Pigo kwa KNH kumpoteza mtaalamu wa tiba ya figo

Na RICHARD MUNGUTI

Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) imepata pigo kuu baada ya mmoja wa madaktari walio na tajriba ya juu kufariki baada ya kuugua virusi vya corona.

Dkt Anthony Were, aliyekuwa mtaalamu wa tiba ya figo alikuwa amelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) kwa muda wa zaidi ya wiki mbili kabla ya kuzidiwa na ugonjwa huo.

Pia alikuwa anasimamia kitengo cha matibabu ya figo katika hospitali hii kuu nchini Kenya na eneo hili la Afrika mashariki.

Katibu mkuu wa Chama cha Kutetea Haki za Madaktari (KMPDU) Dkt Chibanzi Mwachonda alitoa risala za rambirambi kwa jamii na familia ya marehemu.

Katika risala yake , Dkt Mwachonda alisema Dkt Were alikuwa mwalimu, mshauri na kiongozi mstahiki aliyekuwa amechaguliwa kuwa Rais wa Chama cha Matibabu ya Figo Barani Afrika (AAN) na naibu wa mkurugenzi mkuu wa Taasisi ya Figo eneo la Afrika Mashariki (EAKI).

“Siku 14 zilizopita ulikuwa umetuuliza tukuombee baada ya kulazwa tena ICU baada ya kuugua ugonjwa wa corona. Tumeamka na kupashwa habari za kusikitisha kwamba umeaga. Wewe ulikuwa mwalimu, mshauri na kiongozi wa tiba ya figo. Mungu akutunuku,” alisema Dkt Mwachonda katika risala yake kwa familia,marafiki na wafanyakazi wenzake.

Serikali yaonya tiba ya corona isitumiwe ovyo

Na WANDERI KAMAU

WANANCHI wameshauriwa dhidi ya kutumia dawa aina ya dexamethasone kutibu virusi vya corona bila idhini ya daktari.

Dawa hiyo ilibainika kupunguza makali ya virusi hivyo kwa watu walio hali mahututi kwa viwango mbalimbali, baada ya majaribio yaliyofanywa na wataalamu nchini Uingereza.

Mkurugenzi wa Matibabu nchini, Dkt Patrick Amoth jana alisema kutokana na kuwa dawa hiyo hupatikana kirahisi kwa bei nafuu, huenda baadhi ya wananchi wakaanza kuitumia kiholela wakishuku kuambukizwa virusi vya corona.

Serikali ilisema Kenya ingali inashauriana na taasisi za utafiti wa kimatibabu kubaini ikiwa dawa aina ya inafaa kwa matibabu ya ugonjwa wa Covid-19.

Hayo yalijiri huku idadi ya watu walioambukizwa virusi nchini ikifikia 4,044 baada ya visa 184 kuthibitishwa.

Idadi ya wale waliopona iliongezeka na kufikia 1,353 baada ya watu 27 zaidi kuruhusiwa kwenda nyumbani. Hata hivyo, watu wawili zaidi walifariki na kufikisha idadi kuwa 107.

Shirika la Afya Duniani (WHO) liliridhishwa na matokeo ya dawa hiyo, likisema yanaashiria huenda tiba ya virusi hivyo ikapatikana katika siku za hivi karibuni.

Waziri Msaidizi wa Afya, Dkt Rashid Aman alisema Kenya inafanya mazungumzo na WHO na taasisi zingine za kimatibabu, kubaini ufaafu wa dawa hiyo kwa matumizi ya wale walioambukizwa.

“Tunafuatilia kwa kina majaribio hayo. WHO imeeleza kuridhishwa na matokeo ya kwanza ya majaribio yake. Vivyo hivyo, tunashauriana na taasisi zetu za utafiti wa kimatibabu kubaini uhalisia wake kuihusu,” akasema.

Hata hivyo, alisema kuwa Kenya itafuata taratibu zote za kimataifa kuhusu utafiti, kwani bado haijaidhinishwa rasmi kutumika.

Dawa hiyo husababisha madhara mwilini isipotumiwa ifaavyo. Baadhi ya madhara yake ni kuongeza uzani mwilini, ongezeko la shinikizo la damu, kisukari kati ya mengine.

SHINA LA UHAI: Mzigo mkubwa wa gharama ya matibabu ni kizingiti kikuu

Na PAULINE ONGAJI

ALIPOGUNDUA kwamba alikuwa na maradhi ya kansa ya Mlango wa Uzazi (Cervical Cancer), dunia ilimpasukia Rose Adero, 41, huku akipoteza matumaini ya kuendelea kuishi.

Ilikuwa ni mwaka wa 2015, mkazi huyu wa mtaa wa Umoja Innercore jijini Nairobi, alipogundua hali yake ya kiafya ambayo kwa takriban miaka minne sasa imemkosesha usingizi na kufyonza hela zote za familia yake.

“Masaibu yangu yalianza mwaka wa 2015 ambapo baada ya kufanyiwa uchunguzi na mwanajinalokojia, nilipatikana kuwa na kansa ya mlango wa uzazi,” aeleza mama huyu wa watoto wanne.

Alianza kufanyiwa matibabu yaliyohusisha upasuaji, taratibu za tibakemia (chemotherapy) na tibaredio (radiotherapy). Lakini akiwa katika harakati, hizo alipata pigo baada ya mumewe kupatikana na kansa ya ini ambayo ilikuwa katika hatua ya nne (stage four).

“Nililazimika kusitisha matibabu yangu mara moja kwani nilikuwa nimepoteza ajira kama keshia katika mojawapo ya maduka makuu ya jumla nchini, na huku mume wangu akianza kupokea matibabu, hatungeweza kumudu gharama ya matibabu,” aeleza Bi Adero ambaye kwa sasa amesalia mjane baada ya mumewe kuaga dunia mwezi Mei 2018.

Lakini huo haukuwa mwisho wa masaibu yake kwani kutokana na gharama ya matibabu yake na ya mumewe, amelazimika kuuza baadhi ya mali waliyokuwa wamekusanya huku wanawe kati ya miaka mitano na 22 wakilazimika kusitisha masomo kutokana na ukosefu wa karo.

“Uchunguzi wa mwisho ulikuwa mwezi Julai mwaka jana ambapo daktari aliamuru nifanyiwe utaratibu a MRI katika sehemu ya tumbo na fupanyonga, uchunguzi ambao ungegharimu Sh36, 000. Aidha, nilipaswa kufanyiwa uchunguzi wa seli na tishu katika sehemu hii (biopsy) kubaini kiwango cha kansa hiyo mwilini mwangu, lakini sikuwa na pesa,” aeleza.

Kulingana na utafiti, ni asilimia tatu pekee ya wanawake nchini Kenya ambao huenda hospitalini kufanyiwa uchunguzi wa kansa hii huku hata wanaotafuta tiba mapema wakikumbwa na mzigo mkubwa wa gharama ya matibabu.

Mpango wa Kitaifa wa Kudhibiti Kansa unaashiria kwamba gharama ya matibabu inasalia kuwa kizingiti kikuu katika vita dhidi ya ugonjwa huu ambapo uchunguzi wa kansa ya uzazi nchini Kenya humgarimu mwanamke angaa Sh3, 000.

Aidha, tiba ni ghali sana huku ikigharimu kati ya Sh172, 000 na Sh759, 000 kutibu kansa hii bila upasuaji, na Sh672,000 na Sh 1.2m kutibu maradhi haya endapo upasuaji utafanywa.

Haya yakijiri, takwimu za maradhi haya zaendelea kutisha ambapo kulingana na shirika la kimataifa la utafiti wa kansa, ni ya pili miongoni mwa kansa zilizokithiri sana nchini Kenya, baada ya ile ya matiti.

Kulingana na utafiti wa wizara ya Afya, maradhi haya husababisha vifo vya wanawake wanane kila siku nchini Kenya, idadi ambayo ni sawa na vifo 3,286 kila mwaka. Aidha, kansa hii husababisha vifo vingi; asilimia 12 miongoni mwa watu wanaopatikana kuugua ikilinganishwa na kansa ya matiti ambayo asilimia tisa ya wanaopatikana na maradhi haya hufariki.

Isitoshe, wanawake watatu kati ya 100 nchini Kenya wamo katika hatari ya kuugua maradhi haya, huku visa 5,250 vikiripotiwa kila mwaka nchini.

Jinsi inavyosambaa

Husambaa katika hatua nne.

• Katika hatua ya kwanza, kansa husambaa kwenye mlango wa uzazi hadi kwenye uterasi. Hapa, tiba inahusisha upasuaji unaojulikana kama hysterectomy ambapo sehemu au uterasi yote inaondolewa.

• Hatua ya pili inahusisha seli za kansa kuenea mbali kwenye mlango wa uzazi na hata kufikia sehemu ya uke. Hapa, tiba huhusisha tibakemia (chemotherapy) na tibaredio (radiotherapy).

• Katika hatua ya tatu, maradhi haya huwa yameenea hadi kwenye ukuta wa fupanyonga na huenda ikachukua asilimia 33 ya sehemu ya uke na hata kusababisha figo kuvimba na kutatiza au hata kusitisha kabisa shughuli za kiungo hiki. Hapa pia, utaratibu wa tiba unahusisha tibakemia na tibaredio.

• Hatua ya nne na ya mwisho ni mbaya zaidi ambapo huenea hadi kwenye kibofu cha mkojo na hata kuathiri vinundu vya limfu na baada ya muda huenea katika sehemu zingine za mwili.

Chanzo

Kwa hivyo nini hasa kinachochea maradhi haya? Kulingana na Dkt John Ong’ech, mtafiti mkuu wa kimatibabu na mwanajinakolojia katika hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta, baadhi ya mambo yanayoongeza uwezekano wa kukumbwa na maradhi haya ni pamoja na kushiriki ngono na watu kadha bila kinga.

“Hii huongeza uwezekano wa kuambukizwa virusi vya HPV vinavyosababisha kansa hii,” aeleza.

Pia, anasema kwamba wanawake wanaoishi na virusi vya HIV wana uwezekano mkubwa wa kukumbwa na maradhi haya baada ya kuambukizwa virusi vya HPV wakilinganishwa na wale wasio na virusi vya HIV.

Ishara

• Kuvuja damu katika sehemu ya uke baada ya tendo la ndoa

• Kuvuja damu katikati ya siku za hedhi au baada ya kukatikiwa

• Maji maji ya damu kutoka sehemu ya uke ambayo huenda yakawa mengi na kuandamana na harufu mbaya

• Uchungu wa fupanyonga au uchungu baada ya tendo la ndoa

Uchunguzi

Kulingana na Dkt Ong’ech, ugonjwa huu waweza kutambuliwa kupitia kipimo cha saratani ya mlango wa uzazi ( pap smear) kinachosaidia madaktari kugundua vidonda au seli zisizo za kawaida na ambazo zaweza kutibiwa kabla ya kusababisha kansa.

“Kila mwanamke anapaswa kufanyiwa uchunguzi huu angaa mara moja baada ya miaka mitatu hadi uhitimu miaka 70. Wanawake wengi huenda hospitalini wakiwa wamechelewa ambapo mara nyingi kansa hii huwa imeenea katika sehemu zingine, na hivyo kufanya iwe vigumu kupokea matibabu na kuokoa maisha ya mgonjwa,” aeleza.

Kulingana naye, hakuna mtu anayepaswa kufa kutokana na kansa kwani ni ugonjwa ambao waweza kukabiliwa iwapo utatambuliwa mapema.

Madaktari wa mitishamba wasifu marufuku ya ukataji miti

Na TTUS OMINDE

MADAKTARI wa mitishamba kutoka eneo la North Rift wamesifia marufuku ya ukataji miti katika misitu ya umma kote nchini.

Walisema jana kuwa hatua hiyo itasaidia kulinda misitu ambayo ni chanzo cha dawa za kiasili.

Wakiongozwa na daktari Shadrack Moimet wa zahanati ya Koibatek Herbal mjini Elodret, walisema ukataji miti kiholela pia ni tishio kwa tiba za kiasili.

Daktari Moimet alisema marufuku hiyo ya miezi mitatu haitoshi bali yapaswa kuongezwa na kuwa angalau miezi sita.

“Kama daktari wa tiba za kiasili tunapongeza serikali kupitia kwa wizara ya mazingira kwa kupiga marufuku ukataji miti misituni,miti hii ni chanzo kikubwa kwa dawa za kiasili ambazo sisi hutumia kwa kutibu Wakenya,” alisema Dkt Moimet.

Walipongeza waziri wa mazingira Bw Keriako Tobiko huku wakitaka wale ambao wanapinga marufuku hiyo kutilia maanani afya ya Wakenya na mahitaji ya Wakenya kwa jumla pasipokuzingatia tu maswlaa ya biashara yao.

Wakati huo huo madaktari hao walitaka bunge kupitisha sheria kuhusu tiba za kiasili ambao umekuwa bungeni yapata miaka 10 zilizopita.

Dkt Moimet alisema iwapo sheria hiyo itapitishwa itasaidiz kudhibiti sekta ya tiba za kiasili kwa ushirikiano na tiba za kisasa.

 

Wataka bunge lipitishe sheria kulinda tiba za kiasili

Na TITUS OMINDE

MADAKTARI wa tiba za kiasili wanataka bunge kupitisha sheria kuhusu tiba hizo. 

Madaktari hao walisema kupitishwa kwa sheria hiyo kutakabiliana na matapeli katika sekta hiyo mbali nakutoa mazingira bora ya wahudumu wa tiba za kiasili.

Daktari Shadrack Moimet wa zahanati ya Koibatek mjini Eldoret alisema kukosekana kwa sheria na sera kuhusu tiba hizo kumechangia katika ongezekeo la matapeli katika tiba husika.

Dkt Moimet alisema iwapo wabunge watapitisha sheria hiyo Wakenya wataondoa dhana potovu kwamba tiba za kiasili ni uchawi.

“Ikiwa sheria hii itapitishwa matapeli ambao wamevamia sekta hii watadhibitiwa mbali na kuondoa dhana potovu kwamba tiba za kiasili ni ushirikina na uchawi.”

Anataka wahudumu katika tiba hizo kushirikiana ili kuona kwamba matakwa yao yanatekelezwa.

Mswada kuhusu tiba hizo umekuwa bungeni tangu bunge la tisa ambapo umekuwa ikihairishwa mara kwa mara.

Madaktari wa tiba za kiasli wanadai kuwa iwapo watapewa mazingira bora ya kuendelezea kazi zao watashirikiana na madaktari wa tiba za kisasa kukubiliana na changamoto ya maradhi tata.

“Dawa zetu zina uwezo wa kutibu ugonjwa kama vile saratani na maradhi mengine ambayo hayana tiba zakisasa, kile tunataka ni kutambuliwa na kushirikishwa vilivyo katika utafiti wa maradhi husika,” akasema.

Vile madaktari hao wanataka serikali kuwatengea fedha za kuendeleza utafiti kupitia tiba za kiasili kama ilivyo nchini Uchina.