Sofapaka wampa kigogo Elly Asieche utepe wa unahodha

Na CHRIS ADUNGO

KUONDOKA kwa beki na nahodha George Maelo kambini mwa Sofapaka kumechochea kikosi hicho kilichotawazwa mabingwa wa Ligi Kuu ya Kenya mnamo 2009 kumpokeza kiungo Elly Asieche utepe wa ukapteni.

Asieche ambaye ni miongoni mwa wachezaji ambao wamehudumu kambini mwa Sofapaka kwa kipindi kirefu zaidi, amekuwa msaidizi wa Maelo.

Wachezaji wengine wanne ambao wamekatiza rasmi uhusiano wao na Sofapaka ni Waganda Nicholas Sebwato na Brian Kajuba, Ronald Okoth ambaye amestaafu soka na kiungo wa zamani wa Gor Mahia na Tusker, Lulumba Okeyo.

Rais Elly Kalekwa amesema kwamba mapengo yaliyoachwa na Sebwato na Kajuba yatajazwa na wanasoka wawili wazawa wa Rwanda.

“Kuna mabeki matata kutoka ugenini wakaojiunga nasi bila ada yoyote. Tumeafikiana na mawakala wao, wao wenyewe na familia zao. Ilivyo, dalili zote zinaashiria kuwa watajiunga nasi kufikia mwisho wa wiki hii,” akasema Kalekwa.

“Asieche ndiye nahodha wetu mpya. Anajaza nafasi ya Maelo ambaye ameagana nasi kwa pamoja na wanasoka wengine wanne. Usimamizi kwa sasa unajishughulisha sokoni ili kujaza nafasi walizoziacha wazi,” akaongeza katika kauli iliyoungwa na meneja wa timu ya Sofapaka, Hillary Echesa.

Sofapaka wamethibitisha kwamba juhudi zao za kumsajili beki wa zamani wa Gor Mahia, Musa Mohammed zimegonga ukuta baada ya nyota huyo wa Harambee Stars anayewaniwa na Yanga SC nchini Tanzania, kutaka Sofapaka kuweka mezani Sh6 milioni kwa ajili ya saini yake.

Musa alikuwa pua na mdomo kuingia katika sajili rasmi ya Sofapaka mnamo Aprili 2018 baada ya kuagana na FK Tirana ya Albania. Mkataba wake na mabingwa mara 12 wa Ligi Kuu ya Zambia, Nkana FC ulitamatika Juni 2020.

Wakati uo huo, fowadi veterani wa Sofapaka, Kepha Aswani anasema analenga kustaafu soka baada ya miaka mitatu ijayo na kubwa zaidi katika matamanio yake ya sasa ni kutwaa taji la mfungaji bora katika msimu wa 2020-21. Aswani alikuwa sehemu ya kikosi cha Mathare United kilichonyanya ubingwa wa Ligi Kuu ya humu nchini mnamo 2008.

Sofapaka wataka AFC Leopards waombe msamaha kwa kuwadunisha

Na CHRIS ADUNGO

KIKOSI cha Sofapaka kinachoshiriki Ligi Kuu ya Kenya (KPL) sasa kinataka mwenyekiti wa AFC Leopards, Dan Shikanda, awaombe msamaha.

Mnamo Jumamosi ya Mei 23, 2020, Shikanda aliyekuwa akihojiwa na mojawapo ya mashirika ya habari ya humu nchini, alisema kwamba hakuna soka yoyote humu nchini bila Gor Mahia na AFC Leopards.

Kauli hiyo haikupokelewa vyema na Rais wa Sofapaka, Elly Kalekwa.

Katika mahojiano hayo, Shikanda alizidi kueleza kuwa alifahamu KCB kuwa benki wala si timu ya soka na kwamba aliwahi kusikia pia kuwepo kwa kikosi kilichojiita Sofapaka katika kipute cha KPL.

Katika taarifa kwenye mtandao rasmi wa kijamii wa Sofapaka, Kalekwa alishikilia kwamba kauli za Shikanda kuhusu vikosi vingine vya KPL, hususan Sofapaka, zilikosa kuzingatia heshima na akamtaka kuomba msamaha.

Kalekwa ambaye ni mzawa wa Congo, alisema Sofapaka wanastahiki heshima hasa ikizingatiwa ukubwa wa mafanikio yao katika soka ya bara Afrika na Ligi Kuu ya KPL walioanza kuinogesha mnamo 2009.

Aidha, alisisitiza kwamba vikosi vyote vya KPL vinastahili kuzungumziwa kwa hadhi hasa ikizingatiwa kwamba Leopards waliwahi kuteremshwa daraja kwenye kipute cha KPL mnamo 2008.

Mt Kenya, Vihiga washuka ngazi, Bandari namba 2

Na JOHN ASHIHUNDU

LIGI Kuu ya Kenya (KPL) inayodhaminiwa na kampuni ya kamari ya SportPesa ilimalizika jana katika viwanja mbalimbali, huku timu za Mount Kenya United na Vihiga United zilizomaliza katika nafasi mbili za mwisho zikishuka hadi daraja ya Supa Ligi.

Wakati timu hizo zikiteremshwa, Gor Mahia ambao waliibuka mabingwa wa ligi hiyo baada ya kutwaa ushindi zikisalia mechi tatu, hii ikiwa mara yao ya 18 kuibuka mabingwa, waliagana sare tasa ya mabao 2-2 na Mathare United.

Bandari walimaliza katika nafasi ya pili baada ya kuagana 2-2 na Nzoia Sugar jana katika mechi yao ya mwisho, wakifuatiwa na Sofapaka walioubuka na ushindi wa 2-0 dhidi ya Kakamega Homeboyz katika mechi iliyochezewa Kenyatta Stadium mjini Machakos.

Ulinzi Stars walijipa ushindi wa bwerere uwanjani Afraha jana baada ya Mount Kenya United kufika ugani humo wakiwa wamechelewa.

Hii ni mara ya tatu kwa vijana hao kugawa pointi za bwerere baada ya hapo awali kuzitunuku timu za Gor Mahia na Mathare United.

Mechi hiyo ilitakiwa kuanza saa nane lakini ikaahirishwa ili ianze saa tisa na dakika 45, lakini hata kufikia wakati huo walikuwa hawajafika uwanjani humo.

Hatimaye walifika huku wakiwa wamevalia nguo nyekundu ambazo pia zilikuwa zimevaliwa na wenyeji.

Mwamuzi wa mechi hiyo, Anthony Oweyo na wasaidizi wake Anne Njambo na Elizabeth Njoroge walisisitiza lazima wageni hao wabadilishe mavazi, lakini hawakufanya hivyo.

Tuzo ya mfungaji bora

Ulinzi walikuwa wameingojea mechi hiyo kwa hamu huku wakiitegemea kumwezesha mshambuliaji wao, Enosh Ochieng aliyefunga mabao 17 kufunga mabao ya kumwezesha kutwaa Kiatu cha Dhahabu.

Mshindi wa tuzo hiyo ni Allan Wanga wa Kakamega Homeboyz ambaye alifikisha mabao 18 kutokana na mechi 33. Nyota huyo wa zamani AFC Leopards alitawazwa mhsindi ugani Mbaraki SC licha ya kutofunga bao lolote kwenye mnechi ambayo walichapwa 2-0 na wenyeji, Bandari FC.

Posta Rangers waliomaliza katika nafasi ya 16 (tatu kutoka mkiani) baada ya kuchapwa mabao 2-1 na Tusker, watashiriki katika mechi ya mchujo wa kuwania nafasi ya kubakia ligini.

Bandari, Sofapaka ni toka nipite wakiwania namba 2

Na GEOFFREY ANENE

MABADILIKO sita yameshuhudiwa kwenye jedwali la Ligi Kuu ya Kenya (KPL) ambayo Gor Mahia inaongoza bila presha kutoka kwa mpinzani wa karibu Bandari baada ya mechi 31 kusakatwa, wikendi.

Mabingwa watetezi Gor wananusia taji lao la tatu mfululizo na 18 kwa jumla ya alama 69 baada ya kunyamazisha mahasimu wa tangu jadi AFC Leopards kwa mabao 3-1 Jumapili.

Bandari iliepushia washindi mara 13 Leopards aibu ya kufanyia Gor gwaride la heshima ilipokanyaga Zoo Kericho 3-0, na hivyo kusalia alama nane nyuma ya vijana wa Hassan Oktay.

Baada ya kumaliza mechi mbili bila ushindi, washindi wa mwaka 2009 Sofapaka wameachwa kwa alama nne na Bandari, ingawa wamesalia katika nafasi ya tatu.

Vilevile, Kakamega Homeboyz hawajasonga kutoka nafasi ya nne baada ya kujiongezea alama moja kutokana na sare tasa dhidi ya Posta Rangers.

Homeboyz na Sofapaka, ambazo zimevuna alama 52 na 57 mtawalia, ndizo zinazojivunia wachezaji wanaofukuzana vilivyo katika vita vya kutoa mfungaji bora.

Allan Wanga anaongoza ufungaji wa mabao baada ya kucheka na nyavu mara 18 naye Mganda Umaru Kasumba yuko goli moja nyuma baada ya kupachika bao lake la 17 Sofapaka ilipotoka 1-1 dhidi ya Nzoia Sugar.

Mabingwa wa mwaka 2006 SoNy Sugar wameruka juu nafasi moja na kutua katika nafasi ya tano baada ya kulima Mount Kenya United 3-1.

Wanasukari hawa wamezoa alama 52. Wamesukuma washindi wa mwaka 2008 Mathare United nafasi moja chini hadi nambari sita. Mathare ilikabwa 0-0 dhidi ya Western Stima ugenini.

Badiliko halikushuhudiwa katika nafasi ya saba pale mabingwa mara 11 Tusker waliposalia katika nafasi hiyo baada ya kulemea Vihiga United 2-1. Wanamvinyo hawa wana alama 49.

Wanabenki wa KCB ndio waliimarika zaidi katika raundi ya 31.

Ushindi wao wa mabao 3-2 dhidi ya Kariobangi Sharks uliwapaisha kutoka nafasi ya 11 hadi nambari nane. KCB imezoa alama 40.

Imezidia nambari tisa Ulinzi Stars kwa tofauti ya magoli. Wanajeshi wa Ulinzi walitoka Chemelil na alama moja baada ya kukaba Chemelil Sugar 0-0.
Leopards almaarufu kama Ingwe, ambayo imeambulia alama mbili katika mechi tano zilizopita, inafunga mduara wa 10-bora kwa alama 39. Ulinzi na Ingwe zilishuka nafasi moja kila mmoja.

Sharks chini nafasi moja

Vilevile, Sharks sasa iko chini nafasi moja hadi nambari 11 baada ya kupokea vichapo viwili mfululizo.

Nzoia, Stima, Rangers na Chemelil zimesalia katika nafasi ya 12, 13, 14 na 15 baada ya kupiga sare kila moja na kufikisha alama 37, 32, 31 na 30 mtawalia.

Zoo na Vihiga zilipata pigo katika juhudi zao za kujiondoa katika maeneo hatari ya kutemwa baada ya kupoteza mechi zao. Zoo ina alama 28.

Inashikilia nafasi ya 16, ambayo ni timu itakayokamliza katika nafasi hiyo itakayomenyana na nambari tatu kutoka Ligi ya Supa kuamua itakayoshiriki Ligi Kuu 2019-2020.

Vihiga ni ya 17 kwa alama 25. Mount Kenya ilitemwa baada ya mechi za raundi ya 31 kwa sababu alama nyingi inayoweza kukusanya ikishinda mechi tatu zilizosalia msimu huu ni 27. Ilipoteza mechi yake ya tano mfululizo ilipocharazwa na SoNy.

Kigonya aishangaa Sofapaka kumnyima barua licha ya kandarasi kukatizwa

Na CECIL ODONGO

ALIYEKUWA mnyakaji wa Sofapaka Mathias Kigonya ameulaumu uongozi wa Sofapaka kwa kukataa kumpa barua ya kuondoka, wiki moja baada ya kukatiza rasmi kandarasi yake na mabingwa hao wa KPL mwaka wa 2009.

Kigonya ambaye ni raia wa Uganda aliwakimbia Sofapaka kutokana na sababu za kibinafsi na sasa anasema hana jingine ila kutafuta ujira kwingine ingawa kikwazo kikuu anachokumbana nacho ni kukosa kukabidhiwa barua hiyo muhimu na waajiri wake wa zamani.

“Sina shida kurejea kusakatia klabu nyingine katika ligi ya KPL ila tatizo kuu kwangu ni Sofapaka kukataa kunipa barua ya kuondoka ndipo niweze kupata timu nyingine,” akasema nyani huyo aliyefungia Sofapaka mabao manne kupitia mikwaju ya penalti msimu uliotamatika wa 2017/18.

Hata hivyo taarifa zimeibuka kwamba kilichochangia Kigonya kuagana na ‘Batoto ba Mungu’ ni kukosa kuafikiana kuhusu kandarasi mpya.

Ingawa hivyo, kipa huyo amefichua kwamba anazingatia ofa alizowasilishiwa kutoka klabu mbalimbali ndani na nje ya nchi kabla ya kuamua na kutangaza timu mpya atakayodakia msimu ujao.

Sofapaka yabandua Tusker SportPesa Shield

Na Geoffrey Anene

SOFAPAKA imeingia nusu-fainali ya Soka ya SportPesa Shield baada ya kutoka nyuma bao moja na kuzamisha Tusker 2-1 uwanjani Kenyatta mjini Machakos, Jumapili.

Jackson Macharia alifungia Tusker ya kocha Robert Matano bao la ufunguzi dakika ya tano baada ya kumegewa pasi nzuri na Boniface Muchiri. Hata hivyo, uongozi huu haukudumu kwani Mganda Umar Kasumba alisawazishia mabingwa wa mwaka 2007, 2010 na 2014 Sofapaka dakika tatu baadaye. Ezekiel Okare alifunga bao lililobandua nje mabingwa mara nne Tusker katika dakika ya 75.

Sofapaka inaungana na mabingwa watetezi AFC Leopards, ambao wameshinda kombe hili la ngao mara nane, na Ulinzi Stars katika nusu-fainali. Leopards na Ulinzi zililemea Kenya Police na Riverplate kwa mabao 4-1 uwanjani Bukhungu mjini Kakamega mnamo Jumamosi.

Mshindi wa mashindano haya hufuzu kuwakilisha Kenya katika Kombe la Mashirikisho la Afrika. Leopards ilibanduliwa nje na Fosa Juniors ya Madagascar katika makala ya mwaka huu katika awamu ya kuingia raundi ya kwanza. Sofapaka na Ulinzi zilishiriki mashindano ya Afrika mara ya mwisho mwaka 2015 na 2017, mtawalia.

Ulinzi ilitolewa katika raundi ya kwanza na Smouha kutoka Misri kwa jumla ya mabao 4-3. Ilifuzu kukutana na Smouha baada ya kulemea Al-Hilal Benghazi ya Libya kwa njia ya penalti 5-4. Sofapaka ilicharazwa 4-2 na Platinum ya Zimbabwe katika mechi ya kuingia raundi ya kwanza.

Nilijua tungeinyorosha Ulinzi Stars, asema kocha Baraza

Na CHRIS ADUNGO

KOCHA wa Sofapaka, John Baraza amesema alikuwa na hakika kuwa timu yake ingeizaba Ulinzi Stas wikendi.

Mabao kutoka kwa Umaru Kasumba na Kepha Aswani yalifuta bao la Elvis Nandwa la kufuta machozi, huku mabingwa hao wa ligi 2009 wakiwafikia Ulinzi kwa pointi.

Kocha huyo anatumai ushindi huo utasaidia vijana wake kuandikisha matokeo bora zaidi katika meci zijazo, huku ubingwa bado ukiwa kiganjani.

“Motisha ilikuwa juu kabla ya mechi, wachezaji waliahidi wangefanya makubwa na hawakufeli. Tulijua tungewanyorosha na nina furaha tuliwazima. Wiki hiyo imekuwa nzuri kwetu, tulifanya mazoezi ya kutosha na nafurahi mbinu zetu zilileta matokeo mema.

“Kwa sasa tunaangazia mechi zijazo tukilenga kuzoa alama za juu zaidi,” aaksema Baraza.

Kufikia sasa, Batoto ba Mungu wako katika nafasi ya tatu kwa jedwali wakiwa na pointi 17.

Sofapaka yamtimua Waliaula baada ya Ssimbwa kujiuzulu

Na CHRIS ADUNGO

SIKU moja baada ya kocha mkuu Sam Ssimbwa kujiuzulu, Sofapaka Jumanne imempiga kalamu meneja wa timu hiyo Willis Waliaula.

Afisa wa klabu hiyo aliyesema na Goal.com alithibitisha taarifa hizo akisema: “Ndiyo, Waliaula si meneja wetu tena. Nafasi yake kwa sasa imetwaliwa na Hillary Echesa.”

“Ni uamuzi ambao ulifikiwa na usimamizi wa timu ili kuleta amani na maelewano kwa timu. Kumekuwa na  migogoro baina ya benchi la kiufundi na wachezaji.”

“John Baraza atasalia kuwa kocha wetu mkuu kwa sasa, lakini mipango ipo kumleta kocha mwenye uzoefu na tajriba katika soka.”

Batoto ba Mungu kwa sasa wako katika nafasi ya nne ligini wakiwa na pointi 16.

John Baraza sasa kuwaongoza ‘Batoto Ba Mungu’

Na CHRIS ADUNGO

MCHEZAJI wa zamani wa Harambee Stars John Baraza amepata nafasi ya pili kuongoza kikosi cha Sofapaka baaada ya kocha Sam Ssimbwa kujiuzulu. Taarifa kutoka kwa klabu hiyo imethinitiha haya.

Taarifa hiyo inasema kuwa Baraza, ambaye alipata ufanisi akiichezea ‘Batoto ba Mungu’, atakuwa kocha mkuu wa muda hadi pale klabu hiyo itapata kocha wa kudumu katikati ya msimu.

Baraza, ambaye alishinda ubingwa wa Ligi Kuu ya Kenya mnamo 2009, alichangia pakubwa timu hiyo kuponea 2016 wakati ilipitia wakati mgumu ligini na kupewa nafasi ya naibu kocha mkuu baada ya SSimbwa kuwasili Januari 2017 kutoka Uganda.

“Sofapaka ingependa kutangaza kuwa kocha kutoka Uganda Sam Ssimbwa alijiuzulu akilalamikia matokeo duni ya timu na kulemewa kuiletea ushindi.

“Nafasi ya Ssimbwa itachukuliwa na John Baraza kwa muda, hadi katikati ya msimu ambapo uongozi wa klabu utatathmini matokeo ya timu na kikosi cha ufundi. Baraza amekuwa naibu kocha wa timu hii,” ataarifa hiyo ilisema.

 

 

Ssimbwa ajiuzulu akilalamikia wachezaji kumgomea

Na CHRIS ADUNGO

MKUFUNZI wa Batoto Ba Mungu, Sam Ssimbwa amejiuzulu nafasi ya kocha mkuu Jumapili.

Kocha huyo mzaliwa wa Uganda aliamua kugura kazi hiyo kufuatia kichapo cha 2-1 mikononi mwa Thika United ambayo imedhalilishwa mno katika Ligi Kuu ya Kenya.

Mwenyekiti wa Sofapaka Elly Kalekwa amethibitisha habari hizo, akisema Ssimbwa aliomba kujiondoa akilalamikia tabia ya wachezaji kutojituma kwa mechi ili wamuaibishe.

 

“Amejiuzulu. Amewapa wachezaji buriani ya kuonana na tunaheshimu hilo. Anadai kuwa wachezaji wanamgomea, hawataki kusikiza anachosema,” akasema.

“Hakuna haja kwake kuandika barua ya kujiuzulu, tumekubali uamuzi wake.”

“Hakuna uhusiano mbaya kati yetu naye, jinsi amesema mwenyewe, atasalia kuwa mwandani na kututakia mema kwa mechi,|” akaongeza.

 

Kufikia sasa, Sofapaka imeshinda mechi tano, ikapata sare moja na kulimwa mechi tatu.

Zoo yajifufua, Sofapaka yazikwa

Na CHRIS ADUNGO

TIMU ya Zoo Kericho Jumapili ilipata sababu ya kutabasamu baada ya kumaliza msururu wa kupoteza mechi ilipoizima Posta Rangers 1-0 katika uwanja wa Kericho.

Bao la pekee la mechi hiyo lilifungwa na Mike Madoya na kufuta matumaini ya vijana wa Sammy ‘Pamzo’ Omollo  kupata ushindi.

Sofapaka nao walipewa kichapo tena na Thika United. Kepha Aswani alipata bao la kwanza na kuwapa Batoto ba Mungu imani ya kupata pointi tatu lakini Mata Masakidi akasawazisha dakika chache baadaye.

Adem Edmond alihakikisha vijana wa Nicholas Muyoti wamepata ushindi wao wa kwanza msimu huu na kuwaacha vijana wa Sam Ssimbwa wakitafakari kuhsu mechi inayofuata.

Katika uwanja wa Bukhungu, Nakumatt iliendelea kurekodi matokeo duni baada ya kulimwa 2-0 na Kakamega Homeboyz.