Afya na JamiiMakala

Ugonjwa wa Kisukari ulivyosababisha mama kujifungua watoto wenye uzito kupindukia

Na WANGU KANURI August 28th, 2024 3 min read

WAKATI Faith Thuo, 27, alipokuwa mjamzito alianza kupata maumivu kichwani, ujauzito wake ulipokuwa na miezi sita. 

Bi Thuo alimwona daktari wake wa uzazi akapewa tembe kadhaa lakini maumivu yale hayakutoweka ndiposa akalazwa.

Vipimo tofauti mwilini mwake vilionyesha kuwa Bi Thuo alikuwa akiugua ugonjwa wa Kisukari unaotokana na ujauzito (gestational diabetes).

“Hapo awali sikuwa na ugonjwa wowote ule wa Kisukari,” anasema.

“Nilianza matibabu lakini sababu ya ugonjwa huu kujulikana ukiwa umechelewa ilibidi nijifungue kabla wakati kutimia (baada ya wiki 37).”

Kwa sababu ya ugonjwa huo, mtoto wake Bi Thuo alizaliwa akiwa mkubwa sana (kilo 3.9).

“Viwango vyangu vya sukari vilirejea kawaida baada ya kujifungua. Niliposhika mimba tena, niliugua ugonjwa huu tena na mtoto wangu akazaliwa akiwa na uzito wa kilo 4.”

Kama ilivyokuwa ada, baada ya kujifungua viwango vya sukari vilirudi hali yake ya kawaida lakini kwa muda tu. “Hivi sasa vinadhibitiwa.”

 Ugonjwa huu wa Kisukari ni upi?

Dkt Odero Ong’ech, mtalaamu wa afya ya uzazi katika Nairobi Reproductive Health Services, anasema kuwa ugonjwa wa Kisukari unaompata mama akiwa mja mzito ni mojawapo ya ujauzito ulio na hatari sana (high risk pregnancy).

Kwa wanawake wengi, viwango vyao vya sukari hurejea kama awali wanapojifungua. “Hii ndiyo tofauti ya ugonjwa huu wa Kisukari na hayo mengine; ule unaofanya kongosho kutotengeneza insulini (diabetes type 1) na ule unaofanya kongosho kutengeneza insulini kidogo (diabetes type 2),” anasema Dkt Odero.

Mwanamke aliye na hatari ya kuugua ugonjwa huu wa Kisukari sababu ya kuwa mjamzito ni yule anayetoka kwenye familia ambayo wengi wa wanafamilia wake wanaugua ugonjwa wa Kisukari.

Pili, Dkt Odero anasema ni mwanamke mwenye uzito wa kupindukia (obesity), alikuwa na ugonjwa huu alipokuwa na mimba hapo awali, amejifungua watoto wakubwa (walio na zaidi ya kilo 4), watoto wake wamekuwa wakifariki tumboni (still-births) na wale walio na matatizo ya kihomoni kwa mfano, wanaougua polycystic ovarian syndrome (PCOS).

“Visa vya ugonjwa huu wa PCOS vimeongezeka sana sasa sababu ya kutozingatia lishe bora na afya njema,” anafafanua.

Dkt Odero Ong’ech, mtalaamu wa afya ya uzazi katika Nairobi Reproductive Health Services. PICHA|HISANI

“Nchini Kenya, ugonjwa huu unaathiri angalau asilimia 4 ya wanawake huku asilimia 14 ikirekodiwa duniani. Hata hivyo, idadi haswa ya wanawake nchini inaweza kuwa zaidi sababu ripoti za aina hii hazizingatiwi kwa kina,” anaeleza Dkt Odero.

Utajuaje unaugua ugonjwa huu?

Ugonjwa huu huweza kujulikana katika kipindi cha pili cha ujauzito (second trimester) angalau kutoka wiki 20 hadi 28. Dkt Odero anasema kuwa wakati huo mama hufanyiwa vipimo mbalimbali kuangalia viwango vyake vya sukari.

“Kwa mfano, mama huyo anaweza akapimwa viwango vyake vya sukari kabla hajala chochote au apatiwe sukari nyingi ili mwili wake upigane nayo almaarufu oral glucose tolerance test (OGTT). Iwapo sukari hiyo itaathiri mwili wake basi itaonyesha na tutarekebisha kupitia matibabu mbalimbali.”

Hali kadhalika, Dkt Odero anasema kuwa vipimo vya viwango vya sukari hupendekezwa kwa kina mama wote wajawazito. Kwa wale wanaotoka katika maeneo yenye mapato ya chini, Dkt Odero anashauri kupimwa kwa kutolewa damu kwa kidole (fasting blood sugar) ili kutathmini viwango hivyo vya sukari.

“Pia, kina mama hao wanaweza wakafanyiwa vipimo vya HbA1C ambavyo huangalia wastani wa viwango vyako vya sukari kwa kipindi cha miezi mitatu.”

Mama mjamzito ataweza kujua kama anapata dalili za ugonjwa huu wa Kisukari iwapo anakunywa maji mengi, anaenda haja ndogo sana, ana hamu nyingi ya kula, na anaongezea uzito wake sana. Lakini, iwapo ugonjwa huu umeendelea sana mwilini, Dkt Odero anasema kuwa uwezo wa kuona kwa mama huyo huathiriwa.

“Cha kushangaza ni kwamba, wanawake wengi wajawazito huugua ugonjwa huu bila wao kujua,” anaeleza.

Ili kudhibiti ugonjwa huu, Dkt Odero anasema kuwa ushirikiano wa watalaamu mbalimbali; wakiwemo madaktari wa afya ya uzazi, Kisukari (endocrinologist) na mtalaamu wa lishe (nutritionist) huzingatiwa. Japo tembe (oral hypoglycemic drugs) husaidia kurekebisha hali hiyo, wagonjwa wengine hudungwa sindano za insulini.

Athari za ugonjwa huu kwa mama na mtoto

Iwapo ugonjwa huu hautadhibitiwa ipasavyo, Dkt Odero anafafanua kuwa madhara yake yatamwandama mtoto na mama.

Athari zake kwa mtoto ni pamoja na kuwa mkubwa zaidi (fetal macrosomia) anazaliwa kwa njia ya upasuaji, azaliwe kabla viungo vyake havijakua vizuri (congenital abnormalities), au azaliwe kabla muda wake kufika (preterm babies).

Isitoshe, mtoto huyu anaweza akafia tumboni mwa mamake, au mapafu yake yachelewe kukua.

“Hii ndiyo changamoto kubwa sana ambayo tunakumbana nayo lakini mtoto huyu hupatiwa dawa za kusaidia mapafu yake kukua.”

Kwa upande wa pili, athari za ugonjwa huu kwa mama zinaweza kumfanya apoteze maisha yake au awe mgonjwa mahututi.

Dkt Odero anaongezea kuwa iwapo viwango vyake vya sukari havitadhibitiwa, mama anaweza kuwa kipofu (diabetic retinopathy), figo zake zishindwe kufanya kazi ipasavyo, au mishipa yake iathirike.

“Mama huyu pia yupo katika hatari ya kuugua shinikizo la damu, prekilampsia au augue ugonjwa wa Kisukari maisha yake yote.”

[email protected]