Ni idadi ndogo tu ya wanaojitokeza Thika kujisajili wawe wapigakura

Na LAWRENCE ONGARO

HUKU uandikishaji wa wapigakura ukiendelea tangu uanze Jumatatu wiki hii, ni watu wachache wanaojitokeza katika kituo cha Huduma Centre kilichoko mjini Thika.

Baadhi ya maafisa wa kusajili wapigaji kura wakionekana kuketi bure bila cha kufanya, huku wakiwa na matumaini kwamba hatimaye watu watajitokeza kujisajili.

Kulingana na afisa msimamizi wa IEBC mjini Thika Bw Jeremiah Gatheci, ni kwamba mnamo Jumatano baadhi ya watu waliojitokeza hawakubeba vitambulisho vyao na pia walipoelezwa kuvirudia makwao, hawakuonekana tena.

“Bado wale wanaotarajia kujisajili ni wachache na ni vyema kuwahamasisha ili waelezwe umuhimu wa shughuli hii,” alisema Bw Gatheci.

Alisema licha ya kwamba IEBC inawahimiza watu kujitokeza kwa wingi kujisajili ni vyema nao viongozi kuwarai wananchi kujitokeza kwa wingi.

Bw Nduati Njuguna ambaye ni mfanyabiashara na mkazi wa Thika, aliwashauri wakazi wa Thika wajitokeza kwa wingi kujisajili ili waweze kuwachagua viongozi wanaostahili.

“Hakuna haja ya kufurika kwenye vituo vya kujiandikisha dakika ya mwisho na wakati huu kuna muda mrefu wa kujiandikisha,” alisema Bw Njuguna.

Aliwahimiza vijana kujitokeza kwa wingi ili kujiandikisha ili kuleta mabadiliko wanayotaka maishani mwao.

Bi Mary Kirika aliyewania kiti cha Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Kiambu katika uchaguzi uliopita wa 2017, aliwahimiza vijana chipukizi kujiandikisha kwa wingi kwa huu mwezi mmoja waliopewa.

“Vijana ndio wana kura nyingi wakati huu tunapoelekea uchaguzini na kwa hivyo wasichukulie jambo hilo kwa mzaha,” alisema Bi Kirika.

Alisema wakifanya uamuzi mbaya, basi wataendelea kulalamika kila mara.

Aliwahimiza wanawake kuwarai watu kwenye familia zao wachukue kura kwa wingi ili kutumika kama silaha ya kupata viongozi wanaostahili wakati wa uchaguzi kupitia njia ya demokrasia.

Bi Gladys Chania ambaye ni mwanaharakati anayepinga matumizi ya dawa za kulevya na pombe haramu, aliwashauri vijana kutumia wingi wao kuchukua kura kwa wingi.

“Vijana wana nafasi nzuri ya kubadilisha mambo na kwa hivyo huu ndio wakati wao mzuri wa kujisajili kwa wingi,” alifafanua Bi Chania.

Alisema viongozi wana jukumu la kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi ili kujisajili.

“Ninatoa wito kwa vijana kutoka eneo hili la Thika na Kaunti ya Kiambu kwa ujumla wajitokeza kwa wingi hasa kwa muda huu mchache wa mwezi mmoja,” akashauri.

ODM yafanya uchaguzi wa wasimamizi tawi la Thika

Na LAWRENCE ONGARO

HUKUn siasa za kutafuta uungwaji mkono zikiendelea kuchacha, chama cha Orange Democratic Movement (ODM) kimefanya uchaguzi wa wanachama wake kutoka kaunti ndogo ya Thika.

Baadhi ya maafisa wakuu waliochaguliwa kuendesha shughuli za chama ni mwenyekiti Andrew Ng’ang’a Wanjukira. Naibu wake ni Richard Kioni. Katibu ni Michael Orao huku naibu wake akiwa ni Anne Nyokabi. Mwekahazina ni Alice Juma ambaye naibu wake ni Albert Mugeni Osoro.

Katibu mpya wa ODM tawi la Thika aliyechaguliwa Bw Michael Orao alipokuwa akihutubia wanachama wa chama hicho mjini Thika. Picha/ Lawrence Ongaro

Katibu mtendaji ni John Dames akisaidiwa na Virginia Wanjiru. Mwenyekiti wa wanawake ni Bi Dinah Owago. Mwakilishi wa kikundi maalum ni Ageyio Ali Huyo. Mwakilishi wa vijana ni Kennedy Odoyo.

Wanakamati wa chama hicho ni Mumbi Ng’aru, Elizabeth Wanjiru Matere, David Mureka, Charles Gikaria, Mwaura Mbugua, Kagiri Gicia, Francis Ngunjiri, James Maina, Eunice Maluki.

Kiongozi wa vijana ni Kennedy Odoyo na naibu wake ni Simon Kinyanjui. Mwekahazina ni Japheth Onditi. Maslahi ya walemavu yanalindwa na Fresher Akinyi.

Katibu wa wanawake ni Silpa Anyango naye mwekahazina ni Rose Muhonja.

Mwenyekiti wa chama katika tawi hilo Bw Wanjukira aliwahimiza wanachama wote wa chama cha ODM wawe mstari wa mbele kukipigia debe kote katika Kaunti ya Kiambu.

“Sisi kama wanachama ni lazima tumpigie debe kinara mkuu wa ODM Bw Raila Odinga. Wakati huu kila mmoja ana jukumu la kuwarai watu wa Mlima Kenya kumpigia kura Bw Odinga,” alifafanua Bw Wanjukira.

Alisema wakati kampeni zitang’oa nanga, kila mmoja miongni mwao atakuwa na jukumu la “kumtetea ‘Baba’ bila kurudi nyuma.”

Alisema kutakuwa na propaganda nyingi kuhusu ubaya wa Raila lakini hayo yasiwatishe hata kidogo kwani kiongozi huyo tayari amewafanyia Wakenya mambo mengi.

Katibu wake Bw Orao aliwashauri wanachama wa ODM walio eneo hilo la Mlima Kenya wawe na msimamo mmoja bila kuyumbayumba.

” Iwapo umeamua kutetea chama cha ODM tafadhali fanya hivyo na moyo mmoja bila kuwa na wasiwasi,” alisema katibu huyo.

Alisema hivi karibuni kinara wa ODM atazuru maeneo mengi ya Mlima Kenya na kwa hivyo akifika “ni sharti wanachama wake waonyeshe umaarufu wao katika eneo hili la Mlima Kenya.”

Wito viongozi wa Mlima Kenya wajipange wawe pamoja kisauti

Na LAWRENCE ONGARO

VIONGOZI wa Mlima Kenya wamehimizwa kuwa na mwelekeo mmoja wakati huu Kenya inapoelekea kuandaa uchaguzi wa mwaka wa 2022.

Mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina, alisema vyama vya kisiasa havistahili kuvunjwa ili kuingia kwa chama kingine.

“Kila chama kina mwelekeo wake kwa sababu ndicho kitakachotumika kutafuta vyeo vya uongozi,” alifafanua Bw Wainaina.

Alitoa wito kwa wananchi popote walipo wawe makini sana wanapowachagua viongozi.

“Ni vyema kuwachagua viongozi wenye maono ambao hawatajihusisha na siasa za migawanyiko. Cha muhimu ni kuwajali wananchi,” alisema mbunge huyo.

Alisema viongozi watakaochaguliwa wakati huu wanastahili kuweka nguvu zao kwa kubuni ajira kwa vijana.

Alisema hata ingawa viongozi wengi wanaangazia kuwania viti vya uongozi, ni sharti pia wawe na ajenda maalum ya namna ya kuwasaidia vijana.

Wananchi pia walihimizwa kutathmini tabia za kiongozi anayewania kiti chochote cha uongozi.

“Wananchi hawafai kuchagua viongozi kutokana na msisimko. Ni sharti maswala kadha ya kimaadili yazingatiwe,” alisema Bw Wainaina.

Aliongeza kuwa asilimia kubwa ya watu wasio na ajira ni vijana na kwa hivyo ajenda muhimu kwa kiongozi yeyote ni jinsi ya kubuni ajira kwa vijana.

Aliyasema hayo alipohutubia waandishi wa habari mjini Thika akiwaeleza maoni yake.

Bw Wainaina ambaye tayari ametangaza azma yake ya kuwania kiti cha ugavana Kaunti ya Kiambu, mwaka ujao wa 2022, alisema ajenda yake kuu itakuwa kubuni ajira kwa vijana.

“Kwanza ningependekeza vijana wajipange kwa vikundi ili waweze kupewa mikopo itakayowapa mwelekeo wa kujisimamia kibiashara. Hiyo ni njia moja ya kujiajiri wenyewe,” alifafanua mbunge huyo.

Alisema mpango huo utafanikiwa iwapo kutakuwa na ushirikiano mwema na wafanyikazi na kuwepo na mazingira mazuri ya kufanya kazi.

Wanafunzi 94 kutoka Thika kupata ufadhili masomoni

Na LAWRENCE ONGARO

WANAFUNZI kutoka familia maskini wapatao 94 katika kaunti ndogo ya Thika watanufaika na mpango wa serikali kuwasaidia kusoma katika shule za upili.

Waziri wa Elimu Prof George Magoha amezuru Thika mnamo Alhamisi na kushuhudia wanafunzi hao wakihojiwa na washika dau katika sekta tofauti.

Kila mwanafunzi na mzazi wake walihojiwa wakati tofauti ili kupata picha kamili ya familia yao, kabla ya kupata nafasi hiyo.

Waziri amewahimiza wadau wote walioshiriki katika uteuzi huo kuhakikisha kila mwanafunzi anatendewa haki bila kubaguliwa kwa njia yoyote ile.

Wanafunzi wapatao 171 walifika kujaribu kupata fursa kwenye uteuzi huo huku wakiwa wameandamana na wazazi wao.

Maswali mengi yaliangazia kuhusu familia, maeneo wanakotoka, uhusiano wa mzazi na mtoto, na kuhusu hali ya maisha kwa ujumla, pamoja na matarajio yao ya siku za usoni.

Kati ya wanafunzi hao wote waliohojiwa, ni 86 watakaonufaika na mpango wa Elimu Scholarship Program halafu wanane nao watapata nafasi ya usaidizi kupitia mpango wa Wings To Fly ambao ni udhamini kutoka benki ya Equity.

Prof Magoha ameeleza kuwa serikali imejitolea kuona ya kwamba wanafunzi wasio na uwezo wa karo wanapata nafasi ya kuendelea na masomo yao bila kutatizwa.

“Nitahakikisha ninatekeleza wajibu wangu katika wizara nikifuata maagizo ya Rais Uhuru Kenyatta. Pia nataka maafisa wakuu katika Wizara ya Elimu waniunge mkono,” alifafanua waziri huyo.

Amezipongeza; benki ya Equity, chini ya mkurugenzi wake James Mwangi, KCB, na benki ya Co-operative kwa kujitolea pia kuona ya kwamba zinatoa ufadhili kwa maswala ya elimu.

Waziri alitoa changamoto kwa wazazi na kuwashauri wasibague shule wanazopeleka wana wao kwa sababu shule zote zinafundisha masomo sawa kuambatana na mtaala uliotolewa na Wizara ya Elimu.

Nyumba za kisasa kujengwa Ruiru na Thika

Na LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa Ruiru watanufaika kwa ujenzi wa nyumba 500 eneo la Majengo karibu na soko kuu la eneo hilo.

Gavana wa Kiambu, Dkt James Nyoro, alieleza kuwa mji wa Ruiru unastahili kujengwa nyumba za kisasa kutokana na ongezeko la watu.

Alieleza kuwa nyumba za hapo awali zilijengwa zaidi ya miaka 50 iliyopita na kwa hivyo tayari zimepoteza umuhimu wake.

Wakati huo pia alieleza kuwa nyumba zote zilizojengwa na manispaa ya hapo awali ya Thika, zitafanyiwa ukarabati ili ziwe katika hali ya kisasa.

Nyumba hizo in zile za Depot, na Jamafosa zilizoko mjini Thika.

“Tunaelewa nyumba hizo zilijengwa zamani na kwa hivyo zimepoteza uzuri wake. Kwa hivyo ni vyema kujenga nyingine mpya za kisasa,” alisema Dkt Nyoro.

Alitoa wito kwa wawekezaji wajitokeze mjini Thika ili waweze kupata nafasi ya kujenga nyumba katika ardhi ya ekari 23.

Aliyasema hayo mjini Thika mnamo Alhamisi alipohudhuria hafla iliyojumuisha zaidi ya vyuo vya masomo 10 vilivyofika katika uwanja wa Mama Ngina ili kuonyesha baadhi ya kozi wanazosoma kwa mwongozo unaotangazwa kama (Smart Education Expo), iliyohudhuriwa na vyuo tofauti na wawakilishi wao.

Zaidi ya vyuo vya mafunzo 10 vilihudhuria ikiwemo Mount Kenya, Zetech, na Cascade miongoni mwa vingine.

Alisema wanafunzi wengi waliokamilisha elimu ya sekondari walitarajiwa kuhudhuria hafla hiyo ili wapate mwongozo wa kujichagulia masomo watakayochagua watakapojiunga na vyuo hivyo.

Alithibitisha kuwa kwa mwaka mmoja na nusu uliosalia serikali ya Kaunti ya Kiambu itafanya juhudi kuona ya kwamba mji wa Thika iumepiga hatua ili kuona ya kwamba Ajenda Nne muhimu za serikali ya kitaifa ambapo ujenzi wa nyumba mpya unahusika, zinatimizwa kabla ya mwaka mmoja na nusu ujao.

Uchunguzi waanzishwa kufuatia kifo cha mfanyabiashara Thika

Na MWANGI MUIRURI

IDARA ya polisi imeanzisha uchunguzi kufuatia kifo cha mfanyabiashara mmoja Thika, ambapo mwili wake ulipatikana akiwa nusu uchi kwenye gari lake katika egesho la magari, Kaunti Ndogo ya Gatanga.

Kulingana na ripoti iliyoandikishwa na mke wa mfanyabiashara huyo aliyetambulika kama Samuel Murigi katika kituo cha polisi cha Kaunti Ndogo ya Gatanga, aliondoka nyumbani kwake mtaa wa Landless, kiungani mwa mji wa Thika Machi 13, kuhudhuria hafla ya mchango wa rafikiye Kenol, kilomita 16 kutoka wanakoishi.

Hakurejea nyumbani, hatua ambayo ilishinikiza mke wake, Bi Catherine Nduta kuandikisha ripoti ya mtu aliyetoweka.

Alisema aliingiwa na wasiwasi baada ya kumpigia simu, mwanamke akaipokea na kueleza walikuwa pamoja katika eneo la burudani.

Aliambia maafisa wa polisi kwamba aliamua kuenda eneo hilo, Jogoo Kimakia Country Club, kuthibitisha ikiwa alikuwepo.

“Nilitembelea baa hiyo na gari lake aina ya Toyota double cabin pickup lenye nambari za usajili KAQ 553 P, lilikuwa katika egesho la magari,” ripoti ya Catherine inaelezea.

Kulingana naye, alipolikagua aliona mwili wa mume wake.

Mkuu wa Polisi Gatanga, Peter Muchemi aliambia Taifa Leo Dijitali kwamba uchunguzi utategua kitendawili cha maafa ya mfanyabiashara huyo.

“Hatuna uhakika alivyokumbana na mauti. Tunafuatilia nyayo na nyakati zake za mwisho. Tutatoa taarifa tukipata mwelekeo,” akasema afisa huyo.

Uchunguzi utabaini iwapo alikuwa Kenol kuhudhuria hafla ya mchango, alivyopatikana katika baa na alikuwa na kina nani.

Aidha, upasuaji wa maiti utafichua kilichosababisha kifo cha mfanyabiashara huyo.

“Tukipata mwelekeo tutajua iwapo ni kisa cha kujiondoa uhai, kuuawa au kifo cha kawaida,” Bw Muchemi akasema.

Afisa huyo alisema tayari faili ya kesi hiyo imefunguliwa katika Idara ya Uchunguzi wa Jinai (DCI). Mkuu wa DCI eneo hilo, Bw John Kanda, alisema matokeo ya kwanza yatatolewa Jumatano.

“Tumekagua eneo la mkasa na kukusanya sampuli zitakazofanyiwa uchunguzi. Kwa sasa, tunashughulikia mashahidi watakaoandikisha taarifa. Upasuaji wa mwili ukifanyika, tutajua hatua tutakayochukua,” Bw Kanda akasema.

Mfanyabiashara huyo alikuwa amewekeza katika nyumba za kukodi, uchukuzi na uuzaji wa bidhaa.

Mwenyekiti wa Jamii ya Wafanyabiashara Thika, Bw Alfred Wanyoike amemuomboleza mwendazake, akimtaja kama mfanyabiashara milionea aliyekuwa na bidii.

TAFSIRI: Sammy Waweru.

Mbunge wa Thika awatetea wakandarasi

Na LAWRENCE ONGARO

WANANCHI wamehimizwa kutoka maoni yao kuhusu mswada wa zabuni uliowasilishwa bungeni wa mwaka 2020 na ambao unapendekeza aliyepewa kazi na serikali alipwe haki yake bila kucheleweshwa.

Mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina akihutubia waandishi wa habari mjini Thika mnamo Jumanne, alisema tayari amewasilisha mswada bungeni wa kutaka serikali kuu na za kaunti zifanye haki kwa kuwalipa haki yao wakandarasi wanaopewa zabuni ya kufanya kazi yoyote ile.

“Tayari mswada huo uko katika awamu ya kwanza ambapo bado unaendelea kujadiliwa na wabunge,” alisema Bw Wainaina.

Mbunge huyo ambaye ndiye aliwasilisha mswada huo bungeni ili safu hiyo iujadili kikamilifu, alisema wananchi pia wana nafasi ya kutoa maoni yao kabla ya mswada huo kupelekwa katika awamu ya pili.

Kulingana na mbunge huyo, ni vyema kuwa na ushirikiano wa serikali na benki za humu nchini ambapo iwapo serikali itachelewa kulipa makontrakta fedha zao walizofanyia kazi, kwa muda wa siku 90, basi inabidi wahusika waende katika benki na kupokea fedha zao ili serikali ilipe benki baadaye deni hilo.

“Mpango huo kulingana na maoni yetu ni wa kuridhisha kwa sababu wale waliopewa zabuni na serikali watapata afueni ya kupokea haki yao bila kucheleweshwa jinsi hali ilivyo sasa,” alisema mbunge huyo.

Alisema sababu kuu ya kutetea hali hiyo ni kuwa, watu wengi waliopewa kazi na serikali huchelewa kupewa haki yao na hivyo kusababisha wengine kuuza mali zao baada ya kukosa namna.

“Jambo hilo limesababisha madalali kutwaa na kupiga mnada mali za watu na kuwaacha maskini. Kwa hivyo, tunajaribu kutetea kikundi hicho,” alisema Bw Wainaina.

Alisema mswada huo pia umeweka vikwazo kadha kwa wanaotaka kupewa zabuni kwa sababu kutakuwa na kutaka maelezo ya fedha wanazotarajia kulipwa kulingana na kazi ilivyofanywa, bila kuzidisha malipo zaidi.

“Tunajua mswada huo ukipitishwa rasmi bila shaka pande zote mbili zitakuwa na maelewano mwafaka kuhusu jinsi zabuni zitakavyotolewa,” alisema Bw Wainaina.

Mbunge ahimiza vijana watumie ubunifu kujiendeleza

Na LAWRENCE ONGARO

MBUNGE wa Thika Bw Patrick Wainaina alipendezwa na akaelezea kufurahishwa kwake na ubunifu uliofanywa na vijana watano waliounda kibanda maalum cha kunyunyuzia dawa ya kuzuia viini wakati huu dunia inakabiliana na janga la Covid-19.

Kibanda hicho ni cha kipekee ambacho watu wanapita ndani huku kikipuliza dawa hiyo kama mojawapo ya tahadhari ya kujikinga dhidi ya ugonjwa huo.

Vijana hao kutoka kanisa la PCEA Makongeni, Thika wameonyesha wazi kuwa ubunifu pia ni talanta ya kipekee.

Bw Wainaina alisema vijana hao wanastahili kupewa motisha zaidi ili waweze kujiendeleza katika hatua nyingine.

Ili kuonyesha ukarimu wake kwa vijana hao, mbunge huyo aliwapa Sh50,000 zitakazowasaidia kujiendeleza zaidi.

“Nimeridhishwa na ujuzi wa hali ya juu wa vijana hawa chipukizi,” alisema Bw Wainaina.

Kiongozi wa vijana waliounda kibanda hicho, Eric Karau Ng’ang’a alisema lengo lao kuu lilikuwa ni kwa minajili ya kupambana na Covid-19.

“Mimi nimesomea uhandisi wa umeme katika Chuo Kikuu cha Dedan Kimathi, na kwa hivyo niliona ni muhimu tushirikiane na vijana wenzangu ili kuunda kibanda hicho,” alisema Bw Ng’ang’a.

Alisema kuunda kibanda hicho kimewagharimu Sh138,000 na wakipewa ufadhili zaidi wanaweza kuunda vingine.

“Tutaendelea kuunda vingine tukipata ufadhili zaidi na kibanda hiki kinastahili kuwekwa pahala ambapo kuna watu wengi kama sokoni, makanisani, vituo vya magari na sehemu nyinginezo za umma,” alifafanua Bw Ng’ang’a.

Katibu anayehusika na nyumba na makazi aahidi serikali itaboresha Kiandutu

Na LAWRENCE ONGARO

MPANGO wa kazi kwa vijana mitaani utazidi kuboreshwa zaidi ili kukabiliana na hali ngumu ya kiuchumi iliyosababishwa na janga la Covid-19.

Katibu Mkuu katika Wizara ya Nyumba na Maendeleo ya Mijini Bw Charles Hinga alisema Jumatano serikali ina mpango mwafaka wa kuhakikisha vijana wa hapa nchini wanapata mbinu na shughuli ambazo zinaweza kuwapa ujira.

Alisema ameridhishwa na kazi inayoendelea katika kijiji cha Kiandutu mjini Thika kwa sababu vijana wameonyesha bidii ya kufanya kazi bila kubagua.

Hivi majuzi serikali iliajiri vijana 1,500 kutoka vijiji vya Kiang’ombe na Kiandutu ili wasaidie kufyeka mitaani na kuzibua mitaro ya majitaka katika mji wa Thika na vitongoji vyake.

Baadhi ya vijana wa kutoka kijiji cha Kiandutu wafyeka Mei 20, 2020, katika mradi wa ‘Kazi kwa Vijana Kupitia Covid-19’. Picha/ Lawrence Ongaro

Alisema serikali imebuni mpango maalum wa kuajiri vijana 26,114 kutoka katika kaunti nane za humu nchini.

Baadhi ya kaunti hizo ni Nairobi, Mombasa, Kilifi, Kwale, Nakuru, na Kiambu.

Alisema atafanya juhudi kuona ya kwamba kijiji cha Kiandutu kinafanyiwa mabadiliko kutoka miundomsingi hadi nyumba za kisasa.

“Kazi zote zitakazoendeshwa katika kijiji hicho zitafanywa na vijana wa huko na hiyo ni njia mojawapo ya kubuni kazi kwa vijana,” alisema Bw Hinga.

Alisema vijana watakuwa wakilipwa fedha zao kupitia M-Pesa.

Alisema mradi huo wa vijana umegharimu takribani Sh354 milioni na serikali itahakikisha kila kitu kinaendeshwa jinsi inavyostahili.

Gavana wa Kiambu Dkt James Nyoro, aliwashauri wakazi wa Thika wafuate sheria zote za afya ili “tuweze kukabiliana na janga la Covid-19.”

“Tayari hospitali ya Tigoni imegeuzwa kuwa Kiambu Covid-19 Centre Limuru. Nayo Thika Level 5 imetenga chumba chenye vitanda 20 kwa wagonjwa wa Covid-19,”alisema Dkt Nyoro.

Alibainisha kwamba Kaunti ya Kiambu imetenga Sh153 milioni zitakazotumika kwa minajili ya kuunda barabara za kuingia maeneo ya mashinani na umeme kusambazwa katika njia za kupitia mitaani.

Alisema wanapanga kuajiri wafanyakazi wapya ifikapo Julai mosi na hiyo itafanyika tu kwa watu wenye mienendo na tabia njema vijijini.

Kamishna wa Kiambu Bw Wilson Wanyanga alisema kazi kwa vijana inaendelea vyema na tayari maeneo yaliyonufaika na mradi huo ni Kiandutu, Kibarage, Kikuyu, Kiang’ombe, na Kiambu.

“Serikali itaendelea kuona ya kwamba vijana wanapata nafasi ya ajira ili kupunguza uhuni unaoshuhudiwa kila mara. Hata siku hizi uhalifu umepungua kwa kiwango kikubwa katika kaunti nzima ya Kambu,” alisema Bw Wanyanga.

Wakazi wa Kiandutu walipojitokeza kuzungumza walipongeza serikali kwa kazi njema ambayo imefanya ya kuwajali vijana lakini walitaja mambo kadha waliyotaka yarekebishwe.

Walisema wangetaka vyoo vijengwe kwa wingi, huku wakitaka pia njia za kuingia maeneo ya ndani zipanuliwe kwa wingi.

 

Naivas yawapa wahudumu wa afya wa Thika Level 5 vyakula na sabuni

Na LAWRENCE ONGARO

WAHUDUMU wa afya katika hospitali ya Thika Level 5 wapatao 100 walipokea vyakula kutoka kwa supamaketi ya Naivas tawi la Thika.

Daktari mkuu katika hospitali hiyo Jesse Ngugi, alithibitisha jambo hilo akisema hiyo ni njia moja ya kuwapa matumaini wahudumu hao kuwa pia wanatambulika “kule nje.”

“Kwa niaba ya hospitali, tunashukuru sana dukakuu la Naivas kwa kuonyesha ukarimu wao wa kuwajali wengine. Wameonyesha ya kwamba kutoa kwa umma ni jambo la kujitolea na ni kutoka moyoni,” alisema Dkt Ngugi.

Alisema wahudumu hao wa afya katika hospitali hiyo wamajitolea mhanga kukabiliana kwa vyovyote kuwahudumia wagonjwa bila kusita.

“Kwa wakati huu tumejiandaa vilivyo ambapo tumetenga wadi maalum ya kuwaweka wagonjwa endapo watapatikana na Covid-19. Wodi hiyo ina vitanda 10,” alisema Dkt Ngugi.

Alisema masharti yaliyowekwa na serikali ya kudumisha usafi na hasa kunawa mikono, yameleta mabadiliko makubwa kwa mwananchi wa kawaida.

“Siku hizi hata homa ya kawaida imepungua pamoja na maradhi ya kuharisha na homa ya matumbo,” alisema Dkt Ngugi.

Kudumisha usafi

Alitoa mwito kwa wananchi popote walipo wazidi kudumisha usafi kwa sababu “tutapunguza magonjwa mengi kwa  asilimia 70 hivi.”

Hafla hiyo iliyofanyika Jumatatu iliwaacha wahudumu hao na mshangao kwani hawakutarajia ukarimu kama huo ungeonekana siku hiyo.

Baadhi ya vyakula walivyopokea ni unga wa ugali, sharubati, sabuni ya kuoga na ya kufua nguo, mchele, na sukari, ambapo kila kifurushi kiligharimu Sh2,000.

Kampuni hiyo ya Naivas, kwa niaba ya wasimamizi wake, iliwapongeza wahudumu hao kwa kazi ngumu wanayofanya ya kutibu wagonjwa bila kusita.

Ilizidi kusema ya kwamba watazidi kushirikiana na hospitali ya Thika Level 5 na kila mara kukiwa na haja watawatembelea tena na mazuri.

Vijana 1,500 mjini Thika kunufaika na mpango wa serikali kuwapa ajira

Na LAWRENCE ONGARO

VIJANA mjini Thika watanufaika na mpango wa serikali wa kuwaajiri kazi mitaani ili wajikimu kimaisha.

Mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina alithibitisha Ijumaa kuwa vijana wapatao 1,500 kutoka mji wa Thika na vitongoji vyake wataajiriwa.

“Tunapongeza Rais Uhuru Kenyatta kwa kutoa amri ya kuajiriwa kwa vijana hao ambao watajipatia riziki yao hasa wakati kama huu tunapopitia hali ngumu ya homa ya corona,” alisema Bw Wainaina.

Alisema vijana hao watatambuliwa kutoka mitaa duni kama Kiandutu, Kiang’ombe, na mitaa mingine katika eneo la Thika.

Baadhi ya kazi watakazotekeleza ni kuzibua mitaro ya maji, kufyeka mitaani na kazi zingine muhimu watakazopewa.

Alisema hiyo itakuwa njia moja ya kuokoa vijana wengi wanaoendelea kuathirika kutokana na janga hilo la corona.

Aliyasema hayo mjini Thika ambapo alibainisha vijana hao watakuwa wakipokea Sh600 kila mmoja kila siku jioni baada ya kufanya kazi mchana.

Alipongeza juhudi za kampuni ya Broadway Group of Companies (Bakex Ltd), kwa kuchanga takribani Sh12.5 milioni na unga beli 10,000 ili kusaidia kaunti kadha hapa nchini.

“Juhudi iliyofanywa na kampuni hiyo ni muhimu na wahisani wengine wanastahili kufuata pia mwito huo,” alisema Bw Wainaina.

Alisema mwezi mmoja uliopita wakfu wa ‘Jungle’ Foundation ulifanya juhudi na kuchangisha Sh5 milioni za kuingia kwa hazina ya Covid-19.

Wakati huo pia alisambaza zaidi ya mitungi 200 ya kutumika kunawa na sanitaiza ili kupambana na corona.

Kuna gari la Ambulansi la ‘Jungle’ Foundation linalozunguka kila mtaa kutafuta wagonjwa wa corona.

Alitoa mwito kwa serikali kutoa maafisa wa KDF ili kuokoa watu wanne waliosombwa na maji ya mto Athi eneo la Ngoliba, Thika Mashariki mnamo Alhamisi.

“Kuna watu sita waliojaribu kuvuka mto Athi, lakini kutokana na maji hayo kwenda kasi watu wanne waliangamia huku wawili wakinusurika,” alisema Bw Wainaina.

Aliwahimiza wakazi wa Thika na maeneo mengine wafuate mwito wa serikali kudumisha usafi kila mara kwa kunawa mikono, kuvalia barakoa, na kujitenga na mtu kukaa umbali wa mita moja au zaidi baina yake na mwenzake.

“Iwapo kila mmoja atafuata maagizo hayo bila shaka janga hili tutalizuia kwa kiwango kikubwa na kwa hivyo tuweze kuwa wangwana na tujikinge na janga hilo,” alifafanua mbunge huyo.

KAFYU: Mji wa Thika wageuka mahame

Na LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa Thika walitii agizo la serikali kwa kurejea nyumbani mapema ili wasije wakakwaruzana vibaya na maafisa wa usalama.

Ilipofika saa tisa alasiri mnamo Ijumaa wafanyabiashara wengi walianza kufunga maduka yao huku wakijiandaa kuabiri matatu mapema ili kurejea nyumbani.

Ilipofika saa kumi na mbili na nusu za jioni mji wa Thika ulionekana mahame huku kila mwananchi akiwa amerejea nyumbani kuepukana na walinda usalama.

Naibu kamishna wa Thika Magharibi Bw Douglas Mutai amesema ameridhika na jinsi ambavyo wakazi wa Thika walitii serikali bila kulazimishwa.

“Maafisa wa usalama walipiga doria usiku wote hadi alfajiri ambapo barabara zote zilikuwa mahame huku kila dula la kibiashara likiwa limefungwa kabisa. Iwapo wananchi watafuata maagizo yote ya serikali bila shaka tutaweza kudhibiti Covid-19,” amesema Bw Mutai.

Amesema baadhi ya masoko makubwa katika Kaunti ya Kiambu yamefungwa ili kukabiliana maambukizi ya virusi vya corona.

Baadhi ya masoko yaliyofungwa wiki hii ni Madaraka, Makongeni, Jamhuri, Ruiru, na Githurai.

“Lengo letu kuu ni kuona ya kwamba wananchi wanafuata maagizo yote wanayopewa na serikali ili kuangamiza janga hili la Corona,” amesema Bw Mutai.

Amepogeza juhudi ambazo zimechukuliwa na wahisani kadha mjini Thika kwa kutoa mitungi ya kuhifadhi maji, dawa, na sabuni ya kutumika wakati wa kunawa mikono.

Amesema tayari amewafahamisha machifu wafanye juhudi kuona ya kwamba wanawahamasisha wananchi kila mara mashinani ili wanawe mikono.

Amesema kwa muda wa wiki mbili sasa mji wa Thika umegeuka mahame kwa sababu biashara chache ndizo zinaendelea huku ofisi nyingi za serikali zikiwa zimefungwa.

Biashara chache

Leo Jumamosi biashara chache mno ziliendelea mjini Thika kwani maduka mengi yamesalia kufungwa huku wafanyabiashara wengi wakiamua kubaki nyumbani.

Uchunguzi uliofanywa unaonyesha ya kwamba mikahawa mikubwa, na maduka kadhaa hayakufunguliwa kwani kafyu ya Ijumaa iliwapa watu wengi hofu huku wengine wakisafiri kutoka mbali ili kufungua biashara zao.

Baada ya kushuhudia yale yaliteyondeka Ijumaa usiku wengi wa wafanyabiashara wamesisitiza wataendelea kufunga maduka yao kuanzia mwendo wa saa kumi za jioni ili kupata muda wa kutosha kufika nyumbani na kujumuika na familia zao.

“Mimi leo nitafanya juhudi kuona ya kwamba ninarejea nyumbani mapema ili nitulie kwangu taratibu bila mabishano na yeyote,” amesema James Mungai ambaye ni muuzaji wa simu katika duka moja mjini Thika.

Hata matatu nyingi hazikuonekana mjini Thika kwani wamiliki wengi wameamua kwanza watulie wajionee mambo yalivyo kwani wanasema bado wanapata hasara kwa sababu ya kubeba abiria wachache.

Marehemu Mundia akumbukwa na watu wengi Thika

Na LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wengi wa Thika walihudhuria misa ya kumuenzi marehemu Douglas Kariuki Mundia aliyefariki wiki mbili zilizopita.

Bw Mundia ambaye alikuwa Meya wa mji wa Thika kwa miaka 20 alifariki Februari 13, 2020, na kuzikwa keshoye ambayo ilikuwa ni Februari 14, 2020, kulingana na matakwa yake.

Hata hivyo, familia ya marehemu ilipanga misa Ijumaa, Februari 28, 2020.

Spika wa bunge la kaunti ya Kiambu ambaye alihudhuria hafla hiyo katika uwanja wa michezo wa Thika Stadium, alimsifu marehemu Mundia kama mtu aliyejitolea kuinua mji wa Thika hadi pale ulipofikia sasa.

Ili kumkumbuka marehemu kwa njia ya heshima, Bw Ndichu alipendekeza uwanja wa michezo wa Thika ubadilishwe jina uitwe Mundia Stadium, Thika.

“Ninawahimiza madiwani wa Thika, walete mswada katika bunge la kaunti ili kupendekeza jambo hilo nami bila kuchelewa nitaidhinisha,” alisema Bw Ndichu.

Kuhusu mpango wa maridhiano wa BBI, alisema mjadala huo ni wa maana sana katika nchi hii lakini akawataka viongozi wachache wanaojaribu kuingiza siasa zao duni wakome.

“Sisi kama viongozi tunaunga mkono BBI tukijua ya kwamba Rais Uhuru Kenyatta ana nia njema na nchi yetu akitarajia kuacha Wakenya wakiwa kitu kimoja. Kwa hivyo, wale wenye nia mbaya na potovu wakome kuingiza siasa,” akasema.

Misa ilihudhuriwa na aliyekuwa wakati mmoja meya wa Nairobi kwa muda mrefu Bw Nathan Kahara, pamoja na waliokuwa madiwani wapatao wanane wa hapo awali katika mji wa Thika.

Bw Karuga Wandai ambaye ni wakili mashuhuri mjini Thika – na wakati mmoja alikuwa naibu wa meya wa Thika – alimtaja marehemu Mundia kama rafiki mkubwa na waliofanya kazi kwa uelewano.

“Marehemu alileta mabadiliko mengo katika mji wa Thika ambapo miradi mingi inayoonekana kwa sasa hapa mjini ni kutokana na juhudi zake,” alisema Bw Wandai.

Bw David Njihia aliyekuwa meya wa Thika alisema wakati wao, viongozi walifanya kazi bila kujali maslahi ya pesa bali walijitolea na nguvu zao zote.

“Tungetaka kuona mfano huo kwa wakati huu ili wananchi waweze kupata huduma kwa njia inayostahili. Hata hivyo, hayo yote yatafanikiwa tu iwapo kunakuwepo na ushirikiano,” alisema Bw Njihia.

Bw Nathan Kahara ambaye alikuwa meya wa Nairobi aliwahimiza madiwani kufanya kazi kama kitu kimoja ili kufanikisha maendeleo ya kaunti ya Kiambu.

Alishauri familia ya marehemu Mundia kuwa kitu kimoja kwa kushirikiana bila ubaguzi wowote.

“Nyinyi sasa ni kitu kimoja; msikubali kuletewa fitina na watu kutoka nje kwani ni lazima mfanye jinsi marehemu alivyotaka kuona mkiishi,” alisema Bw Kahara.

Wakazi wa Thika wapata maji kwa wingi

Na LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa Landless, Thika na maeneo ya karibu wamepata afueni baada ya kuletewa maji kwa wingi katika makazi yao.

Kikosi cha jeshi cha 12th Engineering Batalion, kwa mapatano na mbunge wa Thika Bw Patrick Wainaina kilifanikisha juhudi hiyo ya kupata maji.

Maji hayo yalichimbwa na kikosi hicho kwa siku mbili pekee kabla ya maji hayo kuonekana.

Bw Wainaina alisema alilazimika kuzungumza na kikosi cha jeshi kwa sababu wao wana uwezo wa kuchimba maji katika maeneo tofauti nchini.

“Ninapongeza juhudi za wanajeshi hao ambao walionyesha ujasiri wao kwa kufanya kazi hiyo mara moja bila kusita. Nimeridhika kwa sababu wakazi wa Thika sasa watanufaika na maji safi,” alisema Wainaina.

Alisema baadhi ya mitaa itakayonufaika pakubwa na maji hayo ni Landless, Gatundu, Muguga, na Ngoliba.

Alisema baada ya wakazi hao kupitia shida hiyo ya maji sasa atafanya juhudi kuona ya kwamba barabara za kisasa zinakarabatiwa ili waweze kuendesha biashara zao bila matata.

Afisa mkuu wa jeshi kikosi cha 12th Batalion Brigadier Geoffrey Radina, alisema maji hayo yatazidi kunywewa kwa muda mrefu na wakazi wa Thika.

“Sisi tayari tumefanya kazi yetu na sasa kilichobaki ni wananchi walinde mali yao ili wahalifu wasije wakaiba vifaa vilivyo hapo,” alisema Bw Radina.

Alisema kikosi chao cha Engineering Batalion kinafanya kazi kila sehemu nchini na kwa hivyo wameridhika na kazi hiyo waliyofanya.

Alieleza ya kwamba mradi huo umegharimu takribani Sh720 milioni, huku ukiwa ni wa kima cha urefu wa mita 130 ambapo ni fiti 400.

Mkurugenzi wa kampuni ya maji ya Thiwasco Water Company Ltd Bw Moses Kinya alisema kampuni hiyo itafanya juhudi kuona ya kwamba maji hayo yamefanyiwa ukaguzi maalum katika maabara ili kuhakikisha ni safi kwa binadamu.

Mbunge wa Thika Bw Patrick Wainaina ahutubu. Picha/ Lawrence Ongaro

Alisema watalazimika kuona ya kwamba wanaweka mabomba za kisasa za kusambaza maji katika mitaa tofauti.

“Tayari Benki ya Dunia imewasilisha Sh764 milioni kwa kampuni ya Thiwasco Water Company Ltd ili kujenga kituo cha kusambaza maji katika eneo la Mary Hill Mang’u,” alisema Bw Kinya.

Alisema kuongezeka kwa wakazi wa Thika kumewapatia changamoto kubwa na hivyo kutakikana kutafuta mbinu ya kuongeza maji kwa wingi.

Bi Stella Njeri ambaye ni mkazi wa mtaa wa Landless amefurahia kupata maji katika nyumba yake akisema shida ya zaidi ya miaka sita imekwisha.

“Kwa muda mrefu sasa sisi kama wakazi wa eneo hili tumepata shida kubwa ya maji lakini kwa huruma wa mbunge wetu sasa tuna maji,” alisema Bi Njeri na kuongeza “tutahakikisha tunalinda eneo hili lisije likavamiwa na wezi wa vifaa vya maji”.

Thiwasco yaimarisha huduma ya usambazaji maji Thika

Na LAWRENCE ONGARO

KAMPUNI ya Maji ya Thiwasco Water Company Ltd imeweka mikakati ya kuboresha huduma kwa wateja.

Mkurugenzi mkuu wa kampuni hiyo, Bw Moses Kinya, alisema tayari wameanza kufanya mabadiliko ya kuweka mabomba ya kusambaza maji ili kutosheleza mahitaji ya wateja wao.

“Tumeanza kuweka mabomba mapana ya kusambaza maji maeneo tofauti na kuhakikisha tunaongeza kiwango cha maji tunayosambaza kwa wateja. Pia wateja wetu wameongezeka kwa wingi kwa kipindi cha miaka michache tu ambayo imepita,” alisema Bw Kinya.

Alitaja maeneo ya Githunguri, Landless, na Witeithie kama zile zilizoongezeka na wakaaji na kwa hivyo usambazaji wa maji lazima uongezeke.

Alisema kampuni ya Thiwasco ndiyo inayotambulika kama inayosambaza maji kwa njia ya kisasa kote nchini, baada ya kupata kibali maalum cha ISO 9001-2015.

Mkurugenzi wa Thiwasco Water Company Ltd Bw Moses Kinya akihutubia washikadau waliohudhuria mkutano wa kila mwaka. Picha/ Lawrence Ongaro

Alisema kampuni hiyo inasambaza maji mjini Thika na maeneo ya karibu ambapo wateja ni zaidi ya 300,000.

Alisema bado wanapitia changamoto za hapa na pale kwa sababu wanakosa ardhi ya kutosha ya kupanua mipango yao ya kusambaza maji kwingineko.

“Iwapo tutapata kipande cha ardhi cha kutosha bila shaka tutaweza kusambaza maji maeneo mengine na wateja wetu wataongezeka kwa wingi,” alisema Bw Kinya.

Alisema maeneo mengine ambayo anatarajia kuongeza mabomba ya maji ni Makongeni na Kiganjo mjini Thika kutokana na ongezeko la idadi ya watu.

“Kulingana na ukuaji wa teknolojia ya kisasa ni sharti hata sisi tufuate mkondo huo ili tuhudumie wateja wetu kwa njia ifaayo,” alisema mkurugenzi huyo.

Waziri wa Maji na Mazingira katika Kaunti ya Kiambu, Bw David Kuria alipongeza juhudi zinazofanywa na kampuni ya Thiwasco za kusambaza maji kwa wakazi wa Thika kwa jumla.

Alipendekeza kuwe na mpango wa kuhifadhi maji kwa wingi hasa wakati kuna mvua nyingi ili maji hayo yaweze kunufaisha watu wakati wa kiangazi.

“Ni jambo la busara kuhifadhi maji ili kusiwe na upungufu wowote. Maji ni uhai na kwa hivyo si vyema kuwa na upungufu ilhali maji mengi hupotea bure wakati wa mvua,” alisema Bw Kuria.

Alisema visima pia ni muhimu katika makazi ili wakati wowote ule kusiwe na shida ya maji kukiwa na ukame.

Naye Bw John Mwangi alisema kampuni ya Thiwasco imekuwa mstari wa mbele kusambaza maji kwa wakazi wa Thika kwa miaka mingi na kwa hivyo ni vyema kufanya kazi nao kwa ushirikiano wa karibu.

“Cha muhimu ni kuhakikisha watu wanaonyakua vipande vya ardhi wanakabiliwa vilivyo kwa sababu Thiwasco imeshindwa kujipanua kwa sababu hakuna kipande cha ardhi cha kutosha,” alisema Bw Mwangi.

Madiwani (MCAs), waliohudhuria hafla hiyo walisema watafanya juhudi kuona ya kwamba kampuni hiyo inafanikiwa katika juhudi zake za kusambazia wateja maji mjini Thika na hata Kiambu kwa jumla.

Bw Lawrence Kamangathi alisema gavana Bw James Nyoro amejitolea kuona ya kwamba anafanya kazi kwa ushirikiano na kampuni ya Thiwasco ili wakazi wa Kaunti ya Kiambu wapate maji ya kutosha.

Viongozi wahimizwa wamche Mungu na wawatumikie wananchi

Na LAWRENCE ONGARO

VIONGOZI nchini wamehimizwa kuzingatia maendeleo na kutendea wananchi kazi badala ya siasa za kila mara.

Mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina aliwashauri wananchi kuwachagua viongozi wenye maono ambao wanawajali kwa kuleta maendeleo na kuwatumikia kwa uwazi.

“Nchi hii mahali imefika sasa inataka wananchi wajisahili na wachague viongozi waliowajibika na walio na maono ya kufanikisha maisha ya wananchi,” alisema Bw Wainaina.

Alisema viongozi wengi wanapenda kupumbaza wananchi kila mara bila kuwa na ajenda yoyote ya maendeleo mawazoni mwao.

Aliyasema hayo manamo Alhamisi wakati wa maombi rasmi ya kufungua mwaka yaliyofanyika kwenye afisi yake ya NG-CDF mjini Thika.

Alitoa mfano wa nchi ya Rwanda ambayo alisema imeinuliwa kiuchumi na Rais Paul Kagame kwa kuwateua mawaziri wenye maono na uwajibikaji.

“Nchi hii ina utajiri mwingi ajabu ambapo ikiwa kila kiongozi na mwananchi anaweza akafanya uamuzi wa kuwajibika katika kila jambo, bila shaka tutatambulika kama nchi iliyopiga hatua kimataifa,” alisema Bw Wainaina.

Alisema eneo lake la Thika lilitajwa kama lilotumia fedha zake za maendeleo kwa uwajibikaji na uwazi.

Alitoa mfano na kueleza ya kwamba kwa fedha za maendeleo alizopokea mwaka wa 2019, Sh 48 milioni ziliweza kukarabati shule 30 za msingi zilizokuwa katika hali mbovu.

Askofu mkuu wa kanisa la Evanjelisti la Christian Church International (CCI), Bw Henry Mulandi, alikishauri kizazi cha sasa kuwa makini na kufuata mienendo ya wazee wao.

Kuwatumikia wananchi

Aliwahimiza viongozi popote walipo kupunguza joto la siasa linaloshuhudiwa kwa wakati huu nchini na kujihusisha na kutumikia wananchi.

“Wakati huu sio wakati wa kupiga siasa lakini ni vyema kuona ya kwamba majukumu waliyopewa na wananchi yanatekelezwa vilivyo,” alisema Askofu Mulandi.

“Siku hizi vijana wamejawa na tamaa nyingi kiasi kwamba wanaabudu vitu vya dunia kuliko kumcha Mungu,” alisema askofu Mulandi.

Aliwahimiza pia wazee kuwapa wosia wana wao ili nao waweze kuelewa hali ya maisha ya baadaye ni ipi.

Aliwataka viongozi kuachana na siasa za kila mara na kuzingatia maendeleo.

“Kwa wakati huu siasa za nchi yetu zimechacha kweli ambapo wananchi wameachwa pweke wasijue la kufanya,” alisema mchungaji huyo.

Aliwataka wananchi wamrudie Mwenyezi Mungu ili waweze kupata mwelekeo mwema.

Wazazi, watoto waelezwa njia za kufuata mkondo bora maishani

Na LAWRENCE ONGARO

WACHUNGAJI wa makanisa wamewahimiza vijana wajiepushe na maovu na badala yake kufuata mkondo bora wa kuwa tegemeo siku za usoni.

Naye Mbunge wa Thika amewahimiza wazazi wawe makini na wana wao ili wasije wakaangamizwa na dawa za kulevya.

Mchungaji wa Kanisa la Chrisco Church, Magogoni, Thika Bw Simon Mbatia, alisema kanisa ni eneo takatifu laMwenyezi Mungu, wala sio mahala pa kuzungumzia maswala ya siasa holela.

“Sisi kama wachungaji tunataka kuweka wazi kuwa tunataka kusambaza neno la Mungu kanisani lakini sio kukubalia viongozi kurushiana cheche za matusi,” alisema Bw Mbatia.

Alisema cha muhimu kwa wakati huu ni viongozi kuzingatia maendeleo hadi mwaka wa 2022 ili wananchi wapate maendeleo walioahidiwa nao.

Aliyasema hayo Ijumaa katika kongamano la wachungaji 120 wa madhehebu mbalimbali kutoka Kaunti ya Kiambu lililofanyika kituo cha mafunzo cha Kolping, Kilimambogo, Thika Mashariki.

Kamari

Lilihudhuriwa pia na Mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina aliyetoa mwito kwa wazazi kuwalinda wana wao kujiepusha na uchezaji wa kamari na dawa za kulevya.

Alisema familia nyingi zimepoteza matumaini kwa sababu ya msongo wa mawazo.

Mbunge wa Thika, Mhandisi Patrick ‘Jungle’ Wainaina, akagua nguo zinazoshonwa na wanafunzi wa chuo cha Kolping’, Kilimambogo, Thika Mashariki. Aliandamana na Mchungaji wa Kanisa la Chrisco Church, Bw Simon Mbatia. Picha/ Lawrence Ongaro

“Siku hizi vijana wengi wamepoteza mwelekeo kwa kujiingiza kwa uchezaji wa kamari na kusahau kufanya kazi kwa bidii. Wengi wanaamini kutajirika kwa haraka,” alisema Bw Wainaina.

Aliwaomba wachungaji kuwa mstari wa mbele kuzipatia ushauri familia nyingi zilizo na shida za kifamilia.

“Siku hizi tunashuhudia kesi nyingi za watu kujinyonga kwa sababu ya matatizo ya kifamilia. Kwa hivyo, ni vyema wachungaji kujitokeza kuwapa ushauri wa kiroho,” alisema Wainaina.

Alisema huu ni wakati wa kuchapa kazi wala sio wakati wa kujipanga kwa uchaguzi wa mwaka wa 2022.

“Iwapo tutafanyia wananchi kazi ipasavyo bila shaka watapata nafasi nzuri ya kuchagua viongozi wao ifikapo wakati huo,” alisema Bw Wainaina.

Askofu wa Kanisa la Regeneration Evangelistic Church Bw Francis Maina aliwahimiza viongozi wafuate maagizo ya Rais Uhuru Kenyatta ya kufanyia wananchi kazi.

“Iwapo mwongozo huo utafuatwa bila shaka mwananchi wa kawaida atakuwa amefaidika pakubwa na maendeleo,” alisema Askofu Maina.

Wakazi wamtaka Waititu awape huduma bora

Na LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa Thika wameikejeli serikali ya Kaunti ya Kiambu kwa kuzembea katika utendakazi wake katika kile wanachoamini ni kupuuzwa na usimamizi wa kaunti.

Wakiongozwa na mwenyekiti wa wafanyabiashara Bw Alfred Wanyoike, walisema mashimo mengi ya maji taka yameachwa wazi jambo ambalo ni hatari kwa usalama kwa wapitanjia na wenye magari.

“Sisi kama wakazi wa eneo hilo tumebaki tukijiuliza kama kweli tuna viongozi. Haya mashimo ya maji taka yanatuweka na wasiwasi mwingi,” alisema Bw Wanyoike.

Alisema hivi majuzi mwanamke mmoja mjamzito alivujika miguu akijaribu kuruka mojawapo ya mashimo  ambapo aliumia vibaya.

Alifafanua kuwa mahali mambo yamefika sio kuulizia kutendewa kazi bali ni kuwalazimisha kimambavu  kwa sababu wanatoa kodi ya huduma.

Iwapo watazidi kuzembea kazini wananchi wameapa kuwashurutisha wahusika kufanya kazi hiyo.

 

“Tutaandamana ili kuonyesha ghadhabu zetu kwa serikali ya Kaunti ya Kiambu, inayoongozwa na Bw Ferdinand Waititu,” alisema Bw Wanyoike.

Baadhi ya maeneo yaliyoathirika kwa kupata mashimo hayo ni barabara Za Uhuru, Mama Ngina, Nkrumah, na Kenyatta.

 

Mmiliki wa kiwanda cha pombe haramu Thika aingia mitini

Na LAWRENCE ONGARO

KIWANDA cha pombe ya mvinyo cha African Spirit Distillers Ltd, mjini Thika, Ijumaa kilifungwa uchunguzi dhidi yake ukiendelea, hali iliyolazimisha mmiliki wake kwenda mafichoni.

Inspekta Mkuu wa Polisi Bw Joseph Boinet, alisema kwa muda mrefu kiwanda hicho kimekuwa kikitengeneza pombe gushi huku kikikosa pia kulipia ushuru wa KRA.

Siku chache zilizopita wafanyikazi watatu wakuu wa kiwanda hicho walitiwa nguvuni baada ya kupatikana wakiendesha shughuli zao kwa njia isiyo halali.

Bw Boinett alisema Ijumaa kwamba baada ya maafisa wa upelelezi kufanya uchunguzi wao kwenye kiwanda hicho walipata vibandiko gushi 21 milioni vya KRA huku wakikwepa kulipia takribani Sh1.2 bilioni za ushuru.

“Tumepata ya kwamba mkurugenzi wa kiwanda hicho amekwenda mafichoni jambo linalofanya tushuku kuwa anategeneza bidhaa gushi. Tutahakikisha mmiliki wa kiwanda hicho anafikishwa mahakamani ili kujibu mashtaka,” alisema Bw Boinett.

Alisema kiwanda hicho kitakuwa chini ya ulinzi wa polisi na hakuna mtu yeyote ataruhusiwa kuingia mle ndani hadi uchunguzi kamili ukamilike.

Kamishna wa KRA kitengo cha uchunguzi Bw Githii Mburu alisema kampuni hiyo imekuwa ikifanya biashara kwa kutumia njia ya mkato.

“Tumegundua ya kwamba hawalipi ushuru wa KRA huku wakiuza pombe wakitumia vyeti gushi vya KRA.”

Alisema kemikali wanayotumia ni hatari na watalazimika kuendelea na uchunguzi ili kuharamisha biashara hiyo ya pombe.

Afisa mkuu wa upelelezi DCI Bw George Kinoti, alisema wanataka kuchunguza uhalali wa pombe ya mvinyo inayotengenezwa hapo.

“Tunataka kuelewa jinsi pombe hiyo hukaguliwa kwenye kiwango chake cha mwisho kabla ya kujazwa kwenye chupa. Na pia ni vituongapi inayopitia kabla ya pombe hiyo kuwekwa kwenye chupa,” alisema Bw Kinoti.

Alisema iwapo kutapatikana afisa yeyote wa KRA ama polisi wanaoshirikiana kwa biashara mbovu na kiwanda hicho bila shaka watanaswa bila huruma na kushtakiwa kwa mauaji kwa kuuza bidhaa haramu.

KRA ilitangaza kuwa kampuni hiyo ilianza kuchunguzwa Januari 31, 2019 na lita 312,000 za bidhaa haramu  zilinaswa kwenye kampuni hiyo.

KRA ilisema kwamba kampuni hiyo ina leseni ya kutengeneza mvinyo aina ya Glen Rock, Legend Black, Blue Moon, Legend Brandy, Gypsy King na Furaha.

Mbunge ateua baraza la mawaziri kumsaidia kazini

Na MARY WAMBUI

MBUNGE wa Thika Mjini Patrick Wainaina amezindua baraza la mawaziri wanane, ambalo litamsaidia kutimiza ahadi alizotoa kwa wakazi wa eneobunge hilo.

Kulingana naye, kundi hilo litaangazia uimarishaji wa uchumi, miundomsingi, kilimo, elimu/talanta, afya, mazingira na hali ya usalama.

Kundi hilo pia litamsaidia kuimarisha hali ya masomo katika shule zote za umma, kufufua sekta ya Jua Kali, kuimarisha usambazaji wa umeme kwa wakazi kati ya masuala mengine.

Akizungumza na Taifa Leo kwa mara ya kwanza, Bw Munene alisema kwamba mkakati huo unalenga kuhakikisha ametekeleza mipango yake ya maendeleo.

“Kaulimbiu yangu ni: Hapa Kazi Tu. Ningetaka kukumbukwa kwa kutoa uongozi bora ambao utachangia kuimarisha maisha ya wakazi. Lazima tuhakikishe kwamba eneo hilo limerejesha hadhi yake kama kitovu cha biashara,” akasema.