Habari

Uhuru atuliza joto Tanzania, apata mapokezi mazuri

July 6th, 2019 3 min read

Na CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta alitumia ziara yake ya siku mbili Tanzania kutuliza joto kati ya nchi hiyo na Kenya kufuatia matamshi ya Mbunge wa Starehe, Charles Njagua ya kutisha raia wa kigeni wanaoishi Nairobi.

Rais Kenyatta aliyelakiwa kwa furaha alipowasili kijiji cha Chato, wilaya ya Geita aliwataka raia wa Tanzania kupuuza madai ya mbunge huyo akisema ni mshamba ambaye hajatembea sana ulimwenguni.

Akihutubia wakazi akiandamana na mwenyeji wa Rais John Magufuli, Rais Kenyatta alihimiza udumishaji wa umoja kati ya watu wa Afrika Mashariki kwa ajili ya kuchochea maendeleo.

Japo ziara hiyo ilisemekana kuwa ya kibinafsi, Rais Kenyatta alionekana kulenga kuitumia kutuliza joto lililoibuliwa na vitisho vilivyotolewa na Bw Njagua dhidi ya raia wa kigeni wanaoendesha biashara Nairobi, wakiwemo Watanzania.

Bw Njagua aliitaka serikali kuwafurusha watu hao kwa msingi kuwa wanatoa ushindani usiofaa kwa wafanyabiashara wa eneo bunge lake.

Rais Kenyatta alipuuzilia mbali matamshi ya Bw Njagua huku akisema hakuna kiongozi wa Kenya ataruhusiwa kusababisha uhasama kati ya watu wa Afrika Mashariki.

“Unawezaje kumwambia Mtanzania asizuru Kenya au kufanya biashara huko? Na vilevile ninyi hampaswi kuwazuia Wakenya kuendesha biashara hapa Tanzania,” Rais Kenyatta alisema huku akishangiliwa kwa furaha.

Bw Njagua maarufu kama “Jaguar” alikamatwa majuzi baada ya matamshi yake kuibua kero katika bunge la Tanzania na hofu miongoni mwa Watanzania wanaendesha biashara humu nchini. Aliachiliwa kwa dhamana ya Sh500,000 pesa taslimu lakini baada ya kuzuiliwa kwenye seli ya polisi kwa zaidi ya siku saba.

Rais Kenyatta vilevile alipendekeza ndoa kati ya raia wa Kenya na Tanzania kama njia mojawapo ya kukuza na kudumisha umoja na utangamano kati ya raia wa mataifa ya Afrika Mashariki.

“Itakuwa jambo la busara ikiwa vijana wa hapa Tanzania wataoana na wenzao wa Kenya kujenga uhusiano thabiti. Hii ni kwa sababu watoto watakaozaliwa katika ndoa kama hiyo hawatasema wao ni Wakenya au Watanzania bali watajihisi kama raia wa Afrika Mashariki,” alisema Rais Kenyatta na kuibua kicheko miongoni mwa hadhira.

Maombi

Kiongozi wa Kenya pia alimwombea mamake Rais wa Tanzania, John Magufuli, mama Suzana Magufuli, na kumtakia afueni.

Bw Kenyatta ambaye alikuwa amefanya ziara ya kibinafsi ya siku mbili, alifanya mazungumzo na mwenyeji wake kwanza kabla ya kuelekea nyumbani mwa Mama Magufuli karibu na mji wa Chato ambako amekuwa akiuguzwa.

Kwenye video inayosambaa mitandaoni  Rais Kenyatta anaonekana akimwambia mamake Rais Magufuli kwamba taifa la Kenya linamtakia uponyaji.

 “Sisi tumekuja kukutembelea na kukuhakikishia ya kwamba twakutakia nafuu,” akasema.

Baada ya hapo, Rais Kenyatta alionyesha ishara ya msalaba na kuanza kuomba.

“Tunafika mbele yako ewe Bwana, tukiandamana na ndugu yangu Magufuli. Tumekuja kumtembelea mama yake ambaye anaugua, tunaomba kwamba umpe nguvu na baraka. Umwezesha kupata nafuu ili aweze kutunza familia yake. Kwa kujitolea kwake kukuza Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mungu umsaidie,” akasema.

Bw Kenyatta anaendelea, “Tunaomba kwamba kama majirani tuweze kulinda masilahi ya ndugu na dada zetu. Bariki mataifa yetu na uyawezeshe kupata amani ya kudumu.”

Baadaye akihutubia mamia ya wakazi mjini Chato, kaskazini mwa Tanzani, Rais Kenyatta aliwaonya wanasiasa wa Kenya dhidi ya kutoa matamshi ambayo yanaweza kuvuruga amani katika kanda ya Afrika Mashariki.

Hii ni baada ya Mbunge wa Starehe Charles Njagua Kanyi, almaarufu Jaguar, kudaiwa kutisha kuwashambulia na kuwafurusha raia wa kigeni ambao wanaendesha biashara Nairobi, wakiwemo Watanzania.

Wabunge na maafisa wakuu wa serikali ya Tanzania walikerwa na matamshi hayo, ikizingatiwa kuwa kuna idadi kubwa ya Watanzania wanaoendesha biashara katika eneo la Kamukunji na Soko Kuu la Gikomba.

Ilibidi balozi wa Kenya nchini Tanzania Dan Kazungu kutakiwa kufafanua ikiwa matamshi ya Bw Jaguar yalikuwa yakiakisi msimamo wa serikali ya Kenya au la.

Wabunge wa Tanzania wakiongozwa na kiongozi wa upinzani Freeman Mbowe waliitaka serikali sio tu kujitenga na vitisho hivyo bali imchukulie hatua za kisheria Bw Jaguar.

Ndiposa Mbunge huyo wa chama cha Jubilee alikamatwa na kuzuiliwa korokoroni kwa zaidi ya wiki mmoja kabla ya kufunguliwa mashtaka kortini.

Aliachiliwa huru kwa dhamana ya Sh500,000 pesa taslimu na kesi yake itaendelea mnamo Julai 17 katika mahakama kuu ya Milimani.