SIHA NA LISHE: Machungwa yana manufaa tele mwilini

Na MARGARET MAINA

mwmaina@ke.nationmedia.com

Mmeng’enyo wa chakula

CHUNGWA lina kiwango kikubwa cha nyuzinyuzi ‘fibre’ ambazo husaidia usagaji wa chakula tumboni na humpa afueni mtu mwenye matatizo ya tumbo.

Shinikizo la damu

Madini ya Magnesium yaliyomo kwenye chungwa husaidia kuondoa tatizo la shinikizo la damu (high blood pressure), hivyo machungwa ni mazuri kwa wagonjwa wa presha.

Ugonjwa ya mapafu

Chungwa pia lina kiasi kikubwa cha Vitamini B6 na madini ya chuma, virubisho ambavyo ni muhimu kwa uzalishaji wa seli nyekundu za damu, ambazo hufanya kazi ya kusafirisha hewa ya oksijeni mwilini, hivyo kuwa muhimu kwa kujikinga dhidi ya ugonjwa wa mapafu.

Mifupa na meno

Chungwa lina kiasi kingi cha madini ya calcium ambayo ni muhimu kwa uimarishaji wa mifupa na meno.

Afya ya ngozi

‘Anti-oxidants’ zilizomo kwenye chungwa huweka kinga thabiti kwenye ngozi ili isiharibike au kushambuliwa na magonjwa ya ngozi yanayoweza kujitokeza kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa. Pia huifanya ngozi ‘isizeeke’.

Lehemu

Virutubisho vilivyomo kwenye chungwa, hasa kwenye ngozi yake, hupunguza kiwango cha mafuta mabaya mwilini (bad cholesterol).

Kinga ya mwili

Vitamini C iliyomo kwenye chungwa huimarisha uzalishaji wa seli nyeupe ambazo ni muhimu kwa uimarishaji wa kinga ya mwili. Unapokuwa na kinga imara, huwezi kusumbuliwa na magonjwa mara kwa mara.

Mafua

Kutokana na wingi wa virutubisho vya kinga vilivyomo kwenye chungwa, ulaji wake mara kwa mara utakuepusha na magonjwa yanayoambukizwa na virusi kama vile mafua.

SIHA NA ULIMBWENDE: Manufaa ya kutumia mafuta ya ‘Bio-Oil’ mwilini

Na MARGARET MAINA

mwmaina@ke.nationmedia.com

BIO-Oil ni mafuta yanayosifika sana na wengi hupenda kuyatumia.

Kuondoa michirizi

Moja kati ya matumizi makubwa sana ya Bio-Oil ni kuondolea michirizi. Michirizi ni mistari inayotokea kwenye ngozi sanasana tumboni na mapajani kutokana na ngozi kupoteza uwezo wake wa kuvutika. Matumizi ya Bio-Oil kwa usahihi husaidia kupunguza ama kuondoa kabisa tatizo la michirizi katika ngozi.

Kuondoa makovu

Bio-Oil husaidia sana kuondoa makovu, hasa mtu anapoanza kutumia mapema mara tu baada ya kidonda au jeraha kupona.

Makovu machanga hupona haraka zaidi kuliko makovu ya muda mrefu.

Kutibu ngozi iliyosinyaa na kunyauka

Kwa mtu mwenye ngozi iliyoanza kuzeeka au iliyozeeka, basi atumie Bio-Oil. Baada ya muda, ngozi yake itarejea hali ya uzuri na yenye afya.

Kutibu ngozi kavu/ Ngozi iliyokauka

Bio-Oil inasaidia kuboresha afya ya ngozi na kuiwezesha iwe na maji na unyevu wa kutosha. Ngozi kavu ni rahisi kuzeeka na kwa hiyo matumizi ya Bio-Oil yatasaidia kuzuia ngozi kuzeeka kwa urahisi.

Kurekebisha rangi tofauti za ngozi na kuifanya iwe rangi moja

Bio-Oil husaidia kurejesha afya ya seli za ngozi na kusaidia mwonekano wake mzuri.

Husaidia kuondoa rangi mbaya zisizopendeza zinazotokana na athari za jua, vipodozi, kuungua na kadhalika.

Matokeo yake ni kuwa na ngozi nzuri yenye kupendeza na rangi inayofanana.

Bio-Oil hupatikana kwenye maduka ya dawa na maduka ya vipodozi.

SIHA NA ULIMBWENDE: Jinsi ya kutumia juisi ya karoti kuondoa mikunjo kwenye ngozi

Na MARGARET MAINA

mwmaina@ke.nationmedia.com

MIKUNJO katika ngozi ni miongoni mwa matatizo yanayowakabili wanawake wengi.

Tofauti na mikunjo ya uzee, mikunjo hii hutokana na kuchoka kwa ngozi kunakosababishwa na mambo mbalimbali.

Katika kupambana na tatizo hilo, zifuatazo ni njia mbalimbali zinazoweza kutumika kutatua tatizo hili.

Unashauriwa kumwona mtaalamu wa afya kwa ushauri zaidi wa matumizi ya njia hizo za asili kabla ya kuanza kuzitumia.

Unaweza kutumia viungo vinavyopatikana jikoni kwako kupambana na mikunjo katika ngozi. Baadhi ya viungo hivyo ni pamoja na:

Karoti

Tumia juisi ya karoti kwa kupaka katika ngozi yako, hasa katika maeneo yaliyoathirika.

Karoti ina virutubisho muhimu kwa ngozi yako. Pia ina uwezo mkubwa wa kuondoa sumu ndani ya ngozi.

Si hivyo tu, karoti inaweza kuondoa kabisa tatizo la mikunjo ya ngozi hasa sehemu za pembeni ya macho, shingo na maeneo kama hayo.

Namna ya kufanya

Chukua karoti, saga kwenye blenda kisha kamua ili kupata juisi yake. Tumia pamba kupaka katika maeneo yaliyoathirika, fanya hivyo mara kwa mara, itakusaidia kupunguza ama kuondoa kabisa tatizo hilo.

Maziwa

 

Maziwa yakiwa katika kibuyu na vilevile katika glasi. Picha/ Margaret Maina

Maziwa yana virutubisho vinavyochochea kunawiri kwa ngozi. Pia yana chembechembe za ‘Alfa-Hydroxide Acid’ ambazo zina uwezo mkubwa kuondoa seli zilizokufa mwilini. Hivyo vyote husaidia kwa kiasi kikubwa kuondoa tatizo la mikunjo katika ngozi. Unachotakiwa kufanya ni kuchukua maziwa kiasi na kisha kuyachovya pamba ndani yake halafu taratibu unapaka maeneo yaliyoathirika.

Mshubiri; yaani Aloe vera

Jani la Aloe vera. Picha/ Margaret Maina

Jeli ya Aloe vera ndiyo hasa inayotakiwa katika shughuli hii.

Chukua jani lake na kisha likate ili kupata utomvu wake.

Chukua utomvu au jeli hiyo kama wengine wanavyoita na kisha pakaa sehemu iliyoathirika.

Itapunguza ama kuondoa kabisa tatizo hilo.

SIHA NA LISHE: Njia mbalimbali za kupunguza uzani bila kujinyima chakula

Na MARGARET MAINA

mwmaina@ke.nationmedia.com

BAADA ya shamrashamra za Krismasi na Mwaka Mpya ni dhahiri kwamba wengi wamefurahia mapochopocho tofauti; na sasa baadhi wanajiuliza ni vipi wanavyoweza kupunguza uzani bila ya kufanya mazoezi na kujinyima vyakula.

Kuna njia rahisi kama unaweza kujizoesha kufanya basi unaweza kupunguza uzani lakini pia kuwa na afya kipindi chote.

Maji mengi

Washauri wengi wa mambo na masuala yanayohusu afya wanashauri kunywa maji lita zaidi ya mbili kwa siku kama mtu angependa kuwa na afya nzuri huku pia akilenga kupunguza uzani.

Unapoyaywa maji mara kwa mara unahisi umeshiba na hata ni hali inayoweza kukufanya kutotaka kula sana.

Chai ya kijani yaani ‘green tea’

Wachina wamekuwa wakizingatia kunywa chai ya kijani kwa miaka mingi.

Wanaiamini na kuithamini kwa sababu ina uwezo wa kusafisha mwili kutokana na sumu yoyote kwa kuwa inaaminika kuwa na anti-oxidant nyingi.

Zaidi ya hayo, kunywa kikombe cha chai ya kijani baada au wakati wa mlo husaidia kuondokana na tamaa ya kunywa vinywaji vingine visivyo na afya kama soda au mvinyo.

Kula chakula cha usiku kabla ya saa mbili usiku

Watu wengi huwa na mazoea ya kulala kuanzia saa tatu mpaka saa nne.

Ukila chakula baada ya saa mbili usiku inamaanisha chakula hakipati muda mzuri wa kumemenyeka kabla hujalala, unashauriwa kula chajio kuanzia saa kumi na mbili na nusu jioni mpaka saa mbili usiku hii hufanya chakula chao kimemenyeke vyema kabla ya kwenda kulala.

Chagua vyakula vya kuoka na supu zaidi kuliko vya kukaanga

Mafuta si mazuri mwilini, kwa kuwa mafuta huganda mwilini.

Kutumia vyombo vidogo

Unapaswa kutumia vyombo vidogo, iwe sahani, bakuli au kikombe. Hii ni kutaka kutokupakua vyakula vingi. Kuna msemo usemao “smaller bowls = smaller portion” lakini pia kama una vyombo vikubwa basi jitahidi kujikadiria chakula cha wastani na sio kutaka kujaza chakula kutokana na ukubwa wa chombo chako.

Matunda na mbogamboga

Kuzoea kula mbogamboga na matunda kunasaidia pia kufanya mwili upungue na uwe na afya nzuri. Unaweza kula mbogamboga kama main dish na kula matunda unapojisikia hamu ya kula kitu kingine baada ya kula chakula kikuu. Hii husaidia kutokula vitu visivyo na afya kama chokoleti na biskuti.

SIHA NA LISHE: Huzioka keki kwa kutumia unga asilia

Na PETER CHANGTOEK

UMBALI wa mita 800 kutoka mjini Chuka, nyuma ya shule ya Upili ya Wasichana ya Chuka, Nancy Kendi, 29, hushughulika na utengenezaji wa vyakula mbalimbali kwa kuutumia unga wa nafaka tofauti tofauti.

Yeye huvitengeneza vyakula kama vile keki kutoka kwa unga wa mtama, ndizi, wimbi, na mihogo.

Kendi amekuwa na uchu wa kuvitayarisha vyakula vya sampuli hiyo kwa kuutumia unga ambao wengi huupuuza.

Aghalabu, waja wengi huutumia unga wa ngano kuvitengeneza vyakula kama vile keki, lakini Bi Kendi ameamua kuutumia unga asilia.

Kendi, ambaye ana shahada katika masuala ya usimamizi wa biashara, anasema kuwa unga huo una virutubisho ambavyo ni bora kwa watu, hususan wale ambao ni wakongwe na watoto. Hata hivyo, anasikitika kuwa watu wengi mno hukosa kuutumia unga uo huo, kwa kupuuza tu.

“Ili kutoa fursa kwa watu kula vyakula vyenye virutubisho kwa wingi, katika maeneo yanayokabiliwa na ukame kama Tharaka Nithi, ilibidi nitumie njia za kuvutia, ili kuwafanya wakazi kula hivyo virutubisho vilivyomo kwa vyakula ambavyo vinapatikana kwa urahisi, lakini hupuuzwa sana,’’ anasema Kendi.

Bi Kendi alianza kupika kwa kuutumia unga ambao ni nadra kupatikana, mnamo mwaka 2016, ili kujiepusha na mbinu za ‘kuchosha’ za kupika mathalani; kuchemsha, kupondaponda, na kuchoma.

Mjasiriamali huyo, huzitengeneza chapati za ndizi, keki za ndizi, kaukau za ndizi (banana crisps), keki za bitiruti (beetroot cakes), miongoni mwa vyakula vinginevyo.

Alianza kwa kuvipika vyakula hivyo ili viliwe na aila yake, kisha baadaye akaanza kuviuza kwa wateja wake.

Kendi huununua unga wa nafaka mbalimbali kutoka kwa vikundi tofauti tofauti vilivyosajiliwa rasmi. Baada ya kuununua unga huo, yeye huuchanganya vyema, kabla hajaanza kuutumia.

Anadokeza kwamba watu wengi mno hawana ufahamu kuwa unga asilia unaweza kuboresha afya zao.

Alijifunza jinsi ya kuoka kupitia kwa mikutano iliyokuwa ikiandaliwa na idara ya kilimo ya kaunti hiyo.

Pia, alihudhuria warsha zilizoandaliwa na Shirika la Kilimo na Chakula (FAO), mwezi Februari, zilizokuwa zimeandaliwa katika shamba la Kaguru Farm, katika kaunti ya Meru.

Aidha, Kendi amewahi kupata fursa ya kuonyesha bidhaa zake kwa hadhira, katika mokongamano mengi; kama vile kongamano la ugatuzi lililoandaliwa katika Kaunti ya Kirinyaga na katika lile lililokuwa limeandaliwa mjini Njoro, Kaunti ya Nakuru, mnamo Oktoba 16, 2018, wakati wa kusherehekea siku ya chakula duniani.

Fauka ya hayo, katika jitihada za kuboresha ujuzi wake wa uokaji, Kendi aliamua kujisajili ili awe akipata mafunzo ya ziada kwa kozi ya uokaji mitandaoni.

Anaongeza kuwa chakula na virutubisho husaidia pakubwa kuimarisha afya ya binadamu.

“Aina hizi nyingi za unga zina manufaa mengi. Vyakula hivi humeng’enywa kwa urahisi. Unga huo hupatikana kwa urahisi na si ghali,’’ anafichua.

Wimbi, kwa mfano, huwa na manufaa mengi. Huwa na protini na aina fulani za madini. Pia, huwa na vitamini.

Mitama, nayo, husaidia kurahisisha shughuli ya mmeng’enyo wa chakula tumboni. Huondoa kuvimbiwa tumboni baada ya kukila chakula.

“Husaidia kupunguza athari za maradhi ya kisukari na husaidia kuimarisha afya ya mifupa kwa sababu ina kalisiamu (Calcium). Mitama husaidia kusambazwa kwa madini ya shaba, zinki, chuma, ‘magnesium’, kalisiamu na madini mengine kwa mwili,’’ anasema.

Kwa mujibu wa Kendi, mihogo ina vitamini, madini, na huwa na vitamini C.

Bw Benard Kinoti, mtaalamu wa lishe, ambaye pia ni afisa wa kilimo nyanjani mjini Meru, anasema kuwa unga asilia una manufaa yasiyohesabika.

Anafichua kuwa unga uo huo hauna kuvu ambayo ni sumu, na ni bora kuliko aina yoyote ya unga wa ngano.

 

SIHA, LISHE NA ULIMBWENDE: Manufaa ya ukwaju katika mwili wa binadamu

Na MARGARET MAINA

mwmaina@ke.nationmedia.com

UKWAJU ni tunda la mkwaju ambalo hupatikana katika maeneo ya kitropiki.

Kwa Kiingereza hujulikana kama tamarind na ambapo jina la kisayansi la mkwaju ni Tamarindus indica.

Katika baadhi ya maeneo, ukwaju hutumiwa kama kiungo katika mboga.

Ukwaju una madini ambayo ni muhimu sana kwa afya zetu. Una calcium, vitamini C, copper, phosphorus, madini ya chuma, na magnisium.

Namna ya kuutumia ukwaju

Tengeneza juisi nzuri ya ukwaju. Anza kuitumia kama kiungo katika chakula. Unaweza pia kuyatafuna majani ya mkwaju yenye ladha ya chumvichumvi au kuyakausha majani hayo kivulini na kuweka katika uji, au supu au juisi ya matunda.

Zifuatazo ni baadhi ya faida zitokanazo na matumizi ya ukwaju

Ukwaju husaidia kuongeza uwezo wa macho kuona. Matumizi ya ukwaju, ama kwa kula au kutumia kama juisi huondoa matatizo ya macho na kukufanya uwe na macho yenye afya.

Tunda hili ni muhimu na husaidia wenye ugonjwa wa kisukari kwa sababu ukwaju una viambata muhimu kama polyphenols na flavonoids ambavyo ni madhubuti katika kurekebisha au kusawazisha kiwango cha sukari mwilini na kupunguza vitambi.

Husaidia kwa wenye shinikizo la damu. Hivyo ni muhimu kunywa juisi ya ukwaju mara kwa mara.

Ifahamike kwamba ukwaju hupunguza kiwango kikubwa cha lehemu (cholesterol) mwilini.

Ukwaju una faida kwani pia hutoa mchango muhimu katika kusafisha damu.

Huondoa tatizo la nywele kukatika, na kuzipa mng’aro halisi. Anayetumia tunda hili kwa ajili ya kutunza nywele anafaa kuchemsha ukwaju, kisha kuanza kuyatumia maji yake ambapo anahitajika kuyachanganya na vijiko viwili vya bizari kabla ya kutumia kusafisha nywele kwa njia iliyo taratibu. Mtumiaji akishafanya hivyo anashauriwa kuziache nywele kwa muda wa nusu saa na azioshe kwa maji fufutende.

Ukwaju huboresha mfumo wa mmeng ‘enyo na kuondoa gesi. Anayetumia kupata faida hii anahitaji juisi ya ukwaju.

Manufaa ya mwisho katika makala hii ni kwamba tunda hili husaidia kupunguza uzani na pia kuboresha ngozi ya mtumiaji.

SIHA NA LISHE: Mazoezi yanaenda sambamba na mlo

Na MARGARET MAINA

mwmaina@ke.nationmedia.com

NI muhimu kufahamu jinsi vyakula vinavyoweza ama kuimarisha au kuharibu matokeo ya mazoezi.

Unapotaka kuwa na afya njema, unastahili kufanya mazoezi na ule vizuri.

Huwezi kuafikia malengo ya kuwa na afya bora bila kuzingatia mazoezi na lishe bora kwa wakati mmoja. Maana yake ni kwamba, hata kama utafanya mazoezi mara kwa mara, lakini lishe yako ikawa mbovu, basi usitegemee kupata mafanikio makubwa ya malengo yako.

Watu wengi hufanya mazoezi, lakini huishia kulalamika kutokuafikia malengo waliyojipangia.

Hapa zipo mada kadha za kuelekeza mwenye malengo ya kuwa na afya njema. Mada zimezingatia yale yasiyofaa kisha uchanganuzi ukabainisha kinachostahili kufanyika.

Kula chakula kingi mara baada ya mazoezi

Kwa kawaida unapofanya mazoezi mwili hutumia nguvu nyingi. Hii ni mojawapo ya sababu zinazokufanya uhisi njaa na hamu ya kula mara baada ya kufanya mazoezi. Jizoeshe tabia ya kula mlo mdogo badala ya kula chakula kingi kwa sababu hurudisha mwilini nishati-lishe (calories) ulizozitumia wakati wa mazoezi, hivyo ‘kufuta’ faida ulizokuwa umezipata kwa kufanya mazoezi.

Kula chakula kisichofaa baada ya mazoezi

Nguvu au nishati-lishe inayokuwa imetumiwa wakati wa mazoezi hukufanya uwe na hamu ya vyakula vyenye sukari, mafuta na wanga.

Hii inatokana na mabadiliko ya vichocheo au homoni (hormones) zinazoendana na utumiaji wa nishati-lishe mwilini wakati wa mazoezi. Hii ndiyo sababu ya watu wengi kuwa na hamu na vyakula vya aina hii. Lakini epuka vitu kama soda, juisi zenye sukari nyingi na baadala yake kula mlo wenye sukari ya asili, kama vile juisi ya matunda isiyoongezwa sukari. Pia kula mlo wenye kiasi kikubwa cha protini ili kuusaidia mwili kurudi katika hali yake.

Kula chakula kingi zaidi ya kiasi cha mazoezi unayofanya

Watu wengi hudhani kwamba, kwa kuwa wanafanya mazoezi hawana haja ya kujali kiasi na aina ya chakula wanachokula. Ikumbukwe kwamba kinachotakiwa ni uwiano kati ya nishati-lishe inayoingia na ile inayotoka mwilini.

Nishati-lishe huingia mwilini kwa njia ya chakula, na hutumika au kutoka mwilini kwa kufanya mazoezi. Kutokana na malengo mbalimbali ni muhimu kufahamu jinsi ya kufikia uwiano utakaokufanya ufaidike.

Kwa mfano, endapo lengo lako ni kupungua uzani, ni sharti utumie nishati-lishe nyingi zaidi ya zile unazoingiza mwilini.

Maana yake ni kwamba, kiasi na kiwango cha mazoezi kizidi kiasi cha chakula unachokula. Ukikosea uwiano huu huwezi kufaidika na mazoezi.

Kutumia kiasi kidogo cha protini na wanga kwa wingi

Mafuta hujengeka na kuongezeka mwilini kutokana na kiasi kikubwa cha nishati-lishe kinachoingia mwilini kama chakula.

Vyakula vya wanga na vile vya mafuta hutoa nishati-lishe nyingi zaidi ya vyakula vya protini. Ifahamike pia kwamba uyeyushaji wa vyakula vya protini hutumia nishati-lishe nyingi hivyo kusaidia kutumia nishati-lishe ya ziada mwilini.

Kwa maana hiyo, pamoja na kufanya mazoezi, vyakula vyenye protini nyingi na wanga kidogo husaidia kuzuia ongezeko la mafuta mwilini.

Kunywa pombe kupita kiasi

Pombe ina nishati-lishe nyingi. Kwa maana hiyo, unywaji pombe kupita kiwango kilichoshauriwa huchangia katika kuongeza mafuta mwilini. Hata kama unafanya mazoezi kwa kiwango kikubwa, kunywa pombe kupindukia kutarudisha nyuma juhudi zako.

Kula chakula kingi chenye wanga usiku

Wengi wetu hupumzika usiku. Kwa maana hiyo, hatuhitaji nguvu nyingi mwilini. Kula kiasi kikubwa cha wanga hutupa nguvu ya ziada, ambayo hatuitumii.

Nguvu hii ya ziada hutunzwa mwilini kama mafuta. Kwa maana hiyo, hata kama utakuwa ulichoma mafuta ya kutosha wakati wa mazoezi, kula chakula kingi cha aina ya wanga wakati wa usiku hupoteza juhudi zako za mazoezi.

SIHA NA LISHE: Vyakula vinavyoimarisha uwezo wa kuona

Na MARGARET MAINA

mwmaina@ke.nationmedia.com

KULA vizuri kuna manufaa mengi kwa ajili ya miili yetu.

Kando na karoti, kuna virutubisho mbalimbali vinavyohitajika kwenye macho.

Samaki

Samaki ni bora kwa afya ya macho kwani ni chakula ambacho kina mafuta ya Omega-3 ambayo ni muhimu kwa ajili ya kuzuia macho angavu (kunyauka kwa macho), na hali ya kudhoofika kwa misuli ya macho. Kama umeshindwa kula vyakula hivi vya baharini unaweza kula matunda kama vile matunda damu ili kupata Omega-3.

Mboga za majani

Mboga muhimu kwa afya. Picha/ Margaret Maina

Watu wengi hufikiri kuwa kula mboga za majani ni dalili za umaskini; lakini ukweli ni kuwa mboga za majani zina manufaa makubwa kwenye miili yetu.

Mboga za majani zina kemikali ya luteini na zeaxanthini ambazo ni muhimu katika kulinda na kujenga uwezo wa macho kuona vizuri.

Mayai

Mayai yana manufaa kwa ajili ya afya ya macho na miili yetu kwani yamejaa vitamini. Vitamini A inayopatikana kwenye mayai hulinda macho dhidi ya kutokuona usiku pamoja na kukauka kwa macho (macho angavu).

Matunda jamii ya mchungwa na zabibu

Matunda kama vile malimau, machungwa na zabibu yamesheheni vitamini C. Hivyo, yatawezesha macho yako kujikinga na magonjwa kama vile kudhoofika kwa misuli ya macho.

 Karanga na jamii zake

Vyakula hivi vimejaa mafuta aina ya Omega-3 na vitamini E ambavyo kwa pamoja ni muhimu kwa ajili ya afya ya macho.

Matunda ya rangirangi

Chakula kama karoti, nyanya, pilipili mboga, na mahindi ni vyanzo bora vya vitamini A na C.

Inaaminika kuwa kemikali ya carotenoids inayoyapa matunda haya rangi zake ni muhimu kwa afya ya macho.

Vyakula vya jamii ya kunde

Vyakula vya jamii ya kunde vina kemikali kama vile Bioflavonoid na Zinc ambavo ni muhimu kwa ajili ya ulinzi wa retina na kuzuia kudhoofu kwa misuli ya jicho.

Nyama ya ng’ombe

Nyama imejaa madini ya zinc ambayo huuwezesha mwili kufyonza vitamini A ambayo ni muhimu kwa macho pia.

Ikumbukwe kuwa vitamini A huuwezesha mwili kukabiliana na matatizo yatokanayo na umri au uzee.

Nyama ya ng’ombe kabla ya kupikwa. Picha/ Margaret Maina

Kwa hakika maradhi mengi humpata mwanadamu kutokana na kuharibu au kuacha mfumo wa ulaji wa asili.

Ni kweli kuwa matunda na mboga ni ya manufaa makubwa kwa ajili ya macho yetu pamoja na mwili mzima kwa ujumla.

Jitahidi kufanya angalau nusu ya mlo wako uwe ni matunda na mboga. Usisahau pia kumwona daktari mara kwa mara ili kupima afya ya macho yako pamoja na kupata ushauri.

SIHA NA LISHE: Faida ya kula matango

Na MARGARET MAINA

mwmaina@ke.nationmedia.com

MWILI wa binadamu unahitaji kuwa na virutubisho vya kutosha.

Virutubisho hivi tunavipata katika vyakula, matunda na hata kupitia katika vinywaji mbalimbali.

Miongoni mwa faida tunazozipata kwa kula matango ni kama zifuatazo:

Kuboresha kiwango cha maji ambayo huhitajika mwilini

Hii ni kutokana na matango kuwa na kiwango kikubwa cha maji. Maji haya husaidia kuondoa sumu mwilini; sumu ambazo tunazipata kupitia vyakula, dawa na hata vinywaji.

Kupunguza uzani wa mwili

Kutokana na matango kuwa na asili ya nyuzi nyuzi, humfanya mlaji ajisikie kushiba bila ya kuongeza vitu mwilini ambavyo husababisha mtu aongezeke uzani.

Hupunguza uchovu

Hii ni kutokana na kuwa na vitamini B na maji mengi; vitu ambavyo vitamfanya mlaji asubuhi asiamke huku akiwa na uchovu.

Husaidia katika mmeng’enyo wa chakula

Matatizo ya tumbo kama vile kuvimba, tumbo kujaa gesi, vidonda vya tumbo na mengineyo hupungua kutokana na ulaji wa matango, husaidia kuondoa sumu tumboni na kurahisisha ufyonzwaji wa protini mwilini .

Husaidia kuondoa msongo wa mawazo

Matango yana kiwango kikubwa cha vitamini B ambayo husaidia kuboresha utendaji kazi wa mishipa mbalimbali ya fahamu mwilini na hivyo kuondoa hatari ya mtu kukumbwa na msongo wa mawazo unaosababishwa na maisha ya kila siku.

Husaidia kuondoa harufu mbaya kinywani

Kwa kukiweka kipande cha tango mdomoni kwa dakika kadhaa, huua bakteria mbalimbali wasababishao magonjwa mbalimbali ya kinywa na harufu mbaya mdomoni.

Tango lina virutubisho vingi na madini muhimu sana katika mwili wa binadamu. tango ni chanzo kizuri cha Kalshiamu, Chuma, Phosphorus Potassium, Zinc, Vitamini B, C na E.

Tango linaaminika kupunguza kiwango cha mafuta mabaya mwilini, huimarisha misuli ya mwili wa ngozi. Watu wengi hutumia tango kwa njia mbalimbali kutunza ngozi zao na kupendezesha sura zao.

Juisi ya tango. Picha/ Margaret Maina

 

AKILIMALI: Mtaalamu wa kilimo na balozi wa siha njema

Na SAMMY WAWERU

CHAKULA kinachoenziwa na kuliwa kwa wingi ni kilichosindikwa.

Baadhi ya vyakula vya kusindikiwa, aghalabu hutiwa kemikali ili kuvihifadhi kwa muda mrefu.

Wataalamu wa masuala ya afya huonya dhidi ya kuvila sana kwa sababu ya athari zinazoibuka siku za usoni, uuguaji wa magonjwa kama Jongo, Kisukari, Shinikizo la damu na Saratani yakiwa miongoni mwazo.

Aidha, wataalamu wa afya wanahoji yanaweza yakadhibitiwa kwa kiwango kikubwa iwapo kila mmoja atazingatia lishe kamilifu. Isemwavyo; kinga ni bora kuliko tiba, ulaji wa matunda ainati, uzingatiaji wa chakula asilia na kile hai, ni baadhi tu ya unachohimizwa kutilia maanani mara kwa mara.

Mbali na kuwa mtaalamu wa kilimo, James Macharia ni balozi wa siha bora kupitia jitihada zake za zaraa ya kipekee.

Malalamishi ya kila wakati watu kuugua ndwele zinazowahangaisha kupata matibabu kama vile Saratani, zilishinikiza mdau huyu kutafuta njia mbadala kuyaangazia.

Ukizuru kiunga chake cha Green Oasis Plants Centre kilichoko Kabati, kaunti ya Murang’a, pembezoni mwa lango utakaribishwa na mimea mbalimbali ya kusawazisha hewa chumbani almaarufu Indoor Air Cleaners, yenye maumbo sawa na maua.

Spider plant, Areca Palm, Peace plant, Mothers-in-law palm, Boston Fern na Rubber plant, ni baadhi tu ya mimea hii anayokuza Bw Macharia.

Mazingira ya makazi tunayoishi, aghalabu kiambaza hupakwa rangi zilizochanganywa na bidhaa za petroli, jokofu, vifaa vya plastiki vya kulia na kunywa, chupa za vinywaji, na mazulia, vyote kwa jumla vikiundwa kwa malighafi yasiyokosa kemikali.

“Nyingi ya bidhaa hizo inapozidiwa na kiwango cha joto huachilia gesi ya Carbon, Benzene na Formaldehyde. Kemikali hizo husababisha magonjwa kama ya Kansa, na mimea ya Indoor Air Cleaners imeumbwa na uwezo wa kuzivuta, na kuachilia hewa safi ya oksijeni,” afafanua mtaalamu huyu.

Shirika la usafiri wa Anga ya Juu Amerika (NASA)mwaka wa 1989 lilifanya jaribio la mimea 50 katika safari yake kwa Sayari mbalimbali, na kugundua inaweza kutumika kuzalisha oksijeni badala ya ile ya kujiundia.

Utafiti wake pia uliashiria kwamba mimea hiyo ni bora katika kusawazisha hewa ya nyumba.

Kiunga cha Bw Macharia na chenye ukubwa wa ekari moja na nusu kimesheheni miche ya matunda aina mbalimbali na miti. Ukila tunda kwa siku husemekana “humuweka daktari mbali nawe”, amekipamba kwa matufaha, mapapai, mapera, tree tomato (ya kuongeza damu mwilini), zabibu, Brazilian cherry, bukini, maembe, ndizi, macadamia, hayo yakiwa machache tu kuyaorodhesha.

Isitoshe, amepanda mimea asilia inayokabiliana na matatizo ya tumbo, kudhibiti usambaaji wa Saratani, ugonjwa wa shinikizo la damu na Kisukari, nayo ni; Lemon grass, Herbal Hibiscuss, Mulberry na Herbal Rosemary.

“Nina mashine maalumu ya kuisaga inapokomaa, unga wake hutengeneza sharubati kwa kuuchanganya na maji moto na asali,” aelezea.

Wataalamu wa afya hupendekeza viungo asilia vya mapishi vitumike, na mkulima huyu wa aina yake huvikuza na kuvizalisha. Wakati wa mahojiano alifichua aina saba ya mimea anayolima, na kuunda bidhaa za aina mbalimbali akiitambua kama ‘mints’.

“Kuna mints aina saba kila moja na matumizi yake. Tropical ni ya kuunda peremende, chokoleti (kando na kuunda chokoleti yenyewe, ni ya kutengeneza dawa za kupiga meno mswaki), pepper (mapishi), spear (kubadilisha rangi ya chakula) na corsican (minukato). Apple na orange, pia zinatengeneza dawa za kupiga meno mswaki,” alifafanua.

Kilimo chake kimeegemea mimea yenye ukwasi wa madini ya Calcium, Potassium, Vitamins na Magnesium. Macharia ambaye ni mzaliwa wa Nyeri, anasema mapenzi yake kwa kilimo ameyapalilia tangu akiwa mchanga. Akivuta mawazo yake nyuma, akiwa katika shule ya msingi alikuwa na kiunga kidogo alichopanda matunda na miti.

Wavyele wake walifurahishwa na juhudi zake na hata kumpiga jeki.

Alikuwa na bahati kama mtende kwani shule ya upili aliyojiunga nayo ilitilia maanani masomo ya zaraa, ambapo alishiriki miradi kadhaa ya kilimo.

La kutia moyo, baada ya kuhitimu kidato cha nne, ombi lake kujiunga na Chuo Kikuu cha Egerton, Nakuru liliitikiwa na akasomea Stashahada ya Kilimo-mseto, masuala ya mimea.

Elimu bora ya kilimo

Egerton ni miongoni mwa vyuo vikuu tajika nchini katika utoaji wa mafunzo bora ya kilimo, na kusomea humo kulimnoa na kumuimarisha katika ari yake.

Safari ya mbali huanza kwa hatua moja, mtaalamu huyu aling’oa nanga mwaka wa 2008 kwa kiunga kilichomgharimu mtaji wa Sh23,000 mtaani Kahawa Sukari, kaunti ya Nairobi. Aidha, kilikuwa pembezoni mwa Thika Super Highway, na mradi wa ujenzi wa barabara hii ulipoanza alilazimika kuondoka akahamia Ruiru, Kiambu mwaka wa 2009.

Changamoto kuu eneo hilo ilikuwa ukosefu wa maji, ikizingatiwa kuwa ufanisi katika kilimo unategemea kiungo hiki muhimu.

Mwaka wa 2010 alipata kiunga Murang’a, alichoko kwa sasa. Hata ingawa hakufichua mapato yake wakati wa mahojiano, alisema bei ya bidhaa zake ni kati ya Sh50-500. Ameajiri wafanyakazi sita, na mitandao ya kijamii kama vile; Facebook, Whats App, OLX na Instagram imemsaidia pakubwa kupata soko la mazao yake.

Ili kufanikisha kilimo cha aina hii, anasema mkulima chipukizi sharti awe na chanzo cha maji ya kutosha na ambayo ni safi.

“Ni muhimu kujua kiwango cha asidi (pH) cha udongo, unaopania kufanya kilimo. Wakulima wanapaswa kutibu udongo kwa kutumia lime, haswa kwa kuzingatia maelekezo ya mtaalamu. Wajaribu kadri wawezavyo kupunguza matumizi ya fataliaza ya kisasa, ili uhifadhi virutubisho,” ashauri mdau huyu, akihimiza haja ya kutumia mbolea hai.