Habari

Timu ya voliboli ya KCB yaenda Misri kupigania ubingwa wa Afrika

March 8th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

MALKIA wa voliboli ya klabu za Bara Afrika mwaka 2006 KCB wameondoka nchini Kenya mapema Ijumaa kuelekea nchini Misri kupigania ubingwa wa Afrika.

Mashindano ya mwaka 2019 ya Bara Afrika ya klabu za wanawake yatafanyika Machi 16-25 jijini Cairo.

Wanabenki wa KCB, ambao wanarejea katika Klabu Bingwa baada ya kukosa makala matatu yaliyopita, wananolewa na kocha mkuu wa timu ya taifa ya Kenya Japheth Munala. Walinyakua tiketi baada ya kumaliza Ligi Kuu ya mwaka 2018 katika nafasi ya pili nyuma ya mabingwa Kenya Prisons.

Wachezaji sita kati ya saba wapya walionunuliwa na KCB mwisho wa msimu 2018 kutoka mabingwa wa zamani wa Afrika na Kenya, Kenya Pipeline, wamo kikosini. Wachezaji hao ni Murambi (nahodha), Violet Makuto, Leonida Kasaya, Jemimah Siangu, Truphosa Samoei na Christine Njambi.

Maafisa wa benki ya KCB Samuel Makome na Judith Sidi Odhiambo wampa nahodha wa klabu ya voliboli ya wanawake ya KCB Noel Murambi bendera kabla ya timu hiyo kuelekea nchini Misri kwa mashindano ya Bara Afrika. Picha/ Geoffrey Anene

Munala aliwahi kunoa KCB kati ya mwaka 2008 na 2011 kabla ya kujiunga na Pipeline na kushinda nayo ligi mwaka 2014, 2015, 2016 na 2017. Alirejea KCB mnamo Desemba 7, 2018 siku chache tu baada ya msimu wa mwaka 2018 kutamatika.

Pipeline na Prisons bado ziko jijini Nairobi zikipiga msasa kwa mashindano haya ya kifahari. Kocha wa Prisons, Josp Barasa ameambia Taifa Leo Dijitali kwamba atatangaza kikosi chake cha mwisho Jumatatu kabla ya timu hiyo kuelekea Misri.

“Bado sijataja kikosi changu cha mwisho. Niko na wachezaji 18 kambini. Nitatangaza kikosi change cha mwisho cha wachezaji 14 mnamo Jumatatu halafu tuelekee Misri mnamo Machi 13,” Barasa amesema Ijumaa.

Kenya inajivunia kushinda mataji mengi ya Afrika katika klabu za wanawake. Imeshinda mataji 14. Pipeline imetwaa mataji sita, Prisons (matano), Posta (mawili) na KCB (moja). Droo ya makala ya mwaka huu inatarajiwa kufanywa Machi 13 ama Machi 14 baada ya timu zote kuwasili.

Kikosi cha KCB

Noel Murambi (nahodha), Violet Makuto, Leonida Kasaya, Jemimah Siangu, Truphosa Samoei, Christine Njambi, Milgreen Lituva, Metrine Nabwire, Eglay Kuloba, Lincy Jeruto, Doreen Marani na Modesta Chepchirchir.