boga ambaye ndiye anapeperusha bendera ya chama cha ODM huku Bw Ruto naye akiegemea upande wa Feisal Bader ambaye anawania kiti hicho kama mgombeaji huru.Tayari, washirika wa wawili hao walikuwa wameanza kampeni za kuwapigia debe wawaniaji wao.

Upande wa Bw Ruto unaongozwa na waliokuwa maseneta Johnson Muthama (Machakos), Hassan Omar (Mombasa) na Boni Khalwale wa Kakamega.Kundi hilo limekuwa likiendeleza siasa eneo hilo kwa muda wa wiki mbili mfululizo sasa.

Wanasiasa wa ODM wakiongozwa na katibu wa chama Edwin Sifuna pia walikuwa wamepigga kambi eneo hilo.Kufuatia agizo hilo, pande zote mbili zimetangaza kusitisha siasa zake za mikutano ya hadhara.

Bw Ruto amesema atafanya hilo hadi pale ataeleza wafuasi wake tofauti. “Nimeamua kusitisha mikutano mpaka baadaye. Mikutano ambayo ilikuwa nimepanga katika kaunti tofauti pia nimesitisha,” akasema Bw Ruto kwenye mtandao wake wa Twitter.ODM nao walisema kuwa watafuata agizo la serikali kama lilivyotangazwa na Rais Kenyatta.

“Leo tumechangisha pesa kwa ajili ya kampeni zetu za maeneo bunge ya Msambweni, Wundanyi/Mbale, Kisumu Kaskazini na Dabaso kwa ajili ya uchaguzi wa Disemba 15. Katibu wetu Edwin Sifuna ametangaza kuwa kampeni zetu zitafanywa chini ya kanuni mpya ambazo zimetangazwa,” ilisema taarifa ya ODM.

Kampeni hizo zimeanza kuchukua mkondo mpya huku wale wanaongoza kampeni wakionekana kufuata agizo la serikali la kufanya mikutano kwenye kumbi.

Hali hiyo tayari imeondoa mihemko ya kisiasa ambayo huletwa na mikutano ya siasa inayozua hisia tofauti.Kwa sasa, itasubiriwa kuonekana ni vipi siasa hizo zitaendelea hadi siku ya kura huku ikiwa wazi kuwa wale wanaowania watapata wakati mgumu kuuza sera zao.

Wengine wanaowania kiti hicho ni pamoja na wale wa vyama huru, Bi Sharlet Mariam Akinyi, Mansury Kumaka, Charles Bilali, Shee Abdulrahman (Wiper), Ali Hassan Mwakulonda (Party of Economic Democracy), Marere Wamwachai (National Vision Party) and Khamis Mwakaonje (United Green Movement).

Gavana wa Mombasa, Hassan Joho na mwenzake wa Kwale, Salim Mvurya pia walikuwa wameahidi kuonyeshana kivumbi. Bw Joho anamuunga Bw Boga naye Mvurya anampigia debe Bw Bader.

Tayari, uhasama wa kisiasa ulikuwa umeanza kujitokeza kati ya magavana hao wawili kuhusiana na uchaguzi huo mdogo. ? Bw Mvurya alikuwa amemuonya Bw Joho na kusema kuwa hatakubali kaunti yake ya Kwale itumike kama ‘kiwanja cha vita’ akimaanisha siasa za ubabe ambazo Bw Joho ametambulika nazo.

Kwa sasa, itasalia kutazamwa namna viongozi hao watakavyomenyana kisiasa kwenye uchaguzi huo mdogo ambao wengi wamesema kampeni zake zimekosa makali kufuatia kusitishwa kwa mikutano ya hadhara.

Huu wimbo wa Reggae kamwe haumlengi Ruto – Raila

Na MARY WANGARI

KIONGOZI wa Orange Democratic Movement (ODM) Raila Odinga amefafanua kuhusu wimbo anaopenda wa mtindo wa reggae almaarufu “Nobody Can Stop Reggae” akikanusha madai kwamba unamlenga kisiasa Naibu Rais William Ruto.

Waziri mkuu huyo wa zamani alifafanua kwamba wimbo huo unaoashiria kwamba hakuna anayeweza kwa vyovyote kulemaza juhudi za kufanikisha Mpango wa Maridhiano (BBI), ulikuwepo tangu zamani.

“Huu ni wimbo wa zamani, haukuimbwa jana kuwalenga watu mahsusi. Watu hawa wanaoona mabaya kwa kila jambo, wanajihofia. Wimbo huu haumlengi Dkt William Ruto. Ruto ni miongoni mwa Wakenya milioni 47, hatuwezi kubuni mpango wa kumlenga,” alisema Bw Odinga.

Katika mahojiano na vyombo vya habari, Bw Odinga alieleza kwamba Naibu Rais hapo mbeleni alikuwa amejiunga naye pamoja na Rais Uhuru Kenyatta kupigia debe BBI kabla ya kugeuka na kukosa msimamo.

Huku akifichua kwamba ndiye aliyemnoa kisiasa Dkt Ruto, Bw Raila alionekana kuwa na uhakika kwamba juhudi za naibu rais za kupinga BBI zingeambulia patupu hatimaye.

“Nani angefikiri kwamba Ruto angepinga BBI. Kwanza alikuwa akiiunga mkono kisha akaanza kukosa msimamo thabiti. Sasa anasema anapinga. Anasema atakomesha reggae, tunamtakia kila la kheri,” alisema kiongozi huyo wa ODM.

 

Hii ‘reggae’ ya BBI nitaizima, aapa Ezekiel Mutua

NA CECIL ODONGO

AFISA Mkuu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Nchini (KFCB) Dkt Ezekiel Mutua ameonya MaDJ ambao hukodishwa kutumbuiza kwenye mikutano ya Jopokazi la Maridhiano (BBI) kwamba watakamatwa kwa kucheza muziki uliopigwa marufuku.

Dkt Mutua alisema muziki ambao umekuwa ukisakatwa kwenye mikutano hiyo si wa kimaadili huku pia akiwakashifu viongozi wa kisiasa kwa kutoa matamshi yaliyosheheni lugha chafu dhidi ya wapinzani.

“Nitasimamisha ‘Reggae’ kwa kuwanyaka MaDJ wanaocheza muziki kwenye mikutano ya BBI. Wakati wa mkutano wa wikendi mjini Narok, walichezesha nyimbo ambazo nilizipiga marufuku na tutawachukulia hatua za kisheria iwapo watadhubutu kurudia hilo,” akasema Dkt Mutua Jumatatu afisini mwake.

Baadhi ya nyimbo alizolalamika zimekuwa zikichezwa mara kwa mara kwenye hafla za BBI ni ‘Tetema’ ya msanii Diamond Platnumz kutoka nchi jirani ya Tanzania na ule wa ‘Wamlambez’ ulioimbwa na kundi wanamuziki kwa jina Ethic.

Alifichua kwamba kuna muziki ambao umeteuliwa kimakusudi kutumika wakati wa mikutano ya umma na sherehe za kitaifa badala ya muziki chafu unaoyeyusha maadili na usiomtukuza Mungu.

Dkt Mutua alisema hayo wakati wa kuzindua mabalozi wa KFCB watakaohakikisha kwamba muziki na video chafu zinakomezwa katika kaunti zote 47 nchini.

Mabalozi hao watasimamiwa na mchekeshaji nguli Walter Mong’are na mwanafasheni maarufu Betty Adera.

Aidha afisa huyo alipendekeza sheria zibadilishwe ili KFCB iondoe kizuizi cha kudhibiti muziki unaochezwa kutoka saa tano asubuhi hadi saa nne usiku pekee.

“Sheria zinafaa kubadilishwa ili muda tuliowekwa wa kuhakikisha kwamba muziki na video chafu hazienei unaondolewa na KFCB kuruhusiwa kufanya kazi kwa saa 24.

“Kuna baadhi ya vipindi vichafu kwenye runinga zetu lakini huanza baada ya saa nne usiku. Ni jukumu la wazazi kuhakikisha watoto wao hawatazami vipindi hivyo,” akaongeza Dkt Mutua.

Hata hivyo, aliwasifu wahudumu wa matatu kwa kutii sheria na kukoma kuonyesha kanda za video za ngono kwenye magari yao. Pia aliwataka raia kupiga simu kupitia nambari maalum inayopatikana kwenye mtandao wao ili kuripoti magari yanayokiuka masharti ya KFCB.

Vilevile Dkt Mutua alipuuza dhana miongoni mwa Wakenya kwamba muziki au video chafu huuza na kumpa mwanamuziki umaarufu kuliko ule uliotungwa bila masuala ya ngono.

Alisema ushawishi huo hupotea baada ya muda mfupi na nyimbo hizo kusahaulika haraka.

Mhemuko Uhuru na Raila wakijipa raha mtindo wa Reggae

Na LEONARD ONYANGO

RAIS Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga walikuwa miongoni mwa mamia ya wapenzi wa muziki wa reggae waliojumuika katika ukumbi wa Carnivore jijini Nairobi kutumbuizwa na bendi kutoka Uingereza, Jumamosi usiku.

Kabla ya kwenda kuburudika, Rais Kenyatta Jumamosi alihudhuria hafla mbalimbali katika Kaunti za Meru na Kirinyaga huku Bw Odinga akiongoza mkutano wa kupigia debe ripoti ya Muafaka wa Maridhiano (BBI) katika Kaunti ya Kitui.

Video zilizosambazwa katika mitandao ya kijamii zinawaonyesha Rais Kenyatta na Bw Odinga wakionyesha weledi wao katika usakataji wa reggae ambao ni muziki unaohusishwa zaidi na jamii ya Rasta.

Rais Kenyatta husema wazi katika mahojiano jinsi anavyokienzi kikundi cha reggae cha UB40.

Miaka michache iliyopita, Bw Odinga pia aliambia kipindi cha Churchill Show ambacho hupeperushwa katika runinga ya NTV kila Jumapili jioni kwamba ni mpenzi wa muziki wa reggae.

“Wanamuziki wa reggae ninaowapenda zaidi ni kikundi cha UB40, Gregory Isaac na Bob Marley,” akasema Bw Odinga.

Katika mikutano ya BBI, Bw Odinga amekuwa akitumia wimbo wa Nobody Can Stop Reggae (hakuna mtu anayeweza kuzuia rege) wake Lucky Dube.

Bw Odinga amekuwa akitumia kibao hicho kwa maana kwamba hakuna mtu atakayezuia kura ya maamuzi ya kubadili katiba ili kujumuisha mapendekezo yaliyomo ndani ya ripoti ya BBI.

Kibao hicho chake Lucky Dube pia kilichezwa katika ukumbi wa Carnivore.

Katika moja ya video, Bw Odinga anaonekana jukwaani akisakata densi huku akipinda mgongo na kuchuchumaa.

Jana, Raila Odinga Junior, mwanawe Raila, alitia picha mtandaoni akimkabidhi kiongozi wa ODM mchongo wa picha ya Bob Marley.

“Nimemwonyesha Baba Raila Odinga mchongo huu wa Bob Marley aliopewa na ndugu yangu marehemu Fidel tuliporejea kutoka Kingston, Jamaica. Hakika hakuna mtu anayeweza kuzuia reggae,” akasema Raila Odinga.

Kwa upande mwingine, Rais Kenyatta aliyekuwa akisakata densi karibu na mwanahabari Jeff Koinange, anaonekana akiimba kwa kufuata mapigo ya muziki.

Kikosi cha UB40 kilichobuniwa mnamo 1978, kimejizolea umaarufu kutokana na nyimbo zake motomoto kama vile Red Red Wine. Kikundi hicho kiliundwa na ndugu wawili Ali Campbell na Robin Campbell kabla ya kukosana na kugawanyika mnamo 2008.

Waziri wa Michezo na Utamaduni Amina Mohamed alikaribisha bendi hiyo akisema uwepo wake nchini ni motisha kubwa kwa vijana wasanii.

UNESCO kulinda muziki wa Reggae kimataifa

VALENTINE OBARA na AFP

MUZIKI wa reggae umepata ulinzi mkuu wa kitamaduni baada ya kutambuliwa na shirika la Umoja wa Mataifa linalosimamia masuala ya Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kama utamaduni unaopaswa kuhifadhiwa.

Kwa mujibu wa UNESCO, muziki wa Reggae, ambao mizizi yake ni Jamaica, unastahili kulindwa na kukuzwa kwa sababu ya mchango wake kwenye midahalo ya kimataifa kuhusu ukiukaji wa haki, mapinduzi, upendo na utu.

Shirika hilo lilieleza kwenye taarifa kwamba Reggae, ambayo pia ina ushabiki mkubwa Kenya, ina misingi ya kijamii, kisiasa na kiimani.

Wakati huo huo, tamaduni za jamii ya Wamaasai za Enkipaata, Eunoto na Olng’esherr sasa zitalindwa kimataifa zisiangamie baada ya kuzitambua

Tamaduni hizi za kuingiza wavulana kwa utu uzima zimetambuliwa kama zinazostahili kulindwa kwani zimo kwenye hatari ya kumalizwa na mienendo ya maisha ya kisasa.

Kutambuliwa kwa tamaduni hizi ni heshima kubwa kwa jamii ya Maasai, ambayo imefanikiwa kwa kiwango kikubwa kuliko zingine nchini kulinda tamaduni zake.

Tamaduni hizo sasa zimeingia kwenye orodha moja na densi ya Isikuti ya jamii za Isukha na Idakho kutoka Magharibi mwa Kenya, ambayo ilitambuliwa mnamo 2014, na tamaduni za Kaya katika jamii za Mijikenda zilizoidhinishwa na UNESCO mwaka wa 2009.

Uharibifu wa tamaduni au sehemu zinazolindwa na UNESCO huwa unaweza kupelekea mtu kuadhibiwa kwa msingi wa sheria za kimataifa, ikiwemo kufunguliwa mashtaka katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC).

Wakati Reggae ilipoanza kuchipuka, ilisifiwa kama muziki wa watu wanaokandamizwa kwani maneno ya nyimbo hizo yalihusu masuala ya siasa za kijamii, watu kufungwa gerezani bila hatia, na ukosefu wa usawa katika jamii.

Miongoni mwa wasanii waliopatia muziki huu umaarufu ulimwenguni ni Bob Marley, Mighty Culture, Burning Spear na Lucky Dube aliyekuwa raia wa Afrika Kusini.

UNESCO huwa inalinda sanaa na tamaduni nyingine zaidi ya 300 zikiwemo zinazohusu mapishi ya kitamaduni na hija za madhehebu ya kidini.

Shirika lataja Reggea kama kikwazo kwa elimu ya watoto

Na CHARLES LWANGA

SHIRIKA la kijamii la kupambana na mihadarati mjini Malindi limesemaa miziki ya kisasa aina ya Reggea inachangia katika uzorotaji wa viwango vya masomo miongoni mwa vijana na kusababisha takriban vijana 300 kuacha masomo kila mwaka.

Bw Edison Mwabonga, ambaye ni afisa wa miradi katika shirika la Omar Project mjini Malindi, linalohudumia waathiriwa wa mihadarati katika Kaunti ya Kilifi, Tana River na Lamu alisema vijana wengi huanza kuvuta bangi jinsi wanavyoshuhudia katika nyimbo hizo kabla ya kuacha masomo.

“Mara nyingi vijana huiga wanachotazama katika televisheni kama vile kuvuta bangi, uhalifu na uasherati ambao huwafanya kuwa watundu,” aliambia Taifa Leo.

Baadhi ya wasanii maarufu wa Raggae kama vile marehemu Bob Marley, Joseph Hill na wengineo kutoka Jamaica wamesifia sana bangi na hata kuvuta katikati ya nyimbo zao.

Vilevile, haya yameletwa na disko matanga na uongezekaji wa maskani za kunywa pombe maarufu kama mangwe ambazo pia zimeongeza visa vya uhalifu Mnarani na Maweni.

Kamishna wa Kaunti Magu Mutindika pamoja na Gavana Amason Kingi wamepiga marufuku disko matanga kama njia mojawapo ya kuwawezesha vijana kuhudhuria shule na kupunguza mimba za mapema.

Bw Mwabonga ambaye amehudumia shirika hilo tangu mwaka wa 1990 alisema vijana 900 wenye umri wa miaka 18 hadi 37 walioathiriwa na mihadarati wanapokea matibabu ya Methadone katika hospitali ya Malindi.

“Vijana wengine 2,446 katika Kaunti ya Lamu, Tana River na Kilifi wanapokea sindano za kuwasaidia kuepuka mihadarati wanayotumia kujidungia dawa ya methadone,” alisema.

Alisema pia baadhi ya vijana hao walikuwa wemejiingiza katika sekta ya utalii na ukahaba kabla ya kuokolewa na shirika hilo kutokana na dawa za kulevya.

Kwa upande wake, Bw Khamid Mudaris, ambaye ni mpangaji maalum katika Shirika la Omar Project alisema upatikanaji wa mihadarati hizo kama vile miraa, mugoka na bangi ndio chanzo cha ongozeko la ujambazi na mimba za mapema.