Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Nadharia ya Udhanaishi

February 27th, 2019 2 min read

Na MARY WANGARI

NI nadharia inayoangazia maisha ya mwanadamu. Udhanaishi hujikita katika kuhakiki yafuatayo:

  1. Fujo na udhaifu wa maisha ya mwanadamu
  2. Upweke na usiri unaomkumba binadamu
  3. Kihoro na hofu kubwa anazozipitia
  4. Utupu na ubwege wa maisha
  5. Suala la uhuru
  6. Kifo
  7. Uhusiano uliopo baina ya binadamu na Mwenyezi Mungu

Nadharia hii imetafasiriwa na kupambanuliwa na wataalamu anuwai jinsi ifuatavyo:

Kimani Njogu na Rocha Chimerah (1999), wanafasiri Udhanaishi kuwa nadharia ambayo inajibidiisha na dhana ya maisha. Wasomi hawa wanajaribu kuuliza swali la kifalsafa hivi: Maisha ni nini?. Kwa undani wanajikita kutafiti nafasi ya mwanadamu ulimwenguni.

Wamitila, K. W. (2003), katika Kamusi ya Fasihi, Istilahi na Nadharia anaeleza kwamba Udhanaishi ni dhana inayotumiwa kuelezea falsafa ya kuwako na maisha. Dhana hii inatumiwa kueleza Maono au Mitazamo inayohusiana na hali ya maisha ya binadamu, nafasi na jukumu lake ulimwenguni na uhusiano wake na Mungu.

Wanjala Simiyu (2012), kwa upande mwingine katika Kitovu cha Fasihi Simulizi anasema kuwa Udhanaishi ni falsafa au Mtazamo wa Maisha ulio na kitovu chake katika swali kuwa, anaeleza kuwa maisha ni nini na yana maana gani kwa binadamu?, ni kwa njia gani mwanadamu anaweza kuyabadilisha maisha yake yaliyojaa dhiki, mashaka na simanzi?

Nadharia ya udhanaishi ni falsafa inayoshugulikia maswala kuhusu maisha; ni mtazamo unaokagua hali ya nafasi ya mtu katika ulimwengu anamoishi na pia ni falsafa inayozungumzia uhusianao uliomo kati ya mtu na Mungu na iwapo mtu anapaswa kuamini kuwepo kwa Mungu.

Aidha, nadharia hii inatusaidia kuhakiki maisha ya mwanadamu anayeishi katika ulimwengu uliojaa shida na matatizo mengi ambayo aghalabu yanasababishwa na binadamu mwenyewe. Shida zinayoyapitia ni kama vita, njaa na uchumi kuzorota, kukosa kazi, ajali barabarani na kadhalika.

Matatizo haya yanafanya mwanadamu kukata tamaa na kushuku iwapo kweli Mungu yuko. Waasisi wa nadharia wanajumuisha wanafalsafa wafuatao:

  1. Soren KierKegaard wa Ki-Den,
  2. Mjerumani Friedrich Nietzsche,
  3. Martin Heidegger
  4. Gabriel Marcel.

 

Baruapepe ya mwandishi: [email protected]

 

Marejeo

Wamitila, K. W. (2003). Kamusi ya Fasihi: Istilahi na Nadharia. Nairobi: Focus.

Wa Thiong’o, Ngugi (1998). Penpoints Gunpoints and Dreams. Oxford: Clarendon.

Wellek Rene & Austin Warren ( 1986). Theory of Literature. Harmondworth: Penguin