Michezo

Tupo tayari kwa kipute na DRC, Stars wajitanua

June 14th, 2019 2 min read

Na JOHN ASHIHUNDU

BEKI matata wa kushoto, Aboud Omar na kipa Farouk Shikalo wa Harambee Stars wamesema kikosi hicho kipo tayari kabisa kukabiliana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kesho Jumamosi katika mechi ya kirafiki nchini Uhispania kwa ajili ya michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON).

Katika mechi ya kwanza ya kupimana nguvu dhidi ya Madagascar iliyochezewa nchini Ufaransa, Stars walishinda 1-0.

Kwenye fainali za AFCON, Harambee Stars imepangwa katika kundi moja na Tanzania, Senegal na Algeria, lakini licha ya vikosi hivyo kuwa na mastaa kadhaa wanaosakata barani Ulaya, Omar na Farouk wamesema kikosi cha Sebastien Migne kipo katika hali ya kuwashangaza wapenzi wengi wa soka.

Farouk ambaye huchezea klabu ya Bandari hapa nchini alisema mazoezi wanayofanya nchini Ufaransa yamewapa matumaini makubwa.

“Timu yetu kwa sasa ina uwiano mzuri, mbali na kikosi kuchaganyika vyema kiumri. Hapa tumechanganyika vijana na wakongwe, hali inayotuongezea uwajibikaji kuwa kikosini na matarajio makubwa,” alisema kipa huyo aliyesaidia Bandari kutwaa ubingwa wa SportPesa Shield kabla ya kuondoka nchini kuelekea Ufaransa.

“Tunaweza kufanya vizuri kutokana na ushirikiano wetu mzuri,” alisema Omar ambaye kwa sasa anaichezea klabu ya Sepsi Sfantu Gheorghe nchini Ufaransa.

“Nitatumia uzoefu wangu kusaidia Harambee Stars kupiga hatua nchini Misri,” alisema nyota huyo ambaye pia aliwahi kuchezea klabu ya Bandari.

Omar ni miongoni mwa wachezaji wa Harambee Stars ambao wamekuwa kwenye timu hii kwa muda mrefu chini ya makocha tofauti.

Mbali na Tanzania ambayo tumekuwa tukiilemea, itakuwa mlima mkubwa kupanda mbele ya Senegal na Algeria ambazo zinajivunia wachezaji kadhaa wanaosakatia klabu kubwa katika ligi maarufu barani Ulaya.

Nyota hao ni pamoja na Sadio Mane wa Liverpool, Diara Sakho wa West Ham United na Pepe Abou Cisse miongoni mwa wengine.

Kadhalika kutakuwa na Riyad Mahrez (Manchester City), Yacine Brahimi (FC Porto, Ureno), Aissa Mandi (Real Beits, Uhispania), Mehdi Zeffane (Rennes, Ufaransa), Mehdi Tahrat (Lens, Ufaransa), Sofiane Feghouli (Galatasaray, Uturuki).

Nyota wa Tanzania

Tanzania kwa upande wake inajivunia nyota kadhaa chipukizi wanaotarajiwa kuzua upinzani mkali.

Pia kuna mkali Mbwana Ally Samatta wa Genk ya Ubelgiji pamoja na kinda mahiri, Kelvin John ‘Mbappe’.

Baada ya maandalizi hayo ya wiki tatu, Harambee Stars watafunga safari ya kuelekea Misri amwishoni mwa wiki mbapo wamepangiwa kuanza dhidi ya Algeria mnamo Juni 23.

Mechi ya pili itakuwa dhidi ya Tanzania mnamo Juni27 Juni na kumaliza dhidia ya Senegal Julai Mosi, na kusubiri kuona kama matokeo yao itatupeleka hatua ya mwondoano.

Harambee Stars ilifuzu kwa Afcon 2019 baada ya kumaliza ya pili nyuma ya Ghana katika Kundi F, huku timu za Ethiopia na Sierra Leone zikiambulia patupu matawaliwa.