Makala

‘Uji Power’ wa mukombero unaoweka wanaume raha ya kula!

January 20th, 2024 2 min read

NA LABAAN SHABAAN

KATIKA barabara ya Ronald Ngala jijini Nairobi, wanaume hawaishi kwenye foleni wakimezea mate uji maalum maarufu Uji Power.

Hapa, kivutio kikubwa ni kiungo cha mukombero chenye harufu ya kuvutia inayoaminiwa na wanaume kuwaongeza nguvu za kiume.

Mukombero ni jina la jamii ya Luhya kutaja mmea ambao ni dawa ya kienyeji kutibu uvimbe, mafadhaiko, uchovu na huaminiwa kuongeza nguvu za kiume.

Mmiliki wa biashara hii Anne Wambui anaambia Taifa Leo kuwa wanaume wakikosa mukombero wanampita kama gari la miraa.

Soma pia Mukombero kutumika kama kiungio cha uji   

Kwa hivyo yeye huhakikisha kiungo hiki hakikosi kwenye ubwabwa kila siku.

Tangu alipoongeza uji huu kwenye menyu yake mwaka wa 2018, wateja waliongezeka sana akiwauzia uji angalau wateja 1,000 kwa siku.

Anne Wambui na wafanyakazi wake wakiandaa uji power kwa wateja jijini Nairobi. PICHA | LABAAN SHABAAN
Bob Ouma akinywa uji power. Anasema ni chakula cha bei nafuu kwake awapo jijini kila siku. PICHA | LABAAN SHABAAN

“Nilipogundua uji huu unapendwa, ilibidi niongeze wafanyakazi hadi kumi na kuhakikisha kazi inaendelea usiku na mchana,” Wambui alikiri.

Kisha akaongeza: “Changamoto ya kazi hii ni kuwa inahitaji shughuli nyingi kwa hivyo mara kadhaa wafanyakazi huchoka na kutoroka.”

Japo Wambui huwa mgumu kueleza siri yake ya mapishi, aliorodhesha yaliyomo katika uji kuwa unga wa mahindi, njugu, muhogo, malenge, maziwa na viungo kama tangawizi, asali, mukombero na kadhalika.

Wilson Mugalia aliyesifu uji huu alisema humpa nguvu sana katika tendo la ndoa na humfanya kuwa na ujasiri katika mchezo.

“Kama sina mtu siwezi kunywa uji huu. Labda ninywe bila kuweka mukombero tu hadi mke wangu arejee,” aliungama.

Bob Ouma, mteja wa kila siku, alieleza kuwa chakula chake cha kawaida mchana ni uji power.

Ouma alidokeza harufu ya kiungo cha mukombero huumpa hamu sana ya kula.

“Kwa Sh50 tu kila siku ninapata chakula cha mchana na siwezi kula tena sababu sihisi njaa haraka,” alisema.

Naye Fidel Ouma alikariri kauli hii akisema uji huu ni mzuri kwa wanaume wasio na nguvu za kiume.

“Najua rafiki zangu ambao husema uji huu huwapa nguvu za mchezo lakini mimi sina matatizo kama lao kwa hivyo nanywa kama kinywaji tu,” alikiri.

Katika mkahawa huu utawaona wanawake wawili tu kwa kila kundi la wateja kumi.

Na wanapotiliwa uji hawana haja ya kuongeza kiungo cha mukombero; labda tangawizi, asali na kadhalika.

“Mukombero ni wa wanaume kwa sababu sisi wanawake hatuna shida ya nguvu za mapenzi. Kama mwanamke hana nguvu, pengine ni mgonjwa tu,” alisema mteja asiyetaka kutajwa.

Mteja huyu alikiri kuvutiwa na harufu ya mukombero kila siku ila hakuwahi kunywa sababu ya foleni ndefu ya wateja anapopita akitoka kazini mida ya jioni.

“Nimeambiwa eti ukinywa uji huu huendi haja ndogo sana kama uji wa kawaida ndiyo maana nimekuja kujaribu,” aliongeza.

Wambui hukumbwa na changamoto za mitambo ya kusindika vinywaji hivi na wafanyakazi kuacha kazi tu kwa uchovu.

Hata bei ya vyakula ilipopanda, wateja wake waliongezeka alipokuwa kimbilio kwa waliotafuta mlo wa bei nafuu.

Uji huu ulikuwa kibadala cha juisi ya miwa na matunda nyakati za baridi.

Kwa mujibu wa Wambui, biashara hii ilianza mwaka wa 2014 kwa kuuza sharubati kwa wateja hususan wakati wa jua kali.