Jubilee kuachia kila raia deni la Sh180,000

Na BENSON MATHEKA

SERIKALI ya Jubilee itaachia kila raia wa Kenya, wakiwemo watoto watakaozaliwa mwaka 2022, mzigo wa kulipa Sh180,000 kwa sababu ya madeni inayoendelea kukopa.

Kufikia sasa, deni la Kenya ni Sh7.7 trilioni na kulingana na makadirio ya ukopaji unaotarajiwa, itaongeza Sh1.8 trilioni kufikia Juni 2022.

Ikizingatiwa kuwa idadi ya Wakenya inakadiriwa kuwa milioni 50, Jubilee itakapoondoka mamlakani mwaka 2022, kila Mkenya atakayekuwa amezaliwa atakuwa na deni la Sh180,000.

Tamaa ya madeni ya serikali ya Jubilee imefanya maisha ya Wakenya kuwa magumu huku ikitumia asilimia 85 ya ushuru inaokusanya kuyalipa.

Wizara ya Fedha iliambia bunge kwamba ilichukua mikopo 10 mipya ya jumla ya Sh293.5 bilioni kati ya Aprili 1 na Agosti 31, 2021.

Wataalamu wa masuala ya uchumi wanasema kwamba nusu ya mikopo hiyo italipwa na serikali ijayo, kumaanisha kuwa Wakenya hawatapata afueni baada ya Jubilee kuondoka mamlakani.

“Ilivyo ni kuwa Wakenya watalipa madeni ya serikali ya Jubilee miaka mingi baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuondoka mamlakani. Huu ndio ukweli wa mambo,” mwanauchumi Silvester Ochuka aliambia Taifa Leo jana Alhamisi.

Kulingana na Mhasibu Mkuu wa serikali, Nancy Gathungu, serikali imeongeza madeni kwa asilimia 125 ikiwa ni kima cha asilimia Sh4.2 trilioni ndani ya miaka sita na kuyafanya kukaribia kiwango cha juu cha madeni, Sh9 trilioni, kilichowekwa na bunge.

Dkt Gathungu aliambia Kamati ya Fedha ya Seneti kwamba deni la Kenya la Sh7.7 trilioni ni asilimia 85 ya kiwango cha Sh9 trilioni ambacho wabunge waliweka 2019.

Kumekuwa na mipango ya kuongeza kiwango hicho hadi Sh12 trilioni, jambo ambalo wanauchumi wanasema bunge likipitisha, Jubilee itaacha nchi na zigo kubwa zaidi la madeni.

Asilimia 84 ya madeni ya Kenya yalikopwa na serikali ya Jubilee ilipoingia mamlakani 2013 ikiahidi kutekeleza miradi kabambe ya miundomsingi.

Kulingana na gazeti la Business Daily, serikali ya Rais Uhuru Kenyatta imekopa zaidi ya Sh6.1 trilioni kwa miaka tisa ambayo imekuwa mamlakani.

Ilipoingia mamlakani mnamo 2013, deni la Kenya lilikuwa Sh1.79 trilioni. Ikiwa serikali itakopa Sh1.87 trilioni inavyokadiria, serikali ya Jubilee itakakuwa imekopa Sh2.5 bilioni kila siku na kuongeza deni la Kenya kuwa Sh8.06 trilioni mwishoni mwa mwaka huu.

Serikali inaendelea kubebesha Wakenya mzigo kwa kuwa inavyoendelea kulipa madeni ndivyo inavyoendelea kukopa zaidi kutoka katika taasisi za kifedha za kimataifa na za humu nchini.

Baadhi ya madeni huwa na masharti makali yanayoumiza raia.

Rais Uhuru Kenyatta amekuwa akitetea madeni ya serikali yake akisema yamesaidia kuimarisha miundomisingi nchini kama ujenzi wa reli ya kisasa, barabara na mabwawa.

Hata hivyo, madeni hayo yamekuwa ‘yakimeza’ nusu ya pesa ambazo serikali inakusanya kama ushuru na kuiacha ikitatizika kuendesha serikali na miradi ya maendeleo, elimu na idara ya afya. Deni hili linapotishia Wakenya, Dkt Gathungu anaibua maswali kuhusu rekodi za ulipaji mikopo hiyo akisema zinaonyesha kuna dosari.

Hasa, Mhasibu Mkuu huyo wa serikali anadadisi jinsi Sh2 bilioni zilivyotumika kwenye mwaka wa kifedha uliomalizika Juni 2020.

“Kulikuwa na Sh2 bilioni zaidi ambazo Benki Kuu ya Kenya (CBK) haikudhihirisha na huenda hazitapatikana,” alisema Dkt Gathungu.

Mwelekezi wa Bajeti, Margaret Nyakango pia ameibua maswali kuhusu jinsi mikopo hiyo ilivyotumiwa akisema kiwango kikubwa kilitumiwa kulipa madeni kinyume cha sheria ya Usimamizi wa Pesa za Umma ya 2012.

UhuRuto wazua wasiwasi

Na WANDERI KAMAU

TOFAUTI za kisiasa na majibizano ya hadharani kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Naibu Rais William Ruto zimetajwa kuwa tishio kwa amani na uthabiti wa kitaifa.

Wanaharakati, wanasiasa na wananchi waliozungumza na ‘Taifa Leo’ Jumatano walieleza hofu kuwa Rais Kenyatta na Dkt Ruto wanaweza kuitumbukiza Kenya katika hali sawa na ilivyokuwa kwenye uchaguzi wa 2007, ambapo mamia walikufa na maelfu wakapoteza makao.

Rais Kenyatta na Dkt Ruto ndio waliokuwa washukiwa wakuu wa ghasia hizo na walishtakiwa katika Mahakama ya Kimataifa kuhusu Uhalifu (ICC) lakini kesi zao zikaporomoka.

Wadadisi wa siasa wanasema kiini cha kuungana kwa wawili hao ni ghasia za 2007 baada ya kushtakiwa katika ICC, lakini sasa wanaonekana kutojali. Wanasema ni hali inayoweza kuirejesha Kenya katika hali sawa na hiyo.

Aliyekuwa kiongozi wa Kanisa la Christ Is The Answer Ministries (CITAM) nchini, Dkt David Oginde, alisema ni wakati wawili hao wafahamu wanaubeba mustakabali wa Kenya mikononi mwao na vitendo vyao vitaamua mwelekeo wa nchi.

“Inasikitisha kumwona Rais na naibu wake wakijibizana peupe bila kufahamu hali zilizochangia wao kuungana. Wakati umefika kwao kutathmini athari za ndimi zao, hasa wakati huu nchi inaelekea kwenye uchaguzi mkuu mwingine,” akasema Dkt Oginde.

Aliyekuwa mbunge wa Mukurwe-ini, Kabando wa Kabando, ambaye pia ni mwanaharakati wa kisiasa, anasema majibizano hayo yanazua taswira kama kuwa uchaguzi wa 2022 ni wa kufa kupona kwa Wakenya.

“Ingawa ni kawaida siasa kushika kasi wakati wa urithi, uchaguzi wa 2022 ni tofauti sana na ilivyokuwa 1978 wakati marehemu Daniel Moi alikuwa akichukua uongozi baada ya kifo cha Mzee Kenyatta na 2002, wakati Rais Mstaafu Mwai Kibaki alichukua uongozi kutoka kwa Bw Moi. Msingi wa utawala wa UhuRuto umekuwa ni mashtaka yaliyowakabili katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC),” akasema Bw Kabando.

Rais Kenyatta na Dkt Ruto wanalaumiwa kwa kuwasaliti Wakenya, wakati wanapitia hali ngumu za kiuchumi kutokana na athari za janga la virusi vya corona.

Tangu walipochukua uongozi mnamo 2013, utawala wa UhuRuto umeandamwa na maovu kama sakata za ufisadi, kuwatoza Wakenya ushuru wa juu, uongezeko la deni la kitaifa, ukosefu wa usalama kati ya changamoto nyingine nyingi.

Serikali ya UhuRuto pia imekuwa ikilaumiwa kwa kuendeleza ubomozi katika katika sehemu mbalimbali nchini, hivyo kuwaathiri maelfu ya wafanyabiashara wadogo wadogo, licha ya kuahidi kuwainua kiuchumi.

Kwenye sakata hizo, Wakenya wamepoteza mabilioni ya pesa, huku washukiwa wakuu wakikosa kuchukuliwa hatua zozote au kesi zao kucheleweshwa katika hali tatanishi.

Baadhi ya sakata hizo ni wizi wa fedha zilizokusudiwa kujenga mabwawa ya Arror na Kimwarer, juhudi za kukabiliana na makali ya virusi vya corona kati ya sakata zingine.

Deni la kitaifa pia limekuwa likiongezeka karibu kila mwaka, kwa sasa likikisiwa Sh8 trilioni.

Kwenye mahojiano jana, kiongozi wa chama cha Narc-Kenya, Martha Karua alisema wakati umefika kwa Rais Kenyatta kuungana na Dkt Ruto ili kutimiza ahadi walizotoa kwa Wakenya wakati wa kampeni zao mnamo 2013.

Anasema kuwa kuharamishwa kwa Mpango wa Kubadilisha Katiba (BBI) hakupaswi kuwa chanzo chao kuvutana, lakini wanapaswa kuungana tena kuhakikisha wametimiza Ajenda Nne Kuu za Maendeleo.

Mwanaharakati Mutemi wa Kiama kutoka vuguvugu la Linda Katiba anasema UhuRuto wamesahau msingi uliowaunganisha mara tu walipopata mamlaka.

“Malumbano yanayoendelea baina yao ni dhihirisho la wazi wanavutania maslahi yao wenyewe wala hawawajali Wakenya. Wamepofushwa na mamlaka kiasi cha kusahau hali zilizowafanya kuumgana,” asema Bw Kiama.

Kasisi Sammy Wainaina wa All Saints Cathedral, Nairobi, anasema wawili hao ndio wataubeba msalaba ikiwa kuna damu yoyote itamwagika 2022 kutokana na kutojali kwao.

“Viongozi wanapaswa kufahamu wanawajibikia lolote litokeapo nchini. Wanapaswa kuwa katika mstari wa mbele kuhakikisha nchi imeungana badala ya kuendeleza migawanyiko,” asema.

Hata hivyo, washirika wa viongozi hao wawili wanalaumiana baina yao, kila mmoja akiutetea mrengo wake.

Mbunge Ngunjiri Wambugu (Nyeri Mjini) anamlaumu Dkt Ruto kwa “kuanza uchokozi dhidi ya Rais” kwa kupinga ajenda za serikali ambayo anahudumu.

 

Hata hivyo, mbunge Nelson Koech (Belgut) anataja kiini cha mzozo kati viongozi hao kuwa mtindo wa Rais kumtenga Dkt Ruto, licha yake (Ruto) kuchangia pakubwa ushindi wa serikali ya Jubilee katika chaguzi kuu za 2013 na 2017.

“Ni kinaya kuwa Rais amekuwa akitumia washirika wake wa karibu kama Naibu Mwenyekiti wa Jubilee David Murathe, Katibu Mkuu Raphel Tuju kati ya wengine kuendeleza dhuluma za wazi dhidi ya kiongozi ambaye alichagia zaidi ya nusu za kura alizopata. Ni wakati Rais afahamu kuwa Dkt Ruto si kiongozi aliyeteuliwa bali mshirika sawa waliochaguliwa pamoja naye,” akaeleza Bw Koech.

Wananchi waliozungumza na ‘Taifa Leo’ walisema ni wakati viongozi hao kufahamu kuwa wananchi ndio watakaoumia kutokana na majibizano yao.

“Maombi ya Wakenya kwa Rais na naibu wake ni kufahamu kuwa walichaguliwa na wananchi ili kuwafanyia kazi na kutimiza ahadi zao. Wanapaswa kushirikiana pamoja kwa miezi michache iliyopita ili kutimiza ahadi walizotoa,” asema Bi Stela Saru, kutoka Maseno, Kaunti ya Kisumu.

Bi Felistas Ndonyi kutoka Kaunti ya Machakos anasema wawili hao wanapaswa kujua wao ni kama mume na mkewe, na wanatazamwa na Wakenya wote kama watoto wao.

“Wakati wazazi wanapogombana na hatimaye, watoto wao ndio huteseka. Vivyo hivyo, viongozi hao wanapaswa kufahamu Wakenya ndio wanaoendelea kuteseka wanaporushiana cheche za maneno,” akasema Bi Ndonyi.

Uhuru na Ruto wajiuzulu ikiwa hawawezi kushirikiana – Karua

Na Wanderi Kamau

KIONGOZI wa Narc-Kenya, Bi Martha Karua, amesema Rais Uhuru Kenyatta ameonyesha mfano mbaya katika uzingatiaji wa Katiba kwa kumtenga Naibu Rais William Ruto katika uendeshaji wa serikali.

Kwenye mahojiano jana, Bi Karua alisema Rais Kenyatta amevunja sheria kwa kumtenga Dkt Ruto. Bi Karua alisema kuwa ijapokuwa wawili hao wameruhusiwa kutofautiana kuhusu masuala fulani, wanapaswa kubuni ushirikiano katika utendakazi wao kwa manufaa ya Wakenya.

Alisema ikiwa watafeli kufanya hivyo, basi wanapaswa kujiuzulu na kuwapa nafasi wananchi kuwachagua viongozi watakaofanya kazi kwa ushirikiano mzuri.

“Ikiwa watashindwa kushirikiana, basi wajiuzulu na kuwapa Wakenya nafasi kuwachagua viongozi wapya. Walichaguliwa pamoja, hivyo wanapaswa kufanya kazi kwa ushirikiano. Ikiwa rais anahisi hawezi kushirikiana na naibu wake, na ikiwa (rais) anahisi naibu amefanya kitendo kinachokiuka Katiba, basi anapaswa kubuni mchakato wa kumwondoa mamlakani au ashirikiane naye,” akasema.

Uhusiano wa wawili hao ulianza kudorora Machi 2018, baada ya Rais Kenyatta kubuni handisheki na kiongozi wa ODM, Raila Odinga.

 

UHURUTO WALIVYOFUTA REKODI YA KIBAKI

BENSON MATHEKA NA PAUL WAFULA

MATATIZO ya kiuchumi yanayokumba Kenya kwa wakati huu yanatokana na hatua ya serikali ya Jubilee kudunisha demokrasia na sera za kiuchumi ambazo ambayo Wakenya walifurahia katika utawala wa miaka 10 wa Rais Mstaafu Mwai Kibaki, wataalamu wanasema.

“Demokrasia ndiyo oksijeni inayofanya uchumi kukua na maendeleo kupatikana. Unapoua demokrasia na kuzima uhuru wa raia kujieleza huwa unaua uchumi wa nchi,” asema Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Kimataifa kuhusu Sera na Migogoro, Ndung’u Wainaina.

Alipokabidhi madaraka kwa Rais Uhuru Kenyatta na William Ruto mnamo Aprili 9, 2013, Mzee Kibaki aliwaambia kuwa amewaachia nchi iliyokuwa tayari kupaa kiuchumi na ustawi.

Lakini miaka tisa baadaye ndege ya uchumi iko katika hali mbaya zaidi, na itachukua juhudi kubwa kuirudisha katika hali aliyoiacha Mzee Kibaki.

Mara baada ya kupokea madaraka, utawala wa Jubilee ulipuuza sera za kiuchumi za Mzee Kibaki zilizosaidia Kenya kustawi kiuchumi bila ukopaji.

Rais Kenyatta na Dkt Ruto walianza utekelezaji wa miradi mikubwa mikubwa waliyofadhili kwa mikopo.

Hii ndiyo sababu deni la Kenya limepanda kutoka Sh1.8 trilioni aliloacha Mzee Kibaki hadi Sh7.2 trilioni kufikia mwishoni mwa mwaka jana.

Madhara ya deni hili ni uchumi hafifu huku serikali ikianza kuchelewesha mishahara ya wafanyikazi wake na pesa za kaunti.

Mzee Kibaki alipostaafu, kila Mkenya alikuwa akidaiwa Sh40,000, lakini sasa kila mwananchi anadaiwa Sh137,000.

Hali pia ni mbaya hivi kwamba kwa kila Sh100 zinazokusanywa na KRA kama ushuru, Sh60 zinatumiwa kulipa madeni.

Hii imelazimisha serikali kuendelea kuwaongezea Wakenya ushuru licha ya matatizo yanayowakabili kutokana na kuzorota kwa uchumi na janga la Covid-19.

Utawala wa Mzee Kibaki ulifanikiwa kupunguza kutegemea mikopo na kuondoa Kenya chini ya minyororo ya mashirika ya IMF na Benki ya Dunia.

Bw Wainaina anasema kilichosaidia zaidi utawala wa Mzee Kibaki kujenga uchumi imara ni kudhamini demokrasia na utawala wa sheria.

Anasema chini ya utawala wake, Mzee Kibaki aliruhusu Wakenya kukosoa serikali na kutumia maoni yao kuimarisha uchumi wa nchi bila kuwatisha.

“Kibaki alikumbatia maoni ya kufaa nchi ya wakosoaji wake wakuu. Hakujibizana nao au kutumia idara za usalama kuwanyamazisha. Watu waliomtusi walitembea huru bila wasiwasi wa kukamatwa. Pia aliruhusu bunge kutekeleza majukumu yake kwa njia huru tofauti na inachofanya serikali ya Jubilee,” asema Bw Wainaina.

Mzee Kibaki pia aliruhusu upinzani ndani ya serikali yake na alichotarajia kutoka kwa maafisa wake ni utendakazi.

Kulingana na Bw Wainaina, uchumi wa nchi hauwezi kustawi iwapo serikali inapuuza utawala wa sheria ambao ni nguzo ya demokrasia.

“Wawekezaji huwa wanakosa imani na nchi ambayo serikali haiheshimu utawala wa sheria na kukiuka maagizo ya mahakama,” asema kuhusu hulka ya Rais Kenyatta na maafisa wakuu wa serikali yake kudharau maagizo ya mahakama. Kulingana na Bw Wainaina, Jubilee imewafunga vinywa Wakenya na kuwatisha ili wasiulize maswali wanapokadamizwa.

“Kibaki aliamini kuwa serikali ni ya raia na sio walio mamlakani. Aliruhusu upinzani kuendelea kukosoa serikali na kwa kufanya hivi aliweza kujua maafisa waliokuwa wakizembea kazini na hivyo kumwezesha kuchukua hatua. Hakuwa na kisasi na upinzani au waliomkosoa kwa kuwa aliheshimu demokrasia,” asema mwanaharakati Lucia Ayiela wa Kongamano la Mageuzi. Wanaharakati wanasema serikali inayoua demokrasia hufanya hivyo kwa nia ya ku maovu na udhaifu wake.

“Wanataka kuwatoza Wakenya ushuru, wakope na watumie pesa kwa njia isiyoeleweka lakini wasiulizwe maswali. Wakati wa Kibaki, Wakenya walifichua kashfa bila hofu yoyote ya kukamatwa,” asema.

Muungano wa Mashirika ya Kutetea Haki za Binadamu unasema kushuka kwa demokrasia nchini kulishika kasi 2018.

Watetezi hao wanasema ni wazi kuwa Kenya imerejea katika enzi za utawala wa mabavu, ambao ulitumbukiza Kenya katika hali mbaya ya kiuchumi miaka ya themanini na tisini. Kwa upande wake serikali inasema kwamba haki zote zina mipaka, na Wakenya hawafai kutumia uhuru wanaohakikishiwa na Katiba kukiuka sheria wakisingizia demokrasia.

WANDERI KAMAU: Uhuru, Ruto wajue dunia nzima inawatazama

Na WANDERI KAMAU

MOJAWAPO ya matukio ambayo daima yatakumbukwa na vizazi vijavyo nchini, ni ghasia za kikabila zilizotokea baada ya uchaguzi tata wa 2007.

Ni machafuko ambayo yalishangaza dunia nzima kwani Kenya ilikuwa imesifika kwa muda mrefu kama taifa linalozingatia demokrasia.Taifa letu linaheshimika sana kote duniani kutokana na uwezo wetu mkubwa na michango muhimu ambayo tumetoa katika nyanja mbalimbali.

Kwa mfano, ufanisi wetu katika riadha umetutambulisha kipekee tangu miaka ya sitin; enzi ambazo watimkaji wakongwe kama Kipchoge Keino, Moses Tanui, Naftali Temu, Douglas Wakiihuri na wengineo walikuwa waking’aa katika mashindano ya kimataifa.

Hatua hizo ndizo zilibadilisha dhana ya wengi, hasa wakoloni, wakatambua kwamba Waafrika si viumbe duni kama walivyofikiria.Wazungu walikuwa wamewadunisha Waafrika tangu karne ya 18 walipovamia bara hili, wakawateka nyara na kuwauza kama watumwa katika mabara ya Ulaya na Amerika.

Hata hivyo, michango muhimu ya Wakenya na raia kutoka nchi zingine za Afrika imegeuza kabisa fikra za Wazungu, kiasi kwamba baadhi yao walianza kubuni mikataba na nchi hizo katika nyanja mbalimbali za ushirikiano, kama vile utafiti wa masuala ya kisayansi.

Umoja wa Mataifa (UN) nao uliweka makao ya Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Mazingira (UNEP) kuwa jijini Nairobi, kutokana na imani kubwa iliyo nayo kwa Kenya.

Kwa sasa, Kenya inahudumu kwa mara ya pili kama mwanachama wa muda katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC). Hili ni baada ya kupata uungwaji mkono kutoka nchi nyingi duniani zinazoamini uwezo wake.

Hatua hizi zote zinaashiria kuwa Kenya si nchi yetu tu; bali ni taifa lililo na wajibu muhimu wa kutimiza katika ulimwengu nzima.Kinaya ni kwamba, inashangaza sisi wenyewe hatutambui hilo.

Moja ya dalili ni cheche ambazo viongozi wa kisiasa wameanza kuelekezeana kuhusiana na Uchaguzi Mkuu wa 2022. Sikitiko kuu ni kwamba miongoni mwa wale ambao wameanzisha mwelekeo huu hatari ni Rais Uhuru Kenyatta, Naibu Rais Wiliam Ruto na Kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga.

Uhalisia mwingine mchungu unaoshangaza ni kwamba Rais Kenyatta na Dkt Ruto walikuwa miongoni mwa Wakenya sita waliofunguliwa mashtaka ya uchochezi katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), jijini Hague, Uholanzi.

Mashtaka hayo ndiyo yalikuwa msingi mkuu wa Muungano wa Jubilee, waliobuni mnamo 2012 na kuahidi kuanzisha mchakato wa kuunganisha nchi.

Maswali yanaibuka: Wamesahau ahadi walizotoa kwa Wakenya? Wamesahau yaliyowakumba binafsi na familia zao baada ya mashtaka hayo?Sijui ikiwa huo ndio ukweli, lakini itakuwa sikitiko kubwa ikiwa ndivyo.

Ni sikitiko pia ikiwa wamesahau kuhusu Wakenya waliomwaga damu na wengine kuachwa bila makao kutokana na mapigano hayo.Ujumbe mkuu wa Rais Kenyatta na Dkt Ruto ni kukumbuka kuwa Kenya si yao pekee, bali ina maslahi ya watu na nchi zingine duniani. Watahadhari wanakotuelekeza!

akamau@ke.nationmedia.com

CHARLES WASONGA: Ni aibu sana Rais na Naibu wake wake kupakana tope hadharani

Na CHARLES WASONGA

ILIKUWA makosa makubwa kwa Naibu Rais William Ruto kumjibu hadharani bosi wake, Rais Uhuru Kenyatta, kufuatia kauli ya kiongozi huyo wa taifa kwamba watu kutoka jamii zingine wanapasa kupewa nafasi ya kuliongoza taifa hili 2022.

Rais Kenyatta ambaye alikuwa akihutubu Jumamosi katika kaunti ya Vihiga alipohudhuria mazishi ya mamake kiongozi wa ANC, Musalia Mudavadi, Mama Hanna Atsianzale Mudavadi, aliripotiwa kudai, kimzaha, kuwa jamii mbili za Kikuyu na Kalenjin ambazo zimewahi kutoa marais wa taifa sasa zinapasa “kutoa nafasi kwa watu kutoka jamii zingine kuongoza.”

Lakini Jumapili akihutubu katika kanisa moja mtaani Kayole Nairobi, Dkt Ruto (anayetoka jamiii ya Kalenjin) alilaani tamko hilo akisema linachochea ukabila na migawanyiko nchini, kwa imani kuwa kauli ya Rais ililenga kuvuruga ndoto yake ya kuingia Ikulu 2022.

Kimsingi, ikiwa ni kweli kwamba Rais Kenyatta alitoa kauli kama hiyo, basi alipotoka kwa sababu Katiba haina kipengele kinachosema kiti cha urais kinapasa kushikiliwa kwa mzunguko miongoni mwa makabila ya Kenya.

Isitoshe, Katiba ya sasa (katika kipengele cha 38) inalinda haki ya Wakenya kufanya maamuzi ya kuchagua viongozi wanaowataka bila kushurutishwa kwa misingi yoyote ile.

Hata hivyo, endapo Dkt Ruto alihisi kukerwa na kauli ya bosi wake kile angefanya ni kumfikia kwa njia ya simu na kuwasilisha lalama zake.

Aidha, anaweka kukutana naye katika Ikulu na kuwasilisha hisia zake kwa faraghani. Hakupasa kumjibu hadharani alivyofanya kanisani.Vilevile, hakufaa kuwaachilia wabunge na maseneta 20 walioandamana naye kumkaripia kiongozi wa taifa hadharani walivyofanya ndani ya kanisa hilo la House of Hope.

Ingawa Rais Kenyatta, kama mwanadamu, anaweza kukosea kimatamshi au kwa vitendo, Dkt Ruto kama naibu wake hafai kumkosoa hadharani. Hii ni kwa sababu afisi ya urais ni yenye heshima na taadhima kando na kwamba ni nembo na ishara ya umoja wa kitaifa.

Ni wazi kwamba Rais Kenyatta alitoa kauli hiyo kujibu propaganda ambazo zimekuwa zikienezwa na Dkt Ruto pamoja na wandani wake kwamba wakati umewadia kwa watu wa tabaka la chini, almaarufu, mahasla, kupewa nafasi ya kuliongoza taifa hili na wala sio viongozi ambao wazazi wao waliwahi kuongoza Kenya.

Tasnifu yangu ni kwamba Rais Kenyatta na Dkt Ruto wanapasa kukoma kulumbana hadharani kwani wanajiaibisha machoni pa Wakenya waliowatwika jukumu la kuwaongoza kwa kuwapa kura zao miaka ya 2013 na 2017.

Kibarua cha kuokoa UhuRuto

Na BENSON MATHEKA

JUHUDI za viongozi wa kidini za kupatanisha Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto, huenda zikakumbwa na vizingiti kutokana na misimamo ya wawili hao kuhusu masuala yaliyowatenganisha.

Wadadisi wa kisiasa wanasema Rais Kenyatta yuko njia panda kwa sababu ya ushirika wake wa kisiasa na kiongozi wa upinzani Raila Odinga, ambao Dkt Ruto hajakumbatia.

Dkt Ruto amekuwa akisema Bw Odinga anatumia handisheki kuvunja chama cha Jubilee ili kumzuia asikitumie kugombea urais 2022.

Kwa upande wake, Rais Kenyatta amekuwa akimtetea Bw Odinga akisema lengo la ushirikiano wao ni kuunganisha nchi na kupigana na ufisadi kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI), ambao Dkt Ruto amekosoa vikali.

Kulingana na wachanganuzi wa siasa, kuridhiana na Dkt Ruto kunaweza kuvunja handisheki, jambo ambalo linaweza pia kulemaza BBI.

Kulingana na mdadisi wa siasa Tom Maosa, itabidi Rais Kenyatta asawazishe kati ya maslahi ya Dkt Ruto na mipango yake na Bw Odinga.

“Kuna kizingiti kwa upande wa Rais kwa sababu kuridhiana na Dkt Ruto kunaweza kuhatarisha uhusiano wake na Bw Odinga na mpango mzima wa BBI. Kwa maoni yangu, anaweza kuvuka kizingiti hiki kwa kuhakikisha mazungumzo ya kupatana na Dkt Ruto yanahusu kufanikisha mchakato huo,” asema.

Wachanganuzi wanasema ikizingatiwa uhasama kati ya viongozi hao wawili umejikita katika chama tawala cha Jubilee na serikalini, kuna uwezekano wa wandani wa Rais na washauri wake kutochangamkia juhudi za kuwapatanisha, hasa miongoni mwa maafisa wakuu wa chama wa Jubilee na wa serikali, wakiwemo mawaziri ambao wamekuwa wakimdharau Dkt Ruto hadharani.

Baadhi yao wametumia kutengwa kwa Dkt Ruto serikalini kujipendekeza kwa Rais. Miezi miwili iliyopita, Waziri wa Mazingira Keriako Tobiko alidai Dkt Ruto ni karani tu na hafai kumkaidi Rais. Naye waziri wa Usalama Fred Matiang’i amekuwa mstari wa mbele kumhujumu Dkt Ruto kwa kutumia polisi kuvunja mikutano yake.

Naibu mwenyekiti wa chama cha Jubilee David Murathe amewahi kuapa kwamba Dkt Ruto hatakuwa rais, naye Katibu Mkuu wa chama hicho Raphael Tuju majuzi alimkemea akidai amekwepa majukumu yake.

“Hawa ni watu wa karibu sana na Rais ambao kwa njia moja au nyingine wamenufaika na uhusiano baridi kati ya viongozi hao wawili. Ikizingatiwa baadhi yao ni wandani wa Rais na wana maslahi ya kulinda, huenda wakawa kizingiti kwa juhudi za upatanishi zinazoendeshwa na viongozi wa kidini,” asema mchanganuzi wa masuala ya siasa, Benard Kamau.

Anasema Rais Kenyatta ana kibarua kwa sababu ya matakwa ya Dkt Ruto na washirika wake wa kisiasa ambao wanaweza kutumia juhudi hizo kushinikiza avunje uhusiano wake na Bw Odinga: “Akifanya hivyo, huu utakuwa mwisho wa BBI ambayo ameunga mkono.”

Mdadisi huyo anasema hii inaweza kurejesha nchi ilipokuwa imegawanyika kabla ya handisheki,” asema.

Hii inaweza kufanya hali kuwa mbaya zaidi ikizingatiwa kuwa wafadhili wa kimataifa wameanza kuwa na wasiwasi kuhusu migawanyiko ya kisiasa nchini miaka miwili kabla ya uchaguzi mkuu.

Aliyekuwa mbunge wa Mukurweini, Kabando wa Kabando, anasema Rais Kenyatta yuko katika njia panda: “Kuna uwezekano wa Uhuruto kufufuka lakini ili Rais Kenyatta kujikwamua, suluhisho ni kuachana na BBI na kuelekeza juhudi zake kufufua uchumi. Ruto hawezi kuzimwa, na Odinga hawezi kuthibitiwa,” Bw Kabando asema.

Katika hatua ya kuonyesha anayopitia Rais kwa wakati huu, washirika wa Dkt Ruto walishabikia juhudi za viongozi wa kidini.

“Sasa uchumi utakuwa thabiti kupitia handisheki ya nguvu ambayo itatangazwa hivi karibuni kati ya Uhuru na Ruto,” alisema Seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen.

Wataalamu wailaumu ICC kwa kusitisha kesi za UhuRuto

NA VALENTINE OBARA

MAHAKAMA ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) imekosolewa kwa kufanya Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake, Dkt William Ruto, kuendelea kuwa na wasiwasi hata baada ya kesi zao kusitishwa.

Wawili hao walikuwa wameshtakiwa ICC kwa madai ya kuhusika katika ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007, lakini kesi zao zikasitishwa kutokana na ukosefu wa ushahidi wa kutosha.

Katika ripoti iliyotolewa na kikundi cha wataalamu kilichoajiriwa na Baraza la Mataifa Wanachama wa ICC, almaarufu kama ASP, kuchunguza utendakazi wa mahakama hiyo, ilibainika kulikuwa na madoa kadhaa jinsi kesi za Rais Kenyatta na Dkt Ruto ziliendeshwa.

Wataalamu hao wa kisheria kutoka nchi mbalimbali waliikosoa ICC kwa kutosema wazi kama viongozi hao wawili pamoja na mwanahabari Joshua arap Sang, sasa wako huru au waendelee kujiandaa kwa kesi baadaye.

Wakati kesi zao zilisitishwa majaji walisema upande wa mashtaka, unaoongozwa na Bi Fatou Bensouda, uko huru kuwasilisha kesi upya baadaye endapo ushahidi zaidi utapatikana.

Tangu wakati huo wapelelezi wa ICC huendeleza upelelezi wao, hasa kuhusu kesi ya Dkt Ruto, humu nchini kisiri kila mwaka.

Wataalamu hao walioanza kazi yao Desemba 2019 sasa wanasema mwenendo huu si wa haki kwani kisheria, mshtakiwa anafaa kufahamishwa iwapo ana hatia au la kesi inapotamatika.

“Maamuzi haya hayaendi sambamba na hali ya kawaida ambapo uamuzi unastahili kuwa kwamba, mshtakiwa hana kesi ya kujibu au kesi itamatishwe,” inasema ripoti hiyo iliyotolewa Jumatano jioni.

Kando na suala hilo, ICC ilikosolewa kwa kutotilia maanani malalamishi ya washtakiwa kwamba upande wa mashtaka ulihujumu mashahidi ambao washtakiwa waliwategemea katika kujitetea.

Katika kesi ya Rais na naibu wake, wataalamu walikosoa afisi ya Bi Bensouda kwa kukataa kuchunguza madai kwamba washirika wake walibuni ushahidi ambao ulitegemewa kuwashtaki wawili hao.

Mawakili wa washtakiwa walikuwa wameibua malalamishi tele kwamba upande wa mashtaka ulishirikiana na mashirika ya kijamii nchini Kenya kubuni ushahidi wa uongo na kuwafunza mashahidi jinsi ya kudanganya mahakamani.

“Mahakama ilikataa kuteua mpelelezi huru kuchunguza madai hayo. Wakati wa kesi ya Kenyatta, kulikuwa na madai mazito kuhusu kuhujumiwa kwa watetezi wake na washirika wa upande wa mashtaka. Japo madai haya yaliripotiwa na mawakili wa walalamishi kwa afisi ya kiongozi wa mashtaka, hakuna hatua yoyote ilichukuliwa,” ripoti iliendelea kueleza.

Wataalamu hao walipendekeza kuwa kuendelea mbele, ICC ibuni mfumo mwafaka wa kuhakikisha malalamishi yote kuhusu hujuma za haki yanachunguzwa kikamilifu na adhabu kutolewa haraka.

Aidha, waliongeza, wakati malalamishi kama hayo yanatolewa kuhusu upande wa mashtaka, ni vyema Msajili wa Mahakama aagizwe kuajiri mpelelezi huru kisha ripoti ya uchunguzi iwasilishe ili uamuzi ufanywe.

Akipokea ripoti hiyo, Rais wa ASP Bw O-Gon Kwon alisema ripoti itafanyiwa tathmini kisha hatua zichukuliwe.

Uundaji wa kamati hiyo ya wataalamu ulitokana na malalamishi mengi ya nchi mbalimbali, hasa za Afrika kuhusu utendakazi wa ICC.Baadhi ya viongozi wa Afrika hulalamika kwamba mahakama hiyo inatumiwa kuhujumu uhuru wa utawala wao.

Mgogoro wa Sudi ulivyofichua siri ya vita vya UhuRuto

Na LEONARD ONYANGO

KIZAAZAA wakati wa kukamatwa kwa Mbunge wa Kapseret, Bw Oscar Sudi kimefichua namna uhusiano baina ya Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto ulivyodorora kwa kiasi kikubwa.

Maafisa wa Polisi wiki iliyopita walishindwa kumkamata Bw Sudi kutokana na madai kwamba walizuiliwa na maafisa wa usalama wanaolinda Naibu wa Rais.Kwa mujibu wa ripoti, maafisa hao ndio walimtorosha Bw Sudi ili kumnusuru kutoka mikononi mwa polisi.

Maafisa hao, hata hivyo, waliachiliwa huru huku polisi wakiendelea kufanya uchunguzi ili kubaini kwa nini maafisa hao wanaolinda watu mashuhuri walikuwa nyumbani kwa Bw Sudi.

Mbunge wa Kimilili Didmus Barasa alinukuliwa akisema kuwa maafisa hao walikuwa wamealikwa na Bw Sudi kwa ajili ya chakula cha jioni.

Maafisa hao walikuwa wamesindikiza Naibu wa Rais hadi nyumbani kwake katika eneo la Sugoi, Kaunti ya Uasi Gishu, kabla ya kuelekea nyumbani kwa Bw Sudi.

Chama cha ODM kikiongozwa na kinara wake Raila Odinga kimemtaka Naibu wa Rais kuwajibika na kuwaeleza Wakenya kwa nini maafisa wake walijipata nyumbani kwa mbunge wa Kapseret.

Wadadisi wa masuala ya siasa wanasema kuwa kizaazaa hicho ni ithibati kwamba Dkt Ruto amepoteza usemi ndani ya Jubilee.“Bw Sudi ni mtetezi mkuu wa Dkt Ruto na kuna uwezekano kwamba alijaribu kumwokoa mbunge huyo bila mafanikio.

“Hilo linaashiria namna naibu wa rais amepoteza ushawishi serikalini na hata hawezi kutoa amri kwa afisa yeyote wa serikali,” anasema BwGeorge Mboya , mdadisi wa siasa.

Kudorora kwa uhusiano huo kumesababisha Naibu wa Rais Ruto kuanza ‘kujitenga’ na serikali ya Uhuru Kenyatta ili kujiongezea umaarufu wa kisiasa.

Dkt Ruto amekuwa akitoa kauli zinazofanya serikali ya Rais Kenyatta kuonekana kama isiyojali masilahi ya wananchi maskini, iliyojaa ufisadi na dhuluma.Dkt Ruto, hata hivyo, atakuwa ajihusisha na miradi mizuri inayoanzishwa na serikali ya Jubilee.

Hilo lilibainika wiki iliyopita ambapo Baraza la Mawaziri liliidhinisha kubuniwa kwa hazina ya kutoa mikopo kwa wafanyabiashara wadogo walioathiriwa na janga la virusi vya corona.

Kulingana na Baraza la Mawaziri, Sh10 bilioni zitatolewa kama mikopo kwa wafanyabiashara wadogo kat yam waka huu wa fedha wa 2020/2021 na mwaka wa 2021/2022.

Baada ya kikao hicho, wanasiasa wa Tangatanga walimmiminia sifa tele Dkt Ruto wakisema kuwa uwepo wake katika Baraza la Mawaziri ndio ulisababisha serikali kuidhinisha fedha hizo zinazolenga wananchi wa mapato ya chini.

Naibu wa Rais pia anaonekana kuanza kumshambulia Rais Kenyatta moja kwa moja tofauti na hapo awali ambapo alizungumza kwa mafumbo na kuelekeza hasira zake kwa Bw Odinga.

Alipokuwa akizungumza Jumapili iliyopita mjini Kitengela, Kaunti ya Kajiado, Dkt Ruto alisema kuwa hatishiki yuko tayari kukabiliana na ‘system’- yaani watu wenye ushawishi mkubwa serkalini.

“Kuna watu wanatutisha ati wako na ‘system’, na mimi niliwaambia tuko na Mungu na tuko na wananchi. Wakuje na system na sisi tuko tayari tunawangojea,” Dkt Ruto akaambia wafuasi wake.

Naibu wa Rais pia amejitokeza na kupinga Rais Kenyatta huku akisema kuwa Mpango wa Maridhiano (BBI) unalenga kugawanya Wakenya na ni mradi wa watu kunufaisha wanasiasa wachache.

“Wakennya wanataka ajira, huduma bora za matibabu na viongozi ambao watawawezesha kujiinua kimaendeleo sio kugawanywa kwa masilahi ya watu binafsi,” akasema Dkt Ruto.

Rais Kenyatta, amekuwa akikwepa kumjibu Dkt Ruto huku akishikilia kuwa huu si wakati wa siasa.Akizungumza Alhamisi alipokuwa akizindua mradi wa Sh1.9 bilioni wa kutengeneza madawati, Rais Kenyatta alisema kuwa hana wakati wa kujihusisha bali anashughulikia maendeleo.

Naibu wa Rais amekuwa akikutana na viongozi wa madhehebu mbalimbali ili kujipatia uungwaji mkono.Ijumaa, Dkt Ruto alikutana na viongozi wa Kanisa la African Church of the Holy Spirit la Embu waliokuwa wameandamana na mbunge Maalumu Cecily Mbarire.

Baadaye alikutana na aliyekuwa mbunge wa Starehe Margaret Wanjiru ambaye pia ni kiongozi wa kanisa la Jesus Is Alive Ministries.

Wadadisi wanasema kuwa Dkt Ruto anataka kuvutia viongozi wa makanisa upande wake sawa na alivyofanya 2010 wakati wa kupinga rasimu ya katiba mpya.

Viongozi wa makanisa walikataa rasmu ya katiba wakidai kuwa ilikuwa ikiendeleza ushoga. Naye, Dkt Ruto aliipinga kutokana na kigezo kuwa ingetoa mwanya kwa watu kupokonywa mashamba yao.

Refarenda ndiyo cheti rasmi cha ‘talaka’ ya UhuRuto?

Na MWANGI MUIRURI

HUENDA refarenda iwe ndiyo barabara kuu ya kupisha utengano kati ya Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake Dkt William Ruto.

Uhusiano wao ambao kwa muda sasa umeonekana kujawa na baridi hasa katika awamu ya pili mamlakani unatazamiwa kuhitaji tu msukumo mdogo tu na usambaratike.

“Mimi binafsi nimekuwa nikisema kuna mambo ambayo hayaendi vizuri lakini sio yale ambayo hayawezi yakasuluhishwa. Kwa muda Wakenya wameshuhudia ushirika mpya ndani ya Jubilee na mambo yakifanyika tofauti na hali ilivyokuwa hapo awali, hayo yote ni sawa hata kama ni kutukanwa na wadogo wangu ndani ya serikali,”akasema Dkt Ruto Alhamisi jioni katika mahojiano na runinga moja hapa nchini.

Lakini cha kuvutia wadadisi wa kisiasa ni wakati Dkt Ruto alisema kuwa “kwa sasa hatuoni haja kuu ya mabadiliko ya Katiba ikiwa ni harakati zitakazotii maslahi tu ya wachache”.

“Hatuwezi tukakubali kuingia katika sarakasi za kuundia watu watano nafasi kuwakilisha jamii tano ndani ya serikali huku jamii hizo zingine zote zikibaguliwa,” akasema Dkt Ruto.

Msimamo huu una uzito zaidi ikizingatiwa kuwa Jumatano Rais Kenyatta alitangaza kuwa kuna haja kubwa ya kupanua serikali “pale juu” ndipo Wakenya wengi zaidi wajihisi kuwa wanamiliki serikali na ni wadau katika utawala na uchumi wa nchi wala sio watakaoshindwa kwa kura kujihisi kuwa wageni katika taifa lao.

Dkt Ruto alisema ikiwa ni Wakenya wanasema hivyo “tuko sawa lakini ikiwa ni viongozi wachache wanaosukuma hilo sisi tutabakia pale sauti ya Mkenya itakuwa.”

Hali hii ya kuviziana kati ya Rais na naibu wake inaangazia mchezo wa paka na panya ambao unaelekeza ndoa yao kuibuka na talaka hadharani na hali ya mshikemshike kisiasa iibuke kati ya wafuasi wao na hatimaye taifa liingie katika siasa propa za 2022.

Cha kuvutia mno ni sadfa ya Dkt Ruto kujitokeza katika mahojiano hayo na kukariri tu msimamo uliotolewa na wanaompigia debe Mlima Kenya ambao Jumatano usiku walikuwa katika mkahawa mmoja mjini Sagana, Kaunti ya Kirinyaga; hali inayoangazia kuwa Dkt Ruto anapanga timu yake na anajadiliana nayo mara kwa mara.

Mkutano huo uliwaleta pamoja wabunge Ndindi Nyoro, Rigathi Gachagua na Alice Wahome wakiwakilisha Kiharu, Mathira na Kandara mtawalia, John Kiarie wa Dagoretti Kusini, Kimani Ichung’wa wa Kikuyu, Francis Theuri na Moses Gakuya wa Embakasi ya Kati na Mashariki mtawalia na Wangui Ngirici wa Kirinyaga miongoni mwa wengine waliokaribisha mwandani wa Dkt Ruto Rift Valley—Oscar Sudi – mbunge wa Kapseret.

Nyoro alifahamisha Taifa Leo kuwa walikuwa wanajipiga msasa kule wametoka, walikofika na wanakoelekea kama wandani wa serikali ya Jubilee na mirengo ibuka ndani ya serikali hiyo.

“Tulijadiliana kuhusu msimamo wetu wa kumuunga mkono Dkt Ruto kwa kila hali ya siasa zinazoendelea kuchezwa dhidi yake, nafasi yetu ndani ya serikali na chama cha Jubilee na siasa za kutulenga zinazoendelea kuchezwa, vita dhidi ya ufisadi na pia mvutano ulioko kati ya maseneta kuhusu mfumo wa ugavi pesa kwa ugatuzi.”

Walisema kuwa wataendelea kushirikiana na serikali ya Jubilee na kumuunga mkono Rais Kenyatta kuafikia malengo yake ya kiutawala “lakini kwa msingi kuwa yanayoendelezwa yanawiana na masharti ya kikatiba.”

Aidha, walisema kuwa watabakia katika kila kona ya siasa ndani ya himaya ya wananchi wala sio kwa matakwa ya wachache wanaotafutiwa au wanaojitafutia makuu; huu ukiwa ni mshale wa kisiasa ukielekezewa kinara wa ODM Raila Odinga na wengine kama Gideon Moi wa Kanu, Kalonzo Musyoka wa Wiper na Isaac Ruto wa Chama cha Mashinani ambao wako ndani ya Jubilee sasa kama washirika wa kiutawala na wanaochambuliwa kuwa wanajengwa kama mrengo wa kugombea urais 2022 dhidi ya Dkt Ruto.

Kuhusu refarenda, walisema watasubiri kuona kielelezo kitakachotolewa na wakishachambua waone ni matakwa ya wananchi yanayopendekezwa, na wananchi wenyewe waseme ni maoni yao, basi Dkt Ruto na wafuasi wake sugu watatii.

“Ikigundulika Wakenya hawatakuwa wamewakilishwa katika mapendekezo hayo na iwe ni mradi wa kundi la wachache kutuhadaa eti ni refarenda ya kitaifa ambayo itafadhiliwa na rasilimali za umma, basi ule upinzani tutazua haujawahi kushuhudiwa hapa nchini,” akasema.

Kuhusu hali kwamba Rais huenda apenyeze ajenda yake ya kung’oa mizizi ya Dkt Ruto kutoka serikali yake katika mabadiliko ya baraza la mawaziri yanayonukia, Nyoro alisema “sisi tushazoea.”

“Tumetengwa ndani ya Jubilee, tukatimuliwa kutoka nyadhifa bungeni; yaani madharau siku hizi ndiyo mengi kutoka kwa wanaojifanya ndio wawakilishi wa Rais katika chama na serikali. Sasa hicho kingine kinachoweza letwa kitushtue ni kitu gani?” akahoji Nyoro.

Walisema kuwa chama cha Jubilee kimetekwa nyara na matapeli, wakisistiza kuwa njia ya kugawa rasilmali kwa ugatuzi iwe ni ya kuunganisha Wakenya na kuwapa haki ya ushuru wao bila ubaguzi.

Nyoro alisema kuwa kubakia ndani ya Jubilee ndilo lengo kuu lakini “ikishindikana, kuna mianya tele ya kusaka utulivu na nafasi ya kukimbizana na ndoto zetu za kisiasa.”

Walisema kuwa kwa sasa “hali yetu ni ile ile tu ya kuyapa masuala yanayoendelea kuibuka ndani ya serikali macho tu, msimamo wetu ukiwa ni kuunga mkono yale mema lakini mabaya tumenyane nayo kwa wakati ufaao.”

Uhuru na Ruto wapeleka vita vyao vya ubabe katika makanisa

VIONGOZI wa makanisa wamejipata katikati ya ubabe wa kisiasa baina ya Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto.

Rais Uhuru Kenyatta ameanzisha harakati za kupitia kwa viongozi wa makanisa na wazee kuzima ushawishi wa Dkt Ruto katika maeneo ya Mlima Kenya, Bonde la Ufa na Magharibi.

Naibu wa Rais amekuwa akitumia viongozi wa makanisa kupenya katika eneo la Mlima Kenya ambayo ni ngome ya Rais Kenyatta.

Naibu wa Rais pia amekuwa akijaribu kujipendekeza kwa vijana na kujionyesha kama ‘mwakilishi’wa maskini ili kujipatia uungwaji mkono miongoni mwa Wakenya wa mapato ya chini.

Wadadisi wanasema kuwa kwa kujifanya ‘maskini’, Dkt Ruto analenga kuwafanya Rais Kenyatta, kinara wa ODM Raila Odinga na Seneta wa Baringo Gideon Moi kuonekana kama watoto wa matajiri wasiojali masilahi ya watu wa mapato ya chini.

Kulingana na Kiranja wa Wengi katika Seneti Irungu Kang’ata, Rais Kenyatta amekuwa akiendeleza kampeni ya chini kwa chini kuwafikia viongozi wa makanisa na wazee katika eneo la Mlima Kenya ili waunge ajenda yake ya maendeleo.

Rais Kenyatta, kulingana na duru za kuaminika, alichukua hatua hiyo kutokana na ukweli kwamba umaarufu wa Dkt Ruto umekuwa ukiongezeka katika eneo la Mlima Kenya licha ya kiongozi kuonyesha wazi kuwa hana haja naye kisiasa.

Rais Kenyatta pia amekuwa akitumia mmoja wa mawaziri kutoka Bonde la Ufa kuwafikia viongozi wa makanisa na wazee ili kuwashawishi kuunga mkono handisheki baina yake na kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Rais Kenyatta analenga kuondoa madai ambayo yamekuwa yakienezwa na wanasiasa kutoka Bonde la Ufa kwamba handisheki imetenga jamii ya Wakalenjin.

Katika eneo la Magharibi, Rais Kenyatta amekuwa akitumia Gavana wa Kakamega na Waziri wa Ugatuzi Eugine Wamalwa kufikia viongozi wa makanisa na wazee.Dkt Ruto alijitokeza na kuwa mtetezi wa makanisa, maeneo ya ibada yalipofungwa kufuatia janga la virusi vya corona.

Naibu wa Rais amekuwa akikutana na viongozi wa kidini kutoka eneo la Mlima Kenya, hatua ambayo imetia tumbojoto kambi ya Rais Kenyatta.

Alhamisi, Dkt Ruto alikutana na viongozi wa Kanisa la Africa Inland (AIC) kutoka Kaunti ya Baringo ambayo ni ngome ya kiongozi wa Kanu Bw Moi.

Katika mkutano huo, Naibu wa Rais aliahidi kuwasaidia kujenga hoteli inayoendelea mtaani Karen, Nairobi.

“Ninaahidi kusaidia kanisa ili kuwawezesha kujikimu kimaisha kufuatia hali ngumu ambayo imesababishwa na janga la virusi vya corona,” akasema Dkt Ruto kupitia akaunti yake ya Twitter.

Siku hiyo hiyo, Naibu wa Rais alikutana na viongozi wa Kanisa kutoka Kaunti za Kiambu, Murang’a na Laikipia ambazo ni ngome ya Rais Kenyatta.

Viongozi hao wa makanisa waliandamana na mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria ambaye ni mwandani wa Dkt Ruto.

JAMVI: Ukabaila ulivyowapasua UhuRuto

Na MWANGI MUIRURI

IMEIBUKA kuwa shinikizo za kibiashara, ukabila na unabii wa Mugo wa Kibiru wa Karne ya 18/19 ndio kiini cha utengano wa sasa wa Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake Dkt William Ruto.

Kwa mujibu wa wachanganuzi, mikutano ya mabwanyenye wa jamii ya Agikuyu pamoja na mabaraza ya wazee na Rais Uhuru yalimwekea presha za kuchukulia suala la uchumi wa Mlima Kenya pamoja na ushawishi wa eneo hilo kisiasa kiasi kwamba Dkt Ruto alitambuliwa kama asiye na uwezo wa kuyalinda maslahi hayo.

Katika mikutano hiyo ambayo ilianza punde tu baada ya Rais Uhuru kuchaguliwa mwaka wa 2013, makundi hayo mawili yalikuwa na wasiwasi kwamba Dkt Ruto alikuwa ametunukiwa urithi wa urais mapema sana na pia kwa urahisi bila kuzingatia masuala nyeti ya kijamii eneo la Mlimani.

“Ni katika mikutano hiyo ambapo Rais Uhuru alikumbushwa kuhusu unabii wa mwendazake Mzee Kibiru ambaye ameorodheshwa katikia kumbukumbu za jamii hiyo akisema kuwa “Urais wa Kenya baada ya mwanzilishi hayati Mzee Jomo Kenyatta (1963-1978) utamwendea mtu mwingine wa jamii ndogo (Daniel Moi 1978-2002) na ukisharejea kwa Agikuyu (Rais Mwai Kibaki na Uhuru (2002-2022), hautawahi kutoka huko tena,” afichulia Jamvi la Siasa mmoja wa aliyeshiriki mikutano hiyo.

Kwa mujibu wa aliyekuwa mkuu wa mikoa kadhaa kwa muda mrefu Joseph Kaguthi, “Rais alikumbushwa kuwa yalikuwa makosa kumuahidi Dkt Ruto urais kwa urahisi na pia mapema hata kabla ya majadiliano ya kina kutekelezwa kati ya wadau wa kijamii.”

Mwaka wa 2013 na 2017 Rais Uhuru alinukuliwa kwa kiwango kikuu akitangaza kuwa angetawala kwa kipindi cha miaka 10 na kisha Dkt Ruto achukue usukani kwa kipindi cha miaka 10.

Kaguthi aliambia ukumbi huu kuwa wandani wengi wa Rais hawakuridhishwa na suala hilo kwa kuwa hisia za urais wa Mzee Daniel Moi wa miaka 24 za jinsi alivyofukarisha eneo hilo zilikuwa zingalipo na machungu yake.

“Rais alikumbushwa kuwa wakati urais ulipowatoka watu wa eneo la Mlimani, hata tekenye/funza ziliwavamia wenyeji kutokana na umasikini na hawakuwa tayari kuona urais ukiwatoka kwa urahisi jinsi Uhuru alikuwa akiupokeza Ruto,” asema.

Rais anasemwa kuwa alikubaliana na ushauri huo na ndipo akawaagiza wote wasubiri Dkt Ruto awasaidie kujipa awamu ya pili Ikuluni na baada ya hapo mikakati iwekwe ya kulinda maslahi hayo ya kibiashara (kikabaila), kikabila na kiuchumi.

Na ndipo baada ya uchaguzi wa 2017 ambapo baada ya Dkt Ruto kumsaidia Uhuru kushinda, masaibu ya uhasama, kutengwa na kudharauliwa yakaanza kutekelezwa hadi sasa ambapo wandani wake wametimuliwa kutoka kwa nyadhifa za hadhi katika kamati za bunge na pia wakitengwa kutoka makao makuu ya chama cha Jubilee.

Kwa mujibu wa mbunge wa Kiharu, Bw Ndindi Nyoro, maslahi hayo ya ukoloni mamboleo yakitetewa na mabwanyenye wenye ukwasi mkuu nchini kutoka Mlima Kenya yalichochea pia uhasama kati ya Rais na Dkt Ruto.

“Tunaongea kuhusu wafanyabiashara ambao haja yao kuu ni pesa katika kila kona ya maisha yao hapa duniani. Hawana fikira zozote za mwananchi wa kawaida na vile angetaka kuishi maisha yake ya kisiasa na kiuchumi. Kwao, maisha ya watu ni ya kuchuuzwa pesa,” asema.

Anasema mabwanyenye hao walimwendea Rais Uhuru na njama fiche kuwa ni lazima angeacha taifa hili katika mikono inayoaminika kuwa haitasambaratisha biashara zao kupitia njia za kupora na kuhangaisha.

Hapo ndipo kulizinduliwa njama za kumwangazia Dkt Ruto kama mwizi na mnyakuaji ili Rais aelekeze vitengo vya kupambana na makosa ya jinai na pia ufisadi dhidi ya Dkt Ruto.

“Nia kuu ya mabwanyenye hao ilikuwa kupenyeza biashara zao katika ngome nyingine za nchi hii kwa kuwa tayari wamejipenyeza Mlima Kenya. Kwa kuwa Raila Odinga ndiye mwanasiasa anayeorodheshwa wa pili katika uwezo wa kuwaleta pamoja raia wengi kwa mrengo wake wa kisiasa, wakamshawishi Rais amkumbatie.”

ndio awasaidie kupenya maeneo yanayoorodheshwa kama ngome zake. Ndio sababu unapata kwamba mabweanyenye wengi wa Mlima Kenya hujumuika katika siasa za Raila,” akasema.

Aidha, mabaraza ya wazee yalimkumbusha Rais kuwa alikuwa akifanya makosa kwa kumtwika DP Ruto makuu ya kiserikali bila ya kuzingatia masilahi ya Mlimani.

Kwa mujibu wa Mwakilishi wa wanawake wa Murang’a Bi Sabina Chege, kuliibuka siasa za “ni nani amejengwa katika Mlima Kenya ili hata ikiwa Dkt Ruto angeibuka na urais, asimamie masilahi ya Mlimani katika serikali hiyo.”

Bi Chege anasema kuwa “Dkt Ruto mwenyewe ako na viungo vyake thabiti, Raila ako na wandani wake aliowajenga na pia maeneo mengine yako na wao ambao wanatambulika kama wawakilishi wao katika hali za kisiasa 2022.”

Anahoji ni kwanini Mlima Kenya hakuna amejengwa na Rais na ndipo, Mbunge wa Gatanga Bw Nduati Ngugi anafichua, kulizuka haja ya kumjenga msimamizi wa Mlimani katika siasa za 2022.

“Hapo ndipo unapata kwa sasa tukiwa mbioni kumweka aliyekuwa mbunge wa Gatanga, Peter Kenneth katika siasa za urithi. Ni lazima sasa tuwe na atakayetuwakilisha katika siasa hizo za 2022. Pia, ni katika hali hii ambapo kumeibuka haja kubwa ya kusukuma mpango wa, na ripoti ya, maridhiano (BBI) ili serikali ipanuliwe pale juu na kuwe na vyeo vya kugawanwa kulingana na kura za kimaeneo,” asema.

Aliyekuwa mbunge wa Maragua, Elias Mbau anakiri kwamba “rais ameshinikizwa kuona kwamba alikuwa amenoa kuahidiana urais kwa urahisi hivyo na sasa tuko katika mkondo wa kurekebisha hali. Hatuko na Dkt Ruto ikiwa hatakubali kwanza kura zetu 8 milioni haziwezi zikamwendea ndio aongeze zake 2 milioni na kisha awe rais ambaye hata hajatwambia atatupa nini kama fidia ya kura hizo.”

Anasema kuwa masuala hayo yote ndiyo yamechangia uhasama wa kimaoni kati ya Rais Uhuru na Dkt Ruto “lakini sio eti tuna shida na mtu yeyote, bali tunataka tu eneo la Mlima Kenya lilindwe lisijipeleke kwa ndoa ya kisiasa 2022 ambayo itarejesha funza katika maisha ya wenyeji kupitia utawala wa kutoka nje ya Mlima Kenya.

ICC yazua baridi mpya kwa UhuRuto

Na VALENTINE OBARA

WASIWASI kuhusu kufufuliwa kwa kesi dhidi ya Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto kuhusu ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa 2007 katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), umeibuka upya.

Hii ni baada ya kufichuka kuwa aliyekuwa wakili wa waathiriwa wa ghasia hizo, Fergal Gaynor ana nafasi bora zaidi kuchukua mahali pa Bi Fatou Bensouda, ambaye anatarajiwa kukamilisha hatamu yake Juni 2021.

Tayari Kenya imepinga orodha ya walioteuliwa kuwania wadhifa huo ikisema mtu mmoja anapendelewa.

Katika barua iliyofichuliwa Jumatano, Balozi wa Kenya nchini Uholanzi ambako ni makao makuu ya ICC, Bw Lawrence Lenayapa, aliambia mahakama hiyo kwamba Kenya inapinga majina ya walioteuliwa kumrithi Bi Bensouda.

Ijapokuwa Bw Lenayapa hakutaja mteuliwa ambaye Kenya inaamini anapendelewa kuwa mkuu mpya wa mashtaka, wataalamu wa sheria za kimataifa wanasema ni wazi Kenya ina wasiwasi endapo Bw Gaynor atamrithi Bi Bensouda.

Kwa msingi wa kuwakilisha waathiriwa wa ghasia za baada ya uchaguzi nchini, Bw Gaynor ana ufahamu mkubwa kuhusu kesi zote za Kenya.

Ijapokuwa kesi za Rais Kenyatta na Dkt Ruto zilisitishwa kwa madai kwamba hapakuwa na ushahidi wa kutosha , majaji wa ICC walitoa fursa kwa Afisi ya Kiongozi wa Mashtaka (OTP) kuzifufua tena endapo wapelelezi wataridhishwa kwamba wamepata ushahidi mpya ulio na uzito.

Wasiwasi wa Kenya ni kuwa iwapo Bw Gaynor atapewa kazi hiyo, kuna uwezekano mkubwa wa kufufua kesi dhidi ya Rais Kenyatta na Dkt Ruto, ikizingatiwa alikuwa wakili wa waathiriwa wa ghasia za 2007/08.

Bw Mark Kersten, ambaye ni mtaalamu wa sheria za kimataifa, alisema wasiwasi wa Kenya hauhusu utaalamu wa watu walioteuliwa kujaza nafasi ya Bi Bensouda mbali kesi kufufuliwa.

“Kesi zile za awali hazifai kutumiwa kama kigezo cha kuamua ufaafu wa wakuu wa mashtaka wanaoteuliwa. Naamini malalamishi ya Kenya yametokana na kuwa Morris na Gaynor walihusika katika kesi za Kenya. Wale walioshtakiwa bado wako mamlakani na wana wasiwasi kuhusu uwezekano wa ICC kufufua kesi za Kenya,” akasema.

Ripoti za kila mwaka kutoka kwa afisi ya Bi Bensouda huonyesha kwamba, licha ya kesi kusitishwa, wapelelezi wa ICC bado huzuru Kenya mara kwa mara kuendeleza ukusanyaji wa ushahidi mpya kuhusu kesi za ghasia zilizoua watu zaidi ya 1,300 na kuacha maelfu wengine bila makao hadi leo hii.

Mnamo Januari 2020 Dkt Ruto alisema anafahamu kuhusu mipango ya kufufua kesi hizo, tena akadai ni kati ya njama za kuzima maazimio yake ya kumrithi Rais Kenyatta ifikapo mwaka wa 2022.

Hata hivyo, ICC ilipuuza madai yake ikasema uamuzi wa korti mnamo 2016 ulikuwa wazi kwamba kesi zinaweza kufufuliwa ushahidi ukipatikana, na shughuli za mahakama hazifai kuingiziwa siasa.

Kando na Bw Gaynor, wengine walioteuliwa ni Bi Susan Okalany kutoka Uganda, Bw Richard Roy ambaye ni raia wa Canada na Bw Morris Anyah wa Nigeria, ambaye pia aliwakilisha waathiriwa wa ghasia za Kenya katika ICC kwa muda mfupi.

Mtaalamu wa sheria za kimataifa, Bw Astrid Coracini, alieleza kuwa ni desturi katika mashirika ya kimataifa kwamba nyadhifa kubwa hushikiliwa kwa mzunguko kutoka kwa ukanda mmoja hadi mwingine, hali inayomweka Bw Gaynor katika nafasi bora zaidi kupata kazi hiyo.

Hivyo basi, kutokana na kuwa Bi Bensouda ni Mwafrika aliye raia wa Gambia, itakuwa vigumu kushawishi mataifa kumchagua mwafrika kwa mara nyingine kumrithi.

Kwa upande mwingine, Naibu Mkuu wa Mashtaka aliye mamlakani kwa sasa ni raia wa Canada, Bw James Stewart, kwa hivyo haitawezekana kumchagua Bw Roy kujaza nafasi ya mkuu wa mashtaka.

JAMVI: Vita vya ubabe kati ya Uhuru na Ruto vyahamia Magharibi

Na LEONARD ONYANGO

VITA vya ubabe wa kisiasa baina ya Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto sasa vimehamia katika eneo la Magharibi baada ya viongozi hao kugawana wanasiasa wa eneo hilo.

Ubabe huo ulijitokeza wazi Ijumaa ambapo kiongozi wa chama cha Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi na mwenzake wa Ford Kenya Moses Wetang’ula pamoja na wabunge wapatao 20 kutoka Magharibi kuandaa mkutano wa wanahabari na kumshambulia Rais Kenyatta.

Walidai kuwa Rais Kenyatta ametelekeza ukanda wa Magharibi na amekuwa akielekeza miradi yote ya maendeleo katika eneo la Mlima Kenya.

Kulingana na duru za kuaminika, viongozi hao wa Magharibi walihutubia wanahabari baada ya baadhi yao kukutana na Dkt Ruto.

Naibu Rais Ruto alikiri kwamba alikutana na wanasiasa wa chama cha Ford-Kenya na ANC afisini kwake katika mtaa wa Karen, Nairobi.

“Tulifanya majadiliano kuhusu miradi ya maendeleo nchini na viongozi wa Magharibi kutoka chama cha Jubilee, Ford Kenya na ANC,” akasema Dkt Ruto kupitia ukurasa wake wa Twitter.

Kulingana na Wetang’ula, wabunge na maseneta 27 kutoka Magharibi waliandaa mkutano kujadili suala la maendeleo katika ukanda wa Magharibi kabla ya kuhutubia wanahabari.

Miongoni mwa waliohudhuria mkutano huo ni mbunge Charles Gimose (Hamisi), Petronila Were (Seneta Maalumu) Dan Wanyama (Webuye Magharibi), Justus Murunga (Matungu), Injendi Malulu (Malava), Janet Nangabo (Mwakilishi wa Kike, Tans Nzoia), Mwambu Mabonga (Bumula) na John Waluke (Sirisia).

Wengine ni Chris Wamalwa (Kiminini), Benjamin Washiali (Mumias Mashariki), Alfred Agoi (sabatia), Sakwa Bunyasi (Nambale), Tindi Mwale (Butere), Didmus Barasa (Kimilili), Catherine Wambilianga (Mwakilishi wa Kike, Bungoma), Ayub Savula (Lugari), Omboko a (Emuhaya), Ferdinand Wanyonyi (Kwanza) na Edward Oku Kaunya wa Teso Kaskazini.

“Bajeti iliyosomwa Alhamisi na waziri wa Fedha, Ukur Yatani, haikutenga mradi wowote kwa ajili ya eneo la Magharibi. Sekta ya sukari imesambaratika. Sekta za pamba, mahindi na kahawa zimeporomoka,” akasema Bw Wetang’ula.

“Benki ya Dunia iliipa Kenya mabilioni ya fedha kuinua sekta ya kahawa. Lakini Rais Kenyatta amepeleka fedha zote katika eneo la Mlima Kenya na kuacha eneo la Magharibi ambalo linakuza pamba,” akaongezea.

Bw Wetang’ula alidai kuwa fedha zilizotengewa kilimo cha pamba zimewekwa katika utanzu wa serikali badala ya kuwapelekea wakulima.

Bw Mudavadi alimshutumu Rais Kenyatta na Gavana wa Kakamega, Bw Wycliffe Oparanya kwa ‘kuwahadaa’ wakazi wa eneo la Magharibi kuhusu ufufuaji wa sekta ya sukari.

“Rais Kenyatta alibuni jopokazi lililochunguza kiini cha kuporomoka kwa sekta ya sukari katika eneo la Magharibi. Jopo hilo lililoongozwa na Gavana Oparanya, lilitoa ripoti yake na imefichwa wala hakuna chochote kinachoendelea,” akadai Bw Mudavadi.

Hiyo si mara ya kwanza kwa Naibu Rais kukutana na viongozi wa vyama hivyo viwili vyenye ufuasi mwingi kutoka magharibi mwa Kenya. Mnamo Juni 1, 2020, viongozi wa vyama hivyo walikutana nyumbani kwa Dkt Ruto mtaani Karen.

Watatu hao walikutana kabla ya Dkt Ruto kuelekea katika Ikulu kwa ajili ya sherehe ya Madaraka. Siku hiyo, Seneta Wetang’ula na Bw Mudavadi walienda kufanya kikao na wanahabari ambapo walimshutumu Bw Odinga kwa kupanga njama ya kujaribu kusambaratisha chama cha Ford Kenya ambacho sasa kinakumbwa na mvutano.

Dkt Ruto, Bw Wetang’ula na Bw Mudavadi wamekuwa wakiunda mpango wa kuanzisha kampeni ya kumaliza ushawishi wa Bw Odinga katika eneo la Magharibi kwa kumtaja kama msaliti na mlaghai wa kisiasa aliyetelekeza watu wa eneo hilo.

Viongozi hao walimshambulia Rais Kenyatta na Gavana Oparanya, Alhmaisi, siku moja baada ya Bw Odinga kukutana na viongozi wa Magharibi na Nyanza kujadili jinsi ya kuboresha sekta ya sukari ambayo imekuwa ikidorora kila uchao.

Viongozi waliokutana na Raila ni magavana Oparanya, Sospeter Ojaamong (Busia), Obado Okoth (Migori), Prof Anyang’ Nyong’o, mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (Eala) Oburu Odinga na Seneta wa Kakamega, Bw Cleophas Malala.

Rais Kenyatta amekuwa akitumia Bw Odinga, Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi (Cotu) Francis Atwoli, Gavana Oparanya na Waziri wa Ugatuzi, Bw Eugine Wamalwa kupenya katika eneo la Magharibi.

Katika mkutano wa viongozi wa Magharibi uliofanyika nyumbani kwa Bw Atwoli katika Kaunti ya Kajiado, Bw Oparanya na Wamalwa waliteuliwa kuwa wawakilishi wa jamii ya Waluhya watakaozungumza na serikali ili kupeleka miradi ya maendeleo katika eneo la Magharibi.

Duru zinasema kuwa Rais Kenyatta alimua kutenga Bw Mudavadi na Wetang’ula baada ya kukataa kushirikiana na serikali huku nchi ikijiandaa kwa kura ya maamuzi kurekebisha Katiba kwa kuzingatia mapendekezo yaliyomo katika ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI).

Kulingana na duru za kuaminika, Naibu wa Rais, Bw Mudavadi na Seneta Wetang’ula wanaelekea kuafikiana kubuni kamati ambayo itatafuta nani atakuwa mwaniaji-mwenza wa Dkt Ruto mwaka wa 2022.

Lakini wadadisi wanaonya kuwa iwapo Dkt Ruto atachukua mwaniaji-mwenza wa urais kutoka eneo la Magharibi huenda akapoteza kura katika eneo la Mlima Kenya.

“Wafuasi wa Dkt Ruto katika eneo la Mlima Kenya huenda wakamkimbia ikiwa atachukua mwaniaji-mwenza kutoka eneo tofauti,” anasema wakili Felix Otieno.

UhuRuto warejelea ‘urafiki’ wao

CHARLES WASONGA na SAMMY WAWERU 

RAIS Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto Jumatatu walijizatiti kuonyesha kuwa ukuruba kati yao ungalipo walipovalia mavazi yanayofanana wakati wa maadhimisho ya Sherehe za 57 za Siku Kuu ya Madaraka Dei.

Kutokana na janga la ugonjwa hatari wa Covid-19 sikukuu hiyo ya kitaifa iliadhamishwa kwa namna ya kipekee katika Ikulu ya Nairobi ambapo ilihudhuria na wageni wachache waalikwa.

Licha ya uwepo wa uhasama kati ya vinara hao wawili wa Jubilee na ambao umepelekea Rais Kenyatta kuwapokonya wandani wa Dkt Ruto nyadhifa za uongozi katika seneti, Jumatatu wawili hao walionekana wakicheka pamoja.

Isitoshe, walikuwa wamevalia mavazi yanayofanana; suti nyeusi, shati nyeupe, viatu vyeusi na tai nyekundu.

Wakenya walishangazwa na mavazi ya Rais Kenyatta pamoja na Dkt Ruto wengi wakisema haikuwa sadfa bali ni jambo ambalo walipanga. Lengo hapa lilikuwa kuonyesha umma kwamba “bado tuko pamoja kama zamani” licha ya uhasama unaotokota ndani ya Jubilee.

Licha ya uhusiano wa Rais na Naibu Rais kuonekana kuwa na doa, picha ya wawili hao wakipiga gumzo na kuzua ucheshi imezua mdahalo mkali mitandaoni.

“Inachanganya kama hesabu ya wagonjwa wa Covid – 19. Kuna waliopata afueni na kupona na maafa kadhaa kuripotiwa, ila hesabu ni ileile haipunguzi,” Franklin Omwembula akaeleza kwenye mtandao wa Facebook.

Wawili hao kuonekana pamoja wakizungumza na kucheka Ikuluni, wachangiaji wa mitandao wanahoji ni kitendawili kisichokuwa na mteguzi, isijulikane walichokuwa wakijadili. “Ni mtihani usio na majibu. Niliacha kuunga yeyote mkono kwa kuwa utapata mshtuko wa moyo bure tu,” Wilson Kimuyu akachangia.

Kulingana na Esther Wangari, wanasiasa nchini hawana msimamo na si maadui, akishauri Wakenya kupevuka na kufumbua macho, wawe na hekima na kudumisha amani kila wakati.

Katika hotuba ya Naibu Rais katika maadhimisho ya Madaraka Dei 2020, Dkt Ruto alieleza kuwa na Imani na serikali ya Jubilee chini ya kigogo wake Rais Uhuru Kenyatta, hasa katika mikakati iliyowekwa kufanya maendeleo na pia kuangazia janga la corona. Baada ya kumkaribisha Rais, Rais Kenyatta alitambua kuwepo kwa Dkt Ruto, “Asante William”.

Wakati akihitimisha hotuba yake, huku akisihi wananchi kuzingatia mikakati na taratibu zilizotolewa na wizara ya afya kuzuia msambao wa Covid – 19, Rais Kenyatta alisisitiza maelezo ya Ruto akimtaja “vile Naibu wa Rais amesema” katika mchakato wa kudhibiti maenezi.

Baadhi ya Wakenya wanahisi, viongozi hao wanajua mahesabu wanayocheza. “Hawa watu huwa pamoja. Baba (akimaanisha Raila Odinga) hana bahati,” Khadasia Mavindi, akachangia akitoa hisia zake kuhusu picha ya Rais na Naibu wake kuonekana wakitangamana na kuzua ucheshi.

“Sote tunataka kuona Kenya iliyoungana. Wanaoshabikia utengano wakome, tuungane tufanye maendeleo,” Elijah Ndirangu akaeleza, Festus Mutwol akiongeza kuwa viongozi hao wawilili wanapaswa kuonyesha umoja wa aina hiyo ili Kenya isonge mbele kimaendeleo.

Baada ya gumzo, Rais Kenyatta na Naibu wake waliandamana na kuingia Ikulu.

Itakumbukuwa kuwa ni wakati wa muhula wa kwanza wa uongozi wa Jubilee ambapo wawili hao walipenda kujitokeza katika Ikulu wakiwa wamevalia mavazi yanayofanana, haswa Rais alitoa tangazo muhimu kwa taifa.

Lakini kuanzia mapema mwaka huu, imekuwa nadra zaidi kwa Rais Kenyatta na Dkt Ruto kuonekana hadharani pamoja. Isitoshe, inasemekana kuwa Naibu Rais amekuwa akikosa kuhudhuria baadhi ya mikutano ya Baraza la Kitaifa la Usalama (NSC) kuzunguzia suala la Covid-19.

Mnamo Aprili mwaka huu Naibu Rais alisema kuwa yeye na Rais hawapasi kuwa pamoja, wakati mmoja, kwa sababu ni “hatari kwa usalama,” kutokana na janga la Covid-19.

Lakini Jumatano katika Ikulu ya Nairobi Rais Kenyatta na Dkt Ruto walikaa katika jukwaa moja japo kwa umbali wa mita moja na nusu, kulingana na kanuni ya kuzuia kuenea kwa maambukizi ya Covid-19.

Akasema Dkt Ruto: “Chini ya uongozi wako, serikali itachukua hitajika ya kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huu huku tukijiandaa mwelekeo mpya wa maisha.”

Nimefika mwisho!

Na CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta amemnyooshea kidole cha lawama naibu wake William Ruto kama kikwazo chake katika kutimiza ahadi alizowapatia Wakenya.

Ingawa hakumtaja Dkt Ruto moja kwa moja, Rais Kenyatta kwenye mahojiano na gazeti la Daily Nation alionyesha kuvunjika moyo na naibu wake kwa kukosa kuunga mkono utekelezaji wa ajenda zake, na badala yake kuanza kampeni za mapema za kumrithi 2022.

“2019 yote nilikuwa nikiwasihi watu: ‘Tafadhalini acheni tuangazie Ajenda Nne Kuu kwanza, kwani wakati wa siasa bado’… Siwezi kuendelea kubembeleza watu. Sina muda!” akasema Rais Kenyatta.

Mwaka 2019 Rais alieleza kukasirishwa na kundi la ‘Tangatanga’ linalojumuisha wanaounga azma ya Dkt Ruto kuwania urais 2022, kwa kutumia muda mwingi kwenye ziara maeneo mengi ya nchi wakimpigia debe.

“Usikubali matarajio ya kesho yakuzuie kufanya mambo ya leo kwa sababu unachofanya leo ndicho kitaamua utakapokuwa kesho,” akasema Rais akionekana kumlenga Dkt Ruto kwa kuanza mapema siasa za kumrithi.

Kwenye mahojiano hayo, Rais Kenyatta alionekana kumlimbikizia lawama Naibu Rais kuhusu kufifia kwa kasi ya utekelezaji wa Ajenda Nne Kuu na vita dhidi ya ufisadi.

“Iwapo hutaki kuunga mkono miradi, ni sawa! Unaweza kwenda kufanya mambo mengine,” akasema Rais Kenyatta.

“Ikiwa unahisi huwezi kufanya kazi kufanikisha ajenda zangu, mbona usiondoke na uniache niweke mtu ambaye yuko makini katika kunisaidia kutimiza ahadi nilizowapa Wakenya 2017 na 2013? Kama unahisi hujatosheka, uko huru kufanya mambo mengine yote unayotaka,” akaeleza.

“Ninataka kufanya kazi na watu ambao hawapingi ajenda zangu kwa Wakenya. Ninataka watu ambao wataunga mkono ajenda hizo. Katika demokrasia, iwapo hufurahishwi na jinsi kiongozi anavyoelekea, basi! Hakuna lingine,” akaeleza Rais.

Akaongeza: “Kuna mambo ambayo niliwaahidi Wakenya uwanjani Kasarani nilipoapishwa. Niliahidi nitatimiza Ajenda Nne Kuu na bado niko kwenye mkondo huo. Pia nilisema nitamaliza ufisadi nchini.”

Ajenda Nne Kuu alizotangaza Rais alipoapishwa kwa muhula wa pili mnamo 2017 ni makazi, viwanda, afya na chakula. Lakini kufikia sasa hakuna hatua kubwa zilizopigwa huku ikibaki miaka miwili pekee Rais Kenyatta kung’atuka madarakani.

Msukumo wa vita vya ufisadi pia umefifia.

Kulingana na mahojiano na Daily Nation, Rais Kenyatta alionyesha mtazamo kuwa naibu wake alizingatia zaidi azma yake ya kisiasa badala ya kuunga mkono ajenda ya bosi wake.

Rais alionyesha dalili za mwanzo za kupoteza imani na Dkt Ruto mwaka 2019 alipomwondoa kama msimamizi mkuu wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kukabidhi wajibu huo kwa Waziri wa Usalama, Fred Matiang’i.

Kwa miezi kadhaa sasa Dkt Ruto pia hajakuwa akihudhuria hafla katika Ikulu wala mikutano ya Baraza la Kitaifa la Usalama ambapo ni mwanachama.

Wakati Rais Kenyatta alipotangaza vita dhidi ya ufisadi, Dkt Ruto alikosoa jinsi mchakato huo ulivyokuwa ukiendeshwa akisema ulionekana kulenga wandani wake kisiasa.

Dkt Ruto pia amekwaruzana na bosi wake kwa kupinga Mpango wa Maridhiano (BBBI) na handisheki kati ya Rais Kenyatta na Kiongozi wa ODM Raila Odinga, akidai waziri huyo mkuu wa zamani ana nia ya kuvunja Jubilee na kuingia serikalini kwa njia za mkato.

“Nasikita kuwa ninapojaribu kuunganisha Kenya, baadhi ya watu wanaona kama ninawatenga. Simpigi vita mtu yeyote. Ninawafanyia kazi Wakenya wote milioni 47,” akasema Rais Kenyatta.

Katika mchakato unaoendeshwa na Rais dhidi ya Dkt Ruto, wandani wake wameanza kuondolewa kwenye nyadhifa za Seneti na Bunge la Kitaifa.

Katika Seneti wandani wa Naibu Rais waliolishwa sakafu ni Kipchumba Murkomen (Kiongozi wa Wengi), Kithure Kindiki (Naibu Spika) na Susan Kihika (Kiranja wa Wengi) kati ya wengine walioondolewa kwenye kamati za Seneti.

Wiki ijayo inatarajiwa kuwa zamu ya kuwaondoa wafuasi wa Dkt Ruto katika Bunge la Kitaifa. Kati ya wanaolengwa ni Aden Duale (Kiongozi wa Wengi), Ben Washiali (Kiranja wa Wengi) na Kimani Ichung’wah (Kamati ya Bajeti).

Uhuru atawaweka hadi 2022?

Na WANDERI KAMAU

MASWALI yameibuka iwapo Rais Uhuru Kenyatta atafaulu kudumisha usemi wake katika chama cha Jubilee kuelekea 2022, kwa kubuni miungano na vigogo mbalimbali wa kisiasa.

Tashwishi hizo pia zimezungumziwa ikiwa Rais atafaulu kuendelea na kasi ya mabadiliko ya sasa, ambayo wengi wamefasiri kuwa yanalenga kumtenga Naibu Rais William Ruto.

Kulingana na wadadisi, hofu hiyo inatokana na historia ya kutodumu kwa miungano ya kisiasa nchini tangu mwanzoni mwa mfumo wa utawala wa vyama vingi vya kisiasa 1992.

Rais Kenyatta amepanua mbawa zake kisiasa na kukumbatia viongozi wenye ushawishi nchini, kwenye hatua ambayo duru zinasema inalenga kumng’oa mamlakani Dkt Ruto kupitia hoja ya kutokuwa na imani kwenye Bunge la Kitaifa.

Tayari, Rais amebuni mkataba wa kisiasa na Seneta Gideon Moi (Baringo), aliye pia kiongozi wa Kanu.

Mkataba huo ushawasilishwa kwa Afisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa.

Kinara wa ODM, Bw Raila Odinga, ndiye aliyekuwa kiongozi wa kwanza kisiasa nchini kuanza kushirikiana na Rais Kenyatta kupitia handisheki mnamo Machi 2018. Zaidi ya hayo, kinara wa Wiper, Bw Kalonzo Musyoka, pia ameeleza nia yake ya kutaka kubuni ushirikiano sawia na Rais Kenyatta.

Kiongozi mwingine ambaye pia ameripotiwa kujumuishwa kwenye mpango huo ni Bw Isaac Ruto, ambaye ni kiongozi wa Chama Cha Mashinani (CCM). Bw Ruto alihudumu kama Gavana wa Bomet kati ya 2013 na 2017.

Lakini licha ya hatua hiyo, wadadisi wanasema hata kama Rais Kenyatta atafanikiwa kubuni muungano huo na kuwashirikisha wanasiasa hao serikalini, mtihani mkuu utakuwa kuudumisha na kutimiza matakwa yao hadi 2022.

Kulingana na Bw Charles Mulila ambaye ni mchanganuzi wa siasa, huenda wanasiasa wakaanza kutoa masharti yao ya kujumuishwa kwenye serikali, hali ambayo inaweza kumlazimu Rais Kenyatta kubuni nyadhifa ambazo hazitambuliwi kikatiba.

Mdadisi huyo pia anarejelea historia ya miungano ya kisiasa nchini, akisema haidumu hata kidogo, kwani huwa inasambaratika mara tu baada ya wanasiasa kutimiza malengo yao.

“Tumeshuhudia miungano mingi ya siasa nchini tangu 1990, wakati Wakenya walianza kumshinikiza Rais Mstaafu Daniel Moi kurejesha mfumo wa vyama vingi vya siasa. Muungano wa kwanza ulikuwa wa chama cha FORD (Forum for the Restoration of Democracy). Huu ulikuwa ni muungano ulioonekana kuwapa matumaini wanaharakati wengi waliokuwa wakipigania mfumo wa demokrasia ya vyama vingi,” asema Bw Mulila.

Kulingana naye, uwepo wa viongozi wakuu kama Jaramogi Oginga Odinga, Kenneth Matiba, Charles Rubia kati ya viongozi wengine ulizua taswira ya muungano ambao ungedumu kwa kuiondoa Kanu mamlakani.

Wadadisi wanaeleza kuwa huenda isishangaze kwa baadhi ya wanasiasa kuondoka serikalini, ikiwa matakwa yao hayatatimizwa na kubuni muungano na Dkt Ruto, iwapo atang’olewa mamlakani.

Ikizingatiwa kuwa wanasiasa kama Dkt Ruto na Bw Odinga washawahi kuwa pamoja katika ODM, wadadisi wanaeleza kuwa hakuna lisilowezekana katika siasa, kwani wote wanaongozwa na nia ya kufanikikisha maslahi yao.

Uhuru azidi kumkalia Ruto

Na CHARLES WASONGA

MSIMAMO wa kiongozi wa chama cha Jubilee, Rais Uhuru Kenyatta uliendelea kudhihirika wazi Ijumaa wandani wa Naibu Rais William Ruto wakishindwa kumwokoa Naibu Spika wa Seneti Kithure Kindiki.

Hatua hiyo ilijiri baada ya maseneta wa upinzani kuungana na wale wa Jubilee ambao ingawa walisifia utendakazi wa Profesa Kindiki, walisalimu amri ya chama cha Jubilee.

Chama cha Jubilee kimeendelea kuwatenga wanaoonekana kwenda kinyume na msimamo wa chama hasa wanaoegemea kwa Dkt Ruto, ambaye pia ameendelea kukimya kuhusu yanayoendelea chamani, na kuangazia kutoa msaada kwa waathiriwa wa virusi vya corona.

Baadhi ya maseneta ambao wamekuwa waaminifu kwa Dkt Ruto, hasa maseneta maalum, walilazimika kusaliti imani yao kwake kwa kuunga mkono hoja hiyo iliyowasilishwa na kiranja wa wengi Irungu Kang’ata.

Prof Kindiki ni mwandani wa Dkt Ruto na masaibu yaliyomfika yanasawiriwa kama pigo kwa mustakabali wa kisiasa wa naibu huyo wa Rais katika azma yake ya kuingia Ikulu 2022.

Na licha ya wandani wa Naibu Rais wakiongozwa na Seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen kulalamika kuwa hoja hiyo ilikwenda kinyume cha Katiba na Sheria za Bunge, Seneta James Orengo alipuuzilia mbali madai hayo.

“Mheshimiwa Spika wapi orodha ya mashtaka dhidi ya Prof Kindiki? Na je, wapi ushahidi kuonyesha kuwa alipewa nafasi ya kujitetea? Ni udikteta kwa bunge hili kumsulubisha mwenzetu kinyume cha sheria,” Murkomen akasema kwa hasira.

Bw Orengo, ambaye ni kiongozi wa wachache, alisisitiza kuwa kanuni hiyo huzingatiwa katika hoja ya kumfuta kazi Rais na Naibu wake pekee, akisema Kindiki anaondolewa kwa kuwa chama chake hakina tena imani naye.

Kauli yake iliungwa mkono na kiranja wa wachache, Bw Mutula Kilonzo Junior ambaye alisema kosa kubwa la Prof Kindiki ni kutokuwa mwaminifu kwa chama.

“Hoja hii haina uhusiano wowote na utendakazi wa ndugu yangu Prof Kindiki. Suala ni kwamba chama cha Jubilee kilichompa cheo hiki kimekosa imani naye,” akasema Seneta huyo wa Makueni.

Miongoni mwa maseneta waliohudhuria mkutano huo ni wale sita ambao walikwepa mkutano wa awali, ulioitishwa na Rais Uhuru Kenyatta.

Wao ni Millicent Omanga, Falhada Iman, Naomi Waqo, Victor Prengei, Mary Seneta na Christine Zawadi ambao wameitwa kufika mbele ya kamati ya nidhamu ya Jubilee ili waadhibiwe.

Hata hivyo, licha ya kuhudhuria mkutano huo Seneta Linturi alikataa kuunga mkono hoja hiyo akisema sharti apewe “orodha ya makosa ya Kindiki niyachunguze kwanza kabla ya kufanya uamuzi.”

Mnamo Alhamisi Bw Kang’ata aliwatumia jumbe maseneta wote 38 wa Jubilee wakitakiwa kuhudhuria kikao maalum cha seneti na kuunga mkono hoja ya kumwondoa Kindiki.

Seneta wa Kaunti ya Tharaka Nithi Prof Kithure Kindiki. Picha/ Maktaba

Wale ambao watakosa kuhudhuria kikao hicho wanaweza kupewa adhabu, ambayo inaweza kujumuisha kufurushwa kutoka Jubilee kulingana na kipengee 17 (2) na (3) ya katiba ya chama hicho.

“Msimamo wa chama ni kwamba, kimepoteza imani na Naibu Spika na hivyo kinataka aondolewe. Kwa hivyo, sharti uhudhurie kikao maalum cha seneti na upige kura kulingana na msimamo wa chama,” Bw Kang’ata akasema katika barua yake.

“Tafadhali zingatia kuwa msimamo chama katika suala hili ni kuunga mkono hoja hiyo,” barua hiyo ikaongeza.

Ni kutokana na tishio hilo ambapo wengi wa maseneta waliokuwa katika kambi ya Dkt Ruto walilazimika kubadili msimamo na kuunga mrengo wa Rais.

Upande wa Dkt Ruto uliachwa na idadi ndogo ya maseneta ambao hawawangeweza kubatilisha uamuzi wa kumfurusha Kindiki.

Maseneta waliopiga kura kuunga hoja kutimua Naibu Spika huyo walikuwa 54 dhidi ya 7 waliopinga.

Alikosea wapi?

BENSON MATHEKA na CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta Jumatano aliendelea na harakati zake za ‘kusafisha’ chama cha Jubilee baada ya kuwatema maseneta watano maalumu wanaoegemea upande wa Naibu Rais William Ruto.

Hatua zake, hasa zinazomlenga naibu wake zimeendelea kuibua maswali mengi miongoni mwa Wakenya, baadhi wakishangaa wawili hao walikosania wapi.

Uhusiano wao umeonekana kukumbwa na uhasama hivi kwamba, ni bayana Rais Kenyatta hatamuunga Dkt Ruto katika uchaguzi mkuu wa 2022.

Wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa 2017 Rais Kenyatta aliahidi wafuasi wa Jubilee kwamba, angetawala kwa miaka 10 na kumpisha Ruto atawale kwa miaka mingine 10 pia.

Uhasama wao unadhihirika katika matukio ya hivi punde ambapo Rais Kenyatta anawatimua wandani wa naibu wake wanaoshikilia nyadhifa za juu serikalini, bungeni na katika mashirika ya serikali.

Jumatano, maseneta hao walifurushwa kwa kususia mkutano ulioongozwa na Rais Kenyatta katika Ikulu ya Nairobi Jumatatu.

Walioandikiwa barua za kufurushwa ni pamoja na Millicent Omanga, Falhada Dekow Iman, Naomi Jillo Waqo, Victor Prengei na Mary Seneta.

Watano hao ni washirika wa Naibu Rais William Ruto na ndiye alishawishi uteuzi wao.

Kulingana na taarifa fupi iliyotolewa na Katibu Mkuu Raphael Tuju mnamo Jumatano, watano hao walifukuzwa kwa mienendo mibaya na kukosa heshima kwa uongozi wa chama.

“Walipokea mwaliko wa mkutano lakini hawakujali hata kuomba radhi kwa kutohudhuria,” akasema Tuju.

Hata hivyo, wandani wa Dkt Ruto katika Seneti wameshikilia kuwa hawakualikwa katika mkutano huo.

Ni katika kikao hicho kilichohudhuriwa na maseneta 20 kati ya 35 ambapo maseneta Kipchumba Murkomen na Susan Kihika, waliovuliwa nyadhifa za kiongozi wa wengi na kiranja wa wengi, mtawalia.

Wadadisi wa siasa wanasema Rais Kenyatta alikosa imani na Dkt Ruto kwa kuonekana kukaidi maagizo yake na mwelekeo alioutaka kiongozi wa nchi.

“Ruto alikosea kwa kumdharau Rais na hivyo kufanya kiongozi wa nchi na wandani wake kukosa imani naye. Hisia zao wandani wa Rais ni kuwa, Ruto ni hatari na hafai kuwa Rais na wakaanza mipango ya kumkata kucha polepole. Tunachoshuhudia sasa ni kilele cha njama iliyoanza kabla ya uchaguzi mkuu wa 2017,” asema Bw David Gatura mdadisi wa masuala ya siasa.

Anasema Rais Kenyatta amekuwa akimvumilia Dkt Ruto lakini akazidisha kiburi.

“Hakuna kiongozi wa nchi anayeweza kufurahishwa na naibu anayejipiga kifua kuwa ana umaarufu kumliko. Hivyo ndivyo Dkt Ruto alivyofanya kwa kuendeleza siasa na kuvamia ngome yake ya Mlima Kenya. Ilikuwa ni kumhujumu Rais na hii ni sawa na mapinduzi,” alisema Bw Gatura.

Kulingana na naibu mwenyekiti wa chama cha Jubilee, Bw David Murathe, wandani wa Rais Kenyatta walikosa imani na Dkt Ruto kwa sababu ya tabia yake.

Bw Murathe amenukuliwa mara kadhaa akisema Dkt Ruto ni mkaidi na hawezi kulinda maslahi ya wakazi wa Mlima Kenya akiwa Rais.

“Ikiwa anamkaidi Rais akiwa naibu wake, itakuwaje akiwa mamlakani?” Bw Murathe amekuwa akiuliza.

Mbunge mmoja wa Jubilee ambaye hakutaka tutaje jina lake alisema kiburi cha Dkt Ruto kilimfanya aamrishe baadhi ya mawaziri.

“Haya yalikuwa makosa makubwa na Rais alikasirika. Alianza kushawishi wabunge kumuasi Rais Kenyatta hasa katika vita dhidi ya ufisadi na Mpango wa Maridhiano (BBI). Licha ya kushauriwa na Rais mara kwa mara alimpuuza na kutaka kuonekana kuwa kiongozi wa chama akijigamba alivyo na idadi kubwa ya wabunge. Nafikiri kulikuwa na njama dhidi ya Rais ambayo ilitibuliwa na handisheki,” alisema mbunge huyo.

Msimamo wa Dkt Ruto kuhusu BBI na vita dhidi ya ufisadi, uligawanya chama cha Jubilee katika makundi ya ‘Tangatanga’ la wabunge wanaomuunga mkono na ‘Kieleweke’ linalomuunga Rais Kenyatta.

Baadhi ya wadadisi wanahisi Rais Kenyatta na Dkt Ruto walitofautiana kisera katika kipindi cha pili uongozini.

“Rais alitaka kuacha kumbukumbu na mwingine alitaka kujiandaa kwa uchaguzi wa 2022 na wakajipata njia panda,” mdadisi wa siasa Geff Kamwanah anaeleza.

Uhuru aundiwa chama kipya?

Na WANDERI KAMAU

IMEIBUKA kwamba mabwanyenye katika eneo la Mlima Kenya wanapanga kukitumia chama cha PNU kuwa “dau mpya” la eneo hilo kwenye uchaguzi wa 2022, ikiwa Chama cha Jubilee (JP) kitasambaratika.

Wadadisi pia wanataja hilo kama mkakati wa Rais Uhuru Kenyatta “kumnyang’anya” Naibu Rais William Ruto udhibiti wa kisiasa katika eneo hilo, ambalo ni ngome yake.

Duru zinaeleza kuwa mipango ya kukibadili jina chama hicho kuwa The National Unity Party (TNU) tayari iko karibu kukamilika na usajili wake rasmi kukabidhiwa Afisi ya Msajili Mkuu wa Vyama vya Kisiasa.

Kulingana na ripoti, mabwanyenye hao walikutana katika hoteli moja viungani mwa jiji la Nairobi wiki iliyopita, ambako mchango mfupi wa kufadhili shughuli za chama hicho kipya ulifanyika.

Baadhi ya viongozi wakuu serikalini waliohudhuria ni Waziri wa Kilimo Peter Munya, kwani ndiye amekuwa kiongozi wa chama hicho kwa sasa.

Na kutokana na hatua hiyo, wadadisi wa siasa wanasema kuwa huenda hilo likawa mojawapo ya hatua za kichinichini za Rais Kenyatta na waandani wake wa karibu kisiasa katika Chama cha Jubilee (JP) kubuni mkakati watakaofuata kisiasa, ikiwa mustakabali na uthabiti wa JP utaendelea kuyumba kama ilivyo sasa.

Vilevile, wanataja hali hiyo kama “plan B” ya Rais kwenye mpango wa kubuni muungano wa kisiasa na kinara wa ODM, Bw Raila Odinga, Seneta Gideon Moi katika Kanu miongoni mwa wanasiasa wengine.

Kulingana na Prof Macharia Munene, ambaye ni mchanganuzi wa siasa, huenda isiwe furaha ya Rais Kenyatta kubuni muungano huo chini ya mazingira ya mafarakano na hali ya kutoelewana kama ilivyo sasa katika Jubilee.

“Si kwamba Rais Kenyatta hashuhudii wala hafuatilii yanayoendelea katika Jubilee. Yeye ni mwanasiasa, ambaye licha ya muda wake kuhudumu kukaribia kuisha, lazima atazame mbele kwa kubuni mazingira, ambapo yeye, familia yake na washirika wake kisiasa watakuwa salama chini yake,” asema Prof Munene.

Wadadisi wanaeleza kuwa kwa kuwashirikisha tena mabwanyenye na watu maarufu kwenye usajili mpya wa PNU, viongozi wakuu katika Mlima Kenya, akiwemo Rais Kenyatta, wanalenga kuanza kukinadi kama “dau” litakalotumika na eneo hilo kufanikisha mipango ya kubuni muungano wa kisiasa na Odinga, Moi miongoni mwa viongozi wengine.

Wanataja hilo kama njia ya pekee kwa Rais Kenyatta kuchukua mwelekeo mpya kisiasa, ikiwa “itakuwa vigumu kwake kutwaa udhibiti” wa Jubilee kutoka kwa Dkt Ruto na waandani wake kisiasa.

Kumekuwa na makabiliano makali kati ya waandani wa Rais na Dkt Ruto kuhusu udhibiti wa Jubilee, pande zote zikiapa kufanya kila ziwezalo “kutetea maslahi yao chamani.”

Waandani wa Dkt Ruto wamekuwa wakimlaumu Katibu Mkuu, Bw Raphael Tuju na Naibu Mwenyekiti, Bw David Murathe, kwa kuendesha njama za kichinichini kumwondoa Dkt Ruto kwenye udhibiti wa chama hicho.

Na kama Rais Kenyatta, Dkt Ruto pia ameripotiwa kubuni vyama viwili vya siasa, ikiwa atapoteza udhibiti wa Jubilee.

Lakini kufuatia uzinduzi mpya wa PNU, wadadisi wanatilia shaka ikiwa juhudi hizo zitafaulu kufuta dhana ya usaliti wa Dkt Ruto na wandani wa Rais Kenyatta katika eneo hilo.

Hili ni kutokana na mpenyo mkubwa ambao alikuwa amefanya, kabla ya kuzuka kwa janga la virusi vya corona, ambalo limesambaratisha shughuli nyingi za kisiasa nchini.

Wadadisi wanasema kuwa ingawa huo ni mpango mzuri kwa Rais Kenyatta, idadi kubwa ya wakazi bado inaona njama hizo kama mpango wa wazi kumsaliti kisiasa Dkt Ruto.

Wanasema kuwa ni sababu hiyo ambapo huenda iwe vigumu kukiuza upya chama hicho, ikiwa baadhi ya viongozi wanaoonekana “kumpiga vita” Dkt Ruto kama Mabwana Murathe na Tuju watakuwa sehemu ya muundo mpya wa TNU.

“Ikiwa Jubilee hatimaye itasambaratika na TNU kuonekana kama chama kipya kitakachookoa jahazi Mlima Kenya, basi lazima viongozi wa zamani katika Jubilee kama Bw Murathe wasionekane hata kidogo. Hii ni kwa kuwa itafasiriwa kuwa wao ni mwendelezo tu wa njama za kumsaliti Ruto kisiasa,” asema Bw Charles Mulira, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.

Vilevile, uwepo wa vyama vya kisiasa kama Transformation National Party (TNAP) na The Service Party (TSP) vinavyohusishwa na mbunge Moses Kuria (Gatundu Kusini) na aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Mwangi Kiunjuri mtawalia, pia unatajwa kuwa hali itakayowapa waandani wa Rais Kenyatta ugumu kukiuza chama hicho kipya.

Wawili hao ni waandani wa karibu wa Dkt Ruto na wamekuwa miongoni mwa watetezi wake wakuu Mlimani.

Vyama hivyo vilisajiliwa mapema mwaka huu na tayari vimeanza kuwasajili wanachama na kufungua matawi katika sehemu mbalimbali nchini.

Hata hivyo, baadhi ya watetezi wa Rais Kenyatta wanasema kuwa yeye ni mwanasiasa mwenye tajriba, na haitakuwa mara yake ya kwanza kuacha chama na kubuni safari yake huru kisiasa.

“Rais Kenyatta aliacha Kanu na kubuni TNA mnamo 2012 na kushinda urais mnamo 2013, licha ya masaibu yaliyomwandama kama mashtaka katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC). Hivyo, huu ni mtihani rahisi kwake,” asema mbunge wa Kieni, Kanini Keega, ambaye ni mojawapo ya watetezi sugu wa Rais.

Kelele na Uhuru na Ruto zinavyowatesa wananchi

Na BENSON MATHEKA

MATUMAINI ya Wakenya kuwa na maisha bora, umoja na usalama yanaendelea kudidimia Rais Uhuru Kenyatta na Naibu Rais William Ruto wakiendelea kupambana.

Wachanganuzi wanasema Rais Kenyatta na Dkt Ruto wameweka mbele maslahi na tamaa zao za kibinafsi badala ya maslahi ya raia.

Wabunge, magavana na maseneta wa vyama mbalimbali nao wamefuata nyayo za wawili hao kwa kuegemea upande wa Rais Kenyatta ama wa Dkt Ruto.

Hii imesababisha mijadala ya kusaidia mwananchi wa kawaida kupuuzwa na nafasi yake kuchukuliwa na kelele za siasa.

Wadadisi wanasema wanasiasa wakiongozwa na rais na naibu wake wameteka nyara nchi na hivyo kutatiza maendeleo pamoja na kuigawanya nchi kisiasa badala ya kuiunganisha wanavyodai.

“Badala ya kuonyesha mfano mwema wa kuigwa na viongozi wengine katika kutafuta suluhu kwa changamoto zinazowakumba Wakenya, rais na naibu wake wanaelekeza nchi pabaya. Hawaaminiani na wamegawa nchi katika mirengo. Huu ndio mwanzo wa masaibu ya Wakenya kwa sababu katika mazingira haya ni vigumu kwa serikali kuhudumia Wakenya kwa njia ifaayo,” aeleza mdadisi wa siasa Tom Maosa.

“Inasikitisha kwamba wanasiasa wanaonekana kutojali matatizo yanayoathiri mwananchi wa kawaida na badala yake wamepagawa na siasa za kubadilisha katiba,” mwanasiasa na mtaalamu wa masuala ya usimamizi Eliud Owalo anafafanua.

“Katika mijadala inayoendelea, anayeumia zaudi ni Mkenya wa kawaida. Wanasiasa hawajali mwananchi. Hata BBI ambayo imetajwa kuwa ya kuunganisha Wakenya imebadilika kuwa ya kuwagawanya zaidi,” asema Bw Maosa.

Aendelea: “Kwa sasa wabunge wanapaswa kuwa wakijadili masuala kama virusi vya corona, gharama ya maisha na nzige. Pia wanafaa kuangazia mbinu za kufanikisha mtaala mpya wa elimu, usalama wa taifa, kufanikisha vita dhidi ya ufisadi na kutafuta suluhu kwa janga la ukosefu wa ajira nchini. Badala yake wanatumia muda wao mwingi kujadili ni nani atakayekuwa rais 2022 na BBI ambayo inagawanya Wakenya zaidi.”

Vita kati ya Rais Kenyatta na Dkt Ruto navyo vimeingia baridi huku ofisi ya Mkurugenzi wa Idara ya Kupeleleza Uhalifu (DCI) na ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) zikilaumiana.

Lawama za kufifia kwa vita dhidi ya ufisadi imeelekezwa kwa rais na naibu wake kwa kutofautiana kuhusu jinsi ya kuendeleza vita hivyo.

Dkt Ruto amekuwa akikosoa DCI na DPP akisema idara hizo zinatumiwa kumpiga kisiasa huku Rais Kenyatta akitangaza imani yake kamili katika idara hizo.

Bw Owalo anasema vita dhidi ya ufisadi havitafaulu kwani Kenya imetekwa na mitandao ya wafisadi wenye uhusiano na maafisa wa ngazi za juu serikalini.

“Hakuna hatua mathubuti zinazochukuliwa isipokuwa watu kukamatwa Ijumaa na kufikishwa kortini Jumatatu. Kisha wanaachiliwa huru kwa dhamana. Huo ndio unaokuwa mwisho wa vita hivyo,” asema Bw Owalo.

Kulingana na Bw Owalo, suala kuu ambapo wanasiasa kwa sasa wanapaswa kuwa wakijadili ni jinsi ya kupunguza deni la taifa ambalo linaendelea kuongezeka.

“Tumekuwa nchi ya madeni. Hii imesababisha Wakenya kulipa ushuru zaidi. Gharama ya maisha inapanda, hakuna kazi, uchumi unaelekea kukwama na umaskini kuongezeka,” asema.

Kulingana na takwimu, Wakenya zaidi ya 4 milioni hawana kazi, hali inayotokana na viwanda kufungwa kutokana na mazingira mabovu ya kiuchumi na kisiasa nchini.

Ustawi wa viwanda ni moja ya Ajenda Nne Kuu za serikali ya Jubilee ambazo wadadisi wanasema zitabakia ndoto.

Wiki jana, Ofisi ya Bunge kuhusu Bajeti ilisema hakuna pesa za kufanikisha miradi ya Ajenda Nne Kuu ambazo ni utoshelezaji wa chakula, afya kwa wote, makao nafuu na viwanda.

Mpango wa afya kwa wote nao unakabiliwa na hatari ya kusambaratika kwa kukosa pesa. Ofisi ya Bajeti imesema tangu mpango wa afya kwa wote ulipozinduliwa 2018, hakuna hatua zilizochukuliwa kufanyia mageuzi mashirika yanayohusika ili kufanikisha ajenda hiyo.

Uhuru na Ruto, nani anamsaliti mwingine?

Na BENSON MATHEKA

UHUSIANO kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto, unaendelea kuwa baridi huku makundi mawili katika chama tawala cha Jubilee yakilaumiana kwa usaliti.

Washirika wa Dkt Ruto wanamlaumu Rais Kenyatta kwa kumsaliti na kumtenga serikalini kinyume na maafikiano yao walipounda chama cha Jubilee.

Wanahisi kwamba Dkt Ruto alimsaidia Uhuru kuwa rais lakini sasa kuna njama ya kumzuia kuwa na usemi katika chama tawala na hata serikalini.

Ingawa Dkt Ruto amekuwa akidai uhusiano wake na Rais Kenyatta uko thabiti, washirika wake wa kisiasa wamekuwa wakimlaumu Rais hadharani wakidai baadhi ya maamuzi yake yanalenga kumtenga naibu wake, mshirika wake wa kisiasa tangu 2013.

Nao washirika wa Rais Kenyatta wamekuwa wakimlaumu Dkt Ruto kwa kumkaidi mkubwa wake wakisema kufanya hivyo ni kusaliti kiapo cha ofisi yake.

Wanaomuunga Rais wanadai kwamba amekuwa na kiburi na huwa anatuma washirika wake kumshambulia Uhuru. Wale wanaounga Ruto wanasisitiza kuwa Rais ameagiza maafisa wa serikali kumhangaisha naibu wake.

Kulingana na washirika wa Dkt Ruto, Rais Kenyatta amesaliti naibu wake kwa kukosa kumwidhinisha kuwa mrithi wake kwenye uchaguzi mkuu wa 2022 na kumzima asitekeleze wajibu wowote katika kufanikisha ajenda za serikali.

Dkt Ruto amekuwa akisisitiza kuwa manifesto ya Jubilee na Ajenda Nne Kuu za serikali ndizo zinazofaa kupewa kipaumbele. Hata hivyo, Rais Kenyatta amepatia kipaumbele mchakato wa Jopokazi la Maridhiano (BBI) na vita dhidi ya ufisadi ambazo washirika wa Dkt Ruto wanahisi zinamlenga.

Wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa 2017, Rais Kenyatta alikuwa akifahamisha wafuasi wa Jubilee kwamba atahudumu kwa miaka kumi na kisha ampishe Ruto kutawala wa miaka kumi.

“Tunasema hivi, nipeni nafasi nimalize miaka yangu kumi na Ruto afanye yake kumi,” Rais alisema kwenye mikutano ya kampeni hasa eneo la Rift Valley, ngome ya Dkt Ruto.

Hata hivyo, Rais Kenyatta amekuwa akisema ni Mungu anayejua atakayekuwa rais baada yake na kuwa chaguo la atakayemrithi litawashangaza Wakenya. Washirika wa Dkt Ruto wanahisi kwamba Rais Kenyatta amesaliti Dkt Ruto na kusahau manifesto ya Jubilee na kuungana na kiongozi wa upinzani Raila Odinga ili kuzima azma ya naibu wake ya kuwa rais.

Dkt Ruto mwenyewe amekuwa akimlaumu Bw Odinga kwa kuwa na njama ya kusambaratisha chama cha Jubilee na kumfanya atengwe serikalini.

“Tulipounda Jubilee tulikuwa na manifesto na mwelekeo wa kuunganisha Wakenya na kufanikisha maendeleo. Lakini tumeona usaliti wa hali ya juu katika kipindi hiki cha pili,” alisema mwandani wa Ruto aliyeomba tusitaje jina lake akisema washirika wa naibu rais wamekuwa wakidhulumiwa.

Baada ya kuapishwa kwa kipindi cha pili, Rais Kenyatta alitangaza kipindi cha siasa kilikuwa kimeisha lakini Dkt Ruto aliendelea kutembelea maeneo tofauti nchini kuendeleza siasa akidai alikuwa akizindua miradi ya maendeleo.

Katika mikutano yake kote nchini, washirika wake huwa wanaidhinisha azima yake ya kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Wadadisi wanasema kwamba Dkt Ruto alimsaidia Rais Kenyatta kushinda urais kwenye chaguzi za 2013 na 2017 akiwa na matumaini kwamba atarudisha mkono lakini kwa sasa haonekani kuwa na mipango hiyo.

Ingawa Dkt Ruto anahisi kwamba Rais Kenyatta ameacha kutekeleza manifesto ya Jubilee, wandani wa Rais wanahisi kwamba ni yeye aliyejisaliti kwa kuhujumu mkubwa wake hasa kwa kutokomesha siasa, kupinga vita dhidi ya ufisadi na kupuuza Jopokazi la Maridhiano (BBI).

Dkt Ruto na washirika wake wamekuwa wakidai kuwa mchakato wa kubadilisha katiba kupitia BBI unalenga kumzima kisiasa.

“Ruto na wandani wake wamekuwa wakipinga miradi ambayo Uhuru anapenda sana kama BBI na kusahau kuwa ni mchakato ulioanzishwa na mkubwa wake na kwa rais na washauri wake, huu ni usaliti wa hali ya juu na kukosa heshima. Naibu Rais hafai kumpinga mkubwa wake hadharani,” alisema mdadisi wa siasa David Bosire.

Ndoa ya unafiki

Na MWANDISHI WETU

SASA ni wazi kuwa ndoa ya kisiasa kati ya Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto imesambaratika.

Hii ni licha ya wawili hawa kuendelea kuwapumbaza Wakenya kuwa wangali pamoja katika upeo wa uongozi wa nchi.

Maneno yao hayalingani na vitendo vyao vinavyoonyesha uhusiano ambao kila mmoja anahujumu mwenzake.

Ingawa hawashambuliani moja kwa moja, washirika wa Rais Kenyatta na Dkt Ruto ndio wamekuwa tarumbeta za kutangaza hisia na misimamo yao kwa umma.

Rais Kenyatta pia amekuwa akitoa matamshi kwa mafumbo akimshambulia Dkt Ruto kuhusu masuala tofauti.

Kwa upande wake Dkt Ruto anashikilia kuwa uhusiano wao uko imara na kuwa wanafanya kazi pamoja.

Wandani wa rais wakiongozwa na David Murathe na kundi la ‘Kieleweke’ likiongozwa na wabunge Maina Kamanda (kuteuliwa) na Ngunjiri Wambugu (Nyeri Mjini) wamekuwa ndio mijeledi ya kumgonga Naibu Rais.

Kwa upande mwingine, Dkt Ruto naye anatumia kundi la ‘Tangatanga’ likishirikisha baadhi ya wabunge wa Mlima Kenya na Rift Valley kumshambulia Rais Kenyatta.

Hisia kali za wabunge Alice Wahome (Kandara), Moses Kuria (Gatundu Kusini) na Oscar Sudi (Kapseret) ndizo zimekuwa za juu zaidi katika malumbano kati ya Rais Kenyatta na Dkt Ruto.

Baadhi ya vitendo vya Rais Kenyatta pia zinaonyesha hamdhamini tena mshirika wake hasa katika uwakilishi wake kwenye hafla.

Kulingana na utaratibu, naibu rais ndiye anayefaa kumwakilisha rais kwenye hafla, lakini katika siku za majuzi amekuwa akiwatuma maafisa wa serikali ama wabunge kumwakilisha licha ya Dkt Ruto kuwepo kwenye hafla hizo.

Wiki iliyopita kulitokea mtafaruku katika mazishi ya mamake Mbunge wa Mathira, Rigathi Gachagua wakati Mbunge wa Kieni, Kanini Kega aliposema ametumwa na rais kupatia familia hiyo Sh500,000 za kuifariji licha ya kuwa Dkt Ruto alikuwepo.

Mwaka jana Waziri wa Utumishi wa Umma, Margaret Kobia alimwakilishi rais kwenye hafla iliyohudhuriwa na naibu rais katika Kaunti ya Nyeri.

Vitendo vya maafisa wakuu serikalini wakiongozwa na Waziri wa Usalama, Fred Matiang’i na katibu wake Karanja Kibicho pia zinaonyesha mfarakano unaokumba ndoa ya Uhuruto.

Rais alimdhalalisha Dkt Ruto mwaka jana alipomwondoa kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Baraza la Mawaziri kuhusu Maendeleo na kukabidhi wadhifa huo kwa Dkt Matiang’i.

Kudhalalishwa kwa Dkt Ruto kupitia maafisa wa serikali nako kumefika upeo mpya ikifichuka kuwa wiki iliyopita alikatazwa kulala katika makao rasmi ya Naibu Rais jijini Mombasa kwa agizo la afisa wa ngazi ya juu serikalini.

Maafisa wa usalama, utawala wa mikoa na mashirika ya serikali pia wamekuwa wakikwepa hafla za naibu rais kwa kile kimejitokeza kuwa ni kuogopa kuadhibiwa kwa kujihusisha naye.

Vita katika ndoa ya wawili hao vimekuwa vikitokota tangu handisheki kati ya Rais na Kiongozi wa ODM, Raila Odinga mnamo 2018.

Matokeo ya fujo katika urais yamekuwa ni migawanyiko zaidi nchini kwa misingi ya kikabilia na kisiasa, kutatizika kwa mipango ya maendeleo na ongezeko la gharama ya maisha kwa wawili hao kukosa kumakinika katika kutatua matatizo ya wananchi.

Vita vya wawili hao pia vimegawanya chama cha Jubilee huku rais akionekana kutokuwa makini kuhusu kukihusu.

Wakati wa uzinduzi wa ripoti ya Jopo la Maridhiano (BBI) mnamo Novemba, Rais Kenyatta alionekana akiangua kicheko wakati Mbunge wa Suna Mashariki (ODM), Junet Mohamed aliposuta Jubilee kwa migawanyiko inayokikumba.

Pia wakati wa uchaguzi mdogo wa Kibra mwezi Novemba Rais hakushiriki kwenye kampeni za Jubilee na baadaye alikejeli wanasiasa wa Jubilee waliovamiwa na makundi ya vijana wa ODM wakati wa shughuli hiyo.

‘Ndoa ya UhuRuto ilivunjika kitambo’

Na WAANDISHI WETU

WABUNGE wa Jubilee wanaopinga azma ya Naibu Rais William Ruto ya kugombea urais 2022, sasa wanadai alivunja uhusiano wake na Rais Uhuru Kenyatta kwa kutaka kupimana nguvu naye.

Wabunge hao walifichua kuwa, Rais Kenyatta ataungana na wanasiasa wanaounga sera zake kubuni muungano utakaounda serikali ijayo.

“Ni sharti ieleweke kwamba Naibu Rais alimuacha Rais kitambo na akaanza kumpinga. Anawafadhili wabunge wanaohudumu mara ya kwanza bungeni kupigia debe azma yake ya urais 2022 na kumharibia Uhuru,” alisema mbunge wa kuteuliwa Maina Kamanda.

Bw Kamanda alisema mipango inaendelea kati ya rais na viongozi wa vyama vya ODM, Wiper, ANC na KANU ya kuwa na muungano mkubwa wa kuunganisha Wakenya.

Wabunge Maoka Maore (Igembe Kaskazini), Joshua Kutuny (Cherangany) Peter Mwathi (Limuru) na Robert Mbui wa Kathiani waliunga kauli ya Bw Kamanda.

Kundi la ‘Kieleweke’ analoongoza Bw Kamanda, limeanza kupigia debe muungano huo utakaoshirikisha vigogo watatu wa upinzani pamoja na Rais Uhuru ili kumenyana na Naibu Rais Ruto, katika Uchaguzi Mkuu 2022.

Wadhifa tofauti

Pia limedokeza kuwa linaunga mkono mabadiliko ya kikatiba ili kumwezesha Rais Kenyatta kuendelea kuhudumu baada ya 2022 japo katika wadhifa tofauti, Katiba ikibadilishwa.

Kulingana na aliyekuwa mbunge wa Dagoreti Kaskazini Dennis Waweru, wanaodhani Rais Kenyatta atastaafu watashangaa sana.

Aliyekuwa mbunge Mukurweini Kabando wa Kabando amepuuzilia mbali umaarufu wa kundi la ‘Tangatanga’ linalomuunga Dkt Ruto akisema muungano mpya unaotarajiwa kubuniwa hauwezi kutishwa au kushindwa kwa vyovyote na kwamba mabadiliko ya Katiba yanayosubiriwa ndiyo yatakayoamua hatima ya taifa.

“Sio kuhusu 2022 lakini ni kuhusu kizazi kijacho. Kikosi cha ‘Tangatanga’ kinatikisa Mlima Kenya lakini punde ujasiri wa ‘Tangatanga’ utatokomea mbali. Wanacheza kabla ya ngoma kupigwa. BBI itaangaza mwanga utakaokuwa vigumu kukataa,” alisema Kabando.

Kulingana na Bw Kabando, Dkt Ruto amekuwa akiwafadhili wabunge kupigia debe azma yake ya urais 2022 na kueneza madai kwamba familia za Jomo Kenyatta, Daniel Moi na Jaramogi Oginga Odinga zinataka kuendeleza tawala za kifamilia.

“Rais ni sharti awe imara kwa sababu kuna propaganda nyingi lakini tuko tayari kukabiliana nazo. Ni sharti Rais asimame kuwatafuta marafiki wake,” akashauri Kabando.

Uhuru amfuata Ruto afisini

Na BENSON MATHEKA

Rais Uhuru Kenyatta, jana alimtembelea Naibu Wake William Ruto katika afisi yake katika kile ambacho wadadisi wanasema ni juhudi za kutuliza joto la kisiasa nchini.

Rais Kenyatta alifika katika afisi ya Bw Ruto kwenye jumba la Harambee House Annex kwenye barabara ya Harambee mwendo wa saa saba mchana siku moja baada ya malumbano kuchacha ndani ya chama cha Jubilee na nchi kwa jumla.

Ujumbe kutoka Ikulu ulisema kwamba, viongozi hao wawili walikutana kwa chakula cha mchana na kujadili masuala yanayohusu ajenda za maendeleo ya serikali.

“Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake Dkt William Rut leo walishiriki chakula cha mchana ya kikazi katika afisi ya Naibu Rais Harambee House Annex, Nairobi ambapo viongozi hao wawili walijadili masuala yanayohusu ajenda ya maendeleo ya serikali,” ulisema ujumbe kutoka ikulu.

Wawili hao walikutana wakati ambao chama cha Jubilee kimegawanyika huku makundi mawili yakilumbana vikali kuhusu vita dhidi ya ufisadi na siasa za uchaguzi wa 2022.

Kundi moja linalomuunga Dkt Ruto linapinga muafaka kati ya Rais Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga, vita dhidi ya ufisadi na juhudi za kuleta uwiano nchini chini ya muafaka huo.

Wadadisi wanasema Rais Kenyatta alilenga kudhihirisha kwamba hajamtenga Naibu wake serikalini au kumlenga katika vita dhidi ya ufisadi yeye ( Ruto) na wandani wake wanavyodai.

“Kila hatua ambayo rais wa nchi anayochukua sio ajali, huwa imepangwa na inanuiwa kutimiza lengo fulani. Ikizingatiwa kwamba alimtembelea Naibu Rais wakati kuna msukosuko katika chama cha Jubilee, kuna ujumbe ambao alitaka kutuma kwa Wakenya kwamba hana kinyongo na Dkt Ruto kikazi,” alisema mdadisi wa kisiasa Tom Maosa.

Bw Ruto amekuwa akilaumu vita dhidi ya ufisadi akisema vimeingizwa siasa. Hasa, amekuwa akimtaja Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai, Bw George Kinoti kwa kutumiwa kisiasa kuvuruga ajenda yake ya kisiasa.

Wiki jana, Rais Kenyatta alisisitiza kuwa vita dhidi ya ufisadi havitamsaza yeyote hata akiwa mshirika wake wa karibu wa kisiasa, ndugu au dada yake, kauli ambayo wengi walichukulia alikuwa akimlenga Dkt Ruto.

Siku moja baadaye, wabunge wa Jubilee walilaumiana vikali kundi linalounga vita hivyo likimtaka Ruto kujiuzulu iwapo hafurahishwi na vita dhidi ya ufisadi.

Mnamo Jumatatu, seneta wa Siaya James Orengo ambaye ni mwandani wa Bw Odinga aliapa kuanza mipango ya kumtimua Bw Ruto afisini akidai amekiuka maadili.

Bw Ruto amekuwa akisisitiza kuwa Bw Odinga anatumia handisheki yake na rais kuvuruga mipango ya maendeleo ya serikali na upokezanaji wa mamlaka katika chama cha Jubilee.

Mwishoni mwa wiki, mgawanyiko katika chama cha Jubilee ulichacha wakati ambapo wabunge 12, wakiwemo tisa kutoka Jubilee, walipomlaumu Bw Ruto kwa kutomtii Rais Kenyatta na kumtaka ajiuzulu.

Mawakili wataka Uhuru na Ruto watangaze mali yao

PETER MBURU na WAIKWA MAINA

MAWAKILI wanamtaka Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto pamoja na maafisa wakuu wa serikali watangaze utajiri wao wazi ili kudhihirisha wamejitolea kupambana na ufisadi kikamilifu.

Wanachama wa Chama cha Mawakili wa Kenya (LSK) tawi la Rift Valley wakiongozwa na mwenyekiti wao John Ochang’ walitaka pia Jaji Mkuu David Maraga, naibu wake, maspika wa bunge la taifa na seneti, mawaziri, magavana na watumishi wengine wakuu wa umma wafanyiwe uchunguzi wa hali yao ya kimaisha na pia watangaze utajiri wao kwa Wakenya.

Kulingana na mwanachama wa LSK, Bw Bernard Kipkoech Ng’etich, vita dhidi ya ufisadi vinafaa kuanza katika afisi kuu zaidi za serikali.

“Haifai iwe tu inalenga sehemu chache. Tunataka kuona juhudi za kupambana na ufisadi kuanzia katika afisi ya rais. Tunataka kuona rais akitangaza kwa hiari amepata kiasi kipi cha mali tangu alipoingia mamlakani,” akasema Bw Ng’etich.

Hata hivyo, Rais wa LSK, Bw Allen Gichuhi, jana alikiri ufisadi unahitaji suluhisho katika sehemu zote za uongozi lakini akasema LSK kitatoa msimamo wake rasmi baada ya baraza lake kukutana.

Mawakili wa Rift Valley walikuwa wakizungumza wakati wa uchaguzi wa wanachama wa tawi hilo katika Rift Valley Sports Club mnamo Jumamosi.

Kulingana nao, kama maafisa wa ngazi za juu serikalini hawatadhihirisha kujitolea kwao kupambana na ufisadi, hatua zinazoshuhudiwa sasa dhidi ya washukiwa wa ufisadi katika shirika la Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS) hazitazaa matunda.

Wabunge wawakilishi wa wanawake wa kaunti tatu pia waliunga mkono juhudi za kupambana na ufisadi.

Wakizungumza mjini Ol Kalou wikendi, Wambui Ngirici (Kirinyaga), Rahab Mukami (Nyeri) na Faith Gitau (Nyandarua) walitaka uchunguzi wa sakata ya NYS ufanywe kwa kina zaidi na kusiwe na ubaguzi.

“Kiwango cha fedha kinachotajwa mahakamani hakilingani na kile kilichoripotiwa kwa umma. Tunataka kuwe na uchunguzi wa kina na kila mmoja aliyehusika atajwe wazi. Tuantaka wahusika wakuu pia wafike mahakamani kushtakiwa na kuhukumiwa,” akasema Bi Ngirici.

Majaji wapya wateuliwa ICC kusikiza kesi za Uhuru na Ruto zikifufuliwa

Na VALENTINE OBARA

MAHAKAMA ya Kimataifa kuhusu Uhalifu (ICC) imechagua majaji wapya kusimamia kesi za Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake, Bw William Ruto kuhusu ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007, iwapo Kiongozi wa Mashtaka wa korti hiyo ataamua kuzifufua.

Ingawa kesi hizo zilisitishwa kufuatia ukosefu wa ushahidi wa kutosha, Kiongozi wa Mashtaka, Bi Fatou Bensouda, aliambiwa yuko huru kuzifufua endapo atafanikiwa kukusanya ushahidi mpya.

Mwishoni mwa 2017, ilifichuka wapelelezi wa ICC walikuwa nchini Kenya kuchunguza masuala yanayohusiana na kesi ya Bw Ruto ambaye alishtakiwa pamoja na mtangazaji wa zamani wa redio, Bw Joshua Sang.

Ufichuzi huo ulitolewa kupitia kwa ripoti ya kila mwaka kuhusu shughuli za afisi ya upande wa mashtaka.

Mahakama hiyo Jumamosi ilifanya mabadiliko ya majaji baada ya majaji sita wapya kuchaguliwa wiki mbili zilizopita huku wengine waliokuwepo wakipewa majukumu mapya na baadhi yao kukamilisha muda wao wa kuhudumu.

Jaji Chile Eboe-Osuji ambaye wiki iliyopita alichaguliwa kuwa rais wa ICC, sasa atakuwa akihudumu kwenye kitengo cha rufaa cha mahakama hiyo. Awali, alikuwa Jaji Msimamizi wa kesi ya Mabw Ruto na Sang.

Kesi hiyo sasa itaendeshwa na Majaji Robert Fremr, Reine Alapini-Gansou na Kimberly Prost, ambao pia wataendesha kesi dhidi ya Rais Kenyatta.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari, mahakama hiyo jana ilisema mabadiliko hayo ambayo yameathiri kesi karibu zote zilizo mbele yake yamechukuliwa ili kuboresha utoaji huduma.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa afisi ya rais wa ICC ilizingatia uwezo na weledi wa majaji katika sheria za uhalifu wa kimataifa wakati mabadiliko hayo yalipofanywa.

“Majaji watahudumu kwa miaka mitatu, na baadaye hadi wakati kesi zitakapokamilika,” ikasema taarifa hiyo.

Kufuatia hatua hii, vyumba vya mahakama vya Tano (A) na Tano (B) ambavyo vilikuwa vikutumika kusikiliza kesi ya Bw Ruto na Rais Kenyatta mtawalia vilivunjiliwa mbali.

Kesi zote za Wakenya sita waliodaiwa kuhusika pakubaa zaidi na ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007 zilisitishwa baada ya kukosekana ushahidi wa kutosha kuthibitisha kuhusika kwao.

Bi Bensouda alilalamika kuwa uamuzi wake kusitisha kesi za Rais Kenyatta, Bw Ruto na Bw Sanga ulitokana na kuwa mashahidi walishawishiwa kujiondoa ambapo baadhi walitishiwa maisha yao, wengine wakauawa na wengine wakatoweka katika hali ya kutatanisha.

Alidai pia serikali ya Kenya ilikataa kumsaidia kukusanya ushahidi aliohitaji ilhali serikali ina jukumu hilo kwani taifa hili ni mwanachama wa ICC kupitia uratibishaji wa Mkataba wa Roma ambao ndio msingi wa sheria za mahakama hiyo iliyo The Hague, Uholanzi.

Hata hivyo, madai haya yalikanushwa na serikali ambayo iliwakilishwa na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu, Prof Githu Muigai.

JAMVI: Sababu ya Uhuruto kufurahia ukaidi wa Raila kwa urais wao

Na MWANGI MUIRURI

Kifupi:

  • Moses Kuria asema “sisi hatuna presha kwa kuwa Odinga anatumalizia mambo yetu ya 2022.”
  • Upinzani wa Odinga huwaweka wafuasi wa Jubilee wakiwa chonjo kwa kila hali na ambapo bora tu anaendelea kubishana, huwa anasaidia ngome muhimu za Jubilee kujitokeza kujisajili kama wapiga kura
  • Mlima Kenya hufurahia juhudi na uaminifu wa Ruto kwa Uhuru Kenyatta, na ndizo humwezesha ‘mtu wao’ kujinasua katika mtego wa Odinga
  • Bw Odinga angekuwa na wa kumshauri vilivyo, angetambua hawa wawili walio mamlakani kwa sasa, “lakini azidishe njama zake za kuangazia ufisadi ambao ni utamaduni wa Jubilee

WANDANI wa Jubilee wameelezea furaha yao kutokana na harakati za kinara wa chama cha ODM, Bw Raila Odinga za kutotambua urais wa Uhuru Kenyatta kwani kwa kufanya hivyo anaendelea kumjenga Naibu Rais William Ruto katika urithi wa Ikulu 2022.

Furaha yao inatokana na ukweli kuwa Jubilee imejengwa katika msingi wa makabila mawili yanayosakini ngome mbili kuu; Mlima Kenya (Gema) na Rift Valley (Kamatusa) ambapo katika kutotambua kwake Rais Kenyatta, upinzaani unazidi kuimarisha umoja wa ngome za Rais na naibu wake.

Katika hali hiyo, mchanganuzi wa siasa kutoka Mlima Kenya, Peter Kagwanja anasema “ukitaka taifa lote lilegeze misimamo mikali ya kuegemea Jubilee au muungano wa Nasa, itambidi Waziri Mkuu wa zamani atambue urais wa Kenyatta.”

Anasema kuwa hilo litawatuma wafuasi wa Nasa nje ya siasa za ukaidi na uasi huku nao wafuasi wa Jubilee wakiingiwa na mtazamo mpana wa kuanza kudai huduma bora kutoka kwa serikali yao badala ya kuitetea hata inapokosea.

Waziri wa Kilimo Mwangi Kiujuri akiwa katika hafla ya kikazi katika Kaunti ya Laikipia alifichua kuwa “wacha Odinga aendelee kupambana na UhuRuto akisema hawatambui lakini sisi kimyakimya tunajua kwamba anatujenga kwa kuwa anatupa ile motisha ya kuikinga serikali yetu”.

Kiunjuri alisema kuwa hadi sasa ni bayana kuwa mrengo wa Nasa uko katika hatari ya kusambaratika na harakati za Odinga ni mojawapo ya vichocheo hivyo vya uhasama ndani ya vyama tanzu ndani ya muungano wake.

“Akiendelea hivyo na akose kuelewana na vyama tanzu ndani ya Nasa, ina maana kuwa uchaguzi wa 2022 tutaingia tukiwa na uwezekano mkubwa wa kuwa na mrengo mwingine ndani ya Nasa, ugawe kura za Nasa na Ruto aibuke na ushindi wa zaidi ya asilimia 70,” akasema.

Aliwataka wenyeji wamuombee Odinga aendelee na mkondo wake wa sasa wa siasa “ili aendelee kuvurugika huku sisi tukiwa imara bila mawazo mengi”.

Naye mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria akihutubu katika mazishi ya Esther Nyaruai Wachira ambaye ni dadake mwakilishi wa wanawake wa Nyeri, Winnie Mukami, alisema kuwa “sisi hatuna presha kwa kuwa Odinga anatumalizia mambo yetu ya 2022.”

Alisema jinsi anavyoendelea kuhangaika akisaka kura ya 2017 iandaliwe tena kabla ya Agosti 2018, ndivyo anavyotupa shinikizo za dhati za kuendelea kuunga mkono hawa wetu ambao tulijichagulia. Anasema kila siku ya Odinga akiwa katika siasa za ukaidi na uasi ni siku ya kampeni kwa Jubilee na njama yake ya 2022 ya kumpa urais Ruto.

 

Ghasia za 2007

“Sisi tunajua hatari ya kusambaratika kama Jubilee. Tunajua kuwa tumewekeza si haba katika mikakati ya kuleta amani kati ya jamii zetu ambazo zilikuwa zinazozana kisiasa na kutumbukia katika ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007.

Kila harakati za Odinga ambazo zinaangazia njama ya kuturejesha katika hali hiyo ya ghasia ni baraka kwetu kwa kuwa tutazidi kuwa pamoja ili tumfungie nje,” akasema.

Naye mwakilishi wa wanawake wa Murang’a, Bi Sabina Chege anasema “Odinga amekuwa baraka kwetu katika msukumo wake wa siasa za upinzani.

Jinsi arukavyo juu akilenga kutuangamiza kisiasa, ndivyo sisi humngojea arejee chini tukiwa ngome thabiti.”

Anasema kuwa hali hiyo ya upinzani wa Odinga huwaweka wafuasi wa Jubilee wakiwa chonjo kwa kila hali na ambapo bora tu anaendelea kubishana, huwa anasaidia ngome muhimu za Jubilee kujitokeza kujisajili kama wapiga kura na pia kupiga kura katika siku ya uchaguzi.

Bi Chege anatoa mfano wa jinsi idadi Mlima Kenya na Rift Valley zilipendeza katika usajili na upigaji kura, lakini kujiondoa kwa Odinga katika kura ya marudio ya Oktoba 26 kukapunguza idadi hizo.

 

Kumwandama debeni

“Msingi wetu wa dhati ni kuwa, bora tu Odinga ana makali yake ya kisiasa, huwa anatufaa zaidi katika kuwasukuma wafuasi wetu kuwajibikia vita vya kumwandama ndani ya debe kupitia upigaji kura wa uhakika,” asema.

Mchanganuzi wa siasa, Prof Ngugi Njoroge anasema kuwa “Mlima Kenya na Rift Valley pamoja na jamii zingine ambazo hujihusisha na mpangilio huo wa kisiasa ungependa zaidi Odinga azidishe makali yake ya upinzani hadi 2022, ashindwe na kwa uhakika awe sasa amewakoma Jubilee.

Anasema kuwa ikiwa Odinga ataendelea na mkondo wake wa sasa wa kupinga ushindi wa rais Kenyatta, ako na hatari ya kutumiwa na Jubilee kuwa kama mwandani wao wa kimikakati “ambapo ataendelea kuwaweka wafuasi hawa katika ngome zao za kikabila wakiwa wameungana.”

Anasema Mlima Kenya hufurahia juhudi na uaminifu wa Ruto kwa Uhuru Kenyatta, na ndizo humwezesha ‘mtu wao’ kujinasua katika mtego wa Odinga.

“Kwa hilo, Mlima Kenya huendelea kukwamilia dhana kuwa wana deni kwa ngome ya Ruto ambayo ingekuwa haikujiunga na Uhuru, basi 2013 rais angeishia kuwa Odinga na apate awamu ya pili 2017,” asema.

 

Kuunganisha Mlima Kenya na Rift Valley

Katika hali hiyo, Prof Njoroge anasema kuwa “hakuna cha kupendeza Ruto na Uhuru kuliko kumwona Odinga akiendelea mbele na kuwakosea heshima wakiwa mamlakani kwa sasa kwa kuwa kufanya hivyo kuna baraka zake katika kudumisha Mlima Kenya na Rift Valley pamoja.

Mhathiri wa somo la kisiasa, Gasper Odhiambo anasema kuwa mtazamo huo umegonga ndipo kwa kuwa “Odinga huwa ni mwaathiriwa wa mbinu mbovu za kisiasa”.

Anasema kuwa Odinga angekuwa na wa kumshauri vilivyo, angetambua hawa wawili walio mamlakani kwa sasa, “lakini azidishe njama zake za kuangazia ufisadi ambao ni utamaduni wa Jubilee na katika hali hiyo ajipange upya katika kuunda muungano mwingine.”

Anasema kuwa kwa sasa kile Jubilee inadhaniwa kufanya ni kumtenga Odinga aonekane kama aliye tu na upinzani kwa Jubilee, “huku ikidaiwa kuwa inagawa pesa kama njugu kwa vyama tanzu vya Nasa kwa nia ya kuvunja muungano huo.”

 

Mhaini

Katika hali hiyo, Odhiambo anasema kuwa Odinga anabakia tu kuwa “mhaini wa kisiasa kwa Mlima Kenya na Rift Valley, huku ngome za washirika wake ndani ya kabila zao wakionyeshwa kuwa kuwekeza kwa Odinga ni kujihakikishia hasara ya kura 2022, lakini kukerwa na Odinga kuendelee kuweka ngome za Jubilee za sasa pamoja.”

Odhiambo anasema kuwa “wazo la busara kwa Odinga hadi sasa ni ajipange kama upinzani ambao alizindua kupitia kuapishwa kwake kama rais wa wananchi na hatimaye aanze harakati za uhakika za kulenga wandani wa Jubilee ambao daima hawatawahi kujiuzuia kupora uchumi wa taifa.”

Anaeleza kuwa wakati Odinga anaangazia ufisadi ndani ya “hizi serikali za jamii za ukiritimba wa urais, ndivyo hujivunia umaarufu katika maeneo yote ya hapa nchini.”

Anasema kuwa Odinga ni mwaniaji anayependeza ngome zote lakini wapinzani wake ni wale tu wa kupendeza vijiji vyao na ambapo huviunganisha kuzua kura ya ushindi.

 

‘Ufisadi ni utamaduni wa Jubilee’

Anaongeza kuwa Odinga angekuwa na wa kumshauri vilivyo, angetambua hawa wawili walio mamlakani kwa sasa, “lakini azidishe njama zake za kuangazia ufisadi ambao ni utamaduni wa Jubilee na katika hali hiyo ajipange upya katika kuunda muungano mwingine.”

Kwa sasa kile Jubilee inadhaniwa kufanya ni kumtenga Odinga aonekane kama aliye tu na upinzani kwa Jubilee, “huku ikidaiwa kuwa inagawa pesa kama njugu kwa vyama tanzu vya Nasa kwa nia ya kuvunja muungano huo.”

Katika hali hiyo, Odhiambo anasema kuwa Odinga anabakia tu kuwa “haini wa kisiasa kwa Mlima Kenya na Rift Valley, huku ngome za washirika wake ndani ya kabila zao wakionyeshwa kuwa kuwekeza kwa Odinga ni kujihakikishia hasara ya kura 2022, lakini kukerwa na Odinga kuendelee kuweka ngome za Jubilee za sasa pamoja.”

Odhiambo anasema kuwa “wazo la busara kwa Odinga hadi sasa ni ajipange kama upinzani ambao alizindua kupitia kuapishwa kwake kama rais wa wananchi na hatimaye aanze harakati za uhakika za kulenga wandani wa Jubilee ambao daima hawatawahi kujiuzuia kupora uchumi wa taifa.”